Alipohakikisha
amemuweka sawa mkewe, akampigia sasa Tino. “Vipi kaka?
Mjini kwema?” Tino akapokea na kumuuliza Max. “Kwema
kabisa. Vipi wewe maendeleo?” Max naye akamuuliza. “Namshukuru Mungu naendelea vizuri.” “Vipi maendeleo ya mkono?”
“Naona sio mbaya kwa kweli. Kuna picha nimechora, nimeona imepata uungwaji
mkono mkubwa tu na imeuzika vizuri.” Hilo likazidi kumfurahisha Max, akajua
kwa hiyo pesa ipo. “Hongera sana. Kwa hiyo mambo
yakienda sawa, lini unarudi?” “Daah! Sijui kaka. Napatwa uzito kweli!”
Tino akasikika kama hana mpango wakurdi tena nchini Tanzania. Hilo halikuwa
sawa kwa Max. Alimtaka Tino nchini.
“Kwa nini tena! Mbona
sasa hivi kila kitu kipo sawa? Nyumba umeshaikomboa, upo huru. Nini kinakufanya
usirudi bwana?” Max akaendelea kusisitiza. “Aaah!
Sijui bwana! Kama naanza kukosa sababu yakuwepo huko! Hata hivyo nilisikia ni
kama Lela aliondoka na kila kitu mle ndani. Inabidi kuanza upya kabisa.
Nahitaji pesa nzuri, na...” Akasita. “Wewe sio
wakushindwa kujaza ile nyumba Tino? Acha kuniangusha bwana! Na labda
nikuongezee sababu ya kurudi.” “Nini tena?” Tino akauliza. “Nisikilize tu, usikate simu.” Tino akatulia.
“Ulipompeleka Sabrina siku ile kutoa ile mimba, ulihakikisha
ameshugulikiwa kabisa?” “Tafadhali naomba tusije zungumzia hilo tena. Naomba
tuache kabisa.” “Ninayo sababu yangu Tino. Naomba nisikilize tu. Usikasirike.”
Max akaendelea kabla hajampoteza. “Muda sio mrefu
nimetoka kuachana naye Sabrina hapo KIA, yupo na familia yake wanasubiria ndege
ya kuelekea Singida ambako wanaishi. Lakini Tino, watoto alio nao ndio
wamenifanya nikupigie simu.” “Sijaelewa!” Tino akauliza akiwa ameshabadilika
hata sauti. “Nahisi Sabrina amekuchezea akili. Kama
unauhakika mlipokuwa naye Moshi hakuwa na wanaume wengine, kwamba ulivyomuacha
kule akaendelea nao, basi fikiria pamoja na mimi.” Max akaanza
kutengeneza hoja yake kumvuta Tino. “Piga mahesabu
ukiwa umetuliza mawazo. Kuanzia muda wa Sabrina kuachana na wewe Moshi, kuolewa
na kujifungua watoto wakizungu kabisa!” Moyo wa Tino ukaanza kwenda
mbio.
“Nikisema ni wa kizungu ni wazungu haswa! Japo wamefanana na mama
yao. Ni kama Sabrina amejizaa kabisa. Lakini Tino, wale watoto ni wazuri,
hujapata kuona. Anayejiita baba yao huyo Jackson Msindai, alikuwa amewabeba, na
picha nakutumia sasa hivi, alivuta macho na masikio ya abiria wote mpaka wazungu!”
Max akaendelea. Safari hii akaamua kumtoa kwenye sababu ya kwanza
aliyomshawishi kumuacha Sabrina na kuhakikisha anatoa mimba. Akabadilisha
karata kama siye yeye aliyekuwa hamwachii Tino apumue mpaka ahakikishe Sabrina
ametoa mimba!
“Ni mapacha wakike wawili. Wanafanana, huwezi kuwatofautisha. Nywele
zao ni za kizungu haswaa kama za yule ndugu yako uliyetutumia picha mmesimama
naye! Wana afya nzuri, wazuri sana! Jackson mwenyewe anashindwa kuwaweka chini
jinsi hao watoto walivyo wazuri hao watoto! Kwenye ndege kule tulipokuwa
tumekaa, abiria walikuwa wakisikiliza vicheho vya hao watoto tu na kucheka.
Kama huna sababu ya kurudi dogo, hawa watoto iwe sababu. Kwa hakika ni damu
yako wewe tupu! Na hata Sabrina akisema hukuwa ukiwataka wale watoto, mimi nipo
na wewe Tino. Na hata sheria itakuwa upande wako. Wakati ule ulikuwa mgonjwa
sana huna uwezo wa kufikiria vizuri na ulikuwa mgonjwa sana, hata madaktari walishauri
ufanyiwe matibabu mazuri ndio ikabidi kuondoka ukatibiwe. Sasa alichokifanya
Sabrina wakati wewe ukitibiwa KCMC mpaka kwenda nje ya nchi kwa matibabu, wewe
hujui!” “Max!? Naanzaje kumbadilikia Sabrina niliyemuacha hospitalini nikijua
ametoa mimba!?” Tino akamshangaa sana jinsi anavyoanza
kumfundisha tena kuja kusema uongo kwamba hakuwa akijua kinachoendelea! “Ewaa! Sasa iweje leo Sabrina mwenye mume mswahili mwenzangu
ana watoto wa umri unaofanana na kipindi mlichokuwa naye pamoja, tena wakizungu?”
Tino kimya akijua Max ameanza kusuka kesi.
“Si umeona hata wewe hujui? Sabrina amekuchezea kipindi kile ulikuwa
mgonjwa. Kama watoto wapo, basi ni wako na wewe una haki nao! Hata kama huyo
Jackson anadai watoto ni wake kwa jeuri akifikiri kwa sababu anajua kwao ni wakubwa
hapa nchini, njoo tupambane upate watoto wako, wasikuletee mchezo tutawashinda
tu.” Kimya. “Umeona
picha zao lakini?” Akauliza Max kishawishi. “Ndio
naziangalia.” “Mmoja anaitwa Jeiline, mwingine Keiline. Usikubali damu yako
ipotee Tino.” Max akaweka msisitizo na kuendelea kuchochea. Tino kimya.
“Umeona wanao dogo?” “Hawa watoto si wangu ni wa Sabrina.” Max akashangaa, hakutegemea. Tino alijibu kwa upole kama anayekata kauli. “Tino vipi wewe? Wakati ule ulikuwa na sababu! Ulikuwa mgonjwa na Lela akikusumbua. Sasa hivi upo huru. Lela hayupo kwenye picha, na umepona kwa asilimia kubwa sana. Kweli unataka mtu baki akulelee damu yako!? Watoto wazuri hivyo wanamtambua mtu baki tu kama baba yao!? Kwanza haitawahi kuleta maana. Hawaendani na wale wazazi kabisa. Usikane wanao. Njoo tudai wanao.” “Nimekwambia watoto si wangu. Unataka nije kudai watoto wasio haki yangu?” Tino akajibu kwa ukali. Max akashangaa na simu imekatwa. Alipojaribu kumpigia tena, hakumpata tena Tino. Akabaki ameshika simu haamini!
Kwa Pendo.
A |
lipomaliza
kuzungumza na Sabrina, Pendo akapata nguvu, akaoga hapohapo nyumbani kwao,
akaenda kazini. Wala hakulala tena. Jioni wakati anatoka kazini akampigia simu
Sabrina. “Mlifika salama mwali wangu?” “Nilishafika,
hapa nipo mtaani, nimewaacha Jack na wanae wamelala, hawana habari.”
Wakacheka. “Sasa wewe umeenda wapi?” “Nina projects
nyingi nashugulikia, acha tu dada yangu. Bila kufuatilia mimi mwenyewe, hazitakamilika
kwa muda niliopanga.” “Ni nini? Maana unasema tu projects?”
Sabrina akacheka. “Kuna ujenzi unaendelea wa ndani na
nje ya kituo cha vijana. Hiyo ndio kubwa. Na pili nashugulikia projects
au miradi ya kumsaidia kujikimu mtoto wa kike hapa Singida. Upande wa vijana wa
kiume ni kama tupo vizuri, Jack mwenyewe amesimamia na naona vijana wa kiume
wao wapo pamoja tokea zamani, imekua rahisi kwangu mimi na Jack. Nakamilisha ya
mtoto wa kike.”
“Haya, nimepata wafadhili wa kunichimbia kisima nje ya hilo jengo. Nimeambiwa
juzi maji masafi yalianza kutoka. Ndio nataka wajengee vizuri kibiashara. Wawe
wanauzia watu maji, hiyo nayo itakuwa moja ya ajira ya mtu, na kipato kwenye
mfuko wa Chama. Kingine, nataka hayo maji yaweze kuingia ndani na kwenye tanki
kubwa ambalo nalo nililetewa week iliyopita ila nikataka lijengewe juu kwa
sababu za kiusalama. Haya, hilo nalo limekamilika ndio nipo hapa kukagua isiwe
limejengwa hovyo likaja kuanza nyufa baada ya kujazwa maji.”
“Haya, na ndani ya hilo jengo nilimwambia Jack wazo la mgahawa kwa
mradi wa wanawake. Ndio ujenzi ulikuwa ukiendelea kwa frame za maduka na
mgahawa. Si umeona kulivyo na vitu vingi na hapo bado sijamaliza utekelezaji wa
ndani kwenye hiyo miradi ili kukamilika hatua kwa hatua, ndio maana naishia tu
kusema projects.” Pendo akashangaa sana.“Wee Sabrina!” Sabrina akaanza kucheka. “Hongera Sabrina! Hongera sana.” “Nashukuru dada. Mungu yupo.
Huwezi amini uungwaji mkono niliopata. Shemeji amenikutanisha na vichwa hivyo!
Mpaka huwa naogopa lakini Mungu amenipa kibali, nikizungumza nao naona
wananikubali. Kwa mfano ameniunganisha na mama Mkapa mwenyewe. Nikazungumza
naye, akafurahia wazo langu. Huwezi amini dada, mama Mkapa ameniunganisha na mwanamke
mwingine wakizungu, ambaye anahusika kusaidia wanawake wa nchi zinazoendelea,
bwana huyo mama naona ni kama Mungu anatembea nami kumtumia yeye. Sina
ninachomuomba akashindwa kunisaidia na kunishauri. Tukizungumza na mama Mkapa,
utafikiri ni kama tulishaonana na yeye ameniahidi wakati wakufungua lazima aje
kuniunga mkono. Lakini wote hao ni sababu ya shemeji Junior! Nilizungumza naye,
akapenda mawazo yangu ndio akasema lazima anitafutie watu watakao fanikisha
hayo mawazo.” “Hongera sana Sabrina.” “Ni Mungu dada. Wala si mimi. Mungu
amenipa mawazo, na kunisimamishia watu wa kusimama na sisi. Na wote wameniambia
nikikamilisha watakuja kwenye ufunguzi. Ila sijapata uhakika na raisi,
ameniambia atanijibu. Ila wengine wote wapo tayari kuja ndio maana nahangaika
kuhakikisha wakija waje wakutane na vitu vya maana. Vipi lakini wewe dada yangu?”
Akabadili mazungumzo.
“Nashukuru kuzungumza na wewe asubuhi, Sabrina. Nilikuwa nimejawa
fedheha sana. Lakini nimeweza hata kwenda kazini, hapa nipo njiani narudi
nyumbani. Kaka ameniambia nilazima kuzungumza na Willy, ili tujue hatima yetu.
Ndipo sheria ichukue mkondo wake. Nimeona ni kweli. Nitajifungia nikilia mpaka
lini? Mwisho nitakuja kushitukia anamuhamishia mwanamke wake nyumbani kwangu,
mimi nalia nyumbani.” “Umeona ukitulia jinsi unavyofikiria vizuri? Tulia tu
dada, Mungu wako yupo. Sema sasa hivi nipo na hekaheka najua wakiamka wale
watataka kula, na hapa sijamaliza. Lakini kama Mungu alinipitisha mimi
niliyekuwa na dhambi, akanisamehe na akanibariki, atashindwa vipi kwako wewe
dada yangu mwenye moyo wa upendo hivyo?” “Amina.” Pendo
akaitika.
“Nakuombea hekima dada. Mungu akupe na utulivu ili mfikie muafaka
mzuri.” “Nina maumivu Sabrina mdogo wangu, acha tu. Nampenda sana Willy. Ndio
faraja yangu, mwenzio. Tumetoka mbali na najua ananipenda. Ila amechoka
kusubiri.” “Basi na hayo umwambie Mungu. Mweleze tu, halafu tusubiri tuone
atatujibu nini.” Akamfariji kidogo, akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Pendo
alirudi nyumbani kwake, akatamani kama akimbie ili ajisikie vizuri, lakini
akaogopa asije kuwa ameshika mimba, ikatoka. Akakaa hapo ndani mpaka saa 12
jioni, Willy akawa hajarudi ila msichana wa kazi alimwambia alirudi hapo nyumbani
asubuhi. Akajua alirudi kubadili nguo. Pendo akasubiri akaona heri tu hata
akatembee kwenye mashine. Akatembea kama dakika 45, akarudi kuoga. Wakati
anavaa Willy akaingia. Pendo akatulia kabisa. Willy akazunguka hapo chumbani
kama anayemsubiria au aliyetegemea Pendo angemuanza ili amalize, lakini Pendo akawa
kimya tu. Akamaliza kuvaa, akaamua kukaa kwenye kiti chake mbele ya kioo chake
chakujitengenezea kama anayesafisha kucha zake.
“Kuna
chakula.” Pendo akazungumza taratibu tu. “Naomba tusijidai kama kila kitu kipo
sawa wakati wote sasahivi tunajua.” Pendo akamgeukia na kubaki akimwangalia. Kama
anayemwambia nakusikiliza. “Namaanisha kuhusu Zelda na mtoto wangu.”
“Nakusikiliza Willy.” “Ndio hivyo. Zelda ana mtoto wangu, na sasa hivi
ananihitaji mimi zaidi. Siwezi kumuacha akiteseka na mtoto wangu peke yake.”
“Unajaribu kusema nini?” Pendo akamuuliza kwa taratibu tu. “Come on Pendo!
You are smart than that.” Pendo akakunja uso. “Unataka nijaribu kukisia
au?” “Unajua nini Pendo, najua unachotaka kufanya.” Pendo akanyamaza.
“Nakuachia
hii nyumba, lakini kiwanja kile cha Kigamboni tulichoanza kujenga, eneo zima,
na kila kitu pale, nitachukua mimi.” “Sawa.” Pendo akakubali bila shida mpaka
akamshangaza Willy. “Unaelewa kuwa nachukua na shamba, sio lile eneo tuliloanza
kujenga tu?” “Nimeelewa Willy. Na haya makubaliano yatawekwa kwenye maandishi
kabisa, kesho tutaweka saini.” Willy akakunja uso. “Vipi?” “Nini kinaendelea
Pendo!?” “Kwa nini?” Willy akakunja uso na kutingisha kichwa kama aliyeingiwa
na wasiwasi.
“Zungumza
wasiwasi wako Willy. Maana mimi na wewe sio mamilionea kwamba tuna mali nyingi
sana eti mpaka tukeshe na kushindwa kuelewana! Hapana Willy. Halafu ukituliza
mawazo, utagundua maisha yetu yote mimi na wewe, kwenye magumu yote, hatukuwa
tukishindwana. Wote sio wagomvi na sio watu wakushindwa kuelewana. Katika yote
na kote, miaka yote, tumekuwa tukifanya mambo yetu bila matatizo mengi. Au
umesahau?” Willy akatulia kidogo. “Au ulitaka katika hili ndio tuanze
utaratibu mwingine wa kushindwa kuelewana kwa maeneo mawili tu!? Hapa
nimewekeza sana, na wewe ni shahidi. Kumebeba kumbukumbu zetu nyingi sana
ambazo mwenzio bado sipo tayari kuziachia. Na nafikiri ndio maana na wewe
ulikuwa muungwana, ukaniachia hapa tokea mwanzo.” Willy akakaa.
“Willy?”
“Nahisi mimi mwenyewe ni kama nimechanganyikiwa tu.” Akaongea Willy akiwa
ameinama. Pendo akarudi kugeukia kioo hakutaka kumjibu katika hilo. “Inabidi niondoke
Pendo. Kwa manufaa yako na yangu pia. Sitaki tuishie pabaya.” “Tumeishia pabaya
Willy. Huu sio mwisho tuliowahi kuufikiria mimi na wewe. Sikulaumu, ila
nakushukuru kunivumulia. Umesimama na mimi kwa muda mrefu mno. Kwa madaktari,
kwenye matibabu. Umeniuguza kwa kuchukua likizo
kazini kabisa. Ukakaa na mimi nyumbani. Haya, hakuna njia ambayo tulishauriwa
kutumia mimi na wewe ili kupata mtoto, ukashindwa au hata kubisha. Ulinitetea
kwa dada zako, hata mama yako pia. Hakika umesimama na mimi Willy. Katika hilo
nakutetea.” Pendo akajifuta machozi.
“Nilikuwa nikijilaumu kuwa nimekuwa mjinga wa kiasi kikubwa,
kuwa mambo yalikuwa yakitokea na mimi nipo! Sio mara ya kwanza kumkuta Zelda na
mama yako au nyumbani kwenu! Alikuwepo tu, lakini sikuwahi hata kuhisi.
Nikajilaumu, lakini leo nikafikiria, nikajiambia sio kwamba mimi ni mjinga, ni
kwa kuwa uliniheshimu Willy. Katika ugumba wangu wote...”
“Naomba usijiite hivyo Pendo. Nachukia hilo jina na wewe unajua. Hata mama
nilimkataza.” “Hata lisipotamkwa, ila ni uhalisia
na ndio sababu ya wewe kuondoka kwenye hii ndoa. Sidhani kama unaniacha tu Willy.
Najua na maswala ya watoto yanachangia. Ninachotaka kukwambia ni kwamba,
tumeishia pabaya, lakini katika safari nzima uliniheshimu sana. Nakushukuru.”
Pendo akajieleza taratibu kwa upendo na machozi juu. Willy akainama.
“Unataka nikusaidie nini?” Pendo
akauliza. “Naomba nipe masaa matatu tu humu ndani.” “Unamaanisha
nini?” Pendo akauliza. “Naomba usiwepo hapa wakati naondoka.” “Okay.” Pendo akakubali na kusimama. “Unamaana hatutakuja kuonana tena Willy? Sisi ni marafiki
mbali ya kuwa wanandoa. Kuna vitu tulikuwa tukizungumza na kushauriana vizuri
tu tokea chuo. Kweli tutatupa mahusiano yote hayo sababu ya mimi kushindwa
kukupa watoto?” “Hapana Pendo!” Willy akasimama. “Hata kidogo. Ni kwa
sasa tu. Tutakuwa tukiwasiliana. Kukiwa na chochote tutazungumza bila shida. Umeongea
kitu cha kweli. Mimi na wewe hatujawahi kushindwana kwenye lolote kiasi chakushindwa
kufikia muafaka kwenye mambo yetu. Hatuna haja yakupelekana mahakamani. Tutakuwa
tukipigiana simu na kupanga kama zamani.” Pendo akatoa tabasamu la kuridhika.
Akambusu shavuni, akachukua pochi yake na funguo za gari baada ya kuvaaa,
akaondoka.
Usiku wa Simanzi.
Hakurudi
nyumbani kwao tena. Akatafuta sehemu ya kuangalia sinema usiku huo, akaingia
humo. Akakaa peke yake. Akasikia kummiss Willy, mwanaume waliyeanzana tokea
chuoni. Wawili hao walianzana wakiwa mwaka wa pili, wakakutana wote wakimya
sana. Ungependa kuwaona wakiwa pamoja. Wengi walipenda couple yao tokea
hata hawajaoana. Popote walipo kulikuwa na utulivu wa namna yake. Hata nyumba
yao ilikuwa tulivu sana. Msichana wa kazi mwenyewe aliwajua. Usingekuta kelele
nyumbani kwao, na wakiwa humo ndani walifuatana kila mahali. Walipendana bila unafiki.
Pendo akajisugua pembeni ya mkono karibu na begani taratibu kama kujituliza,
lakini machozi yaliendelea kumtoka. Tayari upweke ulishamwingia. “Kuwa mbali na Willy!” Akawaza na kuumia sana.
Pendo Kwa Sabrina.
A |
lilia sana
hapo kwenye ukumbi wa sinema wala asijue kinachoendelea. Akaona ampigie tu simu
Sabrina. Akatoka nje, akaka kwenye gari. “Da Pendo?”
Sabrina akaita, akamsikia akilia sana. “Pole dada, pole
sana.” “Najiuliza Sabrina, huyu Mungu
aliyenipa Willy, kweli ananinyang’anya hivihivi! Wasichana wangapi wanatoa
mimba? Wangapi wanaua watoto? Mimi ameshindwa kunipa hata kamoja tu? Willy
anaondoka leo kwenda kuanza maisha na mwanamke ambaye najua wazi hawezi kumjali
mpenzi wangu kama mimi mwenyewe!” Pendo alikuwa akilia sana.
“Nimetoka mbali na Willy, Sabrina! Sijakutana naye mtaani mimi. Namfahamu
na ninamjua! Kweli Mungu anamtoa kwangu na kumpeleka kwa mwanamke mwingine?”
Sabrina akabaki akimsikiliza. “Nimemkosea nini mimi
Mungu, Sabrina? Dhambi gani niliyokosa na kushindwa kusamehewa?” Akalia
Pendo, akamsikia Sabrina anaanza kuomba. Akamuombea faraja huku akiendelea
kulia. Akaomba huku akimkumbusha jinsi Mungu alivyomtoa yeye kwenye hiyo hali,
akamwambia amkumbuke na Pendo. Akamuombea mpaka akamsikia Pendo ametulia.
“Asante.” Pendo akashukuru. “Nilitaka sehemu na mtu wakunisikiliza.” “Pole dada yangu.
Njoo basi huku hata weekend hii tukae kidogo.” “Naona nitafanya hivyo. Kesho
nitakuja na kuondoka jumapili.” “Basi nitakupokea. Unataka nikupikie nini?”
Pendo akacheka. “Ugali na mlenda ambao umekuwa
ukiuimba.” Wakacheka. “Ila ujue hapa utulivu
hutaupata. Nina watoto watatu wanao tambaa.” Pendo akacheka sana. “Tena bora hao wawili wa kike wanajitahidi kutambaa na
kujitegemea, lakini huyo wakiume!” Pendo akazidi kucheka. “Uje unisaidie kulea dada yangu.” Angalau wakacheka
kidogo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi
nyumbani akiwa angalau ametulia. Hakukuta hata mswaki wa Willy. Alibeba vitu
vyake vyote. Akavuta pumzi kwa nguvu. Akakaa akiangalia kile chumba jinsi
kilivyo kikubwa na vile kilivyojaa kumbukumbu zake na Willy. Mapenzi mazito
yaliyofanywa humo ndani. Maamuzi magumu waliyoyapitisha pamoja hapo chumbani
kwao. Hatua za uponyaji walizopitia humo ndani chumbani wakibebana kwa upendo
mwingi. Pendo akabaki amekaa tu kwenye kochi.
Kaka
yake akampigia. “Dada mdogo?” Kenton akaanza. “Nipo kaka yangu.” Kwa kuwa yeye ni mwanasheria, mbali
yakujua maendeleo yake, akataka kujua maamuzi waliyofikia na Willy. Pendo
akamueleza kaka yake. “Nitaweka kwa maandishi sasahivi,
kisha nitamtumia mtu ambaye nina uhakika atawasaidia kwa haraka. Kesho mmalizane
kwa heshima.” “Nashukuru kaka.” “Utakuwa sawa, Pendo. Ukiwa na lolote, muda
wowote, hata kama ni usiku sana, nipigie tuzungumze.” “Asante.” Kaka
yake aliwapenda sana na kujali hao wadogo zake wakike wawili, lakini wakatokea
kumdekeza Pendo mtoto wa mwisho. Na kwa kuwa hakuwa na mtoto, akabaki kuwa
mtoto tu kwao. Pendo akabaki asiamini kama kinachozungumziwa kwa wakati huo ni
talaka ya kuachana na Willy! Roho ikazidi kumuuma. Usingizi ukapaa ikawa
kama ndio ameamka asubuhi. Akajilaza
kwenye kochi na kuwasha tv. Akaanza kuangailia movie lakini kumbukumbu
ikamchukua mpaka mwanzo wake na Willy wakiwa chuoni.
Mwanzo wa Willy na Pendo Chuoni!
I |
likuwa
mida ya mchana, wakati wakula. “Naomba kukaa hapa.” “Bila shaka. Karibu.” Willy
akajibu. “Ndio maana mimi huwa sipendi kuja kula mida hii, kunakuwa kunajaa,
hamna nafasi hata yakukaa!” Pendo akakaa akilalamika na sauti yake ya deko. “Mida gani ni mizuri?” Willy akauliza akiwa
anamwangalia, Pendo akiweka chakula na kuweka mkoba wake vizuri. “Wakati
mwingine huwa naacha kabisa kula! Fujo! Hata chakula kinakosa raha yake! Mimi
sipendi hivi.” Pendo akaendelea kulalamika hata asimwangalie vizuri Willy. Mara
akaja rafiki yake Pendo.. “Heri uje tule wote kuliko kupanga huo mstari hapo!”
Willy akaendelea kuwasikiliza. “Njoo tule wote, acha kujishauri.” Pendo
akamsisitiza Eva, mwenzie. Na yeye Eva kweli akaona hakuna muujiza wakupata
chakula kwa wakati kabla ya muda wa kipindi chao cha darasani kinachofuata.
Kulikuwa kumejaa wanafunzi hapo na wote wanataka chakula. Akakaa kiti cha
pembeni. Wakaanza kula chakula cha Pendo. Hawajafika hata nusu ya chakula,
wakaja wasichana wawili. “Willy!”
Wakaita kama wanao shangaa huku wakiwaangalia Pendo na Eva, nao
wakawaangalia.
“Sikujua
kama mnakuja sasa hivi bwana, nikawaambia wakae.” Willy akajibu na tabasamu
usoni. “Haya, waambie waondoke sasa!”
Warembo hao wawili wakaongea kwa kujiamini. “Samahanini, sikujua kama ni
viti vyenu!” Pendo akaongea kwa sauti yake ya taratibu. “Twende Eva.” Pendo
akaanza kukusanya vitu vyake pale mezani. “Acha mambo yako na wewe Pendo! Hivi
viti havina majina. Kaa hapo tumalize kula. Wasituletee urembo sisi!” Pendo
akashangaa. “Eva! Twende bwana, acha kuanzisha ugomvi hapa. Twende tukamalizie
chakula sehemu nyingine.” “Hapa nitanyanyuka nikiwa nimemaliza kula. Nikisimama
hapa kabla, napindua meza.” Pendo alimjua Eva. “Naomba usianze leo Eva, bwana!
Nilimkuta huyu kaka ndio..” “Willy.” Willy akajitambulisha kwa haraka. Wote
wakamgeukia. “Naitwa Willy.” Akarudia Willy akimtizama Pendo, akitaka amtambue
kwa jina lake halisi sio ‘huyu kaka’.
“Ndiyo.
Nilimkuta Willy amekaa hapa, ndio nikamuomba kukaa. Hawa ni wenzake, wanakaa
wote. Naomba tuondoke bwana!” Pendo akajieleza kwa undani akitamani Eva
amuelewe na waondoke hapo kwa amani. “Acha kujieleza, kaa ule. Kaa Pendo.” Eva
akamuamuru maana Pendo alishasimama. “Eva!” Pendo akaita kwa sauti ya chini
akimshangaa. “Nimekwambia kaa, umalize kula.” “Acha bwana Eva! Ngoja
nikwambie.” Wakati Pendo anarudi kukaa ili azungumze na Eva vizuri, mmoja wa
wale waliokuwa wakidai vile viti, wakavuta kile kiti ambacho Pendo alitaka
kukalia, Pendo akaanguka chini kabisa na kujigonga kichwa kwa nguvu kwenye kiti
cha mtu aliyekuwa amekaa pembeni yao.
Eva
akarusha ile meza upande wa pembeni kwa nguvu. Chakula kiasi kikammwagikia
Willy na wale wasichana wawili wakataka kukimbia. Eva akawakamata kwa nyuma, kisha
akawavuta wote wawili mpaka pale alipokuwa ameanguka Pendo. “Mnyanyue, kisha
muombe msamaha kabla sijakutoa meno ya mbele.” Eva akagomba akiwa anamuamuru
yule aliyevuta kiti na kusababisha Pendo kuanguka. Kimya. “Nitakuumiza wewe,
usiniletee urembo mimi!” Eva akagomba akiweka msisitizo. Pendo akajitahidi
akitaka kusimama, Willy akamkimbilia baada ya kujitoa na yeye chakula
kilichokuwa kimemmwagikia na kumsaidia Pendo kusimama. “Pole.” “Asante.” Pendo
akaitika wakati Willy akijaribu kumuokotea vitu vyake na kumuweka sawa. “Twende
Eva. Achana nao.” “Hakika siondoki mpaka akuombe msamaha. Lasivyo namvunja
taya.” Eva akamkazia macho. “Samahani.” “Ungeniumiza vibaya! Usifanye hivyo
tena.” Pendo akamjibu kwa upole yule aliyesababisha kuanguka, Eva akamuachia. Wakaondoka
huku Eva akiendelea kumuuliza kama ameumia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni
alipotoka kuoga, Pendo akasikia mlango unagongwa. “Subiri kidogo.” Pendo
akasikika. Akajifunika juu maana alikuwa na taulo tu, ndipo akafungua mlango.
“Willy!” Akashangaa, hakutegemea kumuona Willy pale. Lakini Willy akacheka.
“Nimekuja kukuangalia unaendeleaje. Hukuumia?” “Kidogo tu hapa kichwani, lakini
nitakuwa sawa. Asante kujali.” Pendo akaongea taratibu. “Naweza kuona?” Pendo
akashangaa kidogo, lakini akafurahia huko kujaliwa. Akageuka ili kumuonyesha
nyuma ya kichwa alipojigonga wakati alipoanguka. “Kwa hapa.” Willy akajitahidi
kuangalia na yeye akimsaidia kusogeza nywele alizokuwa amesuka. Akamshika
kidogo. “Pamekuwa pekundu! Pole.” Akampuliza kidogo. “Asante. Lakini nitakuwa
sawa tu. Nashukuru kujali.” “Bila shaka.” “Ningekukaribisha ndani, lakini
mwenzangu amelala, na mimi nataka kuvaa kwa haraka nitoke.” “Weekend
ndio imeanza?” Pendo akacheka kwa aibu kidogo. Willy akajua ndio anatoka na
mpenzi.
“Lakini
nimefurahi umekuja kuniona. Imeonyesha kujali. Nimefurahi.” Willy akacheka huku
akimtizama. Simu yake ikaanza kuita ndani. “Itakuwa ni Chris huyo anapiga
kunitaarifu ndio anaanza kuja huku kunichukua. Naomba nikuage.” Pendo akaongea
kwa upendo, akiangalia ndani chumbani kwake na pale aliposimama Willy. “Oooh
yeah! Kabisa. Nisikucheleweshe.” Willy akaongea kiiungwana na kuaga. Pendo
akavaa harakaharaka akiwa amependeza kwa kutoka kwa chakula cha usiku, siku
hiyo ya ijumaa. Chris alipompigia tena kuwa amefika yupo nje ya geti chuoni,
akatoka akiwa amependeza haswa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Pendo
hakuwa mrefu sana, lakini alikuwa na weupe mkali kama mama yake. Kwa kuwa upande
wa mama yake ambako anafanana nao walikuwa na umbile la unene, basi Pendo
alikuwa akijiwinda sana na kila kinachoingia mdomoni ili asinenepe. Alikuwa na
umbile zuri, alipendeza kwenye kila anachoweka mwilini mwake, na kwa kuwa
alikuwa mtoto wa jiji, tena alitoka kwenye familia inayojiweza au yenye nafuu,
alijua kuvaa. Na wakati huo kaka yao Kenton alikuwa ameshaanza kazi, yeye na
Nancy walikuwa wakiomba pesa kwa wazazi na kaka yao ambaye aliwapenda sana hao
dada zake wawili. Walijaliwa uzuri, lakini walitulia na hawakusumbua maswala ya
shule. Wakati Pendo anasoma chuo cha biashara hapo hapo jijini, Nancy
alishaanza shahada yake ya pili katika chuo cha Mlimani. Na kwa asilimia kubwa
Nancy na Pendo walifanana, ila Pendo alideka kama mtoto wa mwisho kweli.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipofika
getini akamkuta tena Willy kama na yeye anatoka. Akacheka wakati akimsogelea.
“Umependeza sana Pendo.” Pendo akacheka. “Asante Willy. Naona na wewe unatoka.”
“Kidogo tu, kutafuta chakula.” “Basi uwe na usiku mwema.” “Na wewe uwe na
wakati mzuri huko.” “Asante.” Pendo akashukuru na kutoka, Willy akimfuata kwa
nyuma. Akamuona anaingia kwenye gari nzuri ya maana. Akajua Pendo anatoka na
mtu mwenye pesa nzuri. Sio mwanafunzi kama yeye wa mwaka wa kwanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
huo Willy na yeye yupo mwaka wa kwanza lakini akisomea uhasibu, na Pendo upande
wa masoko. Chuo kilikuwa katikati ya jiji na wanafunzi walikuwa wengi sana.
Wengine waliingia jioni, wengine asubuhi. Willy alishamuona Pendo kwenye moja
ya somo ambalo darasa lao, yaani watu wanao somea uhasibu huwa
wanachanganyikana kufundishwa na watu wanao somea mambo ya masoko ambao ndio darasa
la kina Pendo na Eva. Alishamuona mara nyingi tu akiwa na Eva. Alishajua ni
marafiki wakaribu sana. Akatamani kumsalimia Pendo. Akatafuta sababu, lakini
wakati wote kila walipokuwa wakiingia hapo, walikaa viti vya mbele kabisa
kwenye darasa hilo ambalo wanakuwepo kina Willy.
Siku
hiyo mchana ikawa kama bahati alipomuomba Willy akae kwenye meza yake wakati
wakula, lakini Juli na Wema, wasichana walio kwenye darasa moja na kundi moja
la kujisomea na Willy, walimuharibia Willy kupata muda na Pendo kwa mara ya
kwanza. Wema ndiye aliyempenda Willy karibu kuchanganyikiwa, hakutaka msichana
yeyote amkaribie labda kimasomo tu, na umuache usimfuate kwengine. Na yeye ni
kama ndiye aliyemuwahi Willy tokea wanafika hapo chuoni, akavutiwa na umbile na
uzuri wa Willy akaanza kumganda Willy bila hata kutongozwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Willy
akasubiri hapo getini siku hiyo mpaka usiku wa saa 5, Pendo hakurudi. Akajua
ndio ameamua kulala kwa mpenzi wake. Akaumia, na kurudi chumbani kwao. Hata
rafiki zake wakamuona amebadilika, wasijue alikuwa akilinda geti akimsubiria
Pendo. “Nilijua umekwenda home!” Mwenzake mmoja akashangaa kumkuta
chumbani akiwa anaangalia movie, wakati wao wakiwa wametoka club. “Nipo.”
Akajibu Willy na kurudisha macho kwenye luninga. Mwenzie akajitupa kitandani na
kulala. Alikuwa amelewa.
Jumamosi
huwa cafteria ya chuo panakuwa hakuna watu wengi kabisa. Wengi wanakuwa
majumbani kwa ndugu, jamaa na marafiki. Ukorofi wa baba yake ndio ulikuwa
ukimfanya Willy aone ni heri abaki chuoni tu kuliko kwenda nyumbani kwao. Kwa
hiyo hakuwa akienda nyumbani mara kwa mara maana kila alipokuwa akienda mara
nyingi waliishia kugombana na baba yake kwa hili au lile. Na pia Willy hawakuwa
karibu sana na kaka zake. Wakati huo yeye na mdogo wake Prisca ndio bado
walikuwa wakisoma. Kaka zake wawili na Stella walishaondoka nyumbani. Kwa hiyo weekend
nyingi alikuwa akibaki tu chuoni akijisomea na kufanya shuguli zake. Na ndio
maana Willy alikuwa mzuri sana darasani na wengi wakimtegemea. Na kwa sababu ya
hayo manyanyaso ya baba yake, Willy aliomba mtaji kwa mama yake akaanza
biashara, nia ni asiwe anamuomba baba yake pesa na akitoka tu chuoni, asirudi
nyumbani.
Wakati
yupo cafteria akila jioni hiyo, akamuona Pendo anaingia akiwa amevaa gauni lake
refu mpaka chini. Kata mikono. Mabega wazi. Alibana nywele juu akazifunga
pamoja na kuvaa hereni kubwa za alama ya moyo. Lakini dhahabu. Lilimkaa vizuri haswa.
Mapigo ya moyo ya Willy yakaanza kwenda kasi alipomuona. Akaweka simu juu ya
meza, akajiweka sawa akawa anamuangalia kuanzia analipia, anapanga mstari
kuchagua chakula, Willy akaendelea kumsindikiza kwa macho. Kwa aina ya chombo
alichokuwa amebeba, akajua hatakaa pale kula, anaondoka na chakula chake.
Akatamani kama angekaa naye ale, akafikiria jinsi ya kumfanya akae pale. Akaona
akanunue soda.
Akasimama
na kwenda upande uleule ila kwenye vinywaji. “Willy!” Pendo akamuita kwa sauti
nzuri ila ya mshangao kumuona Willy. Nusura Willy ashangilie, ila akajikaza
kiume na kugeuka kana kwamba hakuwa amemuona! “Mzima Pendo?” “Mzima. Umekuja
kula?” Pendo akauliza taratibu. “Nilikuwa nakula pale. Nimesikia kiu ndio
naongezea soda.” “Jumamosi kunakuwa kumetulia, panafaa kukaa na kula bila
ugomvi wa wakina Eva.” Wakacheka.
“Sasa
mbona hukai kula?” “Nimejiona nitakuwa peke yangu, kina Eva leo hawapo wanarudi
kesho. Nikaona nikale tu chumbani huku najisomea.” “Mimi nipo, tukae wote.” Pendo
akacheka akionyesha wasiwasi. “Nini?” Willy akauliza. “Nasikia msichana wako
mkorofi bwana! Hapendi watu wakusogelee.” Willy akashituka kidogo. “Msichana
wangu ni nani!?” “Si Wema yule aliyeniangusha jana!” Pendo aliongea akitabasamu
na sauti yake ya deko.
“Huyo
aliyekupa habari zangu sidhani kama amezikamilisha.” Pendo akacheka. “Mimi mwenzio
sipendi ugomvi. Acha nikale tu chumbani kwetu. Wewe endelea.” Willy akabaki
akimwangalia, Pendo akacheka tena. “Kwanza nataka nile huku nasoma. Nina
Economics inanisumbua kichwa, ndio maana nimerudi. Nitakuona wakati mwingine
Willy, uwe na jioni njema.” “Na mimi naruhusiwa kuja kusoma huko unakosomea
wewe?” Willy akauliza. Pendo akacheka kama anayesita, Willy akimwangalia.
“Sitaki matatizo bwana. Ujue jana angeniumiza yule!” “Kwanza vipi maumivu.”
“Bado nasikia maumivu. Kidogo lakini.” Akaongea kwa kulalamika kidogo,
akitabasamu. “Pole.” “Asante.” Pendo akajibu.
“Ni
kweli unataka uje usome chumbani kwetu!?” Pendo akauliza. “Kwani mnasoma kwenye
kundi?” “Wameondoka wote. Nipo tu peke yangu.” “Basi nakuja.” Pendo akacheka na
kufikiria kidogo. “Nikuombe kitu Willy?” Willy akatulia kama anayemsikiliza.
“Naomba usije.” Pendo akaongea kwa upendo kama anayebembeleza, lakini na
tabasamu la hofu kidogo. Willy akashituka moyoni na kuumia sana. Pendo akamuona
amebadilika mpaka usoni. “Samahani Willy.” Tabasamu ikamwisha Pendo usoni.
“Samahani.” Pendo akarudia kwa sauti ya chini zaidi. “Okay.” Willy akakubali na
kuondoka kitu kilichomuuma tena Pendo, lakini Eva alishapata habari za Willy na
Wema kutoka kwa mtu anayesoma nao kwenye kundi moja, Pendo akaingiwa na hofu.
Akatoka hapo cafteria Pendo akiwa amepoa mbali na alivyoingia. Willy akarudi
kukaa kwenye ile meza aliyoacha chakula chake. Weekend hiyo hawakukutana tena.
Jumatatu!
Siku
ya jumatatu ambayo watu wote wanarudi chuo kuendelea na masomo ikabidi Willy amuulize
mmoja wa wanaosoma wote kwenye kundi lao, Kyande. “Kuna kitu nimesikia, lakini
sijaelewa.” Willy akaanza. “Nini?” Kyande akamuuliza. “Inasemekana mimi nipo
kwenye mahusiano na Wema!” Mpaka Kyande akamshangaa. “Wewe upo serious
au masihara!?” “Kwa nini na mimi nauliza?” “Acha masihara wewe! Yeye mwenyewe
anakuita babe!” Hapo ikabidi Willy mwenyewe atulie afikirie. “Kila mtu anajua
ni mwanamke wako na yeye ashapiga marufuku kila mtu asikusogelee! Kutwa yupo
chumbani kwako akisoma na kila mtu anajua ukitaka kumpata Wema, ni chumbani
kwako!” Willy akakunja uso na kufunguka macho. “Vipi wewe!? Au umesikia ana mtu
mwingine nini!?” “Hapana. Nafikiri mimi ndio nilikuwa sijaelewa.” “Ni nini
tena? Mpo wawili nini, ndio hukujua?” Willy akajua hata yeye anajua ni wapenzi.
“Hapana.
Nasemea swala la Wema. Sikujua kama lina picha nzito ya kiasi hicho!” “Ipi?”
Bado Kyande akawa hamuelewi. “Kwamba ni mpenzi wangu!” Kyande akatulia kidogo.
“Sikujua kama yeye ndivyo anavyochukulia hivyo.” “Kumbe wewe unachezea tu huna
mpango naye?” “Hapana. Sijawahi kumgusa Wema. Na ninajua ni msichana
anayejiheshimu. Sija...” Akamuona Kyande
anacheka. “Nini?” “Jamaa wamemkuta amelala kitandani kwako!” “Sasa kulala
kitandani kwangu ndio nini? Wakati mwingine tunakuwa labda tumesoma, anasema amechoka,
anapumzika kidogo, anajilaza kitandani kisha tunaendelea! Haina maana ya
kimapenzi hata kidogo! Na wala simchukulii hivyo!” “Mbona nasikia alifanya fujo
majuzi ijumaa, kule kwenye kibanda cha chips nyuma ya chuo, nasikia alikukuta
umekaa na demu mmoja hivi wa masoko. Akamuangusha chini na wala hukusema kitu?”
Willy akazidi kuchanganyikiwa.
“Mbona
kila mtu anajua kaka! Au haikuwa hivyo?” “Daah! Nahisi sasa hivi ndio nafunguka
macho. Mimi nilijua alifanya hivyo kwa kuwa tulipokuwa tukimaliza darasa la namba,
akaniambia kama nakwenda kwenye chips, nimuwahie kiti yeye na mwenzie. Sasa
mimi nikaenda kweli, nikachukua meza nzima. Akaja huyo msichana uliyemsikia.
Anaitwa Pendo, hata wewe unamjua. Tuna kipindi nao kimoja cha..” “Mimi namjua
yule demu. Nimeonyeshwa! Mtoto wa mama hivi! Amezungushia hivi chini ya kiuno, halafu
ana hips fulani hivi za...” “Anaitwa Pendo.” Willy akamkatisha kama ambaye
hakutaka aendelee kueleza umbile la Pendo kiundani vile.
Kisha
akaendelea Kyande akimtizama. “Sasa kwa kuwa kina Wema wakawa hawakutokea, na
ukumbuke ilikuwa baada ya mapumziko yale ya mchana, tulikuwa tukirudi tena
kwenye test ya namba, basi nikajua kina Wema wamegairi kula, wameamua waendelee
kujisomea mpaka baada ya test. Pendo aliponiomba kukaa, nikamruhusu. Sasa lile
tukio lilitokea kama kufunga na kufungua. Na yeye alikuwa na rafiki yake,
mjeshi hivi!” “Anaitwa Eva. Mtoto wa jeshini yule. Tunamjua, ngumi mkononi.”
Wakacheka.
“Basi
akatembeza fujo pale akataka kuwapiga kina Wema.” “Nasikia alirusha meza!” Wakacheka zaidi. “Namjua Eva. Mkorofi sana,
hajui kuomba. Hata kule maktaba ya chuo nilisikia wakimsema. Neno lake ni
‘NIPE’.” Wakacheka tena. “Na kweli alifanya fujo yakutosha tu pale. Mimi
nikamsaidia Pendo kusimama, wakaondoka na mimi nikaondoka maana chakula
chenyewe huyo Eva alikimwaga chote.” Wakaendelea kucheka. “Basi washikaji
wanajua unapenda vile Wema anavyokugombania kwa mademu wenzake.” “Hakika wewe
ndio umenifungua macho.” Wakaendelea kuzungumza, akimfungua macho Willy kwenye
mengi aliyokuwa akifanyiwa na Wema, asijue ni mapenzi, yeye akidhani ni
shukurani ya kumfundisha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
hiyo Willy akawa amepoa sana. Wema akajua ni fujo alizozifanya siku ya ijumaa.
Baada ya darasa la mwisho, Wema akamfuata Willy kumuomba wazungumze. Willy
akashukuru Mungu akijua ndio wakati wakumuweka sawa. “Samahani kwa fujo za
ijumaa, Willy. Sijui nilipatwa na nini!”
Akaanza Wema baada yakuridhika wapo peke yao. “Na mimi ningependa kujua Wema!
Sidhani kama ulimtendea haki Pendo!” “Kumbe unamfahamu mpaka jina!?” Akashangaa sana Wema nakuonyesha kuumia.
“Kwenye ule ugomvi wewe hukusikia wakitajana majina? Umetengeneza tukio kubwa
bila sababu! Ni nini kinaendelea!?”
Akauliza Willy taratibu lakini akionyesha kutaka majibu yakueleweka.
“Sijui
nilipatwa na nini Willy! Naomba unisamehe.” Willy akabaki kama asiyeridhika
akimtaka ajieleze zaidi lakini Wema akaonyesha kuishia kwenye msamaha tu.
“Lazima ipo sababu Wema. Usingeweza kufanya fujo kwa mtu aliyekuwa amekujibu
kwa upole kwa kiasi kile! Tena hakuonyesha hata kukataa kuondoka, ila mwenzie!
Ungemfanyia fujo yule mwenzie ningeelewa, lakini si Pendo ambaye alishasimama
na alikuwa akimshawishi Eva, waondoke! Ulimfanyia ubaya usio na sababu!” Wema
akanyamaza. Willy akaamua aweke kikomo hata kama hatafunguka kwake zaidi.
“Inawezekana
nimekuonyesha dalili ambazo sizo Wema.” Akamuona anashituka kidogo. “Naomba
tuheshimiane na kuwe na mipaka. Unanivunjia heshima kwa watu, sieleweki!” Willy
akaongea kwa ukali kidogo. “Si sawa kunikuta nimekaa na mtu, halafu unaanza
fujo zisizo na sababu, tena nikiwa nimekupa maelezo kuwa, nilidhani mmegairi
kula ndio maana nikamkaribisha yule msichana. Ukanivunjia heshima mbele yake,
ukashindwa kunisikiliza ukafanya fujo! Hapana Wema. Naomba tuheshimiane.
Tafadhali. Mimi sizunguki kukufanyia fujo na watu wako. Nakuheshimu na mimi
tafadhali fanya hivyo hivyo.” Willy akaendelea akiweka msisitizo.
“Muda
wakusoma naomba tukutane darasani au tupange sehemu ingine, sio chumbani
kwangu. Naomba heshima ninayokupa wewe na faragha ya mambo yako, tafadhali iwe
na kwangu pia.” Wema Kimya. “Sijui unamahusiano na nani na wala hainihusu.
Nafanya kile kinachotuweka hapa chuoni. Shule, basi. Ukikwama kwenye masomo,
tafadhali uwe huru kuniuliza. Na mimi kama nina uwezo, nitakuelekeza. Kama
sina, tusubiri kwenye kundi la wenzetu, tuelekezane.” “Sawa.” Wema akajibu
hivyo na kuondoka, mpaka Willy akashangaa. Lakini baada yakuzungumza na Kyande na
kumueleza mengi juu ya vitisho vya Wema kwa wenzie huko kwenye hosteli za
wanawake ndipo akajua ni kwa nini Pendo alikataa hata asifike chumbani kwake. Sasa
swali likaja, anampataje tena Pendo na kumueleza au hata kumuomba msamaha
wakutomtetea siku ile!
Akasubiri
siku hiyo cafteria, hakumuona Pendo. Akatamani kumfuata chumbani kwao, lakini
akajua Eva atakuwepo. Akajipitisha huku na kule, hakumuona Pendo akizagaa
kokote.
Siku
hiyo hakutaka hata kwenda kusoma na wenzake. Akatoa udhuru, akaenda maktaba ya
chuo. Akajiambia ili asiulizwe maswali na wenzake, atafute kona, ajifiche
kabisa. Alipozunguka nyuma, mwisho kabisa wa makabati ya vitabu, akamuona Pendo
ni kama amejificha peke yake anasoma. Moyo wa Willy ukaanza kwenda mbio tena.
Akasimama kwa muda akimwangalia pale alipokaa.
Akakusanya
nguvu akamsogelea. Akavuta kiti cha pembeni yake akakaa. Pendo akamtizama.
Alipogundua ni yeye, akanyanyua kichwa vizuri. “Pole Willy, nilikuudhi.” Moyo
wa Willy ukazidi kuvutiwa na Pendo. “Hapana. Nilielewa. Mimi ndio natakiwa
kukuomba msamaha. Siku ile ya tukio nilishindwa kukutetea vyakutosha. Ukaishia
kuumia.” “Wala usijali. Nilielewa tu.” Willy akakunja uso kama yeye ndiye
hajaelewa tena. “Namaanisha nilielewa kuwa tulifanya makosa yakukalia meza
yenu. Makosa yalikuwa ni yangu mimi. Nilikaa tu bila hata kujua nina kaa na
nani. Yaani mawazo yangu hayakuwa pale. Nilipoona viti vitupu, nikakuomba na
kukaa mawazo hayakuwa yakifikiria labda kuna mwenzio anakuja. Halafu jua
lilikuwa kali! Nilizunguka mpaka nikachoka. Unajua nilianzia Cafteria? Niliingia
pale nikidhani nitapata nafasi, lakini foleni ikawa kubwa. Nikazunguka kila
mahali! Pale ilikuwa mwisho nikajiambia nitakula nimesimama. Kwa hiyo nilipoona
vile viti, wala sikufikiria mara mbili.” Pendo alijieleza taratibu kwa sauti ya
chini zaidi kwa kuwa walikuwa makitaba.
Willy
akapata nafasi yakumwangalia vizuri nakuzidi kuchanganywa na Pendo. Macho,
midomo hiyo! Akatamani ambusu hapohapo. Sauti ndio ikamfanya atulie kabisa.
Mpaka Pendo anamaliza hapo kujieleza, hajajua kama ndio anakosa au ndio Pendo
amezidi kuamini kama yeye ni wa Wema! “Kwa hiyo mimi ndio niombe radhi.
Niliingilia.” “Hata kidogo. Hakuna ulichoingilia.” Pendo akamtizama kidogo na
kucheka. “Haya bwana! Acha mimi nirudi kwenye mahesabu niliyokimbia sekondari
nakuja kukutana nayo tena!” Willy akacheka. “Unachukia hesabu?” “Kuliko
nitakavyokwambia. Na ndio maana ‘A’ level nilihakikisha nasoma kila kitu
kisicho na namba isipokuwa tarehe tu. Nikachagua kusoma masoko, nashangaa
nakutana na hesabu tena! Nakaribia kuchanganyikiwa!” “Sasa hizo ni hesabu za
nini?” Willy akamuuliza akicheka taratibu. “Economics! Niambie ni nani anaweka
hesabu kwenye uchumi jamani!” Pendo akalalamika, Willy akazidi kucheka.
“Eva
ametoka kunielekeza, nikamwambia wakati yeye analala, mimi nije huku nijaribu
tena peke yangu. Sijui kama nitaweza!” “Chakwanza, jiambie kama Eva ameweza, na
wewe utaweza.” “Siwezi kujifananisha na Eva hata kidogo! Anaakili yule.” Willy
akacheka. “Namaanisha kama wapo wanao weza, na wewe utaweza Pendo. Hicho unachokifanya
hapo ni sahihi kabisa. Endelea kufanya peke yako. Kadiri unavyoshindwa, ndivyo
utatafuta njia yakuelewa kuliko kuacha kabisa. Kwa hiyo unafanya vizuri.” Pendo
akacheka. “Asante. Basi heri niendelee kabla sijasahau.” “Ndio hali ni mbaya
hivyo?” Wakacheka. “Kama ni mgonjwa, basi anakaribia kupelekwa ICU.” “Maadamu
hajafikishwa ICU, basi lipo tumaini.” “Kweli?” Pendo akauliza na kisauti chake.
“Kabisa. Pambana.” Akacheka na kurudisha mawazo kwenye alichokuwa akifanya.
Pakatulia.
Baada
kama ya lisaa, simu yake ikaanza kutetemeka hapo mezani kama aliyoweka kwenye vibration.
“Samahani.” Akanong’ona na kuiwahi. “Nafanya hesabu
Chris!” Akasikia upande wa pili akicheka. “Wewe
cheka kwa kadiri ya uwezo wako, na ninakata simu.” Akamuona anacheka na
kuchora chini. “Nilimalizia kile ulichoniletea mchana.
Kwa hiyo nimeshiba.” Willy akajua ndio sababu hakumuona Cafteria kumbe
mpenzi wake alimletea chakula! “Asante na wewe.”
Akamsikia akicheka taratibu. “Love you too.”
Akajibu hivyo na kukata akiwa na tabasamu usoni. Akaweka simu chini. Akamuona
anasoma ujumbe na kucheka, kisha kung’ata midomo yake ya chini taratibu kama
aliyefurahishwa na ule ujumbe. Akafikiri chakujibu, kisha akarudisha majibu ya
ujumbe aliosoma na kurudisha simu mezani. Hapo ndio ukawa mwisho wa Willy
wakusoma.
Pendo
alirudisha mawazo kwenye alichokuwa akikisoma na kukifanyia mazoezi, akaendelea
kama aliye peke yake hapo bila hata kumgeukia tena Willy. Willy akabaki
akimtizama upande ule aliokuwa amekaa akimfikiria. Akajua ameshapoteza nafasi
ya kuwa naye sababu ya maneno yaliyozagaa juu yake na Wema. Anamtongozaje tena
wakati anajua yupo Chris, na yeye Pendo anajua yupo Wema! Akajua ndio amekosa
mwanya wa kumkana Wema. Akabaki anafikiria. Hana anachosoma.
Baada
ya lisaa na kama dakika 35 hivi, akamuona ametulia anapitia kule alipoandika.
Akamuona ni kama ameridhika. Akaanza kukusanya vitu vyake. “Shule imeisha
nini?” Willy akarusha swali. Pendo akacheka taratibu. “Nimeishia pale pale
mwalimu wangu alipoishia kunielekeza. Naenda kumuamsha sasa hivi tuendelee na
kingine.” “Kwa maana nyingine ulichoelekezwa umekielewa?” “Wewe umenitia moyo.
Umeniambia nitaweza, nikajiaminisha na mimi, nimeweza.” Willy akacheka akaona
maneno yake yamethaminiwa. “Itabidi na mimi unifundishe.” “Usinitanie bwana!” Pendo
akalalamika huku akiweka vitu vyake kwenye mkoba wake.
“Kwa
nini tena?” Willy akauliza. “Au nimekosea kuomba msaada?” “Wakati nimesikia
darasani kwenu ndio wanakutegemea wewe!” “Unaonekana una habari zangu nyingi
sana Pendo!” Pendo akacheka sana, lakini taratibu. “Sio nyingi.” “Wamekwambia
nini kingine?” Willy akauliza akitaka kujua. “Ndio hivyo tu, hamna kingine.”
“Unanidanganya Pendo!” “Kweli tena. Hivyo tu.” Willy akamwangalia kama ambaye
hajaridhika. “Sina habari zako nyingine Willy, ni hizo tu.” “Kwanza nani
amekwambia habari zangu?” Pendo akatingisha kichwa kukataa kumwambia.
“Naomba
niambie Pendo.” “Siku nyingine, na si hapa.” Akamuona na yeye anakusanya vitu
vyake. “Tunatoka wote.” “Willy!” “Kweli Pendo. Unaonekana unazo habari zangu
nyingi, na kwa vile nilivyokusikia jumamosi, sio sahihi.” Pendo akamwangalia na
kucheka kidogo, akainama. “Kwa vile ulivyoniambia tu jumamosi, kweli sio sahihi
Pendo.” Willy akaongea kama anayetaka Pendo amuamini. Pendo akamwangalia na
kutulia kama anayefikiria. “Huniamini?” Willy akauliza taratibu.
“Haijalishi
Willy. Ila mtu aliyemwambia Eva, ni mtu wako wewe na Wema, wakaribu sana.
Anaonekana anawafahamu vizuri.” Willy akakunja uso. “Mimi sikuwa hata
nikiwafahamu, lakini wakasema nyinyi ni couple ya muda mrefu tokea
tunaanza chuo. Hayo yote Eva alitaka kuyajua kwa sababu alitaka kwenda kumpiga
tena Wema kama kumuadabisha asiwahi kurudia kutuvunjia heshima. Ndio akaanza
kumuulizia yeye ni nani na wapi atampata. Akaambiwa huwa analala chumbani
kwako.” Willy akashituka mpaka akaishiwa nguvu. Pendo akacheka kidogo kisha
akaendelea. “Na akaambiwa akimtaka atampata chumbani kwako. Akaambiwa mpaka
chumba unachoishi na Wema. Lakini akaambiwa wewe ni baunsa.” Hapo Pendo akaanza
kucheka mwenyewe.
“Sijaelewa!”
“Yaani Eva aliambiwa ajiandae kupambana na wewe, eti utamchapa kama mtoto
mdogo. Wakamwambia kule nyuma ya lile jengo lenu, una kama gym ya nje. Wenzako
wanakujaga kufanya mazoezi na wewe. Unanyayua vyuma ndio maana una mikono
mikubwa na kifua. Nahisi walimtisha sana Eva.” Pendo akazidi kucheka. “Eva na
ukorofi wake wote, akapoa na kuja kunielezea kuwa amekwama kumuadabisha Wema.”
Pendo akazidi kucheka taratibu. “Ndio maana na wewe uliniwahi kwa kuniomba
msamaha!?” Willy akamuuliza kwa mshangao. “Mwenzio mimi ugomvi siwezi.
Kilichonileta hapa chenyewe kinaniweka macho, sijakimudu. Halafu eti ndio nianze
bifu na watu, au nijiwinde! Mimi siwezi ndio maana nikaamua nijisalimishe kwako
na ukamwambie na Wema mimi nilikaa tu pale, kwa kuwa nilikuta viti vitupu.”
Willy akaishiwa nguvu kabisa.
“Usiku
mwema Willy. Nakwenda kumuamsha Eva, aliniomba nimuamshe sasa hivi ili asome.”
“Mbona hutaki kujua ukweli wa hayo uliyozungumza?” “Kwa kuwa sioni madhara
yake, na umemtuliza Eva. Hakika angempiga mwanamke wako. Wewe humjui Eva! Mwache
hivyo hivyo aogope, akili aweke shule, tumalize hii miaka mitatu, tuondoke hapa
chuoni. Hata kama wewe sio baunsa, usikanushe.” Pendo akaongeza huku
akinyanyuka na kucheka taratibu. “Usiku mwema Willy.” “Asante na wewe Pendo.
Lakini natamani wewe ndio unisikilize.” Pendo akacheka kwa wasiwasi,
akamwangalia Willy nakuondoka bila yakumjibu kitu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usikose Kufuatilia Mwanzo Wa Pendo Na Willy. Alimpataje Na Kuendelea
Kumng’ang’ania Mtoto Huyo Wa Mama Waliyepitishwa Naye Kwenye Shoruba Nyingi
Mpaka Kuja Kusalimu amri kwa Zelda?
0 Comments:
Post a Comment