Jumamosi Ya Naya na Joshua.
![]() |
Jumamosi Ya Naya na
Joshua.
Jumamosi
asubuhi Naya alikwenda kazini kama kawaida. Akajikuta wa kwanza vilevile.
Hakukosa kazi. Akaanza bila kutumwa na Jamal. Akafanya kazi mpaka saa mbili
kasoro wakaanza kuingia wenzie. Ilipofika saa mbili na dakika tano, wakiwa
wafanyakazi wenzie wapo hapo, wakamsikia Jamal na viongozi wenzie wanakuja
wakishangilia na kubishana. Ile kelele ikaendelea kuja mpaka wakaingia pale
ofisini. Mpaka Njama alikuwepo. “Eti Naya! Naya!” Naya akageuka.
“Aliyekaribia jibu lako kati yetu ni nani?” Ikabidi tu Naya acheke. “Sema
usiogope ili tujue anayerudi leo shamba akalime nani, atupishe mjini
tufanye kazi ya masoko sisi.” Jamal akasisitiza wote wakisubiria. “Na sio
umpendelee Jamal kwa kuwa ni bosi wako.” Naya akazidi kucheka akishindwa kujibu
kwa hofu.
“Haya
Njama, ondoa kiwingu chako hapo na hiyo timu yako wote, Naya afanye kazi.” Wote
wakashitukia Joshua amesimama nyuma kwenye sehemu ya kuingilia hapo. “Ni mambo
ya kazi tu.” Akajibu Njama lakini akiondoka. Naya akachungulia katikati ya
waliokuwa wamesimama pale mbele ya meza yake, macho yakagongana na Joshua.
Akamfanyia ishara kumuita, akimtaka amsogelea kwa haraka. “Kwema lakini
Kiongozi?” Jamal akamtupia neno wakati akipita. “Ni asubuhi sana kwa mabishano
Jamal! Hudhani hivyo?” “Mimi nilikuwa namshauri Njama, kazi za mjini
zimemshinda, arudi shamba tu akalime, aachie meza kwa wanaoweza kuitumia,
nashangaa Njama ananigeukia mimi, eti mimi ndio natakiwa kuwahi shamba wakati
Naya alisema kabisa, jibu lake limeendana na langu!” Joshua akacheka na kumpita
Jamal kwenda kwa Naya.
“Leo
unanukia tofauti Joshua!” “Daah! Nimebadili pafyumu kwa ajili yako Naya!” Naya
alicheka mpaka akainama. “Kwa nini!?” “Mimi mpaka nikasema ile pafyumu ya
mwanzoni pengine hujaipenda wakati mpaka Fina huwa ananisifia na ile pafyumu
lakini sijawahi kukusikia hata ukiongelea kama nanukia!” Naya alicheka sana.
“Joshua wewe!” “Kweli. Nikaona kwa nini nijitese! Nimeanza kutumia nyingine ili
tu uipate harufu nzuri.” “Pole Joshua. Naipenda ile pafyumu pia. Inanukia
vizuri, imetulia mpaka kwenye gari unaloendeshwa pia ipo harufu yako. Na
nimeipata hiyo harufu hata ofisini kwako jana usiku. Nzuri sana.” “Sasa ipi
ndio ipi?” “Zote nzuri.” “Daah! Kumbe nisingehangaika! Yaani hii nimeifuata
asubuhi hii ndio maana nimechelewa kuingia kazini.” “Jamani Joshua! Pole.” Naya
akashangaa sana asiamini kama Joshua anajali vile anavyomuona. Naya akasimama
na kwambia asogee.
Joshua
akacheka akijua anataka kumnong’oneza. Na kweli. “Napenda kila kitu chako.
Kuanzia utosi mpaka unyayo. Hakuna kitu natamani kibadilishwe kwako, Joshua.
Nakupenda hiyo ulivyo. Wewe ni zaidi ya ningeomba Mungu anipe. Upo zaidi ya
maombi yangu.” Kisha Naya akambusu shavuni. Joshua akafunga macho na kupumua
kwa nguvu. Naya akacheka taratibu. Akafungua macho na kumkuta Naya
akimwangalia. “Kwa hiyo sihitaji kujenga misuli?” Joshua akauliza kwa sauti ya
chini sana lakini Naya alimsoma midomo yake akaelewa na kushangaa sana.
Ndipo
akakumbuka ile ni harufu ya pafyumu ya Malon. Akakumbuka Joshua alimuona Malon
vile alivyo, kifua kikubwa, mikono ya misuli, ndio akili zikamjia Naya kuwa
anataka kumuiga, ajibadilishe awe kama Malon. Naya akakunja uso akitingisha
kichwa kukataa kabisa. “Hapana Joshua! Hata kidogo! Na isiwe kwa ajili nyingine
yeyote ila kupenda kwako wewe na unao muda. Mimi nakutaka hivyo ulivyo.”
Akamuona kama amepata aghueni.
“Nakupenda
Joshua.” “Unafikiri baba Naya na kaka zako watanipokea?” Naya akamcheka na
kushindwa kujizuia. “Kweli unanicheka Naya?” “Kumbe ndio hofu yako hiyo?” “Acha
basi kucheka Naya!” Wakajisahau kama wapo mbele za watu. Na Joshua ni kiongozi
mkubwa sana hapo, na anaheshimika. “Naya?” “Acha nifurahi kwanza.” “Ujue
unapoteza muda wa kazi, Naya!” “Mimi mwenzio nimemaliza kazi zote za leo, tokea
saa mbili kamili. Hapa namsubiria Jamal anipangie nyingine. Acha nifurahie..”
“Hofu yangu?” Akamalizia na kumfanya Naya azidi kucheka. “Sawa bwana!” Joshua
akawa anaondoka Naya akazidi kucheka. Mwishoe akamkimbilia koridoni.
“Pale
nyumbani, wanachotaka niwe na furaha tu. Kwanza familia yetu ni ya kawaida mno.
Hawana makuu. Ila baba ni mkimya mno kama Zayoni mdogo wetu wa mwisho na
wamefanana. Mimi na Bale, ni kama tulizaliwa mapacha. Tunafanana mpaka kidole
kidogo cha mguu, na tupo kama mama, mpaka urefu na hii rangi yangu ya mwili.
Angalau mimi na Bale ndio huwa utakuta tunazungumza na kuleta fujo pale ndani,
ila si Zayoni. Zayoni mpole sana na mkimya.” “Na baba Naya?” “Wewe si unajua
kusoma watu?” “Sana.” “Basi si baba Naya. Mimi najua mabadiliko yake kwa jinsi
atakavyonitizama. Na ni kwakuwa nimekua mikononi mwake. Tena wakati mwingine
unaweza usijue kinachoendelea ndani yake mpaka aamue kuzungumza. Mkimya wa
kupitiliza.”
“Kulikuwa
na Joshua mwingine. Yeye mama alimpenda, akataka niolewe naye.” Naya
akamsimulia juu ya Joshi kwa ufupi sana, Joshua akabaki haamini. “Haiwezekani
Naya.” “Nikikwambia nimepita Joshua, amini nimepita kwenye safari ya mapenzi.
Naona Mungu amemuhurumia baba yangu na kuamua kukuleta kwangu. Baba alikuwa akiniombea
sana. Nikikwambia sana, mpaka kufunga na kuomba akimsihi Mungu aingilie kati
swala langu la mahusiano, akihofia nisije nikaangukia kwa mwanaume asiye sahihi
sababu ya pressure ya mama, nafikiri na Malon pia alichangia. Nakumbuka siku
moja nikiomba naye, baba alilia akimsihi Mungu anitetea na kumkatalia shetani kuwa
mimi sio kiwanja chake chakuchezea. Au kufanyia mazoezi. Niliumia sana Joshua.
Sana.”
“Lakini
turudi kwa haiba yake. Katika yote hayo, baba hakumsemesha Joshi mpaka
aliponiacha mjini. Wakati mwingine kabisa ile nilikwambia aliniletea makaratasi
ya chuo cha huko nje ya nchi, ndipo baba alimwambia maneno machache tu.”
“Alimwambia nini?” “Alimwambia siku aliponiacha katikati ya jiji, tena usiku,
alifanya kosa kubwa sana. Akamwambia ni heri angempigia simu, aje anifuate baba
mwenyewe, kuliko kunitelekeza. Hivyo tu. Basi. Ila vinginevyo baba ni mtu mzuri
sana. Usigope hata kidogo. Ila usile, Bale anaandaa chakula cha mchana kwa
ajili yetu wote.” “Bora umeniambia.” “Acha mimi nirudi kazini. Nimefurahi
umekuja kuniona.” Joshua akacheka na kuondoka. Naya akarudi kuendelea na kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mchana
Naya alitoka na kurudi nyumbani moja kwa moja. Joshua alimwambia na
yeye ni lazima arudi nyumbani, ajiandae kwa safari yao kabisa ili wakitoka
nyumbani kwao, waende huko alikopanga kumpeleka Naya. Naya alifika nyumbani
akakuta nyumba safi, kumepangwa vizuri mpaka meza iliwekwa kama hotelini,
wakatoa vyombo vizuri vya mama yao. Na kunanukia harufu nzuri ya chakula. Na
kwa kuwa Naya alishamwambia Bale kuwa huyo Joshua anampishi maalumu wa
kumpikia, Bale naye akahakikisha anatendea haki huo mlo.
“Nawashukuru
sana. Asante Bale. Asante Zayon. Na baba umependeza sana. Wote mmependeza, mpo
wasafi.” “Wote tulienda kunyoa nywele.” Zayoni akaongea, Naya akacheka.
“Asanteni sana. Joshua atafika hapa baada ya lisaa. Na mimi nataka nijiandae
ili akija anikute tayari. Tule, tuondoke.” Bila kusubiri jibu, Naya akakimbilia
chumbani kwake. Bafu lilikuwa moja tu nyumba nzima. Wakamuona anatoka kwenda
kuoga akikimbia.
Joshua
Ukweni.
Baada
ya lisaa wakaona gari nzuri sana inaingia hapo. Naya alikuwa kwenye simu
akimuelekeza mpaka akafika. Akatoka kwenda kumpokea. Akashuka akiwa na chupa ya
kinywaji mkononi. “Naya wewe ni mtaalamu! Angalia jinsi ilivyopendeza!” “Kweli
Joshua au unanitia tu moyo?” “Labda uniambie kama sijapendeza. Lakini mimi
nimependa mno. Katika kuvaa, nisingekudanganya Naya. Mimi napenda kuvaa vizuri
na huwa najua vitu vizuri.” Naya akacheka. “Na wewe umependeza sana. Isingekuwa
ni wewe, kweli ningekusahau.” Naya alicheka sana. Joshua akamsogelea pale
karibu na mlangoni maana alianza kuongea tu aliposhuka garini.
“Kweli
umetutendea haki. Na nimependa hii linen. Safi sana. Kuanzia leo hii ndio
itakuwa kazi yako. Kuhakikisha tunatoka vizuri.” “Kweli Joshua?’ “Kabisa.” Naya
akacheka. “Sasa hiyo uliyobeba ni nini?” “Kinywaji tu.” Naya akampokea na
kumshuru.
“Karibu
nyumbani kwetu. A humble home. Karibu sana.” “Asante kwa ukaribisho.”
“Twende nikakutambulishe kwa baba Naya.” Joshua akacheka. Akamshika mkono
wakaingia ndani.
“Baba,
nimekuletea Joshua.” Joshua akacheka huku akimsogelea kwa heshima. “Sijui kama
unanikumbuka?” “Nakukumbuka sana.” Wakapeana mikono. “Shikamoo mzee wangu.”
“Marahaba Joshua. Naona mmevaa vyakufanana.” Joshua akacheka. “Kazi ya Naya
hii. Mungu amempa kipaji cha ajabu sana. Acha nikuibie siri.” Akaanza Joshua
wakiwa bado wamesimama.
“Jana.
Yaani jana tu jioni. Ile kampuni imemfahamu Naya ambaye hawakuwahi kumfamu
kabla. Sijui kama amewasimulia?” “Siku hizi kumpata Naya nishida! Anakuwa
chumbani muda wote.” Naya akacheka na isivyo kawaida wakashangaa anajificha
nyuma ya Joshua kwa cheko la furaha na aibu na si kwa baba yake. Wote
wakacheka, Joshua alipomchungulia kule nyuma yake. “Kulikuwa na kikao jana.”
Joshua akaendelea. “Cha viongozi wa ngazi ya juu wa kitengo chetu cha masoko na
watu wengine baadhi nilitaka wawepo kutoka idara ya stoo. Nilijua Naya
ameshaondoka kurudi nyumbani. Katikati ya kikao nikapata ujumbe wake ndipo
nikajua yupo pale kazini. Nikaomba kumuona. Kufupisha habari akajikuta ameishia
kuwa kwenye kile chumba cha mkutano.” “Nikakalia kiti cha Joshua Kumu.” Naya
akaongeza wote wakacheka.
“Tulikuwa
tumekwama kwenye swala fulani la kikazi. Tulikaa hapo muda wote, hakuna mtu
aliweza kutoa jibu nikaridhika na mimi nilitaka kufika alhamisi niwe
nimefanikisha jambo fulani. Kama utani tu. Nafikiri ulikuwa wakati wa Mungu
kujipatia utukufu kupitia Naya au ulikuwa wakati wa Naya kung’aa. Nikataka na
yeye atuambie ni kwa nini tuko pale na tumekwama wapi. Baada ya wote kukwama,
nikamuuliza yeye, akiwa tena amekaa pembeni kabisa. Na nilimpa ipad yangu
aandike, lakini nikiwa najua itamsaidia kusogeza muda wakati akinisubiria.”
Wakamuona Joshua akicheka.
“Naya
alijibu ile hoja, mpaka nikahofia pengine wangefikiri nilishazungumza naye,
nikampa yale majibu.” Wakacheka wote. “Kweli Joshua. Na mimi niliwaza hivyo
hivyo.” “Lakini uzuri uliponiambia upo ofisini, nikashangaa na kumuuliza Jamal,
kuwa Naya anafanya nini ofisini mpaka sasa na huwa ngazi za kina Naya hawalipwi
overtime! Akanijibu kwa kujigamba tu, kuwa ndio nielewe anaposema safari
hii amepata jembe, ndio hivyo. Kwamba Naya ni jembe ambalo
halibakishi jani.” “Acha masihara Joshua! Jamal?” Naya akashi
“Hakika alisema tena kwa sauti bila kuogopa
mbele yetu wote na wale watu wa stoo walikuwepo. Wakadhania anaongea vile kwa
sababu nilikuwepo, anakusifia tu. Sasa ulipokuja pale, bila mimi kuweka
mipango, na ukajibu vizuri vile, ilikuwa kero kutoka kwa Jamal. Alipiga kelele
pale. Nasikia akaendeleza yeye kikao, akisema yale uliyozungumza wewe ni kwa
niaba ya kitengo chenu. Acha ajibebee utukufu, ndio maana leo asubuhi walikuja
kubishana pale mezani kwako.” Naya akacheka kwa furaha.
“Ninachotaka
kusema ni kuwa, una binti mwenye akili sana. Za kufikiria kwa kiwango cha juu
sana. Jana mimi nilijivunia kumfahamu Naya.” Wakacheka. “Nashukuru
kunikaribisha. Naamini wewe ni Zayoni.” Akampa mkono na kumsalimia. “Na wewe
ndiye pacha wa nje wa Naya, Bale.” Wakacheka. “Kweli mmefana sana. Kama
mapacha!” “Karibu sana Joshua. Hapa ndio nyumbani kwetu.” Bale akamkaribisha
kwa heshima zote. “Nashukuru sana.” Wakapeana mikono. “Naya ameniambia upo hapo
chuo kikuu cha Mlimani.” “Namalizia mwaka wa mwisho. Tupo ukingoni kabisa.”
“Hongera sana.” “Naya ameniambia na wewe umemaliza shahada yako ya tatu.”
Joshua akacheka na kumtizama Naya.
“Ndiyo,
lakini mimi nilianzia chuo kuanzia ngazi ya chini kabisa, certificate.” Wote
wakashangaa. “Joshua! Sikujua!” “Ndio maana nakwambia namfahamu Jamal. Alikuwa
kiongozi wetu chuoni. Mkali hivyohivyo. Lakini wakati Jamal anafanya advance
diploma, mimi ndio nilikuwa nikisoma mwaka mmoja, tena mambo ya stoo tu nikiwa
na matokeo yasiyo mazuri ya kidato cha nne. Ndipo nilipokutana na Jamal.
Nimepambana mpaka kupata hizo shahada tatu.” “Ndio maana Jamal alikwambia uache
kusoma sasa, unawatia ubaya!” Joshua akacheka. “Kumbe unakumbuka?” “Nakumbuka.
Wakati tukitokea Mbeya.” “Basi ndio hivyo. Na wewe Zayoni?” “Na mimi najiandaa
kumaliza darasa la saba.” “Vipi lakini?” “Ninauhakika nitafaulu tu.” Wote
wakacheka. “Saafi sana.” Joshua akampongeza.
“Joshua
ameleta na hiki kinywaji.” Naya akaingilia. “Asante sana.” Baba yake
akashukuru. “Kuna vitu vingine kwenye gari, labda tutasaidiana na Bale kutoa.”
Naya akakunja uso akimshangaa huku akicheka. “Umeleta nini tena?” “Vyakula tu.”
“Usinge hangaika Joshua!” “Ni kweli, usinge hangaika.” Akaongeza baba Naya kwa
Naya. “Sio usumbufu hata kidogo mzee wangu. Nimefurahi mmenikaribisha. Kwangu
huu ni muujiza, nyinyi mnaweza msielewe. Lakini...” Wakamuona amepoa.
“Nashukuru mmenifungulia milango ya nyumbani kwenu. Nashukuru sana.” Naya
akamshika mkono. “Karibu. Na sisi tumefurahi umekuja.” Joshua akamwangalia na
kumrudishia tabasamu. Pakatulia. Naya na Joshua wakiangaliana na wengine
wamebaki wamesimama.
“Labda
tungekaa mezani. Naya alisema mna safari.” “Ni kweli.” Akajibu Joshua.
“Mmependeza sana. Niwapige picha kabla hamjala?” Akaanza Zayoni. “Mimi ni mpiga
picha mzuri. Naya anajua.” Wote wakacheka. “Kweli Zayoni ni mpiga picha mzuri.”
“Basi acha nikupe simu yangu ili nibakiwe nazo mimi. Ndio nitawatumia.”
“Nitatumia na kamera yangu pia. Naya alininunulia.” Zayoni akakimbilia ndani.
Akatoka na kuanza kazi ya kuwapiga picha Naya na Joshua. Kwa hakika
walipendeza, kisha akamwambia na baba yao aungane nao, pamoja na Bale. Kisha
akategesha kamera na yeye akaongezeka.
“Kweli
wewe mtaalamu.” Joshua akampongeza. “Basi Naya atakuletea na za kwangu ni
kiprinti ili uone.” “Hapo utafanya vizuri. Na ikiwezekana uniwekee kwenye
albumu kabisa ili iwe kumbukumbu yetu.” “Sawa. Nitafanya hivyo.” Zayoni
akaafikiana naye.
Wakakaa
mezani wote watano. Naya akamsaidia kumpakulia. Hilo nalo likamfurahisha sana
Joshua. “Asante sana Naya. Nashukuru.” Wakaangaliana wakati Joshua akishukuru.
Wakaanza kula. “Kweli Bale unajua kupika vizuri sana.” “Asante. Mama
alinifundisha tokea mdogo zaidi ya Zayoni. Nafikiri sababu yakupenda kumfuata
kila mahali. Michezo yote nilikuwa nikicheza karibu yake, nafikiri ndio maana
nikajua mambo mengi ya jikoni.” “Saafi sana. Hii ni ajira ya mtu kabisa!” Bale
akacheka wakaendelea kula.
“Wewe
Joshua wazazi wapo wapi?” Akaanza baba Naya. Joshua akameza kwanza.
“Kwa jibu fupi tu, ni kwamba walifariki. Nikiwa mdogo tu.” “Pole sana. Kwa hiyo
ulilelewa na ndugu tu?” Joshua akacheka na kuinama kama anayefikiria. Kisha
akacheka tena. “Hapana mzee wangu. Mama alipofariki nikiwa ndio nimemaliza
kidato cha nne tu, ndugu wa upande wa mama, ambako ndiko nilikokuwa huko
nikimuuguza mama mpaka kifo chake, walinitaka niende kwa baba yangu ambaye na
yeye alikuwa na familia yake. Nilikuwa mtoto ambaye familia yake hata hawakuwa
wakinifahamu kuwa nipo.”
“Kwa
hiyo nilikwenda wakati mbaya. Baba naye alikuwa akiugua, walijua asingepona.
Uwepo wangu pale kwa wakati ule ukatafarisiwa nipo pale kwa ajili ya mali. Kwa
hiyo mkewe baba na watoto wake, hawakutaka kabisa niishi pale. Sidhani
hata kama nilimaliza mwezi, na wao wakanifukuza rasmi.” “Pole sana Joshua.”
Naya akamuhurumia, akamshika mkono ambao hakuwa akitumia kula. Joshua
akamwangalia na kucheka. “Asante.” “Pole sana Joshua.” Na Zayoni pamoja na baba
yake wakampa pole.
“Si
ungerudi kule kwa ndugu wa mama?” Akauliza Zayoni akimuhurumia
Joshua. “Nilifanya hivyo Zayoni, lakini nako nilikuta milango ilishafungwa. Sikupokelewa.
Nilimwambia Naya, kwangu mimi Mungu siye wa kwenye bibilia au Mungu anayekaa
kanisani. Hapana. Kwangu Mungu ni baba kama hivyo Zayoni unavyomuona baba Naya.
Amenitoa kwenye hatari nyingi sana mtaani. Ikiwemo hatari ya kutaka kubakwa,
kuuwawa kabisa kwa kuwa nilikuwa nikiishi mtaani tu. Niliteseka sana mpaka
alipoona yeye inatosha, ndipo akaninyanyua na kunipa sehemu ya kuishi.” Wote
walipoa wakimwangalia.
“Nilifika
mahali, nilibakiwa na Mungu tu. Nazungumza naye kama hivi nyinyi
mnavyozungumza hapa ndani. Sikuwa na mtu wala kitu. Pesa aliyonipa baba kwa
siri wakati nafukuzwa nyumbani kwake na mkewe na watoto wake, ndizo
zilizonisaidia kulipia hicho chuo cha mwaka mmoja. Nikasomea mambo ya stoo
ambayo sikupata ajira. Ndipo nikarudi mtaani. Nikisema niliishi mtaani,
namaanisha kulala nje kabisa. Huko ndiko nikakutana na mengi, lakini katika
rehema za Mungu, nikapata kazi kwa mtu fulani. Kama mesenja tu.”
“Lakini
Mungu ameweka ndani yangu kipaji kama cha Naya. Wakati namfanyia kazi yule
mzee, nikijua kabisa kitu nilichosomea kitasumbua kazi, nikaanza kujifunza
biashara yake. Kwa kuwa nilikuwa mtu wa kutumwa tu, nilikuwa nikiingia kila
idara ndani ya ile ofisi. Ikanirahisishia kujua kinachoendelea kwenye ile
kampuni. Ilikuwa ndogo tu.” Joshua akanywa kinywaji chake na kuendelea.
“Siku
moja wakati nampelekea kahawa ofisini kwake, nikamwambia hivi, nina njia ambayo
itamsaidia kubadili historia ya biashara yake. Lakini kwa sharti ya kwamba,
anipe pesa ambayo nilishapigia mahesabu ni ada ya shule ya mambo ya masoko. Ila
kwa miaka miwili sasa. Maana tayari nilikuwa na certificate. Kwa hiyo
nikamtajia hiyo pesa yote. Akahisi kama nimechanganyikiwa. Nikafanya sawa
kabisa na kama alichokifanya Naya jana pale kikaoni. Nikamtajia tatizo
alilonalo pale kwenye ile kampuni. Nikamwambia ninayo suluhu sahihi kabisa la
hilo tatizo la kampuni yake. Sitampa mpaka aiweke hiyo pesa kwenye
akaunti yangu ya benki. Nikamuhakikishia sitaitumia mpaka afanikiwe. Na
nikamwambia asipofanikiwa, nitarudisha pesa yote kama alivyoiweka.” “Joshua!
Alikubali?” “Hakuwa na jinsi Naya. Maana nilimweleza mambo ambayo hata yeye
hakuwa akiyajua. Sema na yeye alifariki miaka michache iliyopita, ila alikufa
tajiri.” “Ulimsaidia?” Naya akauliza. Joshua akacheka. “Na yeye alinisaidia.
Ndio ukawa mwanzo wakurudi tena shule.”
Joshua
akaendelea. “Naya, sikuwahi kusoma kama kipindi kile. Hapo nikijua shule
ndiye atakuwa mkombozi. Hakuna somo au mtihani ambao sikupata zote.” Wote
wakacheka. “100?” Zayon akauliza akicheka. “Kabisa. Nikisema kupata
zote, namaanisha zote na si kwakukisia! Ni kwa kujua haswa. Na ndio kwa mara ya
kwanza nikaweza kurudi kulala kitandani, baada ya karibia mwaka mzima
wakuhangaika mtaani. Yaani kurudi kulala kwenye vitanda vya hosteli.”
“Hostel!?” Naya akamshangaa. “Acha Naya. Nimelala mpaka msikitini mimi.
Kanisani kwenye viti, tena kwa kujificha ili nisifukuzwe, maana sikuwa na
jinsi.” Daah!” Bale akashangaa.
“Basi
kuanzia hapo nilipomaliza hiyo miaka miwili, huyohuyo mzee akanisaidia
kuniunganisha na kijana wake, alikuwa akifanya kazi benki. Na mimi nikapata
hapo kazi kama Benk Teller tu. Wale wagawa na wapokea pesa. Lakini kile
nilichokuwa nikijisikia ni kama hivi anavyosema Zayoni, nilijua kwa hakika mimi
ni nani.” Zayoni akacheka.
“Nilijua
kwa hakika pale napita tu. Si sehemu yangu. Na nikajua mimi ndio nina hatima ya
lini natakiwa nitoke pale. Mnajua SWIFT?” Wote wakaangaliana. “Ni njia
yakuhamisha pesa kimataifa. Sasa hivi nafikiri mabenki mengi sana wanayo. Sasa
ile ni mimi ndiye mwanzilishi.” Wote wakamshangaa sana. “Hakika. Sijisifii,
lakini ndiyo ilinitoa pale na kunisogeza kwenye kitengo cha masoko. Nilikaa
pale nikipokea tu pesa huku nikihesabu kwa siku benki inapoteza kiasi gani cha
pesa kwa wateja wanaokuja kuulizia hiyo huduma ya kutuma pesa nje ya nchi na
kuambiwa hakuna, kisha wanaondoka na ile pesa. Nikaipigia mahesabu huku
nikimuomba sana Mungu kwa kufunga na kuomba anipe kibali maana niliambiwa na
mama, amenirithisha roho ya kukataliwa kama yeye. Sijui kama hicho kitu
nyinyi mmeshakisikia.” Baba yake Naya akawa anajua anachozungumzia.
“Basi
nahisi na mimi nilikuwa nayo hiyo roho. Nilifukuzwa na hata watu wanaopokea
kila mtu! Ikabidi kupambana magotini nikimsihi Mungu anitetea. Nilipokamilisha
uchunguzi juu ya SWIFT, nikaomba kikao na meneja masoko mkuu wa pale pamoja na
wasaidizi wake.” “Kwa nini sasa?” “Sikutaka tuje kuwa wawili tu, halafu aje
anigeuke baadaye aseme ni wazo lake. Sijui kama unanielewa?” “Unaakili wewe!”
Wakacheka.
“Nilishawajua
binadamu. Na mimi nilijua hiyo ndio tiketi yangu yakutokea ambayo Mungu
amenipa, nilijua nikichezea tu, sitatoka. Wakiwa hawajui
ni nini nataka, ila tu kuwaambia jambo zito. Kiongozi wangu wa tawi
akanilazimisha sana nimwambie lakini nilikataa kabisa. Nikaitwa makao
makuu. Nikakuta mpaka wazungu wapo hapo. Bwana wakati wa Mungu ukifika, umefika
tu. Halafu huyu Mungu, jamani haitaji jopo la watu kumsaidia kukamilisha ajenda
yake.” Joshua akacheka na kutingisha kichwa. Akatulia kidogo. Wote kimya.
“Hapo
nilikuwa nimeshafanyia mazoezi jinsi ya kuzungumza. Ilikuwa kila nikirudi
nyumbani kutoka kazini, nafanya majaribio kuwa nimesimama mbele za watu wengi,
nazungumza.” “Joshua!?” “Hakika Naya. Vile unavyoona naweza kuzungumza mbele ya
watu kwa ujasiri, nikujifunza. Nilijifunza kuzungumza kingereza mimi mwenyewe
kwa kuwa nilisomea shule za kawaida kabisa. Na kidato cha nne nilimalizia shule
ya kijijini nikiwa nimerudi kumuuguza mama. Sikupenda vile walivyokuwa wakimuhudumia
mama yangu. Nikaamua kurudi nyumbani kwao, nisomee pale ili tu kumsaidia.”
“Maana
mama aliposhindwa kulipa kodi na mambo mengine mjini, akiwa mgonjwa akaamua
arudi kwa wazazi kijijini, mimi akaniombea niishi kwa rafiki yake mjini ili
nimalize shule. Nilipokuwa likizo nikaenda kumuona, sikupenda hali niliyomkuta
nayo. Alikuwa mgonjwa halafu na masimango mengi mno. Nikaamua kubaki naye ili
kumuuguza ndipo nilipomalizia shule huko. Kwahiyo kingereza unachosikia
nakizungumza Naya, ningekijua wapi kama si Mungu kunifundisha?” “Aisee!” Naya
akashangaa.
“Nilikuwa
nakula mara chache sana sababu yakufunga na kuomba. Halafu nikirudi tu
najifungia chumbani naanza kufanya mazoezi ya kuzungumza. Naweza nikarudia hoja
niliyoandika hata mara ishirini kwa siku moja, nikiiongea kwa kichwa bila
kusoma. Hivyohivyo huku nikijiambia siku Mungu atakaponifungulia tu mlango
wakaniita kwenye kikao na kunisikiliza, hawataweza kukataa. Na kweli. Niliingia
pale nikiwa sijala siku tatu. Nimefunga. Nilijawa ujasiri ambao haukuwahi
kuondoka. Nilizungumza mpaka wote wakasimama nakunipigia makofi kama vile
walivyokufanyia wewe jana. Kuanzia hapo maisha yangu yakabadilika.
Kutoka ofisi moja kwenda nyingine nikinunuliwa kwa pesa nyingi. Ila nikajiambia
siwezi kuishi maisha yakuomba omba kibali tu kwa Mungu, yaani kubahatisha
bahatisha tu. Lazima nijiongezee thamani mimi mwenyewe. Kwa hiyo
nikawa nasoma huku nafanya kazi, mpaka leo.” Wote wakabaki wamepoa. Joshua
akacheka.
“Mimi
ninaposema Mungu yupo, kwangu si msemo. Ni kwa kuwa nimemthibitisha, na
nikajua kweli Mungu yupo. Yupo. Na ukimtaka atembee, anatembea. Kuna neno
nilimwambia Naya, na ndilo najikumbusha kila siku kutoka kwenye bibilia kitabu
cha 1 wakorintho 2 mlango wa 9.” “Hakuna jicho
limepata kuona, wala sikio limepata kusikia, wala hayajawahi kuingia moyoni
yale Mungu amewaandalia wale wampendao?” Baba Naya akaongea hilo
andiko kwa kichwa kama lilivyoandikwa kwenye bibilia, tena kwa ufasaha sana
mpaka Joshua akafurahi sana.
“Halafu
Isaya 64:4 imemalizia ‘kwa wale wamngojeao’.
Hakuna jinsi ukanitoa kwenye kumsubiria Bwana. Ilimradi nikijua yeye ndiye
ameniambia nisubiri, hakika nitasubiri. Nilimwambia Naya, ndio maana
wakati mwingine watu huniona kama nachelewa kwenye mambo fulani fulani, lakini
huwezi kunitoa kwenye kusubiri, endapo Mungu ameniambia nisubiri.”
Wakacheka.
“Nilimwambia
Naya, nilipomuona mara ya kwanza, nusura nimkimbilie nimsalimie. Alikuwa
amekuja pale kwenye usahili tu.” Wote wakacheka. Joshua akajua Naya
alishawasimulia. “Naya amewasimulia eeh?” “Ndiyo.” Wote wakakubali. “Ilikuwa
nusura nimkimbilie, lakini Roho akanionya kabisa na kunitaka nimuache.
Nikiwa sijui kama atakuja kufanya kazi pale, lakini kulikuwa na tumaini kubwa
sana moyoni mwangu. Ikatokea hivyo kama mara tatu. Nilipobahatika kukaa naye
Mbeya, Malon naye akaja.” “Ni Zayoni huyo ndiye aliyemwambia kama nipo Mbeya.”
Wote wakacheka. “Ulisema umenisamehe Naya!” Zayoni akamkumbusha dada yake.
“Hapana Naya. Ulikuwa ni wakati wa Mungu.” Joshua akaingilia na kunywa
kinywaji.
“Nikiwa
nimekata tamaa. Maana Malon alituingilia, Naya akarudi chumbani kitu ambacho
nilikuwa nikizuia kisitokee angalau mpaka niweze kuzungumza na Naya vizuri.
Lakini Naya akawa ameondoka. Ametuacha mimi na Malon pale mgahawani. Sijui tena
chakufanya!” “Pale nilikimbilia chumbani kumpigia simu baba ili nilie ndipo
nilale.” “Naya!?” “Kweli. Ndiye anayenisikiliza nikilia. Sasa nifanyaje?”
Joshua akacheka kidogo na kunyamaza kwa muda kama anayefikiria. “Huyo Naya
ndivyo alivyo Joshua. Utamzoea tu. Kwanza ndio maana tulikuwa na hamu ya
kukuona, mtu unayemfanya ajifungie chumbani muda wote akizungumza na asitoke
hapa kwa baba! Wote tulitaka kukuona tukujue wewe ni mtu wa namna gani.” Joshua
akalifurahia sana hilo. Akamwangalia Naya na kucheka. Naya akacheka na kuinama.
“Nikiwa
nimekata tamaa ya kumuona tena, lakini akawa alishaniambia jambo zito mno.
Mungu akatumia hilo aliloniambia. Akaliongezea uzito, ikawa kama amekamilisha
kusudi zima la mimi kumfuata Mbeya. Kwa upande fulani nikaridhika kwamba
angalau nimeweza kuzungumza naye, nikamjua moyo wake, lakini nikawa
nikimlalamikia Mungu kuwa mbona hakunitengenezea mazingira tukapata muda mrefu
kidogo?” Wakacheka.
“Sasa
Jamal, kiongozi wake aliponifuata chumbani kumuombea mtu mmoja nafasi! Kwanza
nikashangaa. Jamal atake kusafiri na mmoja wa watu waliopo chini yake! Tena
nikacheka tu nikamuuliza ni nani huyo aliyebahatika kuombewa lifti na Jamal?
Aliposema Naya, tena akawa akinielekeza akidhani simfahamu Naya. Nilimshangaa
Mungu mpaka nikashindwa kuongea. Jamal alipoondoka, nilipiga magoti na
kumwambia hivi Mungu, ‘wewe ni Mungu, badala
yako hakuna mwingine, na wala hatawahi kutokea mwingine.’ hivyo tu
tena kwa hofu kubwa sana. Nikasema lile andiko la Zaburi 37:23” “Hatua za mwenye haki huongozwa na Bwana?” Baba
Naya akalisema tena hilo andiko kwa muundo wa swali. Wote wakacheka.
“Sawasawa
mzee wangu. Hapo ndipo Mungu akaniachia uwanja. Mpaka leo nimekaa hapa! Hakika
ni Mungu. Hakuna jinsi ukaniambia vinginevyo nikaelewa, isipokuwa ni Mungu.
Mimi Joshua, leo amenikalisha hapa! Nakula chakula na watu kama nyinyi! Wenye
familia bora! Nipo hapa na binti kama Naya!” Wakamuona anatingisha kichwa na
kucheka. “Hakika ni Mungu. Nilimwambia Naya, nimpaka apite nilipopita
mimi ndipo atanielewa. Ndugu zangu, huyo ni Mungu tu. Na narudia kuwashukuru
sana.” Wote wakaelewa vile Naya alivyosema anajua kujishusha. Mpaka
hapo akawa ameshauvuta na moyo wa baba Naya.
“Karibu
sana Joshua. Ujisikie nyumbani. Naya anatujua. Hapa kwetu hatuna makuu. Hivi
tulivyo ndio tumemaliza. Karibu sana.” Joshua akasimama na kumpa mkono baba Naya.
“Asante mzee wangu.” “Karibu sana.” Wote walijua kama baba yao amefurahi.
“Asante baba.” Wakamsikia Naya akishukuru kwa deko, mtoto huyo wa baba akajua
baba yake amempokea. Wote wakacheka
“Basi
nisirudi kukaa, naomba Bale unisaidie kama utaweza ili tuwahi kutoka na Naya.”
“Bila shida.” Bale akasimama. “Mbona hujamaliza chakula?” Naya akamuuliza
taratibu. “Inatosha. Asante sana.” Naya akabaki akisafisha pale mezani Joshua
na Bale wakatoka kurudi kwenye gari ya Joshua hata Naya hakuwa akiifahamu. Kwanza
hakuwahi kumuona akijiendesha. Ilikuwa gari mpyaa, hata kwa muonekano
ilionekana safi. Wakaanza kuingiza vitu ndani mpaka baba yake Naya akasimama.
“Naona hammalizi! Nisaidie?” “Tunamalizia mzee wangu. Pumzika tu.” Joshua
akakazana hapo ukweni akajaza hapo sehemu ya kuingilia. “Asante Joshua.
Tunashukuru.” Naya akatoka na kushukuru. “Karibu.”
Akamsogelea
pale mezani na kumnong’oneza. “Si twende sasa? Au kuna kitu unataka nikusaidie
ndipo tuondoke?” “Nimemaliza.” Joshua akamshika mkono na kusogea naye pale
sebuleni alipokuwa amekaa baba yake Naya. “Nikuombe mzee wangu.” Baba Naya
akawaangalia. “Naomba nitoke na Naya. Nitahakikisha anarudi salama.” “Hilo
ndilo ombi langu Joshua. Hata mkishindwana huko, wewe nipigie tu simu,
nitamfuata mwenyewe.” Naya akacheka taratibu nyuma ya Joshua. “Naamini
hatutafika huko mzee wangu. Niombee tu niweze kuwa kile Mungu anatarajia niwe
kwa Naya.” “Ninaomba sana tu. Nilianza mapema sana tokea Naya ana mwaka,
nafikiri.” “Waw! Kwa hiyo umeona Naya, tupo salama.” Akamgeukia Naya. Naya
akacheka.
“Asante
sana mzee wangu. Tutaonana baadaye.” Wakatoka Naya akiwapungia mkono na cheko
kubwa. Wakachungulia dirishani, wakamuona anamfungulia mlango. “Anamfunga mpaka
mkanda!” Zayoni akashangaa. “Atakuona wewe Zayoni!” Wakacheka. “Naya
anavyocheka! Sasa pale sijui anacheka nini!?” Bale akajiuliza ila kwa sauti ya
chini. Baba yao alibaki amekaa tu. Lakini wazi alionyesha kufurahi.
Joshua
& Naya.
“Tunakwenda
wapi kwanza?” “Moja kwa moja kule club nilipokwambia. Kuna vitu vingi
vyakufanya, ila naomba kwa wakati huu usiogelee. Tuache hiyo kwa wakati
mwingine.” Naya akawa kama amemuelewa ila akajaribu kufikiria. “Au ulitaka sana
kuogelea?” “Mwenzio sijui kuogelea Joshua.” “Basi nitakufundisha. Mimi naogelea
sana. Sana. Ndio mazoezi pekee ninayofanya, vinginevyo sina muda. Lakini
nitakufundisha wakati mwingine sio sasa. Si umesema unatunda la uvumilivu pia?”
Naya akacheka. “Hiyo hata si kuvumilia. Ni kitu ambacho hakikuwahi hata kupita
akilini mwangu.” Joshua akacheka kidogo na kutulia.
“Mbali nakuogelea,
huwa unapenda kufanya nini?” Naya akamuuliza. “Kuimba.” Naya akacheka.
“Huamini?” “Hakika siamini.” “Ngoja nikwambie habari za mama yangu ambazo
sikuwa nimewaambia pale.” Naya akakaa sawa. “Mama yangu hakuwa amesoma sana. Aliishia
darasa la saba tu, akaenda mjini kutafuta kazi. Akapata kazi hotelini. Hoteli
tu ya mkoani. Sio mahoteli ya kisasa. Akawa akifanya kazi hapo na akapewa
chumba na mwenye hiyo hoteli. Mama akawa anaishi chumba cha nje. Kwa mujibu
wake, hakuwa mtu wa wanaume mpaka akakutana na baba yangu mimi. Anasema
hakumwambia kama anafamilia. Wakaanza mahusiano. Kila baba alipokuwa akienda
hapo mkoani, akawa anashukia kwa mama, mpaka mama akapata ujauzito na kunizaa.
Pale kazini akafukuzwa, baba akampangishia chumba, akawa akitutunza mimi na
mama.” Joshua akaendelea.
“Naya,
mama yangu mzazi alikuwa akiimba bila kuchoka. Nimekuwa mimi, nikimsikia mama
akiimba. Ilikuwa kama ndio maisha yetu ya kuzungumza kwa kuimba, tunapokuwa
mimi na mama. Nakumbuka wakati mdogo, alikuwa akiniamsha kwa maneno ya kuimba.
Pale tulipokuwa tukiishi wapangaji wenzetu walikuwa wakijua tumeamka ndani kwa
mama kuimba.” Naya akacheka. “Alikuwa akinisimulia eti wakati mimi ni mtoto
mchanga kabisa, nilikuwa nikilia, eti ananiimbia mpaka nanyamaza. Kwa hiyo mimi
naimba tokea mtoto. Hata nyumbani kwangu, walinzi wanajua nimeamka ndani kwa
kuimba. Na sipangi. Najikuta tu. Kwa hiyo mimi ni mwimbaji.”
“Utaniimbia?” Joshua akacheka sana.
“Na
mimi nataka kukusikia.” “Utanisikia na utazoea. Mziki ni sehemu yangu. Na wewe
unapenda kuimba?” “Nilikuwa nikiimba sana kabla sijaanzan...” Akamuona ametulia
kwa muda, akamuona ameinama kama anayefikiria kisha akaendelea. “Maisha yangu
yalibadilika sana Joshua. Sana. Lakini nilikuwa nikiimba na kina Ino.” “Ino ni
nani tena?” Naya akacheka. “Ni kijana tuliyekuwa wote kanisani. Kama amenipita
ni kidogo sana. Ana vipaji yule kiumbe, mpaka namshangaa. Hakuna chombo cha
mziki pale kanisani hajui kutumia. Tena kutumia kifasaha. Sasa mara nyingi
tulikuwa tukiimba naye na Bale pia, mpaka mimi nilipokuja kubadilika au
nilipoanza na Malon. Maisha yakachanganyikana! Na wao pale kanisani wakawa
wameshanichosha kwa kumdharau baba yangu au niseme wazazi au sisi kwa
ujumla. Nikaacha kwenda kabisa. Ila jumapili iliyopita tumerudi tena.” “Ino ameoa?”
Naya akacheka sana.
“Niambie.”
“Alishaoa na wanakaribia mtoto wa tatu. Usiwe na wivu.” Joshua akacheka na
kunyamaza. “Nimalizie habari ya mama Joshua.” Joshua akacheka. “Mama anasema ni
kama baba akaanza kupotea kwenye picha. Kadiri siku zilivyozidi kwenda,
mawasiliano yakawa magumu. Na ubaya mama hakuwa akifahamu wapi anaishi huku
Dar, wala hakuwahi kumtambulisha kwa ndugu yeyote. Mwishoe ikawa kama
ametelekezwa kabisa. Akabakia yeye tu akihangaika kunilea peke yake. Nilipofika
darasa la 6, mama akasema amepata mwanaume anataka kumuoa. Kumbe yule jamaa
alikuwa muathirika. Nafikiri alimdanganya tu mama akamuachia ugonjwa, sikuona
ndoa na wala yeye sikujua muendelezo ulivyokuwa.” “Pole sana Joshua.” “Asante.”
Joshua akatulia kidogo na kuendelea.
“Basi,
mama akaanza matibabu. Akawa akitumia madawa hayo ya waathirika. Akaonekana
kuendelea vizuri tu kwa miaka hiyo yote mpaka mimi nikafika kidato cha nne,
ndipo akaanza kuugua. Sijui nini kilitokea maana nilisikia wapo wanaoishi miaka
mingi zaidi ya hiyo 5. Akapoteza kazi, na ukumbuke hapo tunaishi
nyumba ya kupanga. Tunalipia kila kitu. Ndipo mama akamuomba mpangaji mwenzake
anihifadhi mpaka nimalizie kidato cha nne, ndipo nimfuate kwa wazazi wake
kijijini. Haikuwa shida sana. Nyumbani ni nyumbani, na kwa mtu mwingine ni
tofauti. Ila kwa kuwa ni kwa kitambo, mama akaniambia nivumilie kila shida,
nimalize shule. Ikawa nikipata mwanya, nakwenda kumuona mama yangu kule kwa
bibi.” Joshua akacheka kwa kusikitika.
“Naya,
nyumbani kwa babu na bibi yangu sikuwa mgeni. Tulikuwa tukienda siku za
sikukuu, na nakumbuka mama alikuwa akibeba zawadi. Lakini ghafla mama
akaonekana ni kama mtoto aliyekuwa hajali nyumbani kwao, eti amerudi akiwa
mgonjwa, wakati mzima hakuwa akiwataka wazazi! Nikashangaa sana maana karibu
kila mwaka siku za siku kuu, tulikuwa tukirudi kijijini na tunakaa mpaka
sikukuu ziishe ndipo tunarudi mjini! Wakaanza kumnyanyasa mama ambaye alikuwa
mgonjwa.”
“Kuna
siku nilikwenda kumuona, nikamkuta na hali mbaya sana, nilishindwa kuondoka
Naya. Nikaona ni bora nibaki nimuuguze mimi mwenyewe. Nikahangaika mpaka
nikahamishiwa shule pale kijijini. Ikawa shule na mama. Maisha yakaendelea
mpaka mama alipofariki. Hapo nikawa nimeshamaliza shule na matokeo yametoka
nina daraja la 4.” “Pole sana Joshua.” “Asante. Nafikiri nilikaa kama miezi
miwili tu, wakanishauri nije huku Dar nimtafute baba, anisaidie kusoma. Mungu
akawa amesaidia. Nikawa na jina kamili la baba, na wizara ya fedha, ambako mama
alinimbia ndiko alikokuwa akifanyia kazi. Nikaja mpaka huku, moja kwa moja
ofisini kwake.”
“Nikakutana
na mtu ambaye nirafiki yake wa karibu sana, na wanaishi naye Tabata, mtaa
mmoja. Aliniambia walinunua naye kiwanja, wakajenga kwa pamoja. Sawa.
Akanichukua mpaka kwa mzee. Kufika mzee mwenyewe yupo hoi, kwa ugonjwa wa
kisukari. Hata hakunikataa ila akashangaa sana jinsi nilivyokuwa mkubwa.
Nikamueleza kuwa mama aliugua, akafariki. Nikakaribishwa pale lakini kumbe
familia yake wenyewe wanasubiri urithi, pesa watakayolipwa kazini akifa na
mengineyo. Mimi sina habari ila baba alijua.”
“Siku
moja akaniita na kuniambia nikafungue akaunti benki, kisha yule rafiki yake
atanipa pesa, nikaifiche huko. Nisiitumie mpaka itakaponilazimu sana.
Nikamuelewa. Na kweli nikafanya hivyo. Sijui ni pesa ya nini alilipwa huko
kazini miezi michache kabla hajafa, mimi nikaitunza ndio hiyo ikanisaidia
kuanza shule ya mambo ya stoo. Mengine ni kama nilivyosimulia pale nyumbani.”
“Nikuulize
kitu Joshua?” “Karibu.” “Kwa nini kule kwa bibi yako, au upande wa mama yako
walikufukuza?” “Waliniambia nirudi mjini nikapiganie haki yangu kama mzaliwa wa
yule mzee. Niliporudi tena, nilisimulia uhalisia wa mazingira niliyoyakuta kule
kwa baba, na wao wakaniambia hawawezi kunitunza pale. Nikapambane mpaka wanipe
na mimi mali. Niliondoka, sikurudi tena Naya. Kwa sababu nilishawaona tokea
mama ni mgonjwa. Jinsi walivyokuwa wakinifanyia na mengineyo. Nilivumilia tu
kwa sababu mama alikuwa mgonjwa. Sikuweza kuondoka na kumuacha. Kwa kifupi
haikuwa mara ya kwanza kunifukuza.” “Pole sana. Hivi uliniambia ni kama
ulishakuwa kwenye mahusiano au nimekosea?” Joshua akacheka.
“Nilipokuwa
chuoni. Hapo ndio nilikuwa nimefukuzwa upande wa mama na baba, unakumbuka
nilikuwa na zile pesa?” “Ndiyo.” “Basi, nafikiri sijui uoga wa maisha, kuhofia
nitakuwa peke yangu! Sijui. Ila nikapata msichana pale chuoni. Yeye alikuwa
akisoma diploma ya mambo ya uhasibu. Akasema tuishi naye mtaani. Na yeye hakuwa
na ndugu hapa mjini.” Akamuona anacheka kwa kusikitika. “Nini?” “Hivi unajua
Naya, yule binti, au mwanamke maana sasa hivi ameolewa. Alinisaidia kuimaliza
ile pesa yote benki, na kunikimbia mchana hivi!” “Jamani Joshua! Kwa nini?”
“Aliniambia hakuwa akiona maisha kati yetu. Amepata mwanaume mwingine.”
“Haiwezekani!” “Acha Naya. Yule dada aliniacha Naya. Aliniacha nikiwa
nimemueleza hali yangu ya maisha. Nipo peke yangu. Sina ndugu ila yeye.
Aliondoka si kwa kujificha. Nikiwa namtizama hivi, na hapo nilikuwa nimelipia
chumba kodi ya mwaka, kodi inakaribia kuisha, sina pakwenda! Sikuamini.
Akafungasha vitu vyake huku akiniaga, jamaa yake akaja kumchukua na gari,
akaondoka bwana.” “Joshua!” Joshua akacheka.
“Acha
Naya. Niliingiwa na hofu. Ndipo nikaamini usemi wa mama kuwa pengine ni kweli
nina hiyo roho ya kukataliwa, akasema nimeipata kutoka kwake. Nakwambia Naya,
unaweza usiamini. Bibi na babu walikuwa wakitunza watoto baki pale nyumbani
kwao, sio ndugu kabisa, lakini walinifukuza mimi! Na upande wa baba nao walinifukuza,
hawakutaka hata nikae pale kwa maandishi kuwa sitaki mali. Si unajua makanisani
wanapokea watu, na kuwasaidia?” Naya akaumia sana. “Basi mimi nilikuwa nikifukuzwa,
Naya. Niliijua misikiti inayogawa sadaka siku za ijumaa, na kugawa chakula.
Nilijua makanisa yanayofanya mikesha usiku. Nikikwambia nilishaishi msikitini,
ni zaidi ya usiku mmoja. Nayajua maisha kwa kuyaishi.”
“Nikikwambia
Mungu ni baba yangu, sio kwa sababu nilihubiriwa! Ni kwa kuwa alinihurumia,
na kuamua kujitambulisha kwangu kwamba yeye ni ‘Niko,
ambaye Niko’. Alinifundisha kumtambua yeye. Siku moja usiku nililia
sana. Walinikamata wahuni, wakataka kinibaka. Ni usiku, sina mtetezi,
nipo peke yangu sehemu niliyokuwa nimejificha ili nilale. Naya, nililia ule
usiku maana walikuwa vijana watatu. Tena wachafu tu. Nikakumbuka vile mama
yangu alivyokufa kifo cha mateso kwa lile gonjwa, nikajua watanibaka na
kuniachia magonjwa, halafu sina wakuniuguza. Naya, binadamu muone hivihivi.
Akikubali kutumiwa na shetani, ni mnyama hatari kuliko simba mwenye njaa.” Naya
alishaanza kulia.
“Wale
vijana walishanivua nguo kabisa, na wawili wamenishikilia ili mwenzao aanze.
Nililia kwa uchungu nikimwita Mungu aniokoe, ndipo nilipomuona Mungu. Hapakuwa
na mvua, lakini Naya, radi ilianza kupiga. Ilikuwa sehemu ya fundi
viatu. Ameweka kama mifuko ya safleti tu juu. Kufunika mchana jua lisimpige
wakati akifanya kazi zake. Sasa mimi ndio nilikuwa nikienda kulala pale usiku
na aliniruhusu. Sijui radi ilipotokea Naya, kile kibanda kiliraruliwa na kikawa
kama kiliteketezwa kwa moto.” “Joshua!” “Sikudanganyi
Naya. Wale vijana walikimbia, na mimi mwenyewe nilikimbia uchi. Sina nguo ya
chini.” Naya alilia sana. “Acha Naya. Sijui nini kilitokea usiku ule, ila mimi
nachukulia ni Mungu alinitetea. Nililia ule usiku, sitakaa nikasahau.”
“Ndipo
nikaanza kujificha misikitini na makanisani sasa na ndipo nikakutana na huyo
mzee ambaye alinipa hiyo kazi. Hakuwa hata akijua ninapoishi. Wakati mwingine
nilikuwa namwambia aniachie funguo ili nisafishe usiku, kumbe nia ni kulala
hapo ofisini kwake, mpaka nikapata pesa ya kupanga, nikapanga na kupata chumba,
lakini hamna kitanda wala godoro na niliishi hivyo nikilala juu ya nguo kwa
muda mrefu sana tu, mpaka nilipoanza tena chuo.” “Pole
sana Joshua. Pole.” “Kwa hiyo ndio yamekuwa maisha yangu. Sikurudia
tena kuwa na mahusiano yakaribu na mwanamke kimapenzi ila kazi. Nafikiri nikawa
kama nimezira! Sikutaka tena kutafuta ndugu wa pande zote. Nikaona nikae nao
mbali kabisa.” “Pole sana Joshua.”
“Naamini
Mungu ameanza kunipumzisha Naya. Amenitoa mbali sana. Ila nilikuwa nikijijua
mimi ni zaidi ya kile nilicho kwa wakati ule. Kulikuwa na kilio ndani yangu chakutaka
zaidi na zaidi kila wakati. Sikuwahi kuridhika.” “Sasa hivi umeridhika?” Naya
akauliza. “Ndiyo na hapana. Mungu amenipa kila kitu, bado namlilia familia.
Natamani na mimi nije kuwa na familia, Naya. Ila nimejiapia sitafanya kosa kama
la baba. Kwenda kuzaa nje. Tokea yule msichana anikimbie, nikajiambia sitagusa
mwanamke isipokuwa niliyekabidhiwa na Mungu, nikajua kwamba ni wangu.
Na hilo Jema amelielewa kwa wazi kabisa. Akaongeza nidhamu kwangu na
kutaarifu wengine.” Naya akainama. Kimya. Mpaka wakafika.
“Naona
tumefika muda mzuri.” Akamfungulia mlango wakashuka. Ukweli Naya na
Joshua walipendeza sana. Ikaonekana sehemu nzuri sana wanayofahamiana kwa
karibu. Wengi Joshua aliwasalimia kwa furaha na cheko kubwa, wakaonekana ni
kweli watu wa hadhi ya Joshua. “Kuna mambo mengi sana yakufanya hapa. Tunaweza
tukachukua boti, tukaenda kuzunguka kidogo, au tukakaa huko kwa muda kisha
tukarudi.” “Sijawahi kupanda hata pantoni mwenzio.” Joshua akacheka.
“Naya
wewe mtundu bwana.” “Kweli Joshua. Sasa nakwenda wapi?” “Basi twende
nikakuzungushe baharini.” “Sasa nani anatuendesha?” “Mimi mwenyewe. Nimejifunza
kuendesha.” “Kweli you are full of suprises.” Joshua akacheka na
kumshika mkono mpaka sehemu. Akaandikisha mambo kadhaa, wakaongozana mpaka huko
kwenye boti Naya akishangaa tu.
Akamsaidia
kuingia ndani. “Hatuwezi kupinduka?” “Na Mungu naye atakuwa wapi?” Naya
akacheka, kidogo akatulia. Joshua akafungua kamba zilizokuwa zikishikilia hiyo
boti, akatoa nanga, akaenda sehemu ya kuendesha. “Ni rahisi sana. Njoo karibu
yangu uone. Naya akamsogelea, akawasha na kuanza kuondoka taratibu tu sio kwa
haraka. Naya akaanza kucheka. “Woga umeisha?” “Nipo na wewe, siogopi tena.”
Hilo likamfurahisha Joshua. Akaendesha mpaka mbali kidogo na nchi kavu, kisha
akasimamisha hapo boti ila wakiona nchi kavu kwa mbali. Akamwambia wakae tu
hapo.
“Nikwambie
kitu Joshua?” “Nakusikiliza Naya. Njoo tukae hapa.” Akamsogelea na kukaa sehemu
ya juu. Maalumu kwa kukaa. “Niambie.” “Mimi sitakukimbia wala sitakusaliti. Na
mimi sina tamaa. Nitakaa na wewe mpaka wewe mwenyewe uje unichoke.” “Hiyo
itakuwa kifo Naya.” “Kuna kuchokana Joshua!” “Sio mimi. Najua ninachoongelea.
Ndio maana mimi uliponifungulia tu mlango, sijasita. Si umeona?” “Mpaka
umenishangaza!” “Nataka watu wajue Joshua huyu akiwa na mtu. Nimevumilia ati
Naya! Unafikiri na mimi sitamani kupendwa?” Naya kimya akicheka.
“Tulikuwa
tukija huku na wenzangu wakiwa na wapenzi wao, mimi nipo peke yangu. Mpaka
unachoka kuwa msindikizaji kila wakati, wakati mwingine nakuja tu peke yangu.
Nikikwambia mpweke, ndio hivyo. Nilikuwa nakuja kukaa hapa peke yangu. Ila huwa
nakwenda mbali zaidi ya hapa. Nakaa huko nachakula changu, nitaimba na kusoma
mpaka nikichoka ndipo narudi nyumbani.” “Ukiwa unajisikia mpweke uwe unanipigia
mimi.” “Ndicho ninachofanya. Na hivi umesema si tatizo! Ndio maana napenda niwe
na wewe kwenye simu muda wote mpaka wakati wakulala.” Naya akanyamaza.
“Unataka nikuimbie wimbo gani?” “Wowote unaotaka wewe. Ule unaoupenda sanaaa.” Joshua akacheka akifikiria. “Ehe! Unajua wimbo wa ‘Great is your Mercy’?” Naya akatulia akijaribu kuvuta kumbukumbu. “Umeimbwa na Donnie McClurkin.” “Mimi nyingi najua za kiswahili. Za kingereza ni zile za zamani alizokuwa anachagua Ino. Na ni zile za zamani sana. Niimbie huo nione kama naufahamu.” “Una beti mbili tu, lakini unaweza kurudia kwa sauti tofauti tofauti mpaka uridhike. Maneno yake ndio mazuri sana. Yanasema hivi. ‘Great is You mercy towards me, Your love and kindness towards me, Your tender mercy I see, Day after day. Forever faithful towards me, And You're always providing for me, Great is Your mercy towards me, Great is Your grace.
“Nataka
uyapate hayo maneno vizuri. Angalia haya meneno hapa.” Akamkabidhi simu yake
sehemu yenye huo wimbo. Naya akaanza kutafasiri. “Kuwa, ‘Rehema za Mungu kwako ni kubwa, upendo na wema wake viko
kwako, Rehema zake unaziona kila siku’.” Joshua akafurahi sana vile
anavyotafasiri. “Sijamaliza.” “Nakusikiliza Naya.” “Unasema, ‘Uwaminifu wake kwako ni wa kudumu’.” “Milele.”
“Sawasawa. ‘Kuwa yeye Mungu wakati wote anakubariki’.”
“Hajawahi kunipungukia.” Akaongeza Joshua kwa hisia zote. Naya akamwangalia na
kucheka, kisha akaendelea. “Rehema zake kuu ziko
kwako Joshua Kumu.” Basi Joshua akaanza. “Naanza kukutambulisha wimbo.”
Naya kimya na cheko.
Joshua
akaanza kuimba tu kama kawaida. “Na kwenda ya pili Naya.” “Nakusikiliza.”
Alipourudia ule wimbo kuuimba kwa mara ya pili, Naya hakuamini. Ya tatu, mwili
mzima ulisisimka. Naya akabaki ametoa macho. Joshua aliimba kwa sauti ya ajabu,
nzuri na kwa hisia zote. Akipanda juu sana, akawa katikati na kupiga sauti
nzito ya kiume. Naya akabaki ametoa macho.
Joshua
akamalizia kwa kutulia, Naya akabaki amepigwa na butwaa. Joshua akamcheka.
“Mbona hukuniambia kama unajua kuimba!?” “Nilikwambia Naya.” “Hapana.
Hukuniambia kama UNAJUA, kuimba!” Joshua alicheka sana. “Basi mimi sitakaa
nikakuimbia! Mimi nilifikiri unasema ule uimbaji wa kawaida, kumbe mpaka
kutetemesha sauti!” Joshua akazidi kucheka. “Joshua! Hakika you are full of
suprises! Umejawa maajabu mengi! Sikuwahi hata kufikiria kama unajua kuimba
hivyo!” “Nimekuleta huku ili umfahamu Joshua huyu ambaye akifika mbele za
Mungu, anajishusha chini kabisa, ili yeye azidi. Huwa nakaa huku peke yangu,
naimba mpaka nasikia uwepo wa Mungu kama yupo hapa. Wakati mwingine nakaa huku
mpaka walinzi wanakuja kuniangalia kama nipo salama, wananikuta nikiomba.”
“Joshua
wewe unampenda Mungu!” “Naya, elewa sina mtu mwingine maishani ila yeye
Mungu.” “Mbona na mimi hunihesabu?” Naya akaongea kwa kulalamika. “Nimekwambia
sitakuacha Joshua. Na sitaki Joshua mwingine, hata muonekano, namtaka huyu
Joshua aliyesimama mbele yangu. Mimi nipo Joshua.” “Hujui inanifariji
kiasi gani kusikia hivyo. Na kwa kuwa sijazoea, tafadhali usichoke
kunikumbusha. Nahitaji kusikia mara kwa mara mpaka huyu mtu wa nje, huyu
Joshua, aelewe kuwa sipo peke yangu tena.” Naya akacheka kidogo na kutulia.
Joshua
akarudi kukaa. “Na wewe niimbie.” Naya akacheka sana. “Heri ningeanza mimi.
Hivi nishakusikia wewe, acha tu mimi nikuonyeshe mitindo ya nguo.” Joshua
akacheka sana. “Hutaki tena?” Joshua akamuuliza akicheka sana. “Nitaharibu
uwepo mzima uliovuta kwa kuimba kwako. Nipe muda akili irudi vizuri, nitulie
nafsini kwangu, ndipo naweza hata kukumbuka kuimba. Nimekuwa na miaka ya
uchungu Joshua! Hakuna jinsi nikakueleza ukaelewa. Maisha yalinipokonya kabisa hali
fulani niliyokuwa nayo mwanzoni. Ule ujasiri wa ndani, utulivu na kujiamini,
nilivipoteza vyote, nikabaki kuona kama natembea uchi na kila mtu ananitizama
na kunidharau!” “Kwa nini?!” “Hapakuwa na sehemu, au wanawake zaidi ya kumi
sehemu moja na mimi, Malon awe hajalala nao japo wawili kwa uchache, au wote
tumejikuta tumeshalala naye. Ilikuwa ikiniuma Joshua, kupita nitakavyokueleza,
halafu mimi ndio nikawa najulikana ni mwanamke wake!”
“Pole
Naya.” “Lakini ungeniona kwa nje! Ungejua mimi ni mwanamke wa Malon. Nilikuwa
navaa, Joshua! Chuoni watu walikuwa wakisubiri nitoke siku hiyo, waone nimevaa
nini. Na nilikuwa sijikosei. Malon alikuwa akinipa pesa. Tulikuwa tukienda
Dubai tulikuwa tukirudi na masanduku kama tunafanya biashara! Kumbe nguo na
viatu vyangu tu. Nilikuwa nikienda shule, kidato cha tano na sita, na SUV gari.
Safi. Kwa hiyo kwa nje hivi, nilionekana bora mno, lakini hiyo shida
niliyokuwa nikijisikia ndani, hamna mtu akaelewa. Kilio kila siku
kumuomba Malon atulie. Hofu ya pengine atakuja kuniua kwa maradhi ilikuwa
imenijaa sana.” “Kwa nini uliendelea kuwa naye Naya?” Naya akajicheka.
“Hakuna
mtu alikuwa anaelewa Joshua. Hata watu wake wakaribu walikuwa hawanielewi,
wananishangaa. Lakini Malon ndio alikuwa mwanaume wangu wa kwanza. Malon akiwa
na mimi, hashiki simu. Na watu walijua hata marafiki na wafanyakazi wake kuwa
Naya yupo. Ni kama kila kitu kinasimama ila mimi. Alikuwa na jinsi fulani
kwangu, siwezi kueleza. Kabla sijalia shida, Malon ametatua. Kwanza hakuwa
akitaka niwe na shida hata kuumwa tumbo kwenye siku zangu tu. Alikuwa anakuja
huku Dar, ananiuguza mpaka napona. Usiku unaweza kuamka ukamkuta bado anakusugua
kiuno, ili maumivu ya hedhi yasirudi nilale. Alikuwa akithamini mawazo yangu,
mpaka nilikuwa nikishangaa.” Naya akacheka.
“Hivyo
watu ambavyo wanakusikiliza wewe ukiongea hivyo, mimi nilipata hiyo kwa Malon.
Ananiami mpaka alinipa nguvu yakufikiria zaidi na zaidi. Hii mitindo ninayotaka
kukuonyesha hii, Malon aliiweka kwenye uhalisia. Kutoka kuwa michoro, mpaka
kuitisha tamasha! Acha nikuonyeshe.” Akamfungulia website yake ya mitindo.
“Naya hii ni kazi yako!?” “Nilijaza watu pale Plaza, nguo zilinunuliwa kwa
silimia 85. Alinunua kiwanja, tukajenga kiwanda. Tukanunua mashine za kisasa,
nikaajiri watu, wakatengeneza hayo mavazi, huku nikisoma, Malon akinisaidia
bila kuchoka. Lakini na vyenyewe vikakosa ladha kwenye onyesho la kwanza tu,
warembo wote hawa niliokuwa nimeletewa wanisaidie kutangaza mavazi, mmoja
alitoka kulala na Malon, na wengine walikuwa wa zamani. Wakaanza kusimuliana
wasijue mimi nipo.”
“Haiwezekani
Naya!” “Acha Joshua. Nilikuwa nikilia mchana, na usiku. Baba ndiye anakazi ya
kunibembeleza. Malon! Acha jamani. Akanitoa kwenye amani niliyokuwa nayo
kabla hajanikuta nikiwa sina kitu, tunahangaika na baba pesa hata ya ada hatuna!
Akajaa kwenye maisha yangu, akaleta na mapesa, lakini Joshua! Ilikuwa ni furaha
na uchungu kila wakati. Vyote vikawepo kwa wakati mmoja.”
“Nimempoteza
Naya wa ndani. Hii ndiyo week ya kwanza, baada ya miaka mingi sana, nalala
nimetulia kwa sababu najua ni wewe upo masikioni kwangu, halafu sina
hofu ya alipo Malon, na yupo na nani. Hivi jumatatu nataka niwahi kutoka,
nikabadilishe jina lake kwenye lile gari, mambo yaishe.” Joshua akakunja uso.
“Sijaelewa.” “Ile gari ninayotumia au tunayotumia nyumbani, alinipa Malon ikiwa
mpya. Hata miezi miwili sidhani kama imetimia tangia anipe.” Joshua akatulia
kabisa. “Alikuja akakuta nahangaika usafiri, ndipo akaninunulia hiyo gari.”
Naya akamuona Joshua amebadilika kabisa akainamia michoro ya Naya,
akaendelea kuperuzi. Kimya.
“Lakini
amenipa mpaka kadi zake zote. Ameniambia hatakaa akaniulizia juu ya hilo gari
na hata nilipomkatalia asinioe, nikamrudishia pete yake, akaondoka bila hata
kuulizia gari. Amenipa kabisa. Ni langu, alininunulia mimi. Kwanza ni kama
jasho langu tu kutokana na ile pesa aliyorudishiwa baada ya kutoka jela,
niliyomuwekea mimi dhamana.” Ikawa kama Naya anajitetea tena. “Kwa nini
aliandika jina lake na si lako?” Naya akapoa kidogo kama anayefikiria, Joshua
akarudisha macho kitabuni. “Lakini amesema nipo huru kubadili iwe jina langu.
Na jumatatu nakwenda kubadili jina.” “Lakini itabakia palepale, kuwa ni kumbukumbu
ya gari uliyopewa na Malon. Si ndiyo?” Naya akanyamaza, Joshua akarudisha macho
kitabuni na kuendelea kuangalia mpaka mwisho. Akarudia tena.
Akamuomba
na simu yake aangalie tena picha mtandaoni. “Katika hili, Malon alikuwa
sahihi. Unakipaji kikubwa sana.” “Huna haja ya kumnukuu, Joshua!”
“Nafikiri ndivyo ulivyomtambulisha kuwa yeye ndiye ameweka haya mawazo kwenye
uhalisia. Sasa kama yeye ndio mwanzilishi, wengine si tunarudia tu?” Naya
akajua anaanza kusumbuliwa na wivu. Akanyanyuka pale na kusimama akasogea
mwisho kabisa wa boti, akainama kama anayejaribu kushika maji.
“Hii
ni kazi, ambayo nikiingalia mimi, ni kubwa kama ile kampuni yetu. Ambayo
ikiwekezwa na kichwa kama chako, inamaana utahitaji kina Jema, Njama, Jamal na
kila unayemuona pale.” Naya akacheka na kugeuka. “Sikutanii. Kile unachokifanya
pale sasa hivi, na vile nilivyokusikia, na kuona jinsi ulivyofanya hizi nguo zetu!
Pale ulipo sasa hivi, sio hata robo ya hichi ninachokiona hapa.” Joshua
akaongea huku akiendelea kuangalia.
“Unajua
ninazo nguo kama hizi lakini suruali na shati ila ni vya rangi ya maziwa. Off
white. Sikuwahi hata kuwaza kama mtu anaweza akaongeza kitu kwenye nguo kama
hizi! Lakini jinsi ulivyounganisha hivi vitambaa na kutoa hizi nguo kama hivi,
unakipaji kikubwa sana. Sana Naya. Najua inaweza isilete maana kwa kuwa
narudia kwa wenzangu walio tangulia. Lakini upo vizuri Naya.” Naya akainama
bila ya kujibu. “Mimi najua vitu vizuri, na si muongo. Hii kazi ni nzuri.”
“Asante.” Naya akashukuru bila yakumtizama. Akageuka baharini akaangalia kidogo
akamgeukia Joshua akamkuta bado macho yapo kwenye michoro.
“Mimi
nataka kurudi nyumbani kwetu.” Naya akaongea kwa
upole. “Umeshachoka?” “Nataka kurudi kwa baba Naya.” Naya akajibu
macho chini. Joshua akatulia akimwangalia, Naya hakumwangalia. “Asante
umenileta huku.” Naya akaangalia kuzunguka baharini. “Ndio kwa mara ya kwanza
leo nimepanda boti. Na tumepata muda wa kuzungumza, naona mimi nirudi tu
nyumbani.” “Nilifikiri tungekaa muda mrefu kidogo!” “Wewe bado unataka kukaa
hapa na mimi?” Naya akauliza taratibu tu. “Ndiyo, Naya. Naona kama unanikimbia!”
“Sitaki kukuudhi Joshua. Sitaki kuongezeka katika watu watakaokunyima raha au
watakao ongeza shida kwako na si furaha. Binafsi najua niliishi maisha ambayo
itabidi kuyalipia gharama tu. Sitaki na wewe nikuchoshe au kukuumiza na
historia ya maisha yangu ya nyuma. Ndio maana naona bora niondoke tu
ili nisikuumize.” “Ukiniacha ndio utaniumiza Naya.” Joshua akaongea kwa
upole akimtizama.
“Sijui
chakufanya Joshua! Ni kweli Malon ametengeneza historia kwenye maisha yangu,
lakini sasa hivi hayupo. Sina uwezo wakubadili nyuma, nipo katika kutengeneza
mbele. Pengine nahitaji muda zaidi. Nitulie, nijijenge tena. Labda nitakuwa mtu
wa kufaa.” “Uliniambia ni kama unanipenda. Ile hisia imeisha?” Naya akainama.
“Eti Naya?” “Nakupenda wewe Joshua. Lakini najiona sipo sawa. Sitaki
kukuumiza.” “Ukiniacha sasa hivi, ndio utaniumiza zaidi.” “Basi niambie
kitu chakufanya Joshua. Usinyamaze kama hujafurahia jambo! Kama kuna
kurekebisha turekebishe. Nikishindwa nitakwambia.” “Na mimi sitakwambia
jambo ninalojua hutaweza kufanya.” Naya akaenda kukaa pembeni yake.
“Sikwambii
habari za Malon kukuumiza Joshua. Na kama nimezungumza vibaya, naomba
unisamehe. Sitazungumza tena habari za Malon. Ni sawa?” Joshua akamwangalia na
kutoa tabasamu lakini bado akamuona hayupo sawa. “Niambie Joshua.” “Ulikaribia
kuniacha Naya!” Naya akaumia sana. “Nilitaka utulie kwanza Joshua. Unajua
nisingeweza kukaa mbali na wewe.” Ikawa Naya anajirudi akibembeleza.
“Ningejuaje Naya?” “Kwa sababu mimi ndiye nakwambia. Sitakuacha ila nilitaka tu
angalau kutulie, nije nianze upya. Samahani. Ila bado nafikiri ni heri tu nirudi
nyumbani. Kwa leo itoshe Joshua.” Akamuona amenyong’onyea.
“Nakupenda
Joshua. Nilikuahidi sitakuacha mpaka wewe mwenyewe utakapoamua iwe basi.”
Joshua akamwangalia na kucheka kidogo, macho yalishakuwa mekundu. “Kama upo
tayari kurudi nyumbani, nitakurudisha.” “Unafikiri tutakuja kuonana tena kama
hivi?” Naya akamuuliza kwa upendo. Joshua akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha
taratibu. “Binafsi ningetamani kuwa na wewe wakati wote.” “Basi tubaki tena
kidogo.” “Sawa. Nashukuru.” Naya akaonana na Joshua wa tofauti kabisa ambaye hafahamika
na watu wengine. Joshua huyu ni watofauti na wanaume wote ambao amekuwa nao.
Akabaki kimya akimtafakari.
Wakatulia
hapo, Joshua akarudisha macho kwenye ile michoro. “Haichoshi!” Akarudia Joshua.
“Acha nikuonyeshe ya kitabuni. Fungua hizo kurasa za mwanzo, kisha chagua moja
nikuonyeshe nguo iliyokamilika kutoka mtandaoni.” Joshua akacheka akaanza
kuchagua, Naya anamuonyesha. “Picha hizi ni za Zayoni, hizi nilikuja kuongeza
baadaye kutoka kwa mpiga picha aliyepiga siku ya shindano.” “Hakika ni nzuri
sana!” Akasifia na kumwangalia. “Kuna usemi unasema ‘beauty with brain’.
Ulishawahi kusikia?” Naya akaanza kucheka akitingisha kichwa kukataa. “Naya
wewe ni mzuri sana. Sana. Na kichwa chako kinafanya kazi sana.” Naya akajificha
mgongoni kwake akicheka. “Kweli. Upo mzuri na umebeba uwezo mkubwa sana ndani
yako.” Naya akacheka akiwa amejificha nyuma yake.
Akamchungulia
kule alikokuwa amejificha. “Sema basi asante.” “Asante. Ila ujue nimefurahi
kusikia kutoka kwa mtu kama wewe.” Joshua akacheka kidogo akimtizama kule
alikojificha. “Mtu kama mimi nikoje?” “Umesoma. Unauelewa mkubwa wa mambo, sio
muongo, halafu unajua mavazi kwa kuyavaa.” Joshua akacheka nakutulia. “Mbona
kama kuna kitu kimekushikilia kimekufanya umekosa raha Joshua? Au ukapumzike?”
Joshua akacheka. “Natafuta jinsi ya kukwambia juu ya gari ya Malon ambalo
unalo, lakini nashindwa nizungumze vipi!” Naya akashituka sana.
“Ile
gari ni yangu Joshua!” “Ni ya Malon, aliyokupa kama vile ile pete aliyokuletea,
ukaikataa. Ni kama unachagua nini cha kuchukua kutoka kwake, na nini uache.”
“Joshua, tafadhali usichukulie hivyo! Halafu ile gari sio kwamba ni mimi tu
natumia. Inatumiwa na kutegemewa na kila mtu pale nyumbani!” “Wakijua ni msaada
wa Malon.” Naya akachoka kabisa. “Yaani unakuwa upo na mimi, lakini ukitunzwa
na Malon!” “Malon hayupo Joshua!” “Ila gari yake ipo, tena ikiwasaidia
nyinyi wote.” “Joshua! Tafadhali usiende mbali. Mimi nitakwenda kubadili jina
jumatatu.” “Lakini bado itabakia ni gari aliyokupa Malon!” Naya akabaki
hajui chakufanya. Ukweli ile gari ilikuwa ikitegemewa sana nyumbani kwao, na
Joshua ni kama alitaka hiyo gari irudishwe. Anafanyaje Naya anayeishi Kiluvya,
anatakiwa kuja kazini siku 6 kwa juma! Akabaki kama amemwagiwa maji.
“Kabla
hujaondoka, twende nikuzungushe kidogo nikuonyeshe kuzunguka hii bahari. Pazuri
sana. Siku nyingine nitakupeleka kisiwani.” Joshua akasimama na kuondoa boti.
Naya na yeye akamfuta baada ya muda kidogo, akaenda akasimama pembeni yake
wakati akiendesha. “Mimi nilijua leo tutapata wakati mzuri!” Akalalamika Naya
pembeni yake. “Nilifikiri unafurahia?” “Mimi nakutaka wewe Joshua. Sio haya
unayonionyesha. Nataka mimi na wewe tuwe kitu kimoja.” Joshua akasimamisha boti
na kumgeukia. Akamshika mikono yote miwili.
“Kitu
kimoja, inamaana mimi na wewe tu, si ndiyo?” “Ndiyo. Sisi tuelewane.
Mimi sitaki vitu Joshua. Lasivyo sasa hivi bado ningekuwa na Malon. Malon
anapesa, lakini hakuwahi kunichagua mimi. Ndio maana nilikwambia ubora wa mtu
kwa mtu, unatofautiana na mtazamo wa mtu.” “Basi tuanze kwa kujenga msingi wetu
mimi na wewe, kuanzia chini.” “Sawa.” “Hapana Naya. Nataka ukubali ukiwa
umeelewa na umekusudia. Nimesema, tuanze kujenga msingi wetu, mimi na wewe tu.
Ambao hauna muingiliano wa Malon, wala kukimbilia kwa baba, mambo
yanapokuwa magumu.” Hapo pakawa pagumu. “Labda maswala ya baba tungeyaacha tu.”
“Sasa utajengaje huku, wakati mwenzangu unapo pakukimbilia? Mimi sina familia
yakusema eti mambo yakiwa magumu nikimbie.” “Nikimbilie mimi.” Ikabidi tu
Joshua acheke.
“Mimi
nimkimbilie baba Naya, wewe nikimbilie mimi.” Joshua akacheka mpaka
akaenda kukaa. “Naya!” “Wewe achana na baba Naya. Ila tujenge msingi wetu bila
Malon. Ukitaka nisimtaje tena, hutamsikia tena. Nini kingine unataka.” “Niambie
ukweli Naya. Kwa mfano mimi ningekuwa ndio kama wewe. Halafu wewe kama mimi.
Kila siku unaniona na kitu alichoniachia mwanamke wangu. Tena ndio kama msaada
mkubwa sana mpaka familia inatambua huo msaada! Ungejisikiaje?” Naya akatulia.
“Kama
kweli unanipenda Naya. Na umekusudia kuwa na mimi, tafakari hilo.” Naya akapoa
kabisa. “Inamaana naonekana na mimi ni kama nipo kwenye huo msaada wa Malon!
Kwamba na mimi ananisaidia kukutunza! Unakataaje vingine halafu vingine
vyenye manufaa kwako unang’ang’ania?” “Basi Joshua. Kwa kuwa tumezungumza sasa
hivi, tafadhali nipe muda na mimi nifikirie na kujipanga. Maana kama
nilivyokwambia, ni usafiri unaotegemewa na kila mtu pale nyumbani. Si
sawa kufanya maamuzi bila kuwashirikisha. Tafadhali nivumilie katika hili.
Uliniambia wewe ni mvumilivu sana.” “Naya!” “Wewe mwenyewe uliniambia.” “Acha
bwana kutumia maneno yangu mwenyewe kunifunga.” “Mungu amenileta kwako niwe
nakukumbusha Joshua.” Joshua akaanza kucheka.
“Twende
ukanizururishe majini, kisha unirudishe kwa baba Naya. Mengine niachie mimi
nitarekebisha tu au sema jingine.” Akasimama. “Ni hilo tu. Na asante hata kwa
kusema utafikiria.” “Basi ungenifundisha kuendesha boti ili hata
nikirudi nyumbani niwe na chakuringishia!” Joshua akaanza kucheka. “Naya wewe ni
mtundu!” Akaanza kumuelekeza na kumuachia afanye. Naya alikuwa akicheka sana
tena kwa sauti. Baada ya muda ile hali ya uzito ikaisha, wakawa wanacheka sana.
Wakazunguka mpaka wakaona giza litawakuta huko na mafuta kuwaishia, wakaanza
kurudi ila wakiwa wamejawa sana furaha na wakiwa wamepiga picha nyingi tu.
“Naomba
tule pamoja ndipo urudi nyumbani.” Joshua akaongea kwa kubembeleza. “Sawa.”
Naya akakubali bila shida. “Ila kumeanza kuwa na baridi. Tukae ndani.” Wote
walikuwa wamevaa pensi. Na nje kulishaanza kupokea upepo mkali wa baharini.
Wakatafuta sehemu na kukaa ndani. Joshua akawa akimwangalia. “Sasa unafikiria
nini?” “Nimefurahi tumeweza kuwa wote mpaka sasa hivi.” Naya akacheka na
kutulia. Muhudumu akaja kuwahumumia kila mtu akaagiza chake, wakatulia.
“Siku
nyingine kama leo. Siku za jumamosi, huwa unafanya nini?” “Kama nakuwa sijaja
hapa, nakuwepo tu nyumbani nikifanya shuguli zangu tu. Na pia mimi si mtu wa
marafiki sana ila ninao watu wawili hao, huwa wananivutia sana. Nikiwa na muda
huwa nawatafuta japo niwe nao karibu.” Naya akacheka. “Wakoje hao?!” “Ni
wanandoa. Wenyewe wanasimulia walipita kwenye mengi, lakini Naya!” “Nini?”
“Hakika namsihi Mungu aje anipe ndoa si chini ya ile. Wale watu wanapendana na
wanaendana. Wamezaa watoto wazuri, utatamani kuwa nao karibu. Na wenyewe ni
wanachama wa hii club. Huwa wanakuja hapa na watoto wao, na mimi
nilitambulishwa kwao na kaka aliyemlea huyo mke mtu. Nikafanya juhudi zote niwe
nao karibu. Na pia wamefanikiwa sana kiuchumi.” Naya akacheka.
“Mimi
nikikwambia najisogeza kwa mtu, jua huyo mtu ana kitu cha ziada. Sina marafiki
wengi, au niseme sina marafiki kabisa. Ila huyo kaka mtu ambaye nimemfahamu
kupitia maswala ya kazi, na ndio akanitambulisha kwa mdogo wake kama mtoto
wake, ndipo nikakutana nao hao kina Magesa. Ila vinginevyo nakuwepo tu
nyumbani, kama si kazini.” “Naona kweli kuna mambo mengi tunafanana.” “Kwa
nini?” “Hata mimi si mtu wa marafiki sana. Sina tatizo na watu, lakini najikuta
sina muda na watu. Sijui kama unanielewa? Hata kabla ya Malon kuja na
kunichanganya hapo katikati na kunitia hofu ya marafiki sababu ya tabia zake,
lakini pia mimi ni mtu wa nyumbani. Na nyumbani ni pale alipo baba Naya. Basi.”
Joshua akacheka.
“Hakuna
kazi anafanya baba, mimi nisijue. Tokea nina akili zangu ndio imekuwa hivyo. Ni
miezi michache tu kabla mama hajazidiwa, ndipo alinirudisha ndani, kufanya kazi
kama mtoto wa kike. Napo ilikuwa kama adhabu, lakini baadaye ikageuka kitu
kizuri sana na kuniunganisha naye.” “Kwa nini uadhibiwe tena?” Naya akacheka.
“Mama alitamani sana niolewe na Joshi.” “Na wewe hukuwa ukimtaka.” “Huwezi
kumlinganisha na...” Naya akasita na kumtizama Joshua vizuri. “Alikuwa mbahili
kupita kiasi. Halafu kuna jinsi alikuwa akinidharau, ilikuwa ikiingia mpaka
rohoni. Halafu alikuwa kama mchana na usiku ukimlinganisha
n...” Akaona anyamaze kabisa.
Joshua
akacheka. “Wewe ongea. Ndio njia moja yakufahamiana.” “Inakuumiza sasa.”
“Kuendelea kumiliki vitu vyake ndio inaniumiza. Lakini si historia za nyuma.
Nakuelewa kabisa wala sina tatizo. Malon ulianza naye ukiwa mtoto sana. Umeishi
naye kama wanandoa. Nikimaanisha zile shida wanazopitia wanandoa zote, akiwa
ameyatawala maisha yako kabisa. Hapakuwa na mtu mwingine kwa muda wote huo ila
yeye tu. Kwa hiyo najua sitaepuka kumsikia au hata na mimi kulinganishwa kama
hivyo Joshi ulivyomlinganisha naye. Kwa hiyo endelea tu. Uwe na amani.” Naya
akamwangalia na kunyamaza.
Wakaletewa
vinywaji wakati wakisubiria chakula. “Unajua mambo yako pale kazini
yatabadilika Naya.” “Kwa nini tena!?” “Lile wazo ulilolitoa, nimehakikisha
linawekwa sawa na ijulikane ni wewe ndio ulitoa hilo wazo. Utafanya kazi kwa
karibu sana na Njama, kuhakikisha kile unachokifikiria kichwani, kinatokea.”
Naya akacheka kwa hofu kidogo. “Kwahiyo, hiyo itakuwa project mpya ambayo
itabidi ubadili kitu ulichokuwa ukifanya. Na Jamal mwenyewe anashugulikia ajira
yako ya kudumu. Yeye mwenyewe ametaka bila mimi kumwambia. Aliniambia lazima
wakutunze pale ili usaidie zaidi.”
“Natakiwa
nifanyaje? Nisaidie mawazo.” “Cha kwanza, jiamini. Beba wazo lako kama mmiliki
haswa kuhakikisha hakuna anayekupora. Ukisimama katikati yao, usijione upo
chini yao, jiamini. Simaanishi ufanye kwa kiburi, ila jibebe kwa
ujasiri. Ukitakiwa kuzungumza zungumza kwa makini kama ndio nafasi yako ya
pekee. Tendea haki, usiwe mropokoji katikati yao. Hata kama watafanya mizaha
ofisini, usiwe katikati ya hiyo mizaha. Kama tu hivi unavyofanya sasa,
itakutunzia heshima sana.” Hilo Naya akalifurahia.
“Kumbe
ni bora nilivyokuuliza! Asante.” “Na endelea kufikiria. Usiishie hapo. Akili
ifikirie kila wakati. Kuwa mbunifu wa kidogo unachopewa. Utafika mbali sana.”
“Asante Joshua. Lakini nilikuwa nikitamani kazi ambayo sitahitajika kazini
mpaka siku za jumamosi ili siku za jumamosi niwe nafanya mambo yangu haya ya
mavazi.” “Mwanzoni hutakuwa na jinsi ya kuepuka kulipa gharama, Naya. Hakuna
kitu kizuri kinakuja kwa urahisi. Inamaana itabidi kukata muda wako kwenye
mambo fulanifulani ili kupata yote, au sasa, kuchukua hatua ya imani ukijiamini
na upande wa mavazi, uachie ajira.” “Hii kazi ninayofanya mimi, ndiyo
inategemewa kwa asilimia kubwa sana pale nyumbani. Baba hana kazi na biashara
nyingi zilimfia. Malon alimpa kazi kule Mbeya. Lakini si kitu ambacho
ataendelea kufanya. Kuwepo Mbeya na kutuacha sisi!” “Ni kweli familia
itayumba.” Joshua akakubaliana naye.
“Tulikuwa
tukifikiria naye awe anachukua mchele kutoka kwa Malon kwa bei ya jumla na
kuuza, lakini nafikiri amenihurumia. Amesema kama nimeamua kutoendelea kuwa na
Malon, tumuache kabisa. Tutafute njia nyingine ya kuianza hiyo biashara.”
“Kwani si mlitaka tu bidhaa? Sioni tatizo.” “Ni bidhaa tu, ndiyo. Ila kwa mkopo
ili pesa aliyo nayo na nitakayopata mimi kwenye mshahara, isaidie kukodi sehemu
yakuhifadhia huo mchele utakapokuja. Na tulitaka iwe sehemu ya wazi, penye watu
wengi. Kibaha, aliona sehemu inayofaa. Lakini tumeona tuache kwanza, tufikirie
kufanya biashara tutakayomudu bila kumwingiza tena Malon kwenye maisha yetu.”
Joshua akanyamaza.
“Ila
nimefurahi kama wazo langu umelithamini Joshua. Maana hiyo ndio fani yako na
wewe ndio unajulikana mzaa maono ya ile kampuni. Kwa kuhakikisha na mimi
najulikana, imenigusa sana. Asante.” “Karibu. Ni wazo lako. Mungu alikupa wewe
wala si mimi. Siwezi kuchukua kisicho changu. Nilikwambia Naya.” Naya akacheka
taratibu. “Mimi sina tamaa. Vyangu navijua, na ninajua kuvimiliki.” “Nimeamini.”
Naya akajibu akiendelea kucheka taratibu akimfikiria Joshua Kumu huyu ambaye
nilaini ndani kuliko yai. Alijawa na kushangaa pamoja na kumuhurumia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Joshua?”
Naya akaita wakiwa njiani kurudi nyumbani kwao. “Niambie Naya.” “Nashukuru
nimekuwa na wakati mzuri. Sana.” “Karibu, hata mimi nimekuwa na wakati mzuri.
Nikuulize swali Naya?” “Nakusikiliza.” “Nikipanga tena kutoka, ungependa?”
“Popote na wewe, Joshua.” Joshua akacheka akimwangalia. “Kweli. Kama
nisingekuwa na wewe leo, ningelala tena nikilia. Lakini umejishusha,
umenivumilia mpaka nikapata wakati ambao hata sikutegemea! Wewe ni mnyenyekevu
Joshua! Mpaka umenishangaza.” “Kwa kuwa najua Mungu amekuleta kwangu kwa
makusudi Naya.” “Nashukuru Joshua. Tafadhali nivumilie tu. Naamini nitakuwa mtu
ambaye utakuja kunifurahia.” “Hata sasa nakufurahia Naya. Sijaona tatizo
lakuvumilia bado.” “Kweli Joshua?” “Nisingetaka uwe na mimi kwa muda mrefu
hivi. Ni kwakuwa nakufurahia.” Naya akaridhika na kutulia.
Joshua
akaanza kuimba tena, lakini taratibu tu Naya akimsikiliza na kucheka huku
akimsifia hapa na pale mpaka wakafika nyumbani kwao. Wakaingia wakionekana
walikuwa na wakati mzuri. Naya alijawa cheko lililoonekana tokea anaingia
mlangoni. “Mmeshakula?” Baba yake akawauliza. “Tumekula tayari.” Akajibu Naya.
“Najua kuendesha boti, baba.” Naya akajivuna. “Mara hii!?” “Amenifundisha
Joshua. Tumekaa baharini muda wote. Joshua amenifundisha.” “Nawahurumia samaki
huko baharini!” Bale akafanya wote wacheke mpaka Joshua. “Wivu tu Bale. Muulize
Joshua kama sijamshangaza kwa uhodari wangu.” Wakazidi kumcheka. “Umeendesha
vizuri sana utafikiri mzoefu!” Joshua akamsifia.
“Ngoja
niwaonyeshe picha labda mtamuamini na Joshua.” “Nilikuchukua video Naya. Acha
niwaonyeshe video.” “Kweli!? Hata sikuwa najua!” “Ningekwambia
ningekuchanganya.” Joshua akawawekea video wakaanza kuangalia. “Kweli bwana!”
Bale akaamini. “Umeniona sasa?” “Hapa nimeamini.” Picha walizojipiga zilikuwa
nyingi na nzuri sana. Walipendeza na wote walikuwa wakicheka. “Naya ulivyokuwa
ukicheka!” “Sikupata muda kama huu kwa muda mrefu sana. Ni kweli nimekuwa na
wakati mzuri.” “Umekumbuka kushukuru?” Baba yake akamuuliza. “Nimemshukuru.”
Naya akajibu na kumuangalia Joshua. “Hata mimi nimeshukuru, nimekuwa na wakati
mzuri sana na Naya.” Joshua naye akaongeza. Wakaangaliana na kucheka.
Wakawaona.
“Labda
mngekaa.” Zayoni akafanya wacheke. Wakaenda kukaa upande wa sehemu yakulia
chakula. Wakaanza kuonyeshana picha. “Hii nzuri Joshua. Nitumie.” Wakawasikia
wakizungumza. “Na mimi hii nimeipenda Naya. Naiweka screen server yangu.”
“Joshua wewe!” “Kweli. Au wewe hujaipenda?” “Nimecheka sana bwana! Meno yote
nje!” “Ndio nzuri, na ikakufanya uvutie zaidi.” Bale na Zayon wakaangaliana,
baba yao akawafanyia ishara wasicheke. Naya na Joshua walikaa pale mpaka Zayoni
akaaga kwenda kulala. Joshua akaaga na yeye.
“Acha
nimsindikize.” Naya akawahi na kutoka na Joshua nje baada ya kuagana ndani.
Wakawasikia wamekaa nje kwenye ngazi, maongezi yakaanza upya tena Naya ndiye
anayecheka kama saa tano asubuhi. Bale naye akasubiri mpaka akachoka na kwenda
kulala. Saa tano usiku ndipo Naya akaingia ndani, Joshua naye akaondoka baada
ya kuhakikisha Naya amefunga mlango. Baba yake bado alikuwa amekaa tu sebuleni
akisinzia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Haya, Joshua amejiacha wazi kabisa kwa Naya. Lakini anataka kujenga
msingi wao wawili tu. Yeye yupo tayari, kazi na wajibu ni kwa Naya ambaye
ameshaanza kukiri kumpenda Joshua na linaonekana tumaini kubwa sana. Si kwenye
mapenzi tu ambapo amemfanya awe na furaha juma zima na kuitimisha siku hiyo ya
jumamosi botini, hata kwenye taaluma pia. Amemnyanyua Naya kutoka chini ambako
hakuwa akijulikana na yeyote kwenye kampuni yao, mpaka sasa ni gumzo kwenye
kampuni! Juhudi za Naya zinaonekana
kuanza kuzaa matunda pale kazini. Karama yake ya ubunifu inaanza kumketisha na
wakuu.
Ø
Je, Watafanikiwa?
Ø
Je, Umbali gani Naya atakwenda kwa ajili ya kuwa na Joshua tu?
Amekiri wazi kama ni mali, basi angezipata kwa Malon. Malon hakuwa mchoyo kwa
Naya. Anamtaka mtu wake, sasa kampata Joshua mwenye sharti linalosikika gumu.
Gari.
Ø
Je, Naya ataweza kulipa gharama?
Ø
Familia itachukuliaje hilo?
Ø Changamoto gani
watapata kazini?
Usikose
Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment