Jumatano
![]() |
Joshua alijua anachofanya, akatulia tu akimsikiliza Jamal bila
yakumwangalia yeye. Jema akamwangalia akimshangaa. “Sio hapa Joshua! Ni...”
“Shhh! Come on Jema! Quiet.” Akamtaka anyamaze kwa sauti ya ukali kidogo. Jema
akamwangalia na kurudisha macho akimsikiliza na yeye Jamal akawa kama haelewi.
Kila mtu akawa kwenye tabia njema, Jamal hakuzungumza sana, akamkaribisha Joshua.
“Jamani. Na mimi nilitaka kusikia tu. Napita.” Jamal akajichekesha kidogo na
kufunga kikao. “Kikao kinaanza baada ya dakika 5, Joshua!” Jema akaongea kwa msisitizo. “Nakuja.”
Akajibu na kusogea kwenye meza ya Naya.
Naya akacheka kwa aibu. “Uliamka salama?” Naya akamuuliza kwa kujali. “Nililala kama mtoto mchanga, nimekuja kuripoti kwamba, naanza kazi.” Naya akacheka akikumbuka mazungumzo yao ya usiku uliopita. Hakuna aliyeelewa, ila wao wawili walielewa. “Haya, wahi kwenye kikao, usichelewe.” Naya akamnong’oneza. “Nashukuru!” Joshua akajibu kwa heshima, na kuondoka kwa haraka Jema alikuwa akimsubiria pale alipomuacha macho kwenye tablet iliyo na ratiba ya Joshua ya siku hiyo nzima. “Simu ya kwanza nimemwambia Fina aitume hapa kama bado utakuwa hujafika ofisini. Ila kikaoni tumebakisha dakika 3.” Naya akasikia akipokea maelezo huku wakiondoka pale. Naya akajisikia vizuri. Ila akarudisha macho kwenye kompyuta bila yakutizama watu aliojua fika wanamtizama kwa wakati huo Joshua ameondoka.
Njama!
K |
wenye mida ya kama saa nne hivi Naya akashitukia Njama amemsimamia
mezani kwake. Kidogo Naya akaingiwa na hofu, maana hawakuishia pazuri na Njama.
Alimjua kama ni mmoja wa wasaidizi wakaribu sana na Joshua, na wote wawili
Njama na Jema wakiongozwa na huyo kiongozi wao Joshua walijulikana kwa maringo.
Ila Njama aliongeza na jeuri ya madaraka. Alipomtongoza Naya akijua kwa hakika
Naya angembabaikia na kumkubali kwa haraka, tena akiwa mgeni kabisa na wenzie
waliyeanza naye kazi kwa wakati mmoja, walishaanzisha mahusiano, Naya
alimkatalia bila kumumunya maneno, wala kutaka kuzungushana.
Njama alianza
kwa ubabe kidogo akimtaka watoke naye kwa chakula cha mchana, Naya hakuweka
sura ya kike ila ya kazi, akamwambia hatatoka, ana mambo ya kufanya. Njama
akajaribisha tena kumwambia amtoe mida ya jioni baada ya kazi, Naya akamwambia
‘Hapana, asante kwa ofa lakini nisingependelea’. Naya alimjibu akimtizama machoni kumuashiria hampi jibu la mtoto wa kike kumzungusha kwanza
ndipo amkubalie baadaye. Akamuonyesha hana shida kwa wakati ule wala baadaye.
Ilimuuma sana Njama hasa jinsi alivyojiona, wadhifa wake na vile
alivyo halafu kuja kukataliwa na mtu kama Naya, tena mgeni tu pale kwenye
kampuni! Alijua wazi wenzie Naya, wangemtamani na kumkubalia kwa haraka ili
kuja kupata ajira za kudumu kwa haraka. Ni yeye Njama, mtu wa karibu sana na
Joshua, kiongozi wa bosi wao Jamal! Ikamshangaza sana Njama. “Anaweza vipi
kunikataa mtu kama mimi!” Akawaza
bila kuamini. Halafu Naya aliyeanza kazi kwenye kampuni hiyo hakuwa wala wa
viwango kama enzi akiwa na Malon! Hakuwa hata na mvuto wowote ule. Hakuweka urembo
wowote usoni, kichwani hata masikioni hakuwa akivaa hereni, uso wa maombolezo, kuondokewa na mama yake.
Akaendelea hivyo mpaka aliposhauriwa na Malon arudishe urembo wa nywele, ndipo
akaanza kujitengeneza tena.
Naya akarudisha mvuto wa hali yake, na umbile alilojaliwa, sura
nzuri, rangi tulivu ya mwili wake, vikachanganya wengi. Ndipo Njama sasa akaamua
kumwambia waziwazi kabisa kuwa anataka mahusiano naye. Na hapo napo Naya
hakumzungusha, alimpa jibu la moja kwa moja. “Hapana Njama. Sitafuti kuwa na
mahusiano kwa sasa.” Alimjibu hivyo na kuondoka ofisini kwake akiwa ametumwa na
Jamal ofisini kwake kumpelekea mafaili aliyokuwa akiyafanyia kazi yeye mwenyewe
Naya. Kile kitendo kilimuuma sana Njama, akahisi atakuja kudhalilika sana pindi
watu wakija kujua amekataliwa na Naya, asijue Naya hakumwambia mtu.
Sasa kuja kuona baada ya muda mfupi sana Naya yupo na Joshua bosi
wake, ikamuuma zaidi. Akahesabu Naya anamdharau yeye kwa kuwa hana cheo kama
cha Joshua. Asijue Joshua mwenzie alitokea wakati muafaka kwa Naya ambaye
alishajivua kwenye mahusiano yaliyokuwa yamemfunga ya kimapenzi. Yeye Njama
alitokea wakati Malon ndio amerudi tena kwenye maisha ya Naya aliyekuwa na
majonzi ya kupotelewa na mama. Hilo ni moja. Pili alikuwa amechanganywa na
Malon huyu aliyerudi na mwanamke wa safari hii ambaye anajielewa, sio kama
wanawake zake aliokuwa akiwatoa tu nguo bila thamani, Rita. Mwanamke msomi,
ametulia, hana shida ya pesa ya Malon ila mahusiano ya kweli.
Na Malon huyu akarudi akionekana amemfanyia Rita kama yeye tu
Naya. Anafahamika mpaka nyumbani kwa kina Rita, kama nyumbani kwa kina Naya!
Anamfahamu Nolan kama Bale tu. Halafu wamesafiri kwenda mapumzikoni/ kwenye
safari za kibiashara za Malon kama vile alivyokuwa akienda naye Dubai. Kwa Naya
yakawa mapumziko, ila kwa Malon biashara na mapumziko. Hilo likamtingisha Naya
vilivyo na kumnyima raha zaidi. Kwamba kwa mwanamke huyu naye amekwenda naye
umbali mwingine zaidi kama kwake! Mbaya zaidi hakuwa amemtambulisha kwa Rita au
hata kuonyesha anamfahamu!
Akawa kwenye kipindi cha kusubiria pengine Malon hata atamtafuta
baada ya kurudi safari, lakini kimya. Akasema pengine baada ya kukutana kwenye
kesi na kuwapa pole ya kumpoteza mama, pengine atamtafuta tena lakini kikawa
kipindi cha kusubiri tu. Kila wakati macho kwenye simu, akirudi nyumbani akawa
akitegemea kusiki pengine alipita hapo, lakini kimya.
Naya akabaki akisubiri na
kusubiri bila kutaka kujichanganya na mwanaume yeyote yule ili Malon
atakapomrudia asimkute na mahusino yeyote yale wakashindwa kurudiana. Na ndio
kipindi hicho nacho Njama eti ndio akajiweka wazi kwa Naya. Naya alimkatalia
bila kufikiria mara mbili akijua Malon wake amerudi tena. Watarudiana. Lakini
napo kama kawaida ya Malon hakutokea mpaka Naya alipomfuata yeye mwenyewe na
zawadi. Njama akakosa, Malon akakosa ndipo akajitokeza Joshua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa Naya!” Naya akageuka vizuri wakati akifungua huo mfuko
aliokuja nao. “Habari yako Njama?” Naya
akajaribu kumsalimia lakini Njama hakujibu ile salamu, akafungua mfuko aliokuwa
amekuja nao. “Hii ni bluetooth. Nafikiri una smartphone yenye uwezo wa
kuunganisha bluetooth. Si ndivyo?” “Ndiyo.” Naya akaitika akiivuta simu yake.
“Nimesha zichaji zote mbili. Hii ina uwezo mkubwa sana. Unaweza kuitumia si
chini ya masaa 12 bila kuishiwa chaji. Lakini hii ya pili, ni masaa 6 tu. Kwa
hiyo wakati hii ukiwa umeiweka kwenye umeme, unaweza kutumia hii. Nafikiri
ukisoma maelezo yake hapa, utaweza kujiunganishia mwenyewe kwenye simu yako.”
“Ndiyo, nashukuru.” Naya akamshukuru lakini akajua japokuwa hajamwambia kama
inatoka kwa Joshua, alijua ametumwa ndio maana amekuja pale kama na hasira
fulani hivi na kushindwa hata kuitika salamu yake. Ofisi nzima kimya.
“Kwa hiyo si unaelewa badala ya kuweka simu masikioni, unapachika
hizo bluetooth masikioni, unasikia kama kawaida? Au huelewi lolote juu ya
bluetooth?” Akamuuliza kwa sauti ya juu tu kama kumdhalilisha. Naya
akamwangalia machoni akijua ni wivu tu ndio unaomsumbua. “Nafahamu.” Naya
akajibu kwa kifupi tu akimtizama lakini akiwa ameshangazwa sana na Joshua! Katikati ya mambo yake mengi hapo
kazini na bado ameweza kumfikiria kumnunulia bluetooth! Akakumbuka pengine ni
vile walivyozungumza muda mrefu usiku uliopita mpaka akaishiwa chaji kwenye
simu yake!
Akavuta zile bluetooth, akacheka
asijue Njama anamwangalia. “Sijui kuna swali lolote kabla sijaondoka?” “Hamna
swali. Nimeelewa. Asante na nitamshukuru Joshua mimi mwenyewe.” Naya akafanya
makusudi kumwambia hivyo tena macho yakiwa kwenye zile bluetooth zilizoonekana
ni za hali ya juu sana, Njama akaondoka pale bila ya kuaga.
Mbaya zaidi akakutana na Jamal koridoni akiwa anatoka hapo kwa
Naya na hasira. “Naona siku hizi mnatutembelea tembelea sana huku kwetu!” “Sasa
hivi ndipo kwenye mzinga.” Njama akajibu akiondoka Jamal akicheka kwa uzuri tu,
asijue kinachoendelea moyoni kwa Njama. “Nimekusikia Njama.” “Basi ujue nyuki
tutarudi tu hata kwa kutumwa. Kazi kwako kusafisha mazingira.” “Mbona nishaanza
tokea manyunyu!” Naya alikuwa akiwasikiliza tu. Njama akasikika akifunga mlango
kwa nguvu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hapohapo Naya akamtumia ujumbe Joshua. ‘Nashukuru sana
kwa bluetooth za hadhi ya juu.’ Joshua alicheka wakati akisoma. ‘Acha utundu
Naya. Nipo kikaoni. Nitakupigia.’ Akiwa katikati ya kikao, akiwa
anazungumza wakamuona ametoa simu mfukoni. Akasoma ujumbe, wakamuona akitoa
tabasamu. Bila shaka, akajibu hapohapo mbele za watu, kisha akaendelea.
“Samahanini. Kama nilivyokuwa nikisema....” Jema na Njama wakaangalina. Siku
hiyo ikaisha, Naya hakumuona tena Joshua.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwenye mida ya saa 6:30 jioni, akiwa chumbani kwake akampigia. “Ulisema na
wewe ni mvumilivu, si ndiyo?” Naya akacheka. “Pole na kazi na hongera kwa
majukumu.” “Nashukuru. Nivumilie tu. Leo ilikuwa mbiombio muda wote mpaka sasa
hivi nipo ofisini.” “Ulikula sasa?” “Hata sikupata muda. Nitakula nikifika
nyumbani.” “Mwenzio hapa naongelea bluetooth zangu. Sitaki mchezo.” Joshua
alicheka sana. “Naya!” “Usinione hivi. Nishaachana na mambo ya kubeba simu kila
wakati au kushika kama andazi! Mimi sio mwenzio.” Joshua akazidi kucheka. “Ushakuwa
matawi?” “Ya juu mno. Sitaki mchezo mimi . Siku hizi na paa na wale ndege aina
ya tai tu. Sio ndege kama mwewe. Huwezi kuniweza hata kidogo.” Joshua alizidi kucheka.
“Kumbe ni afadhali nilivyokupigia simu sasa hivi! Nilikuwa
nimechoka! Nikasema nikupigie, nikusikie, nipate nguvu yakurudia nyumbani.”
“Nikwambie ukweli Joshua?” “Nakusikiliza Naya.” “Unanifanya nijione ni wa
muhimu sana kwako!” Joshua akacheka kidogo. “Kweli.” “Na ndivyo ulivyo Naya. Najua
wewe unaweza usielewe sasa hivi. Ukahisi ninakurupuka, lakini sikurupuki. Wewe
siku unaniona kwa mara ya kwanza, kwangu ilikuwa mara ya tatu.” Naya
akashangaa sana. “Au umenifananisha Joshua!?” “Hata kidogo. Hivi si nilikwambia huwa
nakosea kidogo sana?” Joshua akamuuliza kwa kujiamini tu.
“Uliniambia.” “Basi amini ulikuwa ni wewe Naya. Siwezi
kukufananisha.” “Ulinionea wapi!?” Akamsikia Joshua akicheka taratibu. “Ya kwanza
ulipokuja kwenye usahili. Mlikuwa mkisubiria nje ya ofisi za mwajiri. Ulikuwa
na wasichana wengine, mmefika pale kwa usaili. Nakumbuka mpaka nguo uliyokuwa
umevaa.” “Joshua!!” “Hakika. Kwa kuwa nilikuwa ndani nikizungumza na meneja wao
pale, na Jamal alikuwepo akipitia CV zenu walizokuwa nazo pale ofisi za mwajiri
ili kuanza huo usahili. Nyinyi mlikuwa mkisubiria nje ili usahili uanze,
muingie ndani. Nilikuona kwa kupitia kioo ndani ya ofisi ya mkuu wa kitengo
chao cha waajiri.” Joshua akacheka.
“Mimi huwa sichanganywi hovyo Naya! Sikujaliwa tamaa za wanawake.
Hata Jema anaweza kuja kukwambia ukija
kumzoea. Lakini nilishangaa kwako ilikuwa tofauti.” Naya
akatulia kabisa. “Baadaye nikataka kumuulizia Jamal kama ulipita kwenye usaili,
lakini Roho wa Mungu akanionya kabisa. Nikaanza kukuombea.” “Joshua!?” Naya akashangaa sana. “Sikudanganyi Naya. Sasa nikamsikia Njama akimchokoza Jamal
kama amefanikiwa kupata warembo. Si unajua jina wanalo waita pale?” Naya akacheka.
“Basi akauliza mmepata kuku wageni wangapi? Kama unavyomjua Jamal,
akawa hajaridhishwa na wengi wenu mliokuja pale. Akasema angalau mmoja, ila
wawili ndio wasindikizaji. Angalau akikwama kabisa, anaweza kuwatafuta hao
watatu. Akawa analalamikia wasomi wanaohitimu wa kizazi hiki. Akalalamika weee
kama unavyomjua, lakini pia nilishindwa kumuuliza katika huyo mmoja
aliyemfurahisha ni nani!” Joshua akaendelea.
“Ndio maana mliona hamkuitwa kazini muda mrefu, maana Jamal akaona
kama mtampotezea tu muda, akaomba nizungumze na HR ili wale waliokuwepo
waajiriwe kwa haraka na wapewe mafunzo waweze kufanya mpaka kazi alizotaka
nyinyi mfanye. Kufupisha habari, nafikiri wale vijana umefanya nao kazi,
umeshawajua kwa sehemu. Ndio maana ulikuwa ukimsikia Jamal akigomba kila
wakati.” Naya akacheka tu bila kuwasema wenzie. “Katika
kusitasita kwake yeye mwenyewe Jamal, mara aseme wapewe ajira, mara akirudi
anakuwa amekasirika anataka wafukuzwe ndipo nikamkumbusha nyinyi watatu ambao
alisema ni afadhali. Akalalamika zaidi ya siku mbili akisema anahisi atakuwa ni
kama anajiongezea tu maradhi. Sikumlazimisha, ila nikamuonya kuwa, lazima mimi
nipate matokeo ninayotaka, na sitaweza kumsubiri kwa kuwa malengo yangu yote
yanategemeana na watu wa ngazi ya chini kabisa.”
“Nikamwambia nitakapotaka matokeo mazuri, sitaangalia sura, wala wao
anao walalamikia, nitamuwajibisha yeye. Nafikiri ndipo akaingiwa hofu,
akawapigia nyinyi. Hata sikujua kama na wewe ni mmoja wapo. Sasa mlipoanza kazi
tu, niliambiwa natakiwa kuja kuzungumza na nyinyi kama kiongozi wa kitengo.
Siku hiyo nikawa na mambo mengi, Jema akafuta hiyo ratiba, akamwambia Jamal
atamjulisha lini nitakuwa na nafasi. Hayo nilisikia tu kutoka kwa Fina.
Nilimkuta akizungumza na Jamal pale mezani kwake. Jamal aliponiona tu akaondoka
kwa haraka, mimi wala sikumsemesha, nikapitiliza ofisini kwangu. Ndio Fina
akaja ofisini kwangu kuniambia Jamal alikuwa pale akilalamika kuwa Jema
anadharau mipango yake ndio maana inakuwa rahisi kuifuta kwenye ratiba zangu.
Mimi hata sikujua kama Jema alibadili hiyo ratiba. Basi, lakini nilikuwa na
shauku sana kujua kama ulirudi pale, yaani kama na wewe ni miongoni mwao.” Naya alikuwa
ametulia kimya akisikiliza na mshangao mkubwa sana.
“Siku moja nikiwa kwenye gari nazungumza na simu. Tulikuwa ndio
tumerudi tu hapa ofisini, nikawaona mnapita nyinyi watatu na Jamal. Nafikiri
mlikuwa mkiendelea na kuzungushwa kwenye vitengo vingine ili mvifahamu, sina
uhakika. Naya?” “Nipo Joshua!” “Nilishindwa kuzungumza kwa sekunde kadhaa kwenye
simu mpaka niliyekuwa nikizungumza naye akahisi simu imekatika. Nilibaki
nimeduaa, nikijiuliza kama kweli nimekuona tena! Ila safari hii ulirudi ukiwa
umekata nywele, ukawa umepungua zaidi na umenyongea, sio kama nilivyokuona mara
ya kwanza.” “Na bado uliweza kunitambua Joshua!? Maana ni kweli najua
nilibadilika sana.” “Nakwambia Naya, naangalia kwa macho yangu haya ya binadamu
wanayaona watu, na ya rohoni Mungu anaponiongoza. Ipo connection naipata nikiwa
nawewe, sijawahi ipata kwa mwingine.” “Jamani Joshua! Mpaka
nasikia machozi yanatoka!”
“Mimi sio mtu wa kuzungumza baada ya kazi Naya. Nakuwa nimechoka
maana kazi yangu ni kama nazungumza siku nzima. Huwa nikirudi nyumbani hata
Jema anajua. Sitaki kuzungumza na yeyote. Nataka pawe kimya kabisa ili akili
zangu zitulie. Kila kitu kinachonihitaji mimi, Jema na Njama wakijua nimeshashushwa
nyumbani, wanahangaika nacho mpaka siku inayofuata. Lasivyo nisingeweza kufanya
mambo ninayoyafanya. Nilishawaambia nikiwa nyumbani, ni muda ambao huwa sitaki
mwingiliano. Na hilo wamelielewa. Ila sio kwako. Nikizungumza na wewe, nasikia
faraja na najikuta natulia.” “Jamani Joshua!” “Sikutanii Naya. Jana
nilipokwambia huna haja ya kukata simu hata ukilala, nilibaki na wewe pale, na
nitakuonyesha kazi kubwa niliyofanya usiku wa jana.” Akamsikia
Naya akilia.
“Usilie sasa.” “Natamani ungeniambia hivyo mapema! Nilikuwa kwenye mateso
Joshua wewe! Upweke mkubwa sana.” “Haukuwa wakati wa Mungu Naya. Na mimi
nilitaka kukwambia wakati ule, lakini pia Mungu akanionya. Nafikiri haukuwa
tayari kwa ajili yangu, na nafikiri Mungu hakutaka nianze kwenye mwingiliano.” Naya akaelewa
kuwa ni sababu ya Malon bado alikuwa kwenye picha. “Njia za Mungu
sio zetu Naya. Na ugumu mwingine tunakutana nao ni kwa sababu ya kujaribu
kuwahi kabla ya wakati wa Mungu.” “Mimi ni muhanga wa hilo.” “Lakini naomba
iwe ni shule uliyohitimu, Naya. Usikubali kuteswa sana na shetani. Jisamehe, na
utoke hapo. Naahidi kukuombea pia.” “Asante. Endelea kunisimulia.” Joshua
akacheka. “Acha nitoke hapa, ili na kina Jema nao wakapumzike.” “Kwani bado
hawajaondoka tu mpaka sasa!?” “Sasa wanaondoka vipi na mimi bado nipo?” Joshua
akaongea kwa kujivuna kidogo. Naya akacheka. Wakaagana.
Akiwa njiani, akampigia tena simu. “Usinichoke.” “Ungejua jinsi
ninavyofurahia! Natamani ningekujua mapema.” Joshua akacheka sana. “Kweli Joshua.”
“Haukuwa tayari kwa ajili yangu Naya. Hata ulivyonitizama siku nilipokuja
kufanya kikao na nyinyi pamoja na viongozi wote wa kitengo chetu, pia hukuwa
tayari. Unakumbuka mimi mwenyewe niliomba tujitambulishe ili tufahamiane?” Naya
akatulia kukumbuka. “Tena nilisema tujitambulishe na kusema hata kabla ya pale tulikuwa
tukifanya kazi sehemu gani nyingine. Unakumbuka?” “Joshua, yote hayo wewe
unakumbuka!?” “Siwezi kusahau kwa kuwa nilikuwa na sababu. Nia yangu nilikuwa nikitaka
nikusikie wewe vizuri. Maana pia nilijua haupo tayari na sikupata kibali cha kukufuata.”
“Joshua!” Naya akashangaa sana.
“Na nilijua pia hukutilia maanani wakati najitambulisha maana
uliinama tu, ukiangalia simu yako.” “Joshua!” “Kweli Naya. Muda mwingi macho
yalikuwa kwenye simu na mimi sikuwa nimezoea hivyo. Huwa nikizungumza ni kweli
watu wananisikiliza kwa makini. Wewe hukunitilia maanani kabisa. Ukaonekana upo
mbali kabisa na pale, ni kama uliyetaka tumalize, tuondoke pale.” Naya
akakumbuka ndio kipindi alikutana na Malon, akahisi pengine angekuja kumtafuta
tena. Ni kweli alikuwa akiangalia simu yake kila wakati akitaraji hata ujumbe
wa salamu kutoka kwa Malon, lakini hakukosea hata kumtumia ujumbe wa kumwambia
alifurahi kumuona. Naya akapoa.
“Basi mimi nakumbuka mpaka leo jinsi ulivyojitambulisha. Ilikuwa kwa
kifupi sana.” “Pale Jamal alikuwa ashatutisha vyakutosha kuwa tukileta urembo
tu, anatufukuza kazi.” Joshua akacheka. “Alishachoshwa na watu wa kile kiofisi chenu.
Lakini turudi kwako Naya. Ulijitambulisha jina lako, kuwa unaitwa Naya.
Hukusema hata jina la mzee. Ukataka kukaa, Jamal akakukumbusha useme ulitokea
wapi kabla ya hapo. Unakumbuka?” “Joshua wewe!” Naya akashangaa sana.
“Ndio ujue sijakurupuka. Mwenzio nakufahamu. Tena na hapo ukasema kwa
kifupi tu bila hata kutaja jina, kuwa ulikuwa ukifanya kazi katika shule, basi.
Ukakaa. Ila nikahisi kama Jamal alikustahi! Maana mimi namjua yule, angekusimamisha
mara kadhaa. Ndipo nikajua kwa hakika wewe ndiye aliyekuwa amekutaka tokea mwanzo, na wale wengine ni wasindikizaji kama
alivyosema. Na baada ya hapo akawa anasema kule ofisini kwetu bila kuwaambia
nyinyi kuwa, isingekuwa wewe, angeshafunga kile kitengo afanye kazi zote
mwenyewe huku akianza kuajiri upya. Nilifurahi sana.” “Haiwezekani Joshua!
Jamal?” Naya akashangaa sana.
“Ni vile hataki wengine wajue. Lakini Jamal anapenda sana utendaji
kazi wako. Kwanza anasema unaonekana umetulia
na unajielewa. Huna papara na husubiri kupangiwa. Anasema ingekuwa mwingine
vile unavyowahi kuingia asubuhi, ungekuwa kwenye mitandao tu ukifanya yako, lakini
anasema kila wakiingia ofisini, anakuta umesogeza kazi za idara tena bila
kutumwa. Anasema hujui kubishana kama wengine, na anasema hujawahi kumlalamikia
kwenye lolote. Ni siri nakuibia, ili kukutia moyo. Na ndio maana kila safari
anayowapangia pale, anataka na wewe uende.” Naya akashangaa sana.
“Nilisikia kuna safari moja mlipangiwa, na wewe akataka uende,
nilisikia tu kuwa umeomba usiende, kwa sababu za kifamilia.” Akakumbuka
Malon alimshauri hivyo ili abaki na Zayon wakati anaongozana na baba yao. “Unakumbuka?”
“Nakumbuka Joshua. Jamani nilishukuru Mungu sikwenda nao kwenye ile safari maana
waliporudi Jamal alikuwa akigomba, mpaka ofisi ilikuwa ikizizima. Mimi nilijua
atawafukuza kazi.” “Hakuna walichofanya
na ukumbuke hapo tuliwekeza pesa nyingi ya kitengo, kwenye ile safari.
Ilinibidi kufikiria kwa haraka, ili tufanye kitu, ili ile safari isiwe bure.
Katika ujinga na uzembe wao, nikautumia kwa haraka, ili nitimize lengo. Na
kweli tukafanikiwa kuuza mpaka kufikia lengo.” “Lakini mbona nilisikia kama
wamepewa onyo, wakirudia tena ndio wamejifukuzisha kazi.” Joshua
akacheka.
“Ni wewe nini?” “Ni Jamal kwa sababu nilimwajibisha na yeye. Na ndio
maana unamuona na yeye ameongeza umakini. Tuache hayo turudi kwako. Ile hali niliyokuona
nayo ya kunyongea, macho kwenye simu muda wote kama ambaye unatarajia kitu kisichokuja, na ukawa
umekata nywele, nikazidi kukuombea kwamba Mungu akukutanishe na muujiza wako
ili upate furaha. Nikawa nikikukumbuka sana lakini ikawa kuonana kwetu ni kama
hakupo. Sikuoni popote hata ukipita. Lakini nilijua wakati wa Mungu haukuwa tayari,
maana Mungu wangu huwa ana njia zake za kunikutanisha na vilivyo vyangu. Nikawa
mpole tu.” Naya akacheka taratibu.
“Sasa niliposikia safari ya Mbeya, Jamal akaniomba niongozane naye
kufunga ile kazi. Nikaona ni kama njia yakumpongeza, maana nilikuwa nimemkaba
sana Jamal mpaka nikamuhurumia. Nikaona hiyo itamtia moyo lakini pia kwa kuwa
nilijua na wewe ungekuwepo, nikaona utakuwa wakati mwafaka! Sikutaka
mwingiliano wa Jema wala Njama. Nikawaambia wabaki ofisini, nikataka muda usio
na mwingiliano kabisa. Nikiamini ningeweza kukuona na kupata muda na wewe. Sasa siku ile
ya mwisho kule Mbeya, uliporudi pale hotelini na kwenda chumbani kwako moja kwa
moja, na mimi nikasema nisile mpaka utakapotoka. Pale nilikuwa nikikuwinda
utoke, nije kukaa na wewe.” “Kweli Joshua!?” “Hakika, sina sababu ya
kukudanganya.” Naya alizidi kushangazwa sana.
“Sikuwahi hata kufikiria!” “Na nilikaa kwenye kona kabisa na laptop
yangu kuashiria sitaki mtu anisogelee, nipo busy. Nikatulia pale mpaka ukaja,
ndipo nikarudisha vitu vyangu chumbani kwa haraka na kukufuata kabla hajafika
kukaa mtu mwingine kwenye ile meza yako.” Naya akacheka akisikika anavuta
kumbukumbua.
“Nikahangaika sana kukutuliza ili angalau usinikimbie, uweze
kuzungumza na mimi.” Naya akacheka sana. “Niligopa sana. Sikutegemea eti mtu
kama wewe uje ukae na mimi!” “Nilijua. Na vile ulivyokuwa ukinijibu kwa ufupi,
nilijua hutakawia kuniaga, ukale chakula chako chumbani, halafu gharama yangu
yote ya kukufuata Mbeya, tena kwa gari, ingekuwa bure.” Naya
akacheka sana. “Kwa hiyo unasema isingekuwa mimi usingekuja?” Naya
akauliza kwa deko. “Naya! Hivi unajua majukumu niliyo nayo lakini?” Naya
akacheka sana.
“Sasa ulipotulia na kuweza kuzungumza na mimi, ndio nikaelewa ni kwa
nini moyo wangu uliunganishwa na wewe. Mungu alijua hicho kichwa, na hiyo
hekima, itanifaa mimi.” “Lakini hata sikuzungumza sana!” “Ulizungumza kile
Mungu alitaka nikisikie. Basi.” Naya akacheka taratibu akifikiria.
“Sasa Naya, nimefika nyumbani. Niruhusu nikaoge, ndipo nikupigie. Si ulisema utanivumilia?” “Mimi ndio nafurahia. Tunakuwa wote japo kwa simu.” Joshua akacheka taratibu. “Basi nashukuru. Baada ya muda mfupi tu, nitakupigia ili tuimalize hii siku pamoja.” “Nitakuwa nasubiri simu yako.” “Sawa.” Naya akakata, akabaki akimfikiria Joshua. Ni kama alishafunga kwa Naya na kujihakikishia kwa asilimia zote, kuwa ni wake. Naya alikuwa amejawa furaha, hakuonekana tena kukaa sebuleni. Wakati wote walimsikia chumbani akizungumza kwa sauti ya chini, na kucheka. Angalau vilio vikaanza kupungua humo ndani kwao. Hatimae kwa amara nyingine tena ikatokea sababu ya kumtoa kwapani kwa baba yake muda wote.
Alhamisi.
A |
subuhi tena akiwa amewahi kama kawaida yake, akashitukia Joshua
anavuta kiti mbele yake. Naya akacheka. “Ulilala salama?” “Kama mtoto mchanga.”
Naya akacheka. “Na wewe?” “Tokea nilipokwambia nasinzia, ukaniambia nilale tu,
utakata simu ukitaka kulala, sijaamka mpaka alam iliponiamsha asubuhi hii.
Nikachukia nikatamani ingekuwa naamkia jumapili, nilale ukiwa umeniombea na
unanisubiria.” Joshua akacheka. “Usizoee. Wakati mwingine nakuwa safarini, nchi
zinazotofautiana masaa na huku.” “Nitaridhika na kuombewa tu, bila kulala ukiwa
masikioni kwangu.” Joshua akatoa tabasamu la kuridhika. “Kama ni hivyo basi
zoea.” Naya akacheka sana.
“Kwa hiyo sitakuja kujuta?” “Sio kutokana na mimi. Nikwambie siri
yangu nyingine?” Naya akacheka. “Niambie.” “Chochote kilicho changu. Hata
soksi. Ilimradi iwe yangu mimi, nikajua ni yangu, ujue nitaitunza na kuienzi.”
Naya akajisikia vizuri sana, akainama. “Siri nyingine hiyo. Na ndio maana huwa
sina vitu vingi. Vichache, na huwa nahakikisha navitunza vizuri sana na kwa viwango
vya juu. Ili Mungu aniamini kwa makubwa zaidi. Ndiyo siri yangu hiyo.
Naruhusiwa kuanza siku?” “Asante Joshua. Nimejisikia vizuri.” “Na ndivyo
utakavyokuwa kwangu. Mengine utagundua ni ubinadamu tu. Lakini sitakusudia
kukuumiza. Na nitafanya juhudi za makusudi ili nisikuumize.” “Asante Joshua.”
Joshua akabaki akimwangalia na tabasamu kubwa usoni, Naya akacheka kama hajui
aseme nini zaidi.
“Jema atanifuata sasa hivi akiwa na Njama.” Naya akacheka.
“Natamani uhamishie ofisi yako hapa kwangu.” Joshua akacheka sana. “Utaweza?
Maana mimi ili kazi zangu zifanyike, nilazima watu wangu watatu wanao nizunguka
kila ninapokaa kwenye meza yangu, wawepo ndipo siku ya kazi iende vizuri. Sasa
utatuweka wapi hapa?” “Nitashindwa kufanya kazi za Jamal.” Joshua akacheka.
“Hapana Njama. Lazima aanze nao kwanza.” “Acha kulazimishia vitu
visivyo na maana Jema! Ulazima unatoka wapi?” Wakawasikia Jema na Njama
wanakuja wakibishana. Naya na Joshua wakaangaliana. Naya akacheka. “Uwe na siku
njema. Ufanikishe kila kitu.” “Amina. Na wewe hivyohivyo.” “Kwanza mimi
nilishamtumia tokea saa moja kasoro.” Akaongeza Jema wakiwa wameshafika pale.
Joshua akasimama na kupita katikati yao, na wao wakageuza bila hata kupoteza
sekunde. Wakawa wakitembea nyuma yake. “Nilizungumza na wewe jana wakati
tukiagana, tukakubaliana vizuri tu na kupanga. Wanategemea simu saa moja na
nusu na wewe unalijua hilo tokea jana. Hiki unachotaka kufanya sasa hivi ni
fujo, Jema!” “Muulize kama hana....” Naya akaanza kufikiria jinsi atakavyokuwa
busy siku hiyo. Walisikika wakibishana wawili hao huku wakielekea ofisini kwao,
Joshua akisalimiana na wafanyakazi wengine hapo njiani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya karibia chakula cha mchana, Joshua akampigia simu. “Mlo uliotamani
jana usiku wakati nakula, unaletewa sasa hivi. Nilimwambia akupikie kisha akuletee,
uone kilivyo kizuri. Nimpishi mzuri sana. Naamini na wewe utapenda.” “Sasa na
wewe umeshakula?” “Nilimwagiza smoothie tu. Leo ratiba hairuhusu. Atakuletea na
matunda. Mlo mwema.” “Asante kujali Joshua. Sikutegemea!” Joshua
akacheka. “Karibu. Baadaye.” Wakaagana na kukata, Naya akabaki akimtafakari
Joshua.
Mara simu ya Fina, sekretari wa Joshua akimtaka Naya, ikaingia hapo
osifini kwao. Safari hii Naya akasimama na kufuata simu yeye mwenyewe. “Hujambo Naya?”
“Mzima kabisa, dada yangu.” “Sasa Joshua ametoka, ila chakula kimeletwa hapa.
Nataka kujua unakuja kula huku au kiletwe huko?” “Huku tafadhali dada yangu.
Asante.” Akamsikia akicheka. “Basi kinakuja.” “Asante.” Naya akakata
simu na kuvuta pumzi kwa nguvu.
Baada ya kama dakika 5 hivi akaingia kijana kama umri wa Joshua
tu, akamuulizia Naya akiwa na begi maalumu la kubebea chakula kisipoe. Naya
akasimama. “Mimi ndio Naya. Karibu.” Akamsogelea. “Mzigo wako huu.” Akaweka ule
mfuko pale mezani. “Asante sana, nashukuru.” Akaondoka, Naya akabaki na cheko
bila ya kumtizama mtu. Akachukua simu yake na ule mfuko akaenda sehemu ambayo
hula chakula. Wafanyakazi wenzake kimya. Naya hakujali, alijua kinachoendelea
mioyoni mwao. Hawakuwa wageni kwake, hakujishughulisha nao hata kidogo.
Simu ya Joshua ikaingia wakati akila. “Nahisi
nitajing’ata ulimi!” Joshua akacheka sana. “Taratibu Naya!” “Si kwa utamu huu!
Kumbe ndio unakula vizuri hivi!?” Joshua akasikika akicheka sana. “Anajua sana
kupika. Ni ndugu wa mmoja wa wale vijana niliokwambia niliwasomesha. Huyo ni
mdogo wake. Aliwahi kuja kumtembelea kaka yake pale nyumbani kipindi nikiishi
naye, akatupikia, kuanzia siku hiyo nikamchukua mimi. Nilimpeleka tu kuongeza
ustadi tu, lakini upishi ni karama yake. Anapika sana.” “Mimi nahisi
ningepasuka kwa kunenepa.” Joshua akazidi kucheka .
“Unafanya nini sasa hivi?” “Ndio napata mapumziko yale ya dakika 5,
ndipo niendelee na siku. Nimerudi ofisini muda si mrefu.” “Joshua?” Naya
akamuita kwa upole. “Nakusikiliza Naya.” “Asante kunijali na kunifikiria. Sikutegemea
kama ungefikiria kunifanyia yote haya. Asante.” “Karibu. Na nimefurahi kama
umefurahia chakula. Natamani na mimi ningekuwepo hapo tupate mlo wa pamoja.
Lakini ratiba yangu hairuhusu.” “Pole. Ipo siku tutapata muda wa pamoja. Mungu
atajalia.” “Jumamosi. Hiyo naisubiria kwa vitendo nikihakikisha hakuna kitu
kinaingilia siku hiyo, na Mungu asaidie.” Naya akacheka taratibu.
“Tena nimekuletea nguo. Zipo kwenye gari.” “Umeona mambo hayo? Asante sana. Njama atakuja kuchukua kwa ajili yakumpa dereva apeleke dry cleaner.” Naya akacheka akimfikiria Joshua. “Tutazungumza baadaye. Dakika 5 zinaisha. Acha nikasafishe kinywa.” “Sawa. Nakuombea ufanikiwe. Ila ujue unanifanya nakuwa na furaha.” “Karibu, na hiyo ndio ninataka kusikia.” “Asante.” “Byee.” Naya akaendelea kula.
Joshua kwa Naya.
Joshua akawa kama mtu wa kubuni kitu cha kumfurahisha Naya kila
siku awapo ofisini na ni kama alimuonyesha hamfichi kwa yeyote na anataka watu
wamjue ni wake. Aliweka umiliki mzuri kwa Naya, ambao haukuwa mzigo.
Alimuonyesha kumthamini sana na kumuhitaji. Alijishusha kwake akimuonyesha huwa
anamfikiria kwa maneno na vitendo. Alilizwa kutotambuliwa na Malon kwa Rita,
sasa hivi Joshua anamuweka mwangani, ashindwe tu yeye mwenyewe. Naya alijawa
furaha. Machungu yote yakafutwa ndani ya juma moja tu.
Kwa muda huo mfupi habari zao zikaenea kama moshi mkali,
usiofichika hapo kwenye hiyo kampuni. Akajulikana kwenye kampuni nzima. Kila
mtu akataka kumuona huyo msichana aliyemchanganya Joshua kiasi cha kujibu jumbe
katikati ya vikao! Akaunyanyua uthamani wa Naya kutoka mfanyakazi mgeni kabisa
ambao bado walikuwa wakisubiri ajira ya kudumu ndani ya hiyo kampuni, mpaka
kuwa mashuhuri.
Naye Naya akaongeza umakini sana ili asiharibu na kumwaribia sifa
Joshua. Hakuna kazi Jamal alitaka ifanywe pale kwenye ofisi yao Naya
asiichangamkie, tena kwa umakini mno ili asiharibu. Kuwahi kazini kukabaki
paleple. Alikuwa wa kwanza ofisini na alitulia, usingemkuta akizurula hovyo au
kwenye simu kila wakati nakushindwa kufanya kazi. Wengine walisema pengine ndio
maana Joshua alimpenda. Gafla kila kitu mwilini kwa Naya kikaanza kuonekana
kizuri. Watu wakaanza kusifia umbile, rangi ya mwili, muundo wa nywele anazoweka
kichwani. Nywele fupi. Kila kitu cha Naya kikaanza kuvutia sababu ya kuwa
karibu na Joshua.
IJUMAA.
S |
iku hiyo ya ijumaa nayo mida ya kabla ya kazi kuanza, Joshua
akatokea tena mezani kwa Naya. Alimtegemea Joshua kwa kuwa ndio muda alioweza
kukutana naye wakiwa ofisini japo kwa kifupu. “Pole, jana simu iliishiwa chaji
mapema wakati wa taarifa ya habari. Na huwa inachukua muda mrefu kuingia chaji,
nikapitiwa usingizi wakati nikiisubiria. Nimekuja kuamka saa 6 usiku. Nikajua
utakuwa umeshalala. Nimekosa kuagwa ili nilale unono.” Joshua akacheka sana
maana Naya aliongea kwa kulalamika. “Nilijua tu simu imekata. Pole. Kwa hiyo hukurudi
kulala tena?” “Nilirudi kulala kama kwenye saa 9, na saa 10 na robo huwa ndio
naamka ili saa 10:45 niondoke nyumbani. Nikachukia!” “Naomba kuiona simu yako.”
“Ila siyo mbovu. Usijali. Nilikosea tu muda wa kuichaji na...” “Naya! Nimeomba
kuona simu.” Naya akacheka na kuitoa mfukoni.
Akamkabidhi. “Nilikuaga na simu nzuri sana. Tulinunua Dubai.
Nikaja kuiuza.” “Kwa nini unauza simu!?” Naya akasita kidogo, ila akaona
amwambie tu maana Joshua akamwangalia akijua kuna kitu hapo. “Nilikuwa kwenye
kukusanya pesa ili kumuwekea dhamana Malon, wamtoe jela.” Joshua akashangaa
kidogo. “Subiri kwanza Naya. Kwa nini uuze vitu kumtoa jela na kwa nini
walimfunga?” “Malon alikuwa akiuza bangi. Na...” Naya akamsimulia kwa kifupi,
Joshua akabaki akimwangalia. Akamsimulia mpaka akamaliza na kumshangaza sana. “Naya wewe una moyo mkuu!” “Ila sikuwa nikijua
kama ndio biashara inayomwingizia sana pesa. Nilijua hiyo biashara ya sukari
ndiyo inayompa pesa. Halafu mpaka nikamuuliza. Unajua sikuwahi kumuhisi hata
mara moja kwa harufu! Mpaka nikahisi wanamsingizia nilipokuwa nikisikia anavuta
bangi! Ila alikuja kukiri mwenyewe kuwa ni kweli na ndio ilikuwa ikimpelekea
kulala na wanawake hovyo. Anyway lakini hiyo simu sio mbaya.” “Na pia sio
nzuri.” “Joshua wewe!” Wote wakacheka.
“Unataka nikudanganye? Wewe huoni hata jina lake halieleweki!”
“Bwana linaeleweka. Nione yako.” “Nilikwambia huwa nakuwa na vitu vichache na
vizuri?” Naya akacheka sana. “Acha basi mimi nikusifie Joshua!” “Wanadamu
wanachelewesha Naya. Acha tu niisifie kabla sijakuja kukuonyesha.” “Iko wapi
sasa?” “Ningekuwa nayo sasa hivi hapa, tusingeweza kuzungumza. Nimeiacha
ofisini makusudi ili nipate muda mfupi na wewe. Nikuone japo kwa muda mfupi
nipate nguvu yakufanya kazi.” “Nimefurahi kuja kuniona. Ila ujue Naya huyu
unayemuona hapa, kesho unaweza usimtambue.” Joshua alicheka sana mpaka kupiga
makofi.
“Jinsi utakavyokuwa umependeza?” “Sitaki utani. Naenda kuketishwa
na wakuu mimi!” Joshua akazidi kucheka. “Umepania?” Joshua akauliza akicheka. “Vizuri
sana. Nakwambia hutanitambua.” “Nilikwambia siwezi kukuchanganya Naya. Ni lini
utaelewa huwa nina vitu vichache sana na huwa navijua?” Naya akacheka kwa
furaha. “Uwe na nywele, usiwe na nywele, nitakutambua tu. Unenepe, ukonde, mimi
nitakutambua tu. Kabla haya macho yangu ya nje hayajakuona, ya ndani
yanakuwa yameshapata taarifa zako. Kwa hiyo hata uweje, upo hapa.” Akamuonyeshea moyoni,
ilimgusa Naya mpaka akainama, akaona machozi yakimtoka. “Naomba uniage kwa
furaha Naya! Mwenzio nimekuja kuchukua nguvu yakuanza siku.” Naya akabaki
ameinama tu akifikiria. Akakumbuka maombi ya baba yake juu yake. Akashindwa
kujizuia, akainamia meza kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati baba yake akimuombea akiwa anamlilia Malon, yale maombi
hayakuleta maana kabisa. Alikuwa amejawa uchungu wakupitiliza. Hakujua kama
anaweza pata mwanaume kama Malon. Na Malon mwenyewe alishamuhakikishia hivyo
kuwa hatapata mwanaume atakayempenda na kumjali kama yeye. Na kweli ikawa
hivyo. Kila aliyejaribisha naye, hakufikia viwango vya Malon. Hofu ya kuendelea
kwenye maisha na mwanaume mwingine ikamwingia, akabakia akimsubiria Malon kila
wakati.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua akasimama na kwenda
kuegemea meza upande wa nyuma na kumvuta amuegemee miguuni. Naya akajua
watakutwa pale. Akatulia kidogo na kusimama. “Uwe na siku njema. Acha mimi
nikaoshe uso.” “Twende wote.” “Chooni!?” “Nitasubiria nje. Usijali. Hata hivyo
hamna watu.” Wakatoka hapo, na kweli akamsubiria nje ya choo, ila mlangoni
kabisa. Wafanyakazi wengine wakaanza kuingia wakimshangaa kwa nini amesimama
mlangoni, tena choo cha kike!
Naya akatoka akamkuta hapo nje. Akamshika mkono kwa upendo kwa kupishanisha vidole akiutizama. Kisha akatingisha kidogo Joshua akimtizama. “Asante Joshua.” Joshua akacheka. “Kesho tutakuwa na wakati mzuri.” Akavuta ile mikono yao, akabusu wa Naya. Akamuona Naya amecheka. “Asante.” “Karibu.” Akamwangalia vizuri kwa kumthamini. “Za asubuhi?” Jema akawasogelea. “Baada ya dakika 4 kuanzia sasa, nimemwambia Fina atume simu kwenye hii simu ya mkononi. Tayari wote wapo hewani wanakusubiria.” Naya akamwangalia Joshua. “Uwe na siku njema.” “Aisee wanakusubiri.” Njama naye akaja akikimbia. “Na wewe Joshua. Ufanikiwe.” “Amina. Na wewe.” Akamwachia mkono na kupita katikati yao. Naya akagundua ndivyo anavyowafanyia, wakaanza kukimbia wakimfuata nyuma. “Acha kupaniki Njama!” Akamsikia Joshua. “Wote wapo hewani!” “Jema ameniambia baada ya dakika 4, kwa hiyo inamaana nimebakiwa na dakika ......” Akaitizama saa yake ya mkononi. Naya akaondoka pale kurudi mezani kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mchana Joshua, Jema na Njama wakaja hapo wote watatu wakizungumza
kwa zamu na Joshua akiwa mbele yao. Kila mmoja na tablet yake mkononi. Naya
akashangaa wote wanafanya nini pale! “Upo busy sana?” Joshua akamuuliza.
“Nimeshamtumia Jamal kazi aliyonipa. Nilikuwa nasubiria kama atanitumia
nyingine.” Bado Njama alikuwa akiongea
bila hata kunyamaza. Mpaka Naya akashangaa kama Joshua anasikilia. “Basi,
twende ukasubirie wakati tunakula.” Akamnyooshea mkono ili amshike. Naya
akachukua simu yake na kusimama. Akamshika mkono. Wakawapisha, Jema na yeye
akaendelea kuzungumza, Joshua ametulia tu akiwa anatembea amemshika mkono Naya
wanatoka hapo. Naya akamwangalia na kukunja uso. “Nawasikiliza kila kitu
wanachoongea na wanajua ndio maana hawanyamazi mpaka wamalize. Usijali.” Naya
akacheka taratibu kama aliyesoma mawazo yake. Hakuzungumza kitu ili
asiwaingilie.
“Iwe hivyo ulivyosema, Jema. Usiongeze neno. Na waambie
tunategemea jibu kwa haraka. Ifikapo jumatatu hawajajibu, tunapeleka biashara
yetu kwenye mall nyingine. Nashukuru sana.” “Sawa.” Akashangaa Jema anaondoka bila ya kuaga.
“Sio siku ya alhamisi, Njama. Hatuwezi kufanikisha kwa wakati. Weka jumatatu.
Ili mpaka jumanne tuwe tumeshakusanya
kila kitu, jumatano uhakiki tu. Alhamisi tunafunga kazi ya juma.” Akaona Njama
amesimama, haondoki. “Hakuna mjadala kwenye hilo Njama.” Joshua akaongea bila
kusimama wala kugeuka nyuma. “Tumekata siku tatu nzima!?” Joshua akasimama na
kugeuka. Ikabidi na Naya naye asimame maana alimwachia mkono na kuweka mikono
mfukoni.
“Ni nani anayelalamika?” Akamsikia akiuliza kwa ukali kidogo. “Ni
wewe niliyekwambia hakuna mjadala au wao kwa kuwa wameshindwa kufanya kwa
wakati niliokwambia sasa hivi?” Naya akaingiwa hofu. “Hapana. Nilikuwa
nikiwafikiria. Maana kutoka alhamisi mpaka kurudi jumatatu ni kama papana sana!”
“Ni kwa kuwa nimepima nimeona hizo siku tatu ulizokuwa umeziweka tokea mwanzo
ni kupoteza tu muda na kuvuta jambo dogo kwa muda mrefu bila sababu. Waambie
wote leo ni ijumaa. Siku ya kesho wanakuja kazini na jumatatu wote watakuwepo
kwenye meza zao. Siku nzima. Watumie hizo siku ipasavyo.” Akaangalia tena saa
yake ya mkononi.
“Halafu hata hivyo mpaka sasa hivi hapa, ni nusu siku. Yamebaki
masaa mengi tu kumaliza siku ya kazi. Wapo tu kwenye simu zao, hakuna soko
jipya! Au wewe unataarifa ambazo hujanipa?” “Hapana. Hakuna mpya.” “Basi usikatae kazi. Anayeshindwa mwambie
aniandikie mimi barua kabisa, yakunitaarifu ameshindwa. Niikute ofisini kwangu
jumanne asubuhi. Sijui kama tunaelewana Njama?” “Sawasawa. Naona huo mchanganua
mzuri. Tuanze mapema leo. Nitaitisha kikao...” Joshua akageuka na kuanza
kundoka. Naya naye akafuata. “Leo baada ya chakula tu cha mchana.” Njama
akamalizia bila kupata jibu kutoka kwa kiongozi wake, na yeye safari yake
ikaishia pale, Naya akajikuta amebaki yeye na Joshua wakitembea.
“Tunakwenda wapi?” “Kula kwa utulivu. Maana wote wawili wanakazi
ambazo zina wahitaji kuchangamka, hutawasikia wakinifuata tena leo mpaka nitoke
jioni. Kwanza watakuwa wananikwepa mpaka kila mmoja akamilishe chake. Kwa hiyo
twende tukale.” “Tusiende mbali Joshua. Mwenzio hata sijaajiriwa bado.” Joshua
akamcheka. “Wewe si unataka kukaa na wakuu!” “Basi nitafukuzwa kazi.” Joshua
akazidi kumcheka. “Kwani hujaajiriwa mpaka leo!” “Acha kunicheka bwana!” Joshua
akazidi kucheka. “Jamal anawachelewesha makusudi ili mkimtibua iwe rahisi
kuwafukuza. Sasa hicho nilichompa Njama sasa hivi, najua ataenda kuwachemsha
kina Jamal, mjiandae. Kama unafikiri Jamal ni mkali, utamuona leo akiwa anakazi
yenye deadline yangu ya jumatatu.” “Usinitishe bwana!” Joshua akazidi kumcheka.
Wakakuta gari haijafungwa. Akamfungulia mlango, Naya akapanda
baada ya kushukuru. Akakuta ndani kuna vyakula. Akacheka. Na yeye Joshua
akapanda upande mwingine. Akamtolea lunchbox yake na yeye akachukua yake.
“Njama ndiye alikwenda kununua baada ya kutoka kununu simu yako.” Naya
akamwangalia kwa mshangao. “Nataka kukusikia mpaka mimi ndio nikate simu Naya.
Hii simu yako ambayo siielewi naona itakuwa ikinikatili kila siku.” Naya
alicheka sana. “Ujue unadharau hii simu wakati watu wanalilia!” “Acha waililie,
lakini mimi nataka mawasiliano na wewe yakueleweka.” Naya akacheka kidogo kama
anayefikiria kisha akamwangalia.
“Asante sana Joshua.” “Nataka uniambie ulichofikiria sasa hivi
hapa.” Naya akaguna. “Nafikiria jinsi nilivyoteseka Joshua! Nilikuwa kama
mgonjwa! Ungeniambia kama leo, mida hii ya mchana ningekuwa nafuraha hivi,
ninacheka! Hakika nisingeamini. Kweli Mungu kwake siku moja inamtosha
kubadilisha mengi sana. Sikutegemea!” Naya akafungua chakula chake na
kukifunga, akacheka kwa kuguna. “Baba alikuwa akinifuata kitandani kwangu
nikilia. Sina tumaini. Nimeumia. Nimejawa aibu na fedheha hata kwa baba
mwenyewe. Basi anaingia na kunishika mikono na kuanza kuniombea. Mambo
aliyokuwa akimsihi Mungu juu yangu nilikuwa siamini Joshua, lakini akaniomba
niamini tu pamoja naye.” “Kwa nini aibu na fedheha.” Joshua akauliza.
“Baba alikuwepo wakati nikimuhangaikia Malon, Joshua! Aibu
niliyomuingiza baba yangu wakati nikikusanya pesa!” Naya akamsimulia
kilichoendelea kipindi hicho. “Niliuza kila kitu changu mpaka viatu vyangu vya
thamani kwa wanafunzi niliokuwa nikifanya nao kazi za ushering, ili tu nimtoe
Malon jela. Nikijua ni mwanaume atakayekuja kuwa mume wangu!” Naya akatulia.
“Hakika sikutegemea kuja kuachwa na Malon na kumkuta eti na mahusiano mengine!
Hakika sikutegemea!”
“Aliponiacha tena, ni kama nilikuja kupona. Lakini kuja kumkuta
tena na Rita, na wapo tu hapa mjini akishindwa hata kunitafuta, niliumwa
Joshua, lakini sikuwa na jinsi yakumueleza mtu akanielewa. Siwezi tena kukaa
chini nikalia. Sina mama. Familia inanitegemea, na nina kazi. Halafu eti
anarudi na pete! Nilihisi ni kunidharau kupita kiasi. Nilimwambia ni heri
nizeekee pale kwa baba Naya, kuliko kuongozana naye popote pale.” “Pole Naya.
Pole sana. Na mimi ninahistoria mbaya hivyohivyo, kasoro mimi sikuwa hata na
mtu wakuniombea. Niliachwa peke yangu, mpaka Mungu alipojitokeza na kuni adopt,
mimi kama mtoto wake.” Joshua naye akacheka.
“Vurugu za mapenzi, mimi nazijua Naya. Nazijua kwa kuishi.” “Hivi
kwa nini inakuwa ngumu hivyo jamani!? Haiwezi ikawa tu rahisi watu wakafurahia!”
“Inawezekana Naya. Inawezekana kabisa. Nahisi nikukusudia na kuamua kwa
makusudi kufanya iwe rahisi.” Wakatulia na kuanza kula kila mmoja akiwaza lake.
“Umetoa kitu kipya?” Naya
akauliza. “Ni msingi wa ile kubwa niliyokwambia inakaribiwa kuzaliwa. Naweka
mazingira mazuri ili mtoto akizaliwa, nikiweka sokoni, ijibu kwa haraka.”
“Hongera Joshua.” “Hizo pongezi nitazipokea vizuri siku ya jumatano
nitakapoweza kuona kila kitu kipo pamoja. Acha Njama awachemshe kwanza, najua
lazima jumanne nitakuwa na kila kitu. Jumatano nitakusanya kila kitu kiwe
pamoja. Alhamisi nataka iwe hewani. Hapahapa ndani kwanza, ikiwezekana weekend
ijayo iwe kwenye tv.” Naya akamwangalia kwa kumpongeza.
“Kama mimi nakufurahia hivi na kujivunia, mama yako ingekuaje?” Akamuona
ametulia kisha akacheka kidogo na kutulia kabisa. “Malizia chakula.” Ikawa kama
Naya anamrudisha pale. “Kweli.” Akaangalia saa na kuanza kula tena. “Nilikwambia
kesho nitakueleza habari za mama yangu?” “Ninahamu yakusikia.” “Basi kesho
nitakutambulisha kwake. Utamfahamu japo hutabahatika kumuona, ila utapata
picha ni mtu wa namna gani.” “Sawa.” Naya akaangalia muda, akaona muda wa
chakula umeisha.
“Acha niwahi Joshua. Sipendi kuchelewa popote. Napenda Jamal
akiingia pale ofisini anikute nikimsubiri yeye. Asante kwa chakula.” “Ndio
maana Jamal anakusifia! Unanidhamu ya kazi, Naya. Na unaonekana na wewe
unapenda vitu vyako hata kama kwa wengine havina thamani.” “Nafurahia kazi
yangu Joshua. Kwanza nilihangaika sana kupata kazi mpaka nilikata tamaa. Huu ni
muujiza ambao siwezi kuchezea. Naona wengine wakilalamikia mshahara na
mazingira ya kazi, mimi bado nipo kwenye kutoamini hata kama nimeipata!”
“Utafanikiwa sana. Kazana. Na iwe hivyo kwenye kila kitu.” Naya akawa
amemuelewa. Lakini bado moyo haukuwa umefunguka kwake kabisa.
Alijua ni nini Joshua anatamani kumsikia akisema, lakini alijawa
hofu ya uthubutu na pia kuhofia pengine Joshua atamuhisi anamdanganya. Akaona
anyamaze tu. “Umehamia wapi huko, ukaniacha mimi hapa?” Naya akacheka na
kumwangalia Joshua. “Upo makini Joshua! Unakuwa kama unayasoma mawazo yangu!”
“Nilikwambia ndio moja ya jukumu langu. Kusoma nini jamii inataka, na kutoa
kitu sahihi ili mimi ndio nibakie sokoni. Sasa siwezi kukushindwa wewe mmoja,
Naya.” Naya alicheka sana. Akakumbuka kwa hilo juma moja tu, mpaka hapo,
alishamteka mpaka fahamu zake. Kila alipotaka kumkumbuka Malon, akajikuta
Joshua amejaza furaha kweli. “Mimi nawahi kazini.” “Si tutazungumza baadaye?”
“Kabisa.” Naya akakusanya uchafu, nakutoka kwa haraka. Alijua watu wanajua
alikuwa hapo garini.
Alipoingia tu ofisini, Jamal akamfuata. “Nisogezee hiki kimeo, leo
kisilale. Tafadhali Naya. Ukiona kazi kubwa, niambie nifanye mwenyewe. Leo
siwezi kuondoka hapa bila kukamilisha hii. Na nasikia baadaye tuna kikao na
Njama.” “Hamna shida. Acha nianze sasa hivi.” Naya akapokea mafaili yote kutoka
kwa Jamal, akatulia hapo mezani akaanza kazi. Ilikuwa kazi kubwa na alijua
alipewa asubuhi ya siku hiyo mmoja ya mwenzie waliyeanza naye kazi lakini
akamlalamikia Jamal mchana kuwa kompyuta yake ilimgomea. Ndio alikuwa
akihangaika nayo tangia asubuhi. Jamal alikasirika, akaanza kugomba kwa nini
hakusema mapema. Ndio kazi anapewa Naya. Na akaipokea bila shida na kuanza kufanyia kazi.
Jamal alishaondoka hapo. Wengine wakaanza kutoka Naya hakuwa amemaliza
kazi. Na kwa kuwa Jamal alimwambia asipomaliza yeye, itabidi aje amalizie baada
ya kikao, hakutaka iwe hivyo. Alishakusudia kujipendekeza kwa Jamal. Kwa hiyo
alikuwa akifanya kila kazi anayopewa, tena kwa ufasaha. Akafanya mpaka ikafika
saa 10 na nusu, wenzie wote wakawa wametoka, amebaki yeye peke yake hapo
ofisini. Mawazo juu ya Joshua yakamjia. Vile alivyojifunua mbele ya kila mtu
kuonyesha Naya ni wake. Akatulia akimfikiria.
‘Kuna kitu natamani kukwambia Joshua. Lakini moyo unasita. Nahofia
pengine unaweza usisadiki au ukafikiria vinginevyo. Lakini ipo siku nitakwambia
tu. Nitataka ujue. Inaweza isiwe leo, au kesho. Lakini ipo siku nitataka ujue.’ Akamtumia
huo ujumbe tena kwa kutumia simu yake mpya aliyopewa mchana wa siku hiyo, alishabadilisha
kutoka ya zamani kwenda hiyo mpya. ‘Sijawahi kukuhisi ni muongo hata mara
moja. Ningependa kujua.’ ‘Kama unaniamini, umenipa moyo. Kesho tukionana
nitakwambia. Nataka nikwambie tukiwa wote, si kwa simu wala ujumbe.’ Naya akatuma
tena huo ujumbe.
‘Umeshafika mbali? Naweza kukufuata japo bado nina kazi ofisini.’ Naya akasoma
na kujibu. ‘Bado nipo ofisini ndio nataka kutoka. Kuna kazi alinipa Jamal,
nilitaka kuimaliza kabla ya kesho. Naweza kukufuata. Sitachukua muda mrefu.’ Hakupata
jibu. Akajua ametingwa. Naya akafunga mafaili yote na kufunga kompyuta. Wakati
anatoka ili akaweke yale mafaili mezani kwa Jamal, atoke ofisini, akasikia simu
yake ikiita. “Joshua!” “Njoo chumba namba 5.” Akashituka sana. Alijua ndipo
wanakofanyia kikao kina Jamal. “Sikujua kama na wewe upo kikaoni Joshua! Naogopa.”
“Njoo nakusubiria mlangoni.” Naya aliingiwa na hofu kubwa sana ila ikabidi
kwenda. Ilikuwa jengo hilohilo ila mwishoni kabisa.
Mwili ulikuwa ukitetemeka mpaka akaanza kusikia baridi. Akatembea
kuelekea huko na kweli kwa mbali akamuona Joshua amesimama katikati ya mlango
kama ambaye yupo ndani na nje. Naya akaongeza mwendo mpaka akamfikia. “Naomba
unisubiri. Tutatoka wote. Ni sawa?” “Sawa. Ila naomba nikusubirie hapa nje.”
“Hiki ni kikao cha watu wa kitengo chako. Ingia nimekuwekea kiti.” Naya alijua
ndani wanamsikia. “Joshua!” Akanong’ona. “Jamal alishakwambia huwa hatuli
watu. Umesahau?” Naya akatingisha kichwa kukubali kwa hofu. Joshua akamshika
mkono na kuingia naye ndani mpaka kwenye kiti alichojua ni cha Joshua mwenyewe maana
Jema na Njama walikuwa pembeni ya hicho kiti. Jema upande wa kulia, Njama
upande wa kushoto. Ilikuwa kama wakijadiliana kitu kwa makundi, Joshua
akisubiria jibu.
“Kwa manufaa ya Naya. Nauliza tena swali. Asije fikiri tunapiga tu
kelele humu ndani.” Joshua akaanza. “Jema?” Ni kama akataka Jema ndiye arudie.
“Nani mwenye bidhaa zetu kwa wingi sasa hivi huko sokoni? Kwa nini? Na nini
kifanyike?” Jema akarudia swali. Wote wakamwangalia Naya. Naya akamwangalia
Joshua. “Ukitaka kuchangia. Karibu.” Naya akatoa tabasamu kama anayefikiria.
“Na mimi naomba muda wakufikiria.” Naya akajibu kwa kujiamini, wengine
wakiwatizama.
“Ukitaka sehemu ya kuandika.” Joshua akasogea na kumfungulia ipad
yake. “Andika hapa.” Akashangaa Naya hakatai. Akaivuta ile Ipad na kuvuta kiti
nyuma kabisa mpaka pale aliposimama Joshua. Kiti kilikuwa na matairi. “Mbona
unakimbia meza?” “Pale uliponiweka, naogopa, kutanifanya nishindwe kufikiria.”
Joshua akacheka kwa furaha. Akamuona Naya anaanza kuandika huku akifikiria.
Makundi yalikuwa matatu. Kundi la kwanza likanyoosha
mkono na kusema, ‘Kwa wakati ule wenye bidhaa zao kwa wingi ni watu wa
mahotelini. Kwa sababu wanao wateja wa uhakika na uwezo wa kununu bidhaa zao.’
Kundi la pili wakasema, ‘wanaouza kwa jumla ndio wanazo bidhaa zao kwa wingi kwakuwa
wanapelekewa mpaka madukani na wanapewa kwa bei ya jumla, ipo chini.’ Kundi la tatu wakasema, ‘Wanayo
watu wenye maduka ya kawaida, wao ndio wenye bidhaa zao kwa wingi kwa kuwa
wanawateja wa uhakika kila siku, kila wakati, tofauti na mahotelini na maduka
ya jumla.’ Joshua akaonekana kama hajapata kitu alichokuwa akikitafuta.
“Sijapata vizuri. Halafu kuna kipengele kimoja ni kama sijakisikia kutoka kwenu
wote.” Joshua akaongea akisogea katikati, na uso wakutoridhika.
“Jamani kwenye ofisi yangu kuna mwakilishi. Acha na yeye
azungumze.” Alikuwa Jamal. Naya akaanza kutetemeka. Wote wakamgeukia.
Akasimama. “Natetemeka.” Akanong’ona akimwambia Joshua. “Upo sawa kabisa. Ongea
mawazo yako.” Joshua akamgeukia na yeye akitaka kumsikia. “Labda nianze kwa
kusema sikutegemea kama ningekuwa hapa. Kwa hiyo ni kama nimeshitukizwa,
sijajiandaa. Lakini nina mchango kidogo tu.” “Karibu.” Joshua akamkaribisha
asiamini kama Naya ndio mwepesi vile! Shauku ikaongezeka. Kisha Joshua akamsogelea
na kusimama mbele yake ili amwangalie tu yeye. Wakamsikia akimwambia kwa
utulivu. “Jaribu kuvuta pumzi kwa nguvu na kuachia taratibu ili kukutuliza. Na
fukuza hisia za hofu kabisa. Ona kama
upo na watu wanaohitaji msaada, na wewe unayo suluhu. Itakupunguzia hofu na
kukuongezea ujasiri. Sawa?” Watu wote kimya wakiwasikiliza. Wengine vichwa
chini maana Joshua huyu, anabembeleza, siye Joshua wanayemfahamu anayetaka
majibu yakueleweka.
“Nimetulia.” Joshua akacheka. “Karibu.” Akasogea pale mbele yake,
wengine nao wakamuona. “Okay. Mimi sitakuwa mbali sana na wengine. Kundi la
kwanza lilisema wenye maduka ya jumla, wengine mahoteli makubwa, halafu kundi
la bosi wangu Jamal walisema maduka ya rejareja. Naomba niweke hapo msisitizo
lakini tofauti kidogo.” Naya akaanza lakini macho yalikuwa kwenye ipad muda
mwingi kisha kwa Joshua tu. Hakutaka kuwatizama wengine.
Akaendelea. “Nafikiri tukisema kwa hao watu watatu, ni kweli
lakini mimi nafikiri wenye bidhaa yetu au anayetakiwa awe nayo ni third part.
Huyu mnywaji ambaye haihitaji friji wala duka kuhifadhi bidhaa yetu. Yeye
akiipata ni kuitumia moja kwa moja. Uwekezaji wetu kwake upo chini, sana.
Kuizalisha, utunzwaji kwenye chupa au kopo na kumfikia. Yeye ndiye anayetakiwa
kuwa na bidhaa yetu. Na yeye ndiye tunatakiwa kuwekeza kwake.” Wakaanza
kumpigia makofi. Naya akacheka maana Joshua alishaanza kutingisha kichwa
kukubali.
“Sijamaliza.” Watu wakacheka. “Uwanja ni wako.” “Tangazo
tunaloweka kwenye tv, linamgusa mwenye hoteli, mwenye duka la jumla, rejareja
na huyu mtumiaji wa mwisho kabisa. Wazo langu na ndicho nilichokuwa
nikifikiria. Kama tukikubaliana mtu wa mwisho ambaye anatakiwa kuwa na bidhaa
yetu awe ni mtumiaji. Kwamba tukijua watu wenye maduka ya jumla, tukimpa vitu
tuseme 1000, itachukua muda mrefu kidogo kuja kuleta pesa moja kwa moja maana
na yeye atahangaika mpaka aje auze vyote. Lakini yule mwenye duka la rejareja
anamfikia moja kwa moja huyu mtumiaji. Na huyu mtumiaji hata akiwa nazo mbili,
moja anatumia palepale na akitaka kubeba
nyingine ataondoka nayo na lazima atakwenda kuitumia siku hiyohiyo bila
kusubiri kesho na kuamsha shauku kwa hata wengine watakayemuona nayo.” Watu
wote wakatulia kimya.
“Ndio swali langu ikawa hivi, tufanyaje ili hayo yote yatimie kwa huyu
mtumiaji? Awe kila akiwepo sehemu. Mchana au usiku. Akiwa ameshiba au ananjaa.
Juani au kivulini. Awe mtoto au mkubwa. Kipofu au anayeona. Mgonjwa au mzima.
Masikini au tajiri. Wote watake bidhaa yetu tu kiasi ya kwamba hawawezi bila
hiyo, na wakiwa nayo hawawezi kutunza ila kutumia na kesho watafute tena kwa
lile kundi la tatu, muuzaji wa rejareja!” Hapo mpaka Joshua akakunja mikono
kifuani na kurudi nyuma akajiegemeza, akiwa anamtizama Naya.
Naya akacheka kidogo akimtizama. “Nimekuachia ukumbi.” “Njoo.”
Naya akamnong’oneza kwa mdomo, lakini kila mtu alikuwa akiwaangalia. Walikaa
pande tofauti za chumba maana Joshua ni kama alisogea pale alipokuwa amesimama
naye kumpisha watu wamwangalie yeye, na yeye aweze kumuona vizuri. Alijivuta
upande mwingine dirishani. Joshua akamsogelea baada ya kumwita. “Waambie kama
kuna mwenye wazo anaweza kuchangia.” Joshua akacheka sana. “Sasa si useme
Naya?” “Wewe ndio muendesha kikao bwana Joshua! Mimi naogopa.” “Huwezi ku drop the
ball now! Umefika pazuri sana. Naomba uongeze ujasiri zaidi. Unakumbuka
ninapokwambia huwa nazaa?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Upo leba sasa
hivi. Kazana huyo mtoto atoke. Mimi mwenyewe unanishangaza. Unafanya vizuri
sana.” Naya akacheka kwa furaha. Akasogea pembeni ya Joshua.
“Nimepewa ruhusa kuwauliza. Kama kuna anayetaka kuchangia.” Naya
akaongea kwa hofu kidogo. “Kwa ufupi Naya amesema bidhaa yetu ibakie kwa
mtumiaji kwa kuwa wao wapo wengi kuliko hayo makundi matatu tuliyotajwa.
Tukichukulia tu huu mkoa tu mmoja wa Dar. Asilimia 85, watumie bidhaa zetu kila
siku. Wagonjwa, wazima, masikini, vijana, wazeee, watoto, na...” “Mpaka vipofu
ambao hawawezi kuona bidhaa zetu. Kwamba ndio ameshushwa leo hapa mjini,
ametoka kijijini ambako soda ni mpaka sikukuu. Tunafanyaje hao watu wote
wabakiwe na shauku ya bidhaa zetu tu?” Pakazuka ukimya. Joshua akazungusha macho chumba
chote na kurudi kwa Naya.
Ikabidi Naya aendelee. “Matangazo. Na si matangazo yale
yakuonyesha mtu anatokwa jasho ndio anataka maji au soda zetu! Hapana. Tangazo
litakaloimbwa na watoto mtaani. Tangazo ambalo likiwekwa hata kipofu
atasisimkwa na kutaka kuweka mdomoni na akiondoka ataweza kumsimulia hata
kipofu mwingine. Mgonjwa ambaye hata amezidiwa hataki kula kitu, adai bidhaa
zetu. Hata kama mtu amebakiwa na pesa ya nauli tu, basi awe radhi kutembea
ilimradi tu aweke bidhaa yetu mdomoni.” Wakaanza kupiga makofi.
“Sijamaliza Joshua.” Watu wakacheka maana Naya aliongea akimtizama
Joshua kwa kulalamika. “Naya hupigiwi, unacheza!” Joshua akafanya kila mtu
acheke, Naya naye akacheka sana mpaka kujifunika ipad usoni. “Utanifanya
nishindwe kumalizia bwana!” “Haya samahani. Endelea kabla huo moto haujazima.”
“Basi.” Naya akaanza tena na cheko. “Kuna jinsi yakufanya mtu azungumze lugha
yako, au kile unachokitaka akizungumze bila hata yakumwambia arudie. Si
mnajua?” Kimya. Naya akawaangalia na kurudisha macho kwa Joshua. “Leo
nimekwambia uwanja ni wako. Wewe endelea.” Naya akacheka. “Wimbo na milio.”
Kila mtu akapiga makofi ikawa kama wamekumbuka. Ikaanza kelele kila mtu akiunga
mkono.
“Ila mimi bado sijamaliza!” Akamlalamikia tena Joshua. Joshua alicheka mpaka akapiga makofi
mfululizo. “Naya leo umetuamulia watu wa masoko! Umeona tunacheza tu hapa mjini
nini!” Watu wakazidi kucheka. “Sawa mama tupange. Leo nakuachia ukumbi.”
“Usindoke sasa. Simama hapahapa.” Watu wakaanza kucheka tena maana alimvuta
mkono. “Hapa ni sawa?” “Usisogee sasa.” Joshua akacheka na kutulia.
“Mwimbaji anapoimba wimbo wake. Akaurudia mara kwa mara, haitaji
kuwaambia watu rudia kuimba huu wimba. Utashangaa wimbo unaenea mpaka watoto ambao
hawajui kuongea vizuri, mtaani, kule uswahilini kabisa, watauimba. Wanaosoma
shule za kata pia wataimba wimbo uleule kama wale watoto wanaosoma zile shule
za wenye kipato kikubwa.” Wakacheka sana.
“Kweli tena. Utashangaa nguvu iliyopo kwenye wimbo. Mimi nimefanya
kazi kwenye shule ya watoto wa walio nazo hapa mjini, na hawazungumzi lugha ya
kiswahili, ila utashangaa sana nyimbo wanazoimba! Ni kama watoto wa uswahilini
tu.” Watu wakazidi kucheka. “Linapofika swala la wimbo, kila mtu anaimba. Ndipo
ninapokuja kwenye swala langu la mwisho la mlio. Tajiri na maskini, wakiume
wote wanapiga mluzi.” Mpaka Joshua akacheka sana. “Hata wasomi na wasio soma
pia.” Joshua akaongeza. “Sawasawa. Ipo nguvu pia kwenye mlio. Naomba
niwasikilizishe mlio mmoja hivi.” Wote kimya. Naya akatoa simu yake.
Akabonyeza vitu kadhaa. Wote kimya kabisa. “Huu mlio nikiusikia
mimi, hata kama pale ofisini kumewashwa baridi kali ya namna gani, nakunywa
maji.” Naya akaweka. Ilisikika kama kinywaji kinamiminwa. Watu wakashangilia
sana. “Nimejiwekea mimi mwenyewe makusudi kunikumbusha kunywa maji, maana mimi
ni msahaulifu sana wa kunywa maji. Au huwa nazembea. Sasa fikiria mlio huuhuu,
uongezwe sauti. Utoke kwa sauti kubwa yakuvutia! Kisha kusikika na jina ya
bidhaa zetu.” Wengi wakasimama na kupiga makofi wakishangilia. Naya akakimbilia
nje.
“That’s my girl!” Joshua akaongea kwa kutamba sana. Watu wakazidi
kushangilia. Joshua akabaki akitingisha kichwa. “That’s what I am talking
about.” Joshua akaongeza na kupiga ngumi kwenye mkono wake mwenyewe. Alijisikia
vizuri sana na kushindwa kuficha hisia zake juu ya Naya. Miluzi ikaanza
kusikika humo ndani, Joshua akacheka sana. “Njama, nakuachia kikao. Naona Naya
ashatumalizia kazi kubwa sana. Hakikisha tunapata picha nzuri ya kinywaji kikimiminwa
iwe kwa glasi, mdomoni na kila mahali. Kwengine mmalizie wenyewe.” “Na sauti ya
hata umezwaji wake. Hapa kwenye koo.” Naya akachungulia na kuongeza hapo kwa
Joshua, akionyesha koo lake. Watu wakacheka sana. Joshua akatoka.
Akamkimbilia na kumbemba juu kabisa. “Naya! Naya! Naya! Naya!
Naya!” Eti akawa anamshangilia huku amemnyanyua juu kabisa. Naya alikuwa akicheka
sana na ipad imemfunika usoni kwa aibu. Akamshusha na kumuwekea mkono mabegani,
wakawa wakitembea. “Duuuuh! Wewe mtoto!!” “Umeniambia mwenyewe niseme.” “Hakika
Mungu alikuleta kwenye kile chumba kwa makusudi na muda muafaka! Nilikuwa
nishachoka, hakuna majibu yakueleweka!” Naya akajisikia vizuri sana.
Akajiegemeza kidogo.
“Uuuuu! Unaona Mungu alivyo wa ajabu? Umeona jinsi ulivyotoa wazo
zuri leo?” “Nimefurahi kama hata wewe umekubaliana na mimi Joshua.” “Nikwambie
ukweli Naya?” Naya akatingisha kichwa kukubali. “Umefikiria vizuri sana, hakika
sikutegemea kama kwa muda mfupi vile ungeweza kufikiria jambo zito vile na
kuliweka kwa urahisi vile! Umenifanya nijivunie sana kuwa na wewe.” Naya
akacheka huku akifikiria.
“Nikwambi Joshua, hizo zilikuwa moja ya ndoto zangu ambazo sijui
niseme zimekufa?” “Tukae kidogo. Au baba atakasirika?” “Anajua nipo kazini.
Hamna neno.” Wakawa wanaelekea ofisini kwa Joshua. Ilikuwa mara ya kwanza kwa
Naya kwenda huko. “Utaniruhusu nikae kwenye kiti chako?” Joshua alicheka sana.
“Nataka upako wako.” “Sasa si uuchukue hapa nilipo?” “Nataka kila mahali. Na
mimi nikalie kiti cha Joshua Kumu.” Joshua akazidi kucheka.
“Niambie. Ni ndoto gani hiyo unafikiri imekufa?” “Nilikuwa nimefikiria kufanya biashara ya sabuni. Nikamshirikisha hilo wazo Malon. Mpaka jina nilikuwa nimepata. Nika...” “Jina gani?” “Nilifikiria MaNa. Hiyo sabuni iitwe MaNa. Kwamba ilianguka kutoka jangwani na...” “Naya unaakili yakufikiria wewe! Japokuwa nimeelewa ni kifupisho cha majina yenu, lakini hiyo akili yakufikiria MaNa, na kuinganisha na MaNa, chakula kilichoanguka jangwani na kulisha wana wa Israel WOTE! Inamaana hiyo MaNa, kama sabuni, ingeunganishwa na ahadi za Mungu, ingeanguka mpaka vijijini!” “Naona wewe umenielewa zaidi Joshua. Nilitaka iimbwe mtaani kama ile sabuni ya Komoa ilivyoimbwa na kila mtu, kisha kuhakikisha inamfikia mtumiaji bila shida."
"Halafu Joshua. Kuongezea katika
nilichosema pale kwenye kikao. Najua wewe ndiye umeanzisha zile soda za chupa ndogo
kabisa. Niseme nimeambiwa. Ulianzisha vile visoda vidogo kwa bei ndogo ili kila
mtu aweze kumudu kununua bidhaa zetu. Si ni kweli?” “Ndio wazo langu la kwanza
hapa. Na waliuza, mpaka wakabaki kunipigia simu kunipongeza. Na nikuibie siri
tu, vile visoda vidogo, vina faida kubwa kuliko haya machupa makubwa.” “Kweli?”
“Kabisa. Na kuna mkakati mwingine nipo kwenye kuusimamia huo, mpaka wanakuja
kufunga hiki kiwanda. Au vizazi na vizazi watakuja kuambiwa Joshua Kumu,
alipita kwenye hii ofisi na nikaitendea haki.” Naya akacheka sana.
“Mimi mwenyewe najivunia wewe!” Joshua akacheka sana. “Na hivi
hukuwahi kuwa na mwanamke hapa! Basi umaana wa Naya umeongezeka mara dufu.”
Joshua akazidi kucheka. Akamfungulia mlango Naya akaingia. “Mungu wangu Joshua!
Ndio una ofisi nzuri hivi!” “Karibu.” Naya akabaki akishangaa. “Daah! Ndio maana
hata ukifikiria mawazo yanakuja masafi. Sio kama sisi kule utafikiri tunafanya
kazi stoo!” Joshua alicheka sana. “Kweli. Tuna maboksi ya kila matangazo.” “Uwe
unakuja huku kupumzika.” “Mwenzio nimeamini kweli Jamal ananitegemea.
Wakishindwa kazi zao, ananiomba nifanye mimi.” “Sasa na yeye asikufanye
mtumwa.” “Mwenzio napenda. Anazidi kuniheshimu.” “Nilikwambia Jamal huwa
anaheshimu watu wanaostahili kuheshimiwa. Ukiwa hovyo, hawezi kukuheshimu. Kila
mtu anamfahamu alivyo mkorofi.” Naya akacheka kidogo na kutulia kama
anayefikiri.
Joshua akatulia. Akajua anataka kumwambia kitu alichomwandikia
kwenye ujumbe. Akakaa kabisa na kutulia kabisa. Akamuona anaanza kuingiwa hofu
kama anayetaka kugairi. “Tafadhali niambie Naya. Usigairi.” “Umejuaje!?”
“Niambie.” Joshua akaweka msisitizo akionyesha kama na yeye ameanza kuingiwa
hofu na anachotaka kuambiwa. “Niambie chochote kile unachokifikiria.” “Nahofia
unaweza kusema sio kweli, pengine nimepatwa tu na tamaa!” “Mimi sio mtu wakutoa
hukumu kwa mtu kwa haraka. Usiogope.” “Najua nimekuwa karibu na wewe hata siku
saba hazijatimia. Halafu ni kama wewe ndio ulionekana kunifahamu zaidi mimi
kuliko...” Naya akasita. Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama
anayejaribu kutulia kwa hofu.
Akamwangalia Joshua. “Au labda nitakuja kukwambia wakati
mwingine.” “Hapana Naya. Tafadhali niambie.” “Ninachotaka kusema, umezivuta
hisia zangu kwa namna ya tofauti sana. Haikuwa hivi hata nilipokuwa...” Akasita.
Akatulia kwa muda akiwa ameinama, kisha akaendelea. “Nakupenda Joshua.”
Akamuona Joshua amefunga macho na kucheka kwa mbali. “Asante Mungu wangu.”
Akamsikia akiongea vile akiwa amefunga macho. Naya akashangaa. Akavuta pumzi
kwa nguvu na kurudisha kichwa nyuma kabisa akakilaza kwenye kiti alichokuwa
amekalia akiangalia juu lakini amefunga macho.
Akatulia kidogo kisha akavuta kiti mpaka pale alipokuwa amesimama
Naya, akamshika mikono yake yote miwili. “Huo upendo uliosikia kwangu. Hata
kama sasa hivi upo kama mawingu. Kwako haujaleta maana yakueleweka. Huo ukiri
tu. Nilikuwa nikiusubiri kwa hamu mno ili nimlilie Mungu wangu, aukuze. Kutoka
kwenye mawingi mpaka iwe mvua yakukata ukame ndani ya maisha yangu yote
niliyoishi hapa duniani. Hujui ni kiasi gani nilivyokuwa nikimlilia Mungu
aniunganishe na mwanamke atakayenipenda mimi kama Joshua sio wadhifa nilio nao
sasa hivi.” “Sasa unaniaminije mimi?
Pengine na mimi ni wadhifa wako tu!” Naya akauliza kwa upole.
“Namjua mwanadamu kwa kumsikiliza na kumuona. Kwa kuwa nilikwambia
naanza kusikiliza na kuona kwa kupitia macho ya ndani kwanza kabla ya haya ya
nje ambayo dunia imeshayaharibu wakati mwingine ni ngumu kutambua kwa macho
haya ya kawaida. Nakwambia nilichokuwa nikimuomba Mungu ni huo ukiri tu, kutoka
kwako. Nilikuwa nikitamani jinsi unavyomzungumzia Malon! Ilionekana unahisia
kubwa sana kwake mpaka nikaanza kupatwa na wasiwasi kama nitaweza kupenya
kwenye moyo wako! Hukuwahi hata kuropoka au kunidanganya kama unanipenda Naya.
Hata nilipokuwa nikikuwekea mazingira useme jambo tu, japo kunionyesha unaelewa
ninachokwambia, hukusema.” Naya akajisikia kuumia kusikia hivyo.
“Wapo wengine nikiwanunulia tu chakula. Hata kama tupo kwenye
shuguli za kikazi, tayari wanaanza kumsumbua Jema awaunganishe na mimi kuwa
wananipenda. Lakini haikuwa hivyo kwako. Nikawa nikimwambia Mungu, hata uropoke
tu, ning’ang’anie hapohapo magotini, lakini ukawa kimya. Nimefurahi sana Naya.
Asante. Hata kama bado hujanielewa vizuri, nakuombea Mungu akufungamanishe na
moyo wangu.” Naya akajisikia kumpenda zaidi Joshua.
“Unaweza usinielewe Naya, lakini ujue nilikuwa nikikusubiri uje
kwenye maisha yangu. Ninashahada tatu. Kazi ambayo nipo kiwango cha juu sana
kwenye taaluma yetu. Najua unajua jinsi ninavyolipwa maana kila mtu anaimba
mshahara wangu mpaka kero!” Naya akacheka taratibu maana na yeye aliambiwa huo
mshahara wa Kumu, ikawa ndio habari ya kwanza kuisikia alipoingia hapo kwenye
hiyo kampuni. “Basi ujue ni wewe tu ndiye niliyekuwa nikikisubiri, ndio maana
unaniona mwenzio sipotezi muda. Najua wewe ni wangu. Nimethibitisha, ndio maana
nilikwambia nakusubiri, nikitaka uelewe kuwa mimi nimeshamaliza. Ni wewe tu.”
“Nilielewa Joshua. Lakini pia ukumbuke sikuwa nakufahamu, halafu
nilitoka kwenye mahusiano magumu. Bado nilikuwa na hofu. Lakini jinsi
ulivyofanya kwangu, umeonyesha urahisi wa mambo! Mpaka umenishangaza!” “Ni
kwakuwa sidhani kama ilikusudiwa na Mungu iwe ngumu Naya. Naona binadamu ndio
tunafanya mahusiano kuwa magumu mpaka watu mliowahi kupendana sana, mnageuka
kuwa maadui!” “Kumbe na wewe umeona?!” “Haikukusudiwa kuwa hivyo Naya. Tuache
upande huo, nataka ujue umenifurahisha sana. Leo nitalala tena kama mtoto
mchanga.” Naya akacheka akimtizama vile anayomaanisha.
“Twende nikusindikize kwenye gari yako, ili urudi nyumbani.
Tutaendelea kwa simu.” “Sasa na wewe unaondoka saa ngapi?” “Naona tuongozane na
mimi nikapumzike. Nilikupa asante wa mchango mzuri uliotoa?” “Si ndio kesho
unakwenda kunipongeza?” “Hapana. Kesho namtoa Naya mpenzi wangu, sio mfanyakazi
wa kampuni ya Coca. Wasinitanie kabisa.” Naya akacheka sana. “Waache
wakupongeze kama kampuni, na mimi nikafurahie na mpenzi wangu.” Akamuona
anafikiria kidogo.
“Duuh! Siamini kama na Joshua naye anampenzi. Usije tu kubadilika
Naya.” “Si mimi Joshua. Kwa kuwa nimekwambia leo nakupenda wewe, hutanisikia na
mwanaume mwingine, labda uniache kama alivyofanya...” Naya akanyamaza. “Sijui
kubadika Joshua. Mimi si muhuni. Na sina tamaa. Nikiwa kwako ni kwako mpaka
utanihurumia kama wewe ni mwanadamu mwenye utu, halafu ukinitesa, au ukiwa
unaniumiza moyo wangu. Wewe ni mtu wa pili kukwambia nakupenda. Nakuomba uwe wa
mwisho Joshua. Tafadhali usije nibadilikia.” Naya akaanza kulia.
“Mpaka najiona ninamkosi Joshua. Unakuwa umetulia, lakini hupati
mtu anayethamini hilo. Unamridhisha mtu kwa kila namna na bado!” Joshua
akamshika tena mikono yote miwili wakiwa wameshafika nje. “Mungu ameniagiza,
nikupende wewe kama Kristo alivyolipenda kanisa na kujitoa kwa ajili yake.
Nitajitoa kwako Naya, na Mungu anisaidie. Kabla sijafikiria kukuumiza wewe,
ujue mimi nitakuwa nimeumia zaidi. Na mimi nilikwambia sikujaliwa tamaa na visivyo
vyangu. Ila vilivyo vyangu, utavitambua kama ni vyangu.” Naya akatingisha
kichwa kukubali.
“Basi wahi, na mimi nikiingia tu kwenye gari nitakupigia. Usisahau
kuweka bluetooth. Usishike simu wakati ukiendesha na tafadhali kuwa makini,
Naya.” Tayari giza lilishaingia. “Nitakuwa makini.” Naya akacheka na kumuachia
mikono. Akachukua funguo za gari ya Naya mikononi kwake wakati
akijifungulia mlango. Akamfungulia yeye mlango, Naya akapanda. Akamfunga mkanda
kabisa ndipo akamkabidhi funguo na kumsaidia kufunga mlango. “Asante.” Joshua
akacheka taratibu akimtizama. Naya akawasha gari, akampungia mkono, nakuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua Kumu ameingia pichani kwa nguvu zote tena kivingine. Ndani ya
juma moja tu, amepata ukiri hadimu wa Naya, na kubadilisha moyo wa Naya
vilivyo. Usikose siku ya jumamosi ambayo Joshua alisema alikuwa akiisubiria kwa
hamu sana hata kabla hajazungumza na kuanzana na Naya mwenyewe. Huko ndipo amemuahidi Naya
atamfahamu Joshua Kumu halisi. Ipi historia yake na yeye? Naya anakwenda
kuketishwa na wakuu!
_ Njama ambaye alimtongoza Naya wa kwanza, anaonekana na hasira
pamoja na Wivu. Amebakia akitumwa kwa Naya, na huyohuyo Joshua. Wanasema hakuna vita
mbaya kama vita ya mapenzi.
Usikose muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment