Baada ya
talaka yake, Willy akaamua kuanza majukumu ya ubaba kwa roho moja. Alipomalizana
na Pendo asubuhi hiyo ya talaka yeye alirudi kazini mpaka jioni alipoamua
kumfuata Zelda nyumbani kwao. Bado alikuwa akiishi hotelini ambako alihamia
hapo tokea aondoke na mizigo yake kulikokuwa nyumbani kwake na Pendo. Na Zelda
naye bado alikuwa akiishi nyumbani kwao, yaani kwa mzee Ngoi, hakuwa ameondoka
tokea alipohamia wakati wa uhai wa mama yao.
Alifika
jioni hiyo baada ya kutoka kazini, akaenda hotelini akabadili nguo za kazi
ndipo akaenda huko kwao. Alimkuta Zelda na baba yake hapo sebuleni pamoja na
dada yake mkubwa Stella. Akawaambia ndio ameondoka rasmi kwenye maisha ya
Pendo. Dada yake akampongeza kwa kitendo cha kijasiri alichochelewa kukifanya
kwa muda wote. Akamwambia hata mama yao huko alipo, atakuwa na furaha sana.
Akawatakia mwanzo mwema yeye na Zelda, Stella akaondoka baada yakuzungumza na
Zelda na kumpa maagizo ya hapo ndani.
Willy
alipoaga kuwa anaondoka na Zelda, wataelekea hotelini kwa muda mpaka wapate
nyumba ya kupanga, kwa kuwa amemuachia mkewe nyumba kwa makubaliano ya yeye
kuchukua eneo la Kigamboni, ndipo baba yake akawaambia hakuna sababu ya kwenda
kupanga wakati wanatarajia mtoto na Willy anataka kuendeleza ujenzi huko kwenye
eneo alilochukua baada ya kuachana na Pendo, akawaambia waanzie maisha hapo
kwake. Na kweli jumba la mzee Ngoi lilikuwa kubwa haswa halafu mama amefariki.
Yupo Mzee Ngoi tu na msichana wa kazi. Willy akaona wazo si baya. Akamshukuru mzee,
akaenda hotelini kuchukua mizigo yake.
Willy
anahamia hapo nyumbani kwao kuishi kama mgeni lakini si Zelda. Hata kipindi cha
uhai wa mama Ngoi, Zelda alikuwa akienda hapo na kulala mara nyingi tu
akimuuguza. Kwa hiyo wote walijua Zelda yupo hapo kumsaidia kwa karibu mama yao
aliyekuwa mgonjwa. Hata alipokuwa akilazwa, basi Zelda akawa kama mtoto wa hapo
nyumbani. Mpeleka vyakula hospitalini, na kusaidia mambo ya hapo ndani. Kwa
hiyo wakati huo Willy anahamia kuishi naye hapo kama mkewe, Zelda alishakuwa
mwenyeji haswa. Hata Willy alifanya kuhamishia nguo zake kwenye chumba ambacho
tayari alikuwa akiishi Zelda ndani ya hilo jumba.
Mama
mwenye nyumba amefariki, mawifi wanampenda, basi Zelda akawa ndio mama mwenye
nyumba hapo. Anajua kunapikwa nini na kunaliwa nini kwa muda mrefu sana. Alikuwa
akimtunza Mzee Ngoi tokea mkewe yupo hai ni mgonjwa. Kilichoongezeka ni Willy
tu. Hapakuwa na jipya. Akawa mwanamke wa wanaume wawili hapo ndani. Baba yake Willy
yaani mzee Ngoi na mumewe sasa ambaye ndio Willy. Mimba hiyo ikalelewa kwa
tahadhari yote, kila jicho likawa hapo.
Mzee
Ngoi alikuwa mfanyabiashara na shuguli zake. Willy na Zelda wote waajiriwa.
Zelda alikuwa mwalimu kwenye shule ya Internatiol school iliyopo Mbezi. Kabla
hata ya mwezi wa pili kuhamia hapo kuisha Willy akamuona Zelda anatoka jumamosi
hiyo kwenda saluni na gari ya mama yake. Ikamsumbua kidogo. Hiyo gari ilikuwa
imefungiwa kwa muda mrefu tokea huyo mama ameanza kuugua. Na ilikuwa ni gari ya
thamani sana na bado mpya kabisa. Aliiagiza mama Ngoi mwenyewe alipoanza tu
kuugua na ilipofika nchini, aliiendesha muda mfupi sana, na kuifungia kwa baada
ya kuzidiwa. Akabaki akiendeshwa na watu wengine na magari yao akipelekwa zaidi
hospitalini maana alibaki mtu wa kitandani tu kwa muda mrefu kabla mauti kumfika.
Zelda aliporudi akamuuliza. “Baba amenipa.
Ameniambia naweza kulitumia tu. Au unaona shida?” Zelda akauliza. “Hapana,
nilishangaa kuona unaondoka nalo bila taarifa!” “Wewe ulishangaa nini wakati
limekaa tu hapo ndani!?” “Sina nia mbaya. Lakini kuna utaratibu wa kugawa vitu
vya marehemu.” “Si ulisikia siku ile kutoka kwa kina wifi Stella wenyewe kuwa
mama anataka kwa asilimia kubwa mimi ndio nichukue vitu vyake? Sasa kila mtu
ana gari, ubaya uko wapi na mimi kuwa na gari kuliko haya maisha ya kupewa lift
kila siku!?” Zelda akawa kama anamshangaa Willy, na Willy naye anashangaa baba
yake anawezaje kufanya maamuzi makubwa vile bila kumshirikisha yeye au watoto
wengine! Akanyamaza.
Baba
yake aliaga anasafiri siku hiyo ya jumamosi asubuhi, kwenda Mwanza kikazi.
Ilipofika jioni baada ya kula wakati wapo kitandani Zelda akaanza. “Kesho
asubuhi nakwenda kwa mama. Kuna sehemu alitaka nimsindikize. Nahisi nikichelewa
naweza kurudi jumatatu.” “Sehemu gani hiyo itakayokushinda kurudi kesho hiyo
hiyo?” “Kuna shuguli ya mtoto wa rafiki yake Segera.” “Unamaanisha Tanga!?”
“Ndiyo, kwani vipi?” Zelda akauliza kwa ukali kidogo. “Kwa nini unapanga safari
za mbali na ujauzito huo?” “Kwani mimba ugonjwa! Hee! Acha woga bwana Willy.
Tutakuwa hatuna maisha basi! Unataka ndugu wanione nimebadilika baada ya kuhamia
hapa? Nitatengwa na ndugu bure sababu ya mimba. Najua hukuzoea haya maisha
sababu ya mwanamke uliyekuwa naye mwanzo. Na ndio maana hata mama yako alikuwa
hampendi. Hajui kujichanganya na watu. Anakuwa na kama mambo ya kizungu fulani
hivi! Sisi ni watanzania Willy. Ndugu ndio utajiri wetu. Hatuwezi kutenga ndugu
na kuwaonyesha sisi tupo bora zaidi yao.” Willy akanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa
hiyo hapo alipolala Willy, hakuwa mume wa mtu kihalali. Alitaka kumsoma Zelda
tabia ili aone kama ni mwanamke wa kuoa au la. Lakini hata yeye akajua
hatamtendea haki kama atamlinganisha na Pendo. Pendo alipitiliza kimaadili.
Mtulivu haswa. Halafu walishaishi muda mrefu sana mpaka wakazoeana mapungufu
yao, kiasi ya kwamba hata ukiwauliza kila mmoja mapungufu ya mwenzie, wanaweza wakashindwa
kuyataja. Ni Willy na Pendo! Hata wao walijua wanapatana. Tatizo likawa mtoto
tu.
Willy akalala hapo pembeni ya Zelda ambaye
alikuwa akiendelea kuperuzi simu yake, kitu ambacho kilikuwa kigeni kwa Willy.
Alishazoea wakiwa kitandani, simu zinawekwa pembeni, inabakia wao tu hapo
kitandani. Lakini kwa Zelda ikawa kama ndio kunapambazuka! Akajiambia na hilo
nilakulichukulia.
Asubuhi
na mapema alimuacha Willy kitandani, akahakikisha msichana ameandaa kifungua
kinywa. Akala kwa haraka. Ilikuwa saa moja kamili, Willy akaangalia saa wakati
Zelda anamuaga akiwa anapochi kubwa mkononi kuashiria wazi si wakurudi siku ile.
Kwa hakika alikuwa amependeza. Willy akabaki akimtizama wakati anatoka. Akabaki
akimtafakari.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ni
kama amebadilika gafla na kuwa na pesa nyingi! Akamfikiria. Zelda alikuwa
msichana wa kawaida tu. Mwalimu shuleni kwa mtoto wa mdogo wake Willy. Mziwanda
wa hiyo familia. Prisca. Na Prisca kipenzi cha mama ndiye aliyemtambulisha
Zelda hapo nyumbani kwao baada yakuona mapenzi ya Zelda kwa mtoto wake
huko shuleni yamezidi, akajua atamfaa Willy, kaka yake. Akampanga
mama yao mpaka mama Ngoi akaona wazo lake sio baya. Pendo anaweza kupinduliwa
tu. Kwanza hawakuwa wakimpenda huyo Pendo, halafu hazai. Ndio
mpango wa kumuunganisha Zelda kwa Willy ukaanza. Prisca akiwa ndiye ameshikia
bango kuvunjika kwa ndoa ya kaka yake, ili Zelda aolewe yeye. Kwa asili Prisca
na Stela walikuwa wakorofi haswa. Watoto wa kike kwenye hiyo familia walikuwa
wakorofi kuliko hao kina kaka watatu.
Mbio za Sakafuni.…
Jumapili
hiyo asubuhi Willy akaachwa hapo kitandani akifikiria mpaka akarudi tena
kulala. Kwenye majira ya saa nne asubuhi akaamka, akawa tu yupo hapohapo
nyumbani kwao. Ilipofika mida ya saa sita mchana, mdogo wake Zelda wa kiume
akaja pale kumuulizia Zelda. Willy akamwambia msichana wa kazi amkaribishe
ndani. Ilikuwa mara yao ya kwanza hao mashemeji kukutana. Wakasalimiana akamwambia
anaitwa Paul, anasoma shule ya bweni. Alikuja kuomba ada kwa Zelda, na
anatakiwa kurudi shule siku ileile akasema ndio maana yupo pale hakwenda
nyumbani kwao.
“Mama
ameniambia nije kwa dada Zelda.” Willy akashangaa kidogo. “Umezungumza na mama
leo?” “Yeye ndiye aliyenielekeza hapa. Mimi nilikuwa nikipafahamu kule
alikokuwa akiishi dada zamani, Keko. Akanielekeza hapa na kuniambia sitapotea,
nije tu.” “Lini hiyo?” Willy akataka uhakika. “Unamaanisha nini!?” Akawa
ameshamchanganya na Paul. Maana Paul alihisi amemueleza kila kitu kwa wazi tu.
“Kuzungumza na mama.” “Ndiye amenielekeza kwa simu mpaka hapo getini! Mimi
nilikuwa sipafahamu kabisa hapa.” Paul akaweka msisitizo akiwa kama hana
uhakika tena na jinsi gani yakumuelewesha huyo shemeji mtu.
“Kwani
anarudi saa ngapi?” “Sijui. Umejaribu kumpigia?” Willy akauliza. “Simu yake
haipo hewani. Mama naye amejaribu, hajampata na anasema hata ujumbe
haujaonyesha kufika.” Na Willy naye akajaribu kumpigia, hakumpata. Paul
akasubiri hapo mpaka saa 10 jioni, ndipo akamuona dada yake yupo online Whatsapp. Akampigia kwa
haraka. Alichosikia Willy ni matusi kutoka kwa Zelda akimgombesha sana mdogo
wake. Akamuona Paul ananyanyuka, na kuondoka hapo bila yakuaga, simu masikioni.
Willy akawa hajaelewa. Alimkarimu vizuri tu Paul, iweje leo aondoke bila
yakumuaga! Willy akabaki akifikiria huku akijiuliza ni nini kinaendelea? Zelda
aliaga anasafari na mama yake, mama yake naye anamtafuta! Akanyamaza.
Kufika
saa tatu usiku Zelda akarudi akiwa amekasirika karibu kupasuka. Alikuwa amevuta
mdomo kama aliyetayari kwa lolote. Akaelekea chumbani kwao moja kwa moja. Willy
akamfuata. “Kwema?” Akauliza vizuri tu. “Kwema, kwani vipi?” “Nauliza tu Zelda.
Mbona kama umekasirika wakati nafikiri mimi ndio nilitakiwa nikasirike kwa
kilichotokea leo?” “Nisikilize Willy, sijui ulikuwa ukiishi maisha gani
mwanzoni, lakini ninachojua ulikuwa na mimi wakati na wewe ulikuwa na mtu wako.” “Mke wangu.” “Ewaa! Tulikuwa
tukikutana, unakaa kidogo tu unamuwahi mkeo. Nilishawahi kukulalamikia?” Willy
akashangaa sana.
“Jibu?”
“Sasa huo mfano unaendana vipi na hili lililotokea leo? Umenidanganya Zelda!”
“Sikukudanganya, ila nilibadili mawazo. Nikaamua kwenda kwenye shuguli zangu
nyingine, nisiende na mama. Tatizo liko wapi? Siruhusiwi kubadili mipango?”
Zelda akamjia juu. “Ulinikuta na mipango yangu, na wewe nilikukuta na mipango
yako. Nikaheshimu mipango yako bila kukuweka chini kikao na kukuhoji kama hivi.
Leo unapata wapi haki yakunihoji mimi kama mtoto mdogo au kulalamika?” Willy
akakamatwa pabaya sana, akanywea kidogo.
“Naomba
unisahihishe Zelda, nakuhisi kama umebadilika sana!” “Kivipi?” Zelda akauliza.
“Sijui! Lakini japo sikuwa nikikufahamu sana zamani, lakini hivi ulivyo sasa,
sivyo mwanzoni ulivyokuwa.” “Kama ulivyosema, hukuwa ukinifahamu na pengine
ndio maana ulinichukulia poa.” “Unamaanisha nini Zelda!? Mbona kama
nilikuheshimu sana tu!” Akaongea kwa mshangao mkubwa Willy. “Sijui nyinyi mama
yenu aliwafundisha heshima ni nini, lakini wote nyinyi, mimi siwaelewi.” “Na
nani tena!?” “Nimechoka Willy, nataka kulala. Sina muda wa kesi. Upo hapa kwa
hiari yako. Sijawahi kukudanganya kwa lolote, sijawahi kukurubuni na wala mimi
sina shida na pesa zako kama mwanamke wako aliyekupokonya nyumba.” Willy
akazidi kuchanganywa.
“Wewe
unazungumza nini Zelda?” “Usichoelewa nini? Mwanaume mzima unapokonywa nyumba,
unahamia kuishi kwa baba yako! Yaani unaishi kwa mwanaume mwenzio! Unategemea
tuishi hapa mpaka lini?” “Wewe ulidhania nikiachana na mke wangu nimpokonye
nyumba, halafu sisi ndio tuhamie pale!? Ndivyo ulivyotegemea!?” “Yeye mgumba,
ha…” “Usimuite hivyo. Tafadhali sana.” Willy akamuwahi. “Hata mama yako
aliniambia unajaribu kukwepa ukweli. Mwanamke wako ni mgumba, mgumba
tu. Ukubali ukatae. Ndio ukweli wenyewe huo. Inawezekana Mungu ameiona roho
yake mbaya na mabaya aliyokuwa akimfanyia mama aliyemzalia mume, ndio maana
Mungu akaona na yeye amnyime mtoto, kumkomoa.” “Unazungumza nini wewe
Zelda!?” “Unafikiri dada zako walikuwa wakinificha? Mama yako anakufa huku na
yeye akinionya niwe makini na huyo mwanamke wako. Wote wanajua amekushika
masikio. Mwanaume mzima umerudi kuishi kwa baba!” Willy akakaa.
“Kwa
hiyo haya yote unaongea kwa hasira ya mke wangu kuchukua nyumba?” “Utajijua
mwenyewe. Mimi sijali, ila jua maisha yangu yanaendelea kama kawaida. Usifikiri
utanirudisha nyuma kimaendeleo.” Zelda alionyesha wazi hababaishwi. Akavua nguo
palepale na kuelekea bafuni. Willy akabaki akishangaa. Jeuri kubwa vile anaitoa
wapi! Akamuhisi kama anatafuta sababu ya kuachana. Lakini Willy akajiuliza, na
ile mimba na mshahara wa ualimu, anafikiria ataishije! Akahisi labda ni
ujauzito tu. Amchukulie taratibu.
Akamsubiria
atoke kuoga. Alipotoka akaanza tena taratibu tu. “Kama hapa unaona ni shida
kuishi, tunaweza kwenda kupanga wakati naendelea kujenga.” Akamcheka kama
mjinga wa mwisho. “Unataka kunirudisha kwenye nyumba za kupanga mimi! Huthubutu
Willy. Kama wewe umeshindwa na hapa, ndio uondoke. Hapa mimi nimefika.”
“Sasa mbona sikuelewi tena? Umetaka kuwa na kwetu, nakwambia tukaanze....” “Na
nani!?” Zelda akamuuliza akimtolea macho. “Unataka ukaanze na nani na utuuzima
huu?” Willy kimya.
“Asinishangae
kwa kunitolea macho kama vile niliyekugeuka Willy! Mimi sikukugeuka. Au sema
neno hata moja nililowahi kukwambia, leo limebadilika!” Kimya. “Nilitaka
kukushangaa. Maana ulinikuta nimeshaanza maisha yangu. Hukunikuta barabarani.”
“Nilikukuta hapa na mama, Zelda! Hapa nyumbani kwetu!” “Sawa sawa. Ulinikuta hapa,
kwa wazazi wako. Sio kwenu. Wewe ulikuwa kwako, na maisha yako. Mtumzima huwezi kulilia kwa
wazazi unasema kwetu! Wewe vipi Willy!?” Willy kimya. “Sasa eti unikute hapa,
aliponileta mama yako, halafu utake kunitoa hapa, unipeleke wapi tena!?” Willy
akaondoka kabisa pale chumbani.
Usiku
ule akalala kwenye chumba kingine. Ukweli Zelda hakumdanganya wala kuongeza
neno, ila amebadilika sana tabia. Si mnyenyekevu kama alivyokuwa na mama yake
akitoa tabasamu kila wakati kitu walichovutiwa nacho hapo nyumbani kwao na
kuona atamfaa Willy! “Kweli hajadanganya. Lakini ni kama ametoa
makucha yake kwa wazi kabisa!” Willy akawaza. Akaanza kufikiria maneno ya
Zelda. “Ni kama haonyeshi kunitaka! Nilijichanganya vipi!?” Akajiuliza
na kujishangaa sana. “Lakini sasa yeye anategemea tulee vipi mtoto!” Willy
akashangaa na kuhisi aliharakisha mambo. Alifikiria Zelda atafurahia kitendo
chakumuacha mke wake na kumfuata yeye, kama ishara ya kuwa amemchagua yeye na
mtoto, lakini ikawa tofauti kabisa! Zelda anaonekana ana mipango yake asiyotaka
kuingiliwa! Willy akashangaa msichana kama Zelda, anawezaje kumkataa mwanaume
kama yeye! Akidhani anampa nafasi ya upendeleo kuwa naye, Zelda hana hata
mpango. Mwenzie macho yanaangalia kwengine.
Singida.
S |
iku moja
kabla ya ufunguzi ya miradi aliyohangaika kubuni Sabrina na mumewe kumuunga
mkono, zilianza kugawiwa tisheti za chama hapo mjini. Kukafungwa majukwaa na
spika. Hekaheka ikawa kubwa. Pendo kipenzi cha Sabrina alishamtumia nguo za
rangi ya chama. Sabrina mwenyewe alijua atapendeza. Kesho yake watu wakaanza
kukusanyika uwanjani, mapema sana kwani hiyo shuguli ilikuwa inaanza saa sita
mchana, mara baada ya wageni kuwasili. Sabrina na Jack walishatoka nyumbani
tokea saa moja asubuhi kuhakikisha mambo hayaharibiki. Mji mzima ukasikika nyimbo
za chama tawala zikiimbwa. Kuanzia siku iliyopita, mji ulishaanza kupokea
viongozi wa ngazi ya juu wa chama, kutoka Dodoma na Dar. Ikawa hekaheka ya
namna yake. Ilishajulikana nani atakuwepo siku hiyo ya ufunguzi. Mida hiyo ya
asubuhi watu wakazidi kumiminika uwanjani, kwani nyimbo zilikuwa zikivutia na
wasanii mbalimbali kutoka jijini Dar walishawasili hapo. Basi ikawa jambo ni
moja tu siku hiyo, hiyo shuguli uwanjani. Kila mwenye uwezo wakutembea na
akasikia, akataka kwenda. “MmmH!” Sabrina akaguna. “Nini?” Jack akauliza. “Kama
uchaguzi mkuu, tuko kwenye kampeni!” Wakawa wanacheka tu.
Mida
ya saa sita wakaona msafara unaingia uwanjani, ukipeperusha bendera za chama na
ya taifa. Wakajua mgeni rasmi anaingia. Jack alijua mama yake yupo hapo kwenye
msafara na Junior. Alijawa furaha na majivuno, Sabrina alikuwa kimwangalia na
kumcheka. “Upo kama toto dogo Jack jamani!” Jack akawa anacheka na kufurahia
mama yake kuwepo hapo akishuhudia. Sauti za waimbaji zikaongezeka wakisifu
chama tawala. Ikawa shangwe kwelikweli. Na kweli, mgeni rasmi na wageni maalumu
wakashuka hapo karibu na jukwaa, Junior na mama yake walikuwepo miongoni mwa
wageni, wakapanda jukwaani, wakisifu chama.
Jackson
Msindai mwenyekiti wa tawi hilo la vijana hapo Singida akafungua huo mkutano
kwa hotuba fupi. Akataja majina ya watu walioshiriki kukamilisha hapo, kisha
akamtaka mkewe asogee pale mbele. Vijana wa hapo walianza kupiga kelele na
miluzi wakati Sabrina akisimama. Alikaa viti vya nyuma kabisa. Wakaanza kuimba
wimbo wa, “Mama, mama!” Wote waliimba wakati Sabrina anasogea mbele. Ni vijana
wake aliokuwa akifanya nao kazi bega kwa bega wakitaniana kila wakati wakazidi
kumshangilia. Sabrina akawa anacheka huku akitetemeka kwa hofu. Alishamwambia
mumewe asimtaje pale lakini Jack akamtaja.
“Karibu
wageni wetu wote wamefika hapa, kwa kuwasiliana na mke wangu zaidi.” Wakampigia
makofu, Sabrina akaondoka kwa haraka kama kumwambia asipoteze lengo, ajisifie
yeye ndio mlengwa. Kijana huyo wa Msindai aliyekuwa akiongoza tokea shule ya
msingi, akakaribisha wageni akisifia chama na kutoa hotuba nzuri sana akisema
mazuri ya chama tawala. Yale Chama waliyoyafanya hapo tawini na mipango
waliyonayo kwa kijana wa chama tawala. Jackson Msindai akaongea vizuri sana kuvutia
watu na kweli watu walivutika hata yeye alijua amezungumza vizuri. Alipomaliza
yeye ndipo akasimama sasa raisi na viongozi mbalimbali wa chama kupongeza na
kusifia chama chao. Likawa tukio
lililovutia kila mmoja aliyehudhuria hapo uwanjani hata wasio wa chama tawala.
Vijana wengi wakarudisha kadi za vyama vyao pinzani. Tena kwa kuchana palepale mbele
ya jukwaa wakati wakipokea kadi mpya za chama tawala zilizokuwa zikigawiwa.
Kulikuwa
na hekaheka, mpaka inafika saa kumi jioni, sherehe zikaisha, wageni wakawa
wanaondoka bila mama Msindai kutajwa popote na mtoto wake ila kuzagaa sifa za
Sabrina. Kikamuu huyo mama. “Huyu Sabrina amefika kwenye maisha ya Jack
niliyemuwekea mimi msingi tokea anazaliwa, nikimtia moyo kwenye uongozi wote
mpaka leo ameweza kusimama hapa, anasifiwa Sabrina!” Kikamsumbua yule mama
lakini kwa kuwa alikusudia kurudi kwenye maisha ya Jackson, na alishajiambia
Sabrina na wanae hawawezi kumtenganisha na mziwanda wake! “Hawa walinikuta,
na wataniach…” Akasita baada ya kukumbuka Sabrina amebeba mtoto wa Jack,
tena wa kiume. Hapo akashindwa kumalizia ni nini chakufanya na huyo Sabrina
akishafanikiwa kuupata tena moyo wa mwanae. Akaona ajibaraguze tu hapo Singida,
yaishe akajipange kwa upya.
Sabrina akiwa anaagana na mama Mkapa ambaye
walishakuwa karibu kwa mawasiliano ya hapa na pale, akashitukia mama Msindai na
Jack wamemsimamia. Akamsalimia. “Hongera sana kwa kazi nzuri.” Sabrina
akacheka. “Asante. Nimefurahi na wewe umekuja kuona maendeleo ya Jack.”
“Nashukuru kunikaribisha. Naona wajukuu wamekua wakubwa!” Sabrina akacheka
lakini hakutegemea, akamwangalia Jack. Wakacheka. “Wanashika sehemu wanatembea
sasa hivi.” Sabrina akaongeza. “Kwa nilivyowaona, wamebakisha kidogo tu watachanganya.”
Mama Msindai akahakikisha wanajua kama anawafuatilia. “Tunaamini hivyo.”
“Niliwaletea zawadi zao.” Sabrina kwa hofu mbele ya huyo mama akawa
ameshachanganywa. “Nani?” Akawa ameshapoteza mtiririko wa maongezi, akauliza wakati
walikuwa wakizungumzia watoto. “Zawadi za kina Jeiline.” Akajibu Jack kumsaidia
mama yake. “Aaah! Nashukuru sana. Asante.” Jack akawa anamkonyeza, Sabrina
haelewi.
“Kungekuwa
na uwezekano ningewakabidhi mwenyewe.” Hapo ndipo Sabrina akaelewa kuwa Jack alikuwa
akimwambia amkaribishe nyumbani. “Watafurahi kukuona mama. Karibu nyumbani.”
“Sitawabana?” Akauliza mama Msindai kiiungwana akicheka. Ndipo Sabrina akajua
kumbe alikusudia kulala! Japokuwa bado hakuwa ameupata moyo wake. Akajisikia moyoni
ni kama moyo wa huyo mama haujafunguka moja kwa moja kwake, lakini akaona
furaha ya mumewe, akaona afunike kombe, mwanaharamu apite. Akamualika nyumbani akiwa
na maswali mengi sana. Huyu mama alimsema vibaya sana yeye na wanae hao aliowaita
wakizungu. Alishindwa hata kuwashika hao watoto baada ya kuwaona ni wa kizungu!
Tokea aondoke siku ya kujifungua hao watoto, hajamuona tena ndio wanakutana
hapo akionyesha upendo kwa watoto haohao ambao wanazidi kuonyesha uzungu! Leo anatoa
taarifa kuwa anawafuatilia na kuonyesha ni kama anawajali sana na zawadi juu!
Sabrina akahisi hila iliyofunikwa na kujirudi kwa maneno ya kimama kwa
Jack. Akanyamazia tu. Baada ya wageni kuondoka, pamoja na Junior aliyekataa
kulala Singida, aliwaambia yeye ni lazima arudi Dar siku hiyohiyo. Akaondoka na
ndege ya hao viongozi wengine, mama Msindai yeye akabaki na kuongozana nao
kurudi nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ikawa ndio kwa mara ya kwanza kwa mama Msindai
kufika nyumbani kwa Jack akiwa amemuoa Sabrina. “Hawa watoto ni wazuri
kuwatizama hivi zaidi ya kwenye picha! Halafu wamekufanana sana Sabrina. Una
damu kali!” Sabrina akacheka akiwaangalia hao wanae ambao hawakuwa hata na
dalili ya kuja kuchukua rangi yake. Jack akawafanya mpaka wakakubali angalau kumsogelea
huyo mama japokuwa walikataa kabisa asiwashike. “Wakiwa na Jack hao, huwa
hawaoni kiumbe mwingine yeyote ila Jack tu. Mimi mwenyewe huwa inabidi
kuwachukua kwa nguvu au mpaka Jack aondoke ndio angalau hata huwa wanakumbuka
majina yao.” Ikabidi Sabrina kulainisha wakati hao watoto wakilia hawamtaki
huyo mama. Kidogo wakacheka.
Wakawa wanacheza wote watatu karibu na bibi
yao, Jack akitaka angalau wamzoee mama yake wamkubali na yeye apate muda na
mama yake. Sabrina akatoka jikoni na kuwakuta hapo. Akacheka. “Naona Jack ndio
anacheza kuliko watoto wenyewe!” Sabrina akafanya wote wacheke. “Watu na wivu
wenu!” Jack akaongea huku akicheza na wanae. Wakamkarimu huyo mama kwa upendo
wote. Ila ni kweli alileta zawadi nyingi kwa hao watoto. Kama aliyekuwa
anatangaza kurudi kwenye maisha yao moja kwa moja. Urembo wa kichwani ndio
ulikuwa mwingi kwa hao watoto na nguo zao. Sabrina na Jack wakawa na kazi ya
kushukuru tu hapo. Kesho yake asubuhi, mama Msindai akaondoka kurudi kwake. Angalau
hilo likawa limesawazika.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Itakuaje Kwa Willy Na Zelda?
Mahusiano Ya Jack Na Mama Yake Ni Kama
Yametengemaa. Sabrina Na Mama Msindai Katikati Ya Mafanikio Ya Jack! Nini
Mikakati Ya Mama Msindai Katika Karakati Za Kurudi Kwenye Chati Na Kuchukua Sifa Zake Anazoona
Sabrina Amezipora?
Inaendelea….
0 Comments:
Post a Comment