Wakati
wanaingia na Jacinta pamoja na Pendo na mumewe nao wakawa wanaaga. “Ngoja
nikapike cha mchana na usiku. Mama ubakiwe na kazi ya kumlisha tu.” Pendo
akaaga wakati anakusanya vitu. “Nashukuru sana mwanangu. Mungu akubariki kwa
moyo wako wakujitoa kwa Sabrina.” “Amina mama.” Pendo akaitika kwa suati yake
ya upendo kama jina lake. “Lakini unipigie kwanza Pendo. Unaweza kukuta mpaka
umalize kupika, na sisi tumeruhusiwa.” “Sawa Jack.” “Nakushukuru sana Pendo.
Asante sana. SANA.” Pendo akacheka. “Karibu Jack. Na mimi mnanihusu sana. Sasa
hivi nyinyi ni jukumu langu.” Sabrina akajisikia vizuri, akafurahia hilo.
“Asante da Pendo.” “Basi nitawaona baadaye. Popote mtakapokuwa, nitawaona.”
Wakaaga na kuondoka Jack, akatoka kuwasindikiza.
Wakabakia
wao tu watatu na watoto. Sabina akajua ndio wakati mzuri wakumuweka sawa
Sabrina. Lakini Sabina akashindwa pakuanzia. Ni kama wote walishakuwa
wakimuogopa sana Sabrina. Akatulia akifikiria pakumuanzia. Sabrina akamuona
mama yake vile anavyohangaika na wajukuu. “Nakushukuru mama yangu. Umenifaa
kweli! Maana nilikuwa hata sijui jinsi yakuvishika hivyo vitoto na hivyo
vitomvi vinavyoning’inia! Natamani tukakae wote mpaka watoto wachangamke
kidogo!” Sabrina mwenyewe akaanza. “Kwani mama wewe unashida? Tena ingekuwa
vizuri ukae na wajukuu wako mpaka hamu iishe.” Sabina akadakia kwa haraka sana.
“Hamu ya wajukuu haiishi, Sabina mwanangu.” Mama Sabina akajibu huku akimuweka
sawa mjukuu wake na kumbusu. “Kweli mama? Unaweza kukubali tukakae wote kwa
muda?” Sabrina akahamasika kweli.
“Bila
shida Sabrina mwanangu. Nikishindwa na hapa tena, basi nitakuwa sifai tena kuwa
mama.” “Nakushukuru mama yangu. Basi ngoja Jack akirudi nitazungumza naye.”
Hilo likamfurahisha sana Sabrina. Jack akarudi. “Vipi?” Akamsogelea na kumbusu.
“Nipo sawa tu. Vipi wewe?” “Mimi natamani kutoka hapa. Nishachoka. Tena hivyo
nikiwaona wote mpo sawa, sioni sababu yakukaa hapa. Naona wanawabana wanangu
tu.” Sabrina akacheka. “Tena nataka kumuomba mama twende naye.” “Singida!” Jack
akashituka. “Akanisaidie kidogo mpaka watoto wakue.” Sabina mama yake wakabaki
wakisikiliza. “Wewe unataka kuniponza ukweni Sabrina.” Wote wakacheka. “Kweli
tena huyu anataka kuniponza mapema, nipokonywe mke! Tumchukue mama, baba abaki
na nani? Labda wakubali tuongozane wote.” Mama Sabina akatamani kuruka kwa
furaha. “Sasa ugeni wote huo si mtalemewa?” Akajibaraguza mama Sabina. “Hata
kidogo mama. Sabrina huyu ametengeneza kinyumba cha nje, amekitolea muundo
mzuri, wala hamtambana mtu. Mtaishi kwa utulivu kabisa, labda muwe mnahofia
majukumu yenu, lakini kwetu sisi milango ipo wazi. Tena naona mtamchangamsha
Sabrina, nitakapoanza kazi.”
“Hakuna
majukumu baba. Kuku aliokuwa akitusaidia kufuga Sabrina, walikufa kufa pamoja
na ng’ombe nao wakaugua. Lilibaki dume moja, ndio hilo tunafanyia biashara ya
kupandisha majike ya watu. Wakileta jike likapandwa, wanatulipa.” Sabrina akashituka
sana mpaka akakaa akiwa na maumivu. “Mama! Kweli?” “Acha tu. Tumeishiwa kweli.”
“Ng’ombe walipatwa na nini?” Sabrina akauliza kwa kuumia. Ndiye aliyekuwa
akiwatunza. “Magonjwa. Wakafa mmoja baada ya mwingine. Ndio hivyo. Na kuku nao
walikufa, na kuuzika ikawa shida, tukaona tusiendelee kuagiza sababu ya
hasara.” “Poleni mama.” Sabrina akaumia sana.
“Lakini
mama, hawa wakiruhusiwa tu, tunaondoka jijini. Na kama alivyosema jana daktari,
wakiendelea vizuri, leo wataruhusiwa. Mida hii ya saa 4 watapita. Ndipo
tutajua.” “Kwa hiyo mkiruhusiwa leo, mnaondoka leoleo?” Sabina akauliza. “Inategemea.
Kama ni leo asubuhi na nikapata nafasi ya ndege, tunaondoka leo. Kama
tukichelewa, Mungu akipenda kesho asubuhi tunaondoka.” Sabrina akahisi kuna
jambo linaloendelea ndio maana kuna uharaka wa kuondoka. Kwa kutomuona mama
Msindai hapo mpaka muda huo na mumewe, akajua bado mambo si shwari. Lakini
akamshukuru Mungu Jack yupo upande wake, akajiambia hilo linatosha. Moyoni
akatulia. Wakatulia.
“Kama
mama mmekaribishwa, labda upate muda wa kwenda kuzungumza na baba, mjiandae
ndipo muwafuate Singida. Si ni sawa Sabrina? Au unasemaje Jack? Kwa hakika
mtahitaji msaada.” Sabina akatoa wazo. “Kabisa. Muda na wakati wowote
watakapokuwa tayari, wanakaribishwa.” Akajibu Jack kwa jumla tu, akamsogelea
Sabrina. “Vipi, unajisikiaje?” “Vizuri, ila nina hamu ya kulala muda mrefu bila
kuamka.” Jack akamcheka. “Nahisi hapa kazi ndio imeanza mama. Starehe zile
zakulala mpaka asubuhi alam ituamshe, imeisha.” Wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Daktari
akaingia na Mzee Msindai. Sabrina na Jack wakashituka. Wakamsalimia mzee Msindai
kwanza. “Kwema?” “Kwema kabisa. Waliniambia wanataka kuwaruhusu leo, nikasema
lazima niwepo kuangalia watoto ili mkiruhusiwa, tuwe na amani kuwa wapo sawa.”
Akamsogelea Sabrina. “Ulilala vizuri?” “Hapakuwa na matatizo.” “Acha niangalie
wajukuu wakati wewe ukimsubiria daktari wa wakina mama.” Mzee Msindai na
daktari wa watoto wakahamia kwa wajukuu. Wakawatoa nguo zote kasoro diaper na
kuanza vipimo upya. Wakaangalia kila kitu tena kwa upya. Wakapima kwa makini na
mashine walizokuja nazo na nesi akaingiza nyingine, wakaona watoto wapo sawa.
“Hawa
wajukuu wapo sawa kabisa. Hata wakirudi Singida wakapewa jembe kwenda kulima
uwele, nitakuwa sina wasiwasi.” Wakacheka. Msindai akawatania hapo wale manesi
na yule daktari aliyeingia naye, wakatoka. “Naomba tuzungumze nje kidogo baba.”
Jack akamsogelea baba yake. “Sawa.” Wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Sisi
tukiruhusiwa leo, tunaondoka leo kurudi Singida.” “Ameniambia Junior na ndio
maana nipo hapa kuhakikisha hamlali hotelini, mnaondoka leo kurudi nyumbani. Hawa
watoto ni wadogo sana kulazwa mahotelini. Hivi tunavyozungumza hapa, Junior
anashugulika na Jacinta pamoja na Willy, kuhakikisha mizigo yenu yote inapakiwa
vizuri kwenye lori moja, iondoke leoleo kuwahi Singida. Ikichelewa sana, kesho
asubuhi iwe imefika huko.” Jack hakuamini. Alijua kaka yake na familia
wanakwenda kanisani, kumbe bado wanamuhangaikia! “Nashukuru sana baba.”
“Nafikiri Pendo amepata tiketi zenu zakuondoka jioni. Itabidi muunganishe. Ila
atawapigia simu kuwataarifu.” “Nashukuru sana baba. Asante.” “Karibu. Mungu
akusaidie wewe na familia yako. Naamini mambo yatakuwa tu sawa.” “Naamini hivyo
baba. Nampenda mke wangu, na kweli hajawahi kunirubuni. Sabrina amekuwa muwazi
kwangu katika kila jambo. Ninayoyafanya ni katika kupenda kwangu.” Jack
akajieleza kwa utulivu akitaka baba yake amuamini.
“Katika
kila maamuzi, kuna faida zake na hasara zake Jackson. Ni wewe kupima. Kupi
kunalemea? Na ukiridhia kwa moyo mmoja kabisa, ukamuomba Mungu na kuchukua
hatua, utakuja kuona ule upande ambao hukuchagua unaanza kupewa nguvu na ule
uliochagua. Hata kama ulichagua upande wenye hasara. Ukifanya kwa moyo bila
kuchoka, utashangaa ule upande unaanza kuvuta mema taratibu na unakuwa salama
tu. Kikubwa nia, na umuombe Mungu. Utafanikiwa.” “Nashukuru. Asante sana.
Naamini tutakuwa salama.” Baba yake akacheka na kumpiga begani. “Umekuwa sana
Jackson! Umekuwa na akili za kiutuuzima! Unawajibika kiume. Pongezi sana.” Jack
akajisikia furaha kusikia hivyo kutoka kwa baba yake. Wakarudi ndani.
Sabrina aruhusiwa hospitalini
akiwa mzima, waondoka jijini Dar bila kuagana na mama Msindai.
M |
zee Msindai
akaanza utani kwa mama yake Sabrina. Akamtania kwa hili na lile, wakawa
wanacheka tu hapo ndani mpaka daktari wa wakina mama naye akapita. Akamsalimia
Mzee Msindai, naye akamtania kwa hili na lile. “Sasa hawa wajukuu wawili, wanamtaka
mama yao, wawahishwe shamba leo. Mapema kabla jua halijachwa. Uwele unaliwa na
ndege huko Singida.” Wakacheka. Daktari akazungumza na Sabrina kidogo, na kwa
kuwa hakuwa na tatizo, mkwewe ni dokta Msindai, akaruhusiwa. Msindai
akazungumza nao kidogo, akawaaga na kubusu wajukuu, kwa ahadi ya kwenda
kuwatembelea karibuni. “Nikija huko Singida mnipikie ugali na mlenda.”
Akawatania wajukuu zake hapo, akawaweka chini na kuondoka.
“Kwa
kuwa Pendo atakuja kunisaidia kujiandaa hapa na kutusindikiza uwanja wa ndege
na Joy, mama wewe ungeenda kuzungumza na baba. Akiridhia, mpange safari.
Nitakupigia nikifika nyumbani, na kuwatumia nauli.” Akafurahia sana mama
Sabina. Wakachukua vyombo vyao, nakuondoka. Mchana wakarudi Pendo, Joy,
Jacinta. Wakamsaidia Sabrina na kumsindikiza mpaka uwanja wa ndege. Walipofika
uwanja wa ndege tu, na Junior pamoja na Awali nao wakaja. Mpaka hapo Sabrina
akawa hajamuona mama mkwe wake na Jena. Lakini alishukuru Mungu. Hakutaka hiyo
fujo na maneno maneno tena.
“Gari
yenye mizigo yenu imeshaondoka. Mambo yakienda sawa, kesho watafika Singida.
Nimewapa namba zenu wote wawili, na hii ni namba ya dereva na mwenzie
anayemsaidia. Nimeshalipia kila kitu, na nimewaambia wasiondoke mpaka
wahakikishe wanaingiza vitu vyote ndani. Wasiviache nje. Kwa hiyo mkifika,
nyinyi muandae sehemu tu. Zaidi vitu vya watoto.” “Tunawashukuruni sana. Asanteni.” Sabrina naye akashukuru. Pendo
alileta viti vya watoto wachanga aina hiyo ya mapacha ambavyo Sabrina alipata
zawadi kwenye baby shower. Jack na Sabrina wakaaga kwa kuwapa mikono na kukumbatiana,
wakaingia ndani uwanja wa ndege.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sabrina
alikuwa akimuona vile Jack anavyohangaika naye na watoto utafikiri ni watoto
wake wakuwazaa! Alimsaidia Sabrina kwa kila namna hapo uwanja wa ndege wakisubiri
kuondoka na kwenye ndege hivyohivyo kuhakikisha watoto wapo sawa. Alikuwa
akiangalia mpaka diaper kwa kila mtoto! Sabrina akabaki amkimfikiria Jack,
nakumshangaa. Hakutaka Sabrina asumbuke. Alifanya kwa moyo kabisa akijituma
bila kuchoka wala kutumwa. Sabrina akabaki akishangaa upendo mkubwa wa kiasi
kile! Kuwepo hapo na Jack bila kumuona mama yake, inamaana mambo hayapo vizuri
kati ya wapenzi hao wawili. “Inamaana Jack amenichagua mimi dhidi ya mama
yake!” Sabrina akabaki akiwaza kwenye ndege. “Niliwezaje kuwa kipofu kwa
muda wote huo nisione mapenzi makubwa hivi tokea mwanzoni!” Sabrina
akajilaumu akiumia. Mawazo yakamrudisha chuoni.
Walipokuwa Chuoni.
I |
likuwa
mida ya jioni siku ya ijumaa hapo chuoni, Jack alishamsaidia kuweka mambo yake
na uongozi wa chuo sawa, akiwa ameshakusanya ripoti aliyosaidiwa na mpenzi wa
Jack na kurudi darasani rasmi. Ikawa imebaki kazi ya Sabrina kujisomea ili
kuendelea kulingana na wenzake darasani. Alitoka usingizini mida hiyo baada ya kutoka
darasani alipojisikia kichwa kumuuma sana, na baridi akaamua kulala, ndipo
akaamka sasa akijisikia bado mgonjwa. Ilikuwa mwaka wa mwisho. Miezi miwili
ilibaki kumaliza chuo. Ile hali aliyokuwa akijisikia, alihisi ni malaria tu,
kwani bado alitetemeka baridi katika jiji hilo la Dodoma, msimu huo wa
kiangazi. Joto. Na mwili mzima ulikuwa umepatwa moto. Hakuwa na pesa hata
kidogo. Alitoka kuzungumza na wazazi asubuhi hiyo, wakamwambia hawana pesa.
Sabina alikuwa amemtumia pesa mwezi uliopita, akaona aibu kuomba tena. Kaka
yake ndio alikuwa ameanza kazi na hakuwa mtoaji. Mara zote alikuwa hana pesa. Hakuna
aliyekuwa akipata pesa yake.
Sabrina
akaona aende kwa Jack, hata kama atashindwa kuomba pesa, basi dawa ya maumivu.
Akatembea mpaka kwenye jengo hilo lililojulikana ni la viongozi. Moja kwa moja
kwenye chumba cha raisi ambaye alikuwa Jack. Akagonga kidogo tu kwa sauti ya
chini. “Nani?” Akauliza Jack. “Sabrina.” Sabrina akakumbuka kusikia purukushani
kidogo ndani ya hicho chumba. Sabrina akarudi nyuma kidogo akiwa amekunja uso
nje ya mlango uliokuwa bado haujafunguliwa. Akaanza kujiuliza kama aondoke au
asubiri kufunguliwa kwani bado purukushani ndani zilikuwa zikiendelea. “Naweza
kurudi baadaye!” Sabrina akazungumza kwa sauti ya chini na wasiwasi kidogo.
Hapo hapo mlango ukafunguliwa. Akachungulia Jack akiwa na wasiwasi kama
aliyefumaniwa na mkewe, wakati ni Sabrina aliyemkataa hadharani, wapo kumsaidia
tu. Sabrina akakumbuka kumuona akiwa amevaa suruali yake ya jinsi bila hata
mkanda na nguo ndogo ya kiume ya ndani. Singilendi.
“Kwani
anaingia ndani ili na mimi nivae?”
Akasikia sauti ya Phina akiuliza ndani kwa kulalamika. “Halafu angekuwa
hata anapiga simu kukutaarifu kuwa anakuja jamani! Anawezaje kutokezea tu!”
Phina akaendelea kulalamika. Sabrina akazidi kujisikia vibaya. “Samahanini sana
jamani! Ni kweli nilitakiwa hata kupiga simu. Sikukusudia kuingilia.” Sabrina
akaongea kwa hofu na sauti ya chini kama asiyetaka majirani wasikie. Jack
akarudisha kichwa ndani kama kutaka kumjibu Phina, hapohapo Sabrina akaondoka
kwa haraka bila hata kuaga. Jack kutoa tena kichwa nje, Sabrina hayupo, akawa
alishaondoka.
Sabrina
alirudi chumbani kwake akachukua madaftari na kurudi kusoma akiwa mgonjwa na
njaa. Jack alimkimbiza akiwa vilevile bila viatu. Alishuka mpaka chini
hakumuona Sabrina. Akarudi chumbani kuvaa shati na viatu kwa haraka, Phina
akiwa amebaki kitandani, akishangaa. Anaacha mapenzi kumkimbilia Sabrina! Hicho
kitu kikamuuma sana Phina, akashindwa kuelewa, akahisi amedhalilishwa vibaya
sana. “Sikuelewi Jack! Unaniacha hapa, unamkimbilia Sabrina?” Akili ya Jack
wala haikuwa pale tena. Hakumjibu kitu Phina. Akaendelea kuvaa viatu baada ya
soksi kwa haraka. “Wewe Jack!?” “Naomba tuzungumze baadaye Phina.” Jack akavuta
shati na kutoka kwa haraka, akamuacha Phina kitandani.
Phina
akavaa nguo zake akaona machozi yanamtoka. Akajua ndio ameachika, akaanza kuona
aibu jinsi atakavyodhalilika pale chuoni. Kujulikana ameachwa na Jackson
Msindai! Raisi wa chuo! Phina akahisi kuishiwa nguvu kabisa. Akakaa pale
akifikiria, akaamua kumpigia simu Jack. Akaona simu zake zinakatwa, asijue Jack
kwa muda huo hakutaka muingiliano wowote kwenye hiyo simu. Alikuwa akimpigia
simu Sabrina huku akimsaka kila mahali. Alianzia chumbani kwake, akamkuta
msichana anayelala na Sabrina hapo chumbani yupo na wenzake wamekaa wanaangalia
tv. “Sabrina amepita hapa sasa hivi?” Wote wakakaa sawa, ni Jackson Msindai,
raisi wao, ndiye anayeuliza. “Alikuwa amelala hapa. Nafikiri anaumwa, maana
alikuwa akitetemeka baridi. Akatoka mara moja, akarudi tena. Akachukua
madaftari yake na vitabu, akatoka tena. Hakukaa.” Jack akatoka tena hapo kwa
haraka. Akapita maktaba ya chuo. Akazunguka kila meza kila kona. Hakumkuta.
Akaenda darasani kwake. Sabrina hakuwepo. Akaendelea kumtafuta huku akimpigia simu
kama mwehu bila mafanikio.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku
kwa Phina nako akatoka, akaona aende kwa Ibra, rafiki wakaribu sana Jack.
Akamkuta Ibra chumbani kwake. “Mbona kilio tena ‘first Lady’ wetu!” Jina
lililompa heshima kubwa sana Phina hapo chuoni, akijulikana kama first lady,
kwa kuwa alikuwa mpenzi wa Raisi wa chuo. Kote walimuita first lady hata
alipokuwa na Jack mwenyewe. Na Jack hakuona tatizo Phina kuitwa first lady.
Ikabidi Phina amuelezee Ibra mkasa mzima.
Japokuwa
Ibra alishachoshwa na Jack juu ya Sabrina, na hakuwa akimuelewa kabisa, lakini
ilibidi kumchukulia hivyo hivyo na huo udhaifu wake. Ndipo ikabidi kumkalisha
chini Phina na kumuweka sawa. “Kaa kwanza hapo kwenye kiti, uniangalie na
kunisikiliza kwa makini.” Phina akakaa
mbele ya Ibra. “Haya, futa machozi kabisa, kwa kuwa haya mambo hayahitaji
papara. Ukijichanganya tu, utaharibu na utanikumbuka. Ila ukinisikiliza vizuri,
utafaidi kwa kuwa Jack sio mchoyo na ni Msindai. Sijui kama unanielewa?” Phina
akatulia ili kuelewa.
“Sijui
Jack alikwambia nini juu ya mahusinao yenu mwanzoni kabisa mnaanzana na sijui
unamfahamu kwa asilimia ngapi! Lakini ana vitu vichache sana anavyopenda na
kusifia. Hana madhaifu mengi kama mwanadamu. Mimi ni mtu wake wa karibu sana.
Mpaka umuudhi Jack au akuhesabu ni adui, sijui utakuwa umefanya nini! Ndio
maana unamuona anakubalika kila sehemu na kila mtu. Ana hekima yake ya kuishi
kwenye jamii na ana uwezo mkubwa sana wa kuendesha mambo. Nadhani unaona kwenye
uongozi wake.” Hapo hata Phina akakubali.
“Tokea
namfahamu Jack. Tunapokuwa naye nje ya hapa, yaani huko mtaani, nyumbani na
hapa pia chuoni ni mtu mwema sana. Ila anao udhaifu mmoja wa ajabu sana,
unaitwa Sabrina.” Hapo Phina akakunja uso. “Linapokuja swala la Sabrina, hana
mipaka wala undugu. Naweza nisikueleze kwa undani ukanielewa, lakini Ney, huyu
unayetuona tunazunguka naye sana hapa chuoni tukiwa na Felix pamoja na Msindai
mwenyewe, anaweza kukueleza.” Ibra akaendelea kumuweka sawa Phina.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
huku kwa Jack akiendelea kumsaka Sabrina karibu kuchanganyikiwa. Kumbe Sabrina
alipochukua madaftari yake ijumaa hiyo ambayo karibu wanachuo wengi wanakuwa
wameshaanza weekend. Miziki mikubwa vyumbani, wanaokwenda baa wanakwenda
kustarehe, wenye ndoa zao wanakimbilia majumbani mpaka jumapili, yeye Sabrina
ambaye hakuwa hata na rafiki wa kusoma naye, akaona akajifiche kwenye darasa la
certificate. Akaenda kukaa nyuma kabisa ya darasa, akiwa amevaa koti zito,
akajifunika na kitenge chake, akajiinamia akisoma.
Baada
ya muda waliingia wenzake wa darasa moja. Walijulikana kundi lao la kujisomea
na wengi waliwajua kama ni wasongo. Kusoma kupita kiasi. Waliingia
wakatengeneza duara lao mbele kabisa. Wakike na wakiume. Wakaanza kusoma na
vicheko vikiendelea. Hawakumsalimia Sabrina kabisa japo walimuona. Sabrina
akatulia tu akijisomea peke yake. Wakati mwingine mmoja wao alisimama mbele
kabisa ubaoni akiwafundisha kama mwalimu wengine wakiuliza maswali, huku
wakiendelea kusoma.
Baada
ya muda tena Sabrina akaanza kuona watu wachache wakiingia na kukimbilia viti
vya nyuma karibu na yeye ambako kuna utulivu. Sabrina akatulia kabisa,
akaendelea kusoma. Mara akasikia wakimsalimia Jack. “Karibu mkuu uungane nasi.”
Lile kundi kubwa la mbele likaanza. Akijua mkuu ni Jackson Msindai, Sabrina
hakunyanyua hata uso kutizama. Akasikia sauti ya Jack akiwasalimia na kuuliza
maswali machache, kisha akawasikia wakijichekesha. Sabrina akatulia kimya.
Akasikia akiwaaga, pakazuka ukimya.
Kiti
kikavutwa mbele yake. Jack akakaa. “Vipi?” Jack akaanza, Sabrina akaitika,
“Safi tu.” Kwa sauti ya chini bila hata kumtizama. “Simu yako iko wapi?” Jack
akauliza. Sabrina akakunja uso akiwa vilevile ameinamia madaftari yake bila
hata kumwangalia, kisha akaanza kuitafuta mifukoni kwake. Akaikosa, akarudi
kwenye begi lake alilokuwa amebebea vitabu. Akaikuta humo ndani. Akaitoa.
Akakuta missed calls 27 kutoka kwa Jack. Akashangaa na kumwangalia Jack.
“Samahani, sikuona. Simu ipo kwenye silence.” Akaongea kwa sauti ya
chini huku akiitizama simu yake nakuendelea kuhakikisha missed calls zote alizokuta. Akajiridhisha kuwa zote
zimetoka kwa Jack. “Sikuwa nimeshika simu.” Sabrina akarudia kwa sauti ya
chini. Kisha akakumbuka kumwandikia ujumbe kwenye kikaratasi, Jack akimtizama. ‘Samahani, sikukusudia kuingilia au kuwasumbua kule chumbani
kwako. Sitarudia tena. Samahani.’ Akamgeuzia kile kikaratasi, lakini
Jack alishakuwa amekisoma wakati akikiandika. Akakumbuka kumuona Jack kukivuta
kile kikaratasi, akakikunja na kukiweka mfukoni bila yakujibu.
“Mbona
umejifunika vitu vingi na kuvaa koti? Unaumwa?”
Akamuuliza. Walijua wazi watu wa pembeni wanawasikiliza, Jack hakujali.
Kimya, Sabrina ameinama akichora alama ya mshale kwa kurudia rudia. “Brina?”
“Hapana. Nipo tu sawa.” Sabrina akajibu bila yakumtizama. Akashitukia Jack
ameweka mkono kwenye kipanda uso. “Mmmh!” Jack akahamaki. “Una homa kali!
Umekunywa dawa?” Jack akauliza. Sabrina akatingisha kichwa kukataa. “Unafikiri
inaweza kuwa malaria?” Jack akauliza tena. “Sijui!” Sabrina akajibu sauti ya
chini. “Twende tukaangalie mjini mara moja.” Sabrina akakunja uso na kumtizama.
Macho yakagongana. “Twende hospitali.” Jack akaongea akisika kujali. Kwa kuwa
darasa zima lilikuwa kimya gafla, hata waliokuwa wakisoma kama kundi, nao
wakawa kimya, Sabrina akajua kila mmoja anasikiliza. Akakusanya vitu vyake na
kurudisha kwenye begi lake. “Nikusaidie?” Jack akauliza kwa kujali zaidi.
“Hapana, asante.” Sabrina akasimama, wakatoka. Jack mbele, yeye nyuma.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huyu
Sabrina ndiye aliyekuwa amemkataa Jack kwa jeuri kubwa na ukali, akijua ni mke
mtarajiwa wa Emma. Akaachika vibaya sana, tena kwa kudhalilishwa mbele za watu,
chuo kizima kikajua. Jack amerudi kuwa mkombozi. Anamjali kama mpenzi wake!
Akakumbuka kumtongoza tena kwa mara ya pili. Sabrina tena akamkataa akijua
atakuwa mke mtarajiwa wa Tino. Tino akamuacha kikatili akitaka hata asibakie na
watoto wake! Jackson huyo huyo akamfuata Moshi na kumchukua. Amefunga naye ndoa
ya hali ya juu. Amezaa watoto wa kizungu, lakini bado Jack yupo naye hapo
akihangaika naye. Kutokuagana na mama Msindai, na yale aliyoyasikia kutoka kwa
huyo mama akimsengenya na kumsingizia uchawi, inamaana wamekosana na Jack kwa
ajili yake. Sabrina akaumia sana moyoni. Akamtizama Jack ambaye macho yake
yalikuwa kwa mtoto aliyekuwa amekaa naye yeye. Jeiline. Na Sabrina alikaa na Keiline.
Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama kusafisha kifua na
mawazo. “Nilishindwaje kuona mapenzi mazito hivi kutoka kwa Jack!” Akaendelea kujilaumu, jinsi alivyompuuza Jack
na kuwapa wanaume wengine kipaumbele wakati hata hawakustahili. Mawazo
yakamrudisha tena chuoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Ulikula?”
Akakumbuka Jack kumuuliza wakati wakitembea
kufuata gari ya Jack. Jackson Msindai alikuwa na usafiri wake hapo chuoni. Kila
mtu alijua kama Jack anayo gari. Alipokuja mwaka wa kwanza, muhula wa kwanza,
hakuwa na gari. Lakini muhula wa pili, akarudi chuoni na gari yake. Japokuwa
alikuwa akiishi hapohapo chuoni, lakini alikuwa na usafiri wa maana. Gari nzuri
sana ya heshima aliyokuwa akiegesha kwenye sehemu maalumu wanapoegesha walimu
wa hapo chuoni. Na kwa kuwa hakuwa akiitumia kila siku, na Dodoma kulikuwa na
jua kali na vumbi, alikuwa akiivalisha plastiki yake maalumu ambayo ilikuwa
kama nguo ya gari. Akitaka kutoka ndipo alipokuwa akiitoa kirahisi tu, na
kuikunja. Akirudi anaivalisha tena. Hata walinzi hapo chuoni walijua ni gari
yake.
“Brina,
umekula?” Ikabidi Jack amgeukie na kumuuliza akimuonyesha anataka jibu la
hakika. “Nilikunywa chai asubuhi.” Sabrina akajibu taratibu, Jack akataka
kuuliza swali jingine, akaona anyamaze. Wakatembea mpaka kwenye gari yake.
Akatoa plastiki ya juu, Sabrina akimshangaa tu jinsi anavyohangaika naye.
Amejikunyata, akitetemeka baridi ya kutoka ndani ya mwili wake wala haikuwa
baridi ya nje. Akamfungulia mlango. “Twende hospitalini.” Sabrina akapanda
kwenye gari, Jack akaondoa gari. Akapita kwenye baa moja ambayo haikuwa mbali
na hospitalini, akamnunulia chakula, akamletea na soda. “Kula kabla hatujafika,
ili ikitokea unapewa dawa, isikusumbue tumboni.” “Asante.” Sabrina akashukuru
na kupokea. Bila kuchelewa, Sabrina akaanza kula. “Wewe ulikula?” Jack
akamgeukia akiwa anaendesha. “Nina vyakula chumbani. Nipo sawa. Wewe kula.”
Sabrina akaendelea kula mpaka wanafika hospitalini akawa bado hajamaliza kula.
Jack akaegesha gari nje, akamalizia kula ndipo wakaingia ndani.
Akapimwa
na kukutwa na malaria. Jack akamwambia daktari waliyemkuta hapo zamu na
kuwahudumia kuwa Sabrina ana kazi nyingi sana chuoni, kama angeweza kumuandikia
dozi nzuri na zakutumia muda mfupi, ingekuwa jambo zuri. Mtoto huyo wa Msindai
akasema pesa isiwe tatizo. Daktari akacheka na kumuandikia dawa Sabrina, za
kushusha homa na hizo za malaria.
Wakati
wanatoka hospitalini, Ibra akapiga. “Uko wapi wewe?
Hata gari yako haipo!” “Nipo hospitalini, nimemleta Brina. Ana malaria kali na
homa ipo juu.” “Daah! Mpe pole.” “Atasikia.” “Sasa?” Akauliza Ibra. “Ameandikiwa dawa, ndio tunakwenda kununua, kisha turudi
chuo. Kwema?” Jack akauliza wakati wanapanda kwenye gari. “Kwema tu. Nilikuwa nakucheki. Siunakumbuka discussion
ndio muda huu?” “Nyinyi endeleeni tu.” Jack akajitoa kabisa huku akijua
wenzie wanamtegemea. “Labda tuahirishe Jack. Unajua
hakuna kitakachoendelea bila wewe pale. Ile topic ni wewe mwenyewe ndiye
uliyeelewa na ukaahidi washikaji utawasaidia leo.” “Basi waambie nimepatwa na
dharula, iwe kesho.” Kirahisi tu Jack akaahirisha na kuaga. “Tutaongea baadaye basi.” Akakata kabisa simu na
kurudisha mfukoni bila kusubiri majibu ya Ibra.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Unaweza
kunipa hiyo karatasi ya dawa, nikanunue dawa, wewe uwahi chuoni ukasome na
wenzako Jack. Mimi nitakuwa sawa tu.” Sabrina akaona asimuharibie ratiba zake.
“Watakuwa sawa tu. Twende tukanunue dawa, ukapumzike.” Sabrina akajirudisha
kitini, akatulia. Wakaendesha mpaka duka la madawa kubwa hapo Dodoma alipokuwa
ameelekezwa na huyo daktari kuzipata aina hiyo ya dawa. “Naona hapo pembeni
kuna duka. Mbali na maji ya kunywa, unataka nikununulie na nini kingine?” Jack
akauliza walipofika. “Toilet paper na dawa ya mswaki tafadhali.” Sabrina
hakutaka hata kujivunga. “Na nini kingine?” Sabrina akashangaa kuwa bado
anaulizwa tena. “Niongeze tena!?” “Wanaonekana ni duka kubwa, lina vitu vingi.
Sidhani kama utakosa mahitaji yako hapo. Au unataka twende wote?” Sabrina
akababaika kidogo. Kisha akasita. “Brina! Mimi ndiye niliyekwambia. Hujaomba.
Kama umeishiwa na unadhani utapata vitu vyako hapo, shuka umwambie muuzaji,
mimi nitalipa.” “Nimeishiwa vitu vyote vya msingi Jack. Na hapo naona kama ni
super markert. Bei zitakuwa juu sana. Kuna sehemu huwa nakwenda kununua vitu vyangu.
Wanabei nzuri.” “Wewe mbona muoga wakati hata hatujajua bei? Naomba twende.”
Wakashuka wote garini.
Jack
akaenda upande wa dawa, akaagiza, na kulipia. Wakahamia upande wa pili. Sabrina
akabeba kikapu kidogo, wakaingia ndani. Jack akampokea. “Mimi nitabeba. Wewe
chagua.” “Asante Jack.” Sabrina hakujivunga. Hakuwa na vitu vingi tu vya
muhimu, vya kike na vya kawaida. Akaweka vyote, Jack akiwa anamfuata kwa
pembeni. Akawa akichukua kwenye shelfu na kuweka kwenye kapu, mpaka akamaliza.
“Nashukuru Jack.” “Unauhakika umekumbuka kila kitu?” “Ndiyo, asante. Nilikuwa
nimeishiwa mpaka sabuni ya kuogea!” Jack akatabasamu tu. Wakalipia na kurudi
chuoni.
Waliegesha
gari ya Jack palepale walipoitoa mwanzo, Jack akaifunika, wakaelekea chumbani
kwa Sabrina. Walipoingia wakakuta wale wasichana wamejaa pale na wanapiga
kelele. Walipomuona tu Jack, wakatulia. “Samahanini. Sabrina anaumwa. Tumetoka
hospitalini, amepewa dawa anatakiwa kupumzika. Niombe radhi kwa usumbufu, kama
mnaweza kuhamisha hii sherehe chumba kingine ili yeye apumzike, ingemsaidia
sana. Samahanini sana.” Kwa heshima zote wakakubali na kumpa pole Sabrina
wakati hilo kundi ndio waliokuwa miongoni wakumcheka Sabrina na kila wakiingia
humo ndani walimfanya ajisikie kama hayupo. Wakatoka.
“Nakushukuru
Jack. Maana nilikuwa nikiwaza nitalalaje hapa ndani na kelele za hawa watoto
wanaonidharau hivi! Maana walikuwa wakianza kucheka hapa, mpaka inanibidi mimi
ndio niondoke. Na leo kichwa kinaniuma sana, nahitaji kupumzika.” “Pole. Kunywa
dawa zote, ndipo utaamka ukiwa na nafuu.” “Asante sana, na usiku mwema.” “Mbona
kama unanifukuza!?” Sabrina akacheka kidogo kwa aibu. “Nataka nibadili nguo
nilale.” “Oooh! Haya. Usiku mwema, nitakuona kesho.” Jack akatoka.
Sabrina
akabadili nguo, na kumeza dawa. Akaanza kupanga vitu alivyonunuliwa na Jack
kabatini. Baada ya dakika tano tu kumeza dawa, akasikia zinapanda. Akakimbilia
bafuni, akazitapika zote. Aliona zile dawa zote alizomeza amezitapika kama
zilivyo. Akatamani aziokote asiharibu dozi, lakini akashindwa, ilikuwa chooni.
Akatoka hapo akiwa amesikitika sana. Dawa alinunuliwa aghali sana na Jack. Hana
pesa. Anafanya nini tena na kwenda kwa Jack alisikia mpenzi wake akilalamika
kufika kwake bila taarifa! Sabrina akajiambia amebakiwa na dawa za kupunguza tu
maumivu na kushusha homa, dozi ya malaria ilikuwa kunywa tu mara moja. Akapoa
akiwaza chakufanya. Akarudi kunywa maji. Akatapika tena. Kichwa kikaendelea
kumuuma, akajaribu kumeza tena dawa, akatapika. Usiku huo ukawa wakutapika
mpaka mwenzie aliporudi katikati ya usiku, akaondoka tena. Maana Sabrina
aliamua kutapikia ndoo yake ya kuogea baada ya kuchoka kukimbilia chooni,
ikamkera mwenzie akaona ampishe.
Jumamosi.
K |
wenye mida
ya saa mbili na nusu Jack akarudi. “Atakuwa amepitiwa na usingizi muda huuhuu
huyo. Mimi nilishindwa kulala usiku sababu alikuwa akitapika mfululizo
nikashindwa kulala. Nikaenda kulala kwa rafiki yangu, nimerudi kwenye saa moja,
pia nimemkuta akitapika.” Yule binti akamwambia Jack. Jack akashangaa. Sabrina
alimuacha jana yake akiwa na homa tu, hata daktari alipomuuliza kama anatapika,
akakataa na kumwambia vidonge vitamfaa! Akaenda kukaa kitandani kwake. Sabrina akiwa
usingizini akahisi mikono ya kiume ikimpapasa kichwani. Akageuka. “Jack!” “Homa
ipo juu sana. Vipi!?” “Natapika, Jack! Sijui nifanyeje? Kila ninachoweka
mdomoni kikikaa sana dakika mbili, kinatoka.” “Dawa?” “Nilitapika usiku
uleule.” “Pole, sasa kwa nini hukuja kule kwangu?” Sabrina akamtizama kidogo na
kunyamaza. Jack akakumbuka fumanizi. “Au basi hata kunipigia simu?” Jack
akabadili. Sabrina akanyamaza. “Itabidi turudi hospitalini.” “Tena Jack!?”
“Sasa unafikiri utaponaje? Lazima kurudi. Umebakiza muda mfupi sana wakumaliza chuo,
Brina. Huna muda wakuugua.” “Ni kweli.” Wakarudi tena hospitalini.
Daktari
akamuwekea drip ya maji maana Sabrina alimwambia anasikia kizunguzungu na
amechoka sana. Akamwambia Jack, anamuwekea dripu ambayo itamsaidia kumrudishia
nguvu na pia itakuwa na dawa ya kuzuia kutapika. Ilipoanza kuingia mwilini,
Sabrina akaanza kusinzia. “Nasinzia Jack. Sijalala usiku.” “Lala usiwe na
wasiwasi. Ikiisha nitakwenda kumuita nesi.” “Asante.” Sabrina akashukuru.
Mara
Phina akampigia. Jack akapokea. “Nilikwenda chumbani
kwa Sabrina kumuomba msamaha, jana nahisi niliropoka. Nikaambiwa na yule
msichana anayeishi naye, umemrudisha hospitalini. Mko wapi?” Jack
akamuelekeza hospitali walipo. “Lakini hatutalala.
Amewekewa dripu moja tu, kisha tutaruhusiwa.” Jack akaongea bila hata
wazo la pili mpaka akamshangaza Sabrina mwenyewe. Phina akaumia lakini
akajikaza. “Angalau nimletee hata uji tu! Asilale na
njaa.” Hapo akawa amemgusa Jack. “Hilo wazo
zuri. Nashukuru. Kina Ibra pia wanakuja, mpigie Ibra simu mje naye,
wasikuache.” “Sawa.” Jack akakata. Sabrina akapotelea usingizini
asimuelewe Jack.
Kufika
majira ya saa tano asubuhi, uongozi wote wa chuo wakahamia hapo kwenye hicho
chumba alichopumzishwa Sabrina. Kila mmoja akitaka aonekanike kwa Jack kuwa
anajali. Jack alipoona kelele zinazidi, akawaambia wahamie nje. Stori
zikaendelea. Wakahamisha makao hapo. Lakini Phina akajisikia vizuri na yeye
kuwepo hapo na bado wanamtambua kama first lady na Jack hakatai wala hana
wasiwasi juu ya hilo. Akaamini maneno ya Ibra. Kila wakati walimuona Jack
akirudi ndani kumuangalia Sabrina aliyekuwa amelala hana habari. “Vipi lakini?”
Ibra akamuuliza wakati anatoka. “Daktari ameniambia baada ya hiyo dripu,
atakuwa sawa. Analala sana sababu ya dawa, na usiku pia hakulala. Alikesha
akitapika.” Jack akaeleza bila hata wazo la pili mbele ya wenzake na Phina.
Dripu
liliiisha Jack akiwepo chumbani, akaenda kumuita nesi, akarudi naye chumbani na
daktari. “Brina!” Wakamsikia Jack akimuamsha kwa upole. Sabrina akaamka. “Nasikia
usingizi!” “Pole. Lakini daktari anataka kuzungumza na wewe.” Sabrina
akajigeuza taratibu. Unajisikiaje?” Daktari akamuuliza. “Nimelala muda wote,
hata sijaamka kutapika.” “Sasa kwa kuwa umeacha kutapika, nakuandikia tena dawa
ile ile. Utakunywa mara moja tu na kuendelea kunywa dawa za maumivu. Baada ya
ya leo na kesho utaanza kujisikia vizuri.” “Nashukuru sana.” Sabrina
akamshukuru. “Sasa kabla yakuondoka, utakunywa hapahapa hiyo dawa.
Tukihakikisha imekaa humo ndani, ndio tutakuruhusu.” “Hilo litakuwa la msingi
dokta. Ili tusirudi tena.” Akaongeza Jack.
Nesi
akatoa ile dripu akaacha sindano. “Hii nitatoa mwishoni kabisa tukishahakikisha
haitatumika tena.” “Inamaana kama sitatapika tena?” Sabrina akamuuliza yule
nesi na sauti ya usingizi. “Sawa sawa.” Akamalizia alichokuwa akifanya, akaaga.
“Nitarudi na dawa baada ya muda mfupi.” “Asante sana.” Jack akashukuru, yule
nesi akatoka. Phina akarudi ndani. “Vipi Sabrina?” Phina akamsogelea pale
kitandani. “Safi tu, na samahani Phina. Jana sikukusudia kuingilia. Nilikosea
kuja bila taarifa.” Sabrina akaongea kwa sauti ya chini tu na ya taratibu. Jack
alikuwepo hapohapo chumbani nyuma karibu na dirisha, akawa ameinamia simu yake.
Ibra ndiye aliyemshitua Phina kuwa huo ndio wakati wakwenda kuzungumza na
Sabrina, Jack akiwepo. “Wala usijali kabisa. Nahisi na mimi nilipaniki ndio
maana niliongea hivyo.” Phina akajibu kwa upendo, Jack akiwasikiliza. “Naelewa,
lakini naahidi sitafanya hivyo tena Phina. Ikiwa ni lazima sana, nitakuwa
nikikupigia wewe simu. Kuliko kuwatokezea tu! Nakiri si sawa na sina sababu
yakuwafanyia hivyo.” Moyo wa Jack ukapasuka, nusura aangushe simu. Wote
wakamwangalia.
“Huhitaji
kuwasiliana na mimi kupitia Phina!” Jack hakuweza hata kuvumilia wala kuliwekea
kiporo. Hapo hapo akasawazisha. Sabrina na Phina wakabaki wakimwangalia, Phina
akiumia sana moyoni. “Ni kitu kilichotokea mara moja, na tutarekebisha.”
Akaongeza Jack akionekana amebadilika kabisa usoni. Akarudisha macho kwenye
simu yake. Sabrina hakujua azungumze nini tena. Phina alibaki ameduaa akijua
watu wa nje pia wamesikia. Akabaki kama aliyepigwa na bumbuwazi. Jack akawa
muungwana, yeye mwenyewe akajirudi. Akajisogeza kwa Phina na kumshika kiunoni.
“Phina amekuletea uji, ungependa kujaribu?” Akamuuliza Sabrina aliyekuwa
ameshageukia ukutani. “Nashukuru kujali Phina. Lakini naogopa nisije nikaanza
kutapika tena, Jack!” “Sasa tutajuaje kama dawa zimesaidia au la! Sitaki tena
turudi chuo, uanze tena kutapika. Heri ule, ukitapika hapa daktari atajua
chakufanya.” Sabrina akakaa.
“Ni
kweli. Bora ujaribu hata kidogo.” Phina akamuwekea kwenye kikombe, akamkabidhi.
“Nashukuru Phina. Asante sana.” Sabrina akashukuru tena akiwa amejawa wasiwasi
asije kukosana na first lady bila kujua Phina mwenyewe analazimika kumkubali
tu, akiangalia maisha yake ya badaye. Phina alifikishwa kwenye usemi wa
‘mtumikie kafiri...’ Japokuwa alikuwa akimpenda sana Jackson, lakini alishajua
hapatakuja kuwa na ndoa kati yao. Halafu alishajijengea heshima hapo chuoni
yakuitwa first Lady! Phina akaona kama Jackson hatamuacha, kumchukulia
Sabrina aliyemuonyesha anamtambua yeye kama mpenzi wa Jack, haitakuwa ngumu. Na
Ibra naye alishamwambia akae mkao wa kuajiriwa popote anapotaka baada ya
kumaliza chuo, akaona kumchukulia Sabrina kwa kipindi hicho ni garama ndogo
sana. Kwanza alijua Sabrina amebakisha muda mfupi sana amalize chuo, ataondoka na
kumuachia Jackson. Akakaza moyo, akaendelea kujituma.
Sabrina
akaendelea kukumbuka jinsi alivyokuwa akiunywa ule uji kwa makini akiomba Mungu
asitapike ili aruhusiwe aondoke hapo hospitalini na kuondoa hiyo fujo ya Jack
na viongozi wenzie. Akakumbuka wakati akimalizia, nesi naye akaingia. “Vipi?” Nesi
aliuliza. “Nakunywa uji, naona unakwenda vizuri. Ila usingizi ndio umenijaa!”
Sabrina akaongea kwa kulalamika. “Dawa zakuzuia kutapika ndio zinaleta
usingizi. Kunywa hizi dawa za malaria. Zikitulia baada ya nusu saa,
tunakuruhusu ukapumzike nyumbani.” “Nashukuru sana.” Sabrina akashukuru na
kupokea dawa. Akazinywa. Akamalizia uji, akaenda chooni. Akajisaidia na kurudi
kujilaza pale kitandani.
“Vipi?”
Jack akamuuliza wakati amejilaza. “Nipo sawa. Ni usingizi tu. Asante Jack.”
“Karibu. Ila kama una usingizi, wewe lala tu. Muda ukifika, nitakuamsha turudi
chuo.” “Daah! Hapo sawa.” Akavuta shuka, akajifunika vizuri. “Nikuongezee shuka
nyingine?” Jack akauliza kwa kujali. “Kama lipo karibu, lakini sio uende kutafuta
mbali.” Phina akaangalia pale chumbani, akakuta mashuka yamepangwa pembeni.
“Hili hapa. Tena yapo mawili! Nikufunike yote?” “Nitashukuru Phina. Asante.”
Sabrina akapotelea tena usingizini.
Akalala
mpaka alipoamshwa tena na Jack. Akakuta Jack alishalipia, wakaondoka na gari ya
Jack. Ibra alikaa mbele na Jack ambaye ndiye alikuwa dereva. Phina na Sabrina
walikaa nyuma. Alichofanya Sabrina nikujiegemeza dirishani, akajifunika na kulala tena. Kukawa
kimya. Alikuja kuamshwa tena na Phina. “Tumefika chuo.” Sabrina akaangalia nje, akakuta wapo chuoni.
“Jamani niwashukuruni wote. Asanteni sana. Acha mimi nikalale, nimalize huu
usingizi.” “Basi nitakuletea chakula baadaye. Unahamu ya kula nini?” “Naomba
nisikusumbue Phina. Huu uji uliobaki humu kwenye chupa, unatosha. Niruhusu tu
niende na chupa, nikimaliza uji, nitakuletea chupa yako chumbani kwako.”
“Lazima kula Brina. Hata kama husikii hamu ya kula, lazima ujilazimishe ili
usichoke.” Jack akaingilia. “Basi nikiamka, nitatafuta chakula. Naomba
niwaache. Jack, nashukuru sana.” “Karibu.” Sabrina akashuka, Ibra kimya.
Akaondoka.
Sabrina
akakumbuka kuoga na kurudi kitandani kama mlevi. Hakunywa hata huo uji.
Alilala, asijue ni saa ngapi. Chumba kilikuwa kimya kabisa. Kila aliposhituka,
na kupata ule utulivu, alirudi kulala. “Brina!” Baadaye akiwa usingizini, akakumbuka
kusikia sauti ya Jack. Kugeuka, nje kulishakuwa giza. Akamkuta Jack na Phina.
“Vipi?” “Nasikia baridi Jack! Nahisi homa inataka kupanda.” “Tokea mida ile
tulipotoka hospitalini, ulimeza tena dawa za kushusha homa?” Sabrina
akafikiria. “Sidhani!” “Unazo dawa zenyewe lakini?” Phina akauliza. “Ninazo.
Naomba niangalizie kwenye kabati, tafadhali.” Phina akaenda kabatini kwa
Sabrina. “Umepanga vizuri!” Phina akasifia. “Asante.” Sabrina akajibu na kurudi
kulala. “Usilale tena sasa! Meza dawa ule ndipo urudi kulala.” Jack akamuwahi.
“Sisikii njaa Jack! Acha nilale.” “Hapana Brina. Kula hata kidogo.” Sabrina akakumbuka
Jack kumkatalia kwa kujali. Akakumbuka baridi aliyokuwa akiipata siku ile! Alikaa
akitetemeka. Akajifunika vizuri. Phina akampa dawa na maji, akameza.
Kisha
Phina huyohuyo akampa chakula. Walikuwa wamemletea ndizi za mchuzi. Sabrina
akafurahia hicho chakula. Akala chote bila hata kubakisha. Jack na Phina
walikuwa wamekaa wakiangalia simu ya Jack pamoja. Sabrina akataka maji ya
kunywa. Akaona shida kuwasumbua. Akatoka pale kitandani alipokuwa akila. “Wapi
tena?” Jack akauliza. “Naenda kusafisha kinywa bafuni ili nikirudi nilale moja
kwa moja. Nawashukuru sana, kwa kila kitu.” “Sasa hivi hata ukirudi kulala
mpaka asubuhi, hamna tatizo.” Jack akaongeza. “Kweli.” Sabrina akatoka na
mswaki mkononi, akawaacha hapohapo. Alidhani wangeaga waondoke, lakini
wakaonekana kama wamefika. Aliporudi na kupanda kitandani ndipo Jack akaaga.
Kwa Jack na
Sabrina sasa.
Y |
ote hayo
Sabrina aliyakumbuka vile Jack alivyokuwa akimtanguliza yeye popote na kwa
yeyote. Wala safari hii kwa mama yake haikuwa mara yake ya kwanza! Ikawa kama
amefunguliwa macho na kuona kila kitu. Akamtizama tena Jack pale alipokuwa
amekaa na Jeiline. Macho yakagongana. Akacheka. “Ninahamu na wewe!” Sabrina
akanong’ona. “Nikuvulie shati unuse?” Sabrina alicheka mpaka machozi.
Akamwangalia tena Jack, akazidi kucheka. “Au awamu ya kunuswa imeshaisha jana?”
Jack akaendelea kuuliza. “Ujue Jack unahitaji kukua ili watoto wakikua wakute
baba yao alishakuwa!” “Mimi nimeuliza kwa upendo tu mama. Kosa langu lipi?
Maana enzi zetu wenyewe, sasa hivi ungekuwa hapa kifuani ukininusa mpaka
unalala!” “Watu wanakusikia Jack, bwana!” “Gafla unaogopa watu wakati ulikuwa
ukivaa mashati yangu mbele ya Pam tena bila hata wasiwasi!” Sabrina akakumbuka
nakuzidi kucheka.
Kisha
akatulia kama anayejaribu kuvuta kumbukumbu. “Jack wewe!” “Kumbe! Mwenzio
alikaribia kuchanganyikiwa! Lakini wewe ukawa huna habari!” Sabrina akazidi
kucheka. “Usiniambie nimekwisha thamani?” “Hata kidogo. Jana yenyewe nililala
vizuri sababu ulikuwa umelala pale pembeni ya kitanda changu. Nikawa napata
harufu yako sawia!” Jack akacheka sana. “Kwa hiyo bado soko lipo?” “Sana tu.
Wewe wangu.” Wakavuta masikio ya watu. Wakawa wakiwasikiliza wao wakizungumza
sauti ya chini huku wakicheka. Wamekaa viti mbalimbali na watoto wao.
Walifika
nyumbani kwao wakiwa wamejawa cheko. Jack akapitiliza chumbani. Baada ya muda
akatoka Sabrina akiwa anawaweka sawa watoto. “Sasa mzazi wangu? Nipike nini?” Sabrina
akacheka sana. “Unataka kunipikia Jack?” “Nakupikia mzazi wangu. Nimechukua
likizo maalumu kwa ajili yako tu Brina wangu. Wewe pumzika chumbani. Nishaandaa
chumba kwa ajili yako na watoto. Leo itabidi tulale nao wote mpaka kesho
tutakapoletewa vitanda vyao.” Sabrina akasimama na kwenda kumbusu Jack. Jack
akamkumbatia vizuri. “Nakushukuru kwa upendo Jack. Unanipenda sanaaa. Leo
nimekutafakari, mpaka nikaumia moyoni!” “Umeona ulivyojichelewesha kupendwa?” Sabrina
akacheka sana. “Bwana mtoto umeniringia wewe!” “Najuta Jack wewe, acha tu. Nimerudi
mpaka chuoni, nikaumia sana. Kweli nimejichelewesha.” “Tena sana.” Sabrina
akazidi kucheka.
“Bwana
Jack mwenzio nipo serious.” “Aliyekwambia mimi simaanishi ni nani? Nakuhurumia
sana tu.” “Sasa safari hii nipo kupendwa. Ushindwe mwenyewe.” Jack akacheka sana.
“Brina huyo!” “Kumbe!” “Basi wewe utapendwa mpaka ushangae.” “Nishaanza
kushangaa.” Sabrina akajibu. “Unashangaa wakati mambo ndio yanaanza!” “Kwa hiyo
hapa bado?” Sabrina akazidi kucheka. “Nakwambia tulia mtoto wa kike, upendwe.”
Sabrina alicheka mpaka akarudi kukaa. “Sabrina napendwa mimi! Umesikia Keiline?
Mama anapendwa.” “Na anaahadi yakupendwa mpaka ashangae.” Akaongeza Jack na kuelekea
jikoni, akamuacha Sabrina akicheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jack ameondoka jijini bila kumuaga mama yake kitu ambacho hakijawahi
kutokea kwa wapenzi hao. Amemuacha Mama Msindai akiumia, akiona Sabrina na
wanae wakizungu, wamempora
mapenzi ya kiziwanda wake. Na mama Msindai anasifa ya kutokukubali kushindwa.
Usikose Muendelezo kujua kitakachojiri.
Katikati ya ugomvi wa mama mkwe, msomi, mwenye uelewa wa
mambo, Je, Sabrina atafanikiwa kupendwa mpaka kushangaa?
0 Comments:
Post a Comment