Naya akaenda kukaa
pembeni ya baba yake. “Joshua ananipenda sana, baba.” Baba yake akacheka.
“Halafu ananihitaji. Anasema mimi ndiye nitakuwa ndugu yake wa kwanza.”
Akamuona anacheka. “Na mimi nampenda.” “Ndicho nataka kusikia. Uzuri anamjua Mungu.”
“Ni mnyenyekevu sana kwangu. Anajishusha, utafikiri sio Joshua Kumu!”
“Mbona ni kama kuna kingine hapo?” Baba yake alimjua Naya. Akajua kuna kitu
anataka kusema ila anashindwa. |
![]() |
“Hata hivyo naona si sawa, baba. Siwezi nikawa mtu wa kukataa baadhi ya vitu vya Malon, vingine napokea. Naamini Mungu atanipa kwa njia nyingine. Naomba niunge mkono katika hili.” “Sawa mama. Mimi nipo kwenye kukusindikiza kituoni kila siku asubuhi.” Naya akacheka sana. “Tunarudia enzi zetu. Tutakuwa sawa baba yangu.” “Sawa mama. Bora hivi kuliko vile vyakulia kila siku!” Naya akacheka sana na kurudi chumbani kwake. Akampigia simu Joshua. “Nakusindikiza mpaka nyumbani kwako.” “Nashukuru, maana nishaanza kuwa na hamu na wewe.” Wakaanza tena kuzungumza.
Jumapili.
Naya
na familia yake walikwenda kanisani kuabudu kama kawaida yao. Wote wanne.
Walipotoka hapo wakaenda sehemu kula. Joshua akampigia simu Naya. “Tulishatoka kanisani, ndio tumefika hapa tunataka kula.”
“Naweza kuja na mimi au huu ni muda wa familia tu?” “Na wewe ni familia Joshua.
Njoo. Lakini ujue sio zile sehemu za kisu na uma. Huku ni kula nje, tena vumbini.”
“Sijali. Ilimradi niwe na wewe.” Naya akafurahi sana. Akamuelekeza,
Joshua akamwambia atakuwepo hapo baada ya muda mfupi tu.
“Joshua
anakuja. Si ni sawa?” “Mwache aje atulipie. Tena ngoja niongezee kinywaji na
nyama.” “Sio vizuri Bale! Huko ni kumtumia vibaya. Ridhika.” “Asante baba
yangu.” Naya akafurahi sana kumsikia baba yake akizungumza hivyo. Bale
akanyamaza kama ambaye hajaridhika.
Ndani
ya nusu saa Joshua akawa amefika hapo. “Nilipitia nyumbani kubadili.”
Wakamsikia akizungumza na Naya aliyekwenda kumpokea sehemu ya kuegesha magari.
“Umependeza Naya!” “Asante. Hata wewe umependeza. Ila nilitamani kukuona jinsi
unavyovaa kanisani.” Joshua akacheka kama anayefikiria. “Sio tofauti sana na
ofisini. Kanisani huwa pia napenda kuvaa kikanisani, nikapendeza.” “Hata hapa
umependeza.” “Asante lakini sio hivi. Sivai suti wala kufunga tai, lakini navaa
shati na suruali. Sijui kama umepata picha mwanamitindo wangu?” “Nimeelewa.
Tumekaa upande ule kule mwishoni kabisa, twende moja kwa moja.” “Nimefurahi
tutakuwa wote mchana huu.” “Kweli Joshua!?” “Siwezi kukudanganya Naya. Shule
ilikuwa ikinichukulia muda mwingi, sasa sasahivi imeisha, najikuta tu nimekaa.”
Wakawafikia.
“Shikamoo
mzee wangu, na samahani sijui nimeingilia?” “Usijali kabisa. Huu ni muda wa familia.
Acha tule pamoja tumshukuru Mungu kwa wakati kama huu.” “Nashukuruni sana. Vipi
Bale?” “Safi kabisa. Karibu vumbini?” Joshua akacheka. “Nashukuru sana. Zayoni
upo?” “Shikamoo.” Akamsalimia kwa kumpa mkono. Naya akamletea kiti na kumuwekea
hapo pembeni yake, akakaa. Wakaanza kuzungumza wote. “Kwani wewe kanisani huwa
unakwenda wapi?” Bale akamuuliza. “Kinondoni.” Akamuelekeza. Baba yake akawa
akiwafahamu wachungaji wa hapo. Zikaanza stori nyingi tu wakicheka na
kutaniana, Joshua akaipenda familia yao. Walionekana ni watu wa kawaida tu,
lakini wameshikana sana. Wana umoja na kusikilizana. Walikaa hapo mpaka giza
lilipoingia, wakaagana.
Naya
alipopanda tu kwenye gari, simu kwa Joshua. Wakaanza tena kuzungumza mpaka
wakafika nyumbani bado Naya yupo kwenye simu. Wakaangalia taarifa ya habari
pomoja, bado Joshua akabaki kwenye simu masikioni kwa Naya akitumia bluetooth
zake. Zikaanza habari za kiuchumi, zilipokuja za michezo, Naya akahama hapo
sebuleni maana Joshua akaanza kulinganisha habari za uchumi za nchi mbalimbali
alizopata huko mitandaoni na kumshangaza Naya. Wakamuona anahamia chumbani,
ndio wakajua hawatamuona tena mpaka kesho yake.
Jumatatu.
Alishawaambia
Bale na Zayoni kuwa anarudisha gari ya Malon. Wakamsaidia kuisafisha vizuri
lakini Bale alionekana kutofurahia hilo kabisa, ila kwa kuwa Naya ndiye
aliyekuwa na kauli ya mwisho juu ya hiyo gari ikabidi ayaache tu, lakini ukweli
alikereka nakuanza kumuona Joshua watofauti. Asubuhi kama kawaida yake Naya
akadamka na kuwahi kutoka nyumbani. Moja kwa moja mpaka Kunduchi nyumbani kwa
Malon. Alifika getini, akamkabidhi funguo mlinzi na kumwambia hiyo ni gari ya
Malon, akiamka amkabidhi na funguo. Ujumbe akawa ameuacha ndani ya gari. Bila
ya kupoteza muda Naya akawahi tena barabarani kutafuta daladala ya kumpeleka
kazini. Akafanikiwa kupata usafiri, na kujikuta amefika kazini saa 12:15.
Akafarijika kwa kuwa bado alikuwa mtu wa kwanza hapo kwenye kitengo chao.
Akasafisha ofisi kwa kuyapanga maboksi yaliyokuwa yamezagaa hapo. Pakawa pasafi
angalau pakaonekana kama ofisi nyingine. Akakaa mezani kwake nakuanza kuangalia
viporo vya kazi.
Saa
mbili kasoro Joshua akawa amewasili mezani kwake. Naya akatabasamu na kugeuka.
“Upo sawa?” Joshua akamuuliza baada ya kumwangalia vizuri usoni. “Nipo sawa tu,
sema siku imeanza na shughuli nyingi, ila nipo sawa. Vipi na wewe?” “Safi tu.
Unataka nikuonyeshe kitu?” Naya akacheka na kusimama kumfuata alipokuwa
ameegemea meza macho kwenye simu, wengine wakiwaangalia. “Hii hapa ni ya screen
server yangu. Hii hapa ni ya lock, hii...” “Sasa mbona haraka Joshua, hata
sijajiangalia vizuri!” “Acha kukariri picha Naya!” Naya akacheka sana.
“Kwa
hiyo unaniweka kwenye kila kitu?” Naya akauliza kwa deko ila kwa kunong’ona.
“Hii uliyocheka vizuri, ndio screen server ya kila kitu mpaka laptop na ipad
zangu zote.” “Sasa acha mimi nikuonyeshe yangu. Na usiige Joshua!” Joshua
akacheka sana. “Wewe nionyeshe.” “Mbona kama nakuhisi vibaya bwana!” “Acha
woga. Mimi nishachagua zangu, sibadilishi mpaka nipate picha pinzani. Ziwe
zimezidi sana hizi.” “Basi ona sasa simu yangu ilivyopendeza.” Yeye Naya
aliweka picha yao wote wawili Joshua alitegesha kamera walipokuwa kwenye boti.
Ilitoka vizuri sana.
“Hapa
kweli umenitamanisha.” “Nilikuonya Joshua!” “Hata hivyo sibadilishi.” “Leo
tutaonana tena au ndio basi tena mpaka kesho?” Joshua akafikiria. “Ratiba ya
leo bado sijaipenda. Acha tuwasiliane baadaye.” Njama akamfuata mpaka pale.
“Kikao na jamaa wa uzalishaji ni mbili kamili, Joshua. Nimeona wakielekea
kwenye chumba cha mkutano tayari.” “Nipo nyuma yako.” Akajibu Joshua.
“Sasa
Naya, namalizia ratiba za asubuhi, kwenye saa tano kamili nitarudi tujipange
vizuri.” “Sasa tena sio uanze kumtumia Naya, wakati na mimi namtegemea hapa.
Hapo tena tutakosana Njama, na tutavurugana kabisa.” Jamal akaingia na kumjibu
Njama. Joshua akaondoka bila ya kuongeza baada ya kumkonyeza Naya. “Sasa wewe
ulitegemea ile kazi nakamilisha vipi!?” Njama akauliza kwa kushangaa kidogo.
“Sikuoni mbele yangu Njama.” Wakamsikia Joshua akiongea akisikika ameshafika
mbali, Njama akatoka akikimbia. “Uje tuzungumze vizuri Njama. Maana nikiwa na
vimeo hamvitaki. Nikipata jembe, mnachukua nyinyi, mnabaki mkinilaumu tu.” Naya
akatulia kimya hakutaka kuingilia.
“Nani
kahamisha haya maboksi hapa!?” “Ni mimi Jamal. Nimekosea? Kama nimekosea, naweza
kuyarudisha, ila nimeyapanga vizuri na nimeyaandika ili isisumbue wakati wa
kutafuta vilivyomo ndani.” “Hakika hawakutoi humu ndani Naya. Nitapambana nao
mpaka kwa CEO. Hii kazi niliwapa kina Zena, tena nikamwambia Kibasa asimamie
ikamilike. Tena tokea hamjaanza nyinyi kazi. Ikawa maneno na visingizio kwamba
humu ndani hakuna sehemu ya kuyaweka. Bisha Zena.” Zena na Kibasa kimya. “Sasa
mbona Naya amepata? Ona kulivyokaa vizuri! Walinitia shughuli mpaka kutaka
nigombane na uongozi wakitaka tupewe stoo nyingine, eti tuna vitu vingi. Mbona
vimetosha sasa?” Jamal akaanza kugomba tena na kuwasema wengine kwa sauti ya
juu kama kawaida yake. Naya kimya macho kwenye kompyuta yake.
Malon
Malon
alipoamka akiwa anatoka, akakutana na funguo za gari getini. Akaambiwa gari ipo
nje, ina ujumbe ndani. Malon akaumia sana. Akaenda kuchukua huo ujumbe. ‘Malon, naamini upo mzima na Mungu anaendelea kukubariki.
Nashukuru kwa kunifikiria usafiri, lakini naomba nirudishe tu. Sitaweza kuwa na
mali yako nikiwa nimekukosa wewe Malon. Kilio changu na haja yangu ilikuwa wewe
tokea nakufahamu, sio mali. Maadamu nimeshindwa kukupata wewe, vingine najihisi
ninakuwa kama watu wengine ambao huwa wanakutumia tu. Kila la kheri. Mungu
akubariki. Naya.’ Hiyo siku ikawa imeshaharibika kwa Malon.
Akafikiria na kuamua kumfuata Naya ofisini kwake.
Ilikuwa
saa nne na nusu wakati Naya alipopata simu kuwa anamgeni getini.
Akashangaa sana. Hakuwa hata na wazo na Malon. Akatoka kwa haraka kuelekea
getini. Akamkuta Malon. Akatulia kwa muda akimshangaa. “Naomba tuzungumze
Naya.” “Nipo kazini Malon.” “Nafahamu. Sitakuchukulia muda mrefu.” Naya
akafikiria na kuona amsikilize. Akaamua atoke pale getini mbele ya walinzi,
wakazungumze nje kabisa ya geti. Akaandikisha jina lake na muda anaotoka, akatoka.
Wakaongozana mpaka wakajikuta wamebakia wao wawili tu.
“Huu
ni muda wa kazi Malon! Hapa bado mimi ni mgeni hata sijaajiriwa bado. Naomba
tusichukue muda mrefu.” “Samahani, nahisi nilipaniki kuona umerudisha gari!
Kwani umesahau kama nilikwambia lile gari ni lako? Ni lako Naya, tafadhali
usiteseke wakati gari ipo. Sitakaa nikaiulizia hata mara moja. Nimekuahidi
hivyo na nitasimamia hilo. Hata kama mengine nilishindwa, hilo nakuahidi
sitabadilika.” “Cha kwanza ile gari ni yako Malon. Hata jina ni lako.” “Kwa
sababu mimi ndiye niliyelinunua siku ile Naya. Hukuwepo, sikuwa na kitambulisho
chako, ningefanyaje mama?” Naya akaanza kulia. Malon akataka kumshika, Naya
akarudi nyuma.
“Tafadhali
usikubali kujitesa sababu ya makosa yangu Naya. Acha mimi nilipe gharama,
lakini si wewe.” “Mimi sikuwahi kutaka mali
kutoka kwako Malon. Ila wewe. Maadamu wewe nimekukosa, vingine vyote sina haja
navyo. Sina shida na mali Malon. Ndio maana niliuza kila kitu ili niwe na wewe,
lakini ulinikataa. Naomba usiniguse Malon.” “Basi naomba usilie.
Tafadhali Naya. Nimeshakuliza vyakutosha mpenzi wangu. Naomba usilie tena.”
Naya akajifuta machozi. “Kwa heri Malon.” “Nina
hamu na wewe Naya! Nakaribia kurukwa na akili.” Malon akaongea kwa upole
akilalamika. “Utakuwa sawa Malon. Tulia ufikirie
ni nini kinakuchanganya. Lakini nina uhakika sio mimi kabisa kwa kuwa ulikuwa
na mimi kwa miaka zaidi ya mitano, ukinikataa kwa manyanyaso makubwa sana. Mimi
si sababu ya kuchanganyikiwa kwako. Kila la kheri.” Naya akataka
kuondoka.
“Naya?”
Akamwita, Naya akageuka. “Nifanye nini ili uweze kunisamehe?” “Nimekusamehe Malon.” “Naomba unisamehe na
unipe nafasi nyingine, nakuahidi hii ni ya mwisho na nitafanya tofauti.” “Sina nafasi nyingine yamajaribio Malon. Mimi si
mwanamke Mungu anataka niwepo kwenye maisha yako. Tumejaribu mara kadhaa
imeshindikana. Yupo mwanamke mzuri tu Mungu amemuandaa kwa ajili yako, lakini
si mimi Naya.” “Mimi nakutaka wewe Naya.” “Umeyajua hayo lini Malon? Ni lini umejua hilo au si
kutaka kuniumiza tu?” Naya akamuuliza kwa ukali kidogo.
“Ukinirudia
sasa hivi, nakuhakikishia Naya, hutajuta.” “Hivyo
ulivyo sasa hivi, hunifai Malon. Ungekuwa umetoka jela, tukaendelea na
kupambana pamoja mpaka sasa hivi! Hapo sawa. Nilikuomba tuanze pamoja, lakini
ulinikataa Malon. Kwa nini sasa hivi unarudi?” “Kwa kuwa nakupenda
Naya. Hakuna maisha bila wewe.” “Kama kweli
unanipenda Malon, tafadhali niache. Acha kunichanganya kama ulivyozoea
kunifanyia tokea nakufahamu. Endelea na maisha yako, na mimi niache niendelee
na yangu. Kwa heri Malon.” Naya akaondoka bila yakugeuka tena nyuma
huku akijifuta machozi.
Sukari yageuka
kuwa Shubiri kwa Naya.
Akarudi
ndani akijua wazi uso wake unaonyesha alikuwa akilia. Hakutaka watu wamuone
hivyo. Akaingia kwenye choo cha walinzi baada ya kusaini kuwa amerudi ndani.
Akashangaa machozi yakianza kumtoka tena asijue ni kwa nini. Akakaa hapo akilia
kwa muda. Akaosha uso na kujaribu kutulia, ndipo akatoka hapo chooni kurudi
ofisini kwao. Wakati anaingia mlangoni kwenye idara yao akakutana na Njama
mlangoni. “Vipi Naya?!” Njama akauliza kwa ukali kidogo na kumshangaza Naya.
“Safi tu!” Naya akajibu lakini akiwa kama na yeye anaswali ni nini kinaendelea
kwa jinsi alivyouliza Njama.
“Unakumbuka
miahadi yetu ya saa tano au umedharau kwa sababu ni mimi nimeongea na si
Joshua?” Naya akashituka. Kabla hajajibu Njama akaendelea. “Nilikuja ili tuweke
sawa ile kazi kama nilivyokwambia asubuhi, lakini ukanipuuza. Nakuja hapa
kukufuata mama bosi, nikaambiwa unamgeni.
Nikajishusha, tena nikiangalia muda ninaopoteza kukusubiria wewe nikiwa
nimeacha shuguli za muhimu sana. Au unaona mimi sina mambo mengine
yakufanya ila kukufuata tu wewe?” Naya akashangaa ile jazba yote, ila
akajishusha.
“Samahani
nilitoka kidogo. Ila sasa hivi nipo na sitatoka tena. Tunaweza kuendelea.” “Kwa
hiyo sasa hivi wewe ndiye unayeongoza kitengo? Tunafanya mambo vile
unavyojisikia wewe?” Naya alishindwa hata kujibu. Ila akaumia sana. Akajua ndio
amekosa nafasi yakufanya kazi na mtu kama Njama. Njama ni msaidizi wa Joshua,
inamaana kufanya naye ile kazi, ingemsogeza karibu na wakubwa zaidi. “Samahani
Njama.” “Hiyo ni dharau.” Njama akaondoka.
Kwa Baba Naya.
Naya
akajua ndio inamaana Joshua ataambiwa. Akazidi kuumia na kuingiwa hofu. Akajua
Joshua atamuona ni mbambaishaji. Akajutia wazo la kukubali kusimama na
kumsikiliza Malon muda ule. Akatamani kama angemwambia wazungumze wakati
mwingine kama kuna jambo la muhimu. Hapakuwa na jinsi tena. Maji
yalishamwagika. Akaelekea chooni. Naya alilia sana kwa uchungu. Akampigia simu
baba yake na kumuelezea kila kitu akiwa hukohuko chooni.
“Naya mama, kama Mungu amekuandikia chako, ni chako tu.
Nilishakwambia, barua yenye jina lako, hakuna malaika anaweza kuitoa mkononi
mwa Mungu na kwenda kumkabidhi mtu mwingine. Unaweza ukajichelewesha tu
kuipokea, lakini umegundua kosa, rudi pale ambako Mungu amekuweka, atamtuma
tena malaika wake, atakuletea tu. Ila hakikisha safari ya pili, huyo malaika
hakukosi.” Akamtuliza
binti yake, akatulia. Naya akaosha tena uso, akarudi kwenye meza yake kukaa
asijue Njama alipata jukwaa.
Wafanyakazi
wenzie.
“Nasikia
bwana wako wa mtaani amekuja kukufuata kazini leo?” Naya alishituka sana,
akamgeukia Zena. “Unaongea nini wewe!?” “Tumewachungulia na picha tumepiga,
usije bisha baadaye. Tumewaoneni wewe na yule mwanaume wako. Tena ili usigonganishe
magari, ukaenda kuzungumza naye nje kabisa, wakati ni muda wa kazi! Sasa
lilivyokuvujia, Njama naye akawa amekuja, amejua ulikuwa kwa mwanaume wako, nje.
Tena muda huu uliotakiwa kufanyakazi.” “Mtakatifu Naya! Maana wewe ndio
mchapakazi humu, sisi wote hatufai!” Mwenzake Zena, yaani Prisca aliyemkuta
hapo kazini akadakia. Wakaanza kucheka. “Ulitukuta Naya. Ukajidai wewe ndiye
mwenyewe, unajitenga. Sasa hapa ni Coca. Tutakuona mwisho
wako.” Wakawa wamemtisha Naya. Naya akawatizama tu bila kuwajibu,
akarudi kufanya kazi.
Akajua
tayari maneno yataenea. Aliingiwa na hofu, akatamani kutoka kumpigia simu baba
yake amwambie tena, lakini miguu ikawa kama imekufa ganzi. Wasiwasi ukamzidi
juu ya atakachopelekewa Joshua, na Njama aliyeondoka hapo kwa jazba akiwa
amejazwa maneno ya kina Zena wanao muonea wivu nakuona anawapita. Akabaki
ametulia hapo kwenye kiti chake, macho kwenye kompyuta hana afanyalo. Akatamani
kumtumia ujumbe Joshua, lakini amwambie nini! Akabaki ametulia tu kitini.
Moyo Wa Mtu, Msitu.
Baada
ya kikao cha asubuhi, Joshua alitoka na Jema, wakamuacha Njama. Lakini Joshua
alimwacha Njama kwa makubaliano kuwa afanyie kazi wazo alilotoa Naya, tena kwa
kumshirikisha Naya mwenyewe. Waweke pamoja hata kwa kurikodi ndipo wawatumie
watu wa matangazo ambao pia, wangefanya kazi kwa karibu na Naya ili watoe kitu
kilichopendwa kwenye kikao, Joshua asijue kinachoendelea kwa Njama.
Joshua
alirudi akiwa amejawa furahi sana baada ya kuingia mkataba mkubwa kwenye moja
ya plaza kubwa sana hapo mjini ambao walikubali kufanya kazi nao. Kwamba katika
hiyo Plaza nzima, kuanzia nje ambako wangeweka mafriji yao mpaka ndani ambapo
kuna migahawa mikubwa na watu wengi wanakwenda kula hapo, zitauzwa bidhaa za
kampuni yao tu.
Hata
Jema alijua Joshua amefurahi. Ni wazo alilokuwa amelifikiria, na kumtuma Jema
amtafute mmiliki wa hiyo Plaza kisha amuunganishe naye, ili wazungumze. Na
kweli Jema akafanikisha ndipo wakaenda pamoja na kukubaliana.
Fina
sekretari wake alimuona jinsi Joshua alivyoingia akiwa na furaha, akajua mambo
yamekwenda vizuri. Ila akamuhurumia akijua moto umewaka. Bila kujua Joshua
akagonga na kuingia ofisini kwa Njama bila kusikia kukaribishwa. Ila halikuwa
jambo la ajabu. Akaingia akiwa amechangamka ila akashangaa Naya hayupo. “Vipi
ile kazi, mara hii mmeshamaliza!?” Akauliza Joshua vizuri tu akiwa amesimama
mlangoni ameshikilia kitasa cha mlango hata Fina pale nje anamuona. “Ndio
naifanyia kazi.” Njama akajibu.
Joshua
akakunja uso kidogo. “Kwani vipi? Si unataka kazi ifanyike?” Isivyo kawaida,
Njama akamuuliza kwa kumfoka kidogo Joshua, Joshua akatulia akimtizama Njama
ambaye alipotoka kwa Naya, akaingia hapo kwa Fina, Joshua na Jema wakiwa
hawapo, akaongea mengi sana mabaya, ndipo akaingia ofisini kwake.
“Ndio
nafanya kazi. Au ghafla unaona mimi sina uwezo wa kufanya kazi kama hii, ila
Naya?” Joshua akaachia kitasa, akasimama wima, mikono akakunja kifuani
akamkazia macho Njama. Jema aliposikia akashituka sana na kumwangalia Fina kwa
mshangao. Fina akamwandikia kwenye kikaratasi ‘MOTO’.
Jema akakunja uso. “Maana hili ni wazo la kawaida tu ambalo kila mtu analijua.
Na yeye Naya alizungumza pale akitumia mawazo ya watu tu. Nashangaa vipi ghafla
ije kuwa jambo la mpaka ashirikishwe yeye na wakati kwanza si mwajiriwa hapa,
na wala hawezi kuajiriwa.” Jema akasogea karibu kujua kulikoni. Akampita Joshua
pale mlangoni akaingia ndani kabisa ofisini kwa Njama.
“Kuna
nini Njama, mbona kama unawaka kupita kiasi?” “Huyu mtoto anakiburi sana.
Kaongea jambo moja mbele yetu, sijui kaambiwa na nani kuwa ashapata ajira hapa,
eti mimi namwambia kabisa, saa tano nitamfuata ili tufanye kazi, halafu
anaondoka ofisini muda wa kazi, tena bila hata kiongozi wake kujua alipo! Mimi
nakwenda pale, namuulizia, wenzie wananiambia kafuatwa na mwanaume wake,
wametoka. Saa nne na nusu asubuhi, muda wa kazi!” Njama akaendelea kwa jazba,
Joshua kimya akisikiliza.
“Nikamfuata
Jamal kumuuliza kama muda ule wa kazi kama Naya amemuaga, maana nilimwambia
tena mbele ya Jamal kuwa ningemfuata tufanye kazi, Jamal ananiambia hajamuaga,
ametoka tu. Nikapiga simu getini, naambiwa amesaini kabisa, ametoka! Anatoka vipi
mida ile ya kazi, nikiwa nimemwambia kuna kazi ya kufanya, anakwenda kukaa nje
anazungumza na mwanaume wake kwa kujiamini kama si dharau kwangu ni
nini? Lazima nitamuwajibisha.” Njama akaweka mkwara mzito.
“Mimi
nashauri utulie kwanza Njama. Naona umepaniki sana.” Jema
akamtuliza. Joshua kimya. “Sijapaniki! Naongea ukweli. Huo ni utovu wa nidhamu
na nimemwambia sitaweza kufanya naye kazi.” “Kumbe alisharudi na
mkaonana?” Joshua akauliza taratibu tu. “Amekuja kurudi baadaye sana muda wa
kikao ulishaisha!” Njama akasimama kabisa kama ambaye hakutaka ababaishwe na
Joshua.
“Hiyo
ni dharau kwangu kwa kuwa anajua sasa hivi na wewe...” “Njama! Nashauri utulie.
Tafadhali tulia Njama. Maneno huwa yakitoka hayarudi hata ukiomba msamaha.
Tafadhali tulia Njama.” “Na wewe Jema unaona alichofanya ni kizuri au kutaka
kujipendekeza tu? Na nimemwambia Jamal anipe majibu ya kueleweka juu yake Naya.
Lasivyo na yeye nitamuwajibisha. Inamaana hafanyi kazi zake vizuri. Hajui
kuongoza idara. Anakuwepo vipi tu pale na watu wa chini yake wanaingia na
kutoka tu ofisini kama wanavyotaka! Hatuwezi kuendesha kampuni kwa namna hiyo.”
“Kweli Njama!?” Jema akashangaa sana. “Kweli nini?” Njama akamuuliza kwa ukali
sana.
“Umeingiwa
nini kaka? Kwani Naya ndio amekuwa wa kwanza kupata mgeni hapa kwenye hii
kampuni!” Jema akashangaa sana. “Mbona kama huelewi hoja yangu Jema au
unajipendekeza tu kwa jamaa hapa? Anatokaje nje kabisa ya kampuni, muda wa
kazi, eti sababu ya kutembelewa na mwanamme wake!? Hii kampuni
ikiendeshwa kwa kuendekeza mapenzi si itatufia mikononi
mwetu?” Joshua akacheka kidogo akimtizama Njama kisha akaondoka.
“Fina,
naomba vitabu wanavyosaini wafanyakazi wote vilivyopo getini, sasa hivi,
ofisini kwangu. Nataka mpaka vya miezi miwili nyuma.” Wakamsikia Joshua
akiongea na Fina. Jema akamshangaa sana Njama. “Ni nini Njama? Mbona unawasha moto
ambao huna uwezo wa kuja kuzima!?” “Hakuna wakunitisha mimi. Nayajua majukumu
yangu, ndio ninayoyasimamia. Kama mtu atanifikiria vibaya kwa kuwajibika
kwangu, basi. Hakuna mwajiri wangu hapa. Wote tumeajiriwa. Mtu hawezi
kunibabaisha. Kila mtu anashida zake, na tunatakiwa kuwajibika. Kama mnataka mapenzi
ndio yaongoze hii kampuni, waambieni wamiliki.” Njama alipaza sauti kama
anayetaka Joshua amsikie. Jema alikuwa akimshangaa Njama, kama ameona mzimu.
“Unashangaa
nini kama huelewi? Au jamaa ashakutisha sana mpaka unashindwa
kufikiria?” “Labda nikuulize Njama, ni hilihili unalozungumzia hapa au kuna
jingine nyuma ya hili?” Jema akamuuliza kwa upole tu. “Maana kama ni kweli ni
hili, nashauri leo ukapumzike nyumbani, uje kesho ukiwa umetulia. Unaharibu.”
“Kwa lipi na kwa nani?” Njama akauliza kwa kujiamini.
“Hivi
huyu Naya, siye sifa zake zinaimbwa hapa na Jamal tokea walipoanza kazi kuwa
anafanya kazi zaidi ya alivyopangiwa?” “Si anajipendekeza tu Jamal ili
jamaa hapa amuone yupo upande wake.” “Tulia Njama wewe! Vita
unayoanzisha hiyo ni hatari mno! Huyu Jamal anamtegemea sana Naya kwenye ile
ofisi. Na alianza kutaka Naya apewe ajira tokea muda mrefu tu akisema anazo
sifa zote. Ukakataa Njama.” “Kwa kuwa hata hakuwa ametimiza muda wa
probetion!? Ulitaka niidhinishe ajira kwa mtu ambaye hata hatumjui! Sasa umeona
jinsi tabia zake zilivyo baada ya kuitwa kwenye kikao kimoja tu?” Jema akafunga
mlango.
“Mimi
siogopi hata wakisikia. Nishamtumia Jamal email yamkutaka maelezo juu ya
Naya, na nimemtumia HR pia. Sitaki mambo kiholela.” Jema akashituka
sana. “Njama!” “Kabisa. Tulizungumza nini kikao cha asubuhi? Si tuwajibike?
Tena Joshua mwenyewe alisema tuchape kazi. Ndio nachapa kazi sasa. Mbona
mnalalamika. Panga linapita kotekote.” Jema akamshangaa sana
Njama. “Mimi nakuonya Njama. Tulia, kaka. Huko kilipo kichwa chako
leo, tafadhali kitoe, kirudishe kwenye uhalisia. Sasa hivi unacheza na ajira za
watu muhimu sana. Jamal umemkuta hapa kazini, kisha Joshua ni kiongozi wako
hata iweje. Na hawa watu wawili unaotaka kushindana nao, ni watu
muhimu sana kwenye hiki kitengo. Nashauri tulia.” “Usinione mimi mjinga.
Nafanya mambo yangu kwa umakini sana. Nimejidhatiti. Siwezi kuwa
kibaraka wa mtu.” Jema akamtizama, nakufungua mlango akatoka kurudi ofisini
kwake akamuacha Njama akifoka haswa.
Kwa Naya.
Jamal
akamfuata. “Naya, naomba uje ofisini kwangu.” Mwili mzima wa Naya ulikuwa
ukitetemeka. Akasimama na kumfuata nyuma, wenzake wakaanza kumcheka. Akaingia
ndani akakuta wenzie Jamal wapo hapo. Jamal akakaa. “Niambie ni nini
kinaendelea? Mbona sielewi?” Jamal akaanza. “Asubuhi wakati na wewe
upo pale, unakumbuka Njama alisema anakwenda kuweka mambo yake sawa, kisha kwenye
saa tano. Tena akasema kama kwenye saa tano hivi, akasema angerudi
tufanye kazi!” “Nakumbuka.” Jamal akaongeza. “Basi, nikiwa nafanya kazi
ulizonipangia wewe, nikapigiwa simu nina mgeni getini. Samahani Jamal,
sikufikiria bosi wangu. Mimi nikatoka bila kuangalia muda wala sikukuaga kwa
kuwa nilijua sitachukua muda mrefu. Kwa kuwa sikutaka kuzungumzia pale, ikabidi
nitoke naye nje nikazungumze naye. Niliporudi nikakutana na Njama na yeye
anatoka.” Kila mtu akakunja uso.
“Mmmh!
Wewe Naya, hebu zungumza vizuri. Hakuna ulipojibishana na Njama?” Mwenzie Jamal
akauliza. Naya akashangaa kidogo. “Hapana dada yangu. Nilimuomba msamaha na
kumwambia nimerudi, tunaweza kuendelea. Lakini nafikiri alishakuwa
amekasirika.” “Sasa hiyo yakusema Naya anataka kuendesha hiki kitengo kama
anavyotaka yeye ametoa wapi?” “Sijui Jamal kaka yangu. Mimi nilikosea, nipo
tayari kuwajibika.” Naya akaongea kwa unyenyekevu ila akitetemeka haswa.
“Huyu
Njama ana lake huyu! Kwani Naya ndio wakwanza kutoka hapa muda wa kazi?” Jamal
akacheka. “Na ananitafuta. Anatafuta ugali wa wanangu! Kwa hili
tu ndio aniandikie barua na kumtumia nakala mpaka Afisa Mwajiri!?” Jamal
akauliza akishangaa sana. “Sasa acha nicheze naye. Wewe nenda kaandike barua ya
kujieleza kama hivi.” “Wewe Jamal, si ndio anajifunga?! Naya amekiri kutoka
muda wa kazi.” Mwingine akadakia.
“Sina
jinsi. Maana na yeye ameshapiga simu getini, ameomba nakala ya aliposaini Naya
kutoka. Inamaana hatuwezi kukwepa. Wewe Naya kaandike barua. Kazi zako zote
nazihamishia kwa kina Kibasa. Najua hazitaisha leo, lakini najua
wameshakuchanganya, huwezi kufikiria tena.” “Hapana Jamal. Nitafanya tu.
Maadamu bado sijafukuzwa kazi, mimi bado nipo chini yako, nitazifanya tu.
Nakuandikia barua sasa hivi, nakutumia. Na samahani sana Jamal. Naomba
nisamehe.” “Wewe usijali. Ungekuwa mtu mwingine, hakika ungeondoka sasa hivi
Naya. Lakini najua huwa unafanya kazi zaidi ya muda tunaokulipa tena bila
kulalamika.” “Halafu si huyuhuyu Naya ulikwenda kumuombea kwa Njama amlipe
overtime na amwajiri, akakataa.” “Nenda Naya.” Jamal akamtoa pale kama hakutaka
asikie zaidi.
Naya
akarudi mezani kwake, ili anaandike hiyo barua. Wenzie wakaanza kumkebehi na
kumcheka tena. Muda wa chakula cha mchana ukawa umefika. Wakatoka huku
wakicheka na kurusha maneno ya kebehi, ambayo Naya alijua wanamrushia tu yeye.
Naya akaandika ile barua kama alivyomueleza Jamal. Wakati anamalizia, Joshua
akawa ameingia. Naya akageuka aliposikia hatua zikimkaribia. Akabaki
akimwangalia na kushindwa hata kumsalimia. Hakujua amesikia nini tayari!
Akabaki akimwangalia. Joshua akasimama mbele yake, mikono mfukoni.
“Umeshakamilisha barua uliyotakiwa kuandika?” “Ndiyo. Hii hapa.” Naya
akainyanyua na kumkabidhi. Mikono ilikuwa ikitetemeka, karatasi ilikuwa
ikicheza haswa. Joshua akaipokea. Akamuona ameisoma ndani ya sekunde chache
sana akawa amemaliza.
“Twende.”
Akamnyooshea mkono. “Siwezi hata kusimama
Joshua!” Naya akaanza kulia. Joshua akazunguka kule alipokuwa
amekaa, akamsaidia kusimama. Wakatoka hapo mpaka ofisini kwa Jamal. “Mbali na hii
barua, kuna kitu kingine unataka kutoka kwa Naya, sasa hivi?” “Bado Njama
hajanipa maelezo mengine. Ametaka iandikwe kwa mkono kabisa, kisha itolewe
kopi. Nakala moja iwekwe kwenye faili apelekewe yeye, halafu hiyo ya pili
nipeleke kwa Afisa Mwajiri.” Joshua akamkabidhi ile barua, Naya amesimama nyuma
yake. “Tafadhali angalia kama kuna kitu kingine kinahitajika kabla sijaondoka
na Naya.” Jamal akasoma mwanzo mpaka mwisho. “Nafikiri anachotaka Njama kipo
hapa. Kuwa Naya alitoka muda wa kazi. Na Naya ameandika hapa kwa uwazi tu. Acha
nitoe kopi kisha niwapelekee, nipate muongozo mwingine. Nitamjulisha Naya.”
Joshua akatoka akiwa amemshika mkono Naya.
Joshua
Katika Nafasi yake.
Kila
mtu akaona wakitoka hapo kuelekea sehemu ya kuegesha magari, akiwa amemshika
mkono Naya akilia taratibu. Kabla ya kumfungulia mlango Naya akamvuta mkono
kidogo, Joshua akageuka. “Sisikii kula kitu.” Naya
alikuwa akitetemeka sana. Mpaka midomo. “Halafu
sidhani kama sasa hivi ni sawa tukionekana pamoja Joshua. Nimeshajiingiza doa, sitaki
nikuharibie na wewe.” Joshua akamgeuka vizuri. “Ikiwa mimi ndio
nakuharibia?” Naya kawa hajaelewa. “Unajuaje pengine mimi ndiye ninayesababisha
uwe matatizoni?” “Hapana Joshua. Nilikosea
kutoka muda wa kazi bila kuaga.” “Unafikiri wewe ndio wa kwanza
kufanya hivyo? Unafikiri hiki ulichokifanya wewe ni kitu kigeni sana kwamba
uongozi hautambui kuna watu wanatoka?” Naya akaendelea kulia.
“Nimeangalia
muda uliotoka na kurudi kutoka kwenye chati uliyo saini pale getini, hukumaliza
hata dakika 10 tokea utoke na urudi.” Naya akashangaa kidogo. “Ninazo rikodi
zote ofisini kwangu. Hujafanya jambo la ajabu Naya, na si kigeni kabisa.
Hujatoroka kwamba ulionekana nje ukiwa hujaandikisha popote. Tena uliitwa na
walinzi kutokea ofisini kwako ukifanya kazi. Ila hukumuaga mkuu wa
idara.” “Nilipaniki kusikia nina mgeni. Sikuwa
hata nikitegemea kuwa na mgeni hapa! Sikujua kama ni Malon amekuja.” “Ingia
ndani ya gari tuzungumze.” Akamfungulia mlango, Joshua akawasha gari na kurudi
kukaa nyuma ya gari pamoja na Naya.
“Kwanza
naomba utulie Naya.” “Naogopa sana siwezi
kujisaidia.” Naya akazidi kulia, akiendelea kufuta machozi kwa
mikono bila kumaliza. “Niangalie mimi.” “Mwili
unatetemeka sana Joshua. Labda nimuite baba.” “Huwezi kuwa
ukifanya hivyo Naya. Hii ni kazi ambayo watu wengi wanakuamini. Umekosea padogo
tu, ndipo Njama amepata sababu. Baba hawezi kukusaidia hapa ila wewe
mwenyewe.” “Labda hata nizungumze naye kidogo
tu, akili inaweza kutulia nikaweza hata kufikiria. Sijawahi kuogopa hivi
Joshua. Naomba nimpigie tu baba ili nitulie.” Naya alijawa kwikwi
kwa hofu.
“Kila
baraka inakuja na kuwajibika Naya. Usifikiri mimi nimefika hapa nilipo kwa
urahisi tu! Kwamba eti niliomba, halafu kila kitu kikatokea! Na kwa taarifa
yako tu, hii si yako peke yako. Ibilisi amepata huo mlango ili kunifikia
mimi aharibu mimba niliyokwambia inakaribia kuzaliwa.” Naya akatulia
kidogo kwa alichoongea Joshua. “Hakuna mtu amepata mwanya kwangu, hata mara
moja isipokuwa sasa hivi. Shetani amenitafuta katika mengi mno. Sasa hivi ndipo
anataka kunivuruga kupitia wewe.” “Samahani
Joshua.” “Huna haja yakuomba msamaha. Hili ni jaribu langu mimi,
nakuhakikishia Naya, tutashinda na tutatoka tukiwa tunang’aa. Simama, utauona
mkono wa Mungu.” Naya akamshangaa sana Joshua.
“Mbona sasa hata huulizi habari za Malon!?” “Nilikwambia kila
kilicho changu Mungu ananiletea mwenyewe. Sikukutafuta mimi. Mungu alikuleta
kwangu, najua wewe ni wangu Naya. Sina hofu. Tabia yangu inapimwa sasa hivi
nikiwa kwenye mahusiano. Si na Mungu tu, hata watu wengine. Na kwa taarifa yako
tu, sasa hivi kampuni nzima, macho na masikio yao yapo kwangu wala si
kwako. Kila mtu anataka kujua nitafanya nini.” Naya akaumia sana.
“Sikukusudia Joshua. Asubuhi nilikwenda mpaka nyumbani kwa
Malon. Sikutaka kuonana naye, nikamuachia ujumbe kwenye gari na funguo nikaacha
getini kwa mlinzi. Ujumbe niliomwachia kwenye gari, nilijua ungemtosha
kumuelewesha Malon kuwa nimemrudishia gari yake, na sihitaji tena. Wakati tupo
wote asubuhi, Njama aliongea vile kuwa kama kwenye saa tano, atakuja
tufanye kazi.” “Subiri
kwanza Naya. Ni wakati ule ndipo Njama alipokwambia na si kwamba pengine
alikupigia simu na kukwambia umsubirie anakuja saa tano kamili, kuweka miahadi
kamili?”
“Hapana Joshua. Lakini pia hilo lisingekuwa lazima. Unajua
sijawahi hata kutoka tokea nianze kazi! Sijawahi hata kuomba ruhusa kutoka
kabla ya muda wa kazi! Tena nilipanga leo ndipo nimuombe Jamal, niwahi kutoka,
tena ni kwa kuwa najiona nafanya kazi zaidi ya masaa niliyopangiwa, nilitaka
niwahi kutoka ili nikabadili jina la gari. Lakini tulipokubaliana na familia
nilirudishe tu gari, nikaona niwahi zaidi asubuhi, nilipeleke Kunduchi kabla ya
kazi, ili nisiombe ruhusa. Kwa hiyo nilijua muda wowote atakao kuja Njama,
tungeweza kufanya naye kazi.” Naya akaendelea.
“Nilipopigiwa simu kama kwenye saa...” “Ulionyesha umetoka
getini saa 4:30 asubuhi na kurudi saa 4:39.” Mpaka Naya akashangaa, maana
alikuwa akiandika tu muda pale getini bila kujua kama kungekuwa na kesi.
“Nilikwambia nilichukua vitabu vyote vya getini na mahudhurio yenu wote pale
ofisini kwenu, kwa miezi miwili.” Mpaka machozi yakakauka. “Utafanyaje Joshua?”
“Hakuna aliyewahi kuniona nikiwa na mwanamke.” Joshua akazungumza kwa kujiamini
mpaka akamtia moyo Naya.
“Samahani
Joshua. Sikutaka kukuletea matatizo, tena mapema hivi! Mimi nilijua tutazungumza
kwa muda mfupi tu. Tena palepale getini, nirudi ndani. Lakini aliposema anataka
tuzungumze, na kulikuwa na watu wengine pale getini, nikajua maneno yatasambaa,
na mimi namjua Malon anapotaka jambo lake. Huwa anatabia yakulazimishia.
Nikatoka naye, tena wala hakufanya fujo. Nikamueleza tu kuwa nilirudisha gari
kwa kuwa lilikuwa lake na kwa kuwa sasa hivi hatupo pamoja, na sina mpango wa
kumrudia tena, ni heri nimrudishie. Tena Malon akawa tu muungwana wala hakuleta
fujo zake, akanieleza lile gari alilinunua kwa ajili yangu. Ilimlazimu kuweka
jina lake kwa kuwa mimi sikuwepo wakati akilinunua, ikamlazimu kutumia
kitambulisho chake. Akanishauri nisikatae usafiri, niende nikabadilishe jina.
Nitoe kabisa jina lake niweke langu na ahadi yakunisaidia hata barua ya maelezo
kuwa alinipa mimi ili nisisumbuke kwenye vyombo vya usalama wakati nabadili
jina. Nikamkatalia na kurudi ndani.” Joshua kimya akisikiliza.
“Nilipoingia
getini nikatumia vile vyoo vya pale karibu na getini, ndipo nikarudi ofisini,
mlangoni nikakutana na Njama ndio anatoka. Akawa mkali. Ila nikamuomba msamaha,
nikamwambia nilipatwa dharula, ila nimerudi, tunaweza kuendelea. Ndipo akasema
mimi nimemdharau, nataka kuendesha idara nitakavyo mimi na mengine
mengi. Basi mimi nikarudi ndani ndipo Jamal akaniita na yeye akaniuliza
kulikoni. Nikawaeleza. Wote wakashangaa wakidhani kuna kitu naficha. Mimi
nikawaambia ndivyo ilivyokuwa, hivyo tu. Wote wakawa hawaelewi.” “Ni kweli
haieleweki!” “Ndio Jamal akaniambia natakiwa kuandika barua, tena Njama anataka
niandike kwa mkono, kisha nimpelekee yeye.” Joshua akacheka na kufikiria
kidogo.
“Samahani
sana Joshua.” “Kwa hiyo ulirudisha gari?” “Sitaki kukunyima raha Joshua. Mali
sitaki ziwe tatizo kwetu, hata baba nilimwambia. Sitaki mali zinitenge
na wewe.” “Sasa baba si atakuwa amenichukia?” “Baba yangu ana imani sana
Joshua. Wakati wote huwa ananiambia barua yenye jina langu, malaika hawezi
kukosea akampa mtu mwingine. Inaweza kuchelewa tu, lakini itanifikia.
Ameniambia nisiwe na wasiwasi, atakuwa akinipeleka kituoni kama zamani na
kunisubiria mpaka niondoke kituoni na kuja kunipokea jioni.” Joshua akajisikia
vibaya sana. Akagundua amesababisha usumbufu mkubwa. Akatulia.
“Nitafanyaje
Joshua?” “Nisikilize Naya. Mama akiwa mjamzito kabla hajapata furaha ya kunyonyesha
si anapita kwenye uchungu mkali sana?” “Ndiyo.” “Dhahabu ili ing’ae si lazima
ipitishwe kwenye moto?” “Ndiyo.” “Unajua ili matofali yawe imara sana, yale
yakuchomwa, si unajua lazima yawekwe kwenye moto?” “Sikujua.” “Mimi nimekulia
kwenye hayo mazingira ya matofali ya kuchomwa. Lazima yapangwe, ndipo chini
yake uwekwe moto mkali sana. Yakishakaa kwenye moto mkali sana kwa muda mrefu,
ndipo yanatolewa yakiwa yameshakuwa imara. Sasa hata katika hili, lipo kubwa
litazaliwa.” “Joshua!?” Naya akashangaa sana.
“Usikimbie,
wala usikate tamaa. Hayo machozi yawe kwangu tu. Mbele za watu usiwahi kulia.
Sasa hivi, muda huu, tabia yako inapimwa. Usiniulize na nani. Sijui kama ni
Mungu au Mungu anataka kumthibitishia nani! Mimi sijui. Lakini huwa namjua
Mungu anapotaka kufanya jambo lake.” Joshua akaongea kwa hisia.
“Hawezi
kuweka msingi juu ya msingi wa mwanadamu. Sijui kama unaelewa?” Naya akabaki
kimya. “Huyu Mungu ninayemjua mimi. Anapotaka kufanya yake! Yale yakufanya
masikio ya wanadamu yawashe, anamtindo wa kutingisha misingi. Na anapotingisha
huwa hajali kipi hakijakaa sawa. Hata wewe mwenyewe kama hujakaa sawa,
unakwenda na maji. Nilichojifunza, tena kwa msaada wa Roho mtakatifu,
nikuhakikisha Mungu anapotingisha kila msingi ili kujenga upya, mimi nabaki
nimesimama. Sasa hata katika hili, lazima uhakikishe wewe unasimama. Hawezi kuweka
divai mpya kwenye chombo kilicho chakaa! Huyo si Mungu ninayemjua
mimi, bwana!” Tayari ujasiri ukaanza kuongezeka kwa Naya.
“Lakini
nasikia amefikisha jina langu mpaka kwa HR, Afisa mwajiri!” “Ungejulikana vipi
kwa Afisa Mwajiri, bila hili?” Naya akaanza kucheka. “Mungu hutumia hata
wapumbavu kukufanikishia mambo yako. Acha pangurume. Acha Simba wa kabila la
Yuda angurume hapa mpaka wajue Mungu wetu yupo. Atanguruma hapa Coca,
mpaka watachanganyikiwa, lakini hakikisha unabaki wewe umesimama. Kila mtu
atajua yupo Naya hapa. Mungu akisharidhika pako sawa, ndipo atatuliza bahari.”
Naya akaanza kufurahia. “Acha kushangilia. Sio rahisi Naya! Njama amejipanga
kwelikweli. Ameomba kikao cha dharula na viongozi wa ngazi za juu. Lakini najua
shida yake ni mimi wala si wewe.” “Joshua! Huogopi?” “Hivi unafikiri wangekuwa
wakininunua kwa mamilioni ya pesa kama nababaishwa na ujinga kama huu? Nimethibitishwa
mimi, Naya! Na nikaonekana nimesimama.” Naya akacheka sana.
“Joshua!”
“Naya, nimetoka kwingi! Nimekutana na watu zaidi ya Njama ambao nilichukua
nafasi zao, tena wakiwa wamekaa kwenye hivi vitengo kwa muda mrefu sana. Eti
mimi natokea tu na wazo, tena nikiwa mdogo tu, nachukua nafasi zao, unafikiri
ilikuwa rahisi tu?” “Lakini kweli?” “Sasa. Wewe umetukuta tunasugua vichwa
juzi, ukatoa wazo lililopendwa na kila mtu, leo Njama anaambiwa na kiongozi
wake hawezi kuifanya kazi ya Naya bila Naya mwenyewe, unafikiri atafurahia tu?
Lazima patibuke. Sasa pakitibuka halafu wewe ukakimbia, ujue ndio hayo
anayokwambia baba yako, barua yako inachelewa. Mimi sina baba waziri wa uchumi
wala mkurugenzi sehemu fulani. Bila kusimama pale Mungu anapotaka niwepo kwa
wakati wake ili malaika aliyemtuma anikute na kunikabidhi barua yangu,
nisingefika hapa Naya! Huwezi kunitoa sehemu ninayojua Mungu anataka niwepo.
Hata mafuriko yaje. Nitashika sehemu moja, nitaogelea ilimradi kuhakikisha
baada ya wote kuondoka, malaika anikute MIMI nimesimama palepale na kunikabidhi
barua yangu. Ndio maana unaniona nipo hivi, umri huu, na nimekumbatia baraka
zangu zote.” Naya akacheka akimtafakari Joshua na yeye mwenyewe.
“Ubinadamu
ulitaka kunizidia kidogo tu leo, Njama aliponipandishia mbele ya kina Jema.”
“Haiwezekani Joshua!” “Ilikuwa mbaya sana. Tena hapo anatangaza ulitoka kwenda
kuzungumza na mwanaume wako! Nikatamani kuzungumza jambo fulani, lakini
nikakumbuka kutozungumza nikiwa na hasira na Jema akawa anamwambia Njama kuwa
huwa maneno yakitamkwa hayarudi, hata ukiomba msamaha. Japokuwa alikuwa
akimwambia Njama, lakini ikaniingia mimi mwenyewe. Nikanyamaza kabisa na
kuondoka pale, ndipo Mungu akanipa akili ya nini chakufanya kwa haraka na
kukumbuka wakati wote kabla sijatoa kitu kikubwa, huwa kuna jambo linatokea. Nikajua
wakati wa kujifungua umefika, shetani anataka kuniangusha kupitia wewe.
Nikacheka sana nafsi mwangu. Nikamwambia shetani, nimekukamata. Huniwezi.”
“Sasa
utafanyaje Joshua?” “Wajibu wangu wa kwanza ni wewe Naya. Wewe ukitulia
na mimi nitatulia na kuweza hata kumsikiliza Mungu kwa muongozo. Ila ukianza na
kumuita baba Naya!” “Basi Joshua. Nakusikiliza wewe.” “Basi tulia uone wokovu
wa Bwana. Si rahisi kama inavyosikika, lakini nimekwambia nini?” “Nihakikishe
katika yote, nibaki mimi ndio nimesimama.” “Safi sana. Sasa huu mchana wa leo,
tunatembeza mfungo, ili kuweza kumsikia Mungu vizuri. Shibe itatufanya
tushindwe kusikia vizuri. Masikio ya rohoni yanataka utulivu.” Naya akambusu
shavuni.
“Asante
Joshua. Niliingiwa hofu nilikuwa sijui itakuaje! Kwanza kwako baada yakusikia
Malon amekuja mpaka hapa, na nilitoka bila kuaga!” “Ulikosa Naya. Ulitakiwa
kumuaga Jamal. Na ujue umemuharibia na Jamal. Ataonekana anazembea.” “Nimekosa
Joshua. Hata Jamal nimemuomba msamaha. Akaniambia nishukuru kwa sababu ni mimi
na huwa namsaidia sana kwenye mengi. Amesema ingekuwa mwingine angeshanifukuza
muda mrefu sana.” “Unaona mbegu ya uadilifu imeshaanza kutoa mazao?
Haikukulipa wakati uleule, lakini wakati unaohitaji imejibu.” Naya akatulia
akifikiria.
“Ni
nini?” “Nikwambie kitu Joshua?” “Nakusikiliza.” Joshua akaangalia saa yake ya
mkononi. “Nahisi Njama anahasira na mimi kwa sababu nilimkataa yeye,
nimekukubali wewe.” Joshua akacheka na kumtolea simu yake akamuonyesha
ujumbe. ‘Analia wivu huyo. Naya alimkataa.’ Ulikuwa
ujumbe ametumiwa Joshua. Naya akashituka sana. “Nani amekutumia huu ujumbe.”
“Mimi hata sikujua kama Njama alishawahi kukutongoza mpaka Fina aliponitumia
huu ujumbe baada ya kuniletea mahudhurio yenu. Hapo ndipo nikafunguka macho.
Lakini pia, amechukia kutambuliwa wazo lako wala si yeye. Ameona unampita. Sasa
wewe usiwe na hofu. Baada ya yoote, mimi na wewe tutoke tumesimama.” “Acha
nikuombee Joshua.” Akamshika mkono na kumuombea kwa ufupi tu.
Wakati
wanaomba Jamal akagonga kioo. Wakamaliza, Joshua akafungua. “Namuhitaji Naya,
Kiongozi. Naona habari imegeuka.” “Nini tena?” “Jamaa anashitaki kuwa wazo
alilotoa Naya, wewe ulimpa ili aje aseme pale, aonekane wa maana, apewe ajira
ya kudumu. Hapa ameomba kamati ya nidhamu pia ifanye kikao na sisi. HR mkuu
akiwepo.” “Mungu wangu!” Naya akashituka sana na kumwangalia Joshua. Joshua
akacheka. “Show time.” Joshua akaongea hivyo kwa kujiamini, Jamal na
Naya wasielewe. “Kiongozi unaelewa lakini upana wa hili jambo?” “Oooh Sana tu
Jamal. Ni kubwa zaidi ya hivyo ulivyosikia.” “Nitafanyaje Joshua?” “Kumbuka
kila kitu tulichozungumza. Nenda na Jamal. Kumbuka, it may get worse before it
gets better.” Akashuka garini.
Akaenda
kumfungulia mlango Naya, akashuka. Jamal akasogea pembeni kidogo. Akawa kama
amemkumbatia Naya, akamnong’oneza. “Fanya kila utakachoambiwa, ila fanya kwa
ufasaha sana. Ukiitwa mbele ya wakubwa, hakikisha unamuwakilisha Naya vizuri,
tena nenda umbali mkubwa ila kwa kifupi na ufasaha sana. Hii ni nafasi ya pekee
Mungu anakupa kukutana na wakubwa wa hii kampuni. Inaweza isirudie tena. Ni
nafasi ya pekee. Wewe ndio unahatima ya huo mwisho. Hujajiandaa, lakini Mungu
atakupigania.” Akambusu karibu sana na sikio Naya akasisimka mwili mzima,
akafurahi.
Joshua
akamgeukia Jamal. “Jamal hii sura niione hivi hivi jioni baada ya kazi.”
Akimuonyeshea Naya anayecheka. “Mbona kama huelewi ukubwa wa hili jambo kaka!”
Joshua akacheka. “Kazi yangu ya wakati wa chakula cha mchana, nimeifanya kwa
uaminifu, tena vizuri sana Jamal. Nimekurudishia mfanyakazi wako akiwa
ametulia, na anauwezo wa kufanya kazi vizuri. Si ndio maana yupo hapa?
Kazi.” “Kweli kaka.” “Basi chapakazi, jembe unalo nimekukabidhi, tayari
kwa kazi.” Joshua akandoka kwa ujasiri wote. “Huyo ndio Joshua Kumu
bwana!” Jamal akaongea akimtizama anavyopotelea bila shida. “Kichwa chake sijui
kina nini huyu Jamaa!” Jamal akaendelea kuongea akimshangaa Joshua ambaye
alishaondoka. Naya akajisikia furaha, ujasiri ulishaongezeka.
“Halafu
wewe Naya, kwa nini hukuniambia kama Njama alishakutongoza?” Naya akamshangaa
Jamal kama anayemwambia haikuwa ikikuhusu. “Mwenzio analia wivu tu.” Naya
akajua Fina ashasambaza. “Umemkataa yeye, ukamkubali bosi wake!” “Kweli Jamal
unashangaa hilo? Wewe mwenyewe unaona akili yake kwa kile anachokifanya sasa
hivi. Atakuwa mwanaume wakuongoza familia gani yule!?” Jamal alicheka
sana. “Naona Joshua ameshakuambukiza Naya!?” “Kweli bosi wangu. Ona fujo yote
hii anayofanya! Ni nini sasa?” “Kwa hiyo sasa hivi huogopi tena?” Naya
akapandisha mabega kukataa macho chini. Jamal akacheka sana. “Mimi ilimradi Joshua
wangu yupo sawa, wengine sijali.” Hilo lilimgusa sana Jamal. “Kumbe mpo serious
na Jamaa!?” “Sitaki kucheza Jamal! Mimi sio mtoto mdogo.” “Ndio maana nakupenda
Naya. Twende tukapige kazi.” Jamal na Naya wakarudi ofisini hata Jamal
akaonekana ametulia sasa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alipoingia
tu ofisini ujumbe ukaingia kutoka kwa Joshua. ‘Tokea
uanze kazi, haya ndiyo masaa uliyofanya kazi. Na kuzalishia kampuni.’ Akamtumia
jumla ya masaa yote. ‘Lakini umelipwa kwa masaa
haya tu.’ Akamtumia ujumbe mwingine. ‘Ndio
mambo yakuzungumza mbele ya Uongozi, kikaoni, sio upuuzi wa dakika 9 ulizotoka.
Umenielewa?’ ‘Nashukuru kwa hizi taarifa. Nitazitumia vizuri sana.’ ‘That’s my
girl.’ Joshua akamrudishia huo ujumbe. Naya akacheka akijua
amemfurahisha. Naya aliyerudi siye waliyemuacha wakimcheka. Naya alirudi
jasiri, akarudi kitini na kuanza kuchapa kazi akiwa ametulia.
Baada
ya lisaa Jamal akamfuata. “Nusu saa kuanzia sasa unatakiwa kwenye kamati ya nidhamu.”
“Mpaka hapo na mimi nitakuwa nimekamilisha kila kitu. Acha nimalizie kabla ya
muda kufika. Tunakwenda wote?” “Na mimi natakiwa Naya! Hili jambo limekuwa
kubwa na naona linaibua mengine mengi.” Wote wakawa wakiwasikiliza. “Nisamehe
bosi wangu. Sikukusudia kukuingiza matatizoni.” “Daah!” “Nisamehe Jamal.
Sikujua kama itakugharimu hivi.” “Naamini na hili litapita.” “Hata mimi nina
matumaini. Acha nimalizie kwa haraka.” Naya akarudisha akili kwenye kompyuta na
kuendelea na kazi, Jamal akaondoka, nakushangaza wenzie waliokuwa wakifurahia
anguko lake. Kimya akiendelea kufanya kazi.
“Ndio
muda wenyewe Naya. Tusogee.” “Hata hivyo nishamaliza kazi uliyonipa.” Ghafla
Jamal na Naya wakawa watu wakuzungumza lugha moja. Naya akatoka hapo na pochi
yake na kijalida pamoja na simu yake akamfuata Jamal nyuma. “Niliwaambia
nyinyi, atatuacha tu.” Naya na Jamal wakawasikia wakimsema Naya. “Yako wapi?
Hekaheka za kudamka, kujidai mfanyakazi bora! Yako wapi?!” Wakaongea kwa
kejeli wakimcheka Naya. Jamal akamwangalia Naya, Naya akacheka tu akiendelea
kutembea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo yanazidi
kupamba moto. Usipitwe kujua kitakachoendelea kwa Naya.
0 Comments:
Post a Comment