“Sasa
naelewa ni kwa nini moyo wangu ulikuwa tayari kukusubiri miaka yote hiyo Brina
wangu.” Jack akaanza taratibu, mbele ya Sabrina aliyekuwa akitokwa na machozi na
wageni wote. “Unanikamilisha katika kila eneo la maisha yangu. Unanipenda kwa
dhati. Unanijali na kunitakia mema wakati wote. Unafanya mengiii kwa ajili
yangu Brina. Furaha yako ni kuniona na mimi ninafuraha, nataka mimi ndio niwe
mume wako mpaka kifo.” Watu wakashangilia sana. “Nataka mimi ndio nimiliki
upendo huo, mwingine asije kukuwahi. Nataka uwe mke wangu Brina. Utakubali nikuoe?”
Sabrina alilia mpaka akainama mbele ya Jack. Jack akacheka.
“Brina, will you marry me?” Ikabidi kijana huyo wa
Msindai, aweke msisitizo. Makubwa na mazito ambayo Sabrina alijua kwa hadhi
yake yasingeweza kumtokea ila watu wengine, akiamini kwa imani tu kuwa siku
moja yatakuja kuwa na kwake pia, kama wale warembo mashuhuri wa mjini.
Akimuomba Mungu siku moja yatokee na yeye kama alivyomwambia Tino mwanzoni
kabisa, kuwa yapo maombi anamuomba Mungu. Akamwambia Tino, hata yeye
angemwambia, angeona amechanganyikiwa, yaani mtu kama yeye Sabrina hayawezi
kumtokea. Lakini siku hiyo Mungu asiye na upendeleo amejibu. Sabrina anayashuhudia
majibu ya maombi yake kwa macho yake mwenyewe! Kilikuwa kipindi
kilichomuogopesha hata Sabrina mwenyewe mbele za Mungu.
“Sabrina?”
Jack akamwita kwa upendo. Akasema, “Yes Jack.”
Watu walishangilia sana. Jack akamvalisha pete, na kusimama kumkumbatia bila
kumbusu. Walishangilia watu. Wakapiga vigelegele na kucheza. Jack alimkumbatia
vizuri sana, kwa muda mfupi tu, akamwachia. “Baba aliniambia mpaka tulipe
mahari ndio utakuwa wangu. Nitakuja kudai busu langu, Mzee Msindai
akishanilipia mahari.” Jack akafanya waliokaribu wacheke na kushangilia. “She
said ‘Yes’, mama!” Jackson mtoto wa mama akamwambia mama yake kwanza kwa sauti.
“She said Yes.” Jack akaongeza sauti na kufanya watu wazidi kushangilia.
Wakacheza kwa shangwe, hata mzee Msindai alicheza na wanae. Kisha akaomba
kuzungumza.
“Sasa
kwa kuwa tushamuona mke wetu. Sasa tunaomba tumalizane kabisa, tumiliki
kihalali. Tumekuja tukiwa tumejiandaa. Si ndiyo Junior?” Baba yake akamuuliza
kijana wake mkubwa, Junior akasimama. Waziri huyo, kijana mdogo kabisa. “Ndiyo
baba. Sisi tupo tayari.” Akajibu nakufanya watu wazidi kushangilia. “Sijui
utaratibu wenu ulivyo, lakini tunaomba faragha wakati wakulipana ili kama
kunakushindwana, tumalizane kimya kimya kwa amani.” “Hatuwezi kushindwana!” Wakajibu
wakishangilia upande wa kina Sabrina.
Sabrina
akarudishwa ndani, ndipo sasa wahusika wa kulipa hiyo mahari na wazazi wa
Sabrina na wazee waliowachagua wao, wakaingia ndani pamoja na Mzee Msindai
mwenyewe, wazee wenzake waliomsindikiza, Junior na baadhi ya marafiki zake
pamoja na Jack akiwa na kina Felix rafiki zake na yeye. Ibra rafiki kipenzi wa
Jack hakuwepo. Mama msindai na mabinti zake pia wakafuata nyuma wakiwa wamebeba
masanduku ya maana pamoja na wanawake waliokuja nao. Wakazi wa Chalinze wakiwashangaa
jinsi walivyo wa mama wa maana. Ilijaa neema tupu kwenye hilo eneo. Wakakaribishwa
sebuleni ili walipe mahari.
Mzee
Msindai akamuachia Junior. “Kwanza tushukuru kwa kutukaribisha nyumbani kwenu
tuje kuoa, tena kwa muda mfupi sana.” Sabrina akiwa chumbani akawa akisikiliza.
Wamama wakapiga vigelegele. “Kama hakuna aliyetuhujumu kwa kufuta chochote
kwenye orodha ya mahari mliyotupa, mama alihakikisha imekamilika.” Wamama
wakapiga tena vigelegele. Junior akaanza kusoma kimoja baada ya kingine
wakivitoa nakumkabidhi baba na mama yake Sabrina. Wakaja swala la ng’ombe. Mzee
Msindai mwenyewe akatoa hundi. Akasema ni kwa sababu za kiusalama. Watu
wakazidi kushangilia huku zikipigwa picha nakuchukuliwa video. Ukafanywa huo
utaratibu mpaka wakamaliza. Wakwe wakaridhika. Ndipo wakasema sasa, wanaweza
wakaletewa hata maji wafurahie pamoja, kuunganisha undugu. Wakalifanya hilo
ndipo nyimbo zikaanza sasa wakitoka nje.
Walimuacha
Jack ndani ili atoke na Sabrina sasa, wakae sehemu maalumu iliyoandaliwa kwa
ajili yao. Walipotoka wote, ndipo MC akatangaza sasa, wote wasimame wakati Jackson
anatoka na mkewe. Akasema kimilia Sabrina
alishakuwa mke wa Jackson rasmi, ila kwa kuwa ni wakristo, wanasubiri kuwekewa
mkono kanisani, ramsi. Wakasimama, wimbo ukaanza kupigwa ndipo Jackson akatoka
na Sabrina. Wao wawili tu. Walipendeza sana. Sabrina alitoka akiwa amevaa gauni
lilelile zuri sana la rangi ya njano iliyotulia. Lilimkaa vizuri mno wala
usingejua ni mjamzito. Na rangi yake ya mwili, akazidi kupendeza. Jackson alivaa shati la njano ndani, nje suti
iliyokuwa imemkaa vizuri sana ya rangi ya bluu kama kaka yake, na baba yake
pia. Watu wakashangilia wakati wakitoka, wakacheza na kupiga vigelegele.
“Hapa
sikuachi mama. Nikiondoka leo, tunaondoka wote. Sirudi Singida bila wewe.
Usiniletee mchezo mimi!” Sabrina alicheka mpaka akainama mbele ya watu
waliokuwa wakiwashangilia. “Mimi nilifikiri mpaka ndoa!” “Subutu! Unataka
niahamie hapa nini? Tunaondoka Sabrina. Acha mambo ya kwenu yakusema
watakutunza mpaka ndoa. Nani atanipikia mimi?” Sabrina akazidi kucheka watu
wakiendelea kushangilia na kucheza. “Hivi unanielewa Brina?” “Bwana tutaondoka!
Acha kulalamika.” “Wewe mtu gani umeondoka nyumbani tokea alhamisi!” Sabrina
akazidi kucheka. “Emma amekula chakula chote! Inafika ijumaa nataka kula ndio
niondoke, eti hamna chakula!” “Haiwezekani Jack! Chakula chote kile?” “Wewe
unamchezea Emma? Mimi naomba turudi tu nyumbani haya mambo ya mila tutayafuata
tukiwa kwetu.” “Naona maharusi wenyewe wamefurahi sana.” Wakashitushwa na MC
alipoongea hivyo. Jack akapunga mkono na tabasamu lakuzuga.
Kukaliwa na kunywewa. Marafiki wa Jack wote waliofika hapo wakahamisha viti pale juu, wakaendeleza stori wakicheka kwa sauti tu. Kwa kuwa walimfahamu Sabrina tokea chuo, utani ukawa mwingi. Sabrina akapata nafasi ya kuwasalimia kwa karibu wazazi na ndugu wa Jack. Na yeye Sabrina akatambulisha wazazi wake na kaka yao na Sabina. Akawaambia wadogo zake wapo shuleni. Ndipo na wageni waliokuja wakajitambulisha sasa na kuacha wenyeji mdomo wazi. Watu wazito watupu ndio na nyadhifa mbalimbali ndio waliokuwepo hapo. Wake kwa waume.
Shuguli
iliisha. Mzee Msindai akatoa neno la shukurani. Kwa walio sindikiza pale na
wenyeji. “Mmetulisha na kutunywesha, tunashukuru sana.” Watu wakashangilia.
“Sasa huyu Jackson amesema hapa haondoki bila Sabrina.” Watu wakacheka na
kushangilia. “Na huyu Jackson ni mziwanda wetu. Mama yake anampa kile
anachokitaka.” Ndugu wakacheka sana na kushangilia, mama Msindai akacheka na
kutingisha kichwa. “Sasa mkimnyima Sabrina leo, Jackson atabaki hapa mpaka
mumpe mke wake. Na Jackson akibaki hapa, mama yake lazima atabaki hapa
kuhakikisha mnamlisha huyo mtoto wake.” Watu wakazidi kucheka. “Na mke wangu
akibaki hapa, inamaana kitanda changu kimehamia hapa, na mimi itabidi nibaki
hapahapa.” Watu wakazidi kucheka. “Sasa sidhani kama mnataka ugeni mkubwa
hivyo, tena wa muda mrefu.” Watu wakapiga makofi. “Kama kuna malipo mengine
yakututoza, mtutoze, sisi tuondoke na Sabrina, usiku wa leo kila mtu akalale kwake.”
Mzee Msindai alionekana mcheshi sana. Wakakabidhiwa Sabrina rasmi, wakaagana,
wageni wakaanza kupanda kwenye magari.
Sabrina akaomba kuzungumza na wazazi wake
ndani, pamoja na Sabina na kaka yake. Akawashukuru sana sana. “Hakuna jinsi
mnaweza kuelewa shukurani niliyonayo moyoni jamani. Asante kwa maandalizi
mazuri sana. Nyumba ilikuwa safi, pakapambwa vizuri kwa hadhi ya juu. Vyakula
vilikuwa vizuri. Jamani nashukuru sana. Na Mungu wangu awabariki. Jack
ananisubiri nje, lakini nitakapopata tarehe ya harusi, nitawajulisha. Kama
mlivyosikia, itafanyika Dar, ambako ndugu wengi na marafiki wa familia ya
Msindai wapo.”
“Huna
hata fununu ya tarehe?” Kaka yake akamuuliza. “Bado hawajapanga tarehe rasmi,
kwa kuwa Jack ameniambia mpaka kesho wazazi wakazungumze na mchungaji wao
ambaye kama ni rafiki wa familia, waombe atufungishe hiyo ndoa yeye, na pale
kanisani kwao, kwa haraka. Ikipatikana nafasi na huyo mchungaji, ndio
watatuambia. Kingine, ukumbi wanaotaka hao kina Msindai kwa tarehe hiyo
ulishakodiwa, upo wazi kwa tarehe za mbeleni sana. Jack hataki kusogeza mbele kwa
tarehe hizo, na ndugu wanataka huo ukumbi. Kwa hiyo kuna mambo wanamalizia
kuweka sawa. Na mimi nitaenda kuzungumza na Jack vizuri, nitawajulisha. Lakini
nawashukuru sana.” Sabrina mpaka akapiga magoti. Akawashika mkono wazazi wake
akitambaa kuwafikia. “Nashukuru sana kwa kujitoa kwenu kwangu.” Hilo likawagusa
wote. Ni kweli Sabrina alionyesha hakutegemea huo wema kutoka kwao. Wakumtakia
kila la kheri, wakamsindikiza kwenye gari ambalo alikuwa Jack na kina Felix.
Wakamuaga Sabrina kwa nyimbo zilizomfanya
mpaka Sabrina alie humo ndani ya gari. Wakazunguka hilo gari wakiimba nyimbo za
kumuaga Sabrina. Wakaimba kwa kucheza kwa muda, Jack akamvuta Sabrina kifuani,
akawa amemkumbatia kwenye hicho kiti cha nyuma, wakisikiliza wanavyoimbiwa. Mwishoe
ndugu zake Sabrina wakamaliza, wakaondoka wenyewe. Ndipo safari ya kurudi Dar
ikaanza Jack akiwa amemkumbatia Sabrina, asiamini kama ameagwa nyumbani kwa
heshima kiasi hicho. Kwa mara ya kwanza, Sabrina akajisikia kupendwa na
kuthaminiwa kwa hali ya juu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jack
na Sabrina walishushwa hotelini. Jack akafurahi sana. “Lakini hakuna kuvuka
mipaka Jack!” Jack akacheka sana. “Kwani mimi nimesemaje? Si nimesema mazingira
leo yametubananisha! Kwani umesikia nini?” “Wewe endelea kushangilia kama
sijakupandisha taksii na kukurudisha kwa mama yako.” “Utamnusa nani usiku kucha?”
Sabrina alicheka sana. “Halafu nilisahau kubeba ile tisheti yako.” “Niliiona
juu ya kitanda chako, nikajua haraka zimekuponza.” Wakazungumza usiku huo,
Sabrina akimshukuru Jack kumletea heshima nyumbani kwao. Jack akawa anacheka
tu.
Wakapanda
kitandani, Sabrina akajivuta mpaka kifuani. “Asante sana Jack.” “Na mimi
nakushukuru sana Brina. Hakika unanijali na kuniwazia yaliyo mema.” “Nakupenda
Jack.” “Na mimi nakupenda Brina wangu. Nilikwambia wakati Mungu alipokuwa
akikuumba alikuwa akinifikiria mimi?” Machozi yakamtoka Sabrina. “Ndio maana hukuwa
ukifiti au kuenea huko ulikokuwa ukienda kwa wanaume wengine. Kwa kuwa hapa.”
Jack akajionyeshea ubavu wake. “Hapa ndipo ulipotolewa na Mungu, ndipo
akakuumba.” Sabrina akajisikia vizuri sana. Akamsogelea mdomoni kuanza kupata busu.
Akaanza kusikia mikono ya Jack kwenye chupi. “Unakaribia kuhamia kwenye kochi
Jack.” Jack akacheka sana. “Kidogo tu Brina!” “Hapana Jack. Kumbuka jinsi Mungu
alivyosimama na sisi mpaka kufika hapa. Angalau na sisi tumuonyeshe
tunamthamini.” “Duuh! Mimi naona tuoane hata kesho bwana!” Jack akatoka
kitandani akilalamika. Akaenda chooni. Sabrina akaona amuache atulie.
Akatoka
mnyonge. “Njoo nikubembeleze ulale Jack wangu.” “Wewe ukinigusa unanifanya
nikutake zaidi. Halafu nikikutaka unamwita Mungu mpaka napata hukumu!” Sabrina
alicheka mpaka akatokwa na machozi. “Jack!” “Mimi naona tuone tu haya mambo
yaishe.” Akachukua shuka akahamia kwenye kochi. Sabrina afikiria, akamuhurumia.
“Njoo ulale hapa, sitakupapasa. Usilale kwenye kochi.” Kama mtoto mdogo,
akarudi akilalamika. Sabrina akampa mgongo akiwa ameshika shati alilokuwa
amevaa Jack siku hiyo, akawa ananusa. Jack akamuwekea mkono juu yake. “Kesho
baada ya kifungua kinywa kwa mama, tunarudi Singida.” “Uliniambia. Ila
naogopa?” “Ndio utapata nafasi yakuwafahamu ndugu zangu kwa karibu.” Sabrina
akanyamaza.
“Acha
woga wewe. Utakuwa na mimi. Kwanza mwanangu anaendeleaje?” Sabrina akageuka na
kumuachia tumbo. “Vizuri. Nahisi nyumbani hawajagundua.” “Kwani hujawaambia!?”
Jack akashangaa. “Namwambia nani Jack? Wale watu yaani jana na leo ndio
nimeweza kuona ukaribu wao kwangu. Halafu sikutaka kumfanya da Sabina ajue,
halafu apige mahesabu. Aanze maswali yake, halafu ugundue mimba ni ya nani. Sikutaka
kufanya hilo kosa.” Jack kimya.
“Nataka
Tino asiwahi kuja kujua kama ninaye mtoto wake. Kama vile alivyokusudia tumuue
huyu mtoto, ndipo alipoua mahusiani na huyu mtoto. Najua kwake ndio itakuwa
nafuu, lakini wakati anakuwa huyu mtoto, kabla hajajua kwa kuambiwa na watu,
baba atakayekuwa akimfahamu ni wewe tu. Hata iweje, itabaki hivyo.” Jack
akajisikia vizuri sana. Akaendelea kumpapasa tumboni. Akakumbuka alivyowaambia
familia yake kuwa huyo mtoto atakuwa Msindai. “Akiwa wa kike tutamuita nani?”
Jack akauliza. Sabrina akacheka taratibu. Jack akambusu tumboni. “Eti
nilifikiria tumwite Brina.” Jack akashituka sana. “Acha masihana Brina! Brina
ndio jina langu kwako! Mwenyewe nikikuita hivyo najisikia vizuri zaidi ya
kukuita mpenzi, sijui honey au sweetie! Brina jina lako wewe. Acha kabisa.”
Sabrina akacheka sana. “Basi mwenzio ndio nilifikiria kumwita hivyo.” “Hapana.
Tufikirie jina jingine.” Wawili hao wakaanza kuzungumza kama wazazi kweli.
Gafla hali ya kumilikiana kama wanandoa kweli na wazazi ikawaingia. Wakalala
kwa furaha, wakimshukuru Mungu kuwavusha hatua ya kwanza.
Sabrina
ukweni.
S |
abrina na
Jack walifika nyumbani kwa wazazi wao mida hiyo ya saa tatu na nusu asubuhi,
wakakuta wote walishafika. Jena akaanza kwa vigelegele. “Acha bwana Jena! Sasa
vigelegele vya nini?” Jack akakataa. “Huyu bwana harusi vipi?” Wakaanza
kucheka. “Sasa hapa unaona kuna harusi kama sio kutaka kumtia wasiwasi Brina
wangu?” Jena akaendelea kupiga
vigelegele. “Unakera wewe!” Jack akapitiliza chumbani. “Huyu mbona anazunguka
na suruali na singlendi tu? We Jack?” Mama yake akamwita alikuwa jikoni
alimuona akipita. “Navaa mama!” Jack akajibu akiwa chumbani. “Kwa nini
unazunguka uchi bwana!?” “Sikubeba nguo jana, nilikwenda hotelini nikiwa na
suti tu.” Wote wakacheka mama yake akaguna. “Sasa si ungevaa koti, kuliko
kubeba tu koti mkononi!?” “Mama ameanza. Mwanao anaoa huyo. Sio mtoto.” “Sasa
ndio aoe huku anakohoa! Anazunguka jiji zima kifua wazi bwana!” Akalalamika
mama Msindai. Sabrina akajua kazi atakuwa nayo.
“Naomba
mumleteeni chai ya moto. Ashaingiwa na baridi.” Wote wakashangaa. “Hivi ujue
mama mpaka wajukuu pia hawajala, tulikuwa tukiwasubiria hawa maharusi!” Juniour
akaongea nakufanya mpaka baba yake acheke. “Sasa nyinyi si mmevalisha watoto
wenu nguo! Jack atakuwa ameingiwa baridi.” Kila mtu akaanza kucheka. Sabrina
hakujua kama huyo mama yuko kwa undani hivyo kwa Jack. “Huko nje ni jato mama
Msindai. Acha wasiwasi.” Jack akatoka akiwa amevaa suruli ya jinsi na tisheti.
“Sasa
ngoja nikutambulishe rasmi, Sabrina.” Jack akaaanza. Akatambulisha mmoja baada
ya mwingine mpaka mwisho. Wakaonekana kumchangamkia Sabrina vizuri tu. Jacinta,
Joy na Jena wakamuuliza maswali machache juu ya nini anafikiria kwenye harusi
yake. “Ile njano uliyovaa jana ilikupendeza sana. Unaweza kufanya rangi ya
harusi ikawa hiyohiyo, au unasemaje?” Jena akamuuliza Sabrina. “Itapendeza
kweli?” Sabrina akauliza akiwa ametulia tu. “Ipo njano fulani hivi. Ikiwekwa
vizuri, itafanya ukumbi upendeze. Au Jack na wewe unasemaje?” “Mimi ninachotaka
harusi iwe ya haraka, na Sabrina awepo. Rangi yeyote ile mimi kwangi sawa.”
Wakacheka na kujaribu kuweka mambo sawa.
Wote
walikuwa wamevaa nguo za kanisani tayari kwenda kanisani muda ukifika. Joy
akapata nafasi ya kumuombea mtoto wake. “Naomba kiziwanda wa dady na yeye asimamie.”
Sabrina akashangaa wote wanacheka mpaka Junior kaka mkubwa. “Mimi
nitapendezesha harusi, Antie.” Wakazidi kucheka. “Ataharibu huyo. Kwanza bado
analala mchana. Asipolala, anaanza kulia hovyo hata shule wanamjua, ikifika
mchana anaanza kunyonya vidole.” Kaka yake akaingilia, wakaanza kubishana.
“Sasa wewe utalia, Cleiton.” Joy akamtisha mtoto wake wa kiume. “Kwani uongo
mami? Atasimamia harusi huku ananyonya vidole? Claire ataharibu harusi huyo.” Claire
akaanza kulia.
“Bwana
Cleiton utalia wewe mtoto wewe!” Mama yao akamtisha tena. “Sawa mami. Lakini
mtakuja kunikumbuka mimi. Si unamuona
anavyolia hivyo, basi anti Sabrina, uliaji wake ni hivyohivyo. Kitu kidogo tu
mwenzio analia. Sasa usishangae katikati ya harusi anaanza kukulilia.” Watu wakazidi kucheka, Joy akaanza kumkimbiza
mwanae wa pili huyo Cleiton. “Nikikukamata wewe!” Joy akatisha, Cleiton
akakimbilia chumbani. “Mwanangu halii hovyo, si eti mama yangu mzazi?” “Mimi silii hovyo, dady. Clei ndio mchokozi.”
“Basi nyamaza ili anti akuone hulii hovyo. Njoo mama.” Baba yake akamuita.
Akaenda na kuanza kunyonya kidole chake gumba. Kila mtu akaanza kucheka. “Sasa
haya si ndio aliyokuwa akiyasema mwanangu Clei, mkaishia kutaka kumpiga?”
Jacinta akaongea kwa sauti ya chini wote wakamwangalia Claire nakuzidi kucheka.
Kidole mdomoni, analia huku baba yake amempakata akimbembeleza. “Hapo ndio
katikati ya harusi, hali imemjia hivyo.” Jena akaongeza nakufanya wazidi
kucheka. “Mnamuharibia mwanangu soko jamani! Hatalia. Si ndio mama?” “Mimi silii mami!” Akajibu Claire huku akilia, wakazidi
kucheka.
“Hata
hivyo bado hatuna wasimamizi, kwa hiyo naona tutamuhitaji tu Claire.” Sabrina
akaongea huku akicheka. “Kwanza njoo nikuone msimamizi wangu.” Jack akamuita.
Claire akatoka kwa baba akahamia kwa anko wake na kidole mdomoni. “Una nywele
nzuri Claire!” Jack akamsifia. “Asante.” “Toa sasa kidole mdomoni ili Clei
asizidi kukucheka.” “Clei mchokozi anko!” Akamsemelea kwa Jack. “Sasa mama atamchapa.
Ushajua utavaa gauni gani siku ya harusi?” Wakamuona anacheka. “Kwanza nywele
zangu nzuri, nitazibana.” Wote wakazidi kucheka. Huyo mtoto ni mrembo na alijipenda
sana. Alifanana na mama yake wala si baba. Akajielezea atakavyopendeza wote
wakimsikiliza na kucheka.
Wakapata
wakati mzuri. Wakala pamoja. Sabrina aliona ni familia ya kawaida tu sio kama
ukubwa wa jina lao. Walikuwa waungwana. Ila macho ya mama yao ukweli yalikuwa
kwa Jack muda wote. Mara amshike. Mara ampanguse hapa na pale, ilimradi tu.
Wengine hawakuonekana kushangaa, hata Jack mwenyewe alitulia tu akiendelea na
mambo mengine huku mama yake akimfanyia hili na lile, ila yeye Sabrina ndio
akawa anashangaa sana vile Jack anavyofanywa kama mtoto mdogo! Muda wa kwenda
ibadani ulipofika, wao walipelekwa uwanja wa ndege na dereva, wengine wakaelekea
kanisani.
Sabrina&
Jack.
J |
ack na Sabrina
walirudi Singida, kila mtu akajua wamechumbiana. Walionyesha picha nyingi na
kuwaambia watu karibuni sana watafunga ndoa. Ni kweli heshima iliongezeka hata
wao waliona. Vile walivyoanza kumchukulia Sabrina, kila mtu kwa heshima kama
mke wa Msindai kweli. Hata vijana walimsikiliza kama mke wa Msindai.
Ikamuongezea heshima na nguvu ya amri kuongoza. Na kwa Jack vile vile ofisini.
Bado pongezi ziliendelea kila leo wakimtania kwa hili na lile. Mambo ya
maandalizi yote yakaendelea. Simu za hapa na pale wakiulizwa hili na lile juu
ya harusi yao navyo vikaendelea.
Kanisani
walishaanza kutangaza ndoa yao. Na wao wawili wakaanza kwenda kanisani pamoja. Siku
moja walipotoka kanisani Sabrina akiwa amekaa tu kwenye kochi, akaanza kusikia mtoto
anacheka. Alishituka mpaka akasimama. “Nini!?” Jack akamuuliza. “Nimesikia
mtoto akicheka.” Akaingiwa hofu. “Njoo bwana! Ndio kitu kizuri.” Jack akasimama
na kumvuta arudi kukaa. Akaweka mkono hapo kusubiria kucheza. Akacheza tena. Yeye
Jack akaanza kupiga kelele. “Acha bwana Jack!” Emma akatoka kwa haraka. “Mtoto
ameanza kucheza na mimi nikiwepo.” Jack akafurahia kuliko Sabrina mwenyewe.
Sabrina akashangaa anapiga simu. “Ni nani unampigia?” “Mama!
Mama!” Sabrina hakuamini alipokuwa akimwita mama yake. “Mwanangu amecheza, nimemsikia.” Mpaka Sabrina
hakuamini. Akamsikia mama yake akicheka. “Hongera.
Ameshaanza kliniki?” Mama yake
akauliza. “Bado. Lakini nimepatwa hamu yakumuona.
Anacheza bwana!” Akacheza tena, Jack akaona. Akaweka simu pembeni
akarudi tumboni.
“Naona
leo mwanangu ameamua.” Jack akarudi tumboni akicheka kwa furaha mpaka Emma
alikuwa akimshangaa. Wakati anakua Jack, alikuwa akimuomba sana mama yake atafutiwe
mdogo wake. Kwa hiyo akakua akipenda sana watoto tangia mdogo. Ilikuwa
akipelekwa nyumba zenye watoto, kuaga ilikuwa shida. Akammliki huyo mtoto,
akajawa furaha kama wake. Kila alipokuwa akicheza, Jack alitaka amshike. Naye
Sabrina anaegesha tumbo, Jack anashangilia hapo.
Wakati
familia ya Msindai wakihangaika na maandalizi ya harusi ya baada ya mwezi na
siku, Sabrina na Jack wakaendelea kuimarisha kambi ya chama. Kwa muda mfupi tu,
wawili hao wakaweza kuwa na kitu kinachoeleweka. Miradi miwili wakaifufua na
timu ikawa ikifanyiwa mazoezi ya uhakika maana walikuwa na kocha wakueleweka.
Minong’ona ikaanza. Vijana wa chama wakaanza kujisifia mtaani. Jina la Jack na
Sabrina kuwa wanafanya mambo makubwa likaanza. Sabrina alifanya bila kuchoka,
huku akimtia moyo Jack.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ujauzito
ulipofika mwezi wa tano na siku chache, na Jack kuona vurugu huko tumboni
zinazidi, akamlazimisha Sabrina waanze kliniki. Sabrina ndiye aliyekuwa akiona
uzito wa kuanza. Kwa kuwa hakuwa na mabadiliko makubwa sana zaidi ya kuanza
kuchoka, kulala sana, hakuona mabadiliko makubwa zaidi, kwa hiyo akawa
anamwambia Jack nitaanza kesho, au jumatatu. Jumatatu ikifika jumatano.
Jumatano ikifika basi atamwambia asubiri tena jumatatu. Akaendelea kusogeza
mpaka Jack akachoka akaona aingilie kati, kwani mama Msindai naye akaanza
kuweka pressure akitaka Sabrina aanze kliniki. “Tumechelewa sana. Hakuna mama
anaanza kliniki akiwa na mimba kubwa hivyo Brina. Si sawa kwako wala mtoto.”
Hapo Sabrina akaamua kwenda. Siku hiyo Jack akaongozana naye. Hakutaka kuja
kuambiwa hakwenda. Alikwenda kazini kuripoti, ndipo akarudi kumchukua.
Tumbo lilishaanza kuonyesha kabisa mpaka
Sabrina akawa analalamika lipo kubwa zaidi ya wakati wake. Alishabadilisha
mavazi, akawa akivaa nguo za ujauzito. Na kwa kuwa alikuwa mwembamba, huulizi.
Unaona tu. Kama kawaida ya utaratibu wa wakinamama wengine. Kupimwa mkojo,
pressure na uzito. Akatakiwa kwenda kupimwa na damu kabla hajaingia kwa
daktari. Sabrina akafanya yote hayo wakiongozana na Jack. “Nachoka haraka siku
hizi! Kama ambaye nimelemewa wakati bado kabisa!” “Mimba ya miezi mitano Brina.
Usiseme bado.” Alipimwa kila kitu akabaki akisubiria kwenda kwa daktari.
Zamu
yao ilipofika, kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza huyo daktari akasalimiana nao na
kuuliza maswali machache. Akawapa majibu. Damu tu ndiyo aliambiwa nilazima
aanze kutumia vidonge vyakuongeza damu na vya virutubisho kwao wote wawili.
Mama na mtoto. Ndipo akaambiwa apande kitandani asikilize mapigo ya mtoto. Wakamuona
daktari anarudia tena na tena kumpima na kusikiliza mapigo ya mtoto mpaka
akawatia wasiwasi Jack na Sabrina. “Kwema?” Ikabidi Jack aulize. “Nyinyi mnajua
kama wapo wawili hawa?” Sabrina alishituka mpaka akakaa, Jack akasimama.
“Mapacha!?” Akauliza Sabrina kwa mshituko kama anayetaka kuanza kulia. “Ndiyo.
Kwani hamkuwa mkijua? Rudi kulala nikuonyeshe.” Sabrina akabaki amekaa akiwa
ameduaa. Jack akamsogelea. “Naomba niangalie mimi Brina.” Sabrina akaanza
kutokwa na machozi. “Niangalie mimi.” Sabrina akainama akitetemeka. “Maadamu
kila kitu kipo sawa, acha sisi tuondoke, tutarudi wakati mwingine. Nashukuru
sana.” Jack akaaga huku akimsaidia kumvalisha Sabrina, daktari akishangaa.
Akamsaidia
kushuka pale kwenye kitanda, Jack akaaga baada yakukusanya kila kitu, akamshika
mkono na kutoka naye akiwa yeye ndio amebeba kila kitu. Akamsaidia kupanda
kwenye gari, wakaondoka. Alikwenda kununua dawa alizoandikiwa Sabrina. Akapitia
sokoni kununua matunda. Akaongeza juisi kwa ajili ya Sabrina kumsaidia kuongeza
damu. Wakarudi nyumbani. Sabrina akaongoza njia moja kwa moja chumbani kwake.
Jack akamfuata.
“Naomba
niambie hofu yako ilipo Brina. Bila kunificha.” Jack akakaa pembeni yake pale
alipoinama akilia kitandani. “Naona mimi sitaweza
Jack?” “Kuwa muwazi zaidi. Kwamba hutaweza kuwabeba sasa hivi, au
kujifungua, au unamaanisha kunyonyesha?” Sabrina akazidi kulia. “Naomba
tuzungumze bila kupaniki mama. Maana mimi nauona uwezo mkubwa sana ndani yako.
Umekuja kufufua ari mpya ndani yangu. Umefufua miradi iliyokuwa imekufa ya
chama. Umemudu kuwa katikati ya wale wanawake wenye midomo michungu kama
shubiri!” Sabrina akaanza kucheka huku akilia.
“Kweli.
Imani mwenyewe alishawashindwa, ndio maana umeona chama kilikufa sababu ya
maneno yao. Wewe ukaweza. Sasa nataka kujua kwa ukweli kabisa, ugumu huu
uliokushitua ni upi? Na kama nikuzaa, nilisikia siku hizi wanachoma sindano za
kukata maumivu. Dar lakini. Sijui hapa. Unajifungua vizuri bila shida wala
maumivu. Sasa naomba nipe hofu yako nyingine.” “Sikutaka
kuwa na watoto wa Tino wawili?” Sabrina akaongea akilia sana.
“Watoto
wa Tino wapi tena mbona unanichanganya!?” Jack akamfanya Sabrina ashituke.
“Tino aliua watoto wake. Alikuacha akiwa ameridhia ameua watoto wake. Mimi nipo
hapa na wewe, nikijua tumekubaliana kuwa watoto hao ni kina Msindai. Kila mtu
namwambia nasubiria mwanangu, kumbe mwenzangu moyoni umenikataa!” “Sijakukataa Jack.” Ikabidi Sabrina akae kwa
haraka. “Kumbe ni nini? Si umetoka kusema ulitaka kuwa na mtoto mmoja tu na
Tino!? Au mimi sikuwa nimesikia vizuri!?” Jack aliongea kwa mshangao na kuumia
sana. Ikabidi machozi ya Sabrina yakauke.
“Naomba usiumie Jack. Mimi nilikuwa
nakuhurumia wewe. Niliona ni kama nakupa mzigo mzito sana. Utalemewa kwa watoto
wawili!” “Ambao ni wa Tino au wangu sasa!? Maana naona gafla nipo njia panda,
sijui nafasi yangu tena! Nilijua huko tulishapita muda mrefu sana. Nasubiria
watoto kumbe mwenzangu moyoni unajua si wangu!” Jack akasimama. “Ulinidanganya
Brina.” Jack akalalamika. “Sijakudanganya Jack, naomba utulie.” “Hapana. Leo
umezungumza moyo wako.” Jack akaonekana ameumia kupita kiasi, Sabrina hakuelewa
kama neno dogo vile linaweza kuchukua maana ya tofauti.
“Unakumbuka
usiku ule baada ya kukulipia mahari tukiwa mimi na wewe hotelini ulisema nini?”
“Naomba Jack utulie mpenzi.” “Hapana Brina. Naomba zungumza ukweli wako. Usije
kuniumiza baadaye. Ulisema nini juu ya huyo mtoto au hao watoto?” Sabrina
akajua ameshaharibu. “Niambie ukweli Brina.” “Nilisema baba watakayemfahamu ni
wewe, mengine watasikia kwa wengine lakini si kwangu.” Jack akapandisha nyusi
zote juu kama anayemsuta. “Sasa, sasahivi Tino anaingiaje hapa?” Jack akauliza.
Sabrina kimya. “Brina? Tino anaingiaje hapa?” Sabrina akabaki akifikiria.
“Sikujua
kama ndivyo unavyofikiria moyoni mwako! Na ndio maana japokuwa tumelipa mahari
na kila kitu kilichohitajika kwa wazazi wako na baba yangu alitangaza pale
hadharani mpaka Mungu akasikia kuwa Jack haondoki hapa bila mke wake! Lakini upo
radhi mimi nikalale kule peke yangu, wewe ulale hapa, ukimtumia Mungu kama
sababu kumbe ni kwa sababu umenikataa moyoni! Ndio maana hutaki hata nikuguse!”
Jack akaendelea kulalamika. Sabrina akabaki amekufa ganzi hajui aseme nini.
“Unajua
nini Sabrina, mimi nimefanya kwa sehemu yangu bila unafiki wala kificho moyoni.
Nakuachia wewe uamue. Na naomba jibu la haraka tafadhali, ili nisikupotezee
muda wako na muda wa wazazi wangu wanao hangaika sasa hivi kuandaa harusi yetu.
Pata muda wa kujifikiria, kisha jioni nikitoka kazini, utanijibu. Sitakulaumu.
Maana najua, unaweza kumpeleka punda kisimani, lakini huwezi kumlazimisha
kunywa maji. Sina uwezo wa kukufanya unipende na kunihitaji kwenye maisha yako.
Nashukuru Mungu nimefanya kwa nafasi yangu. Na Mungu anajua jinsi
ninavyokupenda Brina. Sijawahi kumpeleka msichana nyumbani kumtambulisha rasmi
ila wewe. Nimefuata hatua zote mpaka nikakabidhiwa wewe rasmi kama mke, lakini
bado tu!” Jack akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati kina Msindai wakiandaa
harusi ya kijana wao, huku nako kwa bibi harusi na bwana harusi maisha ya ndoa
yanaendelea kama kawaida. Ugomvi wao wa kwanza huo. Maneno yakitamkwa huwa
hayarudi. Kipi kitaendelea kwao kwenye vita ya ndani baada ya Jack kushinda ya nje,
ambayo ilikuwa ya nyumbani kwao mpaka
kufanikisha kulipa mahari? Harusi ipo? Usikose muendelezo…
0 Comments:
Post a Comment