![]() |
H |
awakujua Nelly,
dada yake Jax alipotokea, wakashangaa anaegesha gari kwa fujo pembeni ya gari
ya Jax. Akashuka. Jax mwenyewe akaonekana ameshituka. Akamwangalia Tino. Tino
akarudi nyuma kabisa. “Kuna nini?” Akauliza Nelly. Tula akatoa mikono pale
dirishani kwa haraka. “Tula..” Jax akataka kujibu lakini dada yake akamwangalia
kwa ukali. “Ninapozungumza na wewe, usikae ndani ya gari ukinichungulia nje
wakati mimi napigwa na jua nje.” Kwa
haraka Tula akampisha Jax mlangoni, akashuka. Lakini gari aliliacha likiwa
linawaka. Lara akabaki ndani akitetemeka.
“Nilikuja ku..” “Sijakuruhusu uzungumze na mimi. Nyamaza.” Akamkata Tula, akamwangalia Jax. Jax akajua ndio anaulizwa yeye. “Nilitoka ofisini, nikaenda kumchukua Lara ili nimpeleke hospitalini akaangaliwe afya yake. Lara bado anasikia baridi hata kwenye jua.” “Hana damu.” Dada yake akaongeza. “Ndilo hilo nilihisi. Tukakazana na matunda na juisi ya kuongeza damu, sasa hivi ni kama miezi miwili, bado hali yake ipo vilevile.” Nelly akamwangalia Lara ndani ya gari, Lara akainama.
“Sasa hakuwa amekula.” Jax akaendelea. “Nikasema nimlete hapa ale
kwanza kabla ya kwenda hospitalini. Hata hatujaanza kula, Tula akanifuata hapa
kuwa ni mjamzito mimba ni yangu.” “Anajuaje kama mimba ni yako!?” Akauliza Nelly
kwa kushangaa. “Mimba ni...” “Sijakuuliza wewe. Nazungumza na Jax. Nyamaza
kabisa.” Wakamsikia Tino anacheka. “Mimi sijui dada yangu! Ila nilimwambia
sikatai majukumu kwa mtoto wangu. Mtoto akizaliwa na akawa ni wangu, nitamtunza
mtoto wangu. Akauliza kwa sasa hivi yeye ataishi wapi?” “Kwani mliishia wapi?
Si mlikimbia mkaenda kuishi pamoja?” Tino akakohoa. Na Nelly alimuuliza kwa
kumkejeli tu. Hakuna linaloendelea kwa huyo mdogo wake asijue. Zaidi aliporudi
Tula.
“Alishaondoka nyumbani kwangu. Siishi na Tula. Lakini napo hapo
nilimwambia anayo magari yangu mawili. Moja alilochukua kwa Lara, na jingine
nilimnunulia wakati naishi naye. Ndio nikamwambia atafute kazi, na wakati
anatafuta kazi, ayafanyie hayo magari biashara mpaka atakapojifungua na
kuthibitika mtoto ni wangu.” Akataka kubisha lakini akasita, akakumbuka
aliambiwa anyamaze. “Muulize Lara kama sijamuhakikishia kuwa nitatunza mtoto kama
ni wangu?” “Lakini..” “Nitakubamiza Tula, mpaka nikuvunje taya! Acha kutufanya
sisi wote hapa watoto wadogo. Nimekwambia nyamaza. Huna adabu wewe!
Hujafundishwa kwenu jinsi ya kusikiliza watu wakiongea?” Nelly akambadilikia,
mpaka Jax akarudi nyuma.
Akamtizama Jax. Jax akajua ndio anatakiwa kuendelea. Hakupoteza muda,
akaendelea. “Akaanza fujo pale ndani, mpaka Tino akaja. Tukazungumza na
nikamwambia Tino, na wewe nakwambia dada Nelly. Nimemalizana na Tula. Kama
mtoto kweli ni wangu, nitamlea mwanangu bila shida. Lakini sitarudi kuwa na
mahusiano na Tula. Hata leo mkisema nirudiane na Tula sababu ya hili, kweli
mnataka watoto wangu wazaliwe waone
jinsi ninavyodhalilishwa kila siku? Nitakuwa baba wa namna gani mimi? Hapajawahi
kuwa na mahusiano kati yangu na Tula. Ila yeye Tula akitaka nifanye anachotaka
yeye! Hata yeye amekiri kwangu.” Jax akaendelea.
“Matusi anayonitukana Tula, hata kama ninastahili, nimeishi na Lara
karibia miaka miwili, mbona yeye hajawahi kunitukana hata mara moja?” “Hilo
umelikumbuka lini?” Dada yake akamuuliza kwa kumsuta huku akimwangalia machoni.
Tino akacheka kiumbea taratibu huku akijificha. “Si ndio nimegundua kosa dada
yangu! Nipo kwenye kurekebisha. Hata Lara nimemuomba anipe muda nirekebishe.”
“Muda wa kurekebisha wakati hawara yako anamkera? Anafikiria saa ngapi huyo
Lara wakati unamletea mahawara zako karibu? Nilikwambia nini Jax?” Dada yake
akawa mkali.
“Nakwambia ukweli dada yangu. Mimi sijamleta Tula karibu na Lara.
Lara ni shahidi yangu. Tula amenifuata mwenyewe. Na Tula huyu hapa, muulize
kama sikumpiga marufuku asiwahi kumfuata tena Lara. Muulize.” “Sina muda
wakijinga mimi.” Akafyonza Nelly na kuendelea. “Alimfuata Lara ofisini akimdai
gari, ukaendelea kumchekea huku ukimbembeleza! Amepewa tena gari na pete bila
kukwambia, ukajua, bado unamchekea! Unafikiri ni kipi kitakachomfanya aelewe
sasa hivi kama unamaanisha?” Dada yake akamuuliza kwa ukali.
“Lakini nilimfukuza.” Jax
akajitetea kama mtoto mdogo mbele ya dada yake. “Ulimfukuza au ulimtolea nguo
nje akiwa ameondoka?” Jax akashangaa kidogo. “Unafikiri mimi sijui?” Akamuuliza kwa ukali. “Wewe mwanaume mzima,
upo nyumbani kwako, unamfukuza hawara. Hawara anakwambia hatoki, ulivyo mjinga
wewe, unasubiri aondoke, ndio unamtolea mizigo nje na kuwaomba walinzi
wakusaidie kumzuia kuingia ndani! Anapelekwa polisi, unaenda kumtoa! Kama huo
sio upumbavu na ujinga wa kupindukia wa kupigwa makofi ni nini?” Nelly
akamuuliza kwa ukali.
“Halafu eti leo upo na mwanamke wako, yeye anakuzuia kuondoka, na
wewe ulivyo dhaifu unaita askari wakusaidie kumtoa! Una nini Jax!? Upumbavu huo
umerithi wapi wewe? Unarudi kwa Lara, ili iweje wakati hata wewe mwenyewe
hujielewi?” “Najielewa?” Jax akajitetea. “Mbona umeshindwa kumtoa hapa Tula?” Kimya.
“Anakudharau kwa sababu anakujia upo dhaifu! Once and for all, simama
kama mwanaume. Muonyeshe wewe ni mwanaume unayejielewa uone kama atakufanyia
michezo ya kipuuzi. Ameshakusoma na kukujua wewe ni dhaifu sana.” Nelly
akaendelea.
“Hujui hali yake Lara kwa kuwa hukuwepo kushuhudia madhara
uliyoyasababisha baada yakupotea. Tino alimuona. Kwa kifupi tu. Ulimdhalilisha
vibaya sana mpaka kuugua. Ya pili ya mtoto wenu. Nafikiri hilo unalijua na ndio
maana yupo na hiyo hali mpaka sasa. Ya tatu ndiyo hii inatokea hapa mbele yetu.
Na mimi nashuhudia! Unaacha hawara, mpumbavu kama huyu, anaongea na mwanamke
wako ambaye ni mdhaifu, kwa kumsababishia wewe mwenyewe, na wewe umetulia tu
ndani ya gari! Inatofauti gani na mama?” Jax akanyamaza ila mpaka macho yalikuwa
mekundu. Kimya, akainama.
“Umelaaniwa na nani wewe mtoto?” Kimya. Jax akabaki ameinama. “We
Jax?” Akamuita kwa ukali kila mtu akashituka. Jax akamwangalia dada yake.
“Mwanaume gani unashindwa kulinda watu wa nyumbani kwako wewe! Ulishindwa kwa
maamuzi ya kufunga zipu ya suruali tu. Ona yanayokupata! Unafuatwa na mimba
mpaka baa! Umelogwa wewe! Una hamu gani usizoweza kuzizuia?” “Mimi sio muhuni
dada.” Jax akajitetea. “Kama sio hukumu
ya kumsaliti Lara baada ya kulala na Tula, na kushindwa kurudi kwake, ukajificha
mpaka mwenzio Tino kukufuata na kukulazimisha ni lazima ukaonane na Lara
uyamalize kiume, ni nini?” Kimya.
“Kama wewe mwanaume kweli, mbona ulishindwa kumfukuza Tula nyumbani
kwako, ukasubiri mpaka aondoke ndio mtupie nguo nje? Kama kweli wewe mwanaume
kweli, mbona amekushinda hapa kumtoa?” “Naomba unisikilize dada Nelly. Tula ni
mzushi na muongo. Muulize Tino. Niliogopa nisije nikafanya chochote hapa,
akanisingizia jambo kubwa na baya zaidi hata kufungwa jela.” Jax akajitetea.
“Nakuhakikishia dada yangu, simu ambayo ungeipata sasa hivi baada ya
mimi kumtoa Tula hapa, ingekuwa unifuate jela, wala sio hapa. Tena akiwa
amenisingizia jambo zito sana. Mimi namjua Tula kwa kuishi naye.” Jax
akaendelea. “Nimeamua kuishi maisha ninayoyataka mimi bila yeye kunifanya
mtumwa zaidi. Sikubali mitego yake tena. Ndio maana kwa amani kabisa, nataka
kuachana naye. Mimi sio mjinga, ila nafanya ili kujinusuru mimi mwenyewe.
Nisipokuwa mwangalifu, Tula anaweza akanifunga dada.” Nelly akamgeukia Tula.
“Gari ya Lara liko wapi?” Nelly akamuuliza. “Lara hakunipa gari
mimi.” “Haaa!” Kila mtu akashangaa. “Mnashangaa nini? Lara anadanganya,
hajanipa gari. Labda amehonga wanaume zake. Kama ningekuwa na gari yake si hata
Jax angeiona!” “Tula!” Jax akashangaa sana mpaka Lara ndani ya gari akahisi
hajamsikia vizuri.
“Subiri kwanza Jax.” Nelly
akataka atulie. Akamgeukia tena Tula. “Gari aliyokupa Jax iko wapi?” “Gari
aliyonipa Jax?” Na yeye akamuuliza swali lile lile, Nelly akabaki akimwangalia.
“Lipo.” Akajibu. “Lakini ni langu. Nina haki nalo maana niliishi na Jax kama
mkewe. Na Jax ananipenda, anachohitaji ni kukumbushwa tu.” “Nakupa dakika tatu,
mkumbushe.” Akaanza kubabaika.
“Sasa hivi hawezi akiwa kwenye hali hiyo. Na hasa Tino akiwepo.” Kila
mtu akashangaa. “Subirini kwanza.” Nelly akawatuliza. “Tino yuko pale nyuma.
Hajaongea chochote. Na hataongea chochote. Wewe ongea na Jax hapa. Na ninamaana
yangu, maana leo nataka kuweka kikomo. Huu mchezo mnaotaka kumchezea Lara,
nyinyi wawili, sitauruhusu.” “Kabisa dada Nelly.” Akaitikia Tino.
“Maana nyinyi wawili haya ni maisha yenu yatokea enzi na enzi. Mmeona
havinogi tena, mnataka kuongeza mtu mwingine katikati yenu wa kumvuruga akili.
Sasa leo nataka kuweka kikomo. Ni aidha mnaondoka nyinyi wenyewe wawili,
mkaendelee kutoana roho, na mumuache Lara kabisa. Kwanza Lara mrembo sana, hata
mimi naweza kumtafutia mwanaume anayejielewa akamuoa aachane na ujinga
huu!” Akamnyooshea kidole mdogo wake.
“Lara ni wangu mimi. Na mimi nimeamua kutulia na Lara. Mimi nimeharibu, na
nitatengeneza mimi mwenyewe. Na nimeapa. Iwe na Lara au mwanamke mwingine, mimi
nitaanzisha familia, na wewe Tula hutakuwepo. Hakuna atakachozungumza sasa
hivi, kikanibadilisha msimamo.” “Unauhakika?” “Ndio dada.” Akajibu kwa
kujiamini.
“Hata itokee hapa ni chumbani na kitanda kipo pembeni yenu na yeye
yupo uchi?” Mpaka Tino akacheka kwa sauti. “Mimi sio mdhaifu wa ngono.” Akajibu
Jax akijitetea. “Nakuuliza Jax, usinichezee akili.” “Ndiyo dada. Hata kama tupo
peke yetu, sehemu ya faragha, sitabadili mawazo. Nina uhakika na ninachokujibu
dada yangu. Kwa sababu hata baada ya kumtoa polisi, nilihakikisha namtoa kwa
chakula cha usiku. Mimi na yeye tu ili tupate muda mtulivu, peke yetu bila
muingiliano. Nikazungumza naye Tula, kuhakikisha ananielewa na yeye anapata
muda wa kuzungumza na mimi. Akaongea na kuuliza maswali yote ndipo nikaachana
naye rasmi. Hana jipya atakalozungumza sasa hivi.” “Mtoto je?” Akauliza Tula.
“Sasa ni hivi Tula. Nazungumza na wewe, na nikitoka hapa, mimi na Jax
tunaenda polisi kuandikisha hili. Usimfuate Jax popote pale.” “Mtoto..”
“Nimekuonya na sitarudia kukuonya Tula. Usiniingilie ninapozungumza.” Tula
akanyamaza. “Dada, barua ya polisi ya kuonywa asinifuate ninayo na yeye nimempa
nakala yake, anayo na hata polisi walimwambia. Wala hakuna haja yakurudi tena
polisi labda sasa nikamshitaki tu.” “Sasa kama huwa akiongea Jax huwa humsikii
unamona ni kama yupo tu uchi mbele yako, nisikilize mimi maana hutabahatika
kupata kikao kingine kama hiki na mimi.” Tino akacheka tena kishabiki.
“Usimfuate tena Jax. Nakupa ONYO Tula. Siku ingine kuiona sura yangu
ukiwa umekiuka hiki ninachokwambia, nitakapokuwa nimekufuata kukuangalia
itakuwa jela kuhakikisha hutoki huko.” Tula kimya. “Unanisikia?” Nelly akauliza
kwa ukali. “Nimesikia lakini...” “Sina muda wa kukusikiliza Tula. Nitaishia
kukuchapa makofi na kukupeleka polisi sasa hivi. Salama yako hapa, kwa kukiuka
onyo la polisi kwa kukaa mbali na Jax,
ni kunyamaza na kunisikiliza. Unanielewa? Au unataka nikakueleweshe polisi
baada ya kukucharaza hapahapa sasa hivi? Tena nitakuchapa kama mwizi, sina
utani na wewe. Unajibu swali nitakalokuruhusu kujibu bila nyongeza.
Umenielewa?” “Ndiyo.” Tula akapoa haswa na hofu.
“Sasa ni hivi, kesho kutwa. Siku ya jumatatu. Saa nne na nusu,
tukutane hospitali ya Muhimbili. Tupime. Mimi nikiwepo sio Jax. Mimi na wewe.
Ukikutwa ni mjamzito, tukajua ni mimba ya miezi mingapi. Bila maswali,
nitalipia kliniki yako. Tena private. Mimi nitalipa mpaka siku ya kujifungua
kwako.” Nelly akaendelea. “Nitakuja mimi, si Jax. Tutachukua DNA ya huyo mtoto
sio sasa hivi akiwa tumboni, akiwa amezaliwa, atapimwa. Akiwa ni wa Jax,
tutakwenda Ustawi wa jamii, watusaidie kwa haki kabisa, jinsi ya kumtunza mtoto
wetu. Na jinsi Jax atakavyopata muda na mtoto wake. Sijui umenielewa?”
Kimya.
“Narudia tena Tula. Kwa kuwa sitavumilia huu upuuzi. Jax ameshatamka
hapa, hakutaki tena, anataka kuendelea na maisha yake. Na mimi sitakuruhusu uje
uharibu maisha ya Jax kwa sababu zako mwenyewe. Sasa je, umenielewa?” “Sasa kwa
nini Jax mwenyewe asilee mimba yake?” “Haa!” Tino akashangaa sana.
“Subiri kwanza Tino. Wewe Tula, ulitaka Jax aleeje hiyo mimba?
Tuambie vile unavyotaka wewe.” “Kuna kuugua usiku. Nani ataniuguza?” Wakaanza
kucheka ila si Lara wala Nelly. “Najua shida yako ni kutaka kurudi pale kwangu
Tula. Nimekuhakikishia hutawahi kuja kurudi pale. Sahau. Nenda kanishitaki
popote, usinibabaishe.” Jax akawa amekasirika. “Wewe hutaki majukumu Jax.
Unakimbia majukumu. Ulikimbia mimba ya Lara, sasa hivi unakimbia yangu.” “Sema
chochote unachotaka wewe kusema. Lakini hutarudi pale. Na kuhusu mimi na Lara,
haikuhusu tena. Lara ni wangu, wewe tuache.” Akamgeukia dada yake.
“Mimi nashukuru kwa hilo. Na nina kuhakikishia dada yangu, sitatupa
damu yangu. Kama mtoto ni wangu, mimi nitalea bila shida. Ila naomba
nimuwahishe Lara hospitalini. Tula ninamjua. Hatutamaliza hapa.
Nimemshauri kama hajaridhika, akashitaki Ustawi wa jamii. Basi. Na swala la
kukaa mbali na mimi alishaambiwa polisi. Wala si geni na yeye. Na ameambiwa
akirudia tena, nikamshitaki, ni kesi.” Kila mtu akamgeukia Tula.
“Naombeni niondoke jamani.” Jax akaweka msisitizo kwa dada yake.
“Nataka kukusikia Tula. Unakubali tulichokushauri au unataka kwenda Ustawi wa
jamii?” “Kama Jax hataki kulea mimba yake, ni heri nikatafute msaada mbele ya
vyombo vya sheria.” “Sawa kabisa. Na mimi nakushukuru kwa kunipunguzia kazi.
Ila nakupa onyo, kaa mbali na Jax. Kama amekwambia hakutaki na umepewa restrain
order, nashauri kuwa makini kuifuata. Mimi sijui kucheza na wapumbavu.
Nitakuweka ndani, ukazalie jela. Usinitanie.” Kimya.
Nelly akarudi kwenye gari yake, na Jax naye akarudi kwenye gari yake
alipokuwa amekaa Lara. Akaondoka kabla ya dada yake, maana dada yake alibaki
ametulia ndani ya gari yake kuhakikisha Jax na Lara wanaondoka bila Tula
kufanya tena fujo yeyote tena. Lara akavuta pumzi kwa nguvu na kujirudisha
nyuma na kunyamaza.
|
Jax & Lara Hospitalini.
Walifika hospitalini kila mtu kimya. Ilikuwa hospitali nzuri na yenye vifaa vya kisasa. “Unajua ni kwa nini nilichagua hapa?” Akamuuliza Lara, Lara akamgeukia wakati wanaingia. “Wanavifaa ambavyo hata kama ulipata maambukizi jana, leo wataona.” Lara akamwangalia na kunyamaza. “Lakini nilishapima Lara. Nataka tu kurudia nikiwa na wewe.” Akarudia tena Jax. “Sawa.” Lara akajibu taratibu.
Akafikiria tena kidogo, na kuongeza. “Tula
anaonekana anakupenda sana Jax. Nimemuangalia jinsi anavyokugombania! Hana hofu
mbele ya yeyote kuonyesha wewe ni wake na anakuhitaji! Unawezaje kuachia upendo
mkubwa kiasi hicho!? Tena kutoka kwa msichana mzuri vile!?” Lara akauliza
taratibu tu akishangaa.
“Humjui Tula, Lara. Tula hanipendi. Ananihitaji kwenye maisha yake.
Yaani mtu wa kumfanikishia mipango yake. Hujawahi kutuona maisha ninayoishi na
Tula, Lara. Tino mwenyewe alikuwa ananiambia ni aibu kuwa na sisi wawili.” “Kwa
nini sasa uliendelea kuwa naye!? Au kwa nini ulimrudia, Jax!?” Lara akauliza
akiwa haelewi wala haamini. “Lara, naomba uniamini nipo hapa na wewe nikiwa
najua ni kitu gani nafanya na kutaka. Nimegundua najipunja kwa kuwa nilishaishi
na wewe na Tula pia. Nitatafuta furaha ya maisha kwa garama yeyote ile. Naomba
tu Mungu uwe wewe.” Lara akamtizama akiwa kama bado hajaelewa.
Wakaingia kupimwa wote. Jax hakuwa na ugonjwa wowote, ila damu ya
Lara ilikuwa bado ipo chini. Dokta akawaandikia dawa, wakaenda kuchukua upande
wa dawa. Wakarudi kwenye gari.
“Twende tukanunue chakula twende tukale kwenye gari, sehemu
iliyotulia.” Lara akakubali. Wakafanya hivyo, kisha wakaenda kuegesha gari
maeneo ya Gymkhana. Wakabaki ndani ya gari wakawa wanakula. “Kesho nitasafiri
kwa majuma mawili. Kama nilivyokwambia. Nakwenda Uswiz.” Lara akanyamaza. Jax
akamwangalia. “Lara?” “Abee!” Akaitika
akiwa hata hamwangalii. “Ni safari ya kikazi na nafikiri itakusaidia kufikiria
kama unanihitaji au la!” Lara akamwangalia na kunyamaza.
“Lara?” “Nakusikiliza unavyozungumza kirahisi Jax! Hivi unajua
ulichonifanyia?” “Najua Lara, na ndio maana nimeomba nafasi ya kurekebisha mimi
mwenyewe kwa kuwa najua ni wapi nimeharibu. Sina jinsi nyingine Lara, labda
unishauri wewe.” Kimya. “Na hata ukinikataa pia sitakulaumu. Naelewa nimekuwa
mtu ambaye sio wakuaminika. Hilo nalijua. Ila ninachojua, kama utakubali
kusimama na mimi, nakuhakikishia utaona mabadiliko.” Lara akabaki kimya tu.
“Sihitaji ufanye chochote kile, ila niahidi hutabadilika. Namtaka
Lara wangu yule yule.” Hata hapo Lara akakosa jibu. Akanyamaza na kuendelea
kula. “Mimi ndio nitafanya kila kitu.” Lara akamwangalia tena. “Au
umeshanipatia jibu langu? Niondoke nikiwa najijua kabisa. Kama nimekosa bara na
pwani!” “Nani bara na nani ni pwani?” Lara akauliza, Jax akanyamaza.
Wakaendelea kula.
“Nikuulize swali Lara?” “Langu hujanijibu.” “Kuwa nani bara na nani
pwani?” Akauliza Jax. “Ndiyo.” “Ni mama na mtoto, Lara. Naomba mawazo yasiende
mbali. Mimi nipo hapa na wewe. Na nimekusudia hivyo.” Lara akanyamaza. “Eti
Lara? Unafikiri kwa jinsi nilivyokuumiza, utakuja kusamehe na tukarudi kuja
kuwa pamoja, au yatakuwa yale maisha ya kukumbushana mpaka mwisho?” “Sijui Jax.
Sikuwahi kuishi na wewe baadaye ila nina kumbukumbu ya jinsi tulivyoishi kabla
ya yote haya.” Lara akafikiria kidogo na kumeza mate.
“Sikumbuki kama tulikuwa na shida kati yetu. Hivyo ndivyo
ninavyokumbuka. Hata nikikaa peke yangu nikitafuta wapi pengine nilikosea, sipati
jibu! Wapi pengine nilitakiwa kurekebisha! Nini nilitakiwa kufanya tofauti! Pengine
nakuwa mbinafsi, lakini sioni Jax!” “Kwa kuwa hakuna. Hakuna ulipokosea Lara.
Nakutetea kabisa hakuna uliponisababisha nikafanya niliyoyafanya. Na ingekuwa
ipo sababu uliyonitenda, kwa hakika nisingerudi kwako tena. Hii aibu yangu
ningetafuta kuanza kwengine lakini si kurudi kwako nikijua si kwamba narudi tu
kwako bali na kwa wengine wote wanaojua nilikosa vibaya sana. Ni kama
kujidhalilisha zaidi! Lakini kwa vile ulivyo, maisha tuliyoishi zamani, ndio
maana narudi nikijua kwako nitakuwa salama kama hakutakuwa na mabadiliko.” Jax
akajieleza vizuri tu. Lara akanyamaza.
“Kwa hiyo?” Jax akauliza.
“Hata sijui Jax! Sina jibu sasa hivi, lakini ninachojua kwa hakika mimi sikuwa
kama wewe. Yale maneno uliyonifuata na kuniambia juu ya upendo wako kwa Tula,
mimi nisingeweza kukwambia Jax. Hata iweje. Kwa kuwa mwenzio nakupenda Jax.
Nakwambia ukweli na Mungu wangu ni shahidi, nilipokuwa na wewe nilikuwa
nimemaliza. Sikuwa hata nikiangalia nje wala sikuwa na nyuma pakuangalia.
Mawazo yangu yalikuwa kwako tu.” Jax akavuta pumzi kwa nguvu.
“Narudia tena kukuomba msamaha Lara. Naomba nipe nafasi nyingine,
naamini safari hii mambo yatakuwa mazuri zaidi kwa kuwa nimejifunza na nitakuwa
nimetulia kama wewe. Nitajifunga kwako tu na sitayumbishwa tena. Na nikirudi
naaamini tutapata muda mrefu mzuri wa pamoja. Nimejifunza Lara. Nakuahidi
sitarudia kosa.” Lara na hapo akashindwa chakuongea. Jax akamuona amefikiria
kidogo na kurudi kula. Akaona bado haamini au bado yupo na maumivu. Akaona
amuache. Wakatulia mpaka wote wakamaliza kula.
“Utanisindikiza uwanja wa ndege kesho?” Lara akamwangalia kama
kumkumbusha kitu, Jax akabaki akimwangalia akisubiria jibu. “Sina usafiri Jax.”
“Nitakufuata na hili halafu twende mpaka uwanja wa ndege, kisha utarudi nalo na
kuja kunichukua siku narudi.” “Na hii gari yako, Jax!?” “Oooh yeah. Kwani si
gari au lina nini?” “Naona kubwa halafu la thamani sana!” “Sijaelewa!” “Pale
uswahilini tunapoishi, litavuta wezi bure! Mimi sina ulinzi wa hivyo. Si
unakumbuka ile gari ya mwanzoni nilikuwa nikiicha CCM?” “Sasa kwa nini na hii
usiache CCM?” “Naogopa Jax. Naomba nikusindikize lakini si kwa hili gari.” Jax
akafikiria.
“Basi unisindikize halafu ukaliache nyumbani.” “Nyumbani kwako!?”
“Ndiyo.” Lara akashangaa kidogo. “Sipafahamu Jax!” “Unataka kupafahamu?” Lara
akainama kama anayefikiria. “Tunaweza kwenda wote, ukapafahamu. Ili kesho
usipate shida.” Lara akasita. “Hapapotezi. Pako wazi kabisa. Na ninaamini
utapapenda. Twende.” “Sijui Jax! Naona kama sio sawa tena!” “Kwa nini?” “Nia
yako ilikuwa sio kunipeleka hapo mpaka niwe mke wako.” “Ni lini unakuwa mke
wangu?” Akauliza Jax. “Sijui Jax!”
“Hapana Lara. Sasa hivi wewe ndio una majibu ya haya mahusiano. Nimekwambia
nakusubiri wewe. Ni lini, ni inategemea na wewe na utayari wako.” Lara
akainama.
“Lara?” “Sitaki twende huko halafu...” Lara akasita kwa muda. “Lara,
kuna tatizo gani?” “Bado hujaweka sawa mambo yako na Tula, Jax! Tusianze kitu
ambacho hatuna uhakika na mwisho wake.” “Wewe ulikuwepo leo pale. Mpaka dada Nelly
akaingilia. Kwa vile ulivyoona na kusikia, kutakuwa na mwisho wa Tula kwangu?”
Lara akanyamaza.
“Nakuhakikishia Lara, kama unamsubiria Tula, hakuna matokeo mazuri
yatakayotokea kati yetu kwenye kusubiri kwako. Mimi nipo na wewe. Naomba mawazo
yako yawe kwangu mimi. Achana kabisa na Tula. Utajichelewesha sana. Sijui kama
unanielewa?” Lara akamwangalia. “Naomba fanya kile moyo wako unajisikia na wala
usijiwekee mipaka, ukijua mimi nipo na wewe. Unanisikia?” Sio kwamba Lara
hakuwa akisikia, lakini tayari ameshachanganyikiwa.
Ni kweli hakuna mwisho wake Jax na Tula, zaidi kama kweli amebeba
mtoto wake. Lara akashindwa kujua ndio itakuaje! Tula anayo nguvu kubwa sana
kwa Jax. Aliweza kumbadilisha mawazo wakiwa wanakaribia harusi iliyokuwa
imegarimu sana na Jax akijua pesa iliyokuwa imeshakusanywa hapo kwa ajili ya
harusi yao! Pesa za nguo zao tu wao mpaka wasimamizi wa harusi! Ilikuwa
mamilioni ya mapesa. Achilia mipango iliyokuwa imepangwa na watu na akili zao!
Wenye nyadhifa kubwa mpaka Nelly dada yake! Tula alifanikiwa kumuingia vizuri
Jax mpaka yote akayatupa mbali! Sasa aongezeke mtoto! Lara akaishiwa tumaini
kabisa. Akavuta pumzi kwa nguvu na kujirudisha nyuma kwenye kiti akaegemea
kitini na kuangalia nje.
“Naomba niangalie na kunisikiliza Lara. Najua na wewe Tula amefanikiwa kwako. Kwa sekunde chache tu ulizomruhusu kuingiza maneno yake kwako najua amekuchanganya vilivyo. Usimruhusu. Nakuhakikishia nimemalizana na Tula, nipo hapa na wewe. Na mimi nakuhitaji sana Lara. Nilikuwa na hamu na wewe kuanzia siku ya kwanza nahamia kwenye ile nyumba.” Lara akawa bado haamini. “Kweli Jax!?” “Kwani huwa inachukua muda kugombana na Tula? Siku yenyewe tunahamia pale tuligombana, nikaishia kulala kwenye makochi.” Lara akamwangalia kama haelewi.
“Lakini anaonekana anakupenda sana!” “Ananihitaji sana. Naujua upendo
sasa hivi sababu niliishi na wewe na nikaheshimiwa. Najua nilichokuwa nakikosa.
Mimi najua, wewe unaweza usielewe. Naomba usinizirie ile nyumba.” Lara
akatamani ingekuwa wakati ule sio sasa moyo ukiwa umekinahiwa vilivyo. Ni kweli
angefurahia nyumba nzuri. Hakuzaliwa kwenye jumba kubwa au hata mazingira ya
kifahari.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Lara alizaliwa kwenye nyumba ndogo tu wakibanana ndugu wote na bado
ndugu wa familia wakija kutembea mjini walifikia kwao. Wakaishi na huyo Jax
sehemu ilikuwa ndogo tu. Joto la Sinza hata feni ikipepea ni joto tu. Nyumba
zimebanana, hakuna nafasi. Anapoishi na rafiki zake ni uswahilini tu. Kelele
nje ya dirisha la chumbani kwa Lara, zilikuwa zikipotea pale anapofanikiwa
kulala. Hata Jax alijua moja ya kitu angemfurahisha Lara ni hiyo nyumba.
Kuhamia sehemu yenye nafasi. Lakini hata yeye alimuona hata hamu imemuisha
kabisa. Akapoa. Swala la nyumba ikawa sio kitu chakufurahia tena. Jax akaumia
maana na hilo nalo amepoteza. Heshima ya kumpa Lara nyumba sio tena kitu
anachohitaji tena Lara. Imeshakosa maana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Lara akabaki kimya akiwaza kama anayejishauri. “Hiyo nyumba ipo
sehemu nzuri sana. Niliinunua makusudi nikijua ni sehemu kwa mara ya kwanza
kwenye maisha yetu tutapata utulivu. Hakuna kelele. Na ndani kuna ua mkubwa tu
sio vile tulivyokuwa tukizima redio yetu ili kusikiliza ya jirani!” Kidogo Lara
akacheka. “Mwenzio najua mpaka tarabu zilizotoka juzi, kwa kusikiliza usiku
kabla sijalala na asubuhi nikiamka, kutoka kwa jirani.” Wakacheka. Jax
hakukosea. Hiyo nyumba ingekuwa pumziko kubwa kwa Lara.
“Twende tu ukapaone. Najua inaweza ikakosa maana, lakini twende tu
angalau na wewe uone.” Lara akaona hilo si wazo baya. Wakaondoka. Njiani kimya.
Mara kadhaa Jax alijaribu kumtizama Lara, akamuona amepotea kabisa pale ni kama
ni sanamu tu amekaa nayo. Alikuwa amepandisha miguu hapo kwenye kiti cha gari
na kuegemeza kichwa chake akiangalia nje tu. Mara kadhaa alimsikia akivuta
pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
Walifika mpaka nyumbani kwa Jax. Getini akamsalimia mlinzi na
kumtambulisha Lara. Kwamba atakuwa akiingia na kutoka na lile gari, wakimuona,
wamfungulie. Mlinzi akaelewa, wakaenda kuegesha ndani, Lara akiwa kimya tu
akisikiliza. Hata salamu hakutoa. Lara akapaangalia akiwa ndani ya gari na
kushindwa kushuka kwa haraka. Nje ilionekana nyumba ndogo tu, na haikuwa ya
ajabu sana. Ila ni kweli ilikuwa maeneo matulivu.
“Karibu Lara.” “Asante.” Lara akajua ndio anaambiwa ashuke garini. Taratibu akajifungua mkanda wa gari na kuvaa viatu vyake, akashuka. Akaangaza macho. “Pazuri!” “Nimefurahi kama umepapenda. Unataka kuzunguka nyuma ndio ukaangalie ndani?” Akatulia kidogo akiendelea kuangalia. Jax akamuona ni kama anajilazimisha tu, lakini sio kitu anachofurahia.
“Twende tukaangalie na nyuma,
upaone.” Jax akatangulia, Lara akamfuata. Akamzungusha nyuma ya ile nyumba.
“Aliyekuwa akiishi hapa mwanzoni anaonekana alikuwa akipenda maua! Alikuwa na
vyungu vizuri!” “Sina muda wa maua. Kwanza sina hata wazo la maua. Labda uje
kuanza wewe.” Jax akamwangalia, lakini Lara hakujibu. Wakazunguka kidogo Lara
akifuata nyuma nyuma.
“Twende ndani.” Jax akaongoza tena njia. Wakaingilia jikoni, mlango
wa nyuma tu. “Kusafi!” “Yupo mtu anasafisha. Twende ukaone na kwengine.”
Akamtembeza hapo ndani. Hapakuwa pakubwa sana ila panatoshea. “Nilipoambiwa tu
panauzwa, na ofisini walikuwa wakitoa mikopo ya nyumba, nikapachangamkia.
Pakuanzia hapa sio pabaya.” “Ni kweli. Huwezi kupalinganisha na pale tulipokuwa
tukiishi Sinza. Hongera Jax.” “Asante. Unataka kupaona na chumbani.” Lara
akacheka akionekana wazi anasita. “Nitapaona wakati mwingine. Acha nikusubirie
hapa sebuleni.” Jax akamtizama kwa uchu, Lara akacheka na kurudi sebuleni. Jax
akaingia ndani upande wa vyumba.
Baada ya muda akamfuata pale sebuleni bila shati ila nguo ya juu ya
ndani. “Nikuulize swali?” “Jax kwa maswali!” “Ni latokea wakati ule ila
hukujibu.” Lara akajaribu kufikiria. “Ni juu ya mtoto?” Jax akacheka.
“Ulijuaje?” “Nakujua Jax. Kila swali
unataka liwe na majibu wakati nilikwambia kuna mambo mengine hayana majibu!”
Akaenda kukaa pembeni yake.
“Mbona umekalia mikono? Baridi imekuzidia?” “Umewasha baridi kali
sana.” Nyumba hiyo ilikuwa na A/C sio kama walivyokuwa wakipepewa na feni.
“Njoo ni kukumbatie hapa.” Akamvuta bila kusubiri jibu. Lara akapandisha miguu
kwenye kochi akajikunja vizuri mwilini kwa Jax. “Umekuwa katoto! Kazama kula.”
Akambusu. “Nakula. Si umeona nilivyokula pale kwenye gari? Na ile ni mara ya
pili.” Akampapasa juu ya mwili. Akambusu tena.
“Kwa nini hukuniambia kama ni mjamzito?” Lara akataka kukaa, Jax
akamvuta karibu kama kumzuia kutoka pale mikononi mwake. Akacheka. “Nataka
kukuelezea vizuri.” “Nakusikiliza. Wewe ongea tu hapahapa.” Lara akatulia
kidogo kama anayefikiria. Mikono ya Jax ikaendelea kupita mwilini mwake, Lara
akisikilizia asijue kama ni kitu anahitaji kwa wakati ule au ilishapitwa na
wakati! Kwa hakika kila kitu kati yake na Jax ni kama kilipoteza maana. Lara akatulia
kidogo, akashindwa.
“Naomba nikae tu hapa pembeni yako Jax. Acha, usinikumbatie.” Lara akajitoa kwa nguvu na kujiweka pembeni. Kabla Jax hajaongea kitu akiwa na mshangao usoni, Lara akaendelea. “Kujibu swali lako maana najua hutaacha kuuliza. Ni niliogopa.” Lara akaanza. Jax akakunja uso. “Kwa nini!?” “Unakumbuka siku ile tulipokuwa na Tino, akauliza tunampango wa kuwa na watoto wangapi na lini, ukajibu kwa haraka kuwa sio kwa wakati huu. Unakumbuka?” Jax akatulia kabisa.
“Ulisema kwa wakati huu unataka kujijenga kwenye kazi yako
kama Nelly dada yako alivyofanya. Ukasema huna haraka na watoto. Ndio nikaanza
kujichunguza. Maana nilikuwa nimejisahau mambo ya kuhesabu siku za hatari. Ni
kama mipango ya harusi ilipochanganya, nikajisahau kabisa kwenye swala la
kuangalia mzunguko wangu wa mwezi ili kuzuia mimba. Sasa baada ya kusema vile
ndipo nikawa kama umenistua. Kuja kuhesabu nikagundua ni miezi miwili
ilishapita bila kuona siku zangu.” Lara akaendelea.
“Nikagundua ndio maana nilikuwa nikilala sana na harufu nyingi
zilishaanza kunisumbua. Nikaogopa kukwambia ili usije badili mawazo ukaona
nakuletea matatizo. Nikajiambia ninyamaze mpaka tukishaoana ndipo nikwambie.
Ndio pressure nayo ikaanza kusumbua. Nikaenda kuzungumza na daktari wa kawaida
tu, sio daktari wa mambo ya wakina mama. Akaniambia nipunguze shuguli, nipate
muda mwingi wa kupumzika.” Lara akatulia.
“Nilikaa kama siku 13 nikiwa najisikia vizuri, na kweli nilikuwa
nikijitahidi kupumzika ili kuhakikisha pressure inatulia. Kila nikipata nafasi,
nilikuwa nalala. Ndio maana ulikuwa ukiniona nalala sana. Ili kufanya akili na
mawazo vitulie kabisa. Siku nilipogundua umenidanganya hukuwa Kisarawe,
niliingiwa na hofu sana. Kwa sababu ukweli Jax, ulikuwa ukinijali sana tokea
zamani. Nikashangaa umeweza kutonipokea nikiwa natoka safari ambayo hatukuonana
zaidi ya siku nne! Mbaya zaidi hatukuwa tumefanya mapenzi kwa zaidi ya kama
siku 20! Nikajua kwa vile ulivyo wewe, kupenda kuwa na mimi ukinishika kama
hivi, lakini ukamudu bila kulalamika! Nikajua kwa hakika utakuwa umeshapata mtu
mwingine.” Lara akaendelea.
“Hofu ikaniingia. Nikajua utaniacha. Kumbe pressure nayo inazidi
kupanda. Na kweli. Usiku niliomtuma Tino kwa dada Nelly, ilipanda nikashindwa
hata kuendesha. Nikasimamisha gari njiani. Tino akaja kukaa na mimi.
Akanifariji sana. Angalau nikaweza kuendesha mpaka pale nyumbani tunakoishi.”
Lara akatulia kama anayetafuta jinsi ya kuendelea. Jax kimya akisikiliza.
“Nilirudi pale tunapoishi na
wenzangu nikajaribu kutulia, huku nikijiambia lazima nitulie ili mtoto asitoke.
Lakini nilishindwa Jax. Nahisi labda Tino
angeniambia pengine ningetulia hospitalini, nikaweza kutibiwa. Maana hata
hospitalini nilishindwa kutulia.” Lara akaanza kutokwa na machozi.
Jax akazidi kushangaa hizo juhudi za kuokoa huyo mtoto akawa amesahau yote aliyosimuliwa na Tino. “Mpaka hospitalini!?” “Nilikuwa na hali mbaya sana. Nilijawa na hofu Jax,
siwezi kukwambia. Moyo ulikuwa ukienda mbio sijawahi pitia hiyo hali. Sasa kwa
kuwa nilikusudia kuwa na huyo mtoto, nikasema nikimbilie hospitalini ili
wanisaidie. Lakini haikusaidia. Nilikwenda tena peke yangu usiku, wenzangu
wakiwa wamelala. Na kwenyewe nikashindwa kukaa nikarudi nyumbani eti kwa
kugundua simu haikuwa na chaji, ilikuwa inazima. Nikahofia Tino atanikosa.
Nikiwa nimeambiwa nilale pale kwa kuwa pressure ilikuwa juu sana, nikaondoka
ili nikachaji simu, Tino asinikose.” Lara akajifuta machozi na
kuendelea.
“Basi ndio mpaka asubuhi nikawa sijamsikia Tino wala
wewe, ila Tula aliponifuata ofisini. Nilipatwa na mshituko ambao sikutegemea.
Tula alionekana ananifahamu vizuri tu. Na hakuonyesha kama anaongopa. Halafu
sio kwamba alikuwa akizungumza na mimi kwa jazba! Hapana. Taratibu tu, kwa
kituo kama aliyekuwa amekusudia kunifikishia ujumbe wote aliopanga, mimi na
watu wote waliokuwepo pale tusikie. Taratibu ila kwa sauti iliyoweza kusikika
na wote pale mpaka wateja. Akanitajia na majina ya marafiki zenu wote. Hapo
ndipo nilishituka sana maana ni kama alinithibitishia kila kitu. Na ninahisi
ndipo pressure ililipolipuka zaidi.”
“Sesi alikuja kunitoa pale kwenye kiti, nilikuwa siwezi
hata kujisogeza. Ile nimepanda tu kwenye gari akiwa ananirudisha nyumbani,
nikasikia tumbo linakoroga, hapo hapo damu zikaanza kumwagika kama bomba.
Nikajua mtoto ameshatoka.”
Lara akatulia kidogo.
“Ukaja sasa na wewe kunithibitishia aliyozungumza Tula,
na kuniambia unampenda Tula. Umemchagua yeye.” “Sikusema hivyo.” Jax akajaribu kukanusha. “Sijui Jax, ila matendo yako yalizungumza hivyo na maneno
ya namna hiyo.” Jax akanyamaza. “Pale ulipokuwa
ukiniambia vile, muda ule, nilikuwa natamani nife palepale nipotee. Ni kama
ulimwengu mzima ulikuwa umewekwa kichwani kwangu! Nilikuwa nimelemewa!
Najiuliza maswali ambayo hayana majibu.” Lara akajifuta machozi
yaliyokuwa yakiendelea kumtoka. Akajifuta na kutulia ili kuweza kuzungumza.
“Unajua swali kubwa lililonisumbua ni nini?” Lara akauliza baada ya kutulia. Jax
kimya. “Jax?” “Wapi ulikosea?” “Hilo, lakini kubwa ni nini alichonacho Tula ambacho mimi
Mungu alininyima! Siri yake kubwa ni nini kiasi cha kukufanya kuwa tayari
kutupa kila kitu tulichokuwa nacho kwa miaka karibu miwili, na kumfuta yeye!
Nilijiuliza na kupatwa na wivu wa ajabu. Ila nilimuheshimu sana. Nikajiambia ni
wa thamani sana. Hata nilipokuwa nikizungumza naye, nilimuheshimu mno yule
msichana. Kwangu hakuwa mshari. Jinsi alivyojibeba, unadhifu wake, uzuri, na
ujasiri wake! Nikajiambia amebeba kitu cha thamani sana ndani yake kiasi cha
wewe kuniacha, Jax!” Lara akaendelea taratibu kama anayejaribu kuvuta
kumbukumbu.
“Unajua angalau kama tungekuwa ni watu wakugombana au
hata kupishana! Lakini tulikuwa tukiishi kwa utulivu ambao hata sasa sijui
ilikuwaje! Ulilokuwa ukiniambia au nililokuwa nikikwambia tukawa tunakubaliana
kirahisi sana kama tuliokuwa tukisomana mawazo! Sijui kama unakumbuka mpaka
wakati mwingine tulikuwa tukicheka jinsi tunavyowaza mawazo yanayofanana!” Jax alikuwa amebadilika sura,
anashindwa hata kuongea. Lara akaendelea. “Halafu
ile hali ya kunisifia kwa watu kuwa mimi ni mke wakuoa, gafla unaniambia
umemchagua Tula, unaniacha! Nilivurugukiwa mno Jax.” Lara akafikiria
tena kidogo.
“Naweza kusema nilishituka kuliko kuumia. Kwa sababu sikuwahi hata kukuhisi na mwanamke! Unajua kama ingekuwa ni tabia yako, ingekuwa rahisi. Sasa kutoka katika yale maisha tuliyokuwa nayo, mpaka kuja kuniacha gafla! Tena unanitamkia waziwazi ni kwa sababu ya mwanamke mwingine! Nilishituka sana. Anyways, nafikiri nimeongea mambo mengi lakini nafikiri utakuwa umepata jibu lako.”
“Nimeelewa Lara. Na naomba nisamehe. Kwa hakika nilikukosea sana. Ila juu ya
mtoto, ningefurahi kama ungeniambia. Nisingechukia na kuona kama ni tatizo.
Kwanza mimi nilikuwa nikikuhofia wewe Lara. Hivyo ulivyo, halafu kuja kubeba
mtoto! Nilikuona kama haupo tayari au sio jambo unalitaka kwa wakati ule. Kwa
hiyo nilimjibu vile Tino kuhofia asije kukuogopesha ukaona unawajibika kuja
kuanza kunibebea watoto ukaharibu kaumbile kako! Nikahofia usije ukadhani kama
nina mpango wakuja kukuuzeesha bure!” Lara akacheka kidogo.
“Kweli! Hata hapa kukusikia katika yote yale na bado ulikuwa na
mpango wa kumtunza huyo mtoto, siamini!” “Ukweli sikuwa nimepanga. Lakini sijui
nilipatwa na nini! Japokuwa nilikuwa nikikuhofia wewe, lakini ni jambo
nililolifurahia mno. Nikawa namfikiria yule mtoto jinsi atakavyokuwa au
atakavyofanana na wewe au jinsi atakavyochanganya sura zetu! Nikafurahia sana.
Nikajiambia ni kitu chakutunza tu kwa garama yeyote ile.” Wakanyamaza kila mtu
akiwaza lake.
Baada ya muda akaona aage tu. “Acha
mimi niende Jax. Nitakuja kukutembelea wakati mwingine.” “Kwa hiyo kesho
utaweza kunipeleka uwanja wa ndege?” “Nitakupeleka. Ila nikipata usafiri kabla,
naweza kuja kukufuata hapa. Ili usihangaike kuja mpaka kule!” “Basi
tutawasiliana.” Lara akasimama. “Mbona unaharaka?” Lara akacheka na kuinama
kama anayefikiria. “Hatutaonana kwa week mbili Lara!” “Nilijua utataka
muda wa kujiandaa na safari, Jax.” “Hutaki kunisaidia?” Lara akacheka akionyesha
kutokuwa radhi na hilo kabisa.
“Nilikuomba usibadilike Lara.
Ulikuwa ukinijali sana, kiasi nilikuwa nakumiss mno! Nilikuwa nikikaa hapa
nafikiria kama ndio wewe ungekuwa ukiishi hapa na mimi, pasingekuwa na zile
siku nilizokuwa nikilala na njaa au hasira, tena wakati mwingine hapahapa kwenye
makochi wakati kitanda kizuri kipo ndani! Vyakula vizuri vinakuwepo hapahapa
ndani na pesa zipo! Ni wewe ulikuwa ukikosekana Lara. Nimekiri nilikosa, naomba
usibadilike na kunipuuza.” “Unajua siwezi kukupuuza Jax, ila naomba nipe muda
tafadhali. Sipo kwenye hali nzuri hata kidogo. Natamani kama ningekuwa kama
hivyo wewe ambavyo umeweza. Unafanya inaonekana rahisi sana, kama kuzima na
kuwasha taa!” Lara akaongea taratibu huku akiwa amesimama.
“Sio rahisi Lara! Si rahisi hata kidogo, lakini nimeamua. Nimepoteza
mengi mno mpaka heshima ambayo nilitarajia ningekuwa nayo sasa hivi sababu ya
kazi nzuri niliyonayo. Lakini maamuzi yangu mabovu yananigarimu mno. Furaha ya
mabadiliko yangu ya kiuchumi yalileta maana tu tulipokuwa wote.” “Nipe muda
Jax. Tafadhali. Nahitaji muda. Pengine nikipona na kurudia hali yangu nitaweza
kufikiria sawasawa. Lakini sasa hivi nina mengi yanayoendelea! Mengi mno.” “Ni
nini?” Lara akafikiria kidogo.
“Kama ni pesa nitakusaidia Lara.” “Natamani kama ingekuwa ni pesa tu
Jax!” “Sasa ni nini?” Lara akafikiria tena kidogo. “Nafikiri hata kuweza
kulijibu hilo pia nahitaji muda. Nifikirie, ili niweze kujipanga tena kwa upya.
Kwa sasa sina jibu hata kwangu mimi mwenyewe. Nasikia mvurugano, fujo na kelele
tu kutoka ndani yangu mimi mwenyewe. Wakati mwingine natamani hata hizo kelele
ziwe nazisikia kutoka nje, lakini zaidi zipo ndani yangu mwenyewe! Acha niweze
kutulia kwanza. Nirudishe hali yangu ya zamani. Japo tu hata kujiamini tena.
Sasa hivi najidharau mno! Nina majuto ambayo si kwa maneno hata kutoka kwako
yatakayosaidia. Nafikiri ni mimi mwenyewe. Mbaya zaidi nimejawa hofu yakupita
kiasi. Moyo, nafsi, akili na mwili wangu vyote vinakataa kurudi kwenye
mahusiano. Sipo tayari kabisa.” Hapo Lara akafunga mjadala mzima.
Lakini Jax akajikaza na kuuliza. “Ni kwangu tu, au?” Jax akauliza.
“Kwa yeyote yule sipo tayari Jax. Nimefilisika ndani yangu, sina kitu chakumpa
yeyote yule. Nimechanganyikiwa kupita kiasi. Kila kitu kimepoteza maana hata
sijui tena kupenda mtu kukoje! Kujali ndio inakuwa vipi! Mahusiano ndio kabisa!
Hata sijui tena unapokuwa kwenye mahusiano ndio inakuaje, au inatakiwa iweje!
Nahitaji muda. Mpaka lini, ndio wasiwasi wangu. Sijui. Nafikiri muda ndio
utajibu.” Jax akaishiwa nguvu kabisa.
“Naomba mimi niondoke Jax. Nakuona upo na moyo wa kuendelea mbele
ambao mimi huko sipo kabisa. Sitaki kukurudisha nyuma.” “Kwa hiyo unaniambia
nini Lara?” Jax akauliza. “Kile unachokisikia nakuongea, nashauri kifanyie
kazi. Hata mimi sijui Jax. Pengine baada ya leo na kesho kama alivyosema dada Nelly,
labda. Mbali na wewe na Tula, nikapata nafasi yakutafakari kilichonitokea,
tulipo na kitakachoendelea. Nikijua nikirudi kwako hutakuwa tu wewe Jax
niliyedhani tupo wote ila yupo Tula, na ataongezeka mtoto wenu. Kwamba inabidi
nifikirie kama nilidhania Tula anayo nguvu kwako, basi inaongezeka nguvu ya
mtoto wenu pia. Sasa je, nipo tayari kuwa na mtoto wako uliyezaa na Tula,
nikiwa nimepoteza wangu!” Jax akawa kama anafunguliwa mawazo na Lara. Akabaki
anamsikiliza akionekana amefunguka zaidi.
“Kwa hiyo kabla sijajibu chochote kile, nafikiri nahitajika
kufikiria. Inawezekana wewe ndio utahitajika kunipa
nafasi mimi ili unisome kama nimebakia Lara unayemfahamu na ambaye unataka
kumuoa au Lara uliyekuwa ukimfahamu alikufa na mtoto wake!” Jax
akashituka moyoni. Lara akajifuta machozi. “Yote
hayo ni yakuyafikiria Jax. Hata mimi sipo salama sana. Unaweza ukawa unamuacha
mwanamke unayempenda na yeye anakupenda au kukuhitaji, ukarudi kwangu ukakuta
mambo mengi sana yamekufa. Ukidhani hofu ya kukumbushwa yaliyotokea kati yetu ndio
itakukabili kwangu, kumbe ukaja kukutana na Lara ambaye amejeruhiwa vibaya
sana. Kila kitu kikakosa maana. Ikawa unakosa tena bara na pwani ya Tula. Tula
na mtoto wenu.” Jax akawa kama amemwagiwa maji. Taratibu Lara alirudia
maneno yake yeye mwenyewe. Jax akainama.
Lara akachukua pochi yake na kutaka kutoka. “Naomba nikusindikize
Lara. Utapata shida ya usafiri.” “Nitashukuru.” Jax akaingia ndani kuvaa shati.
Akatoka akiwa anajirekebisha. Wakatoka hapo ndani kimyakimya mpaka kwenye gari.
Wakaondoka hapo. Njiani pia hapakuwa na mazungumzo tena. Lara aliongea moyo
wake na kumuacha Jax na yeye akifikiria.
Walifika anakoishi Lara na wenzake, wakabakia ndani ya gari. “Naomba
nisiingie Lara. Naona kila mtu hapo ndani hana hamu yakuiona sura yangu.”
“Sawa. Usiku mwema.” Lara naye hata hakubembeleza tena, Jax akajua kweli
amembadilikia. “Kama bado ungependa nikusindikize kesho, unijulishe tu.” Jax
akabaki akimuangalia. Lara akainama kidogo.
“Unafikiri ukiamua kuja kuwa kwenye mahusiano tena, mimi nitafanikiwa
hata kufikiriwa au ndio nisahau kabisa?” “Sijui Jax. Ila nashauri usinisubiri
mimi. Kama ulivyosema, umekusudia kuendelea. Na unaonekana huna shida na utakayeendelea
naye. Ulisema unaendelea tu, iwe na mimi au mwingine. Nashauri uendelee tu
Jax. Mimi sijui nitakuwa tayari lini. Sitaki kukuchelewesha. Usiku mwema.” Lara
akashuka na kuondoka bila kugeuka nyuma. Jax alibaki ameduaa akikumbuka maneno
aliyozungumza alipokuwa na hasira za Tula, kwa Lara aliyejeruhiwa moyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usiku wakati analala, ujumbe ukaingia. ‘Inaweza
ikakuchukua kipigo kama nilichopigwa mimi huko nje yetu ili kuja kugundua
tulichokuwa nacho mimi na wewe hakipatikaniki kwa urahisi. Ni cha pekee mno
Lara. Niamini nikikwambia hivyo na ndio maana nipo tayari kurudi na
kurekebisha. Sitaki upitishwe nilikopitishwa mimi. Unaweza usifanikiwe kutoka
salama. Tafadhali fikiria kwa upya. Naamini nikirudi kutoka safari tutapata
muda zaidi. Ubaki salama.’ ‘Asante na wewe safari njema.’ Lara alijibu
hivyo tu kirahisi na kuweka simu pembeni. Jax alipoona hayo majibu, hakuamini.
Lara hakujali hata Jax anafikaje uwanja wa ndege! Jax akaanza kuhisi
ameshampoteza Lara, lakini akajiambia pengine anahitaji tu muda. Atakuja kupona
na kumpata Lara wake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kiburi cha kiume kikaanza kuisha. Mafanikio yake ni kama yakapoteza
maana kabisa. Lara amekataa hata hilo gari ambalo Tula alikuwa akiliabudu!
Alitaka kumuachia atumie mpaka atakaporudi, lakini Lara akakataa bila hata
kuonyesha atapungukiwa na kitu. Amempeleka kwenye nyumba aliyodhani ingemuhadaa
lakini Lara hakuonyesha hata kama kuna utofauti! Jax alilala na mawazo, lakini
Lara akameza dawa zake za usingizi, akalala bila kujali zaidi.
Lara!
A |
subuhi yake,
Lara hata hakujisumbua kumtafuta tena Jax hata kujua kama aliondoka salama au
la. Siku hiyo ikapita kimyakimya. Siku ya jumatatu akatoka mapema tu kuwahi
kazini kabla hata ya foleni. Akawa wa kwanza kutoka hapo na kuacha wenzie.
Alipofika tu ofisini bosi wao akamuita hata kabla ya kikao. Hata hivyo watu
hawakuwa wamefika wengi. Lara akamsalimia. “Kuna jambo nimefikiria nikasema
nikushirikishe pengine utapenda. Sijamwambia yeyote. Hili ni wazo langu moja
kwa moja kwako.” Lara akajiweka sawa. “Kwa haya yaliyotokea hapa. Unafikiri
kama ungepata sehemu nyingine yakuhama kikazi, kampuni nyingine ya simu,
unafikiri ungependa?” “Sana. Angalau nikafiche huu uso kidogo.” Lara akakubali
kwa haraka bila kufikiria.
“Sikwambii ukimbie!” “Wote tunajua sikimbii bosi wangu. Ni
nimekimbiwa ndio nakwenda kupumzika. Na kabla sijajua ni wapi unafikiria
kunihamishia, naomba nikushukuru kunisaidia. Sio kwa hili tu. Tokea mwanzo.
Najua ningefukuzwa kazi kama si wewe. Nakushukuru.” “Karibu. Sasa kuna nafasi
nimeiona imetokea Zanzibar. Nimesoma kwenye gazeti. Kampuni ingine lakini.”
Akamtajia. “Sasa afisa mwajiri wao nafahamiana naye sana. Nilimpigia jumamosi,
akasema ni kweli wanatafuta mtu, wapo kwenye usahili. Ni kama hiki
unachokifanya hapa, lakini kwa kuwa unajuhudi na uzoefu, utakuwa ukiwasimamia
wenzio. Naweza kukuandikia barua ya kukupendekeza, kisha tuone.” Lara
hakuamini.
“Unaweza usiwaambie watu kama nitaondoka?” “Lara! Hutaki kuaga?”
“Nina maana yangu. Nataka nikaanze upya bosi wangu. Hata kama nitakuja kukutana
na wanao nifahamu, basi angalau niwe nimeshapona ndani. Wanao nizunguka wote
wananikumbusha machungu yangu. Labda nikiwa mbali angalau itanisaidia.”
“Wakikuulizia?” “Kwa kuwa nakujua huwezi kudanganya, naomba na mimi nikuapishe
kuwa hutasema.” “Hapo sawa. Na mimi nitawaambia nilikuahidi sitasema, basi
itabakia hivyo.” Bosi wao alikuwa mwenye maadili sana. Wakasaidiana na Lara
kuandika barua ya maombi asubuhi hiyohiyo watu wakiwa hawajafika hapo. Lara
akamtumia na CV yake, bosi wake akamtumia huyo rafiki yake afisa mwajiri wa
hiyo kampuni. Lara akatoka wakati wanazungumza kwenye simu.
Mwanzo Mwingine.
Baada ya siku tatu Lara akaitwa kwenye usaili. Na mshahara pia
aliotajiwa ulikuwa wa juu kidogo na ule. Aliambiwa atalipwa na pesa ya usafiri
na marupurupu mengi tu. Na kwa kuwa walihitaji mtu kwa haraka, Lara akatakiwa
baada ya siku tano awasili kazini. Hakufikiria mara mbili wala hakumwambia
yeyote yule. Akaandika barua yakuacha kazi. Akamkabidhi bosi wake. Maandalizi
ya kuacha jiji la Dar yakaanza kimyakimya bila hata kuwaambia kina Sesi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku ya ijumaa karibu wote pale walitoka kwenda kwenye starehe,
lakini Lara hakutaka kuongozana nao. Walielewa tu bado yupo kwenye majonzi.
Kumbe alibakia usiku kufungasha. Tino alitoka na Suzy akitaka muda naye, na
wengine walitoka kivyao. Lara akabaki peke yake kwenye hiyo nyumba na kupata
uhuru wote. Alikusanya kila kitu chake na kuwaachia ujumbe pale. Aliwashukuru
sana kwa kusimama na yeye kipindi chote. Ushirikiano waliomuonyesha. Na
kuwaambia amepata nafasi ya kwenda kuanza upya maisha sehemu nyingine. Akaahidi
mambo yakikaa sawa, atawatafuta. Aliandika huo ujumbe kwenye kikaratasi wala si
simu. Akafunga vizuri na kuweka juu ya kitanda chake. Akaita usafiri,
akapandisha mizigo yake yote. Lara akaondoka hapo. Usiku huo akatafuta nyumba
ya kulala wageni. Akalala hapo huku akijipanga na angalau kujawa furaha ya
kuanza upya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ukweli Jax aliomba msamaha, lakini kila kitu kilishapoteza maana.
Lara hakujua hata wakirudiana wanaanzia wapi! Nini atafanya na huyo Jax
aliyemtamkia wazi hatamuoa, amemchagua Tula. Lara akajiangalia vile alivyo na
kujifananisha na Tula, akajua hataweza hiyo vurugu kwenye maisha yake yote.
Akajua kurudiana na Jax, ni kama kuanzisha mahusiano yenye hekaheka tupu! Zaidi
akiumia kuona Tula yeye ndiye atafanikiwa kumzalia Jax mtoto, halafu wake
amekufa! Akajiona hayupo tayari. Ana mengi yakufanya na kufikiria, kuliko
hekaheka ya Jax na Tula. Mbaya zaidi, hakuona kama kutakuwa na mwisho.
Halafu akajiambia, inamaana kama Tula asingeharibu, Jax asingemrudia
yeye. Hilo likazidi kumtesa sana Lara. Akajiambia inamaana Jax amemrudia kwa
kuwa kule imeshindikana! Anataka kwenda kumtumia tu. Kwa kuwa amekosa heshima
kwa Tula, basi anarudi kwake si mapenzi! Akahesabu yote hayo. Alijua ipo
heshima kuolewa na mtu kama Jax. Mwenye pesa na muonekano ambao unapokelewa na
jicho lolote lile, lakini akajiambia garama ni kubwa. “Nimeshalipa garama kwa kifo cha mtoto wangu. Mwishoe nitafuata mimi
mwenyewe.” Lara akawaza na kuamua kujiweka pembeni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alifika Zanzibar na kukutana na wenyeji wazuri sana. Watu wazima ambao
hawana mambo ya kitoto. Halafu akajikuta wapo wachache sana hapo ofisini.
Kijana alikuwa mmoja tu na yeye alitokea bara, lakini Iringa. Hakuwa hata
ameanzisha familia. Wengine wote walikuwa wenyeji wa hapohapo Zanzibar. Huyo
kijana akamsaidia kumuonyesha mazingira. Akapata pakuishi, akatoka hotelini
baada ya siku chache tu. Hakutumia pesa nyingi. Hakuna anayemfahamu, ikabidi
kuanza kujichangamsha tu kwani kuanza kazi na huzuni, nikuibua maswali ambayo
itabidi aeleze alichokikimbia Dar. Hata wazazi wake hakuwaambia kama alihamia
Zanzibar. Ila aliwaambia alicha pale kazi.
Huku Nyuma jijini.
Huku nyuma alipokuwa ameondoka, wenzie walirudi kutoka kwenye
starehe, wakijua Lara amelala ndani. Hawakutaka hata kumuamsha. Siku inayofuata
ya jumamosi, wakashangaa hatoki chumbani, wakahisi siku hiyo na yenyewe aliwahi
kazini kwani jumamosi hiyo ilikuwa zamu yao kwenda kazini. Na tokea ampe Tula
gari, wote walirudi kupanda daladala. Ila Lara yeye alikuwa akitoka alfajiri
zaidi kuepuka adha ya usafiri. Lakini walipofika kazini hakuwepo. Wasiwasi
ukawaingia wakajilaumu kuondoka bila kumtizama chumbani kwake. Wote walijua
Lara anapitia kipindi kigumu, wakahofia asijekuwa aliamua kujidhuru, lakini
wakakumbuka Jax ni kama anajirudi. Wakajua amekusudia tu kulala.
Bila kujua kinachoendelea, wakamtetea kwa bosi wao kuwa Lara ni
mngonjwa, wamemuacha amelala. Wakadanganya. Bosi wao hakusema kitu. Simu yake
haikuwa ikipatikanika. Kwa kuwa ilikuwa ni nusu siku ya kazi, walipotoka tu
moja kwa moja mpaka nyumbani kwao, chumbani kwa Lara. Ndipo wakakutana na huo
ujumbe. Walitaka wasiamini, lakini wakagundua hakuacha chochote kilicho chake.
Walihuzunika sana. Wakampigia simu Tino kutaka kujua kama yeye aliagwa na kama
anajua wapi alipo Lara. Wakagundua hata Tino hajui, ndio na yeye wanampa habari
za kusikitisha.
Kwa Jax.
K |
idume huyo
mwenye mafanikio ya kiuchumi, kazi nzuri na wanawake wazuri wawili
akiwachanganya akili wasijue nani ndio zaidi maana kila mmoja alitesa na Jax
kwa wakati wake ndipo kugonganisha sasa magari, wakidai wote walipewa mimba na
huyohuyo Jax, alirudi nchini kutokea nchini Uswiz, baada ya siku 15 zakuondoka
bila hata kusindikizwa na yeyote yule. Akachukua tu taksii hapo uwanja wa ndege
na kurudi kwake.
Nyumba ikawa kubwa zaidi. Na pweke. Akajiambia siku 15 zitakuwa
zimetosha kwa Lara kutulia kabisa na kutoa majibu ya kueleweka kwake. Jax
akajipima ubora wake, akagundua amejaa kwenye mizani. Hakuna mwanamke angepata
nafasi ya kuwa naye akaikataa. Akakumbuka Tula anavyomlilia mpaka baa mbele za
watu! Nini chakumfanya Lara aliyemuhakikishia kutulia naye asimkubali tena!
Mafanikio si ya ahadi. Jax amefanikiwa kiuchumi na anakokwenda ni bora zaidi
kuliko hata hapo alipo. Hapo alipo tu alikuwa ametokea nje ya nchi, bado
ananukia harufu ya Ulaya. Akajisifia kwa hili na lile, akajiaminisha kwa yote.
Akajaribu kumtumia ujumbe Lara kumtaarifu amerudi nchini. Haukuonyesha
kama huo ujumbe umefika. Akakumbuka pia alipokuwa kule alijaribu kumpigia mara
mbili hakumpata. Akafikiria, na kuamua kwenda kumuona. Ilikuwa siku ya
jumapili. Akagonga akasikia akiambiwa subiri. Hakufurahia Suzy alipomfungulia.
Alitamani angekuwa mtu mwingine sio yeye.
“Tukusaidie nini?” Akauliza Suzy kwa jeuri. “Hata salamu Suzy!?”
“Salamu yangu itakusaidia nini wewe, matawi ya juu?” Suzy akaanza. “Unaongea na
kulala na waliofika nchi za nje na wenye migongo mikubwa. Mimi nyuma sijajaliwa
kama mwanamke wako. Sina...” “Suzy, nipo hapa kwa amani tu. Sitaki kukuudhi.”
Jax akamtuliza. “Basi umechelewa, maana sitaki hata kuiona hiyo sura yako. Na
huna sababu yakurudi tena hapa maana wote humu ndani hawataki kukuona.” “Naomba
basi niitie Lara.” “Lara haishi hapa. Haya potea.” Suzy akataka kufunga mlango,
Jax akauwahi.
“Nitakuitia mwizi Jax wewe! Jifanye wewe ndio mwanaume hapa mjini.” “Sitaki ugomvi Suzy, namuomba Lara.” “Unatatizo lakusikia? Nimekwambia Lara haishi hapa.” “Amehama?” Jax akauliza. “Kama hujui, inamaana hayakuhusu.” Suzy akafunga mlango kwa nguvu na kumuacha Jax hapohapo mlangoni. “Na nakupa dakika 5, upotee mlangoni kwetu, lasivyo nakuitia mwizi. Na siku nyingine ukirudi pia nakuitia mwizi. Hatutaki kuiona sura yako hapa.” Akamsikia Suzy akizungumza ndani. Jax akaondoka maana alimjua Suzy, huwa hajui kutania.
Kwa Tino.
Akarudi kwenye gari na kujaribu tena simu ya Lara. Haikuwa hewani.
Akampigia Tino. “Mzee wa benki ya dunia!” Akaanza Tino. “Vipi
Tino?” “Nipo kwa bi Mkubwa. Umesharudi mjini?” “Nipo mjini ndio nimerudi.
Namtafuta Lara.” Kidogo Tino akashangaa. “Hata
wewe hujui alipo!?” “Sijawasiliana naye tokea usiku mmoja sijaondoka nchini. Kuanzia
hapo akawa hapokei simu halafu baada ya siku kadhaa nikawa simpati kabisa.
Nimemfuata hapa alipokuwa akiishi na kina Suzy, Suzy ameniambia haishi hapo
tena. Unajua alipohamia?” Jax akauliza ila safari hii akisikika hali ya
uwanaume imeanza kupungua.
“Daah! Basi naona ameamua kweli. Lara hajulikani alipo. Na
kazi pia aliacha. Mimi nilikwenda kumchukua Suzy siku hiyo usiku, nikamuacha chumbani
kwake hakuniambia chochote. Kesho yake wenzie ndipo wakagundua ameondoka na
ameacha ujumbe kuwa ameamua kwenda kuanza upya, akiweka mambo sawa,
atawatafuta.” Jax alihisi
jasho jembemba likimtoka wakati gari ilikuwa ikitoa hewa safi iliyochunjwa.
“Amesema ni wapi amehamia?” “Nimekwambia hakuna anayejua
Jax! Nilichosikia ameacha tu kazi na kuondoka.” Jax akawa ni kama haamini. “Lara hawezi kuacha tu kazi. Anahitaji sana ile kazi.
Umejaribu kumuuliza bosi wake?” “Mimi nimeheshimu maamuzi yake. Binafsi nimeona
anastahili kupata mapumziko mbali na sisi wote, zaidi wewe na Tula.” “Kwa nini
una...” “Subiri kwanza Jax.” Tino akamkatisha.
“Nisikilize tu Jax. Najua wewe una akili nzuri tu.
Ulifikiria kwa fujo yote ile siku ile pale baa. Kati yako na Tula, tena Tula
akisema ana mimba yako, ulifikiri Lara angebaki?” Tino akamuuliza. “Eti Jax!? Maana nilimwambia
hata dada Nelly. Kwanza amefurahia sana kuondoka kwa Lara. Nakwambia hujawahi
kumuona dada Nelly akiwa na furaha vile! Kafurahi mno. Na kwa taarifa yako tu,
amesema sasa hivi hajali tena na wala nisimtafute hata nikikuona unafungwa jela
na Tula. Amesema wazi siku ile alikuja pale sababu ya Lara tu. Kwa heshima ya
wazazi wake. Lakini amesema sasa hivi hataki kusikia tena habari zako na Tula.
Ameniambia nikwambie ukijisikia kwenda kwake iwe ni salamu tu. Hata ukifungwa
jela na Tula, nisimwambie wala kumtafuta. Labda ukiwa umekufa ili akakuzike
karibu na kaburi la baba yenu.”
Jax akaumia sana.
“Sasa mimi nimefanya nini tena!?” “Samahani nilisahau.
Amesema hataki kukusikia wewe, Tula na huyo mtoto wenu pia usiwahi kumpeleka
nyumbani kwake. Amesema wewe endelea kuzaa tu na Tula mpaka mayai yakuishie.
Lakini asione sura zenu nyumbani kwake.” “Kwani..” “Sijamaliza.” Tino mshabiki akaendelea kutoa ujumbe.
“Amesema dada Nelly siku ukiwa naye, halafu ukataja
jina la Tula, anakutoa meno ya mbele. Na ukijichanganya ukaenda wewe na Tula
nyumbani kwake, anawakata miguu. Amesema nihakikishe unapata huu ujumbe kwa
kuwa na yeye amemuwekea restrain oder
Tula.” Kimya.
“Umesikia vizuri Jax?” “Nashukuru kwa ujumbe. Kwaheri.” “Sasa hakuna zawadi za Ulaya hata kidogo!?” Tino alijua wazi Jax amekasirika ila kutaka kumkera tu. “Nilimletea Lara tu.” “Ulifikiri atasamehe kila kitu kwa zawadi za Ulaya?” Tino akauliza akicheka kwa kejeli. “Naomba nikuage Tino.” “Sawa kaka. Msamilie Tula wakuchorwa. Lakini mwenzangu utafia pazuri! Tula huwezi kumlinganisha na Lara hata kidogo! Tula yupo kama umemchonga mwenyewe!” “Unatafuta kuniudhi tu Tino!” “Mimi nakusifia kaka! Uchaguzi wako mzuri. Tula si mchezo. Huwezi kumlinganisha na Lara ambaye sasa hivi ni kimbaumbau. Halafu amewapisha na kuwapa uhuru wote. Mshindwe wenyewe, hakuna tena hukumu. Si kwa Lara au kwa dada Nelly. Wote wamewapa baraka zote. Sasa hivi nenda kamfaidi Tula wako tu, mlee watoto wenu.” Alipoona Jax ametulia, akaona amkere zaidi.
“Kalee kaka. Nenda kalee watoto wa wanaume wenzako huku ukipoozwa na penzi. Na
wewe unakuwa unagawiwa kidogo kama pongezi ya kulea watoto wa mabwana zake
Tula. Unashika pembe, wenzio wanakamua tu.” “Tino!” Tino akacheka na
kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment