![]() |
Mama Yake Lara.
Z |
ikiwa
zimebaki siku 9 tu harusi ifungwe, mama yake Lara akatua jijini Dar si kwa
sherehe tena kama walivyokuwa wakitizamia kufika siku ya 7 yake, yaani alhamisi
ya juma linalofuata, ila ikawa matatizo. Suzy, Sesi na Tino ndio waliokwenda
kumpokea. “Kwema? Mbona Lara hajaja?” “Lara anaumwa mama. Hatujui kitu
chakufanya, ndio maana tumekuita labda utusaidie.” Mama yake Lara akatulia
kidogo.
“Hazungumzi, hali wala kunywa.” “Tokea
lini?” Akauliza mama yake. Akaona wanaangaliana. “Kuna nini Tino mwanangu?” Akaona
amuulize Tino moja kwa moja, kwa kuwa Tino ndiye alikuwa mtu wa Jax wa karibu.
Hata nyumbani kwa kina Lara, alijulikana ndiye anayesimamia mambo hayo ya
harusi kwa karibu kama mwenyekiti wa kamati ya harusi.
“Ni vile kwa kuwa nawaheshimu wazazi
wangu, na Lara amefanyika kama ndugu sasa. Lakini kama ingekuwa ni mtu
mwingine, hata mimi usingenikuta hapa, kwa aibu.” Akaanza Tino. “Ni aibu na
fedheha mama yangu. Sijui niseme nini!” Akasita Tino, lakini mwishowe ikabidi
kumueleza huyo mama kabla hawajafika na kumkuta Lara mwenyewe.
Wakashangaa yule mama naye kimya.
Hakujibu kitu wala kuongeza neno. Akajirudisha nyuma kitini, akakaa kimya mpaka
walipofika. Akamshukuru Tino kwa kwenda kumchukua kituo cha mabasi, akaingia
ndani. Tino naye akafuata nyuma. Hakuondoka.
Yule mama aliiingia moja kwa moja mpaka
chumbani kwa Lara. Alishalala humo mara kadhaa kila alipokuwa akifika Dar.
Alimkuta binti yake amejifunika shuka, anatetemeka baridi. “Sesi mama, naomba
niongezee blangeti, halafu naomba chai ya rangi.” Sesi hakutoka hata nje,
alijua ni wapi Lara mwenyewe anaweka vitu vyake. Akafungua kabati la Lara. Juu
kabisa, akavuta blangeti. Akamsaidia kumfunika. Suzy alishaanza kutengeneza
chai ya rangi. Tino akaingia. “Nisaidie nini mama?” “Tiketi mbili za kurudi
Dodoma kesho.” Sesi na Tino wakaangaliana.
“Kwa hali hii, hataweza kufanya kazi si
kesho wala kesho kutwa. Lazima atulie kabisa na mimi siwezi kukaa hapa Dar.
Natakiwa kazini. Likizo ilikuwa nichukue jumatano ile ijayo ili alhamisi tuje
huku kusubiria harusi hiyo siku ya jumamosi.” “Basi mama, mimi
nitawasindikiza.” Tino akajitolea.
“Tino mwanangu, usione unawajibika.
Tulia tu kazini ili tusiharibu kotekote. Lara akaja kukosa pakukimbilia
atakapopona. Tulia kazini, baba. Sisi tutaondoka tu na basi.” “Usijali mama
yangu. Nyinyi jiandaeni, kesho nitakuja asubuhi kwenye saa nne. Nitaanzia
ofisini kwanza.” “Nashukuru baba. Mungu akukumbuke katika hili.” “Amina mama
yangu. Poleni sana na samahani.” “Inatokea baba. Wala Lara si wakwanza. Atakuwa
tu sawa.” Wakatulia mama yake akimsugua upande wa mgongoni taratibu.
Suzy akaingia na ile chai. Akajaribu
kumfanya anywe ile chai, lakini Lara alikuwa akitetemeka kama yupo kwenye
baridi kali. Mpaka midomo ilikuwa ikicheza. Alikuwa amekaa. Akajivuta ukutani
akajikunja huku akitetemeka. Mama yake akasimama na kumzungushia lile blangeti,
Lara akainama. Kimya. Wakamuona Tino anaondoka kimya kimya bila ya kuaga. “Mimi
naona tusimpe hiyo chai mama. Ni moto sana. Na hivyo anavyotetemeka, itammwagikia.”
Sesi akatoa wazo.
“Lara!” Mama yake akamuita taratibu.
Lara akanyanyua kichwa kumwangalia mama yake huku akitetemeka. “Utakuwa sawa
mama. Umesikia? Usiogope. Hata katika hili naamini, Mungu wetu yupo.” Wakamuona
anatoa machozi huku akimwangalia mama yake. “Hata hili, litapita tu mama yangu
mzazi. Umesikia Lara? Utakuja kugeuka nyuma, utashangaa ulivuka vipi. Mpe
nafasi Mungu akubebe. Sawa?” Wakamuona anarudisha kichwa chini.
Yule mama alikuwa ni nesi. Mtaratibu sana. Kama si kufanana na Lara mpaka rangi ya
mwili, usingesema Lara ni binti yake. Walikuwa na haiba tofauti. Lara mtundu na
mcheshi sana. Huyo mama akizungumza, utafikiri amesahau anachotaka kusema.
Mtaratibu na mtulivu kama dada zake Lara. Akamwangalia mtoto wake, akaona
amrudishe tu alale. Lara akarudi kujilaza. “Sasa hivi usilie tena. Tulia tu.
Jitahidi kutulia.” Akamwambia mtoto wake.
“Sesi mama, nipeleke duka la madawa.”
Sesi akatoka na mama yake Lara, akamsindikiza mpaka kwenye duka la madawa.
Akaagiza dawa alizotaka, Sesi akimtizama tu. Ila alimuona amenunua dripu tatu. Wakarudi
nyumbani. Akamuwekea mtoto wake dripu. Ile dripu ilipofika katikati wakaona
ameacha kutetemeka. “Amelala. Hiyo itamsaidia.” Akanong’ona mama yake huku
akimwangalia mwanae. Sesi, Suzy na Warda walikuwa kimya hapo chumbani kama wapo
msibani.
Mama yake Lara akawageukia. “Na nyinyi
mnaendeleje na kazi?” “Vizuri.” Wote wakajibu kwa pamoja. “Mkazane, msizembee
kazini.” Akaongeza mama yake Lara akitaka kuwatoa hofu. Kidogo wakajisogeza na
kukaa. “Sasa na wewe utakula nini mama? Leo hatujapika, ila tunaweza kwenda
kukuletea chips.” “Wala msihangaike. Chai ya rangi itanitosha, lakini kwanza
nikaoge.” “Basi tunakuandalia maji bafuni, wakati unabadili nguo.” Sesi
akamtolea kitenge na taulo kutoka kabatini kwa Lara. Wakampisha hapo chumbani.
K |
esho
yake asubuhi na mapema, warembo hao waliamka mapema kama kawaida yao. Wote
wakaenda kumgongea Lara na mama yake kuwajulia hali na kutaka kuwaaga.
“Tumelala vizuri.” Akajibu mama Chiwanga akiwakaribisha ndani. “Mimi nakwenda
kuandika barua ya likizo ya Lara, na mimi kuomba ruhusa, niwasindikize.
Nitarudi na Tino.” “Hapo utakuwa umemsaidia mwenzio. Nashukuru Sesi mwanangu.
Na wewe Mungu akukumbuke siku utakapomuhitaji.” “Amina mama.” Wakaondoka lakini
walikuwa wamemuachia chai na kitafunwa mezani.
Mida ya saa 4, Tino na Sesi wakarudi
hapo nyumbani. Walikuta yule mama alishamuandaa mtoto wake, na sanduku lake.
“Sisi tupo tayari.” Akaongea mama Lara wakati anawafungulia mlango Tino na
Sesi. Baada ya kama dakika 20, safari ya Dodoma ikaanza Lara akiwa amemlalia
mama yake, amemfunika blangeti.
Haikuwa safari yenye mazungumzo ila
Lara kubadilishwa mara kwa mara njiani sababu ya hedhi kali aliyoipata. Ilibidi
uanaume na aibu imuishe Tino ili kufanikisha hiyo safari kwani ni kweli Lara
alikuwa akitokwa na damu nyingi sana. Kila wakati ilibidi kusimamisha gari ili
Lara asafishwe na kubadili matandiko aliyokuwa anakalia na kulowa. Ilikuwa ni
hali ambayo hakuna mtu angetamani kuwepo hapo. Ilikuwa ni maumivu ya namna yake
kwa kila aliyekuwepo hapo na Lara.
Walifika Dodoma, Tino akaomba wao
warudi Dar siku hiyohiyo. Akawaambia analazimika kuwepo kazini siku inayofuata,
hakuwa na likizo. Kwa kuwa kila mtu pale nyumbani kwa Chiwanga alikuwa kwenye
mshituko wakumuona bibi harusi huyo amerudishwa mgonjwa, mahututi hakuna
aliyekuwa na laziada kwa Tito na Sesi, zaidi ya kuwashukuru. Wakaondoka.
Usiku huo walipofika nyumbani,
hawakulala. Lara alizidiwa. Ikabidi kupelekwa tu hospitalini alikokuwa akifanya
kazi mama yake Lara. Mpaka inafika asubuhi kila mfanyakazi pale hospitalini
alishajua juu ya kurudishwa nyumbani kwa Lara. Maneno yakaanza kuenea.
Kwa Tino.
T |
ino
alimrudisha Sesi nyumbani kwao Kinondoni na kwenda moja kwa moja mpaka nyumbani
kwa Nelly. “Mbona kama umetoka msibani?” Nelly akauliza wakati akimpisha
mlangoni. “Kwanza nashukuru kwa kurudishiwa pesa yangu yote.” Tino akakunja
uso. “Nani amekurudishia?” “Jax mwenyewe.” Tino akawa hajaelewa. Akaenda kukaa.
“Naomba nilewe hapa kwako na nilale kabisa.” “Hapana Tino. Wewe unajua mimi
sipendi pombe ya siku za kazi.” “Nitanywea chumbani.” “Si uende kwako!” “Nipo
kwenye mshituko dada yangu! Nimeshindwa hata kupitia baa.” Nelly akaenda kukaa.
“Kutokea wapi?” “Dodoma. Kumrudisha
Lara nyumbani kwao.” Nelly hakuwa anaelewa. “Mapenzi sumu dada! Bora wewe
ulijiamulia kuwa peke yako. Yule binti ana hali mbaya, imebidi rafiki zake
wampigie mama yake simu, aje. Wanasema ameshindwa kuongea tokea Tula amfuate
ofisini kwenda kumdai gari na kumwambia Jax anamuacha yeye kwa ajili yake.” Nelly
akatoa macho.
“Subiri kwanza. Anzia mwanzo. Eti Tula
amefanya nini!?” Tino akamsimulia kila kitu, Nelly akabaki ametoa macho. Tino
akajua hata yeye mwenye roho ngumu, imemuingia. “Yaani dada Nelly, tulisimama
njiani mara kadhaa ili kubadilishwa sababu yakujichafua. Anatokwa na damu kama
bomba! Ilibidi kuweka plastiki chini ili akalie. Yule mama alikuwa ametulia,
mpaka akatushangaza! Hakulaumu wala kuendeleza swala la harusi. Tulisafiri
akiwa amemuwekea dripu mtoto wake.” “Isijekuwa alikuwa ni mjamzito, mimba
ilitoka kwa mshituko!” Nelly akafikiria kwa sauti.
Wakabaki kimya kwa muda. “Lakini ni
kama Lara alihama au walisimamisha mapenzi na Jax, kwa muda.” “Kwa nini na
wakati yule binti alikuwa akiishi naye!?” Akauliza Nelly. “Jax alisema Lara
alimshauri waachane kwa muda mpaka siku ya harusi yao. Halafu si unajua ndio
zikafika siku za shug...” Tino akasita kama aliyekumbuka kitu.
“Oooh!” Akasimama kwa mshituko kama
aliyefunguliwa na yeye macho. “Nini?” Nelly akamuuliza. “Yule binti alikuwa
mjamzito dada, lakini Jax hakujua. Au hata mimi sikuwa nimeelewa. Yaani hapa
ndio umenifanya nifikirie.” “Kaa chini acha kunitia wasiwasi zaidi.” “Dada,
yule binti alikuwa mjamzito!” “Kwa nini unafikiria hivyo?” “Miezi miwili
iliyopita, akaanza uzito wa kupika mle ndani. Wote tukaanza kula nje. Nikawa
namcheka Jax, namwambia amerudi kuwa seja kama mimi. Wote tunakula mtaani.
Akasema Lara ameanza kubadilika. Hapiki tena. Na mara nyingi akifika pale,
anaishia kulala kwenye kochi hata chumbani hafiki. Nikamuuliza kama ni mgonjwa
au waligombana. Lakini dada Nelly, ushawahi kukutana na watu walioweza
kuelewana?” Tino akauliza. Nelly akabaki kimya kama aliyetingwa na lake.
“Basi ni Lara na Jax. Wale watu
walikutana wote hawana makuu. Kila kitu kilikuwa kikienda sawa. Sijawahi
kumsikia Jax akimlalamikia Lara, isipokuwa kipindi hicho tena haikuwa kama ni
tatizo kubwa. Akapunguza kwenda kwa Jax, ndio mwishoe Jax akaniambia Lara
ameshauri waache mapenzi ili wafaidi kwenye fungate. Hatukulizungumzia sana
hilo kwa kuwa hata Jax mwenyewe alikuwa busy kazini, na mimi ndio nilikuwa na
maswala la vikao vyao vya harusi.” Tino akazidi kuvuta kumbukumbu.
“Ila nakumbuka nilijaribu kumuuliza
labda kama anamshuku kama Lara anaweza kuwa na mwanaume mwingine, akasema
anauhakika Lara si muhuni. Ametulia sana. Na kama hatakuwa amelala nyumbani
kwake, basi atakuwa amelala kwa Jax. Akasema ni mabadiliko ya namna yake,
lakini akanihakikishia sio mwanaume mwingine. Tukasema labda anachoka na
maswala ya harusi.” “Yule binti alikuwa mjamzito Tino! Iwe alijua na kutaka
kuja kumwambia Jax baadaye au na yeye pia hakuwa akijua. Lakini Jax ameua mtoto
wake yeye mwenyewe.” Nelly akaongea akifikiria.
“Lakini dada, nimemvulia kofia Jax.
Hakika Jax ni mwanaume! Au niseme, yapo mapenzi ambayo mimi sijawahi kuyapata
hapa duniani.” “Kwa nini unasema hivyo?” Nelly akauliza. “Jax amemuacha Lara!
Mimi bado sijaamini! Nahisi ni kama ndoto ambayo itakuja kuisha, nitaamka.
Lara! Hakika siamini.” Tino bado alikuwa kwenye mshituko.
“Wewe dada hukubahatika kukaa na Lara.
Lakini yule binti ni tofauti na alivyo. Mwanzoni Jax alikuwa akiogopa
kumtongoza akihofia atakuja kumsumbua sana. Lakini uzalendo ukamshinda,
nafikiri akazidi kuvutiwa naye, akaja kuniambia amezungumza naye, Lara
amekubali kutoka naye. Yeye mwenyewe Jax hakuamini.” “Mimi mwenyewe sikuwa
naamini. Nikajua atamsumbua sana. Nikamwambia kwanza ni mdogo, pili ni karembo
kamjini. Akija kupata mwenye pesa zaidi yake, atamkimbia tu. Nilimuonya sana
Jax amuache. Lakini kama unavyomjua Jax, alinijibu kuwa tatizo langu mimi
ninamtizama yeye kama ni mtoto mdogo wa jana na hawezi kufikiria. Basi
nikamuacha. Leo kuja kuona Jax ndiye anamuacha kwa ajili ya Tula! Nahisi na
mimi sijayajua hayo mapenzi.” Wote wakanyamaza.
Tino amesimama, Nelly amekaa. Kimya kwa muda kila mtu akiwaza lake. Mwishoe Tino akaguna. “Namuhurumia Lara, kupita kiasi! Sidhani kama maisha yake yatakuja kuwa sawa. Alimpenda sana Jax!” “Mimi namuombea Mungu Jax mdogo wangu, awe amepatia. Lasivyo!” Dada yake akatulia kidogo. “Ila Tula naye anamaswali mengi kuliko majibu! Mmmh!” Akaona anyamaze.
Kwa Jax.
K |
weli
Jax alikuwa na mpango wa kumsuprise Lara kwenye nyumba kubwa. Alipata nyumba
iliyokuwa ikiuzwa kwenye mnada wa benki. Jax asiyependa makuu, sijui ramani
iweje au bustani iwe mbele au nyuma, alipoona ni nyumba ya kisasa, vyumba
vitatu, bei nzuri, na pesa alikuwa nayo baadhi na kazini kwao anaweza kuchukua
mkopo bila shida, akafanya utaratibu wa kuimiliki, tena kimyakimya ila kwa
haraka na kutaka kuja kumuonyesha Lara baada ya fungate, wahamie pamoja na
kumuacha Lara aitengeneze atakavyo.
Ni kweli akili na mawazo ya Jax
yalikuwa yametulia kwa Lara tu. Baada ya kutendwa na Tula, akaangukia kwa Lara.
Mrembo, mtundu, maneno mengi, mchangamfu kiasi chakumfanya Jax kutulia na
kufurahia penzi lake. Tula aliporudi pichani na kufanikiwa kumpora tonge Lara,
hakulazia damu. Akamwambia Jax wahame pale walipokuwa wakiishi na Lara
wakatafute sehemu yao wao, waanze upya. Ndipo Jax akaona kuliko kupanga tena,
ni heri kuhamia kwenye nyumba aliyokuwa amenunua ambayo ilikuwa ikifanyiwa
marekebisho tu madogo. Zaidi kubadilishwa rangi iliyokuwepo. Jax alitaka ipakwe
rangi nyumba nzima, na matengenezo ya jikoni tu.
Tula alipogundua kuwa kuna hiyo nyumba, hakutaka kusubiri, akamwambia wahamie tu hivyohivyo, mambo mengine yaendelee wakiwa wanaishi humohumo ndani kwenye hiyo nyumba. Kama kawaida ya Tula, alijaliwa uwezo mkubwa sana wakuingia akilini na moyoni kwa Jax. Jax alikuwa hawezi kusema hapana kwa lolote, kwa Tula, tokea wapo chuoni. Wakahamia.
Tula & Jax
T |
ula
na Jax walikuwa wapenzi kama kumbikumbi walipokuwa chuoni. Kuanzia mwaka wa
kwanza mpaka wakamaliza. Hata Tino alikuwa akimlalamikia Jax kuwa anatumia muda
mwingi na Tula kuliko mtu mwingine yeyote. Nelly yeye alimwambia asipokuwa
mwangalifu, atafeli sababu ya Tula. Mapenzi popote, wakati wowote wanapopata
nafasi. Tula alishawahi kwenda kulala kwa Jax wakati akiishi na dada yake. Nelly
aliporudi kutoka safari na kukuta Tula amehamia nyumbani kwake, aliwafukuza usiku
uleule, hakutaka hata pakuche.
Wawili hawa walivumiliana kwa mengi
bila kukata tamaa. Jax na Nelly wakiwa yatima waliojikuza wenyewe, Tula
akaongezeka kwenye maisha ya Jax, akawa faraja kweli. Alimjua Jax kwa
kumtizama. Hakuwahi kumsaliti japo ugomvi kwao ilikuwa kitu cha kawaida kwa
kuwa Tula alikuwa na tabia yakupenda kutawala mambo. Alipenda kila
anachomwambia Jax, awe anafanya. Na ikitokea hafanyi hapo ndipo kulikuwa na
kupishana. Au ikitokea Jax anatumia muda mwingi na kina Tino sio yeye, basi
hapo kulikuwa na wivu. Alimtawala Jax kwa kila namna.
Yeye Tula alitokea kwenye familia yenye
uwezo sio shida. Wakati wa uhai wa baba yake, Tula alikuwa na pesa. Kwa hiyo hata
chuoni hakuwa akiishiwa, na mara kadhaa na yeye alimsaidia Jax kwenye mambo
madogomadogo kama vile Nelly alivyokuwa akimsaidia Jax. Kuanzia ada mpaka
malazi, ilikuwa ni Nelly. Jax hakuwa na akili nyingi za darasani kama za dada
yake. Kwa hiyo alipomaliza kidato cha sita, matokeo yalipotoka amepata daraja
la 2 karibu tatu, haraka bila kuchelewa, Nelly akamtafutia nafasi chuo kikuu
cha Tumaini, palepale Dar. Na ndipo alipokutana na kina Tino, Tula na wengineo.
Mapenzi kati ya Tula na Jax yakaendelea
mpaka wakamaliza chuo. Ikaanza kazi yakutafuta ajira. Rafiki zake karibia wote,
walipata kazi, kasoro Jax. Jax akakaa nyumbani kwa muda mrefu sana. Mambo
yakaanza kuwa magumu kati yao. Tula anataka ndoa, na Jax hakuwa tayari kwa ndoa
kwakua hakuwa na kipato chochote chakuweza kumuweka Tula ndani. Ikawa tatizo
kati yao. Jax hapati kazi, Tula anaharaka na ndoa waishi pamoja. Ugomvi na
kupishana kukazidi. Tula akawa akilalamika mahusiano yao hayana baraka kama
wengine. Mifano ya rafiki zake kuolewa kwa haraka yeye akiwa hana mbele wala
nyuma ikaendelea kila wanapokuwa na Jax na kwa simu pia.
Na ndio kipindi hichohicho baba yake
Tula kama nguzo ya familia akafariki, na yeye Tula akaanza kuhangaika maisha.
Akiwa yeye ndio msaada wa kifedha kwenye mahusiano yao ya kimapenzi, na yeye
akaanza kuishiwa kupitiliza. Tula aliyekuwa akiishi maisha ya kutapanya akawa
hana pesa. Baba aliyekuwa akimpa pesa ameondoka, Jax hapati kazi. Tula alishazoea
kuchukua chumba hotelini, anakwenda kukaa huko na Jax mpaka anaishiwa ndipo
anarudi kwao kuomba zingine na Jax anarudi hosteli kwa kina Tino au nyumbani
kwa dada yake baada ya kumaliza chuo. Mambo yakawabadilikia.
Huku na kule Tula mtoto huyo wa namna
yake, mwenye uzuri wake, katika hangaika zake na yeye hapati kazi, akapata
mwanaume wa kizungu kutokea Norway. Akamualika Tula kwenda kutembea nchini
kwao. Bila kusita au kupinga na bila kumshirikisha Jax au kumuaga, akapanga
safari, akaondoka nchini. Jax na rafiki zake wakaona tu picha za Tula huko
Facebook na Instagram akiwa na mzungu. Mara akabadili status, ‘engage’. Picha zake na mzungu wake kama wapenzi
zikaenea mitandaoni. Mawasiliano kwa Jax akakata kabisa. Ili asijiumize, Jax
akafunga akaunti zote za Facebook na Istagram. Akabaki mtaani. Hana kazi wala
mwanamke. Kula kulala kwa dada yake, na dada yake kimya kama hamuoni hapo
ndani.
Japokuwa aliumia sana, lakini Jax
alibaki kumtetea Tula kuwa yeye kama binadamu alichoka kusubiri. Akawaambia
watu anajuta, angekubali kumuoa Tula vilevile alivyokuwa amekubali aolewe naye
bila kazi au kipato. Mwaka ukaisha, kimya. Hamna kazi wala mawasiliano kati
yake na Tula.
Baadaye Mungu akaja kumsaidia Jax, nafasi
za kazi CRDB zikatangazwa. Tino akamwambia. Jax akatuma maombi na kwa kuwa Tino
alifahamiana na wengi, akamuombea rafiki yake, Jax akapata kazi. Jax hanywi
pombe, hana mwanamke. Alikuwa akiishi na Nelly dada yake, ameumizwa kwenye
mapenzi, akili yote akaweka kazini. Mchana na usiku, akili na mawazo ya Jax
yakawa kazini, na hakutaka kuharibu akikumbuka shida aliyopata mtaani muda
mrefu bila ajira.
Baada ya mwaka tu, Jax akaanza kuhamishwa
vitengo kwa sifa njema. Viongozi wake wakampenda kuliko cheti alichokuwa
amekileta hapo kazini, ambacho kilikuwa chini kuliko kina Tino. Wenzake
walifaulu vizuri, yeye alipata daraja la chini sababu ya kukimbizana na Tula
bila kuchoka. Jumanne na jumatano anakuwa chuoni, alhamisi mpaka jumatatu jioni
anakuwa nyumba za kulala wageni na Tula. Mitihani ya mwisho hakufanya vizuri
kama wenzake. Alipofika kazini akaweka nidhamu ya hali ya juu, akarudi tena
chuo kufanya shahada ya pili. Safari hii Jax alikuwa akihangaika mpaka dada
yake akamuhurumia na kuona amebadilika. Kazini, chuoni. Tena chuoni akawa
anafanya vizuri sana, kama anayelipa kisasi.
Nelly alisoma tokea binti mdogo tu. Nje
na ndani ya nchi akijiendeleza mwenyewe mpaka ngazi ya juu kabisa, Phd, na
kufanikiwa kupata kazi mapema huko TRA. Ukisikia mwadilifu na mchapa kazi, basi
ni Nelly. Kazi ndio baba, mama, mume, mtoto na rafiki. Hakuwa na maisha mengine
ila kazi tu. Alitoka TRA akaajiriwa na NGO moja kubwa sana hapo nchini, Nelly
akawa mkurugenzi hapo. Anatengeneza pesa ya kigeni inayoingia mfukoni mwake,
mpaka ikawa inakosa matumizi. Ukimtizama tu Nelly, utajua pesa ipo. Anamsimamo
wa waziwazi, akikutizama tu, utajua hababaishwi na utajua anao uelewa wa mambo.
Ameishi nje ya nchi akisoma, na kazi yake hapo nchini anafanya na watu wa
mataifa tofautitofauti akiwakilisha Tanzania.
Kwa haiba yake, hakuwa na shida kugonga
kokote, kwa mkubwa yeyote akapewa nafasi yakueleza shida yake, akashindwa
kusaidiwa. Alipomuona Jax ametia akili. Amejifunza kutokana na makosa, baada ya
miaka mitatu hapo benki, Jax akiwa amempita mbali Tino aliyemkuta hapo kazini, na
amemaliza shahada yake ya pili, Nelly akamuunganishia huko benki ya dunia.
Viongozi wake walimuandikia barua nzuri za uadilifu kazini, na mambo aliyofanya
hapo kazini kuongezea benki faida, akaambatanisha na vyeti vyake vyote, yeye na
dada yake wakatuma huko benki ya dunia, Jax akaitwa kwa usahili, akafanya
vizuri, akapata kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Lara na yeye alipata kazi kwenye
kampuni hiyo ya simu. Akakutana na kina Sesi, Warda na Suzy ambaye alishatembea
na Tino. Mchana wanapokwenda kula kwenye kibanda hicho cha chips, nyuma ya
kwenye mgahawa wa Best Bite walikuwa wakikutana na wafanyakazi tofautitofauti
wakiwepo na hao wa benki, kina Tino, kipindi hicho hata Jax hajahamia kufanya
kazi benki ya dunia. Tino alishamshindwa Suzy. Alimwambia Jax, Suzy ni msichana
mzuri lakini amemshindwa kama mpenzi. Suzy hakuwa akijua kuchuja neno analotaka
kulitoa mdomoni mwake, japo si muhuni. Ataongea lolote kwa yeyote. Hana soni.
Basi mida hiyo ya mchana wafanyakazi
wengi wanakutana hapo kibandani kila mmoja akitaka kula. Hapo Suzy atamchokoza
yeyote amtakaye, kutoka kampuni yeyote. Haitaji kumzoea mtu. Ataongea tu. Basi
yeye Jax akajitahidi kumkwepa kabisa yeye na marafiki zake wanaokuja kula hapo.
Zaidi ya salamu, hatamjibu kitu zaidi ya kutoa tabasamu tu. Na hata kama
watakwenda kukaa kwenye meza moja waliokaa yeye na Tino, basi Jax hatazungumza
lolote. Kimya. Mpaka amalize kula. Suzy
ataongea hili na lile wakitaniana na Tino na wafanyakazi wengine. Mara
watukanane na Tino hapohapo mezani. Ilimradi kila mtu atajua Suzy yupo hapo na
hakuwa akijua kuongea kwa sauti ya chini. Akicheka mpaka watu wote watawageukia
wao kwa kelele, lakini Jax hakutaka mazoea naye kabisa.
Tino yeye ndio akageuka mtu wa kupenda
kumchokoza ili tu aanze kupayuka. Wakati mwingine Jax alikuwa akimkataza na
kumwambia Tino, akianza kumchokoza, yeye ataondoka. Na Suzy akajua Jax
hampendi. Ikabaki hivyo.
Mambo yalibadilika alipoanza kazi Lara,
na kuungana na kina Suzy kwenda kula. Suzy mwenyewe akaanza kumnadi. “Siku hizi
tunatembea na modo, watoto wakizungu, hatutaki kufuatwa.” Akaanza Suzy
akitangaza hapo kibandani ambako huwa wanakuwepo wafanyakazi wengi wa kutoka maofisi
tofautitofauti maeneo hayo ya Posta wakitaka kupata mlo wa mchana hapo.
Mpaka wauza chips walikuwa wakimjua
Suzy. Akifika anatoa oda yake kwa kelele, na lazima apewe. “Maswala ya kuniita Suzy
bonge, mkome. Sasa hivi tunakwenda mwendo wa kizungu. Hakuna kula sana.” Tino
alicheka sana aliposikia hivyo. “Utaweza lakini?” Tino akiwa mbali kidogo
wakiwa wao walishapata chakula, wamekaa kwenye meza yao, wafanyakazi wa benki,
vijana watupu, Suzy alipomsikia, akamfuata.
“Na kwa taarifa yako, watu
wanabadilika. Kuanzia sasa hivi naanza gym, kula kwa kisu na uma, tena matunda
tu. Kasoro leo ndio nakula chips yai.” Tino alicheka sana, tena kwa sauti. Na
wenzake wakainama huku wakicheka kwa hofu wakimuogopa Suzy, maana hakawii
kumbadilikia mtu. “Tatizo lako wewe dharau.” “Sio wote waliubwa wembamba, mama.
Wewe endelea tu kula chips yai.” “Sasa kwa taarifa yako nishamwambia Lara kuwa
nimetembea na wewe, na hawezi kukukubali.” “Kwani mimi nimekwambia namtaka!?” Tino
akauliza kwa kushangaa sana. “Nimeona sana jinsi unavyomwangaliaga.” Wakaanza
kubishana kama kawaida yao, na Lara mwenyewe yupo upande mwingine na kina Sesi
pamoja na Warda wakimsikiliza mwenzao anavyojibizana, wakishindwa hata kugeuka
kwa aibu.
Hapo ikabidi sasa Jax na yeye kumuangalia
vizuri huyo Lara, ambaye Tino alimwambia Suzy bila kusita tena kwa sauti ya juu
tu kuwa wao wote wanamuangalia tu huyo Lara kama fahari ya macho tu. Kusuuza
mioyo. Ndipo Jax akaanza kumtizama vizuri Lara.
Taratibu na yeye akavutiwa na Lara. Wakaanza
kwa salamu. Mara kupungiana mkono wanapokuwa mbali kidogo. Tino akaona na
kushangazwa. Jax alishasema hatakuja kupenda tena. Alirudia rudia kila wakati
ule usemi wa ‘Love come once in a life time’. Kwamba mapenzi huja mara
moja tu maishani. Alishampenda Tula, hatakuja kupenda tena. Hakutaka
kujihusisha na wasichana wengine.
Lakini akaona inaanza kuwa tofauti kwa
Lara. Kila kina Suzy wakifika hapo kibandani, macho hayabanduki kwa Lara.
Atamfuatilia kuanzia wanafika hapo mpaka wanapata sehemu ya kukaa, anakuwa
akimwangalia kwa muda mrefu tu, wakati mwingine alimuona Jax akitabasamu peke
yake. Tino akajua ameshanasa. Sasa kuja kusikia anatoka naye kwa chakula cha
usiku siku ya jumamosi, akajua tayari. Jax sio mkurupukaji.
Mapenzi kati yao yakaanza taratibu. Kwa
mara ya kwanza Jax akasikika akisifia mwanamke mwingine mbali na Tula!
Akaonekana amefika kikomo, aoe kabisa, amalize. “Hakuna nitataka zaidi, Tino.
Acha nimalize kabisa.” Maneno yake kwa Tino na marafiki wengine, tena baada ya mwaka
mmoja tu kuwa na Lara.
Marafiki wote wakaridhia na kujua hatimae Jax amepona mawazo ya Tula, yupo tayari kuendelea na maisha yake kwenye maswala ya mapenzi. Wakamuunga mkono katika kila hatua ya kukamilisha kuoa. Kwanza alikuwa ni Lara. Anapendeka.
Ujanja Kupata.
J |
ax
akiwa ametingwa na majukumu ya kazi na vikao vya harusi ambavyo Tino alikuwa
akiwaitisha akijisikia yeye, zaidi akiwa amelewa, akiwa baa. Anapojisikia yeye
Tino kama mwenyekiti wa kamati ya harusi, iwe mara au baada ya tarehe ya kikao,
yeye atapigia simu kila mtu kutaka wakutane kwa muda mfupi kwenye baa
aliyochagua yeye ili wafanye kikao. Sasa katikati ya yote hayo wakihangaika
kufanikisha mambo ya harusi yao, ndipo shilingi ikapinduka.
Jax akawa busy na Lara naye busy na
mambo ya harusi yao. Mara Dodoma nyumbani kwao, mara Dar kwa maandalizi ya kitchen
party ya marafiki pamoja na harusi na mambo mengine mengi ilimradi
shamrashamra. Akiwa anatoka kazini mida hiyo ya jioni akapokea ujumbe kutoka
kwa Tula. ‘Naomba kukuona, nipo mjini kwa siku chache.
Tula.’ Moyo wa Jax ulipasuka, akashindwa hata kuwasha gari. Akabaki
ametulia kwenye gari yake akiutizama ule ujumbe.
Tula akapiga hapohapo baada ya kuona
Jax anesoma ujumbe wake. “Naomba unione Jax. Sitachukua
muda mrefu.” Kimya. “Jax?” “Unataka nini Tula?”
“Njoo kwanza ndipo nitakwambia.” “Wapi?” “Nimechukua chumba hapa hotelini.” “Naoa
Tula.” Tula akatulia, hakujibu. “Umenisikia?”
“Unafikiri unaweza kuja au hutaweza, sasa hivi mimi sina maana tena?”
“Nitakuja, lakini sitakaa.” Akamuelekeza alipo. Jax akaondoa gari
kumfuata.
Njia nzima, kumbukumbu za Tula zikaanza
kumrudia. Jinsi alivyomsubiri hata baada yakumuona na huyo mwanaume wa kizungu
huko Norway. Alishajiapia hata kama angerudi wakati ule, angesamehe yote,
warudiane. Lakini ndipo akatokea Lara, akamtoa mawazo ya Tula mpaka hapo Tula
anamtafuta, ndipo akamkumbuka tena Tula. Akaendelea kuwaza mengi akikanyaga
mafuta kwenda kumuona Tula.
Akafika hapo hotelini na kwenda mpaka
kwenye chumba alichoelekezwa na Tula. Ilikuwa ni saa mbili, akamkuta Tula ndio
anatoka kuoga. Alimfungulia mlango na nusu taulo. Macho yakamtoka Jax. Ni Tula!
“Ingia ndani. Mimi sili watu.” “Mumeo yuko wapi?” Jax akauliza wakati anaingia.
Tula hakujibu, akanyamaza na kurudishia mlango.
“Mbona sioni pete hapo kidoleni?” Akauliza
tena Jax, akikusudia kumkejeli Tula. “Nilishindwa kuendelea Jax.” Tula akajisikitisha
huku anakaa kitandani mbele ya Jax. Jax akabaki akimtizama. “Yule mwanaume
hatukukaa naye muda mrefu Jax. Nilishindwa. Hamfanani hata kidogo! Nilikataa
ndoa. Aliumia, lakini ilibidi kumwambia ukweli, kuwa nampenda mtu mwingine.
Nisingeweza kuolewa naye. Nilijua madhara yake, lakini sikuwa na jinsi.” Jax
akabaki kimya akimsikiliza.
Alitegemea Jax amuulize madhara gani,
lakini kimya. “Nilikuwa radhi anifukuze kwake kuliko kuingia kwenye ndoa ambayo
sitakuwa na furaha daima, Jax. Kumbuka mapenzi yetu.” Akaanza Tula. “Yule
mwanaume alikuwa hawezi mapenzi yako, Jax. Hata kidogo.” Akaanza kumsifia hapo
na kumkumbusha waliyoyafanya huku na kule. Mapenzi waliyokuwa wakifanya kwa
kujinafasi na kuridhishana. Shida walizopitia wakiwa pamoja.
Akampamba hapo kwa hili na lile, na kwa
kuwa alimjua Jax ndani na nje alimteka fikra, alikuja kuamka hapo hotelini, asubuhi,
Tula pembeni yake, uchi kama alivyozaliwa. Walifanya mapenzi ya haja usiku huo
bila kupumzika. Jax aliyekuwa amekubaliana na Lara wapumzike penzi mpaka ndoa,
akakatwa hamu vilivyo. Asubuhi yake nayo kabla Jax hajaenda kuoga awahi kazini,
akampa penzi la funga mwaka, ndipo Jax akaondoka. Akili ya Jax ilirudishwa
mbali sana. Kwenye mapenzi yake na Tula.
Jioni alikwenda kwake, akaoga na
kubadili nguo, na kumfuata tena Tula pale hotelini. Walizungumza mengi sana.
Jax alimsimulia maumivu aliyopitia baada yakumuacha. Tula akalia sana akiomba
msamaha na kumuhakikishia kuwa amerudi nchini kwa ajili yake. Anaomba nafasi ya
pili na ya mwisho. Bila kutegemea wakaanza mapenzi tena. Kesho yake ilikuwa
siku ya jumamosi, Jax akawepo hapo hotelini siku nzima na Tula. Wakati wote
Tula alihakikisha anamkumbusha Jax maisha yao ya zamani. Jinsi walivyopendana
na watu walijua.
Kuja kufika siku ya tatu, Jax akaona
atajipunja maishani kama atamuacha Tula aondoke tena. Kwani Tula alimwambia
akimkataa, anaondoka na hatakuja kumuona tena maishani. Jax akaona hataweza
kupitia tena kile kipindi cha upweke bila Tula. Akakumbuka siku nyingi
alizoshindwa kulala sababu ya kumpoteza Tula. Akachukia kuchelewa kupata kazi
na kumpitisha Tula kwenye ugumu wa maisha kiasi cha kusaliti penzi lao. Alimtetea
Tula kwa kila mtu. Kuwa Tula alimvumilia, na yeye kama binadamu akachoka. Kama
wangekuwa hawajapitia kwenye ugumu kwa muda mrefu, Tula asingeondoka nchini.
Hakutaka mtu amseme vibaya Tula wake.
Sasa Tula amerudi. Nini chakuwazuia
tena! Kama ni mapenzi, wawili hao walijua walipendana kiukweli. Tatizo ilikuwa
pesa. Sasa, sasahivi pesa ipo, nini kipingamizi! Kama ni Lara, hata yeye Tula alimwambia
amemuacha mchumba wake karibu kabisa na harusi kwa sababu yake yeye Jax. Hapo
Tula akamwambia maneno mengi akimueleza ile garama aliyolipa kuwa naye hapo.
Lakini akamwambia Jax ilimpasa kulipa garama kubwa hivyo sababu kwanza
aligundua alifanya kosa kumuacha yeye Jax, na pili akamwambia amejua hakuna mapenzi
ya kweli hapa duniani atakayoridhika nayo kama hayo ya Jax. Ikabaki yeye sasa
Jax. Alipe garama ili wawe pamoja.
Kama kawaida ya Tula. Alipoona Jax
anachukua muda mrefu akifikiria, akampanga yeye. Akampa mikakati Jax akimpanga
kwa hili na lile, mpaka yeye Tula akafanikiwa kuongoza mambo yote. Wakahama
pale hotelini na kuhamia kwenye nyumba aliyonunua Jax kwa ajili yake na Lara.
Tena Jax ndiye aliyelipia garama za hapo hotelini tokea Tula anamuita hapo na
yeye kufanya kambi.
Ni kama Jax alihamia hapo hotelini na
hapakuwa na maswali kutoka kwa yeyote yule. Hata Lara mwenyewe japokuwa alikuwa
mjini lakini hakugundua kama mchumba Jax amehamia hotelini, yupo na Tula. Kwani
Lara alikuwa busy na mambo ya harusi, na bado kazini alihitajika kama kawaida.
Na alishamwambia waache mapenzi kwa muda, na akawa hataki vishawishi.
Akataniana na Jax, kuwa kwenda pale nyumbani kwa Jax, ndipo wataishia
kitandani. Waachane kwa muda kumbe ndio kipindi hicho na yeye Tula akamkamata
Jax.
Wakati Lara akiendelea kuvaa magauni ya
shuguli na kufanyiwa sherehe mbalimbali wakingojea shuguli kubwa ya harusi,
akiwa hana wasiwasi kabisa na Jax, kwani kwa asili Jax hakuwa muhuni kabisa,
Lara akawa hana wasiwasi, anaendeleza sherehe kumbe mchumba kahama nyumba, yupo
hotelini na mpenzi wa zamani, Tula. Lakini huku akiwasiliana kwa simu na Lara
pale Lara anapomtafuta.
Kipindi cha mwanzoni wakati akiiba
kotekote kabla Tula hajamzidi nguvu, mida ya mchana ambapo Lara alilazimishia
kukutana, bila Tula kujua, aliweza kukutana na Lara kwa chakula cha mchana
wakiwa kazini, tena kwa muda mfupi sana, Lara ndiye alikuwa akiongea yote bila
kuhisi mabadiliko kwa mpenzi wake. Basi Jax atatulia akimsikiliza tu kisha
anamuaga akimwambia anawahi kazini. Wanaachana na Lara akiwa ameridhika
amemuona Jax, asijue mwenzie akitoka tu kazini na kulala ni kwa Tula, hotelini
mpaka Tula alipomwambia lazima wahame hapo.
Umbali ambao walisharudi na Tula, hapakuwa na muujiza wa Jax kuja kurudi kwa Lara na kuwa mume tena. Akili zilijaa Tula, na Tula hakuwa akijua kuacha mwanya kwa Jax, tokea chuoni. Ndipo Tula ameibuka mshindi tena. Amempata Jax, tena kwa kuvunja ndoa yeye mwenyewe Jax na kumtangaza Tula ndio mmiliki wa nafsi yake.
Kwa Lara.
L |
ara
alitibiwa mpaka akapona. Damu ilikoma, akaruhusiwa kurudi nyumbani. Kwa kuwa
alikuwa kwenye likizo, basi akaamua kupumzika kwelikweli, ila kukaa ndani tu
hata nje hakuwa akitoka kwa aibu. Hawezi kutembea mtaani kwa fedheha. Wengine
wakaanza kumdai mama Chiwanga zawadi zao wakitaka warudishiwe, wakisema kwa
sababu Lara hakuolewa na wao walishachanga na kumpa zawadi, basi wazazi hao
wawe waungwana. Warudishe vitu vya watu. Ukweli Lara alipata zawadi kwenye sendoff
na kitchen party aliyofanyiwa kwao na wanawake rafiki za mama yake, vikundi
vya kina mama wa mtaani, kanisani, kazini kwa mama yake, marafiki waliokuwa
kwenye kikundi kimoja na mama Lara, walitoa zawadi mbalimbali.
Na kwa kuwa ilikuwa ni Dodoma, na bado
hajaolewa, Lara aliacha zawadi zote nyumbani kwao Dodoma. Alimwambia mama yake
hana nafasi ya kuviweka huko Dar. Atakuja kuvichukua watakapopata nafasi kubwa.
Alipotoka hospitalini na kusikia hiyo minong’ono alimuhurumia sana mama yake.
“Samahani mama. Sikujua kama hiyo ndoa haitakuwepo. Nisingewaingiza kwenye
fedheha ya kiasi hiki.” Lara alimfuata mama yake jikoni.
Majuma mawili yalishapita, hata alipotoka
hospitalini yeye alikuwa mtu wa kulala tu. Hata hivyo alikuwa amedhoofu sana. Hata
maji kupita kooni ilikuwa kwa shida. Ilikuwa akilazimishia kila kitu kupita
mdomoni, angalau vifike tumboni asife kwa njaa. Kila kitu kilikosa ladha.
“Lara mama yangu mzazi, hakuna anayepanga
kupatwa na baya. Na wala huna sababu ya kuona haya. Hukuchagua.” Lara akakaa. “Ingekuwa
kuchagua, kila mtu asingekuwa alivyo. Pengine wengine wangekuwa wameshakufa.
Mungu pekee ndiye anayejua siri ya maisha. Kila mtu anapatwa na lake. Lakini
tunaendelea.” Lara akanyamaza.
“Ila nilitaka upumzike, nikuombe kitu
mama.” Lara akamwangalia mama yake. “Naomba turudishe vitu vya watu. Watu
wanalalamika sana.” “Sawa mama.” Lara akakubali bila shida tena kwa haraka sana.
“Lakini mimi siku ya alhamisi narudi
Dar, mama.” Mpaka dada zake wakageuka na kushangaa. “We Lara! Kwa kipi mno?
Huoni haya?” Dada yake mkubwa akashangaa na kushindwa kujizuia. “Nikimbie wapi,
nikajifiche dada Lily?” Lara akauliza swali lilowafanya wote watulie. “Maana kila
anayenifahamu anajua niliachwa. Sasa niende wapi? Siwezi kukosa ndoa na kazi.
Nilikutwa kazini, siwezi kuacha kazi yangu. Halafu nifanye nini?” “Mimi binafsi
nakupongeza Lara. Hongera sana mama. Jax alik...” “Naomba usilitaje jina lake
mama. Tafadhali.” Lara akanyanyuka na kuondoka.
Hata baba yake alimpongeza. Ingekuwa aibu zaidi kama mabinti wote wangerudi kuishi hapo nyumbani. Lily ambaye ni dada mkubwa ndiye huyo alizaa akiwa sekondari na hakujiendeleza tena. Yupo tu nyumbani. Hana kazi wala hana dalili ya kuja kuolewa. Anatunzwa hapo nyumbani kwao yeye na mtoto wake. Haya, Lea naye anayemfuata Lara ndiye huyo mwalimu. Naye anaishi hapohapo nyumbani, kila mwanaume anakasoro, hataki kuolewa. Lara kufanikiwa kuondoka hapo, ilikuwa aghueni. Leo arudi aishi hapo kama dada zake, akaona sio sawa, bora arudi tu kule kulikoungua mpini.
Kimfaaye Mtu, Chake.
Alhamisi.
L |
ara
alitua jijini na kwenda alikokuwa akiishi na wenzake kimyakimya bila kumtaarifu
mtu. Kina Sesi walitoka kazini mida hiyo ya jioni, wakamkuta Lara amekaa nje
akiwasubiri. Wote walifurahi na kushangaa. Wengi walisema atakimbia mji kwa
aibu. “Lara!” Wakamkumbatia kwa pamoja. “Mbona umerudi?” Warda akajikuta ameropoka
na kuuliza na kumshangaza kila mmoja. “Naishi hapa!” Akajibu Lara huku akishangaa
na yeye. “We Warda!?” Sesi na Suzy wakashangaa kwa pamoja. “Jamani! Nauliza tu.
Kwanza kazini si mpaka mpaka...” Akaishiwa maneno. “Naombeni mnifungulie mlango,
niingie ndani.” Lara akasimama. “Sikuwa na nia mbaya jamani!” Kweli Warda
aliropoka tu, hakuwa na nia mbaya. Wakamkonyeza, wakaingia ndani.
Lara aliyekuwa ameondoka, siye huyu.
Lara alirudi kama katoto kadogo. Alikwisha kama aliyetoka kwenye dhiki kali
nchi yenye vita ya muda mrefu isiyo na chakula. Halafu akawa kama mfupi zaidi. Kitu
kilichomfanya aonekane kama katoto na kwa kuwa alisuka yeboyebo akawa mdogo
zaidi.
Siku ya ijumaa, kabla Sesi hajaondoka
kwenda kazini Lara akaamka na kumfuata. “Naomba ukifika kazini, nisaidie
kuingia kwenye simu ya ya ya...” Akanyamaza kwa muda na kuamua kubadili jinsi
ya kuongea. “Nina shida na namba ya simu ya Tula.” Mpaka Suzy akageuka. “Tulaaa,
Tula...” “Ndiyo. Nina shida naye.” Wakabaki wameduaa. “Yaani uingine kwenye
simu ya Ja..” “Naomba usitaje jina lake.” Akamkatiza Warda, akarudi chumbani
kwake. Wakaondoka kwenda kazini, wakamuacha Lara hapo.
Ilipofika kwenye saa nne, Sesi
akamtumia Lara namba ya simu ya Tula. ‘Naomba kuwa
makini kipenzi. Na usinitaje.’ ‘Usiwe na wasiwasi. Ni jambo la amani tu.
Nitakwambia ukija.’ Lara akarudisha hayo majibu. Akakaa na kufikiria. Akamtumia
ujumbe mwingine Sesi. ‘Nakushukuru kuwa na mimi katika
kipindi chote kile kigumu. Nakushukuru Sesi. Mungu akulipe mema.’ ‘Amina.’
Sesi akafurahi sana.
Lara & Tula.
L |
ara
akaamua kumtumia ujumbe mfupi tu Tula. ‘Mimi ni Lara.
Nashukuru kwa kuja kuwa muwazi kwangu. Samahani nilishindwa kukujibu wakati
ule, kwa kuwa nilikuwa kwenye mshituko. Lakini mengi uliyozungumza ulikuwa
sahihi. Kama tunaweza kuonana, ingekuwa vizuri. Nina vitu ambavyo nafikiri vipo
kwangu kimakosa, ni kweli unatakiwa wewe ndiwe uwe navyo.’ Akautuma huo
ujumbe. Baada ya muda mfupi Tula akapiga. “Mimi nipo
tu. Naweza kukufuata popote, nina usafiri.” “Nashauri uje na taksii ili kuweza
kurudi na gari yako.” Tula akatulia kwa muda. “Umenisikia?”
Lara akauliza. “Nikufuate wapi?” “Tukutane Manyanya
kituoni.” “Sawa. Baada kama ya lisaa nitakuwa hapo.” Akajibu Tula
akisikika mwenye mshangao ila furaha. “Sawa.”
Akajibu Lara na kukata simu.
Lara alitoka hapo, akasafisha kidogo
lile gari ndani na nje. Akahakikisha lipo kwenye hali nzuri. Akatoka ili asije
kumchelewa Tula. Alifika kituo cha Manyanya, akaegesha gari nyuma kidogo ambako
daladala hazisimami. Akatoka kukaa nje. Baada ya muda akaona gari nzuri tu,
Tula akashuka. Alikuwa amependeza sana. Kuanzia juu mpaka chini, alikuwa
nadhifu haswa. Alinukia vizuri, pochi safi. Lara akasimama.
“Nashukuru kwa kuja. Nimeona wewe ni
mtu sahihi wa kukukabidhi.” Akafungua mkoba. Akatoa kadi ya gari. “Hii hapa.
Bado sijabadilisha jina. Lipo kwa jina lilelile.” Akatoa funguo. “Na hizi ni
funguo za gari. Zilikuwa mbili. Zote hizi hapa.” Akapokea Tula. Lara akavuta pumzi kwa nguvu. Akainama kwa
muda. Akanyanyua uso, akaona Tula ametulia akimwangalia. Akajifuta machozi. “Na hii.” Akatoa pete ya uchumba. “Nafikiri hii ni haki yako.” Mpaka Tula akatoa
macho. Ilikuwa nzuri sana. Kubwa na ilionekana ya thamani. Tula akaipokea kwa
haraka.
Akabaki amekodolea macho vile vitu
alivyopewa na Lara. Wakatulia kidogo. Mwishoe Lara akaondoka kwenda upande wa
daladala. Akakaa hapo kituoni akisubiri daladala. Tula akapanda ile gari na
kuondoka nayo. Lara alivuta pumzi kwa nguvu mara kadhaa kujaribu kutulia.
Zilipita daladala kadhaa, Lara akishindwa kuondoka hapo kituoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kitu cha kwanza alichofanya Sesi
aliporudi nyumbani ni kwenda chumbani kwa Lara. Alimkuta amejilaza kitandani.
“Gari iko wapi!?” “Nimempa Tula.” Sesi alishangaa sana. “Una wazimu wewe
Lara!?” “Ile gari nilipewa kishika uchumba Sesi. Tula hakukosea. Kwa nini nikae
na kishika uchumba ambao haupo? Ni mali yake Tula.” “Umefanya haraka Lara.
Hukutakiwa kurudisha. Kwa yote aliyokufanyia, bado unamrudishia! Angalau
ungebakiwa nalo kama kifuta jasho chako! Mshenzi..” “Usimtukane.” Lara
akamkataza.
“Na sijakurupuka Sesi. Niliwaza hivyo tokea
nilipokuwa nyumbani. Nikamshirikisha na mama, akaona si wazo baya, ili
kupunguza kufuatwa tena na kudaiwa tena na hilo gari.” Sesi akaumia sana. “Unakumbuka
zile zawadi zote ulizokuwa ukiziangalia kule chumbani kwetu, nyumbani?” “Lara
please! Usiniambie kama na zenyewe unataka kuzirudisha!” “Zimerudisha Sesi.
Watu walikuwa wakiwasimanga baba na mama mpaka nikawahurumia. Wanahisi
niliwatapeli kuwaletea kijana wa uongo ili wazazi wangu wajinufaishe na pesa na
hivyo vitu.” “Jamani wanadhambi!” Sesi akazidi kuumia.
“Sio kosa lao. Kwetu tunahistoria ya
kutokuolewa. Kwa hiyo niliposema mimi naolewa, wengi pale mtaani hawakuamini.
Sasa kwa hili lililotokea, imekuwa kama uthibitisho.” “Pole Lara.” “Asante
Sesi. Nakushukuru. Nashukuru kwa kunisaidi kipindi kile. Pengine isingekuwa
wewe sasa hivi ningekuwa nimepoteza na kazi.” Sesi alizidi kuumia.
“Mungu atakupa mwingine.” “Mmmh! Hapana
Sesi. Nahisi kweli, sio wote tumeandikiwa ndoa kipenzi.” “Acha hizo Lara.”
“Hapana kwa kweli. Hiyo njia nimepita, huko sirudi tena. Kwanza naomba tubadili
mazungumzo. Vipi kazini? Lipi jipya?” Wakaanza kuzungumza hili na lile. Suzy wa
maneno mengi naye akaingia. Akaanza stori. Mara hili na lile, ilimradi yeye
ndio asikilizwe. Warda naye akaingia akijihami. “Umeninunia?” “Kwani umefanyaje
tena?” “Nahisi kila neno ninaloongea nakosea!” Wote wakacheka. Walimjua Warda.
Hakuwa akipenda ugomvi wala kumuudhi mtu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jumatatu Lara alikwenda na wenzake
kazini kama kawaida. Habari kuwa aliondoka akiwa mgonjwa sana, ilienea kila
mahali. Wafanyakazi wengine hawakujua kama wamkaribishe kazini au waseme pole.
Na yeye akaona anyamaze tu. Bosi wao akawa muungwana. Akamuhamishia kitengo cha
nyuma angalau kumuweka mbali na wateja waliokuwa wanajua anaolewa. Maisha yake
yakaendelea kama kawaida.
Ila kwa hakika alibadilika. Lara
akarudi kuwa mkimya sana tofauti na haiba yake ya utundu. Kila mtu pale ofisini
walimjua jinsi alivyo mtundu, maneno mengi ya utani kwa kila mtu. Na ndio maana
kwenye harusi yake, wengi walijitoa sana, wakitaka kumuunga mkono. Lakini Lara
huyu alirudi siye. Hakusikika kabisa kama ambaye hakuwepo hapo ofisini. Kimya.
Hata akisikia watu wakiongea, hatachangia chochote, kimya kama ambaye hayupo
hapo.
Kwenye vikao vya asubuhi kabla ya kazi,
hakuwa akiuliza tena maswali yake ya kiuchozi kwa bosi wao. Kimya mpaka kikao
kinaisha, anakwenda kwenye meza yake ndani, kazi inaanza. Kimya. Wote wakarudia
maisha ya kupanda daladala, hakuna tena gari ya Lara. Asubuhi wakienda kazini
na jioni hivyohivyo, haso ya daladala. Kila mtu alionja uchungu wa kuachwa kwa
Lara kwa namna moja au nyingine. Maisha yakaendelea kimya kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya mwezi tokea arudi kazini, Lara
aliweza kutoka kwenda kula chakula nje. Akaacha kumuagizia Sesi kumletea chakula
pale ndani. Sesi alipokwenda kumuuliza amletee chakula gani siku hiyo,
akamwambia waongozane. Walishangaa kidogo, lakini Suzy akafurahia kutoka na
Lara pia.
Baadhi ya wafanyakazi wa CRDB ambao pia
hula hapohapo, na wenyewe walichanga kwenye harusi yao kutaka kumuunga mkono
Jax aliyekwisha kufanya nao kazi, na Tino rafiki wa karibu wa Jax na mwenyekiti
wa kamati hiyo nao walijua kashfa ya kuachwa kwa Lara walikuwepo hapo siku hiyo
wakitaka kupata mlo wa mchana.
Lara na wenzie walifika hapo, kila mtu
alikuwa akimtizama Lara. Na yeye alijua, lakini akajikaza. “Nitakimbia au
kujificha mpaka lini?” Hayo alishajiuliza
Lara na kukosa jibu lake. Mwishoe akajitia moyo. Hakuwa na pakukimbilia. Ajira
ni ngumu kila mahali. Hawezi kuacha kazi pale. Arudi kwao! Nako hapakaliki.
Heri kubaki alipo.
Wakati wamekaa wanasubiria chakula,
Tino akawasogelea pale mezani. Lara akainamia simu yake kama ambaye hajamuona.
Wote wakajua. Tino akasalimia, Lara akawa kama hajamuona wala kusikia kabisa. Akajiongelesha
hili na lile, lakini Lara hata hakumtizama. Chakula kililetwa, Lara akainamia
sahani yake. Tino akaamua kuondoka. Siku hiyo hata Suzy hakuweka utani.
Tino na Lara walitokea kuelewana sana
kipindi hicho kabla ya kuachwa kwake Lara. Ule ukimya pale na kushindwa hata
kumtizama usoni, Tito akaumia sana. Jioni walipotoka tu kazini, wakati ndio
wanatulia. Warda anapika kama kawaida yake. Suzy, Sesi na Lara wapo sebuleni
wanaangalia kipindi kwenye luninga, Tino akaingia. Safari hii akaamua kabisa
kumsalimia kwa kumtaja jina Lara. “Vipi Lara?” Hata hakugeuka. Akanyamaza
kimya. “Lara!” Kimya. Lara alitulia kama ambaye hakuwa akitajwa jina lake.
Alikuwa amepandisha miguu kwenye kochi dogo, amejikunja, macho kwenye tv.
“Naomba usiniweke kundi moja la
wasaliti, Lara! Mimi sikuwa najua. Na tangia wakati ule hata sijui alipo na
wala hatujatafutana tena. Jax..” Lara akanyanyuka na kuondoka. “Hilo jina
halitamkwi humu ndani wewe Tino! Mbona kama huelewi?” “Sasa mimi nimefanyaje
jamani!?” Tino akashangaa akilalamika. “Alishakuonyesha tokea mchana hataki
kukuona. Halafu na wewe ukaleta kichwa chako hapa!” Suzy akaanza.
“Hawataki nyinyi wala vitu vyenu.
Kasharudisha pete ya uchumba na gari lenu. Achaneni na Lara.” “Subiri kwanza
Suzy. Lara amemrudishia Jax gari na pete!?” “Tumekwambia usitaje hilo jina humu
ndani.” Suzy akamkoromea Tino. “Sawa. Amerudisha!?” “Alimrudishia Tula ambaye
alikuja ofisini kumdai.” “Mungu wangu!” Tino akashika kichwa.
“Lakini mimi nimefanya nini!?” Tino
akaendelea kuhoji akilalamika. Wakasikia mlango wa Lara ukifunguliwa. Akasogea
pale. “Wewe ni mbaya kuliko mwenzako Tino.” Akaanza Lara. Wote wakashituka na
kugeuka vizuri. “Unakumbuka nilikupigia simu kukwambia nina hali mbaya, simpati
mwenzio?” Tino kimya. “Unakumbuka ulinifuata, tukakaa wote kwenye gari?” Kimya.
“Nilikwambia nina hali mbaya Tino. Nikakuomba sana, katafute ukweli ili nitoke
kwenye ile hali.” Lara akaanza kutokwa na machozi.
“Tuliachana tukiwa
tumekubaliana unakwenda kuzungumza na dada Nelly, kisha unitaarifu. Ulivyo
mbaya wewe, ukapata ukweli na kunifungia simu zangu zisiingie kwako. Nilikaa
nikikusubiri huku nikikupigia simu bila kuchoka.” Lara akaendelea kulia. “Hali yangu ilizidi kuwa mbaya, nikajua nikiendelea
kubaki hapa ndani, nitapoteza mtoto wangu.” Kila mtu akashituka zaidi.
“Ikabidi niondoke, kwenda
hospitalini ili wanisaidie huku nikijipa moyo pengine utanipigia simu.
Nilikutwa na pressure juu sana. Wakaniambia kama sitatulia nitapoteza mtoto
wangu. Nikawekewa dripu na kuambiwa nilale pale.” Lara akaendelea kulia kwa uchungu sana.
Kati ya hao marafiki anao ishi nao hapo
hakuna hata mmoja kati yao aliyejua kama alikuwa ni mjamzito. “Nilishindwa kutulia hospitalini. Kwa kuwa simu iliishiwa
chaji, na wewe sikupati, nikajiambia nisipopata jibu siwezi kutulia hata
wangenipa matibabu ya namna gani. Huku nikitumaini utanitafuta Tino. Nilikwambia
kwa machozi, usiniache vile nilivyo. Niambie chochote, nijue jinsi ya
kujipanga. Niliondoka kwa haraka kutoka hospitalini, tena bila ruhusa ya
daktari kurudi nyumbani kuwahi chaji nikijua wewe ndio utakuwa dawa yangu,
mbali na yale matibabu ya pale hospitalini. Kwa ile imani niliyokuwa nayo kwako
Tino.”
“Nilikutafuta bila
mafanikio. Mpaka muda wa kwenda kazini mimi macho kwenye simu, nilikesha
nikikusubiri. Nilikuwa na hali mbaya. Nikakutetea mawazoni mwangu kuwa, pengine
uliishiwa chaji, utakuja kunifuata kazini.” Lara akaendelea akilia. “Ulivyo na roho ngumu wewe, ulikaa kimya, mpaka
nikafuatwa na shemeji yako wa ukweli, Tula. Ukaacha nadhalilika mbele za watu,
Tino! Mimi najua ukweli kwa kupitia shemeji yako, uliyejua usiku uliopita, yupo
na ametulia na ...” Akasita.
“Ulisababisha kifo cha
mwanangu Tino. Ule mshituko wa kusikia kutoka kwa Tula moja kwa moja,
kulisababisha kifo cha mwanangu Tino. Mlimchagua Tula zaidi yangu. Nilikusihi
Tino, tena kwa machozi, nikikwambia nipo kwenye hali mbaya. Nipe ukweli.
Ulishindwa. Wewe na mwenzako, mlishindwa.” Lara akajifuta machozi.
“Kwa kuwa ulishindwa kuwa
msaada mdogo tu kwangu. Nikiwa nimekuomba kitu kidogo tu. Ukashindwa wakati
ule, sitakuhitaji tena Tino. Wewe na lile gari, mnanikumbusha kifo cha mtoto
wangu. Mimba yangu ilitoka kwenye lile gari, ukiwa wewe umesababisha kwa
asilimia kubwa tu.”
Tino akainama. Hapo ndipo kila mtu akaelewa ni kwa nini Lara alilitoa lile
gari.
“Usinitafute,
sitakutafuta. Usinisemeshe, sitakusemesha. Ukiniona, uninyamazie kama usiku ule
uliponinyamazia. Popote tutakapokutana, iwe kama sipo. Ulinifungia kwenye simu
zako, endelea kunifungia. Ukija hapa, njoo kwa ajili ya kina Suzy.” “Hapa tusikuone
Tino. Hata sisi hatutaki salamu yako.” Suzy akadakia. “Na mimi unanijua Tino,
maneno na ngumi mkononi. Haya, nyanyua, ondoka.”
“Lara!” Tino akaita wakati anasimama.
“Nao..” Lara hakutaka hata kumsikiliza, akaondoka. “Haya, mlango ule pale.” Suzy
akaongeza. Tino akaondoka. Wote wakaenda chumbani kwa Lara aliyekuwa akilia
sana. Hasira zilimfanya aongee ambayo hakutaka kuyaongea, akijua yataenea tena.
Kwa Nelly.
Tino alitoka hapo moja kwa moja kwa Nelly,
alifika akiwa anaonekana alikuwa akilia kabla yakufunguliwa mlango. Alimsimulia
Nelly kila kitu. Nelly akaumia sana. “Lakini sikutaka mimi ndio niwe mvunja
uchumba wao, dada yangu. Nilitaka Jax mwenyewe ndio awe wakwanza kuzungumza
naye. Na ndio maana kitu cha kwanza nilichofanya siku inayofuata, nikumfuata
Jax ofisini na kumwambia akazungumze na Lara. Sikujua kama ndio naharibu.
Sikukusudia.”
Nelly akabaki kimya kwa muda. Akamtumia
ujumbe Jax. ‘Naomba kesho jioni baada ya kazi, tupate
chakula cha pamoja.’ ‘Wapi?’ Akauliza Jax bila kupoteza muda. ‘Popote unapotaka. Ila naomba safari hii iwe mimi na wewe
tu.’ Jax akaelewa kuwa Tula hatakiwi. Hakushangaa. Alimjua dada yake.
Nelly Kwa Jax.
J |
ioni
baada ya kazi, Jax akampigia simu dada yake, na kumwambia anaelekea hapo
walipokubaliana kukutana. Na yeye akamwambia hatachelewa. Wakakutana.
Walipoagiza tu vinywaji bila kuchelewa, Nelly akatoa picha ya baba yao na mama
yao. “Unawakumbuka hawa watu?” Akamuuliza Jax. Jax akatizama vizuri. “Huyu si
baba na mama!” “Ewaaa!” Akavuta ile picha. “Sasa huyu. Huyuu!” Akaweka kidole
kwenye sura ya mama yake. “Mama!?” “Huyo ndiye amenifanya kuchukia ndoa,
mahusiano hata na watu wengine wakawaida, na kunifanya niwe hivi kama tembo
niliye jeruhiwa.” Jax akashangaa sana.
Muhudumu akaleta vinywaji, lakini Jax
akabaki akimshangaa dada yake. “Najua hukumbuki maisha tuliyoishi wakati wazazi
wetu wapo hai. Mimi nilikuwa mkubwa. Nakumbuka vizuri sana.” Nelly akanywa wine
yake. “Nakumbuka mpaka nachukia. Kama kuna muujiza namuomba Mungu aje anitendee,
nikusahau maisha yao hao. Zaidi huyu. Maana inanifanya nashindwa kuishi kwa
amani.” “Mama!?” Jax akashangaa sana.
“Yeap. Huyo huyo. Muangalie baba.”
Akamrudishia ile picha. Jax akawa anaangalia huku amekunja uso. “Bwana
mnafanana na huyo mwanaume! Mpaka wakati mwingine nikikukuta umekaa sehemu,
nahisi ni kama yeye amefufuka! Tabia, sura, mpaka sauti! Ni baba mtupu.” Jax
hakujua dada yake anataka kuongea nini.
Akamaliza ile wine kwa mara moja, akamuita
muhudumu tena. Jax akajua lipo jambo. Dada yake hakuwa mnywaji sana zaidi
hakuwa akinywa siku za kazi ambazo kesho yake anatakiwa kazini. Alijaliwa
nidhamu ya kazi ya hali ya juu. Na kazi yake kwake ilikuwa ni kila kitu. Na
ndio maana alipanda cheo kwa haraka na zamani sana.
Ikaletwa wine nyingine. Akanywa nusu.
Jax akimtizama. “Bwana huyo mwanaume alimfanya mama kile atakacho. Kama mpira!
Alimchezea, akamnyanyasa, na kumfanya vile alivyojisikia yeye.” Nelly akanywa
tena ile wine. “Kilichonikera kwa huyo mkewe, nikujifanya kama mjinga!
Akikubali afanywe kile atakacho mumewe.” Nelly akamaliza ile wine yote. Hiyo
ikawa glasi ya pili ya wine kwa muda mfupi sana.
“Unajua hatima ya yote? Namaanisha hatima
ya ule ujinga wa mama?” Jax kimya. “Ni kutuacha sisi yatima, tukinyanyaswa,
tukihangaika hovyo.” Jax kimya. “Baba alihakikisha anamuua mama kabisa.” Jax
akashituka sana. Akamtizima dada yake vizuri. “Aliondoka kwa miaka kama miwili
hivi. Au mmoja na miezi yakutosha kabisa. Hajui kula yetu, wala vaa yetu. Akaja
kurudi baada ya muda wote huo. Na mama naye akamfungulia mlango mpaka kitandani
bila kutufikiria sisi. Na wala hakubadilika. Aliendelea kumnyanyasa mama vilevile,
hata alipokuwa amemuambukiza Ukimwi, hakumjali hata kidogo. Aliugua mama, peke
yake. Mumewe akiendelea na maisha yake ya starehe na uhuni kama kawaida yake.” Nelly
akaomba kinywaji kingine.
“Mbaya zaidi, ndugu wa upande wote,
mpaka ndugu zake baba, walishamtaka mama aondoke pale. Wakimwambia wazi atakuja
kuuwawa, aache watoto. Mama alibaki. Na kweli, hakuchukua muda, alikufa tukiwa
peke yetu. Baba hakuwa hata na muda wakumuuguza.” Wine yake ikaletwa tena. Akainywa
tena mpaka nusu. “Kesho kazini!” Jax akamkumbusha dada yake. Nelly akacheka.
Akamalizia ile wine. Hiyo ilikuwa glasi ya tatu.
“Baba alikuwa mjuaji kama hivyo wewe.
Hakuwa akiambilika hata na ndugu zake. Akaishia kumuua mama. Anyway, siwezi
kusema kwake ilikuwa jambo baya. Kwa kuwa hakujali kifo cha mama.” Akamuita
muhudumu. “Nelly!” Jax akamuita kwa kushangaa anavyoendelea kunywa. Muhudumu
akaja kwa haraka. “Kule unakotoa hizi wine za vipimo, leta chupa nzima.” Nelly
akaagiza. Muhudumu akaondoka, Jax akabaki ametoa macho. Ni Nelly, anakunywa
pombe siku ya kazi! Jax akajiweka sawa.
“Kifo chake na yeye hakikuwa mbali.
Unajua ni kwa nini?” Akamuuliza mdogo wake. “Nitakwambia kile ambacho wengi
huwa hawajui. Alikosa kimbilio ambalo mwanzoni aliliona dhaifu sana. Halifai.
Mama. Pale ambapo alikuwa akikimbilia baada ya kuchoshwa na yale aliyokuwa
akiyatizama nje, kwa kuyathamini kuliko mwanamke aliyemuacha ndani. Alikosa
kile alichokuwa anakipuuza. Yeye hakuugua sana kama mama. Kwanza hakutaka hata
augue, kwa kuwa hapakuwa na wakumuuguza. Ni kama akili ilimrudia pale tulipobaki
sasa, sisi watatu. Mimi nikawa sina muda na chochote isipokuwa wewe na shule.”
Chupa ya wine ikaletwa. Muhudumu akataka kumimina kwenye glasi, Nelly
akamuwahi. Akampokonya.
“Hii itakwenda hivihivi ikiwa kwenye
chupa.” Muhudumu akacheka na kuondoka akiwa anashangaa kidogo. “Baba akaona
ayafanye marefu kuwa mafupi. Bwana yule mwanaume akajinyonga usiku! Bila huruma
akijua sisi bado ni wadogo, na tupo humohumo ndani, akaacha mwili wake
ukining’inia chumbani kwake.” Nelly akamtizama Jax kwa muda.
Wakabaki wakitizamana. Nelly
akaendelea. “Yule mwanaume alihakikisha anamuua mkewe kwanza, ndipo akajiondoa
na yeye. Aliondoka vilevile mjuaji lakini aliondoka akiwa haelewani na yeyote
yule hata mahawara zake.” Akatulia Nelly akimtizama mdogo wake. Jax kimya
akimtizama na yeye dada yake akitaka kujua mwisho ya hayo yote, siku hiyo, yeye
anahusikaje au kwa nini siku hiyo ndio aambiwe yote hayo!
“Sasa nikikuangalia wewe, naona wewe umeanza
mapema sana tena kuliko hata baba. Wewe umeanza kwa kumuua mtoto wako mwenyewe.
Tena bila hofu, kikatili, wala kufikiria, kama baba.” Jax akakunja uso. “Unaongea
nini Nelly!?” “Nafikiri hata baba alikuwa akiwaambia hivyohivyo ndugu zake. Kwa
kuwa alijiamini sana. Sauti nyingine mbali na yeye mwenyewe, hakuwa akizielewa.
Kama hivyo unavyonitizama mimi kama mpuuzi fulani hivi!” “Dada Nelly, sikuoni
wewe mpuuzi! Ila sikuelewi! Ni hivyo tu. Na kama nikuhusu Lara..” “Wala
usimtaje huyo binti kwangu Jax. Acha kabisa.” Jax akashangaa sana. Nelly
akanywa ile wine akitumia chupa yenyewe wala si glasi.
“Kwanza wewe mwenyewe hukuwa hata
ukimpenda Lara! Kwa nini leo unanishutumu vibaya hivyo!?” Jax akalalamika. “Hata
nilipokwambia nimemuacha, hukuongea chochote!” “Kwani uliponiambia unamuoa
nilikwambia lolote?” Jax kimya. “Nakuuliza Jax. Tokea lini umefanya jambo
nililokushauri juu ya maisha yako mbali na shule na ukanisikiliza?” “Sio kweli Nelly.
Mimi mbona nakusikiliza sana tu!” “Nilikwambia nini juu ya Tula kabla na baada
ya kumaliza chuo?” Kimya.
“Nilishauri nini juu ya Tula kabla
hajakuacha na kwenda Norway na mwanaume mwingine?” Kimya. “Ulinipuuza kabisa.
Tula akaondoka. Akaenda kuishi maisha yake huko. Hujui ni kwanini amerudi!
Hujui aliyokwambia mpaka ukamuacha Lara ni kweli au la! Hukutaka hata kujipa
muda wa kuchunguza lolote lile juu yake. Ukampokea kwa mikono miwili! Ukamuacha
kikatili Lara akiwa na mtoto wako!” Jax alishituka, dada yake akamuona
nakumcheka kwa kumkejeli.
“Ulivyo mjuaji wewe. Hata usiombe
ushauri, au kuuliza! Ukampokea Tula kwa maneno yake ya ushawishi na kibabe kwako.
Ninauhakika ukaanza naye mapenzi kavukavu.” Nelly akanywa tena. “Nina uhakika
ulianza mapenzi na Tula bila hata kufikiria madhara yatakayowapata wengine,
kama vile alivyokuwa akifanya baba yako. Ilimradi wewe roho yako yakibinafsi
imepata ulichotaka, basi. Ukasahau madhara ya yule binti ambaye ulibakisha siku
chache sana umuoe. Lara ana wazazi, marafiki, majirani, wafanyakazi wenzake
wanao mzunguka. Hivi hata ulipata muda wakufikiria kwa upande wake?” Kimya.
Nelly akabaki amemtolea macho. “Si..”
“Ile tu kumfikiria yeye kama mwanadamu iliyejulikana kila mahali kuwa anaolewa.
Ukamuacha yule binti ameagwa mpaka nyumbani kwao! Ulinitoa mimi hapa Dar, mpaka
Dodoma! Nikaacha majukumu yangu yote ukiniambia mimi na Tino, Lara ndio mkeo. Nakuuliza
Jax, wakati unamvulia nguo Tula, ulikumbuka hata kama yupo Lara?” Nelly
akauliza tena. Kimya.
“Na mara ya pili na ya tatu je?” Kimya.
“Wakati unamkimbia. Unahama nyumba na Tula, ulikumbuka ulikuwa ukiishi na yule
binti pengine ana mimba yako?” “Si..” “Offcourse hukujua.” Akadakia Nelly kwa
ukali. “Huwezi kujua, kwa kuwa unajiangalia wewe mwenyewe. Peke yako. Kile
unachotaka kufanya ndicho unafanya. Hufikirii yeyote hata watu wa muhimu sana
kwako, kama vile baba!” Nelly akaendelea.
“Ukaua mtoto wako bila hofu! Kijasiri
kabisa, ukimwambia Lara kuwa unarudi kwa mwanamke unayempenda. Uliwezaje Jax!?”
Mpaka Nelly mwenyewe akashangaa. “Yaani mimi huwa watu wananisifu kwa roho
ngumu, lakini sikufikii wewe Jax. Pale uliponiacha siku uliponiambia unamuacha
Lara kwa ajili ya Tula, nilishindwa hata kusimama, mpaka alipokuja Tino! Kwa
ile hofu iliyonikamata, nikimkumbuka baba.”
“Sikutaka kumwambia hata Tino, ila
nilibaki nikimuuliza Mungu, ni kwa nini anamrudisha baba kwenye maisha yangu!?
Nikamuuliza Mungu kama anatatizo la kumbukumbu! Nikamuuliza Mungu kama kweli
amemsahau Nelly na Jax, au ameamua na yeye kunitelekeza! Baya gani nililotenda
kiasi chakumrudisha baba kwenye maisha yangu!” Nelly akamaliza ile wine yote
kwenye chupa.
“Ulijua wazi Tula alimfuata Lara kazini
kwake. Akamdhihaki mbele ya watu waliomchangia kwenye harusi yenu. Niambie
ukweli Jax, hivi hata ilikuuma kweli au ulimfuta Lara kwa kuwa Tino alikufuata
na kukwambia? Kabla hujajibu, nikukumbushe tu pengine ulikuwa mdogo sana hukuwa
unakumbuka. Baba alikuwa akifanya hivyo hivyo kwa mama, na hakuwa akijali, Jax.
Kwa kushuhudia. Alikuwa akitembea mpaka na rafiki za mama. Walimdhihaki mama
vile watakavyo, baba hakujali kama hivyo wewe!” Nelly akaongea kwa kuumia sana.
“Lara ametolewa hapa Dar kurudishwa
kwao, anavuja damu, mgonjwa. Tino ndiye aliyemsindikiza Lara kurudi kwao! Ulipomuacha
Lara pale kitandani ukimwambia umemchagua Tula badala yake, yule binti alipatwa
na shock kama aliyepigwa na umeme. Hakula wala kunywa, ikabidi aitwe mama yake.
Alikuwa akivuja damu, Tino anasema kama ng’ombe aliyekatwa mshipa wa shingo.
Njiani kurudi Dodoma, anasema walikuwa na kazi ya kubadili plastiki alizokuwa
amelalia yule binti, na dripu alizokuwa anawekewa na mama yake. Huku wewe
ukiendelea kufaidi penzi la Tula. Uliwezaje Jax!? Unawezaje hata kupata
usingizi katikati ya hali tete kama hiyo!? Tuseme upande wa Lara hukufahamu. Na
marafiki je!? Uliowahangaisha kwenda na kurudi, mara mbili Dodoma kwa kina
Lara?” Jax kimya.
“Je, marafiki waliotoa pesa zao, na
muda kukuunga mkono kwa mwanamke uliyetuhakikishia wote, anafaa kuwa mama wa
watoto wako?” Kimya. “Wazazi wa Lara nao?” Nelly akaendelea kuhoji. “Nakuuliza
Jax, uliweza hata kuwafikiria au kwa kuwa nafsi yako ilipata unachotaka ikawa basi?”
Kimya. “Jax!?” Kimya. “Utulivu huo mdogo wangu, na uwezo wa kuendelea na maisha
yako kana kwamba hakuna kilichotokea, unawezaje Jax!?”
“Leo Lara anarudi mjini. Akiwa
amekupoteza wewe na mtoto wenu. Anawarudishia gari na pete ya uchumba, hata hujali!
Mnapokea kila kitu na unabaki kimya kama hakuna kilichotokea?” “Gari lipo kwa
Lara! Nilimpelekea mpaka na kadi ya gari! Nikamruhusu abadili iwe kwa jina
lake. Na nilizungumza na Tula, kumuonya asiwahi kurudi tena kwa Lara.” Nelly akamtizama
kwa kumsikitikia. “Kweli dada yangu, sidanganyi. Gari ipo kwa Lara, sijachukua.”
“Najiuliza. Kama hili hulifahamu! Na mnalala naye kitanda kimoja! Ni mangapi
huyafahamu juu yake!?” Jax akakunja uso.
“Jax? Mangapi huyafahamu juu ya huyu
Tula aliyerudi tu, akakutoa katikati ya mipango mizito kama ile, ukakimbia
naye, bila kufikiria? Kama amefanikiwa kukutoa kwenye jambo zito kama hilo.
Macho ya wengi ya kikutizama. Ukiwa umevunja mioyo ya wengi. Mpaka kumwaga damu
ya mtoto wako mwenyewe, unafikiri atakubadili na kukutoa kwenye mangapi?” Nelly
akaongea kwa kuumia sana.
“Namuomba Mungu, anisamehe kwa kile
nilichokosa jamani! Hata kama ni kosa la kuzaliwa na wale wazazi, pia anisamehe.
Lakini asimrudishe baba kwenye maisha yangu. Sitaweza tena Jax. Muda wote
nilivumilia yoote, nikijua nakuza mtu ambaye atakuwa na mimi maishani. Kama
wewe ukiwa ndiye baba, hakika Jax, sitaweza. Ni heri nitangulie ili nisije ona
kile alichopitia mama, kwa mwanamke mwingine kupitia wewe Jax.” Nelly
akasimama. Akachukua pochi yake, nakuondoka bila kula.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Duuuuuuuu ni hali tete sana,bora Nelly amesimama kama dada
ReplyDelete