Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! – Sehemu ya 27 - Naomi Simulizi

Nilipotea! – Sehemu ya 27

 

“Subiri kwanza mama Cote.” Tunda akamkata. “Wewe si upo safi mbele za Mungu? Unaamini kwenye wokovu na nguvu ya damu ya Yesu? Sasa kwa nini humkomboi mwanao kwa maombi ili atoke kwangu? Kwa nini humtoi kwangu kwa maombi? Unahangaika tu na mimi kwa maneno mengiii! Au huamini kama Mungu wako ananguvu kuliko nguvu ya shetani?”  Tunda alimshtua sana Ritha. Akababaika sana akiongea hili na kujibu lile, Tunda akimtizama kwa kumsuta.

“Subiri kwanza Ritha. Acha maneno mengi. Wewe si mama yake Net? Inamaana unazo haki zote za kumkomboa mwanao kwa njia takatifu kama wewe ulivyo mtakatifu. Mbingu inajua unayo haki, hata kuzimu kule unakosema mimi ninaenda, wanajua kuwa wewe kama mama yake Net, unayo haki na Net. Sasa kwa nini unahangaika na mimi ambaye hata sijaunganishwa na Net kwenye agano lolote!?” Tunda akamuuliza taratibu tu bila jazba kama yeye alivyokuwa akiongea kwa jazba.

“Usifikiri ndio umeshinda Tunda. Namuombea mwanangu. Ila ujue maombi ni kotekote. Ni mimi, na Net mwenyewe aamini.” Tunda akamtizama kwa kumsuta. “Na usifikiri nimeshindwa. Nipo kwenye maombi yakumfungua akili zake mpaka afunguke. Net ni kama amechanganyikiwa kwa kuwa anataka kuwa mtumishi wa Mungu kama babu yake, ila hajui ni jinsi gani atumike. Kwa kuwa wewe ulikuwa malaya, na bibi yake anapambana na haki za wanawake na kutoa wanawake wenye hali kama yako na kuwawezesha kimaisha ili waweze kujitegemea, ndio anaona wewe utafaa.” Akaanza kuropoka, Tunda akimtizama kwa mshangao.

“Kwanza atakutumia wewe kama kielelezo cha kufikia roho za watu waliopotea na pili anaona anamfurahisha bibi yake kwa kumuunga mkono kwa kile anachokifanya kwako wala si mapenzi. Ndio maana anadhani wewe utamfaa.” Hilo likamwingia Tunda na kumuumiza sana. Ila akajikaza mbele ya Ritha.

“Upo wewe kama daraja kutimiza ndoto zake, na ndio maana hata bibi yake pia yupo hapa leo kuhakikisha Net anafikia ndoto zake na yule bibi anajipatia sifa kimataifa. Kuwa ni mkweli kwa kile anachokipigania. Kwani ameweza kuruhusu hata changudoa kama wewe kuolewa na mjukuu wake. Usifurahie jinsi unavyoitwa Mama Cote leo, ukadhani kuna kitu cha maana walichokiona kwako au uchawi wako pekee ndio umeshinda. Hamna kitu.” Tunda alibaki kimya ametoa macho. Habari zilikuwa mpya, ngeni lakini kweli zilianza kumuumiza.

“Wewe loga utakavyo. Lala makaburini utakavyo. Lakini jua mimi nipo. Na uelewe kabisa nawajua wazungu kuliko wewe. Wanajua kutumia watu. Umeruhusiwa na yule bibi kuwepo na Net kwa ajili ya kumnufaisha yeye mwenyewe yule bibi. Kimataifa na kiuchumi. Na kwa upande wa Net, kama nilivyokwambia. Ila sasa, ujue wazi, MIMI nipo. Sitakubali kwa nia yao yeyote ile, wewe unufaike kwa kile ninachostahili mimi.”

“Nimehangaika sana kufika hapa. Mchana na usiku kujenga hili jina huku Tanzania. Nani alijua Cote huku Tanzania kama sio mimi? Hapa uliposimama, ni kwangu nimejenga kwa jasho langu. Hata kama Net alikwambia babu yake ndiye alijenga hapa, lakini ujue mimi ndiye niliyekuwepo hapa kuhakikisha jengo linasimama.” Na hapo napo Ritha akajikuta anaropoka mengiii kwa hasira huku Tunda akimshangaa. Hakuwa anaelewa chochote anachozungumza pale.

“Kwa hiyo ujue sitakubali. Wakati wewe unahangaika na suruali za wanaume, mimi nilijua kufunga miguu yangu, nikatumia akili, mpaka kumfikisha hapo alipo hata huyu Net ambaye sasa hivi unafurahia mali zake hapa nchini Tanzania. Yupo hapa nchini kwa sababu ya juhudi zangu wala sio pesa. Hawezi kuishi Tanzania bila idhini yangu mimi ambaye ni raia wa Tanzania.” Hapo napo Tunda hakuwa hata akielewa.

“Sasa, sitakubali hata iweje uvune usipopanda. Labda usubiri niwe nimekufa ndio utakuja kuitwa mama Cote. Vinginevyo ujue utapambana na mimi na utajuta, malaya mkubwa wewe.” Tunda akatabasamu. “Umemaliza?” Tunda akamuuliza mama Cote swali lililomshangaza, tena akiwa ametulia tu. Kimya.

“Acha kuniogopesha Ritha. Wala sitakuita Mama Cote maana umejishusha sana. Mimi huwa sitishwi. Na wewe wala usifikiri ndio wa kwanza kunijia na vitisho. Tokea napata akili zangu, nimeishi na watu wa aina yako. Vitisho imekuwa sehemu ya maisha yangu. Yaani wewe hapo ulipo hivyo, hunitishi hata kidogo.” Tunda akaendelea taratibu tu.

“Unanisikia Ritha? Sikuogopi. Halafu na uache kujipa kazi zitakazo kuchosha bure! Ngoja nikusaidie tu kwa kuwa umenizalia Net. Huko unakonitafuta mimi simo tena. Nimetoka na nimeamua kupumzika. Mungu alishanitoa makaburi na kwa waganga wa kienyeji, muda mrefu sana. Nimeacha kuvua suruali za wanaume muda mrefu sana na wala sijivunii kwa hilo. Najua nimesamehewa, lakini bado nipo na majuto tu. Nasikitika kuwa na wewe umekuwa muhanga na maisha niliyoishi zama...” “Acha kunipa maneno unayomdanganya nayo Net. Mimi ni Ritha Cote. Najielewa. Na nimekwambia hata Net anakutimia tu.” Ritha akamkata. Tunda akacheka kwa kumuhurumia.

“Hata kama Net ananitumia tu. Au bibi yake ananitumia. Sijali. Nataka ujue na mimi msaada ndio nilio kuwa nikiutaka siku zote za maisha yangu. Net amepata alichokuwa anakitaka maishani mwake, na mimi nimempata mwanaume ambaye hata sikuwahi kumuota na heshima kubwa ambayo hata sikuwahi kufikiria nina stahili. Wewe ni shahidi kwa kile tu kilichonitokea leo. Ulikuwepo tokea asubuhi ukishuhudia kile kinachonitokea mpaka sasa hivi uliposhindwa kuvumilia. Umeona heshima iliyowekwa kwa Tunda tu!” Tunda akacheka taratibu.

“Kwa hiyo kwa upande wangu mimi, kwa ufupi, sina chakupoteza hata kidogo. Kama Net na bibi yake wataendelea hivi, aisee ujue mimi ndio nilichokuwa nikikihangaikia tokea zamani mpaka kulala makaburini nakushindwa kukipata kwa shetani ila kwa huyu Mungu ninayemtumikia sasa hivi. Sasa kama na yeye unamwita shetani, hakuna injili itakayowahi kuja kunitoa kwa huyu Mungu ninayemtumikia sasa hivi. Nakushauri na wewe umfuate. Analipa. Na itakupunguzia kupambana na watu au kuzunguka kwenye maofisi ya watu ukijidhalilisha bila wewe mwenyewe kujijua.” Ritha alishtuka sana asiamini.

Tunda akataka kufungua mlango ili aondoke lakini akageuka. “Na wala usipate shida na uwepo wangu. Nitajitahidi tusionane kabisa mpaka utakapo kuwa tayari kuniona tena. Naomba uniagie Net.” Tunda akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda kupita bila kumuona Tunda, Net akaanza kumtafuta. Aliingia ndani na kutoka mara kadhaa, mwishowe akakumbuka kumuona mama yake akiingia ndani wakati Tunda yupo ndani. Akamsogelea, “Umemuona wapi Tunda?” “Aaah! Nilisahau kukwambia. Aliniambia nikuage yeye ameondoka.” Net akakunja uso na kujiweka sawa.

“Umemwambia nini tena, Tunda?” “Kwa nini unafikiria maneno yangu ndio yamemuondoa hapa?” “Mama?” Net akaita kwa ukali kidogo. “Umemwambia nini Tunda?” “Labda atakuwa hajanielewa.” “Juu ya nini?” Net akauliza. “Acha kunihoji maswali mengi. Hapa ni nyumbani kwangu.” Ritha akambadilikia mwanae.

“Ni nini kinaendelea mama!? Shida yako ni nini? Kwa nini umeshindwa kumpokea Tunda kama mwanamke ninayempenda?” “Kwa kuwa umekataa kukaa chini na kumfikiria vizuri.” “Unataka nifanye nini kukuthibitishia kuwa Tunda amebadilika? Umempa mtego wa Gab, ameshinda. Nini unataka kutoka kwake!? Ulitaka afanye nini!?” Net alikuwa anamshangaa mama yake nakushindwa hata kuelewa.

 

“Nishakujibu kuhusu Gab. Ule sio mtihani wakumpima mtu kama Tunda, nakusema ameshinda. Gab angekuwa mwanaume mwingine, hakika asingemkataa. Mbali na sababu nyingine nyingi za mwanamke kama Tunda, kwanza lazima ujue bado ana uchungu na Gabriel ndio maana alimkataa. Na yeye si binadamu bwana! Anaweza kuumizwa. Huwezi kumpima mtu kama Tunda na Gab wakati amekukamata wewe. Nini atanufaishwa na Gab ambacho hatapata kwako? Anajua hilo ndio maana anajifanya mtakatifu kwako.” Yule mama akaendelea.

“Siwezi kuwa mjinga au kudanganywa na Tunda kama alivyofanya kwa Gab na wewe sasa hivi. Eti nimekaa hapa, namwangalia tu anavyojidai kuwa amebadilika, ameokoka, eti sasa hivi ni malaika na wewe unataka kumuoa! Hata kidogo. Sikubali.”

“Wageni wote hapa wakiume, karibia asilimia 90, kasoro ya aliokuja nao bibi yako tu, amelala nao. Kwa nini unataka kunidhalilisha hapa mjini? Wasichana wote waliojaa humo makanisani, leo unakuja kumuoa yeye!? Kwa nini Net? Naomba pata muda ufikirie. Tunda hawezi kuwa mke wako. Naomba mwanangu punguza mwendo. Umefanya haraka sana juu ya huyu Tunda.” Net akazidi kuumia.

 

“Nafikiri nimefanya sana haraka kwako mama. Hata hii shuguli sikutakiwa kuifanyia hapa. Nana angeshukia nyumbani kwangu, na mambo mengine yangeendelea kama kawaida, nyumbani kwangu. Lakini sikutaka haya mambo yaende mbali. Sikutaka tumuingize Nana katika hili ndio maana nikamleta hapa na kumrudisha Tunda kwako japo ulimuumiza sana.”

“Nakupa muda zaidi. Utakapokuwa tayari utanitafuta. Lakini ukae ukijua nitamuoa Tunda, tena haraka iwezekanavyo. Unajua pakunipata pindi utakapo kuwa tayari. Na kwa kuwa Tunda ni kero kwako, nitajitahidi kumuweka mbali sana na wewe, ili asikukere na usimuumize.” Mama Cote alishtuka sana. Akajua Net akihama pale ndani tena, akarudi nyumbani kwake, bibi Cote atafahamu na kuibua maswali zaidi.

“Kwa hiyo na wewe unaondoka!?” “Humtaki Tunda, na Tunda atakuwa mke wangu hivi karibuni, unafikiri nitafanya nini?” “Na kazi unaacha?” “Kwa nini niache kazi!?” “Sijui. Labda unataka kuniadhibu.” Mama Cote alitumia silaha yake kwa haraka, aliyojua kumvuta nayo Net. Machozi. Net akamsogelea. “Nakupenda sana mama yangu. Na nilimuahidi baba nitakuwa na wewe wakati wote. Hakuna mtu wala kitu kitaingilia katikati yetu. Siwezi kuacha kazi. Nilikuahidi maisha yangu ya familia hayataingilia kazi yangu, na bado itabaki hivyo.”

“Siwezi kukuadhibu kwa kutokumkubali mwanamke ninayempenda mimi, lakini naona haitakuwa sawa kuendelea kukuletea Tunda, halafu unaiishia kumuumiza. Sio sawa kwako wala kwake. Nilikubali kuja naye hapa leo, kwa kuwa ulisema huna neno. Lakini sasa hivi nimejua kuwa ulikubali sababu ya Nana. Ulijua Nana asingefurahia kuona Tunda hakaribishwi nyumbani. Lakini usiwe na wasiwasi, Tunda hatakubugudhi tena na wala haya mambo hayatafika kwa Nana. Usiwe na wasiwasi juu ya hilo. Usiku mwema mama.” Net akambusu mama yake, akaenda kumsindikiza bibi yake kitandani huku wakitaniana. Waliomba naye, kisha akondoka kwenda kumfuata Tunda.

Net kwa Tunda.

Net alimkuta Tunda, ameshaogo na kuvaa nguo zake za kulalia, amejilaza kwenye kochi anaangalia tv. “Nilikuomba usiwe unanikimbia Tunda.” “Nilimuomba mama yako aniagie.” “Tangia lini mimi na wewe tunawasiliana kwa kupitia mama yangu? Ingechukua dakika ngapi kuniaga pale wakati unaondoka?” “Sikutaka kukusumbua katikati ya wageni. Halafu nilikuwa nimekasirika Net, sikutaka kuongea kabisa. Kuhofia kuongea neno ambalo lingekuudhi bure, wakati nilikuona unafurahia na wenzako.” Net akakaa, Tunda akasogeza miguu vizuri kama kumpisha apate nafasi vizuri.

“Net!” Tunda akaita na kukaa vizuri. Net akabaki akimwangalia. “Naomba uniambie ukweli. Na kumbuka maisha ambayo nimeishi. Tokea nazaliwa nimekuwa mtu wa kukataliwa na watu, nimeishi kwenye majumba ya watu kwa kubembeleza. Nataka kujua ukweli ni kwa nini unataka kunioa wakati…” Tunda akaanza kulia. “Mimi naona..” Tunda akakwama.

“Unaona nini Tunda? Niambie unachotaka.” “Sijui Net. Naona kama najiingiza kwenye matatizo. Nilitegemea kupata faraja kwenye ndoa, lakini inaanza na vipingamizi vikali! Tena kutoka kwa mtu wa muhimu sana kwako, anayenitangazia vita mpaka kifo chake. Niambie itakuaje? Tutakuwa na ndoa ya namna gani?” Net akavuta pumzi kwa nguvu, akakaa vizuri na kujiegemeza kwenye kochi.

“Hata mimi sijui Tunda. Sikuwahi kupenda kabla, na wala sijawahi kuoa. Sitakuwa na majibu yote ya maswali yako.” Net akanyamaza kwa muda. Kisha akaendelea. “Unajua umenifanya nijiulize Tunda. Hivi kweli unanipenda wewe au ni kwa kuwa nimetokea tu unanifahamu? Hivi mtu akikuuliza kwa nini unakubali kuolewa na Net, utasemaje?” “Nakupenda Net.” Net akakaa sawa.

“Kweli? Naomba usichanganye upendo, na wewe kujikuta umeangukia mikononi mwangu. Mtu unayempenda huwezi ukawa ukimfanyia hivi. Hii ni mara ya pili kunikimbia Tunda. Tena leo umeniacha katikati ya tafrija yetu, mbele ya wageni niliowaalika kuja kuona nikimvisha pete ya uchumba mwanamke niliyewatangazia nina mpenda. Mimi ndiye nimekuwa mtu wakukukimbilia kila wakati na kukuomba urudi. Mimi ndiye nimekuwa mtu wakupigania haya mahusiano yetu kila wakati!” Net alikuwa amekasirika na yeye.

“Unamuacha Nana, Maya na marafiki zangu waliosafiri safari ndefu kuja maalumu kwa ajili ya hili tukio. Bila kuaga, tena katikati yao!  Huonekani kama mwenzangu unahaja na haya mahusiano hata kidogo. Unanifanya nitilie mashaka viwango vyangu vya uanaume. Labda sijafikia viwango vya mwanaume unayemtaka maishani mwako.” “Hapana Net.” Tunda alijua angebembelezwa, kumbe ameharibu uzunguni.

“Naomba nikuombe kitu kimoja Tunda, tena kabla hatujafika mbali. Pata muda wakufikiria. Nataka ufikirie kama kweli mimi nafaa kuwa mume wako au la. Usiogope kuniambia, nitakuelewa tu.” “Net na..” “Usiharakishe Tunda.” Tunda alitaka kujibu, Net akamkatisha. “Naomba pata muda. Tutaongea zaidi baada ya hapo.” Net akasimama.

“Ukiondoka humu ndani, ujue unaondoka na mimi Net. Hutaniacha nikilia tena. Nimeamua kuwa mke wako, wala sihitaji kufikiria. Niliondoka kuepusha vurugu pale mbele za wageni. Mama hataki kuniona na wewe. Naomba usiondoke tafadhali. Nakupenda na nimeamua kuwa na wewe. Ila naomba nisiwe naenda pale kwa mama yako kwa kipindi hiki. Naomba tumpe nafasi.” Tunda alikuwa amesimama na yeye. Net akarudi kukaa.

 “Kweli nakupenda Net, wala sihitaji kufikiria juu ya hilo. Umekuja kwangu nikiwa sijajiandaa kama naweza kuolewa na mtu kama wewe na mpaka sasa siamini kama utakuwa mume wangu. Naona kama naota!” “Usicheke Tunda! Unanitia wasiwasi bwana! Kila wakati wewe unanikimbia tu!” “Mimi mkeo, Net. Wala huna haja yakunikimbia.” “Wewe ndio unakimbia.” “Napaniki vibaya sana, hasa nikivamiwa na watu kama mama Cote. Huo ndio udhaifu wangu. Nitajirekebisha.”

“Kwani alikwambiaje?” “Haitasaidia hata nikikwambia. Ila nimemuahidi sitamsumbua kwa kufika nyumbani kwake au sitafika mahali ninapojua atakuwepo, mpaka atakapokuwa tayari kuniona.” Tunda akarudi kukaa pembeni ya Net na kuanza kuangalia pete yake.

“Umeipenda?” Net akauliza. “Sanaaaaa! Imetoka kidoleni kwa bibi Cote! Usinitanie kabisa. Nahisi nipo ndotoni. Sasa unajua kinachofuata nini?” “Sijui.” Net akajibu huku akicheka. “Na wewe uende ukweni.” “Wapi tena? Nishamuona baba na akanipa baraka zote.” “Ujue siamini! Baba atakuwa amefurahi sana!” “Sana. Ila nimemuhurumia. Alitamani kuwepo. Na anaonekana mgonjwa. Umefikia wapi maswala yake?”

“Naona nimepata wakili mzuri kweli. Anafanya mambo kwa haraka! Ameshaanza kukusanya uthibitisho. Yaani hii ni siku kama ya 10 tokea aanze, ameshakwenda kuzungumza na baba zaidi ya mara tatu, ashakata rufaa. Ijumaa alinipigia simu kuwa anashugulikia jumanne apate ruhusa ya kwenda hospitalini. Japokuwa kampuni yao inadai pesa nyingi, lakini naona wanafanya kazi kwa ukweli.” Tunda akaendelea.

“Pesa ya kodi ya hapa nimemuomba mwenye nyumba anisubirie kidogo. Ili kuwalipa wao wanasheria kwanza, ili wajue ninampa baba kipaumbele, wafanye haraka. Na nimelipa kodi yote ya kule ofisini. Ili mwenye nyumba asinitoe. Pale napapenda. Ni rahisi watu kufika, halafu pako wazi, barabarani. Panajiuza penyewe. Sitaki kupapoteza kwa sasa. Kwa hiyo kuhusu baba, naona jumanne, anaweza kupata ruhusa ya kwenda kutibiwa. ” Tunda akamalizia hivyo.

“Cha kwanza nakupongeza Tunda. Umekuwa na malengo unayohakikisha unayafuatilia. Unanifanya nijisikie vizuri.” Tunda akacheka. “Najitahidi hivyo hivyo.” “Unafanya vizuri sana. Halafu kuhusu hapa, kwani unampango wa kupafanyia nini baada ya kufunga ndoa?” Tunda akacheka tena, nakuzungusha pete yake ya uchumba.

“Bado siamini!” “Ndio tunatakiwa kufikiria hilo.” “Kwani ulitaka tufunge ndoa lini?” “Haraka iwezekanavyo.” Tunda akatulia kidogo kama anayemtaka afikirie zaidi. “Au wewe ulifikiriaje?” “Mimi tena! Sina kipingamizi Net. Nasubiria kwa hamu kweli!” “Kwani kodi ya hapa inaisha lini?” “Mwisho wa mwezi huu. Nilitakiwa kulipa kodi tokea tarehe moja.” “Basi mwambie mwenye nyumba kuwa utahama. Unaomba umlipe ya mwezi mmoja mwingine, lakini unaweza usikae mpaka huo muda ukaisha.”  “Akipata mmpangaji kabla hatujafunga ndoa?” Tunda akauliza.

“Cha kwanza nitajitahidi kuhakikisha tunafunga ndoa haraka. Nitazungumza na mchungaji wako na wangu. Japo walishatangulia kuniambia, ni lazima itangazwe mara tatu. Inamaana kama tukifanya kwa haraka, wataanza jumapili ijayo. Zipite jumapili tatu, Mungu akisaidia pakawa hakuna kipingamizi, basi, jumamosi ya nne yake, itakuwa harusi yetu.” Tunda akacheka kama asiyeamini.

“Ikitokea kuna jambo hapo katikati, tukashindwa kuona kwa muda huo, sitashindwa pakukuweka mpaka tufunge ndoa.” Tunda akajisikia vizuri sana. “Asante Net. Ninafuraha yakupitiliza.” Net akacheka. “Karibu.” Akajibu Net.

“Lakini Net, baba akitoka jela, nilitamani kuishi naye kwa muda. Angalau arudie hali yake ndipo nimtafutie kitu chakufanya awe na maisha yake.” “Na mkewe?” Net akauliza. “Kwa jinsi alivyonisimulia, ni kama yule mwanamke alimwambia waachane siku tatu kabla ya hukumu. Akambembeleza wasiachane, amsamehe kwa lolote linalomsababisha kumuomba talaka. Lakini anasema siku moja kabla ya kwenda mahakamani, mama Chale, alimwambia ameshafuatilia mipango ya talaka. Hamtaki tena. Hata kama atashinda kesi, akitoka mahakamani asirudi tena nyumani. Aendelee na maisha yake. Na baba anasema hajamona tena tokea afungwe.”

“Alishajaribu kumtafuta kwa simu?” “Hizi ni jela za Tanzania Net. Anamtafutaje? Ila anasema alipokuwa mahakamani siku ile, alimwambia dada yake, mama Sera, akamwambie Mama Chale kuwa amehukumiwa kifungo na atakuwa Segerea. Hakumtafuta mpaka juzi ijumaa mimi nazungumza naye, baba hajamuona wala kumsikia.” Net akanyamaza.

“Sitaki akitoka jela ajikute peke yake mtaani.” “Hata mimi nisingetaka iwe hivyo. Tutajua chakufanya siku hiyo. Ila kwa sasa chamuhimu ni kumkazania huyo wakili wake, ahakikishe anakwenda kutibiwa. Amedhoofu sana. Halafu nilimshika ni kama anahoma.” Tunda aliinama na kunyamaza.

“Atakuwa sawa tu. Jumanne sio mbali. Nikuwatafuta tena kesho na kuweka msisitizo.” “Nitampigia tena kesho kujua amefikia wapi. Na nitakwenda kumuona baba kama nitaruhusiwa kumuona. Nijue anaendeleaje.” Net akamsogelea na kumbusu kichwani pale alipokuwa amekaa na kuinama kama anayefikiria. “Asante.” Tunda akamgeukia na kumshukuru. Akampa tabasamu.

“Unafikiria nini tena? Mbona hilo la baba ni kama limekaa vizuri?” “Kuna sehemu mbili nataka kwenda.” “Wapi?” Net akauliza wakati anamvuta mkono. Akaubusu. Tunda akacheka. “Kwa shangazi. Huko ni lazima twende wote, kama kuwaringishia tu kina Sera, lakini nitajidai nimeenda kuwashukuru kwa kunipa hifadhi wakati ule mpaka nikakutanishwa na wewe.” Net akacheka sana.

“Tunda!” “Oooh kabisa Net. Walijaribu kuzuia baraka zangu, lakini ona Mungu alivyohakikisha mpaka nimepata, japo kwa kuchelewa!” Tunda akamuonyeshea Net kidole chake chenye pete. Wakacheka.

“Usifanye mchezo na Mungu wangu! Hatatulia mpaka aone napata aliyonikusudia.” “Sasa mbona unatingishwa na mama kama unalijua hilo?” “Mama yako yule habari nyingine. Kwanza ujue ni kama kwake inabidi kujirudi kidogo. Nimemuumiza yule mama. Anahaki. Tuendelee na sehemu nyingine ninayotaka kwenda. Japo...” Akasita na kumwangalia Net, macho yakagongana, ikawa kama ameamsha kitu kwa Net. Akashangaa Net anamvuta karibu nakuanza kumbusu.

Tunda akaona alitendee haki lile busu. Akapandisha miguu yote kwenye kochi, akamgeukia Net akawa kama amejilaza kwake. Walipeana mabusu ya muda huku Net akimpapasa vizuri, mpaka akamuamsha Tunda, nakuanza mihemo. Ile hali ikaendelea, Tunda akiendelea kupata busu huku akisikia mikono ya Net mwilini mwake nakumfanya azidi kujisogeza. Kasi ikaongezeka, wakaanza kung’ang’aniana kwa uchu na tamaa, kila mmoja anamtaka mwenzake zaidi. Net alipoona na yeye anakaribia kupitiliza, akasimama kwa haraka, akaenda kwenye friji ya Tunda.

“Kuna maji ya kunywa humu?” Tunda akaendelea kuvuta pumzi taratibu huku ameinama kwa aibu akijaribu kutulia na Net mwenyewe akijaribu kutulia huko alipokua. Tunda hakumjibu wala kumwangalia. Akamsikia anafungua friji. Kimya kikazuka. Akamuona anaelekea chooni. Tunda kimya, ameinama palepale sebuleni. Nyumba ikawa kimya kama hakuna mtu.

          “Niambie sehemu nyingine unayotaka kwenda.” Baada ya muda akamsikia akiongea akiwa anatokea chooni. “Kwa mama.” Tunda akatulia kidogo. Net akarudi kukaa palepale kwenye kochi. Akambusu tu kichwani. Tunda akacheka kwa aibu bila hata kumtizama akaona aendelee. “Nataka nikamuombe msamaha, kwa chochote nilichokosea, ilimradi tu yaishe. Nataka kuanza maisha mapya. Hata asiponisamehe, lakini nataka niwe nimefanya upande wangu, hayo mengine namwachia Mungu kama ulivyonishauri.” “Ni uamuzi mzuri.” Tunda akatulia kidogo.

“Nakuonea wivu Net! Unaye mama anayekupigania. Hataki akuone unaingia matatizoni, kitu ambacho mimi sikuwahi kukipata maishani. Hicho tu ndio kitu ninacho muheshimu mama yako. Anakupenda sana.” “Ila natamani ajifunze kuheshimu maamuzi yangu. Naona anavuka mipaka.” “Hapana Net. Yupo sahihi. Sio rahisi kwa mama mwenye upendo wa kiasi kile kwa wanae eti kuruhusu tu, mwanae awe na mtu kama mimi! Haijalishi Net. Niwe nimebadilika au la, bado ni ngumu. Ndio maana naona nimpishe kabisa. Anione pale itakapo lazimu tu, sio vinginevyo. Lakini sijui nifanyaje upande wa mali.” Net akakunja uso.

“Mali tena?” Net akauliza akiwa hajaelewa. “Hata sielewi Net. Ujue mama yako anapokuwa na mimi anapandwa sana na hasira sana. Anazungumza mambo mengi, sijui lipi ni lipi.” “Niambie kuhusu mali. Alikwambia nini?” “Naweza nisipatie sana, lakini ni kama alitamka kuwa sasa hivi nakung’ang’ania wewe simtaki tena Gabriel kwa kuwa wewe una mali nyingi kuliko Gabriel.” Moyo wa Net ulipasuka paa! Walimuonya mama Cote asije zungumza na Tunda mambo ya utajiri unaozunguka hiyo familia ya Cote.

“Umesema nini juu ya mali!?” Net akataka kujua sasa zaidi kile mama yake amesema. Kama ameharibu mpango mzima au bado. “Ni kama alisema nimejua kuwa umeachiwa urithi mkubwa sana na babu yako, na ni kama bibi yako pia akifa, wewe ndio mtawala wa mali zote huko nchini Canada. Kitu kama hicho, sijui! Akasisitiza kuwa siwezi kuwa mtawala kwenye Cote. Yeye ndio anastahili kwa kuwa amehangaika tokea mwanzo kujenga. Akasema hata kama babu yako ndio amelipia kujenga ile nyumba pale anakoishi, au sijui alisema nini, ila amesisitiza uwa yeye ndio amesimamia ujenzi wa ile nyumba kuanzia mwanzo mpaka mwisho.”

“Amesisitiza hakuna Cote hapa nchini bila yeye. Yaani hata wewe upo hapa nchini kwa sababu yake. Kitu kama hicho. Halafu anasema  nakudanganya wewe na bibi yako kuwa nimebadilika. Lakini yeye sio mjinga na wala nisidhani kuwa nimeshinda. Mnanitumia tu.” “Kivipi!?” Net akauliza akiwa hajaelewa.

“Ni mambo mengi magumu hayaelewiki Net.” “Lakini yeye alisemaje? Niambie kile alichokwambia yeye.” “Amesema wewe na bibi yako mnanitumia kila mmoja kwa sababu zenu tofauti tofauti. Vile bibi yako leo alivyonitangaza mimi kama ndiye mama Cote au mrithi sijui wa kiti chake! Wale rafiki zako na Maya wakachangamka sana pale?” Tunda akataka kumkumbusha Net, asijue Net mwenyewe bado yupo kwenye mshtuko wa hilo tangazo.

“Nakumbuka. Ehe?” Net akataka aendelee. “Mimi sikuelewa pale. Lakini yeye anasema ni kwa ajili ya mambo yake anayoyafanya. Ametangaza vile kwa ajili sijui ya watu wa chama anachokiongoza na wakubwa sijui wanaomfuatilia au watu wanaomfuatilia sijui sina uhakika! Lakini amesema amenitangaza mimi malaya ili kuonyesha na kuaminisha ulimwengu kuwa anakubali malaya, au machagudoa kwa kiasi cha kukubali malaya kama mimi kuolewa na mjukuu wake ambaye alikuwa akisubiriwa na kila mtu kujua atamuoa nani!” Net akaumia sana.

          “Haya. Akasema na wewe umenichagua mimi sio sababu ya mapenzi, ila ni sababu kama za bibi yako. Lakini zaidi kumfurahisha bibi yako kumuonyesha unamuunga mkono kwenye hizo harakati za wanawake, sijui kitu kama hicho! Yaani kuoa kahaba, au Changudoa kama mimi ni kumuunga mkono kwenye anachokifanya! Sijui bwana Net! Lakini ni  mambo yanayofanana na hayo lakini sikuelewa vizuri kwa kuwa zilikuwa shutuma nzito, zinazoendana na kweli.” Tunda akaendelea.

“Haya, ukimsikiliza tena zaidi ni kama hata mimi mwenyewe haniamini! Anasema nimekuloga. Nimekuzika makaburini ili nirithi mapesa yenu ambayo mnayo mengi, sijui! Kwa hiyo hatakubali huo utajiri au urithi ukaja kwangu wakati yeye amehangaika sana na kina Cote. Hapo napo aliongea sana Net. Mambo mengi. Sikuelewa na wala sijui katika hilo namsaidiaje.” Tunda ndiye hakuwa ameelewa. Lakini Net akafunguka macho na akili ikapata mwanga, juu ya chuki kubwa ya mama yake kwa Tunda.

Aliumia sana Net, akabaki akijiuliza hili na kujumlisha lile. Akajua mengi yanatokana na mali tu! Yeye akidhani ni mapenzi kutoka kwa mama yake, kumbe analinda mali! Ilimuumiza sana Net. Mama yake alimwambia Tunda mambo mengi ambayo alishaomba familia nzima, wasimuhusishe nayo Tunda, ili yeye Tunda aweze kumtenga Net na mali kama wasichana wengi nchini Canada. Wanaompenda yeye Net kwa kuwa ni Cote.

Net alimtaka Tunda amtizame yeye kama Net kwanza. Kabla ya Nathaniel Cote anayetangazwa na kuabudiwa huko alikozaliwa, aliko bibi yake. Kitu kinachomkera na kuona ni bora kuwepo nchini Tanzania ambapo yupo huru, hakuna anayemfahamu isipokuwa huyo mama yake na kina Gabriel. Alikotoka Net, chochote watakachofanya familia hiyo, ni tukio la kuuza magazeti kitu kinachowanyima uhuru wakuishi maisha yao.

Leo mama yake amemkosea sana, na kumuumiza sababu ya pesa! Tena akiwa amejitoa akimtumikia kwa kiwango cha chini sana akizunguka kumtafutia tenda zilizokuwa zikimuingizia yeye pesa wala si Net. Hakumdai zaidi ya mshahara wake tu. Net aliumia sana.

“Lini sasa tunaenda ukweni?” Tunda akauliza na kujisogeza kwa Net aliyekuwa amepotelea mawazoni akiwa amefunga macho. “Au umebadili mawazo, ndoa hutaki tena?” “Kukuoa wewe, sijambo nililokurupuka Tunda. Mungu alisha niandaa kwa muda mrefu sana. Nakupenda na lazima nitakuoa tu. Lakini siku kama ya kesho, jumatatu nakuwa na kazi nyingi sana, labda twende jioni.” “Sawa kwa kuwa itakuwa jioni, tuanze kwanza kwa mama. Kesho iwe mama tu.”

“Nataka nimalize hili la mama kwanza. Ikiwezekana tuwekane sawa ndipo niende kwa kina Sera. Lakini kwa kina Sera lazima.” “Sawa.” Waliendelea kuongea wakiweka mipango, mwishowe Net akaaga na kuondoka akiwa ameumia sana, Tunda sijue.

Jumatatu!

Siku hiyo ilianza na hekaheka kweli hasa kwa Tunda. Alianzia ofisini kwa wakili wa baba yake. Wakazungumza na kumuhimiza ni lazima baba yake kesho apelekwe hospitalini. Baada yakumsikia mikakati yake na pale alipofikia, akaridhika na kuondoka kurudi ofisini kwake. Siku za jumatatu hawakuwa wakiwasiliana sana na Net zaidi ya salamu ya asubuhi kabla hawajatoka kitandani. Watapeana mipango ya siku nzima, siku inaanza.

Hakuwa amemsikia Net siku hiyo, na yeye akaendelea na kazi zake akiwa na Betty tu, wakiongea hapa na pale. Betty alikuwepo kanisani siku iliyopita. Akataka kuiona kwa karibu pete hiyo ya Tunda. Basi, akaitizama na kuishika. “Umeuchinja dada Tunda!” Pesa huleta heshima. Japokuwa Betty alikuwa mkubwa kwa Tunda bosi wake, aliweka heshima. Tunda alicheka tu.

Kazi ziliendelea, ilipofika mchana Jaz, msichana aliyemkimbia Tunda pale kazini, akarudi kuomba kazi tena. Week ilishapita, hakuwepo kazini, na siku ya jumatano alipokwenda kwenye bible study, hakumsalimia Tunda bosi wake. “Kwa nini unataka kurudi na kwa nini uliondoka Jaz?” Kimya. “Umesambaza maneno mengi machafu kanisani juu yangu.” “Nisamehe.” “Nimekusamehe lakini hapa sitahitaji tena mtu wa pili. Tumeshauriana na mama Penny, tumeona Betty peke yake atatosha. Kwanza ameweza kufanya kazi zote bila shida. Ni kweli hata ukirudi humu, hutakuwa na kazi ya kufanya. Halafu sitaweza tena kukulipa na wewe kwa kuwa nimeamua kumuongezea mshahara Betty, kwa kuwa nimemuona ameweza kufanya kazi zako vizuri bila shida wala kulalamika kama wewe Jaz. Nashauri urudi kwa mama Penny, anafahamiana na watu wengi. Atakusaidia kupata kazi kwengine.” Tunda akamuaga, ikabidi Jaz aondoke. Hata Betty hakuamini kama Tunda amefanya hivyo. Na yeye nidhamu ikaongezeka.

Baada ya miaka mingi, Net mrudisha Tunda kwa mama yake mzazi, Akiwa mchumba.

Ilipofika kwenye mida ya saa 10 jioni, Tunda alirudi nyumbani kwake kwenda kujitayarisha kwa kwenda kumuona mama yake. Wasiwasi ulizidi kumsumbua. Hofu ya kuja kuiona tena sura ya baba Tom, ikazidi kumkandamiza nakutamani kama asiende tena. Baba Tom alikuwa msaliti mkubwa sana kwake. Alimtelekeza akiwa na mimba yake!

Net alifika nyumbani kwa Tunda. Alimkuta ameshajiandaa lakini anawasiwasi sana. “Umependeza sana. Lakini usoni unaonekana una hofu yakupitiliza!” “Nimeshindwa kula siku nzima, namuwaza yule baba. Nafikiria kwenda kuomba msamaha ambao nilikuwa nikisubiri miaka yote kuja kuombwa mimi!” Tunda akaanza kulia.

“Hujui jinsi alivyonitesa, tena bila msaada wa mama, Net.” “Nisikilize Tunda. Unafanya kitu sahihi. Unasamehe kwa ajili ya nafsi yako si kwa ajili yao. Utaona amani utakayopata baada ya hapo. Muachie Mungu atapambana naye. Wewe twende ukafanye kwa nafasi yako.” “Mama akinifukuza?” “Tutaondoka. Wala usiwaze upande wao, twende ukafanye upande wako.” Tunda na Net wakaondoka mpaka nyumbani kwa mama yake Tunda huko mitaa ya Kitunda alipowaacha wakiishi.

Kitunda kwa Mama Tunda!

Tunda alishangaa kukuta familia ngeni kabisa kwake. Akamsalimia mama aliyemfungulia mlango, kisha akaeleza shida yake. “Tunaweza kumuona Mama Tom?” Akaguna yule mama akiwa amesimama palepale mlangoni. “Sipendi usumbufu wa usiku usiku!” “Samahani. Tumechelewa kwenye foleni.” Tunda akajibu kiustarabu. “Sijui kama huyo Mama Tom Yupo! Labda mpite huko nyuma.” Alijibu mwanamke aliyewafungulia mlango, huku akionyesha kidole kuwaashiria wapite. “Asante sana.” Tunda akashukuru na kumvuta Net mkono.

Nyumba ilikuwa imejaa watu asiowafahamu kabisa. Ule usafi aliouacha kwenye ile nyumba haukuwepo kabisa. Kwa kuwa alikuwa akiifahamu ile nyumba, Tunda hakupata shida kutokea vyumba vya nyuma, ambavyo havikuwa vikitumiwa kipindi anaishi kwenye nyumba hiyo isipokuwa chumba kimoja kilikuwa kama stoo na kingine alikuwa akilala mfanyakazi wa kiume.

Na huko uwani nako Tunda alikuta watu wengine.  Alisita kidogo. “Habari zenu?” Wote walibaki wakimtizama. Mara ukagongwa mlango wa nyuma, mtoto akitaka auziwe icecream. Alisimama binti ambaye alikuwa na umri unaokaribiana na Tunda, akaingia ndani na kutoka na icecream. Tunda akabaki ameshangaa.

“Tunda!” Net akamshtua kidogo. “Samahanini jamani. Tunataka kumuona Mama Tom.” Wakatizamana na kucheka. “Na nyinyi pia mnamdai?” Walimuuliza Tunda na Net. “Kama mnamdai muandike maumivu tu. Wenzenu wanapishana hapa! Hivi ni jana tu walikuja kumbeba wanawake wenzake wakampeleka polisi. Kala pesa ya kikoba!” Wakacheka wote kwa kupokezana. Tunda aliumia sana.

“Sisi hatumdai. Mimi ni mwanae na huyu ni mchumba wangu.” Wote wakabaki wametoa macho. “Wewe ndio Tunda!?” Mmoja wao akauliza. “Ndiyo.” Tunda akajibu. “Mama Shangazi! Mama Shangazi!” Mmoja aliita. “Njoo umuone Tunda!” Tunda akabaki ametulia. Alishangaa kuona watu wengine wanatoka nyumba kubwa na wengine vyumbani kuja kumshangaa yeye kama mnyama wa mbuga za wanyama.

“Jamani, kwani Mama Tom yuko wapi?” Ikabidi Tunda kuuliza tu. “Wanae wapo chumba hicho hapo. Anawafungia kama kuku!” Tunda akasogea mpaka kwenye hicho chumba alichoonyeshwa, huku Net akimfuata nyuma.

Akaanza kugonga. “Nani?” Sauti kutoka ndani ikauliza. “We Tom! Ni mimi Tunda. Fungua mlango.” Waliona taa ya ndani imewashwa kisha mtu akachungulia dirishani. “Umesema Tunda, dada Tunda?” “Ndiyo. Ni mimi, fungua usiogope.” “Wewe Tom, mama amesema tusimfungulie mtu yeyote. Shauri yako.” Walisikia sauti ya mtoto wa kike ikimuonya Tom.

“Ni Tunda. Tunda yule dada yetu. Wewe humjui ulikuwa mdogo sana. Tena alikulea. Nimfungulie?” “Sijui.” Walikaa kimya kwa muda. “Kwani mama yuko wapi?” Tunda akauliza. “Ametoka muda kweli! Amesema tusitoke wala kufungua mlango mpaka yeye mwenyewe awepo.” Tom akajibu. “Basi sisi tunaenda kumsubiria nje kwenye gari. Akirudi mama, mje kutuita.” Tunda akashangaa mlango unafunguliwa, kisha Tom akatoka.

“Mbona uliondoka bila kuniaga?” Ndio swali la kwanza Tom akamuuliza Tunda. “Sikujua kama sitarudi tena. Mnaendeleaje?” “Njooni ndani.” Tom aliwataka waingie ndani. Tunda na Net wakaingia kisha akafunga mlango tena. “Aneti amekuwa mkubwa! Njoo unisalimie. Sijui unanikumbuka?” Tunda alimuongelesha yule mtoto wa kike kwa upendo.

“Mimi ndiye nilikuwa nikikulea.” Tunda aliongeza, lakini Aneti hakujibu. “Umekuwa mkubwa Tom! Mnaendeleaje?” “Umependeza sana Tunda, dada yangu!” Tom akajibu. “Asante.” “Huyo ni nani?” Tom akauliza. “Ni mchumba wangu, anaitwa Net.” “Umepata mchumba wa kizungu!? Ndio maana umebadilika Tunda. Anaonekana ni mzungu mwenye hela. Anasikia Kiswahili?” Tunda akacheka. Akakumbuka utundu wa Tom.

“Anaelewa kila kitu. Hapo alipo anakusikiliza na anaelewa kila kitu unachoongea.” “Acha masihara bwana Tunda! Usiniogopeshe. Mbona haongei sasa?” Tunda akazidi kucheka. “We Tom hujaacha utundu tu?” “Mambo yamebadilika dada! Mama amekuwa kama kichaa.” “Baba yako yuko wapi?” “Amefungwa.” Tunda akashtuka sana. “Nini tena!?” Tom akanyamaza, akaonekana kusita.

“Kuna nini Tom?” “Alikuwa akimfanyia mambo mabaya Aneti, halafu alimbaka dada wa kazi.” “Yule niliyemuacha?” “Yule alizaa naye, mama akamfukuza na kuletewa na bibi mtoto mdogo kutoka kijijini. Ndiye aliyekuwa akitusaidia kazi.” Tunda alimwangalia Aneti kwa kumuhurumia sana. “Pole Aneti.” “Hapo bado yupo kwenye matibabu. Tulikuwa hatujui kitu anachomfanyia Aneti, mpaka akaanza kunuka sana.” Tom akaendelea.

“Kumbe alimuambukiza mtoto ugonjwa wa zinaa, mama kuja kumpeleka hospitalini akaambiwa Aneti ameharibika sana na anaugonjwa wa gonorea. Ikabidi asafishwe sana. Alikuwa ameoza. Wakati mama yupo hospitalini amelazwa na Aneti, baba akambaka yule msichana wa kazi. Sasa mimi wakati najiandaa kwenda shule asubuhi, nikashangaa yule mtoto haamki kunisaidia kuandaa chai. Kwenda kugonga, nikamkuta amepoteza fahamu.”

“Ndio ikabidi nimpigie simu mama, baba alikuwa ameshatoroka. Nahisi alimziba mdomo na pua ili asipige kelele wakati anambaka, ndio akapoteza fahamu. Mama akatuma majirani waje wamchukue na kumkimbiza hospitalini. Mambo yakafika polisi, baba akatafutwa na kukamatwa.”

“Hivi hao wote unaowaona hapo ni ndugu zake baba, wametuchukia sana. Wanatulaumu eti kwa nini tulimshitaki baba ambaye anategemewa sana huko kwao. Wanatuambia ni mambo ambayo tungepaswa kuyamaliza kindugu tu. Tangia waje baada ya baba kukamatwa, hawajaondoka tena. Wametufukuza kwenye hiyo nyumba kubwa, lakini mama amekataa kuondoka, ndio ameomba tupewe angalau hiki chumba kimoja wakati anatafuta pakwenda kuishi. Mama amechanganyikiwa kabisa, Tunda. Kazi imemshinda, anakazi ya kukopa mpaka aibu! Kila siku anakuja kudaiwa hapa, tena anadhalilishwa kweli!” Tunda alizidi kuumia.

“Amekwenda wapi sasa?” “Anasema kuna mahali anadai pesa zake. Ni mwezi sasa, anazifuatilia hizo pesa. Nikimshauri aachane nazo tuanze kuhangaika kutafuta pesa kwa njia nyingine, anakuwa mkali kweli. Anatufungia mchana na usiku. Hataki tutoke. Akitukuta nje, utamuonea huruma. Anakuwa kama mwehu. Biashara zote zimemshinda. Anazurula tu mtaani.”

“Sasa na wewe shule?” “Na kwambia siruhusiwi kumuacha Aneti hata sekunde. Nampeleka mpaka chooni. Hataki nisogee hata hatua moja mbali na Aneti. Nikimwambia maswala ya shule, ni kama haelewi naongea nini. Nikikwambia hali ni mbaya, si utani.” Tunda akabaki amepigwa na butwaa. Net alikuwa kimya akisikiliza tu. Akavuta mkono wa Tunda na kuubusu. Tunda akavuta pumzi kwa nguvu nakubaki kimya akiwatizama wale watoto.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usikose muendelezo kujua kitakachojiri mbeleni...

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment