Alielekezwa
mpaka akafika nyumbani kwa kina Pendo, akamkuta mama yake na baba yake pamoja
na msichana wa kazi wakimsubiria. Wakatoka nje baada ya geti kufunguliwa. “Kuna
nini mama?” Mama yake akafungua mlango alipokuwa amekaa Pendo. “Najisikia
vibaya mama, sijui nieleze nini?” “Kwa nini!?” Pendo akalia kwa muda, baba yake
akaja kumtoa garini wakaingia ndani. “Kuna nini Sabrina?” Sabrina mwenyewe
alibaki kama amepigwa na butwaa. “Naomba mumpe nafasi Pendo aeleze mwenyewe.”
Sabrina akaongea huku akifikiria.
“Willy ana mwanamke mwingine ambaye anafahamika kwao. Yaani yule
mama amekufa akimtambua yeye kama mke wa Willy, na anaomba apewe urithi mkubwa
kama kumbukumbu yake kwa wajukuu atakaozaa na kuendelea kuzaa na Willy.”
“Subiri kwanza Pendo, huyo mwanamke ni mjamzito!?” Mama yake akauliza. “Tumbo
kubwa kabisa mama yangu! Naumia kuwa mjinga. Ni kama Willy alibadilika kidogo,
si sana lakini kuna vimabadiliko niliviona kwake na si kawaida yake, nikawa nikimtetea
nafsini mwangu kumbe mwenzangu ana mke huko!” Pendo akalia weee. Wazazi
wake wakawa kama wamepigwa na butwaa hawaamini. Willy kwa Pendo! Bora ingekuwa
wanandoa wengine si wao! Wote wakabaki wamepigwa na bumbuwazi.
“Naomba
twende ukaoge ulale da Pendo. Kesho nitakuja kukuona kabla hatujaondoka.” “Sidhani kama nitaweza kulala Sabrina! Willy!”
“Nitakuombea na kukupa dawa ya usingizi. Utalala tu.” Akili ya mama yake ikamjia.
Akasimama na yeye. Wakampeleka chumbani, sababu ya vumbi la makaburini, Pendo
akaoga vizuri, mama yake akamletea dawa za usingizi na nguo za kulalia, Sabrina
akabaki naye hapo kitandani mpaka akalala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jack
akapiga simu. “Uko wapi mama, nataka maziwa ya
wanangu.” Sabrina ndio na yeye akakumbuka ana mapacha. “Kwani niliyoacha wamemaliza?” “Bibi yao anasema walimaliza
mapema tu, na ameshawalisha viazi vyakupondwa, wanataka kulala. Ndio nikaona
wapate maziwa kabla hawajalala.” “Nakuja sasa hivi, nipo karibu. Msiwape
chochote wala kuwalaza mpaka nije, hapa maziwa yanamwagika. Wawekeni chini
waendelea kuchangamka.” “Sawa.” Jack akakubali kwa haraka. “Hapana bwana Jack, umejibu bila kufikiria, usiwapakate,
watalala.” Jack akacheka. “Ulijuaje?” “Nakujua wewe.
Tena sasa hivi wanasinzia, najua utakuwa umewaweka kifuani hapo.”
Akamsikia Jack anacheka. “Umejuaje? Hapa nasikia raha!”
“Bwana Jack! Watalala wakati mimi maziwa yamejaa, yanauma! Waweke chini.” “Sawa
mama.” Jack akakubali bila ubishi.
Baba
yake Pendo ndiye aliyemshusha Sabrina nyumbani kwa Pendo na wala hakuingia.
Jack akawa hajaelewa. “Pendo yuko wapi?” “Leo atalala nyumbani kwao. Waone hawa
walivyofurahi! Washike bwana Jack nikaoge mara moja!” “Mpaka wanangu wakuzirie hilo
ziwa!” Jack akalalamika mpaka mama yake Sabrina akacheka. “Naoga mara moja tu.
Mama nenda kapumzike mwaya. Pole na ulezi.” “Kwani wanao wanashida! Ilimradi
washibe na wawe wakavu. Watazunguka hapo na michezo yao, na wala hawaendi
mbali. Hapohapo ulipowaacha. Baba yao alipokuja ndio nikaona wanamfuata kila anaposogea.
Na kula nako wala si shida. Tena nimewakalisha hapo chini, ukiwasogezea kijiko,
wanafungua mdomo.” “Nishamwambia baba yao, usichana utawashinda hao wanae. Watakuwa
vibonge mpaka nguo zishindwe kuenea. Waone wanavyoniangalia!” “Naomba uende
bwana Brina, kabla hawajalia! Umekuta wanangu wametulia, unataka walale na
machozi?” Sabrina akakimbilia chumbani. Kweli wakaanza kulia. “Nilijua tu.”
Jack akalalamika. Akawabeba wote. “Nenda kapumzike mama. Hawa wakishanyonya tu,
watalala.” Jack akamuaga mama mkwe wake na kupotelea chumbani.
Sabrina
akasikia watoto wake wakilia hapo chumbani. “Natoka sasa hivi.” “Wewe usiongee,
toka.” “Sasa nitatoka na mapovu Jack?” “Sasa ukiongea hivyo ndio wanazidi
kulia.” Jack akawasogeza mpaka mlangoni kwa mama yao. “Jeiline mama?” Sabrina
akamuita, Jeiline akasikia na kunyamaza. Na mwenzie pia akanyamaza. “Mnalia
nini?” “Bwana Sabrina!” Sabrina akaanza kucheka bafuni. Wanae wakaanza kulia
tena. “Kwani mimi nimefanya nini?” Akaanza kuwaimbia, wote wakanyamaza.
Alichofanya Sabrina ni kutoka bafuni, akajikausha akajifunga khanga na kukaa
kitandani kifua wazi. Jack akawaweka wale watoto kitandani, kila mmoja akasogelea
ziwa lake, wakaanza kuvuta wakiwa wamepiga magoti. Jack akaanza kucheka. “Kama watoto
wa mbuzi!” Wakacheka.
Alipoona
wanaanza kulemewa, akawapanga sasa pembeni ya makwapa na kuwaegemezea juu ya
mito kila mmoja na ziwa lake. Wakanyonya mpaka wakalala. “Walikuwa wamechoka.”
Akanong’ona wakati Jack akimchukua Keiline ili kumfanya ateuke, Sabrina
akamuweka Jeiline begani. Akamsugua kidogo tu akateuka. Wakawalaza kwenye
kitanda kimoja cha watoto. “Watakanyagana leo, mpaka wachoke.” Jack akawafunika
vizuri na kurudi kukaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Imekuaje
Brina? Kwa nini hujarudi na Pendo? Wakati ndiye anayetupeleka uwanja wa ndege
kesho?” “Makubwa na mazito yamejiri. Acha nikamwangalie mama yangu kwanza,
nakuja.” Sabrina akavaa nakutoka. Akahakikisha mama yake amelala vizuri,
akarudi kumsimulia Jack mwanzo mpaka mwisho. Jack akainama. “Jack?” Sabrina
akamuita kama kutaka kumsikia maoni yake. “Ile siku ya baby shower nilimuhisi
vibaya Willy, mpaka nikamuuliza kama ni kwema! Alikuwa akiingia na kutoka pale
kwa kaka, hatulii. Na kuna muda akapotea kama lisaa hivi. Wakawa wakimtafuta
ili anionyeshe kitu, hakuonekanika. Aliporudi nikamuuliza kama kila kitu kipo
sawa, akakubali. Sasa si unajua Willy ni mweupe, kwa hiyo nikaona lipstick
shingoni kwake. Nikamwambia kwa kifupi tu, ‘labda hiyo iwe lipstick ya Pendo,
lakini kama siyo, bora ukaoshe shingo.’ Sasa kule kuondoka kwa haraka akielekea
chooni kama aliyepaniki, kukanitia wasiwasi. Nikasema kama ingekuwa ni Pendo,
asingepaniki hivyo. Na nikajiambia huyo msichana ni mkorofi. Anawezaje kumuacha
mwenzie na lipstiki kama sio anataka kumfikishia Pendo ujumbe! Nikaumia sana,
lakini nikanyamaza wala sikuzungumza naye tena.” “Ungemuonea Pendo huruma, Jack!
Aliingiwa kama baridi kwa mshituko.”
“Hawakumfanyia
vizuri hata kidogo.” “Lakini niliwapenda wale wake wenzake. Wake wa kaka zake Willy,
walimtetea sana. Nusu zipigwe pale. Wote wawili wakataka kumchangia Stella yule
dada yao mkubwa.” “Sasa yule ni kopi ya mama yake. Ukorofi na roho zao
zinafanana kabisa. Na haogopi mtu yule dada.” “Nilimuona alivyo na jeuri.
Halafu baba yao alikuwa kimya mpaka mimi nikashangaa kwa nini haingilii! Wanae
wanagombana, yeye kimya.” “Nasikia hata yeye na mke wake hawakuwa wakipata hata
kidogo.” Wakabaki kimya wakifikiria, wakaamua walale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mpaka
asubuhi wanaondoka hapo, wenye nyumba wao hawakuwa wamerudi. Jack akampigia
simu Willy kumuaga, hakupokea, akamtumia ujumbe. Sabrina naye akampigia Pendo
simu kumwambia wamechelewa kuamka, inabidi wawahi uwanja wa ndege. “Nani sasa anawapeleka?” “Da Sabina alishafika muda mrefu.
Hapa tunavyozungumza mimi ndio wa mwisho kupanda kwenye gari tuondoke, Jack
kashatangulia na wanae. Ukichoka na kelele za Dar, njoo Singida upumzike.”
“Kweli Sabrina?” “Jamani da Pendo! Kila siku nakuimbia huu wimbo.”
Akamsikia ameanza kulia. “Usilie bwana. Naomba utulie
ili uweze kufikiria vizuri dada. Kulia haitasaidia tena.”
“Sikuchagua ugumba Sabrina mdogo wangu!”
“Najua na ninaelewa. Ndipo tutamuita Mungu tuliyemuomba
na kumwamini. Hata katika hili atoe suluhu. Nishakuwa kwenye hali ngumu kuliko
hiyo dada, lakini Mungu alinitoa kwa heshima.” “Hakuna
mwanadamu amepita hapa nilipo Sabrina!” Pendo akapinga akilia kwa
kusononeka. “Dada! Unaweza usiamini, lakini nakwambia
hapo ulipo, wala si pa aibu! Kama binadamu kwa sasa utajisikia vibaya sana
nakuona ulimwengu wote unakukodolea wewe macho, unakuzomea na hujui chakufanya.”
“Lakini dada, kama usipo kata tamaa, upo mlango wako wakutokea.
Mungu wako anakujali. Wala hajasinzia kuwa asikuone muda huu unapolia. Dada,
Mungu wa haki yupo, na anajibu. Sema yeye huwa hana kelele nyingi kama shetani
na kazi zake. Ila hiyo siku akinguruma yeye, kila kitu kinawekwa chini yako na
watakaosikia kile atatenda, masikio yatawasha. Naomba tulia dada, muonyeshe
shetani kuwa mtetezi wako yu hai, na atapambana naye tu. Hata kama hujisikii,
piga magoti, lia mbele za Mungu wala si mwanadamu ukazidi kuwapa sababu ya
kukufedhehesha. Futa machozi mbele za watu, mlilie Mungu sirini. Sijui kama
unanielewa?” “Nashukuru
Sabrina mdogo wangu.” Kidogo Pendo akasikika kutulia. “Tutazungumza nikifika. Acha nisichelewe.” Wakaagana,
Sabrina akapanda garini na kuondoka.
Hasidi na
Asili Yake.
J |
ack akasukuma
watoto kwenye kigari chao, Sabrina anafuata nyuma na begi la watoto ambalo
wataingia nalo ndani kwenye ndege. Wakakaguliwa kila kitu, wakaenda kukaa
sehemu ya kusubiri juu kabisa. Kama asiyeweza kutulia akaanza kucheza na
watoto. “Jack! Waache bwana ili hapa pawe na utulivu! Unataka wakulilie ili
upate sababu ya kuwatoa hapo wakati wametulia.” “Ulijuaje!?” Jack akawa
anacheka huku akiendelea kuwachokoza makusudi ili watake kutoka pale
walipofungwa. “Kuna unachotafuta Jack wewe! Utafukuzwa hapa na hao wanao!” Jack
akaendelea kucheka. Mara awabusu, mara awapungie mkono. Wote wakaanza kumlilia.
“Umefurahi sasa?” Sabrina akamuuliza. “Sanaa! Njooni wanangu.” Akaanza
kuwafugua, mmoja baada ya mwingine. “Hakika mimi siwajui nyinyi.” Sabrina
akageuka upande mwingine kabisa. Jack akazidi kucheka. “Eti mami hatujui sisi
watatu? Ametugawa bureeee!” Jack akatoa watoto wote kwenye kigari chao, akaanza
kucheza nao.
Sabrina
akasikia wakicheka na kelele zao, yeye mwenyewe akaanza kucheka. Akasikia
baadhi ya watu wakimsifia Jack kuwa ana watoto wazuri sana, na wenyewe
wanacheka. Sabrina akavutiwa akawageukia. Wala hawakuwa na habari naye, wapo
busy wakicheza na baba yao. Akagundua kuna mtu ameshika gazeti anawatizama
sana. Hakuwa mbali na walipokuwa wamekaa wao ni kama na yeye alikuwa upande
huohuo wanao subiria hiyo ndege. Alipomuangalia vizuri akagundua ni Max. Sabrina
alishituka akatamani akusanye familia yake akimbie hapo huyo mwanaume asione
wanae, akatibua mambo.
Alimjua
Max mpenda kesi. Ataunganisha habari, atagundua ni watoto wa Tino na kuanzisha
kesi tena. Akabaki ameduaa macho yakashindwa kutoka kwa Max. Wakajikuta
wanaangaliana. Max akasimama na kumsogelea Sabrina pale alipokuwa amekaa. Ili
kujituliza, Sabrina akaona asalimie. “Shikamoo!” “Marahaba. Niliwaona wakati
mnaingia, nikasema labda nimewafananisha!” Sabrina akaingiwa na wasiwasi zaidi
akajua ameshawaona tokea wanangia, hawezi kujificha tena. Jack mwenyewe alikuwa
amejaa pale na watoto wake, huwezi kuwakana. “Hapana. Ni mimi na timu yangu
yote. Kelele hizo za watoto hao watatu zinanihusu.” Max akacheka, kwamba na
Jack ni mtoto.
“Umebadilika
na kupendeza sana Sabrina! Nilisikia mnaishi Singida.” Sabrina akashangaa na kuzidi kuingiwa hofu,
kwamba mpaka anajua anapoishi! “Tulikuja kwenye msiba.” Hakutaka kumuhakikishia
wanapoishi. “Poleni sana. Nani amefariki?” Max akaendelea kudadisi, Sabrina
asimuelewe nia yake. Lakini akajibu tu. “Kama utamkumbuka yule msimamizi wa kiume
wa kwenye harusi yetu, aliyesimama na Jack, mama yake alifariki jumatano iliyopita,
nchini India.” “Poleni sana. Kumbe alikuwa mgonjwa?” “Kwa muda mrefu tu. Watoto
na mama hawajambo?” Sabrina akaona abadili mazungumzo kumtoa kwake.
“Tunamshukuru
Mungu, hatujambo. Ukaribie tena nyumbani.” Jack akasogea na watoto. “Nimehesabu
dakika za hii salamu, nimeona zinazidi kwenda, nikajua naibiwa mke hapa Dar.
Mimi ni mume wa Sabrina. Huyu dada mkubwa anaitwa Jeiline, na huyu dada mdogo
anaitwa Keiline. Watoto wetu.” Sabrina akajisikia vizuri mbele ya Max aliyekuwa
akijua hila yake dhidi yake hata asiogope tena kukutwa na hao watoto wa kizungu.
“Huyu ni Max. Unakumbuka nilikutambulisha ukumbini na mkewe siku ya harusi
yetu?” Sabrina akataka amkumbuke Max vizuri. “Akili siku ile, tena mida ile, haikuwa
pale kabisaa. Mawazo yalishahamia honeymoon.” Sabrina akampiga ngumi Jack akiwa
ameshangaa asiamini ameongea hivyo. Jack akacheka na kukimbilia pembeni kidogo.
“Watu tunaadhibiwa kwa kuwa wakweli!” Jack akalalamika. Akamgeukia Max. “Ningekupa
mkono lakini kama unavyoona, binti zangu wamejaa kila mkono wa dad yao!” Jack
akabusu mikono yao kwa pamoja. Max akacheka akiwatizama.
“Mnafamilia
nzuri sana. Hongereni.” “Asante.” Wakaitika kwa pamoja wazazi hao kama walioiba
watoto wakizungu. “Basi mkiwa hapa mjini msiache kuja kututembelea. Mke wangu
alikupenda sana Sabrina.” Sabrina akacheka kinafiki akishangaa kipi
kilichobadilika! Ni kweli walimkaribisha nyumbani kwao na kuwaaga vizuri sana.
Lakini Max akaja kubadilika sana baadaye na kuchangia kumbadilisha Tino kwa
hali ya juu. Sabrina akawa anamshangaa moyoni asimuelewe sasa hivi anachokitaka
ni kipi baada yakufanikiwa kumtoa kwa Tino! Au kwa kuwa amemuona kwa kina
Msindai ndio anajikomba!
Jack
kimya akiendelea kucheza na watoto kama hawasikii, ila amesimama pale pale. “Hivi
unajua mke wangu anafanya kazi chini ya kaka yako?” Jack kimya, akaendelea kupeana
mabusu na wanae palepale mbele yao. Sabrina na Max. Walikuwa wakipeana zamu,
Jack anambusu mmoja baada ya mwingine, wanachekaa kisha na wao wanarudisha mabusu
kwa baba yao kwa pamoja, kisha wanacheka tena kwa sauti na kujipigia makofi
kama kujipongeza.
“We
Jack?” Sabrina akamshitua kwani walibaki wakiwatizama wao. “Kumbe unamzungumzia
kaka yangu mimi!?” Kumbe Jack alisikia! “Yeah!
Tena wanafahamiana vizuri tu na mke wangu. Wapo ofisi moja kabisa.” “Safi sana.”
Jack akajibu tu hivyo akarudisha akili kwa watoto wake. Max akamgeukia Sabrina.
“Kama hutajali, naomba namba yako ya simu ili tuwasiliane.” Jack akashituka
mpaka akatoa macho. Akamtizama Max akiwa amebadilika kama sio yeye aliyekuwa
akicheka muda mfupi na wanae. Max akababaika kidogo maana Jack aliwasogelea tena
kidogo. “Heki No! Tena ya msisitizo mkubwa kabisa. HAPANA.” Bila
aibu Jack akakataa. “Kwa nini!?” Max akauliza akibabaika, Sabrina akajua mumewe
amemkumbuka Max vizuri tu na ndio maana alisogea pale. Sabrina akabaki kimya
akifurahia moyoni amepata mtetezi dhidi ya Max aliyemtenda kupitia Tino
walipokuwa Moshi, Max asijue Sabrina anajua.
Jack
akawaweka sawa wanae ili kujibu swali la
Max kwa msisitizo. “Nimekataa kwa sababu mimi ni mumewe, sitaki uwe na namba ya
simu ya mke wangu. Nafikiri hiyo ndio sababu kubwa na itoshe!” Akajibu hivyo
Jack akimtizama Max machoni. “Samahani sana, nia ilikuwa njema tu. Kwa salamu. Zaidi
kwa mke wangu. Alimpenda sana Sabrina.” “HAPANA. Leo ndio mnatafuta kuwa na
mawasiliano na mke wangu mimi!? Mlikuwa wapi muda wote huo!? Mlisahau kama
mnampenda!?” Max kimya, Sabrina akainama. “Naomba tuheshimiane na kuwe na mipaka jamani!
Twende Brina. Naona salamu inatosha.” Watu wa karibu walikuwa wakiwatizama,
Sabrina alijua wazi wanafuatilia kila kitu kinachoendelea pale, kwani tayari
walishavutiwa na watoto wao, wakawa wakiwafuatilia tokea zamani.
Sabrina
akakusanya vitu vyake pale mezani, akaondoka pale kuelekea alipokuwa amekaa
Jack na wanae kabla hajawasogelea pale, tena bila kuaga wala kumtizama tena Max,
Jack akafuata nyuma na kuendelea kucheza na wanae bila kuonyesha kama kuna
alilofanya la ajabu. Watoto wake walipoona baba yao amerudisha akili kwao,
wakaanza kucheka tena upya kama mwanzoni. Safari hii Sabrina alikaa nao karibu
kabisa. Walimuacha Max amesimama palepale na hawakuonyesha kumjali tena.
Kwa
bahati mbaya wote wakapanda ndege moja kuelekea KIA, na wote wakakaa viti vya
karibu kabisa huko mbele ila Max alikaa nyuma yao. Huko kwenye ndege ungemsikia
tu Jack na wanae wanavyocheka na kucheza kwa sauti. Ndege ilipotulia tu angani,
akamtoa Jeiline kwenye kiti chake alipokuwa amekaa na mama yake, akahamia naye
alipokuwa amekaa na pacha mwingine. Michezo ikaendelea. “Mnapiga kelele Jack na
wanao jamani! Abiria wengine wamechoka wanataka kupumzika. Mrudishe Jeiline
hapa mtulie.” “Keiline ndio anacheka kwa sauti ya juu.” Akamtekenya na Jeiline.
Akacheka sana na yeye. “Kumbe na Jeiline pia! Mami anasema muache kelele binti
wa Msindai. Mmesikia?” Jack akaendelea kucheza na wanae bila kujali.
“Hakika
mtashushwa njiani.” Jack akacheka sana. “Watatupa na parachuti mimi na
wanangu?” “Hakika watawashusheni bila parachuti!” Jack akazidi kucheka na
abiria wa mbele yao nao wakacheka na kugeuka. Ndio wakajua watu wanawasikiliza.
“Mna watoto wazuri sana. Mke wangu alikuwa akiwaangalieni tokea hatujaondoka!” Jack
na Sabrina wakacheka. “Asanteni, lakini nakaribia kuwafunga mdomo wote watatu.
Ili hapa patulie. Samahanini kwa kelele jamani.” “Hawakeri hata kidogo.” Mkewe
huyo abiria mwenzao akaongeza. “Umesikia Sabrina?” “Wewe acha kelele Jack bwana!”
Wakazidi kucheka. “Tena hivyo wanavyocheka ukiwasikiliza, unapata burudani!”
“Asante mama yangu. Sasa nashangaa Mami anaita kelele na si burudani!” Jack
akarudi kucheza na wanae, Sabrina akaguna. “Safari nyingine mnakwenda kukaa
nyuma kabisa ya ndege. Viti vya mwisho kabisa huko.” Watu wakacheka tena.
“Kwani sisi tunashida! Eti wanangu? Mnajali mlipo nyinyi au ilimradi dad
awepo?” Watoto wakaendelea kucheka huku wakiongea kitoto Jack anafurahi! Max
kimya viti vya nyuma lakini Sabrina alijua anawatizama tu na kusikia ile fujo.
Walimuacha
Max KIA, wao wakasubiri ndege nyingine ya kuunganisha kwenda Singida. Abiria
waliokuwa nao mbele wakawa wanapita wakiwapungia mkono wale watoto, na Jack
naye anajibu kitoto akiwa amewabeba wote wawili, “Bye Byee!” Ilibidi Sabrina ndio asukume tu kigari cha
watoto kwani Jack aliwabeba. Akamuona Max anawapita bila kuaga wala kuwasemesha
chochote, Sabrina akaanza kucheka taratibu, Jack akamuona mkewe akicheka, wala asimuulize
akaendelea na watoto wake.
Max kwa
mkewe na Tino.
M |
ax alikuwa
amejawa na hasira kupindukia. Alidhalilishwa mbele ya watu vibaya sana. Alipotoka
tu hapo uwanja wa ndege akampigia simu mkewe. “Umefika
salama?” Mama Kundi, akamuuliza mumewe. “Nimefika
salama, lakini niliyokutana nayo huku, yamenichanganya haswa!” “Nini na wapi
tena!?” Mama Kundi akaendelea kuhoji. “Sijawahi
kudhalilika duniani kama leo.” Max akalalamika kwa mkewe. “Pole. Ni nini tena!?” Mkewe akamuhurumia na kutaka
kujua kulikoni. “Nimekutana na Sabrina pamoja na
familia yake. Yaani mumewe, yule kijana wa Msindai na watoto wao.” “Ehe!” “Bwana
ulikuwa sahihi. Ni mapacha, halafu nisikilize sasa, wakizungu kabisaaaaaa!”
“Haiwezekani Max!” Mkewe hakusadiki.
“Kabisa. Jack na mkewe si wote maji ya kunde tu, sasa wale watoto
wawili ni wakike. Ni kama Sabrina amejizaa mwenyewe. Lakini mama, wale watoto
ni wazungu.” Max akamuelezea yale aliyoyaona kati
yao hao wanandoa. Vile Jack alivyomdhalilisha mbele ya watu. Max akamlalamikia
mkewe. Akaeleza vile Jack anavyojifanya ni baba kwa wale watoto ambao Max aliendelea
kusisitiza kuwa sio wake hata kidogo. “Bwana watoto ni
wazuri hao, huwezi kuwalinganisha na huyo mtoto wa Msindai hata kidogo! Mpaka
nimewapiga picha.” “Haiwezekani Max!” “Nilishindwa kujizuia, nikasema nipate
ushahidi, na hivi huyo Jack alikuwa mkorofi kwangu, nikahangaika mpaka
nikawapata wote wanne, kisha ingine akiwa amebeba hao watoto.” “Nirushie na
mimi.” “Lakini chonde mama, usije sambaza tukaingia matatizoni.” Max
akamtahadharisha mkewe. “Mimi sio mjinga bwana. Nataka
kupata fahari ya macho tu.” Mama Kundi akaweka msisitizo. Mumewe
akamtumia.
“Umewaona?” Max akamuuliza mkewe. “Max! Hawa watoto huyu Sabrina kazaa na mzungu gani!?
Inamaana alipoondoka hapa na Tino, huko Moshi akapata mwanaume wa kizungu!
Maana kabla hajazaa alikuwa na kaumbo kama Miss Tanzania!” “Hata sasa
ameongezeka, lakini si sana. Ni kunawili tu. Si umemuona?” “Hapa huwezi
kumtambua vizuri, na hivi hujapata uso wake yeye! Bwana mtoto amebadilika huyu!” “Sana! Hakika amebadilika Sabrina. Hata
ukimtizama sasa hivi, utajua mambo yake yapo tofauti. Nadhifu mno. Lakini mimi
nimefikiria.” “Nini tena?” Mkewe akamuuliza, akisikika wazi bado akili
zipo kwenye picha.
“Tunaweza
tukawa tunafikiria mbaliii, ukute hawa watoto ni wa Tino!” Mkewe kimya. “Upo?” “Haiwezekani Max, bwana! Hawa watoto ni wazungu
kabisa!” “Mama yake Tino alikuwa muitaliano kabisa. Uliona picha za watoto wa mama
zake wakubwa Tino?” Mkewe akatulia kama anayevuta kumbukumbu. “Basi kumbuka ile picha aliyotutumia Tino wakati ule
ameondoka tu hapa nchini, akasema ni mmoja wa mtoto wa mama yake mdogo anayeishi
nao huko. Walipiga wawili tu.” “Sasa nakumbuka.”
Mke wa Max akakumbuka. “Sasa uzungu ule na huo unatofauti gani? Ni hivyo hawa
watoto wamefungwa hizo riboni kubwa zenye maua kichwani. Lakini ukiwaona hivi
kwa karibu, nywele sio za mchanganyiko mama, ni za kizungu kabisa kama yule
ndugu yake Tino.” Kimya mama Kundi akiendelea kuangalia picha.
“Hao watoto ni wa Tino kwa hakika. Sabrina haonyeshi kama ni malaya
wa kiasi hicho. Piga mahesabu ya tokea waage hapo nyumbani na mpaka
alipojifungua. Utagundua mimba ni ya kipindi Sabrina yupo na Tino. Hao watoto ni
wa Tino bila ubishi. Tino hakubeba damu kali ya kizungu, wanae ndio wamechukua
damu ya upande wa mama yake Tino.” “Mungu wangu Max! Ujue wewe ndio umesema
kweli!” Baada ya kuhesabu mama Kundi ndio akapata jibu.
“Umeamini sasa?” “Kabisa. Siku zinagongana!” Mkewe
akawa amekubali kabisa.
“Sasa jamaa yeye si anajidai mbabe, ananidhalilisha mimi mbele ya watu,
nampigia Tino mwenyewe kumwambia watoto wake wapo, jamaa anamiliki. Asijidai
mjanja. Namshawishi Tino mpaka akubali aje tudai watoto wake.” “Max!”
Mkewe akaingiwa na wasiwasi kidogo. “Ulaji mwingine huo
mama.” Max akaanza ushawishi. “Kesi dhidi ya
Msindai! Itanguruma mno, kila mtu atajua mimi ndio naisimamia. Mama, nitakuwa
gumzo hapa nchini. Na hivi ushahidi dhidi yake nitakuwa nao! Yaani mpaka sasa
hivi, nishajua jinsi yakumshinda. Nitaua ndege wawili kwa jiwe moja. Nitamfanyia
kazi Tino. Na unamjua Tino huwa analipa bila shida. Na nitazidi kuwa mashuhuri.
Nitajulikana haswa.” Max akaongea kwa kujiamini akiwa amehamasika haswa.
“Naomba kuwa mwangalifu Max, usije niharibia ajira.” “Nikuharibie
ajira kwani serikali ya Msindai hii!?” Max
akashangaa sana tena kwa hasira. “Lakini anao uwezo wa
kunifanya chochote, usije sahau hilo mume wangu.” “Akufanye chochote yeye kama
nani!? Na yeye ameajiriwa kama wewe tu! Akileta na yeye ujuaji tunamtengenezea
zengwe lake. Tena nitahakikisha tunakwenda kisheria kabisa. Tunamwanzishia kesi
nzito tu. Hata kashfa dhidi yako. Tena tunaweza kumuwahi mapema kwa haraka kabla
hajakugusa wewe. Na yeye atatumbuliwa
vilevile. Kwani uwaziri si cheo tu alichopewa? Sasa tutamuonyesha kwamba mjini
wapo watu wanaakili na uwezo kuliko yeye aliyekutana na huo uwaziri wakupewa. Wasilete
ujuaji! Nina uzoefu mama. Nitamuweka sawa na watatupisha tu mjini.” Mkewe
akawa ameingiwa na hofu lakini Max akaendelea kumshawishi mkewe zaidi akimweleza
atafanya nini na nini kwenye hiyo familia ya Msindai mpaka wao watabaki salama.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ø
Max amerudi kazini. Tena
safari hii yupo tayari kupambana na kina Msindai wote mpaka bosi wa mkewe,
waziri Msindai. Na sifa ya Max ni kutoshindwa kesi, na ameshamuweka mkewe
upande wake, wapo tayari kumtengenezea zengwe Waziri Msindai, awapishe mjini.
Kipi kitajiri?
Ø
Usikose kufuatilia na kisa
cha mapenzi ya dhati ya Pendo na Willy na wao tokea chuoni, lakini kuja kuingiliwa
kikatili kwa kiasi hicho! Kisa ni nini? Nani amefanikiwa kupenyeza mkono wake
kwenye penzi zito na la muda mrefu? Ilikuaje? Historia ya Pendo na Willy?
Usikose muendelezo. Mambo ndio yanapamba moto.
0 Comments:
Post a Comment