Alipofika nyumbani akabaki
akishangaa. Nyumba ilikuwa safi sana. Mazingira ya nje yalikuwa masafi sana
kama enzi za uhai wa mama yao, baba yao akiwa anasafisha mara kwa mara
kumridhisha mkewe, kumuonyesha wanapoishi sio pabaya. Alijitahidi kuweka
mazingira safi wakati wote. Sasa tokea mkewe aanze kuugua, hakurudi kusafisha
tena mpaka siku hiyo. Akasimama pale akishangaa. Zayoni akatoka. “Baba
amesafisha nyumba.” “Yuko wapi?” “Ametoka, amesema hatachelewa kurudi.”
“Umekula?” “Nilikuwa nasoma. Nina shida Naya.” Naya akamsogelea. “Unataka
nini?” “Hela.” “Ya nini?” Naya akamuuliza.
![]() |
“Na mimi nataka kusaidia
Naya!” “Naelewa. Unakumbuka ujuzi ulionao wa kupiga picha?” “Kamera iliharibika!”
“Tutanunua nzuri na ya kisasa ili uanze tena. Lakini safari hii tutajitangaza.
Ili ufanye kazi nzuri. Naweza hata kuwa nakusindikiza kama ukipata kazi kubwa.
Nitakuwa nikikusindikiza. Halafu kuna sehemu nzuri tukipata, tunaweza
kupakodisha, ukapatengeneza vizuri, ukawa unawapiga watu picha.” Akamuona
anacheka.
“Unaakili yakufikiria Naya
wewe! Kila ukiongea unatoa wazo zuri.” Naya akacheka. “Ndio urudishe akili
shuleni. Jikaze, umalize shule, ndio tuanze kutengeneza pesa.” “Sawa.”
Wakamuona baba yao anarudi. “Bale amesema leo hatarudi. Anamtihani kesho.” “Na
mimi ameniambia. Shikamoo baba.” Naya akamsogelea huku akicheka. “Unanicheka?”
“Umenyoa, ukapendeza. Nimefurahi.” Baba yake akacheka na kumsogelea Zayoni.
“Vipi shule?” “Naendelea. Umependeza.” Zayoni naye akasifia.
“Sasa kwa kuwa wote mpo
hapa, nataka niwaambie nimepata kibarua kwa Malon. Ni Mbeya.” “Unarudi lini?”
Zayoni akauliza kwa wasiwasi. “Sijajua.” “Mimi naona ni wazo zuri baba. Huwezi
jua ni nini utakutana nacho huko. Na juu ya Zayoni, nitajitahidi kuwa nawahi
kurudi nyumbani. Ili asiwe peke yake.” “Ulisema unasafiri Naya. Nitabaki na
nani wakati Bale amesema atakuwa busy na shule ili amalize huu muhula vizuri? Natamani
mama angekuwepo jamani!” “Hapana Zayoni. Naomba huko tusirudi. Sasa hivi sisi ndio
tumebaki hapa. Lazima tujipange na tujue tutaishije. Umenisikia?” Zayoni
akajifuta machozi.
“Nisikilize Zayoni.
Hatuwezi kuendelea hivi tulivyo. Lazima kuenzi kile mama alichokuwa akitaka.
Sisi tusome sana, na baba atafute pesa. Sasa hatuwezi kuacha sasa hivi. Itakuwa
ni kama kutomuenzi. Lazima tujipange upya. Mama hayupo na hatarudi tena, na
hakuna wakuchukua nafasi yake kwetu. Hilo lazima tulikubali. Ila tusaidiane.
Mimi nimezungumza sana leo na bosi wangu. Nimemwambia mazingira niliyonayo
nyumbani na kuwa wewe unakaribia mitihani yakumaliza shule ya msingi na Bale
hatakuwepo nyumbani. Unahitaji mtu nyumbani. Ameniruhusu niwe nawahi kutoka.
Saa 9 na nusu amesema naweza kutoka na muda huo kutakuwa hakuna foleni. Kwa
hiyo utajikuta nyumbani peke yako kwa muda mfupi sana. Tunahitaji pesa na
tunahitajiana. Umeelewa?” Zayoni akatingisha kichwa kukubali. “Na sitasafiri
mpaka niwe ninauhakika baba yupo nyumbani au Bale. Kwa hiyo usiogope.” Zayoni
akatulia.
“Au nisubiri mpaka Zayoni amalize mitihani?” “Hapana baba. Ulinifundisha linalowezekana leo, lisingoje kesho. Unajuaje kama hapo baadaye kama hatakuhitaji tena?” Kimya. “Tutakuwa sawa baba. Naomba chukua hatua ya imani. Nenda. Ukishindwa kwenda sasa hivi kwa sababu hii, ujue kesho litaibuka jingine. Hutawahi kuondoka humu ndani na hutaweza kuchukua hatua yeyote kwa sababu utajiona upo peke yako na unahitajika kwetu kwa hili au lile. Lakini naomba ukubali kuwa na sisi tupo kukusaidia.” Wakazungumza na kujipanga.
Siku
Inayofuata
Naya &
Malon Tena.
W |
akati wapo madukani wakinunua vitu vya baba yake Naya, Malon akajaribu
tena. “Naruhusiwa kuja kumchukua Zayoni kesho jioni.” Naya akamgeukia na
kusimama akimtizama. “Kwa nini!?” “Kupata naye tu muda. Kuzungumza naye kabla
ya safari.” “Kwa nini!?” “Naya mama! Kwani vipi?” “Huyu mtoto amefiwa na mtu
muhimu sana kwake Malon. Na mimi huwa nakujua. Unaweza kuanzisha kitu kingine
kwenye maisha yake, ukamuacha, tukaanza msiba mwingine. Baada yakuona mama
anafukiwa kule makaburini, aliingiwa na mshtuko mkali sana. Aliumwa muda mrefu
sana, akiwa hawezi hata kutoka kitandani. Tumemjenga kwa shida sana. Nakuogopa
Malon. Hakika nakuogopa.” Naya akafikiria kidogo akamwangalia Malon.
“Unayo jinsi yako kwenye
mioyo ya watu. Nzuri sana. Unajua kupenya kwenye moyo na akili ya mtu bila
shida na kumfanya mtu akajisikia ndio
wewe pekee anakuhitaji duniani. Lakini huwa hudumu Malon. Unaondoka katikati ya
hiyo hali na kuacha mtu anakuhitaji. Mimi sio wa kwanza. Ulipokuwa jela,
nilikutana na hivyo vilio kwa wengi mpaka kwa wazazi wako. Hujui kujifunga
kwenye mahusiano Malo. Hujui kusimama na mtu kwa muda mrefu. Ukianza na Zayoni,
ukamuumiza, inaweza kumuharibu kabisa. Na mama wakumjenga hayupo. Mimi nilikuwa
nikiweza kusimama, sababu ya baba. Nilikuwa na kimbilio. Yeye hatakuwa na
kimbilio. Yaani sasa hivi ndio namfahamu yule mtoto. Maisha yake yalikuwa ni
yeye na mama tu. Hata baba kumbe hamfahamu kabisa Zayoni. Ndio tunajifunza
tabia zake na kumwelewa ili tuweze kumsaidia. Sasa hivi ndio naelewa kilio cha
mama kwa Zayoni. Alijua angepata shida akimuacha.” Naya alibadilika akawa
makini sana kwa Malon.
“Nimekuelewa Naya. Na mimi
sitafanya hilo kosa la kumuunganisha na mimi. Nimekuelewa tokea jana. Ni kweli
mimi ni mtu mbaya sana lakini nataka kumuunganisha kule nilikopata msaada mimi,
nilipokuwa kwenye hali kama yake.” “Hujawahi kuwa, alipo Zayoni! Usijifananishe
naye.” “Naya! Mimi ndio nakwambia.” Naya akamwangalia kwa kumsuta akaona
aachane naye tu ila amuulize kinachomuhusu. “Ni wapi huko unakotaka
kumuunganisha apate msaada?” “Kanisani. Lipo kundi la vijana ambao huwa
nawasadia wasije pita nilikopita mimi. Huwa tunapata muda wa mazungumzo na
michezo mbalimbali zaidi mpira wa miguu. Tumetengeneza timu ya kanisa. Kwa sasa
nawadhamini mimi mwenyewe. Ni vijana wazuri sana, kwa kuwa karibu nao. Wanapata
mafunzo mazuri.” Hapo Naya akatulia.
“Najua mimi sio
wakuaminika, ila yupo ambaye ananisaidia Naya. Najijua mimi ni dhaifu sana, na
wewe ni shahidi mama. Sikuwa hivi. Yesu ananibadilisha kwa hatua. Yapo mengi
mabaya sana Naya. Tafadhali tambua kazi ya msalaba kwangu, angalau katika hilo
nipe pongezi.” Naya akajirudi kidogo. “Ni kwa kuwa umeshaniumiza sana Malo. Ila
ni kweli umebadilika.” “Sasa! Na mimi najua Naya. Najua kabisa nilikuwa mbaya,
na ninajua nahitaji msaada. Wala sikatai.” “Hongera.” “Asante. Kwa hiyo
niruhusu nije kumchukua Zayoni. Tena kwa kuwa unawasiwasi na mimi,
nitamkabidhisha kwa mtu mwingine ambaye yeye ndio anakuwa na hao vijana muda
wote. Kwanza kesho ni ijumaa. Hata akichelewa kurudi haitakuwa na neno.” “Na
nyinyi mnaondoka jumamosi saa ngapi?” “Mapema tu.” “Sawa.” Naya akaafiki kwa
upande wa baba yake lakini si kwa Zayon. Moyo ulishagoma kumrudisha Malon kwa
ndugu zake kama zamani.
“Na kuhusu Zayoni naona
hiyo itamsaidia kumchangamsha, lakini naomba usinielewe vibaya Malon.
Utatusaidia kututambulisha kwa huyo mtu tu, kisha mimi na Bale tutaendelea.
Tafadhali naomba unielewe. Siwezi kumuacha Zayon mikononi mwa mtu mwingine yeyote
isipokuwa mimi au Bale, mbali na baba. Nilimwapia mama, na nitalisimamia hilo.
Hapo sitatoa hata mwanya wa kukujaribisha Malon.” Malon akapoa, akajua ni kweli
Naya amebadilika.
“Sasa lengo si lilikuwa ni
kusaidia? Mbona kama umebadilika tena!?” Naya akauliza akishangaa kidogo na
kijiukali. “Nimeelewa Naya.” “Hapo sina utani. Tafadhali mchukue kesho,
kamtambulishe, sisi tutaendelea tu.” Naya akaweka msisitizo. Wakazunguka, Naya
akapata kila kitu cha baba yake, lakini Malon ndiye aliyelipia kila kitu kwa
kulazimisha sana mpaka wakatia aibu mbele ya wauzaji kwa kubishana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa kwenye gari Malon
akaanza tena. “Naya! Nikuulize swali?” “Niulize tu.” “Unaamini kama nakupenda?”
“Daah! Hakika kila kitu kimepotea akilini mwangu na mawazoni mwangu juu yako
Malo. Kilichobaki kwa hakika ni uthibitisho kuwa, huaminiki. Hilo tu ndilo
nimebakiwa nalo.” “Hivi Naya, si unakumbuka kule nilikotoka na historia ya maisha yangu? Tokea mdogo tu, nilifanya
kile bangi kinaniongoza. Nilikimbia malezi ya wazazi, mimi sio kama Bale au
wewe! Hakuna mwanadamu ameweza kusimama na mimi katika upumbavu wangu isipokuwa
ananufaika na mimi kwa namna moja au nyingine. Nilipokuwa mdogo, walinitoa jela
ili niendelee kuwauzia bangi mtaani. Nilipokuwa na pesa, walinitoa wakijua
nikiwa mtaani wataendelea kunufaika wao na familia zao. Ndio maana walipojua
sitatoka tena, wakanikimbia na mali zangu. Maana kwa uhakika, najua kama
wangejua nitatoka jela, hakuna ambaye angethubutu kutoroka na mali zangu.”
“Kwamba na mimi unanihesabu kama hao watu unaowazungumzia Malon!?” Naya
akauliza kwa ukali akishangaa sana.
“Aisee acha kuniumiza
Malon! Katika yote na matendo yote, bado unanihesabu mimi kama watu wengine
waliowahi kukupendea pesa!?” “Sio wewe, Naya. Naomba usikasirike.” “Nilitaka
kukushangaa maana ni kama unataka kujitetea wakati mimi unanifahamu na hata
nilikwambia Malon. Tena ukiwa na wasiwasi wa elimu yako! Unakumbuka nilikwambia
usiwe na wasiwasi, kwa kuwa umenisomesha mimi, kutakapokuwa na uhitaji ya elimu
mimi nitakuwepo, mengine tuje tufanye pamoja! Nikakupa mawazo mengi sana ya
nini tuje kufanya pamoja, ukaja kunigeuka! Leo unasema watu wote wanaokuzunguka
wanakupendea pesa!? Ni kwa kuwa hukuwahi kuniona mimi kama Naya, Malon.
Japokuwa nilikuwa nikikulilia sana, ulinipuuza, na macho yako yaliendelea
kuangalia waliokuwa wakikutumia, ndio maana japokuwa nilizungumza na wewe kwa
kurudia rudia, hukuwahi kunisikia mimi, ila wengine wote. Tafadhali naomba
tuache tu haya mazungumzo. Sitaki nirudi nyumbani nikiwa nimekasirika.” Malon akanyamaza
kimya kabisa.
Malon akaendelea kuendesha.
Kimya kwa muda, kisha akaanza tena. “Lile gari nimenunua kwa pesa nyingi mama.
Kulikataa mikononi mwangu nikiwa nimekununulia wewe, na siwezi kulirudisha,
nabaki nalo pale nyumbani, halina matumizi naona si sawa. Ili kukuthibitishia
sitakuja kubadilika na kukupokonya, naomba ulichukue lile gari na nitakupa hata
kadi zake. Ujue ni lako kabisa, na wala sitakuja kukuuliza tena.” Naya kimya.
“Ungekuwa na uwezo wa
kuniuzia kila kitu nilipokuwa jela. Lakini sasa hivi nina nyumba, sababu yako
Naya. Biashara niliyonayo ni mtaji wa pesa uliyokuwa umehangaika kuniwekea
dhamana. Tafadhali chukua lile gari. Huna haja hata yakuhesabu kama nimekupa,
bali kama moja ya haki yako. Ni jasho lako Naya. Ulifanya kazi za
kujifedhehesha kwa ajili ya kukusanya ile pesa. Niliondoka bila kukuachia kitu.
Sasa nakupa hii gari si kama nakuhonga. Ni yako Naya. Yako kabisa wala haiitaji
mjadala au kuja kuzungumzia baadaye. Ulihangaika, ni pesa yako ambayo imekujia
hivyo kwa njia ya gari. Usikubali hasira ikakupotezea haki yako.” Hapo Naya
akashawishika ila akatulia tu.
“Eti Naya?” “Malo akitaka
jambo lake! Ndio maana unaniuma sana Malo. Kuna vitu ukivitaka huwa unapambana
mpaka unapata!” “Najua ni ngumu kusahau mabaya yangu. Turudi kwenye usafiri. Huoni
kuwa itakusaidia kuwahi kurudi nyumbani kwa Zayoni, na jumapili kwenda
kanisani? Halafu hujahongwa na mtu. Ni kama pesa yako ilikuwa mahali, sasa
imerudi. Huoni kama unastahili mama? Acha kuendelea kujitesa kusipokuwa na
sababu. Ni jasho lako, na unahitaji. Itakusaidia sana tu.” “Nikweli litasaidia.”
Malo akatulia na kuogopa kuongeza neno asije tibua huku akisubiria kujua
muendelezo akiwa na tumaini kuwa anaanza kukubali gari.
Alipoona wanaendelea kwenda
yupo kimya na wanakaribia kufika Ubungo akimrudisha nyumbani kwao, akaona
ajaribu tena. “Kwa hiyo tunaenda kuchukua gari?” Akawa kama amemtoa Naya
mawazoni. Akamwangalia. “Vipi?” “Nipo tu
sawa. Kwani umeniongelesha?” Ulipomsikia na sauti imetulia akaongeza. “Nilikuwa
nikifikiria tupitie nyumbani ukachukue hilo gari na karatasi zake zote, leo.”
Akamuona anavuta pumzi kwa nguvu kama anayejifikiria. “Ukilichukua leo,
hutanisikia nikilizungumzia tena.” Malon akaongea kwa tahadhari sana.
“Nilikuwa nikikumbuka vile ulivyoyabadilisha
maisha yangu Malon. Ulinionjesha maisha ya usafiri. Nikawa nimeshasahau haso za
daladala ambazo sikuwahi kuona ni tatizo mpaka ulipokuja kwenye maisha yangu na
ile gari yako na yale maisha ya kunilipia taksii pamoja na kunitumia Side anipeleke
nitakako. Nikazoea hayo maisha. Halafu..” Akaamua kunyamaza tu. “Nashukuru kwa
usafiri.” Naya akaamua kushukuru akijiambia ni kweli anastahili hilo gari na ni
haki yake. “Karibu. Basi twende ukachukue.” Malon hakuongeza neno, akatafuta
njia kuelekea nyumbani kwake Kunduchi kimyakimya tu.
Hakuna lililozungumzwa tena
mpaka walipofika nyumbani kwa Malon. Mlinzi akafungua geti, Malon akaingia na
kumwambia asifunge geti, gari ndogo inatoka. Akavuta gari yake na kuiegesha
pembeni ya hiyo gari ndogo. Naya aliona gari ya Rita hapo nje. “Subiri
nikakuletee kabrasha lenye hati zake zote.” “Mbona hunikaribishi sasa!?”
“Naogopa kuharibu mama. Usije ukaniacha nalo na leo tena. Hapa najiwinda kwa
kila neno.” Naya akacheka kidogo. “Karibu mama.” “Nashukuru. Naona wazo
lakuniacha hapa ni zuri, ili nisikawie kurudi kwa baba Naya, nikamtia wasiwasi.”
Malon akaingia ndani baada ya muda mfupi akatoka na kabrasha.
Naya akatoka garini baada
ya kurudi Malon. Akamkabidhi. Naya akacheka kidogo asiamini kama anamiliki usafiri
wa uhakika. “Asante.” “Lakini bado lipo kwa jina langu. Nikitoka safari ukitaka
naweza kukusaidia kufanya taratibu liwe kwa jina lako.” “Siamini! Asante.”
“Nikuombe kitu Naya?” “Nini tena?” “Naomba urudishe nywele kichwani.” Naya akacheka
kidogo na kujishika kichwa. “Najua umefiwa, lakini anza kutoa hayo mazingira ya
majonzi usoni ili hata Zayoni aone kuna mabadiliko. Tumaini jipya.” “Nitarekebisha.
Asante kwa ushauri.” Wakacheka kidogo,
Naya akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bale alitoka tu kwenye
mitihani yake akarudi nyumbani moja kwa moja. Walikuwa wote nje wakimwangalia
na kumsaidia baba yao akijengea senyenge ndani ya michongoma kuzunguka nyumba
yote. Wakashangaa Naya anaingia na gari. Wote wakaduwaa wakati anashuka.
Akawasogelea, wote walikuwa kimya. “Amenipa Malo lakini ni haki yangu kama
jasho langu sio hongo.” Akaanza kwa kujihami akimwangalia baba yake. “Amesema ni
katika zile pesa nilizokusanya wakati ule kumtoa jela. Alishindwa kunipa wakati
ule ili nianze biashara. Sasa safari hii amenipa gari akisema itanisaidia usafiri
wa kwenda kazini, na hapa nyumbani nikibaki na Zayoni. Alitaka kunipa jana
alipolinunua, lakini nikamkatalia nikidhani ameanza mambo yake yaleyale.
Sikutaka hongo zake. Au vile anavyo...…” “Wakati unajieleza, naomba funguo
nizunguke nalo kidogo tu.” Bale akadakia.
“Subiri kwanza Bale bwana, nimwambie
baba. Akikataa na kutaka nilirudishe je?” “Mbona usiniulize kabla hujapokea?”
Baba yake akamuuliza kwa kumsuta. “Mimi naomba niendeshe kidogo. Hata kama baba
akisema ulirudishe, niwe na mimi nimeendesha.” Akampokonya dada yake funguo. “Acha
nishushe mizigo ya baba kwanza, bwana Bale!” Akamfuata Bale kwa nyuma kwa
haraka.
“Umemnunulia nini?” “Vitu
vyake vya huko safarini.” “Sasa na mimi umeninunulia nini?” Bale akauliza.
“Miwani ya jua na tsheti zakuvaa chuoni.” “Basi nipe miwani yangu nivae sasa
hivi.” “Na giza lote hili! Hapana Bale. Utagonga gari wakati hata sijui kama
baba atakubali libaki au atataka lirudi.” “Wewe mlilie tu. Mimi namjua baba. Wewe
ukilia tu huwa anakukubalia chochote umuombacho.” “Mwenzenu baba anawasikia.” Zayoni
akawashtua. Bale na Naya wakageuka. “Usimfundishe huyo ujinga.” Baba yao akamwambia
Bale huku akiendelea kufanya kazi. Bale akacheka, na kuondoka na gari. “Na mimi
umeniletea nini Naya?” Zayoni akamfuata dada yake. “Chupi, tisheti, singlendi, soksi
na miwani ya jua. Huna shupi Zayoni.” “Kweli. Asante Naya. Unajua mama ndio
alikuwa ananibadilishia kila mara?” “Aliniambia. Alisema unapenda sana chupi.”
Zayoni akacheka. “Sasa tokea azidiwe, sijabadilisha chupi. Nashukuru sana.”
Naya akacheka.
“Malon anataka aje
akuchukue kesho akupeleke kanisani kwao kwenye kundi la vijana. Wanacheza
mpira. Ungependa kwenda?” “Sijui Naya.” “Nenda. Itakusaidia kutengeneza
marafiki na kukufanya uchangamke. Umekula?” “Nimekula na kusoma. Nimetoka muda
sio mrefu kumsaidia baba. Anataka kujenga geti kabla hajaondoka.” Naya
akamsogelea baba yake.
“Kwani nimekuudhi?” Baba
yake akamwangalia na kuendelea. “Nimekununulia kila kitu cha safari.” “Asante.
Hata sikujua kama natakiwa vitu vya safari.” Naya akasogea. “Mbona unatokwa
jasho hivyo?” “Kazi ya tokea niliporudi asubuhi kutoka kukusindikiza kituoni.
Jana nilichimba mashimo na msingi kuzunguka uzio wote huu, kwa ajili yakujengea
msingi. Leo nikatafuta vijana wawili. Wamenisaidia kumwaga zege, ndio namalizia
hapa mwisho. Niweke msingi. Pakauke, nisimamishe geti.” “Pesa umepata wapi?”
“Zile za gari. Wamenilipa, nimechanganya na akiba yangu.” “Hongera,
pamependeza.” “Mimi nataka usalama wenu. Sitaki niondoke, waje waanze
kuwaingilia usiku. Nataka kumuomba Malon nimfuate huko Mbeya siku ya jumapili.
Angalau jumamosi nisimamishe geti. Hizi nguzo zitakuwa zimekauka.” “Sawa. Na
kuhusu gari?” Naya akachomekea.
“Kuhusu nini?” “Malo
amenipa gari baba.” “Si ukakubali? Sasa sasa hivi unaniuliza nini?” Naya
akaanza kucheka taratibu. “Siku nyingine nitakuuliza.” Baba yake akamwangalia.
“Kweli tena.” “Siku zote unauliza kabla hujapokea vitu vya watu. Wala leo
hukukosea. Ulifanya kusudi ukijua wazi jibu langu.” “Mimi sijui jibu lako
baba.” “Unajua sana na ndio maana jana ulilikataa, na hukuniambia. Ukaenda
kubembelezwa huko, ukakumbuka shida ya leo asubuhi karibu uchelewe kazini,
ukaenda kulifuata, nakuja nalo hapa. Halafu unanidanganya kwa kuniuliza!”
“Lakini litatusaidia baba.” Naya akajisogeza karibu.
“Nimefikiria nikajiona
nakuwa mpumbavu bila sababu! Ni haki yangu baba yangu. Umeona jinsi nilivyokuwa
nikihangaika kukusanya ile pesa. Malon mwenyewe ukimsikiliza yupo vilevile si
wakubadilika leo yule wala kesho. Sasa nikajiambia ni kama napigana na upepo. Nikijifanya
kuzira, nikujitesa mimi mwenyewe. Nikaona ni heri nijifute jasho mwenyewe. Sina
sababu yakujitesa. Nimehangaika sana na yule kiumbe. Hata kama vingine
vimeshindikana, acha nipate kiinua mgongo. Hata hivyo nani atakuja kunipa gari?”
Baba yake akamtizama tu.
“Hii gari ni yangu kabisa baba. Amenihakikishia wala hatakuja kuniuliza juu ya hili gari na tumefunga mjadala. Mpaka kadi zake zote za gari amenipa. Kwa hiyo acha litusaidie baba yangu. Tuliteseka naye sana.” Naya akaendelea kumshawishi baba yake akamuona amenyamaza tu akiendelea na kazi. Akatulia kidogo akiwa na wasiwasi wakuambiwa alirudishe. Hata yeye alijua baba yake anamuhofia sana Malon kwa tabia yake ya kutotabirika. “Nenda kale.” “Nataka kukusaidia.” “Kale kwanza, ndio uje uniambie vizuri juu ya habari za gari.” Naya akacheka kwa furaha. Akaondoka na Zayoni akijua ndio amemkubalia abakiwe nalo. “Umeoga?” Akamsikia akimuuliza mdogo wake. “Bado.” “Usilale bila kuoga Zayoni.” “Mbona sasa hunipi zawadi zangu?” “Nimeweka kwenye hilo begi la baba. Twende ndani nitakupa.”
Malon na Zayoni.
S |
iku hiyo ya ijumaa Malon alifika nyumbani kwa kina Naya, akamkuta
baba yake na mafundi. Busy anatokwa jasho. “Natengeneza ulinzi wa mama mzazi.
Wasije kuniibia wakati sipo.” Malon akacheka. “Hongera. Naona umezungushia
pote.” “Bado geti. Sio zuri sana, lakini angalau nitaondoka nikiwa na amani
yupo ndani sio hivi yupo nje! Tena nilitaka kukuomba nikufuate. Ili kesho
nijengee. Nikiliona limesimama hapa, ndio hata nikiondoka kichwa kitafanya kazi
huko. Hivi hivi, siwezi baba.” Malon akabaki kama anayefikiria.
“Na kwa kuwa sasa hivi anausafiri
ndio imesaidia kabisa. Nimemwambia Bale awe anakuja kulala nao hapa. Asiwaache
peke yao. Dada yake akienda kazini asubuhi, amshushe chuoni, jioni arudi naye.”
“Wazo zuri. Au tutafute mlinzi?” “Unafikiri sijafikiria hilo? Nimezunguka tokea
tumezungumza, wanataka pesa nyingi. Na kwa sababu wananifahamu uwezo wangu,
wanaona hakuna chakulinda hapa, kiasi chakuja kuwalipa baadaye. Nikaona heri
nijenge tu. Wasije kuniibia binti yangu bure.” Baba yake Naya alikuwa akiongea
huku akiendelea na kazi.
“Kuna watu
nafahamiana nao, nilishawafanyia kazi kipindi fulani.” “Kazi ya ulinzi?”
“Ndiyo. Nafikiri wanaweza kuwa na watu wanawafahamu maeneo ya huku. Tukienda
wote, wanaweza wasikusumbue.” “Hilo nitashukuru. Japo kwa muda tu baba.
Nitalipia huo ulinzi mimi mwenyewe. Niondoke nikijua yupo mtu ananilindia mama
yangu.” “Sawa. Lakini leo nilitaka tutoke na Zayoni. Mazungumzo tu na
kumtambulisha kwenye kikundi cha vijana pale kanisani. Wengine wanalingana au
anaweza kupata watu wa umri wake. Pale kanisani kwetu wamewekeza sana kwa
vijana.” “Ameniambia Naya. Na kaka yake ameona ni wazo zuri, atakuwa naye huko
baada ya wewe kumtambulisha.” Malon akajua ndio kwa hakika haaminiki tena pale.
Akawa mpole tu.
“Alisita
mwanzoni ila naona baadaye akakubali. Muda si mrefu atarudi hapa. Kifo cha mama
yake kimemuharibu sana akili. Aliugua sana. Hakuwa akiweza hata kutoka
kitandani kwa muda mrefu sana!” “Poleni sana.” “Ila mimi nilishamuonya mama
yake hata kabla hajaanza kuugua. Alimlea vibaya sana Zayoni. Itamchukua muda
kuwa sawa. Hana marafiki. Hajui kucheza mchezo wa aina yeyote ule. Hata mpira
wa miguu hawezi. Kutwa alikuwa mgongoni kwa mama yake. Anamenya vitunguu au
nyanya akitaka awepo alipo mama yake!” Malon akacheka.
“Enzi za uhai wa mama yake
alipokuwa shuleni, ilikuwa hivyohivyo. Wakati wote kama hayupo darasani basi
ujue yupo ofisini kwa walimu pembeni ya mama yake. Hana anayemjua wala
kumfahamu isipokuwa mama yake tu. Sasa hivi inamuia ngumu hajui maisha
yanakuaje hapa duniani bila mama yake. Sio tu kama mama, ndiye aliyekuwa rafiki
yake na msiri wake haswa. Kwenda na kurudi naye kutoka shule. Wao wawili kila
mahali. Kwa hiyo ukimsogeza huko, itamsaidia.” “Nimefurahi kama nimepata baraka
zenu. Na ninaamini itasaidia tu.” Malon akasaidia kazi mpaka Zayoni akarudi
kutoka shule.
Akasalimia. “Nenda ukaoge,
ubadili hizo nguo, ule, ndio uondoke.” Baba yake alimpa maagizo. “Kuna sehemu
nataka nikupeleke ukale ndio twende kanisani. Muda bado.” Malon akaingilia.
Zayoni akatulia kidogo kama anayesita. Baba yake akasimama. “Nini?” “Naya
atakuja?” “Utamkuta Naya hapa nyumbani. Bale alishakwambia ukajichanganye
Zayoni. Utakuwa sawa.” Akabaki amesimama huku ameinama. “Vipi?” “Sitaki
kwenda baba.” Akaanza kulia. Baba yake alitegemea hilo. Akabaki akimwangalia.
“Nisikilize Zayoni. Sio lazima kabisa, lakini ninauhakika utafurahia. Naomba
ujaribu tu. Tukifika, halafu usipopenda, nitakurudisha nyumbani. Sawa?”
“Sitaki waanze kunicheka
sijui kucheza!” “Usiwe na wasiwasi. Wale vijana wamefundishwa kucheza palepale
kanisani. Wengi walikuwa hawajui kitu. Hata mimi nimewasaidia, na wewe
tutakusaidia. Na sio lazima ukifika leo leo ucheze! Hapana. Unaweza tu kuwa
muangaliaji mpaka ukazoea. Leo utakuwa na mimi, ijumaa ijayo utakuwa na Naya.
Usiogope.” “Hutaniacha hapo peke yangu na wao tu?” “Hata
kidogo. Nitakuwepo na wewe mpaka nikurudishe hapa nyumbani.” “Umesema
hutaniacha nao peke yetu na si lazima nicheze?” “Ndiyo.” Malon
akamkubalia. Ndio akakubali kwenda kuoga.
Alitoka amevaa vitu
alivyonunuliwa na Naya siku iliyopita, akawa msafi. “Unataka tupitie kunyoa
nywele kwanza?” Malon akamuuliza wakiwa wanaondoka. “Mama alikuwa akinipeleka
kunyoa, au anamlipa yule kijana aninyoe palepale nyumbani.” “Basi naweza kukupitisha
mahali ukanyolewa ndio tukaenda kula. Au njaa inauma sana?” “Hapana. Nikanyoe
kwanza ili niwe msafi.” Akanyamza.
“Vipi shuleni?” Malon
akajaribu kumuuliza. “Naendelea kwenda. Lakini sasa hivi naenda peke yangu.
Unajua nilikuwa nasoma shule anayofundisha mama?” “Ndiyo.” “Tokea naanza darasa
la kwanza mpaka alipoanza kuumwa tulikuwa tunaenda naye shule. Mara nyingine
alikuwa mgonjwa, lakini alikuwa anakwenda ili tuwe naye.” “Sasa sasa hivi
unafanyaje?” “Ni ngumu! Lakini Naya ameniambia kila nikimkumbuka niwe nafanya
kitu chakumuenzi.” “Kwa hiyo sasa hivi unafanya nini?” Malon aliendelea
kumdadisi taratibu.
“Najitahidi nikifika shule
niwe na kitu chakufanya wakati wote ili muda uende haraka nitoke pale. Natamani
nimalize haraka niondoke pale. Pananikumbusha sana mama.” “Pole sana Zayoni.
Umejaribu kutengeneza marafiki?” Akanyamaza
kwa muda akamuona anakunja uso na kujibu. “Mimi sijui michezo Malo. Watataka
twende tukacheze, wakati mimi sijui kucheza, halafu sipendi kuchelewa kurudi
nyumbani. Bale hakuwa akichelewa kurudi nyumbani. Sitaki mimi niwe watofauti.”
“Unafanya vizuri. Na upo sahihi.” Wakaendelea kuendesha.
“Sasa umefikiria nini
chakufanya ukimaliza shule?” “Naya ameniahidi kuninunulia tena kamera.
Unakumbuka ulininunulia kamera?” “Nakumbuka.” Malo akajibu. “Iliharibika.
Lakini Naya ameniambia ataninunulia nyingine, halafu atanitafutia sehemu niwe
napiga picha hata za maharusi.” “Yaani kuwe kama studio?” Zayoni akacheka.
“Ndivyo alivyosema Naya.” “Naya anaakili sana.” “Hata mimi nilimwambia hivyo
hivyo. Lakini unajua nimeshangaa?” “Kwa nini?” “Unavyoniamini! Eti anitafutie
studio mimi! Halafu anasema kama wakiniita hata kwenye maharusi au shuguli za
watu, atakuwa ananisindikiza.” “Safi sana. Ni kwa kuwa ameona kazi zako. Hata
mimi niliona picha ulizokuwa ukipiga wakati ule. Unakumbuka wakati ule anafanya
mambo ya mavazi, ukapiga picha na kuziweka kwenye website?” Akacheka. “Zile
picha zilikuwa nzuri sana. Hicho nikipaji. Naungana mkono na wazo la Naya.”
“Kweli!?” “Kabisa. Na ninauhakika watu watafurahia kazi yako.” Akamuona anaanza
kutulia. Akamuacha.
“Unampenda Naya?” Malon
akashtuka kidogo, na kumwangalia. “Nampenda sana.” Akanyamaza kwa muda. Malon
akamwangalia, akamuona ametulia. “Nikuulize kitu kingine Malon?” “Niulize tu?”
“Umemchukia mama yetu kwa kukufukuza?” “Wewe unajua kwa nini alinifukuza?” “Ili
aolewe na Joshi?” “Hapana. Mama alitaka Naya aolewe na mwanaume mzuri ambaye
ataweza kumtunza vizuri Naya kitu kinachonifanya nimpende zaidi mama na
kumuheshimu.” “Kwa nini?” “Kwa sababu ni mama mzuri. Hakuna mama anayependa
mtoto wake aje kupata shida. Kwa wakati ule, mimi sikuwa mtu sahihi kwa Naya.
Nilikuwa nimefanya makosa mengi sana ambayo kwa maneno pekee, ilikuwa ngumu
kuaminika. Ndio maana mama alikuwa na wasiwasi na mimi. Alitaka mwanaume mzuri
aliyetulia kwa Naya.” Zayoni akatulia.
“Kwa hiyo sijawahi
kumchukia mama. Ila nitamuiga. Na mimi niwe nalinda watoto wangu.” “Lakini Bale
alisema Joshi hakuwahi kumpenda Naya.” “Kwa nini?” “Sijui sana kama Bale.
Lakini ninachohisi hakuwa akimjali kama wewe. Siku moja Joshi alikuja kumchukua
Naya nyumbani, akamuacha mjini. Baba na Bale walichukia sana. Joshi hakuwa kama
hivyo wewe unampa gari Naya. Joshi alikuwa mchoyo sana na hamjali hata kidogo
Naya.” Akatulia tena kidogo akamwangalia.
“Vipi?” “Hivi unajua kama
Naya huwa anakulilia sana?” Malon akapoa. Hakuwahi kukaa na huyo mtoto, hakujua
kama nimzungumzaji na anaangalia mambo kwa makini hivyo. “Unakumbuka siku ile
ulikuja kwenye mahafali yake kule Mzumbe?” “Nakumbuka.” “Basi siku ile alilia
sana. Njia nzima alikuwa anakulilia wewe, tulishindwa hata kula. Tulifika mpaka
hotelini, akawa analia tu. Ndio baba akasema tumrudishe nyumbani. Nikamuuliza
kesho yake kwa nini alikuwa analia sana wakati ulimletea zawadi nzuri, akasema
anahamu na wewe. Nikamwambia baba twende mjini tukakutafute, baba akasema
tuache tu, ila tumuombee. Kwani ulikwenda wapi?” Akauliza kwa upole.
“Nilikuwa nahangaika
kutafuta kazi.” “Naya anaakili sana. Ungetafuta kazi ukiwa naye ili akushauri.
Usingemuacha. Au uliogopa atakusema huna pesa?” “Hapana Zayoni, Naya ni
mvumilivu sana kwangu. Hajawahi kunichukia nikiwa sina kitu. Lakini sikutaka
kumtesa kuwa naye bila pesa.” Akafikiria kidogo, akauliza tena. “Kwani hivi
wanawake wao hawawezi kuwalisha wanaume na kuwatunza nyumbani?” Malon akajua
anauliza pia akikumbuka malalamiko ya mama yao kwa baba yao. “Wanaweza Zayoni.
Lakini Mungu alimuumba mwanaume kuwa mtafutaji. Kuna ile hali yakutamani baba
ndio atunze familia.” Hapo akanyamaza kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya naye alitoka kazini,
na kwenda saluni. Akashonewa wiving ya kawaida tu lakini wakaikata chini kabisa
ila kwa ustadi mzuri. Upande wa juu, katikati ilikuwa na mawimbi ya rangi ya
dhahabu inayowaka kiasi. Halafu kuzunguka kichwa hiyo nywele ikawa nyeusi
iliyochongwa vizuri sana, ikawa imelala kwa ustadi. Akapendeza haswa. Angalau
Naya wa zamani akaanza kuonekana tena. Akampigia simu Malon kabla hajatoka hapo
saluni. “Vipi Kiziwanda?” “Naona amechangamka. Yupo anacheza mpira. Lakini
sio kwenye timu. Pembeni tu na kijana mmoja, yeye ni mtaalamu sana. Ila
mtaratibu. Nimeona ataendana naye. Nimemuomba amchukulie taratibu sana na
amsikilize zaidi. Hapa macho yako kwake. Naona anacheka mara kwa mara.” Naya
akacheka. “Afadhali akirudi awe amechoka, alale. Alikula?” “Aliniambia anahamu
na kitimoto. Nimempeleka, amekula vizuri tu.” “Sasa unataka nimfuate sasa
hivi?” “Acha nimuulize au zungumza naye wewe mwenyewe umsikie.” Malon
akampelekea simu Zayoni.
Akazungumza na Naya. Akamsikia akimwambia, “Nitarudi na Malon.” Wakajua anapata wakati mzuri. Akarudisha simu kwa Malon, akaendelea kucheza. “Naona anafurahia. Muache tu kwa leo nitamrudisha.” “Sawa. Basi tutakutana nyumbani.” “Ulitaka nije na nini?” Naya akafikiria. “Sidhani kama kuna kitu kinahitajika. Tupo tu sawa.” “Naona itabidi nimsubiri baba. Kuna mambo anataka kukamilisha kabla hajaondoka.” “Hapana Malo. Asikukwamishe. Nenda tu, atakuja na basi.” “Tofauti ya siku moja, sidhani kama nitaokoa kitu. Acha nimsubiri tu.” “Sawa.” Wakazungumza kidogo, wakaagana.
Malon na Baba yake Naya.
J |
umapili saa 11 asubuhi, Malon alikuwa akiegesha gari nyumbani kwa
kina Naya kwenda kumpitia baba yake Naya. Wakapata muda wakuomba, Naya akatoka
nje na Malon. “Naomba umwangalie. Tafadhali Malo.” “Usiwe na wasiwasi Naya!
Atakuwa sawa.” “Nitakuwa nawaombea. Mungu awafanikishe.” “Amina mama.”
“Nakushukuru Malo. Asante/ kwa kila kitu. Baadaye tutaenda kanisani kwenu.
Zayoni anataka kurudi kule.” Malon akalifurahia hilo. “Mtakuwa na Bale?”
“Lazima. Tutakuwa wote. Nimefurahi tutakuwa na usafiri.” Malon akacheka.
“Nitakuona tukirudi Naya.
Naomba asije akatokea tena Joshi mwingine mimi nikiwa huko.” Naya akacheka kama
anayefikiria. “Tuzidi kuombeana.” Malo akashangaa kidogo. “Acha majibu ya jumla
Naya bwana! Na hivyo ulivyopendeza! Mpaka nimejuta. Heri ningekushauri
ujitengeneze nikiwa nimerudi.” Naya akacheka tu lakini Malo akagundua kuna
utofauti.
“Vipi mama? Au kuna Joshi
mwingine tayari?” “Tuzidi kuombeana Malon. Tunakuwa tunaweka mipango mingi
ambayo haijawahi kutimia tokea tunafahamiana, ndio maana nasema tuombeane tu.
Naomba safari hii kusiwe na ahadi tena. Wakati wewe maisha yako yakiendelea,
mimi huwa hizo ahadi zinanifunga na kuniumiza vibaya sana. Ndio maana safari
hii nimeshauri kwa mara ya kwanza, hebu tumuachie Mungu aingilie kati na
kutuongoza.” Hilo likampoozesha Malon kabisa. Alijua ni kawaida ya hasira za
Naya, kuzungumza mengi, angepoa tu. Lakini safari hii akaonekana kuna tofauti.
Naya akacheka kidogo
akimtizama. “Safari njema.” “Subiri kwanza Naya! Naomba usiondoke.” Naya
akageuka wakati anataka kurudi ndani. “Nataka kumsaidia baba kumalizia kufunga
mizigo yake.” “Nataka kujua tumekubaliana nini mpaka sasa?” “Sijui Malo.” “Hilo
sio jibu Naya. Na nimeomba usiwe unaniambia sijui. Natamani kujua nafasi yangu
kwa sasa.” “Kwa hakika sijui Malo. Sijui tena. Ndio maana nakwambia
tumuachie Mungu.” “Nimekuelewa tunamuachia Mungu. Lakini angalau nijue ni unanipa
muda wa kunichunguza mpaka uridhike. Ila usikubali watu wengine. Tubaki hivi
hivi.” Naya akarudi pale alipokuwa amesimama Malon.
“Hivi hicho unachozungumza sasa
hivi, sicho nilichokuwa nikikifanya tokea tupo kwenye mahusiano, Malo?!” Naya
akauliza taratibu tu. “Ulishawahi hata kuhisi nimekuwa nikiwa na mahusiano
mengine nikiwa na wewe?” Kimya. “Nafikiri katika hilo ulitakiwa kunisifu Malo!
Wakati wote mimi nimekuwa mtu ninayejua nini nataka. Labda hayo ujiambie wewe mwenyewe.
Ila ukiniambia mimi sidhani kama utakuwa unanitendea haki. Na kwa kuwa sitaki
kukudanganya, ndio maana nimekwambia tumuachie Mungu. Ninayo sababu yakusema
hivyo ndio maana.” “Ipi?” Malon akauliza. “Kubwa na ya kwanza nilishakwambia.
Na...” Baba yake Naya akatoka nakumkatisha Naya.
“Nilikuwa nakuja kumalizia
sanduku, baba.” “Naona kila kitu kilikuwa ndani. Nimeshafunga mama. Asante.” Baba
yake alishawapita na kuelekea nyuma ya gari akiwa na mizigo yake. “Unipigie
simu kila wakati nijue mmefikia wapi?” Naya akaendelea kuzungumza na baba yake,
Malon kimya. “Nitafanya hivyo. Na upunguze woga.” Baba yake akajibu kule nyuma
ya gari. “Wewe nipigie tu baba. Usiache. Ndio nitatulia lasivyo..” “Sawa mama.
Nitapiga kila baada ya lisaa kama ulivyosema.” Naya akacheka na kutaka kumfuata
baba yake, ila Malon akamuwahi na kumdaka mkono na kumshikisha hela mkononi.
Naya akashangaa kidogo. “Tutawasiliana.” Akaongea kwa sauti ya kusihi. Naya
akazitizama zile pesa, na kuzirudisha kwenye mfuko wake wa shati kwa haraka
sana bila hata Malon kutarajia.
Malon akamwangalia kwa
mshangao. “Sasa hivi nina kazi ninayo pesa ya kujikimu.” “Nafahamu Naya!” “Basi
jua nipo sawa tu. Asante.” Naya akaondoka pale na kuzunguka nyuma ya gari
ambako baba yake alipokuwepo akipandisha mizigo.
“Uwe na safari njema baba.”
“Asante mama. Ngoja nifunge hapa uniombee.” “Uvae sweta lile la rangi nyeusi
usiku, halafu lile la kijani kidogo na majivu, iwe mida ya mchana. Malo amesema
kuna baridi.” “Sawa.” “Tisheti za mikono mirefu nimeweka juu, mikono mifupi
chini. Na singilendi zipo. Usivae tisheti bila singilendi, itasaidia kulinda
kifua na baridi. Kuwe na kitu kinachoshika kabisa mwili kabla ya nguo za juu.”
“Sawa.” Baba yake akafunga mlango wa nyuma kabisa.
“Sababu ya baridi usisahau
mafuta ya mdomo ili isipasuke ukaotwa vidonda. Moja nimekuwekea kwenye mfuko wa
suruali, nyingine kwenye begi lako. Mablangeti nime..” “Naya mama, nitakuwa
salama. Na kwa kuwa nitakuwa nikikupigia simu, naona uwe unanipa hayo maelezo.
Lasivyo hatutaondoka leo.” “Naona kama hutilii maanani baba!” Naya akalalamika.
“Tokea jana unanipa
maelekezo, huamini kama nimeelewa?” “Sijui bwana! Wewe uwe muangalifu huko.
Halafu maelezo mengine nitakuwa nakupa kila siku au kutokana na wakati. Kama ni
asubuhi, unanipigia kabla hamjaanza kazi ili kukwamba nini chakuvaa.” “Sawa.”
“Kula na kunywa maji yakutosha ni muhimu. Kulala…” “Mimi nina wazo mama. Ili
bosi wangu asijute kunichukua, labda nipande ndani ya gari, unipigie simu,
halafu tuendelee kupeana maelekezo. Hii kazi isije ikaisha kabla hata sijaanza.
” Naya akacheka.
“Hata hivyo nimemaliza. Ni
msisitizo tu juu ya kupata usingizi wakutosha na..” “Naya, baba atakuwa sawa.
Acha kuwa na wasiwasi.” Ikabidi Malon aingilie. “Najua. Ila nilitaka
kumsisitizia tu.” “Atakuwa sawa.” Naya akacheka. “Unipigie.” “Sawa mama.
Nitapiga, nikisikia kuumwa tu, nirudi nyumbani kwa haraka. Hata kama ni mafua
tu, nisipuuze, nirudi. Baridi ikinizidia, pia nirudi nyumbani kwa haraka.
Mazingira nisipoyapenda, nirudi nyumbani kwa haraka. Si ndio hivyo au kuna nililosahau?”
Naya akazidi kucheka.
“Kumbe jana usiku ulikuwa
ukinisikiliza?” Malon akacheka. “Sana tu. Na ninakumbuka. Kwa hiyo usiwe na
wasiwasi. Naomba turuhusu sisi twende.” Naya akacheka na kurudi upande
aliokuwepo Malon. “Na mimi nina maagizo yangu?” Naya akacheka sana. “Muwe na
safari njema. Nawaombea. Naomba muangalie sana..” “Baba?” Malon akamalizia kwa
kumuuliza swali. Naya akacheka nakuondoka. Wote wakacheka.
Baba yake akaingia na kufunga mlango wa gari. “Usisahau mkanda baba.” Naya akapiga kelele akiwa nje. “Ndio nafunga mama.” Naya akawapungia mkono kuwaaga, lakini akakumbuka hajamuombea baba yake. Akamfanyia ishara Malon asubiri. “Hapa hatutaondoka leo.” Baba yake akanong’ona. Malon akacheka. Akakimbilia alipokuwa amekaa baba yake. Akafungua mlango kabisa. Zayon naye akawa ameamka. “Mbona kelele Naya?” “Nimesahau kumuombea baba. Njoo na wewe tuombe pamoja.” “Kweli mama.” Naya akamshika mkono baba yake na Zayon pia. Wakawa wameshikana mikono wao watatu Malon akiwatizama kwa kujiiba. Naya akaomba vizuri tu, akamaliza. “Amen.” “Amina mama.” Malon na baba yake Naya wakaitikia kwa pamoja hiyo ‘Amina mama’. Wakaangaliana kidogo, wakarudisha macho kwa Naya akacheka. “Sasa hivi mnaweza kwenda. Kuweni waangalifu barabarani.” “Nitafanya hivyo.” “Nitakupigia baba ili kukuaga vizuri. Nilipitiwa na usingizi.” “Hilo wazo zuri Zayon. Unipigie na baadaye muende kanisani.” “Sawa.” Naya akafunga mlango wa gari, akasogea pembeni. Malon na baba yake wakaondoka Naya akipunga mkono, Zayon ametulia tu pembeni.
Kwa Kina Naya.
M |
aisha ya bila wazazi pale nyumbani kwao ndio yakaanza rasmi mara
tu waliporudi ndani. Tena bila Bale ambaye alikuwa chuoni. Naya akasikia kuumia
sana. Nyumba hiyo iliyokuwa imejaa vurugu ikabaki papweke. Wote walijikuta
wamerudi kukaa hapo kwenye makochi kimya. Yeye na Zayon kila mmoja akiwaza
lake. Naya akaanza kujutia kumshauri baba yake aondoke. Akachukia kukubali
ushauri wa Malon, kumchukua baba yao, lakini akajirudi akikumbuka shida ya pesa
na ile hali ya kuomboleza aliyokuwa nayo baba yao. “Maisha yamebadilika Naya!”
Akaongea kwa kulalamika Zayon. “Ni kweli. Mambo hayatakuwa kama zamani Zayoni.
Kuna ukawaida mpya Mungu atatupa, itabidi kuja kuuzoea tu.” “Baba naye atakuwa
akiishi huko huko?” “Kwa muda tu. Ili kumfanya achangamke. Ila najua hata yeye
hataweza kuwa mbali na sisi. Atarudi na kutafuta kitu chakufanya hapa mjini.”
Zayoni akanyamaza, Naya naye akapotelea mawazoni.
Siku hiyo ya jumapili wote
walienda kanisani kwa kina Malon, kwa ajili ya Zayoni akutane na vijana
wenzake. Hata Bale alifika pale akitokea chuoni. Akawaona wameshuka garini wamepoa.
Akaelewa tu kwa kuwa alitoka kuzungumza na baba yake akamwambia amewaacha
nyumbani peke yao, na yeye arudi nyumbani. Bale akamuahidi baba yake siku hiyo
atakuwa nao na akimaliza mitihani atarudi nyumbani. “Dogo umependeza! Naona
unakula pamba za ukweli!” Bale akamsifia
mdogo wake, angalau Zayon akacheka. “Hizi ni nguo mpya na viatu, ameninunulia
Naya.” “Saafi!” Wakasalimiana na Naya na kuingia kanisani vijana hao wasio na
vingi ila wao tu.
Baada ya ibada, Zayoni akaonekana alipata wakati mzuri. Bale na Naya ikabidi wafikirie swala la kuhamia hapo kwenye hilo kanisa kwa ajili ya Zayoni. Alisimulia mengi wakiwa kwenye gari akimtaka Naya awe anampeleka zaidi hapo. “Wanakuwa na mechi siku za ijumaa na jumamosi.” “Basi kazi zitanishinda.” Naya akajibu, Zayoni akacheka. “Siku za jumamosi mimi nitakuwa nakuleta, ila ijumaa itategemea.” “Asante Bale.” Walienda mahali kula. Naya akiwa mlipaji. Walianza kucheka wakitaniana hili na lile. Angalau ile hali ya majonzi ikapungua siku hiyo.
Safarini.
S |
afari ya Dar kwenda Mbeya ilikuwa ndefu vyakutosha. “Nataka kumuoa
Naya.” Malon akavunja ukimya, baba Naya akamtizama na kumuuliza swali.
“Unafikiri upo tayari?” Malon akatulia kidogo akijua hilo swali lina agenda
nyingi sana nyuma yake. “Sijui natakiwa kufanya nini kabla ya kumuoa? Labda
unisaidie. Lakini sitaki kuendelea kusubiri. Hatuna sababu, wakati najua
tunapendana. Nahisi mengine Mungu atatusaidia mbele ya safari.” Malo
akaendelea. “Najua haikuwa sawa, lakini niliishi na Naya zaidi ya miaka mitatu,
kama mke wangu, vizuri sana. Sidhani kama nitapata mwanamke mwingine
atakayeweza kuishi na mimi kama Naya?” “Unamaanisha kukuvumilia?” Baba Naya akauliza.
Malon akatulia kidogo akijua kwa kuwa Naya anazungumza mengi na baba yake, na
yale mabadiliko aliyoyaona kwa Naya, akaona awe mtulivu kidogo. Afikiri kabla
ya kujibu.
“Umekuwa mtu wakuingia na
kutoka kwenye maisha ya Naya vile utakavyo wewe. Unamuacha akiwa mtu wa kulia na
sononeko kila wakati! Ni nini kimebadilika?” “Nimeokoka. Mungu atanisaidia.”
Malo akajitetea. “Ni juzi tu umetoka safari na mwanamke ambaye sio mkeo, Malon!
Mmekaa huko karibu juma zima! Leo unasema unataka kumuoa Naya!? Ni nini unataka
maishani Malo? Huoni kama utamsumbua sana Naya?” “Kwanza wakati namkubalia Rita
kwenda naye, nilijua Naya alishachumbiwa. Juu ya hiyo safari ni mipango au ni
ombi alilokuwa ameniomba kwa muda mrefu baada ya kufahamiana tu. Aliniomba siku
nikija kwenda Brazil, na yeye angetamani twende naye apafahamu. Wakati huo
alikuwa mgeni tu pale kwangu. Hata hatukuwa tukifahamiana sana. Sikuona sababu
ya kumkatalia.” Malon akaendelea.
“Na nilipofika kule, Mungu
wangu ni shahidi, sijamgusa. Na si kwa sababu ya Naya, ni kwa usalama wangu
mimi mwenyewe. Najua madhara ya maisha niliyoishi zamani. Huko nimekusudia
kutorudi, kwa gharama ya kujikana mwenyewe. Na Rita akimaliza mkataba wake,
itakuwa basi. Nitaikarabati nyumba yangu, nihamie mwenyewe nikimsubiria Naya.”
Baba Naya akamtizama vile alivyo jihakikishia. “Sitarudia maisha ya zamani. Na
sitaki tuendelee kusubiri niwe mkamilifu sana. Naona tunazidi kujichelewesha.”
Baba Naya hakuongeza neno.
“Sasa hivi nipo na wala
sitamuacha tena. Na ni kweli nilirudi kwa ajili yake. Nilikuwa nimekufuata siku
ile nikwambie. Ndio nikaishia mikononi kwa mama.” “Alikuja kujuta. Akitaka
kukiri, lakini nilimkatalia nikiwa sijamuelewa ni nini anataka kufanya. Lakini
alijua amefanya kosa.” “Nia ilikuwa nzuri. Naelewa kabisa. Lakini nampenda
Naya. Nina uhakika mimi naweza kuwa naye na kumfanya akawa na furaha. Na yeye najua
bado ananipenda.” Alivyomalizia hivyo,
baba yake Naya akamtizama. Vile alivyomtizama Malo hakufurahia hata kidogo. Ni
kama aliyemuuliza ‘una uhakika?’ Malon akaingiwa na wasiwasi.
Akaona amchokonoe zaidi ili aongee neno. “Nampenda Naya. Safari hii ukiniruhusu mzee wangu, na kunipa baraka zako, nikirudi tu nataka kumchumbia, taratibu za harusi zianze. Hapa ni wewe tu. Mimi na Naya tupo tayari.” “Umezungumza na Naya mwenyewe?” “Namjua Naya. Yupo tayari. Naomba tu na wewe unisaidie kumtia moyo, tukamilishe hili.” Baba Naya akanyamaza kabisa. Hakuongeza neno jingine hata Malon alipoendelea. Akaona anyamaze asije akaharibu. Safari ikaendelea.
Zilipita siku 10 ngumu na
za haso haswa kwa Malon na baba Naya, wakiwa mkoani Mbeya ila vijijini kwa
wakulima kabisa, mashambani wakikusanya mazao mpaka Malani akakamilisha kiasi
alichokusudia na ndipo walipohamisha hayo mazao sasa kwenye eneo
lililomshangaza sana baba Naya. Kwa hakika Malon alijijenga huko vijijini.
Aliweka eneo maalumu kukusanyia mazao na kuweka vitu vya kisasa. Kazi ya
kusafisha mazao na kuyaandaa kwa kusafirishwa ikaanza hapo kwenye ngome ya
Malon. Walikuwa wakifanya kazi mchana na usiku wakisaidiana bila kuchoka. Malon
alikuwa akichoka, lakini akashangaa nguvu aliyonayo yule baba Naya.
Alikuwa akifanya kazi mchana
na usiku bila kuchoka au kutumwa. Tokea alivyojua ni nini anatakiwa afanye,
hakuwa akisubiri atumwe. Alfajiri alimkuta ameshatoka ameanza kazi akiweka
mazao vizuri ndani ya magunia, na kuyapanga. Alikuwa wa kwanza kuamka, na wa
mwisho kulala. Wakati wote Naya alikuwa kwenye simu na baba yake lakini Malon
akagundua kwake ni kama analazimishia mawasiliano. Naya anayemfahamu yeye,
asingekuwa akisubiri Malon ampigie endapo anajua alipo na wapo kwenye mahusiano
fulani. Lakini ikawa ni shida.
Wakati mwingine akajaribu
kumtega asimtafute asubuhi. Basi hatamsikia Naya hata kutuma ujumbe, ila
kumuona baba yake akisoma jumbe na kujibu au kupokea simu mara kwa mara akawa
anajua ni Naya tu. Lakini akashangaa napo hakuna hata salamu anazopewa na baba
yake kutoka kwa Naya. Malon akajua mambo yamebadilika. Akahisi pengine amepata
mwanaume mwingine. “Lakini mbona hapakuwa na dalili ya mwanaume mwingine!
Namfahamu Naya. Kama kungekuwa na mwanaume mwingine, angesema tu.” Akabaki
akiwaza Malon na kujaribu kuvuta kumbukumbu tokea amuone Naya shuleni kwa mtoto
wa Rita mpaka wanaagana. Akajiuliza hayo mabadiliko ni ya nini!? Siku zikazidi
kwenda, mambo ni yaleyale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment