![]() |
“Tokea mtoto huwa anachotaka ni yeye ndio awe anatoka pale
nyumbani, ila mimi niwepo. Awe ananikuta kila anaporudi au anapotaka yeye
niwepo nyumbani. Sasa asipokuwa akinikuta nyumbani hilo ni tatizo ambalo halina
mjadala wala dawa. Sasa kaka zake wameniambia ameanza hata kushindwa kula.
Najua kitakachofuata ni ugonjwa. Na ugonjwa huo lazima atazidiwa na kupelekwa
hospitali na hapo ndipo...” “Itakulazimu uende kwa haraka maana hakuna dawa
itakayomponya.” Malon akamalizia, wakacheka.
“Hata hivyo sioni kama unanihitaji sana kwa huku ghalani. Naona
unao vijana wengi tena wanaonekana ni nafuu sana.” “Ni kweli, ila kwa kazi kama
hiyo uliyoifanya wewe peke yako na wakati mwingine ukisaidiwa na mtu mmoja,
tena kwa muda mfupi sana. Ingenilazimu mimi kuchukua muda mrefu kwa kuwa vijana
wote hapa sijapata wakujituma au mwenye uelewa wa hiki ninachokifanya. Ni wa kuwasimamia
kwa kila hatua lasivyo unajikuta inabidi kurudia kazi zao kila wakati. Kwa hiyo
umenisaidia sana, Nashukuru. Wewe unaweza kuondoka tu wakati nikimalizia hatua
za mwisho ili kuusafirisha huu mzigo salama.” Hiyo ndio ikawa siku ya mwisho ya
baba Naya kuwepo mjini Mbeya. Kwa hakika alifanya kazi kubwa na kumridhisha Malon
mwenyewe.
Baba Naya arejea kwa Familia yake.
N |
aya alilia
sana baba yake aliposhuka kwenye basi. Aliwakuta watoto wake wote wakimsubiria
kituo kikuu hapo Kibaha. Alileta vyakula vingi ndio maana hakutaka kushushiwa karibu
na kwao. “Nimerudi mama.” “Nilikuwa naumwa tumbo mwezio. Silali!” Naya
akalalamika akilia. “Bale aliniambia alikupa dawa. Hazikusaidia?” “Midawa ya
Bale sijui ameikotea wapi! Haifanyi kazi baba.” Bale akacheka na kutingisha
kichwa. Naya alikuwa amekaa kiti cha nyuma na baba yake. Bale akiendesha hiyo
gari ya Naya. Zayon amekaa kiti cha mbele, baba yao akimbembeleza Naya hapo
nyuma walipokaa pamoja.
“Angalia kama sijapandisha homa!” Hilo kila mtu alilitarajia. Baba yake akamshika. “Si unaona kichwa kilivyo cha moto?” Naya akaongeza akilia taratibu. “Labda sababu ya kulia Naya!” Zayon akaingilia. “Kwani nilikuwa...” “Wewe nawe unataka kununua matatizo. Si umuache tu!” Bale akamfanya Zayon acheke kimya kimya. “Nilikuwa najaribu kumtuliza.” “Wewe unamuona ni mtulizwaji huyo? Wewe muache na magonjwa yake yasiyo na tiba.” “Basi baba hali ya hapa ni kama hivyo unavyooona. Hakuna faraja! Hakuna kujaliwa. Napuuzwa tu.” “Kumbe bora nimerudi mwenyewe!” “Mwanao hafarijiki baba na wala haambiliki huyo.” “Muongo Bale. Wala hajanifariji kama hivi wewe, baba. Nimeachwa nikiteseka tu peke yangu.” Kila mtu akacheka, lakini walijua tiba yake imerudi, atatulia tu.
Naya Aongea Ukweli Kile anachojisikia kwa Malon.
W |
akati wanakula,
Naya pembeni ya baba yake, akamuuliza. “Mara ya mwisho kuwasiliana na Malon
ilikuwa lini?” Naya akatulia kidogo na kufanya hata wadogo zake kupatwa shauku
ya kujua jibu. Ni Malon! “Naya?” “Aaah! Naona kama haina maana baba.” Hakuna aliyetegemea.
“Kwa nini tena!?” Ikabidi Bale aulize kwa mshangao. Naya akacheka kwa
kusikitika kidogo. “Unajua sasa hivi Malon amerudi kwenye picha si kwa kutaka
kwake! Ni kwa kuwa nilimfuata kwakwe kumpa zawadi ya kumshukuru kunisaidia
nilipokuwa nikisoma. Ni nadhiri niliyokuwa nimejiwekea tokea nikisoma.
Nikajiambia nikifanikiwa kumaliza shule, nikapata mshahara wangu wa kwanza kwa
kile ninachosomea, na yeye lazima nimshukuru kwa kumnunulia zawadi nzuri. Basi,
nikafanya hivyo. Niliiacha tu getini kwa mlinzi, alipomfikishia ndani kwake
ndipo akanifuata nje.” Naya akatulia kidogo.
“Sijui niseme moyo wangu umechoka au ni kama nimefika mwisho kwa
Malon! Sijui! Nimemlilia sana Malo mpaka nimefika sehemu najiambia haina maana
tena.” Wakamuona kama anafikiria. “Ni kama moyo umekubali kuwa Malo
hakukusudiwa na Mungu kuwa mume wangu. Naanza kuona kama hatukukusudiwa kuwa na
mwendo mrefu sana na Malo. Sijui ni kuchoka au la! Sijui. Ila nahisi sitaki
tena kupita kule nilikopitishwa na Malo. Nishamtafutia sababu nyingi mno ili tu
niwe naye tena, lakini naona haina maana tena.” Wote kimya.
“Kwa hiyo kujibu swali lako baba, sijawasiliana naye kwa kuwa
naona haina maana tena. Nimekuwa nikilazimishia mpaka naanza kujichukia!
Nikijifikiria, najiambia ni kwa nini nilifanya yote hayo! Naishia kujidharau tu.”
Naya akatulia kidogo na kuendelea. “Na yeye ndivyo alivyo. Ukimtafuta, anarudi
kama hivi. Atajaa kila mahali. Kisha anapotea. Na usifikiri haya anayonifanyia
mimi ni mimi peke yangu! Hapana. Malon ni mtoaji sana na ndio maana watu wengi
wanamng’ang’ania akiwa navyo. Anaweza kumpa kitu mtu mpaka ukashangaa.” “Basi
ndio maana hata akipoteza, Mungu anahakikisha anavirudisha mikononi mwake. Kwa
muda mfupi sana aliokuwepo huko Mbeya, ukweli anayo maendeleo. Nimempongeza. Anaonekana
anayo dira.” “Amefanya nini huko?” Bale akauliza kwa shauku kutaka kujua.
“Kwanza ameshanunua mashamba na hilo eneo alilojenga hapo shamba!
Si nyumba ya kisasa. Kawaida sana ya kijijini ila ghala lake ndilo la kisasa.
Anasema amechukua mfano wa huko Brazili alipokwenda. Anamashine nzuri sana
zakujua viwango vya kokoa na kahawa. Mashine za kubebea hayo magunia kutoka
chini mpaka juu kuyapanga kwa mpangilio. Haya, anazo mashine za kufunga vizuri
hayo magunia ili mazao yasimwagike hata yakiwa safarini. Ule uwezo wakufikiria
na kuweka fikra zake kwenye vitendo, ndio umenishangaza sana.” Baba yao
akamsifia Malon.
“Kwa hiyo Naya, humtaki tena Malon?” Zayon akauliza swali
lililowashangaza wote lakini wote wakataka kujua jibu. “Kwa hakika sijui
Zayoni. Ila kwa harakaharaka, kila nikimfikiria Malon, naona hakukusudiwa kuwa
mume wangu. Sasa hivi macho yamefunguka na kuanza kuona hana vigezo
ninavyohitaji kwa mwanaume ambaye nataka awe mume wangu.” “Anazo hela sasa hivi
na amekupa mpaka gari!” Baba yake akamwangalia Zayon, Zayon akajua hapo ndipo
anaambiwa anyamaze. “Haya anayonipa Malon, haina tofauti na atakachompa mwanamke
yeyote yule atakayekutana naye hata leo. Hata hii gari ningeikataa kabisa,
akatokea mtu mwingine akamuomba, angempa bila shida ndio maana nimeona nichukue
tu jasho langu, isiangukue kwa mwingine mimi nikaendelea kujitesa bure. Ni
mtoaji sana, Malo. Na sitashangaa hata nauli ya Rita ya kwenda Brazili na
kurudi ni yeye amelipia Malon! Ndio maana kila nikitafuta tofauti yangu na
wengine kwa Malon, sioni. Na nafikiri ndio maana nimefika mahali vinakosa
ladha.” Akatulia kidogo.
“Kinachoniuma zaidi ni vile alivyonipa pole yakufiwa na mama siku
ile!” Wote wakamwangalia. “Malon alisema aliambiwa na Rita walipokuwa safarini
kuwa nilifiwa na mama! Kweli alishindwa hata kutuma ujumbe wa pole au hata
aliporudi nchini alishindwa kuja nyumbani kutupa pole mpaka kutukuta sisi pale
kwenye kesi! Kila nikifikiria hayo najiona nalazimishia kitu ambacho hakipo.
Mimi nisingefanya hivyo hata kwa mtu baki tu. Kupotelewa na mzazi! Hakika hata
kama ni mtu ambaye hatukuwa karibu sana ila tulikuwa kwenye mahusiano ya
kufahamiana wazazi, ningetafuta wasaa wakutoa pole yangu.” Naya alisikika kama
aliyefika mwisho kabisa sio kama alivyosema hajui.
“Na kwa bahati mbaya safari hii ni kweli nimemkosea sababu yakumtetea
nafsini mwangu kama wakati mwingine. Mpaka nimeogopa na kujithibitishia ni
kweli nimefika mwisho. Sio sawa kuendelea hivi. Najichelewesha na tunapotezeana
tu muda. Hatuendi mbele, sisi siku zote ni tunaanza tu! Mambo yakikaa sawa
ukisema upo mwanga, Malo anarudi nyuma! Hapana. Naona lazima mimi ndio niwe mtu
mzima na nichukue hatua. Ili kutunusuru sisi wote wawili.” Wote kimya. “Mimi
nakwenda kulala baba. Nimefurahi umerudi nyumbani. Nitakuona kesho. Nimefurahi
ulivyofurahia jinsi nilivyobadilisha chumba chako.” Akamuona ametulia na
kuinama. Wote wakatulia wakijua zile taarifa za kuwa kimekuwa chumba chake, sio
cha mama kama walivyozoea kukiita, zimemuuma.
Naya akamchungulia baba yake kule alipo inama. “Nilimwambia hivi
Zayoni.” Baba yake akamwangalia. “Kuna Kawaida mpya Mungu ametuandalia
kwetu sisi wote. Kwa upendo kabisa. Lakini kwa kuwa ni mpya, wote hatujaizoea,
lazima kwanza tuikubali. Tuipokee, na kusaidiana jinsi ya kuiishi ili maisha
yaendelee. Je, itakuwa rahisi? Hata kidogo. Je, tunataka iwe hivyo? Hapana.
Lakini kwa kadiri tutakavyochelewa kuikubali, tujue ndivyo tutakavyojichelewesha
sisi wenyewe. Mungu yupo na sisi kwa hakika. Atatusaidia tu.” Naya akaongea
maneno ambayo baba yake hakutegemea. “Hii hekima ni mpya mama. Itabidi niondoke
ili uendelee...” “Hakuna kuondoka tena baba.” Naya akakataa na kusimama kabisa.
“Tutapambana hapahapa mjini mpaka kitaeleweka tu. Lakini sio kwa wewe kuondoka tena.”
Akaingia chumbani kwake na kuacha wote wapo kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati analala, akaangalia simu yake. Akakuta Malon alimpigia mara
tatu. Akamrudishia simu yake. “Mbona kama unanipuuza Naya?” Malon akaanza kwa kulalamika akisikika kugomba
kidogo. “Nashukuru baba amerudi salama. Asante kwa kuwa naye huko. Tulikuwa
tukipata mlo wa pamoja.” Malon akapoa kidogo. “Mzima lakini? Mbona ni kama inakuwa
ngumu kukupata?” “Sijui kama nilikwambia? Nilipata kazi. Na kazi niliyosomea
pale nimewekwa kwenye masoko, ndiyo, lakini upande wa matangazo. Nakuwa busy
haswa.” Malon akajua ni sababu tu kwani alikuwa akimsikia akizungumza na
baba yake mara kwa mara.
“Sasa bado unaifurahia hiyo kazi?” “Ni kazi Malon.” Akajibu
hivyo tu. “Sawa ni kazi. Lakini wewe unaifurahia?” “Siwezi kulalamika. Ni
hatua. Naamini siku moja nitafikia malengo tu.” “Mungu atatusaidia. Kwani sasa
hivi badala ya hiyo ungetamani kufanya nini?” Malon akauliza. Lakini isivyo kawaida
akamsikia Naya anacheka taratibu. “Mbona unacheka Naya!?” “Usiku mwema
Malon. Mungu azidi kukubariki.” “Mbona unaniaga ukiwa hujanijibu swali langu?”
“Kwa kuwa naona haina maana Malon. Hata nikikwambia TENA, itasaidia nini?” Malon akatulia
kidogo. Akanyamaza.
“Usiku mwema Malon.” “Subiri kwanza Naya! Unamaanisha nini?” “Juu ya
nini tena? Au kutaka kujua mipango yangu?” “Ndiyo, nataka kujua.” “Kwa ugeni upi
ulio nao kwangu, Malon?” Malon akanyamaza. “Yaani unataka kuniambia ghafla hunijui
wala kutambua chochote kile juu yangu?!” Naya akauliza vizuri tu lakini kama
anayemshangaa. Kimya. “Yaani kwa muda wote huo tuliokuwa wote! Machozi yote hayo
niliyomwaga kwako kama mpaka leo hunijui! Tunaulizana maswali kama hayo! Basi
haina maana hata nikikwambia tena Malon. Wewe subiri kusherehekea mafanikio
yangu kama mimi ninavyosherehekea ya kwako unapopambana na kufanikiwa. Acha na
mimi nipambane, nikitokea upande wa pili kama wewe, nitakushirikisha.” Naya akawa
amekasirika kidogo, akashindwa kukata simu. Akaendelea.
“Kwanza kuniuliza maswali kama hayo sasa hivi ni kunidhalilisha na ni kama unakusudia kuniumiza tu, Malon! Unakuwa na wewe ukinidhihirishia kuwa muda wote tokea nakufahamu mpaka sasa, nimekuwa nikipoteza tu muda kwako! Tafadhali acha wengine na mimi mwenyewe nijiambie hivyo ila wewe nihifadhie heshima au stara, usiseme. Hata kama unajua nilikuwa nikipoteza muda kwako, tafadhali usiseme. Acha mimi niendelee na mipango yangu pamoja na maono yangu, ila tu pengine njia yakufikia ndio Mungu ananibadilisha mtazamo.” “Mtazamo wako ni upi ambao Mungu anakubadilisha?” Malon akauliza tena. “Usiku mwema.” Naya akaaga na kukata simu. Alimjua Malon huwa anachagua kitu gani ndio chamsingi na kipi chakupuuza. Akaona anapoteza tu muda na kujiudhi zaidi. Malon akapiga tena lakini Naya hakupokea na huo ndio ukawa mwisho wakupokea simu za Malon. Hata alipokuwa akimpigia hakuwa akipokea tena.
Kakumbuka Shuka kumekuchwa.
M |
alon alipoona
siku zinazidi kwenda simu zake hazipokelewi tena wala Naya hajibu jumbe japo
hakumfungia simu zake, akajua amekusudia kumpuuza. Akafikiria nani wakuzungumza
naye, akapata wazo la Zayon. Akampigia simu muda ambao alijua Naya atakuwepo
kazini na yeye ndio anatoka tu shule. Baada ya salamu akamuuliza. “Naya yupo?”
“Mimi nilijua unanipigia sababu upo naye anataka kuzungumza na mimi?!” Malon
akashangaa kidogo. “Kwani Naya yupo Mbeya?” “Walikuja huko kikazi kufanya matangazo.
Yupo huko tokea...” Zayon akajaribu kukumbuka lakini akaonekana kuchukua muda mrefu
bila yakupata jibu. “Wapo sehemu gani?” Malon akaona aulize kabla yakujua ni kwa muda
gani amekuwa huko. “Baba ndio atakuwa anajua zaidi. Mimi nahisi nimesahau, kama
alisema. Kwani kweli hajakutafuta?” “Bado.” “Basi pengine alichosema ni kweli.
Maana mimi nilimwambia Bale pengine Naya anaongea tu kwa kuwa hajisikii vizuri.
Nikamwambia pengine atabadili mawazo baada ya baba kumwambia umejijenga sana.
Ndio Bale akasema hajawahi kumsikia Naya akikuzungumzia vile hata mara moja. Na
Naya yupo kama baba. Akifika mwish...” “Alisema nini?” Malon
akaendelea kudodosa.
“Amesema yeye amegundua wewe sio mwanaume wakuja kuwa mume wake. Amepata muda wakufikiria, amegundua wewe siye, ndio maana alikuwa akihangaika sana na wewe bila mafanikio. Ni kama mtu aliyekuwa akitaka machungwa kwenye mti wa maembe. Umeelewa mfano wangu?” Akauliza Zayon. “Hiyo ni kwa kifupi tu, nimefikiria mwenyewe kwa jinsi alivyokuwa akiongea siku ile lakini sio kwamba yeye ndio amesema! Ni mimi tu na akili zangu.” Akawa kama anajisifia, Malon kimya.
“Anasema hata sasa hivi tunakuona ni kwa sababu alikufuata kukapa zawadi ya shukurani. Bila hivyo usingetutafuta tena. Anasema kinachomuuma ni vile alivyojua kuwa mama alifarikia, lakini pia hukuja kutoa pole hata kwa ujumbe ulipokuwa huko safarini au pale uliporudi kutoka Brazili pia hukuja hapa nyumbani kutupa pole ni mpaka tulipokuja siku ile pale kwako wakati mwanamke wako alipomsingizia...” “Anaitwa Rita.” Malon akarekebisha akiwa ameishiwa nguvu kabisa.
“Ehe! Huyohuyo Rita mwanamke wako. Anasema inamaana kama
tusingekutana na wewe siku ile kwenye lile tukio la kumsingizia Naya, inamaana
hata hukuwa na mpango wa kuja kurudi kwetu hata kutoa tu pole yakumpoteza mama.” Malon
akaumia sana. Akajua ndio maana Naya amekuwa mzito sana kwake. “Mwenzio Naya
hakutaki tena. Amesema ameshalazimisha mahusiano mpaka moyo wake ume...” Zayoni akawa
anajaribu kufikiria tena. “Ehe! Alisema moyo wake ni kama umekinahi. Hataki
tena.” “Unazungumza na nani?” Malon akasikia sauti ya baba yao akimuuliza
Zayoni. “Naongea na Malon.” Akajibu Zayoni na kuendelea.
“Mwenzio Naya siku ile alikuwa hadanganyi baba! Hajamtafuta tena Malon.” “Umalize, uje ule.” Malon akasikia mlango umefungwa baada ya hayo maagizo aliyopewa na baba yake bila yakumjibu juu ya Naya. “Malon!” “Nipo Zayoni.” Malon akaitika. “Baba anataka nikale. Mwenzio sijala shule. Nilikuaga nakula na mama shuleni. Sasa, sasa hivi siwezi kula tena peke yangu. Nakuja kula nyumbani.” “Pole sana Zayon. Na asante kupokea simu yangu. Msalimie sana baba na Bale.” “Watasikia.” Akajibu kama mama yake, Malon akajua huyo mtoto ni kweli alikuwa wa mama. Akakata simu lakini asiamini alichosikia.
Ofisini Kwa Kina Naya.
Baada yakumpigia tena simu Naya na kutopokea, akaamua kupiga simu ofisini kwa kina Naya. Baada ya sekretari kupokea, akaomba aunganishwe na idara ya masoko. Akatumia akili kuuliza swali lake mpaka akajua watu wa idara ya matangazo, wapo soko la Mwanjelwa, hukohuko Mbeya wakifanya maonyesho ya vinywaji vyao. Kwa hiyo Malon akajua hata hoteli waliyofikia. Naya na timu ya wafanyakazi wenzake walitangulia ndipo wakafuata viongozi wao wawili kuhitimisha. Ilikuwa ni kazi ya siku 5 tu. Mida ile ile ya jioni akatoka shamba kumfuata Naya mjini.
Mbeya.
H |
uku kwa Naya
kazi ikaendelea siku hiyo nayo walikuwa sokoni siku nzima. Miziki, nyimbo na
matangazo ya hapa na pale wakijitahidi kunadi bidhaa zao mpaka wakamaliza. Waliporudi
hotelini yeye hakutaka kula, akapitiliza chumbani kwake kulala akawaacha wenzie
upande wa baa wakila, kunywa kwa kutapanya na kucheka wakipeana habari nyingi
tofauti tofauti. Viongozi wao waliungana nao huko sokoni Mwanjelwa, siku hiyo
ya mwisho.
Naya na wenzie wawili walionza kazi siku moja wao ndio walikuwa
wageni ila hao binti wengine ambao walikaribiana sana umri ila wadogo kidogo
kwa Naya walishaanzisha mahusiano hapo hapo. Mmoja ambaye alionekana mrembo
zaidi, haraka sana akaanzisha mahusiano na mfanyakazi wa hapo ila ngazi ya juu
kitengo kingine cha waajiri, na mwenzao yeye alianzisha na mmoja wao hapohapo
kitengo cha masoko ila yeye alikuwa mwenyeji. Alianza kazi kama miaka miwili
iliyopita. Na walikuwa pamoja safarini na walichukua chumba kimoja. Wote hao na
wapenzi zao na wengine waliwapata wanaume hapohapo baa na kuwaganda ili
wawanunulie pombe, walikuwa baa wakiendeleza starehe kwa raha zote wakati Naya
yupo chumbani akiuchapa usingizi baada ya jua kali la siku nzima.
Aliamka mida ya saa 12 jioni. Akaoga vizuri, akajitengeneza
vizuri tu akiwa bado na nywele yake aliyokuwa ameisuka karibu mwezi umepita,
ila bado aliitunza vizuri akibania pesa. Akaweka hereni ndogo tu masikioni. Ndipo
akatoka kwenda kutafuta chakula. Kadiri alivyokuwa akisogelea eneo lililopo
mgahawa na pembeni baa hapohapo ndani ya hiyo hoteli nzuri sana hapo mjini,
ndivyo alivyokuwa akisikia sauti za wenzake wakishangilia kilevi haswa. Akaelekea
upande wa chakula na kuagiza chakula na kwenda kukaa. Kimya, macho kwenye
luninga ndogo iliyokuwepo hapo mbele ya macho yake mgahawani. Akatulia.
“Acha na mimi nikae hapahapa wakati nasubiria chakula changu.”
Naya alishituka, akajikuta anasimama kwa haraka bila kutarajia. Alikuwa Joshua
Kumu, mmoja wa viongozi waliokuja kuungana nao, kuhitimisha hayo matangazo
mjini Mbeya. Ila yeye ndio mkuu wa idara nzima ya masoko. “Sasa mbona unataka
kunikimbia?” Naya akacheka kwa wasiwasi mwingi usoni. “Si na wewe unataka
kula?” “Nimeshaagiza, ndio nasubiria.” “Utajali mimi kukaa hapa?” “Hapana.
Karibu tu. Nilijua mpo na mwezio ndio niwapishe.” Naya aliropoka tu kwa hofu.
Kwani kulikuwa na viti vingine vingi hapo pembeni yake. Kwa nini watake meza
aliyokaa yeye na ya watu wawili!
“Hapana Naya. Nipo peke yangu.” Joshua akajibu huku akijiweka sawa
kitini akijua wazi Naya amepaniki. “Vipi kazi?” Joshua akamuuliza akiwa bado
amesimama pembeni ya meza. Ilikuwa ni kitendo alichokifanya bila kutarajia,
alisimama kama mshale. “Tunaendelea vizuri.” Naya akajibu kwa kifupi tu akabaki
amesimama kama aondoke. “Karibu kiti chako Naya.” Naya akaangalia kile kiti,
akarudi kukaa taratibu kwa kujihami. Kumu ni bosi wake wakuheshimika haswa.
Akae naye meza moja! Akabaki hajui ashike wapi au afanye nini mbele yake. Ila
akagundua anamtaja mpaka jina lake! ‘Atakuwa amenijulia wapi mimi wakati
hata leo sikuwa nao pale jukwaani!?’ Akawaza Naya akiwa amejawa hofu. ‘Pengine
sijamsikia vizuri, hajanitaja jina langu! Mtu kama huyu hawezi kujua jina
langu.’ Naya akaendelea kuwaza.
Akamwangalia akidhani hamwangalii. Akagundua Joshua anamwangalia
kwa karibu tu. Naya akacheka tena kidogo. Lakini alionekana amejawa hofu haswa na
Joshua alitambua hilo. “Vipi lakini? Naona kazi mliyoijia mmeifanya vizuri na
mmemaliza. Kesho ndio tunarudi Dar, au wewe umepata mwenyeji?” Joshua akajaribu
kumtupia tena swali la kiuchokozi ili tu kuwe na mazungumzo. “Hapana nitarudi
tu nyumbani.” Joshua akacheka vile alivyojibu bila ya nyongeza. Naya
akajishitukia ikabidi ajitulize kwa kumuuliza swali ambalo hata halikuwa na maana kwake. “Kwani wewe unabaki?” Joshua akajua wazi ameropaka tu hilo swali, hajamaanisha. “Hapana. Ila
nimesikia wenzio wanamalizia weekend huku, nikajua na wewe unataka kuunga
tela.” “Hapana. Naona mimi nitarudi tu. Nikakuagizie kinywaji gani?” “Kumbe na
ukarimu pia unao?” Naya akacheka akisimama. “Nashukuru. Maji yatatosha tu.”
Naya akaondoka hapo na kupumua kwa nguvu akijishika mapigo ya moyo.
Joshua Kumu.
S |
i kwamba
hajawahi kumuona Joshua. Alishamuona zaidi ya mara moja akiwa na wasaidizi wake
yeye binafsi wakaribu, wawili, katika vikao vya kitengo, ila hakuwahi kudhani
kama anaweza hata kumuongelesha kwani ni mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu sana
kwenye kitengo chao na kampuni ya Cocacola. Amebeba sifa kubwa sana kwenye
hicho kiwanda. Naya alimfahamu hata kabla hajamuona. Na Jamal ambaye ni
kiongozi wao wa idara yupo chini yake kwa hiyo kuzungumza na mtu kama Naya,
ilikuwa ni kitu kisichowezekana. Kwa nini! Kwanza alikuwa mgeni kabisa kwenye
hiyo kampuni. Ngazi ya chini kabisa ambaye hata bado hakuwa amepata ajira ya kudumu,
bado yupo kwenye ajira ya muda, wakichunguzwa utendaji kazi wao ndipo waweze
kuingizwa kwenye ajira ya kudumu kama Jamal angeridhika nao.
Mtu kama Joshua hakuna kitu anaweza kuhitaji kutoka kwake. Angalau
Jamal na kiongozi wa Jamal hapo idarani
ndio wanaweza kuzungumza naye. Japokuwa alikuwa na wasaidizi wawili
wakaribu mbali na sekretari wake yeye tu, Naya alijua huwa anazunguka na msaidizi
wake binafsi anayeshugulikia au kuratibu ratiba za Joshua Kumu tu. Nani amuone
na saa ngapi. Nani azungumze na Kumu na kwa muda gani. Nini afanye siku hiyo,
nani amuone na nani anazungumza naye tu kwa simu, asimuone, tena kwa muda gani
ili mambo yasigongane. Yeye ndiye aliyekuwa akipokea maagizo na simu za Kumu kutoka
kwa sekretari wa ofisi yake Kumu, na kuzikaimu. Alijulikana kwa jina la Jema. Kwa
ufupi, hakuna jinsi ya kuzungumza au kumuona Kumu kama sio vikaoni kama
hujapitia kwa Jema na akaidhinisha.
Walimjua Jema kwa kuvaa vizuri hapo kwenye kampuni. Usingemkuta na
kiatu cha chini hata siku moja. Waliwajua yeye Jema na Njama wanaringa kama
bosi wao Kumu, na unadhifu vilevile. Na kwa kuwa Jema hakuwa akivaa sare za
kampuni kama wafanyakazi wengine wa kampuni, watu walikuwa wakitaka kumuona
kila anapopita. Nadhifu haswa. Na Njama vilevile. Tai wakati wote kama Kumu.
Njama alikuwa upande wa utendaji. Akiongea Njama, ujue ndio Kumu. Japokuwa
alikuwa msaidizi wake, lakini Njama aliheshimika sana na yeye kwa kuwa ndiye
aliyemuwakilisha Kumu kwenye vikao vingi vya idara na vitengo akihakikisha
mambo yanakwenda.
Lakini safari hiyo hakuwa nao hao wote wawili. Hakujua ni kwa nini
maana hata kwenye vikao ambavyo Naya alibahatika kuhudhuria, na Kumu mwenyewe
akawepo kuviongoza si Njama anayemuwakilisha wakati wote, hakuwahi kumuona Joshua
bila hao watu wawili. Njama na Jema. Na alizijua sifa za Joshua nyingi sana kwa
minong’ono waliyoikuta hapo kwenye kampuni tokea siku ya kwanza wanaingia hapo,
kuwa analipwa pesa nyingi sana kwa kuwa walimnunua kutoka kampuni nyingine, kwa
uwezo mkubwa sana wa kufikiri na kutenda bila kukosea. Akaambiwa yeye ndio
ameshika soko la bidhaa ya kampuni nzima nchini. Hakuna anachosema yeye,
kisifanyike hapo hata makaburu wanamtetemekea. Yote hayo Naya aliyasikia hata
kabla hajamuona Joshua Kumu mwenyewe. Sasa amekaa mbele yake! Naya alitamani
kukimbia asirudi tena pale, lakini alimwagiza maji, ikamlazimu kurudi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda akarudi pale mezani akiwa na maji tu. “Mbona sioni
kinywaji chako?” “Nimewaomba chai. Nasikia baridi naona chai itanituliza.” Naya
akarudi kukaa akifikiria atazungumza nini na Joshua! Alishakuwa na hofu na kina
Joshua sababu ya Joshi aliyejaribu kuwa naye kwenye mahusiano vikashindikana
sababu ya tabia zake ngumu, akahisi yatakuwa ni yaleyale tu hata kwa Joshua
huyu ambaye wanamuita mungu wa Coca. Akatulia akijiwinda.
“Nasikia Mbeya kunakuwa na baridi muda mwingi.” “Hii ndio mara
yangu ya kwanza kufika huku.” “Basi jiandae kuzunguka sana. Kitengo hiki kuna
kuzunguka mno.” “Nimesikia.” Naya akajibu huku akiangalia kama anayeomba Jamal
afike hapo, akae na bosi wake, yeye aondoke. “Niambie mikoa mingapi hapa
nchini, ulishawahi kufika?” Naya akacheka kidogo kwa wasiwasi akijaribu kuvuta
kumbukumbu akirudisha akili zote hapo bila mafanikio kwa hofu. “Sio lazima uwe
umekaa hapo kama hivi.” “Kwa hiyo hata kupita tu?” Naya akauliza. “Hata kupita
ukiwa ndani ya gari.” Naya akacheka tena kidogo ila safari hii akaonyesha hofu
imeanza kupungua. “Iringa. Tumepita wakati tunakuja huku.” Akapataja kwa haraka
kama aliyekumbuka hilo jina. “Ehe?” Joshua akataka aendelee huku akifungua maji
yake.
“Morogoro.” Akaongeza. “Napo ulipita kama Iringa?” “Ndipo
niliposomea huko shahada yangu ya masoko.” “Saafi sana. Ulimaliza mwaka gani?” Kidogo
wakaanza kuzungumza akamuona Naya ameanza kutulia. Wakaongea mengi akimdodosa
hili na lile na yeye akimueleza mambo ya kawaida sana wala si ya kazi mpaka
chakula kikaletwa, akamuona Naya ametulia kabisa hofu imepungua kwa asilimia
kubwa sana.
“Niambie stori yako Naya.” “Ipi tena?” Naya akamuuliza wakati
anajisogezea chakula chake karibu. “Kwa mujibu wa ulichonieleza. Ulimaliza chuo
huu unakaribia mwaka wa pili kuisha. Umeniambia huna mpango wakurudi chuo hivi
karibuni au unaweza usiendelee kusoma tena. Sasa mbona hicho kidole kitupu?”
Naya akajiangalia na kucheka taratibu. “Jamaa anasubiri nini?” Akamuuliza tena, ila bado Naya akashindwa
kujibu. “Maana kwa hivyo ulivyo, lazima najua yupo mtu. Sasa nashangaa kwa nini
aweke kimya kirefu kwenye mikono mizuri hivyo!?” Naya akacheka tena taratibu
bila yakumwangalia. Akakalia mkono wake wakushoto ambao ungetakiwa kweli kuwa
na hizo pete.
Joshua akacheka. “Sasa
ukikalia mikono utatumia nini kula?” Naya akamwangalia. “Na wewe stori yako ni
ipi?” Naya akamtupia na yeye swali bila yakujibu. Joshua akacheka sana. “Acha
kuiga maswali Naya! Mimi ndio nimeanza kukuuliza.” “Mimi sina stori ndefu. Ni
sikubahatika tu.” “Mmmh!” “Huamini?” “Hapo ndipo kwenye stori kwenyewe.” “Ndio
nimemaliza hivyo. Na wewe niambie ya kwako.” “Na mimi ni kama hiyohivyo ila ipo
stori zaidi ya hiyo.” Naya akacheka. “Niambie stori yako.” “Kweli unataka kujua
au unaiga tu?” Naya akafikiria kidogo, Joshua akimtizama. Wakaangaliana. Naya
akarudisha tabasamu. “Umeshagundua hukuwa na haja yakujua eeh?” Joshua akamuuliza.
“Hapana. Ila kama hutajali, sio mbaya nikajua. Wakati mwingine
tunajifunza kupitia wengine.” “Sasa kwa nini hutaki mimi nijifunze kutoka
kwako?” “Ni kwa sababu mimi sina historia nzuri ya kujifunza. Labda nikwambie
hivi. Kutoka katika lile jibu la kutobahatika, ni kama vile uwe unafriji yako
ndani. Umeinunua kwa gharama kubwa, kutokana na uwezo wako. Ukatoa pesa yote
benki, ili kuimiliki hiyo friji na kuiweka ndani. Ukishakuwa nayo, unagundua
haina uwezo wa kukupa kile ulichokwenda umbali mkubwa sana kuigharamia ili kuwa
nayo.” Joshua alikuwa akimsikiliza kwa makini sana.
Akamuona Joshua anakunja uso. “Kwamba hata maji ya kunywa tu
huwezi kupata yakiwa yamepoozeshwa!?” Joshua akauliza kwa utulivu tu. “Haina
hata huo uwezo mdogo.” Wakacheka. “Mmmh! Ukipeleka kwa fundi?” Akauliza tena
Joshua na kuweka chakula kidogo mdomoni. “Kwani huo ushauri wako nimetendea
kazi mara moja?” “Eeh?” “Kazi inakuwa inabakia ni ya kupeleka kwa fundi tu kila
siku na bado hakuna mabadiliko.” “Badili fundi. Nahisi mafundi wako sio
wazuri.” Naya akacheka sana na Joshua akacheka.
“Kweli kabisa. Inawezekana hujapata fundi sahihi.” “Nilijaribu.
Nikapata fundi aliyeongeza nguvu zaidi. Matokeo yake ikawa kugandisha sasa.”
Joshua akacheka, akacheka sana. “Kwamba tatizo likabakia palepale?” Joshua
akauliza akicheka. “Pale pale. Ila tu kilichobadilika ni aina ya tatizo. Ukitaka
maji ya kunywa, yote ni barafu. Hapo unakiu, na huna chakufanya. Na ni zaidi ya
mara moja. Zaidi ya siku moja, Juma, miezi hata miaka. Tatizo lipo palepale.”
“Aisee pole sana. Hatima?” “Swali zuri sana.” “Jibu lake?” Joshua akazidi
kudodosa. “Nitakuja kukwambia siku nyingine.” “Kwa nini sio sasa?” Akamuona ametulia kama anayefikiria.
“Eti Naya? Au hujapata jibu?” “Nafikiri akili, moyo, nafsi na
mwili au kila kitu ndani yangu vimepata jibu. Nipo katika kulipokea hilo jibu.
Nikiweza kupokea na kuliweka sawa, nitakuja kukujibu wakati mwingine, Mungu
akitujalia nafasi.” Joshua akamtizama na kuendelea kula. Pakatulia kidogo.
“Na wewe stori yako ni ipi?” Joshua akacheka kidogo. “Nilitaka
uniulize ndio niseme. Sikutaka nionekane kimbelembele.” Naya akacheka. “Hapana.
Nataka kujua.” “Na mimi sio ndefu sana. Ni ubora wangu ndio ulipungua au
haukufika kiwango. Naona akanichoka na kuamua kuolewa na mwingine.” Naya hakutegemea
stori ya aina hiyo. “Joshua Kumu!” Akawaza na kubaki akimtizama. “Kwa hiyo
nikapatwa na hofu tokea yeye mpaka leo. Nikapatwa na tatizo la kuamini tena
mahusiano. Maana mengi aliyafanya nikiwa naye, lakini sikuwahi hata kumdhania
kwa jinsi nilivyokuwa nimejifunga kwake.” “Na wewe ulipelekwa kwa fundi mara
ngapi, mpaka akanyanyua mikono?” Hilo swali lilimfanya Joshua acheke
sana. Alicheka tena na tena.
“Maana haiwezekani ukimbiwe tu!” Moja kwa moja Naya akamfananisha
na Joshi aliyejaribu kuwa naye. Kwa tabia kama zile, Naya mwenyewe aliyekuwa
akitamani kuolewa alinyanyua mikono. “Aisee inawezekana Naya. Unaweza
ukakimbiwa kabisa bila hata huruma. Kuna watu wanaroho ngumu! Wana roho ngumu
mno! Unaachwa mchana kweupe hivi, ukiambiwa unapendwa ila viwango duni. Hakuna
ubora.” “Na hapo ni papana sana. Mno. Kwa sababu ubora unatofautiana kwa kila
mtu na mtazamo wake.” Ikabidi Joshua amsikilize vizuri.
“Hebu niambie vizuri Naya.” Naya akacheka maana alizungumza kutoka
mawazoni tu hakujua kama Joshua angetilia maanani. “Japokuwa sijui ni uduni upi
uliokufanya uachwe, lakini ninachotaka kukwambia, sio kipimo cha wote. Usiogope
na kujifungia milango.” Naya akajieleza taratibu tu.
“Nipo hapo kwenye kujishauri mimi mwenyewe pia. Najiambia hivihivi
ndio na wewe nakwambia. Inawezekana kwake yeye udhaifu aliouona, ikawa sio
kipaumbele kwa mwanamke mwingine. Tunatofautiana.” “Niambie aina nyingine ya
uduni mbali na pesa!” Naya akacheka kwa kusikitika. “Sijui mtazamo wako Joshua.
Lakini mimi binafsi nimekinahiwa na mapenzi yanayochanganywa na pesa. Nimechoka
kusikia hivyo vitu vikiwa vinaenda pamoja! Hakika nimechoka sana. Ila tuache
tu.” “Hapana Naya. Wewe ni miongoni mwa watu wachache sana hapa duniani haswa
wanawake wanaosema hivyo vitu huwa haviendi pamoja.” “Ni kweli. Hata mimi mpaka
sasa hivi katika wanao nizunguka, asilimia 99, kasoro baba yangu tu, lakini
wengine wote wanaamini mapenzi lazima yatiwe nguvu na pesa. Ni mahubiri nimekuwa
nikiyasikia tokea nakua na kujijua mimi ni mtoto wa kike mpaka sasa nahisi
imenigharimu sana.” “Pole.” Naya akacheka akifikiria.
“Unajua mimi, Joshua. Samahani bosi wangu. Nikuite tu hivyo au
kiongozi kama wengine wanavyokuita.” “Joshua itatosha. Niambie tu.” “Eti mimi nafikiri
hivi. Sijui kama utakubaliana na mimi. Ila kwa sababu ni kitu kipo moyoni
mwangu, najiambia ni kweli na ni halisi.” “Kuhusu nini?” “Mapenzi ya dhati
kwanza. Kisha pesa au maendeleo yavutwe na nyinyi wote wawili.” Joshua
akatingisha kichwa akikubali kwa hisia zote.
“Inawezekana sio hivyo inavyotakiwa, ila mimi napenda iwe hivyo.
Na ninaamini katika wawili kunia pamoja. Haijalishi wapi mnaanzia. Lakini kama
inawalazimu kuanza hata chini kabisa, iwe pamoja. Halafu kuwe na chetu,
sio changu au chako kati yenu nyinyi wawili. Au mkiwa wawili kusiwe na
kuhesabiana kwamba mimi nimemzidi mwenzangu kipato! Halafu kunatokea mvurugano,
kutoelewana, kutengana sababu ya mali! Sijui. Lakini mimi ndivyo ninavyotaka
iwe, na nafikiri ndivyo nitakavyofanya maishani. Sitaishi vinginevyo. Nimeona
wengi wanao ishi hivyo, hakika sijaona kama wamefanikiwa sana! Sijui lakini.
Pengine sijawahi kuzungukwa na mifano mingi, lakini naamini yupo mtu sehemu
fulani, anafikiri kama ninavyofikiri mimi na pengine wanaishi ninavyofikiri
mimi na wamefanikiwa tu. Naamini wapo hao watu Joshua. Na ninahisi wanautulivu
mkubwa sana zaidi ya utulivu wakuwa na mali nyingi.” Joshua akamwangalia kwa
kumfurahia sana Naya. Akaendelea kula huku akimtafakari Naya zaidi.
Malon Tena!
Wakati Naya na Joshua wanaendelea kula, akashangaa Malon
anamuwekea chai mbele yake. “Malon!” Alishituka
sana, hakutegemea hata kidogo. Malon akabakia akimtizama. “Asante kwa chai.
Kwanza umejuaje kama nataka chai?” “Nilikusikia wakati ukiagiza.” Naya akakunja
uso. “Hukuniona, ila mimi nilikuona.” Akajua alikuwepo pale muda mrefu tu.
“Oooh!” Naya akajibu tu hivyo na kuvuta chai yake na kuinywa kidogo. Akagundua
kuna ukimya pale. Akajua anatakiwa kutoa utambulisho. “Joshua, huyu anaitwa
Malon.” Akamgeukia Malon. “Huyu anaitwa Joshua. Ni kiongozi wetu upande wa
masoko. Amekuja kufunga kazi iliyotuleta huku.” Joshua akasimama na kumpa
mkono.
“Sasa sijui nikukaribishe au?” Joshua akauliza. “Malon ni mfanyabiashara.
Kwa hiyo na huku nako ni kama kwake. Anaweza kuwa mwenyeji kuliko sisi.”
Akaongeza Naya na kuendelea kula bila hata kumtizama tena Malon. “Basi
tushukuru kwa mji wenu huu.” “Karibu sana.” Malon akajibu na kumgeukia Naya,
Naya akiendelea kula. Joshua akashangaa kidogo na kuamua kukaa kama asiyejua
chakufanya.
“Karibu chakula Malon. Cha mchana ndio kinaliwa sasa hivi.” Ikabidi
yeye Joshua ndio azungumze. “Nashukuru kaka.” Akajibu Malon macho kwa Naya.
Naya kimya ameinamia sahani yake. Joshua akaangalia ile hali pale akawa hajui
chakufanya. Malon amesimama akimtizama Naya, Naya ni kama hamuoni. “Nimekufuata
wewe Naya.” Malon akavunja ukimya, Naya akamtizama. “Oooh! Nilijua upo kwenye
shuguli zako za kikazi. Karibu ukae.” “Hii meza ni ya watu wawili Naya!” “Basi
nisubiri nimalize kula, nitakufuata ulipo ili tuzungumze. Sikula siku nzima. Na
mimi njaa inaniuma.” “Au mimi niondoke tu?” Akauliza Joshua, Naya hakujibu akaendelea
kula. “Ili kuwapa nafasi.” Joshua akaongeza lakini Naya kimya. “Nitashukuru
Joshua.” Yeye Malon ndio akajibu. Joshua akasimama na sahani yake.
“Basi tutaendelea kuonana Naya. Jioni au usiku mwema.” “Asante na
wewe.” Akajibu kwa heshima. Joshua akapiga hatua kadhaa, kisha akarudi.
“Nilitaka tu kukwambia, was nice talking to you, Naya.” Malon alikuwa akikaa
wakati Joshua akimwambia Naya alifurahia mazungumzo yao. Malon akamwangalia
Naya, akamuona anacheka kisha akamjibu, “Asante.” Ndipo Joshua akaondoka na
kuwaacha hapo.
“Naona unabahati ya kina Joshua?” Naya akacheka. “Naona Mungu
anawaleta tu kwangu! Sijui anataka wanifikishe wapi!” Hicho kikamuuma Malon.
Akajua Naya anazungumzia Joshua wa bibilia aliyewafikisha wana wa Israeli nchi
ya ahadi baada ya kuteseka sana nchini Misri, Musa ndiye aliyeanza nao,
kuwagombania mpaka kuwatoa huko utumwani Misri, kwa ahadi nzuri lakini akafa
njiani kabla ya kuwafikisha nchi
waliyoahidiwa na Mungu ndipo Joshua akafanikiwa kuwafikisha nchi ya ahadi. Naya
akaendelea kula. “Mbona imekuwa shida kukupata kwa simu?” Akauliza Malon.
“Nakuwa na kazi Malon! Hilo nilishakwambia. Juma hili zima tunashinda sokoni.
Nikirudi hapa nakuwa nimechoka. Nikishazungumza na baba pamoja na Zayoni, siku
inakuwa imekamilika. Sina nguvu ya kuzungumza na mwingine yeyote yule.” “Lakini
umezungumza hapa na Joshua kwa muda mrefu sana!” “Hilo nalo ni kosa kwako?”
Naya akamuuliza taratibu tu.
“Labda nikuulize Malon, kwa nini upo hapa?” “Nimekufuata wewe.”
Naya akakunja uso kama hamuelewi. Akamtizama kisha akamuonyesha kama
anajipotezea muda, akaendelea kula. “Mbona unanishangaa?” “Nashangaa hiyo
juhudi yakunitafuta mpaka kunifuata hapa inatoka wapi Malon! Unatuma jumbe na
kupiga simu kila siku mpaka nashangaa! Ni nini kinaendelea safari hii?” “Naya.
Nimeahidi kubadilika.” “Mimi nashauri utafute usemi mwingine maana huo ushakosa
nguvu au niseme umepoteza maana kabisa, Malon.” “Sasa hivi nimeokoka Naya!”
Naya akacheka akimtizama.
“Acha kunidharau Naya!” “Wala si kukudharau Malo. Ila najicheka
mimi mwenyewe, jinsi hayo maneno yanavyosikika tofauti na zamani.” “Unamaanisha
nini?” “Nikuulize swali Malon?” “Mbona mimi hutaki kunijibu?” “Nikuulize swali?”
“Sawa.” “Rita ulimfahamu ukiwa umeokoka au hujaokoka?” Malon akatulia kidogo.
“Eti Malon?” “Mbona mambo ya Rita nilishajieleza kwako?” “Taratibu tu Malo.
Jibu swali.” “Najua jibu unalo Naya.” “Sawasawa. Nilipokuja nyumbani kwako,
kubaki na mtoto wa Rita ambaye alikuwa mpenzi wako, tukiwa watatu na mtoto, mpaka njiani
kuelekea uwanja wa ndege ukimsikia Rita akininyanyasa kwa gari na mengineyo.
Uliweza hata kunitambulisha kwake kuwa unanifahamu?” Malon akaishiwa nguvu kabisa.
“Uliporudi naye je? Nikawapokea uwanja wa ndege mpaka kufika
nyumbani kwako tena. Hukuona sababu ya kunitambua wala kunipa hata pole ukiwa
umejua nimepoteza mama. Ukajifanya kama hunifahamu kabisa mpaka siku ile
nimekuja kwenye kesi nyumbani kwako nikiwa na ndugu zangu ndipo ukatamka eti
kuwa ulikuwa ukinifahamu na kutupa pole! Kuonyesha sina thamani kwako, hata
kesho yake au juma hilo hukufika nyumbani kuja kuniona mpaka nikakufuata kukupa
zawadi! Tena ukaniambia kabisa ulikuwa ndani ukisoma tu kitabu, kuashiria
haukuwa na kazi nyingi kushindwa kuniona au kufika nyumbani kutuona! Halafu eti
sasa hivi ndio unaonyesha kuna ulazima wa mimi kujibu jumbe zako na simu! Kweli
Malon? Ni kunidharau kwa kiasi gani huko?” “Sikudharau Naya.” Naya akacheka.
“Unajua Malon, nimepata muda wa kukufikiria sana. Nikagundua sikutendei haki. Hata katika hili na mengine mengi, si sawa kwako. Nakuwa nikikudai vitu ambavyo huna uwezo wa kunipa. Usiku mwema Malon.” Naya akasimama nakuondoka pale bila hata yakumaliza chakula au kugeuka nyuma ila akamuona Joshua hakuwa amekaa mbali nao, ni meza ya nyuma yao tu. Akajua amesikia. Hakujali tena, akaondoka.
Kesho yake.
N |
aya alitoka
chumbani kwake asubuhi hiyo akiwa na mizigo yake yote tayari kuondoka mjini
Mbeya kurudi kwao Kiluvya. Alijua wenzake wengi watakuwepo hapo kumalizia
weekend lakini yeye akakusudia kurudi nyumbani kwao. Wakati anatoka chumbani
kwake akakutana na Jamal. “Shikamoo.” “Marahaba Naya. Mbona mapema?” “Nataka
kuwahi basi la kunirudisha nyumbani.” “Kwa nini tusiongozane? Nipo na Joshua
tu. Kuliko uhangaike na mabasi, ni bora tuongozane.” Naya akaingiwa hofu. “Hatuli watu
Naya!” Naya akacheka maana ni kama Jamal aliyasoma mawazo yake. “Haitakuwa
usumbufu?” “Hata kidogo. Wewe pata kifungua kinywa, tunakuja muda si mrefu
tuondoke. Acha nimuone Kiongozi hapo chumbani kwake.” Akajua ni Joshua. “Sawa.
Nashukuru.” Naya akashuka chini sehemu ulipokuwepo mgahawa huku akimpigia simu
baba yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Nimekuamsha?” Naya akamuuliza baba yake. “Nilikuwa
nategemea simu yako. Ulilala salama?” “Ndiyo. Shikamoo baba.” “Marahaba.
Umepata basi gani?” “Ndio maana nakupigia.”
Naya akaweka mizigo yake chini na kukaa. “Unamkumbuka
Jamal?” “Bosi wako mkali?” Naya akacheka. “Huyohuyo. Ameniambia watanipa lifti.” Kimya. “Baba?” Naya akaitizama simu yake akakuta baba yake bado hajakata
simu. “Kwa nini tena?” “Amenikuta ndio natoka
chumbani kwangu akaniambia hivyo. Lakini hatutakuwa peke yetu. Atakuwa na
kiongozi wake.” “Hapo sawa. Isiwe peke yenu. Muwe wawili tu! Hapana Naya.
Humfahamu huyo mtu. Sitaki kuje kutokee kosa.” “Sawa. Nitakuwa makini na
nitakupigia nikiwa njiani.” “Hapo sawa. Utanituliza.” Wakaagana na kukata.
“Malon!” Naya akashitukia Malon anakaa mbele yake. Lakini ni kama
alitegemea. Alimjua Malon. “Jana uliondoka bila...” “Kuniona nakulilia?” Naya
akamuuliza akirudisha simu yake mfukoni.
“Ni nini Naya?” “Juu ya nini Malon? Unajua ingekuwa wakati ule, kukuona
hapa ningeshangaa sana. Lakini sasa hivi nimeshakuelewa. Huwa hivi ndivyo
unavyorudi. Kwa nguvu sana. Unajaa kwenye kila sehemu ya maisha yangu. Unakuwa
upo kila mahali mpaka siwezi kufikiria kitu kingine ila wewe tu na mipango yetu
ya wakati huo unayokuwa umerudi nayo. Ukishahakikisha hilo limekaa sawa, ndipo
unapoondoka na kuniacha naanza upya, tena chini zaidi nikiwa sina dira tena.
Halafu mwenzangu wewe maisha yako yanaendelea kama kawaida bila kunijali.” Naya
akawa ameshakasirika.
“Nimekueleza juu ya...” “Unataka kukumbushia nyuma? Nilifikiri
hutaki kukumbushwa mambo ya zamani!” Malon akabaki akimtizama. “Hapa sasa hivi
unataka kunieleza juu ya nani? Maana tokea tunaanza Malon, huu ndio mchezo
wako. Hujawahi kubadilika na ninasikitika hutaki kubadilika.” Kimya. “Japokuwa
uliniomba nisiwe nikikukumbusha mambo ya zamani, lakini haimaanishi tumesahau.
Wote tunakumbuka na ndio maana naona nisipokueleza kinachoendelea moyoni
mwangu, huu mchezo wako huu unaoufanya sasa hivi hautokoma na mimi sina muda
huo tena.” Naya akaendelea.
“Nivumilie tu nikwambie wakati nasubiria lifti.” “Nani anakupa
lifti?” “Unakumbuka ulivyomlala Lulu kule hosteli ukijidai ni njia yakunifikia?
Kwako ilikuwa jambo dogo sana wala hukuona sababu ya mimi kulalamika.” Naya
akamkumbusha mengi tokea wanaanzana mpaka hapo na kumuacha Malon hoi. “Naya!”
“Haswa. Sema nilichodanganya hapo hata kimoja.” Kimya. “Kipi nilichosema
ambacho hukuwahi kukitenda ukiwa na mimi mpaka hapa umeokoka, kwa Rita?” Kimya.
“Huo ukimya unaashiria ni kweli. Sasa badilisha shilingi iwe ndio mimi ndio
huwa nakufanyia hayo yote, halafu niambie ukweli kama leo hii wewe Malon Saduki,
ungekuwa na hamu yakuja kukaa hapa mbele yangu.” Malon kimya.
“Kilio changu siku zote ilikuwa unichague mimi Malon, lakini
haijawahi kutokea wala najua haitatokea.” “Nipo hapa Naya.” “Kwa muda, mipango,
mazingira na wakati wako wewe Malon. Wewe ni wa msimu. Akitokea mrembo kama
Rita, unashindwa hata kutoa tu utambulisho wa jina langu. Bisha.” Malon kimya.
“Najua nilikukumbusha, acha nikukumbushe tena Malon pengine safari
hii utaweza kutilia maanani. Siku unakwenda jela, tukiwa kwenye kile kiwanda
cha nguo, ulisema ukitoka jela nijue utakuwa umefilisika na hujasoma.
Unakumbuka jibu nililokujibu?” Malon kimya. “Kama hukumbuki jibu la hilo basi
unakumbuka chochote nilichokushirikisha tukiwa tumekaa palepale tena siku
ileile?” “Nakumbuka Naya.” “Lakini ulipotoka jela kwa mara nyingine tena,
ukajichagua wewe. Sio sisi Malon. Wewe, kwa kisingizio chakuniona nacheka sana
na Joshi. Sio kufurahia kuniona japo umenipitisha kwenye magumu mengi, ufurahie
kunikuta nimebaki na wewe, na bado nina furaha! Hapana. Hilo lakunikuta
nacheka, ukalihesabu ni kosa la kuniacha kabisa. Unachotaka na kukifurahia
kukiona kwangu ni unione nateseka kama wasichana wengine wanavyokuwa baada ya
wewe kuwatelekeza. Fahari yako nikutuona wote tumekwama tunasubiria rehema zako.”
“Sio kweli.” Naya akacheka.
“Nakujua Malon. Kinachokuahangaisha hapa sio mimi kama Naya, ni
vile kuona chakwanza bado hujashinda kama siku zote unavyorudi na hoja zako tu
kisha nakufungulia milango yote mpaka moyo wangu bila shida. Na unajua chapili
ni nini?” “Nakupenda Naya?” “Hiyo ndiyo PASSWORD yako kwangu. Namba yako ya
siri uliyoitumia tokea tunafahamiana ili kuingia moyoni mwangu na kunifanya
mateka wako. Sio mapenzi. Mimi ndiye niliyekupenda.” “Kwa hiyo sasa hivi
hunipendi tena?” Naya akacheka. “Sababu yako ya pili inayokufanya uhangaike kwa
simu, jumbe na asubuhi kuwa hapa, nikutoona tena chozi langu. Nina uhakika
ungeyaona, sasa hivi usingekuwa hapa. Hicho ndicho cha pili lakini najua ndio
kikubwa. Hata ukibisha, ni kwa kuwa hujijui. Mimi nimeishi na wewe kwa upendo
mkubwa sana. Mwenzio nikajifunza nini Malon anataka, yukoje ili kukufurahisha.
Nakufahamu Malon. Na huo ndio ukweli.”
“Unahangaika kuwa nazo pesa na mali nyingi, ukigawa vitu kwa wingi bila kujali au
kufikiria, ili tu kuhakikisha kila mtu anakuwa chini yako na kukuhitaji wewe.
Hudhani kama unaweza kupendwa wewe kama Malon kitu kinachoniuma maana
nimejaribu kujifunga kwako bila mipaka!” “Najua unanipenda Naya.” Naya akabaki
akimtizama. “Kweli. Wewe najua unanipenda kwa dhati. Hunitumii.” “Ndicho
ulichokuwa ukikifurahia kutoka kwangu bila kunijali mimi mwenyewe na hisia
zangu?” “Nakujali Naya na...” “Ungekuwa ukinijali kama mimi ungekuwa
ukinithamini na hata kujua ndoto zangu, na mipango yangu sio kuniuliza kama
unazungumza na mwanamke mwingine yeyote!”
“Uliniumiza sana kuuliza malengo yangu na nini ningetamani kufanya
badala ya hiki! Hakika umeniumiza sana. Na tafadhali usirudie kuuliza maswali
ambayo ni wewe kwa asilimia 100, zaidi hata ya baba yangu mzazi, unajua kwa
hakika mipango yangu na ndoto zangu.” “Watu wanabadilika Naya!” “Hiyo ni kweli.
Najua watu hubadilika Malon, lakini najua unanijua mimi. Mipango yangu si ya
kukurupuka. Na umekuwa ukiipongeza. Iliyolipa kwa haraka uliwekeza pesa ambayo
ilikurudia zaidi ya ulivyowekeza.” “Naya! Kweli unasema hivyo?” Malon
akashangaa sana.
“Unashangaa nini Malon? Si ni kweli? Pesa uliyowekeza kwenye ile
biashara ya mavazi, haikurudi?” “Ndiyo ilirudi lakini si ilikuwa yetu?” “Yetu!?
Wewe na nani?” Hapo Malon akatulia. “Nilikuwekea dhamana pesa yote. Ukatoka jela,
ukalipwa ile pesa yote Malon. Ukarudi kwangu na mipango? Ukapotea. Ukarudi na
kisingizio cha mama alikufukuza kama ambaye umesahau vile nilivyofukuzwa kwenu,
tena zaidi ya mara moja! Wazazi wako na ndugu zako wakinishauri nikukimbie.
Nikuache kabisa. Marafiki zako walinishauri nichukue changu mapema, nikimbie
lakini nikakung’ang’ania wewe Malon. Nikapambana mpaka nikakutoa jela. Lakini ulikuja
kuondoka na kurudi na sababu tu. Ukaniachia zile ndoto zangu tena ukiniaga
kimungu kabisa ukinisukumia kwenye mahusiano uliyojua wazi ni mabaya kwangu.
Ukaniacha nikikulilia wewe. Hukujali
shida zangu Malon. Uliniacha mikononi mwa mahusiano mabaya, nikiwa sina pesa
wala dalili ya ajira. Ukaondoka mpaka nilipokufuata tena kukupa zawadi ya
shukurani. Ndipo ukarudi tena kwenye picha kama ufanyavyo wakati wote!”
Naya akajisogeza vizuri. “Kwa unavyonifahamu Malon. Unategemea huo
mchezo niendeleze na wewe mpaka lini?” Akamuuliza taratibu tu. “Kwamba eti mimi
nisiendelee na maisha, niwe nakaa tu. Nateseka, nikiendelea kukusubiria wewe.
Nikikulilia wewe tu. Ukirudi unanipa tena sababu. Tunaendelea tena. Mpaka lini
Malon?” “Sasa hivi natulia na wewe Naya.” “Nisubiri na mimi nihangaike nifike
ulipofika wewe. Mungu anifanikishe kama wewe. Kisha tuanze huo mchezo wa wewe
kuniambia umetulia na mimi. KAMA KIPINDI HICHO NITAKUWA NA HUO MUDA TENA.” Naya
akasimama.
“Kwa hiyo unamaanisha nini?” Malon akawa na yeye kama amekasirika.
“Fikiria, chukua hatua kama ufanyavyo wakati wote. Wewe sio mtoto mdogo Malon.
Wala sio mtu wakusubiri mimi nikwambie kitu chakufanya. Fikiria, utapata jibu.
Ukiwa na nafasi, jaribu kufikiria tokea tulipoanzana mpaka sasa. Utapata jibu.
Mimi nilifanya hivyo. Ndipo nikakubaliana na baba yako kuwa, nakudai kitu
ambacho huna uwezo wa kunipa Malon.” “Kwamba mimi ni malaya tu?”
“Wewe wasema. Mimi sijasema haya mambo. Ila nimeishi na wewe, nimepingana na hiyo kauli ambayo ni wengi wanasema na wanawake wengine wakililia kutoka kwako. Nimeona sikutendei haki kukudai kitu usicho nacho na wala huna uwezo wa kuja kunipa. Mungu akubariki Malon.” Naya akasimama na kutaka kuondoka akiwa ameshachukua mizigo yake, lakini akarudi. “Halafu Malon.” Malon akamgeukia. “Sikudai kwa chochote kile. Usijifikirie upo na deni kwangu unatakiwa kulilipa. Kwa chochote kile, jua nilifanya kwa kadiri Mungu alivyoniwezesha na kwa ajili ya wema wako pia. Unastahili kutendewa wema Malo. Wewe ni mtoaji sana. Mtu asipokulipa wema, ni kwa kuwa amenyimwa tu shukurani. Ni hilo tu nilitaka kukuweka huru, usifikiri unajukumu la kukufunga kwangu au kurudi kunifanyia kitu. Hapana. Tafadhali uwe huru.” Naya akaondoka pale mgahawani kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akakuta kina Jamal na Joshua wanashuka ngazi wakizungumza wote wakiwa na vijibegi vidogo tu mkononi. Naya akajikuta akisalimia tena mpaka goti. Jamal akaitika ila Joshua akajibu kwa kuuliza swali. “Jamal ameniambia tunaongozana. Si ndivyo?” Naya akababaika akiwa bado na hasira. Hakujua kama bado yupo tayari kupanda gari na hao viongozi wake au atumie tu basi ili apate uhuru wakutolea uchungu wake kabla hajafika nyumbani kwao. Joshua akamuona ametulia kama ambaye anaogopa kuzungumza kitu. “Umebadili mawazo nini?” Jamal akatoa macho kwenye simu na kurusha hilo swali wakiwa wamesimama kwenye ngazi ya mwisho kabisa. “Naomba niwashukuru kwa lifti lakini. Nafikiri mimi nitatumia tu usafiri wa bas...” “Subiri kwanza Naya. Naomba tuzungumze kwanza.” Joshua akamsogelea, Jamal akarudisha macho kwenye simu kama aliyepata ujumbe uliomlazimu kujibu kwa haraka.
“Nahitaji kufikiria Joshua. Nahisi kwenye gari yenu...” “Chakwanza
utapata utulivu. Dereva tuliyenaye ni mzee Sajo. Mtulivu kama unavyomjua. Hana
makeke barabarani. Ni usafiri wa bure wa kampuni, utatunza pesa yako. Usiachie
hiyo bahati. Labda uwe unatukimbia mimi na Jamal.” “Mimi mtu mzuri sana. Naya
ananijua. Hana sababu yakunikimbia.” Wote akamgeukia Jamal, Naya akacheka
taratibu. “Basi niwashukuru.” “Huu sio msaada. Ni gari ya kampuni. Usijedhania
utakuwa na deni lakulipa baadaye.” Hilo likamfanya Naya kuridhika.
“Hapo sawa.” Jamal akacheka sana tena kwa sauti ya juu. “Nayaaa!
Hutaki madeni?” “Mimi sina uwezo wa kuyalipa kaka yangu.” “Wenzio wanayatafuta
madeni!” “Mmm!!” Naya akaguna nakufanya wote wacheka kwa pamoja. “Sasa Jamal?”
“Nimemwambia Mzee Sajo, chai inaenda kunywewa Njia Panda, Iringa. Tukapate na
mbwa choma. Twendeni.” “Hayo maneno.” Wakaondoka pamoja. Joshua akamsaidia
kubeba mizigo yake yote mpaka akamshangaza Naya. “Nikusaidie nini?” Naya
aliuliza wakati wakitoka hapo ndani. “Nipo tu sawa. Usijali.” Naya akawa
akifuata kwa nyuma. Joshua mwenyewe akamuingizia mizigo garini na kuipanga
vizuri ndipo safari ya kurudi Dar ikaanza.
Safari ya Kurudi Dar.
Naya NA VIONGOZI WAKE SAFARINI.
“Nimewaambia hawa watoto atakayechelewa kufika kazini jumatatu,
ajihesabu hana kazi. Sasa waache waendelee kulewa.” Jamal akaongea kwa vitisho. “Bado wanakula raha?” Mzee Sajo akauliza huku akiendesha.
“Wapuuzi kweli hawa! Wanaibiana waume na wake tu huku Mbeya, ndio maana
hawataki kurudi Dar kwenye familia zao. Sasa acha wajichanganye, ndipo
wataipata habari yangu.” Naya kimya, ametulia kitini. Joshua upande mwingine,
Jamali amekaa mbele na dereva wakicheka.
“Binti yangu wewe starehe huzitaki?” Naya akacheka na kushindwa
kujibu. “Naya hataki madeni.” Jamal akamjibia. “Madeni ndio mpango mzima wa
mjini. Wenzio wanayalilia.” Jamal akacheka sana. “Sikukwambia Naya? Wenzio
wanayataka madeni, ili wayalipe kwa nafasi.” Naya akainama akicheka. “Basi
mama. Tusikunyime raha.” Mzee Sajo akamtuliza akimwangalia kupitia kioo cha
katikati. “Na uendelee hivyohivyo. Wasikubadilishe wale mbweha watu.” Jamal
akawa kama anampongeza. “Nitajitahidi kuongeza umakini.” “Hayo ndio maneno.
Ukikazana hivyo, utajiona unapata ajira kwa haraka kuliko hata wale uliowakuta
pale kazini.” Jamal akaongeza.
Akamuona Joshua anatoa laptop yake kwenye mkoba na kumkumbusha Naya kumtaarifu baba yake. Akatoa na yeye simu yake akakutana na ujumbe wa Malon. Hakutaka hata kusoma. Akampigia baba yake. Akaanza kwa sauti ya chini sana. “Nimepiga simu kukutaarifu ndio tumeanza safari muda si mrefu.” Wakamsikia Naya akinong’ona wakadhani pengine anamtaarifu mpenzi wake ndio maana ananong’ona. “Sijui baba!” Hapo ndipo wakajua anazungumza na nani. “Nitaomba wanishushe palepale kituoni. Si utanisubiri?” Wakamsikia Naya akicheka kisha akasema. “Haya. Nimefunga na macho.” Wakamsikia ametulia. Mwishoe wakasikia. “Amina. Asante baba yangu. Nitakupigia tena baadaye?” Akacheka kidogo. “Baba wewe! Mimi naogopa bwana.” Wakasikia akinong’ona huku akicheka. “Sawa basi. Watasikia.” Kisha akakata. Kimya.
“Sio kwamba nilikuwa nikisikiliza mazungumzo yako. Ila nahisi kama
baba ametutumia salamu!” Jamal akafanya wote wacheke. “Hata mimi nilikuwa
nikingojea hiyo salamu, kisha nikaona kama zimemezwa hivi!” Akaongeza mzee Sajo,
Joshua akacheka na kumtizama Naya. “Baba amewasalimia na kuwakaribisha
nyumbani. Ila nimemwambia...” “Oooh! Ndio vile ulivyosema unaogopa? Hutaki
wageni Naya ?” Naya akacheka kwa hofu. Ni kweli walimuogopa Jamal pale
ofisini kwao. Alikuwa makini sana na hakupenda mzaha. Na wala hakuwa na
mwanamke tokea anaanza kazi mpaka mida hiyo wakati alikuwa yeye ndio
anazungukwa na warembo muda mwingi wa kazi. Kisha Joshua Kumu! Anaanzia wapi
kumkaribisha mtu kama Joshua nyumbani kwao! Jamal mwenyewe alikuwa akimuogopa
na kumuheshimu sana Kumu.
“Nilijua mtakuwa mmechoka
na mnawahi majumbani kwenu.” “Kumbe bado Naya wewe mtoto wa baba?” Naya
akacheka alipoulizwa na mzee Sajo. “Bado unaishi na wazazi?” “Ndiyo. Tunaishi
na baba, mama alifariki hata mwaka haujaisha. Kwa hiyo tumebakiwa na baba tu.”
“Pole sana.” Wote wakampa pole. “Asanteni.” Akajibu Naya na kuinama kwa muda
kisha akarudisha macho nje. Akajiegemeza vizuri, akatulia. Joshua na yeye
akaendelea na shuguli zake kwenye kompyuta, Jamal akizungumza na Mzee Sajo.
“Kaka bado shule haijaisha tu?”
Akamsikia Jamal akiuliza. “Elimu ya uzeeni kuisha kazi!” Joshua akajibu
macho kwenye laptop. “Ila umepambana Joshua, mpaka unanitia wivu! Umenipita na kuniacha!” Joshua
akacheka. “Maamuzi tu, Jamal. Ni maamuzi tu kaka. Halafu wewe sasa hivi
ushaanza kusomesha!” “Usiongee. Ada ya mtoto mdogo kama niliyokuwa nikilipa
mimi chuo!” Wakacheka. “Walahi kuzaa gharama!” “Hutaki tena?” “Nishamwambia
wife. Akiongeza mwingine tu, huyo nitamfundisha mwenyewe.” Walicheka sana.
“Haendi shule?” “Wataniua kwa ada mzee Sajo! Pesa haikai mkononi!” Wakaendelea
kuzungumza wakicheka, Naya kimya tu. Palipotulia akapitiwa na usingizi. Alikuwa
akimka mara kwa mara lakini akawa anarudi kulala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nini kitaendelea kwa Naya huko safarini akiwa na viongozi wake? Usikose
Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment