“Nionyeshe
picha za mwanao, Willy. Amefanana na
wewe au mama yake?” Kimya. Pendo akashangaa ametulia kidogo. “Willy! Nataka tu
kumuona mwanao, au ni vibaya?” Willy akajicheka. “Ni nini?” “Hakuwa mtoto
wangu, Pendo.” “WHAT!?” Pendo akashituka sana. “Mpaka aibu kusema,
lakini ni mdogo wangu si mtoto.” Pendo akatoa macho. “Willy!” Willy akajicheka tena
na kuinama kwa kuegemeza viwiko kwenye magoti, akabaki akijisugua mikono yake.
“Usiniambie Zelda aliangukia kwenye mtege wa mzee Ngoi!” Willy akashituka na
kumgeukia. “Unamaanisha nini?” “Kabla sijaongea mengi, wewe niambie kwanza, si
ni mtoto wa mzee Ngoi?” “Ndiyo. Zelda sasa hivi anaishi na baba kama mke wake
kabisa. Hivi wanapanga kufunga ndoa.” “Mungu wangu!” “Kweli kabisa. Na hawataki
hata mmoja wetu. Baba ni kama alitufukuza.”“Haiwezekani Willy!” Bado Pendo
alikuwa kama haamini!
“Ilikuwa
kesi kubwa sana mpaka tukaomba wajomba na kaka zake baba watusaidie, lakini
wale watu wameshikana Pendo! Wanaongea lugha moja. Mimi nikifikiria Zelda
alitafutwa au anatunzwa pale nyumbani na mama kwa ajili yangu, kumbe
walishakuwa kwenye mahusiano na baba ya muda mrefu tu, mama akiwa mgonjwa. Baba
amesema anazo baraka zote za mama, kwani mama alimuachia ile nyumba Zelda.
Wawili wale walikuwa wakilala chumba kimoja kama mke na mume, mama alipokuwa akilazwa
hospitalini. Na alipokuwa nyumbani, baba anasema alikuwa akihamia chumbani kwa
Zelda, na haikuwa siri. Mama aliridhia hilo ili ajipatie mtoto kutoka kwa
Zelda.” “Subiri kwanza Willy. Hapo sijaelewa.” Willy akacheka.
“Ni
mazito na ya aaibu, wewe acha tu!” “Yaani ilikuwaje?” “Nia ya kwanza kabisa ya
mama, ni mimi nimuoe Zelda.” “Najua. Na wala Zelda si wakwanza.” Pendo
akaongeza. “Sasa Zelda alikuwa mwalimu wa mtoto yule mkubwa wa Prisca. Alikuwa
akienda nyumbani kwao kufanya naye homework, na kumsaidia yule mdogo pia wakati
wazazi wanachelewa kurudi nyumbani. Siku na hiyo mama akiwa anaendelea kuugua,
Prisca akamwambia dereva wao akamchukue Zelda na mtoto, akawashushe kwa bibi
yao, ilikuwa ijumaa, yeye atachelewa kutoka kazini, atampitia mtoto hapo kwa
mama. Ndipo mama alipokutana na Zelda, akampenda vile anavyopenda mjukuu wake,
yaani mtoto wa Prisca. Akanifikiria mimi. Wakapanga mipango yao wao watatu,
ndipo wakaniunganisha na mimi.” Willy akaendelea.
“Wapi
pakukutania Zelda na Willy ambaye anajulikana ni mume wa Pendo, ikawa nyumbani
sasa. Mwanzoni nikamkatalia mama kama kawaida. Safari hii mama akaweka presure,
akisema atakufa bila kuona watoto wangu, akanisihi japo afe akiwa amepata
mjukuu mmoja tu. Tukazungushana naye, tukipelekana kwenye maombi nikimwambia
hatakufa, Mungu atampa umri mrefu tu, mpaka aje aone watoto wetu. Ndio wewe
ukawa hupati mimba. Mama akaniita siku moja pale nyumbani, Akaniambia kama
ugumu ni kukuacha wewe, basi nizae tu na Zelda. Zelda amekubali kunibebea mtoto
wangu. Nisiwe na wasiwasi, wamezungumza hata na baba, wao watamtunza pale
nyumbani, wala hataingilia ndoa yangu. Ikawa sasa, iwe siri, mtoto akizaliwa
ndio tukwambie. Nikawaambia isije ikatokea hata kuropokwa, wewe ukajua.” Willy
akaendelea.
“Basi,
tukakubaliana. Wakati huo Zelda alishahamia pale nyumbani, kumbe kabla na baada
wao wawili walishaanza mahusiano. Baba anaaga yupo kwenye safari za kibiashara,
kumbe yupo Keko kwa Zelda.” “Haiwezekani Willy! Nyinyi nani aliwaambia?” “Baada
ya kutufukuza nyumbani baba na Zelda, maana ni kama Zelda alibadilika sana.
Akawa mbabe hata kwa wapambe zake. Stell na Prisca. Si ndio Prisca sasa ikabidi
aanze kumchunguza kumjua ni mtu wa namna gani. Maana aliacha kazi akawa anaishi
kwa pesa ya mzee Ngoi. Mwalimu mmoja ambaye alikuwa karibu na Zelda pale
shuleni kwa mtoto wa Prisca ndio akamwambia Prisca kuwa mbona Zelda na baba
wanayo mahusiano mazito mno. Yaani Zelda alikuwa akiwasimulia vile baba
anavyochanganywa na mapenzi ya Zelda mpaka yupo tayari kuacha jumba Masaki,
nakwenda kulala kwenye chumba kimoja huko kwa Zelda, Keko.” Pendo akabaki
ametoa macho.
“Mama
anamuombea Zelda aishi pale nyumbani, kumbe anamkabidhi fisi bucha. Mapenzi
yakaendelea kama kawaida. Mama hana habari akilala sababu ya madawa yale,
wenzie wanaendelea. Akamkabidhi mpaka chumba chake. Msichana wa kazi akasema kipindi
mama amelazwa hospitalini, Zelda alikuwa akilala na baba chumbani kwao.”
“Willy!” “Kweli. Sasa sisi wote tunajua Zelda yupo pale kwa ajili yangu, kumbe
ni mama mdogo, mke wa baba. Si ndio kwa papara na ushauri wa familia, mbele ya
baba na Zelda nikashauriwa sasa kuishi na mke wangu kama mama alivyotaka! Kumbe
wao wanatusikiliza na kuumia kuona tunawaharibia. Ilikuwa mipango yao mama akifariki,
mimi niendelee na wewe, wao wawili waendelee kuishi pale. Hata mtoto akizaliwa
nikaambiwa ni wangu, wao wanaendelea na maisha yao, kuna shida gani! It’s a
win win situation.”
“Sasa
si ndio nikakuachia hapa nyumba nikaenda kulala hotelini mpaka siku ile ya
talaka. Usiku ule mimi nikarudi sasa kumchukua mke huyo mwenye mtoto wangu,
twende tukaanze maisha. Nafika pale nikawakuta na dada Stella pale.
Akanipongeza mno kukuacha na kuniambia kwa hakika mama atafurahia
nilichofanya.” “Yaani kuniacha mimi?” “Ndiyo.” Willy akajibu, Pendo akapoa
kabisa na kujiinamia, Willy akamuona. “Naomba nimalizie. Najua ni mbaya, lakini
wewe sitakuficha Pendo. Acha nikwambie aibu yangu tu, kama utazidi kunichukia
sawa, najua nastahili, na kama utanicheka pia sawa, bora tubaki kuwa marafiki.”
Pendo akamwangalia.
“Sasa
namuaga baba kuwa ndio tunaondoka na Zelda, tukakae hotelini wakati natafuta
pakuishi, Zelda akauliza haraka sana. Kwa nini iwe hotelini na sio nyumbani
kwangu. Nikamwambia hii nyumba nilijenga na wewe tokea tupo chuo, tulinunu hiki
kiwanja kwa pamoja. Tukajenga taratibu mpaka tulipomaliza. Nikamwambia sikutaka
kung’ang’ania nyumba, kwanza mimi ndiye niliyeamua kuondoka, sio wewe. Sasa
ukumbuke hapo Zelda anamaslahi mawili ambayo nilikuja kumsikia akitamka yeye
mwenyewe wakati akinitukana.” “Kukutukana tena!?” “Acha Pendo. Mungu alinichapa
hadharani, mbele ya watu bila kunibakiza. Wewe si unasema ulidhalilika kuachwa
sababu ya ugumba? Basi mwenzio ilikuwa mbaya zaidi yako. Bora wewe ni kwa
matatizo yakutojitakia.” Pendo akabaki haelewi.
“Mimi
nilikuwa natukanwa na Zelda kama mtoto mdogo.” “Kwa nini tena!?” “Sikiliza
sasa. Wakati nataka kumtoa Zelda pale, baba akaniambia hakuna sababu yakwenda kuishi
hotelini, wakati pale ni pakubwa na yeye yupo peke yake. Nikafikiria kwa
haraka, nikaona ni kweli. Kwa nini nipoteze pesa hotelini na kupanga wakati
pale pako! Kumbe baba hataki nimtoe mwanamke wake pale. Mimi nikahamishia vitu
vyangu kwenye chumba cha Zelda nikijua ni mwanamke wangu, kumbe kinawauma
haswa. Baba wivu, hataki na mwanamke wake, Zelda ashanichukia haswa. Hanitaki
mimi ambaye sina nyumba, anamtaka baba ambaye anajumba Masaki. Mimi kulala
pale, kwa Zelda sio jambo zuri, nani analala na mzee wake! Si inamaana baba
atachukua dogodogo mwingine. Unaambiwa wakabadilisha utaratibu. Mapenzi mchana
ninapokuwa kazini. Nikirudi nyumbani Zelda amenuna anakaribia kupasuka. Mkali
haswa.”
“Hakuna
ninalomuuliza ananijibu vizuri. Hatukukaa sana sijui week mbili tu nikamuuliza
mbona kama ananitafutia sababu ya kugombana!” Willy akamsimulia Pendo kisa
kizima mpaka kutupiwa nguo nje, na kutukanwa mbele ya familia. “Mungu wangu
Willy, pole!” “Wala usinihurumie Pendo. Nilistahili. Nakwambia siku mbili,
nilikuwa nalala kwenye gari, sina pakwenda.” “Ungerudi nyumbani Willy.” Pendo
akaongea kwa huruma. “Nilijiambia hata iweje, nisingethubutu kurudi.
Nikajiambia itakuwa sio sawa kwako. Ni kama narudi kwa kuwa kule nimekwama! Nikasema
nishakutenda ubaya, acha nitumikie adhabu yangu. Likabaki swala la mtoto. Sasa
mtoto ni wangu au sio wangu!”
“Sasa
kwenye kikao wakati mzee anatufukuza, mimi nikamuuliza Zelda, kwa hiyo mtoto ni
wangu au sio wangu! Akanijibu jibu ambalo sio la moja kwa moja. Nikaondoka pale
sijaridhika.” “Kwani alikujibu nini?” Willy akasita. “Willy?” “Aliniambia kwani
kipindi yeye yupo pale, na mimi niko na wewe, na tunakwenda pale tunamkuta pale
na ninampita nikijifanya simjui yeye sababu nipo na wewe, yeye alishaniuliza
kama nalala na wewe au la! Yeye aliheshimu kuwa nina mahusiano yangu,
hakuniuliza. Sasa iweje mimi nimuulize yeye swali la kijinga kama hilo?”
“Willy!?” “Kama nimeongeza, ni kidogo sana. Alinijibu hivyo mbele ya watu wote,
na baba akiwepo.” Pendo akashangaa sana.
“Sasa
mimi nikawa sijaridhika, ndipo nikawaomba ndugu zangu tutafute msaada wa watu
wazima. Ndipo sasa wakakusanyika wazee, tukiwa tumeshazungumza nao, wakamuomba
baba kikao. Baba hakukataa. Akawakaribisha nyumbani kwake. Tulipokusanyika
wote, akawawahi hao wazee kabla hawajazungumza kilichotupeleka pale yeye akawaambia
amefurahi wamefika pale, alitaka kuwaita kuwaambia amepokea wito wa mama,
ameamua kuhalalisha ndoa. Ndio watu sasa wakashangaa. Kwamba mama alikuwa
anajua! Baba na Zelda wakakiri wazi kuwa mama alijua na alimruhusu Zelda alale
na baba, ili kuona wapi mimba itashika kwa haraka...” “Acha Willy!” “Subiri
kwanza Pendo. Ni mazito mno. Nililia na kuondoka pale kama mtoto aliyechapwa
mstarini mbele ya shule nzima.” “Ehe!” Pendo akataka aendelee.
“Ndio
Zelda akasema mama alimruhusu kulala na baba kwa haraka na mimi kama nitakubali
ili ashike mimba. Akishashika mimba ijulikane kama ni yangu, ili sasa mimi
nikishakuacha wewe sasa, na kukubali kuwa na Zelda na mtoto wangu, hapo ndipo
atulie, anizalie mimi watoto. Lakini huyo wa kwanza asiwe na wasiwasi naye.
Hata hivyo nisingejua, kwa kuwa mtoto atatoka anafanana na sisi tu.” “Mungu
wangu Willy!” “Lakini wazee wakamuuliza, sasa mtoto ni wa nani! Ndio akasema
kwa hakika ni wababa. Maana siku mama alizomruhusu kulala na baba zilikuwa za
hatari. Mimi nilipokuja kukubali, alishakuwa amekosa siku zake zaidi ya siku
kumi. Na bado walikuwa wakiendelea na baba. Zelda alikiri wazi, yeye anampenda
sana baba. Ameishi naye kipindi mama yupo, ameona ndiye mwanaume anayemuhitaji
maishani. Wakatumbia mtoto akizaliwa na akifikisha miezi mitatu tu, wanafunga
ndoa. Hivi tunavyozungumza, mwezi ujao harusi. Baba amesema, tukijisikia kwenda
sawa. Itakuwa njia yakumuenzi mama yetu. Tusipotaka pia ni sawa.” Pendo akabaki
ameduaa.
Ukapita
ukimya wa muda, Pendo akawa kama amefikiria kitu. Akamuuliza. “Sasa unaishi
wapi muda wote huo?” Akamuona anacheka. “Wapi?” “Dada Stella nafikiri alianza
kuhukumiwa moyoni kuona waliniingiza matatizoni, akanikaribisha nikaishi kwake,
lakini Pendo, nilikataa.” “Ulikumbuka matusu ya Zelda na mzee Ngoi?” Pendo
akamuuliza huku akicheka. “Kabisa. Wale watu waliniita mpumbavu, nilishindwa
ndoa yangu! Nikajiambia hapa historia itajirudia na nitazidi kupoteza heshima
kwenye jamii. Nakajitafutia apartment, naishi huko. Nigarama, mpaka moyo unauma.”
Pendo akacheka kidogo na kunyamaza.
Kisa cha
Mzee Ngoi na Pendo.
“Mwanzoni ni kama ulimtaja mzee Ngoi
moja kwa moja. Ulijuaje?” “Sikutaka kukwambia Willy, lakini sababu kubwa iliyonishinda
kufika pale kwenu ni baba yako.” Willy akakunja uso. “Sikuelewi!” “Baba yako
alikuwa akinitongoza na kunitaka kwa nguvu mpaka nikadhani mama amenihisi. Na
ninahisi ndio sababu ya mama yko kunichukia, lakini nikaona ninyamaze tu. Na
sikuwahi kumwambia mtu yeyote.” Willy akakaa vizuri. “Ilikuaje au hukumuelewa?”
“Wewe si unamjua baba yako alivyomuwazi? Hakuuma maneno. Alinitongoza waziwazi
Willy. Nilishituka, nikaondoka kabisa pale nyumbani.”
“Akaja
siku moja pale ofisini, akaomba tukazungumze kwenye gari. Mzee Ngoi akaniambia
yeye ananipenda kiukweli. Amevutiwa na mimi, anataka tuwe na mahusiano. Tena
akasema itatusaidia hata kwenye ndoa yetu, kwa kuwa wewe huna uwezo wa kumpa
mwanamke mimba, yeye atatusaidia. Mtoto atatoka anayefanana na wewe, na DNA
hazitakuwa mbali.” “Haiwezekani Pendo!” Willy hakuamini.
“Mungu
wangu ni shahidi. Siwezi kuongopa sasa hivi wakati namtegemea Mungu sana.
Sitaki hata kumuudhi Mungu wangu. Basi, ndio ilikuwa mwanzoni kabisa tumeoana
tu, tunatafuta mtoto lakini hatujui tatizo ni la nani. Mimi nikamwambia nampenda
mume wangu. Awe hana uwezo wakunizalisha au la, sitamsaliti Willy, yeye ndio
atabaki kuwa mtoto wangu.” Willy akajisikia vibaya sana, akapoa nakushindwa hata
kumtizama tena .
“Hiyo
ikapita, akaondoka. Siku moja mama yako akanipigia simu na kuniambia nikitoka
kazini nipitie kwake, ana mashuka mazuri sana anataka kutupa. Nafikiri niliwahi
kutoka kazini au nilichelewa, lakini tukapishana na mama Ngoi. Mimi naingia
ndani, nikamkuta baba yako tena ni kama alikuwa anataka kutoka. Akanisalimia,
nikamwambia mama aliniita nikafuate mashuka. Akaniambia mama ametoka na
msichana wa kazi, ila anafikiri mashuka yapo chumba kile cha pale karibu na stoo.
Mwisho kabisa. Akaniambia ndiko anakomuona mama yako anaweka vitu vyake kama
mashuka na mapazia.” Pendo akacheka.
“Nini?”
“Bwana mimi nikawa sina wazo wala wasiwasi. Si nikaacha pochi pale nikaenda
kule. Ile nimeingia kwenye kile chumba baba yako naye akaingia.” “Pendo!”
“Nilikaribia kuchanganyikiwa Willy. Akaniambia yeye anavutiwa na rangi yangu,
nina weupe mzuri, na umbile langu linamchanganya kila akiniona. Ananitaka kwa
hali na mali. Tukaanza kurupushani mle ndani, ananiambia nimtolee hata ziwa anyonye
tu.” Willy akafunga macho.
“Nilihangaika
tunazungushana pale chumbani akitaka kunikamata mpaka tukamsikia mama yako
anaita. Ndio akafungua mlango. Mama yako akajua tupo kule. Sasa yeye anatoka, na
mama naye anakuja. Yeye amesimamisha mpaka unamuona kabisa. Mimi nahema ndani,
nimepaniki. Nikasikia kimya cha muda nje ya mlango. Sasa sijui mama alimkamata
na kumuangalia ile hali aliyokuwa nayo, lakini mama akaingia ndani. Akiwa
amebadilika Willy, mimi nikamuwahi nikamwambia nipo pale kwa kuwa baba
alinielekeza mashuka yapo kule. Mama yako akajibu hana tena hayo mashuka,
alishampa Prisca. Nikashangaa maana ndio alikuwa ameniita siku ileile, lakini
nikaondoka tu.” “Ndio maana mama alikuchukia!” “Mbona bado.” Willy akatoa
macho.
“Kuna
siku, sijui kama utakumbuka Willy. Tulikwenda kwenu, mimi na wewe. Tulikuwa sebuleni
wote wanne. Mama alikuwa ametupa chai, ilikuwa jioni. Kabla yakuondoka,
nikasema nisaidie kutoa vyombo. Hiyo ilikuwa kama mwezi baada ya lile tukio.
Maana niliacha kabisa kwenda pale nyumbani mpaka siku hiyo uliniomba
nikusindikize, ukasema hatutakaa sana. Basi nimetoa vyombo pale. Nilibeba
kwenye trei hivi. Na chupa ya chai. Nimefika jikoni nikaamua kusuuza vikombe
ili nisiviche pale juu vichafu. Ile nimesimama kwenye sinki, nikashangaa
nimeshikwa ziwa. Nilishituka mpaka nikavunja ile chupa ya chai ya mama Ngoi. Ilikuwa
kubwa hivi ya rangi ya dhahamu. Unakumbuka wote mkakimbilia jikoni?” “Sasa
nakumbuka.” “Basi mzee Ngoi alinishika ziwa, Willy. Nafikiri mama alijua kuna
jambo lilitokea pale kati yangu na mumewe. Ndio kuanzia hapo, mama
akanibadilikia kabisa. Akawa kama hanitaki pale kwake.” “Kwa nini hukuniambia,
Pendo?” “Ningeanzia wapi!?” Pendo akamuuliza. Willy kimya amebaki na mshangao.
“Mbona
bado!” “Acha masihara Pendo! Aliendelea?” “Kabisa. Siku nyingine akanishika
kwenye matako palepale kwenu ila nje wakati nataka kuondoka. Nikisema kwenye
matako sio juu ya nguo. Yule mzee alinivizia Willy, akanyanyua gauni nililokuwa
nimevaa akanishika kwa nguvu.” Willy akahisia dunia inazunguka. “Sasa si unajua
madirisha ya chumbani kwa wazazi wako yanaangalia upande ule wakuegeshea
magari. Huwezi jua pengine mama aliniona. Lakini niliumia sana. Nililia Willy!
Nililia sana. Kitu kilinishika kooni, nikajikuta nalia njia nzima. Nikaona ni
ujinga. Nikaegesha gari pembeni, nikampigia mzee Ngoi. Nikamwambia siku akija
kunigusa tena, naenda kumwambia baba yangu, wala sio wewe. Nikamwambia ile iwe
mwisho asije kurudia tena. Akaomba msamaha, akaniambia alikuwa anajaribu
kunionyesha yupo serious na mimi, kwa hiyo kama ni hofu, niondoe. Lakini kama
simtaki, basi. Ila akaniambia natupa bahati, yeye angenitunza vizuri sana bila
yakuniharibia ndoa. Nikamkatia simu. Hakurudia tena, ila hatukuwahi kuwa
marafiki tena na mama. Sasa lililokuwa likimtoka mama yako mdomoni kwake
akionyesha ni kwa nini namuumiza, ni kwa sababu sijampatia wajukuu, ila mimi
nilihisi ni mengi Willy.” Willy akainama akiwa na macho mekundi sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mama
yake Pendo akaingia. “Willy Ngoi!” Akashituka karibu aangushe mizigo. Willy
akasimama kwa haraka. “Shikamoo mama.” Akabaki kimya akimtizama, kisha
akahamisha macho kwa Pendo. “Ni nini kinaendelea!?” “Willy amekuja kusalimia
mama. Alikuwa amekaa tu hapa. Mbona hujapokelewa mizigo?” “Sijamuona Sifa hapo,
nikapitiliza tu. Hata hivyo hivi ni vitu vyako vya humu ndani. Milkshake
niliona imekuishia na dawa za watoto. Umeshindaje?” Willy akampokea. “Nimeshinda
vizuri.” “Wajukuu?” Akauliza mama yake.
“Naona hawajambo, namshukuru Mungu. Mbona hujaniomba nikurushie pesa? Hiyo
Milkshake ni gali kweli!” “Na kweli ni garama. Tutakatana juu kwa juu. Nilitaka
usiishiwe kabisa.” “Nashukuru mama yangu.” Akampangia vitu juu ya meza.
Akamgeukia
Willy. “Mtoto anaendeleaje Willy? Na mwenzio na wewe mwenyewe?” “Tunaendelea
vizuri mama. Asante.” “Umetukumbuka leo?” Akauliza tena mama yake Pendo na
sauti yake kama Pendo. “Sijawahi kuwasahau mama yangu.” “Karibu. Mtoto si
atakuwa ameshakuwa mkubwa sasa?” “Miezi miwili sasa.” “Hongera sana Willy. Hivi
Mungu alikubariki wa wakike au wakiume?” “Alizaliwa wa kike.” Willy alijibu
wazi akionyesha kukosa ujasiri. “Hongera sana baba. Mungu ambariki, akue
vizuri.” Kimya.
“Wajukuu
zako wamekusikia, wameanza kucheza.” Pendo akavunja ukimya, mama yake akacheka
na kusogea. Akamshika tumbo. “Mmeamka na njaa? Nimewaletea virutubisho vizuri,
mama yenu anawapa sasa hivi. Mtulie humo ndani mpaka mkomae kabisa, mkitoka
hapa sio kulala hospitalini. Chumba chenu kipo tayari, babu yenu anakuja
kuwatengenezea vitanda jumamosi. Mcheze taratibu msimuumize mama. Sawa?” Pendo
akawa anacheka. Willy kimya amesimama. “Sijui wanacheza mchezo gani! Ona huyu
alivyotuna mama! Sijui ni dada mtu au kaka yake!” Wakaendelea kucheka huku wakiwagusa.
“Walikuwa kimyaa, naona wamekusikia, wakaona wakusalimie kabla hujaondoka.” Bibi
yao akawabusu huku akiwashika.
“Naomba
na mimi niwasalimie Pendo. Sijawahi kushika mtoto akiwa tumboni.” Willy
aliongea kwa huzuni, Pendo na mama yake wakamgeukia. Willy alikuwa amesimama tu
pembeni. “Kama ni sawa lakini. Nilitaka na mimi niwasalimie tu.” Akaongea kwa kurudia
na wasiwasi usoni. Mama yake akamtizama Pendo kama kutaka kujua msimamo wake
kwa Willy aliyemkimbia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment