Jack
na Sabrina walirudi mjini Singida wakiwa wamejawa furaha. Kama mume na mke haswa. Wakipanga mipango inayoeleweka kama wanandoa. Wakiweka juhudi kwa kile
anachokiamini Jack. Sabrina ndiye akawa kama mwenyekiti wa vijana akiongoza
mambo, wakati Jack akichukua sifa zote. Alifanya bila kuchoka, wakati huo pia akisimamia
ujenzi wa nyumba wanayoishi pia, Jack kazini bila kukosa wala kuchelewa. Kwenye
hiyo nyumba waliamua kujenga vyumba vya nje na kurekebisha ndani kuifanya
nyumba ya kisasa haswa kama alivyoona Sabrina kwenye majumba ya watu alimopita
kutumika na kuishi. Akaiga muundo wa ndani ya nyumba ya Tino kwa asilimia 85,
na kwa Pendo alikoishi siku 8 kabla ya harusi yake. Akataka kufanane ndani na
hayo majumba mazuri yaliyomvutia. Pesa walizopowe baada ya harusi yao ikawa
msaada mkubwa sana kwa Sabrina, Jack mwenyewe alikuwa akishangaa hayo
mabadiliko.
Ndani ya miezi miwili, Sabrina akiwa na
ujauzito wa miezi saba, nyumba ya Jack aliyoikuta ya kawaida kabisa, ikabadilika,
ungesahau hiyo nyumba. Alibadilisha hatua kwa hatua. Kuanzia sakafu, Jack
aliagiza vigae vizuri sana vya sakafu ya nyumba nzima. Walifanya kazi chumba
hadi chumba, hatua kwa hatua mpaka wakamaliza sakafu nzima. Rangi ya kuta, safi
na tulivu iliyobadilisha kabisa muonekano. Akabadili thamani za ndani na kuweka
za kisasa kutoka Dar ambako Pendo ndiye aliyekuwa akimsaidia kutafuta na Mama
Msindai kumtumia huko Singida. Jikoni nalo akalitendea haki, ungeona shida
kuacha pachafu. Vyumbani akabadili kabisa na kutoa uhitaji wa makabati kwa
kujengewa makabati ya ukutani kwa kila chumba.
Wakabadili
madirisha na ndipo hiyo nyumba ikafungwa AC. Ungependa kuingia hapo ndani.
Sabrina akapafanya kukawa nadhifu mno, Jack akabaki akijisifia nyumbani kwake.
Nyumba hiyohiyo yakawaida, Sabrina akaipa uhai, pakavutia utafikiri mjengo wa
thamani ulipo sehemu ya tofauti kabisa na ilipo! Nyumba ya nje ilipokamilika, pakatandazwa
vitofali vizuri kwenye ua mzima ila kukaachwa sehemu chache sana za maua ambayo
Sabrina mwenyewe alikuwa akimwagilia. Wakati mama Msindai anamsafirishia
makochi, meza ya chakula, vitanda na thamani nyingine, aliweka na vyungu vya
maua vizuri sana. Sabrina ana mimba ya miezi nane na nusu, nyumba yake ikawa
imekamilika kuanzia ndani mpaka nje. Huku mambo ya chama yakizidi kupamba moto.
Jackson
Msindai akawa akionekana magazetini na kwenye vyombo vya kijamii amefanya hiki,
amefufua kile. Ilimradi kuleta maendeleo kwenye jamii. Na kwa kuwa familia hiyo
alijulikana na wengi, haikumsumbua Jack kufikia watu wakubwa na kumsaidia
kutekeleza kwa haraka mipango yake na Sabrina. “Wanasema
katika kila mafanikio, yupo mwanamke nyuma yake. Kwa upande wangu, mke wangu
ndiye anayesimama na mimi, mchana na usiku ambao hakuna anayetuona. Kuhakikisha
ananijenga, ananitia moyo pale ninapotaka kukata tamaa na kuniombea.”
Usemi wa Jack kila asimamapo au ahojiwapo. Na kwa kuwa alimuamini sana Sabrina,
alikuwa akimsikiliza kwenye kila mtu. Na kweli, Sabrina alipewa uwezo wa ajabu.
Nguvu ya kufufua kila kilichokufa, mpaka Jack alikuwa akimshangaa. Hakuwa na
muonekano wa ajabu sana, lakini alikiri mkewe kichwa chake kipo vizuri na Mungu
huwa na yeye kwenye kila jambo analoweka mkono wake. Heshima Mungu aliyompa
Sabrina huko Singida, na vile Jack alivyokuwa akimbemba mkewe, kila mtu
alimuheshimu pale mjini. Usingemkuta bar, wala kwenye umbea akisutana. Nyumbani
na kama asipokuwa nyumbani, basi kwenye mambo ya muhimu.
Alipokaribia
miezi 9, Sabrina alishalemewa. Tumbo lilikuwa kubwa kuliko mwili wake. Miguu ilikuwa
mizito kunyanyua, akawa anajicheka. Akapunguza safari na shuguli. Uzuri bado Imani
alikuwa naye karibu na wakielewana vizuri. Kwa hiyo ikawa rahisi kwa Sabrina
kumtuma. Na yeye Imani alipenda vile anavyojulikana kuwa yeye ndiye mtu wa karibu
wa Sabrina. Akabaki yeye kuwa miguu ya Sabrina. Akimtuma huku na kule
akamilishe na kufuatilia hili na lile. Na alichopenda zaidi Imani ni vile ambavyo
kila mradi ulipokuwa ukifunguliwa, yeye na Jack ndio walionekana pichani kwenye
magazeti wala si Sabrina ambaye ndiye mtoa mawazo na mipango. Hakujali
kutoonekana popote pale ilimradi afanikishe. Tena siku za uzinduzi ndio alitaka
Imani apendeze zaidi akimwambia lazima kupania magazetini. Basi Imani alikuwa
akilifurahia sana. Sabrina akawa kioo chake kwenye kila shuguli akijua
anamtakia mema, wala hamuonei wivu.
Baby Shower
Ya Sabrina.
A |
lipobakisha
majuma mawili kufika tarahe yakujifungua, Pendo na kina Msindai wakawa wamemwandalia
Sabrina baby shower. Ilibidi amsubirie Jack atoke kazini ndipo wasafiri
kwenda Dar kwa ajili ya sherehe hiyo. Safari hii walifikia nyumbani kwa
Msindai. Sabrina alikuwa akimtizama huyo mama anavyomshika Jack kila wakati
kama mtoto mdogo. Mara ampanguse mdomo. Akumbuke hajanywa maji ya kunywa ya
kutosha. Mara amtengeneze kola. Ilimradi tu mikono yake iwe kwa huyo mtoto. Na
Jack naye ni kama aliyezoea, kama hakuona kitu cha ajabu kinachoendelea. Na
wengine hivyo hivyo waliona ni kitu cha kawaida kabisa, ila si kwa Sabrina!
Ilikuwa mara yake ya kwanza Sabrina kuona wawili hao wakiishi nyumba moja.
Yaani kulala na kuamka nyumba moja. Alijua wanazungumza sana tu. Ni kama kabla
hajalala na kila anapotoka nyumbani kwenda kazini, lazima azungumze na mama
yake, lakini hakujua ukaribu ule wa mama Msindai kwa Jack ni kama kwa mtoto wa
miaka mitatu!
Kwa Sabina.
Ilikuwa
ijumaa. Sabina aliwaalika nyumbani kwake kwa chakula cha usiku. Haikuwa nyumba
kubwa lakini Sabina aliwaalika hivyohivyo. Wazazi wao kina Sabina, Pendo na
mume wake walikuwepo na mzee Msindai pamoja na mkewe pia. Sabina na mama yake walijitahidi
kuandaa chakula kizuri na mazingira yanayoendana na kina Msindai. Wakapata
wakati mzuri wa pamoja, Pendo akaeleza mipango ya kesho yake. Mama Msindai
akamsifia Pendo kwa maandalizi mazuri. “Nilijua tu utamfaa Sabrina. Nakushukuru
sana Pendo mwanangu. Mungu akubariki.” “Karibu na amina mama.” Pendo akaitika
kwa unyenyekevu kama mwenyewe alivyo mtulivu. “Na ni kweli ananifaa Pendo
jamani! Haachi kunipigia simu kunijualia hali yangu na watoto! Akikutana na magauni
mazuri anayojua yatanifaa, lazima aninunulie na kunitumia! Asante mama Matron
wangu. Mungu akupe haja ya moyo wako.” Pendo akacheka. “Amina. Na wewe sio
mgumu Sabrina. Unaridhishwa na vitu vidogo na nirahisi sana kukufanyia jambo.
Huna mambo mengi.” Wakacheka na kuendelea kuzungumza.
“Na
mimi naweza kusaidia kama kunahitajika msaada popote kwenye hiyo shuguli ya
kesho.” Sabina akaingiza hoja yake katikati ya mipango. Pendo akafikiria
kidogo. “Itakuwa jambo zuri. Acha nizungumze na dada Jacinta tuone. Maana yeye
ndio mama mipango. Ndiye aliyenisaidia kuweka mipango. Nani awe wapi na yupi
afanye nini. Ameweka marafiki zake kwenye kila idara. Mipango mingi tunafanya
kwa simu, ila tunakutana mara moja kwa week angalau kujua kila mmoja alipofikia
na kuwekana sawa. Mpaka jana tunazungumza, sijasikia aliyelemewa. Ila kesho
asubuhi tutakutana ukumbini tena. Nitauliza nani atahitaji msaada, kisha
nitakujulisha kama kuna uhitaji.” “Basi naomba na mimi niwepo hiyo asubuhi.”
Sabina akaonekana kukusudia kuwepo.
Alikuwa
na agenda mbili. Moja kama ndugu, lakini alitaka pia kujichanganya na hao
wanawake. Pendo mwenyewe alionekana ni msomi na kazi ya maana. Nyumbani kwake
mwenyewe Sabina alipokwenda alibabaika. Jacinta Msindai na marafiki zake ndio
wapo kwenye kamati! Sabina akajua atapata bahati ya kukutana na wanawake
wanguvu. Akakusudia awepo. Pendo akaona ni jambo zuri, akampa muda na eneo
watakalokutania hapo ukumbini. Wakaondoka.
Mama Kundi.
H |
uku kwa mke
wa Max, mama Kundi, zikawa kama habari za Sabrina zinamtafuta yeye tu. Akiwa ofisini
akasikia fununu za hiyo baby shower ya mke wa kijana wa Misndai. Akatamani sana
na yeye kupata mualiko ili akashuhudie. Lakini tatizo ni baby shower. Akajua
wazi waandaaji ni wanawake. Hakuwa karibu na mke wa bosi wake. Waziri Msindai,
yaani Joy, ili kumuomba mualiko. Alishakutana na Joy mara kadhaa kwenye party
au shuguli za kiofisi, lakini hawakuwahi kuwa karibu. Dada za Msindai mwenyewe,
yaani huyo bosi wake, Junior Msindai, nao ni watu wazito kwenye jamii. Yeye
kama mfanyakazi wa kawaida tu wa wizarani asingeweza kuwa nao karibu. Lakini akamwambia
mumewe lazima aende akaoshe macho kwenye baby shower ya kina dada wasomi na
mashuhuri hapo mjini.
Mama
Kundi akafikiria jinsi ya kupata mualiko akaona hana jinsi, akamvizia siku hiyo
waziri Msindai yupo ofisini kwake na hapakuwa na hekaheka nyingi. Maana yeye
alifanya kazi kwenye wizara hiyohiyo, lakini kwenye ofisi ya waziri mwenyewe.
Wakati anatoka akajidai na yeye anapita. “Hongereni sana muheshimiwa. Nimesikia
bibi harusi wetu anafanyiwa baby shower!” “Yeah!” Junior akajibu. “Hivi leo
ndio wanaingia hapa Dar, tayari kwa shuguli nzima kesho.” “Safi sana. Unajua
kwa namna fulani nafahamiana na Sabrina?” “Oooh yeah!? Sikujua.” Ikabidi Junior
asimame kidogo zaidi kumuonyesha kumsikiliza. “Sema tulipotezana. Alishafika
mpaka nyumbani kwangu. Tukapata chakula cha pamoja. Ile siku ya harusi
tulihudhuria nikiwa sijui kama yeye ndio bibi harusi!” “Acha kunishitua bwana!
Tumeoa mke wa mtu nini?” “No no noooo.” Akajichekesha kidogo mama
Makundi. “Hapana kabisa. Hakuwa ameolewa na wala sikusikia kama aliolewa.”
Wakacheka kidogo. “Ningetamani na mimi kuhudhuria na hiyo baby shower, ili
nilete hata zawadi ya diaper. Nilimpenda sana Sabrina.” “Ingekuwa vizuri. Ila
sihusiki na baby shower.” Wakacheka tena.
“Nafahamu
hayo ni mambo ya wakina mama.” “Namsikia tu Joy akiwa kwenye mipango. Ni kama
msimamizi wake ndio ana shugulika zaidi, wakisaidiana na kina Jacinta. Subiri
kwanza.” Mama Makundi akamuona ametoa simu akapiga. Akamsikia anasikiliza sauti
ya kike upande wa pili. “Na mimi nipo katikati ya kitu
Jacinta. Sikiliza.” Junior akamjibu hivyo Jacinta. “Unanafasi ya mtu mmoja au wawili kwenye baby shower,
kesho?” Akamsikiliza kidogo, akacheka. “Sio mtu
wa mtaani bwana! Ni mtu na heshima zake. Tunafanya naye kazi hapa.” Akamuona
anasikiliza kwa muda. Kisha akajibu. “Naelewa. Upo
sahihi kabisa. Ila huyu niliyekuwa nikimuombea mwaliko ni mfanyakazi wa hapa,
na anafahamiana na Sabrina. Ningejua mapema, ningekuomba mapema. Lakini naamini
ataelewa kabisa.” Akamuona anasikiliza. “It’s
okay. Usilazimishie. Ibaki kama mlivyopanga. Hamna shida kabisa. Ataelewa
tu.” Akasikiliza kidogo. “Sawa sawa. Kazi
njema.” Mama Makundi akawasikia wakiagana lakini akapoa kabisa akajua
ndio amekosa.
“Samahani
sana. Nafikiri tumechelewa. Wameandaa kutokana na idadi ya watu waliowaalika na
waliokubali kuhudhuria. Hata ulinzi wa hapo umewekwa kutokana na wageni. Na
chakula pamoja na vinywaji ni hivyohivyo. Vinaandaliwa kutokana na
walichochagua watakao hudhuria. Anasema mialiko ilikwenda na Menu. Hapatakuwa
na ziada ya chochote hata kiti cha ziada hakitakuwepo. Wanakwenda kwa idadi au
majina. Na kingine jana usiku wameshafikisha kwenye vyombo vya usalama idadi
kamili na majina yamehifandiwa ya watakao hudhuria hapo kwa sababu za kiusalama.
Kuongeza watu leo wakati kesho ndio siku yenyewe...” “Naelewa kabisa
mheshimiwa. Inamaana itabidi zoezi zima lianze upya.” Mama Makundi akaona
amrahisishie tu. Junior alikuwa mstaarabu sana. “Ewaa!” Junior akaafiki. Wakacheka
tena kidogo, Junior akaondoka, mama Makundi akabaki akifikiria hiyo aina ya baby
shower. “Mmmmh!” Akaguna kila akimfikiria Sabrina aliyekutanishwa
naye na huyu! Bado ilikuwa haiingii akilini. Alikwenda nyumbani kwake akiwa
binti wa kawaida sana. Akawa bado yupo kwenye mshangao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Lakini
Max, nahisi kuna kitu hakijakaa sawa. Na Tino hataki kukizungumza.” Max alitoka
kazini na kumkuta mkewe bado kwenye kumfikiria Tino na Sabrina. “Unazungumzia
habari za Sabrina?” “Ndiyo!” “Umepata mwaliko?” Ikabidi mama Kundi acheke.
“Hiyo baby shower sio ya kila mwenye zawadi, baba!” Akaanza mama Makundi.
“Ni kwa mwaliko kamili. Nilimsikia mhehimiwa akizungumza na dada yake, naona
huko sie wa kina sisi hapatufai.” “Eeh!” Max akataka kusikia zaidi. “Eti wageni
walitumiwa mwaliko na menu. Ukisema unakwenda, unachagua aina ya chakula
unachotaka kula siku hiyo na kinywaji chako. Kwa hiyo mpaka leo, wanajua nani
anakwenda, atakula nini na kinywaji gani na washaandaliwa kiti kwa majina.” “Eee
bwana weee!” “Subiri Max. Majina na idadi kamili ya watakao kuwepo kwenye hiyo shuguli,
vipo kwenye vyombo vya usalama kwaajili ya ulinzi wa siku hiyo!” Max akabaki
ametoa macho.
“Ndio
ujue aina ya wageni hapo!” “Hiyo shuguli itakuwa sio mchezo! Wakina mama wazito
watupu watakuwepo huko.” Max akaongeza akifikiria. “Lakini nilimsikia akimwambia
kaka yake, angewahi hata siku tano zilizopita, pengine na mimi wangenichukua!”
Wakabaki kimya kwa muda. “Mimi nahisi kuna jambo limejificha Max. Jaribu
kumdodosa Tino.” “Si nilikwambia anakwepa hilo! Kila nikitaka tumzungumzie
Sabrina, hataki kabisa na anabadili mazungumzo. Mara ya mwisho nilipompigia
simu kuhusu Sabrina, si unakumbuka nilikwambia aliniaga kwa haraka akasema kule
ni usiku anakwenda kulala?” “Nakumbuka. Sasa sijui kulikuwa na nini
kinachoendelea walipotoka hapa kwetu! Maana waliondoka wakionekana wanamipango
mizito! Leo Sabrina anaolewa na ujauzito ambao lazima utakuwa mkubwa tu!” Mama
Kundi akamshitua sana mumewe ambaye bado alikuwa akimficha ukweli.
“Unataka
kuniambia nini!?” Max akauliza na wasiwasi akitamani isiwe vinginevyo. “Sijui
Max! Lakini mimi nilimuhisi ni kama siku ile ya harusi aliolewa akiwa na
ujauzito mkubwa tu. Ile haikuwa mimba changa. Ila ile nguo ya harusi jinsi
ilivyotengenezwa na kwa kuwa mwenyewe ni mwembamba, ndio maana hakuonyesha sana.
Na ujue wazi baby shower nyingi wanafanya wakiwa wanakaribia kujifungua.
Ndio ujue anao ujauzito mkubwa tu, na wa muda mrefu. Sasa wewe piga mahesabu.
Waliondoka hapa lini, harusi ilikuwa lini, na leo Sabrina anajifungua! Wewe
unaona inaleta maana?” Mama Kundi akamuuliza mumewe asijue anaibua jingine
zito. Max akabaki kama amepigwa ganzi akifikiria, nani amemchezea visivyo? Tino
alimuhakikishia Sabrina aliingia chumba chakutolewa mimba, na amemuacha Moshi hospitalini
akiwa amepoteza damu nyingi baada ya kutoa mimba. Na daktari naye alilipwa pesa
ya kutosha tu baada ya kuhakikishia wote kuwa alifanya kazi yake kikamilifu. Akahisi
mkewe anachanganywa na kukosa mualiko tu. Akapoa na kushindwa kuendeleza hayo
mazungumzo asije jikuta anaropoka ya sirini. Akabadili kabisa hayo mazungumzo.
Baby shower.
W |
akati
wanawake wanakutana kwa baby shower, wanaume ndugu na rafiki wa karibu
wa Msindai walifanya nyama choma nyumbani kwa Junior wakimtania Jack na
kumuandaa kuwa baba. Vilijaa vicheko na vitisho kwa Jack kuwa ajiandae kutolala
usiku wala mchana kwa vilio vya watoto. Wakamfundisha kufunga diaper huku wao
wenyewe wakikosoana kwa hili na lile, kwamba hata wao wenyewe hawajaweza au
wameshasahau kufunga diaper. Walikuwa na mdoli mkubwa tu wakifundishana.
Walichekana na kukosoana sana. Mpaka Mzee Msindai mwenyewe aliambiwa akumbushie
enzi. Aingie kwenye hilo zoezi. Wakaamua waanze kutafuta mshindi kati yao hao
wanaume ambaye ataweza kumuogesha huyo mdoli ndani ya beseni, bila kuingia
baridi wala kumdondosha ndani ya beseni. Kuanzia mwanzo mpaka mwisho kwenye
kumkausha, kumpaka mafuta, ndio diaper na nguo. Vilijaa vicheko na vya kilevi hapo,
wababa hao wakawa kwenye ushindani wa hali ya juu akitafutwa mshindi ili wote
wamchangie pesa aondoke nayo siku hiyohiyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huko
ukumbini nako upande wa wanawake, mambo yalikuwa ya namna yake. Kwanza
kulipambwa vizuri sana. Mbali ya sehemu yenyewe hiyo shuguli ilipofanyika, na
ndani pia kulipangiliwa kwa ustadi, pakawa nadhifu haswa. Sabrina alitengenezwa
vizuri akapendeza na mimba yake. Akamshukuru Pendo kwa kumpeleka saluni akatengenezwa
vizuri, na nguo ya thamani aliyomtafutia. Akawa ameendana na wale kina mama
pale. Ilionekana ni shuguli iliyoandaliwa na watu wanao jielewa. Maana aliletewa
hapo ukumbini mpaka daktari wa mambo ya watoto ili kutoa mafunzo. Akafundisha
vitu gani vya kuzingatia kwa mtoto, kuanzia mtoto mchanga kabisa anayetoka
kuzaliwa. Akaja mtu wa mambo ya lishe kwa watoto. Ikawa nzuri na muhimu kwa
wote. Hapo napo Sabrina akajifunza mengi na wengine kuuliza maswali. Ikaongezeka
michezo ya baby shower iliyowafanya wote washiriki. Kukajaa vicheko na
hali ya ushindani pia ikaanzishwa ili wote kushiriki. Ukumbi huo uliojaa
wasomi, wanawake wanaoshika nyadhifa tofautitofauti ndani na nje ya nchi,
wakapata burudani ya namna yake.
Kukaendelea
michezo, vichekesho, wakaja sasa wa mama waliogusa kila mtu hapo ukumbini.
Kwani wao walitakiwa kumfundisha Sabrina jinsi ya kuweka balance kati ya
watoto na mume. Nini chakufanya kama mama na mke. Akasimama mama mwingine msomi
lakini mcha Mungu. Huyo naye akafundisha mama wa kwenye bibilia na mke wa
kibibilia. Naye akaongea mengi na wapi watu wanakokosea. Akawa mcheshi haswa,
akatoa mifano mingi yakukosoa, watu wakacheka mno lakini hapohapo wakajifunza.
Zikaja
zawadi zilizo zidi kugusa moyo wa Sabrina. Zilichaguliwa baadhi tu zakuonyeshwa
pale kama kumfundisha Sabrina, nyingine zikaachwa zimefungwa na kuwekwa upande
wa wageni walipoweka zawadi zao. Wakina mama hao wakawa wanamkabidhi na jinsi
ya kutumia. Mama yake Sabrina mwenyewe hakuwa akiamini kama yote hayo anafanyiwa
Sabrina mtoto wake aliyekuwa akimuhesabu na kumuona si kitu kabisa. Kitendo cha
kuthaminiwa na mwanaume aliyeishi naye na kumuoa kwa kiapo kizito vile! Ni
kigugumizi kilichopata familia nzima.
Mama
Sabina alikuwa amekaa hapo haamini kama kweli yupo hapo kweli au ni ndoto tu,
atakuja kuamka. Maana aina ya wanawake waliokuwa wamemzunguka hapo! Ilikuwa
ngumu kuamini kama na yeye yupo miongoni mwao. Hakuwahi hata kudhania anaweza
kuja kuwa nao chumba kimoja maishani. Wengi aliweza kuwatambua kwa kuwaona
kwenye luninga, wengine walijitambulisha wenyewe wakati wakutoa zawadi au mada
na wengine alikuwa akinong’onezwa na Sabina. Kila mmoja hapo alikuwa mtu mzito.
Aina ya huduma zilizokuwa zikitolewa hapo, hata Sabina mtoto wa jiji alikiri
kwa mama yake kuwa hajawahi kuhudhuria aina hiyo ya baby shower. Kila
kitu kilikwenda kwa wakati na muda sawa sawa na kwenye ratiba.
Mwishoe
Pendo alitoa shukurani kwa waalikwa wote, na akaomba wamuombee bibi harusi
wake. Sabrina akataka kabisa kupiga magoti kabisa. Pendo na yeye akapiga naye
magoti, wakawazunguka nakuanza kuomba nao. Wakamuombea kujifungua salama, kuwa
mama mzuri na mke mwema. Maombezi yalipoisha, akapata muda wa yeye mwenyewe wa
kushukuru. Sabrina alizungumza maneno mazito ya kinyenyekevu, mbele ya hao kina
mama bila woga. Kikubwa aliweka msisitizo akisema, anamshukuru Mungu, amemjibu
maombi yake kabla hajafa. Aliwashukuru kwa kusimama na yeye katika kipindi hicho.
Aliongea Sabrina, mpaka wasomi hao wakapoa. Hakuongea kama msomi, lakini kama
aliyemuona Mungu kwa namna ya kipekee sana.
“Kila
mmoja wenu hapa, kwa nyadhifa zenu, sifa zenu zote, niliwaomba kwa Mungu. Tena
kwa kufunga na kuomba zaidi ya siku tatu, au 7, au 14 au 21. Nilishafunga
nakuomba sana nikabaki kushukuru kwa ajili yenu. Mimi ni mtu wa kawaida sana.
Mama yangu ni yule pale kama mlivyotambulishwa, na dada yangu. Tumetokea kwenye
familia ya kawaida sana, lakini namuabudu Mungu aliye mkuu mno, zaidi tumjuavyo
na tumfikiriavyo. Pale ufahamu wetu unapoishia kumjua yeye, ndipo uwezo wake
unapoanzia.” Watu wote wakapiga makofi wakiwa wameanza kuhamasika.
“Kuna
mtu nilikuwa nikimtia moyo sehemu, akiwa kwenye hali mbaya sana yakufa.
Nikamwambia amini tu. Amini kama utatoka hapo ulipo kwenye hiyo hali.
Nikamwambia inaweza isilete maana sasa hivi kwa kuwa ninayekwambia ni mimi.
Nikamwambia lakini yupo Mkuu aliyezidi vipimo vyote. Nikamwambia mimi nilikutana
naye miaka michache iliyopita. Nikamsoma uweza wake. Nikamwambia huyo mtu
aliyekuwa kwenye hali ya kufa aina ya maombi ninayoomba, nikamwambia
nikimwambia yeye, angeweza kusema nimechanganyikiwa.” Watu wakacheka kidogo. “Nikamwambia
lakini imani yangu haipo kwa kile ninachoomba, ila kwa yule
ninayemuomba.” Watu wakapiga makofi.
“Kwa
ufupi sana, kwa kuwa nilimjua ni nani nimuombaye, sikuomba vitu vidogo.
Sikuomba maombi ya kitoto ambayo mtu yeyote anaweza kufanya. Kwangu kuolewa na
Jackson Msindai, ni muujiza ambao unahitajika siku nzima kusimulia na kuuona
ukuu wa Mungu kupitia kile alichonibariki ili Jack, mwanaume ambaye nimekuwa
naye kwa miaka mingi sana, lakini nikajichelewesha kupokea baraka kubwa sana kuolewa
naye.” Watu wakapiga makofi huku wakicheka.
“Mungu ni mwenye rehema. Ukimuita, huitika kwa wakati wake
yeye Mungu wala si kwa wakati wetu. Japokuwa maisha yalinifinyilia, na
kunikatisha sana tamaa, lakini Mungu alinitunzia Jack wangu mpaka akahakikisha
ananikutanisha naye tena na kunikabidhi. Amekuwa rafiki wa karibu mno kuanzia
tupo chuoni. Amekuwa faraja ambayo hakika, sistahili ila ni Mungu tu ndiye
anayenistahilisha kuwa na mume kama Jack.” Sabrina
akafuta machozi wakati wakampigia makofi. “Na leo kuzungukwa
na watu wa muhimu kama nyinyi, mlioacha shuguli zenu za msingi, kuwepo hapa na
mimi sasa hivi, hakika huyo ni Mungu wala si mimi. Wifi zangu, mama Msindai
mwenyewe, mke mwenzangu Joy, wamekuwa wakinihangaikia mno pamoja na mama matron
wangu ambaye kila siku lazima ajue ninaendeleaje mimi na watoto! Kila
nikitafakari aina ya upendo na heshima ninayopata mimi, na kule ninakotoka, najua
ni Mungu tu.” Watu wakapiga makofi.
“Jamani,
yule Mungu aliyenitoa mimi mavumbini kabisa, nikiwa mnyonge na mpweke,
akakutane na haja za mioyo yenu.” “AMEN!” Wote wakaitika. “Akawatendeeni mema
mpaka mjue kama yeye ndio ametenda kwenu, kwa ule moyo tu wakutenda kazi pamoja
naye kujidhihirisha kwangu kwa namna kuu mno. Kwa kule kukubali bila
kunifahamu, na kutenda mnayonitendea, mlipotoa, pakaongezwe kwa namna ya
ajabu.” “AMEN!” Wakaitika. “Kwa hili mlilonitendea mimi, mume wangu na watoto
wetu, basi huyu Mungu mwenye ENZI yooote, akutane na kazi zenu, biashara zenu,
familia zenu, aguse watoto wenu, asije potea hata mmoja. Na waliopotea Mungu
akawarejeshe salama, kisha siku ya uhitaji wao, awakutanishe na watu sahihi wa
kusimama nao.” “Waooo! AMEEN!” “Mungu akumbuke waume zenu. Aweke ulinzi kwenye
majumba yenu, kilicho kibaya kisipite mchana wala usiku. Akawajaze kwa namna ya
pekee mpaka na nyinyi mjue huyu Mungu amewabariki TENA kwa hili
mlilonitendea mimi na watu wa nyumbani kwangu.” Vigelelegele na “Ameeen!” Wakaitika
wakishangilia na kusimama. Wakafunga na watu wakatoka kwa wakati.
Wakati wakiagana na wageni wao, Sabrina akasikia kichomi kwa nguvu. Akashituka kidogo, akatulia. Akaanza kusikia mvurugano tumboni kama wanae wanageuka na kucheza. Akatafuta sehemu, akakaa wakati wenyeji wake wakimalizia kuagana na waalikwa. Kiuno kikaanza kuuma. Akawa ametulia kabisa kitini. Mama yake na Sabina nao wakapata nafasi yakushukuru. Wakawashukuru kina Msindai na Pendo kwa baby shower nzuri na ya heshima. Na wao wakaondoka. Mwishoe Pendo akaomba awaache ili amrudishe bibi harusi wake nyumbani. Wakaondoka.
Atafafutaye
Hachoki.
P |
endo
akaondoa gari. “Upo sawa mwali wangu?” “Naona sababu ya kucheza sana, kiuno
kinauma kidogo.” Wakacheka story za ukumbini zikaanza. Wakazungumzia juu ya
zawadi. Sabrina akamsisitizia lazima na wao wapange kwenda kuwatembelea
Singida. “Nina chumba kizuri kwa ajili yako matron wangu. Ukichoka tu kelele za
jiji, njoo Singida.” “Lazima. Hivi nilikuwa nikimwambia Willy tutunze siku za
likizo ili ukijifungua tuje.” “Hayo ndio maneno. Nimebakisha majuma mawili tu,
kwa hiyo anza kuandaa begi la safari.” Wakacheka na kuzungumza kidogo.
“Lakini
da Pendo, mimi nataka kusimama na wewe, na tuamini pamoja juu ya wewe kupata
mtoto.” “Wala usijishumbue Sabrina.” “Kwa nini!?” Akauliza Sabrina kwa
mshangao. “Nilipimwa mwaka jana, mayai yalikuwa yamebaki machache mno! Umri
umekwenda, halafu pia nina vimbe zimeota huko kwenye kizazi kama uyoga. Hivi
hapa daktari alikuwa ananiambia nifikirie kutoa tu kizazi kwa kuwa hawawezi
kuingia huko kutoa hizo vimbe bila kuharibu kizazi. Zimeota sehemu mbaya sana.
Kwa hiyo hilo mbona tushafunga mimi na Willy! Naona tushakubali kuishia tu sisi
wenyewe.” Sabrina akatulia kwa muda akimfikiria Pendo. Pendo akashangaa hajibu,
ametulia.
“Maumivu
yamezidi?” “Hapana. Ila nikuulize da Pendo, unakumbuka nyumbani kwetu? Si
ulikuja wakati nalipiwa mahari?” Pendo akacheka. “Na wewe, pale kwenu ni pazuri
bwana. Hujaona kwenye majumba ya watu wengine?” “Hapana da Pendo. Linganisha
maisha yangu na ya kina Msindai au yenu. Kuwa tu muwazi. Mtu kama Jack,
angeniona wapi mtu kama mimi?” Pendo akanyamaza. “Nikikwambia kuwa Jack alikuwa
akipiganiwa chuoni na wadada warembo utaamini?” “Wala usiende mbali. Yule msichana
aliyeleta boksi la baby wipes. Akasema ameleta nyingi kwa ajili ni watoto
mapacha, akawa anakufundisha jinsi ya kufuta mtoto.” “Nimemkumbuka. Anakaumba
kama namba sita hivi.” “Ewaaa! Anaitwa Salome, au Sally kama wengi tulivyozoea
kumuita.” “Sasa amefanyaje?” Sabrina akauliza. “Anampenda Jackson yule, kufa.
Tena wala hafanyi siri, ila tu ni mstaarabu. Hana mambo ya ajabu. Rafiki yake kipenzi
Jena. Na wengine wengi tu. Tena ndio ilikuwa zaidi wakati Jack anaishi hapa
Dar, tukawa tukimtania bora aoe, ili tupumzike” Sabrina akacheka.
“Sasa
hali hiyohiyo ndio ilikuwa chuoni, wasichana kumgombania Jackson Msindai.
Lakini da Pendo, jua tu Mungu yupo na hutoa kwa amtakaye yeye Mungu na hakuna
wa kumuuliza. Mimi sijui amekusudia nini kwako, lakini dada, kama alifanya kwa
Sabrina, hatashindwa kwako. Na usifikiri niliomba mara moja nikaacha!
Nikikwambia siku 21, niamini ni 21 zile ngumu mno. Hivi unavyoniona sikuwa na
marafiki ila Jack tu ndiye alikuwa rafiki kwa simu kipindi nimefungiwa nyumbani
wala sijui nitatoka vipi. Kazi mchana na usiku na mengine mengi ambayo
nilikumbana nayo, ila sitaki kuongea kwa kuwa nimesamehe. Dada Mungu yupo.
Hafanyi mambo ya kijinga au yakawaida. Anataka kufanya jambo kwa watu kama
wewe, ili kufedhehesha wenye hekima. Yaani wakisikia Pendo amepakata mtoto,
masikio yawashe na wamtukuze Mungu. Nina uhakika wanao nifahamu mimi,
wakasikia nimeolewa na Jackson Msindai, hawataamini. Lakini dada, ni Mungu. Mungu
yupo. Kama umekata tamaa, tafadhali acha mimi nikubebe. Acha imani yangu
ikubebe tu.” Akamuona Pendo anafuta machozi yaliyokuwa yamefichwa ndani kwa
tabasamu la nje tu.
Sabrina
akaanza maombi hapo kwenye gari. Aliomba Sabrina akimkumbusha Mungu yale magumu
aliyomtendea yeye. Jinsi alivyomuona hata Singida. Yale amefanya huko kwa muda
mfupi sana. Akamwambia Mungu, anamwamini kwa ajili ya Pendo. Akamkumbusha mengi
Mungu aliyojidhihirisha kwake kwa kupitia Pendo, akamwambia amkumbuke Pendo.
Sabrina aliomba sana. Mpaka Pendo akafika nyumbani kwa mama Msindai, akaegesha
gari nje, akamshika Sabrina mikono. Sabrina akamshikisha ile mikono tumboni
kwake. Akamwambia uwezo uleule na baraka zile zile za mapacha, zimshukie Pendo.
Kisha wakashikana tena kuendelea kuomba.
Jack
aliona gari likiwa linaingia hapo kwao, ila akashangaa Sabrina haingii ndani.
Yeye akatoka akasogea mpaka garini, akakuta wakiomba, akafungua mlango,
akamshika mkewe, na yeye akaungana kwenye maombi. Alipogundua wanamuombea
Pendo, na yeye akaongeza nguvu. Wakaomba pamoja mpaka wakamaliza. “Ameen!” Wakasema
wote kwa pamoja.
Jack akamshukuru Pendo kwa kila kitu, akamsaidia mkewe kushuka
garini, Pendo akaondoka.
Sabrina
ajifungua na kuzua Mtafaruku!
Y |
akaanza
mabusu hapo hapo nje. Jack akamkumbatia mkewe na kumbusu tena na tena.
“Tunaondoka kesho.” “Basi tuwahi kulala. Kiuno kimeanza kuuma ukumbini. Sijui
nimecheza sana!” Sabrina akamsimulia waakaanza kucheka. “Mimi nimepata shule ya
nguvu. Hapa najua kuogesha vichanga na kufunga diaper.” Jack akaanza kujisifia,
Sabrina akamwangalia na kuanza kucheka. Akaendelea kumsimulia aliyojifunza
wakiwa wamesimama palepale nje, mara kichomi kingine kikapita kwa nguvu sana
mpaka Sabrina akakaa kwenye ngazi. “Vipi tena!?” Jack akauliza akionyesha
wasiwasi. “Nasiki.... Aaaah!” Kalalamika Sabrina.
“Basi
twende ukapumzike. Maana kumekuwa na shuguli nyingi kweli! Utakuwa umechoka na
watoto hao washakuwa wakubwa.” Akamsaidia kusimama. Ile anamalizia ngazi ya
mwisho, chupa ikavunjika wote wakabaki wametoa macho. “Si tumeambiwa bado
majuma mawili!” “Naomba tukashangae hukohuko hospitalini. Nasikia maumivu Jack,
naona hawa watoto wamechoka kusubiri.” “Kweli. Sasa nakubeba au naku...” Tayari
Jack akawa kama ameshapaniki. “Acha kupaniki bwana! Wewe si umeniambia
umefundishwa ku...., aaah!” Sabrina akashindwa kuendelea kwa maumivu mengine
yaliyopita gafla.
“Kufundishwa
na uhalisia nitofauti bwana! Niambie nifanye nini?” Sabrina akaanza kushuka
tena ngazi. “Acha nikubebe.” “Naweza kutembea Jack, tulia, acha kupaniki.” “Unamaumivu
makali sana?” Sabrina akanyamaza. “Sasa ukijifungulia njiani, itakuaje?” “Ndio
nitakuwa nimejifungua Jack jamani! Acha kuwa na wasiwasi. Kwanza hebu niangalie.”
Jack akasimama. “Tulia kabisa. Naomba tulia na niambie nitakuwa sawa.
Nitajifungua salama na kila kitu kitakwenda sawa.” Sabrina akataka mumewe
atulize akili. Jack akatulia akakumbuka alitakiwa awe faraja. “Nakuaminia
Sabrina wangu. Hata hili utaweza tu mke wangu. Twende tukawapokee kina Jeiline
na Keiline.” Sabrina akacheka moyoni, wakaondoka pale.
Wakiwa
njiani kila maumivu yalipoongezeka aliamua kuvumilia ili asimtie hofu Jack
ambaye alikuwa akipiga simu kwa kila aliyemjia. “Tupo
njiani tunaelekea hospitalini. Naona wanangu wamechoka kusubiri. Wanataka kuja
kukutana na baba yao.” Sabrina akabaki akimsikiliza akizungumza na simu
yeye akigugumia taratibu. Maumivu yakaongezeka yakawa karibu karibu. Mzee
Msinda akamwambia anampigia simu rafiki yake, ambaye ni daktari wa wakina mama,
ili akutane nao hospitalini. Hilo likamfariji Sabrina kugundua kama yupo mtu wa
kuaminika atakuwa akiwasubiri huko hospitalini.
Sabrina
anafika hospitalini, akawa na maumivu asiyoweza kuvumilia wala kutembea. Jack
akakimbia mapokezi akaomba msaada wa haraka. Wakati yupo mapokezi wanasubiria wheelchair
kuletwa ili akamchukue Sabrina, akashitukia Sabrina anakuja. “Hawa watoto wanatoka Jack. Hakika nitazaa hapahapa.”
Jasho lilikuwa likimtoka Sabrina, macho mekundu kwa maumivu. “Nasikia kabisa kitu kintoka huku chini. Nitaua wanangu
Jack!” Hapo Sabrina akazidi kulia kwa sauti ya wasiwasi maana walikuwa
wanachelewa. Mama mmoja naye alikuwa hapo mapokezi na mgonjwa wake akamkimbilia
na kumshika, “Kaa chini kabisa.” Sabrina akakaa akisaidiwa na yule mama. Jack
alishaanza kupiga kelele kuomba msaada akisema wanachelewa. “Wote uliowakuta
hapa ni wagonjwa kaka yangu.” Akaongea muuguzi mwingine akiendelea kuandika hapo
ndani mapokezi.
Mara
aliyekwenda kuleta kitanda akaja. Wakasaidiana kumpandisha Sabrina na
kumkimbiza labour. Wanaingia tu, muuguzi anamwangalia, kweli kichwa cha mtoto
kilikuwa kinatoka. “Mungu wangu mtoto wa kwanza anatoka!” Jack naye alikuwepo
hapo. Hapakuwa hata na muda wakuchomwa sindano yakumfanya asisikie maumivu, epidural,
Sabrina akasukuma, mtoto wa kwanza akatoka. Akahema kwa nguvu kama aliyepata
aghueni wakati mtoto wake akisikika akilia hapohapo hata kitovu hakijakatwa. “Haaa!”
Wakashangaa wauguzi wote wanashangaa. Jack na Sabrina wakashituka. “Huyo ni Jeiline.
Yupo salama?” Jack akauliza akaona wanaangaliana. Jack akasimama na kusogea.
Akakutana na mtoto wa kizungu. Akatulia kidogo kama na yeye amekutana na kitu
ambacho hajatarajia.
“Kuna
nini Jack!?” Sabrina akauliza kwa wasiwasi. “Mtoto yupo mzima?” Jack akarudia
kuuliza tena kama aliyerudiwa na akili. “Mzima kabisa, ila..” Aliyekuwa
akimalizia kumtenganisha na mama yake akawa kama amepatwa kigugumizi. “Naomba
kumbeba kama ni mzima.” Jack akampokea baada tu ya kufutwa kidogo. “Hey Jeiline!
Njoo umuone mama.” Akamsogeza kwa Sabrina. Sabrina mwenyewe akashituka kukutanishwa
na mtoto wa kizungu. Hakutegemea kabisa. Jack akamuwekea kifuani kama mkunga
alivyomuelekeza ili apate harufu na joto la mama yake.
Wapo
watoto wanazaliwa weupe, na nywele, lakini Jeiline alizaliwa mweupe wa kizungu
kabisa, na nywele nyingi haswa kama mtoto wa kiarabu wala si wakizungu maana
watoto wa kizungu asilimia 99 huzaliwa bila nywele. Uso mwembamba uliochongoka kama
mama yao na midomo ya pinki kabisa. Ndipo akili ikamrudia Sabrina, akakumbuka Tino
alimwambia mama yake alikuwa mwitaliano.
Sabrina akamnyanyua vizuri akiwa kwenye kitanda cha kujifungulia, wakisubiri
mtoto wa pili. Wakamuona anambusu mtoto wake. “Nimefurahi kukuona Jeiline. Umekuja kwa wakati wa Bwana.
Namshukuru Mungu umezaliwa mzima.” Sabrina akaongea kwa sauti ya
taratibu na machozi. “Wewe ni mtoto mzuri sana na
Mungu ana mpango na wewe. Hujaja hapa duniani kwa bahati mbaya. Umebarikiwa kwa
baraka zooote za rohoni na za mwilini. Kila ulimi uliotamka na utakaotamka
kinyume na baraka za Mungu juu yako, na uhukumu mkosa. Katika jina la Yesu.”
Akaongeza Sabrina kama anayemuombea mwanae na kumbusu tena. Wale wakunga wote
pale ndani wakapoa. Jack naye akaitika “Amen.” Na kusogea karibu kabisa
akajilaza pembeni ya bega la Sabrina wakawa wanamwangalia mtoto kwa juu. “Kweli
wewe ni mzuri Jeiline! Na tunakupenda sana mwanangu.” Sabrina aliposikia hivyo,
ikamfariji sana. Jack akajinyanyua na yeye akambusu tena na tena.
“Naruhusiwa
kupiga picha ya sisi watatu kabla mdogo wake hajaja?” Jack akauliza.
Wakamkubalia. Wakawasaidia kupiga picha yule mtoto akiwa vilevile alivyotoka
kuzaliwa. Wakapata picha nyingi tu mpaka Jack akatosheka na picha ndipo
wakamchukua sasa mtoto kumsafisha vizuri na kumvalisha. Wakati wanamsafisha,
Jack akarudi kwa Sabrina. “Pole na hongera Brina. Naona umeniletea mzungu!”
Jack akaongea na kumbusu. Sabrina hakujua kilio kilitokea wapi, akaanza kulia
kwa kwikwi. “No no nooo! Which is good Brina. Usifikirie ni jambo baya.
Ni zuri mnoo. Nimefurahi.” Jack akajua amemuudhi, asijue Sabrina amefurahia,
hakutegemea kama Jack angewakubali watoto wa aina ile. Alimuona jinsi Jack alivyoshituka
mwanzoni mara tu alipomuona mtoto. Lakini ni kama akajirudi kwa haraka. Wauguzi
pale wakawa wanasikiliza, hawaelewi.
“Wazungu
ni wazuri tu. Hata ungenizalia wajaluo, wakijani au wahindi, mimi sawa tu.”
Mpaka Sabrina akacheka. “Kweli?” “Sasa wewe
unafikiri nitaozesha hawa kwa pesa ndogo?” Kila mtu pale akaanza kucheka.
Angalau ule mshangao pale ukapungua. Na Sabrina akasahau kama ana mtoto
mwingine tumboni. Jack akaanza mabusu kwa mkewe wakati wauguzi wakimtayarisha
mtoto na yeye mwenyewe kwa kujifungua tena. Jeiline akarudishwa. Picha
zikaendelea. Jack akaanza kuchukua video ya selfie. Akawa anamuelezea Keiline
kuwa wapo hapo wao watatu, mama yake, yeye na dada yake Jeiline wanamsubiria
yeye. Wanahamu yakumuona na yeye. Sabrina akawa anacheka taratibu huku amemlaza
Jeiline kifuani, yeye bado amejilaza huku amemkumbatia mwanae, Jack akitoa
mabusu ya hapa na pale kwa Sabrina na Jeiline. Mara simu zikaanza kuingia.
“Sijui
nianze kupokea ya nani, niache ya nani!” Wakati Jack akijishauri, daktari akaingia.
“Sabrina Msindai?” Akauliza. “Ndio mimi.” Akamsogelea akionekana alikuwa
akiharakisha kufika hapo. “Naona ushakumbatia mtoto wa kwanza.” Daktari
akaongeza. Jack akamchukua mtoto kutoka kwa mama yake na kumbeba yeye vizuri
kwa upendo na cheko usoni. Yule daktari yeye hakuonekana kumshangaa yule mtoto
wa kizungu. “Hongereni sana bwana. Naona mama na Mzee wana wasiwasi sana na
wewe Jack. Wangeona hiyo furaha! Wasingekuwa na wasiwasi.” Jack akacheka. “Ndio
wajue nimekuwa baba, waache kunifanya mimi kama mtoto mdogo.” Jack akaongea
macho kwa mtoto. Daktari akacheka na kuomba kuona vipimo vya mtoto huyo wa
kwanza. Wakamuona anatingisha kichwa kama anayekubali. Wakamuona anacheka. “Naona
na jina tayari!” “Nimempa huyo nesi ili asinichanganyie watoto.” Jack akajibu
wote wakacheka pale.
Heshima
ikaongezeka mara baada yakugundua ni kina Msindai. Mama Msindai alishakuwa Waziri
wa afya. Mtoto mtu yupo madarakani na yule daktari alishasema wote wapo njiani
na wengine wapo nje wanasubiria. Hata ule uwepo wa yule daktari tu pale kwa
mama ambaye hana tatizo kama Sabrina, inamaana yupo pale kuhakikisha hakuna
linalokwenda vibaya. “Anaonekana mzima kabisa. Huu mwili utaongezeka ukikazana
kunyonyesha.” “Mmmh! Maana nimekaona kadogo! Nikajua amechukua mwili wangu.”
Sabrina akalalamika. “Ni mara chache sana kupata mapacha wanaozaliwa wakubwa.
Hata kwa hizi kilo na siku walizozaliwa, wamejitahidi sana.” Yule daktari
akaongea huku akiendelea kusoma. Akarudisha lile jalada na kumsogelea tena
Sabrina.
Akafanya
baadhi ya vipimo. “Unaonekana upo tayari kuleta wapili.” “Itachukua muda gani,
maana hapa nimepoa kabisa.” Yule daktari akacheka kidogo. “Wengine wanachukua
mpaka masaa. Lakini wewe una dalili za...” “Auuuuh!” Sabrina akalalamika kama
aliyesikia kichomi kwa nguvu. Hawajakaa sawa, Sabrina akasukuma mtoto wa pili
kama mchezo. Wakabaki wametoa macho. “Naona hawa wamekuja na upako wao.”
Akaongea yule daktari wakati akimpokea mtoto. Hapo hapo akalia. “Na watoto wenu
wanaonekana wapo sharp! Wanatoka na kulia!” “Hicho ni kitu kizuri?” Akauliza
Jack. “Sana. Inamaana hata akili yao ipo sharp.” “Yess!” Jack akashangilia huku
amembeba Jeiline. “Unasikia Jeiline? Mmezaliwa kuwa vichwa nyinyi, sio mkia.” Akaongeza
Jack na kumsogelea Sabrina akijua Keiline atawekwa hapo kifuani. Jack alishatoa
simu yake na kuchukua video. Akavuta kiti akakaa upande wa juu alipolala
Sabrina. Kuanzia kiunoni kwenda chini alikuwa amefunikwa. Baada tu yakukatwa kitovu, akawekewa Keiline
kifuani.
“Sasa hapa utakuwa mtihani. Mbona hawana tofauti!”
Sabrina akashangaa machozi yakimtoka, wakacheka. Akambusu. “Kweli bwana! Hebu
mgeuze huku kwangu.” Sabrina akamgeuza. “Oooh my! Jeiline, unamuona baby Keiline?”
Jack akaongea kwa hisia zote. Na yeye akambusu. “Nimefurahi
kukuona Jeiline. Umekuja kwa wakati wa Bwana. Namshukuru Mungu umezaliwa
mzima.” Sabrina akarudia maneno yale yale aliyomwambia Jeiline na
kumuombea pia. Wakapata picha moja, wakaomba wamchukue na yeye asafishwe.
Wakati huo tayari Sabrina alikuwa akishonwa na kusafishwa. “Umechanika, lakini
sio sana. Nitakushona vizuri sana.” “Asante.” Sabrina akashukuru, akamuona Jack
anambusu kila mara Jeiline. Moyoni akaendelea kumshukuru Mungu.
Alipomaliza
kusafishwa na Keiline, Jack akaomba wapigwe picha ya pamoja, akachukuliwa video
akimkaribisha Keiline. Kisha akawaweka wote kwa mama yao. Vikajaa vicheko hapo,
Jack asiwe na wazo la pili. Akaomba atoke na watoto wake wote. Akaruhusiwa.
“Akampigia simu Willy na kumwambia akae tayari na kamera, achukue video wakati
anatoka na watoto. Sabrina akatingisha kichwa. “Unashuguli Jack jamani!”
Sabrina akamshangaa. Akacheka tu na kutoka akiwa amewabeba binti zake wote
wawili.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipotoka
tu wakaanza kupiga makofi. “Asante, asanteni sana.” Jack akaongea kwa cheko
kubwa. “Sasa, naomba niwatambulishe kwenu mabinti zangu wawili. Jeiline Msindai
na Keiline Msindai.” Wakapiga makofi na kusogea. Wote wakapoa gafla baada ya
kukutana na watoto wa kizungu, Jack akawaona. “Msishituke jamani. Binti zangu
ni wakizungu.” Pakazuka ukimya wa gafla. Jack akawaangalia kwa zamu usoni.
Akaanza kwa mama yake, baba, dada zake, Willy, Pendo, Joy na kaka yake. Angalau
kaka yake na Pendo wakaonekana kufurahia. “Naruhusiwa kumbemba? Nimenawa mpaka
mikono.” Kaka mtu akamsogelea. “Na mimi naomba mmoja, nipate upako.” Pendo naye
akaongeza. Wengine kimya.
“Labda
sasa hivi atakuwa ananitaka mimi.” Jack akamsogelea kaka yake na kumchukua Keiline.
“Naona hamu haijakuisha!” “Bado nahisi nipo usingizini kaka. Siamini kama waha
ni wangu kabisa. Yaani nikirudi nyumbani, narudi nao!” Jack akaongea kwa
kuhamasika wala asimfikirie mama yake na dada zake waliokuwa kimya muda wote.
Daktari
mwingine akafika pale walipokuwa wamesimama kina Msindai. “Hongereni sana.
Naona vijana wenyewe wameshatoka nje kabisa, na mganga mkuu upo hapa, sina
wasiwasi.” Mzee Msindai akacheka. “Mganga hajigangi bwana! Bado wanakuhitaji
hawa wawili.” Akajibu Mzee Msindai mwenyewe na kumpa mkono kama kusalimiana.
Wakazungumza kidogo, akaomba akawatizame ndani. Jack akachukua watoto wake,
akarudi nao ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya muda Sabrina na watoto wake wakatolewa kupelekwa wodini. Fist class
kama jina alilopewa na Mungu ukumbwani linavyofanana na hapo. Misindai. Halafu
mzee Msindai mwenyewe daktari mkongwe, bingwa wa watoto hapo nchini alikuwepo
hapo. Waziri yupo hapo na aliyekuwa waziri wa afya naye alikuwepo! Sabrina akapendelewa
chumba kizuri tu. Akaingizwa humo na watoto wake wawili, Jack akaingia akiwa
amechangamka na Pendo yeye akaelekea kwa watoto moja kwa moja. “Sasa naenda
kuchukua baadhi ya vitu nyumbani, nitarudi baada ya muda mfupi.” Akambusu mkewe
na kutoka kwa ahadi ya kurudi bila ya kuchelewa.
Akaingia
Junior, mkewe, Willy na Mzee Msindai. Wakampongeza Sabrina. Joy akamsogelea
Pendo aliyekuwa na watoto, akamchukua mmoja. “Sisi tunaondoka shem ili upumzike.
Najua utakuwa umechoka na hekaheka ya siku nzima ya leo, na hii kazi ya kuleta
hawa watoto wawili hapa duniani! Unahitaji kupumzika. Tutakuona kesho.” Junior akaaga.
Mzee Msindai naye akaongeza pongezi na pole. “Asanteni sana kwa kuja.” Sabrina
akawapa mkono. “Sasa Joy?” Junior akamsogelea mkewe pale kwa watoto. “Naona
twende. Tutakuona kesho Sabrina. Pumzika mama. Naona kazi haikuwa ndogo.
Tumecheza ukumbini, naona kina dada nao wakasikia.” Joy akamfanya Sabrina
acheke kidogo. “Hongera sana. Unahitaji kupumzika.” “Asanteni kwa kila kitu.”
Sabrina akashukuru. “Acha mimi niwasindikize. Nitarudi Pendo.” Akaaga Willy,
Pendo akaitika macho kwa mtoto, Joy akataka kumrudisha mmoja kitandani, Pendo
akataka ampe ili awapakate wote wawili. Joy akampakatisha vizuri. Wakatoka.
Pakawa kimya.
“Hongera
Sabrina na pole.” “Namshukuru Mungu wala sikupata shida dada yangu. Naona Mungu
amenihurumia.” Wakacheka kidogo. “Kwa kuwa watoto wamelala, na wewe pumzika
kidogo, ili wakiamka uwe hata na nguvu. Sitaondoka mpaka Jack arudi, kwa hiyo
usiwe na wasiwasi.” “Asante. Japo nahisi nipo kwenye mshituko. Siamini kama na
mimi nina watoto!” Wakacheka kidogo. “Nimechoka, lakini usingizi naona haupo!”
“Wewe funga macho tu. Ni wako hawa. Utahangaika nao mpaka uchoke. Lala.”
Sabrina akafunga macho. Pakawa kimya. Wakasikia watu nje ya chumba wakizungumza
kwa sauti ya chini kidogo. Ikawavuta masikio kusikiliza.
Kumekucha…
W |
akamsikia
mama Msindai akiongea kwa kulalamika. “Hakika ipo namna! Hii sio akili ya Jack
mwanangu. Hata kama kupenda, kupenda gani kwa fedheha hivi! Anafurahia watoto
wakizungu! Yeye mweusi, na mama yao maji ya kunde tu! Haya wakitokezea na hawa
watoto hadharani si ndio yatakuwa maajabu!” “Mmmh! Heri wangekuwa weusi mama,
angalau unafunika. Wazungu!” Akasikika Jena akiongeza kwa mama yake. Pendo
akaanza kuhisi miguu inamwishia nguvu. Akatamani atoke awaombe wakazungumze
nyumbani, lakini alikuwa amebeba watoto wote wawili na akajua wazi na Sabrina anawasikia.
“Aibu
gani hii!? Niambie unawaambiaje walimwengu jamani! Watoto wanaitwa Msindai!
Wakina Msindai weusi! Hilo hata Jack angelifikiria kama anaakili yake ya
kawaida!” “Sasa wewe mama unahisi nini?” Wakamsikia Jena anamuuliza mama yake.
“Hawa watu wanatoka Bagamoyo jamani! Tusilisahau hilo.” Moyo wa Sabrina akashituka
kama kumeanguka chuma sakafuni. “Na mnakumbuka mara ya mwisho walimpeleka Jack
hukohuko kwao Bagamoyo?” “Jack alisema wanakwenda kumtembelea bibi yao,
aliwakaribisha.” “Sasa huko nahisi ndiko walikomlisha vitu vyakumwaribu akili mwanangu.”
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mungu Ametenda, Mpaka Masikio Yanawasha.
Majibu Yake Sabrina Kutoka Kwa Mungu Ndiyo
Hayooooooo! Yameanza Kuwasha Masikioni Kwa Mama Msindai Aliyeshindwa Hata
Kuiona Sura Ya Sabrina Na Kumpa Japo Pole Na Hongera Ya Kinafiki!
Je, Nani Atahimili Hizo
Baraka Za Mungu Za Kushangaza?
Usikose Muendelezo…..
0 Comments:
Post a Comment