“Njoo sasa hivi wakati wanacheza.” Mama yake
akampisha pale akijua moyo wa Pendo. “Hapo atakuwa kashasahau kama alichwa! Pendo
jamani!” Mama yake akawaza. Willy akaenda kukaa pembeni ya kitanda. “Huyu
mmoja ametuna hapa.” Pendo akamshikisha mkono. “Halafu mwenzake huyu hapa.”
Willy akawashika. Akashituka walivyoanza kuzunguka, Pendo na mama yake
wakacheka. “Ndio wanazunguka hivi! Huumii?”
Willy akauliza, wakashangaa kuona anatokwa machozi. Mama yake Pendo akashangaa.
Willy akaendelea kuwashika huku akilia, mama yake Pendo akaona aondoke tu,
kuwapa nafasi.
Pendo
akamuhurumia Willy. Akajua kinachoendelea moyoni mwake, lakini akaona amuache
tu. Amepitwa kila mahali. “Nakumbuka Jack alikuwa
akisema huwa wakiwa tumboni ukiwaongelesha wana uwezo wa kutambua sauti.”
Pendo akacheka na kufuta machozi na yeye. “Wanasema
hivyo Willy. Sijui! Kila kitu nikufanya kwa imani tu.” “Nasikitika kupitwa!
Najuta sana Pendo. Nilikula ng’ombe mzima, nikakimbia nikiwa nimebakisha mkia
tu! Nimeacha watoto wangu, nikakimbilia nilipofedheheka vibaya sana!”
Pendo na yeye akazidi kulia hapo nakushindwa kujibu. Willy aliwashika hao
watoto taratibu huku akiwabusu na machozi yaliyokuwa yakimlowesha Pendo kwa
muda mrefu mpaka Sifa alipoingia na sinia ya chakula. Ikabidi Willy asimame
aelekee chooni. Pendo akajifuta machozi. “Chakula dada.” “Asante Sifa. Ninakushukuru.” Pendo akakaa. Sifa
akampangia mito. “Bibi alipita.” “Nilimuona wakati anatoka. Nilikuwa uwani
wakati anaingia.” “Sawa. Kuna chakula umpe Willy?” “Mimi nimekula
nilichojipikia mchana. Kama hatawahi kuondoka, naweza kumpikia haraka.”
“Hapana. Msihangaike kwa ajili yangu. Mimi nipo tu sawa. Asanteni.” “Unauhakika
Willy? Usije lala na njaa.” “Nitakuwa sawa. Usijali.” Akakaa.
“Ndio
unakula nini hapo?” Pendo akacheka akikoroga. “Mchemcho wenye samaki, na mboga mboga.
Mama huwa ananiletea matembele. Natakiwa damu nyingi. Kwa hiyo nakula kila
kijani unachojua kinaongeza damu. Nimepunguza wanga sana ili nipate nafasi ya
aina hii ya chakula. Nahangaika kwa kila namna, ilimradi wakue tu.” “Pole Pendo.
Naona kama unajinyima sana!” “Nipe hongera Willy. Unakumbuka tulivyokuwa
tukihangaika? Hii ni garama ndogo sana ya kulipa.” Willy akanyamaza kwa muda.
“Hivyo
virutubisho ambavyo mama anakununulia, ananunua wapi na ni lini vinahitajika
tena?” “Kuna dada anatuuzia. Ni vya GNLD mahususi kwa mama wajawazito.”
“Niandikie na unitumie na namba yake huyo dada ili nikanunue vingine ili
usiishiwe.” “Nashukuru Willy. Asante.” Willy akamtizama na kuinama. “Sasa movie
zenyewe ziko wapi?” “Nimeacha kwenye gari. Acha nikalete.” Willy akatoka, Pendo
akaendelea kula. Akarudi na hizo dvd na maua mazuri. Pendo akacheka. “Nashukuru
Willy.” “Karibu.” Akamkabidhi hayo maua, akayanusa. “Yananukia vizuri sana.
Asante.” “Karibu.” Kisha akayaweka pembeni. Akamaliza kula. Akanywa dawa za virutubisho,
Willy akimtizama tu. Akaenda kusafisha meno.
Aliporudi
kutoka bafuni akaangalia saa. “Mmmmh! Usiku umeendelea Willy, nenda kapumzike,
kesho kazini. Tutaangalia movie kesho.” “Wewe unalala sasa hivi?” “Maisha yangu
ni hapo kitandani. Sijui nalalaga saa ngapi na kuamka saa ngapi! Ndio maana
nakuwa na nguo ya kulalia wakati wote.” “Ni sawa nikikaa tena kidogo ndio
niondoke?” “Hamna shida kabisa.” Pendo akarudi pale kitandani, akapanga mito
vizuri ndipo akapanda hapo kitandani na kujilaza.
“Naomba
kushika tena watoto, labda watanifahamu na mimi.” Pendo akacheka. “Ukitaka
waamke, leta glasi ya maji ya baridi, tuwashikishe halafu wataamka.” “Kweli?!”
“Nenda tujaribu.” Willy akatoka kwa haraka. Akarudi na maji baridi haswa. Wakaanza
kumshikisha tumboni, Pendo anacheka na kuruka kwa baridi. Wakawasumbua huku
wakiwaongelesha, kweli wakaanza. “Hao, wameanza. Ona!” Willy alikuwa akishangaa,
anacheka na kufuta machozi. “Nimefurahi sana
kuwaona, sijui niseme kuwashika!” Willy akaongea taratibu huku akipapasa
tumbo la Pendo. “Nimefurahi sana. Nawapenda kuliko
kitu chochote hapa duniani, nawaahidi nitakuwa baba mzuri sana kwenu.”
Machozi yakaanza kumtoka na Pendo. “Kuanzia leo, na
mimi nitakuwepo.” Willy akaendelea kuwapapasa. Pendo alisikia faraja ya
namna yake. “Mnahitaji kukaa huko kwa mama yenu mpaka
muwe wakubwa kabisa. Tutawaombea, na mtakuwa salama.” Akabusu tumbo la
Pendo na kujifuta machozi.
“Umeridhika
sasa?” “Hapana Pendo! Sidhani kama nitakuja kuridhika. Nikitu nilikuwa natamani
mno! Nilipojua Zelda hana mtoto wangu, nikajiambia basi tena. Nilijua wazi siwezi kupata mtu kama
wewe. Zelda nilikaa naye kidogo tu, lakini alikuwa akinivunjia heshima mno.
Kwangu ilikuwa mshituko. Sikuzoea matusi makubwa. Yaani kutukanana waziwazi!
Kuitana mjinga, sijui fala!” “Willy! Alikuwa anakutukana hivyo!?”
“Mbona hayo ni madogo Pendo! Acha tu. Basi ile hai ikaniogopesha sana.
Nikajiambia maadamu Mungu amenitoa pale salama, nikajiambia sitahangaika tena.
Nimejifunza, nikajiambia inatosha. Sikutegemea kama kuna muujiza wangu huku.”
Pendo akacheka taratibu, mikono ya Willy bado ilikuwa ikizunguka, taratibu tumboni
kwake, watoto wakatulia.
“Naona
wamerudi kulala.” “Wameridhika.” Wakacheka kidogo wote wakiangalia tumbo.
“Nikuache na wewe upumzike Pendo. Nitakuona kesho. Si umeniambia milango ipo
wazi, naruhusiwa kuja muda na wakati wowote?” “Karibu.” “Asante. Usisahau
kunitumia namba ya huyo dada anayewauzia shake na dawa.” “Nilishasahau.
Nitafanya hivyo. Kwani ulibadili namba?” “Hapana. Ni ileile.” Akambusu shavuni,
akasimama. “Nikusaidie nini kabla yakuondoka?” Willy akauliza huku akiangaza.
“Nisogezee rimoti zote na nisaidie kupanga tena mito. Zaidi huku chini miguuni.
Nilale kiuno kikiwa kimenyanyuka kidogo.” “Ndio mpaka asubuhi!?” “Nimeshazoea.
Nalala hivyohivyo.” “Pole Pendo, najua sio ulalaji mzuri, lakini utakuja
kupumzika.” “Pendo akacheka.” Akamuwekea mito vizuri. Akamfunika, akambusu
tumboni na shavuni tena. “Nimeshakusogezea kila kitu. Acha mimi niondoke. Mlale
salama.” “Asante, na wewe.” Willy akaondoka. Pendo alijawa na furaha, akatamani
amwambie Sabrina, lakini ilishakuwa usiku sana. Akaamua amuache, akalala hapohapo
kwa furaha ya kushikwa na Willy.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
S |
iku
inayofuata ya ijumaa mchana siku ya kazi, wakati akizungumza na Sabrina, akashangaa
Sifa anamgongea kuwa Willy yupo sebuleni anataka kumuona. Akamuaga Sabrina, na
kumwambia amkaribishe chumbani. Akajiweka sawa. “Vipi Willy!?” “Simu yako haipo
hewani Pendo. Ulini block?” Willy akauliza kwa kulalamika. “Hapana.
Nilibadilisha namba zote na kubakiwa na moja tu, tena mpya. Nilikusudia kupunguza
stress kutoka kwa watu wa karibu. Pole za kuachika zilikuwa nyingi,
sihemi. Halafu wengine walikuwa wakinipigia eti kujua ninaendeleaje baada ya
wewe kuondoka hapa! Nilichoka. Na nilijua wazi wengine hawamaanishi Willy.
Nikabadili kabisa namba, na kupunguza watu wakuwasiliana nao.” Willy akapoa
kidogo, Pendo alimuona vile alivyoingia na uso wa kulalamika.
“Kwani
ulinipigia sana?” “Uliniahidi kunitumia namba ya yule dada na vitu vya kununua.
Na mimi nataka kusaidia pale nitakapoweza, Pendo. Nahitaji kushiriki! Najua
unaweza ukaniona ni mbambaishaji, sio mtu wa kuaminika, mkimbiaji na...” Akasita,
Pendo akimshangaa yote hayo yanatokea wapi! “Lakini nataka kusaidia. Hata kama
unaniona ni mshindwaji, nipe nafasi hata ndogo ndogo tu ili kurudisha
uaminifu. Na kama hutaki niwe na namba yako, basi naomba uniandikie hata kwenye
karatasi tu.” “Willy! Naomba utulie. Nilisahau mpenzi wangu. Hakika nilisahau.
Sina sababu nyingine yeyote ila ni kusahau.” “Nilifikiri ni vitu vya muhimu!”
“Ni muhimu sana tu. Ila nafikiri sijui ni kwa kuwa mama ametoka kununua jana,
na nishamlipa, nafikiri akili ikatulia, nikaona si muhimu tena. Nilisahau tu.
Kaa kidogo.” Willy akajishauri kidogo akaenda kukaa pembeni yake hapo kitandani,
akajiinamia. Kimya.
“Pole.” Willy akamwangalia, akajisuta na
kunyamaza. “Vipi kazini lakini?” “Safi tu. Bado sijatoka. Nimekuja mara moja
tu, natakiwa nirudi. Nilitaka kukujulia hali yako na watoto. Tokea asubuhi
naangalia simu labda utanikumbuka, naona kumbukumbu zako kwangu na zenyewe
zimekuwa si za muhimu tena, Pendo! Nimekuwa nikisubiria simu yako tokea asubuhi,
naangalia simu yangu kama mwehu nikidhani utanikumbuka lakini hamna kitu!”
“Pole na samahani Willy. Tuliamka salama na watoto hawajambo kabisa. Walicheza asubuhi.
Unataka kuwasalimia?” Willy akamwangalia na kujisogeza.
Pendo
akamvuta mkono wake taratibu na kuuweka juu ya tumbo lake. “Nafikiri sasahivi
watakuwa wamelala! Sijui hata nani ni nani na nini ni nini. Ni mchanganyiko
tu.” Willy akacheka. “Sasa wewe waongeleshe hapo, waambie umeacha kazi, umekuja
kuwaona, waamke wakusalimie, waache uvivu.” Willy akacheka kidogo. Akawashika,
kisha kama aliyekumbuka kitu. Akaacha.
“Unanipuuza Pendo!” “Hapana Willy. Kwenye
mawazo yangu halikuwepo wazo la nini unifanyie, ila kukusubiri kukuona tu.
Nilijua lazima utakuja ukitoka kazini. Naomba usikasirike tafadhali.” Kimya. “Niangalie
Willy, sikupuuzi.” “Nahisi nilikuwa nikisubiria sana ujumbe wako ili nipate namba
yako niwapigie simu kuwajulia hali.” “Naomba nipe simu yako.” Willy akatoa
mfukoni akamkabidhi. Akaandika namba na kumwangalia. “Niweke jina gani?” “Naiomba,
nitamalizia mwenyewe.” Pendo akampa huku akicheka. “Umeridhika sasa?” “Ndiyo.
Sasa unataka watoto waje halafu wakute hata hatuzungumzi!” Pendo akacheka huku
akimwangalia akiandika jina, akamaliza na kurudisha simu mfukoni. Akazungumza
hapo na watoto, akambusu Pendo tumboni mara kadhaa, akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni
akarudi tena. Safari hii akaja na chakula chake na Sifa. Alimwambia Pendo
amwambie ampikie yeye tu, atakuja na chakula chao. Walikaa na Pendo hapo chumbani,
usiku huo wakizungumza na kuangalia movie. Watoto wakicheza, anamuita Willy.
Anawashika. “Naomba na mimi nije kesho kwenye kufunga vitanda vya watoto
chumbani kwao na kuweka michezo yao.” Pendo akatulia, hakujibu. Willy akakunja
uso. “Pendo!?” “Sidhani kama ni wazo zuri Willy. Ni kitu baba alikuwa
akikisubiria kwa hamu sana akawa anahimiza mafundi wamalize haraka ili yeye aje
aanze. Na kaka naye amemwambia atakuja kumsaidia. Shem naye aliposikia, akasema
na yeye atakuja. Mwishoe wakakubaliana familia ya kaka, familia ya Nancy, baba
na mama waje hapa kesho, wafanye nyama choma, wakati wanatayarisha chumba cha
watoto.” Willy akanyamaza kwa muda.
“Kwa
hiyo unafikiri kesho sio siku nzuri ya mimi kuja?” Akauliza tena Willy.
“Jumapili nitakuwa hapahapa. Sitakwenda kanisani.” “Kwa maana nyingine
unaniambia nisije kesho?” “Walikubaliana kuanzia saa 4 asubuhi watakuwa hapa!
Unajua mume wa Nacy akikutana na baba pamoja na kaka. Watakunywa hapa mpaka
usiku. Hawakusema wataondoka saa ngapi. Ndio maana nafikiri labda uje tu jumapili
ukitoka kanisani.” Willy akafikiria tena kidogo na kuona aulize tena. “Kwa
maana nyingine hutaki nikutane na familia yako tena?” Lile swali likawa gumu
kwa Pendo, akafikiria jinsi yakumjibu, akashindwa. Willy akabaki akimtizama.
“Pendo?”
“Hata sijui tena Willy. Sielewi!” “Wewe ndio unayo majibu Pendo. Labda niseme
hivi.” Akamuona anazima tv, akaenda kupiga magoti pembeni ya kitanda, Pendo
akashangaa ni nini anataka kufanya. “Naomba unisamehe Pendo. Kwanza
nilikusaliti, na nikakukimbia.” Pendo akabaki amepigwa na butwaa. “Nimeomba
msamaha Pendo. Naomba unisamehe.” Pendo akabaki kimya. “Najua nimekuumiza,
pengine huniamini tena. Pengine unahitaji muda, lakini naomba unifikirie Pendo.
Nimekosa katika hili, lakini unajua nikiasi gani napenda watoto na jinsi
nilivyokuwa nikiwahangaikia hawa watoto. Kumbuka nilivyosimama na wewe, Pendo.
Njia zote ulizotaka na kushauriwa na daktari nilikubali bila shida. Hata zile
njia ambazo wanaume wenzangu walikuwa wakisema nakwenda kujidhalilisha
hospitalini, akiwepo msimamizi wetu wa harusi, nilifanya Pendo, na wewe ni
shahidi. Au umesahau?” Pendo akajifuta machozi, akakumbuka shida aliyoipata na
Willy wakati wakutafuta watoto.
“Au
maovu yangu yamefuta kila kitu?” “Siwezi kusahau
Willy.” Pendo akajibu. “Basi naomba nafasi ya kuwa baba. Sitakubugudhi
ila kukusaidia. Ilimradi na mimi niwepo tu. Niwepo sasa hivi, hata kukusogezea
mito na maji ya kunywa, na wakizaliwa. Najisikia vibaya wanangu waje kupata
kumbukumbu za picha, waje kuona kila mtu yupo kwenye matayarisho ya chumba
chao, halafu baba hakuwepo! Itawasumbua wanangu Pendo. Watafikiri niliwakimbia,
wakati niliondoka nikiwa hata sijui kama wapo. Kwanza uliwezaje kunificha?”
“Tafadhali usiende huko Willy. Huko ni papana mno, utapachukia.” Pendo
akajiweka sawa.
“Hapana
Pendo. Nimepiga mahesabu, inamaana hata siku tunaandikishana talaka, ulijua ni
mjamzito! Tulikaa meza moja, kiti chapembeni yako. Uliwezaje kuficha kitu
kikubwa kama hicho ulichojua nilikuwa nakisubiria kwa hamu?!” Pendo akashangaa
sana. “Willy! Ulitaka nikwambie nini au ili iweje? Wewe ulikuwa na furaha ya
kwenda kuanza maisha mapya ya mke na mtoto. Kweli nikwambie habari ya ujauzito
ambao hata sikujua kama utafika hapa! Kumbuka mimi nakupenda Willy na
ninakutakia mema. Mwenzangu niliona ulifanikiwa, ulitaka nikushike tena miguu
ubaki njia panda!” Kimya wakati Pendo akigomba.
“Hata
nyumbani kwenyewe niliwaambia baadaye sana, nilikwambia na wewe! Nafikiri mpaka
nilipofika miezi minne! Ndugu mbali na Nancy, kaka na wazazi, hakuna anayejua
wengine. Wale wasimamizi wa harusi ndio sikuwatafuta tena tokea wakati ule
wanakushauri uachane na njia tulizokuwa tukishauriwa kwa kuwa nikujidhalilisha,
mimi sina uwezo wa kuzaa.” Pendo akaendelea.
“Nilikwambia
naogopa na kukwepa fedheha Willy. Hata hiki wanachokifanya kesho ni kwa kuwa ni
baba yangu mzazi ndiye ametaka kufanya, sioni shida wala aibu nikipoteza. Najua
wakati wote atabaki kuwa bega langu la kulilia. Sina hofu. Lakini nikwambie
ukweli kabisa Willy, hata wewe naogopa usije anza kuwekeza kwa hawa watoto sasa
hivi. Sitaki uingie garama wakiwa bado hawajazaliwa. Natembea kwa imani Willy!
Tena wakati mwingine naona kama imani yangu ipo inayumba mno. Niseme natembea
kwa imani ya Sabrina. Ndiye anayenibeba. Kila nikiamka najishika huku chini
kuona kama sio mbichi! Nashinda na kulala na pedi kama nipo kwenye hedhi sababu
ya hofu. Kila wakati nachungulia pedi kama ipo na damu au la!” Pendo
akaendelea.
“Unafikiri mimi ndio nilifurahia kuachika na kubaki peke yangu?”
Pendo akaanza kulia. “Unafikiri nilikuwa nafurahia
kujua ni mjamzito na nitalea watoto peke yangu?” Kimya. “Nilikuwa naogopa Willy! Mpaka sasa sijui itakuaje. Sijui
naleaje hawa watoto nikiwa peke yangu!” “Mimi nimerudi. Na nipo Pendo.
Naongea na Mungu ananisikia. Hata kama Mungu atawachukua hao watoto, mimi bado
utaniona tu. Na mimi nipo mpweke. Kama nilivyokupoteza wewe, ndivyo
nilivyopoteza marafiki, na ndugu ni kama nilivyokwambia. Hatutafutani tena. Nipo kama hivi unavyoniona, nimebakiwa na ile
ahadi ya mwisho tu uliyonipa. Kwamba sisi tutabaki marafiki, ndio angalau nimebakiwa
nikijifariji kwa hilo.” Willy akakaa.
“Namimi
natembea na fedheha Pendo! Wako wanawake wengi tu wanavimbe lakini wanazaa.
Japo wanaweza kuzaa kabla ya muda, lakini wanazaa. Lakini mimi sijawahi kumpa
mwanamke yeyote yule mimba! Jamaa walikuwa wakinicheka, wakidhani ni utani
lakini uliniumiza sana, walikuwa wanasema mpaka mzee Ngoi amenishinda kupiga
bao!” “Willy!” “Mungu nishahidi Pendo. Kitendo cha kulala na mwanamke mmoja,
kisha baba yeye ndio ampe mimba mimi nishindwe, unafikiri nilijisikiaje? Hata
hofu yakuja kuoa tena iliniingia kuepuka fedheha. Nilijiapia sitaoa wala
sitajaribu tena kwa aibu. Na ndio maana na mimi nilijitenga na marafiki. Na
utani huo walinitania tukiwa wengi tu, wala hatukuwa wachache. Uliendelea huo
utani kwa muda wakicheka kila mmoja akiongeza lake kwa utani, mpaka mimi
nikaondoka. Nimekuwa na miezi mitano sasa, lakini migumu mno Pendo. Mno. Kutoka
kuwa juu, nakurudishwa chini mavumbini nikichekwa mpaka na vijana! Sio kitu
najivunia.” Pendo akanyamaza.
“Nihurumie
Pendo, naomba nirudishe japo kwenye maisha ya watoto wangu. Nipe masharti
yeyote yale, angalau na mimi nijisikie kuwa hapa duniani nimefanikiwa kumpa mtu
mimba.” Pendo akamcheka. “Basi mimi mwenzio nilikuwa najua unatembea huko nje
kama mshindi! Kidume cha Ngoi.” “Hata kidogo, unafikiri kwanini nimeisha hivi!
Wala sipo kwenye diet. Ni mawazo.” Pendo akacheka na kubaki akifikiria.
“Niambie nifanye chochote kile, nitafanya Pendo. Nipe masharti, chochote na
mimi niwepo kwenye maisha ya wanangu.” “Mbona mimi sijakataa!” “Mbona sasa
hutaki nije kesho?” “Wewe upo tayari kujibu maswali ya kesho?” “Ndiyo.” “Naomba
ufikirie Willy kabla hujajibu, tafadhali. Jana mama alikuhoji maswali hapa,
ujue ndio yatakayokuwepo kesho. Sasa utakuwa tayari kuyajibu?” “Kabisa. Acha
nionekane mpumbavu, mjinga..” Pendo akaanza kucheka.
Willy Mbele ya Wakwe Zake Tena.
N |
ancy, mtoto
wa pili au wakatikati kuzaliwa kwenye familia ya kina Pendo, na mumewe pamoja
na watoto wake wakawa wa kwanza hapo. Nancy ndiye alikuwa na nyama. Alizilaza
kwenye viungo. Mumewe alikuwa mchomaji mzuri sana wa nyama. Walipenda yeye
akisimama kuchoma. Alitoa nyama nzuri kila mtu alipenda. Kaka yao ambaye ndiye
wa kwanza na wakiume pekee kwenye familia, alikuwa akileta vinywaji, mkewe
kachumbari na mama yao matunda. Msichana wa Pendo aliambiwa atengeneze viazi
vya kukaanga, ugali na mchuzi kidogo. Saa nne na nusu, wote wakawa wameshafika,
wapo chumbani kwa Pendo wakizungumza na kucheka wakati Willy anagonga.
Pakazuka
ukimya wa gafla Willy alipoingia. Akasalimia. Wakaitika, kimya wakimwangalia.
Willy akaona amsogelee Pendo. “Mmeamkaje?” Willy akauliza taratibu, lakini
Nancy akamuwahi. “Ndio baba nani tena?” Akaanza Nancy dada yake Pendo. “Naam!”
Akaitika Willy. “Nimeuliza ndio wanakuita baba nani?” “Bado ni Willy tu.
Sikufanikiwa kubadili.” “Mambo ya kizungu! Hamwitani tena baba fulani?” Nancy
akaongeza. Ikabidi Willy amgeukie vizuri. “Hapana Nancy. Sikufanikiwa kubadili
jina kwa kuwa mtoto hakuwa wangu.” Pakazuka ukimya wote wamekodoa macho. “Haya,
naomba mkacheze sebuleni au muwashe tv muangalie chochote mnachotaka mpaka mama
zenu waje wawakataze. Haya, ongoza njia.” Pendo akafukuza watoto hapo chumbani
kwake.
“Kwa
hiyo inamaana uliparamia mimba isiyo yako?” Akauliza Nancy nakuanza kumcheka kwa
waziwazi baada ya watoto kutoka. “Wifi!” Mke wa kaka yao akashangaa sana na
kumfinya. “Bwana Willy uliondoka mbio!” Nancy akaongeza na kuzidi kucheka huku
akimkimbia mke wa Kenton. “Wenzio wanasubiria kidogo angalau hata mpaka mtoto
azaliwe lakini wewe ukakimbilia mtoto wa mwanaume mwenzio!” “Sio mwanaume
mwenzangu, ni wa baba yangu.” Willy akaongeza. Hapo tena pakazuka ukimya mzito
hata Nancy aliyekuwa akimkejeli akatoa macho, kimya. Pendo akabaki akiwatizama.
“Subiri
kwanza Willy, inamaana ulikuwa ukitembea na mwanamke wa baba yako!?” Baada ya kufikiria kidogo, Kenton akauliza hilo
swali kwa mshangao mkubwa sana. “Hapana! Haikuwa hivyo. Mama alinitafutia yule
binti, akisema atakuwa tayari kunizalia mtoto. Mwanzoni huo ndio ulikuwa mpango waliokuwa wamenipa
mimi. Mama na kina Prisca.” “Sema na Stella. Maana namjua Stella sana.”
Akaongeza Nancy. “Na naomba niweke msisitizo katika hili, makosa yote ni yangu
mimi. Nilifanya kwa akili zangu timamu.” “Lakini kwa ushawishi wa mama yako na
dada zako.” Nancy akaongeza kwa jazba. “Kwani walianza kunishawishi jana au
juzi! Ni miaka mingi tu, sema mimi mwenyewe ndiye niliyedhoofika na kuwa
mpumbavu.” “Wala si kidogo!” Nancy akaongeza. Willy akamtizama na kunyamaza.
“Mimi
bado nataka kukusikia Willy. Ikawaje ukaendelea kulala na mwanamke wa baba yako?”
Kenton akazidi kumbana kwa swali la kumkera kama hakuwa amemsikia Willy utetezi
wake tokea mwanzo kuwa, mwanamke alitafutiwa yeye na mama yake. “Niliambiwa
nimetafutiwa mimi.” Hapo Willy akaweka msisitizo na kuendelea. “Ndio
nikawaambia japokuwa mimi nataka mtoto, lakini siko tayari kumuacha mke wangu.”
“Kwa hiyo ulidanganya ndugu zako au unatudanganya sisi sasa hivi, hapa?” “Ungemuacha
amalizie kwanza!” Mme wa Nancy akamtuliza mkewe. Wazazi na Pendo kimya. “Sitaki
atudanganye! Maana mtu ambaye hataki kumuacha mkewe, angekimbilia talaka kwa
haraka kiasi hicho!” “Mimi sikukimbilia talaka.” Willy akajaribu kujitetea na
kumuudhi Kenton zaidi.
“Sio
wewe uliyerudi hapa nyumbani ukamwambia Pendo unaondoka na kwenda kwa mwanamke
wako, aliyekubebea mtoto wako?” Kenton akauliza kwa ukali. “Nilisema hivyo
ila..” “Ulitaka kuendelea kujulikana ni mume wa Pendo huku ukilala hovyo huko
nje tena na mwanamke ambaye kumbe hata hukuwa ukijua tabia zake? Maana kwa kukusikiliza
tu hapa kwa harakaharaka ni kama unaonekana ulikuwa ukilala huko nje na
mwanamke ambaye na yeye alikuwa akilala na baba yako halafu unarudi hapa kwa
Pendo!” Kenton akawaka. Na walimjua alivyo mkali. Baba yake kimya na mama yao,
wakisikiliza.
“Ulitaka
kuendelea kumuumiza Pendo mpaka lini!? Au wewe ulitegemea wote tukuache tu ucheze
na kumuumiza Pendo vile utakavyo kwa kuwa mlijua hataweza kuzaa?! Uingie na
kutoka vile utakavyo!?” “Hapana. Sikutaka kumuumiza Pendo na sikutaka niendelee
kuonekana na mwanamke na mtoto nje, ndio maana nikamwambia ukweli Pendo kuwa
inabidi nihitimishe kwake.” “Sasa hiyo ilikuwa ina maana gani kama si kuachana?
Na kama uliamua kumuacha si ndio kukimbilia talaka huko anakokuzungumzia Nancy!?”
Hapo Willy akaamini maneno ya Pendo. Kaka huyo alionyesha hasira kali sana. Alimuhoji
hapo kwa ukali mbele ya wote.
“Ndio
maana nilihitimisha kwa Pendo kwa haraka kwa sababu nilihisi ni kama nitakuwa
namdhalilisha mpenzi wangu.” “Mpenzi wako yupi? Unaanza kutuchanganya. Huyo
mpenzi wa baba yako?” Nancy akaendelea kumbana kwa maswali ya kumkejeli. “Halafu acha kusema uliamua kuhitimisha kwa
Pendo kwa haraka. Ulihitimisha baada ya Pendo kujua kama unaye mwanamke
mwingine nje, tena mjamzito wa mimba kubwa tu! Ulikuwa ukimchafua dada yangu
hapa, huku ukienda kuchangia mwanamke na baba yako huko kwenu!” “Na mwanamke wa
namna hiyo hata hamjui mbali ya nyinyi wawili alikuwa na nani mwingine!?
Ungemuua Pendo wewe!” Nancy akaongezea kwa kaka yake kwa hasira. “Na uache kutufanya
sisi ni watoto wadogo Willy. Kama alivyosema Nancy, wewe ulitaka kuondoka hapa
kwa haraka sana ila hukuwa ukijua ni jinsi gani utamkimbia Pendo, ukijua Pendo
ana ndugu wanao mwangalia na kumjali si kama
huko kwenu mlikokuwa mkimuita majina mabaya! Nilichokusaidia nikuweka
kwa maandishi tu. Tena nilifanya kwa haraka ili usilete mahawara zako hapa
ndani.” Kenton akaongeza kwa jazba. “Au kuja kumuua Pendo kwa maradhi.” Nancy
akakazania hilo kuonyesha uchafu wa Willy.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Willy Mbele Ya Ndugu Wa Pendo. Itakuaje?
Usikose muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment