Maamuzi mengine Magumu ya Jax,
Safari hii kwa Tula.
J |
![]() |
Jax alipata nyumba mpakani mwa Kawe na
Mbezi beach. Haikuwa nyumba kubwa sana, lakini nzuri na ya kisasa. Akatoa nje
kabisa ya geti. Mlinzi akamsogelea. “Unataka nikatupe?” “Hapana. Ni mizigo ya
Tula. Akirudi kutoka matembezini, hakikisha anachukua mizigo yake. Mwambie hakuna
kitu chake chochote kilichobakia ndani. Kwa hiyo asiingie. Umenielewa?” Yule
mlinzi akabaki ametoa macho. “Akiingia hapa ndani, ujue umeruhusu mtu hatari
ndani ya nyumba yangu. Na umpigie simu bosi wako, umwambie kwa miezi miwili mfululizo, nataka ulinzi wa
mchana na usiku. Umenielewa?” “Ndiyo.” “Kwa maana nyingine, hilo geti lisikae
bila mlinzi, na Tula ni mtu wa kwanza anayetakiwa kukaa mbali na hii nyumba.”
Jax akarudi ndani.
Akakumbuka Tula ana mabegi stoo.
Akaenda kuyachukua na vitu vyake vyote na kwenda kuvitupa nje. Juu ya lile
furushi lake kubwa la vitu. “Usihangaike kumjibu chochote. Mpe ujumbe wake,
basi. Akibisha, mwambie unamuitia mwizi au unampeleka polisi kama mwizi
mwingine tu.” Akamalizia hayo maagizo kwa mlinzi, akarudi ndani. Kwa mara ya
kwanza akajisikia amepata nafuu kifuani.
Kwa Lara.
K |
esho
yake mchana muda ambao alijua kina Lara huwa wanakwenda kula, Jax akaendesha
mpaka karibu ya ofisi yao. Akaegesha gari ili kujaribu bahati yake kama
atamuona Lara. Lile neno aliloombiwa na Tula kuwa Lara amekonda kama mbwa
aliyezaa na kukosa matunzo, lilimuuma sana Jax. Baada ya muda akamuona Lara
ametoka peke yake akaenda kusimama nje kabisa, sehemu yenye jua kama aliyekuwa
akisikia baridi. Akasimama kwa muda mfupi akamuona Sesi ametoka na sweta, akaja
Suzy akionekana anaongea zaidi anapowasogelea. Sesi na Warda aliyekuwa anakuja
nyuma yao wakaanza kucheka kile anachoongea Suzy. Akajua ni kawaida ya Suzy,
porojo zake. Lara alikuwa akivaa lile sweta aliloletewa na Sesi.
Wakamsubiri amalize kuvaa wakaongozana.
Akajua wanakwenda kwenye kibanda cha chips. Lara nyuma amekunja mikono ndani ya
sweta kama anayesikia baridi kali, kimya! Wenzake wanacheka mbele. Jax akabaki
ameduaa. Kweli Lara alirudi kuwa kama mtoto wa darasa la tatu. Kwa asili hakuwa
mnene. Lakini aliisha sana. “Sasa kwa nini asikie baridi na joto lote hili!”
Jax akaendelea kumuangalia akipita kwa mbali kidogo. Alijua kwa hakika
hawatamuona. Walimpita na kupotea kabisa. Jax akabaki ameduaa.
Mwishoe akatoa simu yake na kuanza ku Google kwa lugha zote mbili. Kingereza na
kiswahili. ‘Kwa nini mtu asikie
baridi kwenye joto?’ Majibu
yakaanza kuja mengi. Akaanza kuyasoma huku akimtafakari Lara vile alivyomuona. “Alionekana
mnyonge, lakini si mgonjwa.” Akajaribu kuvuta kumbukumbu zaidi
akimlinganisha na yale majibu.
Akajiambia sababu itakuwa ni upungufu wa
madini ya chuma. Hana damu yakutosha mwilini. Akakubaliana na hiyo sababu.
Akakumbuka aliambiwa Lara alitokwa na damu nyingi sana kipindi mimba ilipotoka.
“Sasa sijui kama walimuongezea damu! Na kwa kiasi gani!” Kwa mara ya
kwanza Jax akaanza kumuhurumia Lara zaidi. Hali yakujali ikamjaa, akaanza
kufikiria nini chakufanya ili kumsaidia. Akakaa pale kwenye gari akifikiria.
Muda ukizidi kwenda.
Mwishowe wazo likamjia. Akaenda kwenye mgahawa
uliokuwa karibu na ofisini kwa kina Lara. Hakuwa ameegesha mbali na hapo. Ni
kama alizunguka tu mbele yake. Huwa wanauza vyakula vizuri sana, ila bei
ilikuwa juu. Mtu wa mshahara wa kawaida, asingeweza kumudu kula kila mara hapo.
Hata yeye mwenyewe Jax hakuwa akila hapo kipindi anafanya kazi CRDB japo baada
yakumpata Lara, walishakwenda hapo mara kadhaa. Zaidi mwanzoni ili kumtoa
katikati ya Suzy na Sesi. Wapate muda wa chakula cha mchana wakiwa wawili tu.
Jax akaingia hapo na kuomba kuonana na
muhasibu wa hapo. Akaingizwa ofisini kwake. “Nataka kuweka bili ya matunda
yakuongeza damu na juisi. Kuanzia jumatatu mpaka ijumaa. Lakini nitataka huduma
ya delivery.” Yule muhasibu akajua hiyo ni pesa nzuri. “Ulitaka
vipelekwe wapi?” Akamuuliza Jax. “Pale kwenye kampuni ya simu. Afikishiwe Lara.”
Yule muhasibu akakumbuka. Akamtizama vizuri Jax. “Yule binti aliyekuwa aolewe, lakini
mwanamme aka..” Akatulia. Kama aliyejiambia isije kuwa anaongea na huyo bwana
harusi mwenyewe. Akatulia. Jax akabaki ametulia mbele ya kiti chake huyo
muhasibu ambaye ni kama meneja wa huo mgahawa pia.
“Ulitaka apelekewe muda gani?” Akabadili
mazungumzo kwa haraka na kuanza kuandika ili Jax asibadili mawazo. “Kwa leo iwe
kwenye saa 9 mchana. Lakini huyo atakayempelekea, amuulize ni muda gani anataka
awe anapelekewa.” Yule muhasibu akaandika kidogo. “Naomba kujua itagarimu kiasi
gani.” Akataka kumuita muhudumu wa jikoni. “Hapana. Hii nataka iwe kati yangu
mimi na wewe. Mtu yeyote asijue hayo matunda na juisi vinatoka wapi. Sijui
unanielewa?” “Kabisa.” Akajibu kwa haraka.
“Hapana. Nataka uelewe vizuri. Si Lara,
wala wafanyakazi wengine wanatakiwa wajue hili. Yapo matunda niliyoona
yanaongeza damu kwa haraka. Nataka hayo ndio awe anatengenezewa juisi kwa siku
atakazokuwepo kazini na matunda. Apelekewe na akiuliza yanatoka wapi, mpelekaji
aseme hajui. Kwa kuwa ni kweli awe hajui yanakotoka zaidi ya jikoni kwenu.
Sijui unanielewa?” Akatulia kidogo.
“Namaanisha nikitoka hapa, iwe ni
makubaliano kati yangu mimi na wewe tu. Basi. Unafikiri utaweza?” “Nitaweza na
nitahakikisha kila siku anapata matunda yake na juisi.” “Asante. Basi naomba
kujua garama.” Yule muhasibu akapiga simu, akazungumza na muhusika. Akapiga
mahesabu, akampa Jax. Jax akalipia kwa siku tano. “Tutaona itakavyokwenda. Kama
hakuna litakaloharibika, tutaendelea.” Walipowekana sawa, Jax akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika saa 9 mchana, Lara akiwa anafanya
kazi akapokea simu kuwa anaitwa mbele, kuna mgeni wake. Lara akatoka na
mshangao. Akakutana na kijana aliyevaa sare za ile hoteli. “Haya ni matunda
yako, na hii ni juisi yako pia. Nimetumwa nikuletee. Ila nataka kujua, kesho
unataka nikuletee saa ngapi?” Bado Lara hakuwa hata ameelewa. “Hivi vitu
vinatoka wapi?” “Pale mgahawani kwetu.” Akamtajia jina. “Nafahamu hilo ila
nataka kujua nani amekutuma ulete?” “Sifahamu. Ila natakiwa kujua muda unaotaka
uwe unaletewa kila siku.” “Mimi siwezi kupokea vitu ambavyo...” “Wooo! Wooo!”
Suzy akaruka kama mshale na kumuacha mteja aliyekuwa akimuhudumia.
Akamsogelea yule muhudumu. “Naomba
nikupokee.” Akavivuta kutoka mkononi kwa yule muhudumu. “Sasa, uwe unaleta kila
siku saa nne asubuhi.” Suzy akamwambia yule muhudumu. “Suzy!” Lara akashangaa
sana. “Acha habari zako za zamani.” Akamjibu Lara na kumgeukia yule muhudumu.
“Na kesho ulete saa nne asubuhi. Haya, kazi njema.” Suzy akamuaga yule
muhudumu. Watu wakacheka.
“Haya mwali, twende ukale. Unakataa
nini wewe!?” Akamvutia Lara jikoni. “Mwili huo unahitaji chakula. Umekonda
Lara, hutizamiki.” “Matusi hayo Suzy.” “Nakwambia ukweli. Kula.” “Sasa nani
amemtuma?” “Inahusu!? Wewe kula. Atajijua mwenyewe huyo secret admirer.”
Lara akacheka na kufungua ule mfuko.
Matunda yalipangwa vizuri. Akafungua na
juisi. “Hii juisi mbona nyekundu hivi! Nitaweza kweli!” “Kunywa kama dawa.
Huwezi kujua, inaweza kukusaidia Lara. Ulipoteza damu nyingi sana.” Aliposema
tu hivyo akapata wazo. “Nini?” “Nimejua mleta matunda.” Sesi alikuwa
akimuhudumia mteja wakati yale matunda na juisi vikiletwa. Alipomaliza tu, na
yeye akakimbilia jikoni.
“Niambie mwali. Nani secret admirer
wetu?” “Wewe akili zako kama Suzy. Hakuna secret admirer, ni dada Nelly
huyu.” “Kweli.” Wote wakakumbuka alimletea chakula na matunda. Lara akakumbuka
alimwambia alipoteza mtoto, akajua ndio anataka aongeze damu. Lara akacheka na
kuanza kula. Alifurahi sana kuona amemjali zaidi.
“Njooni tule.” “Mmh! Japokuwa natamani, lakini hapana Lara. Unahitaji kula. Umekonda sana.” Akakataa Sesi. “Hata kuonja tu Sesi na wewe?” Akauliza Suzy. “Kidogo tu Suzy na uondoke hapa, umuache mwenzio ale.” Suzy akacheka na kuchukua uma. Akala kidogo, wakamuacha Lara peke yake. Akatamani kumshukuru Nelly, lakini hakuwa na namba yake. Akabaki kujiuliza ni jinsi gani atamshukuru. Asijue. “Tino!” Wazo likamjia. Akakumbuka hazungumzi na Tino. Akaamua kunyamaza na kuendelea kula.
Wema Hauozi.
N |
elly
alikusudia kurudi kwa wazazi wa Lara kuonana nao. Bado hakujua ni nini
atawaambia. Ila aliazimia kwenda kuonana nao. Walikuwa wakarimu sana kwao
kipindi walichoenda kutoa mahari na kwenye sendoff ya Lara. Nyumbani kwao ilikuwa
uswahilini haswa na ni padogo, kwa hiyo wageni wote wa Jax na huyo dada yake
walishukia hotelini, lakini mama yake Lara alihakikisha anawapelekea chakula
kizuri na kila wanapokwenda kwao pia aliwatayarishia vilivyo, ilimradi tu
kuonyesha upendo wao kwao.
Ijumaa akampigi simu Tino. “Nina tiketi yako
ya ndege ya kwenda Dodoma, nyumbani kwa kina Lara. Tunaondoka mimi na wewe tu.
Kesho asubuhi, tunarudi jioni.” Nelly akamaliza. “Hata hujanijulia
hali dada yangu! Kama nipo hospitali?” “Nitakuja kukufuata hukohuko tuondoke.
Usinipotezee muda mimi. Nakutumia picha ya tiketi uone muda halisi.
Usinicheleweshe.” “Au nije nilale kabisa nyumbani kwako ili iwe rahisi?” “Kwa
nini hupendi kwako wewe Tino?” Tino akaanza kucheka.
“Kumbuka nakusindikiza
Dodoma.”
Nelly akacheka. “Na sio uchelewe kuja. Ukikuta
nimefunga mlango, usigonge kengele. Uondoke.” “Sasa si nakuja na njaa kabisa?”
Nelly akamkatia simu. Tino akaanza kucheka mwenyewe. “Nelly!” Akatingisha kichwa huku akimfikiria. Lakini akafurahia
wazo la kurudi kwa kina Lara. Angalau kutengeneza au kuachana kwa amani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tino alipokuwa nyumbani kwa Nelly, akampigia
simu mama yake Lara na kumuomba kama wanaweza kwenda kuwaona siku inayofuata.
Mama yake Lara aliwakaribisha lakini akiwa na wasiwasi sana. Akajua wanakwenda
kudaiwa tu mahari yao. Hapo hapo akampigia simu Lara. “Naona
wakwe zako wanakuja kudai mahari yao.” “Kwa nini udhani hivyo?” Lara
akamuuliza mama yake. “Wanakuja kesho. Tino, yule
kijana aliyeturudisha huku wakati mgonjwa amenipigia, amesema anakuja na dada
yake Jax, ambaye ndio kama mama na baba yake.” Lara akatulia
akimsikiliza mama yake anavyomuelekeza kwa wasiwasi kana kwamba hamfahamu Tino
na Nelly.
Mama yake akajieleza mengi kwa hofu
mpaka akamuingizia hofu hiyo Lara. Akawahurumia wazazi wake. “Lakini vile vitu kama vitenge, blangeti, vipo. Ni pesa tu.
Tulitumia zote. Mambo ya...” “Usijali mama. Wakihitaji mahari yao, waambie
tutawalipa kidogo kidogo. Dada Nelly anapesa sana. Sidhani kama atajali.
Usiingiwe hofu.” Lara akajaribu kumtuliza mama yake. Huo usiku haukuwa
mzuri kwa Lara. Historia ikajirudia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Asubuhi siku ya jumamosi alibaki
amelala tu kitandani akiwaza. “Haiwezekani dada Nelly akawadai wazazi wangu.
Anaonekana alinihurumia na ni kama alisema anataka aende akamalize mambo kwa
amani.” Akajifariji Lara. “Lakini watu wanabadilika!” Akamkumbuka
Jax alivyombadilikia. Akawa mpole akisubiria kusikia kutoka kwa wazazi wake
kujua kitakachojiri.
Japokuwa wazazi wa Lara walikuwa na wasiwasi wa kudaiwa, lakini walijitahidi kuwa wema. Waliandaa chakula cha mchana kizuri na mapema ili wakwe zao wakija, wawakarimu. Hawakuwa na gari la kusema watakwenda kuwapokea uwanja wa ndege, wakabaki tu hapo nyumbani wakiwasubiria. Ilipofika saa tano na nusu, Nelly na Tino wakawa mlangoni wakigonga. Wakakaribishwa kwa ukarimu mpaka Nelly akajisikia vibaya, wasijue ule ukarimu umejawa na hofu ya kudaiwa pia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika kwenye saa 6 mchana, mtu
akagonga wanapoishi Lara na wenzake. Warda akafungua. “Nimetumwa kwa
Lara.” Wote wakatoka. “Nina mizigo yako
hapa. Nimeambiwa ukipokea, ukasaini hapa, ndio nitalipwa.” “Na nani?” Lara
akauliza, akitegemea safari hii pengine atamjua kwa hakika huyo anayemuagizia
vitu. “Mwenye duka.” Lara akashangaa.
“Wakati wewe unashangaa, acha mimi nichangamkie mlo. Tumuwezeshe Warda huko
jikoni.” Suzy akaanza kuingiza ndani mifuko hiyo ya chakula na mafuta yakupikia.
Ikabidi tu Lara aweke saini na kumshukuru huyo dereva, akafunga mlango na
kukimbilia hiyo mifuko. Alikuta mayai trei mbili, mafuta ya kupikia, sukari,
blueband, maziwa fresh na mtindi, pamoja na kuku wabichi wawili. Lara
akawaangalia wenzake.
“Vinatoka wapi jamani!?” Lara akauliza
tena. “Si ulisema kwa dada Nelly!” Sesi akajibu huku akiendelea kuangalia.
“Dada Nelly yupo safarini!” “Si yule aliyeleta alisema ametumwa na mwenye duka.
Pengine alitoa maagizo kabla hajasafiri.” “Labda.” Akajibu Lara huku
akifikiria. “Mimi naomba wakati mnawaza, tumpe huyo kuku Warda, aanze kufanya
vitu vyake.” Suzy akatoa wazo. “Ila Lara apate kwanza supu jamani! Nahisi hawa
kuku wameletwa wakienyeji makusudi ili Lara apate supu. Tusijisahau. Nafikiri
lengo la mletaji, ni kwa ajili ya Lara arudishe huo mwili.” “Sesi naye!”
“Vyakula vipo Suzy, tuwe waungwana.” “Mimi nafikiri tutengeneze tu mchemsho,
tule wote.” Lara akatoa wazo lililomfurahisha sana Suzy akampa mpaka busu.
“Hufai wewe! Si umesema unataka
kupungua?” “Sio kwa kutokula kuku, Sesi bwana! Kwanza kuku hawanenepeshi.”
Wakabishana hapo wakifurahia kuku lakini Lara tumbo joto, akifikiria wazazi
wake na ugeni walio nao huko kwao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika saa nane, Lara akaona simu ya
mama yake. Akakimbilia chumbani kwake. “Wamesema nini?
Wamewadai?” Lara akauliza kwa wasiwasi. “Mwenzangu
imekuwa kinyume! Dada yake mkarimu huyo!” “Dada Nelly!?” Lara hakuamini.
“Sana. Ametuomba radhi na pesa ametoa.” Lara
hakuamini. Zikaanza stori kati yake na mama yake. Kidogo akafarijika. Akaweza
hata kwenda kunywa supu iliyotengenezwa na Warda. Akaamini Nelly ndiye mtumaji.
Akafarijika na angalau akaona imemrudishia sifa kwa wanao mzunguka. Alijua hata
kule kuletewa matunda ofisini, angalau alijua maneno yataenea na kuona hata
kama mchumba alimkataa, basi mkwe anamjali. Akafurahia hilo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika mida ya saa mbili, wakasikia
hodi tena. Suzy akaruka. “Weza kuta mzigo mwingine.” Mpaka Lara akacheka.
Akaenda kufungua. Wakamsikia akisema, “Akhaaa! Kumbe wewe!” Akafunga mlango
bila kumruhusu mgeni kuingia ndani. “Nani!?” Wote wakamuuliza. “Hakuna mtu.
Upepo tu.” Wakasikia hodi tena. Safari hii Lara akasimama yeye ili akafungue
kwa kuwa Warda alikuwa akimsuka Sesi. “Wala usijisumbue. Utakasirika tu.” Suzy
akamuonya.
Lara akafungua. “Kabla hujanifungia
nje..” Lara akaondoka pale mlangoni kurudi sebuleni walipokuwa wamekaa
wakiangalia tv. Tino akafuata nyuma. “Nilikwambia mimi. Usifungue mlango. Ona
ulichoingiza humu ndani!” “Acha hizo Suzy! Mimi nimetumwa na mama yake Lara.”
Lara akamwangalia. “Kweli tena nimetumwa.” Akaweka msisitizo kwa Lara.
“Umetumwa nini kama sio uongo wako, wa kutafuta gia ya kuingilia hapa?” Suzy
akaendelea kumkaba Tino. Lara akabaki akimtizama. Tino akameza mate.
Akaanza. “Kwanza alitaka kujua
unaendeleaje!” “Toka Tino. Huna jipya. Lara anaongea na mama yake kila wakati.
Anajua anavyoendelea. Toka.” Suzy akamfukuza. “Subiri kwanza. Mbona haraka?”
Tino akajaribu kumtuliza Suzy. “Haya, sema.” Lara alibaki akimwangalia tu.
“Amenituma, nimsalimie sanaaaaa.” Mpaka Warda na Sesi wakacheka. “Toka Tino.”
“Lara kipenzi changu, mama anakusalimia sana. Amenituma.” “Ungetuma ujumbe sio
kuleta bichwa lako hapa.” “Si unyamaze Suzy! Hayakuhusu.” “Lara shoga yangu.
Ukimuumiza yeye ujue umeniumiza na mimi.” Lara alikuwa kimya tu.
“Nimekuletea na korosho, Lara.” Tino
akaendelea akibembeleza. “Nashukuru Tino.” Akajibu Lara taratibu tu. Tino
alifurahi mpaka akaruka. Akaenda kukaa pembeni yake. “Lione lilivyofurahi.
Ungelifukuza hilo.” “Suzy kwa wivu! Asione wenzake tunapendwa!” Akauvuta mkono
wa Lara na kuubusu. Lara akacheka. “Bwana nimekumiss! Usinifukuze, wangu! Ujue
mimi siwezi kukuumiza.” “Uliniumiza Tino. Sikutegemea kama na wewe unaweza
kunifanyia hivyo!” “Ni vile nakupenda Lara. Sikutaka mimi ndio nikupe habari za
kukuumiza.” Lara akanyamaza.
“Pole wangu.” “Nimepoa. Asante kwa
kurudi kwa wazazi.” “Wazo la dada Nelly! Mimi mwenyewe kanishangaza! Nilikuwa
siamini kama ni yeye au Mungu ameshusha mwingine.” Angalau wakaanza kucheka.
Tino akampa habari za Dodoma alikotoka kwa wazazi wake, angalau Lara
akafarijika na aibu ya kuachwa ikaanza kupungua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Zawadi za hapa na pale kwa Lara hazikukoma.
Zaidi vyakula. Matunda na juisi vikaendelea kila siku. Jumatatu mpaka ijumaa.
Na kama jumamosi hii aliletewa vyakula vingi, basi jumamosi inayofuata kuna
kuwa kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Angalau kicheko kidogo kikarudi kwa
Lara, Tino naye akajisogeza karibu zaidi. Upendo, kujali kwa hapa na pale.
“Dada Nelly amekuwa akiniletea vyakula, Tino. Natamani kumshukuru lakini sina
namba yake.” Lara alimwambia Tino jioni hiyo wakati wametoka kazini, Tino anawarudisha
nyumbani. Huwapa lifti pale anapoweza. “Naomba niwe mkweli kwako Lara.” Lara
akamtizama. “Dada Nelly hapendi mtu asiyempa yeye mwenyewe namba yake, ampigie.
Si unamjua alivyo mkorofi?” Lara akatulia.
“Na katika watu wagumu kuwaelewa hapa
duniani, ni Nelly. Haileweki muda gani anaweza akawa ametulia au amecharuka. Nelly
niliyemuona Dodoma, sijawahi kumuona tangia namfahamu. Na sitashangaa kuwa
anaweza asinitafute tena mpaka hata baada ya miezi.” Lara akatabasamu.
“Ukimfuta nyumbani?” “Anaweza
akufungulie mlango au asikufungulie, akuongeleshe nje ya mlango.” Mpaka kina
Sesi wakacheka. “Au akakwambia acha matatizo yako kwa mlinzi getini, atamwambia
asubuhi wakati akienda kazini.” “Na bado tu unaenda!?” Akauliza Suzy kwa mshangao.
“Sana tu. Tena wakati mwingine naenda na kulala kabisa.” “Sasa si anakuwa amekufukuza?”
“Kufukuzwa na dada Nelly ni jambo la kawaida. Kuitwa au kufunguliwa mlango ndio
kitu cha ajabu. Nishamzoea nafikiri na ndio maana ananipenda. Sijali
akinifukuza. Naweza nisiondoke, nikaendelea kuongea naye hapohapo. Yeye yupo sebuleni
kwake, mimi nipo nje.” Wakashangaa lakini sio Lara. Lara alimjua huyo dada,
yeye alikuwa akicheka tu.
“Siku akiamua, ananipigia simu nikanywe
naye. Mtakunywa mpaka mchoke, kisha analipia yeye. Jax anasemaga akiwa
anakunywa hivyo anakuwa na kitu kina mkera.” “Hajaolewa?” “Hataki hata kusikia.
Wala hataki mtoto.” Tino akajibu na kuongeza. “Kwanza sijui kama ana moyo wa
umama yule!” “Lakini alimlea mdogo wake mpaka amemfikisha vile! Kwa hiyo
anaweza ila labda hataki ameamua kuweka akili zake kazini tu.” Akaongeza Lara kinyonge.
“Na kweli. Naona amewekeza kazini. Na upande wa kazi, amefanikiwa sana. Ila
ninachojaribu kukushauri Lara, mwache tu.” Lara akamwangalia.
“Kama angetaka shukurani, angekufuata
au angetaka ujue. Kufanya hivyo ni kukufikishia ujumbe kuwa hataki kufuatwa.
Dada Nelly hawezi mahusiano hata ya urafiki wa kike. Hawezi hata simu za
salamu. Jax mwenyewe akimpigia kumsalimia anamuuliza anashida gani?” Wakacheka
na kuanza kusimuliana vituko vya Nelly, lakini Lara akaelewa kuwa ndio
ameambiwa amuache.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo ya Lara yakaendelea kutulia. Ile
aibu na maneno ya kuachwa vibaya yakaanza kubadilika. Habari iliyokuwa imebaki
kuwa Lara amepata secret admirer, anamtunza na kumjali. Suzy maneno
mengi akasaidia kusuta watu kwa kusambaza hiki na kile. Kutoka kurudi kutembea
na daladala, Tino akaanza kuwarudisha jioni anapoweza au kama hajatingwa na
kazi zake. Basi atawachukua wote wanne na kuwarudisha kwao ndipo apitie baa
kunywa. Asubuhi kina Lara walimwambia huwa wanawahi sana kuamka, wanapata daladala
ya mpaka Posta kiurahisi.
Maisha ya Lara yakaendelea. Akaanza
hata kutulia. Kila alipokuwa akimkumbuka Jax, aliweza kujituliza kwa hili na
lile akijiambia Jax hakukusudiwa kuwa wake. Alimtamkia wazi amemchagua Tula,
mpenzi wake wa zamani. Hilo bado lilikuwa likimuuma sana Lara. Kwamba muda wote
huo wa karibu kumaliza miaka miwili, alikuwa naye lakini mawazo yapo kwa Tula!
Ilikuwa ikimuuma sana.
Kwa sababu ni kweli kwa upande wake
Lara, yeye alitulia kabisa. Tokea ampate Jax, akili ilitulia kabisa. Hakuwa
akihitaji chochote kutoka kwa yeyote. Alimkuta Jax anakazi CRDB bank, alikuwa
na pesa ya kawaida ya kumuhonga japo kidogo. Na kwa kuwa Lara mwenyewe alikuwa
na kazi, na hakutoka kwenye familia yenye shida sana ila matatizo tu ya
kawaida, basi, akatosheka na vile alivyo Jax.
Mambo yakazidi kuwa mazuri pale Jax
alipohamia kwenye benki ya dunia. Neema ikaongezeka. Maisha yao yakawa mazuri
hata muonekano wa nje wa Lara, ulionekana mambo ni mazuri. Japokuwa Jax hakuwa
mwanaume wa ajabu sana kwa uzuri. Kijana wa kibantu tu, lakini Lara binti mzuri
wa mjini, akaridhishwa na maadili yake. Si mlevi wala macho juu. Mtulivu.
Ukimuomba chochote ndani ya uwezo wake, anasaidia. Anakula chochote
atakachopikiwa na Lara. Hajui kukosoa, si mkali, Lara akampenda sana Jax.
Alishakuwa na mwanaume mwingine kabla
ya Jax, lakini ujana ulikuwa mwingi. Hakuwa ametulia. Maisha yake ni starehe tu
na Lara, akijionyeshea ufahari kwa kummiliki Lara. Akiwa na Lara atajisifia
kujishindia mrembo wa kutoka jiji kuu. Kina Lara walikuwa wanatoa kwenye kabila
la Warangi, hukohuko Dodoma, wilaya ya Kondoa.
Alikuwa binti mzuri sana kwa
kumwangalia. Hakuwa mrefu wala mfupi. Ila katika udogo wake wa maumbile,
ungependa kumuangalia vile alivyogawanyika vizuri. Mcheshi, na maneno mengi
kama Suzy sema yeye hakujua kutukana na alikuwa na mipaka. Alijua aongee nini
na kwa nani. Si mropokaji hovyo mbele ya asiowajua. Kidogo alijaliwa soni ya
kike.
Nywele nzuri, laini halafu kama za mama
yao. Lakini wao wote watatu nywele zao zikawa nyingi kutokana na baba yao sio kama
mama you zilikuwa chache. Alizijulia hizo nywele na umbile lake! Lara
alijipenda sana tofauti na dada zake. Alipenda vitu vizuri tokea mtoto. Mama yake
alikuwa akimsimulia wakati mtoto kama akimvalisha kitu kibaya, asichopenda
yeye, alikuwa akilia sana na hataki kutoka chumbani. Basi Lara akakua akipenda
vitu vizuri tofauti na dada zake. Aliijua mitumba ya kila mahali, na huko ndiko
alikokuwa akipata mavazi yake. Ukimuuona sehemu, unaweza sema ni toto la
milionea, linaishi uzunguni, kumbe kiziwanda wa mama Chiwanga, anaishi
uswahilini tu.
Kujipenda ndio kipaumbele kwake na
kupenda kujirusha. Weekend ilikuwa lazima waende club. Zaidi siku za jumamosi
ambazo huenda kazini nusu siku na mara nyingine hawakuwa wakienda kabisa,
wanapeana zamu kufanya kazi siku hiyo ya jumamosi. Basi watatumia siku hiyo
kujitengeneza, ikifika jioni wanakwesha club mpaka karibu kunapambazuka
jumapili, ndipo wanarudi nyumbani kulala. Kasoro Warda mtoto wa swala tano.
Walikuwa wakimuacha nyumbani. Ila Lara, usingejua kama anatokea kwenye nyumba
ya baba na mama washika dini, walokole wanaoishi kwa hofu ya Mungu, na yeye
kukuzwa hivyohivyo.
Lara alipoanzana na Jax, akaacha kwenda
club. Siku hizo za weekend akawa akienda kulala nyumbani kwa Jax
aliyeonekana ametulia na anaakili za kiutuuzima kuliko mpenzi wake wa wakati huo.
Alipoona Jax anamuelekeo, akaamua aachane naye kabisa, atulie kwa Jax tu aliyeonekana
anaweza kuja kumuoa lakini akaishia kumuacha na gauni la harusi mkononi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mwezi huo nao ukaisha. Mambo
yakiendelea hivyo hivyo. Mwezi wa pili nao, zawadi za hapa na pale, bila ujumbe
wala kukutana na mletaji ambaye alidhania ni Nelly. Akawa anapokea na kula bila
shida. Akidhani labda siku hiyo ndio mwisho, kesho yake ataletewa tena. Tena
mambo yakazidi kuongezeka. Akiwa kazini akaanza kuletewa chocolate,
wakati mwingine Icecream, ilimradi tu. Ila kwake aliendelea kufurahia.
Faraja ikaongezeka.
Kabla ya mwezi huo wa pili kuisha
tangia aanze kuletewa hivyo vitu, yule muhudumu wa mgahawa aliyekuwa akileta
matunda akamuuliza anataka mchana amletee chakula gani? Akampa na Menu ya
hotelini kwao. Lara akashangaa sana. “Na chakula!?” “Nimetumwa niulize uletewe
chakula gani kwa leo. Sijui kama na kesho, ila leo.” Suzy akaruka na kuivuta
ile menu. Akaanza kuisoma yeye huku akimuuliza yule muhudumu maana ya yale
majina ya vile vyakula, huku yule muhudumu akieleza. Suzy akachagua. “Sasa sio
upunje. Ulete kingi.” Suzy akaweka msisitizo. “Wewe si upo kwenye diet
wewe? Unataka kupungua kweli wewe?” Bosi wao akamuuliza. “Naanza kesho bosi
wangu.” Akajibu Suzy usemi wake wa kila siku na kesho yake haikuwahi kufika.
Ikaenda hivyo juma la kwanza na la
pili. Chakula mara mbili kwa juma ila matunda na juisi mara tano kwa juma.
Chakula kikawa kinaletwa siku ya jumatatu na alhamisi. Walipomletea matunda
siku hiyo ya alhamisi asubuhi wakati muhudumu anataka kujua amletee chakula
gani mchana, Lara aliomba asiletewe. Akasema angependa kwenda kula palepale. Ilipofika
mchana alitoka peke yake, kwa kuwa Suzy, Warda na Sesi hawakwenda naye sababu
ya bei. Wao wakaelekea kibandani, Lara mgahawani.
Lara Mgahawani!
L |
ara
alifika hapo akamuulizia muhudumu ambaye huwa anamletea chakula. Akaenda
kuitiwa. “Mzima Lara?” “Nimekuja kula au ...” Lara akapunguza sauti.
Kulionekana na watu wa maana pale ndani. Na kila mmoja yupo na shuguli zake.
Wengine kama mazungumzo ya muhimu, wengine wakila huku wakisoma magazeti. Lara akababaika.
“Bosi tena! Wewe tafuta nafasi ukae, nitakuhudumia.” Lara akacheka kidogo kwa
kuridhika. Akaanza kutembea kwa kunyata akitafuta sehemu ya kukaa.
Akiwa anaangalia meza ya mbele akagongo
kiti kilichokuwa kimepangwa kwenye meza iliyokuwa imekalia na watu wawili. Watu
wazima tu, walionekana wapo kwenye mazungumzo yao ya maana. Wakamwangalia kwa
kushituka kidogo “Sorry!” Akanong’ona Lara huku ameshituka na uso wa kubabaika.
“Hamna shida.” Wakamjibu. Akaenda kukaa meza ya mbele yao lakini akavuta kiti badala
ya kukinyanyua, kikatoa mlio mwingine uliosumbua wateja wengine. Akawageukia
tena. “Sorry!” Wengine wakatoa tu
tabasamu la kiungwana, na wengine wakageuka kuendelea na mazungumzo yao.
Akaanza kugongagonga meza na vidole
akitumia kucha zake ndefu kama anayejituliza kwa wasiwasi kuwepo sehemu kama
ile, wakamgeukia mpaka wa pembeni yake na mbele kama anayesumbua. “Sorry!”
Akanong’ona tena. “Am trying to calm myself down.” Akaendelea kuongea
taratibu na lugha ya uzaliwa ikawa imepotea kabisa. “Na nikiwa nawasiwasi
naongea kingereza kama mlevi!” Lara akaendelea kuongea kwa sauti ya kunong’ona
akiwaangalia. Wote wakacheka na kugeuka kuendelea kula.
Akaanza kuvuta pumzi kwa nguvu, yule
muhudumu aliyekuwa akimletea chakula akaja na juisi yake. “Uwiii! Heri umekuja.
Na nafikiri uwe unaniletea tu kulekule. Hapa sijawahi kuja peke yangu.
Panaogopesha!” Yule muhudumu akaanza kucheka. “Kweli tena, mpaka nimeanza
kuzungumza kingereza!” Yule muhudumu akaendelea kucheka. “Utazoea tu. Ila
unatakiwa uwe unakuja mara kwa mara sasa. Na ukija uwe unaangalia unakopita,
usigonge meza na viti vya wateja wengine.” “Na wewe kumbe umeona!?” Wakaanza
kucheka taratibu.
“Hapa pametulia sana. Wengi wanakuja
kwa mazungumzo maalumu na watu wenye pesa zao.” “Kwa hiyo watajua mimi mgeni,
eeh?” Akacheka. “Njoo mara kwa mara, hofu itaisha na utaendelea kuongea
kingereza tu.” Lara akacheka sana. Akamtania kidogo, akaagiza chakula, yule
muhudumu akaondoka.
Akaanza kuangaza macho pale. Akajikuta
ni yeye peke yake ndio mshangaaji. Kila mtu ana lake. Waliokuwa wamekaa peke
yao walikuwa kama hawajainamia simu zao, basi wanasoma magazeti. Akavuta pumzi
kwa nguvu, akatoa simu yake na yeye angalau aperuzi, aonekane wa maana.
Jax kwa Lara.
C |
hakula
kikaletwa akaanza kula taratibu, mawazo yakamtoa pale akaanza kufikiria hili na
lile. Akatulia na kupotelea mawazoni. Mara akamuona Jax amevuta kiti mbele yake,
akakaa. Akashituka sana karibu aangushe uma. “Jax!” “Mzima Lara?” Lara akabaki
akimwangalia. Wakatulia kwa muda Lara akishangaa. “Unaendeleaje?” Jax akauliza
tena. Lara kimya. “Lara?” “Sikutegemea...” Akakumbuka anaongea na Jax,
mfanyakazi wa benki ya dunia. Kuwepo pale sio kitu cha ajabu. Akatulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hatimaye
wawili hao wamekutana tena. Jax akiwa amemuacha Lara kikatili sana tena akiwa
mjamzito, wakiwa wameishi vizuri bila tatizo, sasa hivi amerudi mezani kwa Lara.
Baada ya mazungomzo yake ya mwisho kwa Lara akiwa kitandani hajiwezi amepoteza mtoto
na mshituko wa kuachwa vibaya, hatimaye wamekutana tena. Sasa, sasahivi Jax ana
kipi tena chakuzungumza?
Usikose muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment