![]() |
“Mimi nimeshangaa kingereza kinatoka tu!”
“Nimekusikia! Nikasema huyu mwingereza ametokea wapi hapa katikati ya jiji.
Kumbe Lara!” Wakacheka tena. “Kumbe unakuja kula huku!?” Lara akauliza. “Sio
kila siku.” Akajibu Jax. Wakacheka kidogo wakatulia. Akamuona Lara ameinama
kama anayetaka kupotelea mawazoni, akamuwahi. “Wana chakula kizuri.” Jax
akamrudisha pale. “Lakini garama! Nikila hapa week moja tu, mshahara wangu wote
wa mwezi utaishia hapa.” Wakacheka na kutulia tena kidogo.
Lara akainama na kuendelea kupanga
chakula hapo kwenye sahani akitumia uma wake bila kuweka mdomoni. “Lara!” Akamuita,
Lara akamwangalia. “Unaendeleaje?” Lara akamwangalia na kukunja uso. “Nataka
kujua unaendeleaje? Afya yako kwa ujumla.” “Vizuri.” Akajibu Lara taratibu. “Unakula vizuri?” Lara
akainama. “Eti Lara?” Akamuita tena. “Unakula vizuri? Namaanisha milo yote.
Kuanzia asubuhi mpaka jioni na kuhakikisha unakula vitu vya kuongeza damu?”
Lara akamshangaa kidogo na kunyamaza kama anayefikiria.
“Walikupa dawa za kuongeza damu?” Lara
akajua kama alishajua kama alikuwa mjamzito, mimba ikatoka. Akabaki ameinama. “Kwa
nini hukuniambia kama ulikuwa mjamzito?” Kimya. “Eti Lara?” “Inasaidia nini
sasa hivi Jax? Mtoto nilibeba mimi sio Tula. Mahusiano yalikufa na mtoto
alikufa. Si ushukuru Mungu huna sababu ya kuangalia nyuma! Huna sababu ya
kukufunga kwa yeyote, isipokuwa kwenye mapenzi ya kweli.” Lara aliongea
taratibu tu.
“Japokuwa iliniuma sana, lakini naona
ni kama Mungu aliruhusu kwa sababu, Jax. Hebu fikiria huyo mtoto angezaliwa,
nabaki naye mimi tu. Halafu anakuja kujua historia yangu yakuachwa nikiwa nina
mimba yake. Tena naachwa kwa kuwa baba yake hakuwa akinipenda, anampenda mtu
mwingine! Hudhani kama na yeye angeumia sana?” Lara akamuuliza taratibu bila
sauti ya juu akiheshimu watu wengine waliokaa pembeni yao.
“Huyo mtoto angekuwa kwenye mazingira
gani? Angeishi hapa duniani akijiona mimi na yeye wote hatufai.” “Lakini
nilitakiwa kujua Lara. Ilikuwa haki yangu kujua kama yupo mtoto wangu.” Lara akafikiria
kidogo. “Mwenzio nimejifunza kitu, Jax. Sio mambo yote yapo na majibu. Kuna
mambo mengine yalitakiwa yawe na majibu mazuri tu, lakini hayana. Mengine
yalitakiwa kuleta maana, lakini hayaleti maana. Nikujifunza kuishi vile
ilivyo.” Jax akabaki kimya.
Lara akaendela kula chakula chake na
juisi yake, Jax akiwa ametulia mbele yake. “Lara?” Lara akamwangalia. “Kuna
kitu nataka kukwambia. Na ninaomba uamini namaanisha.” Lara akabiki
akimwangalia wakati anamalizia juisi yake.
“Unanisikiliza?” “Naomba usirudie
kuniambia unampenda Tula kuliko mimi. Hilo ulihakikisha nalielewa kwa vitendo.
Tafadhali usirudie tena. Nilielewa na ndio maana nilikaa mbali kabisa na wewe
Jax. Kwa kuwa nakuheshimu na ninajua hujakurupuka. Hilo nimeelewa. Huhitaji
kurudia.” Lara akaendelea kuweka sawa chakula chake kwenye sahani.
“Naomba unisikilize tu.” “Hivi unajua
Jax na mimi nina hisia kama zako na watu wengine? Kama zako zakupenda zilivyo
juu, basi ndivyo ujue zangu za kuumizwa zipo juu. Usiendelee kufurahia kuumia
kwangu, Jax. Au wewe hudhani kama inatosha? Ni nini kibaya nilichokutendea
kiasi..” “Lara! Naomba unisikilize. Sina nia yakutaka kuendelea kukuumiza.”
Lara akatulia.
“Samahani
kwa yote. Zaidi naomba uamini kuwa najuta kwa kusababisha kupotea kwa mtoto
wetu.” Lara akaweka uma chini. “Hivi unajua unaongea na Lara hapa na si Tula?”
Lara akamuuliza taratibu tu. “Nafahamu.” “Basi naomba nikufariji kwa hili.
Hukusababisha kupotea kwa mtoto. Ila Mungu alikusaidia kukupunguzia matatizo.
Na kwa kuwa ni Mungu, atakupa mtoto mwingine kupitia Tula, kama mtataka. Kwa
yule niliyekuwa nimembeba mimi basi jua ni wa bahati mbaya kama watu
walivyozoea kuita mimba zinazoharibika kama kwangu na mwanangu. Kwa kuwa pia
aliingia kwa bahati mbaya.” Lara akasimama.
“Naomba tunapokuja kukutana wakati
mwingine, tuache mambo ya nyuma, yabakie nyuma, Jax. Mwenzio ninapotoka hapa,
sina faraja yeyote ile. Inanichukua muda kujituliza na kuweza hata kwenda
kazini. Tafadhali kuwa na ubinadamu hata kidogo kwangu. Na mimi naomba
unifikirie hata kidogo, Jax.” Lara
akaondoka nakumuacha Jax pale mezani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jax alimuharibia kabisa siku yake.
Badala yakurudi kazini akiwa amefurahia chakula chake, akarudi akiwa amepoa
kabisa. Kila mtu akamshangaa, lakini akakataa kuwaambia kulikoni. Baada ya nusu
saa, bila hofu Jax akamfuata pale kazini. Kila mtu akabaki amemkodolea macho.
Ni bwana harusi aliyeahirisha harusi, tena wakiwa wameshachanga.
Jax akamsogelea kiongozi wao wa pale
mbele. Walifahamiana vizuri tu. “Habari ya saa hizi?” “Nzuri tu, karibu Jax.” “Asante.
Samahani, sijui Lara yupo?” Akawa kama anaangaza pale. “Siku hizi Lara anafanya
kazi huko nyuma ya ofisi.” “Naweza kumuona?” “Subiri kidogo nimwite.”
Akanyanyua simu na kumpigia.
Baada ya muda Lara akatoka. Akashangaa
kumuona Jax pale. Jax akamsogelea. “Naomba tuzungumze kidogo hapo nje.” Lara
akatangulia nje bila ya kumjibu. Jax akafuata. Lara alikwenda kusimama pembeni
kabisa ya jengo. Jax akamsogelea.
“Sikutaka kukuharibia siku yako. Ndio
maana nilikuomba unisikilize.” Lara akatulia tu. Akakumbuka yeye ndiye
aliyemaliza mazungumzo yote. “Naomba nikwambie kile nilichotaka kukwambia.”
Lara akamwangalia. “Nataka ujue tu, kuwa nimeumia tumepoteza mtoto wetu.
Namaanisha wangu mimi na wewe. Najua wewe sio Tula, ni Lara. Msichana
uliyenipenda kwa dhati ila mimi ndio sikujua jinsi ya kuthamini mapenzi ya
kweli na ya dhati. Kwa hiyo najua nazungumza na wewe Lara.” Lara akainama.
Akajisikia kama machozi yanataka kutoka.
“Imeniuma na najutia kuliko mtu yeyote
yule atakavyoamini. Sikukusudia kuleta maafa makubwa hivyo kwako na kwa mtoto
wetu.” “Ulitegemea nini kitokee, Jax!?”
“Nilijua ingekuwa tukio la kushangaza kwa muda, lakini ungekuwa sawa, Lara.
Ungepata mwanaume kwa haraka, akakupenda na kukuthamini. Usingeumia wala kujali
kama nikiendelea na maisha yangu.” Lara akamwangalia kwa kumshangaa, akaona amuache
tu. Haina maana tena.
“Naomba nirudi kazini.” “Sijamaliza.”
Jax akamuwahi. “Ni nini tena!?” Lara akauliza kama aliyechoka tayari. “Pole kwa
kuugua sana baada ya kupoteza mtoto na nasikitika nilishindwa kuwepo
kukuuguza.” Mpaka Lara akakunja uso. “Ni nini unafanya Jax!? Ni nini unataka
kwangu zaidi? Au wewe unanichukuliaje? Kwa nini unanifanya mimi kama mdoli wa
kunifanya kile utakacho? Kama sina akili yakufikiria! Kweli Jax? Umeishi na
mimi zaidi ya mwaka. Kwa upendo na kukuheshimu. Kweli hiki ndicho kipimo
unachofikiria akili zangu zipo? Kwamba siwezi hata kufikiria!?” “Ndio maana
nipo hapa Lara. Ungekuwa mtu mwingine, nisingerudi.” “Kwamba uthamani wangu upo
chini kiasi cha kushindwa kufikiria?” “Sio hivyo Lara! Najua unaakili sana na
wala si mjinga. Ila nilitaka ujue kile ninachofikiria. Sijawahi kukuficha.” Jax
aliongea kwa tahadhari kama asiyetaka kuharibu.
“Kipindi unaniambia hunipendi mimi
unampenda Tula, n..” “Sijawahi kukwambia sikupendi Lara.” Lara akakunja uso.
“Jax!” “Sijawahi kukwambia sikupendi.” “Naomba nimalize kuongea kabla
hujanichanganya zaidi.” “Nakusikiliza Lara. Lakini sijawahi kukwambia
sikupendi.” Hapo Jax akakanusha.
“Vyovyote ulivyoniambia, lakini siku
unanitamkia unampenda Tula, huwezi kuwa na mimi, ndio na mimi nilikuwa
nimepoteza mtoto. Sasa, sasa hivi unaongea nini na uliniambia nini?” Lara
akamuuliza taratibu tu.
“Sio kweli kama ulishindwa kuwepo
kuniuguza kama mimi nilivyokuwepo kwenye maisha yako nikikuuguza vipindi ulivyokuwa
mgonjwa. Ulikuwepo, lakini ulimchagua Tula, badala yangu na mtoto. Ulikuwepo,
lakini ulikuwa na Tula! Tena kwa kuniambia mwenyewe! Sasa, sasahivi unaongea
nini!? Kwa nini unataka kunichanganya tu na kuniharibu zaidi?” “Sio nia yangu.
Nia yangu ni kuomba msamaha kwa yote, Lara.” “Yapi, Jax!? Nashindwa kuelewa! Ni
kama umechagua kuniumiza tu!” “Hata kidogo.” Lara akakunja uso kama asiyemuelewa
na ameshamvuruga.
“Naomba uniamini Lara, najutia.” “Hapo
ndio sikuelewi Jax! Au haya yote yanaletwa na wewe kujua nilipoteza mtoto au ni
nini? Maana hata mtoto mwenyewe hukujua kama yupo! Umesikia tu kuwa mimba
ilitoka. Unajuaje kama ilikuwa yako? Maana sijawahi kumwambia yeyote yule kuwa
nina mimba yako!” “Najua alikuwa wangu. Najua ulitulia Lara. Najua hukuwa na
mwanaume mwingine ulipokuwa na mimi. Najua kwa asilimia 100 kuwa alikuwa
wangu.” “Basi kama unajua hivyo, amini utapata mwengine kwa mwanamke
unayempenda Jax. Tafadhali naomba niache.”
“Sawa. Lakini nilitaka tu ujue hilo.
Najua nimeharibu. Sasa hivi sina haki yakurudi kinyume nyume tena. Ila niliona
nisibaki nalo moyoni. Sitaki kukuficha. Nataka ujue ukweli. Hata kama haita leta
maana kwa yeyote. Hata kama sitaeleweka kwa yeyote. Ila nilitaka
WEWE ujue kuwa, NAJUTIA YOTE, SAMAHANI NA POLE. Hilo ndilo nilitaka ulisikie
kutoka kwangu. Hata kama ukisikia nimekufa leo, nataka uwe umesikia kutoka
kwangu.” Lara akashituka sana.
“Unaumwa?” Akamuuliza kwa kujali kama kawaida ya Lara
kwa Jax. “Hapana siumwi. Lakini vifo vinatokea Lara. Naweza nikatoka hapa,
nikafa ndani ya gari yangu tu. Bila kuumwa au hata kugongwa na gari.” “Hapana
Jax. Wewe bado mdogo sana. Huwezi kufa sasa hivi.” “Huwezi jua Lara.” “Hapana.
Usiseme hivyo. Huwezi kufa. Bado unamaisha marefu na mazuri tu mbeleni. Mungu
atakulinda. Hutakufa bali utaishi.” Lara akawa kama yeye ndio ameingiwa tena na
hofu.
“Lakini nilitaka unisikie mimi mwenyewe
Lara. Sitaki nije nijute, niseme ningejua ningekwambia.” “Japokuwa sijaelewa,
lakini nimesikia Jax. Naomba uwe na amani tu. Kuna mambo mengine yanatokea,
yanakuwa magumu kweli, lakini Mungu anayaruhusu kwa sababu.” Lara akaanza kutoa
faraja.
“Kuna mstari wa bibilia baba anapenda
kunikumbusha tokea nipatwe na matatizo. Hata jana usiku alinipigia
akanikumbusha. Unataka nikwambie na wewe?” Lara akamuuliza kwa upendo tu. Jax akatabasamu
kidogo. Alijua wazazi wa Lara ni wacha Mungu. “Unasemaje?” “Unatoka kwenye
kitabu cha Warumi 8:28 nitakwambia kwa kingereza
kwa kuwa nimetoka kula kwenye mgahawa wakizungu, bado naona ulimi unataka
kuongea kingereza tu.” Jax akacheka sana.
“Lara!” Jax akawa akimwangalia. Kwa asili
Lara alikuwa mtundu na maneno mengi ya utundu kama Suzy kasoro matusi. Pale
kazini kwao wao wawili wakikosekana, kila mtu atataka kujua kulikoni. “Usifanye
mchezo na chakula ya kisu na uma!” Jax akaendelea kucheka. “Haya niambie.” “ ‘And we know, ALL things works together for good to those
who love God...’.” Inaendelea hapo. Lakini katika yote, kumbuka kila
kitu kinatokea kwa sababu. Hata katika lililonipata mimi..” “Na mimi Lara?”
Lara akakunja uso.
“Haya na wewe kupata mpenzi wako. Mimi
kupoteza ndoa na mtoto, hata katika hilo kuna kusudi tu.” “Mimi nilifikiri
umenipoteza mimi, kumbe ndoa!” Jax akalalamika. “Jax, huwezi kupoteza kitu
ambacho hujawahi kuwa nacho wala hujawahi kukimiliki! Ulinithibitishia wazi
kuwa, hukuwahi kuwa wangu japo tulikuwa pamoja. Hata tungekuwa na ndoa, bado
usingekuwa wangu. Kwa hiyo na hilo nalo nashukuru Mungu. Ni bora hata
ulivyonikimbia na kuhama nyumba kwa siri bila kujua, kuliko ningeishi na wewe.
Tukazaa, kumbe mwenzangu mawazo na moyo wako viko kwa mtu mwingine! Isingekuwa
sawa kwako wala kwangu. Ni bora ulifanya maamuzi magumu.” Lara akataka
kuondoka, akarudi.
“Lakini Jax, kwa jinsi tulivyoishi mimi
na wewe, nafikiri nilistahili kuambiwa mapema. Tena kutoka kwako wewe mwenyewe,
si kutoka kwa mpenzi wako. Kule nikunivunjia heshima ambako sidhani kama nilistahili,
Jax. Tuliishi vizuri sana. Tulikuwa marafiki wakucheka usiku kucha, hata mambo
ya kijinga, yalitufanya tucheke. Hatukuwahi kugombana. Tulielewana sana. Tena
katika kila jambo! Sikuwahi kukuvunjia heshima ndani wala hadharani!
Nilistahili kusikia kutoka kwako Jax. Tena mapema. Sio kunidanganya kuwa
ulishinda Kisarawe ukitafuta mashamba, kumbe ulishinda jumapili nzima kitandani
na mpenzi wako!” Jax kimya.
“Nafikiri sikustahili Jax. Ulinilipa
tofauti kabisa na mahusiano yetu. Ulinifanya nivae magauni ya sherehe, huku
ukijua wazi hutanioa! Usingeacha mimi niadhirike hadharani kwa kiasi hicho Jax.
Au kuniacha stendi ya basi nikikusubiri, wakati upo hapa hapa Dar, kitandani na
mpenzi wako! Hebu fikiria Jax. Ingekuchukua dakika ngapi kuja kunitoa pale
kituo cha mabasi, na kuturudisha kwangu na wewe kurudi kitandani kwa mpenzi
wako? Ingekugarimu nini Jax? Hasa ukijua unanifanyia mimi! Hata kama hapakuwa
na mapenzi, lakini tulikuwa marafiki wazuri tu. Wakati mwingine tulikuwa tukiwa
na Tino mahali, tunapata muda mrefu tu wakucheka na kufurahi. Sijui Jax, mimi
nafikiri sikustahili.”
“Kweli hukustahili Lara. Ndio maana
nipo hapa kukuomba msamaha.” “Sawa Jax. Kila la kheri. Mungu akujalie mara dufu.
Yale uliyopoteza, yale uliyokosa kutoka kwangu, yale unayostahili na
usiyoyastahili pia, Mungu akustahilishe na akupe.” Lara akarudi ndani
ofisini akiwa ametulia sio kama mwanzoni aliporudi.
Wakati anaingia kila mtu alimwangalia. Ndio
ilikuwa sehemu ya mbele ya ofisi yao. Ilikuwa wazi tu, sehemu ambayo wafanyakazi
wanaohusika na kuzungumza au kuhudumia wateja ndipo walikaa hapo. Kila mmoja
alikuwa na meza yake na kiti mbele kwa ajili ya kukalia wateja wakiwahudumia.
Na meza ya Lara ilikuwa hapohapo mbele, ila alihamishiwa ofisi ya nyuma. Akapitiliza
ndani back office.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hapohapo Suzy akamtumia ujumbe Tino. ‘Jax alikuwepo hapa muda si mrefu, alikuja kuzungumza na
Lara.’ Tino akampigia simu Lara. Lara akapokea. “Suzy
ameshakwambia kuwa Jax alikuja?” Tino akacheka. “Upo
okay?” “Mimi mzima tu.” “Nilitaka kusikia hivyo.” Lara akacheka. “Asante kujali Tino.” “Basi tutokeni leo, tuunge msafara wa wafanyakazi
wa benki wote kwenye beach Party. Suzy amesema hamna shida, nikuulize wewe.”
“Sasa nyinyi si wafanyakazi wa benki, sisi si watatushangaa?” “Mtakuwa na mimi.
Halafu ipo wazi kwa ndugu, jamaa ya wafanyakazi.” Lara akanyamaza.
“Ni jioni. Najua wazee
wataondoka, tutabaki vijana. Tule mziki mpaka asubuhi. Ukichoka nakurudisha
nyumbani.”
Lara akacheka kidogo. “Umekaa ndani sana. Tutoke kidogo
ucheke.” “Sawa. Si utakuja kutuchukua au unataka tukutane huko huko?”
“Nitawafuata. Nyinyi muwe tayari kwenye saa mbili. Tufike wazee wakiwa
washaondoka. Hasa bosi wangu.” Wakacheka kidogo wakakata.
Baada ya kama dakika 5 akasikia Suzy
anakuja huku akipiga kelele. Akajua tayari Tino amemfikishia ujumbe. “Party!
Ehehe Party! Oooh Party!” Akawa anacheza na kuimba mbele ya Lara. Lara akaishia
kucheka tu.
Juu ya Jax
na Tula.
K |
wenye
mida ya saa moja na nusu usiku Tino akawa amefika. “Lara yuko wapi?” “Naona
bado yupo chumbani kwake anajiandaa.” Tino akaenda kugonga chumbani kwa Lara.
“Ingia Tino.” Akamkaribisha. “Nikwambie kitu?” “Usianze kama mwenzio Jax. Ni
nini mnachoongea kinachoanza na kutaka kuweka msisitizo hivyo?” Tino akacheka.
“Sijamsikia huyo mtu
wala kumuona kwa muda mrefu. Mzima?” “Anaonekana mzima kama mfanyakazi wa benki
ya dunia. Ananukia neema tupu.” Tino akafurahi kuona Lara ameanza kuchangamka
hata akimzungumzia Jax, sio kwa hasira.
“Nataka kukwambia juu ya Jax na Tula.”
Lara akageuka. Maana alikuwa amesimama mbele ya kioo anajitengeneza usoni.
“Nikupe tu historia yao.” “Sidhani kama ni lazima Tino. Haitabadilisha
chochote. Tuache tu.” “Hapana. Kuna kitu natamani ukifahamu juu ya hao watu
wawili. Nisikilize tu.” Lara akafikiria, akaenda kukaa kitandani na
kumwangalia.
“Jax na Nelly ni yatima. Walio na ndugu
lakini walisuswa.” Tino akaanza hivyo. “Jax amelelewa na dada yake tokea mdogo.
Sijui ndipo wote wawili walipo athirika, au la! Lakini kama unavyomuona Nelly. Yeye
Nelly athari yake ipo bayana. Haamini mtu. Hataki ndugu wala rafiki. Hataki
watu wanufaike naye sasa hivi, wakati alihangaika yeye mwenyewe kufika pale.
Haamini watu na pia hataki watu wamsogelee halafu waje kumbadilikia kama
walivyowafanyia tokea watoto. Hapo napo ni parefu tu, anayo yake mengi.”
Akaendelea.
“Kwa upande wa Jax, mapenzi anayoyajua
ni ya dada yake tu. Ndio yupo vile. Haamini kama kuna kitu cha kudumu. Haswa
mahusiano. Mahusiano aliyonayo ni yale ya kijeshi kutoka kwa dada yake. Na
habari aliyokuzwa nayo ni kutoamini mwanadamu kwa asilimia zote. Kuwa,
mwanadamu ni mdanganyifu na anaweza kukubadilikia vibaya sana. Mbaya zaidi
kwake Jax, msichana wa kwanza na wa pekee kuwa naye ni Tula. Akaja kuwa kilekile
Jax alichokuzwa akiaminishwa na dada yake. Halafu sasa, haiba ya Tula haina
tofauti sana na Nelly ila yeye yupo upande wa pili. Ni control freak.
Sijui kama unanielewa?” Lara akanyamaza.
“Hata tulipokuwa na Jax chuoni,
washikaji walikuwa wakigombana na Jax sababu ya Tula. Alitaka kumtawala hata
muda wake, awe na nani na afanye nini. Akawa anafika umbali hampi nafasi Jax
hata na mimi! Akiwakuta mko naye, anaweza kuanza ugomvi makusudi tu, ilimradi
tu amtoe pale Jax.” “Sasa na Jax alikuwa akisemaje?” Tino akafikiria.
“Mimi sijui yule msichana alikuwa
akimwambia nini Jax wanapokuwa naye, aisee! Jax alikuwa hawezi kusema hapana
kwa Tula. Ni kama aliyekuwa na nguvu ya ajabu sana kwa Jax, ambayo kati yetu
wote hata dada yake hakuwa akielewa! Hata amkute katikati ya kujisomea, anaweza
kumtoa hapo, Jax akapotea. Na hapo labda mnakuta mna mtihani kesho yake!
Mtakuja kukutana naye chumba cha mtihani.” Lara akakunja uso.
“Mimi nilivyoona hivyo ilinibidi kwenda
kuzungumza na dada Nelly, ndipo akazungumza naye. Haikusaidia sana, lakini
ndipo akaishia Jax kupata daraja alilopata wakati kwenye kundi letu wote
tulifaulu sana. Nikikwambia tulifaulu, tulifaulu wote tena vizuri. Ndio maana
hata tulipomaliza chuo, japokuwa wote tulipata kazi, na Nelly anakazi nzuri sana,
na anafahamiana na wengi, alisema waziwazi hatamsaidia Jax kupata kazi.
Kuonyesha amekua, ni kuwajibika na makosa yake aliyoyaruhusu chuoni mpaka
kumpelekea kupata daraja alilopata, na ahangaike yeye mwenyewe mpaka afanikiwe.
Alisema atamlisha na kumpa malazi tu, mengine ahangaike mwenyewe. Na kweli Nelly
hakutania. Jax alisota mtaani na dada yake akimtizama tu. Maana sisi wote
kwenye kundi letu ni kama tulipata ajira siku ya mahafali yetu, au kama
tuliwahiwa na hii benki sababu ya kufaulu vizuri. Kwa hiyo hatukuhangaika kazi
kabisa.”
“Sasa kipindi hicho Jax ndipo alipomjua
Tula vizuri.” “Kipindi gani?” Lara akauliza. “Matokeo yalipotoka na yupo mtaani
hapati kazi halafu wenzake wote tuna kazi! Aisee Tula alimnyanyasa. Ndio kidogo
Jax ni kama akapata akili. Na hakuishia hapo, alimkimbia kabisa na kwenda
Norway na mzungu. Jax akajua na kuumia sana. Akajua hakuwa akimpenda ila tu
kumtawala.” Tino akafikiria kidogo. Kisha akaona aseme tu.
“Nimesikia kutoka kwa mtu ambaye anauhakika.
Nasikia Tula hakuolewa na huyo mzungu japo alivalishwa pete ya uchumba. Maisha
yakamshinda huko, akakimbilia London. Huko nako wakamchezea kupita kiasi. Akawa
hapati kazi, kwa kuwa UK bila karatasi au vibali vya kazi vya kueleweka nasikia
hapakaliki. Ndio nasikia akahangaika, akabahatika kupata nauli yakurudi
nyumbani. Sasa Pius anasema siku moja akakutana naye. Si unamkumbuka Pius, yule
jamaa wa auditing? Rafiki yetu na Jax lakini yeye alimaliza CBE, unamkumbuka?”
“Namkumbuka Pius.” Lara akajibu.
“Pius anasema alipokutana na Tula,
akamuulizia Jax. Ndio Pius akamwambia Jax siku hizi mambo yake safi sana.
Akampa habari za Jax. Na akamwambia Jax siku hizi anahonga magari. Anaoa
mwarabu wa jiji kuu la Tanzania. Pius akatusimulia akamrusha sana roho Tula,
kwa kuwa sisi wote tulikuwa tunamjua jinsi alivyokuwa anampelekesha Jax, halafu
alivyoharibikiwa, akamkimbia. Ndio washikaji wanahisi Tula kama kawaida yake
atakuwa alimtafuta Jax, akampanga tena. Hatujui aliongea nini, lakini nataka
ujue Tula anayo nguvu kubwa sana kwa Jax. Sio kwa uzuri au ubora wake tu, ila
mdomo wake. Na ikifika kwenye swala la Tula, Jax anakuwa kama hajielewi. Sasa
sijui kwa kuwa alilelewa na mwanamke! Kuwa amejifunza kumtii mwanamke tu au la!
Hana mfano wa mwanaume aliyejifunza kwake kujua wanaume wanatakiwa wawe vipi,
sielewi!” Lara akaguna akifikiria.
“Sijui Tino! Mimi amenitafuta na
kuniambia mambo matatu aliyohakikisha nayasikia. Alinifuata mpaka kazini
tuliposhindwa kumalizana naye pale mgahawani.” “Mambo gani?” Tino akauliza. “Ameniambia
anajuta, anaomba msamaha na amenipa pole yakupoteza mtoto wetu.” “Wewe
ulimwambia maswala ya mtoto!?” “Hapana Tino. Leo ndio nimemuona Jax tokea aje
hapa aniambie ananiacha sababu ya Tula! Sikumsikia tena wala kumuona kwa bahati
mbaya. Sijui ameambiwa na nani!” Wakanyamaza wakifikiria.
Tino akapata wazo. “Itakuwa dada Nelly.
Maana mimi ndiye niliyemwambia dada Nelly. Atakuwa amezungumza naye. Halafu
pengine Jax amepata muda wa kufikiria.” Tino hakutaka kumwambia Lara kama
alishakutana na Jax na kuzungumzia juu yake. Hakutaka maswali ya nini walizungumza
juu yake. Akaona anyamazie hilo. Kwanza hawakuachana vizuri na Jax. Akaona ayaache
tu. “Lakini Tino, naamini na mimi nastahili mwanaume atakayenipenda kama vile yeye
anavyompenda Tula. Nimeridhika na kuja kwake na kuomba msamaha na kukiri kosa.
Inatosha. Naomba twende tukafurahie maisha.” Tino akacheka.
“Lakini ujue nimefurahi kuona
umefunguka Lara. Ulibadilika ukawa mnyonge sana.” “Kukataliwa kubaya Tino!
Sikia kwa watu, wewe yasikupate. Tena kwa kutamkiwa! Heri uhisi, halafu
mgombane muachane. Lakini si kwa kuambiwa yupo mtu mwingine, eti bora zaidi
yako! Inauma mno. Hata kama nitacheka sasa hivi, haiondoi ukweli.” “Naelewa.
Twende zetu tusirudi nyuma. Tumekubali kwenda kufurahia. Tukafurahie.” Suzy
akaingia.
“Umemuona mke wa Tino? Kibonge wangu
mwenyewe?” “Uringe?” Suzy akamshushua. “Huwezi kuwa na mke kama mimi.” Lara
akacheka. “Mimi nakupenda kama ulivyo Suzy wangu. Sitaki upungue wala nini.
Hivyo hivyo ulivyo mimi nakupenda tu.” “Usijidai wewe ndio unachakunivumilia, mimi sina.
Unakunywa pombe mimi sinywi na sijawahi kulalamika.” “Umeona jinsi tunavyopendana?”
Lara akazidi kucheka.
“Uje
uniache nyumbani ukalewe baa?” “Halafu nikose hizo kelele zako?” Wote
wakacheka. “Achana na mimi Tino. Kwanza siku hizi siongei sana.” “Nitamisi hiyo
sauti yako!” Sesi akaingia. “Ni nini humu ndani?” “Tino anamtongoza Suzy.” Lara
akajibu. “Anataka warudiane?” “Hatukuwahi kuachana wenyewe. Tulipeana tu
mapumziko.” Akajibu Tino. Suzy akabetua midomo. “Humtaki tena?” “Wa nini mimi
Tino? Sina haja. Naombeni twendeni.” “Wanasemaga hivyo hivyo lakini unakuja kushangaa
kesho vigelegele. Tino na Suzy kanisani! Tunaapiana wenyewe mpaka kifo. Wawili
tu.” Lara na Sesi wakaendelea kucheka, Suzy akatoka. Wakamfuata nyuma.
Wakaondoka.
Njia nzima Tino alikuwa akimpamba Suzy.
“Ungekuwa unanuka pombe, ningesema umelewa.” Suzy akaongeza. Kwanza alitaka
kukaa naye mbele. “Tatizo lako Suzy unapenda tupoteze muda mama watoto wangu.
Tuje tuzae watoto matahira, uzeeni.” Lara na Sesi walikuwa wamekaa vitu vya
nyuma, wakicheka. “Utakuwa na nani uzeeni?” Suzy akamuuliza. “Unafikiri
nikikuoa nitakuacha!? Wewe mpaka kifo.” Wakaendelea kutaniana mpaka walipofika
eneo la tukio. Tino akawaambia wapitilize moja kwa moja nje, ndio wapo vijana
upande wa baharini.
Upepo wa Ufukweni,
Hapaharibiki Kitu.
N |
a
kweli upande wa bahari kulishakuwa giza, lakini mziki uliendelea. Kulikuwa na
watu wengi. Wafanyakazi wa mabenki mbalimbali hapo jijini na ndugu, jamaa pamoja
na marafiki. Fujo. Watu wanakunywa na kula bure kwa idhini ya mabenki waliodhamini
hilo tukio la kuwaweka wafanyakazi wao pamoja kama kubadilishana mawazo na
kufurahia tu.
Wakatafuta sehemu wakakaa. Tino akaenda
kuwatafutia vinywaji, akaja navyo. “Sasa twende mama watoto wangu
nikakutambulishe vizuri kwa bosi wangu mpya. Siku ile alikuona ulipokuja
kunitukana tu. Hamkupata muda wa kusalimiana.” Mpaka Suzy mwenyewe akacheka.
Wao wawili wakaondoka. “Hawa watu, huwa wanawezana wao wawili tu!” Sesi
akaongeza na kucheka. Wakabaki hapo Sesi na Lara.
Walikaa hapo kwa muda, Suzy na Tino hawarudi. Sesi naye akaona watu anao fahamiana nao. Akanyanyuka kwenda kucheza mziki. Lara akakataa kwenda kucheza akabaki amekaa pale peke yake. Kila mtu alikuwa akinywa na kucheza, kasoro Lara alikuwa amekaa peke yake. Ametulia tu anaangalia watu wanavyofurahia.
Lara huyu sio Lara mtoto anayependa kujirusha
tena. Enzi zake angekuwa katikati ya umati akicheka na kugonga na kila mtu kwa
furaha akisikika akishangilia. Lakini mapenzi yalimtenda vibaya! Akadhalilika.
Akapunguzwa, hata kwenye mizani alijua hataonyesha uzito. Ujasiri uliondolewa
kabisa. Akabaki aibu tupu! Alinywea hata alipokuwa peke yake alihisi watu
wanamwangalia na kumnyooshea vidole. Akabaki kimya pale akiwaza yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa mawazoni hata asijue alipo akasikia mtu amemfunika koti
mgongoni. Akageuka. “Jax!” Akashituka sana. “Nimekuona unatetemeka baridi.”
Lara akacheka kidogo akijiangalia lile koti mabegani kwake. “Nahisi siku hizi nina
ugonjwa wakusikia baridi! Nalala na mablangeti na joto hili!” Jax akakaa. “Ni
upungufu wa madini ya chuma.” Lara akakunja uso. “Huna damu yakutosha Lara.
Ndio maana nilikuuliza kama walikupa dawa zakuongeza damu.” Lara akanyamaza na
kugeukia pembeni, akatulia kama ambaye hakutaka kujibu asione umuhimu wake.
“Lara? Ni muhimu kujua.” “Sikupewa dawa Jax. Ila nilipokuwa nyumbani
mama alikuwa akinikazania mboga za majani na ile juisi ya losera. Sikuwa na
wasiwasi, nilijua nimerudisha damu vizuri.” Lara akamjibu. “Basi inaonekana bado
hujarudisha damu yakutosha.” “Na mama naye anawasiwasi huohuo. Hata juzi kina
Tino na dada Nelly walipoenda, akawafungashia mboga za majani nyingi! Mpaka
nikamuonea huruma Tino.” Jax akashituka kidogo.
“Dada Nelly na Tino walikwenda Dodoma!?” Lara akashangaa kidogo.
“Kwani dada Nelly hakukwambia kama alirudi kwa wazazi kuzungumza nao baada ya
wewe kunikataa au kuamua kuvunja uchumba na kuahirisha ndoa!?” Jax akanyamaza.
“Mimi sikuwatuma Jax. Naomba usinifikirie vibaya. Ni dada Nelly mwenyewe
alinifuata ofisini akazungumza na mimi. Alitaka kujua ninaendeleaje. Akaleta
chakula na matunda.” Jax akamwangalia kwa mshangao zaidi.
“Hata mimi alinishangaza hivyohivyo. Sikutegemea kama angeweza kuja
kuzungumza na mimi na kuniletea chakula na matunda. Na huwezi amini Jax,
ameniwekea oda ya chakula na matunda pale uliponikuta kwenye ule mgahawa, siku
ile nikizungumza kingereza.” Jax akacheka. “Wewe unafikiri kwenye aina ile ya
migahawa ningefikaje kama sio dada Nelly!” Wakacheka. “Basi mwenzio, naletewa
juisi na matunda kila siku. Jumatatu mpaka ijumaa. Na siku nyingine za weekend
naletewa vyakula nyumbani.” Jax akawa anacheka tu.
“Napendwa mwenzio!” Lara akamringishia. “Nakuona.” “Na ujue napendwa
na dada Nelly!” Wote wakacheka kwa
pamoja. Nelly huwa hajui kupenda mtu. “Lakini bado unaonekana hujarudisha damu,
Lara. Hiyo hali ya baridi kila wakati ni upungufu wa madini ya chuma.”
“Nitakwenda kupima jumatatu. Na nitamuomba daktari aniandikie dawa nzuri.”
“Naomba nikusindikize.” Lara akakunja uso na kumgeukia vizuri akimshangaa.
“Namaanisha Lara.” Jax akamsihi kwa kubembeleza. “Unataka kufanya
nini Jax!?” “Kukusindikiza hospitalini.” “Unajua simaanishi hivyo, Jax!”
“Unakumbuka ulinikumbusha tulikuwa marafiki?” Lara akamtizama na kuamua
kunyamaza tu. “Siwezi kushindwa kila kitu, Lara!” “Kwa hiyo unataka kusema kuwa
urafiki hutashindwa?” “Hata kama ni mjinga wa kiasi gani, na urafiki pia
unishinde! Hapana bwana!” Lara akamtizama na kujiingiza vizuri ndani ya koti
bila ya kumjibu kitu tena.
“Unataka kula nini?”
Akamgeukia na kumwangalia Jax vizuri. “Nikwambie kitu Jax?” “Kitu
unachotaka kula?” “Hapana. Kitu kingine.” “Tule kwanza.” “Hapana Jax. Naomba na
wewe unisikilize.” Lara akaweka msisitizo. “Naomba uwe na amani. Binafsi
nimeshasamehe ndoa na yule mtoto. Naomba usijisikie hukumu au kama unawajibika
kwangu kwa lolote. Sikudai kwa lolote, moyo wangu una amani na kila kitu.
Nahitaji tu muda na matibabu sahihi kama hizo dawa za hayo madini ya chuma.
Naamini nitakuwa tu sawa. Tafadhali acha kujisumbua na mimi. Hunisaidii.
Unaniumiza na kunifanya nishindwe kuendelea. Sijui kama unanielewa?” Kimya.
“Wewe kwangu hukuwa rafiki tu, Jax. Ulikuwa mpenzi! Na sikudanganyi
wala sioni haya kusema. Nilikupenda na kufunga macho na akili zangu nikawa kwako
tu. Swala la kunikataa, tena nikiwa nimebeba mtoto
wako na nikiwa nimeshajiona nakuwa mkeo, tunaishi pamoja, sio kitu naweza
kusahau na kupotea moyoni mwangu kwa haraka.” Lara akajifuta machozi.
“Nahitaji tu muda Jax. Naamini nitakuwa sawa. Kumbuka
mwenzio nimepoteza mtoto na wewe, Jax. Sio kitu kidogo. Siwezi eti nikageuka tu
kuwa rafiki, tukaendelea kuanzia hapo na kusahau kila kitu au kujifanya kila
kitu kipo sawa! Lara unayemfahamu wa zamani, siye huyu Jax. Moyo wangu umejeruhika kupita hivi ninavyoonekana nje.” Lara akajifuta tena machozi.
“Nahitaji tu muda. Naamini nitakuwa sawa. Ila naomba
muda mbali na hivi.” Akajionyeshea
kidole yeye mwenyewe na Jax. “Chochote unachotaka
kukianzisha sasahivi, sipo tayari. Misaada ya muda kwangu, kwa sasa
haitanisaidia. Unipeleke hospitalini, halafu ndio inakuaje?” “Tutajua
kuanzia hapo.” Lara akakunja uso huku machozi yakimtoka. “Jax please!
Usicheze na hisia zangu kwa kuwa unajua nakupenda.” “Na hilo ndilo
linanipa ujasiri wa kurudi kwako Lara. Najua unanipenda kwa dhati. Najua kwangu
ulitaka tu mapenzi. Najua unanipenda.” Lara akamwangalia kwa muda, akaamua
kunyamaza. Wakatulia kwa muda.
“Naenda kukuletea mchemsho wa kuku wa kienyeji na mboga mboga. Au
unataka wa samaki?” “Samaki tafadhali.
Nimekula kuku mfululizo. Asante.” Akambusu kichwani mara mbili. Lara akajikunja
na kuinama.
Baada ya kama dakika 20 akarudi na muhudumu na chakula. “Asante.” Jax
akamshukuru na kumpa pesa kidogo. Muhudumu akaondoka, akampa Lara supu, yeye
akachukua kuku wa kuchoma. “Ukitaka kuonja kuku, chukua hapa.” Lara akaangalia
chakula chake. “Naona hiki kitanitosha. Asante.” Akashukuru na kuendelea kula.
“Tino na Suzy wamenikimbia! Walikuwa hapa.” “Tino yuko kule karibu na
maji, anapiga tu kelele. Naona ameshaanza kulewa.” Jax akaongeza. “Leo amesema
hanywi. Anataka kumthibitishia Suzy kuwa yeye ni mwanaume wa kuoa.” Jax
akacheka na kubaki akifikiria. “Anaonekana anampenda Suzy! Pengine wao
watafanikiwa kuoana.” Lara akaongeza akiwa ameinamia sahani yake. Jax kimya.
“Unajua kesho pia tunaweza kwenda hospitalin?” Mwishoe akavunja
ukimya kwa kubadili mazungumzo. “Jumamosi!?” “Yeah. Naweza kuja kukuchukua
mchana au hata jioni.” Lara akakunja uso, akamwangalia kwa muda akaendelea kula.
Sesi akarudi akiwa amechangamka huku akimuita Lara kwa shangwe.
Akapoa gafla mara alipomuona Jax pembeni ya Lara. Lara akamwangalia na
kuendelea kula. Sesi akamwangalia Lara na lile koti la Jax, kisha akamgeukia
Jax. Wakaangaliana na Jax kwa muda bila salamu, kisha akaenda kukaa pembeni ya
Lara upande mwingine. “Kula.” “Acha nikamtafute Tino na Suzy, tukale. Njaa
inauma.” “Si ndio nakwambia ule hapa?” “Chakula chenyewe kidogo hicho Lara.
Kinakutosha wewe tu. Kula urudishe mwili. Nitarudi baadaye kukuangalia.” Sesi
akaondoka na kuwaacha wamekaa pale wao wawili wengine wakiendelea kusherehekea.
Wakamaliza kula, Lara akawa amechoka. “Tino aliniahidi nikichoka,
atanirudisha.” “Umeshachoka?” “Naona kwangu inatosha. Nataka nikalale. Baridi
inanitesa tu. Acha nimtafute.” “Naweza kukurudisha Lara.” Lara akamwangalia,
nakusimama. “Najua una majukumu yako mengi tu Jax. Naomba na mimi nisiongezeke
kwenye hiyo orodha. Asante kwa chakula na koti. Usiku mwema.” “Sina majukumu
yeyote yale Lara. Sasa hivi ni saa tano usiku, nipo hapa na wewe. Jua sina
majukumu mengine.” Lara akabaki amesimama anafikiria.
“Lara?” Lara akamwangalia. “Naomba nikurudishe mimi nyumbani.” Jax
akasimama na kumsogelea karibu kabisa. “Hamna sababu Jax. Tino atanirudisha.”
“Tino yupo na Suzy, na wanafurahia na wenzao. Yeye ndio ana majukumu kwa sasa.
Mimi sina. Sasa kwa nini hutaki mimi nikurudishe?” Lara akakunja uso huku
ameinama.
“Eti Lara?” “Uliniacha nikiwa nakuhitaji Jax.
Ukaniambia hunipendi. Kwa nini sasa hivi unataka...” Lara akajifuta
machozi. “Sijawahi kukwambia sikupendi Lara! Na sasa hivi nipo na wewe hapa.
Sina pakwenda.” “Unamaanisha nini!?” “Naomba
nipe nafasi na muda ili kila kitu kijijibu.” Lara akabaki akimwangalia kama hamuamini.
“Please Lara.” “Sikuelewi Jax!” Jax akamsogelewa na kumshika mkono.
“Naomba nisiongee chochote. Ulisema unahitaji muda, basi nakupa muda. Ila
usinifukuze. Mimi ndiye niliyeharibu. Naomba nafasi ya kurekebisha kwa namna
Mungu atakayonijalia.” “Iweje uje unigeuke tena,
Jax?” “Naomba tutoke hapa. Tukazungumze sehemu ambayo hamna kelele.”
Lara akakubali. Akaenda kumuaga Tino.
“Naondoka na Jax.” Tino akahisi hajasikia vizuri. Akamvuta pembeni.
“Unaondoka?” “Naondoka na Jax ananirudisha nyumbani.” Tino akamtizama kwa muda.
Lara akainama. “Kuwa mwangalifu Lara!” Lara akatingisha kichwa kukubali
akionyesha hana ujasiri. Akaondoka.
Alipomsogelea tu Jax, akashangaa Tino anampita na kusimama katikati
yake na Jax. “Unataka kufanya nini Jax?” Tino akamuuliza kwa hasira. “Kwa nini
unataka kumchezea Lara wakati sisi wote tunajua hapatakuwa na muendelezo wowote
ule ila kutaka kurudia yale yale?” Jax akatulia akimwangalia.
“Huondoki na Lara hapa.” Lara akainama nyuma ya Tino. “Usitufanye
sisi wote wajinga. Na sitakubali umuumize tena Lara. Ondoka na umuache. Usirudi
tena kwa Lara. Toka Jax.” “Simchezei Lara, Tino. Najua umekasirika lakini...”
“Hapana Jax. Ninakujua jinsi unavyokuwa, linapofika swala la Tula, na akili
yako. Huwezi kujisaidia. Ondoka. Mwache Lara.” Tino alishaanza kuvuta watu kwa
sauti ya juu aliyokuwa akiongea kwa hasira.
“Ondoka Jax. Ondoka. Sitakuruhusu uondoke na Lara, hata iweje. Lara
anabaki hapa, mpaka mimi nimrudishe. Toka Jax. Nenda kwa mwanamke wako.” Jax
akajikaza, watu walishatulia kutaka kusikiliza. “Acha fujo Tino.” “Mimi sifanyi
fujo yeyote hapa. Ila ninachokwambia hutaondoka na Lara hapa. Unataka kumfanya
kama mdoli! Hapana Jax. Sitakuruhusu. Wewe umemchagua Tula, nenda kwa mwanamke
wako. Acha kuchezea hisia za Lara.” Tino akazidi kuwa mkali. Jax kimya akimwangalia
yeye na Lara.
Tino akashangaa sana. “Una nini Jax lakini!? Hebu muangalie Lara
mwenyewe alivyo! Hata bado hajapona, na wewe unataka kurudi tena kumuumiza!
Unataka kuona nini kinatokea kwa huyu binti? Kwa nini humuhurumii?” “Mimi ndiye niliyemsababisha awe hivyo. Mimi
ndiye nimesababisha maradhi ya Lara, nimemuomba nafasi ya kutengeneza nilipo
haribu.” “Ili iweje? Eti Jax!?” Tino akamuuliza.
“Wewe si uliniona nilipokimbia na kujificha? Wewe mwenyewe
ulinitafuta na kunifuata. Ukaniambia mimi ni mjinga, fala na siwezi kufikiria.
Tula ameshika akili zangu, sijiwezi. Sasa nimejirudi, nataka kusimama sasa hivi
na nichukue hatua mimi kama Jax, kwa nini unanizuia!?” “Akirudi tena Tula?”
Tino akauliza. “Aliyekwambia Tula hayupo ni nani!? Tula yupo mjini. Na sasa
hivi nipo hapa na Lara.” “Mimi nakuona upo hapa na Lara. Je, Tula anajua kama
upo hapa na Lara?” “Sihitaji kumjulisha Tula kila ninachofanya Tino! Nina uhuru
wangu mimi mwenyewe.” Jax akajibu.
“Hilo umeligundua lini? Au unaongea sasa hivi kwa kuwa Tula hayupo
hapa?” “Hata angekuwepo hapa bado ningeongea hivihivi. Hanidai kitu. Na kama
makosa kufanya, nilifanya mimi mwenyewe kwa akili zangu. Tula hausiki. Mimi
ndiye niliyekosa.” Jax akaendelea. “Kutenda kosa si kosa, bali kurudia kosa
Tino.” “Jax usiniudhi wewe!” “Sasa kwa nini hutaki kunipa nafasi nyingine Tino!?
Ni lini mimi nilishamkosea Lara?” Kimya.
“Muulize Lara. Hatukuwahi hata kupishana neno. Kwa mara ya kwanza
nilikosea. Nilianguka. Nimegundua kosa, ndio najirudi. Na wewe nilikuita,
nilikuomba msamaha. Kwa nini unashindwa kunisamehe Tino?” “Kwa kuwa tunaijua
historia yako na Tula. Upo leo umesimama hapa, kwa kuwa Tula hayupo. Akikupigia
simu tu, utaondoka hapa kama unakimbizwa! Ondoka Jax.” Mpaka kina Suzy na Sesi
nao wakasogea.
“Basi kama wewe huondoki mimi naondoka na Lara.” Tino akageuka na
kumshika mkono Lara. “Twende Lara.” Wakaanza kuondoka. Jax akamfuata.
“Nisikilize Tino.” “Usinigusee Jax. Niachie.” “Sawa. Simama basi.” “Unataka
nini wewe?” “Unisikilize.” “Huna jipya Jax. Mimi nakujua.” Jax akasimama mbele
yao.
“Tula yupo mjini. Nilishaachana naye zaidi ya mwezi sasa. Akili na
mawazo yangu yapo kwa Lara tu tokea siku ile nilipokuita tuzungumze ukaniacha
pale. Nilitoka pale nikawa na Lara tu.” Lara akakunja uso. “Kivipi?” “Siwezi
kueleza mengi. Lakini naomba mnipe nafasi.” Jax akajiweka sawa. “Tino, punguza
hasira. Lara, nakuomba nipe tu muda. Naomba matendo yangu yaongee.” Tino
akatulia kidogo.
“Tula yuko wapi?” “Mimi sijui na wala hainihusu Tino.” “Sasa
haikuhusu vipi? Akirudi?” “Anarudi wapi?” “Si kwako? Kwani wakati wote huwa
anarudi wapi!?” “Nishamalizana na Tula. Naomba ukubali na uamini. Nimemalizana
naye na yeye anajua.” Wakatulia. Wote. Suzy, Sesi, Lara na Jax wakabaki
wakimwangalia yeye Tino.
“Hakuna baya nakwenda kufanya na Lara. Namrudisha tu nyumbani.
Akilala, mimi naondoka zangu. Kesho narudi kumchukua na kumpeleka hospitalini
kuangalia afya yake. Zaidi damu.” “Na wewe upime ukimwi. Tula alikuwa ana
wanaume zaidi ya 110 huko Uingereza!” Jax akacheka na kutingisha kichwa. “Sitanii
Jax!” “Mbona nilishapima tokea mara ya kwanza uliponiambia?” “Majibu yakawaje?”
“Sijaathirika Tino!” “Na kesho ukapime tena mbele ya Lara.” “Sawa mzee.”
Akamwangalia Lara.
Wakamuona ameinama tu kama anayefikiria. “Twende Lara.” Lara
akamwangalia Tino na Jax. “Twende nikurudishe nyumbani.” Akamgeukia tena Tino. “Utakuja?” Akamuuliza
Tino kwa upole. “Baadaye kidogo. Wewe nenda kapumzike.” “Haya. Usiku mwema.”
Akaondoka na Jax, watu wakiwaangalia.
Lara Ataka
Ukweli zaidi Kwa Jax.
K |
wenye
gari wakawa kimya. Lara ametulia, macho nje ya dirisha akionekana mawazo yapo
mbali na pale. “Unajisikiaje?” Lara akamgeukia. “Baridi?” “Hapana. Nipo tu
sawa. Nikuulize kitu Jax?” “Niulize tu.” Lara akamgeukia vizuri. “Ni nini kilitokea kati yako na Tula?” Lara
akauliza tu taratibu. “Maana mimi uliniambia unampenda. Ikawaje mmeachana tena!
Maana hii ni mara nyingine tena mnaachana. Na kwa maneno yako mwenyewe,
uliniambia unampenda. Japokuwa alikusaliti kwa kuwa na mwanaume au wanaume
wengine, bado alipokurudia, uliweza kuniacha mimi karibu na harusi, ukamrudia
yeye! Hicho ni kiwango kikubwa sana cha upendo, Jax!” Lara akaendelea taratibu
tu.
“Sasa, safari hii ni nini kimetokea kwenu nyinyi wapenzi wenye upendo
mkubwa kiasi hicho!” Lara akaendelea. “Na kabla hujanijibu, naomba nikukumbushe
Jax, unazungumza na mimi. Mwanamke uliyenikimbia kwenye nyumba tuliyokuwa
tukiishi ili uwe naye. Sasa safari hii ni kipi kinaweza kuwatenganisha nyinyi
wapenzi wa muda mrefu kiasi hicho?” Lara akauliza akiwa ametulia tu, akionyesha
kutaka majibu ya uhakika sio kuendeleza mchezo ambao hata yeye hakujua ni
mchezo gani safari hii Jax anataka kucheza naye.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
J |
ax akafikiria kwa haraka, kisha akatoa wazo. “Naomba nikujibu tukiwa tumetulia. Ni sawa?” “Sawa.” Lara akakubali. Walifika nyumbani kwa kina Lara. “Utaingia ndani?” “Ukinikaribisha nitashukuru.” “Karibu.” Wakashuka garini. Lara akafungua mlango wa kuingia ndani. “Natamani nioge kabisa, nitoe michanga ya baharini ndipo niingie ndani ya blangeti.” “Nitakusubiri.” Jax akakaa kwenye makochi, Lara akaelekea chumbani kwake. Baada yakuoga na kuvaa, ndipo akamuita Jax chumbani kwake. Akapanda kitandani na kujifunika. Jax akaenda kukaa pembeni yake.
Lara Apata Upande wa Jax na Tula.
Jax aeleza Kilichotokea Mpaka Kuvunja ndoa.
J |
ax akamfunika
tena vizuri akiwa amekaa hapohapo kitandani “Umechoka sana au unaweza
kunisikiliza juu yangu na Tula?” “Naweza kukusikiliza.” Akamfunika tena vizuri
kama anayerekebisha. Akavuta lile blangeti mpaka juu kabisa. Akaliweka vizuri
mpaka akaridhika kuwa amemfunika Lara vizuri. Ndipo akaanza. “Tula tulianzana
naye tukiwa chuoni. Ni mwanamke aliyekuwa kwenye maisha yangu kwa karibu sana.
Naweza kusema kuliko hata Tino unayefikiria damu yake ikitolewa itakuwa na jina
langu.” Wakacheka kidogo. Maana ndio usemi wa Lara kwa Tino na Jax.
“Tula alikuwa kama mke kwangu. Akanijua na kunielewa udhaifu wangu
wote. Nilikuwa siwezi kujificha kwa Tula. Aliishi na kuongoza mahusiano yetu
vile alivyotaka yeye, kwa kuwa ni kama nilimpa uhuru wote. Hapakuwahi kuwa na
jibu la hapana kutoka kwangu kwa Tula.” Jax akaendelea.
“Japokuwa kina Tino walishanilalamikia sana juu yake, lakini sikujali
kwa kuwa sikuona madhara yake kwangu na kwa yeyote yule. Nikahesabu ni kama mtu
anayenihitaji sana, kitu kilichonifariji mimi kama mtu ambaye sikuwa na ndugu
ila dada Nelly tu. Ile hali yake yakunitaka kupita kiasi, tena nikiwa sina
kitu! Naomba nikwambie ukweli Lara, niliifurahia sana na kunipumbaza kabisa.”
Lara akabaki akimwangalia.
“Najua unaweza usinielewe, lakini sisi ni yatima Lara. Na ndugu
walitususa. Nikabakiwa na dada Nelly tu. Tena yeye peke yake na ndugu tulikuwa
nao wala si mbali. Wako karibu tu na wanauwezo mzuri tu. Sasa kuja kupata
msichana kama Tula, mzuri wa kutamaniwa na wanaume wengi, halafu akaning’ang’ania
vile, kwangu nilihesabu na kutafasiri ni bahati ambayo haijawahi kutokea na
sikuwahi kufikiri inaweza kuja kujirudia maishani. Na mimi nikabakia kwake tu,
nikihakikisha simuudhi kwa lolote ili nisije mpoteza maishani. Nikabaki
nikimsikiliza yeye kwa kila kitu.”
“Aliponiacha na kwenda kwa
mwanaume mwingine, au wengine. Nafikiri nilikwambia kuwa aliniumiza sana.
Unakumbuka?” Lara akatingisha kichwa kukubali. “Aliniacha na hofu ya hali ya
juu nikiona ni kama nimetelekezwa peke yangu, sijui tena chakufanya. Nikapatwa
na ile hali kama mtoto anayemlilia mama yake asiondoke na kumuacha peke yake
mahali, na bado huyo mama akamuacha kikatili. Mimi ndivyo nilivyojisikia kwa
Tula. Narudia tena. Unaweza usielewe hiyo hali maana haieleweki na nimeshindwa
hata kujieleza kwa wengine, najitahidi kwako, kwa kuwa najua nawajibika kwako.”
Jax akaendelea.
“Sasa nakumbuka siku moja mara baada ya kutoka kwenye sendoff yako
Dodoma. Nafikiri juma lilelile, akanipigia simu na kuniomba tukutane kwenye
hoteli aliyofikia kutoka Norway. Hata sikuwa nikijua kama alikuwa Uingereza.
Nilichokosea, hata sikumwambia Tino au wewe, nikaenda.” Jax akatulia kidogo.
Tula akamuona mpaka macho yamebadilika rangi.
“Nakwambia ukweli. Naomba niwe muwazi kwako Lara. Tula hakutumia
nguvu nyingi kunishawishi. Nilikuja kuamka asubuhi pembeni ya Tula.
Nikajiuliza, niliwezaje kulala na mtu ambaye hata sikuwa nimemuona muda wote
huo! Haikuishia hapo. Ni kama ulimwengu mzima ukawa umesimama. Ni mimi na Tula
tu.” “Wakati huo hata ulinikumbuka Jax!?” Lara akauliza kwa upole.
“Ile shauku niliyokuwa nayo wakati ule, nilijiambia hakuna jinsi
nikalinganisha ule upendo ninaojisikia kwa Tula.” Jax akaendelea bila yakujibu
jibu la moja kwa moja. “Akanikumbusha na kunirudisha kule tulipokuwa naye
zamani! Ugumu wa maisha tuliopitia. Na sijui ni kwa vile alivyoniambia
alishindwa kuolewa sababu yangu! Sijui. Lakini nikampokea kwa upendo mkubwa
sana huku nikimuhurumia. Aliniambia aliteseka sana baada ya kumwambia huyo
mwanaume wake kuwa ananipenda mimi.” “Sijaelewa Jax.” Lara akataka maelezo
zaidi.
“Yaani Tula aliniambia alitaka kuolewa na huyo mzungu, akamvalisha
kabisa mpaka pete ya uchumba, akatambulishwa mpaka kwa familia ya huyo mwanaume
wa kizungu, lakini akagundua mapenzi yake yako kwangu. Kwa hiyo akamwambia huyo
mwanaume kuwa ananipenda mimi, huyo mwanaume akakasirika sana. Akaanza kumtesa.
Akaniambia ni kama akamfungia, ndio hapo ameweza kutoroka na kurudi Tanzania
kunitafuta.” “Ni kweli?” Lara akauliza.
“Aliniambia kila kitu alichojua nataka kusikia na kitakachonifanya
nishindwe kufikiria kabisa na nimuhurumie. Basi, akaanza kuweka mipango. Yaani
mambo yakawa yanakwenda kwa haraka. Ikaanza sasa aibu ya kuja kukutizama baada
ya uchafu wote ule. Nikamweleza jinsi ulivyo kwangu na vile ulivyo mwaminifu. Nikamwambia
najisikia vibaya nashindwa hata kurudi kwako. Akanifariji sana na akaniambia
utaelewa tu. Kwa jinsi ulivyo mzuri, utapata mwanaume atakayekupenda. Hilo nalo
likapitishwa kichwani kwangu kwa haraka. Nikasema unaweza kuumia lakini baada
ya muda mfupi, utapata mwanaume mwingine, maisha yataendelea.” “Uliwezaje
kufikiria hivyo Jax!?” Lara akashangaa sana, lakini Jax hakujibu akaendelea.
“Tukaendelea kukutana hotelini. Baadaye akataka tuhame pale.
Nikamwambia sithubutu kuhamia naye pale nilipoishi na wewe. Ile ni kama nyumba
yangu mimi na wewe. Nikamwambia itakuwa mbaya sana.” Jax akatulia kidogo.
Kisha akaendelea. “Kuna kitu nilikuwa sijakwambia Lara. Nilitaka iwe
kama suprise.” “Nini?” “Nilinunua nyumba. Nikasema iwe suprise. Kwamba wakati
tunatoka honeymoon, badala turudi pale Sinza, nikupeleke pale. Kama
kukufurahisha tu. Ni nyumba niliipata kwenye mnada. Nzuri tu na bei ilikuwa
nzuri. Hata Tino sikumwambia kwa kuwa nilijua, akijua tu yeye, atakuja
kukwambia.” Asijue anazidi kumuumiza Lara ambaye alishajua inamaana ndiko
walikohamia na Tula! Lara akaumia sana kuona yeye alijibana naye kwenye sehemu
ndogo, tena yakupanga, halafu Tula akaja kwa muda mfupi tu, na kuhamia kwenye
nyumba kubwa! Lara akazidi kuumia hata kule kuanza kumuelewa kukaanza kupotea.
“Basi, Tula akaweka pressure. Lazima tutafute sehemu yakuishi pamoja.
Huku akinikumbusha jinsi tulivyo hangaika sehemu yakuishi baada ya kumaliza
chuo, maana dada Nelly alishatufukuza nyumbani kwake na kumuonya Tula asiwahi
kurudi pale. Basi Tula akanilalamikia sana akinikumbusha tulikotoka na shida
tuliyopata kwenye maisha akiwa na mimi akinivumilia kwenye vijumba vya kupanga
tena uswahilini! Kama jinga vile, hilo nalo likaniingia, nikahamia naye kwenye
ile nyumba.” Lara akapoa, akawa kama amejibiwa kuwa na Tula naye alitoka naye
mbali sana, tena pengine mbali zaidi yake yeye. Kuwa Tula anayo haki yote
yakulia kivulini na Jax. Lara akapoa kabisa.
“Maisha yakaanza hapo. Yakatokea yote yakutokea kati yetu. Mimi na
wewe. Sikuwa na jinsi ya kujirudi kwa yeyote tena Lara. Nilishafika mbali. Kama
kawaida yake au kama vile nilivyomzoeza zamani nilivyokwambia mpaka wakina Tino
walinionya au kulalamika. Tula akawa tena kama yeye ndio mwenye ile nyumba
pale. Anajua kufanywe nini kuanzia asubuhi mpaka usiku. Hapo nikawa sijui kama
mwenzangu ulikuwa mjamzito na wala kama mimba ilitoka!” Lara akamuona mpaka uso
umebadilika tena.
“Alikuja kunitapikia dada Nelly, sijawahi kumuona akiwa amekasirika
vile! Katika maneno yake machungu, ndipo nikajua kama ulipoteza mtoto! Gari na
pete ulishampa Tula!” “Kwani hukujua!?” Jax akajicheka kwa uchungu. “Mahusiano
yangu na Tula! Wewe utashangaa tu. Anyways, nikachanganyikiwa sasa.
Kwamba Lara aliugua! Lara hana usafiri! Nikapata hukumu kwamba ni kama
nimekuadhibu zaidi ya nilivyotarajia! Nilijua ungeumia tu, ikawa basi, na
ungeendelea na maisha yako. Lakini sio kuugua kwa kiasi hicho! Dada Nelly
aliondoka tulipokuwa tumekutana, kama aliyeniomba nisimtafute tena.”
“Ikabidi kujikaza sasa na kumtafuta Tino. Naye akanitukana kwa kadiri
ya uwezo wake, lakini akanipa ukweli wote. Nikarudi nyumbani kwa Tula. Naye
akaniambia maneno machafu na ya kashifa ambayo hayakuwa mageni, lakini ikawa
kama amenifungua macho na amethibitisha alichoongea Tino miaka yote. Kwa mara
ya kwanza kila kitu kikafunguka mpaka akili zangu anazoita Tino za kijinga.”
Lara akabaki kimya akimsikiliza.
“Usiku uleule nikamuomba aondoke, nikamwambia ndio mwisho wetu na
nikamwambia nimejua amenidanganya.” “Kama angekuwa hajakudanganya je?” Lara
akauliza tena. “Nahisi nilifika mwisho Lara. Yaani kwa mara ya kwanza
nikafunguka macho nakuona yale hayakuwa mahusiano ya watu wawili. Na hayakuwa
sawa kwangu wala kwake. Tula hajui kunisikiliza Lara. Hivi au vile tulivyokuwa
tukiishi mimi na wewe na kupanga mambo yetu kwa pamoja na kuelewana,
usingetukuta hivyo na Tula.” “Sasa mlikuwa mnafanyaje!?” Lara akashangaa, maana
alimjua Jax anaakili nzuri ya maendeleo na mipango mizuri tu, na hakuwa mbishi
kabisa.
“Yeye atoe maagizo, mimi nikubaliane naye. Na nisikosoee hata kwa
kuongeza wazo. Sijui kwa wengine, ila ndivyo ilivyokuwa kwangu. Kwa hiyo
nikajua sitakaa nikamsaidia, na mimi sitakaa nikaweza kufanya hatua yeyote
ninayofikiria ni njema.” Akajicheka tena yeye mwenyewe. “Hata yeye mwenyewe
aliniambia sina akili ya kufikiria.” “Jax!!” Lara akashangaa sana.
“Kwani alikosea? Alikuwa sahihi Lara. Navunja ndoa iliyokuwa imebaki siku
chache tu, kwa maneno yake! Bila hata kuthibitisha! Hata mimi nilikubaliana
naye na kujidharau sana.” Lara akabaki akifikiria. Ni kama akapotea kabisa pale
kimawazo na Jax akamuona hasikilizi tena. Akavuta tena blangeti kama
anayemfunika tena kumbe nikutaka kumrudisha pale. “Asante.” Akashukuru
akionekana amerudisha mawazo pale.
Jax akaona aendelee. “Basi, nikamwambia aondoke pale. Kwa jeuri
kabisa, akakataa.” “Jax!” Lara akashangaa tena. “Tena hapo anavaa ili aende
club. Yaani ananiacha mimi ndani kwa kunitaarifu tu, wala si kuniomba ruhusa.
Sikumsemesha. Nikawa kama nimeshindwa kwa kuwa amenikatalia kuondoka. Nililala
pale kitandani kama lisaa au masaa mawili hivi, ikawa kama kengele masikioni.
Niliruka kama swala. Nikamkusanyia vitu vyake vyoooote. Nikamtupia nje.” “Jax!
Akija kurudi!?” “Nani amekwambia hakurudi? Humjui Tula wewe! Yaani alishajiaminisha
mimi ni mali yake kabisa.”
“Ulifanyaje?” “Ilibidi kusimama kiume haswa ili kumuhakikishia, mimi
ni mwanaume, nimeamua, na sitabadilisha mawazo hata iweje. Na nilihakikisha
tunapata muda wakutulia kama hivi, ili asifikiri namkimbia na kunifuata nyuma.”
Lara akabaki akimtizama. “Alifanya fujo nyingi tu aliporudi nyumbani na kukuta
mizigo yake ipo nje. Mlinzi akampeleka polisi. Nikaenda kumtoa kesho yake.”
“Jax!” “Kabisa. Tula ni mbabe na mkorofi sana.” Jax akafikiria.
“Halafu hatukuwa tumeanzia tu hapo. Unajua tangia tunarudiana hapa
baada ya kuvunja harusi yangu, nikaanza kuona tofauti. Unajua jinsi tulivyoishi
mimi na wewe kwa utulivu! Halafu tukaja kuishi naye, haikuhitaji matusi ya Tino
kuniambia nimejiingiza kwenye shida! Ile hali ya utulivu ikaisha. Jambo moja,
hadi jingine. Hali yakupokonywa uhuru wangu ikaanza kuwa dhahiri kabisa. Hakuna
amani, hakuna heshima!” Jax akatulia kidogo kama anayetafuta jinsi ya kuweka
sawa neno linalofuata, asiharibu.
“Tula anapika. Ni mpishi mzuri sana. Anaweza...” Jax akasita. Akawa
kama anayefikiria tena, ila akaona abadili anachotaka kusema. “Lakini hakuna
utulivu. Sijui yupo na...” Akafikiria
tena. Akawa kama amekosa jinsi ya kumuelezea. “Anyways. Nafikiri heri mimi na
wewe tungekuwa tumeachana kwa ugomvi au labda heri tungekuwa na matatizo,
lakini nikawa ni kama nimetoka kwenye kivuli, nikafuata moto! Kila kitu
kikakosa maana. Lakini nikasema nivumilie tu, nione mwisho wake halafu nikawa
ni kama najiadhibu. Nikajiambia yote yanayonipata ninastahili. Nikatulia.”
“Sasa kuja kusikia wewe ni mgonjwa, na mimi ndiye nilisababisha
kupotea kwa mtoto! Halafu bado hakuna nidhamu! Sio mke wangu wala hatuna mtoto
anayetufunga pamoja mimi na Tula! Nikajiuliza garama yote hiyo ninayolipa ni
kwa ajili ya nini na nani! Nini kinanifunga! Nikajiuliza nitaishi vile mpaka
lini! Kwa nini! Hayo yote yakaibuka kwa wingi na kasi kichwani mwangu
nakujigundua ni kweli sina sababu!”
“Sasa kilichoniuma zaidi ni pale nilipokuja kukuona wewe mwenyewe?”
“Wapi tena!?” Lara akauliza kwani hakukumbuka kumuona Jax ila siku hiyo mchana.
“Nilikuja nikaegesha gari karibu na ofisini kwenu ili kukuona.” Lara akashangaa
sana. “Nilikuona unatoka na kina Sesi mnakwenda kula. Nilikaribia kulia.” Lara
akakwepesha macho. “Ulikuwa umekwisha zaidi ya hivyo. Ulitoka ukawa kama unaota
jua. Nikaanza ku google palepale. Kwa nini
kuwe na joto halafu unatetemeka baridi!” Lara akacheka taratibu. “Na kweli
baridi inanisumbua!” Lara akaongeza.
“Basi na mimi nikashangaa hivyohivyo. Ndio nikajua ni upungufu wa damu. Nikaanza kufikiria vitu vya kuongeza damu. Matunda na jui..” “Subiri kwanza Jax, kwa hiyo wewe ndio umeniwekea bili ya matunda na juisi!?” Jax hakujibu. Ikawa kama ambaye hakutaka Lara ajue. Lara akakaa kwa mshituko. Ni kama akawa amepata jibu.
“Oooh my, Jax! Basi mimi muda wote najua ni dada Nelly,
kwa kuwa yeye ndiye aliyenifuata ofisini kwetu na kunisisitiza nile kwa kuwa
nimekonda sana! Akaleta chakula na matunda. Sasa jioni yake nilipojiwa na
muhudumu wa ule mgahawa, na yeye akasema hajui ni nani muhusika, sisi wote
tukasema ni dada Nelly na anafanya makusudi kutojitambulisha kama ni yeye
muweka bili ili asifuatwe nyuma. Nikaendelea kula bila shida!”
“Sijamtafuta dada Nelly kwa muda mrefu kidogo. Mara ya mwisho alikuwa
na hasira na mimi kama nilivyokwambia. Sijawahi kumuona akiwa hivyo!
Alinionyesha kwa maneno na vitendo kuwa nimemkera mpaka mwisho. Nikaona
nimuache kwanza mpaka nitengeneze. Au mimi mwenyewe nielewe ni nini kinaendelea
kwenye maisha yangu, ndipo nimtafute.” Lara akabaki ameinama akifikiria.
“Nikikuomba tena msamaha, unafikiri itasaidia hata kidogo?” Lara
akamwangalia, na kuinama. Akajivuta mwisho kabisa ya kitanda, Jax akasimama na
kumzungushia blangeti. “Asante.” Akatulia. “Eti Lara?” Jax akauliza tena. “Ili
iweje Jax?” “Tujipe muda tuone kitakachotokea. Please Lara.” “Hivi unajua
tumeishi pamoja kwa zaidi ya mwaka? Tena kama mke na mume mpaka ulipoamua kuwa
mimi sikufai! Sasa, sasahivi ni kipi cha tofauti unataka tufanye tena?” Jax
akanyamaza.
“Nimeingiza aibu na fedheha kubwa nyumbani kwetu, Jax! Watu
wananyanyasa wazazi wangu wanasema ni matapeli. Walitangaza kuwa naolewa ili
kujinufaisha! Watu wawachangie!” Jax akaumia zaidi. “Hapa ninapokwambia zile
zawadi zote nilizokuwa nimepewa, watu walidai. Mama akawa na kazi ya
kuwarudishia mmoja hadi mwingine. Kwa zile ambazo walishatumia pale nyumbani,
maana niliacha vitu vyote nyumbani, imebidi kumsaidia mama kununua na kulipa.
Mshahara wangu wa mwezi uliopita, karibu wote nimewatumia nyumbani uwasaidie
kwa kuwa baba na mama wanakusanya pesa za kulipa michango ya sendoff ambayo
ilishafanyika na watu wakala na kunywa. Lakini leo hii wanadai wazazi wangu!”
Lara akaendelea taratibu na kwa uchungu sana.
“Hali ilikuwa mbaya mno, sina jinsi nikakueleza ukaelewa. Baba
alishukuru vile dada Nelly alivyokwenda na kuwaachia pesa. Angalau anasema
ameweza kumaliza kwa wale waliokuwa wakimsumbua na kutuchafua. Kwa kifupi tu
Jax, ni mimi, mimi Lara, tuliyeishi wote muda wote huo nikikupenda, kukuheshimu
na kukujali kwa moyo wangu wote. Na bado hukunichagua mimi! Uliamua kuniacha,
tena nikiwa nimeshavaa magauni ya sherehe! Nikitangaza naolewa. Niambie Jax,
leo tunajipa muda wa nini tena?” Lara aliongea taratibu akiuliza kwa uchungu
akiwa ni kweli haelewi Jax anataka wafanye nini tena.
“Mimi ndiye niliyeharibu Lara. Nipe nafasi ya kurekebisha. Sihitaji
chochote kutoka kwako. Ila tu niahidi hutabadilika. Nakutaka Lara wangu ubakie
vilevile. Ila mimi ndio nibadilike, niwe mwanaume ambaye ulimstahili.” Jax
akajisogeza karibu. “Niangalie Lara. Niangalie tu.” Lara akamwangalia. “Najua
sasa hivi ni mapema sana. Huwezi kuniamini na bado unamaumivu. Usiharakishe kwa
chochote, usibadili mawazo juu yetu. Niachie mimi nirekebishe pale
nilipoharibu. Tulia tu mpaka utakapoona nimefanikiwa kutengeneza, ndipo wewe
mwenyewe uniambie kama upo tayari kwa ndoa.” Lara akakunja uso.
“Usinijibu kitu sasa hivi wala naomba usinikatalie, tafadhali.
Tumeshafanyiwa kila kitu, ilibaki tu ndoa kanisani. Tuachie hapo. Nipe mimi
muda. Niangalie. Nichunguze mpaka utakapoona nipo tayari kuoa. Kisha niambie.
Na safari hii hatutachangisha watu. Tutafanya harusi kulingana na uwezo wetu.
Hata kama watu watakuwa 10, basi tutafunga ndoa. Ni sawa?” Lara akainama.
“Lara? Nimekosa mama. Nakubali kuwa nimeharibu haswa. Nisamehe mpenzi
wangu. Sasa hivi hakuna mtu mwingine kati yetu, ni mimi na wewe tu. Makosa
yangu yatatokana na mimi sio mwanamke mwingine. Na ninajua na wewe ni shahidi yangu, tokea tuanzane mimi
na wewe, sijawahi kutoka nje ya mahusiano isipokuwa kwa Tula, na nakuahidi
haitakaa ikatokea tena.” Jax akaendelea kujisogeza. “Nakuahidi kutulia.
Nimejifunza kwa kumwaga damu ya mwanangu mwenyewe! Hakika sitarudia Lara.
Nakuapia na Mungu wangu atanisaidia.” Kimya.
“Nijibu basi Lara! Au wewe hutaki nitengeneza nilipoharibu?” “Sijui
tena Jax! Hakika sijui! Nipo kama niliyevurugwa haswa.” “Basi naomba tujipe
muda. Nisubiri huku ukikumbuka nimekosa sana na nimekuomba msamaha. Niangalie
matendo. Ukijiridhisha, niambie tufunge ndoa, tukaishi kama zamani. Tupate ule
usiku wakucheka.” Lara akazidi kuumia akiwa anakosa tumaini. “Lakini hayo yote hayakutusaidia kuwa pamoja Jax!
Hatukuwa na mengi lakini tulikuwa na amani kubwa sana. Sikuwahi kulala na
hasira, nililala..” “Na Jax.” Jax akamalizia maana ndio ulikuwa usemi
wao wakijisifia kwa watu wao wa karibu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jax alikuwa na usemi aliopenda kuusema na kujisifia kwa watu mpaka
watu waliomfahamu Jax wakaanza kuutumia huo usemi. “Siku
hizi hata nikiwa na njaa, sijala usiku, silali na njaa, nalala na mpenzi wangu
Lara.” Au alikuwa akisema. “Maisha yanaweza
yakanipiga nje. Kila kitu kikanipa sababu ya kukasirika. Lakini siku hizi usiku
ninaporudi kwa Lara wangu, anahakikisha anamuondoa hasira kitandani kwetu,
tunabakia kulala sisi tu wawili.” Wakati wote Jax alikuwa akisema
ameacha kuleta wageni kitandani kwake tokea amkaribishe Lara kwenye maisha
yake. Mgeni njaa, hasira, kutokuwa na
usingizi, wote wameondolewa na Lara kitandani. Wamebakia wao tu wawili. Na
kweli ndivyo ilivyokuwa kwa wawili hao mpaka kushangaza watu!
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wote wakawa kama wamepotelea mawazoni tena. Kama wanaojiuliza
walifikaje hapo walipo! Lara ndio alikuwa haamini kama hayo yameweza kuwatokea
wao! Vile walivyokuwa mpaka watu kuwatamania mpaka kufika kuwa gumzo! Ingetokea
kwa wapenzi wengine pengine ingeleta maana. Lakini sio Lara na Jax. Wote
wakabaki kimya mpaka Jax alipovunja ukimya. “Kesho nitakuja kukuchukua twende
hospitalini. Ukaangaliwe damu na mimi nipimwe UKIMWI, mbele yako.” Lara
akacheka kidogo. Akamkumbuka Tino.
“Nitamtafuta tena Tino nizungumze naye, japo najua nishamkera kupita
kiasi. Lakini nitamtafuta tu. Tino amenivumilia kwa muda mrefu sana. Tokea chuoni!
Anahaki yakuchoka.” Lara hakujibu. “Basi nitakuona kesho. Usiku mwema.” “Na
wewe Jax.” Jax akaondoka.
Jumamosi.
Jumamosi asubuhi akiwa anakwenda kazini, Jax akampigia simu Lara. “Uliamka salama?”
“Bado nipo kitandani.” “Samahani nimekuamsha.” “Hamna neno. Mbona asubuhi
asubuhi?” “Nakwenda kazini. Nitatoka kwenye saa sita.” “Oooh! Kazi njema.”
“Asante. Nije kukupitia twende tukale ndio twende hospitalini?” Lara akabaki kimya. “Lara?” Bado moyo wa Lara ulisita. “Naona labda ukitoka kazini ukapumzike tu Jax. Jana
tumechelewa kulala, asubuhi hii upo barabarani kwenda kazini. Usijali. Mimi
nitakwenda tu mwenyewe hospitalini. Nitakujulisha majibu yatakavyokuwa baada ya
vipimo.” “Natamani muda na wewe Lara?” Hapo akagusa moyo wa Lara,
akajisikia vizuri.
“Au unaona shida kuonekana na mimi tena hadharani?”
“Hapana Jax. Sina chakuficha tena. Kila mtu ameshasikia habari zangu.
Wanaonijua na wasio nijua. Sina chakuficha tena, ila nilikuwa nakuhurumia.
Nilifikiri ungependa usingizi wa mchana!” Akajirudi na kuwa muugwana tu. “Usijali. Nitawahi kulala usiku.” “Sawa. Nitakuwa nikikusubiri
basi.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika mida ya saa 7 mchana, Jax akawa ameshafika nyumbani kwa
kina Lara. Aliona kabisa hakuna aliyemchangamkia. Hata Suzy maneno mengi
alifungua tu mlango, alipomuona ni yeye, akaondoka akiwa amemuacha palepale mlangoni.
Jax akaingia mpaka sebuleni. Aliwakuta wote kasoro Lara. Akasalimia, lakini
hakuna aliyeitika. Wote macho kwenye luninga. Kimya. “Lara yupo?” Kimya. Akaona
isiwe tabu, akatoka pale bila kuwaaga.
Alipotoka nje akampigia simu Lara. “Nipo hapa
nje ya nyumba yenu.” “Nipo chumbani, nitatoka baada ya muda mfupi sana.” “Basi
nakusubiria hapa nje kwenye gari.” Jax akarudi
kwenye gari yake akakaa. Baada ya muda Lara akatoka. Alivaa kawaida tu lakini alipendeza
na bado alionekana mnyonge usoni. “Pole na kazi.” Akaanza Lara wakati anapanda
garini. “Asante. Umeshindaje?” “Vizuri tu.” Jax akaondoa gari.
“Unataka kwenda kula wapi?” “Popote pale. Sina uchaguzi.” “Huna hamu
na kitu maalumu?” Lara akafikiria. “Hapana sina chaguzi. Tunaweza kwenda kula pale
unapopenda kula ugali wa muhogo.” Lara akatoa wazo, wakacheka. Kisha kimya.
Mpaka sehemu ya chakula.
Wote waliagiza soda kwanza, ndipo akaja mtu wa jikoni wakaagiza
chakula. Kweli Jax akataka ugali wa muhogo, mboga za majani na samaki wa nazi.
Jax hakupenda pombe kabisa, si kama Nelly au Tino. Lara akataka ndizi mchuzi. Muhudumu
akaandika na kuondoka. Kulikuwa na watu wengi tu pale siku hiyo ya jumamosi mchana.
Lara akajituliza kitini akawa anaangalia pembeni lakini Jax alijua hayupo pale.
“Tunakuwa na hospitali maalumu kwa ajili ya wafanyakazi wa benki na
familia zao kutibiwa. Tunalipiwa matibabu. Tunakuwa na kadi kabisa. Kwa hiyo
nilikuwa nikifikiria, twende kwenye moja ya hizo hospitali, mimi nitakulipia
wewe.” “Hivi siwezi tu nikaenda kununua dawa za kuongeza damu na kuanza kutumia
bila kuhangaika kwenda kupima?” Lara alipomaliza tu swali, Tula akaja.
ATAFUTAYE HACHOKI!
“Mambo!” Akamsalimia Lara na
kuvuta kiti palepale kwenye meza yao, akakaa pembeni yao. Jax alikuwa amekaa
mbele ya Lara. Lara akamwangalia Tula na Jax. Akanyamaza. “Kuna kitu nataka
kukuonyesha Jax. Sina ugomvi na wala sikutaka kukukorofisha.” “Mpaka sasa hivi,
umenikorofisha Tula. Na nilikuonya.” “Nimefanya nini hapa? Nimekuja hapa mezani
kwenu, nimemsalimia Lara kwa heshima, na kukaa. Nimekosea wapi?” Lara kimya.
“Hiki unachokifanya hapa, wewe unaona ni sawa?” Jax akauliza taratibu
akionekana kubadilika kabisa na ameshapandwa na hasira. “Hupokei simu zangu na
umenizuia nisiingie nyumbani kwetu.” Jax akabaki akimwangalia. “Lakini
sitaki kesi Jax. Nimekufuata hapa ili kuzungumza tu.” Jax kimya akimwangalia.
Lara akashangaa hajibu. Ila akatoa simu yake akaangalia na kubonyeza kidogo, na
kuiweka mezani.
Tula naye akafungua mkoba wake akatoa karatasi na kama kijikaratasi
kidogo tu akaweka mezani. “Hiki ni kipimo. Ukiweka kwenye mkojo, kikionyesha
mistari miwili, ni mjamzito, kikionyesha mstari mmoja sio mjamzito.” Moyo wa
Lara ukalipuka ndani kwa ndani. “Sasa mimi nilipima. Ikatokea mistari miwili.
Nikawa sijaamini. Nikaamua kwenda hospitalini. Wakanipima, nikakutwa mjamzito.
Ndio maana nilikuwa nikikupigia tokea week iliyopita ili kukwambia ni
mjamzito.”
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usikose muendelezo kujua kitakachojiri. Jax anaomba nafasi
ya pili kwa Lara aliyeharibikiwa na mimba, huku Tula naye amerudi na habari za
ujauzito, nini kitaendelea...
0 Comments:
Post a Comment