Hata
wakaacha kuonana na Pendo isipokuwa darasani tu ambako wanakuwa na darasa moja.
Na kwakuwa wao watu wanao somea masoko walikuwa wakienda kwenye darasa A
ambalo wanakuwa wapo kina Willy, na wanafunzi wengine wa uhasibu kama
kina Willy ambao ni darasa C&B hukutana na darasa A wanafanya
kipindi chao cha uhasibu kimoja. Wakimaliza hicho darasa C&B
wanatoka ndipo wanaingia sasa darasa la Masoko la kina Pendo wanakua
pamoja na darasa A la uhasibu, ndio hilo la kina Willy. Pendo na Eva
waliendeleza tabia yao ileile. Wakiingia hapo darasani basi hukaa viti vya
mbele pamoja na kundi lao la masoko. Wakimaliza hicho kipindi bila kugeuka
nyuma kwani kilikuwa chumba kikubwa tu. Basi wao huondoka, lakini Willy alikuwa
akimuona Pendo kwani yeye alikuwa akikaa mwisho kabisa na macho yake yanakuwa
kwake kuanzia anaingia mpaka anatoka.
Muhula
huo ukaisha fununu zikienea kuwa Willy ameachana na Wema na amehama pale
chuoni. Pendo akajua ndio sababu hamuoni mara kwa mara.
Muhula
wa pili Willy alirudi chuoni. Lakini safari hii hakuchukua chumba kabisa pale
chuoni. Kupishana kukaendelea. Kina Pendo, watu wa masoko wakapangiwa kipindi
chao na watu wanaosomea uhasibu lakini safari hii na darasa C.
Kwa hiyo hata Willy akawa hamuoni tena Pendo. Mwishoni mwa muhula huo ili
wamalize mwaka wa kwanza, mambo yakazidi kuwa magumu kwa wote kwenye kundi lao
la wanaosomea mambo ya Masoko. Mitihani nayo ikawa inakaribia, ikabidi
watafute msaada. Wakakubaliana siku ya jumamosi, siku chache kabla ya mitihani
wakutane kwenye moja ya madarasa, kila mmoja alete mtu yeyote ambaye anaweza
kuwasaidia.
Weekend
hiyo hakuna hata aliyekwenda nyumbani. Kila mmoja alihangaika kivyake kusoma,
ndio mida ya mwisho ya lala salama ya kumaliza mwaka wa kwanza. Jumamosi
wakakutana kwenye hilo darasa, hakuna aliyemleta mjuaji. Wakakutana
walewale wote wanatatizo hilohilo. Wakabaki kucheka tu. Wakati wanakaribia
kuondoka hapo ili kila mtu akaendelee kuhangaika kivyake, akaingia Willy na Kyande
kujisomea hapo kwenye hilo darasa, ila wakakaa mbele kabisa. Mmoja wao
akawanong’oneza. “Kile ndio kichwa cha watunza pesa, mwaka wa kwanza.” Wote
wakawaangalia. Pendo akamuona Willy amewapa mgongo.
“Naenda
kumuomba atuelekeze kidogo tu. Au mnasemaje?” Wote wakamwambia aende. Alikuwa
mwenzao wanaesoma nae mambo ya masoko. Alikuwa kijana wa kiume. Wakamtia morari
wakamwambia aende. Akasimama na kuwafuata pale walipokuwa wamekaa. “Tunaomba
msaada kidogo.” Willy na Kyande wakamwangalia. “Kuna namba zinatuweka macho.
Tunahisi kuna sehemu kidogo tu tunakosea. Tunaomba msaada wenu, tafadhali.”
Willy na Kyande wakaangaliana. “Nenda kawapige tafu, Kyande.” Kyande akageuka. Akakuta kundi zima
linawaangalia. “Acha kutaka kunidhalilisha mbele ya warembo Willy!” Wakacheka.
“Kwani
ni topic gani?” Willy akauliza. “Labda niwaletee kitabu kabisa.” Wakati mwenzao
kina Pendo anafuata kitabu pale walipokuwa wamekaa kina Pendo, Willy naye
akageuka. Macho yakagongana na Pendo. Pendo akakwepesha haraka, akainamia
kitabu kilichokuwa mbele yake. Hata hakikuwa chake au upande wake. Mapigo ya moyo
ya Willy yakaanza kwenda tena kasi baada ya kumuona Pendo. Akajiambia nilazima
yeye ndio atakwenda pale. Akaletewa kitabu akaangalia. “Ona Kyande! Haya mambo
yako kabisa haya!” “Nenda bwana Willy, nini?” Willy akacheka huku akiangalia.
Akasimama. Pendo akamuona akija pale. Ukweli Willy alikuwa amependeza. Alivaa kiume,
akajipangilia na mwili wake. Akaonekana msafi na amenyoa vizuri, Pendo mwenyewe
akavutiwa.
“Habari
zenu?” Akasalimia Willy. “Nzuri.” Wote wakaitika. Willy macho kwenye kitabu.
“Naona hapa tutaelekezana, tusaidiane wote. Na mimi najifunza. Mnataka niandike
wapi?” Akauliza Willy akiongea
kiungwana, akijua yeye ndio anatakiwa awasaidie. Wote wakatoa madaftari yao na
kumuonyeshea Willy kwa kushindana kila mmoja akitaka aandike kwake. “Chukua
hiki Willy.” “Hapa ndio kuna nafasi yakutosha Willy.” Wakabishana wakimtaja
jina kabisa, Willy akatulia macho kwenye kitabu akipekua na kuwaacha waendelee
kubishana. Akanyanyua macho akamtizama Pendo. Akachukua kijitabu kilichokuwa
mbele ya Pendo ambaye alikuwa amenyamaza kimya, hagombanii kama wenzake. Akajua
ni lake tu.
Akavuta
kiti akakaa na kuanza kuwaelewesha taratibu huku akiuliza kama wameelewa. Mara
nyingi alimtizama Pendo. “Tupo pamoja?” Akimuuliza Pendo. “Kama unaswali uliza
kabla hatujafika mbali.” Wakashangaa ameweka msisitizo zaidi kwa Pendo. Pendo
akaongeza ujasiri akaanza kuuliza ambapo hajaelewa. Willy akaendelea
kuwaelekeza mpaka Kyande alipowasogelea na kumgonga mgongoni. “Ndio muda
wenyewe?” Willy akauliza. “Washaanza kupiga simu.” Kyande akajibu, wakamuona
Willy anatoa simu mfukoni akacheka. “Wanajua unawatosa.” Kyande akaongeza.
“Naona na hapa nimemaliza, nishapata waalimu wengi. Si ndio Pendo?” “Nashukuru
nimeelewa. Asante.” Pendo akashukuru. “Basi. Na kwa kuwa daftari ni lako,
endelea kuwaelekeza wenzio huku mkikumbushana. Acha na mimi nikafundishwe
huko.” Willy akaweka kalamu chini. “Asante.” Wote wakashukuru, Willy na Kyande
wakaondoka kabisa hapo darasani. Pendo akabaki na furaha yakumuona Willy,
akajishangaa mwenyewe.
Darasa
la kina Pendo wakawa wakwanza kumaliza mitihani, wenzao bado. Kwahiyo wakawa na
kazi yakuzurula tu mtaani kabla hawajarudi majumbani kwao. Pendo angeondoka
kurudi nyumbani, lakini akaamua muda huo ndio atumie kuzurula mjini kabla
hajarudi kufungiwa nyumbani. Kwa hiyo wakabaki wakisubiria mwaka wa kwanza wenzao
wamalize wafanye Pikiniki yakuaga mwaka wa kwanza. Walio walevi wakaendelea
kulewa wakifanya fujo hapo chuoni, wakati wenzao wakimalizia mitihani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
moja katika kufurahia kumaliza mitihani Pendo akamsindikiza Eva kwenye kampasi
za chuo kikuu cha Mlimani, Mabibo ambako yuko mpenzi wake Eva. Wakakaa huko
mpaka jioni ya saa 10. Eva alipoamua kulala hukohuko, Pendo akaamua yeye arudi
chuoni. Kwanza alishazunguka sana na Eva siku hiyo. Alimwambia siku hiyo ndio
huwa kuna mitumba mizuri Buguruni. Wakazunguka, wala Pendo hakupata vitu vya
maana, ndipo akamwambia washukie hosteli ya Mabibo, akamsalimie mpenzi wake,
ndipo akaishia hapohapo akitaka kulala. Ikabidi Pendo aondoke.
Akatembea taratibu hutoka ndani mpaka nje
kabisa akielekea kituo cha daladala akiwa amebeba mizigo yake. Akaona gari
imempita na kusimama mbele yake. Kwa kuwa hakuwa anaijua, hakukimbilia.
Akaendelea kutembea taratibu mpaka akaifikia. Akaona kioo cha dereva
kinashushwa. Hakutaka hata kuangalia. “Ungependa nikusogeze?” Pendo akageuka,
alikuwa Willy. Akacheka. “Sikujua kama ni wewe! Unaelekea wapi?” Pendo akauliza
na tabasamu usoni. “Kijitonyama. Lakini naweza kukupeleka wewe kwanza. Mvua
inataka kunyesha, utasumbuka na daladala.” “Haitakuwa usumbufu Willy?” Pendo
akauliza kwa kujali. “Hata kidogo. Twende.” Pendo akazunguka upande wa abiria
akiwa amebeba mizigo yake akapanda garini.
“Unatafuta
nini huku Mabibo?” “Eva huyo! Amenidanganya leo Buguruni ndio wanafungua
mitumba mipya. Tumezunguka karibu siku nzima!” Willy akacheka. “Nakuona na
mifuko.” “Hamna kitu chochote cha maana hapa. Nimenunua tu ili nisirudi mikono
mitupu.” “Sasa mbona sikuoni naye?” “Nimemuacha kwa mpenzi wake.” Willy
akacheka kama haamini. “Eva ana mpenzi!?” Mpaka Pendo akacheka. “Utashangaa
jinsi anavyokuwa mpole, kama sio yeye Eva!” Wakacheka.
“Sasa
siku za mitumba mipya Buguruni si leo.” Akamtajia siku yenyewe. “Siku hiyo ndipo
wanafungua marobota na ndipo unapata nguo nzuri kwa bei nzuri.” Pendo
akashangaa mpaka akamgeukia Willy. Willy akacheka. “Wewe mwana masoko gani
hujui habari za masokoni?” “Wewe umejuaje Willy!?” Willy akacheka sana.
“Niambie bwana!” “Kwa kuwa ndio biashara yangu hiyo.” “Unauza mitumba!?” Willy
akacheka kidogo. “Mimi naingiza yale marobota. Nayauza kwa mnada. Wakishanunua,
ndio wanasambaza masokoni.” Pendo akashangaa sana. “Kweli Willy!?” Willy
akacheka. “Huniamini?” “Samahani kama nimesikika kama sikuamini. Nahisi
nimeshangaa tu. Hongera.” Willy akacheka.
“Kumbe
ndio maana umekimbia kuishi na sisi chuoni!?” Pendo akamfanya Willy aendelee
kucheka. “Umekimbia kukaa na vijana wenye akili za kitoto!” “Si umefurahi kwa
kuwa hunioni tena? Hakuna mtu wa kukuomba umsikilize akanushe habari za uzushi
za mtaani!” Pendo akamwangalia na kuinama. “Eti Pendo? Nilikuwa na kukera?”
“Hapana Willy. Sikutaka matatizo.” “Kwa Wema au Chris?” Pendo akashangaa kidogo
na kumwangalia Willy akaishiwa maneno. “Eti Pendo?” Willy akamwita tena
taratibu. “Hukutaka matatizo kwa nani?” “Sikutaka matatizo tu kwa ujumla,
Willy.” Akajibu kwa upole akiwa ameinama. Willy akamwangalia na kunyamaza.
Mvua
ikaanza kunyesha kama iliyofunguliwa. “Kweli ningekwama njiani! Nashukuru kwa
lifti.” “Subiri kwanza tufike ndipo ushukuru. Mvua za Dar huwa zina mtindo
wakufunga barabara.” “Umemaliza mitihani?” Pendo akamuuliza taratibu.
“Nimebakisha mmoja wa kesho mchana. Najua nyinyi mlimaliza tokea jumatatu
asubuhi.” Pendo akacheka. “Ndio maana tunazurula tu.” “Umeonaje lakini?”
“Nahisi hesabu nitakamatwa tu. Sikuwa nafanya vizuri sana, halafu mtihani wa
mwisho ukawa mgumu kweli! Sidhani kama nitapona.” “Pole.” “Asante. Lakini
nashukuru nimemaliza. Kesho mchana mwalimu amesema ataturudishia matokeo yetu.
Ndio nitajua.” “Naamini utapita tu. Na hata kama utashikwa hiyo moja tu,
hutashindwa kusawazisha.” “Naamini hivyo.” Wakafanikiwa kufika Ubungo. Wakakata
kulia kama wanaelekea Posta, ili Willy amrudishe chuoni. Walipofika Shekilango
karibu na mataa, wakakuta ajali. Basi kubwa likiwa tupu, limegonga gari ndogo.
Wakasimama
hapo kama dakika kumi. Mvua inanyesha, magari ya kutoka posta yanapita kwa
shida sana pembeni ya basi lililosababisha ajali. Na ya kwenda Posta ndio
yakawa yamezuiwa kabisa. “Nikwambie Willy, hapa utakesha na wewe una mtihani
kesho. Wewe katisha hapa Shekilango upite Sinza utafika Kijitonyama kwa haraka.
Mimi nivuke hii ajali kwa miguu, nitatafuta hapo mbele ya ajali usafiri wa
kunifikisha chuoni.” Willy akafikiria, giza lilishaanza kuingia. “Naona sio
sawa kukuacha katikati ya mvua!” “Hamna shida Willy!” “Hapana. Tufuate ushauri
wakuchukua wote njia hii ya Sinza, tukifika Kijitonyama, sio mbali na chuo.”
“Nakuonea huruma wewe.” “Usijali. Mimi nipo sawa.” Willy akaanza kutafuta jinsi
yakutoka hapo kuingia Sinza. Akafanikiwa.
Wakasogea
taratibu wanavuka Sinza madukani, wakakutana na foleni nyingine. “Najisikia
vibaya Willy! Pole.” “Kwa nini?” “Naona nimekuchelewesha. Isingekuwa kuja huku,
ungekuwa umeshafika!” Pendo akalalamika. “Hapana. Mimi nimefurahi angalau
tumepata huu muda Pendo. Ulikuwa ukinikwepa kabisa mpaka kubadili njia kama
ukiona nakuja mbele yako!” Pendo akacheka kwa sauti ya chini na kuinama. “Kwa
nini?” “Nilikuwa naogopa Willy! Ukumbuke wakati ule ulikuwa na Wema. Halafu
nikasikia mliachana. Nikasikia tena Wema ana winda yeyote atakayeonekana na
wewe.” “Haiwezekani!” Willy akashangaa
sana. “Kweli Willy. Mimi nikaingiwa na hofu.” Willy akashangaa sana.
“Hakika
sijui ni kitu gani kilichomfanya Wema adhanie mimi ni mpenzi wake!” Pendo
akamwangalia kwa mshangao. “Mpaka yeye mwenywe ilinibidi kumuomba msamaha.”
“Nani?!” Pendo akauliza kama haelewi tena. “Wema! Nahisi kuna namna ambayo
nilimuonyesha. Au mazingira fulani nilimuwekea, akajiaminisha mimi ni mpenzi
wake wakati mimi sina habari!” Pendo akamwangalia kwa muda kama akimshangaa,
Willy alipomtizama akainama. “Unakumbuka nilikuomba unisikilize upande wangu?”
Pendo akamwangalia tena. “Ni kwa kuwa na mimi baada ya wewe kukataa kabisa nisije
chumbani kwako siku ile na kuniambia mambo ambayo mimi mwenyewe sikuwa naelewi,
ikabidi kumuuliza Kyande, kutaka kujua ni nini kinaendelea kwa Wema. Akaniambia
mambo kama yale na wewe uliyosikia. Nikashituka sana nakujilaumu kuwa
nimetengeneza mazingira mimi mwenyewe.” “Kwani yeye Kyande alikwambia nini?”
Pendo akauliza taratibu.
“Haikutofautiana
na wewe, sema sasa Kyande ndiye aliyenifafanulia zaidi kwa sababu yeye yupo
karibu sana na sisi. Na Kyande alikuwa akilala
chumba kinachofuata kutoka kile nilichokuwa nikikitumia wakati ule naishi
chuoni. Akanieleza vile Wema alivyokuwa akilala chumbani kwangu, na kuwepo pale
kwa muda mrefu. Mambo aliyokuwa akinifanyia au kufanya mbele za watu bila mimi
kupinga, kila mtu akaamini ni mpenzi wangu wakati mimi najua anahitaji msaada
wangu wa shule na anarudisha shukurani kwa ninayomsaidia! Hakika sikutafasiri
vinginevyo kwa kuwa wakati ninapokuwa naye, anaonyesha kuniheshimu sana tu.
Hapakuwa hata na dalili za mapenzi!” “Labda kwako lakini kwake yeye
alikupenda.” “Sikutaka iendelee, ikabidi kuzungumza naye kabisa.” “Willy!
Ukamwambia nini sasa!?” Pendo akashangaa.
“Ilibidi
kumuweka wazi kabisa juu ya mahusiano yaliyokuwepo, ninayoyajua yapo, na
ninayotaka yaendelee kuwepo kati yetu kuanzia hapo. Na kumuomba kabisa radhi
kama kuna mazingira mimi mwenyewe niliyasababisha na kumfanya afikiri
vinginevyo.” Pendo akamwangalia na kunyamaza. “Ilinibidi Pendo. Sikuwa na
jinsi. Niliona amepokonya uhuru wangu! Watu wananiogopa kwa maneno yasiyo
kweli! Angekuwa ni mwanamke wangu, hakika nisingejali.” “Kwa hiyo hukuwahi kuwa
na mahusiano naye hata siku moja!?” Pendo akauliza kiuungwana. “Unamaanisha
kufanya naye mapenzi?” Willy akaweka sawa lile swali, Pendo akainama tena.
“Hata midomo yake sijui ina ladha gani!” Pendo akaona aibu na kugeukia
dirishani kabisa.
“Nasema
kweli na Mungu wangu ni shahidi. Sijawahi hata kubusu midomo yake! Kama alisema
vinginevyo, basi ameongopa.” “Hapana. Mimi sijasikia mambo mengine ya undani.
Ila niliambiwa ni kama mlikuwa mkiishi naye pale hosteli.” “Na ndio maana
nilihama pale hosteli. Sikutaka tena shutuma za kijinga ambazo si za kweli. Nijulikane
nafaidi penzi wakati hamna kitu!” Pendo akacheka taratibu. “Sikutaka kabisa.
Nikaona niondoke kabisa.” Pendo akanyamaza. Willy naye akanyamaza.
Foleni
ikawa inasogea taratibu, Pendo akajiegemeza kitini. “Hii mvua mpaka inanifanya
nitamani kurudi tu nyumbani! Nishuke hapo Sayansi, nichukue daladala au
nimpigie simu baba anifuate.” “Sasa kwa nini bado upo hosteli mpaka sasa?”
“Nipo na Eva. Eva ameniomba nibaki naye mpaka siku ya Pikiniki ya mwaka wa
kwanza ikiisha ndio turudi nyumbani. Aliona tukirudi nyumbani, ndio tuombe
ruhusa ya Pikiniki wazazi hawataturuhusu.” Wakacheka. “Eva mtoto wa mwanajeshi
yule. Baba yake hamruhusu atoke hovyo.” “Na wewe?” Pendo akacheka na kunyamaza.
“Kwa
hiyo unakwenda Pikiniki?” “Nitakwenda Willy. Wewe je?” “Sijui! Mpaka sasa
sijaamua. Naona kutakuwa na fujo nyingi zisizo na sababu! Wewe huogopi?”
“Nikiwa na Eva, mwenzio huwa siogopi.” Wakacheka tena. “Halafu Eva amemchukulia
tiketi mpenzi wake na marafiki zake. Tutakuwa wengi, siogopi.” “Na wewe
umemchukulia Chris tiketi?” Willy akachomekea swali la kiuchokozi, Pendo
akainama. “Eti Pendo?” “Hapana. Hata hivyo Chris asingeweza kukubali kwenda
kwenye vitu kama hivyo.” “Kwa nini?” “Chris anaustaarabu fulani hivi! Anapenda
vitu vyenye viwango vikubwa sana. Kama una moyo mdogo, inachosha. Ni mtu
anayependa vitu sasahihi, na kwa wakati sahihi. Hapendi kelele. Zile shangwe za
huko Pikiniki za vijana, tena usiku! Kwanza atashangaa sana hata nawezaje
kufikiria kwenda.” Pendo akaongea kama anayemfikiria Chris.
“Kwa
maana nyingine wewe una moyo mkubwa ndio maana unamvumilia, au mmekutana sifa
zenu zinaendana?” “Hapana! Hatuendani na Chris hata kidogo. Naona ananivumilia
tu. Mimi nahisi naendana na kila mazingira. Sina kinyaa cha watu.” Willy
akashangaa kidogo. “Kinyaa cha watu!?” “Yaani ile kuona watu wa daraja fulani
ndio wanafaa na wengine hawafai! Au watu wa namna fulani ndio sawa na wengine
sio sawa! Mimi sichagui watu kwa aina ya rangi yao ya mwili, urefu au ufupi,
unene au wembamba. Nakuwa nao sawa tu.” “Mfano wa mtu gani yeye hapendi?” Pendo
akacheka na kunyamaza kama aliyesita.
“Niambie
nisije nikatokezea, nikamuudhi shemeji.” “Chris hawezi kuwa shemeji yako. Wala
usiwe na wasiwasi.” Pendo alimfanya Willy acheke sana. “Kweli Willy! Yaani
unakuwa naye lakini unatamani muagane! Ukiwa kwake huna raha! Ukiwa naye
hotelini pia huna raha! Ukimtambulisha kwa marafiki pia huna raha! Anawakosoa
rafiki zako! Eti wewe umeona wapi hiyo jamani?” “Kwa hiyo alimkosoa Eva?”
“Ulijuaje! Eti ananiuliza nawezaje kuwa karibu na mtu kama Eva! Kweli jamani!?”
“Kwani anasema Eva yukoje?” “Eti vile alivyo na mwili mkubwa kama baunsa,
halafu eti na rangi yake! Mimi nikamwambia akimpa nafasi atagundua muonekano
sivyo jinsi ya mtu alivyo. Halafu ujue Eva ametokea kunipenda sana mimi! Eti
Chris akaniambia kwa mimi kuwa karibu na mtu kama Eva tu, kunaanza kumfanya
anitilie mashaka. Hampendi Eva kabisa. Kuna siku nilipita nyumbani kwake nikiwa
na Eva, ungejisikia vibaya Willy!” “Alifanyaje?” “Mimi sijui labda kwa kuwa
ninamjua Chris anapokuwa na watu wake, lakini sikupenda alivyomchukulia Eva. Ni
kama alimuonyesha dharau za waziwazi! Hakika sikupenda. Tena hasa wakati
nilishamwambia Eva ni rafiki yangu!” Pendo akajisahau na kuanza kulalamika kwa
Willy juu ya mpenzi wake.
“Eva
yeye alihisi kudharauliwa?” “Ni vile Eva huwa hajali watu. Lakini aliniambia
mpenzi wangu anaonekana mtu wa viwango vya juu. Hawezi watu wa kawaida.
Niliumia Willy! Mimi sikupenda.” “Pole. Labda atakuja kubadilika baadaye.”
“Hawezi. Anaamini mafanikio aliyo nayo ni kutokana na hizo kanuni za maisha
alizojiwekea. Tatizo kubwa hata linalonifanya hata kumkwepa ni kutaka mimi
nibadilike niwe kama yeye.” “Unamkwepa?” “Kabisa Willy! Wewe sasa hivi Eva yupo
kwa mpenzi wake, mimi narudi chuo! Unafikiri angekuwa mtu wa kawaida si
ningekuwa kwake! Pale kabla hujanipa lifti nimetoka kumtumia ujumbe nikamwambia
bado tupo kwenye mitihani siwezi kwenda kwake.” “Sasa kwa nini humwambii
ukweli? Ni bora umwambie ukweli kuliko kumdanganya.” “Unaona simfanyii vizuri?”
Pendo akauliza taratibu tu na sauti yake ya taratibu.
“Sio
kwake tu, hata kwako wewe Pendo. Unastahili kuwa huru na kuwa na mtu
anayekufurahisha. Au unataka pesa zake?” “Hapana Willy! Huwezi amini huwa hajui
hata kuhonga! Chamaana atakachokufanyia ni kukutoa kwenye mahoteli mazuri,
ukale vizuri, basi. Akiwa anashuguli ofisini kwao au kwa marafiki zake, akitaka
uende naye, ndio anakupa pesa ukanunue nguo ya gharama na viatu ili upendeze.
Mpaka wakati mwingine nakosa raha ya kwenda.” “Kwa nini?” “Labda ni mimi tu.
Lakini inakuwa kama anakwenda kunifanyia maonyesho tu, sio mapenzi ya kweli.
Kwa nini ni mpaka iwe kwenye shughuli zake tu na si zangu! Halafu ana wivu
ambao hauna sababu mpaka nahisi wakati mwingine ananitafutia sababu tugombane.”
“Kwa nini?” Willy akauliza taratibu tu, akitaka kumjua zaidi.
“Yaani
si mnakuwa mnakwenda kwenye party. Hataki anione nazungumza na wenzake hata
kuwasalimia na wakati wananifuata na yeye akiwepo! Namuuliza sasa wakinisalimia
nifanyaje? Anasema eti ninyamaze, rafiki zake ni wahuni sana wanataka kulala tu
na mimi!” Willy akakunja uso. “Sasa mnakuta mmetoka kwenye party nzuri,
umependeza, umekula vizuri, mnarudi njiani anagomba na kulalamika. Mimi mpaka
nikamwambia nahisi ananitumia tu. Kazi na mimi ikiisha, ndio ananitafutia
sababu. Kama hivi anahangaika ananitafuta, ujue ipo tu sababu. Lakini nimechoka
Willy. Unakuwa naye, unakuwa huna raha! Una winda maneno yakuongea kila wakati,
na nimkosoaji haswa. Popote mbele ya yeyote yule anaweza kukukosoa. Naona
sitamuweza.” “Basi mwambie.” “Naona kweli nitamwambia tu. Mwache aendelee
kupiga piga kwanza. Nikirudi nyumbani nitamtafuta tuzungumze naye.” Willy
akamwangalia.
“Yaani
hamuwezi kuachana kwa simu ni mpaka muonane!? Au unataka mkaagane?” Pendo akashangaa
kidogo na kuinama. “Eti Pendo?” “Hapana Willy! Nilidhani huo ndio utakuwa
ustaarabu!” Willy akamwangalia na kurudisha macho barabarani. “Hata wewe
uliniambia ulimuita Wema, mkawekana sawa.” “Wema hakuwa mpenzi wangu. Na
nilitaka aelewe hilo. Ila kumtafuta mwanaume aliyekuwa mpenzi wako. Mnapata
faragha ya mazungumzo ya kuachana, unafikiri ni nini kitatokea baada ya kutoa
malalamiko yako au unapomuaga?” Pendo akanyamaza. Willy naye kimya. Mvua
ikazidi kunyesha.
“Nina
samaki kwenye cooler box hapo nyuma ya gari. Sikuwa na barafu ya kutosha huko. Nahisi
kadiri muda unavyozidi kwenda na bado tupo barabarani, wanaweza kuharibika.”
“Labda mimi unishushe hapa Willy, nitachukua daladala wewe uwahi nyumbani.”
“Siwezi kukuacha barabarani Pendo. Naomba twende nikaache samaki nyumbani,
halafu nitakupeleka chuo. Ni sawa?” “Kwangu ni sawa. Sina ninapowahi ila
nakuhurumia wewe.” “Usijali.” “Sasa utasoma saa ngapi Willy?” “Huu ni mtihani
wa mwisho na sikuwa na mtihani wowote tokea jumanne. Na kesho tunafanya mchana.
Nitakuwa sawa.” “Hapo sawa. Tukifika kwako naweza kutumia choo?” Pendo
akauliza. “Bila shaka, kama tutafanikiwa kufika mapema. Au unataka tuingie
mahali tuombe ujisaidie?” “Nitajikaza.” “Unauhakika? Maana naweza kusimama
popote tukaomba.” “Sitaki tena kushuka,
halafu nikaloa, nikarudi kwenye gari nachirizika maji! Acha nivumilie.” “Basi
ukizidiwa uniambie.” “Sawa.” Wakaendelea na safari, Willy akiendesha kwa makini.
“Samaki
umewapata wapi huko Mabibo?” Willy akacheka. “Pendo uko makini!?” “Kwa nini?”
“Basi tu. Pale kwenye kafteria ya Mabibo, huwa nawapelekea samaki wa ziwani na
wakati mwingine kuku wakienyeji. Huwa nawauzia pale na hoteli moja ipo Buguruni.
Leo nilikuwa na mzigo uliofika, lakini anaye nisambazia amepatwa na dharula,
ndio maana imenibidi niende mwenyewe.” Pendo akamgeukia vizuri Willy. Willy
akaanza kucheka. “Kabla hujashangaa. Mama yangu ndiye anayefuga kuku wa
kienyeji na wa kisasa. Ana maduka ya nyama. Kwa hiyo huwa nanunua kwake kwa
jumla na kusambaza mahotelini, tena akiwa nao. Kwa hiyo kujibu swali ambalo
ulikuwa unakaribia kuniuliza, nina biashara ya mitumba na hiyo.” Pendo
akacheka. Na Willy akacheka.
“Nimezaliwa
kwenye familia ya wafanya biashara. Mama anafanya bishara, na baba naye hivyo hivyo.
Kwa hiyo unachukua kidogo huku na kule.” “Kumbe akili yako si ya darasani tu,
mpaka nje!” Willy akacheka sana. Ndipo Pendo akahisi mpaka gari anayoendesha ni
yake si ya baba yake. “Hongera Willy.” “Namshukuru Mungu si mbaya japo si kubwa
sana. Ndio ninaanza. Ya mitumba nafikiri hata haijamaliza miezi sita. Ya nyama
ya kuku na samaki nafikiri ni miezi kama miwili tu.” Akafikiria kidogo. “Yeah,
ni mitatu. Kwa kuwa niliaza kipindi tulipotoka ile likizo fupi.” “Hongera.”
“Lakini zina changamoto zake! Si umeona kama sasa hivi nipo kikazi na si
shule?” “Ni kweli. Inabidi uwe una uwezo mzuri darasani, lasivyo shule
itakushinda.” “Nafikiri kujipanga zaidi.” Willy akaongeza, Pendo akapotelea
mawazoni.
Wakaendesha
mpaka wakafanikiwa kufika nyumbani kwa Willy. Akaona geti linafunguliwa. Nyumba
nzuri sana. “Usifikiri hapa ni kwangu. Jamaa amenipangisha nyuma huko, chumba
kimoja tu.” Pendo akaanza kucheka. “Nilishaanza kujipanga kukupa pongezi.”
Willy akacheka. “Ulikuwa unaepuka kuloa, lakini itabidi tu. Gari inaishia hapa.
Huko kwangu inabidi kutembea na sina mwamvuli.” “Nimebanwa Willy, sina jinsi.
Naomba twende tu.” “Sawa. Basi tushuke, halafu nitakuja kuchukua mizigo.” Willy
akawa anakimbia, Pendo anamfuata nyuma. Alikanyaga maji yakutosha tu. Mpaka
wanafika barazani Pendo ameloa kabisa.
“Hamna
choo cha nje, Willy? Ona jinsi nilivyoloa na kuchafuka! Nitakuchafulia ndani
kwako. Heri nisiingie ndani.” Willy akamgeukia. “Pole. Lakini hakuna choo cha
nje. Ingia tu ndani.” “Ona matope Willy! Mwenzio nilikuwa nakanyaga majani sio
vile vimawe kama wewe.” Willy akacheka. “Vua tu viatu. Utajisuuza ndani. Halafu
nitakuoshea viatu.” Willy akafungua mlango, Pendo akavua viatu hapo nje.
Wakaingia kwa haraka Willy akijua amebanwa, akamuonyesha choo kilipo.
Akakuta
bafu safi na bado linaonekana jipya. “Pendo!” Baada ya muda akamsikia Willy
akimuita nje ya mlango. “Tumia taulo hilo hilo unaloliona limening’inia hapo
bafuni, chukua kubwa lake. Ni safi, hilo sijatumia.” “Asante. Lakini naona hata
nikitumia nitaloa tena, haina maana. Bora nikirudi chuoni ndio nioge moja kwa
moja.” “Nikupe nguo ubadili?” Pendo akanyamaza. “Pendo?” “Nitaloa tena Willy.
Acha nikabadili moja kwa moja chuoni.” “Ni sawa tukisubiria mvua na foleni
ipungue?” Pendo akafungua mlango, akachungulia akamkuta Willy amesimama nje ya
huo mlango. “Unamaanisha tusubirie hapa!?” Pendo akauliza. “Ndiyo. Hapa kwangu,
kama hutajali. Lakini ukitaka, nitakupeleka hivyo hivyo. Ila naona foleni
haisogei sababu ya mvua. Barabara zimefunga sababu ya maji. Si umeona njia ya
kuingilia hapa kwangu?” “Mwenzio nilikuwa naogopa usije ukaingia mtaroni, sema
nilishindwa kukwambia.” Willy akacheka. “Nilikuona. Sasa sijui huko mbele
itakuaje. Utajali kusubiria?” “Hapana. Nakushukuru.” “Karibu. Basi anza kuoga,
nikutafutie nguo zitakazokufaa wakati unasubiria.” “Sawa.” Pendo akarudi bafuni
kuoga.
Willy
akamletea tisheti na pensi yake kama ya kuvaa tu ukiwa ndani. Pendo
akajikausha, akavaa na kutoka. “Nimekuwekea chai kwa kuwa ulilowa na kuoga maji
ya baridi.” “Hapa nilikuwa natamani nikuombe blangeti.” “Na hilo utapata.”
“Nilikuwa nakutania bwana!” “Wala usijali. Ninalo blangeti dogo tu, naamini
litakufaa.” Akakaa kwenye kochi, Willy akaenda chumbani. Jikoni, sebuleni
pametenganishwa na makochi tu. Hapakuwa pakubwa, ila kwa mtu mmoja kulitoshea.
Akatoka na blangeti akamfunika pale alipokuwa amekaa kwenye kochi. “Mbona na
wewe hujabadilisha?” “Nilikuwa nakutengenezea wewe chai kwanza, na kukupashia
moto chakula. Wakati unakula, mimi ndio nitakwenda kubadili.” “Nitakunywa tu
chai, chakula nitakusubiri tule wote.” Willy akacheka. Akamuwekea chai kwenye
kikombe, akaacha chakula kwenye microwave, akarudi chumbani kwake, akamuona
anatoka na taulo tu. Pendo akakwepesha macho kwa haraka, Willy akamuona
akacheka. “Bafu lipo moja tu mgeni wangu. Nivumilie.” Pendo akacheka bila yakujibu.
Akamsikia
akioga, baada ya muda akatoka tena na taulo tu. Safari hii akapita mpaka jikoni
kifua wazi. Alipogeuka, Pendo akajiiba kuangalia hicho kifua kilichokuwa
kikisifiwa na watu wa chuoni kwao. Akageuka kwa haraka, akakuta Pendo
akimwangalia. Macho yakagongana. “Unataka nikusaidie wakati unavaa?” “Mgeni sio
siku ya kwanza?” Willy akamuuliza akiwa amemgeukia. Mpaka Pendo akahisi
anajionyesha kifua chake mpaka tumbo lililojaa misuli. “Hamna shida ili
usiingiwe baridi.” Pendo akajibu huku akijaribu kukwepesha macho hapo kifuani.
“Usijali. Hata hivyo namalizia. Sina vyakula vingi. Ni wali tu na nyama.”
Akageuka kupasha nyama. Akaacha tena kwenye microwave akapita hapo mbele ya
Pendo kurudi chumbani kwake. Akatoka na pensi, na singlendi. Vilimkaa vizuri,
Pendo akabakiwa kutokwa mate. Ni kweli Willy alivutia. Alipenda mazoezi na yeye
ndiye aliyemfanya hata Pendo kuanza mazoezi na kudumu kwenye mazoezi wakati
wote.
Akamsogezea
chakula palepale, akamwambia ajiwekee kwenye sahani yake kile kitakachomtosha.
Pendo akajiwekea. Na yeye akajiwekea akakaa pembeni yake. Akawasha tv, wakaanza
kula taratibu. Hapakuwa na maongezi mengi sana wakati wanakula. Pendo akala na
kunywa chai yake, huku wakiangalia taarifa ya habari wakiangalia mafuriko yaliyoanza
hapo jijini yakitangazwa na vyombo vya habari. Wakazungumza hili na lile huku
mvua ikiendelea kunyesha. Pendo akawa mstarabu akatoa vyombo hapo, Willy
akamsaidia kusafisha meza wakati yeye akiosha vyombo vichache walivyotumia.
Akarudi
kukaa kwenye kochi na kujifunika. Willy akarudi kukaa palepale. Akamuona amejikunyata. Akacheka. “Sasa wewe
muoga wa baridi hivyo, nakutoaje kwenye hiyo mvua hapo nje?” “Mvua na matope
Willy!” Pendo akalalamika, Willy akacheka. “Tutajenga yetu yenye cement mpaka
mlangoni! Hakuna kukanyaga tope tena. Sawa mama?” Pendo akacheka sana. “Lakini
ukiwa tayari kunisindikiza, mimi sina neno. Twende tu. Nilikuwa nakutania.”
“Mimi ukiniambia unalala hapa mpaka kesho, ndio itakuwa nafuu na furaha yangu.”
Pendo akamwangalia na kucheka. “Eti Pendo? Si ulisema kama sio kero za Chris
sasa hivi ungekuwa kwake? Kwa maana nyingine huna kinachokukalisha chuo. Kwanza
Eva hayupo.” Pendo akacheka. “Kwa Chris nina kila kitu changu. Kule ni kama
nyumbani. Hapa ugenini.” “Niandikie orodha ya vitu unavyotaka viwepo hapa,
nitanunua ili na hapa pawe nyumbani.” Pendo akamwangalia na kuinama.
“Pendo?”
Pendo akacheka akiwa ameinama. “Au hapa kwenye matope hapawezi kuwa nyumbani?”
Pendo akashituka kidogo. “Hapana Willy! Nyumbani ni popote moyo wako ulipo. Sio
eneo. Mbona kwa Chris ni pazuri sana. Nikikwambia ni pazuri, amini ni pazuri
haswa. Kuna kila kitu cha kisasa. Lakini mbona kumenishinda, nimebakia pale
hosteli nikioga bafu la watu wote? Sio kwa sababu hapa pana matope bwana!
Naomba usichukulie vibaya. Nilikuwa nakutania tu.” “Najua ulikuwa ukitania.
Lakini nikuombe kitu?” Pendo akacheka taratibu, akainama. “Mbona kama umeshajua
ni nini nakuomba na umeshakataa?” “Hapana Willy. Niambie tu.” Pendo akaongea
kwa kubembeleza.
“Naomba
uweke na moyo wako hapa. Hata kwa leo tu. Tulale. Kesho wakati nikienda chuoni
kufanya mtihani wangu wa mwisho, twende wote.” Pendo akababaika kidogo.
“Usiogope, sitafanya wala kukuomba chochote. Najua upo bado kwenye mahusiano.”
Pendo akainama na tabasamu. “Utalala kitandani. Mimi nitalala hapa kwenye kochi
ili nisome baadaye. Ni sawa?” “Sawa. Na ninakushukuru.” “Karibu.” “Basi ukiwa
tayari kulala, uniambie ili nikupeleke.” “Labda niende sasa hivi ili na wewe
upate muda wa kujisomea.” “Hamna haraka. Tunaweza kukaa tu. Naweza hata kuamka
asubuhi na kusoma.” Pendo akajirudisha nyuma vizuri akajiegemeza kichwa kwenye kochi, akajifunika vizuri akatulia.
“Una
mwamvuli?” “Unataka kwenda wapi tena?” Willy akauliza. “Nimeacha simu kwenye
pochi, ndani ya gari yako.” “Okay. Ngoja mimi nikafuate.” Willy akatoka, baada
ya muda akarudi na vitu vyote vya Pendo alivyoacha kwenye gari. “Nimekuta simu
yako ikiita ndani ya pochi.” Akamkabidhi. “Asante.” Pendo akatoa simu. Akakuta
ni Chris amempigia kama mara 4. Akamwandikia na ujumbe. ‘Tafadhali nipigie, ni muhimu.’ Pendo akafikiria, akamrudishia
ujumbe. ‘Nitakupigia kesho.’ ‘Kwa nini kesho na si sasa
hivi!? Tafadhali pokea simu yangu.’ Ujumbe huo ukaingia na simu ikaanza
kuita tena.
Pendo
akaitizama kwa muda, akapokea. “Nini kinaendelea
Pendo?” “Nilikuwa busy Chris, na nimetoka kukuandikia ujumbe masaa machache
yaliyopita. Kuna nini!?” “Wewe ndio nikuulize kuna nini! Hujibu jumbe zangu na
hupokei simu zangu! Is everything okay?” Akauliza Chris kwa wasiwasi. “Nilikutumia ujumbe jumamosi kukwambia sitaweza kuja.
Nilikuwa nasoma na wenzangu na jioni hii pia nimekutumia ujumbe kukwambia
sitaweza kuja bado nina mitihani! Kwani hujapata jumbe zangu?” Pendo
akadanganya tena. Alishamaliza mitihani na Willy alimwambia asimdanganye tena. “Unamaliza lini mitihani?” Akataka kuendelea kumdanganya
lakini akakumbuka maneno ya Willy. “Kuna nini Chris!?”
“Kwa nini unashindwa kujibu swali dogo tu hilo?” Chris akauliza kwa ukali. “Usigombe Chris!” Pendo akasikika akilalamika. “Unanishangaza Pendo!” “Samahani, lakini nimekuwa na mambo
mengi. Kesho naweza kukufuata ofisini kwa ajili ya chakula cha mchana,
tukazungumza vizuri. Ni sawa?” “Nitashukuru. Maana kuna safari nilitaka twende
wote. Kama kunisindikiza, lakini na wewe utapata mapumziko baada ya mitihani.”
Willy akamuona Pendo anacheka taratibu akajua ameshalainika.
“Ni safari ya wapi, na siku ngapi?” “Tutapanga kesho vizuri. Nina
hamu na wewe Pendo! Umekuwa hadimu kupatikana! Ni mitihani tu au kuna jingine
linalo endelea? Sio kawaida yako!” Pendo
akafikiria kidogo. “Pendo?” Akaita Chris kwa
kubembeleza. Pendo alishamjua akiwa na shida huwa anajishusha. “Niambie mpenzi wangu.” “Unavyonibembeleza Chris! Mpaka
napatwa wasiwasi! Sio kawaida yako mpaka uwe na shida. Unataka nikusindikize
wapi huko kunakokufanya ujishushe kwa kiasi hicho!?” Akamsikia Chris akicheka
sana. “Mimi nakupenda sana Pendo, sema mazingira ndio
yanakuwa mabovu.” “Mapenzi yako ya muda Chris! Unakuwa unanihitaji kwa sababu
fulani, ikiisha na wewe unakuwa, sijui nisemeje!” “Nakupenda Pendo.”
“Usinidanganye, wewe niambie unataka nikusindikize wapi, basi.” Chris
akasikika akicheka zaidi, Pendo asijue anavyomuumiza Willy.
“Chris?” “Ni safari
nzuri Pendo. Nakuhakikishia safari hii utafurahi.” “Mmmh! Huwa tunaishia kurudi
kwenye ndege tukiwa hata hatuongeleshani Chris!” “Sio safari hii.
Nakuhakikishia hii utafurahi.” “Acha tuzungumze kesho. Lakini nakuomba wakati
unakwenda kazini, unijie na lile begi langu dogo lina baadhi ya vitu vyangu.
Nimeweka stoo.” “Lakini si unajua utaondoka na vitu vya huku! Huna haja
yakubeba vitu vingine. Utatumia vya huku.” Akapoa baada ya kumkumbusha
unyanyasaji wake. “Pendo?” “Hilo begi nalitaka sababu
ya vitu vyangu vilivyopo ndani. Nina shida nalo. Tafadhali nijie nalo kesho.”
“Sawa. Nakupenda Pendo.” Pendo akanyamaza. “Pendo!”
“Asante Chris, nitakuona kesho.” Akakata na kubaki akifikiria. Willy
alishahamia mezani kujisomea, lakini akabaki akifungua vitabu vyake. Hata akili
haikuwa kwenye kusoma ila kwenye mazungumzo ya Pendo na Chris.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Willy Alimkuta Chris Mwenye Mapungufu Ndiye Mwenye
Kisu Kikali, Na Ndiye Aliyebakia Kula Nyama. Alifanikiwa Vipi Kumpindua Mpaka Yeye
Ndiye Akabakia Na Pendo?
0 Comments:
Post a Comment