![]() |
|
Gafla hofu ya kuambukizwa magonjwa ikamuingia
kwa kasi. Ni kweli alilala na Tula bila maswali mengi wala kinga. Akajikuna
kichwa. Muhudumu akamfuta kumuuliza kama anataka kitu kingine. “Chakula?”
“Naomba kulipia vinywaji tu.” Hamu ya kula ilishamuisha. Akalipa na kuhamia
kwenye gari ambako hakutaka kusumbuliwa. Hakutoa hata gari. Akabaki akifikiria
palepale ndani ya gari.
Baada ya kama lisaa Tula akampigia. “Upo wapi Jax?” “Nilikuwa na dada Nelly ndio tumeachana muda
sio mrefu, nataka kurudi nyumbani. Vipi?” “Nimekumiss tu. Naona muda unakwenda
hurudi!” Akajilalamisha Tula kwa upendo. “Nitakuwepo
hapo muda si mrefu.” “Pitia basi kuku wa Namanga.” “Nilifikiri utakuwa ulinunua
tayari!” “Sikufanikiwa.” Jax akashangaa. “Tula!
Uliniambia umetoka kwenda Namanga kufuata kuku!” “Nilifika hapo nikaishia
kununua vitu vingine, nikasahau chakula.” Jax akanyamaza.
“Kama unaona shida, basi
bwana.” “Sasa basi halafu tule nini!?” “Mbona hivyo Jax! Maswali gani hayo?”
“Nimeuliza tu.” “Si ndio nimekwambia upitie kuku hapo!” Jax akaona amalize. “Nakuja.” “Unakuja vipi sasa?” “Nitaleta chakula.” Jax
akakata simu.
Walikuwa na msichana wa kazi anayekuja
kila siku asubuhi kusaidia kazi zile anazopewa na Tula, na kuondoka jioni,
kasoro siku za jumapili tu kama kwa dada yake. Nelly hakuwa akitaka msichana wa
kazi wa kulala nyumbani kwake. Hiyo ni tokea zamani anamlea huyo Jax. Jax
amekua akiona nyumbani kwao anayeruhusiwa kulala ni yeye na dada yake tu mpaka
alipoongezeka Tino aliyelazimishia undugu kwa nguvu. Kwa hiyo hata huyo
msichana anayewasaidia kazi yeye na Tula, alimpata kutoka kwa msichana wa kazi
za ndani wa Nelly. Ila hakuwa akijua kupika vizuri. Kwa hiyo Tula alikuwa
akipika mwenyewe au wananunua chakula chao.
Kwa Tula.
Jax alinunua chakula na kurudi
nyumbani. Tula akampokea. “Pole na kazi.” “Asante. Nimechoka sana leo. Nahisi
nitawahi kulala.” “Kwema?” Tula akauliza vizuri tu. “Kwema, ni uchovu tu.” Tula
akabaki akimtizama. “Vipi?” “Mbona kama kuna jambo halafu unashindwa
kuniambia?” “Tula! Nimekwambia nimechoka nataka kulala, basi.” “Tokea lini
tunafichana mambo!? Kwani dada Nelly amekwambia nini?” Jax akamtizama na
kuelekea chumbani.
Tula akamfuata. “Mbona sikuelewi Jax!”
“Labda uniulize. Maana mimi sikuelewi wewe unataka kunisikia nikikwambia nini
au ulitaka nikwambie nini!? Kama ni mazungumza na Nelly, ni yakunihusu mimi na
yeye. Mambo ya kifamilia.” Tula akashangaa sana. “Kwa hiyo gafla mimi nimekuwa
sio familia?” “Najua unaelewa ninachokwambia, Tula. Nisichokwambia ujue
hakikuhusu. Kwa kusema hivyo, kama huna swali, naomba nikaoge, nilale.”
“Makubwa! Na chakula?” “Sitakula. Asante. Nimekuletea na chips. Wewe kula tu.”
Jax akatoa nguo, na kuelekea kuoga.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hofu ya kuwa ameshaathirika ilimuingia
sawia. Kufa mapema hakutaka. Ndio kazi ilikuwa imechanganya. Pesa inaingia kwa
dola! Mafanikio ndio yananyesha kama mvua! Aje aanze kuugua! Akajifariji kuwa
zipo dawa kama atakuwa ameathirika. Miezi miwili ilishakuwa imepita tokea
aanzane na Tula.
“Lara!” Akamkumbuka kwa
kuumia sana. Hakutegemea kama Lara angekuja kuumia kwa ajili yake. “Kweli
sikufikiria!” Akawaza wakati akiendelea kuoga. Akaanza kukumbuka mabadiliko
aliyokuwa nayo Lara. Kulala sana na kushindwa hata kupika. “Sikuwa hata na
wazo la ujauzito!” Akajilaumu Jax huku akipitisha mikono yote miwili
kichwani akiwa amesimama katikati ya bomba. Akabaki ameinama maji yakimmwagikia.
“Kwa nini Lara hakuniambia?” Akalaumu mawazoni. Akataka kukasirika.
Kumbukumbu zikamrudia alipokuwa hapokei simu za Lara na mwishoe kumfungia
kabisa simu zake.
Akakumbuka sura ya Lara akilia akiwa
amejilaza kitandani kwake wakati akimtamkia anamuacha sababu ya Tula. “Tula
aliharib..” Akasita kumtupia lawama Tula. Akanyamaza akikumbuka maneno ya
dada yake akimwambia yupo kama baba yake. Alimuua mama yake. Jax akaanza
kujichukia. Na yeye akajiuliza swali alilomuuliza Nelly. “Niliwezaje!? Nini
kilinipata!?” Akaanza kujishangaa na kuumia zaidi kuua mtoto wake! Japokuwa
hakuwa akijua, lakini kilimuuma sana. Akabaki amesimama majini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mbona hutoki huko bafuni?” Akasikia
sauti ya Tula. “We Jax?” “Ni nini leo Tula!? Mpaka bafuni?” “Hivi ujue wewe Jax
mimi nakufahamu kwa kukuangalia tu? Huwezi kujificha kwangu.” Jax akafikiria. “Na
hilo ndilo anguko langu.” Akawaza Jax. Akafikiria jinsi ambavyo hawezi
kusema hapana kwa Tula. Alikuwa mbishi na msimamo mkali kwa kila mtu, lakini si
kwa Tula. Ikifika kwa Tula ni kama hakuwa akifikiria tena.
Alitoka bafuni, akamkuta Tula amejilaza
kitandani, hana nguo hata moja. “Nimechoka Tula. Naomba nilale.” “Wewe usifanye
chochote, jilaze tu, niachie kazi yote mimi.” “Hapana. Sio leo.” Tula
akashangaa sana. “Kuna nini Jax!? Dada Nelly mgonjwa?” Jax akajikausha na kuvaa
boxer yake akapanda kitandani. Tula akaruka kama mshale. “Usiniambie kama
umefukuzwa kazi!” “Unaongea nini wewe? Nani afukuzwe kazi.” Akamuona anajishika
moyo.
“Afadhali. Maana nilikaribia kupata heart
attack! Mjini tukiwa wote hatuna kazi! Hapatakalika.” “Nikikosa mimi si
wewe utapata kazi? Hakuna chakupoteza.” “Kipo sana. Mimi siwezi kupata kazi
kama yako Jax. Naomba tusiombee mabaya yakupate.” “Kwani mimi nilianzia hapa!?
Si unaanzia chini unapanda taratibu!” “Na utuuzima huu!” Tula akashangaa sana.
“Sisi tunakuwa watu wakuanza kila siku! Tokea chuoni mpaka leo, sisi tuwe
tunaanza tu! Kwani tumelaaniwa!?” Jax akaona anyamaze. Akafunga macho kabisa.
I |
likuwa
muda wa mchana Lara yupo ofisi za nyuma akifanya kazi. Kiongozi wao ambaye
anakaa mbele na kina Sesi, Suzy na wengineo, akamfuata. “Unamgeni.” Lara
akanyanyua uso na kubaki akimtizama. “Ni wewe Lara.” Akatoka. Lara akafikiria
kidogo, na kuamua kwenda tu. Hakuamini alipomkuta Nelly pale. Akashindwa hata
kumsalimia. Akabaki ameduaa. “Hujambo Lara?” Ikabidi amuanze yeye. “Shikamoo.”
Lara akasalimia taratibu na wasiwasi mwingi usoni. “Marahaba. Nilikuja
kukusalimia tu. Hamna jambo baya. Tunaweza kuzungumza hapo nje?” Akauliza
kiungwana kama siye Nelly mkorofi. Lara akaangalia kulia na kushoto, akarudisha
macho kwa Nelly. “Sitakuchukulia muda mrefu. Hata mimi nipo kazini.” “Tutoke
hapo nje.” Lara akajibu na kuongoza njia.
Alisogea pembeni kabisa, ili wasisimame
mlangoni. “Pole kwa matatizo.” Lara akabaki asijue ni yepi. “Namaanisha
matatizo yote.” Akainama. “Unakula vizuri?” Nelly akamuuliza kwa upendo. “Nakula.” Lara akajibu huku akifuta machozi. “Kazana
kula. Huo mwili umeisha kabisa!” “Najitahidi.”
Akajibu Lara, asiamini kama anazungumza na Nelly. Nelly mbabe ambaye hajui
kuuma maneno. Hashindwi kukwambia waziwazi kuwa hakupendi na kukufukuza kwake
kwa kukuambia ondoka. ‘Sitaki kuiona sura yako’.
“Nimekuletea kitu cha kula. Twende
kwenye gari yangu.” Akaongoza njia, Lara asiamini. Wakafika kwenye gari yake.
“Unafikiri ni sawa nikirudi Dodoma angalau kuzungumza na wazazi?” Lara
akashangaa sana. “Kwa nini dada Nelly? Itasaidia nini?” “Wazazi wako
walitupokea vizuri sana. Kila wakati tulipokwenda, niliwaona jinsi walivyokuwa
waungwana na wakarimu kwetu. Sitaki wote tuonekane ni wahuni tu. Tulianza kwa
heshima, tunamaliza kihuni tu!” Lara akainama akifikiria.
Mwishoe akamwangalia na kumkuta
akimtizama. “Sijui dada yangu! Ila sioni sababu ya wewe kupoteza tena muda wako
na pesa kurudi mpaka kule tena! Sioni umuhimu.” “Japokuwa hata mimi sijui
itakuaje nikifika huko, lakini acha tu niende. Angalau wasituone wote hatuna
maana.” “Japokuwa hatukuzungumzia chochote, lakini
nimeona mama amechukulia...” Lara akasita. Akajifuta machozi. “Pole
sana.” “Naona wapo tu sawa.” “Mimi ni mtu
mzima. Sidhani kama ni sawa kuacha mambo barabarani. Maadamu tulianzia
nyumbani, naona nitarudi tu nyumbani.” Akamtolea mfuko wa chakula.
“Juu ni matunda, chini ni chakula.”
Lara akapokea. “Asante sana.” “Kazana kula. Namaanisha weka juhudi za makusudi kwenye
kula. Umenisikia Lara?” Lara akanyamaza. “Usijitese au kujiadhibu sababu ya
upuuzi wa Jax. Hukuchagua litokee lililotekea. Hakuna aibu. Aibu ipo kwake.
Yeye ndio anatakiwa kuona aibu na kujutia kuchukua maamuzi ya kijinga. Ni kama
mwehu asiyejua ni nini anataka!” Lara akamshangaa sana Nelly.
“Yaani wewe unatakiwa kutembea mabega
juu, kichwa mbele na kutizama watu usoni. Acha kulia kama uliyedhihakiwa.
Umefanya kwa sehemu yako. Umethibitishia uma au jamii kuwa umekuwa mkubwa.
Unaweza kutulia kama mwanamke wa kawaida na kutunza familia. Lakini umepata
mwanaume mpumbavu aliyeshindwa kuingia kwenye agano. Yeye ndio mjinga.
Aliyeshindwa. Acha kutembea kinyonge.” Lara akainama. “Umesikia Lara?” Lara
akatingisha kichwa kukubali.
“Nitafurahi nikija kukuona wakati mwingine, nikukute
umeongezeka japo kidogo na hiyo sura imepata ujasiri.” “Nilipoteza
mtoto wangu, dada. Sijui kwa nini! Japokuwa hakuwa hata ameanza kucheza huko
tumboni, lakini inaniuma kupita kiasi! Nashindwa kusahau. Nashindwa kupuuzia.
Najilaumu labda siku ile usiku nisingetoka hospitalini, ningemsikiliza yule
nesi na yule daktari, pengine nisingempoteza mtoto wangu! Najuta na kujilaumu
sana dada Nelly.” Lara akazidi kulia.
“Nalala masaa machache. Usiku
nakesha nikijilaumu kwa mengi!” Nelly akaumia sana. “Pole Lara. Pole sana.” Akamshika
begani. “Wala usipuuzie. Ni mtoto wako. Na hakuna njia nyingine ya kukufariji,
lakini kwa ulivyo niambia, naamini ulimpenda mtoto wako, ilikulazimu tu kutoka
hospitalini. Si ndio?” “Simu iliisha chaji. Nikajua
Tino atanipigia kama alivyoniahidi, halafu anikose. Nilimtuma kwako angalau
kukuulizia kulikoni. Nilikuwa na wakati mgumu dada! Sijawahi kupishana hata
neno na mwenzangu. Sasa kuja kuachwa bila kosa! Tena kwa ajili ya mwanamke
mwingine! Ilinidhoofisha sana. Sikujua kama muda wote nipo naye, kumbe alikuwa
na mwanamke mwingine!” Lara akazidi kulalamika taratibu kwa Nelly na
kujisahau kama ni yule Nelly wifie.
“Tula ana nguvu sana. Ana jinsi yake
yakuingia kwenye kichwa cha Jax, nakumfanya ashindwe kufikiria chochote na
yeyote. Anaishia kuwa mbinafsi. Na usifikiri alirudi muda mrefu! Ni kipindi
baada ya sendoff yako. Hapo katikati tu. Jax alikusudia kukuoa. Kilichoendelea
alipomtafuta Jax, ni wao wawili wanajua.”
“Na nimefurahi kwa kuwa mliishia pazuri
na Jax. Hapakuwa na shida. Na mimi najua ulikuwa ukimuongoza Jax vizuri. Hata kama
sikuwahi kukwambia, ila najua ulikuwa ukimuongoza vizuri. Ulimbadilisha, akawa
kijana mzuri. Naomba katika hilo chukulia upande wa kujipongeza kuwa unauwezo
mkubwa sana ndani yako. Kuwa unaweza kupenda na kuendesha familia yako vizuri.
Ni vile tu uliangukia kwa kichwa maji. Lakini naamini Mungu atakupa mwanaume
atakayeweza kupokea huo upendo, na kuuenzi.” Siku hiyo Lara akashangazwa sana
na Nelly. Hakika hakutegemea.
Aliona upande mwingine wa Nelly ambao
haukuwahi kuonekana na yeyote yule hapa duniani. “Jipe muda Lara. Utabeba
watoto mpaka utafute kuwazuia.” Lara akacheka kidogo. “Wala usikate tamaa. Na
hivyo unao moyo wa umama! Mungu hatakuacha. Atakulipa yote uliyopoteza na
zaidi. Kaa mkao wa kusubiri.” “Nashukuru dada yangu. Nimefurahi tumeweza
kuongea kidogo.” Nelly akacheka.
“Kweli watu wanabadilika! Mimi mwenyewe
siamini kama ni mimi!” Lara akacheka na kumwangalia kwa aibu akimuogopa.
“Unafikiri sijijui? Najijua sana, ila siwezi kujisaidia. Kuna maisha
nilipitishwa nilipokuwa mdogo mpaka sasa hivi, sijui kuamini mtu. Lakini wewe
nilikupenda.” Lara akashangaa sana mpaka Nelly akaona.
“Kwani Tino hajakwambia?” “Tino nilimfukuza
dada.” “Ameniambia. Lakini Lara, naomba msamehe tu. Ungemuhurumia kama
ungemuona siku alipokuja kumuulizia mwenzie na kumwambia ukweli. Tino alilia.
Alishindwa akwambie nini ila kumfuata Jax ofisini kwake, na kumtaka aje
azungumze na wewe. Ni vile alichelewa tu. Lakini alimtoa Jax kwenye kikao na
kumtaka aje azungumze na wewe. Na mpaka sasa hawazungumzi. Tino anakupenda
sana, Lara. Hawezi kukuumiza hata kidogo.” Lara akainama.
“Sipo hapa kwamba amenituma! Mimi sio
wakutumwa. Na wala hakuna kati yao anayejua kama nipo hapa na wewe. Kwanza hata
ukiwaambia hawataamini.” Lara akacheka. Alimjua Nelly. “Naomba msamehe Tino.
Alikuwa kwenye mshituko, hakujua ni jinsi gani ya kusaidia. Na ninauhakika kama
angejua kuto kukupigia simu usiku ule kungeleta madhara makubwa hivyo, nina
uhakika Tino asingekupigia tu simu, angekuja kabisa awe na wewe hospitalini.”
Lara akainama na kujifuta machozi.
“Wote wawili wale ni wadogo zangu. Tino
amejilazimishia mpaka imenibidi tu kukumkubali.” Lara akacheka huku akijifuta
machozi. Nelly akatingisha kichwa. “Yaani Tino!” Wakacheka. “Lakini ujue Tino
anakupenda, na asingependa kukuumiza hata kidogo. Kwanza hapendi kumuumiza
yeyote. Ndio moyo wake ulivyo, hapendi kumuumiza mtu. Katika kipindi hiki,
unamuhitaji sana kwenye maisha yako, usimfukuze. Anajutia sana.” Lara
akanyamaza.
“Sasa mimi acha niondoke kabla
sijaongea yatakayonifanya nijute baadaye.” Lara akacheka. “Asante kwa chakula,
kuja na kuzungumza na mimi.” “Karibu. Jumamosi nitamlazimisha Tino anisindikize
Dodoma kwa wazazi, nikaombe radhi.” Lara akainama. “Nitashukuru.” Akashangaa Nelly
anambusu kichwani. Lara akamwangalia. “Nilikwambia heri niondoke kabla
sijafanya mambo ya ajabu. Unaona sasa?” Wote wakacheka, Nelly akapanda kwenye
gari yake, akaondoka.
Ilimfariji sana Lara. Ilikuwa faraja ya
namna yake. Baada ya zaidi ya siku 60 za machungu, hofu, na kunyongea, angalau
amepata faraja. Na faraja yenyewe kutoka kwa Nelly! Na busu! Lara akacheka
wakati anaingia ofisini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wenzake waliridhika alipoingia akiwa
anacheka. Wakamkimbilia jikoni. “Watoto wambea nyinyi!” Mdada mwIngine wa
kitengo kingine aliwaambia alipowaona kina Sesi wanamkimbilia Lara jikoni.
“Tuambie kila kitu.” “Ameniletea hiki chakula na kuzungumza na mimi.” Lara
akawasimulia kila kitu.
Jax.
J |
ax
aliamka asubuhi na kukimbilia hospitalini wala si kazini. Kitu cha kwanza
alitaka kuangalia afya yake. Akatolewa damu na kubaki ameinama akifikiria. Nini
chakufanya kama akikutwa ameathirika ndio jambo lililokuwa likiendelea kichwani
mwake. Akajilaumu kujiua akiwa mdogo. “Ni kwa nini nimeshindwa kufikiria!?”
Akajiuliza Jax. Akafikiria shida zote alizopata Nelly mpaka kumfikisha hapo.
Akakumbuka maneno machungu ya dada yake usiku uliopita. “Siwezi kuwa kama baba. Kama nikigundulika sija..” Akaendelea kupanga mambo yake na kupotelea
mawazoni.
Akasikia jina lake likiitwa kwa ajili
yakupewa majibu yake. Akaambiwa kila kitu kipo sawa. Hana maambukizi yeyote
yale ya vijidudu vya Ukimwi na hana ugonjwa wowote ule wazinaa. Hilo
likamfurahisha sana Jax. Akiwa hapo hapo hospitalini akamtumia ujumbe Tino. ‘Tafadhali Tino, naomba tuonane kwa chakula cha mchana ndugu
yangu. Najua tumeachana pabaya.’ Hapo hapo Tino akampigia. “Wewe ni mshenzi sana Jax. Unapoanza jambo lako unataka
niwepo, ukifika mwisho huniambii. Sasa, sasahivi unataka baraka zangu kwa Tula,
mwanamke aliyekwenda kujaribu maisha Norway, yakamshinda. Akaenda Uk. Amekaa
Birmingham huko, wamemchezea mpaka wamechoka. Ameshindwa kufanya kazi, akawa
hana hata pakuishi, analala kwa kila mwanaume mpaka watanzania wenzake huko wakamkopesha
nauli kurudi nchini. Akawa anamangamanga tu hapa mtaani ndipo akapata habari kuwa
unafanya kazi world benki.” Moyo wa Jax ukapasuka na kuumia sana.
Asijue mjini habari za yeyote, kokote
zinaweza kupatikana. Ni yeye tu hakuwa akifahamu habari za Tula huyu aliyerudi,
asijue kuvunja kwake ndoa na Lara, kukampa Tula umaarufu, watu wakaanza
kuzisaka habari za huyo mwanamke aliyemudu kuvunja harusi iliyokuwa imebakiza
siku chache. Walizisaka na kuzipata habari zote za Tula, kutokea siku anaondoka
nchini mpaka amemuita Jax hotelini.
“Amekuvulia tu chupi, akili yote imekuruka! Unamuacha
mwanamke mzuri kwa ajili ya mal..” Tino akasita. “Wewe ni mpuuzi Jax. Achana na mimi. Umeniponza kwa mengi sana. Nimepoteza
muda wangu nafanya vikao vya harusi ambayo hata wewe mwenyewe huithamini!”
Tino akaendelea, Jax kimya akimjua Tino rafiki yake. “Umenifanya
nimwage damu ya kiumbe kisicho na hatia kwa tamaa zako za kipuuzi tu! Lara
amenifukuza, hataki kuniona kwa ajili yako wewe! Mwenzangu unafaidi mapenzi ya
mwanamke wako, mimi ndio nabaki wakulaumiwa!” Tino akaendelea akijua Jax
anamsikiliza.
“Washikaji wote wananiona
mimi mpuuzi. Mbambaishaji. Silali vizuri kwa sababu yako, halafu wewe unalala
na mwanamke wako bila shida! Acha kunibabaisha.” Tino akakata simu. Jax akampigia tena. “Ni
nini Jax?” “Naomba tukutane kwa chakula cha mchana.” “Safari hii unataka
kunitumia kwa ajili ya harusi yako na Tula?” “Tino! Saa saba, pale kwenye mbuzi
choma. Tafadhali.” Tino akakata. Lakini Jax alimjua. Akajua ndio
amekubali. Akaondoka hapo kwenda kazini.
Jax na
Tino.
Ilipofika mida ya saa saba kasoro
akatoka kwenda sehemu waliyokubaliana na Tino. Alipokaa tu, akamuona na Tino
naye anakuja. Tino akamwangalia kama ampige kofi. “Unamuoa lini? Ila huyo naona
ugaramie mwenyewe. Sisi tuje tu kukuona unavyojifunga kitanzi shingoni.” “Kaa
basi Tino!” “Unataka nini?” “Tutazungumzaje ukiwa umesimama?” Tino akakaa.
“Unasemaje?” “Naomba unisamehe.” Tino
akabaki akimtizama kama haamini. “Kwa yote niliyosababisha upitie, fedheha
ulizonibebea wakati wote mpaka sasa, nisamehe na ninakushukuru.” Tino akabaki
amemkodolea macho.
Jax akaendelea. “Lara anaendeleaje?”
“Wewe unafikiri atakuwa anaendeleaje?” “Acha nikwambie ukweli Tino. Ukweli
kutoka moyoni.” Tino akajisogeza nyuma. “Wewe unajua urembo wa Lara. Unajua
tabia yake. Nilipolala tu na Tula, nakushindwa kujizuia, nikarudia tena na tena
bila hukumu, nikaumia sana kwa upande wa Lara. Nikajiambia kama nitamuoa yule
binti, inamaana tabia yakuiba nje na Tula, itaendelea wakati yeye amekuwa
mwaminifu kwangu.” Jax akaendelea.
“Nilishindwa jinsi ya kujirudi tena kwa
Lara. Ningemwambia nini! Nikajua ataingia tu aibu ya muda, lakini baada ya muda
mfupi tu, atakuja kupata mwanaume mwingine atakayeweza kumfanya awe na furaha.”
“Katika hizo akili zako dhaifu na za kibinafsi, ulishawahi kufikiria kama yule
binti alikupenda kwa dhati?” “Sio kwa kiasi hicho Tino. Kumbuka historia yangu
na wanawake. Tula aliniacha kirahisi tu akahamia kwa mwanaume..” “Sio mwanaume.
Kwa wanaume wengine.” Tino akamkata.
“Kwa hiyo nikajua haitakuwa shida hata
kidogo kwa Lara. Tena ukizingatia uzuri alio nao, sikujua kama Lara anaweza
kuumia kwa kiasi hicho.” Tino akamtizama, na kumuita muhudumu. “Sasa umenisamehe?”
“Inategemea na neno linalofuata kuanzia sasa. Maana mimi nakujua Jax.” “Lara
anaendeleaje?” “Hilo swali linakaribia kuniudhi Jax!” Jax akatulia.
“Umekwenda kumuona siku za karibuni?”
“Ni nini huelewi? Nimekwambia amenifukuza. Na ni wewe Jax ndiye uliyeniponza.”
“Nataka kujua ukweli juu ya gari nililokuwa nimempa siku niliyomchumbia.” Tino
akamtizama. “Tino?” “Wewe si unaishi na Tula?” Tino akauliza kwa hasira.
“Nataka kusikia kutoka kwako kwanza kabla ya Tula.” “Kwamba sasa hivi unaniamini
mimi kuliko Tula!?” “Tino! Gari nililompa Lara?” Jax alikuwa ametulia tu.
Muhudumu akaleta kinywaji cha Tino, Jax
hakutaka kitu. “Ukalete na mbuzi pamoja na ndizi choma. Na mimi leo niwe kama
Tula. Tule pesa ya benki ya dunia.” Tino akaongea kwa kumkashifu Jax. Lakini
Jax akabaki ametulia tu. Muhudumu akaondoka.
“Gari, Tino?” “Alimpa mwanamke wako
pamoja na pete ya uchumba.” “Kwa nini?” “Jax unaniudhi wewe ujue! Unaharibu
zaidi!” Tino akawa kama anamtahadharisha. “Nataka kujua kama Tula alimfuata
tena na kumdai au ilikuaje?” “Hebu subiri kwanza Jax. Wewe unataka nini?
Itasaidia nini wakati umemtamkia wazi yule binti kuwa humtaki, unamtaka Tula.
Sasa unataka nini tena?” Jax akanyamaza kwa muda. Tino akaendelea kunywa.
“Tino?” Jax akauliza tena. “Nisikilize
Jax. Lara alikuwa mjamzito. Usiku ambao alinipigia mimi simu ili niende kwa Nelly
nikaulize upo wapi au nini kinaendelea, alikuwa kumbe ni mgonjwa. Alinipigia
simu akiwa analia. Akaniambia imebidi kusimamisha gari njiani, ameshindwa
kuendesha. Ikabidi nimfuate. Nimtulize na kumuahidi nitakwenda kuzungumza na Nelly.
Lakini nilimtuliza kwa uhakika kabisa kuwa asiwe na wasiwasi, wewe ni
mwaminifu, huwezi kumgeuka.” Tino akaguna.
“Kumbe mshenzi wewe, umemdanganya
ukiniweka mimi kwenye uongo wako, halafu usiniambie. Aliniuliza kimtego tu
akitaka kujua kwa hakika kama tulikwenda wote Kisarawe, mimi nikawa sijui.
Nikamwambia jumapili siku nzima nilikuwa kwa mama. Akajua umemdanganya,
asiniambie. Akanyamaza tu kwa kuwa tulikuwa na wenzake na wameenda kula. Kumbe
kuanzia hapo alipojua haukuwa na mimi Kisarawe, pressure ikaanza kupanda. Mimi
nazungumza naye usiku ule, namtia moyo kila kitu kipo sawa, kumbe presure ipo
juu sana. Tumeachana pale, mimi nikaenda kwa dada Nelly, yeye akarudi nyumbani.
Anasema akajisikia hali inazidi kuwa mbaya. Akahofia mtoto, ikabidi kukimbilia
hospitalini usiku wa saa 6 sijui saa 7! Wakakuta pressure juu sana. Wakamwambia
lazima alale, wamuwekee dripu ili pressure ishuke.” Tino akaendelea.
“Anasema wasiwasi ukamzidia. Simu
imemuishia chaji akiwa hospitalini. Akaogopa nisije nikampigia,
nikamkosa. Kumbe na mimi niliposikia umejificha mjinga wewe na mwanamke wako,
nilifunga simu mapema. Nikiwa nimepanga nimuache usiku ule angalau alale mimi
nisiwe ndio nimempa habari mbaya, mpaka aje asikie kutoka kwako wewe mwenyewe
kidume cha mbegu.” Jax kimya akisikiliza.
“Kumbe Lara anahangaika usiku huo
halali mpaka kutoroka hospitalini ili kuhakikisha simu yake haizimi, ipo hewani
kupata mawasiliano. Akisubiri labda mmoja wetu atamtafuta kumwambia ukweli wa
kile kinachoendelea! Mimi nikaamkia ofisini kwako kukuomba uzungumze naye,
kumbe na mwanamke wako naye kaamkia ofisini kwa Lara, aliyekwenda kazini
pressure ipo juu, ametoroka hospitalini bila matibabu kukamilika.” Tino
akaendelea.
“Mbweha wako akaanza kumpandishia Lara
mbele za watu na kujigamba umemchagua yeye. Na anataka gari uliyompa wakati
unamchumbia. Ile gari ni yake sasa hivi kwakuwa lengo la kupewa lile gari
limekufa, yeye mwenye mme amerudi, anataka kupewa haki zake. Nasikia bosi wa
Lara ndiye aliyemtoa yule mpuuzi mwenzio pale mbele ya Lara na wateja wengine,
tena akivutwa nje na askari kwa kuwa alikuwa akiendelea kumtapikia Lara mbele
ya wateja. Na unapajua pale jinsi panavyojaa. Lara akatolewa pale, pressure
ikalipuka zaidi. Akiwa anarudishwa nyumbani kwenye kile kigari chenu
kinachowatoa mate wewe na yule mwanamke wako, mimba ikatoka. Akaanza kutokwa
damu kama nini sijui!”
“Kufupisha habari kwa kuwa hayakuhusu,
baada ya yote, Lara aliporudi mjini, akawa amefikiria na kushindwa tena kupanda
lile gari. Kwanza anasema ndipo alipofia mtoto wake. Mimba ilitoka ndani ya
lile gari, na akaona alichoongea yule anayeshika akili zako, anayekufundisha
kila kitu chakufanya tokea chuo, ni sahihi.” Macho ya Jax yalikuwa mekundu na
mishipa yote ya kichwa ilimsimama.
“Akamtafuta mwanamke wako. Nasikia
akamuomba msamaha na kumwambia yupo sahihi kwa yote aliyomwambia siku ile
alipomfuata kazini kwake, ila alishindwa kujibu kwa kuwa alikuwa kwenye mshituko.
Anaomba wakutane amkabidhi vitu alivyomdai. Yule mwanamke wako akaenda kukutana
na Lara. Akampa gari, kadi ya gari, funguo na pete ya uchumba. Tula akaondoka
na kumuacha Lara kwa amani bila matusi wala swali.” Tino akaendelea.
“Sasa najua kwa kuwa yeye ndiye
anayekutawala. Anachagua nini akwambie na nini asikwambie, pengine kwa kuwa
anakujua akili yako ni ndogo. Akaona hili asikwambie. Huna akili ya kulibeba na
wala huna uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Ashakupima, akaona wewe ni mjinga.
Akili yako ndogo. Unasubiri akwambie nini ili ufanye. Akikwambia nisubiri miaka
minne mpaka nikalalwe na wanaume wengine ndio na wewe akuletee makombo, huna
shida. Sasa nafikiri ameona mambo mengine yeye kama kichwa cha familia yenu ya
kipuuzi, ayafanye tu bila kukushirikisha. Kwa hiyo subiri mambo ya saizi yako
atakayoona yanakufaa, atakwambia.”
Chakula cha Tino kikaletwa. “Sasa mimi
ninaharaka. Nikimaliza tu kula nataka nirudi kibaruani. Sasa kabla tajiri yangu
na yeye hajaondoka naomba mletee bili kabisa alipe kabla mwanamke wake hajamuita.
Maana akiitwa huyu na mwanamke wake, huwa akili inamruka. Anaweza akakimbia
hapa bila kuaga, halafu wewe ndio ukaingia hasara. Sasa changamka ulipwe kabla
mwanamke wake hajamuita. Ukimuona anaondoka, ujue mimi sikulipi. Kwa hiyo
changamka.” Muhudumu akaondoka kwa haraka.
Tino akainamia chakula chake akaanza
kula bila hata kumtizama Jax. Jax akabaki kimya tu. “Pesa ya benki ya dunia
tamu jamani! Kweli Tula anafaidi.” Akang’ata nyama ya mbuzi, akasukumia na
soda. “Aaaaah!” Tino akamkera zaidi Jax huku akiendelea kula.
“Sasa Lara anatumia usafiri gani kwenda
kazini?” Jax akauliza. Tino akamtizama Jax kama ammeze. Akamuita muhudumu
aliyekuwa akipita. “Naomba nifungie hiki chakula changu, nikale mbele ya
safari.” Tino akasimama. “Hatujamaliza Tino!” “Kamuulize mwanamke wako hayo
maswali ya kijinga. Acha kunifanya mimi mpuuzi kwa kuwa unalipia chakula
ninachokula.” “Nataka kujua Tino.” “Halafu!?” Tino akamuuliza kwa kumsuta.
Kimya.
“Niambie Jax. Ukishajua, utafanyaje?”
“Basi tuache hilo. Naomba ukae tuzungumze.” “Changamsha mdomo maana chakula
changu kikija tu, mimi naondoka. Sikuoni kama una jipya.” Tino hakukaa. “Kwa
kuwa nimelipa karibu watu wote waliochangia harusi, naomba pesa iliyobaki yote
umpe Lara.” “Kama kweli unamaanisha hilo, mwambie Tula anipigie yeye simu,
anipe hayo maelekezo. Nakuhakikishia Jax, Tula akinipigia simu na kunipa hayo
maelekezo, japokuwa Lara amenifukuza, nitafanya juu chini hiyo pesa imfikie.
Lakini sio wewe. Wewe hujui ni kitu gani unaongea. Naweza nikamfikishia hizo
pesa Lara, kumbe mwanamke wako hajakuruhusu. Halafu akazua jingine. Akaenda
kumfuata Lara tena na kumdai.” Chakula chake kikaletwa kikiwa kimefungwa.
“Japokuwa wewe hutaki kufikiria, lakini
nakushauri kabla hujajidhalilisha zaidi kwa unachotaka kufanya baada ya yote
haya, ukaonekana mwehu, hujui unachokitaka, jaribu kufikiria. Na ukumbuke
nafasi yako kwenye mahusiano uliyo nayo sasa hivi. Hakikisha una muomba ruhusa na
ushauri mwanamke wako kwanza, akikukubalia, ndipo utoke kuja kuongea na
wanaume. Acha kujidhalilisha Jax. Anzia kwa Tula, muulize akikushauri ndio
utende ili kuepuka mkanganyiko.”
“Na japokuwa wewe ni mnyama usiyejali
hisia za wengine hata kidogo. Mfikirie Lara. Najua kwako hujali juu ya mtoto
aliyepotea, kwa kuwa alimbeba Lara sio Tula. Lakini jitahidi kuwa binadamu.
Muache yule binti kabisa. Umempitisha katika wakati mgumu sana. Sidhani kama
kwa sasa anashida na gari au pesa yako wewe na Tula. Ukitaka, hiyo pesa nimkabidhi
Tula. Yeye ndio atajua chakufanya na hiyo pesa yenu. Kama alivyokusaidia
kufanyia maamuzi ya gari yenu na ile pete.” Tino akaondoka. Jax naye akakaa
pale kwa muda, akaamua kurudi kazini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wote wawatu, Tino, Tula na Jax, walisoma
chuo kimoja. Mapenzi ya Tula na Jax, Tino anayajua ndani na nje. Wanafahamiana kwa
karibu sana. Na hao wawili ni marafiki wakuongeleshana chochote, ila Tino na
Tula, hawawezi kukaa sehemu moja kwa zaidi ya dakika 5, wasianze kutukanana. Hawapendani
hata kwa kupishana, na sababu ni huyohuyo Jax. Wote wanamtaka Jax mahusiano. Na
wote Jax ameshindwa kuachana nao tokea enzi hizo. Tino amefanyika kama ndugu na
rafiki wa pekee aliyekuja kukubalika na Nelly. Tino tu. Hakuruhusu mtu mwingine
yeyote afike nyumbani kwake kumuona Jax hata kwa kuazima kitabu. Na Jax alijua
na kuheshimu hilo. Hakuwa akikaribisha mtu nyumbani kwao ila huyo Tino na Tula
ambaye Tula alifukuzwa na Nelly vibaya sana, alipomkuta hapo kwake.
Jax kwa Tula.
J |
ax
alirudi nyumbani mapema tu, akamkuta Tula amekaa sebuleni yupo na simu yake mkononi
kama anaye chati huku tv ikiendelea. Nyumba safi na amepika. Akaenda kukaa
kwenye kochi la pembeni. “Pole na kazi.” “Asante. Vipi na wewe siku yako?”
“Safi tu. Naona leo umewahi!” Akajibu Tula kwa kushangaa kidogo, akarudisha
macho kwenye simu. Jax akatulia hakujibu, Tula macho kwenye simu. Moyo wa Jax
ukashituka kuona pete aliyompa Lara, kidoleni kwa Tula.
“Naomba kuuona huo mkono wako wa
kushoto.” Tula akakunja uso kwa mshangao. “Unataka nini!?” “Nimeomba kuona
mkono wako.” “Kwa nini!?” “Hiyo pete umepata wapi?” “Na chupi niliyovaa pia
utaniuliza nimepata wapi?!” Akajibu kwa kumuuliza akiwa na mshangao mkubwa
mpaka usoni. Sio kwamba Tula amemjibu vibaya Jax, ndivyo alivyo Tula. Anaongea kile
anachokifikiria kichwani na mdomo wake haukujaliwa kuchuja neno. Ila hilo
halikuwa tatizo kwa Jax hata rafiki zake walipokuwa wakimlalamikia chuoni, yeye
alisema hiyo ndio haiba yake. ‘Watu hatufanani’. Jax alimtetea. Sasa hapo anapotaka
majibu ya kueleweka, ndipo na yeye anavuna alichopanda.
“Hiyo pete nilimvalisha Lara, imekuaje
ipo kidoleni kwako?” Jax akaendelea kuhoji taratibu tu. “Unashangaa la pete tu!
Mbona huulizi kwa nini mimi ndio nipo kitandani kwako na sio yeye! Acha mambo
ya ajabu Jax! Umechoka nini?” Akamuuliza na kunyanyuka. “Kama unanjaa, chakula
kipo mezani. Acha kupoteza amani humu ndani.” Tula akahama pale sebuleni na
kumuacha Jax amekaa. Jax akabaki akifikiria. Akaamua kumfuata chumbani.
Akamkuta amejilaza kitandani macho
kwenye simu. “Tula, naomba ukae tuzungumze.” “Nani amekwambia sikusikii? Wewe
ongea tu.” Tula akaendelea na simu yake. “Pete ya Lara umeipata wapi?” Tula
akakaa kwa hasira. “Unajua Jax, wewe unataka kunikorofisha tu! Wewe unasema
ulimvalisha Lara, kwa ajili ya uchumba. Sasa unalilia nini!? Eti Jax?” Tula
akauliza kwa hasira.
“Kwani Lara ni mchumba wako? Kwa nini
unataka abakiwe na pete ya uchumba wakati si mchumba wako tena?” “Tula!
Nakuuliza, pete ya Lara umeipata wapi?” Jax akaendelea na swali lake kama
asiyetaka kupotezwa malengo. Alichokifanya Tula, akaivua ile pete na kumrushia
Jax. “Hiyo hapo!” Akafyonza Tula kwa hasira. “Umenikuta nimetulia, umenianza
mwenyewe! Hiyo pete hata ukimrudishia huyo Lara haiwezi hata kumuenea tena!
Ataishia kuifungia tu wakati ni kitu cha thamani. Pesa yetu itapotea
bure! Kimekonda kama kimbwa kilichozaa na kukosa matunzo! Labda uivae wewe kama
unaona mimi nafaidi sana. Ili watu wajue na wewe umechumbiwa.” Tula akatoka. Ilimuuma
Jax, mpaka akakaa chini kabisa sakafuni. Akaiona ile pete pale sakafuni.
Akaiokota na kuitizama. Akabaki ameduaa akiitizama hiyo pete mkononi mwake.
Tula akarudi alikuwa ameacha simu yake
kitandani. “Gari ya Lara iko wapi?” Jax akamuuliza kwa upole tu. “Kwa nini
usimuulize huyo aliyekwambia ninayo?” Tula akachukua simu yake pale kitandani
akataka kutoka. “Nilikununulia gari yako Tula. Kwanini uchukue na gari ya
Lara?” “Nisikilize Jax. Lara mwenyewe ndiye aliyenipigia simu na kuniomba
nikutane naye ili anipe gari. Nilipofika hapo ndipo akanipa na pete.
Nilichofanya kwenye hiyo pete nikuongeza tu ukubwa, basi na kuivaa.”
“Kwa nini hukuniambia kama alikutafuta
kabla ya kwenda kuchukua?” “Wewe Jax vipi!? Ili iweje? Nikwambie ili iweje!?
Kama yeye mwenyewe ameona mimi ndio nastahili kuchukua hivyo vitu sio wewe,
sasa kwa nini nikwambie?! Halafu nakushangaa sana! Kipi kinachokusononesha hapa
mpaka ukae chini!? Vitu ulisema ulimpa Lara. Lara ameamua kunipa mimi, wewe
unaumwa na kipi!?” Tula akamuuliza akimshangaa sana tena kwa ukali kabisa.
“Au wewe kila kitu unachopewa huko nje
huwa unakuja kuniambia au mara ngapi huwa unakuja kuniomba ruhusa kabla
hujapokea? Uliniambia nisimfuate tena, sikumfuata. Amenitafuta yeye mwenyewe!
Ulitaka nikatae ili iweje?” Tula akaendelea kumuhoji. “Yaani mimi nipewe gari
na dhahabu, halafu nikatae!? Kwa lipi? Kwa utajiri gani nilio nao!? Mimi si
mjinga, wewe! Yeye karidhika na maisha, hataki gari wala dhahabu. Mimi nina
dhiki mpaka kichwani. Nijikute tu na mimi nakataa! Sifanyi upuuzi huo.” Tula
akatoka nakumuacha Jax hana swali la nyongeza.
Akaenda kuoga, akapanda kitandani bila
hata kula. Mengi yalikuwa yakipita na kuendelea kichwani mwake. Tula alirudi
pale chumbani. Akabadili nguo zake palepale mbele ya Jax akimwangalia.
“Nakwenda club.” Akamuaga Jax bila ya
kumwangalia huku akivaa. “Nashauri ukitoka club uendelee tu na maisha yako.”
“Unamaanisha nini!?” “Unakumbuka nilikukuta hotelini ukaniambia kama
sitakukubali unarudi Norway sijui London!” Tula akashituka kidogo. Ila
akajikaza. “London!?” Tula akauliza. “Ndiyo. Birmingham, London. Upo huru
kurudi popote unapotaka. Hapa naomba usirudi tena Tula. Naona mimi na wewe
hatutaweza kuja kuishi pamoja na maisha yakaendelea.” “Leo baada yakufanikiwa
ndio unajua hilo? Miaka yote nakulisha pale chuoni hukulijua hilo?”
“Naona kwa mara ya kwanza maishani,
umenifungua macho. Nitakuwa mzigo wako mpaka lini? Wewe ndio mwenye akili kati
yetu. Unajua nini chakuzungumza, na kufanya. Muda na wakati sahihi. Umenisaidia
sana, naona niwakati wa mimi kufikiria mwenyewe.” Jax akaendelea. “Na kwa kuwa
unaakili sana, wewe sio mjinga kama mimi, naamini utafanikiwa zaidi yangu.”
“Mwanaume usiyejua kuishi na mwanamke.
Kila mahusiano huyawezi. Ulianza na mimi, ukashindwa. Ukahangaika, ukampata
yule mjinga mwenzio, ulikaribia kumuoa bila kufikiria. Nimekufungua macho kwa
maneno machache tu, ukaamini sio mkeo, ukanitaka nikurudie. Nimekurudia, umeona
nimetulia, umeanzisha tatizo, ili niondoke. Sasa hapa mimi siondoki,
vimba na upasuke. Ndio ujifunze kuishi na watu. Acha kujifanya mwehu, uliyechanganyikiwa.” Tula
akachukua pochi yake na funguo za gari, alikuwa amependeza haswa. Na vile
alijaliwa uzuri wa umbile na sura, hakuhitaji vipodozi avutie. Na kuvaa vizuri
sio tabia aliyokutana nayo ukubwani. Tula alizaliwa kwenye pesa. Anajua kuvaa
kwa mavazi ya nje na ndani ya nchi. Ikifika kwenye swala la kununua nguo ya
kuweka mwilini mwake, hababaishi. Hajui kujikosea.
Hapo alipo kwa muda mfupi tu aliokuwa
ameamua kutoka, akajiandaa kwenda club, alishapendeza. Akatoka kwa kufunga mlango
kwa nguvu sana. Jax mwenyewe akabaki kama amepigwa na butwaa. Kweli Tula
alikuwa mbabe kwake. Na hakuonyesha kumuhofu hata kidogo tofauti kabisa na Lara.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment