Willy
akajikaza kiume. “Najua wote mnajua kuwa nampenda Pendo. Si kwa kujitetea hapa,
ila najua nyinyi mmekua mashahidi wa maisha yetu kabla. Tokea chuo nimekuwa na
Pendo. Sikuwahi kumtenda vibaya. Nimekuwa naye katika shida na raha. Nilimlinda
hata mbele ya familia yangu, tena wewe Nancy ni shahidi wa karibu sana wa haya
ninayozungumza. Unatujua mimi na Pendo vizuri sana.” “Hata mimi nilidhani
nawajua!” Nancy akajibu. “Nilikosa. Nimekosa. Sio kwa kujitetea, lakini nataka
kuwa mkweli kwenu kwa sababu ya kumpenda Pendo. Nitaongea ukweli tu. Niliingiziwa
hofu kwa muda mrefu mkapa ikafanikiwa kuniingia kuwa mama yetu atakufa bila
kuona hata mjukuu mmoja kutoka kwangu. Mama alinisihi mpaka kwa machozi,
mwishoe nilikubali kuzaa na yule msichana, ili tu kupata mtoto, bila kumuumiza
Pendo.” “Ulimuumiza sana tu.” Akadakia Nancy.
“Nikisema
kumuumiza ni ile heshima niliyoweka kwake hata nikiwa kwenye hiyo shuguli ya kutafuta
mtoto. Nilikuwa makini kiafya nikijua yupo Pendo.” Willy akaendelea kwa
tahadhari. “Mama aliponiwekea pressure na mimi nikamuona ni kweli ni mgonjwa na
madaktari wote wanakiri kuwa hatapona, ndipo nilipokubali kuzaa na yule
msichana kwa masharti. Kuhakikisha anapimwa magonjwa yote, na anakaa nyumbani,
atunzwe pale na kuangaliwa asije kuwa ni malaya, akaishia kutuua mimi na Pendo.
Na sio kwamba nilikuwa nikifanya naye mapenzi kwa starehe! Ilikuwa ni siku
alizokuwa akiniambia ni za hatari ambazo ni za kushika mimba. Ambazo pia
nilikuja kugundua au alikiri wazi kuwa alikuwa akinidanganya. Alilala na mimi
akiwa tayari alishakuwa akilala na baba. Anakuja kuniambia ni siku za kushika
mimba, kumbe zile zakushika mimba alikuwa akizitumia na baba.” Hapo wote kimya.
“Na
katika yote hayo pia, nilitunza heshima ya Pendo, ndio maana hamkuwahi hata kumsikia
Pendo akilalamika kuwa nimebadilika. Nilijitahidi kuwa na mke wangu, japo
nakiri, mwishoni baada ya yule msichana kuniambia ni mjamzito, ni kama juhudi
yakutafuta mtoto na Pendo, ikaisha wala sikupunguza. Niliacha kabisa. Na
ninajua ndio kitu pekee ambacho Pendo atakuwa hata shahidi wangu atasema ndicho
alichoona mabadiliko na uhuru wa mapenzi kwake uliisha kabisa. Ni kwa ile hali
ya hukumu kuona nalala na mwanamke mwingine nje, halafu nakuja kumshika na
yeye.” “Ikawaje?” Kenton akataka aendelee.
“Nilipotoka
sasa hapa ramsi kwa talaka na kwenda kumfuata na kumwambia atoke pale nyumbani
twende tukaanze maisha kama wazazi ndipo yote yalipofunguka. Kumbe walikuwa na
mahusiano mazito yenye ahadi ya kuja kufunga ndoa baada ya kumzika mama ili
sasa walee mtoto waliyejua ni wao wala si wangu. Kufupisha habari, walijaliwa
kupata mtoto wa kike. Ana miezi miwili, na mwezi ujao wanaoana.” Kimya.
“Najua
nimekosa wazazi wangu, lakini naomba mkumbuke mapenzi niliyokuwa nayo kwa Pendo
na jinsi nilivyohangaika kutafuta watoto na Pendo. Tafadhali kumbuka mama
yangu. Kumbuka jinsi nilivyomlinda Pendo na kumkinga na maneno ya watu. Wakati
wote nimesimama na Pendo, Nancy najua unajua. Hata kama umenichukia, lakini
unajua wazi nampenda mdogo wako na sijawahi kumsaliti kwa miaka yote tokea tupo
chuo. Maisha yangu yote nimekuwa nikimtanguliza Pendo. Jamani nyinyi ni
mashahidi, nampenda Pendo. Na nipo hapa si kwa ajili ya watoto tu, hata Pendo
mwenyewe.” Kimya wote wakimtizama.
“Nimemuomba
Pendo anipe muda. Hata kama si kama mume, basi angalau kama mzazi mwenzake. Niwepo
kumsaidia yeye kwanza. Pendo amesimamisha maisha yake yote, kazi nzuri ambayo
anaipenda na ameihangaikia, yupo hapa akipambana kutunza uhai wa watoto wetu.
Na mimi naomba kusaidia. Kwa namna yeyote ile naomba kusaidia. Na mimi niwepo
tu, sio nije nijitokeze wakati watoto wamezaliwa au wamekua! Sidhani kama ni
sawa jamani, na hata nyinyi sidhani kama mnaona itakuwa sawa, eti nije nirudi
hapa watoto ni wakubwa!” “Nafikiri vitanda vyote vipo chumbani kwao. Ni
vyakufunga tu.” Baba yake Pendo akamwambia Willy. “Asante sana Mzee wangu.
Nashukuru.” Pendo akavuta pumzi kwa nguvu maana ni kama baba yake alifunga huo mjadala,
na ndugu zake wakaliheshimu hilo.
Willy
akamgeukia tena Pendo. “Mnaendeleaje?” Akarudia kuuliza. Akaona wanatoka mmoja
baada ya mwingine, wakabakia wao wawili. “Tumeamka vizuri kabisa. Vipi wewe?
Utakuwa ulilala kweli! Uliondoka usiku sana.” “Nililala. Acha nikachangamkie
kazi kabla sijaonekana hovyo zaidi.” Pendo akacheka. Akambusu shavuni na
kutoka. Mara mama yake na Nancy wakarudi. “Kwa hiyo utamsamehe?” Kabla Pendo
hajamjibu Nancy, Willy akarudi na maua. “Niliyaacha kwenye gari. Acha niyatoe
haya yazamani, niweke mapya.” “Nipe niyashike kwanza kidogo, kabla hujayaweka
kwenye maji. Nitayaweka hata jioni. Asante sana.” “Karibu.” Akamkabidhi na
kumbusu shavuni.
Nancy
akakohoa. “Nampenda Pendo, na wewe nishahidi Nancy.” “Upo hapa Willy kwa kuwa
kule kulishindikana. Najiuliza, kama kule mambo yangeenda sawa, ungerudi hapa?
Na kabla hujajibu hilo, je kama Pendo asingekuwa mjamzito leo, ungekuwa hapa?” Kabla
hajajibu, akaongeza swali jingine. “Na kama huna taarifa, Pendo bado yupo
kwenye kubembeleza mimba. Sisemi kama itatokea, ila ikitokea, kesho ukarudi
hapa, ukakuta hakuna watoto, utafanyaje?” Nancy akaendelea kwa jazba. Kabla
hajajibu akaongeza tena. “Kwa taarifa yako tu, ulimuacha akiwa mjamzito. Na
aliteseka sana kubaki hapa bila wewe. Unachotaka sasa hivi hapa, nikumtonesha.
Naku....” Akaingia mume wake Nancy na kumbemba mkewe juu juu. “Niache bwana Leon!
Huyu Willy anamfanyiaga Pendo vitu anavyojua akiondoka, anamuacha mwenzie mnyonge.
Kwa nini..” Akamtoa hapo chumbani kwa nguvu.
Wakabaki
watatu hapo chumbani. “Nilikosea mama yangu. Lakini sasa hivi nimejifunza
kutokana na makosa. Huko nje nimeona panavyotisha mama. Maisha yangu yapo kwa
Pendo. Na nitatulia hapa mpaka Pendo atakaponikubali. Hata kama itachukua
miaka, mimi nitatulia tu. Hutakaa ukasikia tena.” “Mungu akusaidie Willy. Nancy
anaongea hivyo kwa wasiwasi wa sisi wote. Uliumiza kila mtu Willy! Uliondoka
vibaya sana. Uliondoka wakati mwenzio akikuhitaji! Umemchafua sana hapa mjini,
ukamuacha akichekwa.” “Mama, hata mimi nimechekwa mno. Wala si Pendo peke yake.
Mungu amenichapa nje hadharani. Nilikuwa siwezi hata kutizama watu machoni. Siwezi
hata kupokea simu za marafiki zetu. Nimejifunza mama yangu, na nipo hapa si
kujaribu tena. Nimerudi na nimefunga milango yote ya nje, na nimetupa funguo
zote, na Mungu atanisaidia tu. Naombeni mnisamehe kwa kuwafedhehesha. Nisamehe
mama yangu. Nimekosa.” “Watamaliza kutengenezeza chumba cha watoto huko.” Mama
Kenton akaongea taratibu kama Pendo mwenyewe. Willy akatoka kwa haraka.
Willy
alimkuta mkwewe yaani baba K, na shemeji yake, huyo Kenton ndio wapo kwenye
hicho chumba cha watoto. Nancy na mumewe walikuwa nje wakitengeneza nyama. Mke
wa Kenton alikuwa jikoni akimsaidia Sifa kupika. Alipoingia tu hapo, pakazuka
ukimya. Willy akajikaza akabaki tu humo ndani hata hajui ashike nini! Mwishowe
baba Kenton akaanza. “Kwa hiyo sasa hivi unaishi wapi?” “Kwenye apartment zile.”
Akaelekeza anakoishi, wote wakamgeukia. “Zile wanazolipa kwa dola!?” Shemeji
yake akamuuliza kwa mshangao. “Ndiyo. Lakini natafuta sehemu ya bei ya chini
kidogo.” “Kwani kazi bado upo palepale au uliuza kiwanja cha Kigamboni?” Willy
akacheka kidogo kwa kusikitika. “Najua natumia pesa nyingi pale, lakini sikuwa
na pakwenda, ndio nikalipia pale kwa miezi 6. Hivi hapa nakaribia kumaliza
mkataba wangu. Na hapana. Sijauza kiwanja cha Kigamboni. Na kazi nilipata
kwengine.” “Wapi?” Shemeji yake akaendelea
kumuhoji. Willy akamtajia. “Oooohooohh! Ndio maana. Pesa ipo.” Shemeji yake
akaongea hivyo na kuendelea na kazi.
Wazi
Kenton bado alionekana na hasira naye na hawezi kuwa naye karibu. Alimpuuza hapo
ndani akamfanya ajisikie si kitu. Lakini Willy akajiambia atabaki tu mpaka
mwisho wao ndio wamuache hapo. Alitoka mara kwa mara kwenda kumuangalia Pendo. Wakati
mwingine alimkuta na Nancy au mama yake, na kumlazimu kutoka bila kukaa sana.
“Nilikuja kukuangalia kama unahitaji kitu.” Aliishia kusema hivyo alipowakuta
hao wawili na kutoka baada ya Pendo kujibu, “Nipo sawa Willy, asante kujali.” Aliweza
kuona uangaliwaji mbaya kutoka kwa Nancy, lakini si mama yao. Kidogo yeye
alikuwa muugwana. Kule kwenye chumba cha watoto nako, shemeji yake ni kama
alimnyima kazi. Mara nyingi akaishia kuwa mtizamaji tu, lakini hakukata tamaa.
Chakula
kilipokuwa tayari alikaribishwa kama kawaida. Ili asiwaudhi, alipoona Pendo
anakula chakula chake chumbani, na yeye akaenda kwenye chakula cha watu wote,
akachukua chakula chakumtosha na kwenda kukaa nje kabisa upande wa jikoni.
Wakaendelea kuongea na kucheka bila ya kujali. Pendo akatoka na chakula chake
ili ale pamoja nao. Wakamuandalia sehemu ya kukaa, akajipanga vizuri, na kukaa
ili ale. Lakini akagundua Willy hayupo pale katikati yao. “Willy yuko wapi?” Akauliza
Pendo akiangaza macho. “Nilimuona akipakua hapo, labda ameenda kula ndani.”
Akajibu wifi yao. Pendo akatulia kidogo, wakamuona na yeye anasimama. “Wapi
tena mama wawili?” “Naenda kumtizama Willy.” Pendo akajibu kwa upole, akijua
wapo kinyume naye. Pendo mtoto wa mama na baba K, mziwanda wao, hawajui
kumkatalia kitu, akabaki wakimwangalia.
Pendo akaona utizamwaji wake.
“Willy
amekosa, na ametuumiza. Zaidi mimi. Lakini amerudi, halafu ni baba wa watoto
wangu. Angeweza kutorudi na kujaribisha kwengine, lakini
amerudi kwangu akiwa hana uhakika wa watoto, na nilimwambia mara ya kwanza tu
tulipoonana juzi kuwa hawa watoto wanaweza wasizaliwe, lakini Willy alirudi. Na
ninajua wote mnajua ananipenda Willy. Amekosa, naomba mumsamehe tumpe nafasi
nyingine hata yakuwa baba.” Wote kimya. “Kaka
K?” Pendo akamuita kaka yake ambaye ndio mkali kuliko wote. “Mimi
nakufikiria wewe Pendo. Sitaki aje akuumize tena.” “Siwezi
kujibu ya baadaye, lakini wewe mwenyewe ulishaniambia kuwa ni kweli Willy
ananipenda. Ukawa ukimtizama kama mdogo wako. Mnazungumza na kuongea. Amekosa,
naomba msamehe na mpe nafasi nyingine. Hivyo hivyo Nancy. Nyinyi ndio watu
wangu wa muhimu na ndio mpo karibu na mimi na watoto wangu. Mkimchukia Willy
mnaniweka kwenye wakati mgumu.” “Kwa maana nyingine wewe umeshamsamehe?”
Akauliza Nancy. “Ndiyo.” Akajibu Pendo kwa
haraka sana na kumshangaza dada yake.
“Huyu
Willy si amerudi juzi tu? Unajuaje kama atakaa?”
“Sijui dada yangu. Lakini unajua jinsi Willy anayonipenda Nancy, na jinsi
alivyonibeba tokea chuoni, wewe ukiwa shahidi. Lakini amerudi, Nancy. Na sisemi
ndio tunarudiana kimapenzi, lakini ameniomba angalau awepo kwenye maisha ya
watoto wake. Na wote mnajua jinsi mimi na Willy tulivyokuwa tukihangaika
makanisani na mahospitalini kutafuta mtoto. Naombeni kwa swala la ubaba,
tumruhusu. Kama hamtafanya kwa ajili yake, basi naombeni mfanye kwa ajili ya
mimi, mdogo wenu.” Hapo anaongea Pendo machozi yapo kifuani.
“Mimi
naona Pendo yupo sahihi.” Baba yake akaingilia. Lakini wote walijua lazima
Pendo atetewe na baba yao. Alimpenda huyo Pendo kama mtoto wa miaka 7. “Hata
tufanye nini, bado ni mzazi mwenzake. Naona hilo tuliheshimu na tumpe nafasi ya
ubaba. Wote hatujawahi kumuona akiwa baba. Labda katika hili atafanya vizuri.”
“Hata la mume alijitahidi jamani! Tuweni waungwana.” “Asante
mama na baba.” Pendo akashukuru kuona wazazi wanamuunga mkono. “Hapana.
Penye ukweli tunasema, si ndio Nancy mama?” Mama yake akataka Nancy atulie. “Au
nasema uongo Kenton mwanangu?” Kenton na yeye kwa mama yake, huwa wakati wote
mama yake hakosei na baba yake alimjua. Hampi mashitaka ya mama yake, labda
Nancy. Lakini wakati wote Kenton alimtetea mama yake na akiona kama kweli
amekosa, basi atamtafutia sababu ya kumtetea. “Ni kweli mama. Nafikiri
hatukutegemea kukutana naye hapa. Imekuwa gafla.” Wakatulia, Pendo akaingia
ndani.
Akamtafuta
kila mahali, mwishoe akaamua kumuuliza Sifa. “Kaka yupo nje.” Pendo akajivuta
mpaka nje, akamkuta amekaa kwenye ngazi za nje ya jiko, akila. “Unatafuta nini
huku Pendo!? Hizi ngazi ndefu sana!” “Mbona umekaa huku peke yako?” “Nimeona
niwape nafasi. Lakini nipo sawa kabisa.” Willy akasimama. “Umemaliza kula?”
“Bado, nilikuwa nakutafuta.” “Mimi nipo sawa, nimeona nikae huku. Twende
ukamalize kula.” “Unataka tukae wote hapa?” “Nenda tu ukakae na wageni mpaka
watakapoondoka. Mimi sitaondoka mapema. Nitakaa kama jana.” Pendo akabaki
akimtizama. “Kweli mimi nipo sawa kabisa. Nenda ukale.” Mara wakamuona Kenton
anakuja akiwa ameshika sahani yake. Alizunguka nyumba.
Wote
wakamgeukia. “Naona huku nako umepatengeneza vizuri!” Pendo akacheka. “Kazi niliyokuwa
nikifanya usiku nilipokuwa sina usingizi.” “Pamependeza.” Kaka yake aliongea
huku akiangalia maua. Pendo na Willy wakabaki wamesimama kama waliofumaniwa.
“Nashukuru kunijumuisha kwenye matayarisho ya chumba cha watoto.” Willy
akaongea akibabaika. Pendo akamuhurumia Willy. Kama aliyekuwa akijikomba! Gafla
nyumbani kwake mwenyewe. Nyumba aliyojenga kuanzia msingi, akageuka mgeni!
Kenton ni mwanasheria mzuri sana hapo mjini. Alijijenga hapo jijini, na mkewe
alikuwa mfanyabiashara mzuri tu tena wa muda mrefu. Kwahiyo uwezo wa kifedha
ulikuwa upo. Kenton akamgeukia. “Wakati mwingine maji yanapozidi unga, simama
kama mwanaume, uache kukimbia hovyo.” “Nimejifunza kutokana na makosa.” Kenton
akaondoka, ni kama aliyekuja kutangaza msamaha, Pendo akavuta pumzi kwa nguvu
kama aliyepata aughueni.
“Yatapita
Willy.” “Naamini hivyo Pendo. Nimeharibu sana, mpaka najisikia vibaya!” “Lakini
uzuri umerudi Willy. Umerudi na unajua nini unataka. Hilo ni jambo jema.” Pendo
akamfariji. Willy akabaki akifikiria, mwishoe akaona heri atoke kule nje, ili
kumrudisha Pendo ndani. “Acha nikamalizie kusafisha pale chumbani kwa watoto.
Wewe rudi kula.” Akamsaidia kupanda ngazi moja aliyoshuka, wakaingia ndani.
Ilipofika
kwenye mida ya saa 10 jioni wakaanza kuaga, mpaka inafika saa 12 jioni Pendo
akajikuta amebakiwa na Willy. “Unataka kwenda kupumzika?” “Kama ni sawa, naomba
nibaki kidogo. Tukae wote.” Pendo akacheka akimuhurumia. “Njoo basi angalau
ujilaze hapo kwenye kochi.” Willy akaingia na kukaa pembeni yake. “Unakionaje
chumba?” “Naona kipo kwenye hali nzuri. Kuna vitu gani vingine unatamani viwepo
humo?” “Niliandika, nikampa kaka. Naona wamegawana. Hivyo vitanda vya watoto na
makabati yao ni baba na mama ndio wamegaramia. Na vingine waligawana familia ya
Nancy, kaka K na kina Sabrina wamechukua vitu baadhi vya kununua. Kwa hiyo vitu
nilivyokuwa navyo kichwani vimeisha.” Willy akanyamaza akiumia. Alisubiria hao
watoto, kuyumba kwa miezi 6 tu, kumempokonya haki zote. Amekuwa mgeni kwenye
nyumba yake mwenyewe! Amepoteza mamlaka hata kwa watoto wake mwenyewe!
Akabaki
ameinama akisugua mikono. “Nisikilize Willy.” Willy akamwangalia. “Uliondoka,
hakuna aliyejua kama utarudi, na watoto wanaendelea kukua. Kila nilipokuwa
nikiwaambia wasubiri pengine wanaweza hata wasifike miezi mitano, bado wakawa
wanaendelea kukua na kubaki huko tumboni. Sasa kila tulipokuwa tukienda kliniki
na baba na mama, tukawa tunaambiwa wanakua vizuri tu niongeze kula hiki na kile,
ndio maana baba akapata amani, akaniambia niandike kila kitu ninachotaka kukiona
kwa hawa watoto. Ndipo nikatengeneza hiyo orodha yote. Wakaisoma na kuniachia
mimi jukumu la kujilisha tu. Lakini mimi mwenyewe nikataka chumba kiwe na hiyo
rangi uliyoona na kuchorwe kama hivyo, ndio nikajiongezea garama nyingine. Ila
mambo mengine yote ya watoto wakagawana.” Pendo akaendelea.
“Ndio
umerudi. Hakuna anayejua utakaa kwa muda gani, au hakuna anayejua dhamira yako
ya kweli ya kurudi. Kwa sababu uliondoka kwa sababu ambayo bado hakuna mwenye
uhakika kuwa hilo tatizo limetibika. Kwako nilikosa kigezo cha kuwa mke kwa
sababu yakutozaa, ndio maana uliondoka kwangu, ukaniacha.” “Naomba
usiseme hivyo.” “Ni hivyo tu Willy, na hata wewe umekiri hivyo. Najua
usingeniacha kama ningekuwa nimekuzalia watoto. Lakini kwao nilibaki na nitabaki
kuwa jukumu lao. Aidha nitazaa hawa watoto au la. Lakini hakuna mwenye uhakika
na wewe. Kila mtu anawasiwasi wakutobaki kwako endapo hawa watoto hawatazaliwa.
Kwa hiyo hakuna ambaye atakuwa tayari kukuachia chochote sasa hivi. Naomba
uelewe Willy.” Willy akarudisha kichwa chini.
“Pole.”
“Najisikia sina maana Pendo. Pesa yangu yote inakosa maana kama itashindwa
kutumika kwa wanangu.” “Ni kwa sasa tu. Ni kwa muda Willy. Tutakuwa na hawa
watoto kwa muda mrefu sana. Watunzie hiyo pesa, tutahitaji sana tu. Wakizaliwa
tutakuwa na uhitaji mkubwa. Sabrina alikuwa ananiambia vile mapacha walivyo garama.
Vile wanavyotumia pesa nyingi kwa ajili ya wale watoto. Inamaana ndio kitakachotupata
na utashuhudia kama utakuwepo.” “Nitakuwepo Pendo.” “Basi tulia. Fanya kile
utakachoweza, na kama hakuna, basi. Acha watusaidie.” Kimya. “Kwanza uwepo wako
tu hapa unamaana sana. Si kwangu tu, na watoto pia. Ipo faraja ya namna yake na
utulivu. Nakushukuru.” Willy akamfunua miguu na kuanza kuiminya minya. Pendo
akacheka. “Sijafanyiwa masaji muda mrefu! Nahisi nitalala.” “Wewe lala tu,
nitakuwepo hapa mpaka baadaye sana.” Pendo akaanza kusinzia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka
Pendo alikuwa akimuonea huruma Willy. Akitoka tu kazini, anakwenda kukaa naye
mpaka usiku kabisa. Akilala yeye ndio na yeye anaondoka. Akajitahidi hivyo
hivyo. Na jumamosi tena akarudi asubuhi. Akakaa naye mpaka usiku wa saa sita.
Jumapili tena akarudi asubuhi hata Pendo hajaamka. Pendo anaamka, baada ya
kuoga wakati Sifa anampa kifungua kinywa, ndipo akamwambia Willy yupo sebuleni.
Pendo akashangaa. “Naomba mwambie aje huku. Umempa kifungua kinywa?”
“Aliniambia nisisumbuke, yupo sawa.” “Wewe unamjua Willy. Atakuwa na njaa. Naomba
mtayarishie kifungua kinywa. Lakini mwambie aingie huku.” Sifa akatoka, Willy
akaingia.
“Mmeamka
salama?” “Wote naona tupo salama. Walikuwa wakinisalimia huko bafuni wakati
naoga. Njoo ukae hapa.” Willy akakaa. “Mzima?” “Mzima. Nimekuja tukae wote.”
Pendo akamuhurumia maana aitoka hapo usiku wa karibia saa 8. Na mapema hiyo
ameshafika hapo! “Asante Willy. Nashukuru.” Pendo akaendelea kunywa uji, Willy
ametulia tu pembeni. Sifa akamletea na yeye kifungua kinywa. Akashukuru na
kula. Wakamaliza kula, Pendo akamkaribisha ajiegemeze kwenye mto, wakawa
wamejilaza huku wakiangalia mahubiri mpaka wakapitiwa na usingizi.
Baba
na mama yake Pendo wanapita kwenda kumsalimia Pendo wakati wanakwenda kanisani,
wakawakuta wamelala usingizi mzito, hakuna mwenye habari hata kama kuna mtu ameingia
hapo ndani. Willy alikuwa amemshikilia Pendo mkono kwa kupishanisha vidole,
akavuta karibu na uso wake, wakawa wamelala. Wazazi hao wakawaangalia, nakuona
waondoke bila kuwaamsha.
Walikuja
kuamshwa na Sifa akimtaka Pendo anywe supu. “Bibi ameipitisha, alisema saa nne
na nusu kama hujaamka nikuamshe unywe pamoja na dawa na juisi yakuongeza damu.
Ameweka kwenye friji. Amesema ukimaliza ndipo urudi kulala.” “Mama alikuja!?”
“Na babu.” Sifa akaongeza wakati anamuwekea supu.” “Asante. Hata sikuwasikia!”
Willy akakaa na kumsaidia kuweka mito vizuri. “Eti mama na baba walikuwa hapa!”
“Na mimi sikuwasikia.” Willy akajibu na kutulia. Pendo akamuona kama anawasiwasi
wakuuliza kitu. Akamuacha kabisa. Hakutaka yeye ndio awe mstari wa mbele kuongea
chochote juu yao.
Mchana
wazazi wake wakapita tena kutokea kanisani. Willy akawa muungwana, akaona
awapishe. “Nitawaona tena baadaye.” Akaaga mara wazazi walipoingia. “Mbona unaondoka
bila kula? Nina uhakika Sifa anapika au ameshaivisha. Ungekula kabla
hujaondoka.” “Sitakuwa mbali. Nitarudi.” Pendo akaelewa. Akamuacha vile
anavyojisikia. Atoka hapo chumbani. Akamsikia akiwasalimia wazazi sebuleni. Wazazi
wakaingia hapo kukaa naye kwa muda wakimpa habari za kanisani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni,
akarudi tena na mfuko wa matunda, samaki, nyama ya ngombe na kuku watatu wakiwa
wamesha safishwa wamehifadhiwa kwa usafi, mafuta, nyanya, sukari, vitunguu,
karoti, hoho, ndizi, viazi, mchele kwenye gunia, na vingine vingi vyakula mle
ndani na alivyoona akitayarishiwa Pendo. Akashusha kila kitu jikoni, kwa kuwa
hakukuta gari ya baba yake Pendo, akapitiliza chumbani moja kwa moja. Pendo
alijua amefika, na wakati akiingiza vitu ndani Sifa alishamwambia. “Asante kwa
vyakula.” “Karibu, lakini usijali. Huu mfuko ni wako.” Pendo akacheka na
kupokea. Alimnunulia nguo nzuri sana za wajawazito, zakulalia. “Asante kujali
Willy.” “Karibu. Nimeona unatumia muda mwingi kitandani, angalau uvae vitu
vizuri na wewe ujifariji.” Pendo akacheka. “Nashukuru.” Bado akamuona ana kitu
anataka kuzungumza lakini anasita. Alianza, nakubadilisha mbele ya safari.
Pendo akamuacha kabisa.
Ilikuwa
jumapili, lakini Pendo akashangaa anakaa mpaka saa sita usiku wakati kesho yake
ilikuwa siku ya kazi. Akazunguka hapo ndani, kisha akaaga. “Njoo Willy. Kaa
hapa.” Willy akarudi kukaa. “Wakati wote tumekuwa tukizungumza, na hatujawahi
kushindwana. Hata kipindi tunaachana, unakumbuka tulizungumza hapahapa chumbani
tukaweza kuelewana?” Willy akanyamaza. “Hiki chumba hakijawahi kushindwa kutupa
nafasi na utulivu wa kuzungumza mazito na magumu na kupata majibu. Niambie tu.”
Akaona wasiwasi unaongezeka anasugua mikono.
“Willy?”
Pendo akamuita taratibu. “Naomba kurudi nyumbani.” Willy akaenda moja kwa moja
kwenye pointi. Pendo hakutegemea, kidogo akapatwa kigugumizi. “Sio lazima ukanipa
jibu leo. Lakini nilikuwa nikifikiria kutoka kwenye ile apartment ninayolipa
pesa nyingi, halafu hiyo hela nikawawekea watoto, wakati naendelea na ujenzi
kule kigamboni. Naweza kutumia hata kile chumba nilichokuwa nikihifadhia vitu
vyangu, nimekiona bado nikitupu.” “Kumbe ulishaanza kujenga?!” “Pale ofisini
wanatoa mikopo ya nyumba. Uzuri wanakata pesa ndogo sana huwezi hata kuisikia
kwenye mshahara. Baada tu ya miezi mitatu, wakanipa. Nimetafuta contractor,
ndio anapamalizia kuanzia pale tulipoishia mimi na wewe. Kwa mwezi mmoja
nimeona amefanya kazi kubwa! Unataka nikuonyeshe picha?” Pendo akacheka na
mshangao usoni.
“Ningependa
kuona.” Akatoa simu mfukoni. Akaanza kufungua. Kilikuwa kiwanja kikubwa.
Walianza kujenga na walikuwa wakijenga taratibu wakiambiana ndio nyumba ya
ndoto yao. Walianza kuijenga ikiwa na ramani nzuri sana, na kubwa mpaka
marafiki walikuwa wakiwacheka kwamba watakufa kabla hawajamaliza. Na walichimba
mpaka sehemu ya bwawa la kuogelea. Walichofanya wakati wapo na Pendo, ni
kuzungushia ukuta kwanza katika eneo la nyumba, kisha uzio wa kawaida tu wa
fensi na michongoma kuzunguka eneo jingine linalopakana na hapo. Walinunua
viwanja viwili, na ndio maana Willy hakuamini wakati Pendo anakubali kumpa eneo
lile lote na yeye kubakiwa na hiyo nyumba tu!
Pendo
alishangaa sana alipoona hiyo nyumba. “Willy!” “Ndio tofauti ya kuweka
contractor na mjenzi wa kawaida.” “Na kuwa na pesa! Kwani wewe Willy wanakulipa
kiasi gani huko kazini kwako!?” Willy akacheka sana vile Pendo alivyoshangaa.
“Kumbe ulikuwa unamaanisha uliposema kuna marupurupu! Sasa hii nyumba si
imeisha!” “Bado bwana! Yupo kwenye vigae, madirisha na milango. Week ijayo nampelekea
madirisha. Nilisubiri kwanza mtu wa geti amalizie geti zuri kwa usalama ili
wasije ng’oa vitu. Nikimaliza tu geti, amesema atapachika madirisha. Sasa hivi
ndio wanajengea hizo nondo. Na anaonekana ukimpa pesa, analeta vijana wake,
kazi inafanyika kwa haraka sana ndio maana unaona kwa mwezi tu na siku chache,
amesimamisha hilo jengo, na pia ukumbuke tulikuwa tumefika nusu. Kwa hiyo yeye
ameanzia hapo nusu nakupandisha juu.” “Hongera sana Willy. Umejitahidi mno.”
Willy akacheka.
“Matusi
mengine Mungu anayaruhusu kwenye maisha ili kukuchangamsha.” Pendo akacheka
sana. “Zelda huyo?” “Na mumewe mzee Ngoi.” Pendo akazidi kucheka. “Wamekuweka
sawa.” “Si kidogo. Usingizi ulipotea kabisa kama siku tatu mfululizo, silali
mchana wala usiku. Kutoka kwenye kusifiwa na jamii, mpaka kuitishwa kikao cha
kutukanwa! Acha Pendo.” Pendo akazidi kucheka.
“Nimeomba
kurudi nyumbani.” “Sawa sawa, lakini mimi ninawazo la tofauti Willy, naomba
subiri kwanza watoto wazaliwe.” “Pendo!” “Subiri kwanza Willy. Nina maana yangu.
Angalau safari hii iongezeke sababu zaidi ya sisi kuwa pamoja.” “Sijaomba
kukuoa, ila kurudi nyumbani, Pendo!” Hapo Pendo akapoa kabisa. Willy akamuona
akaona aendelee kujieleza ili kumuweka sawa, asiharibu. “Sidhani kama ni sawa
majukumu mengine niendelee kufanyiwa kama zamani nilipoondoka! Sasa hivi nipo,
naweza kufanya mambo mengi kuliko kusumbua wazazi.” “Sidhani kama ni usumbufu
kwao.” Pendo akajibu na kushindwa kabisa kumtizama tena usoni. Ujasiri ukamuisha,
akabaki macho kwenye simu. “Sawa, basi niombe na mimi kushiriki.” “Sawa.” Pendo
akakubali kinyonge. Willy akamtizama kidogo.
“Kwa
hiyo hata kesho naruhusiwa kurudi?” “Muda na wakati wowote ule.” Pendo akajibu
bila kumtizama. “Nashukuru. Asante sana. Acha niwahi nikapate muda wa kukusanya
vitu vyangu.” “Sawa. Naomba wakati unatoka, nipelekee na hiyo trei jikoni.
Asante.” Akaingia chooni na kufunga mlango. Willy akakaa hapo akisubiri akaona
hatoki. Akaenda kumgongea. “Pendo?” “Nipo tu sawa.” “Oooh! Sawa. Basi natoka.”
“Sawa. Usiku mwema.” “Na wewe.” Willy akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usiku
huwa ukawa mbaya sana kwa Pendo. Akajaribu kulala, lakini akashindwa. Kumbukumbu
ya maneno ya Willy akimwambia sio kwamba anaomba kumuoa, akili yake ikayakuza
na kuipa maana iliyomfanya akeshe. Akazidi kuumia kama ndio anachika upya. Yale
maneno yakazidi kumwingia vibaya na kusikika kwa uchungu kuliko hata
alivyomaanisha Willy mwenyewe. Pendo akaanza kulia. Alilia mno usiku huo.
Moyoni bado anampenda Willy. Ni zaidi ya miaka 10 wawili hawa wamekuwa pamoja,
Pendo hakuwahi hata kushawishika na mwanaume mwingine. Ni Willy tu. Kurudi kwa
Willy na juhudi zote kuliibua tumaini jingine, lakini Willy anamtamkia sio
kwamba anaomba ndoa! Pendo akazidi kulia. “Inamaana
anarudi kwa sababu ya watoto sio mimi!” Pendo mpendwa kupendwa
akazidi kulia kila akimfikiria Willy aiyerudi na mafanikio makubwa kuliko hata
alivyoondoka! Mwili umerudi kama kijana mdogo. Pendo akajitazama jinsi
alivyonenepa na hilo tumbo, akajua ndio maana hata Willy amekuwa muwazi kwake.
Pendo
akalia mpaka saa 9 usiku bila kupatwa na usingizi. Akaanza kujisikia vibaya.
Mapigo ya moyo yanakwenda mbio. Akajua pressure aliyoambiwa na daktari apumzike
na kuhakikisha haipandi, imepanda, kwa hiyo atadhuru watoto wake. Akanyamaza
kwa haraka. Akasafisha uso na kitambaa kilichokuwa pembeni ya kitanda baada ya
kukimwagia maji ya baridi. Akajaribu kufunga macho kabisa, lakini akazidi
kujisikia vibaya.
Akampigia
simu mama yake akilia. “Nitapoteza wanangu mama.
Sijisikii vizuri.” Baada ya dakika 10 wazazi wake wakawa wameshafika.
Baba yake akampima pressure, akakuta ipo juu. “Naomba usilie Pendo, mama yangu.
Tulia kabisa ili na pressure itulie.” “Dokta
aliniambia lazima hii pressure ikae chini, baba. Lasivyo ikipanda nitapoteza
watoto wangu. Nimeingiwa hofu siwezi kunyamaza tena. Naogopa baba.” Wakamkimbiza
hospitalini.
0 Comments:
Post a Comment