M |
![]() |
“Kesho
ni siku yangu ya kulipia umeme hapa, pesa leo sijapata hata ya kukopa. Na
wameniambia nisipowapa pesa leo, watanifukuza kwenye hiki chumba mimi na
wanangu. Ndugu wa baba Tom ni wakorofi sana. Kiwanja kile cha Tegeta mwisho,
nimekiuza, lakini hawajanipa pesa yangu wakati nimewapa hati zote!
Wananizungusha tu.” Net na Tunda
wakabaki kimya. Mama huyo hakuwa na kituo. Aliongea kwa kuunganisha.
“Wazazi
wa yule binti aliyekuwa akifanya kazi hapa, akabakwa na baba Tom nao wananidai
fidia. Unajua yule mtoto amekuwa kama tahira? Inaonekana baba Tom alimziba
pumzi vibaya sana na kwa muda mrefu, kwa hiyo hewa ikaacha kufika kwenye ubongo
kwa muda mrefu, ndiyo iliyomuathiri. Wazazi wake wananisumbua kweli! Wanataka
niwatumie pesa kila wakati ili waweze kumtunza mtoto.” Yule mama akaendelea
kuongea kama mwendawazimu. Aliongea mambo mengi sana kwa wakati mmoja.
“Mama!”
Tunda akamwita. “Abee!” Alitaka atulie kidogo ili amwangalie kwakuwa alikuwa
akiongea huku akimbembeleza Anet kwa kumsugua mgongoni bila kupumzika, huku
akimuuliza kila wakati kama anamaumivu. “Hivi na wewe alikubaka?” Akamuuliza
Tunda. Tunda alimuhurumia sana mama yake. Alikaukwa midomo. Nywele hazikuendana
na mwanamke aliyemuacha wakati ule. Chumba alichokuwa anakaa na wanae kilikuwa
kisafi sana kama kawaida ya mama yake. Mama yake Tunda alikuwa msafi sana.
“Mmekula?”
Tunda akauliza bila kutaka kumjibu mama yake. “Hatujala Tunda. Njaa inauma
kweli. Unataka kututoa nini?” Tom akauliza na kumfanya Tunda atabasamu. Net
hakuwa ameongea kitu chochote tangia aingie humo ndani. Alikuwa kimya kabisa
akisikiliza na kushika mkono wa Tunda kama kumtuliza.
“Mnataka
nikawaletee chakula humu humu ndani au mnataka twende wote?” “Naomba tutoke
kidogo mama. Tumekaa sana humu ndani. Tafadhali mama yangu. Tupo na Tunda
hakuna atakaye tudhuru.” Tom alimbembeleza mama yake. Kabla mama yake hajajibu
kitu, wakasikia hodi mlangoni.
“Tunataka
pesa ya umeme. Leo ndio tulikwambia mwisho. Unatukimbia kila siku, na ahadi
haziishi! Huwezi kuendelea kuishi bure, eti sisi ndio tuwe tunakulipia!
Haiwezekani” “Nakuja sasa hivi, nina wageni.” Yule mama akajibu lakini
alionekana na wasiwasi mwingi sana usoni. “Muongo! Kwani wageni wanakuzuia nini
kutoka na kutoa pesa? Tupe pesa bwana.” Tunda aliumia sana kuona jinsi mama
yake anavyo dhalilishwa pale tena mbele ya Net!
Tunda
akatoka. “Kwani mnamdai kiasi gani?” Tunda alipotajiwa hicho kiasi cha pesa
ndipo alipochoka kabisa. Akatoa hiyo pesa kwenye pochi akamkabidhi yule mama,
ambaye ndiye dada yake mkubwa Baba Tom.
Tunda akaamua
kumwita Net nje. “Na nyinyi mnatukimbia nini?” Tom alichungulia mlangoni na
kuuliza. “Hapana Tom. Narudi baada ya muda mfupi tu. Nataka tuongee kidogo.”
“Nakuamini Tunda.” Tom aliongea kwa upole kama kumsihi Tunda asije kuondoka
moja kwa moja. “Nitarudi Tom.” Tom akarudi ndani na kufunga mlango.
Net na
Tunda wakarudi kwenye gari. Tunda akaanza kulia kwa uchungu sana mara baada ya
kupanda kwenye gari. Alikumbuka mateso aliyopitia akiwa mtoto kama Anet,
akimuhudumia baba Tom. Hasira juu ya uzembe kwa mama yake ilimpanda kuona wote
wanateseka akiwemo humo humo ndani. “Anashindwa wapi!?” Tunda alijiuliza akiwa
amejiinamia pale kwenye gari.
“Kwa kipi mno anachohangaikia
na kutelekeza familia kwa kiasi hicho!?” Kwa hali aliyomkuta nayo mama
yake inamaana hata mahangaiko yake ni bure! Amemkuta hana kitu, ila kudaiwa.
Kwa mateso anayosababishia binti zake, basi heri angekuwa na mamilion ya pesa
benki. Pesa hana, umama unamshinda na mume ndio huyo ameshindwa hata kujua
mabaya yake! Ni kama alikwenda kujitonesha madonda tu pale.
“Sasa
mwenzangu wewe ndio unategemewa halafu unalia!?” “Nitafanyaje
Net?” “Wewe unataka nini?” “Kuwasaidia.”
“Kuwasaidiaje?” Tunda akafuta machozi na kubaki akifikiria kidogo.
“Yale
mazingira pale yatamfanya mama azidi kuchanganyikiwa.” “Kwani ile si nyumba aliyojenga
na mumewe?” “Hapana Net. Mama alimkuta yule baba alisha jijenga. Ndio maana
hata ndugu zake wana nguvu ya kumfukuza pale.” “Lakini si amezaa naye!? Anahaki
na ile nyumba!” “Sasa vile unavyomuona mama, anaakili ya kufikiria? Yale
mazingira pale yanazidi kumchanganya. Naona nimtoe pale ndani kwa muda mpaka
akili yake itulie. Au unasemaje?” “Nakusikiliza wewe Tunda, utakavyoamua ni
sawa.”
“Naomba
univumilie Net. Najua nina mambo mengi! Mara nikupeleke jela kwa baba yangu,
mara nimekuleta hapa tena kuna matatizo!” “Mimi nakuhurumia wewe Tunda. Naona
kama mambo yamekuzidia!” “Naamini yote yatakuwa sawa. Usinikimbie tu.” “Siwezi.
Mimi nipo sawa kabisa. Wewe fanya kile unachoona kitasaidia.” “Asante,
lakini..” Tunda akasita kidogo.
“Nini?”
“Usinifikirie mimi ni mbinafsi. Lakini sijawahi kuwa na mahusiano na mama yangu
hata kidogo. Tukionana mimi na yeye ni habari mbaya tu. Ndio maana swali lake
kwangu sio kama mama anayetaka kujua ninaendeleaje! Kama nimzima! Nina
furaha! Yeye kwa miaka yote
tuliyopotezana akiwa ameniacha hospitalini amenitoa mimba ameniuliza, ‘hata wewe alikubaka?’ Hajauliza
chochote kingine au kama ambaye hana uhakika na upande wangu na baba Tom!” Net
kimya. Na yeye aliliona hilo akaamua kumezea.
“Maisha
yangu yamekuwa yakutangatanga Net. Kazi yangu ni ngumu. Pale nyumbani kwangu
ndio kimbilio langu pekee ninapoweza kupumzika. Mbali na kelele nyingi za jiji
na huko kichwani mwangu, nikirudi pale kwangu ndio naweza kupumzisha huu mwili
na kuweza hata kuamka siku inayofuata nakuendelea. Sina kimbilio.”
“Kwa
mahusiano yetu na mama, na hivi alivyo, siwezi kupata utulivu kama nitampeleka
pale kwangu. Wote tutaishia kuchanganyikiwa, hakuna atakayeweza kumsaidia
mwenzake. Naona nimtafutie sehemu ya kuishi kwa muda hata wa siku tatu tu. Kama
hoteli. Nimtafutie ambako haitakuwa garama sana. Lakini wawe wanawahudumia kwa
siku tatu au tano. Wawe wanaletewa chakula, walale, Aneti amalize matibabu,
ndipo nimkutanishe na mwanasheria akiwa ametulia ili ajue atamsaidiaje.”
“Nikiona
itachukua muda mrefu wa yeye kurudishiwa mali zake, basi nitampangishia chumba
chakuishi yeye na wanae. Lakini sio kuishi naye nyumba moja. Unafikiri nitakuwa
nimefanya vibaya?” “Sawa kabisa. Nafikiri wapo kwenye hatua yakupokea aina
yeyote ya msaada watakao letewa.” Net akaafiki kiingwana bila kuonyesha
anapendelea yeyote, ili isije kumgeuka baadaye.
“Asante.
Basi ngoja nikawachukue tuondoke nao.” “Sawa.” Net akakubali bila yakuongeza
hata ushauri. Alikuwa mchache sana wa maneno. Ni kama hakujua aongee nini na
kwa wakati gani. Jibu lake likawa ‘sawa’, na kuunga mkono kila hoja ya Tunda,
tena kwa makini sana. Hata hivyo walizaliwa kwenye tamaduni tofauti kabisa na
hali ya uchumi tofauti. Alihofia anaweza kuongeza, na kuharibu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kitu
ambacho hakuwa akijua Tunda, yupo na mtoto aliyekuzwa na mamilionea. Tena sio
wa Tanzania, wa nchini Canada. Net aliyekuwa naye hapo, amebeba umilionea
unaompeleka mbio mama yake na kumfanya halali akiwinda na kulinda hiyo pesa
isiende sehemu isiyo sahihi. Huyo Net amebeba utajiri, akiwa nchini kwao ni mtu
wakuheshimiwa sana. Hilo jina Cote linafahamika na wakuu wa nchini kwao. Ila
yeye Tunda hakuwa hata na habari wala kumuhisi. Alimtambua Net huyu wa hapa.
Mwenye uwezo wa kawaida na mwenye juhudi na nidhamu ya kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Tunda!”
Net akamwita kabla hajafunga mlango wa gari, akiwa ameshashuka garini. “Naomba
nilipie gharama hizo za hotelini.” Tunda akabaki amesimama pale akifikiria kwa
muda kama anayejishauri. “Acha tu Net. Ninayo hiyo pesa.” “Ndio unataka
kumthibitishia mama yangu kuwa unajitenga na pesa zangu?” Kama aliyekuwepo
mawazoni kwa Tunda. Tunda akaanza kubabaika.
“Najua
una mambo mengi. Na leo tena umetoka kwa mwanasheria. Unahitaji msaada Tunda.
Acha kujiumiza sababu ya mama yangu, unaishi na mimi, na utaendelea kuishi na
mimi. Mama yangu hajui nina akiba kiasi gani na wala simwambii matumizi yangu.
Na kuanzia jana nilipokuchumbia, mambo yangu mimi na wewe yatabakia kwetu tu.
Na ukumbuke mimi sikuhongi. Majukumu yako ni ya kwangu pia.”
“Nashukuru
Net. Basi nikikwama, nitakwambia.” “Hiyo ni kauli unayoirudia kila wakati
ninapotaka kukusaidia, lakini hutekelezi!” Tunda akacheka. “Kwa kuwa bado
sijakwama. Kweli tena. Nikikwama nitakwambia. Nisubiri, nikawachukue. Tutakuja
sasa hivi.” Tunda akafunga mlango wa gari, akarudi ndani. Walikuwa wakitumia
gari moja ya Net.
“Kweli, ‘Kitanda hakizai haramu’.”
Walifurahi sana kuona Tunda amerudi, tena na ahadi ya kuwatoa
pale. “Asante Tunda. Hatutakaa sana hapo hotelini. Kuna mahali nadai pesa
yangu. Wakinilipa tu, tutaondoka.” “Naomba usianze kuzungumzia kuondoka wakati
hata hamjafika. Naomba utulie mama. Mimi sitakutaka uondoke leo wala kesho, ni
mpaka mambo yako yakae sawa. Nitakupeleka kwa mwanasheria. Akisema itachukua
muda mrefu, basi nitawatafutia sehemu ya kuishi mpaka upate mali zako.”
“Kweli?” Yule mama hakuamini.
“Kweli mama. Naomba
wewe utulia, pata muda wakupumzika, ujipange upya.” “Ndicho ninachohitaji.
Nimechanganywa kweli! Limeanza tatizo moja likafuata jingine, mchana na usiku
sipumziki!” “Pole. Basi twendeni.” Walikusanya vitu vyao, wakatoka.
“Unaondoka mama Tom?” “Kama anaondoka, nachukua mimi chumba
chake. Mimi na mwanangu tunabanana na shangazi. Nataka chumba cha mama Tom.”
Wakaanza kubishana. Tunda akamshika mkono Aneti. “Twende Tom.” Tom alikuwa
amebeba mabegi mawili. Tunda akatangulia akiwa amemshika Aneti. Akafuata Tom,
mama yake akafuta nyuma. “Na ukalipe na pale dukani. Usituachie madeni.” Tunda
alisikia wakimrushia maneno mama yake. “Na gengeni pia anadaiwa.” Mwengine
akadakia. Lakini mama Tom hakujibu.
Walipopanda tu kwenye gari baada ya Net kuweka mizigo ndani
ya gari, Tunda akamgeukia mama yake. “Ni wapi huko unakodaiwa?” “Kwa mwarabu na
pale gengeni kwa mpemba. Lakini twende tu Tunda.” “Hapana mama. Isiwe ni kama
unakimbia madeni. Tulipe tu.” “Ukianza kulipa hapa, hatutakaa tukaondoka dada
Tunda. Kila jirani anatudai. Mimi naomba twende tu. Njaa zinauma. Mama arudi
kwa wakati wake.” Tom aliongeza nakumfanya Tunda amgeukie Net.
“Nakusikiliza wewe Tunda.” “Basi tutarudi tena kesho.” Tunda
akajibu. “Na hospitalini?” Net akauliza. Tunda akakumbuka jumanne ndio baba
yake anapelekwa hospitalini. Akataka kuvizia kama anaweza hata kumkuta
hospitalini akajua mambo yanakwendaje. “Nitafanyaje Net? Sitaki hii aibu
iendelee.” “Yaliyobaki sio dharula au mambo ya haraka. Lakini kama ulivyosikia,
wananjaa. Nafikiri cha muhimu nikuwapeleka kula, na wakalale. Hata jumatano
mnaweza kurudi.” Net akatoa wazo, alilokubali Tunda. Net akaondoa gari.
“Unasikia baridi?” Tunda akamsikia mama yake akimuuliza Aneti
kwa upendo. Walikuwa wamekaa kiti cha nyuma, Tunda amekaa mbele, Net ndio
dereva. “Naomba punguza baridi Net. Mtoto anasikia baridi.” Net akapunguza.
“Tom! Ulimpa dawa za maumivu?” Tunda
akauliza. “Mama alisema nisimpe kabla ya kula. Ndio tulikuwa tunasubiria mama
aje na chakula, ndio tumpe na dawa.” Tom akajibu. “Naona na homa ipo juu!” Mama
yake akaongeza. “Pole Aneti. Utapona. Umesikia eeh?” “Asante.” Akaitika Aneti.
“Kwa mida hii nafikiri kitu cha haraka kupata ni chips.
Mtapenda chips?” Tunda akauliza. “Tulivyo na njaa! Halafu unasema chips, natamani
kuruka ruka.” Tom akajibu nakumfanya Tunda acheke. “Tom!” “Wezako tulikuwa
tunashinda na chai ya rangi na mkate mkavu. Sio mchezo.” Tom akaongeza. “Basi
tutashuka wote uchague nini atapenda Aneti na mama.” Net akatafuta sehemu
wanayouza chips, akasimama pembeni kidogo. Tunda na Tom wakashuka.
Baada kama ya dakika 20 wakarudi na chakula na soda. Tunda
akampa Aneti. “Kunywa hii Fanta kwanza, tukifika hotelini ndio mtaanza kula.”
Wakaelewa kuwa hawatakiwi kula ndani ya gari. “Asante.” Mama yake na Aneti wote
wakashukuru kwa pamoja. Net akaondoa tena gari.
“Tunakwenda wapi?” Net akamgeukia Tunda. “Ndio nilikuwa
nikifikiria hapa. Pole mpenzi wangu. Najua umechoka.” “Hamna neno. Wewe ndio
nakuhurumia.” Tunda akafikiria. Mama yake na familia yake walikuwa wakiishi
mbele ya uwanja wa ndege, Kitunda. Net aliendelea kukanyaga mafuta. Walishapita
Tazara, akaingia Buguruni. Alipomuona amenyamaza, akaendelea kutafuta Ubungo.
“Kuna hoteli naifahamu ipo Sinza. Twende mpaka Sinza
madukani. Tukifika pale chukua barabara kama tunaelekea Tandale,
nitakuonyesha.” Net akamgeukia Tunda kama anayemuuliza umepajuaje. Tunda
akainama. Net akaendelea kukanyaga mafuta.
Walipofika hapo hotelini, Tunda alishuka yeye mwenyewe
kwanza. Akaenda kuchukua chumba na kulipia, ndipo akaenda kuwafuata kwenye
gari. “Twendeni.” Akamgeukia Net. “Nisubiri, sitakawia.” “Sawa.” Tunda
aliwasindikiza mpaka chumbani kwao. Kilikuwa ni chumba chenye vitanda viwili.
“Naona muanze kula wakati naenda kununua dawa za Aneti.” “Nakushukuru sana
Tunda. Ngoja nikupe kikaratasi cha dawa.” Mama yake alikuwa akitetemeka mikono.
Tunda akahisi ni njaa. “Asubuhi mpige simu wawaletee kifungua kinywa.” Tunda
aliongeza, wakati mama yake akitafuta kikaratasi.
“Asante Tunda. Nilivyokuwa na hamu na kuku!” Tom aliongea na
chakula mdomoni. Tunda akacheka. “Kaoshe mikono Aneti ili uje kula. Mwenzio Tom
alishanawa mikono pale tuliponunua chips.” Aneti akaelekea chooni, pale pale
ndani ya kile chumba. Bado mama yake hakuwa anakiona kile kikaratasi. “Nilikuwa
nacho siku nzima. Sijui nimekiweka wapi!” “Jaribu kutulia mama. Utakiona tu.
Fikiria kidogo.” Tom akamshauri mama yake. Ni kweli hakuwa ametulia.
Akasimama. “Angalia kwenye sidiria.” Tom akamshauri tena mama
yake. Akaingiza mkono ndani ya sidiria, ni kweli akakipata. “Hiki hapa!
Nilikuwa natembea nacho nikijua labda nitapata pesa, ninunue.” Akamkabidhi
Tunda. “Nakushukuru sana Tunda. Asante.” “Karibu. Basi kaa chini na wewe ule.
Nitarudi nikipata dawa.” Tunda akatoka.
Alimkuta Net ametulia kimya kwenye gari. Akapanda na kufunga
mkanda. “Pole Net.” “Mimi nipo sawa kabisa.” “Mbona kama unamawazo?” Net
akamtolea tabasamu na kumsogelea pale kwenye kiti Tunda alipokuwa amekaa na
kumbusu. Tunda akajua ndio hataki kujibu.
Akambusu kwa muda kidogo, akamwachia. “Usiwe unabeba vitu
peke yako Net. Nishirikishe na mimi.” Tunda hakutaka kupotezea. “Sawa.
Nitafanya hivyo.” Tunda akacheka. “Sasa naomba mimi unirudishe nyumbani,
nikachukue gari yangu ili nikaanze kutafuta dawa za Aneti. Sijui nitazipata
wapi! Sitaki kuendelea kukuzungusha.” Net akacheka na kuondoa gari.
“Nafahamu duka la dawa kubwa pale Mwenge, na jingine
Mikocheni B, kama tukikosa hapa Sinza kwenye maduka ya madawa.” Tunda akaelewa
kuwa ndio ameambiwa atakuwa naye mpaka mwisho. Akakumbuka vile Net
alivyomwambia akianza jambo huwa ni mpaka amalize, hata kama ni gumu kwa kiasi
gani.
“Nakupenda Net.” Tunda akavunja ukimya kwani kila mmoja
alikuwa akiwaza lake. “Asante Tunda. Lakini nipo sawa. Usiwe na wasiwasi.” “Ni
nini?” “Ni mambo yakifamilia tu.” “Mimi nahusika?” Tunda akauliza, lakini Net
akamtizama na kutabasamu. Ndipo Tunda akajua ni yeye tu ndiye anayesababisha
kutokuwa na amani huko nyumbani kwa kina Net.
“Pole Net wangu. Natamani nikwambie tuachane ili kila mtu
apumzike, lakini naona nishanogewa.” Net alicheka sana. “Sasa hivi nakutaka kwa
nguvu zote.” “Hutaki tena tuachane?” “Hata kidogo. Kwanza hiyo sentensi
ishindwe kabisa!” Net alizidi kucheka. “Uje unitoe hii pete kidoleni?”
“Hutaki?” “Sikubali! Nakuhurumia, lakini nakuombea Mungu akutie nguvu huko
kwenye matatizo ya kifamilia, usiahirishe ndoa.” Net alizidi kucheka.
“Sawa mama Cote.” “Tena ukiniita hivyo ndio kabisa. Endelea
kupambana tu mpenzi wangu. Sisi ni washindi zaidi ya kushinda.” Angalau
waliendelea kucheka. “Naona mpaka unatumia maandiko.” “Mbele ya ndoa! Hamna
namna, lazima bibilia ihusike.” Walizidi kucheka, angalau akamuona Net,
ametulia kidogo.
Walipata dawa, wakarudi tena hotelini. Tunda aliwaletea maji
ya kunywa, chupa 6, juisi ya Aneti yakumezea dawa. Aliwakuta wamejilaza, Tom
ndiye aliyemfungulia mlango dada yake. “Sitakaa sana. Nitarudi kesho jioni
kuwaona. Net atakuwa amechoka, inabidi awahi kurudi kwake akapumzike.” “Hongera
Tunda. Tom ameniambia ni mchumba wako. Anaonekana muungwana.” Tunda akacheka
kidogo. “Asante mama. Namshukuru Mungu. Basi muwe na usiku mwema. Dawa zote za
Aneti mpaka amalize dozi nzima zipo hapa, na za kushusha homa. Nitawaona
kesho.” Tunda akatoka.
Kwa Net kumepamba Moto. ipango mikali dhidi yao yaendelea.
W |
akati Tunda anahangaika na
wazazi wake, Net naye alikuwa akipitia changamoto zake. Jumatatu baada ya Tunda
kuvalishwa pete, mama Cote hakutaka hata kupoe. Akamwita tena Bethy na mumewe
Gabriel, ambao hakuwepo kwenye kuchumbiwa kwa Tunda. Kila mmoja wake alimpa Net
sababu ya kutokuweza kuhudhuria kwao kwenye shuguli nzima. Kuanzia kanisani
mpaka jioni kwenye tafrija. Mke na mume wote walisema wasingeweza kufika. Net
hakujali. Aliyetaka awepo ni Tunda, basi.
Gabriel
na mkewe walifika kwenye hoteli hiyo kwa muda tofauti tofauti na wote
walionekana ni kama hawapo kwenye mawasiliano. Alianza kufika Bethy. Alimkuta
mama Cote akiwasubiri. Akasalimia, nakukaa. Baada ya kama dakika 10 hivi, ndipo
Gabriel naye akafika. “Samahani nimechelewa kwa kuwa nilikuwa na miahadi na mtu
ambaye nisingeweza kumuahirisha. Na baada ya dakika 45 kuanzia sasa, natakiwa
kuwa sehemu nyingine.” Gabriel alizungumza hivyo na kukaa bila salamu.
Kaka
huyo mtanashati mwenye mafanikio hapo mjini, na yeye Mungu alimjalia uzuri wa
kiume, ungependa kumtizama. Mkewe hakujibu. Akageukia pembeni. Akajua wapo na
ugomvi. Mama Cote hakujali. Bora yake yamwendee sawa.
“Pole na
majukumu, Gab.” Mama Cote akajibu hivyo, mkewe kimya. “Asante na wewe.” Gabriel
akajibu. “Nashukuru lakini bado tatizo lipo pale pale. Jana Tunda amevalishwa
pete ya uchumba. Na Net anaonekana anataka harusi ya haraka. Tunda amefanikiwa
kumwingia yule bibi. Naona amemtangaza kabisa kama ndiye mrithi.” Akalalamika
mama Cote.
“Kabla
hujaendelea sana mama Cote, mimi binafsi naomba nijitoe. Sioni kama ni tatizo
langu. Bethy alinilazimisha siku ile kukutana na Tunda, akisema ni lazima ili
kuhakikisha kama ni kweli sijawasiliana tena na Tunda. Nikakubali kudhalilika
mbele zenu. Nasikia mmetumia fedheha yangu, kuyanadi mapenzi ya Tunda kwa Net
kanisani, ambaye kwangu amekuwa msaliti.” Kila mtu akashtuka.
Mkewe
akamkazia macho. “Ndiyo. Net alinionya mimi nisiwe na Tunda, halafu akamchukua
yeye! Aka…” “Subiri kwanza Gab! Yaani leo bila hofu unasema hapa umenyang’anywa
mwanamke wako mbele yangu na ukiwa kwenye ndoa!?” “Ndoa gani Bethy? Ndoa ipi?
Unataka kumdanganya mama Cote ili iweje? Ndoa ilishaisha na kwa Tunda mimi
sikukosea kuwa naye. Hata mchungaji nilimwambia kuwa nataka kumuoa Tunda. Na
Net pia nilimwambia. Akatumia ujanja wake, akamchukua mwanamke wangu.” Mama
Cote alibaki ametoa macho.
“Wewe ni mshenzi Gab.” “Wewe ndiye mshenzi.
Ulimuahidi nini Net na mchungaji na unafanya nini sasa hivi!? Hujabadilika hata
kidogo. Kiburi vilevile. Nyumba haikaliki na sina pakukimbilia kwa kuwa Net
amechukua faraja yangu.” Bethy alichukua kinywaji alichokuwa akinywa mama Cote,
akamwagia Gabriel.
“Acha fujo zakijinga Bethy.” Gab akasimama huku
akijikung’uta. “Naombeni mtulie Gab na Bethy. Tulieni.” “Sasa kama ulifikiri
utamuoa Tunda, andika maumivu. Mimi ndiye nitahakikisha Net anamuoa Tunda. Na
nitakuona kama utapasuka. Wewe si unajidai unamlilia Tunda!? Sasa
nitakukomesha.” Bethy akachukua pochi yake nakuondoka kuelekea kwenye gari
yake. Mama Cote akasimama na kumkimbilia Bethy kwa haraka.
Zile hazikuwa habari njema hata kidogo kwa mama
Cote. Bethy hawezi kwenda kinyume naye. Alitaka watu wengi upande wake ili
kuhakikisha anashinda kuwatenganisha Net na Tunda. Kitendo cha Bethy kuapa
atamsaidia Tunda kuolewa na Net, asingeruhusu. “Bethy! Bethy!” “Hapana mama
Cote. Kwa nini unataka kuvunja kwangu ili yako yakuendee sawa? Atakapoachika
Tunda, inamaana atakuwa huru. Unafikiri itakuaje kama sio kuolewa na Gab!?”
Hapo Bethy akawa ametumia akili.
Mama Cote akatumia akili za haraka sana kumrudisha
kwenye mstari. “Tulia nikwambie Bethy. Lazima wote tutumie akili. Na tumjue
adui yetu na kumtoa kabisa. Maana hakuna uhakika kama Tunda akiolewa na Net,
ndio hatarudiana na Gabriel.” Kidogo Bethy akatulia.
“Yule binti ni Malaya, na ananguvu za giza zakuweza
kumwingia mtu au kugeuza watu wawe upande wake. Huwezi amini jinsi mama mkwe
wangu jinsi anavyomsifia! Amekuwa ni kama amemfahamu huyo Tunda kwa miaka
mingi! Maya naye ndio kabisa. Anatoa shukurani zake kwa Tunda kumfanya arudi
shule na kupata shahada yake ya kwanza! Anasema bila Tunda, asingekuwa vile
alivyo wakati mimi nimehangaika sana na wale watoto! Sio kitu cha kawaida.
Lazima wote tusimame pamoja, tumtoe kabisa Tunda kwenye maisha yetu wote.
Tusipoangalia anaweza akapata vyote. Net na Gabriel. Hebu tulia na kumfikiria
Gabriel. Kwa nini gafla aone ndoa yake haifai, wakati matatizo yenu hayakuanza
leo?” Mama Cote akazidi kumvutia Bethy.
“Maana ni kweli. Gab hakuwahi kuwa mlalamishi.
Mambo mengi alikuwa akisema tuombe! Gabriel alikuwa mtu wakufunga na kuomba
kila wakati. Tena yeye ndiye alikuwa mstari wa mbele hata kutotaka watoto
watuone tunapishana maneno. Ugomvi wote alitaka uishie chumbani.” Bethy
akaendelea.
“Hata nilipokuwa nikimpandishia mbele ya watoto au
wafanyakazi pale nyumbani, alikuwa ananyamaza, na kuelekea chumbani. Sasa hivi
amekuwa kama mwehu! Anatoa mambo ya ndani kabisa hadharani! Zile sio akili zake
kabisa. Amegeuzwa.” Angalau hapo mama Cote akampata, japo alikuwa akimshangaa
moyoni. Kwa nini asifikirie labda mwenzie amechoka! Hata mama Cote aliwaza,
akaamua kwenda naye hivyohivyo kutumia ujinga wake kwa manufaa yake.
“Sasa tutafanyaje!?” Bethy akamuuliza mama Cote.
“Net anamsimamo sana. Nilazima kumfungua macho juu ya Tunda. Aelewe kuwa Tunda
ni mshirikina na lazima atakuja kumgeuka tu.” “Sasa uthibitisho tunaupata
wapi?” “Ndio tuanze kuhangaika.” “Kumbuka tumebaki wawili tu na wote
tunamajukumu mazito.” Bethy akaanza kuona ugumu wa hiyo Vita anayotaka
kuianzisha mama Cote dhidi ya Tunda.
“Watu wapo Bethy. Wala usijali. Wewe tulia kabisa,
nitakupa mipango yote. Usiharakishe kumfikisha Tunda kanisani, aolewe na Net.”
Wakacheka. “Mwenzangu niliingiwa na hofu! Siwezi kumruhusu Tunda anichukulie
mume. Hata kama tunaburuzana, hivyo hivyo. Akiniacha sasa hivi Gabriel, si
nitafia mtaani?” “Hawezi. Na hata kama akikuacha, lazima mali mgawane nusu kwa
nusu. Si mmezaa naye bwana? Na watoto bado wadogo, utatakiwa wewe ndio
uwatunze.” Mama Cote akamuona Bethy anababaika wala asifurahie. Akahisi kuna
jambo limejificha hapo.
“Kwani
vipi?” “Ngoja niwahi mama Cote. Nimeacha wateja ofisini kwangu ili nikuwahi.
Sasa maadamu sasa hivi tumefikia muafaka. Na adui yetu ni mmoja, Tunda,
turekebishe mambo mapema.” Bethy akajichekesha na kuingia kwenye gari bila
kutaka kujibu swali la mama Cote. Lakini mama Cote akajua lipo jambo juu ya
hiyo ndoa.
Gabriel kwa Net!
G |
abriel alitoka pale na hasira.
Akampigia simu Net. “Nilifikiri wewe ni rafiki yangu,
kumbe mtu wakunizunguka!” Net akashtuka
kidogo. “Kwema Gab!?” “Kwako ndio kwema, sababu unaye
mwanamke wangu ambaye anakuliwaza. Unashida gani!? Tatizo lipo wapi! Umeniacha
kwangu kunawaka moto. Faraja pekee niliyokuwa nayo umejidai kutumia jina la
Mungu kumchukua mwanamke wangu!” Net kimya.
“Ulipiga mahesabu ya haraka, ukakimbilia kwa wachungaji kwenda
kunishitaki, ukitumia kigezo kuwa nina ndoa takatifu, ili wakusaidie kumtoa Tunda
upande wangu, halafu wewe ndio akuone mwema sana kuliko mimi, halafu akutake
wewe, mimi anihesabu msaliti.” Gabriel alisikika akiongea kwa machungu
sana.
“Niliwaeleza wazi bila kuwaficha juu ya mwanzo wangu mimi na Bethy
mpaka sasa. Matatizo ninayopitia kwenye ndoa yangu kila siku. Mkakazana
kufunika, mkitumia maneno ya kwenye bibilia. Huku mkinikumbusha kuwa Tunda
hakuwahi kunipenda, alikuwa akinitumia mimi kama wanaume wengine anavyowatumia.
Nikae naye mbali. Mbona wewe sasa unamuoa!?” Net kimya.
“Nakuuliza Net. Kama Tunda ni mbaya, kwa nini wewe unamuoa?” “Kwanza
mimi siye niliyefikisha mambo yako kwa mchungaji. Ni mkeo. Mimi niliitwa tu
kueleza kama nafahamu hayo mahusiano na kama ulinishirikisha kama unataka
kumuacha Bethy umuoe Tunda. Ndipo nikaeleza upande wangu kwa kile
ninachokifahamu juu yako na maisha ya Tunda. Pili.” Net
akaendelea.
“Sikuwahi kukwambia kama Tunda ni mbaya, Gab. Nilikueleza kwa kifupi
maisha yaliyompelekea Tunda hata kukutafuta wewe. Alikuwa na shida na pesa yako
sio wewe kama Gabriel. Hata mlipomtega ili kuona kama atakurudia tena,
alikwambia kwa wazi kabisa Gab. Hukuwahi kuwa na mahusiano na Tunda ila Nancy
ambaye sasa hivi hayupo.” Net akajaribu kujitetea.
“Nani alikwambia nilikuwa na tatizo juu ya hilo? Ni afadhali ya Tunda
sijui Nancy ambaye alikuwa anakula pesa yangu, lakini ananiheshimu na kunipa
pumziko, kuliko Bethy ambaye anavuna ambako wala hajapanda! Ukanitibulia
mapenzi ya kweli, kwa wivu wako, ukiona ninafaidi, ili na wewe unufaike
ukisaidiwa na wachungaji! Leo wanakupa baraka kwa mwanamke asiye wako! Na wao
uwafikishie salamu zangu maana huko sitarudi tena.” Hapo
Net hakuwa ameelewa.
Maana
anajua Bethy na Gabriel walianza zamani sana. Tokea Gabriel anarudi
nchini, mwanamke wa maana
aliyemtambulisha kwao ni Bethy, na akaja kumuoa baada ya muda mfupi. Mara
kadhaa alishakwenda na Bethy nchini Canada kuwatembelea kina Cote, akiwa tayari
mkewe.
“Cha pili, mimi sikumtega Tunda.” Gab akaendelea. “Siwezi kujidhalilisha mwenyewe. Mimi sio mjinga. Ni mama
yako ambaye mpaka leo, tena sasa hivi hapa ametoka kutuitisha kikao, akitaka
tuendelee kumuunga mkono kumuangamiza Tunda. Nimejitoa kwa kujiweka wazi
kabisa, kuwa hata mwanzoni nilikubali
sababu ya kelele za Bethy. Lakini sitarudia huo ujinga kwa mwanamke
ninayempenda.” Gab akaendelea, asijue jinsi alivyomshtua Net juu ya
hicho kikao cha siri mama yake alichoitisha.
“Na umwambie mama yako kabisa Net, chochote kibaya atakachomfanyia
Tunda, atapambana na mimi. Wapange mipango yao kukuangamiza wewe ili usimuoe
Tunda, lakini sio Tunda. Na wewe nakuhakikishia kabisa Net, utaiona hii nchi
chungu. Wewe si unajidai mjanja? Sasa nakwambia huwezi kufunga goli kwenye
uwanja wa ugenini. Mtu kwao. Hata kama unamamilioni ya mapesa, nitakuonyesha
mimi ni Mtanzania wa kuzaliwa sio kuombewa vibali vyakufanya kazi.” Gabriel
akakata simu kwa vitisho hivyo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment