Mwanzo mpya na ahadi zakudumu.
Harusi
iliisha, Jack na Sabrina walichukuliwa chumba Hyatt hotel kwa siku mbili,
ambapo siku ya tatu walikuwa wakisafiri kuelekea Afrika ya kusini kwenye mji wa
Cape town, mwisho kabisa kwenye kona ya nchi iliyoingia baharini, eneo
linaloitwa Cape point ambako ndiko Willy na Pendo walikokwenda na wao kwenye
fungate yao na ndio walio watambulisha huko. Wakapasifia sana mpaka Jack na
yeye akaona si mbayana wao waende huko. Sabrina na mumewe walifika huko wakiwa na siku
5 zaidi za mapumziko. Walikutana na hoteli nzuri sana na mazingira mazuri kama
walivyosifia Willy na Pendo.
Mchana
walikuwa wakitoka kutembea kidogo, na kurudi hotelini. Wakapata wakati mzuri
sana wawili hao wa mapumziko. “Nikuombe kitu na kukuapisha Jack?” Sabrina
akamuuliza Jack walipokuwa ufukweni wakitembea. Jack akasimama. “Nini?” Sabrina
akavuta pumzi kwa nguvu na kujiweka sawa. “Usiwahi hata kwa kuropoka, kumtaja jina
la aliyenipa hii mimba.” Jack akanyamaza. “Hata kwa mama yako mzazi. Acha ibaki
hivyohivyo jinsi ilivyo. Ujulikane wewe kuwa baba wa hawa watoto, lakini siye
aliyenipa mimba.” Jack akamtizama na kunyamaza.
“Au
ulishasema?” “Hapana Brina. Ila nyumbani wanafahamu kuwa ulikuwa mjamzito kabla
yangu.” Sabrina akafikiria. “Kwa hiyo unafikiri nilazima uwaambie mimba ni ya
nani?” “Hapana. Nitaheshimu matakwa yako. Kwa wengine wote watabaki kuwa ni
watoto wangu kabisa. Hata nyumbani nimewaambia watakuwa kina Msindai. Hakuna
aliyepinga. Nakupenda Brina, na hata kuwa na hao watoto nahesabu ni upendeleo.
Lakini najua ipo siku ukweli utatakikana kujulikana.” “Nakuhakikishia Jack,
labda kutoka kwako. Kumtaja aliyenipa mimba mimi, litakuwa jambo la mwisho, na
ninaomba Mungu anisaidie.” “Na watoto wakitaka kujua ukweli?” Jack akauliza.
“Mimi si ni mama yao? Nakuhakikishia Jack, baba watakayemsikia kutoka kwangu ni
wewe.” Sabrina akafikiria kidogo.
“Hawa
watoto kama wanahisi na kuelewa, sauti ya mapenzi ya kweli waliyopata na
kuifahamu mpaka sasa ni wewe tu. Mimi mwenyewe sifahamu jinsi unavyofanya wewe.
Hata sijui jinsi ya kuzungumza nao zaidi ya kuwaombea tu.” Jack akajisikia
vizuri sana. “Unajua ni nini ninachowafanyia hawa watoto?” “Nini?” Jack akataka
kujua. “Kuwaombea kwa Mungu, kufuta mkosi waliowekewa na Tino kutaka kuwauwa
wakiwa hawana hatia. Nikiwa peke yangu huwa natamka kama mwenda wazimu, kuwa
wao kuletwa hapa duniani sio tatizo, Mungu hakukosea, analo kusudi nao.
Nawaambia wanae baba wa mbinguni anayewapenda sana, na ndio maana ameamua kuwaonyesha mapenzi ya kweli kupitia wewe.” Jack
akamfuta machozi.
“Ni kwenye maombi tu ndio naweza kuzungumza na hawa watoto,
Jack. Ili kama nafsi zao zilisikia tokea mimba yao ikitungwa, au kama shetani
alisikia na kutaka kuwapatiliza kwenye maisha yao hapa duniani, akome kabisa,
na wao waelewe. Wanaupendo mkubwa sana unaowasubiri huku nje, sio wangu, wako.
Nikikuangalia wewe hivyo, napata moyo wakuendelea Jack, na naamini Mungu
anawajali. Sitathubutu kuja kuwaanzishia kitu kingine au mahusiano mengine ya
mtu mwingine kama baba isipokuwa wewe. Hata wao waje waniulize wakiwa wakubwa
Jack, nitawaambia wewe ndiye baba yao. Hilo halitakaa likabadilika. Ndio maana
nakuomba Jack, usiwaambie vinginevyo. Sio wao wala mtu mwingine. Naomba iwe
siri ambayo mimi na wewe tutazikwa nayo na ninaomba Mungu atusaidie. Kabla
yakukubebesha mzigo mzito hivyo, unafikiri utaweza?”
“Nitaweza Brina. Nitatumia hekima hata kwa mama, ili ibakie kama hivyo
ulivyotaka.” “Asante Jack. Ni hilo tu.” Jack
alijua amepewa jukumu zito, hakuna siri duniani, lakini akafurahia hiyo
heshima.
Wakaanza
kutafuta majina huku wakibishana kama watoto wadogo. Mwishoe wakaamua kuyaandika
majina yote yanayowajia mawazoni. Yakiume na ya kike, wakiambiana kadiri siku
zinavyozidi kwenda, watakuwa wakiyapunguza na wakijua jinsia ndio watakamilisha
kabisa. Ushindani na kubashiri watakuwa watoto wa jinsia gani ukawashinda.
Wakaamua wakifika tu Dar, kitu cha kwanza ni kwenda kuangalia jinsia.
Wakakubaliana hilo. Kwa hakika walipata wakati mzuri. Walipomaliza muda wao,
wakarudi Dar.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walikuta
wasimamizi wao wa harusi wakiwasubiri uwanja wa ndege. Wakapongezana na wao
wakapata nafasi ya kuwashukuru kwa jukumu zima la kuwasimamia harusi, lakini
kwa umbali mkubwa sana Pendo aliokwenda kwa Sabrina hata kabla ya harusi
yenyewe. Kwa hakika Sabrina akawa amepata dada ambaye hakutegemea. Alimsimamia
katika kila jambo na kumshauri kwenye mazuri tu ili kufanania na kina Msindai
na aina ya wageni ambao waliwatarajia. Na kweli Sabrina alitokea katikati yao,
akafanana na hadhi yao. Hiyo yote ni Pendo kumchukulia taratibu Sabrina na
kumuelimisha kwenye mengi. Hakumdharau hata kidogo ila kumbeba kwa unyenyekevu kama
alivyo Pendo mwenyewe.
Walifika
jijini mapema tu. Wakawapeleka mpaka nyumbani kwao. Wakaambiwa mama yake Jack
ameandaa chakula cha usiku, kuwakaribisha nyumbani wao kama familia sasa, na
kufahamiana kwa karibu na ndugu wa Sabrina. Sabrina na Jack walipumzika mpaka
jioni, ndipo wakaongozana mpaka nyumbani kwa Msindai.
Walikuta
ndugu wa karibu wa pande zote wakiwasubiri. Familia ya Sabrina wote walikuwepo
kasoro wadogo zake. Jack na Sabrina wakawashukuru wote kwa harusi nzuri sana
waliyowaandalia, zaidi zawadi kubwa walizopata. Pesa yote iliyobaki baada ya
maandalizi yote, usiku huo Juinor akawakabidhi. Hawakuamini. “Ni pesa yenu. Watu
wasingechanga kama sio nyinyi. Kwa hiyo ni yenu.” “Tunashukuru.” Wakaonyeshwa
zawadi zilizokuwa zimejaa chumbani kwa Jack. “Sasa hizo itabidi kukodishiwa gari
ziwafuate.” Akaongeza mama Msindai. “Kwa kweli. Maana hivyo zilivyo sijui tutamaliza lini
kufungua!” Jack akaongeza na kufunga mlango.
Walipata wakati mzuri sana jioni hiyo. Hawakujua mzee Msindai alipata wapi nyimbo za Kingoni, anakotokea baba yake Sabrina, lakini zikaanza kupigwa. Kila mtu alikuwa akicheka vile anavyocheza. “Unapatia kabisa!” “Nakwambia mimi nimekaa sana na wangoni! Mpaka kuzungumza kingoni nilikuwa nafahamu, sema nimepoteza baadhi ya maneno.” Wakazungumza mengi wakifurahia na kupongezana mpaka wakaagana. Sabina akawarudisha wazazi nyumbani kwake, kwa ahadi ya kuwa kesho kama watawahi kutoka hospitalini, basi wafanye safari ya Bagamoyo kumuona bibi. Hilo likakaa sawa. Pendo naye akaondoka na mumewe na maharusi wao.
Jinsia ya
watoto aliobeba Sabrina.
K |
wa kuwa
walikusudia kuondoka siku inayofuata kurudi kwao Singida, asubuhi na mapema,
Jack na Sabrina wakaanza mipango. Jack akampigia simu dereva wa nyumbani kwao
kumtaka akanunue vyakula vya kupeleka kama zawadi kwa bibi yake Sabrina.
Akamwambia akishanunu orodha nzima, awatafute na kuwapelekea. Sabrina naye
akapiga simu asubuhi hiyo kumtaarisha mama yake kuwa watawapitia mapema tu,
awasindikize Bagamoyo. “Kama kuna nafasi kwenye gari
baba yako naye anaomba aongozane na sisi.” Mama yake akaomba
kinyenyekevu. “Nafasi itakuwepo mama. Hamna shida
kabisa.” Sabrina akajibu. “Na mimi nataka kwenda
Sabrina.” Akasikia sauti ya Sabina dada yake. “Basi
nyinyi mjiandae, naona chakula cha mchana leo tutakula kwa bibi.”
Wakalifurahia hilo na kuagana.
“Naona
safari imepata waumgwaji mkono wengi!” Sabrina akamwambia mumewe. “Na nani tena
yupo safarini?” “Sabina, mama na baba. Nimewaambia ni sawa tu. Au kuna shida?”
“Hata kidogo. Tena tukiwa wengi ndio vizuri. Wakaendelea kuzungumza mpaka
walipofika sehemu ya ultrasound. Walikuwa na appointment ya saa tatu kamili.
Mzee Msindai alifahamika vizuri sana hapo na ndiye aliyeomba wawaone asubuhi
hiyo.
Waliingia
chumbani, Sabrina akabadili nguo. Akaja mtu wakuangalia. Jack akasimama haraka
kusogelea pale alipolala Sabrina. Akaanza kupitisha kifaa tumboni kwa Sabrina. Wakaanza
kusikia mapigo yao ya moyo. Yalisikika vizuri sana. “Naona hawa watakuwa
wakimbiaji!” Jack akaongea macho kwenye screen. Wakacheka, Sabrina ametulia tu.
Wakawaonyesha wote wawili jinsi walivyolala. “Wanaonekana ni wazima kabisa. Mpo
tayari kujua jinsia?” “Kabisa.” Akajibu Jack, Sabrina kimya akiangalia tu.
“Haya, huyu wa kwanza niiii....” Akapitisha kile kitu tumboni kwa Sabrina
taratibu. Kisha akajua. “Huyu wa upande huu huyu ni wa kike.” Jack akacheka.
“Mwenzie?” Jack akauliza. “Na huyuuuu....” Akaendelea taratibu akitaka ageuke.
Akamsumbua mtoto huko tumboni mpaka akageuka. “Na huyu ni wa kike. Mjiandae
kupokea mahari hapa. Mnamapacha wa kike.” “Umesikia Brina? Mbona kimya mama?
Tuna warembo wawili. Ulinzi lazima uwe mkali.” Jack akaonekana kuchangamka
kuliko Sabrina.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Aliingia
kwenye gari akatulia kitini. “Naona neema ya Mungu imenishukia. Anataka nife
tajiri. Nikiozesha kila mmoja hapo kwa ng’ombe 30, 30! Mimi nitakuwa mtu
mwingine kabisa.” Ikabidi Sabrina acheke tu. “Mama, sisi ni watu wengine
kabisa!” “Nakuona ulivyofurahi.” “Hivi wewe umepaona pale nyumbani kwa kina
Pendo kulivyopoa?” Sabrina akajaribu kufikiria. “Wanakila kitu wale, kasoro
watoto. Wamehangaika, mpaka wanafikiria kwenda nje ya nchi kupandikiziwa. Sasa
leo Mungu ametupa wawili kwa mpigo! Acha masihara mama. Kama wewe hujafurahi,
acha mimi nifurahie.” Akaweka mziki, ukaanza kuimba na yeye akiimba. Sabrina
anamsikiliza huku akicheka.
Wakaendesha
mpaka nyumbani kwa Sabina. Kabla hawajashuka garini, akampigia simu dereva
aliyemtuma vyakula vyakumpelekea bibi yake Sabrina. Akamwambia anamalizia. Ampe
kama nusu saa. “Naomba usinicheleweshe Awali bwana!
Nina mambo mengi.” “Nakuja bosi wangu. Mama alinituma pia.” “Sasa niambie
ukweli. Umeshaanza kununua au bado?”
Awali dereva wa Misndai akaanza kubabaika. Jack akajua hajanunua. “Unajua nini? Acha tu, nitanunua mwenyewe. Endelea na shuguli
zako kama umetumwa. Sihitaji tena ununue chochote. Sasa hivi naelekea sokoni
mwenyewe.” “Acha kukasirika Jack. Nitajitahi..” Jack akakata simu. Sabrina akabaki akimtizama. “Nini?” “Naomba
usikasirike Jack. Tuwachukue kina mama hapa, tusimame pale sokoni. Tununue hivi
vitu, twende.” “Amenichelewesha na kuniharibia utaratibu mzima!” Akalalamika
Jack. “Haitachukua muda mrefu. Naomba utulie. Wewe sasa hivi ulikuwa ukiimba
hapa, usiruhusu hasira bwana.” Jack akacheka. “Muone. Wewe unataka kufanya
jambo zuri, liwe baya! Zawadi ni jambo zuri, ukianza kuonyesha ni kazi nzito kupata,
inakosa maana. Tukiona tunachelewa, tutampa bibi pesa, tuachane na vyakula. Kwa
hiyo tulia.” Jack akatulia.
“Sasa
majina ya watoto?” Sabrina akacheka na kushuka garini. Jack akashuka kwa haraka
na kumkimbilia. “Nipe basi hata busu lakunituliza. Si umeona pale kwenye gari
nilishaanza kukasirika?” Sabrina akacheka sana. “Mimi nahisi naongezewa watoto
niwe nao watatu. Haki kweli! Ni nini Jack?” “Nikukumbatie tu, nikubusu. Yule
jamaa alivyokuwa anapitisha kile kitu tumboni kwako akiangalia watoto pale
hospitalini nikawa nameza mate, nikasema ndio ingekuwa mimi pale!” Sabrina
akashangaa sana. “Hivi ujue wewe Jack unahitaji msaada wewe!” Jack akaanza
kucheka. “Ulikuwa uchi Brina!” “Ni tumbo tu ndio lilikuwa wazi Jack!” “Sasa
mwenzio sikuishia tumboni.” Sabrina alicheka mpaka akainama.
“Mimi pale nikajua mwenzangu unaangalia watoto kumbe wala haupo pale!” “Kwa taarifa yako vyote viliendelea kwa wakati mmoja.” Sabrina alicheka na kubaki haamini. Mlango ukafunguliwa. “Karibu maharusi.” Alikuwa Sabina. “Kumbe bado sisi ni maharusi! Umesikia Sabrina?” “Naomba tuingie ndani Jack. Acha kabisa.” Akamvuta mkono, Sabina akawapisha mlangoni. Wakawakuta wazazi wapo tayari. Wakasalimia. “Mimi naona kama nyinyi mpo tayari, twendeni wala tusikae.” “Hamtakunywa hata chai!?” Akauliza Sabina kwa kulalamika. “Naomba iwe siku nyingine shemeji yangu. Muda umetubana haswa. Jumatatu natakiwa kazini. Lazima kesho tuondoke.” Sabina akabaki ameshangaa. Sabrina akacheka tu. “Tunashukuru sana shemeji. Ila naahidi tutakuja tena siku nyingine. Sasa hivi naomba twendeni tu. Sisi tulishapata kifungua kinywa. Na Pendo naye amemfungashia huyu vitu vya kula siku nzima. Hapo alikuwa anakula matunda kwenye gari, hata hajamaliza. Tutakuja siku nyingine, tukae kabisa.” Wakatoka.
Safari ya
Bagamoyo.
“Baba
wewe kaa mbele na dereva wangu.” Sabrina akatoa wazo. Jack akamgeukia Sabrina
akiwa amekunja uso. “Kaa na baba mbele Jack. Mimi nitakaa hapo nyuma yako.” “Au
ukae tu na mwenzio mbele?” Baba yake akaongea kwa kujihami. “Atakuwa sawa tu.
Wewe kaa mbele baba, usibanane nyuma na kina Sabina.” Sabrina akamshika mkono
Jack aliyekuwa ameduaa, akamvuta mpaka upande wa dereva. “Sabrina!” Jack
akanong’ona kama ambaye hajaridhika. “Bwana twende.” Sabrina akamfungulia
mlango, yeye akapanda kiti cha nyuma. Jack akaingia na kucheka kidogo.
“Unacheka nini sasa? Twende.” Sabrina akamuwekea msisitizo. “Naomba mfunge
mikanda tafadhali, ndio tuondoke.” Jack akaomba kwa heshima huku anatuma
ujumbe. “Nahisi utakuwa na ujumbe Sabrina.” Sabrina akacheka akijua Jack
mwenyewe ndiye aliyemtumia.
Wakafika
sokoni, hapakuwa mbali na anapoishi Sabina. “Tutashuka hapa sokoni kidogo.
Hatutachelewa, ndipo tuendelee na safari.” Jack akawataarifu abiria zake wakati
anaegesha gari. Wote wakaitika. “Twende Brina.” “Hamtahitaji msaada?” Akauliza
baba yake Sabrina. “Hapana Mzee wangu. Nitaomba vijana hapo nje watabeba tu,
usijichafue.” Sabrina akashuka. Wakaona wanacheka nje. “Huyu kijana anaonekana
anampenda sana Sabrina.” “Baba anarudia hilo kila wakati!” Sabina akaingilia. “Ni
kweli.” Wakatulia.
Baada
ya muda wakaona Sabrina anarudi na vijana wakiwa wamebeba mizigo. Akawafungulia
nyuma. Wakaanza kuingiza mizigo hapo, wote wakiwa wamegeuka. “Bibi yako
atafurahi sana Sabrina. Asante kumkumbuka na yeye.” Sabrina akacheka tu. Jack
naye akaja na mizigo mingine na vijana wawili. “Naona hapatakuwa na sehemu
nyingine Jack. Inatosha. Tutamwachia pesa ajinunulie huko. Twende tuwahi
kurudi.” “Naona wazo zuri.” Jack akawalipa wale vijana wakaondoka.
Wakati
wanapanda kwenye gari, wakagundua baba yao amerudi kukaa nyuma. “Ungekaa tu
mbele baba.” “Wewe kaa na mwenzio. Kwanza itakusaidia kujinyoosha.” “Nashukuru
baba. Anahitaji kujinyoosha mgongo huyo.” Jack akaingilia haraka sana, Sabrina
akabaki ameshangaa. “Njoo sasa.” Jack akamuita. Sabrina akacheka kidogo na kutingisha
kichwa, Jack akacheka. “Njoo bwana!” Sabrina akaenda. Akamfungulia mlango,
Sabrina akapanda akiwa amemsimamia palepale mlangoni. Akaanza kumtengenezea
kiti. “Hapo vipi?” “Umelaza sana bwana Jack!” “Haya, Nishike mkono unyanyuke
kidogo, nikinyanyue tena kidogo.” Akaendelea kumuwekea, abiria wao
wakiwaangalia kwa kujiiba. Sabrina aliporidhika. Jack akambusu mdomoni,
akafunga mlango. Na yeye akapanda.
“Bibi yenu atafurahia sana hizo zawadi
mnazompelekea.” Akavunja ukimya mama Sabina. Sabrina na Jack wakaangaliana. Jack
hakujua aseme nini akabaki kimya, Sabrina akamuona anakunja uso. Akacheka. “Wewe
ongea chochote bwana. Hakuna kitu sahihi. Ukoje Jack?” Akacheka na kunyamaza. Mara
simu yake ikaita. Ikawa kama ameokolewa na hiyo simu. Alifurahi Jack mpaka
Sabrina akaanza kucheka. Abiria wa nyuma wakiwatizama. “Ndio vizuri akapafahamu
kwa bibi. Si ndio Jack?” “Kabisa.” Akaongeza Jack na kupokea simu kwa haraka
kama ambaye hajui azungumze nini na hao ndugu zake Sabrina.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Kwa hiyo mtakuja nyumbani usiku?”
Jack akanyamaza. “Nitakupikia chakula chako
unachokipenda.” Mama yake akaendelea kumbembeleza, Jack kimya kama
ambaye bado amekasirika. Sabrina akampiga ngumi begani kumshitua. “Auuu! Sasa sijui tunarudi saa ngapi! Na kesho tunaondoka
asubuhi sana, jumatatu nataka nirudi kazini ili nibakishe siku za likizo.
Nizitumie Sabrina akijifungua.” Jack akajibu kisha akahamasika kama
aliyekumbuka kitu. “Kwanza nimejua jinsia ya watoto
wangu.” Hapo akaanza kucheka, mpaka Sabrina akacheka. “Ni jinsia gani?” “Labda nikwambie majina.” Sabrina
akashangaa na kumgeukia.
“Mkubwa ataina Jeiline Msindai, mdogo wake ataitwa Keiline Msindai.
Upo hapo mama Msindai.” Akamsikia mama yake akicheka. “Hongereni. Sabrina anasikia?” “Nasikia mama. Asante.”
Sabrina akajibu akicheka. “Hongera sana mama. Sasa baby
shower lini?” “Hapana mama. Naomba msianze jamani! Huyu Sabrina mlimchukua
karibu siku kumi!” “Ni nane tu.” Mama yake akamrekebisha. “Ndio hizohizo tu hakuna tofauti yeyote ile. Ndio tumeoana tu
mnataka tena habari nyingine! Hapana mama. Acha na mimi nikatulie na mke wangu.
Heee! Shuguli haziishi!” Sabrina na mama Msindai wakaendelea kucheka.
“Wewe bado unalalamikia siku 8 zilizopita lini sijui! Hii shower
itawasaidia kupata vitu vingi vya watoto.” “Hapana bwana mama. Nyinyi mnapenda
shuguli bila kufikiria. Hapa tulipo kwenyewe hatujui tunaweka wapi hizo zawadi
za harusi, leo mnataka kuongeza nyingine za watoto sijui! Nyumba yetu sio kubwa
bwana. Acheni kuweka mipango yakujaza kupita kiasi.”
Jack akaendelea kulalamika.
“Nisikilize Sabrina. Watoto wawili wanakuja na garama za diaper na
baby wipes. Hela zitakuwa zinawaishia mchana na usiku.” “Hapana bwana mama,
acha kumtisha Sabrina. Hatuwezi kushindwa kununua diaper.” “Wewe Sabrina
usimsikilize Jack. Kubali wifi zako na Pendo wakuandalie baby shower nzuri
upate zawadi nzuri. Watakaa chini, watakuandikia orodha nzuri ya vitu muhimu
vitakavyohitajika vya watoto, kisha wagawane wao wenyewe na marafiki zetu.
Halafu mimi mwenyewe nitakodi gari viletwe huko. Hutakuwa na haja yakununua
vitu vya watoto au hata nguo za miezi ya mwanzoni. Sasa wewe umsikilize Jack,
wakati huyo hajui hata vitu vya watoto! Utahangaika mwenyewe. Mimi nataka
upumzike. Ufikirie kubeba tu. Mahitaji mengine acha watu wakusaidie.”
Sabrina akaanza kushawishika.
“Basi ngoja nizungumze na Jack, halafu nitakwambia.” “Umemshawishi
mke wangu mpaka amelainika! Sijui ukoje mama!”
Sabrina na mama Msindai wakazidi kucheka. “Mwenzio
ameona umuhimu wake tayari. Wewe kwa kuwa umekasirika tokea asubuhi ndio maana
kila kitu unanikatalia wakati yote nayafanya kwa ajili yako! Zawadi ni zenu.
Nia yangu ziwafikie zikiwa salama, na bado unakasirika!” “Nia nzuri lakini
hapakuwa na kipaumbele mama. Mimi niliwapa maagizo vizuri tu. Nashangaa mpaka
saa nne hamna vitu nilivyoagiza!” “Lakini si yameisha baba? Tupange mambo
mengine?” “Mipango yako yakulazimisha bwana mama! Unachotaka nikumchukua mke
wangu mje mumfanyie sherehe. Kwa nini msikusanye hivyo vitu bila yeye kuwepo?” “Sasa
raha ya uzazi ataipata wapi mwenzio? Acha watu waje wampongeze, wamfurahie na
yeye ajisikie vizuri.” Mama Msindai akaendelea.
“Mama Msindai siasa mpaka kwa mkwe!”
Wote wakaanza kucheka mpaka ndugu wa Sabrina. “Umeuza
agenda yako mpaka namuona Sabrina amekubali wala si kutaka tuzungumze tena!”
“Sio sasa hivi. Wewe nenda kapumzike na mkeo mpaka karibu kabisa na kujifungua,
akiwa anakuja kujifungua huku ndio...” “Hapana mama, naomba usianze tena.” “Sio
mimi! Ni baba yako.” “Hapana. Nimemwambia baba nitafikiria. Na ninaomba usianze
kulazimishia mama. Huko Singida kuna mapacha wengi
tu wanazaliwa kila leo. Sabrina atakuwa sawa hata akijifungulia Singida.”
“Jack...” “Kwa heri mama. Nakujua wewe. Hilo nalo ukilibebea bango, najua
utamtia hofu Sabrina mpaka akimbilie Dar kujifungua, wakati mimi nipo Singida.”
“Si umesema una siku za likizo wewe?” “Mama Msindai kwaheri. Mimi nakujua wewe
ukitaka jambo lako. Mwishoe nitajikuta naishi Singida, nyinyi ndio mnakaa na
mke wangu huku Dar. Hapana mama, kwaheri.” Sabrina na mama Msindai
wakaendelea kucheka.
“Basi baba. Tutaongea vizuri mkija kwa chakula cha usiku.” “Ona mama
jamani! Kwa nini wewe huwa hujui jibu la hapana? Nimekwambia sijui tunarudi saa
ngapi kutoka Bagamoyo! Naomba usipange mipango yakutuhusisha na sisi.” “Ndizi
za nazi nyingi na samaki!” Jack akaanza kucheka
mwenyewe. “Tena sijui niongeze na lile pilau la
Zanzibari? Niliweke minofu mingiii!” Mama Msindai alifanya gari zima
wacheke. Jack alishalainika na yeye. “Mimi naona niwapikie vyote. Au unasemaje Jack mwanangu?”
“Lakini hatutakaa sana!” Mpaka mama yake akacheka kwa sauti. “Bwana ndizi zako tamu bwana na nimejua kwa nini hukuzipika
jana, ilikuwa kusudi ili nirudi leo.” “Hapana. Ni ndugu zako wenyewe waliamua
kuleta vyakula, na mimi ndio nikaona nipumzike. Wewe acha kufikiria mambo ya
nyuma. Njooni jioni mle vizuri, tuagane kwa amani ndio muondoke.” “Utataka tena
na kesho asubuhi tuje tule pamoja kabla ya kwenda uwanja wa ndege?” “Kwani
itachukua muda gani!?” Mama Msindai akauliza kishawishi. “Si umemsikia mama? Basi ujue hatutakaa tukaondoka hapa Dar.
Mama Msindai kwaheri.” Sabrina akazidi kucheka. Jack akakata mama yake
akisikika akiendelea kucheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Wewe
muendekeze mama Msindai! Raha yake ni kutuona hapa kila wakati. Hata tukienda
kwa chakula cha asubuhi, atataka tukae naye mpaka cha usiku ndio tuondoke.”
Sabrina akacheka. “Anakupenda.” Akaongeza mama Sabina. “Sana. Unafikiri hilo
lina ubishi mama yangu! Tatizo lake ni akitaka jambo lake, lazima liwe. Na
akiona hajapanga hoja zake vizuri ukakubali, hana shida ya kukufuata ulipo
akuweke sawa mpaka ukubali.” Wote wakacheka.
“Yaani
hilo la baby shower kwa jinsi nilivyomsikia hapa, hiyo itafanyika tu. Unaweza
kukuta anasafari ya Singida jumamosi ili kumuweka sawa Sabrina.” “Haiwezekani
Jack!” “Sikutanii. Muulize Jacinta ambaye yeye ni mbishi kidogo. Huwa anamfuata
mpaka ofisini kwenye vikao mpaka Jacinta aseme ‘ndiyo’. Akikataa, hana haraka
wala jazba. Atatafuta tena muda ambao anajua upo na mambo mengi, anakufuata
tena. Sasa na wewe si utachoka, lazima umkubalie tu.” Wakaendelea kucheka,
angalau wakapata kitu chakuzungumza hapo.
“Kwa
hiyo honeymoon mlikwenda wapi?” Akauliza Sabina na kufanya waangaliane na
kucheka. “Sabrina alipapenda huko! Nilijua atakataa kuondoka.” “Jackson wewe!
Sio wewe ndio ulikuwa hutaki kuondoka?” Wakacheka. “Ni Afrika ya kusini. Kwenye
kona kabisa ya bara. Huo mji umeingia baharini. Unaitwa Cape point. Walikwenda
huko Pendo na mumewe kwenye honeymoon yao. Wakapapenda, ndio wakaona na sisi
twende. Nipazuri sana kwakweli. Kuna utulivu wa namna yake. Mipango inapangika,
sema majina ya watoto ndio yaligoma.” Sabrina akacheka.
“Lakini
nimesikia ukimwambia mama yako. Ni mazuri sana.” Sabina akasifia. “Sasa sijui
kama bibi ataweza kuyatamka!” Sabrina akafanya wote wacheke. Walicheka sana
huku wakimfikiria na kusema utundu wa bibi yao. “Umesema nani tena?” akauliza
baba yao. “Jeiline na Keiline. Mabinti wa Msindai.” Jack akaongea kwa kujivuna.
“Upo mama Msindai?” “Nakusikiza Jack. Naona majina yangu umeyakataa!” “Majina
yako yale yakiutuuzima! Yaani unamuita mtoto utafikiri unamwita kibibi kizee!” Wote
wakacheka. “Kwani alitaka kuwaitaje?” “Wala usitake kujua shemeji. Mtaishia
kulala bure! Majina yenyewe mazito!” wakazidi kucheka. “Wewe bakiwa na Jeiline
dada mkubwa, mdogo Keiline. Basi.” Wakaendelea kucheka njiani angalau
pakatulia. Kila wakati walimuona Jack akimkumbusha Sabrina ale hiki na kile na
kutaka kujua kama yupo sawa. Wakaendelea kukonyezana huko nyuma, mpaka wakafika
kwa bibi yao.
Furaha
aliyokuwa nayo huyo bibi, mpaka Jack akafurahia kufika huko. Aliita rafiki zake
kuja kumuona mume wake ambaye ni Jack. Jack alikuwa akicheka kila wakati. Zawadi
walizozileta, vyakula, bibi huyo aliimba kwa kutaja kwa jina akimshukuru kwa
kimoja hadi kingine. Ilipofika saa kumi jioni Jack akaomba waondoke.
Palipo Na
Amani, Uharibifu Nao Hunyemelea.
K |
itendo
chakumuona Sabrina kwenye harusi kubwa vile, iliyohudhuriwa na wakubwa wa nchi!
Ukumbi wa thamani, kila kitu kilikuwa cha thamani na kutangazwa kuwa ule ni
usiku wa Sabrina akiwa amepambwa kwa maneno mazito yaliyojaa sifa! Viapo vizito
kanisani! Wakionekana ni kama waliojuana na Jack kwa muda mrefu! Ikazidi
kumsumbua mkewe Max na kama wivu ukamuingia tena na Max mwenyewe. “Huyu Sabrina
aliondoka hapa akisema anampenda sana Tino!”
Ikashindwa kuingia akili mwa mama Kundi. “Nakumbuka uliniambia
ulimuuliza kabisa Sabrina kama kweli anampenda Tino kwa dhati!” Mama Kundi akaongeza akisikika mawazoni akijaribu kuvuta
kumbukumbu ya picha ya Sabrina na Tino aliowakarimu nyumbani kwake, na huyu
Sabrina aliyekuwa bibi harusi wa Msindai! Max kimya.
“Eti
Max?” “Alikiri kumpenda sana Tino.” Max akajibu. “Sasa haya mapenzi ya kwa
mtoto wa Msindai mpaka kuolewa harusi kubwa hivyo, ni nini kinaendelea kwa huyu
binti au ni tapeli huyu Sabrina?” Hapo Max akawa amepewa njia rahisi ya
kutokea. “Ni tapeli tu. Alikuwa akitafuta pakuponea. Alipoona kwa Tino habari
ndefu, kesi haziishi, mkewe kaja juu, akamtelekeza mwenzie.” Akajibu Max kwa haraka na kuongeza. “Na ndio
maana Tino aliporudi hakutaka tena mumzungumzie naye Sabrina, akakwambia uache
tu. Si nakumbuka mwenyewe?” Max akamuuliza mkewe. “Na kumbuka. Maana mimi
niliwaaga hapa vizuri kuwa wanakwenda anza upya. Tino akaonekana safari hii
Mungu amemkumbuka, na yeye amepata mtu wake wakumfuta machozi! Kumbe ni
yaleyale tu! Sijui Tino huwa anakosea wapi kwa hawa wanawake! Sabrina
alionekana ni mtu anayemjali sana, si kama tapeli! Sijui ni nini kilitokea
jamani!” Bado mama Kundi akashindwa kumuweka Sabrina kwenye kundi la Matapeli.
Kwa jinsi alivyomuona na Tino, moyo wake ukakataa kabisa kumuweka kuwa tapeli.
“Mimi nitazungumza tena na Tino kujua ni nini kilitokea.” “Acha bwana.
Hayatuhusu.” Max akahamaki haswa. “Tino anatuhusu Max. Anatuheshimu sana yule
kijana. Na sisi anatuhesabu kama ndugu zake tuliobaki hapa nchini. Kweli
unataka aje asikie kutoka kwa mtu baki tu? Hapana kwakweli. Akipiga kusalimia,
nitaanzisha hii topic.” “Basi acha mimi nizungumze naye.” Max akaona bora yeye
azungumze na Tino, mkewe asije tibua mambo.
Kwa Tino.
Kipindi
hicho yote hayo yanaendelea nchini Tanzania, Tino alikuwa nchini Italy kwa
ndugu upande wa mama yake. Mengi yalimfanya akakimbilia huko. Lakini pia alikutana
na matibabu mazuri yaliyochangia kuendelea kubaki kwake huko ili kuona kama
watasaidia uponyaji wa huo mkono wake wa kulia. Na kweli, kwa muda mfupi
aliokuwepo huko akifanyiwa matibabu, aliweza kurudisha asilimia 87 za uwezo
wake wa zamani. Walianza kumfanyia mazoezi yaliyomfurahisha zaidi. Mazoezi ya kushika
vifaa vyake vya uchoraji. Akaanza upya kama anayejifunza mwanzo kabisa wa
uchoraji. Muda huo yuko huko, akaamua kuanza masomo ya muda mfupi mfupi kupatia
kipaji chake leseni za kimataifa na akaamua kujifunza lugha ya kiitaliaono pia.
Uzuri upande wa mama yake walikuwa na uwezo kiuchumi, na Tino hakukulia huko,
kwa hiyo wakajisikia kuwajibika kumsaidia kwa mara ya kwanza akiwalilia shida.
Asidi na
Asili Yake.
M |
ax
akampigia Tino. “Kwema huko kaka au kuna jingine tena?”
“Jumamosi ile iliyopita tulihudhuria harusi ya kijana wa Msindai.” “Yule
waziri?” Akauliza Tino. “Hapana bwana. Yule waziri ni bosi wa shemeji yako, yeye waziri
Msindai ana mke na watoto watatu. Yule mama Msindai mwenyewe aliyekuwa waziri
awamu ya Mkapa, ana watoto wanne. Wakwanza na wa mwisho ni wakiume. Sasa huyo
mdogo ndiye aliyekuwa akioa.” Tino akawa hajaelewa kwa nini yeye aambiwe
yote hayo. Akaamua anyamaze asikilize. “Sasa bibi
harusi ndiye ametuacha mdomo wazi na ndio kisa chakukupigia!” Tino
akashangaa kidogo, ikabidi kuuliza. “Ni nani?” “Sabrina!”
Pakazuka ukimya wa hali ya juu. Mpaka Max akaangalia simu. “Tino?” Akaamua kumuita ili kuhakikisha kama bado yupo
naye. “Anaitwa Jack?” Tino akauliza. “Kumbe unamfahamu!?” Kidogo Max akashituka. “Nilimfahamu Jack kwa jina moja tu, tena kwa kupitia Sabrina
mwenyewe tokea mwanzo kabisa naishi na Sabrina hapo Dar. Sikumjua kama ni
Msindai!” Tino alisikika akiwa ameishiwa nguvu asiamini kama Sabrina
alikuwa tayari kumuacha Jackson Msindai ili awe na yeye! Kidogo wasiwasi
ukaanza kumuingia.
“Bwana yule mtoto sijui analoga vipi wanaume! Yaani kwa muda mfupi
sana kumuingiza yule kijana kwenye mstari mpaka kapagawa! Kijana wa Msindai
amechanganyikiwa kabisa! Amekusanya mawaziri wa awamu ya tatu ambao walikuwa wakifanya
kazi na mama yake pamoja na viongozi sasa wa awamu hii wanaofanya kazi na Waziri
Msindai huyu wa sasa. Kulikuwa na ulinzi, bila kadi huingii hata kanisani!
Yaani kanisa lilifungwa kwa ajili hiyo tu. Sijaona watoto wa mtaani pale au
kijiweni. Watu wazito watupu na wakatangaza eti ile ilikuwa ni siku ya Sabrina.
Bwana Jack alimpamba Sabrina! Hicho kiapo alichomuapia Sabrina, mawaziri mwenyewe
walisimama wakati Jack anatoa kiapo chake kanisani. Ikabidi na wengine pia
tusimame tu, dogo! Kilikuwa kizito kisichopimika kikawaida. Nikajua wazi na
yeye yule mtoto wa Msindai kashawekwa sawa. Amelogwa, hajitambui anachofanya. Sabrina
amempika, mpaka akapikika.” Tino kimya.
“Si kawaida aisee! Yaani mpaka sasa shemeji yako haiingii akilini.
Hata kama ni mapenzi, si kuchanganywa kwa aina ile! Maana si mlikuwa naye hata
miezi sita haijaisha? Sasa iweje kijana akolezwe na mwanamke kama Sabrina!? Eti
walipoingia tu ukumbini, eti wakatangaza watu wasikilize wimbo wa Jack kwa
mkewe! Sasa wimbo wenyewe ndio utachoka. Ni ule wa Perfect! Mimi pale ndio nikachorea mstari na kusema huyu kijana wa Msindai kafunikwa
kabisa, hajui nini anazungumza. Na mbaya zaidi mbele ya wasomi tunaojua maana
ya maneno wa ule wimbo bwana!” Max akaendelea kama
anayesoma ngonjera. Tino kimya akisikiliza.
“Eti mapenzi yao yalianza
zamani tokea watoto! Si ‘juju’ hiyo au
nini?” Max akauliza asijue Tino
yupo mbali sana. Amerudi mbali mno. “Huku ishakuwa
usiku sana kaka. Tutazungumza wakati mwingine. Lakini ni kweli, Jack hajakosea.
Alikuwepo kwenye maisha ya Sabrina hata kabla yangu. Na Sabrina alikataa mwaliko
wakumfuata Singida ili abaki na mimi kuniuguza. Kwa hiyo ni watu wa muda mrefu.
Ni kijana aliyekuwa akimfuatilia sana Sabrina tokea wapo chuoni.” Pakazuka
ukimya kwa Max. Tino akakata simu akiwa yupo kwenye hali mbaya asijue ni nini
anachojisikia kwa wakati huo. Simu ya Max ilimvuruga vibaya sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tino
alibakiwa na simu mkononi. Akakumbuka mwanzoni kabisa Sabrina kufika kwake na
kumsaidia, alimwambia aina ya maombi yake kwa Mungu. Kilio chake na matamanio
yake ambayo anamlilia Mungu ampe yeye. Akamwambia ni makubwa sana ambayo
hayaendani na jinsi alivyo. Ni kama ya wale wasichana warembo kabisa, lakini Tino
akakumbuka Sabrina kumwambia anayo imani kubwa sana kuwa Mungu atamfanyia na
yeye. “Au ndio ushirikina huo anaousema Max, sio Mungu?!” Sauti nyingine
ikamtahadharisha Tino, akatulia kidogo.
Lakini
akakumbuka jinsi alivyokuwa akimtia moyo kwa upendo kuwa na yeye ajipe moyo na
amwamini Mungu atamponya tu. “Angegusia hata swala la mganga kidogo!” Akajirudi
Tino, maana neno alilokuwa akilisikia kutoka kinywani mwa Sabrina ni Mungu kila
wakati, wala si kujaribu kumpeleka hata yeye kwa mganga ili apone! Akakumbuka
jinsi Sabrina alivyokuwa akijituma kwake akimwambia anafanya kwa uaminifu kama
akifanya kwa Mungu. Akijua Mungu anaangalia kila anachomfanyia yeye. Kwa mara
ya kwanza Tino akapata muda wakufikiria, akaingiwa hofu ya ajabu na kuweka simu
pembeni. “Iweje niwe nilijichanganya!?” Akajiuliza na kuogopa asije kuwa
alidanganywa, akaamini bila kufikiria akaishia kumtenda Sabrina kinyume na
alivyostahili. “Lakini Max hawezi kuwa alifika umbali wote huo kunidanganya!
Ili iweje?” Akajaribu kumtetea Max huku moyo ukisita kwa hofu akitamani
isiwe tofauti.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment