Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 35. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 35.

 Mimba ilipofikisha miezi 5, Pendo akaandikiwa bed rest. Watoto walikuwa wakikua, na vimbe nazo zinakuwa. Daktari akamshauri lazima apumzike nyumbani aache kazi na shuguli nyingine zote, apumzike kabisa kwa kulala kitandani ili watoto wakomae. Pendo akapeleka barua ya daktari ofisini, hapakuwa na jinsi, akapewa hiyo likizo. Akarudi nyumbani maisha ya kulea mimba yakaendelea mchana na usiku akiwa makini haswa. Mama yake ndio mstari wa mbele akimsaidi binti yake. Na yeye pia akapunguza shuguli. Asubuhi lazima apite kwa Pendo, na jioni pia. Uzuri Pendo alikuwa na msichana mzuri sana wa kazi, kwa hiyo ikawa nafuu kwake. Yeye na Sabrina wanashindana matumbo. Sabrina alimpita mimba kwa miezi miwili. Wakati Pendo ana mimba ya miezi sita, Sabrina nane. Tumbo kubwa wote wanavaa matenite. Wakipigiana simu ni habari za watoto tu. Ukaribu ukaongezeka zaidi.

Kwa Mungu Yote Yanawezekana.

S

iku hiyo Pendo akaamua atoke, aende benki. Alikuwa na shuguli zake zakufanya kwenye benki mbili tofauti. Alitoka kama mida ya saa nne asubuhi. Akaendesha taratibu mpaka Mlimali City. Akawa anatembea taratibu humo ndani kuelekea tawi la CRDB palepale ndani Mlimani City alikojua atapata huduma za benki zote mbili bila kuhangaika. Wakati yupo karibu na benki hiyo macho yakagongana na Willy. Akacheka. “Umegoma kuzeeka Willy! Umepunguza mwili wote!” Pendo akaongea huku akimsogelea taratibu, Willy akabaki ameduaa. “Lakini umependeza.” Pendo akaongeza, akijua wazi anamshangaa. “Ni wewe Pendo!?” Pendo akacheka. “Ni mimi Willy. Unanishangaa nilivyogeuka kuwa kama nyumba?” “Hapana. Umependeza.” “Acha kunidaganya Willy! Si unajua na mimi ninavyo vioo nyumbani kwangu? Najua usichana umeisha. Nakula siku hizi kama mchwa!” “Hongera sana.”  Akacheka. “Asante. Acha niwahi hapo benki kabla muda wa chakula cha mchana kwa wafanyakazi haujafika, wakajaa benki. Sina nguvu ya kusimama muda mrefu.” Willy akawa kama bado anamshangaa.

Pendo akacheka na kuanza kutembea tena. “Nimefurahi kukuona Willy, uwe na siku njema.” Akampita huku akiongea taratibu na kujivuta taratibu kama anayeumwa miguu. Willy akamkimbilia tena akawahi mlango wa benki, akamfungulia. “Nashukuru. Maana nilikuwa nafikiria, nimwite yule askari anifungulie.” “Nakuona unavyotembea! Unamaumivu?”  Pendo akacheka. “Hata kidogo. Ila nabembeleza huu mwili unitunzie wanangu. Nimetoka tu kitandani, lakini siruhusiwi kuzurula hivi, ni basi tu.” “Ungejitahidi kufuata masharti Pendo!” “Najitahidi sana. Mbali ya kutoka kwenda kujisaidia na kuoga, sitoki kitandani. Leo imenilazimu, na sina wakumtuma. Dereva wangu amekuwa mama, na yeye leo anashuguli zake” Pendo akapitiliza mpaka ndani, benki.

Kidogo Willy akawa ameshapata habari kuu mbili. Watoto ni wawili, na hakuna mwanaume mwingine kwenye picha. Ni mama yake tu. Akaingia na yeye ndani akiwa Pendo amemtangulia. Akamtafutia sehemu ya kukaa. “Nitume mimi.” Pendo akacheka. “Wewe wahi kazini. Mwenzio hii ndio kazi yangu kwa leo. Nikitoka hapa, narudi nyumbani kulala.” “Kazini?” Willy akauliza. “Nilipewa mapumziko. Kwa hiyo nipo tu nyumbani. Wala usijali Willy. Mimi nipo sawa. Kwanza nafurahia kupata wakati kama huu. Nachoka kukaa tu nyumbani peke yangu.” Akamwangalia, Pendo akacheka. “Unavyonishangaa! Kwani nimebadilika sana?” “Sana! Sijawahi kukuona ukiwa umenenepa hivyo! Lakini umependeza, ukarudi kuwa mtoto!” Pendo akacheka sana. “Sababu ya mashavu kuongezeka, yameleta baby face.” Akaongeza Pendo, wakacheka.

“Sasa unataka kuweka pesa au kutoa?” “Nataka kutoa. Nina mambo mengi yakufanya hapo nyumbani. Yote yanahitaji pesa. Na nilifungua akaunti ya watoto. Kama hivi mshahara ulitoka, lakini sikuwahamishia pesa. Nilishindwa kuja. Kwa hiyo nataka kutoa pesa hapa, nyingine niwapelekee kwenye akaunti yao. Sio hapa. Nilifungua kwengine, lakini humu humu ndani Mlimani City. Pesa nyingine niondoke nayo.” Akamuona Willy amebaki akimshangaa. Akacheka. “Nilikwambia nina mambo mengi humu ndani. Wala sitoki leo.”  “Subiri tuanze kwa kutoa kwanza pesa.” Akaenda kumchukulia karatasi yakutoa pesa, akamletea. Pendo akajaza kila kitu, Willy akisubiria huku akimshangaa bado. Pendo akamaliza. “Sasa unataka nikupe wewe?” Pendo akamuuliza. “Naenda nayo pale mapokezi, wala si kwa teller. Nisubiri tu.” Akachukua ile karatasi na kadi ya benki, akaenda nayo mpaka hapo mapokezi. Pendo akamuona akizungumza nao, na kumnyooshea yeye kidole.

Wakampokea, mfanyakazi mmoja wa benki aliyemkuta pale akaenda kuchukua pesa kwa teller. Baada ya muda akaona wote wawili wanakuja pale alipokaa. Akamkabidhi baada ya kuhakikisha ni yeye, akaondoka. “Nashukuru Willy. Acha mimi nisogee benki nyingine.” “Twende nikusindikize.” Akamshika mkono, akamsaidia kusimama. “Natembea taratibu sana!” Pendo akaongea kwa deko akijilalamisha kama kawaida yake, mtoto wa mama. “Nimekuona. Sawa tu, twende.” Wakatoka hapo.

“Vipi familia yako lakini?” Pendo akauliza wakati wakitembea taratibu. Kimya. “Si mtoto atakuwa ameshakuwa mkubwa sasa?” Pendo akaendelea kuongea huku akijivuta. “Ndio miezi miwili sasa.” “Hongera Willy. Mungu amekujibu.” Akamuona amenyamaza. “Hivi alikuwa wakike au wakiume?” “Wakike.” “Safi sana. Hongera. Hatimaye na wewe umeitwa baba Willy! Mungu amekufuta machozi.” Akaendelea kuzungumza taratibu huku wakitembea. “Na wewe una miezi mingapi sasa?” “Nakwenda wa saba. Tunabembelezana na wanangu taratibu hivyo hivyo.” “Kwani una matatizo yeyote? Au niulize ni kwa nini umepewa mapumziko?” Willy akauliza. “Acha nikwambie tukitoka hapa.”  Walikuwa wameshafika benki. Akamfungulia tena mlango, akaingia. Akafanya kama alivyofanya mwanzo. Akajaza karatasi za benki, akahesabu kiasi cha pesa alichotaka kiwekwe kwenye akaunti ya watoto wake, nyingine akarudisha kwenye pochi. Willy akamsaidia kwenda kuziweka. Wakatoka.

“Una muda tukae tule?” Willy akauliza. “Hapana Willy. Nimeacha kula barabarani. Najitahidi kula vitu muhimu kwa watoto ili wakomae. Tukae hapa nikwambie.” Wakakaa nje ya hiyo benki ila ndani ya jengo. “Unakumbuka zile vimbe nilizokuwa nazo kwenye kizazi?” Willy akaitikia. “Sasa kadiri watoto wanavyokuwa, na zenyewe zinakuwa.” “Pole Pendo.” Pendo akacheka. “Lakini hazinisumbui, ila hatari yake inaweza kusababisha nikajifungua mapema kabla ya muda. Na ndio maana unaona tumbo kubwa hivi. Zinashindana na watoto. Sasa najitahidi kula na kunywa kila kirutubisho kitakachofaa wanangu, Willy. Sijazi tumbo na vitu vidogo vidogo ambavyo najua havitasaidia watoto. Nimezidisha umakini, ili wakizaliwa wakati wowote ule, angalau wawe wamekomaa. Na ndio maana daktari alishauri nipumzike kabisa ili watunzwe humo ndani.” Willy akainama kama anayefikiria.

“Vipi lakini wewe? Tumepotezana kabisa! Umerudi kuwa kijana Willy! Au ndio maandalizi ya harusi, suti ikae vizuri?” Pendo akampiga begani kidogo. Willy akamwangalia. “Nimekuwa tu na mambo mengi. Mungu alinisaidia nikapata ile kazi. Unakumbuka nilipokwenda kufanya usahili wakati ule?” “Willy! Kumbe walikuita?” “Walikuja kuniita Pendo. Wanamshahara mzuri sana, marupurupu mengi. Na jumamosi na jumapili hakuna kazi. Ni kampuni nzuri sana. Hakuna uswahili kama kule mwanzoni. Kwa kweli namshukuru Mungu.” “Hongera Willy. Ila na wewe unajituma sana na unanidhamu ya kazi tokea zamani. Lazima Mungu akuheshimu kwa hilo, akupe makubwa. Nimefurahi kusikia hivyo.” Wakanyamaza kidogo.

Willy akamwangalia. “Acha niende Willy. Nina mafundi hapo nyumbani, nataka nikawalipe.” “Unajenga nini?” Pendo akacheka taratibu. “Sio kujenga haswa, lakini natengeneza chumba cha watoto. Nimeshamaliza makabati yao. Kuna jinsi nilitaka yakae kwenye kile chumba karibu na chumba kile tulichokuwa tunakitumia mimi na wewe. Naona nilipata fundi mjuzi kweli! Amepatengeneza vizuri! Nikatafuta fundi wa kupaka rangi niliyoona itaendana na wanangu, sasa hivi yupo mchoraji. Nimetaka achore picha za kitoto huko ukutani, ndipo nianze manunuzi ya vitu vyao. Vitanda, nguo na diaper. Nataka niwe na kila kitu kabla hawajaja.” “Hutafanya baby shower!?” Pendo akajicheka na kuinama.

Akamuona amebadilika sura. “Kwenye baby shower utapata vitu vingi Pendo. Umekuwa ukiwafanyia watu baby shower na kushiriki pia kwenye za wengine. Huu ni wakati wa wewe kufanyiwa Pendo! Unastahili.” “Hapana Willy.” “Kwa nini?” Pendo akajicheka tena kidogo. “Kwanza sio watu wengi nimewaambia juu ya huu ujauzito, Willy.” “Kwa nini!? Wakati ni kitu ambacho tumehangaika sana!” Willy akashangaa sana. “Watu wanachoka Willy! Habari zangu na swala la watoto umekuwa wimbo kwenye kila familia inayonifahamu, na marafiki. Tumbo langu bado lina matatizo si kama kina mama wengine. Kwa hawa watoto kuwepo hapa mpaka sasa hivi ni Mungu tu. Kila siku lazima mimi na Sabrina tupigiane simu, tuombe. Kila saa ninayowaona wapo humo tumboni, kwangu ni muujiza ninao ushikilia kama mboni ya jicho! Likitokea lakutokea watoto wasiwepo na nishatangaza kwa watu watoto wanakuja, nahisi sina nafasi ya fedheha nyingine Willy! Swala la kuachika kwangu sababu ya kutokuzaa limevuma na kusemwa kila mahali! Sitaki kuwapa watu sababu nyingine yakunikejeli.” Pendo akaongea taratibu kama kawaida yake, Willy akajisikia vibaya sana.

“Sasa hebu fikiria watu ndio wanakupa vitu vya watoto. Unagarimu watu pesa na muda, halafu inakuja tena kusikika, eti yule mgumba alishika mimba, lakini tumbo lake limeshindwa kutunza watoto!” “Naomba usiseme hivyo Pendo.” Willy akaongea kwa uchungu sana na kujifuta machozi. “Ni kipi si cha kweli hapa, Willy!?” Pendo akauliza taratibu. Willy akainama macho mekundu. Wote wakaanza kutokwa na machozi hapo Mlimani City, mchana huo taa zikimulika pia, na watu wakipita na kuwaona. Mwishoe Pendo akasimama, akaanza kuondoka huku akifuta machozi. Willy akamfuata.

Akajifuta na yeye machozi akaongeza mwendo kumfikia. “Umeegesha wapi gari?” “Upande huu. Karibu na mlangoni tu.” Wakaendelea kutembea. “Kuna kitu chochote unataka hapa?” Willy akamuuliza walipokaribia gari ya Pendo. Ni gari aliyomuacha nayo, anaifahamu gari yake. “Hapana. Mama ndio dereva wangu mwenzio. Wanapokezana na baba. Kila nikiishiwa naandika na kuwatumia orodha nzima. Wananifanyia manunuzi na kuniletea nyumbani. Kwa hiyo nipo tu sawa.” Akabonyeza rimoti za gari yake, gari ikafunguka. Willy akaenda kumfungulia mlango. “Asante.” Pendo akaingia taratibu na kujipanga kitini tena taratibu na kwa tahadhari, Willy amesimama mlangoni akimtizama.

“Wewe Willy ni malaika uliyetumwa leo kwangu na Mungu. Asante sana na Mungu akubariki kwa msaada wote.” Willy akatoa tu tabasamu akimtizama wakati anavuta mkanda. Akamsaidia kuuvuta na kumfunga. “Na asante kwa hili pia.” Pendo akashukuru tena. “Karibu. Naomba kuja kukutembelea nyumbani.” Pendo akamwangalia kama anayemshangaa kidogo.

“Unataka kuja kuniona mimi!?” Pendo akauliza kama ambaye haamini. “Ulisema mbali ya ndoa niliyovunja mimi, sisi ni marafiki tokea zamani, Pendo!” Pendo akacheka. “Kwa hiyo unanifunga kwa maneno yangu mwenyewe?” “Mimi nakukumbusha tu.” “Sasa kama ulilikumbuka hilo mbona hukuja siku zote hizo hata kuniona kujua ninaendeleaje, ndio leo unataka kuja? Au majukumu ya familia yalikuzidia?” Pendo akamuuliza akicheka taratibu kama alivyo hapendi kumuudhi mtu.

“Nilijua utakuwa umenichukia Pendo.” “Kukuchukia hapana Willy. Ila niliumia, au tuseme nina maumivu ya kukupoteza Willy! Unajua sisi tulikuwa marafiki wa muda mrefu sana? Siwezi kukuchukia kwa kutafuta kwengine kile nilichoshindwa kukupa mimi Willy! Nilielewa sana tu. Ila niliumia na kujichukia sana. Na wala sitakudanganyi, bado huwa na kumiss pale ndani.” Willy akainama. Akakumbuka aina ya ndoa aliyokuwa nayo na Pendo. Tulivu mno. Kila mtu aliwasifia. Wakatulia kwa muda, Willy amesimama mlangoni, Pendo amekaa.

“Nakukaribisha muda na wakati wowote Willy. Karibu. Milango ipo wazi.” Willy akanyanyua macho akamtizama. Pendo akamuona vile macho yalivyo mekundu kama anayetaka kulia. Akambusu shavuni. “Asante.” Willy akashukuru na kujifuta machozi mbele ya Pendo. “Nitakuja basi leo na movie tuangalie.” Pendo akacheka akamtizama na kuamua kumuuliza. “Utakuja leo!?” “Ndiyo. Si umesema muda na wakati wowote?” “Acha bwana kunifunga kwa maneno yangu mwenyewe, Willy!” Wakacheka. “Nikitoka kazini, nitakuja. Huna kitu chochote unapenda kula?” “Nakwambia yale mambo sijui yakujisikia hamu zile za mimba kula chochote imebidi kuonya akili. Nina ratiba ya kula vitu maalumu kila wakati. Kabla sijaondoka nyumbani imebidi kunywa juisi ya tembele. Na kwenye hii chupa unaona hapa kama thermosi, nimeweka milkshake ya baridi. Ni ya virutubisho vya protein tupu. Nikirudi nina mlo maalumu. Sasa nikijichanganya tu, nikaweka kitu kingine tumboni, inamaana nilichohitajika kula cha wanangu sitakila.” “Naona mama umejikana haswa!” Pendo akacheka.

“Si kidogo. Sitaki kuja kujilaumu Willy. Acha nifanye kwa sehemu yangu, mengine nimwachie Mungu.” “Na mimi nakuombea Pendo. Mungu atakusaidia.” “Amina na asante sana Willy. Uwe na kazi njema. Ukija utanionyesha picha za mwanao.” “Kwanza hujaniambia Pendo.” “Nini tena?” “Ni watoto gani?” Pendo akacheka. “Mungu amenipa wakiume na wakike Willy. Wakiume nitamuita Samuel. Kama vile Mungu alivyomkumbuka Hana, akamfungua tumbo na kumpa Samweli. Namshukuru na mimi kunikumbuka, nakunipa Samuel. Halafu wa kike ataitwa Sabrina. Amenibeba yule mtoto jamani! Najua Mungu alimleta kwangu kwa sababu Willy. Ni kama ulipoondoka wewe, Mungu akampa nafasi yako. Amekuwa faraja ya ajabu.”  Machozi yalikuwa yakimtoka Willy kama mtoto mdogo, tena wa kike mbele ya mwalimu mkali mwenye kiboko.

“Amenibebea aibu yangu magotini bila kunichoka. Ile hali ya upweke pale kitandani usiku, ilikuwa ikiisha kwa Sabrina. Hata katikati ya usiku nikimpigia, haachi kupokea na kutoka kitandani. Anamuacha mumewe, azungumze na mimi. Basi tutazungumza wee, mpaka akisikia nimetulia ndio anaacha nilale. Nilikuwa nikipatwa na hofu, uchungu, yeye ndiye nilikuwa nikimpigia kama nilivyokuwa nikifanya kwako. Basi nitalia mpaka nijisikie vizuri. Ndipo ananiaga. Hajawahi kunichoka. Na yeye ndiye aliyeniombea nikiwa nimekata tamaa kabisa. Akaniambia marufuku kukata tamaa, hili tumbo lazima libebe mtoto na mimi ninyonyeshe. Aliniombea kwenye hili gari. Na ni yeye pekee alijua ni mjamzito, mpaka nilipofikisha miezi mitatu ndipo nikamwambia mama. Mungu alinipa Sabrina wakati ule si kwa kumsimamia harusi tu, alimleta kwangu kwa sababu, Willy. Ningechanganyikiwa bila yule mtoto. Kwa hiyo huyu mtoto wangu wa kike, ni Sabrina wangu mimi. Mungu amenikumbuka, na Mungu ni faraja yangu.” Willy akaondoka machozi yakimtoka, akashindwa kuongea.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akaondoa hapo gari na kumpigia simu Sabrina. “Nimekutana na Willy wangu, Sabrina.” Sabrina akaanza kucheka. “Da Pendo na Willy! Anaendeleaje?” “Amerudi kuwa kijana mdogo! Mungu amemkumbuka na yeye. Ana mtoto wa kike na alipata kazi nzuri. Yupo vizuri kwakweli, nimemshukuru Mungu kwa anayozidi kumtendea. Amenisaidia sana hapa Mlimani city.” “Hakika nampigia mama simu kumwambia umetoka kitandani!” Pendo akaanza kucheka. “Mwache bwana. Ataanza kuongea hatutamaliza. Lakini huoni hii safari imelipa?” “Kwa kuwa umemuona Willy?” Sabrina akamuuliza kwa kejeli. “Kumbe! Wewe si nilikwambia ninahamu yakumuona hata akipita kwa mbali?” Sabrina akacheka sana. “Hata unicheke, baba watoto wangu yule. Siachi kumuombea afya njema, wanae waje kumuona siku moja.” Sabrina akaendelea kumsikiliza vile alivyohamasika.

“Da Pendo!” “Kumbe? Na kwa taarifa yako tu, jioni akitoka kazini anakuja na movie tungalie. Lakini Sabrina, sijui nimemsoma vibaya?” “Kwa nini?” “Kama anajutia vile! Sijui mdogo wangu.” “Lazima. Na hata Jack alisema. Hakuna sehemu Willy atakwenda asikukumbuke wewe da Pendo. Umetulia bwana.” Pendo akaanza kucheka. “Kweli tena. Mimi nimekwenda kwenye majumba ya watu dada yangu, kwako kumepoa haswa. Kuna ile hali ya utulivu, lazima akumbuke. Halafu dada yangu wewe mzuri! Mungu alikujalia vitu vyako vizuri vitupu mwilini mwako, hakuna sehemu Willy atakwenda akapata mwanamke kama wewe.” “Bwana amelia!” “Da Pendo!” Sabrina akashangaa. “Sana. Amelia kama mtoto mdogo! Amelia ile yakuumia! Sijawahi kumuona akilia hivyo, wala havifanani na vile vya kwenye msiba wa mama yake. Amelia na kushindwa kujizuia mpaka akaondoka bila kuaga.” “Maskini Willy! Atakuwa anakumiss.” “Sijui Sabrina. Lakini namuombea faraja Willy wangu. Alipokosa, Mungu amsamehe, na amfariji.” Ikamgusa sana Sabrina.

“Una upendo da Pendo wewe!” “Nampenda Willy, Sabrina! Wala sijisingizii. Ni mtu wangu wa miaka mingi. Hata hivyo alivumilia Willy jamani! Alivumilia kupita kiasi. Aliniuguza yule mtu, acha Sabrina. Alikuwa akiniuguza bila kuchoka, maana nilikuwa nikianza kutokwa damu, silali. Kama bomba. Kuishiwa damu lilikuwa jambo la kawaida sana. Alinibeba mno. Tena alinibeba akisimangwa na ndugu zake, lakini hakunichoka Willy. Naumia kuona alichoka mwishoni kabisa.” “Lakini Mungu anamrudisha.” “Haitakuwa kama zamani Sabrina. Willy si mume wangu tena. Anamajukumu ya familia yake sasa hivi. Na sitaki kumbembesha mzigo nikamchosha.” Akaongea kiiungwana Pendo, taratibu tu.

“Lakini unakumbuka nilikwambia mwache Mungu akufute machozi na akupiganie?” Wakacheka sana. “Kwa hiyo sasa hivi nafutwa machozi kiuutuuzima?” “Achana na Mungu aliye hai wewe. Ana mtindo wakunyamaza. Akija kutokezea, mbona masikio yatawasha. Utaitwa heri! Walio kinyume na wewe wanakutafuta.” Pendo akazidi kucheka. “Usifanye mchezo na wakati wa Bwana.” “Kweli Sabrina.” “Sasa wewe kaa mkao wa kupokea na kusamehe. Maana maji yameshatibuliwa, baraka zinamiminika. Watarudi mmoja baada ya mwingine. Kazi yako ni kupokea na kusamehe tu. Wala usifanye moyo wako kuwa mgumu. Wakirudi wengi na ukawapokea wengi, ujue ndio wanavyozidi kukuinua. Maana Mungu anakurudishia waliokuwa kinyume na wewe, kusudi wakuinue.” Pendo akazidi kufurahia.

“Sema tena kidogo.” Sabrina akacheka sana. “Niambie Sabrina. Maana sasa hivi ndio naona unayoongea yanatimia. Zamani nilikuwa nikikuamini kwa imani tu. Hakika sasa hivi ndio naona.” “Sasa ili inoge, ufurahi, fungua mikono, lakini kwa tahadhari. Kila anayerudishwa kwako sasahivi, ujue amebeba kusudi la kukusogeza mbele. Wapokee tu, halafu uone jinsi Mungu atakavyowatumia kukupa mema.” “Yaani mimi nasamehe kwa ajili yangu?” “Kumbe! Yaani wao wanakuona wewe kama mjinga, vile unavyowatangazia msamaha na kuwamwagia upendo, kumbe unajua ni vyombo vilivyosogezwa kwako ili Mungu awatumie, kwa ajili yako wewe mwenyewe.” Wakashangilia wawili hao kwa furaha zote wakipeana maneno ya kishabiki. Wakaongea mengi wakitiana moyo, mpaka Pendo akafika kwake. Wakaagana.

Mtakuja.

A

lichofanya Pendo baada ya kufika kwake, ni kuchukua chakula na kwenda nacho chumbani kwake. Akala akiwa kitandani na kulala hapohapo. Msichana wake wa kazi akaja kutoa vyombo na kumfunika vizuri, akamuacha alale. Ilipofika saa 12 na nusu jioni, Willy akaingia hapo. Msichana wao wa kazi aliyekuwa akiwafahamu wanandoa hao akafurahi sana kumuona aliyekuwa baba mwenye nyumba wake. “Karibu kaka. Ulitususa!”  Willy akacheka. “Mahangaiko ya dunia. Hujambo lakini?” “Sisi wazima. Tunaendelea vizuri. Nipo tu na dada hapa.” “Nashukuru kwa kumsaidia dada yako, Sifa. Umekuwa msaada wakati wote!” Sifa akacheka. “Lakini uliondoka ukatuacha wapekwe! Unaendelea vizuri huko?” “Namshukuru Mungu. Yuko wapi dada yako?” “Yupo tu chumbani. Bibi ameniambia nihakikishe hatoki kitandani, akitoka tu niwapigie.” Willy akacheka. “Karibu ukae nikamwambie kama upo.” Willy akaenda kukaa sebuleni.

Alikuta pako vile vile kama alivyopaacha. Akapotelea mawazoni. Ilikuwa ni ndani ya mwaka tu. Lakini mengi makubwa na mazito yalimpata Willy. Akabaki ameinama. “Dada anaomba uingie ndani.” Sifa akamtoa mawazoni. Willy akasimama. Akaanzia kwenye hicho chumba cha watoto. Kweli kilibadilishwa, kikawa kizuri kweli. Akasimama hapo kwa muda. Akasikia Pendo akimuita. “Willy!” “Nilikuwa naangalia chumba cha watoto. Kimependeza sana. Umefanya kazi nzuri.” “Nashukuru nimepata pia watu wazuri.” Willy akaingia chumbani. Na kwenyewe kulikuwa vilevile kama alivyopaacha. Pasafi, kila kitu kipo vilevile.

Pendo akamuona vile alivyopotelea mawazoni akiangaza macho pale chumbani. “Ona ninavyolala sasa hivi!” Akamtoa huko mawazoni kulikoonyesha kumdhoofisha. Willy akageuka na kucheka. “Kwa nini sasa?” “Mahangaiko tu! Ilimradi kujiridhisha tu nafsi yangu. Hata sijui kama vina saidia au la! Nimebuni mwenyewe sijui hata nafikiriaga nini! Naona sababu yakutokuwa na kitu chakufanya.” “Sasa huumii mgongo?” “Naona maumivu nitakuja kusikia nikijifungua. Lakini kwa sasahivi nafanya chochote kitakachonitunzia wanangu humo ndani. Pole na kazi.” Willy akakaa hapo hapo kitandani. “Asante.” Wakabaki wakiangaliana. Pendo akacheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

  • Willy Amerudi Na Habari Za Mtoto Wa Kike Aliyezaa Zelda. 
  • Ilikuwaje Baada Ya Kuondoka Nyumbani Kwa Wazazi Siku walipoitishwa kikao na baba yao na Zelda kushindwa kutoa jibu la moja kwa moja juu ya ujauzito aliobeba? 
  • Marehemu mama Ngoi aliondoka akiwa ameacha makubaliano gani juu ya Zelda? 
  • Akiwa hana kazi, Zelda alimkataa Willy kwa jeuri sana. Jeuri yake anatoa wapi?
  •  Yote Na Mengine Mengi Yaliyojiri siku ile Baada Ya Mzee Ngoi Kuitisha Kikao Wanae, Yatajibiwa na siri zilizokuwa zimefichwa juu ya mahusiano hayo ya usaliti pia zitafichuliwa,

 Sehemu Itakayofuata….

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment