Muulize dada yako kama mimi nimezungumza na Naya. Ila mimi huwa
ni muwazi na linapokuja swala la Naya, huwa nakosa uvumilivu.” Kimya kikatanda
wote wakamgeukia vizuri Malon aliyekuwa amebanwa na Thia. “Mnakumbuka
nilipofika nyumbani kwenu kwa mara ya kwanza, mlinikaribisha kwa ajili ya
chakula cha usiku mimi na Rita, mama ukaniuliza kama nilishawahi kuoa?” Kimya.
“Mnakumbuka habari au kisa nilichowapa juu ya msichana niliyejaribu kutaka
kumuoa. Mpaka nikanunua pete ya uchumba, nikaenda nyumbani kwao ili nikazungumze
na baba yake kwanza, niombe baraka za kumuoa nikaishia mikononi mwa mama yake. Aliyenifukuza
na kuniomba nisiwahi kurudi kwao, kwa kuwa simstahili mtoto wake?” Kimya. Mpaka
wakina Naya wakashangaa.
“Unakumbuka hata Brazil nilikueleza umbali wa huyo msichana
aliokwenda na mimi kwenye maisha? Kwamba hata uhuru nilionao ni kwa ajili yake,
nashindwa kuoa au kujiingiza kwenye mapenzi kwa hofu yakutoweza kutulia kwenye
mahusiano kwa ajili yake?” Kimya. “Sikuwa nimekutajia jina. Ila ujue tu, hata
sisi wote sasa hivi, tupo hapa kwenye hii nyumba kwa sababu ya Naya.” Wote
wakatoa macho, zaidi Rita.
“Usifikiri Naya ni mgeni wa hii nyumba Rita. Au usidhani ni mjinga
kama unavyomuona anafanya kwako. Niliishi na Naya hapa ndani kama mke wangu kwa
zaidi ya miaka mitatu. Tukilindwa na kutumikiwa kama hivyo wanavyokutumikia
wewe tena na zaidi kwa kuwa Naya alikuwa jukumu langu sikuwahi kutaka hata
kuhisi anashida. Maamuzi yangu mabaya ya maisha zamani, ndiyo yametufikisha
hapa tulipo. Nilipoteza kila kitu. Naya akauza kila kitu ili kunitoa jela,
kasoro hii nyumba aliniachia ili nipate pakuja kuishi. Namfahamu Naya ndani na nje.
Hata ukizungumza sentensi nitajua hiyo ni ya Naya au la. Lakini Rita,
unamsingizia Naya, na sitakuruhusu umchafue kwa sababu zako binafsi.”
“Alichokifanya tokea unamfuata kumuomba akusaidie kukaa na mtoto
wako, ni kukuheshimu japo ulimnyanyasa kwa kumwangalia tu na kumuhisi. Naya
hana shida na sehemu ya kulala. Ni vile humfahamu. Hana shida na pesa uliyompa
kiasi cha kutoa utu wake. Ni vile humfahamu, hiyo zawadi uliyomletea Naya, si
kitu cha kukuvunjia heshima. Hana uroho wa mali hata kidogo. Na ndio maana
alikujazia gari yako mafuta japo hukutaka atumie na wewe ulimuachia gari nusu
tanki. Unaweza ukamuona ni fukara kama unavyomsema, lakini Mungu alimjalia
utajiri wa nafsi. Sitakuruhusu umseme vibaya Naya kwa kumchafua. Na ninakuonya Rita,
usiguse kazi yake ya Cocacola. Amekufanyia kazi yako vizuri, mliachana kwa amani,
mwache na yeye aendelee na maisha yake.” Naya na familia yake walibaki wameduaa,
kimya.
“Samahani sana Mzee wangu. Niombe radhi kwa usumbufu. Naombeni
nyinyi mkapumzike tu. Haya mambo mengine, yatamalizwa tu hapa.” Malon
alimgeukia baba yake Naya. “Asante.” Akajibu baba Naya akimtizama Naya. Naya
akatoa pesa kwenye pochi akaweka pale mezani. “Hii ni pesa yako Rita. Naomba
iwe nilikaa tu na Ethan kwa kujitolea, isiwe kama ni kazi. Naona itakusaidia
kutulia. Huwezi na wala huna uwezo wa kunisaidia Rita dada yangu. Nina mahitaji
mengi ambayo hayatimiziki kwa malipo kama haya wala kwa hiyo kazi unayonitisha
nayo ya Cocacola.” “Usikasirike Naya. Hili ni jasho lako. Chukua hiyo pesa,
usiache.” Nolan akamsihi.
“Hapana Nolan. Nimeumia sana. Nikichukua hiyo pesa, ni
kujifedhehesha sana. Acha tu. Pengine itasaidia hata kulipia bili ya maji
niliyooga na umeme niliotumia.” Akamgeukia baba yake. “Twendeni baba.” Naya
akatangulia baba yake akafuata na kaka zake. Malon akamfuata nyuma.
“Naya!” Malon akaita, Naya akageuka. Baba yake na ndugu zake pia
wakageuka na kusimama wote. “Naombeni msinielewe vibaya. Cha kwanza, sikujua
kama Rita atamuomba Naya kumfanyia kazi. Naya ananijua. Nisingekubali.
Nilimkuta humu ndani akiwa ameshamkubalia Rita, na ndio siku tunakwenda safari.
Na pili, sikujua kama kuna kikao kama hiki. Nisingeruhusu Naya kuja kudhalilika
hapa. Mnisamehe sana.” “Hamna neno Malon.” Akajibu Naya. Malon akabaki
akimwangalia. “Kweli kabisa. Sisi hatuna neno na mtu. Hata Rita sijamchukia,
ila tu nimeelewa moyo wake, basi. Naomba muwe na amani. Usiku mwema.” Naya
akasisitiza.
“Poleni kwa kumpoteza mama.
Sikuwa najua. Rita ndiye aliyeniambia tukiwa safarini. Poleni sana.” “Asante.”
Wote wakaitika, Malon akaona ni kama bado wapo na ule uchungu wa kufiwa na
hapakuwa na nyongeza kati yao. Malon aliondoka akiwa na ahadi yakuleta
mabadiliko makubwa, ndio wanakutana naye hapo na sababu ya kufukuzwa na
marehemu mama Naya. “Usiku mwema Malon. Kesho Zayoni anatakiwa kwenda shule na
anahitajika usingi wakutosha, acha sisi tuwahi.” “Ni kweli.” Naya na familia
yake wakaondoka. Malon alibaki amesimama akiwaangalia.
Naya.
W |
aliondoka hapo
nyumbani kwa Malon kila mmoja akiwa na butwaa, hakuna aliyemuongelesha mwenzie
njia nzima, kimya. “Wewe ulijua kama mama alimfukuza Malon nyumbani?” Naya akavunja
ukimya kwa kumuuliza baba yake wakiwa wanakaribia kufika nyumbani kwao. Baba
yake akanyamaza tu bila yakujibu. “Kwa hiyo ulijua?” Naya akasisitiza swali
lake alipoona kimya. “Nia ya mama yako ilikuwa nzuri Naya.” “Kwa hiyo
ulifahamu?” “Aliniambia wakati amezidiwa sana. Lakini nikahisi anaongea tu
sababu ya maumivu. Kipindi kile alikuwa akikiri na kutubu mambo mengi.” “Kwa
nini hukuniambia wakati wewe unajua jinsi nilivyokuwa nimeumia kutokurudi kwa
Malon? Nilikuwa nakushirikisha kila kitu baba. Lakini..” “Naya mama, sasa hivi
ukinilaumu utakuwa unanionea mwanangu. Wakati ule nilikuwa kwenye wakati mgumu
mama. Nilikuwa nimejawa hofu. Chakula chenyewe nilikuwa sili kwa kufunga ili
Mungu anihurumie amponye mke wangu. Akili ya kufikiri ilikuwa haipo. Unakumbuka
wewe na Bale ndio mlikuwa mnaongoza mambo yote mpaka kwenye msiba?” Naya kimya.
“Nisamehe mama yangu. Halafu sijui sikuwa nimemuelewa vizuri!
Nikahisi ni vile alivyokuwa akimpinga tokea mwanzo, nikahisi ndio anaomba
msamaha. Sikujua kama kipindi kile kama Malon alipotoka Dubai alirudi nyumbani.
Mimi mwenyewe nilikuwa nimemchukia Malon. Nilijua alipokwenda ile safari ya
Dubai akafanikiwa, akakusahau. Nilimchukia sana, wala sikuwa nikitaka kumsikia
tena. Ndio maana nilipokuona na wewe umepata amani kuwa naye mbali, nikaona
tuyaache hayo mambo kama yalivyo. Hata mama yako nilimuomba asije akaanzisha
habari za Malon tena.” “Kwani alitaka kuniambia nini?” Naya akauliza huku akifuta
machozi.
“Nafikiri alitaka kukwambia kuwa Malon hakukukimbia. Nafikiri
kukiri mambo yote. Sina uhakika mama yangu. Sasa kwa kuwa maelezo yake
yalichanganyikana na kilio cha maumivu, sikuelewa vizuri. Hivi leo wakati Malon
alipokuwa akisimulia pale, ndipo nimeelewa alichokuwa akiongea mama yako siku
ile. Mimi nilimkatiza mama yako kwa kumuomba kuwa, akuache kabisa wala asimtaje
tena Malon kwako kwa kuwa sasa hivi umeshakubali kuwa Malon hatakaa akawa
kwenye maisha yako. Nikamwambia kwa wakati ule ukiwa unamuuguza, akikutajia
tena Malon itakuwa ni kukuchanganya. Heri akuache akili iwe pale kwenye kumuuguza.”
Naya akanyamaza.
“Umenisamehe mama?” Baba yake akamuuliza kwa upendo. “Hata mama
pia. Najua nia yake ilikuwa nzuri. Mama alitamani kuniona naishi maisha mazuri
kitu ambacho hata mimi ningekitamani kwa watoto wangu. Sina lawama kwa mtu
baba. Ila natamani kama angekuja kuniona naolewa kama ningepata mwanaume
aliyeridhika naye. Kipindi hiki cha mwisho alikuwa kama ananiandaa. Sasa sijui
kwa ajili ya nyumba yake au yangu!” “Vyote.” Baba yake akajibu. “Nahisi
kweli. Alikuwa anahangaika kuniona naelewa na kuishi vile alivyotaka. Wakati
mwingine alikuwa anaamka na maumivu, anakaa na mimi jikoni, kuhakikisha natoa
wali ulioiva.” Wote wakacheka.
“Na mama alihakikisha mpaka unaweza kupika Naya! Umebadilika!”
Bale akaongeza “Nahisi pia na akili zikakua gafla. Alihakikisha naelewa mambo
ya pale ndani. Kuanzia mambo ya Zayoni kibinafsi mpaka baba. Alitaka akiondoka
mambo mengi yasibadilike. Akaniwekea roho ya umama kwa ajili ya Zayoni.” Wote
wakatulia. Wakamsikia Zayoni analia kwa uchungu sana. Bale aliyekuwa amekaa
naye pale nyuma akaanza kumtuliza.
HATIMAYE.
B |
aada ya
kukata tamaa, hatimaye Naya akaanza kazi kwenye kiwanda hicho cha Soda, upande
wa masoko kama shahada aliyosomea. Akapangiwa kitengo cha matangazo ndani ya
idara hiyo ya masoko. Kazi ikaanza kukiwa na shida ya usafiri kila anapokwenda
kazini na kurudi. Alianza kazi hapo akiwa hana pesa kabisa ila kutumia akiba ya
baba yake kumfanya aweze kuwepo kazini. Pesa hiyohiyo ya baba yake alitumia kwa nauli na chakula cha mchana mara moja moja
sana. Wakati mwingine alishindwa hata kula mchana hapo kazini. Alibakia na
njaa, akisubiria kwenda kula nyumbani akitoka hapo kazini ili kubania pesa
ibakie ya nauli tu. Hakujutia kuacha pesa ya Rita.
Kampuni ilikuwa kubwa na vishawishi vingi vya kuvutia kujipatia
pesa kwa haraka, kwani walikuta walionza kazi hapo na walio ajiriwa kabisa
wanayo pesa haswa. Ukweli walikuwa wakilipwa vizuri haswa kwa waajiriwa kabisa.
Walikuwa na marupurupu mengi sio kama wao walioanza kazi tu na hawakuwa
wamepewa ajira ya kudumu. Vishawishi vikawa vingi kwa wao wageni pale kwenye
kampuni, lakini Naya alijikaza. Na kwa kuwa waliajiriwa wasichana watatu kwa
wakati mmoja. Wakapitishwa kila kitengo ili kufahamu hiyo kampuni, wenzake
hawakuchukua muda mrefu wakapata wanaume ambao walikuwa wafanyakazi wa hapo
muda mrefu tu, lakini si Naya. Naya akajikana nafsi yake.
Akajitenga na vishawishi hata kukaribishwa chakula hakuwa akitaka.
Akiwa hana hela kabisa, na hawezi kutoka kwenda kula mida ya mchana hapo
kazini, alibakia peke yake ofisini wakati wenzake wakienda kula yeye anafanya
kazi. Swala la ofa hapo kwenye hiyo kampuni lilikuwa jambo la kawaida kabisa
lakini Naya hakutaka kulizoea. Baada ya muda mfupi sana wakaanza kumtambua hapo
kazini kama ni msichana mwenye tabia za ajabu. Hapendi kujichanganya na
mshamba. Na ule muonekano wake! Nywele fupi tu, hakuna kipodozi wala hereni.
Uso wa majonzi, kukataa kila ofa na kuchapa sana kazi, wakamuona mshamba wa
kupitiliza. Yeye akaendelea na yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku moja Naya
alirudi nyumbani akashangaa kukuta baba yake anahesabu pesa. Alipoingia tu
akamkabidhi pesa zote. “Za nini!?” “Matumizi ya humu ndani na yako pamoja na
kaka zako. Nimetoa hicho kilio chote huko nje.” Naya akabaki ameduaa,
hajaelewa. Bale akatoka chumbani. “Unashangaa nini sasa na wewe? Baba kauza
ng’ombe wote mpaka ndama.” Naya akatoa macho. Baba yake akasimama na kuingia
chumbani kwake. Naya akatoka kwenda kuhakikisha. Akakuta hakuna hata ndama!
Naya akabaki ameduaa pale mabandani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mwezi wa kwanza alipopokea
mshahara wake wa kwanza, akakumbuka nadhiri yake aliyokuwa ameweka mbele za
Mungu akajiambia lazima kuitimiza. Binti huyo alifundishwa na baba yake
kutoweka nadhiri mbele za Mungu. Akimfundisha kutoweza kununua baraka za Mungu.
Lakini akamwambia endapo ikatokea ameweka nadhiri, nilazima aitimize. Sasa katika
hangaika yake ya muda mrefu bila kazi, Naya akiwa amechoka, alimwambia Mungu
endapo akimkumbuka na kumpa kazi, na akilipwa mshahara wake wa kwanza, atatoa
sadaka ya shukurani asilimia 10 ya huo mshahara, atamnunulia zawadi Malon. Kama
shukurani yakumsomesha. Na zawadi kwa wazazi pia. Sasa mama amekufa, amebaki
Malon na baba yake na hiyo sadaka ya shukurani. Ikabidi kuitimiza tu.
Akaenda kumnunulia Malon saa nzuri ya mkononi na kadi ya shukurani. Akaiandika upande wa juu. “Malon, nachukua nafasi hii ya kipekee kukushukuru kwa kusimama na mimi tokea kidato cha nne mpaka namaliza chuo. Asante kwa kusimama na mimi kwa hali na mali. Asante kunisomesha na kunitunza. Umechangia kunifikisha hapa nilipo. Nakuombea na wewe Mungu akuinulie watu wa kusimama na wewe, kukushika mkono na kukufikisha sehemu ya juu zaidi. Nakuombea ufanikiwe, Malo. Asante.” Akaifunga vizuri akiwa chumbani kwake usiku huo akiwa anafunga hiyo zawadi ya Malon, huku akifikiria ni nini chakumnunulia baba yake ambaye amezira maisha.
Naya Kwa Malon Tena.
S |
iku inayofuata alitoka kazini na kuamua kwenda kuipeleka ile
zawadi ya Malon nyumbani kwake. Alifika getini, hata hakutaka kuingia ndani.
Akamuomba mlinzi atoke nje ya geti, akamkabidhi. “Naomba uhakikishe huu mzigo
unamfikia Malon Saduki yeye mwenyewe.” “Huingii?” Mlinzi akauliza. “Hapana.
Asante. Jioni njema.” Naya akaondoka taratibu akirudi barabarani kutafuta
daladala yakumrudisha nyumbani kwao Kiluvya. Bado giza lilikuwa halijaingia, na
kulikuwa na umbali kidogo kutoka nyumbani kwa Malon mpaka barabarani kwenye
daladala. Upande huo kulikuwa na mahoteli, taksii zilikuwa zikiingia upande huo
kupeleka wateja kwenye hayo mahoteli. Lakini Naya alikusudia kupanda daladala,
hakuwa na hela ya ziada ya kupanda taksii ila kujikimu tu. Akawa anatembea tu
taratibu kuelekea barabarani.
“Naya!” Akasikia mtu akimwita. Akageuka kwa haraka.
“Malon!” Akamuona Malon kando ya pili ya
barabara, ndani ya gari yake. Akatoa tabasamu na kumpungia mkono. Malon
akacheka na kurudisha kupungia mkono, akabaki amesimama wakiangaliana. Malon
ndani ya gari upande mwingine, Naya akimtizama. Akampa ishara ya kumwita. Naya
akakunja uso kidogo. Akajinyoshea kidole kama anayeuliza, ‘Mimi!?’ Akageuka kulia na kushoto. Akajikuta yupo peke
yake upande ule. Akajinyoshea tena kidole akimtazama Malon kama asiyeamini kama
Malon anamwita. Safari hii akauliza kwa ishara, akitaka uhakika kama anayeitwa
ni yeye. Malon akacheka kidogo na kutingisha kichwa kuwa ni yeye, na aende.
Akavuka barabara huku
akiangalia magari yanayopita. Akaenda upande wa dirishani. “Mbona hukuingia
ndani, mama?” “Sikutaka kusumbua. Hata hivyo nimetoka kazini tu, ndio nikaja
hapa. Nawahi nyumbani.” Malon akamwangalia kidogo. “Mzima lakini?” “Mzima.”
Naya akajibu na tabasamu kidogo. “Unaendeleaje Naya?” “Namshukuru Mungu
naendelea. Nilitaka kukushukuru Malon. Niliweka nadhiri mbele za Mungu kuwa
nikilipwa mshahara wa kwanza nikununulie zawadi wewe. Uonje matunda ya jasho
lako.” Wakacheka. “Pamoja na mama na baba. Sasa kwa kuwa mama yeye amefariki,
nitamjengea kaburi, ila baba ndio sijui nitafanyaje?” “Kwa nni tena?” “Aaah!
Sijui Malon. Amebadilika kweli, mpaka nina hamu naye!” Akamuona Naya ameinama
kama anayefikiria.
“Pole.” “Nimepoteza mama na
baba. Lakini uchungu nilio nao ni kama yeye baba ndio amekufa! Amebadilika,
amepoteza hamu ya kila kitu. Kumtoa tu hata kitandani ni kazi kweli! Na kama
mimi sipo ndio kabisa. Hapa Bale atakuwa anasubiri nikamlazimishe kula.
Hajapokea simu zangu tokea asubuhi.” “Kwa nini?” “Basi tu. Hataki kutoka
kitandani. Imebidi kumpigia simu Zayoni aende akamwangalie chumbani kwake,
akasema amemkuta amejilaza tu kitandani anaangalia dari. Amekuwa kama amepoteza
dira na hamu ya kufanya mambo! Anasema alikuwa akifanya kila kitu kwa ajili ya
mama. Ili kumfanya aishi vizuri. Lakini anaumia kuona mama amekufa kabla
hajampa alichokuwa akikitaka au hajatimiza ndoto za mama. Amebadilika sana
baba. Siye yule uliyekuwa ukimfahamu.” “Poleni sana Naya.” “Nashukuru. Anyway, acha mimi
niwahi kurudi
nyumbani kupika.” Malon akacheka.
Naya naye akacheka. “Siku hizi napika
mwenzio. Muda mwingi Bale hayupo pale nyumbani.” “Anakuwa wapi?” “Alichukua
chumba chuoni. Wakati mwingine anakuwa chuoni au anarudi usiku. Na akirudi
anataka kusoma. Kwa hiyo mimi ndio nimekuwa mama. Kufua, kupika na usafi.”
“Unaivisha lakini?” Naya akacheka sana. “Mama
alihakikisha anahamisha ujuzi wake wote kwangu kabla hajaondoka. Siku hizi
mpaka Bale anasifia chakula changu.” “Hongera mama.” “Asante. Na asante sana Malo. Asante sanaaa.
Naamini unanielewa. Asante kwa kunisomesha, asante kwa kunitunza. Asante kwa
kuniamini. Asante kwa kila kitu. Nakushukuru kwa dhati. Sijasahau hali
uliyonikuta nayo siku ya kwanza nikienda kuchukua pesa ya mkopo iliyokuwa
imejaa masimango, kanisani. Nakumbuka uliponitoa kwenye ile hali na kuhakikisha
sidaiwi tena na ninasoma kwa utulivu. Asante.” Naya akashukuru kwa dhati
kutokea moyoni.
“Unafurahia kazi yako?”
Malon akauliza. “Sana. Nafanya kitu nilichosomea. Mazingira mazuri, nahusishwa
kwenye mipango na kiongozi wangu wa idara. Ananiamini sana pale idarani. Haya,
tuna safari ya kikazi ya week moja. Kutangaza bidhaa mpya nje ya hapa Dar. Na
mimi amenichagua nimuwakilishe kwenye hilo kundi tunalokwenda. Kuhakikisha
majukumu yanayotupeleka yote yanafanywa kwa usahihi. Nimefurahi kuona japokuwa
mimi bado ni mgeni, ananiamini na anatambua ufanyaji kazi wangu. Kwa kweli
siwezi kulalamika. Ila tu naona imekuja wakati mbaya.” “Hapana Naya. Huu ndio
wakati sahihi. Mungu alikuwekea maalumu kwa ajili ya wakati huu.” “Unafikiri
hivyo Malo?” “Kabisa. Huu ndio wakati sahihi.” Naya akainama tena akiwa
anamchungulia kwenye gari.
“Umeona nimevaa saa yangu?”
Naya akamtizama mkononi na kucheka. “Umeipenda?” “Sana. Asante kushukuru, mama.
Naona katika wote niliowahi kuwasaidia, wewe tu ndio unakumbuka.” Naya akacheka
taratibu. “Watakuwa wanakumbuka ila mambo ni mengi wanashindwa kukwambia.”
Malon akaguna na kucheka kama anayejikejeli. “Kweli Malo. Umesaidia wengi.
Umesomesha wengi sana. Mimi nawakilisha hao wengi. Tunakushukuru.” “Asante
kushukuru.” Naya akainama, Malon alikuwa akimwangalia.
“Unadhoofu Naya! Unakula
lakini?” “Nahisi mawazo tu. Ila nakula sana tu na ninapata muda mwingi
wakupumzika. Siku hizi hatufugi kitu chochote. Kwa hiyo tukimaliza kazi za pale
ndani, ni kukaa tu.” “Baba aliuza kila kitu?!” “Mifugo yote, kila mnyama pale
kwetu kasoro sisi tu.” Wakacheka. “Nakuwa na hamu naye sana. Yaani nakuwa na
hamu naye wakati yupo hapo hapo!” Naya akalalamika. “Tuliambiana na Bale tumpe
muda wakuomboleza, lakini naona wala hapati nafuu ndio anazidi kunyong’onyea.
Hivi naandaa mazingira ya kumuomba tusafiri naye. Kwa kuwa wananilipia chumba
hotelini, nataka nimuombe tusafiri naye. Nimuombe anisindikize. Angalau atoke
pale nyumbani labda itamsaidia.” Malon akazima gari akashuka. Naya alimpisha
pale mlangoni.
“Njoo.” Naya akamwangalia,
nakusita kumsogelea. Alijua anataka kumkumbatia. Akainama. “Sijawahi kulala na Rita.
Bado nimeokoka Naya.” Naya akamwangalia na kukunja uso. “Hakuna kilichotokea
hata safarini. Na unanijua mimi huwa sikudanganyi. Ni heri niseme ukweli niingie
matatizoni kwako, kuliko kukudanganya.” Naya akabaki tu kimya.
“Katika mazungumzo yetu
siku moja nilimwambia nakwenda Brazil kuwaona watu ambao wananiletea sukari.
Maana ile biashara ni kweli imekua. Mungu alinisaidia na kunipa wazo la
kuzungusha, nazungusha nchi mbili. Turudi kwa Rita. Akasema na yeye angependa
kuona Brazil, akataka tuongozane. Sikuwa na sababu ya kukataa. Ila mimi
nilipanga nikifika kule, pia nitembelee mpaka wakulima. Ili tu kujua na kuona
mashamba yao. Na nikawa nimezungumza na huyo anayeniuzia hiyo sukari,
aniandalie safari. Uzuri ni baba au babu mtumzima sana. Yeye ndio mmiliki wa
hayo mashamba pia. Ana nyumba pia huko mashambani. Akanikubalia. Tena Mungu
alifanya kitu ambacho nikashangaa. Hata sikulipia garama za hoteli. Akatukaribisha
kwake siku tuliyofika. Nikisema kwake, namaanisha nyumbani kwake kwa familia
yake. Ni Mzee aliyefanikiwa, lakini anaisha maisha ya kijamaa sana. Ana mke
wake hapo mjini. Siku inayofuata, tukamuacha Rita hapo mjini, mimi na yeye
tukaelekea huko kwenye mashamba yake.” Akamuona
Malo anacheka.
“Nipazuri Naya. Nilitamani
uwepo. Nilikupigia picha nyingi, utapaona. Pazuri sana. Jinsi anavyofanya kazi,
lile eneo lenyewe! Pazuri mno. Nilipata wakati mzuri ambao hata sikutegemea.
Nikajiambia lazima nije kukupeleka.” Naya akacheka. “Sasa kwa nini hukwenda na Rita?”
“Cha kwanza niliona sio sawa kwake. Alikuwa yupo mapumzikoni. Ametumia pesa
yake kusafiri. Sikutaka kumpeleka sehemu nisiyoijua, tena mashambani, wakati
pale tulipewa sehemu nzuri sana. Huyo Mzee ananyumba nzuri Naya! Ungefurahia.
Halafu mkewe ni mkarimu japo hajui sana kuzungumza kingereza. Ila mkarimu.
Nikaona ni heri Rita abaki naye azunguke na kupaona Brazil. Halafu pia sikutaka
kujijaribu. Rita alikuwa na matarajio fulani kwenye ile safari. Sikutaka
kujishawishi. Nikaona maneno na vitendo viende pamoja. Nafikiri ndio maana
alirudi akiwa na hasira kidogo.”
“Anyway, lakini nilitaka
kukuhakikishia bado nimesimama kwa Mungu, sijabadilika. Nakiri nipo hapa kwa
msaada wake Mungu. Nilifikishwa chini, chini sana. Sio akili yangu
iliyonifikisha hapa. Ni Mungu mwenyewe. Sina jeuri yakutoka kwake, kwa kuwa
nimepitishwa mahali nikajiona mimi si kitu. Sina kimbilio au wakumtegemea kwa
hakika ila yeye tu.” Malo akajicheka.
“Nilipoteza kila kitu na
kila mtu Naya. Wewe ni shahidi. Kila kitu! Mungu amekuja kuniokoa, sio nikiwa
nimekaa. Amenitoa chini, kijiweni, nikiwa nimeishiwa na nina mapepo. Niligonga
mwamba. Nikauzunguka huu mji kwa miguu, sio hata daladala nikiwa sina kitu.
Kitendo chakunirudisha ndani ya gari na kitandani wakati nilikuwa nakesha macho
na bunduki mkononi usiku kucha nikilinda majumba ya watu, kutoka katika
kulindwa, nikapokonywa kila kitu, hakika sitarudi nyuma, Naya. Nimelipiwa
garama kubwa sana kuwa hivi nilivyo hapa sasa hivi. Uhuru wangu umekugarimu
wewe na Mungu wangu. Narudije kirahisi kule nilikotoka? Tena nikiwa
nimefikishwa na tamaa za wanawake tu? Maana rafiki wote walinigeuka sababu ya
umalaya. Kulala na wanawake zao, mpaka wake zao! Sasa nirudi tena huko!? Hapana
mama. Naona huku kwa Yesu nipo salama zaidi. Nimekusudia kutulia tu na
nikimuomba Mungu aniwezeshe.” Naya akacheka taratibu kama anayefikiria.
Kisha akaona awe muungwana
t. “Hongera.” “Asante.” Wakatulia kidogo kila mtu akifikiria lake. “Unafikiri
baba atakubali nikimwambia twende naye Mbeya kule ninakokusanya mchele na kokoa
kwa wakulima?” Naya akabaki kimya kama ambaye anafikiria kitu. “Au itakuwa
vibaya?” “Amebadilika sana baba. Sio yule uliyekuwa ukimfahamu, mchapakazi.
Amepoteza ladha ya kila kitu. Alikuwa ananiambia haoni tena sababu kwa kuwa
alikuwa akihangaika zaidi kwa ajili ya mama. Anaumia kuona mama amekufa akiwa hajampa
maisha mazuri.” “Lakini mbona mlikuwa mkiishi maisha mazuri tokea mwanzo,
Naya?” Naya akafikiria.
“Kuna jinsi mama alikuwa
akilalamika, Malo. Hata kitendo cha kunikatalia mimi nisiolewe na wewe, alikuwa
akisema hataki nije kuishia kama yeye. Akimaanisha na yeye aliishia na mwanaume
wa aina kama yako. Sasa yale maneno yalikuwa yakimuingia na kumuuma sana baba
ndio maana ulikuwa ukimuona anapambana muda wote ili kutafuta pesa, kumridhisha
mama angalau amsikie hata mara moja halalamikii maisha yake. Sasa kila baba
alivyokuwa akijitahidi, nafikiri mama hakuwahi kuridhika au kumuonyesha
amefanya vizuri, wakati baba alikuwa akifanya zaidi ya uwezo wake. Nafikiri
unakumbuka wakati wote au mara nyingi ulikuwa ukitukuta na baba bandani?”
“Nakumbuka.” Malon akajibu.
“Basi kumbe vile baba
alikuwa anapambana ili kumridhisha tu mama. Sasa mama alipoanza kuugua
mfululizo, hofu ikamwingia baba. Akaanza kufunga akimsihi Mungu asimchukue mama
kabla hajarudia hali yake ya kiuchumi ya zamani wakati tu wameona, baba akiwa
na pesa. Nafikiri, sina uhakika, nikutaka kumuhakikishia mama kuwa hata
biashara huwa zinalipa. Sasa sijui alikuwa akifanya kwa ajili yangu pia ili
kumfungua mama na kuniacha niwe huru, ili niolewe na yeyote ninayemtaka, sijui!
Lakini Malo, ungemuonea huruma baba jinsi alivyokuwa akiomba. Ila mimi
nilimwambia Bale, baba ameingiwa na hofu. Ni kama alijua, au nafikiri
walimwambia hospitalini kuwa mama hawezi kupona.” “Kwani aliugua sana?” Malon
akauliza.
“Yaani Malon, alianza kama
utani tu! Tunakuja kugundua kama ana kansa, imeshamla mapafu yote, yupo stage
4. Na hiyo ni ndani ya mwaka mmoja. Alianza vichomi. Akapuuza, na kupunguza
kazi. Baba akaja kumlazimisha kwenda hospitalini. Wakasema ni nimonia. Akaanza
dawa. Akatulia kidogo tu, vichomi vikarudi. Kupigwa xray, akaambiwa mapafu yana
maji mengi inabidi kufyozwa. Akafyozwa mara mbili. Wakasema yupo sawa. Sijui
akapata vipi infection, hatujui. Kuja kugutuka, ziwa la kushoto linatoa usaha.
Ndio wakaamua kumfanyia upasuaji. Wanasema walipompasua huko ndani wakakuta
ameharibika kuliko vipimo vilivyoonyesha. Hata kutoka chumba cha upasuji
walisema ni muujiza. Akakaa hospitalini kama mwezi, kidonda kinazidi kuoza.
Wakaendelea na matibabu, ndio akafariki.”
“Ingia kwenye gari twende.”
“Kweli? Maana ni kama ulikuwa umepumzika. Sitaki ujio wangu uwe usumbufu na
ndio maana uliona niliacha mzigo getini. Mimi nitafika tu nyumbani. Usijali.”
“Hamna neno. Twende tu. Hata hivyo kuna mahali nataka kwenda. Kwa hiyo twende
tu. Nitaunganisha na safari yangu baada ya kukushusha.” “Hapo sawa. Asante.
Nashukuru.” “Karibu.” Akazunguka upande wa pili, akamfungulia mlango. Naya
akapanda. Wakaondoka.
“Naona mambo yako safi
Malon! Umenunua gari aina ile ile!” “Nilikuwa nalipenda sana lile gari.
Nilijiambia Mungu akirudisha tu pesa mikononi mwangu, lazima ninunue tena aina
ile gari. Ndio nikaona ninunue la silver.” Naya akacheka huku akiangaza macho
humo ndani ya gari.
“Hongera. Naona umerudia na
hali yako.” “Ni Mungu mama. Na maneno yako yalinitia nguvu. Unajua ninayo ile
barua uliyoniachia siku ile na simu, pamoja na maandazi?” Naya alicheka sana.
“Kweli!?” “Kweli ninavyo mpaka leo. Tena nimeipiga na picha. Naisoma kila
wakati ninapoona nakata tamaa au nikikutana na kitu kigumu. Naisoma,
najikumbusha mimi ni nani, naendelea.” Naya akacheka kidogo.
“Lakini hata mimi
umenisaidia Malo. Uliniamini kupita mtu yeyote yule. Imenijengea imani kwenye
maamuzi yangu na ndoto zangu. Hata kama hazijatimia, najiambia ni za msingi,
ipo siku zitakuja kutimia tu. Natunza, nikijiambia ipo siku zitatimia.” “Mama,
aliniambia mlitoka na Joshi kwenda kutambulishwa ukweni.” Naya akacheka. Akajua
na hilo lilimfanya Malo kukasirika zaidi ya maneno ya mama yake. “Ni kweli
tulitoka Malo. Alikuja kuniomba msamaha mbele ya mama, kama kusudi tu. Tena
mara zote mbili, akitaka twende naye mara ya kwanza kwenye shuguli ya kiofisi
mara ya pili nyumbani kwa dada yake, mdogo wake yule tuliyekuwa tukisoma naye,
alikuwa akilipiwa mahari. Anyaway, lakini mimi sikuwa nataka kwenda Malo.” “Kwa
nini?” Malo akauliza.
“Nilijua hakuna maisha kati
yangu na Joshi. Kuna jinsi Joshi alikuwa akinidharau, nilikuwa nikiisikia mpaka
rohoni! Hata hiyo siku tuliyoenda kwenye shuguli ya ofisini kwao, nilipendeza
Malo, mpaka mwenyewe nilijua.” Malo akacheka. “Kama kawaida yako?” “Haswa! Na
kila mtu akanisifia, kasoro yeye. Njia nzima ananisema jinsi nilivyovaa.” “Anasemaje
sasa? Hakupenda nguo?” “Analalamika kuwa ni kama nili over dress. Yaani nimevaa
kama niliyekamia nikaonekanae huko. Nimefika ukumbini, amenuna, hata haongei na
mimi na wala hakunikaribisha hata kinywaji!” “Haiwezekani Naya!” “Kweli Malo.
Mpaka kaka Mati nafikiri akajua. Akaja kunitoa pale, tukacheza wote. Nilikuwa
nimevaa ile set yote ya dhahabu uliyokuwa umeninunulia. Kumbe anasema
alishaviona ukiwa umevishika, kimoja kimoja ukimwambia ni zawadi ya mtu, ila
unachangisha pesa ili ukamilishe. Akasema ni kama akapata bahati ya kukutana na
wewe ukiwa umeshika kila kimoja wapo kwa wakati tofauti tofauti.” Malon
akajaribu kukumbuka.
Naya akamuona anacheka.
“Halafu kweli bwana. Sasa ikawaje?” “Ndio akanibana nimwambie ukweli nilipotoa.
Ndio nikamwambia ukweli kuwa nimepewa na Malo. Akaniuliza kwa wakati ule nipo
na nani? Wewe au Joshi. Na kama Joshi anajua kama wewe unanipa vitu? Mimi
nikamjibu kwa kifupi tu, lakini nikajua kaka Mati ni mtu mzima, msomi, tena
sheria, nikajua atapata majibu.” “Ulimjibu nini sasa?” Naya akanyamaza kama anafikiria.
Akamuona anafuta machozi kwa haraka. Akatulia.
“Wakati ule unakumbuka
uliniacha kwa upendo sana! Nikiwa natumaini utarudi Malo. Uliniacha kukiwa
natumaini kubwa.” “Nilirudi Naya. Mungu wangu nishahidi nilirudi. Tena nilirudi
na pete, mama. Nilikuacha na Joshi ambaye nilimuona hana uwezo wa kukutunza.
Nikajiambia hakustahili hata kidogo. Siku nimerudi kwenu, ilikuwa nizungumze na
baba yako, niombe baraka zake, nikijua baba akikubali tu, nimekupata na wewe.
Lakini Naya, mama! Ilikuwa ni kama nimeenda kuchapwa makofi ya usoni. Nilimkuta
mama anafua pale nje. Oooh! Ilikuwa mbaya sana. Nilijua mama hakuwa
akinikubali, lakini si kwa kiasi kile. Alijifunua kwa mapana, bila jazba, wala
matusi. Kwa hekima kubwa, akimlinda binti yake. Akanisihi sana nikuache na
nisikuchanganye. Akasema mmefikia pazuri sana na Joshi, anaomba nisiingilie.
Nakuwa ni kama nakuvuruga.” Naya akaumia sana.
“Natamani ungeniambia Malo!”
“Nilikuwa nimeumia sana Naya! Niliumia sana. Nikaona haina sababu kwa kuwa hata
muda huo mimi nakufuata na pete kumbe naambiwa mwenzangu ulikwenda ukweni
kutambulishwa! Nilikaa siku tatu sipati usingizi.” “Katika yote, najua mama alikuwa na nia nzuri.
Alifanya kwa upendo akinitakia mema, japokuwa baba anasema ni kama alikuja
kukiri akitaka kuomba msamaha, lakini baba hakuwa amemuelewa vizuri. Alikufa
akiwa kwenye maumivu makali sana. Muda mwingi alikuwa akilia. Wakati mwingine
tulikuwa tunahisi ni kama anachanganyikiwa. Anaongea mambo ambayo hayaeleweki.
Sasa alipomwambia baba, alikuwa akilia maumivu pia, huku akitaka aje azungumze
na mimi. Sasa hapo baba akamkatalia, kwa kuwa ndio ni kama na mimi nikawa
nimeshakubaliana na wazo lakutokuja kuwa na wewe tena. Maana nilikuwa na hali
mbaya Malon! Karibu kuchanganyikiwa kwa maumivu ya kuniacha kikatili vile.”
“Nilirudi Naya.” Malon akawa kama anajitetea.
“Baba alihangaika sana
kunirudisha kwenye hali ya kawaida hata kuweza kurudi kukaa hivi na kuweza
kuwaza jambo la kawaida. Nikawa kama mgonjwa huku mama naye amenichukia
kumkataa Joshi! Kwa hakika nilikuwa na hali mbaya sana. Lakini baba alisimama
na mimi mpaka nilikuwa nikimuhurumia! Alikuwa akiniombea bila kuchoka huku akinijenga
kwa maneno na kunikumbusha safari niliyopita na wewe, niitumie kama fundisho
kwenye maisha. Chochote kilicho kizuri, nikibebe na kukitumia. Kilicho kibaya,
nihesabu kama ni shule niliyopitishwa, na lazima nikubali kuhitimu ili nisije
rudi tena hapo. Ikaendelea hivyo mpaka nikaafikiana na ile hali kuwa ndio
umeondoka, hutarudi tena. Nikatulia. Sasa mama aliposema anataka kuja kuniomba
tena msamaha juu yako, baba akaona atanichanganya zaidi. Halafu hakuwa amejua
kama alikufukuza. Wote tulijua hukurudi.” “Nilirudi Naya. Nilirudi na pete!”
“Mama hakusema, japo alijua nilikuwa nakusubiri sana.” Wakatulia kidogo.
“Anyways, kile kitendo cha
kucheza na Mati, nafikiri kikamuudhi zaidi Joshi, na yeye akataka kujua ni wapi
nilipata zile cheni na hereni baada yakumuona kaka mati amezishika tukiwa
tunacheza nafikiri hapo ndipo alipoziona na kuibua maswali. Akasema tuondoke.
Hapo njaa inauma, ukumbi mzima unanukia harufu ya chakula kizuri. Joshi
amekasirika, anasema tutoke anawahi kwenda kulala.” “Anawazimu!?” “Sijui. Haya
tukatoka akiwa ametangulia. Tumefika nje, akanivuta kwa hasira anataka kujua
ukweli. Nilikasirika Malo, nikajiambia ananidharau kupita kiasi. Nilichofanya
nikuvua viatu mbele yake, nikaondoka kwenda kutafuta daladala kunirudisha
nyumbani.” “Naya! hakukufuata?”
“Hapana Malo. Na wala
hakutaka kujua kama nilifika nyumbani salama. Baba na Bale walichukia sana,
mimi sikujua. Mama akamtetea.” “Haiwezekani!” “Kweli. Mama shida yake ilikuwa
niolewe na msomi, kwa garama yeyote ile. Basi. Hiyo siku ikaisha, eti akaja kutokea
baadaye ananiomba tena twende naye kesho yake siku ya jumamosi huko kwenye
kulipiwa mahari, ili akanitambulishe kwa ndugu zake! Hapo amenifuata nyumbani
mbele ya mama. Acha mama afurahi. Akakubali hapo hapo. Sasa vile alivyojirudi,
nikajua ni kaka Mati tu. Sio Joshi. Nikasita kwenda.” “Lakini ulikwenda Naya.”
“Mama alikuwa anamtuhumu baba. Anamwambia yeye ndiye ananifanya mimi nisimkubali
Joshi. Nyumba ilikosa amani Malo! Baba akawa ndio analaumiwa.” “Kwa nini sasa?”
“Mambo mengi. Aliona jinsi baba alivyosimama na mimi kipindi kile wewe
umefungwa. Halafu baba usimuone kimya vile, yupo so observant. Makini mno. Kwa
kukuangalia tu, anajua kama mtu ananipenda au la. Ndio maana alikupenda sana
wewe. Alijua unanipenda. Sasa huo upendo kwako, hajawahi kuonyesha kwa kijana
yeyeyote yule aliyeonyesha nia ya kutaka kunioa. Ndio mama akawa analaumu.”
Naya akatulia.
“Sasa ikawaje?” “Nilipoona lawama zinazidi kwa baba, hata Bale akaniambia niende tu ili kuwe na amani mle ndani. Haya. Tukaenda hiyo siku ya jumamosi ambayo wewe ulikuja, ukanikosa. Lakini Malo, mtu ambaye hamuendani, wala haiitaji malaika ashuke akwambie. Na hata ukilazimishia, utakuja kuona madhara zaidi baadaye. Nikamwangalia Joshi na mimi. Jinsi alivyo kwangu na mbele ya watu wengine, ni watu wawili tofauti! Kwangu anakuwa mkatili, hanijali, sio kama anavyojionyesha mbele za watu. Kwenye jamii yao, anaheshimika sana. Sifa zake ziko kwa kila ndugu, lakini sivyo ninavyomfahamu mimi Joshi. Nikajiambia akija kuwa mume wangu, akinitesa, sitakuwa na kimbilio. Nitaonekana mimi nina tatizo. Ndugu zake walionekana watu wa kawaida tu. Hawana neno, ila wanamatarajio makubwa sana kwa Joshi na huyo mke mtarajiwa.”
“Nikajiangalia vile jinsi
mimi nilivyo, nilikotoka na mipango yangu, nikajiambia sina sababu
yakujidanganya. Akanichukulia taksii kunirudisha nyumbani, aka…” “Subiri kwanza
Naya. Hakukurudisha mwenyewe?” “Hapana Malo. Alisema amepata dharula, kuna sehemu
anatakiwa kwenda, tutawasiliana baadaye. Akanipandisha kwenye taksii, akamlipa
mwenye taksi, nikaondoka.” “Naya!” “Lakini sikujali Malo. Akili zangu zilikuwa
kwako tu. Nasubiria simu yako, huku nikijiambia Malo wangu akirudi hiki na kile
kitatokea.” “Pole mama.” Naya akajicheka kwa kujidharau.
“Ila usiku huo akapiga simu
kuhakikisha kama nimefika salama. Hilo akawa muungwana. Lakini alishanikinahi,
niliporudi tu, nikamtoa baba pale ndani. Tukajidai tunaenda kuwapa kuku maji,
kumbe tunaenda kuteta. Nikamuelezea baba kila kitu. Sasa eti kesho yake tupo
kanisani, ananijia na makaratasi ya scholarship za nchi gani sijui! Za huko
Ulaya, eti anataka nikasome! Sasa kasumba yake ile yakulazimishia mambo na
kunidharau. Akaanza kuponda masomo niliyosomea, akajidai ananisaidia. Acha Bale
amjie juu mbele ya kila mtu.” “Naya!” “Weee! Usimuone Bale mpole kwako. Mkali
yule. Alimgombesha na kumshushua palepale. Mimi nilikuwa nimeshamkabidhi
makaratasi yote baba tokea mwanzo.” “Kama nakuona ukakimbilia mgongoni.” Naya
akacheka sana bila kujibu hilo.
“Mama aliyachukua kutoka
kwa baba, akasoma na kuanza kuhamasika. Baba naona akaona ni ujinga ule. Hapo
hapo akayachukua yale makaratasi kutoka kwa mama, baba akamrudishia makaratasi
yake yote na kumwambia siku aliyoniacha katikati ya mji, akiwa amenitoa
nyumbani, alifanya kosa kubwa sana. Na mimi hapohapo nikapata mwanya.
Nikamwambia sitaki kwenda kusoma popote na simtaki tena na yeye. Akaondoka na
karatasi zake asiamini jeuri yule.” “Mama alisemaje?” “Mbona hatukaa ibadani
siku ile? Kwanza Bale alimgombesha na mama. Halafu akaondoka bila kuingia
kanisani. Haya, mimi na baba tukasema tuingie kanisani, Zayoni akaja kututoa
kanisani, kuwa mama anasema turudi nyumbani. Mbona tulikoma!” “Kwa nini?” Naya
akacheka.
“Yaani mama! Alilalamika
zaidi ya miezi miwili.” “Anasemaje?” “Ametukasirikia mimi, baba na Bale kipenzi
chake. Hatumsikilizi, tunamdharau yeye. Basi mtu akawa Zayoni tu. Ndio kipenzi
cha mama na ndio mwema. Anazungumza na Zayoni tu ambaye anamsikiliza. Halafu
ikageuka kuwa msaada bwana.” “Kwa nini?” “Akaanza kunifundisha kazi kwa hasira.
Akanitoa kwenye kazi za nje kule kwa baba. Akasema zile kazi ndizo zinanifanya
nisijitambue kuwa mimi ni mwanamke, nakwepa majukumu kama mwanamke. Nikaanza
kazi za ndani kwa nguvu. Chakula nikipika kama hajapenda yeye, anamwaga hata
saa nne usiku narudi jikoni naanza kupika upya. Mpaka nikaweza.” Malon alikuwa
anacheka sana kila akikumbuka Naya na jikoni.
“Lakini amekusaidia.”
“Sana. Mbona nashukuru. Tulikuja kupatana alipoanza kuumwa. Mimi ndio nikawa
mtu wake wakaribu sasa. Ananiachia maagizo ya mtoto wake Zayoni. Ananisihi kwa
hili na lile juu ya Zayoni. Mama amekufa akimlilia Zayoni!” “Daah!” “Alikuwa akilia
anamwacha mtoto wake bado mdogo.” “Lakini Zayoni ni mkubwa!” “Sio kwa mama.
Hajawahi kukua yule. Nakwambia mama anakufa, anaacha wosia juu ya Zayoni.
Kipindi cha mwisho na yeye alikuwa akimuomba Mungu amuongezee miaka kwa ajili
ya Zayoni. Angalau amsogeze. Lakini ndio hivyo.” Naya akanyamaza. “Pole sana
mama. Pole.” Wakatulia kidogo.
“Umefikiriaje juu ya wazo
langu?” “Lipi?” “Juu ya kuongozana na baba. Naona kama itamsaidia akitoka kwenye
yale mazingira. Na pengine akiondoka ujaribu kubadilisha chumbani kwao hata
kidogo.” Naya akamwangalia. “Anaweza kukasirika, lakini itamsaidia. Zungumza na
Bale, uone na yeye atasemaje?” Naya akanyamaza. “Naya?” “Nafikiria jinsi ulivyo
Malon!” “Nini tena?” “Huwa unarudi na mipango mizuri, halafu unaniacha
katikati.” “Nilirudi Naya. Nilirudi mama.” Naya akanyamaza.
“Naomba hilo
ulikubali. Najua umeshazoea kuwa na Malon mkosaji. Ambaye huwa anakosa au
kuharibu. Lakini sio mimi sasa hivi Naya. Nimebadilika. Na nimevuna malipo kwa
niliyoyafanya. Tena nimevuna kwa garama ya kukuacha wewe kwa mwanaume mwingine.
Hilo lilinilaza macho Naya. Ilikuwa bora walivyokimbia na mali zangu, kuliko
kujua upo na mwanaume mwingine ambaye hakufai, na unaweza kuolewa naye hivyohivyo
kwa mimi kushindwa kusimama kwenye nafasi yangu. Na hilo ndilo lilikuwa
likiniuma sana. Niliporudi na kukuta Joshi anakunyanyasa, hajui wala kuelewa
thamani yako, nikajua ninayo nafasi. Nilirudi Naya.” Naya kimya akiwaza
akionyesha wazi hajaridhika, akabaki kimya macho nje ya gari amejishika shavu.
“Naya?” Malon akauliza
wakiwa wameshafika karibu na kwao. “Unanisikiliza?” “Nimekusikia.” “Unaniamini
kama nilirudi?” “Nimejua kama ulirudi.” “Kwa ajili yako Naya. Wala si kwa
sababu nyingine. Naomba hilo ulikubali na uamini.” “Nitazungumza na Bale. Naona
wazo ni zuri. Itamsaidia.” Malon akaingia mpaka njia yakuelekea nyumbani kwa
kina Naya, kisha akaegesha gari pembeni. Akashuka ndani ya gari akaenda upande
wake. Naya hakujua ni nini anafanya.
Akafungua mlango. Kabla
hajamgusa, Naya akajifungua mkanda wa gari na kushuka garini tena akimpita kama
asiyetaka amguse kabisa. “Nilirudi Naya. Nilirudi mama. Nilirudi kwa ajili
yako. Naomba hilo liingie kichwani mwako.” Naya akaanza kulia kwa uchungu sana.
Alilia kama ndio ameambiwa mama yake amekufa. Malon akamvuta karibu akataka kumkumbatia
lakini isivyo kawaida mpaka Malon akashangaa Naya akajisogeza pembeni kabisa
hakutaka ambusu. “Nilirudi Naya. Ila sikukutafuta tena kwa sababu mama yako
aliniomba. Alinisihi sana nikuache. Akiniambia upo kwenye wakati mzuri na Joshi.
Na ningejua kama mama ni mgonjwa, ningekuja kukusaidia kumuuguza, nisingekuacha
peke yako. Lakini sasa hivi nipo. Nataka kusaidia.” Naya akajaribu kutulia,
Malon akajua ameridhika kumbe Naya hakutaka kurudi kwao akiwa na majonzi.
Walitulia vile kwa muda
Naya akiwa anajaribu kutulia. Akajituliza mpaka akatulia mwenyewe.
“Nakaribishwa nyumbani? Naweza kukusogeza mpaka nyumbani.” Malon akauliza
alipoona Naya ametulia. “Mazingira siyo mazuri. Huwezi jua tukienda sasa hivi tutakutana
na nini. Acha tu mimi niwahi.” “Basi naweza kuja kesho mkiwa nyinyi wote hampo
ili kuweza kupata muda naye. Najua itamsaidia. Anatakiwa aondoe mawazo yake
pale kwa muda. Na akikubali tu, ndio itakuwa mwanzo wake mzuri wa kufanya
maisha yake yaendelee bila mama.” Naya
hakujibu, akabaki kimya kama anayeshindwa hata kumkaribisha nyumbani kwao tena.
“Usiku mwema Malon.” Bila yakusubiri jibu Naya akaondoka.
Alifika nyumbani akamkuta
Bale na mdogo wake mezani wanasoma. “Baba yuko wapi?” “Amesema anawahi kulala
leo.” Bale akajibu. “Amekula?” “Amekula.” Naya akapitiliza chumbani kwa baba
yake. “Baba!” “Ingia.” Akaingia. Naya akaenda kupiga magoti pembeni ya
kitanda cha baba yake. Akanyamaza bila hata kuwasha taa. Baba yake alipoona
kimya akawasha taa akiwa hapohapo kitandani. Akamuona Naya analia. “Ni nini
tena?” “Nina hamu na wewe baba! Maisha yangu yamebadilika. Hunisubiri
tena! Huzungumzi na mimi! Hujui linaloendelea kwenye maisha yangu! Nakuwa kama
nimefiwa na wazazi wote?” “Najua kila kinachoendelea kwenye maisha yako.” “Wewe
unajua kama juzi nimelipwa mshahara?” Baba yake akacheka akiwa
amelala palepale amelala.
“Nimelipwa mshahara wangu
wa kwanza, mwenzio.” “Hongera mama.” “Lakini nipo mkiwa. Unamaliza lini
kuomboleza?” Baba yake akanyamaza. “Zayoni anakuwa
amempoteza mama na wewe! Mwanzoni nilielewa, lakini siku zinazidi kwenda,
hatumalizi msiba!? Hivi unajua hata mimi na Bale tumefiwa? Bale hajapata hata
muda wakuomboleza! Anahangaika mambo ya shule na wewe. Anawasiwasi sana na
wewe. Tumekuwa kama tumepoteza wazazi wote, tupo peke yetu.” Naya
akaendelea kulia. Bale na Zayoni wakaingia. Wakakaa hapo kitandani.
“Mimi baba natamani hata
nikisoma, niwe kama wewe.” Bale akaanza. “Umekuwa mtu wa familia. Nimekuwa
nikikuona jinsi unavyohangaika na sisi. Hiyo imenisaidia sana kuepuka makundi
mabaya na kunifanya nikae nyumbani muda mwingi, kwa sababu nimekuwa nikikuangalia
wewe. Kazi na mambo ya hapa nyumbani. Sikuoni kama mtu uliyeshindwa maisha.
Najivunia sana wewe. Hata kama nilikuwa karibu sana na mama, lakini nilikuwa
nikikuangalia kwa karibu sana.” Akaongea Bale. “Mimi ninahamu na mama.
Uchungu hauishi!” Zayoni akaanza kulia.
“Mimi najua pengo la mama
itachukua muda kuzibika, kwa kuwa tulijizoesha kuwa humu ndani sisi tu watano.
Na muda mwingi tumekuwa tukizunguka pamoja. Itatuchukua muda kuzoea. Lakini
kama tukikubali hii hali mapema, itatusaidia kuendelea vile mama alivyotaka.
Wote tunajua mama alitaka tusome sana. Lakini Zayoni, unaanza kufeli wakati
ulikuwa unakuwa wakwanza darasani kila wakati! Mama alikuwa anakusifia sana.
Naomba umuenzi mama kwa kuwa kile alichokitarajia. Kila ukimkumbuka, naomba
ufanye kitu unachojua hata angekuwepo, angekifurahia.” Naya akaongea jambo
lililomtuliza Zayoni.
“Mimi naomba nikuombe kitu
baba.” Bale akapokea. “Najua unauchungu wakutofika pale mama ulipotamani akuone
umefika. Pole. Lakini naomba unisaidie na mimi nifike hapo. Nisaidie baba
yangu. Bado tuna Zayoni, bado maisha yetu hata sisi tuliobaki hayajakaa vizuri.
Bado tunahitaji pesa zaidi na kuishi vizuri zaidi. Naomba usikate tamaa.
Tuendelee. Na kama ni kukazana, basi tukazane zaidi. Nimebakisha muda mfupi sana
chuo kiishe, naamini kama nikituliza akili chuoni, nitafanya vizuri.” Bale
akaongea kwa hekima na taratibu. “Nimewasikia.” Baba yao akajibu. Wakaa naye
hapo kidogo, kila mmoja akatoka hapo kasoro Zayoni aliyepitiwa na usingizi
hapohapo.
Naya akamvutia Bale
chumbani kwake. “Njoo nikwambie kitu.” Akanong’ona. Bale akaingia wakafunga
mlango. “Bado unampenda Malo?” Naya akamuuliza, Bale akakunja uso.
“Aliyekwambia mimi nampenda Malon ni nani?” “Toka hapa. Kwani mimi sikujui?”
Bale akacheka. “Amefanyaje tena?” Naya akamsimulia mpango wote. “Daah! Hiyo
itakuwa afadhali. Itamchangamsha baba. Au ndio maana leo umeongea vile?”
“Nilikuwa natengeneza njia ili kesho Malo asipate shida.” “Angalau atapata
pakuanzia. Najua amekubali, lakini swala la wapi aanzie najua ndio utakuwa
mtihani.” Wakatulia kidogo.
“Baba akiondoka, atabaki
hapa Zayoni. Na mimi nina mambo mengi kupita kiasi huko chuoni. Nakuwa hapa
lakini wenzangu wanasoma Naya. Najiona nipo nyuma.” “Usijali. Kwa kuwa
tumezungumza nao wote wawili, tutegemee mabadiliko. Baba akiondoka,
nitajitahidi kuwa nawahi kurudi nyumbani ili Zayoni asijikute peke yake. Wewe
rudi chuo, au hosteli mpaka huu muhula uishe.” “Hapo utanisaidia Naya. Na uwe
unarudi nyumbani sio unachelewa sasa kama leo.” “Leo nilikuwa na Malo.”
“Umeanza Naya!” “Siwezi kumuacha mtoto peke yake. Nilikuwa huru kuchelewa
sababu nilijua wewe upo nyumbani. Kuna jambo nilitaka kuliweka naye sawa.
Lakini sitarudia tena kuchelewa. Nakuahidi.” “Hapo sawa.” Wakazungumza kidogo,
Bale akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya akampigia simu Malo,
kumwambia kila kitu. “Hapo umefanya vizuri.” Ikawa kama Naya akakumbuka anafanya
maamuzi kwa haraka tena bila kufikiria. Akajirudi. “Lakini
Malo, nafikiria kama baba akiondoka, na mimi nikitakiwa kusafiri kikazi, nani
atabaki na Zayoni? Ndio anakaribia mitihani yake ya darasa la saba.” “Kuna gharama
yakulipa mama. Lazima ubadilike na wewe ujue unayo majukumu ya kifamilia.
Safari kama hizo kama ni kwa ajili ya pesa ya ziada tu, itabidi zikupite.”
“Malo!” Naya akaongea kwa kusikitika.
“Huna jinsi Naya. Jinsi mlivyomlea Zayoni, ni tofauti. Hawezi kujikuta hapo peke yake. Ataanza msiba upya. Itachukua muda kujijenga kuwa mama hayupo na amekua. Ila kwa sasa, naomba uridhike na mshahara tu. Mungu atatupa kwa njia nyingine. Jaribu kuzungumza na bosi wako umueleze mazingira ya nyumbani kwa sasa. Muombe muda. Mtakapotulia, utakuwa huru kuendelea na kazi.” Naya akaelewa. “Naona itanibidi kufanya hivyo. Nashukuru kwa ushauri. Asante.” “Karibu mama. Nikuache ulale, ili kesho usichelewe kazini.” “Sawa. Usiku mwema.” “Na wewe.” Wakaagana na kukata simu.
Malon kwa baba yake Naya.
I |
likuwa mida ya saa 4 asubuhi wakati Malon akiegesha gari nyumbani
kwao kina Naya. Alimkuta baba Naya akisafisha nje. Anakata majani na michongoma
iliyokuwa imeota sana na kuchanua kama maua. Akawa anaitengenezea vizuri.
Alisimama kidogo ili kumsalimia, akarudi kukata michongoma huku akizungumza
naye kidogo. Malon akachukua reki, akawa anakusanya yale majani na michongoma
anavyokata baba Naya. “Naona kunachukua sura mpya.” Malon akasifia. “Nilipaacha
muda mrefu, naona kumegeuka chaka. Heri nipasafishe kabla simba hawajahamia
hapa.” Wakacheka kidogo.
“Biashara zako zinaendaje?”
“Kwa kweli namshukuru Mungu. Siwezi kulalamika kabisa.” “Nimekuona jinsi
ulivyobadilika!” Malon akacheka. “Na kanisani bado unakwenda?” “Nakwenda. Bado
nimeokoka.” Baba yake Naya akasimama na kumwangalia. “Sidanganyi.” Malon
akajitetea. “Kwa nini upo hapa Malon wakati nimesikia upo na yule dada
anayeishi nyumbani kwako?” “Rita yupo pale kama mpangaji. Na Mungu wangu ni
shahidi. Na yeye anajua yupo Naya.” “Sasa kwa nini ulienda mpaka nyumbani kwa
wazazi wake, ukatambulishwa kwa ndugu zake kama hivi hapa kwa kina Naya, na ulisafiri
naye?” “Alitaka kwenda kupaona Brazil, sikuona sababu ya kumkatalia kuongozana.
Ila Mungu wangu ni shahidi, hakuna lililotokea kati yetu.” “Sio kweli Malon.” Baba
yake Naya akabisha na kumshtua sana Malon.
Akashuka kutoka kwenye
ngazi aliyokuwa akiitumia kufikia juu ya michongoma. Akamsogelea Malon. “Mimi
nitakwambia kwa kuwa naijua historia yako Malon. Usipoangalia, kile ulichoishi
duniani, utakiishi na kanisani pia ila tu ukikitetea au ukikipa sura ya
utauwa.” Baba Naya akaendelea.
“Ninapokataa usemi wa kuwa hakuna
kilichotekea kati yenu, ndivyo hivyo hivyo ulikuwa ukifanya na mabinti
wengine kabla hujasema umeokoka. Kwako hakukuwahi kuleta maana kuwa na binti
kwa muda kisha kumuacha tu. Historia yako tokea zamani mpaka hapa
nikikusikiliza, unaonekana ni hivyohivyo. ‘Hakuna kilichotokea’, kama
unavyosema lakini si kwa unao waacha. Rita ameondoka nchini akiaga anakwenda
kupumzika na wewe kama mpenzi, huko Brazil. Ameacha mtoto wake kwa Naya, wewe
ukiwepo na ukielewa kabisa lengo la Rita. Sijui kilichoendelea huko, ila kwa
kukusikiliza hapa ni kama ulimkatili vibaya sana kwa kutotimiza azma yake
ambayo najua kwa hakika, wewe uliijua, Malon.” “Sio moja kwa moja mzee wangu.”
Baba Naya akatingisha kichwa kukataa.
“Hapo utajichelewesha sana
Malon kwa kuwa kwa upande mmoja unajua ukweli ila umekusudia kutokubali tatizo
lako na hutaki kubadilisha hapo. Hata mtu mjinga kabisa anaweza kujiuliza hili
na kupata jibu kwa haraka tu. Kwani huyu Rita si alikuwa akiishi huko nchi za
nje? Hapafahamu Brazili?” Malon kimya. “Kwani alikuwa na shida ya nauli kufika
huko kwamba alitegemea msaada wako kufika huko?” Baba Naya akauliza swali
jingine lililomziba mdomo Malon. “Mimi na wewe wote tunayo majibu yake, kama
Naya amenieleza sahihi juu ya Rita! Kwa maana nyingine kwa hakika alikwenda
huko Brazili kwa kuwa uliweka mazingira ya kuwa naye huko. Ama si kweli Malon?” Baba huyo akambadilikia
Malon.
“Inamaana na yeye Rita sasa
hivi anapita kama wanawake wote ambao wameshapitishwa kwenye maisha yako,
Malon, akiwepo Naya mmoja wao. Kasoro Rita anapitishwa na wewe wewe Malon ukiwa
kanisani. Ila kilio chake ninahakika kipo kama wanawake wote unaowaacha vibaya
sana.” Baba Naya akaendelea.
“Kama kwa Naya. Umekuwa mtu
wakutoka na kuingia kwenye maisha yake vile utakavyo, kwa sababu unazochagua
wewe, bila kuhesabu madhara yake.” “Najua madhara yake kwa kuwa na mimi huwa
sibaki salama. Nampenda sana Naya na nateseka kuishi bila Naya. Mara ya kwanza
niliamua kumuacha Naya, kwa kuwa nilitoka jela, nikamkuta akiwa na Joshi na amejawa
furaha sana. Nikajiangalia hali yangu, na nilivyo, nikajua kuwepo kwenye maisha
ya Naya, nikuendelea kumtesa. Nikaamua kumuachia Joshi. Niliporudi tena,
nikakuta bado yupo na Joshi, lakini akimnyanyasa sana. Ndipo nikaona ni heri
nirudi tu mwenyewe, tutapambana na maisha tukiwa pamoja na Naya, kwa kuwa huwa
tunaelewana kwa kila kitu.” Malo akaendelea kwa makini sana asije akaharibu.
“Mungu
wangu ni shahidi, nilirudi nikiwa na nia yakumchumbia Naya. Lakini nilitaka
kuzungumza na wewe kwanza. Kukwambia nimebadilika, na nimeamua kumuoa Naya.
Nilitaka kukuahidi nitamtunza Naya kwa kadiri Mungu atakavyonijalia, lakini
nikaishia mikononi mwa mama. Mama Naya aliniomba kwa kunisihi huku akinieleza
alipo Naya na Joshi. Kuwa Naya ameenda kutambulishwa ukweni, na wanafuraha na
wana amani. Hakuishia hapo, akanionya kabisa nisimtafute na wala nisiwahi kumpa
mawazo ya biashara. Itakuwa nikuingilia mahusiano yao na kumchanganya Naya.
Akataka nimuache Naya aendelee na maisha yake na Joshi. Ilibidi niondoke Mzee
wangu, na kutii. Maana aliniambia maneno mengi na mabaya sana ila sitaweza kuyarudia.
Ila sio kwamba najisifia, lakini hakuna mwanaume atakayeweza kumpenda Naya na
kumthamini yeye kama Naya pamoja na kumuenzi kama mimi.” Baba yake Naya akamwangalia
na kurudi kuendelea na kazi zake.
“Ila sina haraka. Nampa
muda anichunguze yeye mwenyewe. Naya huwa ananijua vizuri, na mimi huwa
simdanganyi. Kwa hiyo nimetulia, nampa nafasi mpaka yeye mwenyewe aseme. Hilo
kama la Rita nimelifanya bila kufikiria, naahidi nitaongeza umakini kuanzia
sasa nikimsubiria Naya aridhike na mimi. Na mimi sitasumbua tena.” Baba yake
Naya akamtupia jicho tena na kuendelea na kazi. Kimya.
“Kwa sasa unafanya biashara
gani?” Akauliza Malon kwa tahadhari
kidogo akijua na kwa baba Naya hapako sawa kwake ila akakusudia kupambana tu.
“Vipi, unataka kuniajiri nini?” Akauliza
kwenye swali. “Kama ungependa. Huwa nakwenda Mbeya kukusanya mchele na kokoa.
Nakuwa peke yangu. Ila nikipata msaidizi mwenye uelewa, itanisaidia kutumia
muda mfupi huko mashambani.” Kimya,
akaona aendelee kupambana. “Kokoa huwa nasafirisha nje ya nchi, mchele ni
hapahapa nchini. Nilianza kama utani tu. Sikujua kama ingelipa. Lakini
utashangaa hiyo pesa inayopatikana kwa huo mchele!” “Watoto wangu wananihitaji
sasa hivi.” Akajibu baba Naya akisikika mawazoni. “Sina watoto, lakini nafikiri
wangehitaji uwepo wako na uwezo wako pia.” Akamuona ametulia tu, akiendelea na
kazi. Kwa kuwa Naya alimwambia na anamjua sio mzungumzaji akaona na yeye atulie
kidogo. Pakazuka ukimya, kazi ikaendelea.
“Na kweli sasa hivi
nimeishiwa.” Kama aliyekuwa akiwaza kwa sauti, baba Naya akasikika. “Gari hiyo
imeharibika, sina hata pesa yakutengenezea! Mtoto wangu anahangaika usafiri
wakumpeleka kazini. Nimemsindikiza asubuhi hii kupanda daladala, wanamsukuma, sukuma,
ameishia kusimama tu.” Akajua huyo mtoto anayemlalamikia ni Naya tu. Alijua
jinsi anavyompenda Naya. “Kuna watu nafahamiana nao, ni mafundi wa gari.
Nilifanya nao kazi. Naweza kuwaomba wakaja kulichukua ili waliangalie.” “Aaah!
Hata hivyo ni kwa kuwa nina shida tu. Hiyo gari niyakuuza na kununua yakawaida.
Naya alinisaidia kuinunua hiyo kwa sababu ya kipindi kile nafuga. Hata hivyo,
nimekusikia. Acha nizungumze kwanza na Naya. Maana yeye ndiye anayepanga siku
hizi mambo ya humu ndani. Tuone tunajipangaje kama mimi nikiondoka.” “Sawa
kabisa.” Malon akakubali akijua jibu tayari.
“Kama nikuondoka,
tunaondoka lini? Kwa kuwa nikweli tunahitaji pesa.” Akaongea baba Naya kama
aliyerudishiwa ufahamu wake na kukumbuka wajibu wake kama baba wa familia.
“Mimi lazima jumamosi niondoke. Ukiwa tayari tutaongozana. Lakini kama bado,
unaweza kunifuata na basi muda na wakati wowote utakapokuwa tayari.” “Basi
nitakujibu kesho. Acha leo nizungumze na mama yangu mzazi kwanza.” Akimaanisha
Naya. “Na kuhusu gari, tunaweza kulitengeneza tu. Ukauza likiwa zima.” “Kwa
sasa sina pesa na sitaki kuanzisha huo mjadala kwa Naya. Atatumia pesa yake
yote kwa kutengeneza gari ambayo haitakuwa na faida. Acha tu tuhangaike kwa
muda.” “Naomba basi mimi nilitengeneze.” Baba yake Naya akasimama na
kumwangalia.
“Naya aliniambia huwa hujui
jibu la hapana.” Malo akacheka kama anayekubaliana naye. “Kwa hiyo hapa
utalazimisha mpaka ukalitengeneze?” “Naona ni jambo la msingi.” “Sawa.” Malon
akacheka. “Basi acha nipige simu waje kulichukua.” Baba yake Naya akacheka na
kutingisha kichwa. “Nashukuru.” Akaona ashukuru tu. “Tusubiri wakaliangalie.
Tukiona limeharibika sana, nitawaambia wauze vifaa vyake wakuletee pesa.
Linaonekana limechoka sana. Sidhani kama kwa kuliuza hivyo zima kama lilivyo
sasa kama utapata pesa nyingi.” “Na hiyo ndiyo ilikuwa hofu yangu. Nililinunua
kwa mtu kwa bei nafuu akiwa ameshalitumia sana. Ila limenisaidia vyakutosha.”
Malon akawapigia simu mafundi, akaomba waje walichukue.
Akiwa pale pale akisaidia
kazi, wale mafundi wakaja. Wakazungumza naye, mwishoe mzee akaamua aliuze tu.
Wakalichukua kwa makubaliano ya kumlipa baada ya siku mbili mbeleni. Malon naye
akaondoka pale nyumbani kwao akiridhika kwamba kazi iliyompeleka pale
ameimaliza na angalau amepata nafasi ya kujitetea na kwa baba Naya pia. Hata
kama hakuwa amemuweka sawa, akajua muda utawabadili wote mawazo. Kwa asili
Malon alijua kumfanya mtu akampenda, kama akiamua yeye. Hachoki, na anaweka
juhudi haswa na kuweza kumuonyesha mtu yupo naye mpaka huyo mtu akabweteka
akijua anaye mtu wakuwa naye kwenye jambo. Akajiaminishia kwa familia hiyo
ambayo ilimpenda sana, kwamba hata safari hii aliyorudi tena itakuwa rahisi
sana kwani kipingamizi mama, alishaondoka. Akaendelea kujiwekea mikakati.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
‘Nipigie simu wakati
unakaribia kutoka. Nitakuja kukuchukua.’ Ujumbe ukaingia kwa Naya,
kutoka kwa Malon. Naya akafikiria, akaamua kumtumia ujumbe. ‘Usisumbuke
Malon. Leo nitawahi kutoka, nafikiri sitasumbuka usafiri. Na endepo
nikichelewa, baba amesema atanisubiri kituoni.’ ‘Naweza kupiga?’ Naya
aliposoma ule ujumbe, akampigia yeye. “Ni nini Naya, mama?” “Naona
nisikusumbue. Kwetu mbali Malo. Na wewe najua umechoka, sitaki kukusumbua.”
“Umemaliza?” Naya akacheka kidogo akisikika aliyegoma. “Kuna jambo
nataka kukwambia. Nilikuwa na baba leo.” Hicho kikamvutia Naya
kutaka kujua ni wapi walifikia kabla yakurudi nyumbani. “Sawa
nikiwa nakaribia kutoka nitakupigia. Vipi siku yako?” Naya
akauliza kiuungwana. “Mpaka sasa sio mbaya. Nipo sehemu kuna kitu nafanya, nipigie wakati
unakaribia kutoka ili nisogee.” “Nashukuru.” “Karibu.”
Wakakata.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni Malon alifika hapo na
gari ya tofauti. Kadogo tu aina ya Vitz. Naya akacheka wakati anamsogelea.
“Umepata wapi hii gari?” “Mbaya?” “Hapana. Sio mbaya. Ila sijawahi kukuona
ukiendesha gari ndogo hivi tokea nakufahamu!” Malon akacheka. “Unayo leseni yako?”
“Unataka leo nikuendeshe bosi?” Malon akacheka na kumfungulia mlango wa dereva
na yeye akaenda upande wake. Naya akawasha gari. “Tunaelekea wapi?” “Kwangu
kwanza.” Naya akaondoa gari.
“Uzuri wa hiyo gari,
haitumii mafuta sana. Rahisi kuitengeneza.” Naya akawa anamsikiliza huku
akiendesha. “Hii ukiitumia kwa matumizi yako ya kila siku asubuhi na jioni kwa kazini, na mizunguko ya pale nyumbani,
haitamaliza pesa ya mtaji wa biashara.” Naya akamgeukia. Akakunja uso kama
ambaye hamuelewi, akaendelea kuendesha. “Umenisikia?” “Nimesikia lakini
sijaelewa Malo!” “Nimenunua hili gari, likusaidie usafiri.” Naya akatulia
kidogo. “Baba anaonekana anaweza kwenda na mimi Mbeya. Na yeye ndiye
anayekusindikiza kituoni. Anasema leo aliona jinsi unavyohangaika na usafiri.
Ameshinda siku nzima anasononeka!” “Nilipanga nikipata pesa nitengeneze ile
gari yake.” “Ile gari imechoka Naya. Yazamani. Nimempelekea fundi leo. Wameitizama,
gharama ya kutengeneza mpaka iweze kuwa barabarai ni kubwa sana.” “Kwa hiyo
haitafaa tena?” “Haiwezi. Itawalia pesa zaidi. Lakini wakiichukua wao, wanaweza
kuiuza vifaa vyake, wakapata pesa.” Naya akatulia.
“Ni nini Naya?” “Naona
unamajukumu mengi! Na mimi sitaki kuingia huko. Halafu hili ni gari Malo. Nikiiharibu
kwa sababu yeyote ile?” “Kwa nini usifikirie urahisi utakaopata kukufikisha
kazini na kwenye mizunguko yako kwanza? Kwa nini unafikiria shida wakati wote?
Tukiwa hatuna uwezo, inaeleweka mama. Sasa sasa hivi uwezo upo, bado tuhangaike
tu!” Naya akabaki kimya. “Kama hutaki kuchukua, basi mimi nitakuwa nikija
kukuchukua asubuhi na kukurudisha nyumbani.” Naya akacheka kidogo kwa
kusikitika kisha akaguna.
“Ni nini Naya?” “Nimeshindwa kukutabiri Malo!
Hakika nimeshindwa na kukuelewa. Nilidhani nakufahamu sana. Ukajenga tabia
iliyonifanya nikufahamu kama unayenijali sana kuliko mtu yeyote yule, lakini
inapokuja kwenye uhalisia unageuka tena, unakuwa ni kama usiyejali kabisa.
Unaweza ukawa katili, mpaka najiuliza unawezaje! Hakika nashindwa kukuelewa!”
Kabla hajajibu Naya akaendelea.
“Sijawahi kuogopeshwa na
uwepo wa mtu kwenye maisha yangu kama wewe Malo.” “Haiwezekani Naya!” “Hakika
Malon. Umeyabadili sana maisha yangu na moyo wangu. Imefikia kiasi kwamba
nikiwa na wewe, sifurahii tena ila kuogopa.” “Kwa nini!?” Malon hakutegemea
hata kidogo. “Kwa kuwa unakuwa mtu wa msimu! Unakuwa hivi, unapotea. Ukirudi unanikuta
kwenye hali isiyofaa. Unanipa matumaini makubwa sana. Nakufungulia moyo wote na
akili. Nikishazama kabisa kwako, nikiwa nimejawa tumaini na furaha ya ajabu,
ndipo unapotea! Nabakia nateseka sana. Na wewe huwa hujui kugeuka nyuma hata
kuangalia naendeleaje pale uliponiacha. Unaendelea na maisha yako mpaka nije
kukutafuta tena.” Naya akamgeukia kidogo.
“Sasa kama hivi sasa hivi,
kwanza tupo hapa pamoja kwa sababu jana nilikufuata nyumbani kwako kukupa
zawadi ukiwa upo tu hapa mjini, umekaa tu nyumbani kwako, ndipo umerudi na
mipango mizito na mizuri sana kama kawaida yako. Sijui hii itakuwa ni leo tu!
Sijui kama kesho utakuwepo! Sijui hii gari kama itakuwepo na itakuwepo kwa siku
ngapi! Naogopa hata kwenda nayo nyumbani. Nisije nikawapa tumaini kama ile
biashara uliyoniambia tutafanya. Nikamzungusha baba yangu mjini tukisaka vifaaa.
Tukatafuta mpaka fremu na mkataba tukaingia. Ukaja kuniacha kwa ukali sana, ukinisukumia
kwa Joshi. Nimeingiwa hofu na wewe Malo.”
“Mama alinifukuza Naya!” “Kumbuka
unazungumza na mimi Malo. Sio mtu mgeni kwako. Mimi nakujua. Kama ungenitaka
kwa hakika, hakuna mtu wala kitu kingekuzuia. Linapokuja jambo unalolitaka
wewe, huwa wewe sio mtu wa kukubali ‘hapana’. Hata kama ungeambiwa
nimetambulishwa kwa wakwe na mahari nililipiwa, basi ungenipigania tu. Hujawahi
kunipigania Malon. Hata mara moja. Sitaki kukuhesabia, lakini mimi
nilikupigania Malo. Kwa moyo, nafsi na juhudi zangu zote. Bila aibu, bila
kuchoka. Nilijua ni wewe nakuhitaji. Mvua ilinyesha, jua lilitoka, huku
nikitukanwa juu yako. Lakini nilijua ni wewe nakutaka.” Naya akaendelea
taratibu tu bila jazba.
“Ulijua vile baba yako naye
alivyonifukuza kwenu, akimwambia baba yangu asiniruhusu kuwa na wewe kwa kuwa
nitaharibikiwa kama wengine. Lakini Malo, nilikuchagua wewe. Ila wewe ulitoka
jela, ukanisukumia mikononi kwa wanaume wengine. Ni mapenzi gani hayo?”
“Nilikuwa sina kitu Naya. Nimetoka kila mtu akiniambia sikustahili. Shukurani
pekee kwako nikukuacha. Ningefanyaje?” “Wewe sio wakuniuliza ungefanyaje
Malon, linapofika jambo unalolitaka! Halafu mbona mimi waliniambia mengi hivyo
hivyo tena ya aibu yakupitiliza! Sikuwasikiliza Malo, nilibaki na wewe tu.”
Malo kimya.
“Halafu kwa hiyo kama
ulivyosema mahusiano yetu yanakuwa yanajengwa kwenye pesa tu! Ukiishiwa tena?
Unataka tuje kuwa na ndoa kama ya wazazi wangu wakihesabiana mambo ya mali?
Ukiwa na pesa unarudi, ukifilisika unaondoka! Hayo yanakuwa mahusiano gani
Malon?” Kimya. “Tokea mwanzo nimekuwa nikikuomba unichague mimi Malo. Mvua
inyeshe, jua litoke, uwe umenichagua mimi, hilo lingenipa faraja. Lakini Malo,
hujawahi kunichagua. Unakuwa na sababu nzuri sana na zakueleweka kila wakati unapoamua
kuniacha na kunirudia mimi. Ningefurahi ungesimama na mimi katika shida yako,
halafu sasa hivi tukafurahi pamoja.” Naya akaendelea.
“Lakini huku ni
kunidhalilisha Malo. Najihisi unaniona ni kama nipo dhaifu sana, siwezi kuwa na
wewe katika maisha yako. Nakuwa ni mtu unayeweza kunitoa unapojisikia wewe, na
kuniongeza unapotaka wewe. Nakuwa sina uhakika na wewe Malo. Sijui lini utaamua
nini na utaniacha kwenye wakati gani! Hunifikirii mimi kama Naya!” “Hakuna mtu
namfikiria kama wewe Naya.” “Ni unaponiona au kukutana kama hivi sasa hivi. Narudia
tena Malo, na huo ndio ukweli. Tupo hapa
sasa hivi, safari hii, wakati huu ni kwa sababu mimi nilirudi kwako kukuletea zawadi
ya saa, ya kukushukuru. Inamaana nisingerudi jana kukuletea zawadi, na kukupa
mwanya wa kunirudisha nyumbani, tukazungumza machache ukajua kinachoendelea
kwetu, ukapata sababu ya kurudi nyumbani kuzungumza na baba, ukajua sononeko
lake juu yangu, inamaana usingejua nina shida ya usafiki wakati wa kwenda na
kurudi kazini, na wala hili gari usingenunua, Malo. Maisha yako na Rita
yalikuwa yakiendelea vizuri sana, bila shida.”
“Rita hajawahi
kuwa mwanamke wangu.” “Acha kumfanyia Rita kama ulivyotufanyia sisi wote Malon!
Unatenda dhambi.” Naya akaongea kwa kuumia sana kama baba yake tu alichomwambia
Malon asubuhi hiyohiyo. “Kwa maelezo yako wewe mwenyewe mbele yetu wote,
unasema ulikwenda mpaka nyumbani kwa wale wazazi wao kutambulishwa na kwa ndugu
zake. Najua wewe si mjinga Malon useme hukuwa ukifanya hilo kwa kutofahamu! Kwa
nini mtu kama Rita akupeleke nyumbani kwao na ndugu wakutambue kama mpenzi wa
Rita? Unakuja kuchukua mtoto wa Rita shuleni wewe kama nani kama hamkuwa kwenye
mahusinao? Umemtoa hapa mpaka Brazil!” “Nilikueleza jinsi ilivyokuwa Naya. Rita
alitaka kupaona Brazil, sikuona sababu ya kumkatalia.” Akajibu hoja moja tu.
“Mimi ningefanya hivyo, ingekuwa sawa kwako?
Ulikasirika ulipokuja nyumbani na kuambiwa nilitoka na Joshi kwenda kwao.
Kinachokufanya ufikiri ni sawa kwa wewe kwenda Brazil na Rita, huku ukijua
kabisa anakutaka kimapenzi, amekupeleka mpaka kwao ukakubali kwenda
kutambulishwa, amekuamini mpaka na mtoto wake, ndugu zake wote wanakufahamu
wewe na yeye mpo kwenye mahusino!? Ni nini unaendelea kufanya Malon? Mpaka lini
na kwa umbali gani utaendelea kuumiza watu? Wewe unaweza usielewe madhara
unayoacha kwa watu Malon, kwa sababu kama sasa hivi ushamalizana na Rita,
umerudi hapa. Lakini mimi naweza kuhisi alipo Rita sasa hivi na kule alikokwisha
kukutambulisha. Ni aibu na fedheha Malo, wewe hujawahi kuishi hapo. Maana kama
sasa hivi unayo sababu nzuri tu inayokupa amani kumuacha bila kujali eti kuwa
ulishindwa kumkatalia! Utashindwa kumkatalia kwa mangapi na wangapi Malo?”
Kimya.
“Hivi sivyo ulivyokuwa
ukiwafanyia wasichana wote uliokuwa ukilala nao kipindi tupo wote?” “Naya!”
“Unakataa nini Malo? Unabisha nini wakati nimekukumbusha kabisa kuwa
unazungumza na mimi! Tuache wengine wote, turudi kwa Loi. Ulinipa sababu gani
kama sio kama hii inayofanana na Rita? Alikung’ang’ania au kukuomba ukashindwa
kukataa. Si ni hivihivi Malo? Kanusha kama si kweli?” Malon kimya akainama.
“Najua tupo kwenye wakati
mgumu wa maisha pale nyumbani. Naamini ni kwa muda tu. Mungu atatusaidia. Acha
nizoee maisha yetu, pengine yatakuja kubadilika baadaye. Kuliko haya maisha
yanayoendeshwa kwa hisia, Malo! Ukijisikia kunihurumia, unanitendea jambo
kubwa, zuri lakunisisimua. Hisia zako kwangu zikiisha, unaniacha nateseka sana.”
Naya akafikiria kidogo. “Hapana Malo. Umenichezea hisia zangu vyakutosha. Kwa
sasa ulitakiwa wewe unielewe mimi ni mtu wa namna gani, sio kama hao wasichana
wako wazuri, wasomi wanaokutaka kipindi ukiwa kwenye magari ya thamani! Hapana
Malon. Inatosha.” Wakati huo Naya anazungumza naye, alishageuza njia zamani
sana kuelekea nyumbani kwao wala sio Kunduchi nyumbani kwa Malon.
“Nakushukuru kwa msaada wa
usafiri, lakini tokea tunaanzana Malo, ombi langu kwako lilikuwa moja tu.
Nikikuomba mpaka kwa machozi mpaka Side nilimtuma kwako, nikikuomba unichague
mimi na hujawahi kunichagua Malo.” “Nakupenda Naya. Na nimekuchagua wewe.
Nilirudi kwa ajili yako.” “Sivyo ulivyoniambia siku nakupigia simu na kukuta
upo nchini nikiwa nakusubiri. Sivyo ulivyofanya kwa vitendo vyako baada ya ile
simu. Hata hukuniachia shilingi moja uliyojua nilihusika kuikusanya kwa jasho
langu mpaka kuifikisha kwenye kuwekewa dhamana na kurudi mikononi mwako.
Ulinikuta na shida sana, na ukaniacha na shida vilevile usiniache hata na pesa
kidogo tu! Haya, ukaendelea na maisha yako na Rita bila shida yeyote. Na kwa
jinsi ninavyokujua Malon, Mungu anisamehe kama ni sivyo?” Naya akacheka na
kutingisha kichwa.
“Nini?” “Kwa mahusiano
niliyoyasikia kwa Nolan, pamoja na Rita mwenyewe kabla hujajua mimi
ninayekufahamu nipo na mtoto wa Rita, inaonekana na kusikia ulikuwa pazuri tu
na Rita, mpaka mimi nilipoingia kwenye picha ndipo hapo nikatibua mapumziko
yenu huko Brazili, lakini inaonekana mlikuwa na mipango mizuri sana. Kwa
kumuangalia tu Rita si mpumbavu au mjinga kudandia safari ambayo hakuwa na
uhakika nayo. Kulikuwa na ahadi nzuri tu, na ndio maana akaenda umbali mkubwa
sana hata kuacha mtoto anayempenda vile kwa mtu kama mimi mgeni kabisa. Unajua
sana unalolifanya Malo, acha kuepuka ukweli.” Kimya. “Anyway, nashukuru kwa
usafiri Malo, lakini asante. Tunza tu mali zako na uzitumie kwa furaha.
Unastahili. Ni jasho lako, huwa unahangaika peke yako.” Naya akaegesha karibu
na kituo cha kuelekea nyumbani kwao.
Akamgeukia Malon. “Tafadhali
usije kunichukua asubuhi. Nitapanda tu daladala. Mimi bado nipo palepale
uliponiacha. Acha na mimi nihangaike kama wewe. Ila nashukuru kwa ajira ya
baba. Nitazungumza naye na kumtia moyo, ili muongozane. Naona itamsaidia
kumrudisha kwenye hali ya kufikiria.” Malo akabaki ametulia.
“Nikuulize kitu Malo?”
“Niulize tu.” “Nafikiria zawadi ya kumnunulia. Hivi huko mnakokwenda,
mashambani, mazingira yakoje? Atahitajika nini?” Malon akavuta pumzi kwa nguvu
akijaribu kutulia. “Kama viatu. Aina gani ya viatu, nguo na mashuka
vinahitajika ili niweze kumuandalia begi lake. Mnalala wapi? Vitu kama hivyo.”
Malon akacheka.
“Cha kwanza ujue ni
mashambani. Vijijini kabisa. Wakati mwingine mimi huwa nalala kwenye gari tu. Wakati
mwingine unaweza kupata familia ikakualika nyumbani kwao.” “Malo! Hamna
hoteli?” Malon akacheka sana. “Nilikwambia huwa nakwenda vijijini kabisa, mama.
Kwa wakulima. Lazima nisimamie hiyo kokoa katika kila hatua, ili nisikusanyiwe
na mbaya. Kwa sababu hebu fikiria, nitumie pesa yote kuisafirisha mpaka huko,
halafu waje waniambie mzigo haufai! Si unaona nitakuwa nimeingia hasara
sana?” “Kweli.” Naya akabaki akimfikiria baba yake. Malon akacheka.
“Unamuhurumia baba?” “Ulijuaje? Natamani kuahirisha, asiende.” Malon akabaki
akimwangalia.
“Au uende naye wakati
mwingine. Safari hii muache tu. Tutafikiria kitu kingine chakufanya.” Malon
alimtizama asimmalize. “Nitatafuta biashara nyingine au hata nimpe pesa afanye
kitu kingine.” “Mbona mimi nafanya Naya?” “Wewe ni kijana Malo. Baba mtumzima.
Akienda huko na kuanza matatizo? Ndiye mtu pekee tuliyebaki naye maishani. Heri
tuwe na vichache ila tuwe pamoja, kuliko vingi akiwa yeye hayupo. Tutakuwa sawa
tu. Naona wewe uendelee Malo.” “Acha kuogopa Naya. Huko nako wako watu wazima
na wazee zaidi ya baba yako wanaishi na wananifanyia mimi kazi.” “Mmmh! Hayo ni
mazingira yao Malo. Baba kwa umri alio nao kuanza kitu kipya! Hapana Malo.
Mungu hawezi kutuacha tukalala njaa. Huu mshahara wangu utatosha kwa sasa. Acha
tu tubaki naye.”
“Naya! Umeingiwa hofu mama.
Naomba mpe baba nafasi yakufanya kitu na kuona matunda yake. Sasa hivi hapa
nchini mambo yamebana. Lakini sio nchi nyingine. Kule tunapokwenda atakutana na
watu wazima kama yeye na zaidi yake, ataona jinsi wanavyohangaika bila kuchoka
na kutokata tamaa. Siku nyingine za jioni wanakuwa na starehe zao. Na ngoma za
kwao. Kwa kichache walicho nacho, wanayo furaha. Wanashida nyingi sana, lakini
maisha yanaendelea. Wanakuja siku nzima wananikusanyia kokoa. Wananiuzia mazao
yao. Wacheshi wachangamfu. Ndicho kitu baba anachohitaji kukiona sasa. Kwa
vitendo sio maneno. Kitu kipya na kigeni kitakachochukua mawazo yake. Watu
wanaopitia changamoto ngumu na bado wanapambana. Hiyo itamsaidia na kumsogeza
karibu zaidi na Mungu.” Malo akaendelea.
“Ukifikiri kuwa wewe
unashida, ukienda kule utaelewa. Watu wanashida Naya. Shida haswa. Imenifanya
kuwa mnyenyekevu na kujiona nina bahati kubwa hata hapa nilipo. Utakuja kuona
baba atakaporudi.” Naya akabaki akifikiria. “Atakuwa sawa, usiogope.” “Naomba unisaidie
kumwangalia Malo. Ukiona anashindwa, mtafutie sababu yakurudi. Tafadhali Malo.
Ndio nguzo pekee niliyobakiwa nayo.” “Nitafanya hivyo mama. Usigope. Na kuhusu
nini chakubeba, naweza kukuandikia kwa ujumbe, nikakutumia. Ukipenda, naweza
kukusindikiza ukanunue.” “Nitashukuru sana ili nisinunue vitu visivyo.” Naya
akafikiria kidogo.
“Kwa hiyo hiyo kesho nije kukuchukua kazini au
ungependa tukutane wapi?” “Naweza kukufuata unapojua yapo hayo maduka.”
Malon akacheka na kutingisha kichwa kama anayesikitika. “Nini sasa? Nimekosea
nini tena?” “Naishi Kunduchi. Unafanya kazi CocaCola, njiani na kwangu. Yaani nikupite
pale, niende madukani, halafu wewe unapanda kwenye daladala kunifuata nilipo!
Ni nini unataka kitokee Naya au kunionyesha?” “Nakupunguzia shuguli Malo.”
“Sawa. Ni saa ngapi unafikiri utakuwa na nafasi.” “Jioni nitakuwa nimechelewa
sana?” “Hapana. Tunaweza kufanya jioni baada ya kazi. Sio vitu vingi na
vinapatikanika sehemu za karibu.” “Sawa. Nitakuona kesho Malon.” “Naomba
uchukue hili gari Naya. Tafadhali mama.” “Hapana Malo. Asante.” Naya akashuka,
na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment