Muhudumu akarudi na chakula. Akaanza kuweka pale mezani. Lara akavuta sahani yake, aliponawishwa tu mikono yeye akaanza kula bila yakusubiri. Muhudumu akamsogelea Jax, akamuosha na yeye mikono. Maana alimwambia aanze na Lara. Alipomaliza kumnawisha Jax, muhudumu akaondoka. Na kuwaacha watatu hao mezani.
![]() |
“Namaanisha tokea narudi hapa nchini.” “Tula!” Jax akamsuta.
“Namaanisha tokea nilipoanzana na wewe.” Akarekebisha usemi wake. “Basi isiwe
tatizo. Kama mtoto ni wangu, mimi nitamtunza mtoto wangu bila tatizo lolote.”
Tula akamwangalia kwa kumshangaa. Lara kimya macho kwenye chakula chake. “Wewe
si umesema mtoto ni wangu? Ndio nakwambia nitamtunza mtoto wangu.” “Na mimi?
Maana mambo ya mimba unayajua.” “Naomba uweke swali lako vizuri.” Jax akaendelea
kuongea taratibu bila jazba.
“Namaanisha sasa hivi mimi naishije? Sina sehemu ya kuishi. Sina
kazi. Labda nirudi pale nyumbani kwetu mpaka mtoto atakapozaliwa
akichangamka ndipo nitafute kazi.” Moyo wa Lara ukazidi kuuma, lakini akabaki
ameinama na kuendelea kula.
“Cha kwanza, naomba niongeze msisitizo hapo. Nilikwambia wazi kabisa,
pale ninapoishi sasa hivi sio kwetu. Ni nyumbani kwangu ambapo
nimepanunua kwa pesa ya mkopo ninaokatwa mpaka sasa hivi kazini kwangu. Wewe
sio mke wangu Tula. Usiite pale ni nyumbani kwetu. Hapajawahi na wala
hapatakuwa kwako.” Jax akaendelea.
“Hakuna kitu chetu mimi na wewe.” “Isipokuwa huyu mtoto.” Tula
akamkatiza na kuongeza. “Atakapozaliwa, na vipimo vitakapoonyesha ni wangu,
mtoto wangu nitamtunza bila tatizo. Hilo halina ubishi na wala hutapata shida
juu ya huyo mtoto, endapo ni wangu. Naomba nikuhakikishie hilo. Wala usiwe na wasiwasi
wakunifuata nyuma popote pale. Namaanisha hata kwenye migahawa!” “Kwa kuwa
unanikwepa Jax!” Tula akalalamika.
“Sijakukwepa. Na wewe ni shahidi. Mara ya mwisho nilitoka na wewe,
nikahakikisha tunawekana sawa, na unaniuliza maswali yote ili kusitokee
kufuatana nyuma kama hivi. Na hukuniambia kama ni mjamzito!” “Kwa kuwa sikuwa
nikijua.” Tula akajitetea. “Basi Tula, naomba nikutoe wasiwasi juu ya huyo
mtoto. Kama ni wangu, mimi nitamlea.” “Na sasa hivi?” “Sasa hivi anahitaji
matunzo gani?” “Chakula. Kliniki na sehemu ya kuishi.” Jax akacheka kidogo na
kujivuta nyuma akamwangalia.
“Huyo mtoto kwa sasa hana shida na sehemu ya kuishi. Yupo na wewe
mama yake. Hilo moja. Pili, unayo magari yangu mawili. Ambayo ni jasho langu
Tula. Ulichukua gari ya Lara pia.” “Mimi sikuchukua, alinipa mwenyewe.” “Baada
ya kukukataza, pia ulichukua. Nilikuonya usimfuate Lara, wala usiwahi kumuuliza
kwa chochote ambacho nilishawahi kumpa, lakini hukunisikiliza na bado
ulipokea.” Jax akasisitiza.
“Lara huyo hapo, muulize kama sio yeye mwenyewe ndiye aliyenipigia
simu na kunipa yeye mwenyewe.” “Narudia
tena. Nilikukataza usichukue chochote kutoka kwa Lara. Na bado ulichukua.
Ungeweza kumkatalia pale alipokupa. Lakini kwa siri ulichukua mpaka pete ya
uchumba niliyokuwa nimemvalisha mimi, ukakaa nayo, tena zaidi ya mwezi bila
kuniambia wakati tulikuwa tukiishi nyumba moja! Nilipokuuliza, ukanitukana
matusi ya nguoni, na kunitupia pete ya uchumba niliyokuwa nimemvalisha Lara,
ila hukujibu gari ya Lara uliipeleka wapi, wakati na wewe nilikununulia gari
yako.” Jax akatulia kama kutaka kumsikiliza. Lakini kimya.
“Hivyo basi, ili wewe usife na njaa, ukaua huyo kiumbe asiye na
hatia, nakushauri uanze kuchangamsha akili Tula. Unayo shahada ya utawala.
Tafuta ajira.” “Sasa wakati sijapata kazi nitaishije?” Akauliza Tula bila wasiwasi. “Hujasubiri
nikamaliza. Unaniingilia wakati nilikupa muda wa kuongea.” “Haya,
nakusikiliza.” Tula akatulia. “Kipindi hiki huna ajira, na mtoto hajazaliwa,
badala ya kunifuata nyuma, na kuulizia marafiki zangu wapi nipo na nipo na
nani, anza biashara.” Tula akashangaa kidogo.
“Narudia tena, una magari yangu mawili! Hayo hayo yatumie kwa sasa
kuishi hapa mjini. Lile la Lara, lifanyie biashara ili ikuingizie pesa za
kukutunza hapa mjini na huo ujauzito.” “Sasa...” “Acha nizungumze nimalize
Tula.” Tula alitaka kumkatisha Jax. Tula akatulia. “Mtoto atakapozaliwa tu, na
kufanya vipimo tukajua ni wangu, mimi mwenyewe nitakupa utaratibu ambao
hautakuwa na maswali kwako wala kwangu, na nitahakikisha mtoto wangu anapata
matunzo yote.” “Hala..” “Bado sijamaliza Tula. Usiniingilie. Sitarudia
kubishana na wewe tena. Na nilikwambia iwe mwisho wako kunitukana na kuniongelesha
mimi kama mtoto mdogo.” “Sijakutukana Jax!” “Basi nisikilize.” Tula akatulia.
“Kuna chombo kinaitwa Ustawi wa jamii.” Jax akaendelea. “Kinahusika sana na maswala ya jamii kwa ujumla wake. Kama hujaridhika na chochote hapa, nashauri uende ukazungumze nao, watakushauri vizuri tu. Kama watanihitaji kwa sasa, waambie mimi sina shida ya kukaa nao chini, ili wanishauri njia nzuri na sahihi ya kukabiliana na hili.” Jax akaendelea.
“Kwa kuwa nina uhakika, sisi
sio wa kwanza kujikuta kwenye hii hali, na wala hatutakuwa wa mwisho. Wapo watu,
tena wako kwenye ndoa kabisa za kanisani, na wanazaa nje. Wapo wanaotelekeza
watoto, ila mimi wangu sitamtelekeza na wala hatakuwa jukumu la mwingine.
Nitamtunza kama ni wangu. Sasa ni juu yako. Kufuata hivi nilivyo kushauri, au
nenda Ustawi wa jamii wenye uzoefu, wakushauri zaidi.” Mpaka Lara akamshangaa
Jax.
“Kwa kukusaidia tu ili uache kuhangaika kunifuata kila mahali. Naomba
nikuhakikishie Tula, pale kwangu, HUTARUDI.” “Nilitaka kwa ajili ya
mtoto.” Akajibu tena Tula bila wasiwasi
akionyesha wazi shida ni kurudi nyumbani kwa Jax. “Haitakuwa sawa kwa kiumbe
chochote kile kulelewa pamoja na watu kama sisi.” “Nimekuahidi nitabadilika
Jax.” “Na mimi hilo naliunga mkono kabisa. Itakusaidia sana Tula. Na kwa kuwa
unaakili nyingi kunizidi mimi, na ukaongeza tabia njema, nina uhakika utakuwa
mama mzuri kwa huyo mtoto na kwa mwanaume mwingine, lakini sio mimi.” Lara
kimya, Tula akaanza kulia.
“Nilikwambia na naomba niweke msisitizo kwa mara ya mwisho,
haitatokea mimi na wewe tukarudi kuwa pamoja.” “Nakupenda
Jax.” “Hicho unachotaka kukifanya sasa hivi, ni fujo Tula. Na
sitakuruhusu. Ni aidha uniambie kama wewe unabaki hapa, mimi na Lara tukuache,
au uondoke mimi nile.” Jax aliendelea kuongea taratibu tu bila jazba.
Tula akaanza. “Ulimuacha Lara akiwa
mjamzito hivihivi mpaka mimba ikaharibika, ukaua mtoto wako.” Tula
akavuta masikio ya watu, watu wakawageukia. “Sasa
hivi ndio umerudi kwa Lara ili uue mtoto wangu! Hiyo ni roho ya uuawaji Jax. Na
Mungu anakuona.” Tula akaendelea huku akilia. Jax hakujibu akabaki
akimtizama tu. “Wewe ni mkwepaji wa majukumu Jax.
Ukishaona msichana uliyekuwa naye ni mjamzito, unamkimbia. Ulimfanyia hivyo
Lara, ukanimbililia mimi, tena kwa kuvunja uchumba ambao mlikuwa mnakaribia
ndoa!” Jax akabaki akimwangalia tu. Alimjua Tula, nia yake ilikuwa
kumuharibia kwa Lara.
Na kweli akamgeukia Lara ili amsikilize maana Lara alibaki ameinama. “Lara wewe ni mwanamke kama mimi. Unajua madhara ya
kuachwa ukiwa mjamzito! Wewe yalikupata kutoka kwa Jax huyuhuyu. Alikwambia
anakuacha kwa ajili yangu. Hataweza kukuoa kwa ajili yangu. Sasa wewe kwa nini
hushangai ni kwa nini anarudi tena kwako sasa hivi na kuniacha mwanamke ambaye
alikutamkia wazi hataweza kukuoa kwa kuwa ananipenda mimi?” Lara kimya,
hakumjibu akarudisha macho kwenye chakula chake, akaendelea kula.
Kila mtu aligeukia meza yao. Tula alikuwa akilia kwa uchungu sana. “Unaniacha mimi na mtoto wako! Unaamua kututelekeza!
Unanikimbia unarudi kwa Lara, msichana uliyesema wazi humpenzi, ilikubidi tu
kuwa naye kwa kuwa mimi sikuwepo! Tena uliniomba msamaha, leo unanikimbia! Hata
miezi mitano haijaisha, unabadilika! Wewe ni mtu wa namna gani Jax? Unashindwa
nini kuwa mwanaume unayeweza kuishi na mwanamke mmoja, ukatulia?” Wala
hayo hayakuwa mageni kwa Jax, ila tu safari hii Tula aliyaongea akiwa
mnyenyekevu, akilia kwa uchungu kama aliyeonewa sana.
Hawakujua Tino alipotokea. “Simama Lara.” “Acha Tino.” “Usiniudhi Jax!”
Tino alishakuwa amekasirika sana. “Hivi unajua kelele za mwanamke wako zinafika
mpaka kule baa tulipokuwa tukinywa na washikaji?” Tino akauliza kwa hasira.
“Unataka kumdhalilisha Lara mpaka lini Jax wewe!? Hebu niambie! Unataka nini
kitokee kwa huyu binti?” “Nisikilize Tino. Nampeleka Lara hospitali. Sikutaka
twende akiwa hajala. Ndio maana tupo hapa. Ale ndipo twende.” Jax akaendelea
taratibu tu.
“Tula unamjua. Anachokifanya hapa si kigeni kwako wewe Tino. Ukiondoa
hasira, utagundua ni Tula yuleyule watokea chuoni.” Tino akamgeukia Tula.
“Alipotokea, mimi sijui. Amekuja hapa akanikuta nimetulia na Lara akaanza hichi
unachomuona anafanya, na si kigeni kwako. Tino wewe ni shahidi.” Kidogo Tino
akatulia.
“Acha hasira, na naomba ufikirie kabla hujaondoka na Lara. Ilikuwa ni
wewe. Nikashindwa kusimama kwenye nafasi yangu kama rafiki. Sasa hivi ni Lara.
Niambie ndugu yangu, nitaishi yale maisha mpaka lini? Tula atakuwa mtu wakuendesha
maisha yangu na kunichagulia niwe na nani mpaka lini? Niambie Tino mwenyewe au
nishauri sasa wewe. Natakiwa kufanya nini?” Jax akauliza kwa upole tu.
“Mimi nina mimba yako Jax! Na wala sikufanya kwa
ugomvi.” “Naomba
unisikilize Tino. Nisikilize tu na uwe muungwana. Ni lini Tula amekosa sababu
ya kunitoa kwa ninachokitaka, ili nifanye anachokitaka yeye?” Jax akamuuliza
Tino. “Anabadili tu visa.” Tino akajibu huku akimtizama Tula. “Exactly!
Anachofanya wakati wote nikubadili tu visa na sababu ya kuniyumbisha. Nilitaka
kuoa. Kwa sababu haikuwa ndani ya matakwa yake, akafurahia ujinga wangu na
akahakikisha naharibu mipango yote niliyokuwa nayo na Lara.” Jax aliongea
taratibu tu.
“Sasa ananiona nimejirudi kwa Lara, amekuja na swala la ujauzito huku
akitafuta kunichonganisha zaidi na Lara. Nimkose Lara, halafu aje aniambie
ananisamehe kama mimi ndiye niliyemkosea!” Lara kimya pembeni ya Tino. “Sasa
mimi nawaambia nyinyi wote watatu. Hata kama Lara atanikataa leo, basi. Nitajua
niliharibu mimi mwenyewe. Ila ujue Tula, ndio utakuwa umeharibu mahusiano yetu
kabisa. Hutakaa ukanisikia, na sitakaa nikurudie, hata iweje. Leo na mimi
naweka kikomo.” Jax akabadilika.
“Imekuwa nongwa! Mimi sio wa kwanza kukosea jamani na wala sitakuwa
wa mwisho! Ila nimejirudi, na nimekiri kosa. Ila Tula wewe ni kosa ambalo
sitakaa nikalirudia maishani. Nimekupa njia ya huo ujauzito. Nimekwambia
nitalea mtoto, mimba italelewa na mali zangu zote ambazo unazo. Kwako
nimemaliza Tula. Usinibabaishe na kunichezea akili zangu. Hujaridhika na uamuzi
wangu, nimekwambia nenda Ustawi wa jamii watakushauri chakufanya. Wakitaka
kuzungumza na mimi, nimekwambia nipo tayari. Nitawafuata popote, tulizungumzie
hili. Naomba usiwahi kunifuata tena na wala usinipigie simu. Nitakushitaki.”
“Utajuaje kama nimejifungua sasa?” Tula akauliza bila wasiwasi.
“Nimekwambia litakapofika swala la mtoto wangu, na tukahakikisha kama
mimi ndio baba yake, nitamlea mtoto wangu wala hutawahi kuniomba hata pesa ya
chupi yake. Nitajua chakufanya. Naomba uniache kabisa.” Akamgeukia Tino. “Naomba
uniachie Lara, Tino. Nataka nimpeleke hospitalini, kujua afya yake. Lara ni
wangu mimi. Nimemuomba muda, anichunguze. Sijamtaka chochote kingine ila hicho
tu. Naomba na wewe usinizuie.” Tino akamwangalia Jax akamgekia Lara, Lara
akainama kisha Tino akarudisha macho kwa Jax.
“Na wewe ukapime Ukimwi Jax. Tula hakutulia hata alipokuwa na wewe
alikuwa na mwanaume mwingine hapahapa mjini.” “Unafiki na umbea tu. Tokea
zamani hujabadilika wewe Tino! Sijui unataka kuolewa wewe na Jax?” “Nishakuzoea
wewe mdomo choo! Kwanza ushafukuzwa, unashangaa nini hapo kama sio kutaka
kuharibu zaidi?” Tino akamuuliza.
“Huoni aibu kujilazimishia kwa kila mwanaume?” “Hayajawahi kukuhusu
na wala hayakuhusu. Ni kati yangu mimi, Jax na mtoto wetu.” Jax akasimma,
akamzunguka Tino akamshika Lara mkono. “Twende Lara.” Lara akachukua pochi
yake. “Utakuja baadaye nyumbani?” Akamuuliza Tino wakati Tula anaendelea
kuongea. “Jana sikunywa kabisa sababu ya Suzy. Sasa leo nina kiu ile mbaya.
Acha nikate kiu. Sitaki kuja nikiwa nimelewa.” Lara akacheka kidogo. “Ila kesho
nikitoka kumpeleka mama kanisani, nitakuja.” “Sawa. Nitakuona kesho, Tino.”
Lara akamuaga, wakaondoka na Jax, na Tino naye akarudi upande wa baa alipokuwa
na rafiki zake, wakamuacha Tula pale.
...akichoka,
ameshapata.
Walipoingia tu kwenye gari, Tula akasimama upande wa dereva,
alipokuwa amekaa Jax. Jax akashusha kioo. “Gari yangu haina mafuta.” Jax na
Lara wakabaki wakimwangalia. “Naomba hela.” “Mimi sijatembea na pesa.” “Si
tuende kwenye kituo cha mafuta unijazie mafuta!” Tula akawa kama anamshangaa.
Jax akacheka na kutingisha kichwa, akainama kama anayefikiria. Akamgeukia Lara.
“Una pesa yeyote ile? Nitakurudishia baadaye?” “Nina elfu kumi tu.” Lara
akajibu wakati anafungua pochi yake. “Hiyo hiyo inatosha.” Lara akamkabidhi.
“Leo iwe mwisho wako wakuniomba pesa Tula na kunifuata kwenye mabaa.”
“Ningekupataje na wakati unajidai...” Lara akamuona Jax anapandisha kioo, Tula
akaweka mkono kama kuzia. Jax akashusha tena kioo. “Unataka nini Tula!? Shida
yako ni nini kitokee?” “Jax!” Lara akaita kwa upole. Jax akamgeukia. “Naona
mimi niwaache tu, mpate muda wa kuzungumza zaidi.” “Hicho ndicho alichokuwa
akikifanya maisha yetu yote ya mahusiano. Si kwako tu, ni kwa kila mtu.” Jax
akamgeukia vizuri Lara.
“Nakuhakikishia Lara, ukishuka leo kwenye hili gari, Tula hataishia
hapo. Atahakikisha anatuvuruga zaidi na zaidi. Atakushusha kwenye kila kitu changu
mpaka ahakikishe hurudi tena kuja kuwa karibu yangu. Huwa hawezi kuona
mwanadamu mwingine yeyote yupo karibu na mimi, akaweza hata kupumua.” “Sio
kweli.” Tula akabisha.
“Jiulize mwenyewe Lara. Kama shida kweli ingekuwa ni mtoto, mtu
mwingine angetaka nini zaidi na nilivyomwambia?” Lara kimya. “Na kama kweli
shida ingekuwa ni mafuta ya gari, pesa si umeshampa? Jiulize ni kwa nini yupo
hapa na mikono ipo dirishani?” Lara akanyamaza. “Ni tabia ya Tula, na sio kwa
sababu ananipenda. Ni kwa kuwa alijihakikishia amepata mtumwa wake anayeweza
kumtawala na kumfanya kama anavyotaka.” “Nakupenda Jax.” Tula akadakia.
“Nisikilize Lara. Nipo hapa na wewe kwa kuwa nimekuchagua wewe. Najua
nimekukosea sana. Kila mtu amenichukia na anakutahadharisha juu yangu. Yupo
Tula kama hivyo unavyomuona. Haya nakwambia mbele yake Tula ili uelewe.” Jax
akaendelea. “Muda mfupi uliopita, alinifuata na swala la ujauzito. Na wewe
ulikuwepo. Sasa hivi ametufuata hapa na swala la mafuta ya gari yake. Huyo ndio
Tula. Kwangu hatakosa sababu yakunitafuta. Na usifikiri ni leo tu. Amenitafuta
sana tokea mwezi uliopita.” Jax akaendelea.
“Sababu ya kutomuona jana pale baharini kwenye ile shuguli, ni kwa
kuwa mtu wangu wa karibu ambaye huwa anatoa maneno kwangu na kumpa Tula,
nilimuhakikishia jana sitakwenda kwenye ile shuguli kule baharini. Ndio maana
hukumuona Tula jana. Hakuwa akijua nilipo.” “Sio kweli.” Tula akabisha.
“Nisikilize mimi Lara. Kwa kuwa mimi namjua Tula. Na sio kwamba
nilidanganya, ila ni kweli nilikuwa sina uhakika kama nitakuwepo jana. Nilijua
ningesafiri, ila sikusafiri ndio maana ukaniona pale jana.” Jax akaendelea.
“Ninachotaka kukwambia, maadamu mimi ninaishi, na Tula yupo hapa nchini na
hajabadilika, haya yanayotokea sasa hivi, uyategemee kabisa. Ila yatakuja kwa
sura tofauti tofauti. Sasa mbele yake, nakupa uhuru na wewe kuchagua. Ila ajue
wazi Lara, ni aidha iwe ni wewe au mwanamke mwingine, ila hatakuwa yeye Tula.
Nimechoka, nataka kupumzika.” Lara akashituka moyoni na kuumia sana. “Hii
historia itajirudia tu!” Lara akajitahadharisha moyoni mwake baada
yakumsikia Jax akisema kwa ujasiri kabisa kama si yeye, basi mwanamke mwingine.
“Hapa haitakaa ikatokea nafasi ya mimi peke yangu hata siku moja.” Lara
akaendelea kuwaza Jax akiongea.
Akamsikia anaendelea. Akarudisha mawazo pale. “Kwako nimerudi.
Nimekiri nilikosa. Nipo tayari kurudi kwa wazazi kuomba msamaha. Nimekwambia
nipo nakusubiri mpaka utakapoona upo tayari, mimi nitakuoa wewe. Mimi ndiye
niliyekuharibia mipango. Nafikiri mimi ndiye mtu sahihi kabisa kutengeneza kama
utanipa nafasi.” Jax aliendelea mbele ya warembo hao wawili waliokuwa wakimsikiliza.
“Sasa upo huru kuchagua. Kusimama na mimi sasa hivi na baadaye au...”
“Na mtoto wetu?” Tula akaingilia kuongeza uzito kwa Lara kabla Jax hajamaliza.
“Sawa sawa, na kama mtoto atakapozaliwa, au unaondoka sasa hivi na kuniacha?
Hakuna kiapo kingine nitakachokuapia zaidi ya hiki. Na sina maneno mengine
nitakayokwambi ya ukweli zaidi ya haya. Nakupa muda sasa hivi uamue. Kwa kuwa
utakaposhuka tu hapa kwenye gari, utasikia maneno mengi zaidi ya haya ya Tula.”
“Ambayo ni ya ukweli Lara. Kumbuka Jax atakuwa baba watoto wangu. Na wewe
utakuwa ni kama unaingilia mahusiano yetu.” Tula akaweka msisitizo kumvuruga
zaidi Lara.
“Lara. Nisikilize mimi na
zungumza na mimi tu. Tula amejaliwa mdomo wa ushawishi.” Bado Tula alikuwa
ameshikili dirisha. “Sasa hapa nimemshawishi nini kama si kumwambia ukweli?
Yeye ametukuta kwenye mapenzi. Alikuwa mtu wa nje na namueleza kuwa ataendelea
kuwa mtu wa nje tu maana mtoto ameshaongezeka. Alijue hilo.” Tula akaongeza.
“Lara?” Jax akamuita ili kumtoa macho kwa Tula, amtizame yeye na ampe jibu.
Lara akamwangalia, akawa ameshageuka kuwa mwekundu kwa wasiwasi. Jax alionekana
anataka jibu, na hayupo kubembeleza tena.
“Mhhh!” Lara akaguna kwa sauti kama aliyechoka kabisa. Akafikiria
maisha yake. Pale alipo na yanayomzunguka. “Naweza
kupata mwanaume mwingine, nikatulia.” Akajishauri Lara. “Hii shuguli sitaiweza.” Akajiambia
huku akifikiria. Akanyanyua uso, akakuta wote wanamwangalia.
“Yatakuwa ndio maisha gani haya Jax!?” “Sijui Lara. Kwa sasa sina
jibu lolote. Nimekwambia kile ninachojua na kuelewa. Nakuahidi kile nitakachokisimamia
kuanzia sasa. Nataka kukusikia na wewe.” “Nakupenda Jax, lakini sijui
itakuaje?” “Na mimi sijui Lara. Lakini naamini tutapata njia kila
tunapokabiliana na siku mojamoja kabla hatujakaribisha matatizo ya siku
nyingine.” Jax akamuona amebadilika kabisa. Mwekundu mpaka masikio.
“Au nikupe muda.” Lara akatoa hilo wazi akiwa anatetemeka kwa
wasiwasi. “Mpaka lini?” Jax akamuuliza.
“Eti Lara? Ukumbuke ni maisha yetu mimi na wewe ndiyo yatakwama, ila sio ya
Tula kwa kuwa haja yake itakuwa imetimia. Na mimi sina huo muda wa kumpa Tula.
Nimempa muda mwingi sana mpaka nikatoa kafara mtoto wangu! Hapana Lara. Sina
muda. Ni aidha iwe na wewe au niendelee kwengine.” Lara akamwangalia kwa
kushangaa.
“Sikutanii Lara. Mimi namjua Tula kwa kuishi naye. Nisipoangalia,
nitazeeka niishie sina kitu chakueleweka. Sina mtoto wala familia yangu kitu
ambacho nimekusudia kuwa nacho. Si Tula wala yeyote atanizuia kufanya hivyo.
Sasa ni juu yako. Utakuwa na mimi au?” Lara akanyamaza na kuinama.
Jax akavuta pumzi kwa nguvu. Wakamuona anapiga simu. “Naomba uje na
wenzako hapa nje sehemu ya kuegeshea magari. Samahani lakini.” Akakata simu, Jax akatulia. Hawakujua
Jax alimpigia nani lakini wakahisi atakuwa ni Tino tu, ambaye walimuacha baa.
Pakatulia. Tula akiwa amesimama palepale na mkono ameshikilia dirisha.
Baada ya muda mfupi sana wakamuona Tino na wenzake wanakuja.
Wakasogea mpaka pale. “Nilitaka kuomba ushahidi tu, ili kusitokee kubadilika
maneno baadaye.” Wale wakashangaa vile Tula alivyosimama, Lara ametulia ndani.
“Nataka kuondoka, ila Tula ananizuia. Sasa mimi naondoa gari.” “Hapana Jax.
Huyu Tula anakutafutia sababu. Usimpe hiyo nafasi. Subiri.” Tino akamzuia.
“Mpwa!” Tino akamgeukia mmoja
wa kijana aliyekuja naye. “Naomba katuitie mmoja wa askari anayelinda hapa baa.
Mwambie tunaomba msaada wake.” Mmoja wao akaondoka, Tula akabaki amesimama
palepale. Ila akaanza kumtukana Tino. “Najua sana unamtaka Jax awe mpenzi wako
wewe. Tokea chuo nilikuona jinsi ulivyokuwa ukituingilia. Ukiniona na Jax tu,
roho ilikuwa ikikuuma. Si utafute mwanaume mwingine?” Tino hakujibu kabisa wala
Jax, wakanyamaza. Mpaka Lara akashangaa. Akaendelea kumtukana Tino, Tino na Jax
kimya.
Akarudi yule aliyetumwa na askari. “Naomba msaada wako, Mkuu.
Unamuona huyu?” “Mimi siye huyu, mimi ni mama watoto wake.” Tino akaanza
kucheka. “Unacheka nini na wewe Changu?” “Nakwambia Jax utanikumbuka. Mungu
ameamua kukulipa kwa maovu yako. Mwiba wa kukuchoma huo! Labda uombe awe
anadanganya. Ila kama mtoto ni wako! Utacheza naye ngoma hapa mjini huyo, mpaka
jasho la damu likutoke.” Tino akawa anaongea huku akicheka bila hata hasira.
“Wala hatazicheza na mimi!” “Ashaanza kujiita mama watoto wako, wakati hata
tumbo lenyewe halipo! Kama sio ngoma imeanza hiyo ni nini?” “Hajawahi kukutana
na simba mwenye njaa, au faru aliyejeruhiwa! Michezo yake naijua, na wala
hataninasa tena.” Yule askari alibaki akiwasikiliza.
“Naomba unisaidie kumtoa huyo dada kwenye gari yangu, ili tuondoke.”
“Kwani shida yako wewe ni nini?” Yule askari akamuuliza swali zuri sana na la
kiuungwana. Wote wakafurahia hilo swali. Tula akaanza kutokwa na maneno mengi
wakimsikiliza. Akarudia habari ya kuachwa kwa Lara akiwa mjamzito akamkimbilia
yeye, mpaka mimba ya Lara ikatoka. Akageuza habari. “Sasa hivi ananikimbia
sababu nimemwambia nina mimba yake tena. Aka..” Yule askari akataka kumuuliza
swali. Jax na Tino wakamuwahi kwa pamoja. “Muache amalize.” Kama waliokuwa
wameagana. “Huyo kwa maneno hutamuweza. Mwache amalize yote, ila mpe muda.
Lasivyo giza litatukuta hapahapa akiongea.” Akamalizia Jax. “Hiyo ni dharau kwa
mama watoto wako.” Tino akacheka sana.
Lara akahisi ni kama yupo anaangalia filamu. Hakika Tula
alimng’ang’ania Jax. Tula alijua ni nini anataka, na alitaka akipate. Mpaka
akamvutia Lara, akajiweka sawa kumtizama. Hakuona haya wala hakuyumbishwa na
maneno hata ya Jax mwenyewe. Na Tula mwenyewe hakuwa msichana wa hovyo! Hapo
amesimama, amependeza haswa. Dada aliyejaliwa rangi nyeusi isiyo na ubishi.
Umbile la kibantu lililoshiba na kuonekana kwenye aina yeyote ya nguo
atakayoweka mwilini, japo hapo alivaa gauni ya kumbana kidogo nakufanya umbile
lijichore bayana.
Lara akamtizama vile alivyo nadhifu, safi, jasiri na ule uzuri ambao
mpaka pale Lara mwenyewe mtoto wa mjini, mjua vizuri, hakuona kasoro!
Akastaajabu sana. Huwezi sema ni msichana aliyekosa mwanaume au kama atakuja
kukosa mwanaume. Yupo Tanzania ambako kwa asilimia 90 ya wanaume wanaota kuwa
na wanawake wenye umbile kama lake Tula! Anauwezo wa kupata mwanaume yeyote
anayemtaka yeye, mwenye hadhi yeyote ile! Lakini Tula anamtaka Jax! Lara
akabaki akimtizama Tula bila kutosheka.
“Nashauri haya mambo myamalize mkiwa mmetulia. Toa hiyo mikono hapo
ili usiumie. Wewe si umesema ni mjamzito sasa hivi?” Yule askari akamuuliza
taratibu tu. “Ndiyo.” Tula akajibu kibabe. “Angalia hili jua na hiki
unachokifanya. Si sawa kwako na kwa mtoto wako. Maadamu amekubali kulea mtoto
wake, nashauri utulie. Wenzio wanatelekezwa na watoto wanao fanana nao kabisa,
wala sio mimba ambazo hazina uthibitisho.” “Huyu mtoto ni wa Jax. Na Jax
anahitaji kukumbushwa tu mapenzi yetu.” Jax akainama na kutingisha kichwa.
Tula aliongea hapo, mpaka yule askari akashindwa. “Siwezi kumvuta
mama mjamzito.” Yule askari akataka kuondoka. “Basi naomba tuitie wale askari
wenyewe kabisa kutoka kituo cha polisi. Maana siwezi kulala hapa.” Jax akaomba
msaada kwa yule askari ambaye ni mlinzi wa pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment