Hapo alipo akisubiria Willy asome talaka yake ili waweke saini kuvunja ndoa yao ramsi, Pendo alishajua ni mjamzito. Isivyo kawaida yake alipitisha siku. Akamwambia Sabrina akilia kwamba, tokea anavunja ungo, hajawahi kupitisha siku ila kurudiarudia. Kwa hiyo huko kupitisha siku hata moja ni muujiza kwake. Ndipo Sabrina akamshauri ajipime tu. Akakuta vimistari viwili kwenye kijiti cha kupimia mimba. Hakuamini kwani alishafanya hicho kipimo na Willy akisubiria nje ya choo zaidi ya atakavyohesabu na kupatia, na wakati wote alipata matokea ya mstari mmoja kuashiria kutoshika mimba. Kwa mara ya kwanza maishani, siku tatu zilizopita baada ya kuweka kijiti hicho kwenye mkojo na kuonyesha mistari miwili, ndipo Pendo akaenda sasa kwa daktari kuhakiki. Baada ya vipimo huko hospitalini, akahakikishiwa ni mjamzito.
Lakini
Pendo alijijua anavimbe nyingi sana tumboni na umri umekwenda. Ipo hatari ya
hiyo mimba kutoka wakati wowote ule. Habari alizokuwa akizisubiria kwa miaka
mingi sana, akaamua kuzinyamazia na kuweka usiri mkubwa sana, hata akamuomba
Sabrina asije mwambia mtu.
Alihofia
kutangaza halafu aamke akute mimba ilitoka usiku. Akajua Willy atamchukia zaidi
na kumuona muongo. Hakuwa na tumbo linaloonekana kama Zelda ambaye tumbo lake
lipo dhahiri kabisa kuashiria ni mjamzito wa mimba kubwa. Akajua hawezi
kushindana naye. Akajinyamazia kimya akiwa ameinama. “Pendo, kuna kitu chochote
unachotaka kuongeza au kusema kabla ya kuweka saini kwenye talaka?” Akanyanyua
uso. “Hapana. Mimi nimeridhika na ile nyumba tu. Asante.” Pendo akajibu kwa
upole. “Na wewe Willy?” “Mimi nimeridhika pia.” Akawawekea karatasi kila mmoja
mbele yake. “Ukimaliza kuweka saini, mkabidhi na mwenzio.” Wakafanya hivyo.
Wakaweka saini. Wakabadilishana, wakaweka tena saini na kumrudishia yule
mwanasheria. Akaangalia. “Sawa sawa. Kwa hiyo kwa mujibu wa sheria, kuanzia
sasa nyinyi sio wanandoa tena.” Pakazuka ukimya wa muda. Willy ameacha mke wa
ndoa ya kanisani na ujauzito waliokuwa wakiutafuta kwa muda mrefu zaidi ya
miaka 10, bila kujua! Amepishana kidogo tu, na muujiza wake mlangoni!
Wakatulia kimya kila mmoja wao kama haamini kama ni wao kweli, au wanashuhudia
juu ya wanandoa wengine!
Baada
ya muda Pendo akasimama. “Tunashukuru kutusaidia hili zoezi zima. Acha mimi
niwahi. Asante.” Pendo akachukua pochi yake, akatoka. Akawakuta wazazi wake
wakimsubiria nje. Akajikaza wala asilie. “Umekula mama?” Baba yake akamuuliza.
“Sikula, nilikuwa nawahi hapa ili niwahi kutoka niende kwa Sabrina, Singida.
Shikamooni.” “Marahaba. Twende basi, kaka yako na Nancy wanakusubiri tukapate
chakula cha pamoja.” “Msingeacha shuguli zenu kwa hili baba. Najua wote mpo
busy, mimi nipo tu sawa. Halafu sitaki kuchelewa ndege.” Wakamsikia Pendo
akizungumza na wazazi wake huku wakiondoka.
Pendo
alishaomba ruhusa kazini. Alipotoka kusaini talaka yake, akaelekea Singida kwa
Sabrina. Alikuta Sabrina na wanae wote wakimsubiria. “Mtoto mkubwa yupo wapi?”
“Kazini, na ndio maana unaona hawa wapo kama wana akili timamu. Maana
wakikutana wote watatu, hapakaliki.” Pendo akaanza kucheka. Akamchukua mpaka
nyumbani kwake. Weekend hiyo Sabrina akajitahidi kumuweka busy kwa hili na lile
ili asifikirie kuachwa na Willy. Jumamosi walitoka wote kwenda kutembea. Alimpitisha
kwenye miradi yote. Pendo naye hakuwa mgumu. Moyo wake ulijaa upendo.
Akafurahia fujo za Jack na wanae hapo, jumapili akarudi jijini. Nyumbani kwake.
Maisha yaendelee.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sabrina
akaweka juhudi kukamilisha project nzima huku akiwasiliana na watu mbali
mbali. Ukaribu wake na Junior ukaongezeka. Junior alimpenda sana Sabrina.
Alisifiwa hata na wakubwa alikomtambulisha. Wote walikiri kwa Junior ni
msichana anayejituma na anaakili ya kufikiria. Baada ya yakuweka nguvu yakutosha
na kwa msaada na nguvu ya pesa, Sabrina akakamilisha kila kitu. Jack alikuwa na
furaha ya namna yake.
Ndani
ya muda mfupi tokea Sabrina aje kwenye maisha yake, akayapa uhai kwa kuwa na
yeye Jack alimsikiliza sana Sabrina. Walishauriana, kukubaliana na kukosoana
kama wapo timu moja wakitaka mambo yafanikiwe. Jack alishafungua timu ya mpira
wa miguu ya chama ya mkoa wa Singida. Walikuwa na jezi nzuri na kocha mzuri
sana. Vijana hao walianza kujiingizia kipato kwa kucheza mpira wa mguu. Jack
alishahojiwa kwenye vyombo vya habari wakati anafungua hiyo timu. Wakafungua bucha
ya nyama ya kisasa upande wa sokoni ambako Sabrina alimwambia lazima wadai
sehemu yao na wao ndio wapafanyie biashara. Palijengwa kisasa, Jack na Sabrina
wakaagiza mashine za kukatia nyama za kisasa. Wakaweka kwenye bucha hiyo ya
vijana wa chama, wakaajiri vijana watatu wakaendeleza kazi. Walishaweka mafriza
ambayo walikuwa wanauza mpaka kuku hapo buchani, halafu pembeni, wakaweka
vijana wawili hapohapo sokoni, kuchoma mishikaki na chakula ambacho vijana wa
kike ndio waliokuwa wakiuza. Vijana wa Chama hapo wakaanza kuvutia mpaka vijana
wa upinzani kwa maendeleo yaliyokuja, makubwa na kwa haraka.
Jackson
Msindai sifa zake zikafika mpaka bungeni, akaitwa kwa mara nyingine tena
bungeni ilimradi tu kunadi chama kwenye lile jimbo lililokuwa linaupinzani
mkubwa kwa chama. Safari hii Jack akapata nafasi ya kueleza kwa kina
waliyoyafanya hapo wao kama chama tawala tena mbele ya mbunge wa hilo
jimbo kutoka chama pinzani ambaye na yeye alikuwepo kuhundhuria bunge. Akapewa
sifa kubwa sana. Hiyo ikawa kubwa kuliko safari ya kwanza alipokwenda hapo
bungeni akiwa hajafanya mengi mazuri huko Singida kama safari hii. Na hiyo mara
ya kwanza alipokwenda bungeni ilikuwa kabla ya wanae hawa mapacha hawajazaliwa.
Na kaka yake akamwambia kila mradi anaofungua ni lazima aite waandishi wa
habari na ijulikane hayo yamefanyika chini ya uongozi wake yeye. Basi makubwa
ya Jackson Msindai kama mwenyekiti wa vijana wa chama tawala kwa mkoa wa
Singida yakavuma ndani ya chama, akavutia uongozi wa chama, wakataka kumpa kila
ushirikiano ili uchaguzi ujao, wachukue hilo jimbo.
Hayawi,
Yamekua.
H |
atimaye
kazi ikakamilika, vifaa vyote vikaletwa, na miradi ikawa ikifanya kazi. Jack na
Sabrina wakapanga tarehe rasmi ya ufunguzi wa miradi hiyo. Ikaanza kazi ya
kutangaza ufunguzi wa hapo. Ikajulikana kama raisi mwenyewe atakuwepo hapo
mkoani Singida kuja kufungua ramsi miradi ya chama na mama Mkapa alishasema
angehudhuria pamoja na huyo mwanamke aliyekuwa akimsaidia Sabrina akifadhili mtoto
wa kike. Uzuri Jack alikuwa akifanya kila kitu, hatua kwa hatua akitaarifu kwa
barua, ngazi za juu za chama. Kwa hiyo mwisho wake ukapa mwitikio mkubwa wa viongozi mbali mbali wa chama.
Akashangaa
hilo jambo limebeba sura ya kichama haswa. Walidhani ni kitu kidogo tu
walichofanya mipango na Sabrina nyumbani kwao, lakini ikachukua sura ya tofauti.
Chama kikabeba hilo jambo kwa sura ya tofauti. Mji ukawekwa matangazo kila kona.
Likapigiwa debe haswa. Akatumiwa mpango wa nyongeza kuwa kutakuwa na waimbaji
maalumu watakao kuwa wakiimba nyimbo za chama wakitumbuiza hiyo siku ya
ufunguzi. Akahakikishiwa ulinzi mkubwa na wa kutosha.
Kukawa
na mengi hitifaki zikizingatiwa mpaka Jack akaingiwa wasiwasi. Akampigia simu
kaka yake. “Mbona imekuwa hivi!?” Alipomsikia
kaka yake anacheka, akatulia. “Hilo jimbo limekuwa
mikononi mwa chama pinzani kwa muda mrefu sana. Ndio wanataka kulirudisha mikononi
mwa chama. Hayo unayoyafanya, uongozi wameona ni vizuri watu wajue kwa wazi ili
uchaguzi unaokuja, liwe mikononi mwetu. Nahisi na wewe utasogezwa kwenye
uongozi wa kitaifa dogo. Subiri tutaona.” Jack akamwambia Sabrina,
wakacheka na kumshukuru sana huyo Junior. Aliwasaidia bila kuchoka simu zao
kila wanapomuhitaji hata kwa ushauri.
Akiwa kaka mkubwa kwa Jackson na wazari pia, akasaidia kuwaingiza kirahisi
kwenye milango migumu na wakapata uungwaji mkono mkubwa, kwa ajili yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
A |
lipomuona
mumewe anafuraha, akaona ndio apenyeze agenda yake aliyokuwa amemficha. “Njoo
Jack!” Akamuita pale kwenye kochi alipokuwa amekaa kizembe tu baada ya kazi za
siku nzima. Jack akasogea. “Weka simu chini halafu piga magoti.” Watoto wote
wakaanza kumfuata baba yao, na wao wakaenda kupiga magoti mbele ya Sabrina kama
baba yao. Sabrina akacheka kwa masikitiko. “Ujue Jack umeharibu hawa watoto sana!
Huna unalofanya wasifanye hawa watoto!” Jack akacheka na kuwaangalia vile
walivyofanya kama yeye, wakaanza kupiga makofi. “Sasa kilichobaki muanze
kutembea vizuri. Mmesikia?” Jack akawaambia wakaendelea kucheka. “Mkitembea
vizuri, mnaanza kucheza soka kama baba yenu. Sawa?” Wakapiga tena makofi.
“Unaongea
sana mpaka kitu chenyewe kimepita!” Sabrina akalalamika. “Nini?” “Wewe na wanao
mtulie kimyaa.” Jack akawashika wanae midomo, wakazidi kucheka. Sabrina
akacheka na kutulia. “Haya, nipe mkono wako wakulia.” Watoto wote wakamvuta
Jack kwa nguvu na kusimama wakimchungulia mama yao pale alipokuwa amekaa kwenye
kochi. Sabrina akachukua ule mkono akauweka kwenye tumbo lake. Mtoto alikuwa akicheza.
“OOH MY GOD!” Jack akashituka sana. “Ooooh God!” Jack akapiga
kelele na kunyayua nguo. “Unaniacha uchi bwana Jack! Si ushike hapa juu.” Akamuona
Jack ameshituka sana.
“Huyu
ni mtoto anacheza!?” Sabrina akamuona jinsi alivyobadilika. “Miezi mitano
sasa.” “Haiwezekani Sabrina! Kwa nini hukuniambia?” Akaongea kwa kulalamika kabisa
akionyesha hakufurahia kufichwa. Furaha yote ikamuisha. “Kwa nini umenifanyia
hivyo, Brina!?” “Wote tulikuwa hatujatulia Jack. Naomba usikasirike.
Nikaona...” “Hapana Sabrina, hukufanya vizuri. Nilitakiwa kujua.” “Samahani
Jack.” “Hujanitendea haki Brina, mke wangu. Naishi na mwanangu hanijui kabisa!
Unajua watoto wakiwa tumboni wanajua na kusikia sauti za nje? Wewe kwa nini
hukuona mimi nilikuwa nikizungumza sana na kina Jeiline wakati wapo tumboni? Na
uliona jinsi ambavyo walinijua mapema sana mpaka daktari alikuwa akishangaa!”
“Naomba tulia Jack. Tafadhali.” “Hapana Sabrina, hujafanya vizuri.” Jack
akaendelea kulalamika.
“Nilijua
utaanza kunifungia humu ndani na kushindwa kumaliza kazi zangu.” “Kweli
unafikiri mimi nataka ubunge kwa haraka kiasi hiki!” “Hapana Jack, mimi ndio
nilitaka ukifika muda huu, nitulie kabisa ndani. Kwa maana nyingine
nimekukabidhi kabisa ile miradi yote. Sasa hivi nakaa kabisa ndani.
Nimeanza kuchoka Jack.” “Sasa ulianza kliniki?” “Sio rasmi. Natumia dawa zote
za virutubisho. Nilitaka tukaanze wote.” Jack akarudi kukaa.
“Naomba
ufurahie Jack jamani! Au bado umekasirika?” “Ndiyo Sabrina. Nimekasirika sana.”
Sabrina akanyanyuka na kuondoka pale. Wala watoto hawakumfuata yeye, wakamfuata
baba yao kwa kutambaa. Wote walipofika, wakamshika suruali wakasimama. Kama
waliojua kama amekasirika, wakabaki wakimwangalia kwa huruma. Jack akawanyanyua
na kuamua kumfuata Sabrina chumbani. Alimkuta amepiga magoti kitandani huku akilia
kwa hasira, mpaka Jack akaogopa. Akaenda kuwaweka watoto chumbani kwao, akawawashia
tv na kuwawekea katuni wanazopenda. Akamwaga toys zao hapo chini, akawafungia
mlango, akarudi kwa Sabrina chumbani.
“Mimi pia sikupanga kushika mimba. Sijui nilikosea wapi, lakini
nikajikuta nimeshika mimba. Sikukusudia...” “Hapana Sabrina.
Hujanielewa mpenzi wangu. Mimi nataka sana watoto. Huyo mtoto sio wa bahati
mbaya. Ila naona nimepitwa na miezi yote mitano. Lakini pia hamna shida. Naomba
kumshika tena. Ni sawa?” Sabrina akajifuta machozi, akatulia vilevile amepiga
magoti. “Brina mama, nakushukuru na kukupongeza kwa kila kitu. Asante kwa kuhangaika
kufanya yote haya ukiwa umebeba mtoto mkubwa wa kiasi hiki. Nakupongeza.” Jack
akajirudi akawa mnyenyekevu. “Mbona umekasirika
sasa?” Sabrina akaanza kulia tena. “Oooh no no, nooo Brina! Nafikiri ni
kama nilipaniki kwa furaha. Nimefurahi sana.” Akamnyanyua pale alipokuwa
amepiga magoti pembeni ya kitanda. Yakaanza mabusu hapo, mara wakajikuta
kitandani. Yakaanza mapenzi mpaka mkewe akatulia. Vikaanza vicheko, Jack
tumboni akibusu tumbo wakajisahau kama wana watoto wengine wawili. Wakasikia
wakilia.
“Wanao
wamekusikia ukicheka bila wao. Watoto hawa! Wasinione nipo na wewe!” Jack
akacheka. Akamwita msichana wao wa kazi akawatoe chumbani kwao, awapeleke sebuleni.
Yeye akakimbilia bafuni kuoga akijua watamfuata tu pale chumbani. Na kweli, Jack
akiwa bafuni wakawa wameshafika mlangoni kwa wazazi wao. “Wameshafika Jack.”
Jack akawa akicheka bafuni. Sabrina akawasikia wakiongea nje ya mlango wao,
kisha wakaanza kulia. Akajifunga khanga akaenda kuwafungulia. “Watoto wa
Jackson Msindai, huwa watu wakifika mlangoni wanasema, ‘hodiiii!’. Hawalii.
Haya ingieni.” Wakaingia wakitambaa na cheko lililojaa machozi. “Waone! Dad
anaoga, mtulie hapa, muwe watoto wazuri. Mmesikia?” Wakabaki wakimwangalia mama yao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho
yake asubuhi, Jack na Sabrina wakaanzia hospitalini, wala Jack hakwenda kazini
kwanza. Akahakikisha Sabrina anaandikishwa rasmi kliniki. Anapata vipimo vyote
nakufanyiwa Ultrasound. Jack hakuamini walipoambiwa ni mtoto wa kiume. “We Jack,
unalia tena?” Sabrina akamuuliza kwa upendo, akamshika mkono mkewe pale
alipokuwa amelala kwenye kitanda cha chumba cha ultrasound. Wakafanyiwa yote
ndipo wakatoka hapo, akatamani kama angekuwa kwenye maelewano na mama yake ampe
habari njema.
Sabrina
akamuona anajifuta machozi tena. Akaanza kuhisi. “Si unajua kama unaweza kumtaarifu
tu mama?” Jack akamwangalia. “Mpigie tu.” “Kweli? Sitaki aje aonyeshe upendeleo
kwa huyu wakati dada zake aliwabagua.” “Jack! Wewe ndiye uliyepewa neema ya
hawa watoto, wengine hawakujaliwa. Na pengine mama amekuwa na hamu na wewe ila ameshindwa
kujirudi. Mama yako anakupenda sana, Jack. Na mambo makubwa mawili yanakaribia
kukutokea kwenye maisha yako. Upo juu sana kwenye chama, na unakaribia kupata
mtoto.” “Ninao watoto Brina, huyu ni watatu.” “Sawa mpenzi wangu. Wewe nishushe
mimi nyumbani, mpigie mama. Mtaarifu juu ya hili na umkaribishe kwenye ufunguzi
wa jengo.” “Sabrina!” Jack akashangaa sana.
“Kabisa.
Tena muombe. Najua kwako italeta maana kubwa sana akiwepo kwenye huo ufunguzi
kuliko mtu mwingine yeyote yule. Hata zaidi ya uwepo wa raisi mwenyewe.”
“Naomba niwe muwazi Sabrina, nammiss mno. Tena naumia kuona yote haya yananitokea
maishani bila yeye kushuhudia!” Sabrina akacheka kidogo. “Mimi nipo sawa kabisa
Jack. Wewe mtafute mama. Hata kama hawawataki kina Jeiline na mimi, nyinyi
msikosane.” “Hilo ndilo linakuwa tatizo Brina!” Sabrina akacheka na kupotelea
mawazoni.
“Sasa
akija huku Singida?” “Mpe uhuru bila kumbana. Akitaka kuja kulala nyumbani, ni
sawa. Akitaka kuondoka siku hiyohiyo kama shemeji alivyosema hatalala atageuza
siku hiyohiyo kurudi Dar, pia ni sawa. Usimuwekee pressure. Mchukulie
taratibu.” “Nashukuru Brina. Hiyo inamaana kubwa sana kwangu.” Sabrina akacheka
na kunyamaza. Wakafika nyumbani akataka kuingia ndani kwa muda mfupi aone
watoto kabla ya kwenda kazini. “Hapana bwana Jack! Unataka uniachie mimi kilio,
hapa! Utawaona jioni.” Jack akacheka na kuondoka.
Sabrina kwa
Pendo.
Wawili
hao urafiki ulishanoga. Kufichiana siri na kuomba pamoja kwenye simu likawa
jambo la kawaida kwao. Alipoingia tu ndani baada ya Jack kuondoka, akampigia
Pendo. “Nimemwambia Jack swala la ujauzito.”
Pendo akaanza kucheka. “Hakukasirika?” “Alikasirika.
Lakini acha nimgeuzie kibao! Sikujua kilio kilipotoka, acha nilie dada! Mpaka
ungemuonea huruma.” “Sabrina wewe!” “Sasa ningetoka vipi dada yangu? Alikuwa
amekasirika haswa, ikabidi nimbadilishie gia hukohuko angani. Akapoa kabisa.
Hivi hapa amenishusha tumetoka hospitalini, yeye amekwenda kazini. Nimekupigia
kukwambia jinsia ya mtoto.” “Ehe!” Pendo akataka kusikia. “Ni wakiume dada.” Akamsikia vile Pendo alivyofurahi.
Sabrina akafurahia moyo wake.
“Kweli Mungu yupo Sabrina na anajibu kwa moto. Kama ungeniambia na
mimi naweza kuja kushika mimba!” Wakacheka.
“Ushamwambia mama?” “Bado Sabrina. Acha ikomae kidogo.
Kesho nakwenda tena kwa daktari. Ila nipo makini mno. Daktari ameniambia
nisihangaike na nipumzike sana. Sijigusi kama sina mikono!” Sabrina
akazidi kucheka. “Na nimeshaanza kunenepa.” “Usiwe na
wasiwasi na unene bwana dada! Utapungua ukijifungua.” “Na kweli. Ila nakula
virutubisho mno, kwa ajili ya wanangu wakomae. Daktari anasema wanaweza
wasifike miezi 9 sababu ya vimbe.” “Usiogope dada. Japokuwa tutaongeza umakini,
lakini huyo aliyewaweka huko tumboni atawatunza mpaka wakomae.” “Amina.
Ninahamu yakujua jinsia!” Wakacheka na kuongea mengi. Wakaagana. Swala
la huo ujauzito alijua Sabrina tu na daktari wake, basi.
Mama ni
Mama.
M |
ama
Msindai hakuamini Jack alipompigia. Jack akamsikia akilia tu. “Mama!?” Jack akaita. “Umenikumbuka
Jack mwanangu?” “Sijawahi kukusahau mama yangu. Nina
mambo mengi yanaendelea kwenye maisha yangu, lakini nasikitika unapitwa mama yangu.”
“Nakufuatilia Jack. Naona maendeleo yako kwenye vyombo vya habari na Junior ananiambia.”
“Ni maendeleo yetu mama! Mke wangu anahangaika sana.” “Najua Jack. Mama Mkapa
pia ananiambia.” “Sasa kwa nini unakaa mbali na yote haya?” Mama Msindai
akanyamaza.
“Naomba uje kwenye ufunguzi ili angalau na wewe ushuhudie mama yangu.
Naumia kuona ndoto zangu zinatimia na wewe haupo unakuwa kama uliyekufa kwenye
maisha yangu wakati upo! Tokea nakuwa umekuwa ukiniita, Mheshimiwa
Msindai! Ukiamini mimi ni kiongozi, na ukaniambia
nitafika mbali. Sasa kwa nini unakosa nafasi ya kushuhudia kile
ulichonitabiria?” “Kwa kuwa umenikaribisha ramsi, nitaahirisha kila kitu, nitakuja
Jack.” Jack akacheka. “Hapo nimefurahi. Sasa
nina habari njema nyingine.” Akamsikia mama yake akicheka. “Nimetaka kukwambia wewe wa kwanza, ndipo niwaambie wengine.”
“Ni nini?” Jack akavuta pumzi na kuanza kucheka.
“Acha kuniweka roho juu bwana!” “Mungu ametupa mtoto mwingine wa
kiume.” Akamsikia mama yake akilia. “Sasa unalia nini tena badala ya kufurahi?” “Nimefurahi sana Jack. Mtoto wa kiume! Mungu amekukumbuka
kwa wema wako kupokea watoto wale wa Sabrina.”
“Ni wangu mama.” Mama Msindai akajirudi kwa haraka asiharibu tena.
Akatulia kabisa. “Watoto wote ni wangu, Mungu amenipa.”
“Najua Jack, na usifikiri siwajui. Jacinta huwa ananionyesha video na picha
unazomtumia. Umekuza Jack, hongera.” “Namshukuru Mungu mama. Ni watoto wazuri
sana. Mungu amewajalia afya njema, hawaugui na wala hawasumbui. Tulipata
msichana wa kazi, anawapenda sana.” “Hongera Jackson. Sasa Sabrina anaujauzito
wa miezi mingapi?” “Mitano sasa.” Mama yake akanyamaza kama na yeye
anayeumia kwa kupitwa. Jack anategemea mtoto hajui mpaka miezi mitano! Ikamuuma
mama Msindai. Jack alijua ila akaona alinyamazie tu. “Nimefurahi
tumeongea mama. Nakutegemea kukuona siku ya ufunguzi. Uwe na siku njema.”
“Asante, na wewe Jack.” Jack akakata lakini akiwa na furaha yakuzungumza
na mama yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ø Haya, Willy aliondoka kuanzisha familia mpya. Usikose kujua
yatakayompata huko kwa mke mpya, mwenye baraka za marehemu mama yake. Yapo
mengi mazito ambayo hata Willy hakuwa akiyajua, lakini yalikuwa yakiendeshwa
nyuma ya pazia na marehemu mama Mkwe wake Pendo.
Ø Sabrina kwa moyo mweupe amemrudisha mama Msindai pichani. Wanarudi
kuwa wanawake wawili, kwenye maisha ya Jack. Safari hii Jack akiwa na mafanikio
makubwa na hamu ya mama yake, mizani italemea wapi?
USIKOSE MUENDELEZO.
0 Comments:
Post a Comment