Jumatatu.
![]() |
Ilipofika mchana. Nusu saa kabla ya muda wa chakula Naya akiwa
amegeukia kompyuta yake akiingiza taarifa na kuzipanga, akasikia. “Kiongozi
nifuate nyuki?” Akatambua sauti ya dada mwingine ambaye yupo ofisi moja na
Jamal. “Hii asali hailiwi hovyo.” Sauti ya Joshua. Mapigo ya Naya yakaanza
kwenda kasi, akageuka na kukuta Joshua anaingia hapo na Jamal akatoka ofisini
kwake akikimbilia pale. “Nakamilisha Kiongozi, na Njama anazo taarifa zote.”
“Muda wa chakula huu, Jamal!” Joshua akamjibu huku wakiingia pale ofisini.
“Naona vimefungwa kama vimetoka Kempinski hotel! Ni harufu tu! Na mimi nifuate
nyuki?” “Sio kila asali ni ya kuliwa Jamal! Vipi?” Jamal akaanza kucheka,
akasimama akimwangalia anapokwenda.
Naya akamuona anasogelea pale mezani kwake. Ofisi nzima wakatoa
macho maana ni Joshua Kumu, ofisini kwao! Huwa akiingia kila mtu anajitahidi
kuonyesha anafanya kazi, hakuna stori za mitaani. Panapoa kabisa hapo. Hata
Jamal mwenyewe huwa anaonekana kujibaraguza. Na hata kama ameshika simu,
hurudisha mfukoni kwa haraka au kubadili mazungumzo akijidai ni ya kikazi, ilimradi
tu Joshua awaone wapo kikazi.
“Kwa kuwa ulikataa nisikupigie simu tena, nimeona nije kukuletea
tu hiki chakula. Sijui kama ulikula au la!” Akakiweka kile chakula pale mezani.
“Siku..” Naya akataka kupinga. Lakini akagundua pale ofisini wote wanawatizama
kwa kujiiba na kuwasikiliza. Hata Jamal alikuwa amesimama kwenye sehemu ya
kuingilia hapo akiwatizama. Hapakuwa na mlango, ila korido tu. Chumba cha
mwisho kabisa ndipo ilikuwa ofisi ya kina Naya, kabla ya hapo ndio ofisi za
kina Jamal na wengineo wenye ngazi ya juu zinazo fanana kidogo kama Jamal.
Naya akawatizama watu wengine kisha akarudisha macho kwa Joshua
aliyekuwa amesimama mbele yake. “Asante kwa chakula, lakini...” Akaongea kwa
kunong’ona. Joshua akaanza kucheka. “Naya bwana! Sasa lakini nini?” Joshua
akamuuliza akiwa ametulia tu mikono mfukoni. Hata yeye alijua amefanya jambo la
ajabu na ambalo hakuna ambaye angetarajia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua anao watu wa kumuhudumia mpaka kumpelekea kinywaji ofisini
kwake! Ni mmoja wa wafanyakazi anayelipwa pesa nyingi sana hapo kwenye hiyo
kampuni. Habari zake Naya alizipata hata kabla hajamuona huyo Joshua mwenyewe,
na kuja kumtambua siku akiwakaribisha kwenye kitengo chao cha masoko na
kuwaambia matarajio yake kwao. Akiwaambia wao ni watu wa muhimu sana, na ndio
watabeba bidhaa yote ya kampuni kuitangaza. Akawapamba na kuwaambia bila wao
kufanya kazi yao vizuri, inaamaana wafanyakazi wote wa ile kampuni watakuwa
hawana kazi. Hawawezi kuzalisha kama hakuna kuuzwa. Na hapawezi kuuzwa bila wao
watu wa masoko, zaidi matangazo kutangaza hiyo bidhaa kwa ufanisi. Akaongea ya
kitaalamu ila kwa ufupi na kifanisi, wote walisimama na kupiga makofi. Ndipo
akaambiwa huyo ndio Joshua, kioo cha kampuni. Na mringaji haswa, hataki kuguswa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Lakini usingehangaika kuleta mpaka huku!” Naya akamjibu kwa
kunong’ona kama asisikike. “Nilikuwa na kikao huko nilikopata hiki chakula.
Ndicho walichotupa. Nikakipenda. Nikaagiza wakuwekee na wewe. Wakati naondoka, wakanikabidhi na mimi nikakileta hapa. Kwa hiyo sio usumbufu hata kidogo.” Naya
akajisikia vizuri akacheka taratibu. “Asante kwa chakula, na pole ya uandishi wa
research zako.” Joshua akacheka taratibu akimtizama, mikono bado mfukoni kama
kawaida yake. “Asante kwa maombi. Naona nimemaliza kwa ushindi.” “Hongera.”
Naya akampongeza. Wakawa kama hawajui wazungumze nini tena wakabaki
wanaangaliana.
Akamuona Naya anaandika. Joshua akaangalia. ‘Ulikula vizuri
na kushiba?’ Naya akamwangalia akamuona Joshua anasoma na kucheka. Akatingisha
kichwa kukubali. Naya akacheka nakubaki hajui aseme nini tena. Akamuona Jamal
anaondoka kwa kunyata kule nyuma ya Joshua. “Muda wa kutoka kula unakaribia.
Uende kula. Naamini utakipenda hicho chakula. Nyama yao haina tofauti na ile
Jamal anayoipenda kule tulipokula tulipokuwa safarini.” “Asante.” Naya
akashukuru akiwa haamini. Joshua akacheka kidogo na kuondoka. Naya alivuta
pumzi kwa nguvu na kujishika kama anayejipima mapigo ya moyo. Joshua
alipoondoka tu, kila mtu akatoa macho kwenye kompyuta na kumtizama. Naya
akacheka na kupandisha mabega juu kama anayewaambia na yeye hajui. Wote kimya.
Naya akarudisha macho kwenye kompyuta mikono ikitoa jasho.
Kabla hapajatulia vizuri, Naya akiwa amekodolea macho kwenye
kompyuta yake, Joshua akarudi tena. “Sikujua ungependa na kinywaji gani.
Ningekuuliza lakini sikuwa na jinsi ya kukufikia. Nimekuletea hii juisi ya
nanasi. Walishuka nayo kina Njama, wakidhani ni yangu. Wakanipelekea ofisini
wakati mimi nakuja hapa.” Naya alishasimama bila kujijua, aliposikia tu sauti
ya Joshua. Alipomaliza tu akamuonyeshea ishara asogee karibu. Joshua akiwa na
juisi mkononi akasogea. Naya akamuonyeshea ishara asogee karibu yake zaidi.
Akaweka ile juisi pale mezani akazunguka kabisa kule nyuma ya meza kwenye kiti
cha Naya akiwa haelewi Naya anataka nini.
Naya akamsogelea mpaka sikioni na kuweka kabisa kiganja cha mkono
kama mwingine asisikie. “Ni 07...” Akamtajia taratibu namba yake ya simu
sikioni akinong’ona. Akarudia mara ya pili kuhakikisha anaishika kichwani.
Kisha akarudi kumtizama usoni, akamuona anacheka. Kisha akaondoka bila hata
yakuaga, wengine wasielewe ni nini Naya amemwambia Joshua. Naya kuja kugutuka,
kila mtu amemtolea macho. Akacheka na kuchukua simu yake, chakula na ile juisi,
akatoka pale kwenda sehemu ya kula.
Wakati anakaa tu baada ya kuosha mikono, akasikia ujumbe umeingia.
Akajua ni Joshua tu. ‘Naamini nimepatia namba?’ Naya akacheka akajua atakuwa ni
Joshua tu. ‘Ni mimi Naya.’ Akarudisha huo ujumbe. ‘Asante kwa
namba. Ila sikusikia masharti yake.’ Naya akaelewa. ‘Wakati wowote.
Asante kwa chakula. Asante kujali. Nimefurahi.’ Akarudisha hayo majibu. ‘Karibu.
Naamini kitakuwa kizuri.’ ‘Kwa kuniletea tu mpaka kwangu! Sitajali ladha.
Nimefurahi sana. Tena sana.’ Joshua akacheka aliposoma ule ujumbe. Akajibu. ‘Kumbe na moyo
wa shukurani ndio mkubwa hivyo! Basi asante kushukuru.’ Naya
akagundua anapenda kumwambia hivyo. “Kwani anakuwa ananichunguza au!?”
Akajiuliza Naya na kuanza kula.
Alipomaliza kula akamtumia ujumbe mwingine wa kushukuru tena. ‘Asante sana.
Kweli chakula kilikuwa kizuri sana. Nimekifurahia. Barikiwa. Ulipotoa,
pakaongezwe.’ Kimya. Mpaka wanatoka ofisini, hapakuwa na jibu lolote lile na
aliona gari inayomuendesha yeye bado ipo. Inamaana alikuwepo kazini. Naya
akaumia na kujichukia kwa nini atume tena ujumbe kama ule wakati alisha shukuru!
“Huyu mtu yupo busy na kazi zake. Sio mtu wa kuchat.” Akatamani kama
afute lakini ilikuwa ujumbe wa kawaida, haufutiki. Akajichukia na kukosa raha
mpaka alipofika nyumbani baba yake alijua kuna kitu hakijakaa sawa. Lakini
akajua ni mambo tu ya Malon. Akamuacha. Alifanya shughuli zake zote za
nyumbani, akaoga na kurudi kukaa hapo sebuleni ambapo baba yake alikuwa amekaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Vipi mama? Umekuwa na siku nzuri huko kazini?” “Ilikuwa nzuri
lakini nahisi nimeharibu mimi mwenyewe kwa.....” Akasita. “Ilikuwa nzuri.”
“Hicho unachotaka usiniambie, ndicho kinachokunyima raha?” “Ndiyo.” “Ni nini?”
Naya akacheka kidogo kwa aibu. Baba yake akajua ni mambo ya wanaume tu.
“Unawakumbuka wale viongozi wangu walinipa lifti siku ile?” “Yupi
tunayemzungumzia sasa hivi? Joshua au Jamal?” Naya akacheka sana mpaka baba
yake akacheka. “Ni wote, sio mmoja.” Naya akazungusha. “Mmmh!” Baba yake akaguna
akimuonyesha kutomsadiki. Naya akazidi kucheka.
“Haya. Joshua amefanya nini tena?” “Baba!” Akajidai kushangaa. “Kwa
hiyo ni Jamal?” “Akuuu!” Naya akakataa kabisa mpaka akapandisha mabega juu. “Oooh!
Kwa hiyo ni yule mzee mwenzangu.” “Baba wewe!” “Basi turudi kwa Joshua.” Naya
akatingisha kichwa kukubali huku akicheka. Akamsimulia kuanzia walivyokuwa
Mbeya. Mazungumzo waliyokuwa nayo. Mpaka simu ya jumatatu iliyopita.
“Nikamuombea kwenye simu.” Baba yake akacheka. Kisha akamueleza na chakula cha
siku hiyo. “Sasa ulipoharibu ni wapi?” “Sasa kwa nini nimtumie ujumbe wa asante
tena na tena mpaka amenidharau!” “Kwa kuwa hajajibu?” “Angalau hata angenijibu
tu kusema ‘karibu’! Imeniuma! Nimejidharau.” Naya akajilalamisha kwa baba yake.
“Kwa wadhifa ulioniambia anao, hudhani kama ametingwa na majukumu
na ulisema hakuwepo ofisini juma zima na hata leo pia ulisema hakuwepo ofisni
alikuwa na kikao nje ya ofisi?” “Mimi sijui baba! Ila najilaumu.” “Unachotaka
kufanya hapo ni kuiba furaha yote uliyokuwa nayo.” “Eti eeh baba?” “Kabisa.
Wewe ulifurahia kuletewa chakula na mtu mkubwa kama huyo. Tena mpaka ofisini
kwako, mbele ya wenzio na yeye mwenyewe, sio kumtuma sekretari wake au wasaidizi
wake. Hilo likakufurahisha, sasa hivi unataka kufungua mlango wa huzuni isiyo
na sababu, bure!” “Basi natulia baba yangu. Kumbe heri nimekwambia!” “Wewe
unadhani mtu kama huyo kuleta chakula mpaka hapo ilikuwa bahati mbaya?” Naya
kimya akifikiria na cheko.
“Lazima anamaana kubwa sana. Mpe tu muda. Na usiwahi kumfananisha
na Malon.” “Umejuaje!?” Naya akashituka sana. “Kwani mimi sikujui wewe Naya?”
“Basi nilishasema ingekuwa Malon, angeshanijibu kwa haraka.” “Muone!” “Basi
naacha baba. Sitamfananisha na Malon.” “Na wala si yeye tu. Usiwahi
kumfananisha yeyote yule na Malon huyo wa kichwani kwako maana hata Malon Saduki
mwenyewe alishindwa kuwa kama huyo Malon unayemtaka wewe.” Naya akanyamaza
maana ulikuwa ukweli mtupu. Akagundua na baba yake ametulia kabisa akajua ndio
anampa muda wakutafakari na kuyaingiza kichwani. Akatulia. Baba yake akarudisha
macho kwenye luninga, kaka zake mezani wakisoma.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa amepotelea mawazoni pale kitini, akasikia simu yake inatoa
mlio. Akakwapua haraka, baba yake akamwangalia. Akamuona akisoma. ‘Naweza
kupiga?’ Akamwangalia baba yake, akakukuta akimtizama. “Ni Joshua.
Anauliza kama apige.” “Wewe unataka nini?” “Kumsikia.” Naya akajibu kwa upole.
“Basi msikilize. Na pengine utapata majibu ya wasiwasi wako.” Naya akamrudishia
majibu kumwambia ni sawa akimpigia. Aliposoma tu akampigia.
“Pole na majukumu.” “Kwanza samahani kuchelewa kurudisha majibu kwa
wakati. Muda ule nachati na wewe, tayari nilishakuwa nimeingia kwenye kikao.
Nilipokuacha ukila, nikarudisha simu ili kufanya kikao. Na unakumbuka sikuwepo
kazini karibia juma zima?” Joshua
akauliza kama anayejitetea. “Nakumbuka.” “Basi imekuwa siku ya vikao mpaka mida
hii. Nimekuta ujumbe wako kumbe ulituma mchana, nikaona kwa kukujibu bila kutoa
maelezo isingekuwa sawa. Kwa hiyo unisamehe. Ukubwa unakuja na majukumu.”
“Naelewa na samahani. Pengine sikutakiwa kuendeleza kuchati wakati nikijua
unakuwa na mambo mengi.” “Hata kidogo. Nimefurahi kusikia kutoka kwako. Na usisite
kuwasiliana na mimi. Muda na wakati wowote ule wewe unaruhusiwa kuwasiliana na
mimi. Ila ukiona kimya, ujue sijaona ujumbe. Maana hata nikiwa kwenye kikao,
wewe ujumbe wako au hata simu yako lazima nitajibu tu, hata kwa kifupi tu
kukwambia nipo kikaoni.” Naya akajisikia vizuri asiamini hiyo ruhusa ya mawasiliano na
Kumu moja kwa moja bila kupitia Jema wala Njama! Akabaki akitafakari.
“Umenielewa?” Baba yake akamuona ananyanyuka na kuondoka pale akijibu. “Nimeelewa.”
“Na umenisamehe?” Akauliza kwa kujishusha sana. Ikamgusa Naya. “Sio kukusamehe
Joshua! Hukukosa. Nimeelewa.” Akamsikia akicheka taratibu. “Sasa kama
hivyo ulivyokuwa kazini muda wote huo unafanyaje mambo ya chakula?” “Ninaye
mpishi. Nikiwa nataka kula, basi nampigia simu kumwambia kitu gani
anitayarishie. Lakini ikiwa kama nilivyokula sana mchana, basi usiku nakunywa
tu maziwa na ndizi ya kuiva, basi.” “Hivyo tu?!” “Inakuwa inatosha Naya. Si
unajua kazi yangu ni ya kukaa tu? Kwa hiyo mwili unakuwa hauhitaji chakula
kingi kwa siku.” Ndipo Naya akaelewa asili ya mwili wake vile ulivyo kumbe ni
nidhamu aliyonayo kwenye kuulisha.
“Ila nikiwa na njaa, huwa nakula. Sio mtu wakujivunga chakula.
Nahakikisha njaa haiwi sababu yakunifanya nishindwe kufikiria na kufanya
majukumu yangu, labda niwe nimefunga.” “Kumbe huwa unafunga?!” Naya
akashangaa kwa sauti, Joshua akacheka. “Nisingeweza kufanya ninayoyafanya bila
Mungu, Naya. Nikiwa kwenye maombi akili yangu inakuwa na uwezo mkubwa sana wa
kufikiria, na ndipo ninapozalisha mambo ambayo huwashangaza wengi. Lakini mimi
nilishaijua siri.” “Hongera Joshua! Sikuwa hata nikijua kama unamjua Mungu!” Joshua
akacheka sana.
“Basi umeshajua siri yangu hiyo. Kama Delila kwa Samson. Hiyo ndiyo
asili ya nguvu zangu na mengi unayoyasikia juu yangu.” “Hongera. Na ndio maana
kumbe upo salama!” Joshua akacheka sana. “Sikujua kama naonekana nipo salama!”
“Kwa kuonekana tu unaonekana upo salama sana. Hongera.” “Asante japo ni kweli,
ni kwa neema tu ya Mungu, Naya. Alinihurumia nikiwa nateseka sana. Naona
alipoona naweza kupotea, ndipo akanisogeza kwake.” “Najua sasa hivi umechoka na
pengine una mambo mengine ya kufanya kabla hujaitimisha siku. Ila wakati
mwingine ningependa kujua zaidi ilikuaje.” “Sawa. Naamini tutapata nafasi na
wewe uniambie kile ulichoniambia ukijua, na kukubali, utanijulisha.” Naya
akacheka. “Au bado?” “Tayari.” “Basi kumbe tunayo sababu ya kukutana ili tuzungumze
zaidi.” Naya akacheka taratibu.
“Ni sawa tukiweka mipango ya kukutana au utanijulisha utakapokuwa
tayari?” “Naona wewe ndio una majukumu mengi! Ila mimi nikimaliza kazi jumamosi
mchana, kama sitakwenda saluni, basi narudi nyumbani moja kwa moja. Mpaka
jumapili nakuwa na familia, jumatatu tena kazini.” “Mmmh! Mbali na kazi huna
kitu kingine unafanya?” “Tulikuwa tukifuga zamani, lakini baba aliuza mifugo
yote. Na mimi ndio nilikuwa nikifanya naye huko mabandani. Kwa hiyo sasa hivi
nipo tu.” “Kumbe uchapakazi huo ni wa mpaka nyumbani?” Naya
akacheka.
“Lakini namaanisha kitu chako wewe binafsi unachopenda kufanya mbali
na kazi. Au kazi tu ndiyo inakufurahisha?” “Napenda sana maswala ya ubunifu wa
mavazi.” “Waw!” Akashangaa. Naya akacheka. “You are full of suprises, Naya! Ehe?” Akataka kumsikia zaidi. “Nilifanya kipindi fulani, wakati nipo chuo, Malon alinisaidia
sana. Nikafanya mpaka maonyesho makubwa kabisa pale Plaza.” “Saafi sana. Sasa
kwa nini utupe ndoto zako?” Naya akajicheka
kidogo. “Nilianza vibaya. Nikajenga msingi
kwenye mchanga. Hakuna kilichosimama mpaka leo.”
Akaongea kinyonge.
“Pole sana.” “Lakini nafikiri ni kitu ambacho Mungu ameweka ndani
yangu. Basi najikuta tu wakati mwingine nikikaa mitindo mingi tu inanijia.” “Ungekuwa
ukiandika Naya!” “Naandika na kuchora. Sana. Nitakuja kukuonyesha siku moja.
Nimebuni mitindo mingi mno na michoro yake ipo. Sasa hivi nipo mchoro wa 189.”
“Naya!” “Kweli.” “Na yote umeshaweka kwenye michoro?” “Yote na mingine ipo na
historia zake. Kwa nini nilifikiria aina hiyo ya mchoro! Nimeandika chini ya
hiyo michoro kwa ufupi.” “Hiyo mimba lazima izaliwe mama. Nahisi imeshakomaa
vyakutosha.” Naya akacheka taratibu tu.
“Nikuache upumzike Joshua. Nikutakie usiku mwema.” “Hivi ulisema ni
sawa tukiweka mipango ya kuonana?” Akauliza na kuendelea. “Naamanisha nje
ya ofisini. Ukutane na Joshua sio kama mfanyakazi mwenzio.” “Sema bosi wangu.” Joshua
akacheka sana. “Ningependa.” “Basi nikuombe jumamosi tukutane baada ya kazi.
Nitakupeleka sehemu nzuri, tukae sisi wawili tu, tuzungumze.” “Sawa. Natakiwa
kuvaa nini?” “Chochote utakachopenda ila ujue ni sehemu ya nje tu. Kwa hiyo
casual tu, ila ujitendee haki. Ni sehemu ya hadhi.” “Watu wa aina yako?” Joshua
akacheka kwa sauti ya juu.
“Na zaidi. Ni kwenye beach club yetu. Na mimi ni mwanachama huko.
Tulipanunua na kupatengeneza. Kuna boti za kuendesha. Kuna sehemu wanacheza
golf, kwa wajuaji wa huo mchezo na mengineyo.” “Kumbe afadhali umeniambia! Sasa
wewe utavaa nini?” Naya akauliza kuepuka historia ya Joshi kujirudia tena safari
hii. Akavaa na kuonekana amepania kuliko kawaida ya eneo, shuguli na watakao wazunguka. “Nikiwa huko huwa nataka kupumzika na
suti pamoja na tai. Huwa navaa pensi, shati kata mikono, mara chache sana tisheti
na sendozi ili miguu kupumua.” “Ona ulivyonisaidia! Basi na mimi nitavaa
hivyohivyo.” “Basi kama ndio hivyo unataka kufanana na mimi, ukanunue kabisa
mavazi yatakayoendana.” Naya akashituka mpaka akashindwa kujibu.
“Eti mwanamitindo wangu? Ushakimbia?” “Nipo.” “Basi jumamosi naomba
univalishe wewe. Nitakutumia pesa pamoja na saizi zangu. Kanunue kitu utaona
utakipenda kutokana na nilivyokwambia. Ni sawa au majukumu mazito?” “Kwanza
ujue nimefurahi kuona umeniamini bila kuona.” Joshua akacheka taratibu kama
anayemtafakari Naya zaidi.
“Kweli nimefurahi.” Naya akasisitiza. “Sasa shauri yako ututoe vitu
vya ajabu wakati nimekwambia tunakwenda sehemu ya watu wa hadhi ya juu.” “Imani
yako itakuponya.” Joshua alicheka mpaka Naya akaanza kucheka na yeye. “Naya!” “Kweli.
Hapo umenitia morari. Hata naweza kukugharamia!” “Acha kuiba baraka zangu Naya!
Nimewahi mimi kulipia.” Naya akacheka tena. “Nakushukuru Joshua. Asante sana.”
“Karibu. Usiku mwema.” Wakaagana. Wakamsikia Naya anashangilia chumbani. Baba yake
akatingisha kichwa.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Acha kelele Naya bwana!” Bale akamkemea kidogo. Naya akatoka kwa haraka na kusimama mbele yao. “Nini Naya?
Toka bwana mbele ya tv.” “Mpaka mnisikilize kwanza, mpaka mwisho.” “Haya ongea
harakaharaka.” “Sasa sio nifike mwisho uanze maswali yako Bale. Kuwa makini.”
“Nitakuja kukubeba hapo nikutoe nje kabisa, mpaka nimalize kuangalia kipindi
changu ndio nikufungulie mlango wewe!” Baba yao akaanza kucheka. “Baba hawezi
kukubali. Eti baba Naya?” “Mimi naona uanze kutusimulia tu mama.” “Basi hivi
mnavyoniona, nimepata tenda yakumvalisha meneja masoko wa kampuni yangu.”
“Joshua huyo?” Bale akafanya mpaka baba yao acheke.
“Wewe umemjuaje Joshua!?” “Kwani una siri wewe?” “Mmbea tu Bale!
Ulikuwa ukitusikiliza mimi na baba!” “Bwana wewe endelea.” “Basi ameniambia
nimbunie kitu chochote nitakachopenda ambacho tutavaa siku ya jumamosi.” “Sasa
hapo umeanza kujichanganya. Nasikia na uwingi hapo!” Naya akatulia kidogo, wote
wakamtizama, Bale akaanza kumcheka. “Kione kilivyonywea! Ulisahau kuna kuomba
ruhusa eeh! Sasa anza mwanzo.” “Hayakuhusu. Nitazungumza na baba yangu
mwenyewe, huwa tunaelewana.” “Kwani mlipanga kwenda wapi?” “Na wewe Zayoni acha
umbea! Mimi sijapanga kwenda kokote mpaka niombe ruhusa kwa baba.” Bale na
Zayoni wakazidi kucheka.
“Inamaana hujamkubaliana bado?” Naya akapoa kidogo, Bale akazidi
kumcheka. “Hayakuhusu Bale?” “Bwana patamu hapo! Kama namuona meneja masoko
atakavyoachwa kwenye mataa siku ya jumamosi!” “Hata kama unamuandaa baba
akatae, basi nikwambie kabisa, hila zako zimeshindwa. Toka zako.” Baba yao
akabakia kimya wakibishana.
“Tutazungumza na baba yangu, najua tutaelewana tu. Si ndio baba
yangu?” Naya akaongea akibembeleza.
“Wala mazungumzo si marefu. Kuanzia sasa, kila anayekutaka, ataanzia
hapahapa ndani. Hapa nilipokaa mimi, hapa. Ndipo kitaeleweka. Si barabarani,
mtaani au ofisini tu. Wanataka mchezo wakuweka ahadi zao ambazo kwao zinakuwa hazina
maana lakini kwako zinajenga umaana wakuja kukuumiza! Hapana.” Wote
wakatulia. Naya akakosa raha. “Umesikia Naya?” “Sasa hata hanifahamu au
simfahamu halafu mara ya kwanza tu namwambia aje nyumbani jamani baba!” “Basi
asubiri akishakufahamu, ndipo mtoke.” “Sasa atanifahamu vipi bila kutoka? Labda
ninge...” Baba yake akasimama na kuondoka pale akaelekea chumbani kwake. Naya
akaanza kulia.
“Mimi naona sitakuja kuolewa jamani!” Akalalamika
Naya akilia. “Lakini baba yupo sahihi Naya.” “Sasa na wewe Bale unataka
nimwambie aje kwa wazazi wakati hata hanijui? Huoni kama ataona nataka anioe au
nalazimishia mahusiano fulani, nimfunge ndio maana nataka afike hapa kwa mzazi
moja kwa moja! Tumia akili Bale jamani, halafu nisaidie kuzungumza na baba!” “Hapana
Naya. Kama ni mtu mwenye nia nzuri, atakubali kuja. Ukimuona anakataa ujue
hakuwa na nia nzuri.” “Jamani Bale wewe!?” “Kweli Naya. Unataka historia ya
Malon ijirudie mara ngapi kwenye maisha yako ndipo ujifunze wewe?” Hapo Bale
akawa mkali kidogo. “Baba hataki wakuchezee kama mtoto usiye na maadili Naya!”
Kile kitu kikamuuma sana Naya. Akarudi chumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akalia sana akimlaumu Malon. Kwamba kama angetulia na kuwa na msimamo naye tokea mwanzo, akamuoa asingeonekana amekwenda kujirahisisha tu huko nje. Akalia hapo kwa muda taratibu kisha akamtumia ujumbe Joshua. ‘Uliniruhusu kukutumia ujumbe muda na wakati wowote. Samahani kama nakusumbua Joshua. Lakini nilitaka kukutaarifu ile safari haitawezekana tena.’ ‘Naweza kupiga?’ ‘Sasa hivi sipo kwenye hali nzuri. Hutaweza kunielewa nikizungumza.’ ‘Sio lazima ukazungumza. Ila nataka kuwepo tu na wewe, kama ni sawa.’ Ikamgusa sana Naya. ‘Asante.’ Akamtumia huo ujumbe, Joshua akampigia.
“Pole.” “Niliharibu sana nilipokuwa na Malon, Joshua.” “Pole sana. Tutazungumza vizuri kesho, nikipata muda mzuri wakati wa mchana. Unafikiri tunaweza kupata muda wa chakula pamoja? Ni sawa?” “Naogopa Joshua.” “Nani?” Joshua akauliza taratibu tu. Ikabidi Naya atulie na kufikiria hilo swali. Akakaa kabisa ili ajieleze. “Pale ofisini wewe ni mtu mkubwa sana, sidhani kama ni sawa kuonekana na mtu kama mimi. Naona kama itakuondolea sifa ukionekana na mimi.” “Kama ni kwa upande wangu usiwe na wasiwasi, pengine iwe kwako.” “Nakuhofia wewe. Nimekukuta na jina zuri, sitaki nikuharibie.” “Kwa nini ufikirie kuniharibia na si kuniongezea sifa?” Joshua akamuuliza vizuri tu. “Sijui Joshua.” “Nikwambie kitu Naya?” Naya akajifuta tena machozi na kujaribu kutulia.
“Unanisikiliza?” “Nakusikiliza.” “Mimi si
mkurupukaji. Kabla sijafanya jambo nakuwa nimeshaliangalia na kulipima kwa
macho yangu ya kibinadamu, ndipo namkabidhi Mungu. Nikishapata kibali kwenye
jambo, kwamba Mungu yupo na mimi katika hilo, hakuna umbali sitakwenda
kufanikisha hicho kitu. Hiyo ndio siri yangu ya pili ya mafanikio kwenye mambo
yangu. Ndio maana huwa naonekana kwenye mambo fulanifulani nipo kama sieleweki,
au nachelewa sana kwa vipimo vya kibinadamu, lakini nimejifunza kusubiri. Na
kadiri siku zinavyozidi kwenda ndipo tabia ya subira inavyozidi kujengeka.” Naya
akatulia kabisa akishangazwa na Joshua.
“Sina haraka kwenye mambo ninayotakiwa kusubiri, Naya. Lakini pia
sijui kusubiri kwenye jambo ambalo natakiwa kulifanyia kazi. Ndio maana kama
umesikia, Njama ni moja ya watu napenda kufanya nao kazi kwa kuwa kila kazi
ninayompa, anaifanya kwa muda niliompangia mimi sio anavyotaka yeye. Ni nini
nataka kukwambia?” Joshua akaendelea. “Sasa hivi sizungumzi na wewe hapa kwa
bahati mbaya. Ni kwa kuwa nimeamua, na nipo tayari kuzungumza na wewe. Haya
mazungumzo, au hiyo kutoka na wewe ingefanyika muda mrefu tu nilipotaka kufanya
hivyo, lakini nilionywa nafsini kwangu kuwa haukuwa wakati wa Mungu.” “Kweli Joshua!?” Ilimshangaza
na kumshitua kidogo Naya.
“Ooh kabisa Naya. Nafikiri mpaka sasa utakuwa umesikia habari zangu.
Kama nakosea pale kazini, nikidogo sana. Najulikana kwa kupatia. Na siri nimekwambia.
Sijisifii, lakini ninao muda mwingi sana magotini mbele za Mungu. Katika ratiba
zangu ngumu za siku, pia nahakikisha natulia ili kumsikia Mungu wangu.” Joshua
akaendelea.
“Naya, huyu Mungu ninayekwambia inanilazimu kumsikiliza, ni kwa kuwa
nilifika mahali nilibakiwa na Yeye tu. Tena nikiwa simfahamu hata kidogo.
Lakini nilikuwa peke yangu kwenye huu ulimwengu, ila Mungu. Nitakuja kukwambia
habari zake siku moja, lakini amenifunza kumtegemea kwa asilimia 100. Sina
jinsi kwa kuwa mimi sikubahatika kama wengi wenu. Nimelelewa na Mungu kama baba
wa hapa duniani. Sina ujanja. Mbali na Mungu, mimi si kitu Naya. Chochote
unachokiona kwangu, jua ni kwa kuwa utukufu wa Mungu unanifunika. Na hiyo
haimaanishi kukulazimisha kwa lolote, hata kidogo. Nilikwambia mimi nina
subira?” “Umeniambia Joshua.” “Basi huwa najua kusubiri. Kama ukiona haupo
tayari kuonekana na mimi popote, usiharakishe.” “Basi naomba tuzungumze kesho.” Naya akawa
ameshatulia kwa aliyoyasikia kutoka kwa Joshua. Akatamani kumsikia zaidi.
“Lakini si ahadi. Sitaki nikuumize, Naya. Ile ofisi inajua kuchukua muda wake wa kazi na wangu pia. Nikiingia pale, kichwa changu kinahitajika kwa asilimia zote. Kwa hiyo naweza kushindwa kukuona muda uliopanga wewe kwenda kula.” “Naelewa Joshua. Sio deni. Ukishindwa basi, tutazungumza hata kwa simu ukitoka kazini.” “Nashukuru kunielewa. Ila nikipata mwanya, nitakuja kukuona hata kwa muda mfupi tu.” “Kweli Joshua!?” Akamsikia akicheka. “Usiku mwema Naya. Nimefurahi umetulia.” “Nashukuru tumezungumza. Usiku mwema na wewe.” Wakakata simu lakini Naya akabaki amekaa na simu mkononi.
Jumanne.
A |
subuhi kabla
ya kutoka kwenda kazini, Naya akiwa ameshajiandaa kabisa akaenda kumgongea baba
yake chumbani. Alikuwa akitoka hapo nyumbani kwao kabla ya saa 11 asubuhi.
“Ingia.” Akaingia. “Unisamehe baba. Ila nakuahidi sitarudia tena kosa.
Nitafuata kama ulivyonishauri. Akikataa kuja hapa kwako, basi.” “Uwe na siku
njema. Ukipata nafasi unipigie.” “Nitafanya hivyo. Acha niwahi.” Akatoka kwa
haraka ili kuwahi foleni.
Na kweli aliwahi ofisini akiwa amependeza tu, kawaida na sare yake
ya kampuni. Alikaa hapo ofisini kama nusu saa tu, Joshua naye akaingia hapo.
“Joshua!” Akawa kama amefurahi kumuona. Akavuta kiti na kukaa. “Mbona umewahi
hivyo!?” “Nilikuwa nikikuwahi wewe, uniambie nini kilikuumiza jana usiku. Nataka kujua kabla sijaanza kazi, nikashindwa kufikiria vizuri kwa kutingwa na majukumu
na kushindwa kujua kinachokusibu kama siku ile kwenye gari tukitokea Mbeya,
tukiwa Morogoro.” Naya akakumbuka alimuona na macho mekundu akampa maji ya
kunywa ili atulie. Hakujua kama alijali kiasi cha kukumbuka mpaka siku hiyo.
“Niambie tu.” “Unaweza usinielewe Joshua.” “Ambapo sitaelewa
nakuahidi nitakuuliza.” Naya akafikiria na kuamua kumwambia. “Nimeharibu pale
nyumbani. Nimemuumiza sana baba. Nilianza mahusiano na Malon nikiwa kidato cha
nne. Kidato cha tano na sita niliwadanganya nyumbani nilikuwa nikiishi hosteli,
kumbe nilikuwa nikiishi kwa Malon.” “Kwamba mliishi unyumba kabisa?!” Joshua
akauliza kwa mshangao kidogo. “Ndiyo. Niliishi naye nyumba moja, nyumbani kwake
Kunduchi na Morogoro pia, ila nyumbani wakijua nipo hosteli. Hawakujua mpaka
nilipomaliza chuo, Malon akiwa amefungwa jela, nahangaika kumtoa jela, ndizo
hizo siri zikafichuka. Imemuuma sana baba.” Joshua akatulia kidogo kama ambaye
anafikiria. Naya naye akanyamaza akijua hapo na yeye atachoka.
“Lakini bado hujaniambia nini kilikuliza jana usiku.” “Nilimuaga
baba nikimwambia nitatoka na wewe siku ya jumamosi. Lakini amekataa Joshua.
Amesema hakuna mwanaume atanichukulia tena barabarani au popote pale isipokuwa
pale kwake.” “Kwamba lazima amfahamu mtu anayetoka na wewe?” “Lakini
nimemwambia basi, Joshua. Huna sababu yakufanya hivyo kabisa. Kwanza
nimemwambia hata Bale, itakuwa si sawa kwako kukupeleka pale nyumbani ukiwa hata
hunifahamu! Ndio maana nilikwambia basi.” “Ukiwa unamaanisha nini?” “Sijui
Joshua! Naomba tumuachie tu Mungu. Sina jinsi. Navuna nilichopanda.” Joshua
akatulia tena kidogo.
“Malon kwa sasa yupo wapi?” “Hata sifahamu Joshua.”
“Hamjawasiliana naye tena tokea Mbeya?” “Malon si mtu wa kumfukuza kirahisi
akaelewa. Alikuja kurudi tena nyumbani. Amepazoea pale nyumbani. Wadogo
zangu wanampenda sana Malo, kwa kuwa amekuwa mtu wa kunifuata nyumbani. Na yeye
ndiye aliyeweka huo utaratibu. Na mabaya yake yote aliyokuwa nayo, alihakikisha
anakuja kunichukua nyumbani na kunirudisha yeye mwenyewe.” “Kwa hiyo tokea
mwanzo ndivyo alivyokuwa akifanya?” “Kabisa. Lakini kwa kuongopa kama
ananirudisha hostel lakini ni kwake. Ila hapakuwa na mazingira magumu ya
kudanganya kwa vile baba alivyokuwa akiniamini. Kwa hiyo alipokuwa akija
kunichukua, alijulikana alikuwa akinirudisha hosteli tu.” Akamuona Joshua
ametulia.
“Najua nimeharibu sana. Na mbaya zaidi mimi ni mtoto niliyekuzwa
karibu sana na baba, na pia nimekulia kanisani. Baba ameumia sana. Lakini
anyways, nimefanya kosa, inabidi kujenga tena imani.” “Nikupe pole?” “Hata
sijui Joshua! Lakini hapo ndipo nilipo kwa sasa.” “Uliniambia umepata jibu juu
ya Malon.” Naya akatulia kidogo kama anayefikiria kisha akaona amwambie tu.
“Nikwambie ukweli Joshua?” “Niambie tu.” “Kwa asilimia kubwa sana, nilijua
Malon ndiye angekuwa mume wangu. Nikaishi kwa kulazimishia mno ili anichague
mimi katika wengi ili aje anioe, lakini imeshindikana. Jumamosi iliyopita
alikuja nyumbani kuomba radhi kwa
familia, akiwa tayari kwa ndoa, tena na pete mkononi. Kwa hakika ilikuwa pete
nzuri mno. Malon ni mtoaji kupita nitakavyokwambia. Kwa hiyo hata kwenye ile
pete, hakujipunja. Aliitendea haki. Niliitazama ile pete, nikashindwa kuiweka
kidoleni.” “Pengine ni hasira tu.” Naya akatulia kama anayefikiria kidogo.
“Hapana. Sitarudi kwa Malon.” Akajibu hivyo akiwa ameinama kisha
akamwangalia Joshua. Akakuta akimtizama. “Hata yeye nilimwambia. Siye mwanaume
atakayenitoa kwa baba yangu. Sitajali hata kama sitaolewa tena maishani, ila
hatakuwa Malon. Nimejua kwa hakika, hakukusudiwa kuwa mume wangu. Ameondoka. Na mimi huwa namjua Malon, hatageuka tena nyuma, pengine mpaka nije
kumtafuta tena.” “Unajuaje?” “Kwa kuwa ndivyo mahusiano yetu yalivyokuwa. Ukitukuta
kwenye mahusino naye, ujue ni kwa kuwa mimi nimemtafuta. Hata kama amekosa kwa
kiasi gani. Hatarudi mpaka nimtafute. Na akirudi, unaweza ukasahau shida zote.
Atajaa kila mahali, na mipango mizuri ya kueleweka, kisha anapotea tena. Kwa
sababu yeyote ile. Hata akiwa amekosa yeye, basi anaweza akapotea, mpaka
nikamtafute nimtangazie msamaha. Basi hata kama alikuwa kwenye mahusiano ya
wizi au na mtu mwingine kama vile Rita, hana shida ya kumuacha na kurudiana na
mimi. Sasa huo mchezo naona umeshanichosha. Sitarudia tena huko.” Akaanza
kuingia mfanyakazi wakwanza.
Alishituka sana alipomkuta Joshua pale. Akamsalimia karibu apige
goti kisha akatoka haraka. Naya akamwangalia na kucheka. “Pole Joshua. Pengine
unatamani kama ungeyajua haya tokea mwanzo.” Joshua akacheka taratibu
akisimama. “Namshangaa sana Mungu ndio maana unaniona nimekuwa kimya. Namshangaa
yeye Mungu wala si wewe! Mungu wangu huwa hakawii wala huwa hawahi. Ndio maana
nakwambia inabidi niwe tu mpole, nimsikilize.” Naya akawa hajamuelewa. “Unakumbuka
nilikwambia nilionywa na Mungu kukuacha wakati ule? Sikuwa naelewa kwa wakati
ule maana hapa ofisini ulionekana huna mtu yeyote yule na wala hukuonekana upo
na hehaheka ya wanaume. Ilikuwa nusura kumpuuza Roho wa Mungu na kukufuata
wakati ule, ila mwishoe nikakubali kutiii tu, huku nikimlalamikia Mungu kunichelewesha.
Kumbe bado alikuwa kazini.” Akacheka na kutoka. Naya asimuelewe.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya mchana, lisaa kabla muda wa chakula simu ikaingia
akiuliziwa Naya. Naya akamuomba Kibasa ambaye amepokea hiyo simu, amsogezee simu
kutoka hapo mezani kwake mpaka hapo kwenye meza yake yeye Naya. Alichofanya
Kibasa ni kuiweka hiyo simu chini bila kumkabidhi Naya kama anayemwambia
aifuate mwenyewe. Naya hakujali, akasimama kuifuata kwani alijua Kibasa ameanza
kumchukia sababu ya Jamal kuanza kumuachia yeye maagizo sio yeye tena Kibasa,
kama alivyojulikana ni msaidizi wake. Alishaiona hiyo chuki, lakini Naya
hakujali akaendelea kuchapa kazi.
Akajivutia hiyo simu mpaka mezani kwake. Uzuri hiyo simu ilikuwa
na waya mrefu inafikia kila meza hapo ofisini kwao, ila tu ilikuwa ikikaa
mezani kwa Kibasa kama kiongozi wa hiyo ofisi. Akaipokea. “Mimi Naya.” Naya akasikia
sauti ya kike ikijitambulisha kwa jina la Fina, akitaka kujua atataka kula nini
mchana huo. Naya alimjua vizuri tu Fina japo naye ni walewale kama kina Jema,
maringo. Ni sekretari wa Joshua. Naya akashindwa hata kujibu. “Joshua ndio
amenituma. Nafikiri ni kwa kuwa hataweza kutoka tena. Amebanwa. Anataka chakula
kiletwe hapa ili ale kwa muda mfupi atakao pata.” Naya akatumia akili ya
haraka. “Yeye ameagiza nini?” “Kwani wewe unataka nini?” Akamuuliza
Naya kwa ukali kidogo. “Nitakula atakachokula yeye.” Naye Naya akamjibu hivyo. “Sasa hapo itakuwa
ngumu maana na yeye ameniambia atakula utakachokula wewe!” “Kama ndio hivyo
tafadhali naomba nipigie kama baada ya dakika 6 hivi.” Naya
akakata.
Akamtumia ujumbe Joshua. ‘Upo busy sana?’ Joshua
akampigia akisikika na haraka. “Usiogope. Waagize chochote tu wataleta. Mimi si
mchaguzi. Ila isiwe samaki wala ugali. Sitakuwa na muda mrefu wa kula.
Tafadhali isiwe pia kitu cha michuzi. Asante.” “Kazi njema.” “Nitakuona baada
ya muda mfupi.” Wakaagana na kukata, Naya asiamini anachokifanya Joshua. Akafikiria,
mpaka akapata jibu. Alipopiga simu tena sekretari wa Joshua, Naya akamtaji vitu
vya kuleta. “Na matunda tafadhali.” Akaongeza Naya kwa heshima ila akijiamini.
Alishaishi na Malon, wengine wakimtumikia. Hakuwa mgeni wa kuagiza. “Sawa.” Fina akaitika hivyo na
kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya lisaa tena simu nyingine ikapigwa akiuliziwa Naya.
“Tutakoma mwaka huu!” Aliyepokea akalalamika huku akimpelekea hiyo simu Naya,
maana na yeye aliichukua ili kutumia kupiga simu zake za nje ya ofisi maana
ilikuwa bure, hakuna kulipia muda wa maongezi. Naya akapokea bila kumjibu. “Unataka
chakula kipelekwe wapi?” “Kwenye gari tafadhali.” Naya alishalifikiria hilo,
akajua hawatakula kwa utulivu pale sehemu ya wafanyakazi wote wanapopatumia kula
chakula, maana ulikuwa ni muda wa watu wote kula. Akajua kila mtu atakuwa
akiwatizama wao na kuwasikiliza. “Kwamba ndio mkale chakula kwenye gari!?” Akauliza
kama anamshangaa kwa kumdharau. “Ndiyo tafadhali.” Naya akajibu
hivyo tu na kukata simu. Baada ya dakika 6 akapata ujumbe kutoka kwa Joshua. ‘Nipo garini
tayari. Nina dakika 15 tu.’ Naya akatoka bila yakuchelewa.
Akakuta gari ya kampuni anayoendeshewa Joshua inawaka, akajua yupo
ndani ya gari hiyo. Akachungulia viti vya mbele akamuona amekaa kiti cha nyuma.
Akapanda na yeye. “Samahani nilijua kwengine tusingepata utulivu.” “Nimeelewa.
Wewe kweli ni mbunifu!” Naya akacheka akijua ameridhika. “Nilishanawa mikono.
Nasubiria tu chakula changu. Nimekuta hapo ila sikujua umeniagizia nini.” Naya
akavuta ule mfuko uliokuwa na vyakula. Vile tu vilivyofungwa, akajua vimenunuliwa
sehemu nzuri. “Si umesema utanivumilia tu?” “Kwa nini?” Naya akamuuliza
akimtolea chakula. “Najua pengine hivi sivyo ungependa kula.” Naya akacheka wakati
akitoa chakula. “Niliagiza na matunda. Unaanza matunda kwanza au chakula?”
“Matunda kwanza, tafadhali.” Naya akamkabidhi. “Asante sana.” Akayapokea kwa
heshima zote utafikiri Naya ndiye amemnunulia.
“Ndio unakuwa na muda mfupi wa kula hivi kila siku?” “Na wakati
mwingine muda wa chakula unafika na kupita hata sijui! Leo nimelazimishia hizi
dakika 20, kwa ajili yako?” “Nikupe pole?” Joshua akacheka. “Ongeza na
hongera.” “Pole na hongera.” “Asante.” Akala yale matunda mpaka akamaliza
wakiwa kimya tu.
“Naomba chakula tafadhali.” Naya akamtolea na kumkabidhi. “Naona
mimi matunda nitakula baadaye ofisini. “Na ukitaka kitu chochote, mpigie simu
Jema, atajua jinsi ya kukipata.” “Joshua jamani!” Akaanza kucheka. “Sawa. Basi
uwe unaniambia mimi.” “Hapo sawa. Utanichonganisha mwenzio.” Joshua akafikiria
kidogo, akawa kama ameelewa. “Okay. Uwe unaniambia mimi, mimi nitajua nani wakukileta haraka.”
“Japokuwa sidhani kama nitafanya hivyo, lakini nashukuru.” Joshua akamwangalia
na kucheka kama anayefikiria.
“Unajua kwa nini nimelazimishia hizi dakika 20 za kula pamoja?
Maana usizoee. Huwa hazipatikaniki kirahisi hivi.” Naya akacheka sana. “Leo ni
bahati?” “Sana. Tena ni kwa sababu nilitaka kukwambia sina shida kuja
kukuchukua nyumbani. Lakini kama wewe utaniruhusu. Hata mimi naona itakuwa
jambo la heshima, nisionekane na mimi ni muhuni tu. Sina haraka. Nitasubiri
mpaka utakapokuwa tayari nije, nitakuja kukuchukua, ndipo tukafanye safari
yetu.” “Kwa hiyo hata jumamosi hii unaweza kuja!?” “Oooh yeah! Why not? Sina
kinachonizuia.” “Nashukuru Joshua, na samahani kwa usumbufu.” “Sio usumbufu
Naya. Ni utaratibu mzuri sana. Hata mimi binti yangu nitataka iwe hivyohivyo,
sio kuishia vichochoroni tu. Sio heshima kwako hata na kwa baba pia.” Naya
akapoa.
“Sasa umeshajua tutatoka vipi?”
Akabadilisha mazungumzo nakumfanya Naya acheke kidogo kama anayefikira.
“Nitakuletea hapa jumamosi asubuhi.” “Sio ijumaa ili ikafuliwe kabisa na
kupigwa pasi?” Naya akakumbuka anazungumza na Joshua wa viwango vingine kabisa. “Basi
nitafanya hivyo.” “Sikuharakishi mbunifu wangu. Chukua muda wote unaotaka,
ilimradi tu unitoe vizuri.” Naya akacheka sana. “Joshua!” “Maisha yenyewe ndio
hayahaya! Sina starehe nyingine isipokuwa kula vizuri, kuvaa vizuri na kulala
sehemu nzuri. Basi.” “Wazazi wako wapi?” Joshua akacheka kidogo.
“Kumbe na wewe unataka kunifahamu?” “Nimekuwa na shauku ya
kukufahamu zaidi.” “Jiandae kupata historia nzima ya Joshua siku ya jumamosi.
Ila ujue mimi ni yatima nisie na mama wala baba. Na wewe ndiye utakuwa ndugu
yangu wa kwanza baada ya miaka mingi sana ya upweke.” Japokuwa Naya
alimshangaa, lakini akamuhurumia. “Pole Joshua.” “Asante. Na...” Akasikia
dirisha linagongwa. Joshua akashusha kioo. “Kikao kimeanza, unasubiriwa wewe.”
“Nakuja ndani ya dakika 5.” Jema akaondoka. “Ndio upo busy hivyo!? Mbona sasa
hata dakika 15 hazijaisha?” Naya akalalamika. “Zimeisha Naya. Angalia saa.
Pole. Jumamosi tutapata muda mrefu wakutosha. Acha niwahi, nisiwaweke. Asante sana
kwa chakula.” Akarudisha chakula bila kumaliza, na kujifuta mkono. “Acha tu
vitu vyote humuhumu, watasafisha.” “Siwezi Joshua! Wewe wahi mimi nitasafisha.”
“Hakuna mtu atajali bwana.” “Mimi nitajali.” “Basi sawa. Asante sana.” Akasuuza
mdomo kwa maji aliyokuwa ameletewa akatoka kwa haraka. Akamuacha Naya akila kwa
furaha yote.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Uzuri hakuwa ametengeneza urafiki ule wa karibu na wafanyakazi
wenzake, aliona ni mabinti wenye mambo mengi. Naya kama kawaida yake kama
alivyokuwa shuleni akajitenga nao. Kuangalia mambo yaliyowakutanisha pamoja
pale ofisini, kazi, basi. Alifanya kazi hapo bila kulalamika na hata kama mtu
akimuomba ammalizie kazi zake, hakuwa na shida kwa kuwa alikuwa na muda mwingi
mezani kwake. Hana stori nyingi za mtaani na yeyote isipokuwa kazi. Na wenyewe
wakampuuza tu. Kwanza walimuona anajizeesha bila sababu. Hata wakitoka jioni
baada ya kazi wakikubaliana wakutane sehemu, Naya alikuwa akikataa. Halafu wakaanza
kumsema anakimbelembele na kazi, kama vile ni ya baba yake! Anajifanya mchapakazi!
Anajipendekeza ili Jamal amuone! Na mengine mengi. Wakaachana naye.
Sasa Joshua Kumu kuja kutokezea mezani kwake, kila mtu akataka
kujua cha ajabu kwa huyo Naya. Kama kawaida ya sehemu nyingi, haikuchukua hata
siku nzima, siku ileile ya jumatatu alipomletea Naya chakula na juisi mezani
kwake, habari zilienea kila idara, kuwa hatimae Joshua naye amechukua kuku
mgeni. Sasa ikawa ni Joshua asiyeingilika, na Naya asiyezungumza mambo yake
binafsi. Kwanza wakagundua ni kama hakuna hata anayemjua vizuri huyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akarudi mezani kwake ujumbe ukaingia. ‘Samahani leo wakati wa chakula cha mchana nimekuwa na muda mfupi sana na wewe, nikasahau
kushukuru kwa chakula. Kwanza nimependa chakula ulichoniagizia. Asante sana.’ Naya
akafurahi kusikia hivyo, maana alishapata wasiwasi na chakula alichomwagizia.
Alikula tu bila kusema chochote na pia hakukimaliza. ‘Nimefurahi
kama umependa. Kazi njema.’ Baada ya dakika kadhaa, akajibu. ‘Asante. Nipo
kikaoni bado.’ Naya hakutaka hata kujibu tena. Akashangaa kwa nini ametuma ujumbe
akiwa bado kwenye kikao. Bado akawa hajamuelewa Joshua. Akashangaa pesa
zinaanza kuingia. “Kwani huyu Joshua anavaa nguo za kiasi gani!?” Akajiuliza Naya akikodolea macho kile kiasi
cha pesa kilichoingia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mida ya jioni wakati anatoka akampigia simu baba yake kuwa
atapitia madukani. Naya akaanza kuzunguka kuanzia maduka yale ya kiume aliyojua
wanauza vitu vya thamani vyenye ubora mkubwa akiwa hana shida na bei kwani pesa
ilikuwepo. Akazunguka mpaka akapata vitu anavyopenda. Kuanzia nguo zao na viatu
pia. Tayari alishapanga wavae Linen nyeupe ila aweke rangi ya bluu kama bahari
kwenye hayo mavazi yao. Akaenda kununua na kitambaa kizuri sana cha rangi hiyo
yakuchanganyia, ikafanana na kiblauzi kidogo atakachovaa yeye ndani kufunika
tumbo kwani alitaka chati lake yeye liwe dogo tu, fupi la kufika na kufunga
chini ya matiti. Kwa hiyo chini ndio hicho kiji kiblauzi cha ndani, kata mikono
cha hiyo rangi ya maji ya bahari kionekane nje kikining’inia kwenye pensi
atakayovaa.
Alifanya manunuzi yote na baadhi ya urembo wakuongezea kwenye hizo
nguo na viatu, ndipo akarudi nyumbani. Akatoa cherehani aliyokuwa amembakishia
mama yake baada ya kuuza vitu vyote kwenye kiwanda chake na Malon. Hiyo mashine
ya kushonea, mama yake aliipenda sana na kumuomba rasmi amwachie. Na ndipo hapo
hata Naya akajifunza kushona. Ilikuwa na uwezo wa kutengeneza vitu vingi sana
mpaka kudarizi. Akaenda kuitoa stoo na kuhamishia chumbani kwake, baba yake
akimwangalia tu.
Alipoweka kila kitu sawa hapo chumbani kwake ndipo akarudi kwa
baba yake. “Nilimwambia Joshua kuwa kama anataka kunitoa, lazima aje hapa
kwako. Nikafikiri atakataa, lakini amekubali. Amesema hata yeye angependa iwe
hivyohivyo kwa binti zake. Kwa hiyo atakuja.” “Sawa.” Naya akatulia, baba yake
akajua kuna anachotaka kusema. Na yeye akamuacha tu. “Unisamehe baba.
Nilikudanganya wakati ule.” “Tena nikiwa nimekuamini
sana, Naya!” Naya akaanza kulia. “Nilikosa
baba yangu. Lakini sasa hivi nimejifunza kutokana na makosa, na sitarudia
tena.” “Nakuombea usirudie. Jiwekee thamani
wewe mwenyewe Naya, mama. Lasivyo wengine watakudharau sana.” Naya akatingisha
kichwa kukubali.
Akarudi ndani chumbani kwake, na kutoka na mashati mawili.
“Nilikununulia zawadi.” Baba yake akacheka. “Mbona yanaonekana ya pesa nyingi
sana! Zimebaki za chakula kweli?” “Nataka upendeze baba yangu. Leo nimeingia
kwenye maduka ya wanaume wenye nazo hapa mjini. Nikaona na wewe uonje jinsi
matajiri wanavyovaa baba yangu.” Baba yake akacheka akiyaangalia. “Tena nitavaa
mojawapo siku ya jumapili.” “Na mimi je?”Akadakia Zayon. “Leo ilikuwa baba tu.
Wewe siku nyingine.” Naya akajua baba yake ameyafurahia. “Basi nitakuwa
chumbani kwangu, kuna kitu nafanya.” Akarudi chumbani kwake.
Wakati anachora kitu anachotaka kitokee kabla hajaanza kushona hizo
nguo Joshua akampigia. “Kwani ulitaka nikubadilishie kabati zima?” Joshua
akaelewa na kuanza kucheka. “Kwani chenchi imekuwa kubwa?” “Sana!” “Nataka
tupendeze.” “Unanitisha bwana!” “Jiamini Naya. Niambie utatutoa vizuri. Acha
kujitilia mashaka.” “Sawa. Basi jiandae kupendeza.” “Hayo ndio maneno.” “Lakini
ni kweli pesa ni nyingi sana!” “Zikusaidie kwenye mambo yako pia mengine.”
“Nakushukuru sana. Asante.” “Karibu na asante kushukuru.” “Ndio unatoka
kazini?” “Ndio narudishwa nyumbani nikapumzike.” “Siku yako iliendaje? Vikao?”
“Nashukuru Mungu aliniwezesha. Kila kitu kilienda vizuri.” Wakaanza
kuzungumza mpaka Joshua akafikishwa nyumbani kwake. Akamsikia akimshukuru
dereva.
“Naya?” “Nipo.”
“Utakuwa na mimi mpaka saa ngapi?” Naya akashindwa kumuelewa. “Ulitakaje,
Joshua?” “Tukae wote tu kidogo.” Naya akamuhurumia na kuhisi pengine
ni mpweke. “Nibakie kwenye simu?” “Kama hutajali.” “I would love that.” Akamsikia Joshua akicheka
taratibu kwa kuridhika pale alipomwambia angependa kuwa naye kwa simu. “Nikuulize kitu Joshua?” “Karibu.” “Unaishi na nani?” “Peke
yangu, lakini kulikuwa na vijana wawili nilikuwa nikiishi nao hapa. Nilikuwa
nikiwasomesha. Mmoja alimaliza tu na kuoa. Alikutana na mpenzi wake chuoni.
Mwaka jana tu, wamehamia Dodoma. Au wanaishi Dodoma. Mwingine alitaka shahada
yake akasomee nje ya nchi.” Akamsikia
akicheka.
“Nini?” “Sidhani kama atarudi huku yule! Naona huko alipo amenogewa.
Ila akinikumbuka, huwa tunawasiliana.” “Oooh!” “Ndio hivyo. Kabla sijarudi
kufanya kazi kidogo, nataka nikae kidogo hapa na wewe. Umesema hutajali, si
ndiyo?” “Hata kidogo.” “Wewe unafanya nini sasa hivi?” “Mbali na kuzungumza na
wewe, narekebisha michoro yangu.” “Unajua kuna mambo nimehisi tunafanana!” Naya
akacheka akijidharau. Ikabidi kuuliza tu. “Kama nini?” “Kabla sijatoa wazo langu,
huwa lazima nilichore kwanza na kujaribu kutizama kwa macho ya watu wengine.
Nikiridhika, ndipo nalitendea kazi. Hapa ninapokwambia, nina mimba hiyo,
ikijazaliwa, macho na masikio ya watu lazima yawashe.” Naya
akacheka sana kwa furaha.
“Hongera sana Joshua. Am so proud of you.” “Kweli unajivunia mimi, Naya!?”
“Hakika. Kwani wewe hujui kama ni kioo kwenye taaluma ya masoko?” Joshua
akacheka sana. “Kweli hujui?” “Sasa nitajuaje?” “Joshua wewe!? Kwamba hujui kama
wewe ni kipimo cha akili ya mafanikio kwenye kitengo cha masoko? Sifa zako mimi
nilizisikia hata kabla sijakuona! Tulipofika tu pale, tukaambiwa tutakuwa na
siku maalumu ya kukaribishwa na kichwa chenyewe cha masoko, kilicholeta
mabadiliko makubwa sana kwenye ile kampuni. Tukaambiwa ni bwana mdogo tu,
lakini akifungua mdomo, mpaka madume yakizungu yanasikiliza na kuandika.” Joshua alicheka,
akacheka sana.
“Kweli Joshua! Sisi ndivyo tulivyoambiwa hivyo.” “Jamal huyo?”
“Nakwambia kila mtu aliyetukaribisha pale. Tena tulipokwenda kule uzalishaji
tukaulizwa kama tushakutanishwa na mungu wa Coca?” “Haiwezekani Naya!?” “Siwezi
kukudanganya Joshua. Sisi tuliambiwa eti wewe ukiamua mwezi huo bidhaa fulani
iuzwe mkoa fulani kwa asilimia fulani zaidi, eti hujawahi kukosea. Ndio maana
eti wamekupa hilo jina. Na hakuna anayeweza kuzungumza, unapoongea wewe. Jamal
alisema eti ukiongea wewe, mpaka watu wengine wanarikodi!” Joshua
alizidi kucheka.
“Hupingi kwa kuwa unajua ni kweli.” “Nilikwambia ni
Mungu, Naya. Hakika si mimi. Hata mimi huwa namshangaa huyu Mungu jinsi
anavyoweza kutenda kwa ajabu Naya! Hakika si mimi. Siwezi hata kujisifu. Wakati
mwingine naweza nikapata wazo, la nini chakufanya na ile idara ya masoko, mpaka
mimi mwenyewe naogopa! Na kwa kule nilikotoka mimi, najua ni Mungu tu, wala si
mimi.” Naya akamshangaa sana.
“Unamoyo wa unyenyekevu!” “Ni kwambie ukweli Naya, ni vile bado hujanifahamu
bado. Ila ungeleewa ni nini nakwambia. Katika watu waliostahilishwa hapa
duniani, na mimi ni mmoja wao. Joshua kama Joshua, hakika si kitu nje ya Mungu
wangu.” Akamsikia akicheka kwa kuguna. Kisha akaendelea.
“Naya, kazi ya msalaba ni halisi. Halisi kwa asilimia 100, mimi ni
shahidi wa haya. Mimi ni mfano ulio hai. Na Mungu sio wa kwenye vitabu tu.
Akiamua kutembea, anatembea mpaka utajua ametembea. Akiamua kutenda, anatenda
hajui kubakisha. Lile andiko la 1 Wakorintho2:9 linalosema {Hakuna jicho
limepata kuona, wala sikio limepata kusikia, wala hayakuingia moyoni wowote,
yale Mungu amewaandalia wale wampendao}. Ni kweli. Wewe mpende tu, kisha
uone.” Mpaka Naya akasikia kusisimkwa mwili.
“Ndio maana nimekwambia hicho alichoweka Mungu moyoni mwako.
Ukashindwa kutulia japo mazingira yanakukatalia, jua analo kusudi ambalo
anataka litimie. Ndio maana na mimi nataka kuona hicho anachokilazimishia
kwenye moyo wako, huwezi kutulia. Nataka kumuona tena akitembea kwenye huo
upande maana huku kwangu, hakika anatembea. Hicho ninachokwambia kinataka
kuzaliwa, najua kitawapasua vichwa wale wazungu kwa kuwa mimi mwenyewe
niliyewazoesha kuwashangaza, ninashangaa.” “Hongera sana Joshua. Nakuombea
kizaliwe kwenye mazingira mazuri.” “Hilo ndilo nahitaji Naya. Utulivu wangu
binafsi ili niweze kukizaa vizuri.” “Basi hayo ndio yatabakia maombi yangu
kwako.” “Asante sana.” Wakatulia kidogo.
“Nakwenda kuoga, nikitoka, ni sawa nikikupigia wakati nakula? Ili
nisiwe peke yangu mezani.” Joshua akamuonyesha Naya kumuhitaji sana mpaka
akajisikia vizuri. “Halafu unipigie picha kitu unachokula.” “Nina mpishi mzuri sana.
Nitafanya hivyo.” Wakaagana.
Baada ya muda kweli akampigia. Naya hakutoka hapo chumbani.
Walimsikia tu akicheka chumbani kwake na kuzungumza. Alikuwa naye wakati akila,
akisikiliza taarifa ya habari na kumshirikisha kila kitu kwenye habari kama
yupo naye. Mpaka habari za kiuchumi huko nje ya nchi na hisa kwenye soko la
dunia. “Mimi mwenzio hayo mambo hata sisikilizi au kuangalia.” Joshua
akacheka sana. “Wewe mwana masoko lazima nikuwekee tabia za kimasoko. Huu ndio
ulimwengu wetu zaidi sisi. Kujua uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla ili kujua
na sisi tunaweza kupenya vipi! Nini chakuiga, nini chakuboresha, nini kisubiri
uwekezwaji, kipi kianze kwa haraka, na mengineyo.” Wakazungumza
mengi mpaka mtazamo wa Naya ukaanza kubadilika. Amekutana na msomi haswa, tena
mcha Mungu! Hali mpya ikaanza kujengeka ndani yake. Wakaomba pamoja ndipo
wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua ameingia kwenye picha akiwa na sura ya tofauti na wanaume
wote waliokwisha pita kwenye maisha ya Naya. Na anaonekana kumfahamu na
kumfuatilia Naya tokea zamani bila Naya mwenyewe kujua. Na pia anaonekana
amebeba historia ngumu. Fuatilia ili uwe nao kwenye mtoko wao wa siku ya Jumamosi.
Joshua Kumu ni nani haswa?
Endelea kufuatilia safari ya Mapenzi ya Naya....
0 Comments:
Post a Comment