Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 25. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 25.

“Mama Msindai unataka kuanzisha jambo wewe!”  Kwa mara ya kwanza wakamsikia Jacinta, dada mkubwa akizungumza. “Jambo gani? Si nasema ukweli?” “Jamani acheni mimi niondoke. Sitaki matatizo na Jack. Nilichukua majukumu kumsaidia Pendo kuandaa shuguli ya leo. Nimefanya kwa uaminifu kabisa. Nimekamilisha. Sitaki mniingize kwenye matatizo.” “Kama unajua haya ni matatizo wewe Jacinta, kwa nini umkimbie mtoto wakati huu anapohitaji tumsaidie?” “Naomba nikusaidie mama, pengine utasaidika. Kwanza kabisa, Jack si mtoto. Ni mtumzima sana, mwenye akili na utashi wake. Kingine, Jack alizungumza na sisi wote kabla ya kumuoa huyu binti. Aliongea kwa hekima na ukali kuwa huyu binti ndiye chaguo lake. Anamtaka Sabrina vile alivyo na hao watoto wake. Alilisema hilo wazi. Kama mkiwa wakweli, mtakiri Jack si mkurupukaji wala mjinga. Lasivyo angeshaoa zamani sana, nyinyi ni mashahidi. Sally anamtaka huyo Jack hata leo. Kumuoa huyu binti ni chaguo lake Jack.” “Sio chaguo, wamemchezea mwanangu.” Akabisha mama Msindai.

“Kama ingekuwa kuchezewa, hizi sifa zote Jack anazoimba juu ya mkewe zisingekuwepo jamani! Acheni kuanzisha mambo mnayojua yatavunja amani. Jack amekiri kwetu sisi wote juu ya huyu binti. Ameapa hakuna anayemjulia yeye kama huyu binti. Leo Jack yupo kwenye vyombo vya habari anakiri wazi ni sababu ya mkewe. Jack ameitwa bungeni, kuzungumza na wabunge, mwenyewe amekiri kwetu ni kwa sababu ya kile anachokifanya Sabrina huko Singida. Jack anamwambia Junior, yeye ndiye anayepata sifa lakini anayewajibika ni mkewe. Amekiri Jack zaidi ya mara moja na nyinyi ni mashahidi. Sasa najiuliza, kama huyu Jack amelogwa huku akitumikiwa na mke wake, na kuhakikisha Jack anafikia ndoto zake, tatizo ni nini jamani!?” Jacinta akaongea kwa kuumia na sauti ya chini asisikike.

“Kama wewe mama umeshindwa kuwapokea hawa watoto, ondoka kimya kimya, mwache Jack mwenyewe na mke wake.” “Hawa watoto wakizungu hawawezi kunitenganisha na mwanangu.” Sabrina akaumia sana. “Sasa nakuambia ukweli kabisa mama Msindai. Wewe ni mama yangu, kwa hali niliyomuona nayo Jack leo akitoka na hao watoto huko leba. Jinsi alivyowashika na kuwatambulisha hapa kwetu kuwa ni binti zake kwa furaha na sifa zote, ni lazima ufanye uchaguzi tena nasikitika huna muda. Lazima uchague kwa haraka. Ni ukubali kuwa ni watoto wa kizungu na ni wa Jack, ili uwepo kwenye maisha ya Jack au uwakatae hao watoto, Jack akuone au hata akuhisi tu,” “Atafanyaje?” Akauliza kibabe mama Msindai.

“Unakumbuka alichotuambia siku alipokwambia au alipokuja rasmi Dar kutuambia kuwa Sabrina ni mjamzito, lakini anataka kumuoa hivyohivyo. Unakumbuka hii hali hapa ilikupata siku ile, ukawa mkali sana kwake na kwa Junior? Unakumbuka maneno ya Jack?” Kimya. “Sasa wakati wewe na Jena mnazungumza mnachozungumza hapa, naomba msaidiane kukumbushana. Na kama mmesahau, mkumbuke sasa hivi tupo hapa kwa kutaka kwetu. Jack alikusudia kuachana na Msindai kabisa, awe na Sabrina. Kwa amani kabisa akisema asiwatie aibu kama wewe mama ulivyokuwa ukigomba. Akataka kuondoka arudi Singida kwa Sabrina, baba akamrudisha, wote tukasema tutakuwa naye.” Sabrina akashangaa. Hakujua kama Jack alipambana na upinzani mzito hivyo! Jack hakuwahi hata kuzungumzia hilo. Sabrina akaumia sana.

“Mimi nashauri tu jamani, muwe makini. Ngoja mimi niangalie watoto, nitoke hapa nikahangaike na ya kwangu. Sitaki kujihangaisha na ya Jack. Maana kwa muonekano tu, Jack anaonekana mwenye furaha sana kuliko nyinyi. Ingekuwa mimi ni mwanangu yupo na furaha hivi, kama ni kulogwa, ningefurahia.” “Si kwa kuwa huna mtoto ndio maana!” Akaongeza mama Msindai kwa jazba akimkashifu mwanae. Wakamsikia Jacinta amecheka tu. Akasimama.

Baada ya muda kidogo Pendo na Sabrina wakasikia  hatua za miguu zikisogea hapo. Wakajua ni Jacinta. Pendo mwenyewe alikuwa akitetemeka kwa kuingiwa na hofu kwa kile alichosikia. Sabrina akabaki kimya amefunga macho kitandani. Kisha wakasikia na wa nje wanaondoka. Mama Msindai na Jena hata hawakuingia ndani. Kimya. Ndipo akaingia dada mkubwa, kiongozi wa usalama wa Taifa. Ukimuona na harufu yake tu, akiwepo sehemu utajua ipo neema.

“Kina shangazi wamelala?” Akanong’ona Jacinta akisogelea upande wa vitanda vidogo vya watoto vilivyokuwa vimewekwa pembeni ya kitanda cha mama yao. “Naona hawa hawatamsumbua mama yao. Walalaji.” “Sasa kabla hawajaanza kiswahili kirefu, nipige nao picha ili wakianza tu, niwakumbushe walipotoka.” Pendo akacheka na kumshikisha wote wawili. “Sasa kwa pozi hili, nipige na nichukue video kidogo.” Pendo akacheka na kuchukua simu ya Jacinta mwenyewe. Akampiga picha kadhaa. Mara ambusu huyu, picha. Akambusu na mwingine, picha. Akachukuliwa sasa video. “Haya, nyinyi warembo wa Jack na Sabrina, mimi anti yenu Jacinta. Mnapokuja kuwa mawaziri, msinisahau mkajidai hamnijui. Nitawajia na fimbo huko bungeni.” Mpaka Sabrina akacheka. Wakamgeukia, Pendo na Jacinta na wao wakacheka. “Kwani wanakawia hawa! Utashangaa wanakwambia, ‘kama tulikuona sehemu vile! Au tumekufananisha?’ Hapo ndipo fimbo zitakapoanza.” Kidogo Sabrina na Pendo wakacheka.

“Asante mwaya Pendo. Acha niwaache walale, wasije wakaamka sasa hivi, mama yao akaanza ulezi wa shida leoleo.” Pendo akampokea mmoja. Wakawaweka kitandani. Jacinta akamsogelea pale kitandani. “Hongera na pole Sabrina.” “Asante, nashukuru kwa kila kitu wifi yangu.” “Wewe lala, asubuhi tunakujia na uji, mtori na kila chakula ili maziwa yatoke.” “Nashukuru sana.” Jacinta akatoka.

Mama ni Mama.

K

ama waliopishana na Jacinta, Sabina na mama yake nao wakaingia. Sabrina akaanza kulia. “Pole mama. Pole sana. Hata hatukuwa tunajua. Jack ametupigia simu muda si mrefu. Lakini nikamwambia Sabina, tusije mikono mitupu. Angalau tukoroge uji angalau unywe. Kazi ya kusukuma watoto wawili si mchezo!” Ndio na Pendo akili zikamjia kuwa huyo mzazi anahitajika kula. Mama ni mama. Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa akifikiria kula ya mzazi usiku huo, lakini mama yake kafika hapo na chupa ya uji na chai ya rangi alimfikiria binti yake. Sabrina akaendelea kulia. “Inauma mama! Inauma si kidogo. Mpaka kamasi zilikuwa zikinitoka bila kujijua, Jack ndio akawa anafuta!” Wote wakacheka. Mama yake akaenda kumshika kwa upendo. “Pole sana mama, pole na hongera. Ndio umekua mama sasa. Furaha ya watoto utakuja sahau uchungu wote! Utashangaa mwakani unarudia tena.” “Weee mama! Si mwakani. Labda baada ya miaka mitano au sita.” Sabrina akapinga. “Sawa.” Mama yake akafanya wakacheke tena vile alivyokubali kwa haraka.

“Nimefurahi mmekuja mama.” “Niambie, ulipata sana shida?” Akauliza mama yake akimshika tumbo. “Pale mwanzoni kabla sijaingia leba na nilipoanza na wa kwanza ndio maumivu yalikuwa makali sana. Lakini Keiline, kama niliyepewa! Daktari anaongea, akashangaa ametoka, wala sikusukuma sana.” “Huyu wa pili anakuwa anapita alikokwisha fungua njia mwenzie. Yaani nyonga zote zilishafunguka. Halafu unakuwa ushapata maumivu yote, kwa hiyo pale anapokuja mwenzie, hakuna jipya.” Mama Sabrina akamfafanulia mwanae. “Pole na hongera Sabrina. Umekuwa mama sasa.” “Asante dada.” Sabrina akaitika.

Mara William akaingia. “Tumefika kwenye gari zikaanza stori za mzee Msindai wakati tunamsubiri mama. Tukaanza kazi yakucheka tu mpaka mama akaja. Ndio wameondoka muda si mrefu.” “Oooh! Naona tumepishana.” Akaongea kwa kulalamika mama yake Sabrina, asijue yaliyosemwa hapo. Wakasalimiana na William. “Mimi niwapokeee ulezi jamani. Mkapumzike. Hapa mimi ndio nimefika.” “Kweli mama!?” Akashangaa Sabrina. “Kabisa. Ndio wajukuu zangu wa kwanza hao! Acha nishike.” Akawasogelea pale kitandani, wakawa wamefunikwa vizuri na kufunikwa mpaka vichwa. Wakabakizwa uso tu. Mama Sabina akawaangalia kwa furaha asiamini kama na yeye ni bibi. “Naona umenizalia wajukuu wa nguvu! Weupee!” Akaongea kwa kufurahia mama Sabrina huku akiwatizama kwa upendo asijue watoto wamebeba damu ya kiitaliano. Wakacheka tu kwa furaha.

“Natamani niwashike, lakini hivyo walivyolala, sitaki kuwasumbua.” “Naona si waamkaji hawa mama. Tumebeba na kubeba, lakini wapi! Sabrina naona amependelewa na Mungu huyu, amepata watoto watulivu!” Pendo akaongea. “Lakini wakati wakuzaliwa walilia kama kengele mpaka mimi na Jack tukawa tunasema hakuna kulala.” Sabrina  akaongeza taratibu. Wakacheka kidogo. “Lakini hata wewe Sabrina ulikuwa mtoto mkimya sana. Hukusumbua wakati mchanga.” “Sasa nani aliyesumbua mama na wewe?” “Mmmmh!” Wote wakacheka baada ya mama yao kuguna tu bila kujibu. “Kwa maana nyingine yupo aliyekuwa mlizi?” Sabina akaendelea kuuliza. “Mimi sijamtaja mtu.” Wakaendelea kucheka.

“Sasa mwali wangu! Nikuletee nini kesho?” Pendo akamsogelea Sabrina, Sabina na mama yake wakasogelea watoto. Sabrina akaanza kufikiria nini chakuletewa. Akakumbuka nguo za watoto wake. “Kesho tuwatoe kwenye hizo za hospitali.” Wakacheka. “Basi nitawaletea vitu vyao.” Pendo na William wakaaga, wakatoka.

Hapo hapo mama Sabrina akamuwekea uji. “Kunywa ndio ulale. Usilale na tumbo tupu. Kazi ya kusukuma sio mchezo! Na wakiamka hao watataka kunyonya. Kula ushibe.” “Afadhali mama yangu, hapa nilikuwa nasikia njaa!” “Umeona Sabina? Ulikuwa ukinikatisha tamaa bure. Ona uji umemfaa mzazi.” Wakaendelea kuzungumza wakiwa wamemzunguka mzazi. “Sasa mama kama wewe unalala, bora mimi nirudi nyumbani mapema, kesho niwahi kurudi nije na vitu vyako wewe na chakula cha mzazi.” Hilo likawa jambo jema. Kwa asili Sabina alijua kumjali mama yake. Hakuwa akitaka mama yake aonekane vibaya. Hata kwenye hiyo baby shower alimpendezesha mama yake. Alimnunulia nguo nzuri na akampeleka saluni. Ukweli alipendeza na yeye akafanana na wamjini. Sabina akaondoka, akawaacha hapo.

Kwa Junior.

P

endo na mume wake walipotoka tu, Pendo akaanza kumsimulia Willy kila kitu. Yote aliyoyasikia mama Msindai akizungumza juu ya Sabrina na watoto wake. William akashangaa na kuumia sana. Hapo hapo akampigia simu Junior. “Samahani kaka!” “Hamna shida. Kwema?” Junior akapokea akisikika akiwa kitandani tayari. “Nina ombi ambalo naona lisisubiri.” William akaendelea. “Karibu.” Akaitika Junior, mtoto mkubwa wa Msindai. William akamueleza yote aliyosimuliwa na mkewe. Usingizi ukampaa Junior kwa mshituko. “Unauhakika Sabrina mwenyewe amesikia?” Akauliza Junior akisikika akitamani jibu la ‘hapana’. “Labda nikupe Pendo mwenyewe.” William akamkabidhi simu Pendo.

“Haikuwa nzuri kaka. Mwenyewe niliishiwa nguvu.” “Subiri kwanza Pendo. Unauhakika Sabrina alisikia kila kitu?” “Kabisa. Kwa kuwa tulikuwa naye. Binafsi nashauri uzungumze na mama, pengine kwa sasa awe makini na kila anachozungumza. Swala la ujauzito wa Sabrina kabla ya ndoa, halikuwa kificho kaka. Aina ya watoto aliozaa, nina uhakika na yeye amejua leo. Hili jambo la baraka tusiliharibu. Mimi nalilia watoto, hata nikipewa wekundu nitapokea tu.” Pendo akaanza kulia na yeye. “Ni hilo tu kaka. Mama asilazimishwe kufanya jambo jingine la Sabrina. Hata leo ukumbini haikuwa vizuri sana, alitaka kuharibu haswa, nafikiri Joy atakusimulia. Ilibidi Jacinta awe mkali sana kwake, ndipo akatulia. Nafikiri apewe muda mpaka awe tayari na Sabrina. Ni hilo tu.” Akarudisha simu kwa William. “Ni hayo tu kaka.” “Nashukuru kunitaarifu, ninakwenda kuzungumza naye sasa hivi.”  Junior akakata simu.

Kwa Sabrina.

H

uku kwa Sabrina akajua alishaachwa. Muda ulizidi kwenda bila yakumuona Jack kurudi wakati alimwambia atarudi baada ya muda mfupi. Yale aliyoyasikia kutoka kwa mama yake, akajua wamekutana huko nyumbani, amemuingizia kichwani, mpaka Jack akajiona hastahili kuwa pale. Sabrina alikula vizuri, akashiba, lakini usingizi ukagoma kuja. Akajifikiria ndio anarudi kwao na watoto wasio na baba! “Mungu wangu nirehemu!” Akajikuta akiongea nafsini kwake baada ya kufikiria kurudi tena kwao, tena safari hii na watoto wawili! Akabaki amefunga macho ili kumuaminisha mama yake kama amelala ili na yeye alale, lakini alishakosa amani. Manesi walikuwa wakipita kumwangalia yeye na watoto, kila aliyeingia Sabrina alidhani ni Jack, lakini ikawa sivyo. Masaa yakazidi kuyoyoma bila Jack.

Akakumbuka historia yake na wanaume. Hakuna mwanaume aliyekwisha kuwa naye, aliyewahi kumfanikisha kwenye yake, akarudi kwake. Kumbukumbu zikamrudisha mpaka kwa Emma, akaja Tino aliyemuacha kikatili zaidi kuliko hata Emma! “Heri Emma aliondoka na mali zake kuliko Tino aliondoka na roho za wanangu!” Akaendelea kuwaza Sabrina. Ndio Jack sasa. “Jack ameshakuwa mashuhuri. Mambo yake yanamuendea vizuri sasa hivi. Na yeye hanihitaji tena. Hana sababu ya kurudi tena kwangu.” Sabrina akawaza akilia moyoni kwa hofu. “Naomba usiniache Mungu wangu. Nitakwenda wapi na hawa watoto wawili?” Sabrina akaanza kumkumbusha Mungu kuwa alishamkabidhi hao watoto tokea ameachwa Moshi peke yake. “Naomba usiwaache wanangu, Mungu wangu. Kumbuka maombi niliyokuomba.” Sabrina akaendelea kumkumbusha Mungu moyoni mwake kana kwamba Mungu analo tatizo la kukumbuka, mwishoe uchovu wa shuguli nzima ya baby shawer  ya siku hiyo kuanzia maandalizi aliyoanza na Pendo alfajiri siku hiyo mpaka usiku huo amezaa hao mapacha vikamfanya asinzie katikati ya maombi.

Kwa wazazi.

J

unior anafika mlangoni kwa wazazi, akasikia Jack akigomba sana huko ndani. Baba yake akamfungulia mlango. “Huna haja kuwa karibu na mimi na mke wangu, mama! Sijalazimisha hata mmoja wenu hapa, na ninaomba msiniharibie amani ya nyumbani kwangu. Kama nyinyi mnashindwa kuungana na mimi katika hili, kaeni pembeni sitalazimisha mtu.” Junior aliingia na kumsikia Jack akifoka, baba yake, Jena na Jacinta nao walikuwepo. Akashangaa wote wapo yeye hajui kama kuna kikao. “Ni nini kinaendelea ambacho mimi sijahusishwa?” “Mimi simo Junior. Nimefika nyumbani kwangu nikagundua nina zawadi nyingi na zamuhimu alizopewa Sabrina kwenye baby shower yake. Nikaoana nisilale nazo, pengine atahitaji akiwa hospitalini au niseme wakati huu. Maana vingi ni vya watoto wa umri wa 0 mpaka miezi mitatu. Ndio nakuja hapa, nakutana na yaleyale niliyomkataza mama na Jena kule hospitalini.” “Tafadhalini msiniingize.” Jena akaruka.

“Unafanya nini hapa nyumbani muda huu na wewe huishi hapa, kama si upo hapa na mama ili kuzungumza na Jack?”  Jacinta akamuuliza huku amemtolea macho. “Na mimi nimekuja kushusha mzigo.” “Sawa dokta Msindai! Lakini mimi niliwaonya, na nipo hapa kuwashuhudia mkivuna nilichowatahadharisha pale hospitalini.” Akaongeza Jacinta. “Na kwa taarifa yenu tu, Sabrina amewasikia mambo yenu yote mliyokuwa mkizungumza pale nje hospitalini.” Junior akaongeza na kumshitua sana Jack. “Juu ya nini!?” Jack akauliza kwa kuhamaki.

“Ndio maana nipo hapa usiku huu. Naomba ukae Jack.” “Nataka kuondoka kaka. Nimemuacha mke wangu na watoto kwa muda mrefu. Nilikuwa naoga na kumbembea yeye vitu, wakati natoka ndio mama akanipigia kuniomba nimsubiri hapa. Akitaka kunifungua macho.” Junior akatingisha kichwa kwa kusikitika sana. “Najua sasa hivi hamuwezi kunielewa kwa kuwa fahamu zenu na nyinyi zimefungwa.” Akaongea mama Msindai.

“Mimi nikuombe kwa heshima kubwa sana mama.” “Najua unachotaka kusema.” Akajibu mama yake kwa jeuri. “Basi naomba niongee na wengine wanisikie. Hata Jacinta naomba nivumilie sitachukua muda mrefu.” Jacinta aliyekuwa amesimama atoke, akakaa. Jack akakaa. “Samahani baba, naongoza kikao nyumbani kwako.” “Wewe endelea tu.” Baba yake akamruhusu, Junior akashukuru.

“Naelewa kwa sehemu sitofahamu ya mama na wengineo. Inamuhitaji Jack mwenyewe kupita anakopita na kuwa na amani na uwezo huo wa utulivu na kuchukuliana. Hatuwezi kuepuka huo mshituko wa kuzaliwa watoto wakizungu katikati yetu.” “Asante mwanangu Junior.” Akashangilia mama Msindai. Jack akawa ametulia tu.  “Maana...” “Lakini! Lakini! Tafadhali mama, naomba nimalize.” “Hiyo ‘lakini’ itaanza kutukorofisha.” Mama Misindai akamtisha Junior.

“Mwache amalize. Mpe nafasi tumsikilize kama wewe tulivyokusikiliza wasiwasi wako wote.” Akaingilia mzee msindai. “Asante baba.” Junior akashukuru na kuendelea. “Mwanzoni kabisa, Jack alikuja hapa nyumbani kwa heshima ya hii familia. Akatutaarifu juu yakumuoa Sabrina ambaye tayari alikuwa mjamzito. Nafikiri wote mnakumbuka nini kilitokea.” “Asante Junior. Na hilo niliwakumbusha mama na Jena, muda mfupi sana kule hospitalini. Nikawakumbusha vile Jack alivyokuwa akitaka kuondoka hapa akaendelee na taratibu zake na mpenzi wake, kuepusha hii aibu mnayolalamikia leo.” “Sawa sawa Jacinta.” Junior akakubali.

“Sijui siku ile mama ulikubali kwa umbali gani na...” “Sio kwa watoto wa kizungu jamani!” Akaingilia mama Msindai. “Sawa sawa mama, hilo limesikika na kueleweka waziwazi. Ugumu uliokuwa nao umeongezeka zaidi kwa aina ya watoto waliozaliwa leo. Lakini naomba kuweka angalizo na msisitizo hapo. Msiumize hisia za watu. Hawa watoto waliozaliwa leo, ni kazi ngumu aliyofanya Sabrina. Kuanzia siku ya kwanza anabeba mpaka hivi leo.” Mpaka Jack akalia. “Asante kaka.” Akashukuru Jack kwa uchungu sana. “Tafadhali tusilisahau hilo. Huyu mama ametoka kuzaa watoto wawili ndani ya nusu saa kama nilivyosikia ripoti aliyokuwa akipewa baba.” “Ndani ya dakika 18.” Akarekebisha mzee Msindai.

“Ewaa! Tafadhali ndugu zangu, nawasihi na Mungu atusaidie, msisahau hilo. Huyu Sabrina ana vidonda vibishi kabisa. Hata watoto wake hawajanyonya, kweli mnamfuata sehemu kama ile, hajawaita wala hajalazimisha mtu kwenda pale, mnakwenda kumwita mshirikina!” “Huwezi kuwa umekwenda kuzungumza hayo maneno kwa mke wangu mama!” Jack akashituka sana. “Kwani mimi nilijua kama anasikiliza? Na mimi ni mama, nina haki ya kuzungumza juu ya mwanangu.” Akajibu kibabe mama Msindai.

“Mimi hilo sipingi mama. Lakini si pale. Usimfuate, mwache.” “Nakwenda alipo mtoto wangu.” “Mbona ulikuwa pale wakati Jack hakuwepo, mama? Hujampokea Sabrina moyoni, si kwa hawa watoto aliozaa leo. Hata kabla hukuwa umempokea. Mwache. Mtoto ambaye unamtaka uwe naye karibu, si mtoto huyu mama. Tafadhali fungua macho na uelewe Jack si mtoto.” “Na hilo nilimwambia mama.” Akaongeza Jacinta. “Jamani Jack si mtoto. Baba na mama, Jack ni mtu mzima sana na anamaamuzi yake. Yanaweza yasilete maana kwetu, lakini haina maana amelogwa jamani!” “Unajuaje?” Akauliza mama Msindai.

“Kama hivyo alivyo amelogwa, basi inabidi wanaume wote walogwe na wake zao, mama! Jack anafuraha. Wote tumemuona jinsi anavyokuwa na mkewe. Jack anampenda mke wake. Mke wake anahangaika mchana na usiku akimuhangaikia Jack mpaka Jack anashangaa! Sabrina na tumbo la mapacha, anahangaika kumsaidia mumewe kwenye mambo ya chama ili Jack atulie kazini.” Jack akainama na kulia kwa uchungu sana. “Leo Jack anavuma kwenye siasa, kwa muda mfupi sana Sabrina alipoingia kwenye maisha yake. Sasa kama anamloga na kumuhangaikia hivyo, ubaya upo wapi jamani?” Junior akauliza kwa kuumia sana.

“Eti jamani? Bora lipi? Kulogwa na kutumikiwa au kutologwa na mwanamke anakupinga katika kila kitu? Wapo wanawake wanaojiita wacha Mungu, nyumba zao hazina amani. Jack amejawa furaha, ametulia kwake. Kazini amefanikiwa, kwenye mambo ya chama pia anashamiri. Leo Jack anakuwa gumzo kwenye vyombo vya habari sababu ya kazi kubwa wanayofanya na Sabrina. Nyinyi kama wazazi mnataka nini kitokee kwa huyu kijana wenu?” Junior akawauliza akiwatizama wazazi wao kwa zamu.

“Jamani, mnakumbuka sura aliyotoka nayo Jack kule leba akiwa ameshika watoto wake?” “Asante Junior.” Akaongeza Jacinta. “Mnataka kuona nini kwa Jack jamani! Mnawezaje kumpokonya furaha ya ajabu kiasi kile na kumfanya mnyonge, aliye, huyu baba, mume ambaye anategemewa sana sasa hivi na Sabrina ambaye amekuwa akisimama naye!? Msijisahau jamani, Jackson Msindai anasifika zaidi sasahivi sababu ya mkewe. Jack mwenyewe amekiri mpaka bungeni akimshukuru mkewe!” Junior anakumbusha, asijue hicho ndicho kilimuuma mama Msindai na kumchukia Sabrina zaidi. Kiziwanda wake anamshukuru Sabrina hadharani na si yeye! Hapo ikajengeka chuki wala si upendo kwa Sabrina.

“Sasa hivi ambapo alitakiwa awe pale na watoto wake na mkewe, yupo hapa akijibu shutuma kama hajalogwa! Kweli?” Junior akauliza akitizama kila mmoja wao. “Mimi binafsi sidhani kama ni sawa ndugu zangu. Jack anapo kwake na ana maisha yake. Mwacheni aishi maisha aliyojaliwa na Mungu. Sisi ni wakristo. Mama wewe unaomba sana, muombee kama kuna linaloendelea, Mungu amponye. Lakini kama sio hivyo, waacheni. Msifike alipo yeye na familia yake. Waacheni kabisa. Kwa kusema hivyo, naomba niwaombe Jack aondoke sasa hivi arudi hospitalini kwa familia yake. Yule binti atakuwa na wasiwasi sasa hivi. Naomba Jack aende.” Junior akahitimisha.

“Naona kaka amezungumza mengi na yanatosha. Sina nyongeza. Watoto wale wakizungu ni wangu na watafanyika sehemu ya maisha yangu. Ili msimuumize mke wangu, naomba mimi niwaage rasmi. Kama mtaweza kunitumia mizigo yangu na zawadi zetu Singida, nitashukuru. Nikiona kimya baada ya siku 10 kurudi Singida, nitaanza kununua mimi mwenyewe vile ninavyohitaji, zaidi vya watoto wangu. Naomba niwahi kama kaka alivyoshauri.” Akasimama akarudi chumbani kwake.

Baada ya muda wakamuona anatoka na mizigo yake na mkewe. “Naona vitu nilivyonavyo na mimi kwenye gari ni muhimu Jack. Vichukue usiache. Ni vya watoto wa umri huu.” “Nashukuru.” Jacinta naye akasimama. “Usiku mwema jamani. Natoka kumkabidhi Jack vitu vyake, ndio na mimi nitakuwa nakwenda kupumzika moja kwa moja. Usiku mwema.” Bila kusubiri Jacinta akatoka. Junior naye akasimama na kuondoka bila kuaga.

“Nikusaidie nini?” Wakamsikia Junior akiuliza nje. “Kwa sasa nahisi sijui nimechanganyikiwa tayari! Sikumbuki tena.” Wakamsikia Jack akiongea kwa kulalamika. “Nashauri uende ukatulie, ukikumbuka andika, kesho ukirudi hapa utajua nini chakubeba na kuacha.” “Naona nifanye hivyo.” Jack akaafiki. Jacinta na Junior wakasaidia kumuhamishia vitu kwenye gari, Jack akaondoka.

Hospitalini.

A

kiwa usingizini Sabrina akahisi mtu amembusu mdomo. Akashituka sana na kufungua macho. “Jack!” Akaongea kwa kunong’ona akiwa haamini kama kweli ni Jack au yupo usingizini. “Pole, nimechelewa kurudi.” Jack akambusu tena.“Nilidhani hutarudi tena!” Machozi yakaanza kumtoka Sabrina. “Niende wapi bila wewe Brina? Na wanangu nao?” Sabrina akajifunika nakuzidi kulia taratibu. “Utakapokwenda na mimi ndio hapo nitakuwepo mama. Wala hutanikwepa kirahisi hivyo.” Jack akaendelea kuzungumza naye taratibu akimfariji. Mama yake Sabrina alikuwa amelala kwenye kiti cha pembeni karibu na wajukuu, akawa anasikiliza, kidogo maswali yakaibuka ndani. “Kwa nini awe na wasiwasi mumewe asirudi tena?” Akajiuliza mama Sabina, lakini akaona anyamaze.

Akambembeleza mkewe kwa mabusu ya hapa na pale mpaka Sabrina akatulia. “Warembo wa dady hawajaanza kulia?” Jack akawasogelea. “Naona walalaji hao! Mama amenipa nijaribu kunyonyesha kabla njaa hazijawaanza wakalia kwa pamoja nikiwa sina maziwa, na pia alitaka waanze kuvuta ili maziwa yaanze kutoka, lakini wapi. Tumebembeleza wee, naona kila mmoja ameridhika hapo.” Jack akamnyanyua Jeiline. Sabrina akamuona anambusu. Akamuweka vizuri. “Dad amerudi, ameleta zawadi nyingiii, kwa ajili yako na mdogo wako.” Akaongea Jack kwa sauti ya chini. Akambusu tena na tena na kusogea naye pale kwa Sabrina. “Hapa mama ulinzi lazima uwe mkali!” Sabrina akacheka. “Na ukali utaanza kuongezeka. Ukaribu na vijana wasiooa mwisho. Eti Jeiline? Dady atafuga mbwa wengiii ili alinde warembo wake?” Akaendelea kuzungumza naye taratibu, akakaa pembeni ya kitanda.

“Vipi lakini wewe? Maumivu yameisha kabisa?” “Wamenipa dawa ya maumivu, sasa hivi nipo sawa labda nikikaa ndio naumia sababu ya mshono. Lakini nipo sawa. Na kwa kuwa upo hapa, nahisi nitalala.” “Pole. Nilikuwa nakusanya vitu vyetu na vya watoto. Jacinta naye kanijazia gari kwa ajili ya vitu vyao hawa, vya umri huu. Nikazidi kuchelewa. Nataka ukiruhusiwa tu, turudi nyumbani kwetu.” “Nilifikiri nitarudi naye huyo nyumbani na wajukuu angalau hata wakomae kidogo.” Jack akasimama.

“Pole nimekuamsha mama.” “Hapana. Kulala ngumu sababu ya furaha ya wajukuu baba. Kuona kizazi cha pili ni baraka mwanangu. Hapa nipo kama siamini! Natamani kukaa nao angalau mwezi.” Jack akacheka. “Nitachanganyikiwa mama yangu. Mwezi! Utanifanya na mimi nihamie hukohuko Chalinze, mwishoe nitafukuzwa na kazi.” Sabrina akajisikia vizuri. “Hawa watatu sitawaacha popote mama yangu. Nilipo ndipo na wao watakapokuwepo. Lakini tutakuja kukutembelea wakikua kidogo.” “Sasa huko mnaye msichana wa kazi?” Akauliza mama Sabina. Akaona wanaangaliana. Wakacheka.

“Tunae dada mtumzima kidogo. Huwa anakuja kumsaidia huyu kazi na alituahidi kutuletea msichana kabla Brina hajajifungua. Sasa tunahisi ni kama haweki juhudi katika hilo ili awepo yeye mwenyewe kazini.” “Lakini sio mbaya Jack.” Sabrina akaongeza. “Kweli sio mbaya, lakini kwa hivi umeshajifungua, tutahitaji msichana hata wa usiku.” “Sawa sawa baba. Maana unahitaji kupumzika Sabrina. Kujifungua sio kitu kidogo. Unaweza usione madhara kwa nje, lakini unahitaji kupona ndani. Lazima upumzike kwa muda.” Wakanyamaza.

“Kwa sasa lazima huyo apate msaada.” Mama Sabina akaweka msisitizo. “Nina siku za uzazi na mimi, napata kutoka kazini. Kwa hiyo nitakuwa naye nyumbani. Hatakuwa peke yake. Na zikiisha kama sijapata msaada mwingine wakumsaidia watoto, naweza nikachukua likizo ya hata mwezi. Sitamuacha peke yake na watoto. Usiwe na wasiwasi mama. Tutakuwa sawa tu.” Jack akajaribu kumtuliza, asijue nia na maombi ya huyo mama ni kukaribishwa huko Singida akalee wajukuu. Wakatulia, Jack akamrudisha Jeiline na kumchukua Keiline. “Hey little girl!” Wakamsikia Jack akizungumza na huyo mtoto, akambusu na kurudi kukaa naye hapo kwa Sabrina.

“Nijaribu kumnyonyesha tena? Angalau avute kidogo maziwa yaanze kutoka jamani!” “Basi usikae, lala hivyo hivyo nikuwekee pembeni.” “We Jack! Mwanzio bado mwanafunzi, sijawa mzoefu wa kunyonyesha.” Jack na mama yake wakacheka. “Kweli. Watoto wenyewe ndio nafundishwa kushika vizuri na mama, leo ninyonyeshe nimelala! Si watapaliwa?” “Si umesema maumivu makali ukikaa?” “Acha nijitahidi bwana. Ila asante kunifikiria.” “Basi nyanyuka nikupangie mito huko mgongoni.” Jack akawa ameshika mtoto mkono upande wa kushoto, huku anamsaidia mkewe upande wa kulia. Mpaka Sabrina akakaa vizuri. Akampa mtoto.

“Mkune miguu labda ataamka.” Mama Sabina akatoa wazo. Wakacheka. “Sasa wewe Jack kuna miguu, mimi nimshikilie.” Mama Sabina akaanza kucheka na kusimama. “Mtoto huyo mmoja utafikiri unanyonyesha jeshi bwana! Nilikwambia unapomnyonyesha umkumbatie kwa mkono mmoja. Tumbo lake ligeuke kwenye lako kabisa mpaka apate joto lako, ndipo anyonye.” “Sasa hapo ndio wanapolala sababu ya joto.” Wakacheka. Wawili hao wakaanza kazi ya kunyonyesha. Akavuta titi la mama yake kidogo, akalala. Kila Jack alivyokuwa akimkuna mguu, anavuta. Akiacha na yeye anaacha. “Mimi naona tuwaache. Wakisikia njaa wataamka wenyewe.” “Naona hilo wazo zuri. Sasa na wewe ulale. Ili wakiamka uwe umepunguza uchovu.” Jack akashauri. Wazo likawa jema.

Jack akamrudisha mtoto kwenye kitanda, akarudi kumfunika Sabrina vizuri. Akambusu wee, kisha akamwacha alale. Na yeye akavuta kiti pembeni, akalala. Wazazi hao walilala kama hawana watoto! Mama Sabina aliyekuwa karibu na watoto ndiye akabaki akiangalia wajukuu. Jeiline akaamka karibu panapambazuka. Akambadilisha diaper ndipo akampeleka kwa mama yake. Sabrina akashituka. “Amelia?” “Kidogo tu.” “Nilikuwa nimechoka mama! Nimelala sina habari.” Sabrina akawa anakaa taratibu asimuamshe Jack ambaye amelala kama yupo kitandani. “Ndio mlezi huyo!” Sabrina akamsengenya kwa sauti ya chini, yeye na mama yake wakacheka. “Atakuwa amechoka.” “Sana. Jana alikuwa na siku ndefu sana. Mwache alale, akiamka hapo yeye ndio analea ili na wewe ukapumzike kidogo.”

Sabrina akamuweka kwenye ziwa. Wakashangaa anaanza kunyonya kwa juhudi. Wakaangaliana. “Amejisaidia huyo ndio maana naona tumbo limefunguka, amepatwa na njaa. Ngoja nimwangalie mwenzie.” “Hata sikuwa na habari kama mnabadilishana. Asante mama.” Sabrina akashukuru. Yule mama akapatwa maswali zaidi. Maana wakati wakumbadilisha Keiline akamtoa soksi na kofia ikavuka pia. Akaweza kumuona huyo mtoto kwa wazi kabisa, ana damu ya watu weupe. Tena kali haswa. Sura ilikuwa ya Sabrina. Hilo akaliona, lakini walikuwa kama watoto waliozaliwa na baba na mama wakizungu kabisa. Yule mama akawa hajaelewa. “Naona hivi anavyovuta anafanya maziwa kusisimkwa. Na hili jingine linakuwa kama linataka kutoa!” “Safi sana. Naona na wewe utakuwa na maziwa mengi kama mimi. Mimi yalikuwa yakimwagika haswa kipindi nikinyonyesha. Basi madume yangu yalikuwa hayalii njaa.” Sabrina akacheka. “Nasikia raha hivi anavyonyonya! Siamini kama ni wangu.” “Watoto watamu!” Wakacheka taratibu wakati mama yake akimwangalia Jeiline. “Na yeye amejisaidia?” Akauliza Sabrina. “Naona wamefanana nje na ndani. Wanafanya kila kitu pamoja.” Wakacheka taratibu, wakati akiendelea kumbadilisha na Sabrina akinyonyesha.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Ndio mlezi unalala hivi!” Jack akaamshwa na Willy asubuhi hiyo ya saa moja. Wote wakacheka. Jack ndio akasimama. “Haiwezekani kama pamepambazuka!” Sabrina akabaki akimcheka. “Lakini watoto hawajalia bwana! Eti Brina?” “Nimenyonyesha mwenzio mara mbili! Hapa maziwa yameanza kutoka kidogo.” “Acha utani! Mbona hukuniamsha?” “Najua ulichoka, nikamwambia mama tukuache upumzike.” “Daaah! Nilikuwa nimechoka haswa. Lakini mngeniamsha tu.” Wakaendelea kucheka, Jack akaelekea bafuni na kimkoba chake kidogo.

“Vipi?” Pendo akauliza. “Nimeanza ulezi mwenzio.” Wakacheka. “Lakini mama ndio ananiamsha ninyonyeshe. Naona wazazi sisi tunahitaji kuzoea. Tukilala hapa, hata watoto waamke hakuna anayeamka kati yetu. Nipo kama Jack tu.” Wakacheka tena. “Lakini walikuja mkiwa mmechoka. Jana ilikuwa siku busy sana kwenu nyinyi wote. Na hekaheka za leba, mlichoka.” Pendo akamfariji.

“Acha nikapige mswaki ndio nije kula. Mdomo mchungu, mama alikuwa akinipa vyakula usiku.” “Uzazi, lazima ule.” “Ni kweli mama. Anahitajika kula sana.” Akakubali Pendo. “Au usubiri mwenzio atoke, nije kukusaidia kukusafisha kabisa kabla wageni hawajaanza kuwa wengi?” “Naona hilo wazo zuri mama. Aoge kabisa, wataanza kuingia wageni sasa hivi.” Pendo akakubaliana na wazo la mama Sabrina. Sabrina hakuwahi kumuona mama yake akimjali kwa namna ile. Kwa mara ya kwanza akapata mapenzi ya mama haswa. Alijituma huyo mama, Sabrina akabaki akishukuru tu.

Wakati Sabrina yupo bafuni na mama yake, Pendo naye akawa na kazi yakuvalisha watoto. Walikuwa wadogo, lakini wakapendeza. Aliwavalisha nguo za rangi nyeupe tupu. Akawavalisha na kofia zenye uwa la rozi la pinki kubwa juu. Sabrina alitoka bafuni na kuanza kucheka. “Naona warembo wameshaanza kupendeza.” “Wakichangamka tu, tunawatoboa masikio.” Pendo akaongeza. “Hapana. Sio sasa hivi.” Jack akajibu kwa haraka sana, wote wakamgeukia. “Mnajua yale madude yanaota kwenye masikio sababu yakutoboa?” Willy akaanza kucheka. “Mzee unayaogopa?” “Kabisa. Mnataka kuwaharibu wanangu sura? Hamna haraka. Kwanza wenyewe wanapendeza bila hereni. Hilo zoezi la masikio ni la baadaye sana.” “Basi kazi hawa watoto watakuwa nayo kama ndio hivyo. Dad ndio ana mashariti hivyo!” Pendo akafanya wacheke, Sabrina akacheka tu nakurudi kukaa bila ya kuongeza hapo.

 “Mimi naomba nile kwanza ndio ninyonyeshe.” Mama yake akamuwekea mtori. “Pendo, mama umepika vizuri, na unanukia vizuri!” “Asante mama. Nataka atunyonyeshee watoto wakue haraka.” Wakacheka, stori zikaendelea. Akaingia Junior na familia yake wote wamevaa vizuri. “Mnakwenda kanisani nini?” Jack akauliza. “Yeap! Mzazi unaendeleaje?” “Nina kazi ya kula tu shemeji yangu.” “Unanyonyesha lakini?” Joy akauliza. “Wanaringa hao! Lakini nanyonyesha. Naona bibi yao anawapigania kweli. Hata nikiwa usingizini, ananiamsha wajukuu zake wapate lishe.” Wakacheka. “Kwa ulalaji tuliomkuta nao baba yao, sasa kama na mama mtu naye analala hivyo hivyo! Watoto watashinda njaa.” Wakacheka. “Tulikuwa tumechoka bwana. Siku ya kwanza, leo tutakuwa makini.” Jack akaongeza.

“Claire umependeza msimamizi wangu!”  Sabrina akamuongelesha. “Huyo kwa watoto! Hapo haoni mtu humu ndani ni hao watoto tu.” Mama yake akaongeza. Claire akacheka. “Asante.” “Salimia bwana, vipi wewe?” Baba yake akamwambia. Akasalimia kila mmoja. “Ulisema nitapakata watoto dad.” Claire akamgeukia baba yake. “Sasa usinyonye vidole wakati umepakata watoto, utawaangusha bure.” Wote wakacheka. “Dad unamsikia Clei anaanza uchokozi wake?” “Wewe kaa hapo kwenye kiti, nikuombee kupakata watoto. Na uwe makini ili Clei aone wewe ni dada mzuri.” Akafurahi Claire, mama yake akamuweka sawa kwenye kiti. “Nataka kuwabeba wote.” Watu wote wakacheka. “Sasa hapo ndipo utawaangusha bwana! Anza kwanza mmoja, Jeiline. Mami wake akiona umemshika vizuri, atakuruhusu umshike mdogo wake Keiline.” “Dad, mwambie na asinyonye kidole akasahau mtoto.” “Utalia Clei wewe! Unataka kumliza mwenzio ashindwe kubeba watoto!” Mama yake akamtisha, Clei akacheka na kumsogelea Jack taratibu akijihami. Wote wakacheka. 

“Anapenda kunichokoza kila saa!” “Sasa na wewe ukianza kulia tu, anko anakunyima watoto.” Baba yake akamuwahi. Akajifuta machozi. “Clei mchokozi dad!” “Wewe usimsikilize. Nilikwambia ukiwa unalia tu ndio atazidi kukuchokoza. Wewe usimsikilize. Haya futa machozi mama yangu, nikupe mtoto.” Wakazidi kucheka. “Mlezi huyu atakuwa analia na watoto wanalia!” Pendo akanong’ona. Wakacheka. Akapewa mtoto. Baba yake akachuchumaa mbele yake. “Ona ulivyoshika mtoto vizuri!” Baba yake akamsifia. Claire akacheka. “Mimi ni dada zuri dad!” Clei akacheka kama kumchokoza. “Sasa unanicheka nini?” “Nimekwambia usimsikilize. Kweli wewe dada mzuri.” Wakampiga picha hapo, akafurahi.

Jacinta akaingia. “Naona warembo wamepata mlezi.” “Dad amesema mimi dada mzuri, anti.” “Hata mimi nimekukubali. Acha nikupige picha anti wangu!” Akafurahi Claire. “Halafu umependeza Anti! Si sisi tunafanana?” “Sana. Tumefanana sana mpaka nywele! Halafu na wewe umependeza sana Claire.” Akafurahia. Zikazidi stori humo ndani. Sabina naye akaongezeka. Kila aliyeingia hapo aliingia na maua, na baloons. Kasoro Sabina aliingia na chupa za uji. Chumba kikapendeza.

“Mimi sijaja na chakula, maana Pendo aliniambia anakupikia vitu vingi, nikajua na mimi nikileta asubuhi vitaharibika.” “Nashukuru kwa kujali. Nimekula mtori mzuri sana. Si umependa Jack?” “Makubwa! Na wewe Jack umekula cha mzazi!?” Jacinta akashangaa. “Sasa nile wapi wakati nalea hapa?” Wakacheka. “Tutoke kidogo Jack.” Jack akakubali kwa haraka, akijua kaka yake anataka akazungumze naye. “Sasa Jack?” Pendo akamwita wakati wanataka kutoka. “Vipi?” “Si utaniachia bibi harusi wangu nimsaidie kulea watoto hata mwezi tu? Wakichangamka tu hawa warembo, nakutumia.” Jack akacheka. “Siachi mrembo wangu hata mmoja, Pendo. Nikiondoka hapa jijini, naondoa majeshi yangu yote. Mke na wanangu wote. Tutarudi kusalimia, lakini hao, siachii mtu. Nilipo ndipo watakapokuwepo.”  Wakamtania kidogo, Jack akatoka, Willy na yeye akafuata nyuma. Sabrina akajisikia vizuri, roho ikatulia kabisa.

“Mama na wewe kula. Halafu da Sabina naona umrudishe mama nyumbani akapumzike kidogo, arudi baadaye. Hajalala usiku kucha!” “Hawezi kukubali kuondoka huyu. Muulize mwenyewe.” Wakacheka. “Nakuhurumia!” “Jamani mama yangu. Sasa si utakuwa umechoka sana? Kalale kidogo.” “Wala usijali. Nioge tu, nibadili nguo na kula wakati hawa wamelala, nitakuwa sawa tu. Mkitoka hapa, ndio tutoke wote.” “Nashukuru mama yangu. Asante.” Sabina akaingia na mama yake bafuni. Wakamuacha Sabrina na Jacinta, Joy na Pendo wakizungumza.

Junior kwa mdogo wake.

“Mpango ukoje?”  Kaka yake akamuuliza baadaya ya kutoka hapo ndani na kuhakikisha wapo mbali kidogo. “Wakiruhusiwa tu hawa, tunaondoka kabisa hapa jijini angalau  tukapumzike sasa. Shuguli zote zimeisha, sasa nikulea.” “Ukiruhusiwa leo na mkatoka jioni, ndio nauliza mtakwenda wapi?” “Oooh! Nilifikiria hotelini, ili kumfanya apumzike kabisa, halafu kesho yake ndio turudi Singida.” “Kwa nini hotelini!?” Akauliza Willy na Junior kwa pamoja. “Nyinyi mlifikiria niende wapi? Maana nyumbani mama amekuwa muwazi kabisa, hawezi kumpokea Sabrina na wanangu!” “Hata nyumbani kwangu!” Willy akaongeza kwa mshangao. “Au kwangu!” Junior naye akaongeza.

Jack akakaa sawa. “Fikirieni vizuri tu. Wala msifanye haraka. Mnafikiri mtakuwa salama kwa mama Msindai? Yaani yeye amfukuze Sabrina na wanangu, leo aje ajue nyinyi ndio mnawahifadhi?” Wakatulia. “Watu wake wote wa karibu wanajua mimi na mke wangu tuko nyumbani kwake. Leo ijulikane hatuko kwake, tena nimeondoka bila maelewano naye, halafu nihamie kwa mwingine! Mnamjua mama Msindai au mmemsahau? Mtanunua ugomvi wote na hatakaa akawasamehe. Huu ni ugomvi wangu na mama, na ndio maana mmemuona baba amenyamaza kabisa na kutotaka kuingilia. Mnafikiri ni kwa nini?” Kimya. “Baba anamjua mama. Sisi tunaweza kuondoka kwenda Singida maisha yakaendelea, huku nyuma vita ikahamia kwake au kwa mwingine.” “Bado sidhani kama ni sawa kupeleka watoto wadogo hivyo hotelini Jack.” Junior akaongea kama anayefikiria.

“Bora ingekuwa ni kwa kina Sabrina, lakini si hotelini!” “Kule ni mbali kaka. Siwezi kusafiri mpaka Chalinze na watoto, kwa safari ya usiku mmoja tu! Halafu kesho yake tena turudi huku kwa safari ya kurudi Singida! Hapana, nitamtesa mke wangu. Na nyumbani kwa Sabina ni padogo sana. Sioni sababu yakujibana. Nitakuwa sawa jamani. Naomba muwe na amani.” “Daah!” Junior akasikitika.

“Hata hivyo sitaki tena maneno maneno kwa Sabrina. Nahisi anasimangwa bila kosa! Brina hanakosa kaka. Hajawahi kunilaghai, na wala si eti yupo na mimi kwa sababu amekwama maisha. Mimi ndiye namuhitaji Brina kuliko hata anavyonihitaji mimi! Alipogundua ni mjamzito, alikataa kuja Singida kabisa kaka. Nafikiri nilikwambia. Akijua nipo kwenye mahusiano yangu na maisha yangu. Hakutaka hata kuja ili asinichanganye. Sijamtoa Brina barabarani jamani. Nimemkuta na mipango yake na watoto wake, ametulia vizuri tu kwenye Vila. Mimi ndiye niliyemfuata Brina. Mimi ndiye niliyemuomba tuishi wote Singida. Na tulipofika Singida pia aliponikuta na Pam, akaona haitakuwa vizuri aishi pale nyumbani kwangu, na Pam akiwa yupo kwenye maisha yangu. Brina akaondoka. Sikuweza kulala kaka. Nilihisi kuchanganyikiwa, na nilikuwa na Pam. Ile hali yakujua Brina yupo, na hayupo kwenye maisha yangu, haijawahi kunifanya nikawa na amani. Tokea siku ya kwanza namuona Brina.”

“Watoto aliozaa Brina, nahesabu ni wangu kaka. Wawe wakijani, wawe bluu, ni wangu.” “Naomba nikuulize Jack. Samahani lakini.” Willy akaomba kwa tahadhari. “Baba yao yuko wapi?” “Nimemwapia Sabrina, kwa kuwa ameniomba ramsi, nisiwahi kumzungumzia huyo mtu. Ameniambia mpaka kifo chake, hata hao watoto waje waulize yeye akiwa hayupo, wakiwa wameambiwa na watu vinginevyo, lakini kutoka kwa mdomo wangu ameniomba nisiwahi kumzungumzia huyo mtu kwao, japo mimi ndio mtu pekee ameniambia ukweli wote. Kwa hiyo Brina mwenyewe ameniomba kwa kuniapisha kuwa tusiwahi kumzungumzia huyo mtu kwa mtu na wala hawa watoto, hawatamjua baba mwingine ila mimi.” Wote wakashangaa.

“Wao!” “Hakika kaka. Amesema atakufa akiwatambulisha watoto wake kama ni wangu. Sasa kwa bahati hiyo kaka, kwa mwanamke kama Sabrina, nawezaje kukataa au kubadilika? Nitapata wapi mwanamke kama Brina? Binafsi napenda watoto sana, kaka ananijua. Leo niambiwe nimepewa  watoto wawili! Tena wakike! Jamani msinitanie! Mwenzenu nahesabu nimeokota zaidi ya lulu.” Wakacheka. “Kweli tena. Mungu anipe nini? Nishakuwa na wanawake jamani. Lakini sijawahi kulala usingizi wa amani, kama nilivyokuwa na uhakika kuwa Brina ni wangu. Ananijali haswa. Tunalala tukicheka. Nawezaje kupoteza hiyo furaha?” Kimya.

“Sasa ndio maana, mimi mwenyewe, nitamlinda Brina. Nitatunza amani ya nyumbani kwangu kwa njia yeyote ile. Maneno ya kumuudhi, hayo sitaruhusu, hapo mtanisamehe. Nitamchukua mke wangu na watoto, nitawapeleka sehemu nitakayojua watakuwa salama na amani, kisha tunarudi Singida. Najua watu watasema sana tu, lakini sitajali. Hata wangekuwa weusi, bado wangesema tu. Niliwapokea hawa watoto hata nikiwa sijui kama wapo wawili. Nikaja kujua ni wawili, nikapata amani japo Brina alikaribia kuchanganyikiwa.” “Kweli?” “Kweli kaka. Nimetembea na Brina katika huu ujauzito nikimtia moyo mpaka sasa, sijisikii kubadilika, kwa kuwa mwenyewe pia nawataka hao watoto.” Kila mmoja akavuta pumzi.

“Basi wakati mnaelekea uwanja wa ndege, unitaarifu ili nimwambie Awali aje achukue gari huko uwanjani.” “Hapo utakuwa umenisaidia kaka. Ila naomba muamini nawashukuru sana. Nilihitaji watu kama nyinyi kusimama na mimi katika kipindi hiki. Ibra ambaye ni rafiki yangu wa karibu, na yeye pia ameshindwa kabisa kunielewa. Amekataa hata kuja kwenye harusi yetu. Lakini nimeamua kumuacha kama mama, tutaungana baadaye. Mimi ndiye najua nahitaji nini.” Wakaendelea kuzungumza.

Mama Sabrina kwa Sabina.

M

ama yake akaoga hapohapo ndani kwenye chumba alicholazwa Sabrina na kubadili nguo. Akataka kuteta na Sabina hapo chooni, lakini akajua watasikiwa. Akamnong’oneza kuwa watoke, waage wanakwenda kwenye gari ili wakaweze kuzungumza kwa uhuru. Na kweli wakafanya hivyo. Wakaenda mpaka kwenye gari, wakaangaliana na kuanza kucheka. “Haya mama!” “Kwanza watoto ni wakizungu. Si weupe, hata. Wazungu kabisa.” “Mimi nilihisi jana. Lakini nikasema nisiende mbali.” “Sasa sikiliza. Wewe si uliondoka mumewe akiwa hajarudi?” “Ndiyo.” Sabina akaitika akitaka kujua yaliyojiri usiku.

“Sasa alikuja kurudi usiku sana kama kwenye saa 7 hivi, nikamsikia Sabrina akimwambia alifikiri hatarudi tena.” “Mama! Kwa hiyo alimdanganya mwenzie mimba ni yake?” “Mimi nikahisi hivyo. Lakini mumewe akamuomba msamaha wa kuchelewa, halafu akamuuliza, ‘nisirudi niende wapi bila wewe na wanangu?’.” “Mama!” Sabina akashangaa sana kama ambaye hasadiki. “Kweli tena. Sasa hapo ndipo nilipopatwa na utata.” “Kwa hiyo inamaana mumewe anajua watoto si wake tokea mwanzo basi!” “Ewaa!” Mama yake akaafiki na kuongeza. “Inamaana alimuoa akiwa anajua anayo mimba si yake.” “Mmmh!” Sabina akaguna.

“Kwa hiyo kwa ndugu wa mume kuwepo hapa mpaka leo, wakiona watoto wa kizungu, pia walijua Jack anamuoa mwanamke mjamzito!” “Ndio maana yake mama. Sabrina amebahatika!” Wakaendelea kuteta wasijue moto unao waka ndani ya familia hiyo. “Lakini Sabina, inamaana huyu Sabrina alikuwa na mahusiano na mzungu gani!? Maana hawa watoto sio mchanganyiko. Nakwambia utafikiri wamezaliwa na baba na mama wakizungu kabisa!” Hapo ndipo mama yake akamfunga kumbukumbu kabisa huyo Sabina hata asimuhisi Tino. “Itakuwa ni baada ya kuondoka huko kwa rafiki yangu, alikokwenda kuanza maisha huko ndipo akapata mzungu. Na kwa kamwili kake hako kembamba, rangi ile, lazima alivutia mzungu mmoja huko alikokwenda labda wakalala mara moja, mzungu akaondoka, akamuacha na mimba.” “Au alifanya mahusiano kabisa. Bwana Sabrina amebadilika! Sie Sabrina tunayemfahamu sisi! Atakua aliishi na huyo mzungu kabisa akachukua vijitabia vya kizungu.” “Ulimuona hata alipokuja kwenye mahari kabla hajaolewa?” Wakaendelea kuteta mpaka wakaona Junior na familia yake wanapita kwa mbali kidogo, wakajua wageni wanaanza kuondoka.

“Nataka kwenda nao, nikalee vijukuu Sabina, mwanangu. Niombee kisomi. Mimi nimeshindwa.” Sabina akacheka sana. “Mama! Unataka kwenda mpaka Singida!?” “Sasa nisipokwenda kwa hili, nitakwenda kwa lipi mwanangu? Sina ninalolifanya huko Chalinze. Sasa hebu niambie, watu wajue nimekwenda mpaka Singida kulea!” Sabina akacheka huku akifikiria. “Na baba?” “Ataelewa kabisa. Namwambia nakwenda kumsaidia Sabrina watoto. Lazima atakubali. Na hivi anataka tujirudi kwa Sabrina, na naona amependa sana huyo Jack. Anasema anamthamini sana Sabrina. Kwa hiyo lazima atakubali tu.” “Sawa. Ngoja waondoke wageni wao na mimi nijaribu.” Wakacheka nakuanza kurudi ndani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ø    Kwa wa Nyumbani Sabrina Bado thamani yake iko juu sana, ikaongezwa na msimamo wa Jack. Japo watoto ni wakizungu, lakini bado amesimama na Sabrina. Anamtaka mkewe na watoto wake. Mama yake Sabrina anaonyesha kuhitaji mahusiano naye. Itakuaje kwao?

Ø Huku kwa Msindai Vita ya mama Msindai na Sabrina ndio imeanza rasmi. Sabrina amemchukua kiziwanda chake! Na sifa ya huyu mama hakubali kushindwa japo safari hii Jack ameonekana kumshinda. Hawezi kuishi bila Jack, na chuki inaongezwa zaidi na watoto wa kizungu wa Sabrina. Amekiri hao watoto hawatamtenga na mwanae. Umbali gani atakwenda kumrudisha mwanae upande wake? Usikose kufuatilia. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment