Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com MAKOSA! – SEHEMU YA 22. - Naomi Simulizi

MAKOSA! – SEHEMU YA 22.

Sabrina akabaki ametoa macho asiamini kama anaishi na Jack mwenye malalamiko kiasi hicho. Uzuri ni walipitia kula kabla yakwenda hospitalini. Akajua Jack ameondoka akiwa ameshiba, na yeye ameshiba. Akapanda kitandani akajinyoosha. Watoto wakaanza kucheza tena, ndipo akili ikaanza kumjia kwa nini tumbo limekuwa likikua kiharaka vile, na kwa nini wakianza kucheza inakuwa kama timu ya mpira inashindana tumboni kwake. Akakaa pale akiwasikiliza hao watoto wawili huko tumboni. Akajua Jack angekuwepo angefurahia sana. Akajiambia lazima atengeneze na Jack. Akaamua ampigie tu.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ikaita mara mbili akapokea. “Nimeomba ufikirie unipe jibu Brina. Naomba usiharakishe.” “Sihitaji kufikiria Jack. Kwa kuwa sina chakufikiria. Nilipaniki mpenzi wangu. Nilipaniki kusikia ni watoto wawili. Nikahisi kama giza na nikaona kama utalemewa na watu watakusema zaidi. Najua umekasirika Jack, lakini nakuomba unifikirie na mimi ni binadamu. Kuna sehemu, nawakati naingiwa hofu sana. Huwezi amini jinsi ninavyojilaumu nakutamani kurudisha siku nyuma mpaka siku nilipoenda kumsaidia Tino, niwe nimekuja huku halafu nikosee na wewe, sio yeye. Huyo mtu hayupo mawazoni kwangu kinamna hiyo, nimpaka mtoto aanze kucheza. Unanielewa Jack?” Sabrina akauliza maana Jack alikuwa kimya kabisa.

“Kwa hiyo unachotaka kuniambia kila hao watoto watakapokuwa wakicheza, utakuwa unamkumbuka Tino?” Sabrina akafunga macho, akajua siku hiyo ni yakuteleza maneno. “Sasa hivi walikuwa wakicheza hapa, nikakukumbuka wewe mpenzi wangu. Nikasema Jack wangu angekuwepo, angefurahia. Na ndio maana nikakupigia.” “Unanidanganya Brina.” Akajilalamisha Jack. “Hakuna kiumbe anayenipenda hapa duniani kama wewe Jack. Na mimi si mjinga. Nishafanya kosa, siwezi kurudia kosa. Leo umenithibitishia kwa umbali mkubwa sana kuwa mimi na hawa watoto ni wako. Sasa hivi wala siogopi tena.” Kimya.

“Jack?” Kimya. “Njoo basi mpenzi wangu. Najua nikikushika utatulia. Najua nimekushitua, lakini umepokea ujumbe tofauti, kipenzi changu. Sikuwa na maana uliyofikiria wewe au anayotaka kuitumia shetani kutugombanisha mimi na wewe.” “Sasa nikirudi utanishika tu au utanituliza kidogo? Maana mimi hali mbaya Brina.” “Kuanzia leo tunaishi kama tulivyokabidhiwa siku ya mahari.” “Usinidanganye Brina!”  “Kweli. Mimi si mkeo?” “Ndio mimi nikashangaa, baada ya juhudi zote zile alizofanya baba yangu mpaka kukutoa pale hadharani, na kukulipia tena zaidi, tunatoka pale, baba anajua ameniolea mke! Kila akipiga anauliza mkeo hajambo, kumbe hajui huku nyuma umenigeuka.” Sabrina akaanza kucheka moyoni. Jack alilalamika kama mtoto mdogo.

“Njoo mpenzi wangu. Kuanzia leo tunaishi kwa kuzungumza, hamna kubeba vitu moyoni.” “Kama ndio hivyo basi acha mimi nianze. Wewe ni mke wangu Brina, lakini hunitaki.” Sabrina akashindwa kujizuia akaanza kucheka. “Usicheke bwana.” “Njoo Jack wangu. Mimi mwenyewe nina hamu na wewe, nakaribia kuchanganyikiwa. Hapa nishaanza kutoa nguo.” “Utanifanya nipate ajali Brina. Natafuta sehemu nigeuze gari.” “Taratibu bwana. Sasa unataka unikute wapi? Hapa au chumbani kwako?” “Ukienda kule kwangu ndio nitajua umeamua kabisa.” “Sawa. Utanikuta nikikusubiri.” “Nakushukuru Mungu wangu. Acha nipige simu kazini niwaambia leo siendi, nalala na mke wangu.” Sabrina akacheka na kukata simu.

Aluta Kontinua.

S

iku hiyo akaamua amtulize Jack haswa. Akahamia chumbani kwa Jack na akaoga hukohuko bafuni kwake. Wakati anamalizia, akamsikia Jack ameingia. Akacheka. “Na mimi nije?” “Subiri kwanza nakuja kukupa sababu yakuoga.” Jack akashangilia sana. Sabrina akatoka na tumbo lake akiwa amejikausha. Mchana huo jua kweupe nje, wawili hao wakaanza mapenzi ya kiu. “Asante Brina.” Jack alishukuru huku akiendelea kufaidi penzi. Akashangaa Sabrina ndio akaonyesha uchu kumzidi yeye. Jack hakumuelewa. Aliendelea kumng’ang’ania hapo kitandani mpaka akaridhika yeye na kujitupa pembeni. Jack akashangaa amepotelea usingizini. Akamfunika vizuri na kurudi kumkumbatia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wawili hao maisha yakaanza upya yakichukua picha ya mke na mume. Jack akasaidia kuhamisha mizigo ya Sabrina chumbani kwake. Akampisha kwenye sehemu ya makabati, angalau Sabrina naye akapata nafasi. Akapanga mizigo yake hapo. Maisha yakaendelea kwa wawili hao. Jack akiwa ametulia, hamna tena hasira. Anapata penzi muda na wakati wowote anaotaka, tena Sabrina mwenyewe ndio akaonyesha uhitaji zaidi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Sabrina akashangaa siku hiyo jioni akipika, Sabina anampigia. “Kwema!?” “Mbona unashituka? Nataka kukusalimia tu.” Sabrina akacheka. “Nashukuru dada yangu. Sijazoea kupata simu kutoka kwenu za salamu. Itabidi kuanza kujifunza.” “Sasa mbona na wewe mwenyewe hata huwa hupigi?” “Da Sabina! Napiga nakwambia nini? Naanzia wapi wakati hatukuwahi kuwa na huo utaratibu na wewe wakati wote ulikuwa ukilalamika upo busy!? Naogopa kukusumbua.” Sabina akatulia kidogo. 

“Unaendeleaje lakini?” Sabrina akauliza. “Vizuri tu. Mbali na salamu pia nilitaka nikukaribishe kipindi cha harusi ushukie kwangu.” Sabrina akanyamaza. “Hata wakina mama watakuwa hapa kwangu. Ndio nikaona angalau na wewe utokee hapa. Naona kama itakuwa heshima zaidi! Ndugu wa mke na bibi harusi tunatokea sehemu moja.” “Wazo zuri, lakini nahisi kama tumechelewa.” “Kwa nini?” Sabina akauliza akisikika kuishiwa nguvu kabisa. “Familia ya kina Jack waliweka mipango tayari. Nafikiri Jack aliwaambia huwa nakuwa nashuguli nyingi sana nikiwa huku. Hivi hii jumamosi nitakuwa huko, kushugulikia maswala ya gauni.” “Basi shukia kwangu.” “Nitakuwa na Jack hotelini.” Sabina akanyamaza.

“Natamani kama ningejua mapema.” “Kwa hiyo nani atakusaidia kutafuta hilo gauni?” Sabina akauliza. “Huyo dada anayenisimamia, mama yake Jack na dada yake mkubwa atakuwepo. Nikikamilisha maswala ya gauni, mama yake Jack alitaka nitulie hapo Dar mpaka siku ya harusi nyumbani kwa huyo dada na mume wake wanaotusimamia harusi, lakini Jack amekataa. Anataka nirudi naye hiyo jumapili. Amelalamika anasema week mbili ni nyingi sana. Labda siku tatu. Sasa nilimsikia hapa jana akibishana na mama yake. Mama yake akimwambia nilazima niende Dar week mbili kabla ya harusi ili nipate muda wa matayarisho na kupumzika. Akamwambia sehemu ilishandaliwa. Napo Jack ni kama alikataa, mama yake akaishia kusema ni lazima niende nikapumzike japo hata kwa siku 8 kabla ya harusi. Sasa sijui nitakuja lini huko, ila najua sehemu ilishaandaliwa tayari na kuna mipango kabisa.” “Mmmh! Basi mwaya.” Sabina akaongea kwa kusikitika.

“Lakini nashukuru sana kwa kujali dada yangu. Nashukuru.” “Basi nikuombe kitu Sabrina.” “Karibu.” Sabrina akajibu kwa unyenyekevu tu. “Mimi najua haukuwa na mahusiano mazuri na watu wa humu ndani, yaani sisi kwa ujumla, lakini kumbuka bado sisi ni ndugu zako.” “Sawa dada.” Sabrina hakutaka ubishi. Akakubali. “Yapo makosa ulitendewa hapa nyumbani. Lakini kama ulivyoona, wazazi walijirudi Sabrina. Umewaletea heshima. Wewe ndio wakwanza pale ndani kuolewa. Hapajawahi kufanyika harusi, harusi yako ndio ya kwanza. Usiwanyime hiyo furaha.” Sabrina akatafuta mahali akakaa.

“Labda sijaelewa! Nilitakiwa kufanya nini ambacho sijakifanya kwenye hii familia jamani!?” Sabrina akaanza taratibu tu. “Sitaki tukosane Sabrina. Mimi nilikuwa natoa tu ushauri.” “Sawa kabisa. Ndio nauliza safari hii nilitakiwa kufanya nini tena? Maana niliacha shuguli nzima ya mahari yangu mikononi mwenu, tena nikiomba muiongoze mtakavyo nyinyi mpaka tukafanikiwa. Mimi na Jack hatutaki kitu kingine zaidi ya harusi ambayo inaandaliwa na kina Msindai. Sasa mimi nilitakiwa kufanya nini? Tafadhali niambie tu pale nilipotakiwa kufanya, sikufanya nione kama nitaweza kurekebisha.” Sabrina akaongea kwa kulalamika.

“Mimi sijui, ila nimeongea tu.” “Hapana. Lazima unalo wazo ndio maana umeongea hivyo. Naomba uongee tu. Mimi nitasikiliza.” Kimya. “Da Sabina?” Sabrina akaita. “Mimi naona si sawa wewe kutokea ukweni kuelekea harusini. Mambo yako ya harusi, tulitakiwa sisi ndio tukuandalie.” “Unaposema sisi ndio kina nani dada yangu? Nani ambaye ashawahi kuwa tayari hapo nyumbani kushugulikia mambo yangu bila malalamiko, na kusema nimezidi matatizo? Ambaye leo amenipa msaada nikasema hapana, sihitaji msaada wako, ninaye mtu wakunisaidia? Naomba uwe mkweli dada. Niwakatalie kina Msindai leo, halafu iweje?” Kimya.

“Hivi unajua nimekaa hapo Dar kwa muda gani nikihangaika bila mtu hata mmoja wenu kunitafuta kujua nipo wapi na ninaendeleaje?” Kimya. “Kaka yupo mzima na kazi yake. Wewe upo hapohapo mjini. Mama na baba wapo Chalinze. Nimeondoka nyumbani zaidi ya miezi minne, sijakuta ujumbe hata wa mmoja wenu kunitafuta kujua nipo wapi na ninafanya nini! Leo naanzia wapi kukataa hifadhi ya kina Msindai hapo Dar? Ningejuaje kama safari hii shuguli zimepungua, unaweza kuniweka nyumbani kwako? Hakika ungeniambia mapema, ningeshukia nyumbani kwako! Sina kinyongo na yeyote yule. Ila utaratibu wa nyumbani ndio upo hivyo dada, na wewe ni shahidi.” Sabrina akaendelea taratibu tu.

“Halafu pia sitokei kwa kina Msindai. Natokea kwa dada mmoja anaitwa Pendo, ambaye yeye na mume wake ndio watatusimamia harusi mimi na Jack. Ni msichana ambaye amekuwa na kina Jena dada yake Jack. Anaonekana ni dada mzuri tu. Jack anasema amesoma na ana kazi nzuri sana, pengine wewe wa huko jijini unaweza kumfahamu. Mimi nimeanza kufahamiana naye zaidi kwa kuwa karibu kila siku ananipigia simu kunijulia hali na kuweka mipango ya harusi. Sina chakuongeza huko dada yangu. Wamejipanga haswa. Wanaratiba yangu ya kila kitu, ninachosikia hapa ni wakigombana na Jack sababu ya muda. Sasa hebu niambie dada yangu, nilitakiwa kufanya nini hapo?” Sabrina akauliza taratibu tu.

“Basi Sabrina.” “Hapana. Sitaki lawama baadaye. Niambie tu kile nilichotakiwa kufanya dada. Maana hata mimi mwenyewe kuna mambo Pendo ananipigia na kuniambia hata sikujua kama natakiwa kufanya!” “Kama nini?” “Kuwekwa kwenye sauna, sijui na waxing ya mwili mzima!” Ikabidi hata Sabina acheke.  “Kweli tena. Sasa hayo yote mimi Sabrina ningeyajua wapi kiasi chakuomba msaada?” “Haya mwaya. Sisi tunakutakia kila la kheri. Kwa hiyo na sisi tutakuona ukumbini kama wageni wengine?” “Hilo nalo pia sijui dada yangu. Niamini nikikwambia sina nijualo zaidi ya nini na kipi kipo kwenye ratiba, basi. Ila lini vinafanyika, sijui.” “Basi na mimi naomba uniombee niwe kwenye hizo ratiba zao. Angalau wakuone na wewe una mtu wa kukuwakilisha.” “Sijaelewa dada. Unataka nikuombee ratiba ya nini? Siku ya harusi au?” “Yaani hivyo wanavyotaka kukufanyia. Angalau na mimi na mama tuwepo mdogo wangu. Mama na yeye azunguke madukani au kwenye masaluni na wewe binti yake unayeolewa?” “Oooh! Kwa hiyo mama ndiye amekutuma kwamba na yeye anataka kuwepo au unamuongelea tu?” Sabrina akauliza.

“Nikitu tulichokifikiria kwa pamoja. Kwa ufupi na sisi tunataka kushiriki Sabrina. Hata kama tulishindwa zamani. Tukakuacha peke yako. Basi jua sasa hivi mimi nipo. Nipe tu nafasi ingine hata kwa jambo dogo tu.” “Na mimi pia.” Sabrina akashituka kusikia sauti ya mama yake. “Nimeshindwa kuvumilia. Naona mwenzangu nimemtuma atuongelee wote, anaishia kujiuza peke yake.” Sabrina akacheka. “Shikamoo mama.” “Marahaba Sabrina mwanangu. Mnaendeleaje?” “Tunamshukuru Mungu sisi hatujambo. Nashukuru kwa kutaka kunisaidia.” “Na mimi nijidai mwanangu! Sijawahi kuozesha.” Sabrina akacheka.

“Najua nilikuwa mkatili kwako Sabrina, mama. Nisamehe mwanangu. Najua nimekosa, tumekuwa watu tusio kujali, lakini mimi naongea kwa niaba ya baba pia, tusamehe mama. Tafuta jinsi utusamehe mama.” Mpaka machozi yakamtoka Sabrina. “Mimi kama mama yako nimekuwa nikikutamkia maneno ambayo yamekuumiza. Nimetubu mbele za Mungu. Nimekuwa nikiyabatilisha na kukutamkia kuwa wewe ni mbarikiwa, sio mwenye shida. Naamini Mungu amenisikia na kunisamehe. Nataka tuanze mahusinao mengine. Inawezekana au unataka tukupe muda?” “Wala hakuna sababu yakufanya hivyo mama yangu. Mimi nimesamehe. Na yameisha.” Akasikia ukimya mkubwa.

“Nimesamehe kabisa jamani, na ninashukuru kwa kunikaribisha kwenye umoja wenu. Hakika nilikua nikitamani. Lakini nafikiri wakati wa Mungu ni sasa.” Wote wakajisikia vibaya sana. “Nisamehe mwaya Sabrina mdogo wangu. Nahisi nililemewa na mambo, na mimi nikawa nakusahau ikawa ni mpaka unitafute. Sasa hivi ukitupa uhuru, tutakuwa na sisi tukikupigia kukujulia hali.” Sabrina akacheka akijifuta machozi.

“Sasa mama yangu? Nakaribishwa na mimi huko kwenye maandalizi?”  Mama yake akauliza kwa upendo. “Nitazungumza na Pendo. Nijue utaratibu wote. Nilimuachia yeye kila kitu sikutaka hata kujishugulisha. Lakini sasa hivi nitafuatilia kisha nitawajulisha ili kama mtaweza muwe mnajumuika na sisi.” “Basi labda niseme hivi, nimeona au nimemuomba Sabina niwepo kwake kwa muda. Naweza na mimi nikaenda hapo kwa Sabina week moja kabla ya harusi. Utakapokuwepo, uniambie na mimi niwe nakuja tuongozane. Angalau na mimi nionekane ninashuguli.” Sabrina akacheka tena.

“Au unaona tutakuingilia na wakwe zako?” “Hata kidogo mama. Mimi siwaonei aibu hata kidogo. Ni vile sikuyajua haya yote mapema. Sikujua kama mtataka kujihusisha kwa ukaribu huu. Imenitia moyo, na ninajisikia vizuri sana. Nawashukuru kwa ukweli, wala sidanganyi. Nitazungumza na Jack juu ya kufikia hapo kwa da Sabina. Ili...” Akamsikia Sabina na mama yake wanapiga vigelegele, Sabrina akashangaa sana. “Yaani ndio mnanitaka kwa kiasi hicho!?” “Sanaaa! Mimi nishajidai kwa rafiki zangu, sema tu nimechelewa. Nishatangaza kwa kila mtu kuwa kina Msindai wanaoa kwetu. Wewe hukuona lile kundi la mashoga zangu walivyokuja nyumbani kwenye mahari yako?” Sabina akamfanya Sabrina acheke sana. “Mimi nataka mahusiano Sabrina mama. Na mimi nifurahie uzazi wangu. Mama yangu atanisema sana akiona unatokea ukweni, kwenda harusini.” “Kama namuona bibi!”  Sabrina wakafanya wakacheke.

“Ashaanza kuulizia lini unawekwa ndani.” “Mmmh! Mwambie bibi shachelewa! Alitakiwa kuniweka ndani mapema. Sasa hivi ni mama nakaribia kujifungua mapacha.” Wakashtuka sana. “Nilikuhisi Sabrina, lakini nikaogopa kukuudhi. Nilijua umjamzito. Hongera mama.” “Asante mama yangu.” “Basi mimi hata sikukujua! Niliona tu umependeza.” Sabrina akacheka. “Hongera mdogo wangu. Hongera sana. Unaingia kwenye ndoa na baraka.” Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu akijua pongezi hizo anayesababisha ni Jack. Wasingempongeza hivyo kama angerudi nyumbani na tumbo hilo bila Jackson Msindai, akaeleweka. “Namshukuru Mungu.” Ndio kwa mara ya kwanza wanaweza kumsikia Sabrina akiongea mambo yake ya ndani, na wao kumsikiliza.

“Kwa hiyo ndio miezi mingapi sasa?” Mama yake akauliza. “Wa tano. Ila bado hatujajua jinsia. Jack amesema mpaka tukitoka honeymoon ndio tutakwenda kuangalia jinsia. Ila tulirudi jana kwa daktari. Amesema wote wapo salama, wanaendelea vizuri.” Akamsikia mama yake akipiga vigelegele, Sabrina asiamini kama wamepokea vizuri kwa kiasi hicho! Akawa anacheka tu. “Sasa nani anakusaidia kazi?” Akauliza Sabina kwa kujali. “Hamna hata kazi hapa. Kama kufua naona mama yake Jack amenirahisishia. Jumamosi hii alituma mashine ya kufulia na kukaushia, na fundi kabisa. Wamehangaika hapa na Jack, naona jumatatu wakafanikiwa. Usafi wa nje yupo kijana anakuja kusafisha. Na ndani yupo dada mimi na Jack tulimuomba atusaidie kutafuta msichana wa kazi, lakini Jack anahisi anafanya kusudi ili afanye yeye mwenyewe. Maana alisema wakati anatutafutia, anaomba tumpe yeye hizo kazi. Anakuja asubuhi siku ya ijumaa, anasafisha kila mahali, tunamlipa. Naona siku zinazidi kwenda, haleti msichana, anakuja yeye tu.” Wakacheka. “Sasa chakula nani anapika?” Akauliza mama yake. “Chakula changu na Jack tu! Napika mwenyewe mama. Hapo sitaki msaada wa mtu kunilishia Jack wangu. Hapana kwakweli.” Wakacheka. “Napika mwenyewe.” “Na wewe unapenda kupika! Najua hapo Jack atafaidi.” Mama yake akaongeza kwa kumsifia. Sabrina akacheka. Emma alishamaliza mitihani yake ya kidato cha sita na kuondoka hapo kurudi kwao. Wakabaki Sabrina na Jack tu ndani ya hiyo nyumba.

“Sasa ukijifungua si utataka msaada?” Akaongeza Sabina. “Jack kashamlalamikia mama yake juu ya huyo dada kuwa anamuhisi hataki kutuletea msichana wa kazi ili afanye yeye mwenyewe. Lakini akamwambia tutahitaji msaada zaidi nitakapojifungua na hadhani kama huyo dada ataweza kwa kuwa anamajukumu yake. Ni mke wa mtu na watoto wadogo. Na tupo kwenye mahusiano naye, hataki aone tumemkatili. Ndio mama yake ametuambia atatuletea msichana. Tusiwe na wasiwasi. Kwa hiyo...” “Brina!” Akamsikia Jack.

“Sasa Jack amerudi. Hakuna tena kitakachoendelea hapa. Huwa anataka akiwepo hapa kila kitu kiwe kwake. Macho, masikio, mdomo mpaka mikono viwe kwake tu. Hatutaongea tena...” “Mama Msindai upo?” Akaita tena Jack, Sabrina akacheka. “Njoo jikoni, nazungumza na simu.” “Nani tena sasa hivi wakati mimi ndio nimerudi?” “Nenda kamsikilize Sabrina.” Mama yake akamsikia Jack akilalamika. “Ni mama na Sabina, we Jack. Acha kulalamika.” Akafunga mdomo kwa mikono yote miwili. “Aibu zako.” Sabrina akamcheka. “Shikamoo mama.” Jack akasalimia kwa sauti. Mama yake Sabrina akacheka. “Marahaba Jack mwanangu. Hujambo?” “Sijambo kabisa. Habari za nyumbani? Baba hajambo?” Jack akauliza akiwa amesogea kwenye simu, Sabrina ameishika na kuweka kwenye spika. “Hatujambo baba, nimepiga tu kuwajulia hali.” “Tunashukuru.” Jack akamjibu mama yake Sabrina. “Na mimi nipo shemeji.” Sabina akaingilia, Jack akacheka. “Habari shemeji?” “Salama tu. Haya, tuwaache ili upumzike.” “Tunashukuru kwa simu.” Akamalizia Jack bila kuvunga, kuashiria ni sawa kabisa wakifupisha mazungumzo. “Haya, muwe na jioni njema.” “Asante mama.” Sabrina akashukuru na kukata.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Nilikuwa na hamu na wewe!” Sabrina akacheka. “Mbona umekuja na furaha hivyo? Kuna habari gani njema?” “Nimefurahi kukuona mpenzi wangu! Wewe vipi?” Sabrina akacheka na kusimama. “Sasa unaenda wapi?” “Kumalizia kusafisha, nilikuwa napika kabla hawajanipigia simu.” Akambusu mdomoni akasogea kwenye vyombo. “Kwema?” “Kama hakuna lililojificha nyuma yake, naona wameamua kutafuta undugu na mimi kwa hali na mali.” Sabrina akamsimulia Jack kila kitu, Jack akanyamaza. Hakuongeza. “Sasa mbona kimya?” “Mimi sijui Brina. Mambo ya ndugu ni magumu! Magumu sana. Ninachoogopa ni wasije kuharibu mwishoni. Mimi nataka kuoa Brina.” Sabrina akamgeukia.

“Usifikiri mipango yote inayowekwa ni bure! Ni kwa kuwa nimethibitishia  watu na kuwahakikishia kuwa nimekusudia kuoa kwa wakati tuliokubaliana, Brina. Sitaki kitu kiharibike. Ndio maana unaona ipo mipango inayoeleweka. Haya mambo ya kujitokeza katikati, tena ya gafla, kukiwa na mipango mikamilifu tayari! Inanitia wasiwasi mama. Kumebaki siku chache tu. Watu wameshajipanga kwa kila kitu, kwa nini tena tuingize mambo mapya katikati?” “Nafikiri nia ni nzuri Jack. Wanataka kurudisha mahusiano.” “Basi naomba mama awe anafuatwa hapo kwa Sabina, na kukusindikiza popote atakapotaka, lakini utulie kwa Pendo.” Sabrina akanyamaza.

“Nimekubali Pendo na mume wake watusimamie katika kila jambo kwa sababu Pendo ametulia. Nyumbani kwake pana utulivu wa hali ya juu. Pale hutapata mtu wa kukukera, wala kukusumbua. Hivyo unavyomsikia Pendo kwenye simu, na kumuona siku ile kwa muda mfupi tu, ndio yupo hivyohivyo. Mtulivu sana. Bado hajajaliwa watoto. Wanaishi wawili tu na mumewe pamoja na msichana wao wa kazi, ndio maana hata mama ameona kwake ni sehemu sahihi uende kwa muda upumzike kabla ya harusi. Pendo amejiandaa kwa ajili yako Brina.” “Umejuaje?” Sabrina akauliza. “Ni rafiki wa Jacinta na Jena. Wanafahamiana kwa karibu na anawashirikisha kila kitu anachofanya. Ameshaanza hata kukununulia mahitaji yako a\nayoona utahitaji pale. Namaanisha ameshaanza kukuandalia chumba chako. Sitaki tena michanganyo Brina. Naomba turidhike na mipango iliyopo.” Sabrina akanyamaza

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Maandalizi ya harusi yakaendelea vizuri, hapakuwa na tatizo. Watoto wa Msindai na marafiki waligawana majukumu. Pendo msimamizi wa harusi yeye akawa akihangaika gauni la harusi na vitu vyake. Kila alipoona magauni mazuri huko madukani, alipiga picha na kumtumia Sabrina. Sabrina akapenda matatu, akawa anasubiriwa yeye tu kwenda kujaribisha na kama kunamarekebisho kidogo yafanyike. Joy mke wa waziri Msindai alikuwa akishugulikia wasimamizi wa mbele na nyuma. Akawa akimshirikisha Sabrina juu ya sare na kutuma picha za hao watoto. “Au sio sawa?” Joy akauliza. “Wewe fanya kile unachoona kitafaa na kupendeza Joy. Wala katika hilo sina ushauri. Hao wasimamizi ni juu yako. Ukiharibu ni wewe mwenyewe.” Joy akawa anacheka kila akimtaka Sabrina mawazo na Sabrina kumuachia jukumu zima. Kuanzia nguo zao, viatu mpaka jinsi ya kucheza ikawa juu yake Joy.

Sabrina alitangulia siku 8 kabla ya harusi, tena kwa kulazimisha haswa. Ilibidi mpaka mama Msindai awe mkali kwa Jack ambaye ilimbidi yeye abaki Singida bila Sabrina sababu ya kuendelea na kazi ili kuweka siku za likizo kwenye harusi na honeymoon. Alilalamika sana akitaka Sabrina amsubirie, waondoke naye Singida. Hapo mama yake akawa mkali na kumwambia kama Sabrina hatakuja siku hiyo, basi kesho yake angemuona yeye mwenyewe mama Msindai hapo Singida akimfuata Sabrina. “Usitake kutuharibia shuguli nzima, sisi wote tuje kuonekana hovyo! Huyo bibi harusi mpaka sasa hana gauni la harusi wala viatu vya uhakika! Unataka abaki huko muangaliane tu!” Hapo ndipo Jack akakubali, Sabrina akaondoka.

Sabrina Mjini Kabla Ya Harusi.

Kwa mwezi mmoja tu tokea waachane kwenye mahari, Sabrina alibadilika haswa. Tumbo likawa lipo dhahiri. Pendo na mume wake ndio walikwenda kumpokea uwanja wa ndege, Pendo akabaki anamshangaa. “Usiwe na wasiwasi bwana!” Sabrina akawa anacheka. “Nguo moja lazima nirudishe. Haitakukaa vizuri. Labda ile ambayo inaanza kuchanua chini ya maziwa.” “Ile imejaa sana Pendo. Si itanichosha kutembea?” “Ule mkia wa nyuma unatoka. Ukichoka tutakuwa tunatoa.” Wakaendelea kuzungumza akielekea nyumbani kwa Pendo.

Ni kweli Sabrina alikuta maandalizi mazuri. Kila kitu kipo kisafi na hali ya juu. Vitu vipya na vizuri tupu. Kuanzia nguo za kulalia, mashuka, nguo zake yeye mwenyewe za kuvaa, nje na ndani. Viatu vya kuvaa ndani ya hiyo nyumba na nje. Nyumba ni tulivu kama alivyosema Jack. Safi kila mahali. Na mumewe akaonekana hana tofauti na Pendo, watulivu halafu wote wakakutana wazuri. Akatamania ndoa yao. Kasoro tu, hawakujaliwa watoto. Pendo na Willy walishahangaika kwa kila mtaalamu waliyesikia anaweza kuwasaidia kupata mtoto, lakini ikashindikana. Wamebaki wao tu wawili na msichana wa kazi.

Kulikuwa na ratiba kuanzia siku hiyo anafika mpaka siku ya harusi. Alifika nyumbani na fundi wa nguo akaja usiku. Akajaribisha magauni ya harusi, moja likamkaa vizuri sana, wala usingemtambua kwa haraka kama ni mjamzito. Lilimkaa kama lake, wala halikuhitaji marekebisho. Zuri haswa, Sabrina hakuamini kama ndio linamsubiria yeye. Hilo likaisha na kupita vizuri.

Sabrina akawa mwaminifu, kila anapotoka, lazima ampitie mama yake nyumbani kwa Sabina. Wanaenda kuzunguka naye. Kama ni saluni, basi mama yake alikaa tu kwenye viti akisubiria mpaka amalizwe. Wakati mwingine Sabina alikwenda na kuwa nao, wakati mwingine alimpitia mama yao nyumbani kwa Pendo kama alirudi na Sabrina na kurudi naye mama yao nyumbani kwake Sabina. Siku ambazo Sabrina hakuwa akitoka, mama yake alikwenda kukaa naye hapo mpaka jioni Sabina akitoka kazini. Anakwenda kumfuata na kumrudisha nyumbani mpaka maandalizi yakakamilika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jack alitua jijini tayari kwa kufunga ndoa. Yeye alifikia kwao. “Au na mimi nishukie kwa wasimamizi wetu?” “Acha ujanja Jack. Tulia nyumbani.” Kaka yake akamkatalia. “Unauhakika hakuna mawaidha kwa bwana harusi?” “Ndio maana leo usiku tuna bachelor party. Wanaume tunakwenda kukufunda.” Msimamizi wake, yaani mume wa Pendo, Willy akamuwahi. “Daah! Mafunzo hayo ningepewa na mwenzangu!” Wakazidi kucheka. “Wewe shida yako ni kumuona Sabrina. Pendo hawezi kukubali umuone hata iweje. Wewe twende tukafurahi leo, kesho unapewa mke, ukahangaike naye mwenyewe.” “Daah! Imekuwa ngumu zaidi nilivyofikiria!” Kaka yake akamwangalia na kucheka. “Dogo anaona kukaa mbali na mke siku 8 ni nyingi!” Rafiki wa Junior akachomekea. “Tutamtafuta tena baada ya miaka 5 halafu tumpe mapumziko haya haya tuone kama atayakataa.” Wakaanza kucheka. “Mitano Junior!? Mwaka tu.” Wakaendelea kucheka marafiki hao wa Junior wakitaniana hapoa nyumbani kwa mama Msindai. 

Harusi ya Sabrina & Jack.

I

likuwa mida ya saa kumi kamili jioni wakati kanisa zima limesimama, Sabrina akiingia kanisani akiwa ameshikwa mkono na baba yake. Kweli uzazi mzuri! Mzee huyo mfugaji tu, shule hamna wala salio halisomi vyakueleweka, lakini siku hiyo wakuu wa nchi walisimama akiwa anaingia na binti yake hapo kanisani kulikokuwa kumeimarishwa ulinzi haswa. Alifika mjini akasafishwa vizuri haswa. Kuanzia kichwani mpaka mguuni, Sabina alihakikisha baba yake yupo vizuri. Alivaa suti nyeusi nzuri ya hadhi, na shati jeupe. Akafungwa ua dogo lenye rangi ya njano, pembeni ya mfuko wa suti. Kiatu cheusi, safi kinawaka. Alitembea kwa furaha na ujasiri, akijua kina Msindai wanasubiria binti yake siku hiyo. Ile hali yakutizamwa na yeye, na wakubwa wa nchi, akitembea katikati ya kanisa hilo kubwa, ikaweka furaha ya ajabu sana ndani yake.

Ulinzi nje na ndani ya hilo kanisa ulikuwa mkubwa haswa kwani ni kama bunge kuu ilihamia hapo. Mawaziri wastaafu wa awamu ya tatu ambao walifanya kazi na mama Msindai walikuwepo. Madaktari bingwa wenye majina makubwa nchini ambao walisoma na kufanya kazi na Mzee Msindai, walikuwepo kumsindikiza kwenye kuozesha kijana wao wa mwisho. Wabunge, manaibu waziri, mawaziri wa awamu hiyo ambao wanafanya kazi na kutumika na Junior pamoja na marafiki zake ambao si wana siasa, pia walikuwepo kushuhudia harusi ya mdogo wake, waziri Msindai. Bado marafiki wa Jacinta Msindai ambaye ni kiongozi wa usalama wa taifa nchini. Jena naye alikuwa na marafiki zake ambao nao ni madaktari kama yeye. Kwa hiyo kulikuwa na ulinzi mkali sana.

Wasimamizi wote walishajipanga mbele kabisa ya kanisa pamoja na bwana harusi, wakimsubiria bibi harusi, Sabrina. Maandalizi ya tokea anafika jijini Dar kutokea Singida mpaka anafikishwa hapo kanisani, Sabrina alikuwa akimshangaa sana Mungu. Kazi na kujitoa kote alikokuwa akikufanya gizani, akifanikisha watu wanaosifika hadharani, leo Mungu amemuinua na kumkalisha na wakuu! Yeye mwenyewe hakuwa anaamini. Walishapita watoto wanne wakike kumwaga maua, kabla hajaingia. Kapeti jekundu lililokuwa limetandikwa maalumu kwa ajili yake, lilijaa maua, kiasi ya kwamba alikuwa akitembea, miguu unafunikwa na maua. Alivaa shela ndefu na nzuri sana. Watu wote walikuwa wamesimama wakati Sabrina na baba yake wanatembea taratibu, wakisindikizwa na mziki uliokuwa ukipigwa na vinanda hapo kanisani. Kanisa lilipambwa vilivyo. Hata wadogo zake wakiume wawili, walienda kuombewa ruhusa shuleni ili waweze kuhudhuria harusi hiyo. Hukuhitaji kuambiwa kuwa Sabrina ameinuliwa.

Watu wote pale kanisani walikuwa wakimsindikiza kwa macho binti huyo aliyefunga kuoza kwenye familia ya Msindai. Hakuwa daktari, wala profesa au mwanasheria. Shule yake ya mambo ya stoo ilibaki vilevile kichwani tena kwa ngazi ya diploma tu, na hakuwahi kupata ajira na kuitumia shule yake. Akabaki Sabrina wa kutoka Chalinze. Hakuwa mweupe akiwaka kama jua. Sijui miguu minene, au umbo namba 8 au 6. Alikuwa Sabrina mwenye mimba ya watoto mapacha. Anaolewa na Jackson Msindai! Hata Jack mwenyewe hakuwa akijua ni kwa nini anachanganywa na Sabrina kwa kiasi hicho.

 Alisoma chuo kilichojaa warembo, lakini akampenda Sabrina karibu kurukwa na akili. Alishatembea na warembo, lakini nafsi yake ilimuhitaji Sabrina. Alimtizama akiwa anamsogelea, asiamini kama siku hiyo anakabidhiwa watu watatu kwa mpigo. Wakati wengine waliojua Sabrina kuwa anaujauzito usio wa Jack, wakimshangaa Jack na kumuhurumia, lakini kwa Jack yeye aliona ni kama anakabidhiwa ulimwengu mzima na fahari yake. Tena kaka yake alimtania na kumwambia ni ‘double blessings’.

“Nani anamtoa binti huyo?” Akauliza mchungaji wa kanisa hilo, ambaye alipata bahati yakufungisha ndoa hiyo ya kina Msindai watu wake wakaribu. “Ni mimi.” Baba yake Sabrina akajibu, na kumkabidhisha kwa Jackson akimpa maneno machache kama alivyofundishwa baba huyo. Isivyo kawaida, Jack alivyokabidhiwa tu, akatoa shela na kumbusu kwa kina hapohapo. “JACKSON MSINDAI!” Mama yake akahamaki kwa sauti ya juu, na wengine wote wakashangaa. Jackson akamuachia. “Sijamuona siku karibu 8 sasa! I missed her.” Jack akajibu kwa sauti na kumfunika. Watu wakacheka kidogo wengine wakabaki wanashangaa. “Sorry ma!” Akamgeukia mama yake ambaye alibaki ameduaa. Sabrina akacheka na kuinama. Vigelegele vikaendelea hapo wakishangilia, ikabidi mchungaji aombe watulie. “Bado  Jackson. Muda mfupi sana tutakukabidhi.” Mchungaji akaongea akicheka. Jack akamshika Sabrina mkono, wakasogea mpaka mbele kabisa alipokuwa amesimama mchungaji huyo, ibada ikaanza.

“Umependeza sanaaaaa!” Jack akamnong’oneza Sabrina. Sabrina akacheka. “Na wewe Jack. Nimefurahi umenibusu. Ninahamu na wewe Jack!” “Hata mimi. Mpaka nahisi kuchanganyikiwa. Tukitoka...” Ikabidi msimamizi wa Jack, Willy, amguse. “Mnaongea kwa sauti wakati wa mahubiri Jack! Tulia bwana.” “Okay. Samahani.” Jack na Sabrina wakacheka na kunyamaza. Wakatulia mpaka mahubiri yalipoisha.

Ukafika wakati wa kiapo. Yeye Sabrina akasoma kiapo cha kwenye kitabu tu, akamaliza. Akashangaa mchungaji anatangaza kuwa Jackson ameandaa kiapo chake. Sabrina akashangaa na kumtizama Jack. Jack akasogezewa kipaza sauti. “Mara ya kwanza kabisa kukuona Brina, moyoni nilijua kwa hakika utakuwa mke wangu, wala si rafiki tu, japo ulinikataa.” “Jack!” Sabrina akashangaa sana, tena kwa sauti. Watu wakacheka na vigelegele kidogo. “Muda wote nimekuwa nikikusubiri nikijua wewe ni wangu Brina. Umekuwa ukipenda kusema neno au kutumia neno, ‘wakati wa Bwana’. Kwangu naamini huu ndio wakati wa Bwana kunibariki wewe kuwa mke wangu. Sichukulii hiki kiapo leo kama ahadi tu, lakini nachukulia kama upendeleo mkubwa sana ambao Mungu amenipendelea hapa duniani. Yaani mimi Jackson Msindai, kupata upendeleo wa kuishi na wewe! Kucheka na wewe mchana na usiku! Kulia pamoja na wewe Brina! Mimi Jackson kupewa bahati na Mungu ya kunitumia kuwa faraja yako unapopita katika kipindi kigumu kama magonjwa, maradhi hata kutokuwa na furaha tu! Kwangu ni heshima ya pekee sana ambayo hakuna kitu Mungu atanipa zaidi ya hii.” Watu walishangilia kana kwamba Jackson amemaliza, lakini bado.

Kanisa zima walisimama, Sabrina akifutwa machozi na Pendo kwa kuwa bado Jack alikuwa amemshikilia mikono yote miwili, akitoa kiapo chake. Walipotulia akaendelea, “Nilishakwambia wewe Brina, hata mama nilimwambia hili. Siku Mungu anakuumba wewe Sabrina, alikuwa akinifikiria mimi.” Watu wakasikika wakisema, “Waooo!” Jack akaendelea huku yeye mwenyewe akifuta machozi. “Unanikamilisha katika kila eneo la maisha yangu. Siku ya leo, nikisimama hapa mbele ya mashahidi wengi, namwambia Mungu asante kwa upendeleo alionipa mimi kuniwezesha kuwepo kwenye maisha yako Sabrina. Kwamba katika maisha yangu yote nitayokuwepo hapa duniani, mimi Jackson Msindai, niyatumie kukupenda wewe, kukujali, kukulinda, kuwa faraja yako mpaka kifo kitakapo tutengenisha.” Watu wakazidi kushangilia sana. Ngoma zilipigwa, vinanda, vigelegele, waliokuwa na hisia za karibu wakafuta machozi. “Naahidi kuwa mwaminifu kwako Brina, naomba uendelee kuniombea, Mungu anisaidie.” Jack akamaliza mpaka mchungaji akapiga makofi. “Waooo!” Akasikika mchungaji huyo. Jack aliongea bila kusoma, akiwa amemshika Sabrina mikono yote miwili mpaka mwisho.

Baada ya kutulia, wawili hao wakavalishana pete za ndoa, ndipo mchungaji akawabariki na kumruhusu sasa Jack ambusu mkewe. “Yes!” Akasikika Jackson akishangilia na kufanya kila mtu acheke. Akamgeuza Sabrina, akambumbatia vizuri bila haraka, watu wakicheka, akaanza kumbusu taratibu bila haraka. Akanyanyua mkono mmoja juu kama anayeshangilia huku akiendelea kumbusu mkewe. Mama yake akainama akitingisha kichwa. Watu walicheka sana na vigelegele. Askofu akamalizia ibada baada ya kuweka saini kwenye vyeti vyao vya ndoa. “Naomba niwatambulishe kwenu, bwana na bibi Msindai.” “Yesss!” Jackson akasikika kwa sauti na kumbusu tena Sabrina. “Kissing part is over Jack!” Willy msimamizi wake akamuwahi. Jack akacheka. “Kidogo tu!” Watu waliendelea na vigelegele wakati Jack na Sabrina wakitoka huku wakipunga mikono. Walipewa muda wakutosha kutoka wao wenyewe ili video na picha vichukuliwe vizuri ndipo wakafuata wazazi na wageni wale wa maana huku ulinzi ukizingatiwa. 

Kutokana na muda, lengo la Jack lakutaka wapelekwe kwanza hotelini kumpumzika baada ya ibada, kabla ya ukumbini, halikutimia. Hapo kaka yake akawa mkali kabisa. Jack akapoa. “Tunakwenda na Muda, Jack. Mapema sana tutamaliza.” Wakapelekwa kupiga picha zao wao na familia za pande zote mbili. Bibi yake Sabrina alijawa furaha, Sabrina alikuwa akicheka tu. Zilipigwa picha nyingi mpaka wapiga picha wakaridhika, safari yakurudi ukumbini, ikaanza.

Ukumbini.

W

aliingia wageni wote, ndipo wakaanza kuingia wasimamizi wakicheza. Wote walisimama wakati Jack na Sabrina wakiingia. Wao hawakuingia wakicheza kama wasimamizi wao, ila kupunga tu mkono, Jack akiwa amekumbati mkono wa Sabrina mpaka katikati ya ukumbi. Walipofika tu katikati wimbo ukabadilishwa, wa taratibu ukasikika, wakajipanga wasimamizi vizuri, Jack akamkumbatia Sabrina, akavuta mkono wake wa kushoto mpaka kifuani kwake akiwa ameushikilia vizuri, wakaanza kucheza mziki wa taratibu wa, ‘Perfect’. Jack alikuwa akiimba huku akicheza vizuri sana na mke wake. Ungependa kuwatizama. Walifanyia mazoezi huo wimbo wakiwa Singida kwani Jack alimwambia lazima wataucheza huo wimbo. Na yeye Jack alimuomba kaka yake uwe ndio wimbo wao wa kwanza kabisa kabla ratiba haijaanza.

Jack alicheza na mkewe tu. Hakutaka mwanzoni mtu mwingine yeyote acheze. Mc alishatangaza. Ni wimbo maalumu kwa Sabrina, kutoka kwa Jack. Walicheza vizuri sana. Jack alimzungusha mara kadhaa na kurudi kumkumbatia na kuendelea kucheza. Ukumbi ulipambwa vizuri ukatangaza umaarufu wa Msindai. Hata Jack wenyewe alikiri hakuwahi kwenda kwenye harusi iliyo nadhifu kwa kiasi hicho. Hakika kaka yake alimuandalia mdogo wake harusi nzuri sana. Familia ya Sabrina walibaki wakishangaa wasiamini kama yule bibi harusi ni Sabrina. Kila wakati MC alitangaza na kukumbushia kuwa ule usiku wakina Msindai waliutoa maalumu kwa ajili ya Sabrina. Hakuna cha maana ambacho ungekitazama kwa Sabrina ukakiona kwa nje haraka, ukavutiwa nacho. Msichana wa kawaida tu ila usiku huo ni kweli Mungu alimthaminisha.

Ratiba ilikwenda kwa haraka na ufanisi kama ilivyopangiliwa. Zawadi zilikuwa zikipokelewa na watu maalumu mlangoni. Zilikuwa nyingi mno. Wakati watu wakila na kunywa ndipo Jack na Sabrina walipokuwa wakipita kusalimia watu au wageni wa muhimu na kupongezwa. Usiku huo kwa mara ya kwanza Sabrina akashika mikono watu wakubwa wa nchi. Mawaziri wastaafu na wawakati huo waliokuwa meza za upande wa Msindai. Sabrina mwenyewe hakuwa akiamini.

Akafika kwenye meza ya Joy na mume wake wakiwa wamekaa na marafiki wengine. Junior alikuwa amempakata mwanae Claire akiwa ananyonya kidole chake. Wote wakaanza kucheka. “Lakini amejitahidi mwanangu. Si ndio mama?” Junior akambusu kichwani. Alionekana amezidiwa haswa, anasinzia. Clai akawa anacheka huku akimnyoshea kidole mdogo wake. “Si nilikwambia anti?” “Wewe unataka kulia Clai! Bora unyamaze.” Joy akamuwahi mwanae wakiume huku kaka yao ametulia tu. Sabrina akazidi kucheka. “Si nilikwambia umependeza eeh?” Sabrina akamuuliza kwa upendo, akatingisha kichwa kukubali. “Basi mimi na anko tunakushukuru kwa kazi nzuri uliyofanya.” “Mimi ndio nimemwaga maua mengi.” Akaongea na kidole chake mdomoni. Wote wakacheka. “Niliona.” “Mwenzio aliishiwa maua palepale kanisani. Ikabidi mama amtafutie mengine ya kumwaga hapa ukumbini.” Clai akamsemelea na kufanya wazidi kucheka. Wakawashukuru wote. Junior na mkewe kwa kuwaandalia harusi nzuri sana. Wakakumbatiana hapo. Wakiwa wanatoka hapo wakisogelea meza ya kina Jacinta, wakapita kwenye meza ambayo alikuwa amekaa Max na mkewe.

Sabrina akapigwa na butwaa. Jack akamuona na yeye akasimama. “Hujambo Sabrina?” Akamsalimia mke wa Max. “Sijambo. Shikamoo.” “Marahaba. Hongera sana. Umependeza, na harusi nzuri sana.” “Nashukuru Mungu. Na asanteni kwa kuja.” Sabrina akawapa mkono na kumgeukia Jack. “Jack, huyu ni Max mwanasheria ambaye yupo karibu sana na Tino na mkewe. Tino alinipeleka mpaka nyumbani kwao, ndipo nilipofahamiana na mke wake pia.” “Nimefurahi kuwafahamu. Na asanteni kwa kuja kwenye siku muhimu zaidi kwangu.” Sabrina akamsukuma kidogo na kucheka. Wakaondoka moyo wa Sabrina ukiwa unadunda. Hata Jack alimuona amebadilika kama aliyeingiwa hofu.

Kabla wajafika kwenye meza ya kina Jacinta, Jack akamgeuza. “Niangalie mimi.” Sabrina akamwangalia. “Wewe ni mke wangu. Huna sababu ya kuingiwa hofu wala wasiwasi. Umenisikia?” Sabrina akavuta pumzi kwa nguvu. Jack akamvuta karibu na kuanza kumbusu akiwa amemkumbatia. “Kaka amefanya ratiba ndefu, mpaka maharusi wameanza honeymoon hapahapa ukumbini!” Jena akafanya watu waanze kucheka mpaka wengine wakawageukia. “Mbea wewe!” Jack akamwambia dada yake. “Mimi nimesema tu.” Jena akajitetea huku akicheka. “Hayakuhusu.”  Wakaendelea kusalimia.

Jack hakutegemea kama mkuu wa chuo walichosoma hao wawili angekuwepo. Walifurahi sana. “Sikuwa na uhakika kama ungekuja! Nilimuomba tu kaka akutumie mualiko nikiwa sina uhakika kama ungeweza kuhudhuria sababu ya muda mfupi. Nimefurahi sana na tumejisikia kutuheshimu. Karibu sana.” Jack akampa mkono na kumkumbatia huyo mkuu wa chuo. “Ingekuwa ngumu kukosa tukio la kihistoria kwa nyinyi wawili.” Sabrina na Jack walicheka sana. “Naona Msindai umepambana mpaka ukaoa kabisa!” “Ilikuwa lazima nimiliki mkuu!” Wakaendelea kucheka. Jack akaomba mpiga picha wao achukue kumbukumbu nzuri hapo wakiwa na mkuu wa chuo walichosoma. Wakamshukuru tena kwa kufika, wakaendelea.

Walisalimia upande wa kina Sabrina, Jack akiwa na heshima zote akiwashika mkono kila mmoja mpaka wadogo zake. Wakashangaa akiwataja majina kabisa. “Nawafahamu muda mrefu tu, ni hivyo hatukupata nafasi ya kukutana. Baba!” Akamgeukia baba yake Sabrina. “Nashukuru kuwaombea ruhusa kina Sethi angalau kuhudhuria siku hii muhimu kwetu. Asante sana.” “Karibu baba. Tunashukuru kwa heshima uliyotupa.” Sabrina akamgusa bega. “Bibi anakuuliza lini utakwenda kumtembelea kwake Bagamoyo si Chalinze?” Jack akacheka na kumgeukia bibi yake na kumtizama Sabrina. “Wewe jibu Jack, acha kuniangalia mimi.” Jack akacheka tena kama aliyekosa jibu la haraka kisha akatumia akili ya haraka kujibu. “Naomba tusitoe ahadi ya siku. Lakini niseme nilazima tutakuja kukutembelea nyumbani. Pengine tukitoka mapumzikoni kabla yakurudi Singida, tunaweza kuja kukuona bibi. Tutampitia mama ili atulete.” Mama Sabrina akajisikia vizuri sana. Wakapiga hapo vigelegele. Watu wakawageukia, Jack na mkewe wakazidi kucheka. “Asanteni sana.” Jack akashukuru tena na kuondoka na mkewe. Akiwa amemuwekea heshima kubwa sana Sabrina. 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment