Mimba ya Zelda ilipofika miezi nane karibu tisa, ndivyo maelewano yakazidi kupotea kabisa kati yao wawili. Hakuna analozungumza Willy kwa Zelda likaishia pazuri. Willy alikuja kugundua kuwa alishaacha kazi, tena alisikia kutoka kwa mdogo wake, Prisca. Prisca alifika hapo nyumbani kusalimia zaidi baba yake, akaongea tu vizuri. “Sikujua kama ulishaacha kazi Zelda!” “Na mimi sikujua kama natakiwa kukuaga wewe!” Akajibu Zelda bila wasiwasi. Pakazuka ukimya, Willy akashangaa sana. Sasa pesa anapata wapi huyo Zelda! Maana alizidi kupendeza na manunuzi hayakukoma. Akiwepo nyumbani, utamkuta kwenye kochi muda wote msafi na kucha ndefu akimtaka msichana wa kazi amtumikie kwa hili na lile.
Huku kwa Pendo.
Wakati Zelda anafikisha mimba ya miezi nane kwenda 9, na Pendo naye mimba imeshakuwa ya miezi minne. Tumbo la mapacha lilishaanza kuonekana lakini bado hakuwa amewaambia watu wengine mbali na wanyumbani kwao tu, nao akaomba wasitangaze. Kwa hiyo akawa kama mtu wa kujificha na hivi ilishajulikana aliachwa na Willy sababu ya kutozaa, hakuna hata aliyemdhania ni ujauzito. Watu wakajua ameamua kujiachia tu anenepe sababu ya mawazo ya kuachwa. Basi pole za kuachika hazikukoma kila wamuonapo.
Akaona isiwe shida, akaacha kujitokeza mtaani. Usingeweza kumuona tena mtaani. Ni kazini ambako anatulia mezani kwake, kisha nyumbani muda wote. Akitoka ni kliniki nakufanya manunuzi madogo madogo tena yale ya muhimu ambayo mama yake ambaye ndiye aliyegeuka mtu anayemtumikia, akisahau. Maana mama yake ndiye aliyekuwa akimsaidia kumfanyia manunuzi ya hapo nyumbani kwake na yake binafsi. “Sitaki aibu nyingine mama. Kama ni watoto, waacheni watu waje wawaone. Lakini sio kutangaza ujauzito, halafu waje watoke, niwape watu sababu nyingine ya kunisimanga zaidi.” Pendo akamsisitiza zaidi mama yake aliyekuwa amefurahi kupitiliza, juu ya huyo kiziwanda wake kushika mimba. Basi, mama Kenton kimya kama huyo Pendo mwenyewe. Kunyamaza kwa huyo mama mwenyewe si tatizo kama Pendo, akaelewa na kutunza hiyo siri. Ikawa tena jambo hilo lililongojelewa kwa miaka mingi sana, tena kwa hamu kubwa, likaendelea kuwa siri kubwa iliyoshikiliwa na maombi ya hofu.
Mwana Kulitafuta….
H |
uku kwa Willy siku moja usiku aliamshwa na njozi mbaya. Akakaa kitandani, akaamua kwenda kunywa maji jikoni. Hakuwa akilala chumba kimoja na Zelda. Aliamua kumpa nafasi akijiambia pengine akijifungua, atatulia. Maana alijawa majibu mabaya kweli! Kila mtu alimjibu vibaya, vile atakavyo yeye. Akaamua kwenda chumbani kwake kumtizama tu, kwa mapenzi, kuonyesha anamjali. Akabeba glasi ya maji, akapandisha ngazi mpaka chumbani kwa Zelda. Hakumkuta. Ila simu yake ilikuwepo hapo. Na kitanda kilionyesha wazi alikuwa amelala mtu. Akaingia chooni hakumkuta. Akabaki amepigwa na butwaa. Maana alipotoka jikoni, alipita sebuleni, hakuwepo huko. Akaacha hiyo glasi ya maji pembeni ya kitanda, juu ya meza, akashuka tena chini. Akaangalia milango ikawa imefungwa. Akakumbuka hajaangalia chooni.
Akaamua kurudi juu akiwa ameshaingiwa na wasiwasi. “Itakuaje awe alizimia wakati yupo huko?” Akajiuliza Willy wakati akiongeza mwendo kurudi juu kwa Zelda. Moja kwa moja mpaka chooni. Hakumkuta. Akarudi tena chumbani kwake, akamkuta amekaa kitandani anamwangalia. Willy akashituka sana. “Ulikuwa wapi!?” “Kwani vipi?” Zelda akamuuliza. “Nimeingiwa na wasiwasi Zelda! Hukuwepo hapa chumbani, sebuleni, jikoni na chooni pia hukuwepo, na milango ilikuwa imefungwa!” “Kwa hiyo una kazi ya kupitisha rokoo usiku!?” Zelda akamuuliza kwa kumshangaa sana.
“Ni nini kinaendelea Zelda? Mbona kama unanitafutia sababu?” “Wewe vipi Willy! Nakutafutia sababu kwa lipi!? Kwani mimi mkeo au hawara yako!?” Willy akashituka sana. “Unashangaa nini? Nakuona unanifuatilia, sina raha! Aliyekwambia kuniona na mimba ndio iwe sababu yakunifuata nyuma ni nani?” Willy akabaki ametoa macho. “Sasa unashangaa nini wewe? Nini cha ajabu? Au labda nikuulize Willy, wewe ulitegemea nini kutoka kwangu? Kwamba kwa kuwa wewe umeshindwa ndoa yako, basi uje kwangu uanze tu! Ushindwe na mwanamke uliyeishi naye miaka zaidi ya 10, uje unikurupukie mimi usiyenijua! Utaniweza wapi? Hujui mipango yangu wala hujui ninawaza nini? Hufahamu chochote juu yangu, eti leo unataka ujikute tu unanitawala! Haiwezekani Willy! Mimi sio mkeo, na wala sina mpango wa uje kunioa. Naomba hilo tuwekane wazi. Kama wewe ni mtu wakushindwa kusimama na watu wakati wa matatizo, basi sio mimi. Umeshindwa na mkeo, tafuta mwanamke mwingine. Usitake kuniletea tabia za ajabu! Kwanza ondoa nguo zako chumbani kwangu, na usiwe unaingia hapa bila ruhusa.” Willy akashangaa Zelda anasimama, akafungua kabati aliloweka nguo zake na kuanza kumtupia nguo zake sakafuni. Viatu anatupa kimoja baada ya kingine mlangoni.
“Viatu vyako vinatangulia nje, utavikuta huko. Changamsha mkono, usiniletee upuuzi mimi. Usiku usiku kwenye vyumba vya wanawake, nikipiga kelele umenibaka! Si utafia jela wewe!” Willy akazidi kushangaa. “Tena na hivyo hujalala na mwanamke muda mrefu, lazima uhukumiwe kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka.” Zelda akamtolea vitu vyake vyote na kuvitupa sakafuni. Akaanza kusukuma kwa miguu kuvitoa nje. “Tena uondoke hapa kabla halijakupata la kifungo cha maisha. Sasa kama huniamini, kesho ikukute hapa.” Willy hakuamini.
Akatoka hapo akaenda kumgongea baba yake. Akatoka. “Ni nini tena usiku usiku?” Mzee Ngoi akauliza kama anayesumbuliwa. “Naomba uje hapa chumbani kwa Zelda tuzungumze.” Wakaongozana. Akagonga mlango, Zelda akafungua. “Vitu vyako vyote hivyo hapo nje Willy. Naomba niache nipumzike.” Akashangaa anajibu hivyo mbele ya baba yake bila woga. “Unamsikia lakini baba!?” “Hukusu nini?” “Hivi Zelda anavyonifukuza hapa nyumbani kwetu!” Akaweka msisitizo kwa baba yake. “Jaribu kuwa muungwana Willy! Huyu binti ni mjamzito. Alikuwa hapa tokea mama yako yupo! Akampa hiki chumba wakati wewe ukiishi na mkeo. Iweje leo ushindwe wewe kule, uje utake kumsumbua yeye huku!” Willy akawa kama amemwagiwa maji ya baridi.
“Unasababisha kutokuwa na amani nyumbani kwangu bila sababu, wakati wewe ndiye mgeni humu ndani! Sisi tuliishi humu ndani na mama yako akiwepo, hapakuwepo na fujo za usiku usiku! Sasa wewe tokea ushindwe na ndoa yako, upokonywe nyumba na mkeo, umekuja hapa kuomba hifadhi, tumekupokea vizuri tu, lakini umegeuka kuwa mbambe bwana! Utafikiri wewe ndiye mwenye nyumba wakati mwenyewe bado nipo! Unataka kunipokonya mji wangu nikiwa hai! Kwa nini mnakosa uvumilivu! Nimebakisha miaka mingapi hapa duniani, kiasi cha kuwa na haraka kiasi hicho!” Willy hakuamini. “Usiku usiku unaniamsha nikiwa nimelala, huku ukijua wazi kwa umri wangu nahitaji mapumziko! Halafu unafanya fujo kwa mama mjamzito hivyo! Unataka nini kitokee? Kwa nini unakosa utu na aibu kwenye miji ya watu?” “Samahani sana baba. Sikukusudia ku...” Willy akasita. Akataka kuzungumza tena akasita.
Zelda akafyonza na kufunga mlango kwa nguvu. Baba yake naye akaondoka akilalamika. “Lazima tukae kikao cha familia, tuzungumzie hili jambo. Huwezi kunivunjia heshima nyumbani kwangu!” Mwili mzima wa Willy ulikuwa ukitetemeka. Akakusanya vitu vyake vyote na kuweka kwenye gari yake. Usiku huo anakwenda wapi? Ikawa hotelini tu. Alizunguka huo mji usiku huo mpaka akachoka. Kila anapokwenda kwa bei nafuu aliambiwa kumejaa, labda arudi mchana. Akatafuta sehemu akaegesha gari, akabaki garini. Kufunga na kufungua, Willy aliyekuwa akiheshimika kwenye jamii, yupo mtaani, hana pakwenda, amefukuzwa nyumbani kwa aibu kubwa sana. Alibaki ametoa macho, asiamini yanayomtokea.
Mpaka inafika saa nne asubuhi, hata usingizi wa kusinzia hakuna. Akaona simu ya kaka yake ikiingia. Akapokea. “Kuna kikao cha dharula hapa nyumbani kwa wazazi sasa hivi. Baba ametuita watoto wake wote, haraka sana. Usikose tafadhali.” Akakata. Kwa maana nyingine yeye kaka mkubwa ameshawasili pale nyumbani. Willy hakuamini kama baba yake anatekeleza aliyoyasema usiku uliopita. Akatamani asiende ili asije kudhalilika zaidi, lakini alikuwa na maswali aliyohisi mbele ya ndugu zake pengine yanaweza kujibiwa na Zelda. Akatoa gari hapo alipokuwa ameegesha akarudi mpaka nyumbani kwao Masaki.
Alikuta ndugu zake wote wamefika wapo nje wakisemezana. Yaani kama ndio wamefika hapo. Willy akawasalimia. “Wewe vipi?” Prisca akamshangaa. Willy hakujibu, kaka yao akatoka na kuwaambia baba yao anawasubiri ndani, waingie. Wakaongozana mpaka ndani. Willy yeye alifika akakaa na kuinama. “Tumefika baba.” Kaka mkubwa akaanza. “Nitakwenda kwenye pointi moja kwa moja.” Mzee Ngoi akaanza. “Najua zipo fikra za kurithi. Kuwa nikifa, mrithi mali zangu.” Watoto wote wakashangaa. “Msishangae wakati niliwaona jinsi mlivyokuwa mkipigania mali za mama yenu, siku ile hapa, mlipotoka kumzika tu.” Akaendelea mzee Ngoi.
“Nyinyi wote na wake zenu nyinyi mlikaribia kuuana hapa kwa ajili ya mali za mama yenu alizotafuta kwa jasho lake mwenyewe.” Wote wakabaki kimya. “Siku ile nilinyamaza nikiwafikiria sana nyinyi watoto ambao wote niliwasomesha bila shida. Nikajiuliza, ndio mmemzika tu mama yenu, hata siku haijaisha, mnapigania mali, tena ambazo mwenyewe alitoa wosia! Mkasema wazi ni nani alisema apewe hizo mali! Wenyewe mkasema ni Zelda. Wasiwasi ukaniingia sana siku ile juu yangu mimi mwenyewe, nikabaki kimya kabisa nikiwafikiria nyinyi watoto wenye uchu kama chui! Hivi mtaweza kunizika nyinyi au ndio mtauana kwa kung’angania mali zangu wakati maiti yangu ipo ndani!” “Ukizungumza hivyo baba nahisi unakosea.” Kaka yao mkubwa Patric, akajaribu kuingilia.
“Acha kabisa kuniingilia Patric. Huu ni mji wangu na mimi ndiye niliyewaita.” Akampandishia mwanae mkubwa mbele ya wadogo zake. “Sio mke wako alifanya fujo hapa akitaka kumdhalilisha huyu binti ambaye aliachwa hapa nyumbani na mama yenu, tokea ni mgonjwa! Nyinyi wote mlikuwa mkilalamika mpo busy na majukumu wakati huyu binti akihangaika mchana na usiku akitulea sisi wazazi wenu. Usiku ndiye aliyekuwa akihangaika na mama yenu wakati nyinyi mmelala majumbani kwenu! Nikawashangaa sana nyinyi wawili. Stella na Prisca, safari ya India ikafika, bila aibu eti gafla mkaonekana mnayo sasa nafasi ya safari ya kwenda India, huku mkitegemea pesa yangu! Mwishoe ukajidai wewe Stela kwa kuwa ndie mkubwa, eti uende naye! Mama yenu akijua mioyo yenu, akataka kwa wazi kumkabidhi mali zake mtu aliyejua alimjali katika ugonjwa wake, ndio eti mnapigana hapa nyumbani kwangu! Nani kati yenu na wake zenu, aliyeacha kazi na kuja kumuuguza mama yenu hapa?” Kimya. Mzee Ngoi akawabana kwelikweli.
“Mnakuwa busy kwetu kwa elimu tuliyowapa sisi wenyewe! Lini mtakuja kulipa fadhila kwetu? Mmezembea mpaka mama yenu amefariki, mkaishia bado kuja kugombea mali zake! Aliyekuwa akimuhudumia, mmempa sijui pochi sijui kitu gani, ambacho hata hakieleweki! Mmegawana nyinyi na wadogo wa marehemu waliokuwa wakijua wazi dada yao anaumwa hapa, lakini hawakuweza kumuuguza ila kuja kuchukua mali! Willy ameshindwa na ndoa yake, nimempa hifadhi hapa, gafla yeye ndio anageuka kuwa mwenye nyumba hii ndani ya mji wangu!” Willy akanyanyua kichwa akamtizama baba yake.
“Usiku kucha tunashindwa kulala sisi, kwa fujo zake yeye! Anataka kutawala kwenye mji wangu wakati mimi nipo hai! Ameshindwana na mkewe, anakuja kufanya fujo kwa binti mjamzito!” “Hapo sijaelewa baba, binti mjamzito si ni Zelda au tunamzungumzia nani?” Stella dada mkubwa akauliza. “Maana kama ni Zelda, wote tunajua Willy yuko hapa sababu ya mke wake, Zelda.” “Hee!” Zelda akashituka sana. “Mimi ni mke wa Willy kutokea lini!?” Zelda akashangaa sana. “Si nilikwambia dada Stella.” “Subiri kwanza Zelda. Kwamba unataka kusema wewe haupo hapa sababu ya Willy?” “Acha maswali ya kipuuzi Stella.” Mzee Ngoi akaingilia.
“Huyu Zelda alikuwa hapa, mama yako alimuachia mji tokea Willy yupo na mke wake. Au nyinyi mmesahau leo kwa sababu mama yenu wakumtetea huyu Zelda hayupo?” “Baba!” “Nyamaza! Pumbavu kabisa wewe Prisca. Tena wewe ndio mnafiki mkubwa wakuhamisha maneno humu ndani. Kama nyinyi ni wa kweli, huyu Zelda alikuwa humu ndani akituhudumia mimi na mama yenu, kipindi si Willy yupo na mkewe? Mara ngapi Willy alikuwa akifika hapa na mkewe, wakati Zelda yupo hapa?” Wote kimya. “Swala la ujauzito wa Zelda hajawahi kuficha huyu binti. Amekuwa muwazi hata kwa mama yenu, na mama yenu akaliheshimu hilo. Akawa akihangaika na shuguli za humu ndani na ujauzito wake, huku akimuuguza mama yenu. Nyinyi mnaingia nakutoka bila aibu! Sasa eti leo Willy anashindwa na ndoa yake, wewe Stella bila aibu siku ile nakushangaa, unamkabidhisha huyu binti kwa mtu kama Willy ambaye ameshindwa na mwanamke mtaratibu yule!” Wote wakashangaa wasiamini.
“Yaani nyinyi wema wenu, kwa yote aliyowafanyia huyu binti kumlea mama yenu mpaka kifo, nyinyi mkija tu kumtembelea kama mnakwenda kwenye kituo cha utalii, moja ya vivutio mlivyochagua nyinyi, mkafanikiwa kukutwa na mauti ya mama yenu mkiwa naye, hamuoni aibu, mnapewa pole yakuuguza wakati aliyeuguza ni huyu binti! Shukurani yenu eti mnamuozesha kwa huyu ndugu yenu ambaye hata pakulala yeye mwenyewe hana!” Willy akajisikia kama yupo uchi mbele yao.
“Mnataka kumtoa huyu binti hapa alipoachwa na mama yenu, mnataka akaanze kumangamanga mtaani na mpuuzi huyu ambaye hata kijiko chakulia chakula chake yeye mwenyewe hana! Utu wenu na fadhila zenu ziko wapi nyinyi watoto mliokosa shukurani?” Kila mmoja wao alikuwa akitetemeka kwa hasira, ila kushindwa chakufanya. Walimjua baba yao ni mkorofi haswa, na jeuri ya pesa alikuwa nayo.
“Sasa kuanzia leo, anayetaka kuja hapa nyumbani, aje kwa heshima zake na kuuacha mji wangu kama ulivyoachwa na mke wangu kwa makubaliano yetu. Ukiona unashindwa kuheshimu, tulieni makwenu ambako huko huwa mnajificha mkijidai mpo busy, mpaka muwe na shida na pesa, ndipo mnakuja hapa. Mambo yenu yakiwaendea vizuri, hamji. Sasa ni marufuku kuja hapa na maneno ya uchochezi. Unanisikia wewe Prisca?” Prisca kimya machozi yakimtoka kama maji.
“Mimi naomba kuuliza swali dogo tu kwa Zelda, kabla sijaondoka. Na ninaomba niulize hapa mbele ya wote.” Willy akajikaza na kuuliza. “Unataka nini?” akauliza Zelda kwa jeuri. “Mtoto uliyebeba ni wangu au si wangu?” “Wewe ulipokuwa ukija hapa na mkeo, nilikuwa nikikuuliza kama umelala na mkeo au hujalala naye?” Wote wakashangaa. “Mbona ni swali dogo sana Zelda? Kwa nini unashindwa kujibu?” “Kwa sababu unataka kunifanya mimi mjinga Willy. Unamuulizaje mtu mzima uliyemkuta ukubwani na maisha yake na wewe ulikuwa na yako, eti mimba ni yangu au la! Huko si nikuniingilia undani? Muda wote huo ulipokuwa na mkeo, mbona usiniulize hilo swali? Leo umeshindwa huko, ndio unataka kuniparamia mimi! Ukome Willy.” “Hakika mimi simuachi huyu mtoto!” Stella akasimama, baba yake naye akasimama.
“Ukimgusa tu huyu binti Stella, hapa nisiwahi kukuona, na hata ukisikia nimekufa usikanyage msibani. Ufute jina la Ngoi kwenye maisha yako. Sasa kama wewe ni mbabe, mshike.” Zelda akakusanya mikono juu kifuani, nyusi juu, akatingisha mguu akimtizama Stella. “Nyinyi ndio mnataka kujidai mnaakili kumzidi mama yenu aliyemuamini huyu binti na huu mji! Kama mngekuwa mnataka, mngewahi kabla hajafa. Pumbavu kabisa.” Mzee Ngoi akawatukana bila kumumunya maneno. Stella alishikwa hasira akashindwa kubaki hapo. Akachukua pochi yake na kuondoka. Willy akafuata, akaja Prisca na kaka zake. Wote wakaondoka na kuwaacha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Willy aliondoka pale haamini macho na masikio yake. Mama aliyemsikiliza ameshakufa. Hana mtoto wala mke. Akabaki ameduaa kwenye mataa, hajui aende wapi na mizigo yake kwenye gari. Miezi michache tu iliyopita, japokuwa hakuwa na mtoto lakini alikuwa akiheshimiwa. Mume mwenye mke anayeheshimika kwenye jamii na mji wake. Leo anatukanwa vibaya vile na kuitwa mpumbavu! Willy hakuamini kama ni yeye na mambo yamembadilikia vibaya kwa kiasi kile. Ametoka kudhalilishwa kwa ukweli mtupu!
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kaburi walilochimba, nani anatumbukia? Usikose kufuatilia kujua mkasa mzima wa Zelda! Jeuri anaitoa wapi? Willy alijichanganya vipi?
Pendo na Mapacha wake?
ITAENDELEA…
0 Comments:
Post a Comment