![]() |
Mama
Sabina.
S |
iku
inayofuata usiku mama yake Sabrina akapiga. Sabrina akaanza kucheka. “Vipi?” “Nakwambia leo tumecheza ngoma zote na hawa wajukuu
zako. Mpaka ikabidi Jack akaite nesi atusaidie kuwaogesha lakini pia
ikashindikana.” Wakacheka. “Nesi amekuja,
ameanza kuwaogesha, nayo ikawa shida. Jack anasema wanaumizwa kwenye vitovu. Hilo
zoezi limeendelea hapa, zaidi ya masaa! Mara Jack aseme wafunikwe kwanza, anahisi
huyo nesi anakosea. Sasa yeye Jack mjuaji ndio akawa anamuelimisha huyo nesi
jinsi anavyojua yeye juu ya watoto. Haya, nesi akifanya anavyotaka yeye,
anakasirika anasema anahisi anavyowashika yeye vile wanaumia! Ikawa shida hapa,
mwishoe akasema wafutwe, na kuvalishwa hivyohivyo. Inatosha.” Mama
Sabina alikuwa anacheka mbavu hana.
“Kwa hiyo watoto wakike leo wamelala bila kuoga!?” “Na sidhani kama
wataogeshwa hivi siku za karibuni.” “Basi vitomvu vitaoza!” “Mimi naona bora uje
tu mama. Tumekutana wajuaji wawili tusiojua. Hakuna tulilofanya kwa watoto
zaidi ya kubishana na kunyonyesha siku nzima.”
Mama Sabina akazidi kucheka. “Baba yao ana elimu
aliyopewa siku moja ile ya baby shower, na kuona kwa watoto wengine
kupitia kwa baba yake, daktari bingwa wa watoto hapa nchini! Huna
utakalomwambia akakubali. Mjuaji halafu muoga. Anasema watoto wake ni walaini
sana, anaona sio sawa wakashikwa shikwa bila gloves. Gafla ameamua hakuna tena
kutafuta msichana wa kazi, mpaka wakomae. Lasivyo anaweza kuja mtu
akawaambukiza magonjwa.” Mama yake akazidi kucheka. “Nakwambia ni kazi wala si ndogo. Huyo nesi mwenyewe alimuomba
awashike na gloves.” “Sabrina!” Mama Sabina akashangaa sana. “Kweli mama. Na amesema kuanzia sasa, hakuna mgeni kuwashika
tena. Wawe wanawaangalia tu.” “Kama mbuga za wanyama?” Wakazidi kucheka.
“Naomba tu uje, utusaidie kwa muda mama. Lasivyo hakuna kitakachofanyika
hapa, na naona kazini hatarudi. Tuna hekaheka hapa, haziishi. Kila kitu
anafanya mwenyewe. Kupika na watoto pia ni yeye, mpaka namuonea huruma. Hataki
nifanye chochote, anasema nipumzike. Mpaka nahisi atachanganyikiwa.”
Wakacheka. “Mimi nipo tayari.” “Na baba? Nahisi mkija
naye akili itatulia. Huku tuko wenyewe. Nyumba ni kubwa na kuna nafasi. Jack
mtu mzuri, hana shida.” “Tumemuona. Sasa utatusaidia nauli? Maana hali sio
nzuri. Ile mahari yako ilitusaidia kulipa ada za wadogo zako na kulipalipa
madeni tuliokuwa tukidaiwa. Na ikatusaidia kwenye..” “Mama, ile pesa ilikuwa
yenu. Matumizi ni juu yenu. Huhitaji kuniambia jinsi mlivyotumia. Nakurushia
pesa sasa hivi, au unafikiri Jack awasaidie kukata tiketi? Wanaye mtu wao ni Agent
wa ndege.” Mama Sabrina akashituka.
“Unataka tuje na ndege!?” “Ndio naona itakuwa rahisi, huku mbali! Au unafikirije?” Akasikia mama yake anashangilia. “Tutaondoka na ndege baba Sabina!” Akasikia akimwambia baba yake, wakacheka. Sabina akachukua simu. “Naona unataka kuwafanya kina mama washindwe kulala! Mama haamini!” Sabrina akacheka tu. “Jamani kuzaa kuzuri. Na mimi napanda ndege kwenda Singidaaa!” Sabrina akacheka wala asijue kama wangefurahia hivyo. Wakazungumza wakitaniana. Wakaagana.
Wazazi wa
Sabrina, Singida.
M |
ida ya
mchana Jack alikwenda kuwapokea wazazi wa Sabrina uwanja wa ndege. Ilipofika jioni
wakaingia. Sabrina alikuwa ameshawaandalia sehemu ya kufikia kwenye chumba
alichokuwa akiishi Emma. Nacho walikitengeneza vizuri tu. Wakaongeza choo humo
ndani na kujengea sakafu ya marumaru mpaka bafuni. Kikawa chumba kizuri na
hadhi. Sabrina alitandika mashuka masafi na kuwawekea mataulo safi bafuni.
Kikawa kipo tayari kutumika. Jack akawaingizia mizigo yao hapo ndani kwenye hicho
chumba. “Kweli mnanyumba nzuri sana! Kuanzia nje mpaka ndani pako vizuri sana.”
Baba yake Sabrina akasifia, na mama yake akaongeza. “Asanteni.” “Ni kazi ya Sabrina
hii. Palikuwa jangwa hapo nje. Tulikuwa na kazi ya kumwagia maji uwanja kila
siku asubuhi kupunguza vumbi lisiingie ndani.” Wakacheka.
“Sasa
wajukuu wameogeshwa leo?” Mama Sabina akauliza, Sabrina akaanza kucheka huku akimwangalia
Jack. “Sasa unacheka nini? Si mseme mimi ndio nimewaogesha?” Jack akajibu. “Amewafuta.
Kule sio kuogeshwa bwana.” Sabrina akajibu akicheka. “Vyovyote utakavyosema.
Wanangu hawajaenda kucheza nje. Na mbona husemi jinsi nilivyowafuta vitomvu
vizuri, mpaka nesi mwenyewe amenikubali.” Sabrina akazidi kucheka. “Na leo pia
nesi alikuja!?” Mama Sabina akauliza akishangaa. “Leo alikuja kuangalia tu,
wala hakuruhusiwa kushika mtoto hata mmoja. Baba yao ndio alikuwa akiwahudumia,
sisi watizamaji.” Wakazidi kucheka. “Lakini dad amefanya kazi nzuri sana, mpaka
nesi amemsifia.” “Asante sana Sabrina. Hilo ndilo ulitakiwa kulisema tokea
mwanzo.” Jack akaondoka hapo akaelekea jikoni kuandaa chakula.
“Sasa
hao watoto lazima waoge Sabrina na wanyooshwe.” Mama Sabina akanong’ona baada
ya Jack kuondoka. Sabrina akaanza kucheka. “Mimi naona mazungumzo hayo uyafanye
baba yao akiwepo hapa. Nahisi kwako atakuonea aibu. Huyo nesi mwenyewe ni hivyo wanafahamiana,
anamjua Jack na anaelewa ni watoto wa kwanza. Lakini ingekuwa mtu mwigine, asingerudi
leo. Jana alimgombesha kabisa.” Mpaka baba yake akacheka. “Sasa hapo walipo
kwenye hivyo vibembea, wanatolewa au ndio tunawaangalia tu?” Baba yake
akauliza, huku amewasogelea wakizungushwa kwenye vibembea vyao, wamelala. “Wewe
baba kaoshe mikono hapo sehemu ya kulia chakula kuna sinki linatoa maji. Kuna
sabuni hapohapo na taulo la kukaushia mikono. Uje uwashike utakavyo. Nyinyi atawaonea
aibu. Au unataka nikuletee hapohapo unawe kwenye beseni?” “Wala haina sababu.
Acha nikaoshe kwenye maji mengi. Tumekuwa na safari ndefu, tumeshika kila
mahali. Nahitaji maji mengi. Nitakwenda tu. Ila tu sitaki tumuudhi.” “Hawezi.
Si anajua mpo hapa kutusaidia! Nyinyi atawasikiliza.”
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bila
ya kuchelewa wala kusita mama Sabina akashika kazi ya ulezi kwa hao watoto. Akaowaogesha
hao wajukuu kwenye maji mengi tu na kuwasafisha vizuri. Akawafanyia mazoezi
yakuwanyosha vizuri, akawavalisha nguo za kulalia, wakachanwa na nywele, Jack
mwenyewe akakiri watoto wake wamependeza. Huyo mama alishika usukani wa maisha
ya pale ndani akawa kama mwenyeji. Jack alipomuona anayoyafanya, akajua ndiko Sabrina alikorithi. Akiwa ametulia bila
paniki wala papara alifanya mengi kwa wakati mmoja. Alianza kwa watoto na mzazi.
Inafika muda wa usiku, mzazi na watoto wote amewaogesha. Mzazi akamkanda tumbo
la uzazi. Chakula kizuri kwake, na wanae wakanyonya vizuri akimsaidia kuwachezea
vimiguu vyao, wakanyonyeshwa mpaka bibi yao mwenyewe akaridhika na kwenda kuwalaza.
Usiku huo wa kwanza tu, mambo yakawa yameenda vizuri na kwa utulivu. Jack
mwenyewe alipata muda wa kupumzika.
Siku
zilivyozidi kusogea yule mama akapata uhuru mle ndani, akamsaidia Jack hata
mambo ya mle ndani. Akawa akimuuliza tu Jack anataka kufanywe nini, basi huyo
mama anamsaidia mpaka kupika vyakula vya nyumba nzima, Jack akabaki kushika tu
watoto wasafi, hana kazi, akifurahia likizo yake ya uzazi na wanae. Baba Sabina
yeye akawa amkisaidia kazi za nje. Wazazi hao watu wa shamba, wanajishugulisha.
Kazi za mkono si tatizo. Basi baba Sabina yeye akawa akimka tu, anaanzia nje
kwenye maua na usafi wa ua. Jack alikuwa akiona haya, wakwe kutumika nyumbani
kwake! Lakini Sabrina akamwambia awaache wafanye, ndipo watajisikia kuishi pale
kwa uhuru. Hata baba mkwe wake alimwambia yeye na mkewe ni watu wa shamba.
Maisha yao ni kazi. “Tutakufa haraka sana kama tusipofanya kazi baba.” Jack
akacheka. Walikuwa wazazi washupavu, miili mizuri kama hawana watoto wakubwa
kama kina Sabina. Jack akabaki kushukuru tu.
Vitomvi
vikakauka mpaka kuanguka na watoto wakaendelea kukua vizuri tu hata miili
kuongezeka na kuanza kuonekana vizuri kwani walizaliwa wadogo sana. Huyo bibi yao
akawa akiwapigania lishe, akiona tu muda wao wakula umefika, hata kama yupo
jikoni, ataweka kila kitu pembeni, na kwenda kumuamsha Sabrina aanze
kunyonyesha. Na kweli vitoto vikaonyesha kubadilika vizuri vikawa vikivutia
sana. Swala la kunyolewa nywele zote hapo Jack alikataa kabisa. Akataka wakatwe
tu ncha za juu wasibakishwe upara. Ikabidi mama Sabina akubaliane naye. Nywele zenyewe
zilikuwa zikiota kama uyoga. Vichwa vilijaa nywele nyingi, nyeusi
zilizojiviringa. Vimidomo vya pinki kama Tino. Wakaendelea kukua watoto wasio
walizi kabisa. Ukiwasahau nao hutawasikia wakilia. Kimya hata wakitoka
usingizini, utawakuta tu macho, wametulia. Hilo likampumzisha Sabrina.
Angalau
kwa mara ya kwanza Sabrina naye akaanza kuongezeka mwili kwa kula vizuri na
kupumzika. Mama yake alikuwa akimsisitiza awe anakula mara kwa mara sababu ya
kunyonyesha. Mwili wa umama wa Sabrina ukaanza. Kwa mara ya kwanza maishani,
Sabrina akawa mtu wa kula kulala na kunyonyesha tu. Akapendeza haswa. Akaanza
kujazia sehemu za mwili wake. Uzazi ukawa mzuri. Akawa anamuona vile mama yake
anavyojituma kwa moyo mmoja, baba yake akisaidia nje asiamini Mungu
alivyomkumbuka na kumrejeshea hao watu wa muhimu kwake. Na yeye akabaki
akimshukuru Mungu kwa hao watu alioruhusu wamzunguke kwa wakati huo.
Mwezi ukaisha likizo yake nayo ikaisha Jack akarudi kazini watoto wakiwa wameshachukua sura za tofauti. Wamekomaa japo walizidi kuonekana na asili ya kizungu kabisa. Lakini mapenzi ya Jack hayakuwahi kubadilika. Akitoka kazini, yeye na watoto tu. Imani naye akarudi kusaidia kazi wakati Jack akiwa kazini, basi anafika hapo kumsaidia mama Sabina kazi atakazompangia. Akawa anakuja asubuhi mpaka mchana. Mama Sabrina anampangia kazi, akimaliza zaidi usafi wa nyumba, anaondoka. Sabina naye alikwenda kuwatembelea. Alikaa siku mbili tu, akarudi kazini. Sabrina akakazana na kunyonyesha.
Sabrina
akakazana na kunyonyesha. “Hivyo unavyokazana, watakuwa haraka sana.” Mama yake
akamsifia. Sabrina hakuwa mvivu wa kunyonyesha. Si mchana, si usiku wanae
wakiamka tu, anawanyonyesha. Na alipenda wote wanyonye kifuani si kwa kutumia
chupa akihisi anaweza asiwe msafi wa kusafisha chupa ipasavyo. Na akamwambia mama
yake maadamu yupo tu nyumbani, ni bora wakiwa wadogo vile wanyonye tu. Basi
wakiamka kwa pamoja atatumia mto aliopewa kwenye baby shower yake,
atawapanga hapo, wanaanza kumnyonya mama yao wote kwa pamoja mpaka washibe.
Walipofikisha
miezi mitatu hapo Jack ndio akawa kama amechanganyikiwa na hao watoto. Shingo
zilishakomaa, wakilala na tumbo wanaweza kunyanyua shingo, basi kama hatalala
nao chini kabisa sakafuni chumbani kwao ambako kulitandikwa kapeti, basi
utamkuta Jack kitandani akicheza nao na kuzungumza nao kama mtu mzima. Na
walishaanza kucheka kwa sauti, hapo usingemkuta Jack kwenye simu. “Mgeni akija
hapa, hajui watoto ni wapi, na baba ni yupi!” Sabrina alikuwa akisema kila
wakati. Jack hatajali ataendelea kucheza nao tu. Aliwaita kwa majina yao kila
wakati akitaka wafanye hiki na kile. Na Mungu akawa upande wao, hawakuwa
wakiugua. Ilimradi washibe tu, basi.
Mama
yao alikuwa akiwavalisha vizuri sana. Kila wakati watoto hao ni wasafi na riboni
yenye uwa kichwani. Jack alikuwa na kazi ya kupiga picha mchana na usiku. Akirudi
Jack kutoka kazini, hao watoto wakisikia tu sauti yake, wote vichwa juu
wakimtafuta. “Mtoto mwenzao karudi.” Sabrina alikuwa akimsengenya. Wakiwa na
miezi mitatu tu, waliweza kumjua baba yao na sauti yake. Walipofikisha miezi
minne, wazazi wakaondoka hapo, na kurudi nyumbani kwao. Wakawaacha watoto wamechangamka
kabisa.
Mapenzi
kati ya Jack na Sabrina yakazidi. Usiku nyumba wanaachiwa wao wawili tu na
watoto tu. Hakuna Emma, wala wazazi. Imani anayekuja asubuhi kusaidia kazi akindoka
mchana anabaki Sabrina akimsubiria Jack. Jack akitoka kazini, anarudi nyumbani
kucheza na watoto, anakwenda kwenye mambo ya chama, akirudi watoto tena mpaka
walale wanabaki na Sabrina, mapenzi ya haja yanaanza. Wataridhishana hapo,
ndipo kulala. Mida ya asubuhi ambayo Imani anakua nyumbani, ndipo na yeye
Sabrina alikuwa akitoka kwenda kwenye shuguli za chama. Mpaka muda huo watoto
hao walikuwa hawajatolewa nje zaidi ya kliniki tu.
Sabrina
alibadilika, akanona, umbile la kimama likawa zuri kwake. Mikono ya Jack ikawa
haiishi mwilini kwake akimtaka mkewe. Walikuwa na utulivu wa namna yake hapo
kwao. Hawakuwahi kumzungumzia mama Msindai, ila alikuwa akipata salamu kutoka
kwa mzee Msindai. Wengine wote kasoro Jena, walikuwa wakimpigia simu Sabrina
mwenyewe kumsalimia na kumjulia hali ya watoto.
Baada
ya mwezi mmoja kuondoka wazazi, wanae wakiwa na miezi mitano na siku kadhaa, Sabrina
akagundua hajapata siku zake week moja ilishapita ambayo alitakiwa kupata siku
zake. Wasiwasi ukamwingia, lakini akaona atulie. Siku 15 zikapita, hamna kitu.
Akaona ampigie simu mama yake. “Mwenzio sipati siku
zangu.” Mama yake akaanza kucheka. “Usinicheke
bwana mama!” “Wewe si nilikwambia utumie uzazi wa mpango, ukawa mbishi unasema
ni mjuzi sana wa kuhesabu! Sasa umeruka kidole?” Ikabidi Sabrina acheke.
“Kwa hiyo nimeruka namba?” “Ndio useme sasa.”
Sabrina akazidi kucheka. “Ila wanangu bado wadogo mama!
Kuja kuongeza mtoto wa tatu sasa hivi!” “Sasa hayo unayalalamikia sasa hivi,
wakati mimi kila siku nilikuwa nikikwambia hapo Sabrina? Twende mwanangu
ukawekwe kitanzi, ubishi. Basi jua watatu anakuja.” Sabrina akacheka na
kukata simu. Akawaangalia wanae. “Sasa mnacheka nini na nyinyi? Hayawahusu. Waone.”
Watoto wakazidi kucheka. “Mmetumwa na bibi yenu nyinyi, wala sio bure.” Sabrina
akaendelea kuzungumza na wanae.
Pendo na Willy.
Wasimamizi
wa harusi ya Jack & Sabrina.
P |
endo akaamua
kuamini pamoja na Sabrina. Maana Sabrina hakuacha kumwambia yeye bado
anamuamini Mungu juu ya mtoto kwa niaba yake. Alipomuona Sabrina hakati tamaa
ndipo na yeye akaamua kuchukua hatua ya kutafuta tena mtoto kwa upya kabisa. Kazi
yake ilikuwa ikimchukulia muda mwingi sana na daktari alimshauri akiwa
anatafuta mtoto, basi asiwe kwenye mazingira ya kum stress. Wawe kwenye
mazingira matulivu. Waende hata sehemu kwa mapumziko kwa muda huo. Akamuomba Willy
tena kwa upya. Lakini akamuona Willy anakuwa mzito sana. Swala lakuomba likizo
pamoja nalo likawa lakumbembeleza mno. “Naomba usinikatie tamaa Willy! Naomba
tujaribu mara ya mwisho. Ikishindikana safari hii basi.” Pendo akabembeleza
sana na ikawa hiyo ndio ajenda pekee, mpaka Willy akakubali kuchukua likizo.
Hakumwambia mambo mengi juu ya wanachoamini
na Sabrina ili asimchoshe, halafu akakataa, maana swala la kutafuta
mtoto lilishakuwa la miaka mingi tena la shida.
Alipokubali
tu, Pendo akaandika barua ya kuomba likizo kutokana na siku zake ambazo
angeshika mimba. Akaanza kumeza dawa za kupevusha mayai tena kwa ajili ya
watoto mapacha. Akafuata masharti tena bila kumwambia mtu yeyote. Hata marafiki
walishachoka. Alizinunua hizo dawa kimya kimya na kuzinywa akitegeshea siku
zake za kupevuka yai wawe mapumzikoni. Siku zilipokaribia akiwa anatumia hizo dawa
yeye akaanza likizo, kwa makubaliano siku inayofuata ndipo Willy naye aanze.
Aliondoka
kwenda kazini kama kawaida, akamuacha Pendo nyumbani akijiandaa na safari.
Alikwenda kutengenezwa saluni karibu siku nzima. Pendo akafanyiwa waxing mwili
mzima ili tu kumfurahisha mumewe huko mapumzikoni. Akatengeneza kucha, na kwa
kuwa kwa asili Pendo alikuwa mzuri wa sura na umbile, akapendeza haswa. Akarudi
nyumbani mida ya saa kumi na mbili jioni akitarajia kumkuta Willy, lakini hakuwepo.
Akampigia simu mara kadhaa, hakupokea. Ila akamtumia ujumbe, ‘nitakupigia baadaye kidogo’. Pendo akakunja uso.
Akaweka simu pembeni na kuendelea na shuguli zake.
Usiku
wa saa nne ndipo Willy akarudi. Pendo yupo sebuleni akimsubiria. “Kwema?
Umenitia wasiwasi.” “Nilikuwa nyumbani. Hali ya mama sio nzuri, tunafikiria
kumpeleka India.” Pendo akajua tayari mipango imeshaharibika. “Vipi yule
daktari wake aliyekuwa akimuona hapa?” “Hata yeye ameshauri kama uwezo upo,
apelekwe India.” Pendo hakufurahia jinsi alivyojibu. Akaona atulie. “Chakula?” Akauliza
tena Pendo. “Nilishakula. Nimechoka, nataka tu kulala.” Willy akapitiliza
chumbani. Pendo akabaki akifikiria, kama aulizie swala la safari au anyamaze.
Akamfuata
chumbani, akamkuta anaoga. Akasubiri kitandani. Akatoka. “Kwa hiyo mipango
inakuaje sasa?” Pendo akauliza taratibu tu. “Unatania au unamaanisha Pendo? Au
hujaelewa kuwa mama amezidiwa?” Pendo akatulia. “Unawezaje kufikiria safari ya
kwenda kupumzika wakati mama ni mgonjwa? Najua hamkuwa kwenye maelewano, lakini
ni mama yangu mimi. Onyesha hata utu kidogo basi!” Pendo akashangaa sana.
“Naomba unisahihishe Willy. Lakini ninavyokuona, ni kama unatafuta sababu ya
kugombana na mimi!” “Kwa hiyo..” “No, subiri Willy. Naona hiyo hali imekuanza
hata kabla ya leo. Ni nini kinaendelea?” “Wewe uniambie.” Pendo akakunja uso.
“Mama
amekuwa akiumwa muda mrefu tu. Swala la kumpeleka India sio la leo. Sisi ni
wafanyakazi wa kuajiriwa. Kosa langu ni lipi leo kuuliza mipangilio wakati
ukijua wazi nimechukua likizo twende mapumzikoni?” “Kwa hiyo sasa unataka
kuniambia ugonjwa wa mama ndio umeingilia kushika mimba kwako?” Moyo wa Pendo
ukapasuka, akafungua macho yote wazi. “Tumepoteza pesa kiasi gani na muda kwa
ajili ya swala la mtoto? Ugumu wa wewe wakutoweza kusubiri ili mama apone ni
upi? Kipi kipya tutafanya safari hii ambacho kinakuhakikishia tutapata mtoto?”
Pendo akashindwa kujibu kabisa. Kwa mara ya kwanza Willy akaongea moyo wake
bila kuficha wala huruma kwa mkewe. Pendo akabaki akimtizama jinsi Willy
anavyoendelea kugomba. Aliongea maneno ya hasira mpaka akachoka. Akalala.
Pendo
alikuwa ameumia sana. Alijua watu wanamsema, lakini sio Willy wake ambaye alikuwa
akimpa moyo wakati wote. “Mpaka Willy amechoka!”
Akaanza kulia Pendo pale sebuleni alipokuwa amehamia. Akalia. Akajiambia kwa
uchungu ule muda ule akimpigia simu mama yake, atamuumiza. Akikaa pale kesho
yake bila kwenda kazini, akajiambia atachanganyikiwa, akamtumia ujumbe bosi
wake kumuomba arudi kazini tu. ‘Sawa.’ Hapo hapo
bosi wake akajibu.
Kesho
yake akaenda kazini akiwa amepoteza pesa ya nauli ya tiketi za ndege alizokuwa
amekata Pendo kwa pesa yake, kuelekea nje ya nchi kwa mapumziko. Alitaka waende
mbali kabisa na Tanzania ili akatulie na Willy akijaribu kushika mimba. Asubuhi
hiyo waliondoka bila hata kuongeleshana. Jioni alirudi nyumbani, akakuta
msichana wa kazi alishapika hakuingia hata jikoni. Akaoga na kulala. Kwenye saa
nne tena ndipo Willy akarudi. Pendo akanyamaza. Hata hakugeuka. Kesho yake
ikawa hivyo hivyo.
Akiwa
kazini Sabrina akamtumia picha za wanae na ujumbe. ‘Wanao
wamekumiss.’ “Oooh noo!” Pendo akakumbuka amemeza dawa za
ujauzito. Kadiri wanavyozidi kununiana na Willy, ndivyo siku za kushika mimba
zinavyozidi kuisha na ni hasara kwake. Hapo hapo ikajiambia lazima ajirudi kwa Willy
ili angalau usiku huo wafanye tu tendo la ndoa, lasivyo jitihada za mwezi huo nazo
itakuwa bure. Akamtumia ujumbe, ‘Pole kuuguza mpenzi
wangu. Najua upo kwenye kipindi kigumu. Namuombea mama na wewe pia. Mungu
awafariji familia nzima. Na ninaamini Mungu atafanya njia. Na mimi nipo na wewe.
Niambie tu chakufanya. Na kama kuna mchango, na mimi unihesabu mpenzi.’
Akautuma ule ujumbe akabaki akisubiria.
Kwa
Sabrina.
Akashindwa
kusubiri. Akampigia simu Sabrina hapohapo. “Ili hao
watoto waendelee kuwa na antie, lazima uniombee sasa hivi. Nachanganyikiwa
Sabrina.” “Ni nini tena da Pendo?” Sabrina akauliza kwa kujali. “Mimi sielewi vita vinaanzia wapi, lakini Willy
amenibadilikia Sabrina, hutaamini. Mkali, na wazi ameniambia amechoka.”
Pendo akamsimulia mkasa mzima. “Sasa na mimi nyumbani
kwao hawanipendi kabisa. Hata kwenda huko imeshakuwa tatizo, mpaka mama
akashauri nisiwe nakwenda. Maneno ya kunikashifu ya waziwazi hayajawahi kuisha.”
“Kutoka kwa nani sasa?” “Zaidi mama Ngoi mwenyewe na dada zake wote. Baba yake yeye
tatizo lake ni mtu wa wanawake mno. Huwa najitahidi kukaa naye mbali.” “Da
Pendo!” Sabrina akashangaa.
“Sikutanii Sabrina. Nakwambia wewe tu kwa kuwa nimekuona unakifua
chakubeba mambo, lakini huwezi amini yule mzee alishanitongoza.” “Haiwezekani dada!”
Sabrina akazidi kushangaa. “Mungu wangu nishahidi. Kuna
siku ndio alinichosha zaidi. Nilimkuta nyumbani peke yake, akaniambia kama Willy
anashindwa kunizalisha, yeye anisaidie.” “Mungu wangu!” “Wewe acha tu.
Sikuamini, na akafika umbali wa kuniambia kama naona shida kukutana naye hapa
mjini, tusafiri naye. Si unajua mzee Ngoi anazo pesa?” “Nimesikia.” “Basi pesa anazo kwa
uhakika wala si ya kubabaisha. Akaniambia atanipa pesa yeyote ninayotaka, nitangulie,
yeye atanifuata. Nikaondoka bila hata kumjibu, na wala sikumwambia mwanae, ndio
ugumu wa kwenda kwao ukaongezeka mbali na maneno ya mama yake ambaye ndio
mgonjwa. Willy anakaa huko mpaka usiku. Kesho ndio siku ya mwisho ya kushika
mimba. Sitaki ahadi yakuniombea baadaye. Hapa nipo chooni. Wewe niombee sasahivi,
angalau huyo mwanaume leo aniguse Sabrina.” Sabrina hakupoteza muda,
akaanza maombi hapohapo kwenye simu, akimwita Mungu wa amani na aliyebariki
ndoa yao amkumbuke Pendo. Akamaliza, Pendo akarudi kazini.
Ilipofika
kwenye saa 9 jioni, Pendo akaona ujumbe kutoka kwa mumewe. ‘Nashukuru kujali. Nilikuwa busy kidogo nikishugulikia mambo
ya mama tokea asubuhi. Nitakuona nyumbani.’ Pendo akajisikia kutokwa na
machozi. ‘Umefikia pazuri?’ Pendo akatuma ujumbe
mwingine. ‘Lipo tumaini. Nitakueleza vizuri ukija
nyumbani. nimechoka, naona leo nitawahi kulala.’ ‘Sikujua kama umesharudi
nyumbani!’ ‘Ndio nimeingia muda si mrefu.’ ‘Pole mpenzi wangu. Yatapita tu.
Naamini na mama atapona.’ Pendo akatuma na huo ujumbe huku akikusanya
vitu vyake arudi nyumbani haraka. ‘Amina. Na
nashukuru.’ Ujumbe huo anasoma Pendo, yupo ndani ya gari yake tayari
kurudi nyumbani. Njia nzima akirudia maombi ya Sabrina.
Alifika
nyumbani, msichana wa kazi akamwambia mumewe alifika hapo, akala, na kuingia
chumbani. Pendo aliingia chumbani, akamkuta mumewe amelala kama usiku wa saa
saba. Simu ameweka pembeni, taulo kwenye kochi, wazi kuwa alishaoga ndio
akalala, kuashiria amemaliza siku. Pendo aliumia sana. Kesho ndio ilikuwa
mwisho. Hawezi kumuamsha. Atamwambia nini? Akakaa hapo chumbani kwenye kochi
akimuomba Mungu mumewe aamke lakini wapi. Akaoga na kwenda kula. Mpaka saa tano
usiku Willy alikuwa amelala kama mfu. Pendo akaamua kulala tu akiwa amekata
tamaa kabisa.
Karibu
kuna papambazuka, akasikia mumewe akimpapasa. Hakuamini. Akamgeuza bila hata romance,
akamuinamisha nakuanza mapenzi. Akashangaa ile nguvu aliyokuwa nayo Willy,
Pendo akatoa ushirikiano wote. Willy akafanya mapenzi na mkewe, akamaliza.
“Daah! Samahani. Nahisi nilikuwa nikiota. Sikukusudia kuwa kama mnyama.” Pendo
akacheka. “Hamna neno, japo nilishangaa kidogo.” “Sijakuumiza?” “Hapana. Nipo
tu sawa.” Willy akamvuta vizuri, akamkumbatia na kurudi kulala. Pendo hakutaka
hata kugeuka ili mbegu za mumewe zisije kutoka. Akajiegemeza vizuri hapo
ubavuni, akamshukuru Mungu kwa machozi. “Asante
kunikumbuka Mungu wangu.” Pendo akaendelea kutokwa na machozi ya
furaha kana kwamba alichofanya safari hii ni cha tofauti. Alishakunywa aina hizo
za dawa zaidi ya atakavyokumbuka. Alishategesha hizo mimba nje na ndani ya
hicho kitanda chao zaidi ya atakavyosema. Wakichukua likizo na kwenda sehemu
mbalimbali wakidhani watafanikiwa swala la mtoto bila mafanikio. Lakini
alfajiri hiyo hakujali kama mimba itashika au la, lakini kile kitendo
chakushikwa na Willy, akakifurahia kwa ajabu.
Alikuja
kuamshwa na alarm ya saa 11:30 asubuhi. Akakimbie kwenye machine kidogo ndipo
arudi kuoga awahi kazini. Akakumbuka ujauzito. Akajiambia asubuhi hiyo
asikimbie asije kuharibu mambo. Akazima alarm na kuelekea bafuni kuoga. Wakati
anaoga, Willy akaingia. Bila maneno mengi akamkumbatia na kuanza romance. Pendo
alifurahia, asiamini. Willy hakuonyesha haraka, akamtoa mkewe hapo, wakahamia
kitandani vilevile na maji. Pendo alifurahia hayo mapenzi. Willy alionekana
kutulia na kumfurahia mkewe mwanzo mpaka mwisho, akimnung’unisha mkewe hapo kwa
penzi la kituo, mwenyewe alifurahia kuwa alifanya kazi nzuri asubuhi hiyo.
Pendo akaondoka kwenda kazini, akamuacha mumewe akizungumza na dada yake.
Safari ya
mama Ngoi nchini India.
B |
aada ya
majuma mawili na siku tatu, maandalizi ya safari ya kwenda nchini India kwa
matibabu ya mama Ngoi yakakamilika. Dada yake mkubwa Willy ndiye aliyekuwa akimsindikiza
mama yao nchini India kwa matibabu. Siku moja kabla, Pendo alimuomba Willy
amsubiri ili waongozane nyumbani kwao akamuage huyo mama. Alifika pale akakuta
kuna chakula cha pamoja kwa ndugu na marafiki wa karibu, kama tafrija yakumuaga
huyo mama kwa maombi. Pendo aliumia sana kuona wameshindwa hata kumkaribisha kiunafiki
tu! Inamaana asingeamua yeye kwenda ndio asingejua yote hayo! Lakini akaona anyamazie
tu. Watu walikuwa wengi tu hapo na hekaheka nyingi. Kila alipotaka kusaidia ni
kama alikatazwa. Akaamua ajitulize tu. Hata siku alipokwenda kumuona huyo mama
hospitalini alipokwenda kliniki yake ya kawaida tu, kwa kuwa ilikuwa mjini,
Pendo akajua wapo hapo, akatoka kazini na kwenda kumuona. Alijuta. Walimpuuza
kwa hali ya juu ni kama waliokuwa wakimuuliza amefuata nini hapo! Willy
hakuwepo, aliwakuta dada zake Willy, na marafiki zao. Alipoona wanampuuza na
yule mama hataki hata kumtizama, Pendo akaaga na kuondoka. Walikaa hapo mpaka
mwisho, wakaaga na kuondoka na mumewe.
Willy
alikuwa akiwasiliana na dada yake huko nchini India kujua maendeleo ya mama
yao. Pendo naye akawa akiuliza kila alipoona Willy ametulia. “Operation ya
kwanza imekwenda vizuri. Wameweza kutoa uvimbe wa kwanza, huo wa pili wameamua
kumpa muda kidogo. Upo karibu sana na ubongo.” “Pole babe. Mungu atamponya tu.”
Kwa sauti yake tulivu Pendo akamfariji wakati hakuwa hata akijua kama huyo mama
alifanyiwa upasuaji. Akaona anyamaze tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa
siku ya jumatano ya saa 9 usiku nchini Tanzania, siku ya 13 tokea kuondoka kwa
mama yake Willy nchini, Willy na mkewe wakiwa wamelala, wakati simu kutoka
nchini India kwa dada yake mkubwa Willy aliyekuwa na mgonjwa ilipoingia. Willy
akakaa kwa haraka na kupokea. Alichoweza kusikia Pendo ni kilio cha uchungu
sana. Akajua mambo si mazuri. Na yeye akakaa. “Haiwezekani
jamani! Mbona nimezungumza na mama kabla sijalala na alisikika mzima kabisa!”
Yule dada akazungumza akieleza hata madaktari wameshangaa. “Hakuzidiwa wala kuonyesha mabadiliko yeyote mabaya. Tena
walikuwa wakisema wanashangaa jinsi anavyopona kwa haraka na hata wakafikiria
kumfanyia upasuaji kwa mara ya pili jumatatu ijayo! Tumeshangaa muda mfupi
uliopita mashine zinapiga kelele. Nesi kuingia, akaita madaktari kumsaidia.
Wamehangaika hapo, lakini ikashindikana. Mama ametuacha Willy.” Willy
akaanza kulia hapo, Pendo akimbembeleza.
“Itabidi
kuwataarifu wengine mpenzi wangu. Pole.” Hapo Willy ndio akaanza kusambaza
habari za msiba, na yeye Pendo akamtarifu bosi wake na wazazi wake. Kufika saa
tatu asubuhi wakawa wameshaingia nyumbani kwa kina Willy, Masaki. Saa nne
asubuhi ndugu wote wa pale mjini na marafiki wa karibu wakawa wamefika hapo msibani.
Saa sita mchana kukawa kumeshawekwa turubai nje na viti, watu wa catering
walishakuwa wamepigiwa simu na ndugu wa huyo mama, ikawa hekaheka tupu na vilio
vya hapa na pale.
Kufika
jioni marafiki wa karibu waliokuwa wapo kazini nao pia wakawa wamefika hapo.
Mambo yakaendeshwa kitajiri, na fahari. Pesa ya huyo mzee ikafanya kazi kwenye
msiba huo. Walikuwepo watu maalumu wa chakula na ndio waliogawa vyakula na
vinywaji. Na ndio haohao waliokuwa wakikusanya sahani zao chafu. Kazi kubwa ya
msibani ikawa imepunguzwa. Wafanyakazi wa watoto wake huyo mama wakisaidiana na
wafanyakazi wa hapo ndani kwa mama Ngoi wao wakashika usafi wa nyumba. Kwa hiyo
kazi iliyokuwa imebaki hapo kwa mtu kama Pendo ambaye hata mawifi zake hawakuwa
wakimtaka aguse vitu vya mama yao ilikuwa kukaa kama wageni wengine. Kila
alichoshika aliambiwa aache tu, na yeye akatafuta mahali akahema.
Akamtumia
ujumbe Sabrina kumtaarifu huo msiba.
Sabrina ndiye mtu wake wa karibu aliyebakia sababu ya kuombeana. Sabrina akampigia simu. “Tutakuja kwenye kuzika da Pendo. Pole sana. Nitamwambia na
Jack.” Akamfariji hapo, akamshauri awapigie simu kina Jacinta, Joy na Jena
waende wawe naye asikae hapo peke yake. Akaona jambo zuri. Akawatumia ujumbe
wote. Ilipofika saa mbili na nusu, wote wakawa wamefika hapo mpaka mama Msindai
na mama yake mzazi Pendo. Angalau akapata watu wakumpa pole na yeye na
kuzungumza naye. Wakamzunguka hapo, wakatengeneza kundi lao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jumamapili
ndio mwili ulikuwa ukiingia, mazishi ilikuwa siku ya jumatano. Sabrina, Jack na
watoto wao wote wawili wakatua jijini Dar siku ya jumamosi. Pendo akaenda kuwapokea.
Walikwenda nyumbani kwa Pendo, Jack akaja kuchukuliwa na kaka yake, wakaenda naye
msibani. Pendo akabaki na Sabrina hapo nyumbani wakimsubiria mama yake Sabrina
aje akae na wajukuu zake, wao waende msibani. Baada ya muda kidogo mama yake na
Sabina wakaingia. “Wewe Sabrina! Hao wanao wanazidi kuwa warembo!” Sabina
akashangaa sana. Ungetaka kuwashika watoto wa Sabrina. Walikuwa wazuri mno. “Wana
kazi yakucheka tu kama baba yao.” “Mmemuacha baba yao?” “Subutu! Jack hajiwezi
bila hao watoto. Hapa ilikuwa shida kuwaacha mpaka kaka yake alimwambia
anamuacha ndio akaondoka. Ukimkuta amekaa nao hapo chini, utafikiri na yeye ni
pacha mwenzao!” Wakaanza kucheka.
“Unafikiri
natania? Yaani utafikiri nina watoto watatu humo ndani jamani! Anajifunza
kutambaa nao! Hamna mnaloongea na Jack akiwa ameshika hawa watoto mkaelewana.
Bora wawe wamelala, ukimwambia jambo ndio anaelewa.” “Sasa na wa nne ndio
anakuja.” Mama yake akamfanya Sabrina azidi kucheka. “Wewe Sabrina ni mjamzito
tena!” “Mwaya mama sijui yukoje! Nimemwambia asiseme.” “Wewe si ulisema hurudi
tena leba mpaka miaka saba!?” Sabina akashangaa sana wote wakacheka.
“Wala
mimi sikupanga kushika mimba.” “Ulitaka sana. Mtoto nilimbembeleza huyu!
Namwambia Sabrina mwanangu twende ukawekwe kitanzi au tumia dawa. Akawa mbishi.
Ooh, ‘mimi mzuri sana wakuhesabu. Wala sina sababu ya kutumia njia ya uzazi wa mpango’.
Nashangaa ananipigia simu eti, ‘Mama, mbona sipati siku zangu?’ Nikamwambia...”
“Eti akanijibu labda niliruka kidole kimoja wakati wakuhesabu.” Wote wakazidi
kucheka.
“Ndio
miezi mingapi sasa?” Sabina akauliza. “Naenda wa tatu. Hivi hata Jack hajui.”
“Haiwezekani Sabrina!?” Wote wakashangaa. “Kweli tena. Kuna mambo yangu nafanya
sasa hivi. Namjua Jack. Nikimwambia tu, tutaanza kufuatana nyuma, nitakosa
uhuru. Nataka nimalize kila kitu, vikikaa sawa, ndipo nimwambie, tuanze tena
kulea mimba kwa mara ya pili.” Wote wakashangaa. “Nashauri umwambie Sabrina.”
Pendo akasisitiza. “Sina nitakalofanya da Pendo. Mimi namjua Jack. Au muulize
mama hali aliyonikuta nayo kule Singida.” “Utafikiri mgonjwa mahututi.”
Akamalizia mama yake Sabina wakacheka. “Sasa ndio hiyo hali itazidi mara mbili
akijua ni mjamzito. Mimba ya hawa watoto, ilikuwa mpaka kero. Atataka kujua upo
wapi na unafanya nini. Na kiwe kitu anachoona yeye si hatarishi. Mpaka
nikamuomba daktari azungumze naye na kumwambia natakiwa kutembea. Maana
nilifika hatua, akinisikia nimetoka hapo ndani, utamuonea huruma. Anasema mimba
itatoka.” Wakacheka.
“Kweli.
Acheni tu nimalize project yangu.” “Ni nini?” Akauliza Sabina. “Kuna project ya
chama nafanya na wanawake huko na huku. Naona nimepata uungwaji mkono mzuri!
Kaka yake Jack amenitafutia watu wakutufadhili. Ikikamilika hiyo, mume wangu
akaikubali na kuifungua ramsi, hapo nakaa nyumbani bila shida. Lakini sio sasa
hivi. Atanisumbua sana Jack. Mwache acheze tu na hawa hawa wawili.” Wakacheka.
“Na ukimuachia watoto hapo nyumbani siku za jumamosi ambazo haendi kazini,
ukirudi unaweza kutamani kulia. Unafungua mlango, unakaribishwa na toi mlangoni.
Yeye amelala kwenye sehemu ya watoto na wanae, wanacheza hawana habari. Watoto
wanatambaa, na yeye nahisi amesahau kutembea. Anatambaa kama watoto!” Wakazidi
kucheka. “Nimebakisha kidogo tu nimalize mambo yangu, nitamwambia tu.”
Wakazungumza kidogo, Sabina akawa akiwapiga picha hao watoto wa mdogo wake
mpaka akaridhika. Wakamuacha mama yao na hao watoto, wao watatu wakaondoka
kwenda msibani.
“Nimefurahi
umekuja Sabrina! Nilishapatwa na hamu na wewe.” Sabrina akawa anacheka wakiwa
njiani kuelekea msibani. “Nipo hapa mpaka mzike.” “Bora.” Wakaendelea
kuzungumza mpaka sibani.
Msibani.
W |
alipoingia
ndani getini, Pendo akawaambia waende wakakae wanapokuwa wanakaa na ndugu zake,
haswa wanawake. Wakaongozana. “Naona wewe na mumeo mmependeza!” Jacinta
akamuwahi, Sabrina akacheka. “Shikamoo wifi.” “Marahaba Sabrina, watoto wako
wapi?” “Nimewaacha na mama. Nisingeweza kuja nao hapa, wapo kwenye kutambaa,
ningekuja nao hapa, pasingetosha.” Wakacheka. “Jack anakazi yakunitumia video
zao naona kila week.” “Basi utakuwa umeona hiyo fujo. Hapo kwa da Pendo imebidi
kuondoa meza zote ili wapate uwanja wa kutambaa.” “Hawajachoka na safari?” “Walilala
njia nzima, wameamkia nyumbani kwa da Pendo.” Wakacheka, ndipo Sabrina akaendelea
kusalimia wengine, asijue mama yake mkwe alikuwa ameinamia simu yake pembeni,
akisikiliza tu.
Akawasalimia
wote kwa kuwashika mkono, wakavuta kiti pembeni. “Naona Singida sio pabaya
Sabrina.” Joy akamtania. “Nakwambia uje, uniletee Claire wangu aone watoto,
unaniringia. Singida mlenda unang’arisha.” Joy akacheka sana. “Shauri yako.” “Si
ungetubebea na sisi?” “Mlenda wa Singida, uulie Singida ndio unajibu.” Sabrina
akaongea kwa sauti ya chini na kumfanya Joy azidi kucheka. “Sabrina wewe
mtundu.” Stori zikaanza hapo. Wakajikuta wameungana, Joy, Jacinta, Jena,
Sabrina, Sabina, Pendo, dada yake Pendo, Nancy, na marafiki zao. Mama Msindai
na mama yake Pendo pamoja na wa mama wengine wakaendelea kivyao lakini kundi la
pembeni yao tu. Jena akakaa kidogo, akaondoka bila kuongea chochote na Sabrina
ila salamu tu.
Usiku
wakaondoka kurudi nyumbani, kesho yake tena wakarudi msibani. Mama Sabina ndiye
akawa anabaki na wajukuu zake muda wote. Huko msibani Sabrina akawa akiongozana
na Pendo kila mahali mpaka chooni. Ilipofika siku ya jumapili mchana msafara
ukaelekea uwanja wa ndege kupokea mwili wa marehemu ukaanza. Kukajaa vilio huko
uwanja wa ndege, wakatoka tena huko kurudi nyumbani wakiwa na mwili wa mama
Ngoi.
Msiba
ukaanza rasmi. Jumatatu na jumanne ikawa maombolezo hapo. Jumatano wakaaga
mwili wa marehemu nyumbani, ibada kanisani, mama Ngoi akapelekwa kwenye safari
yake ya mwisho kwenye makaburi ya Kinodnoni. Willy na ndugu zake, kaka na dada
zake walikuwa wakilia sana, hakika ungewahurumia. Maana huyo mama ndiye ni kama
alikuwa ameshika familia yake wala si baba. Mzee Ngoi alikuwa mkorofi ambaye
hafikiki hata na wanae. Kwa hiyo swala la kwenda nyumbani ilikuwa ni kwa sababu
ya mama, na ndiye aliyekuwa akiendesha hata maisha yya wanae kwa ushauri na
msaada kifedha. Kwahiyo hapo walilizwa na mengi. Ni kama nguzo yao ndio ilikuwa
imeondoka. Wakazika, watu wakatawanyika palepale makaburini. Ndugu wa karibu wa
familia tu ndio wakawa wanarudi nyumbani kwa Ngoi kama kumaliza msiba. Sabrina
peke yake ndiye aliyerudi na Pendo nyumbani kwa wakwe zake. Hata wazazi wake Pendo
waliagana makaburini.
Kikao Cha Familia
kilichoibua mapya.
W |
akaingia sebuleni,
baba yao akapata nafasi yakushukuru wote kwa kushiriki. Dada mkubwa aliyekuwa
na mama yao nchini India naye akapata nafasi ya kusimulia tena kwa kifupi yaliyotokea
huko. “Lakini mama alisema kwa kauli yake mwenyewe, ikitokea chochote
kinampata, wakati nagawa vitu vyake, lazima wifi Zelda apewe nafasi ya pekee
achukue kile anachoona kitamfaa yeye na watoto wake ili ije kuwa kumbukumbu kwa
wajukuu zake.” Pendo akashangaa huyo wifi anayezungumziwa hapo ni yupi! Wake za
kaka yake Willy aliwafahamu vizuri tu. Willy ndio kijana wa mama Ngoi mdogo wa
mwisho, yeye ndio mke, mtoto wa mwisho ni wa kike. Pendo akawa hajaelewa.
“Mama
amekufa akiwa anatamani sana kumuona mjukuu wake huyu anayekuja. Lakini Mungu ame...” Wakaanza tena kulia na
kumchanganya Pendo zaidi. Katika watoto wa kike wa huyo mama hapakuwa na
mjamzito na wake za watoto wake wa kiume pia hapakuwa na mjamzito! Ila akamuona
dada mmoja ambaye alishamuona hata na huyo mama hospitalini alipokwenda
kumuona, na hapo yupo ndiye pekee mjamzito. Akamtizama vizuri, kweli tumbo
lilikuwa kubwa ila hakuwa akimfahamu kwa undani zaidi ya kumuona tu na marehemu
mama mkwe wake! Alikuwa akilia na dada zake Willy wakaonekana kumpa sana yeye
pole. Hapo sasa ikabidi kumtizama kwa makini akajua sasa yeye ndiye huyo wifi
wanayemzungumzia, swali mume ni nani!?
Baada
ya vilio vya hapa na pale mwishowe wakatulia tena. Lakini alishangaa wake za kaka
yao Willy hao wawili wao wamenyamaza kimya, hawalii wala hawazungumzi wapo kama
wanahasira. “Kwa hiyo nafikiria, hiyo siku ya 40 ambapo tutatoka kusoma misa ya
mama, wote turudi hapa, tuje tugawane vitu vya mama.” Akamalizia huyo dada
mkubwa kabisa ambaye ndiye mtoto wa kwanza wa hiyo familia. “Labda mimi
niulize. Katika hiyo siku, nani anaruhusiwa kurudi kuja kuchagua hivyo vitu? Maana
wajukuu aliyetambuliwa hapa na bibi yao ni huyo wa Willy ambaye bado hajazaliwa.
Sasa ndio nauliza hiyo siku ya 40 baada ya misa hawa wajukuu wengine tunarudi
nao hapa, au tuwarudishe nyumbani wasije kuanza maswali yasiyo na majibu?” Mke
wa kaka yao mkubwa, akauliza ki ukali kidogo. Sabrina akakunja uso, Pendo
akaanza kutetemeka. “Sijaelewa?” Akaongea Pendo kwa sauti yake ya chini
iliyojaa hofu.
“Sasa
tunamjibu nani na kumuacha nani? Maana wote mnauliza maswali kwa pamoja!” “Hakuna
swali gumu hapa, Stella. Wewe ndiye umeanza kutoa maelekezo. Una...” “Mbona
jazba mama?” Mumewe akamuuliza kwa upole. “Lazima jazba shemeji. Mnachotaka
kufanya hapa sio sawa. Pendo ni mke halali wa Willy. Halafu na sisi ni wake
zenu na tumezaa na nyinyi. Iweje leo Zelda aliyekuja juzi tu hapa ndio apewe
heshima zote, na kutangazwa hapa kwa kishindo kama sisi tunashida na mali bwana!”
Akapokea mke wa kaka wa pili ambaye ni mtoto wa tatu wa hiyo familia. Ugomvi
ukaanza, na kutukanana. Nusura Stella dada mkubwa na wifi yake washikane,
kupigana. Wanaume wakaingilia. Mke mwenzie, yaani wa mtoto wa tatu akawa mkali
akitaka kuchangia kwenye huo ugomvi.
“Msitufanye
sisi watoto wadogo hapa. Zelda, Zelda! Kwani anazaa ulimwengu!” “Mnakuwa kama
sio wakristo nyinyi! Leo gafla Zelda amekuwa wa maana kuliko Pendo mke halali
wa Willy! Acheni kutudhalilisha kwa kiasi hicho jamani!” Pendo alikuwa akitetemeka
hajui hata amwangalie nani amuache nani! Mambo yalikuwa yakiendelea humo ndani
ya familia, yeye hana taarifa! Mumewe ana mwanamke mjamzito, mimba kubwa
kabisa, anafahamika mpaka ukweni, yeye hajui! Pendo akabaki amekufa ganzi.
Sabrina akamshika mkono, wakabaki wakiwaangalia wake wenzake Pendo jinsi
wanavyompigania, Pendo akiwa hajui chakusema. Hata Willy mwenyewe akashindwa
kumtizama mtu usoni, akabaki ameinama.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kikulacho Ki Nguoni Mwako. Yamemfika Pendo. Akidhani Ipo Amani, Kumbe
Uharibifu Umeingia Mpaka Ndani Ya Ndoa Yake.
Nini Kitaendelea Kwa Wapenzi Hao Wa Tokea Wadogo,
Wakiwa Chuoni, Kama Jack Na Sabrina?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment