T |
![]() |
Alishtuka
saa kumi asubuhi akaamua kwenda tu ukumbini kuanza kupamba mara baada yakukosa
ujumbe kutoka kwa Net. Alishinda akipamba siku nzima, akitoka ukumbi mmoja
kwenda mwingine mpaka usiku sana ndipo aliporudi nyumbani.
Akaamua
kutuma ujumbe mwingine kwa Net. ‘Nimekosa Net, nimekosa
kukuficha kuwa niliwasiliana na Gabriel. Nisamehe. Lakini sikuwa na nia mbaya
mpenzi wangu. Sikutaka kuwachonganisha na Gab. Lakini nilimwambia kabisa kuwa
nimebadilika, nimemkataa, na nilimwambia kabisa nakupenda wewe. Nakupenda Net,
na nimejifunza kutokana na makosa, sitarudia kukuficha kitu tena. Naomba
nisamehe.’ Tunda alikaa pale akisubiri mwishowe akaona simu ya Mama
Penny inaingia.
“Mbona unalia na kanisani huji tena?” “Nimechanganyikiwa
dada yangu! Ghafla maisha yamenibadilikia. Net ameniacha na kanisani wananisema
vibaya sana. Nashindwa kurudisha sura yangu pale.” Tunda alikuwa akilia
sana. Tokea jumatano ya juma lililopita alipotoka katikati ya ‘bible study’
wale kina mama wakimsema kwa kujidai wanamuuliza maswali mchungaji, hakurudi
tena. Jumapili yake alimtumia ujumbe mama Penny kumwambia kuna kitu muhimu kule
gerezani kwa baba yake, lazima aende kumuona. Ni kweli alikwenda na mwanasheria
ili kuangalia hiyo afya ya baba yake atengenezee kesi. Jumatano kwenye kipindi
cha ‘bible study’ kanisani pia hakwenda. Akamtumia ujumbe kuwa ana kazi,
hatamaliza kwa wakati.
Sasa
jumamosi hiyo usiku ndipo mama Penny akampigia. “Wale
kina mama wa kanisani, Mchungaji aliniambia nimeshazungumza nao wote, wala
usiwe na wasiwasi. Umesikia?” Tunda aliendelea kulia tu. “Net amekuacha kivipi!?” “Nilikosea
dada. Net akajua kitu nilichofanya bila kumshirikisha. Amenikasirikia kuanzia
siku hiyo, hajanitafuta wala hajibu jumbe zangu. Na nilishamwambia sikuwa na
nia mbaya.” “Labda amesafiri ndio maana
anashindwa kupata na kujibu jumbe zako.” Mama Penny akajaribu kumtuliza.
“Simu ya Net
inapokea ujumbe wa yeyote, kutoka popote hapa ulimwenguni na yeye akiwa popote
hapa ulimwenguni. Muda na wakati wowote, dada. Ni ameamua kuniacha tu.” “Usilie bwana. Naamini anayo sababu tu. Unataka nije?” “Nimechoka sana dada yangu, siwezi hata kusogea.” “Lala basi, kesho nitakuja asubuhi kabla sijaenda kanisani.”
“Sawa.” Tunda akajivuta na kujilaza hapohapo
kitandani bila hata ya kuoga.
Jumapili.
Asubuhi na mapema, mama Penny alifika nyumbani kwa Tunda
kumuona kabla ya kwenda kanisani. Ikabidi Tunda amuelezee kila kitu bila
kumficha. “Nilikosea dada.” “Najua Tunda,
lakini huwezi kufa hapa na ukashindwa kuendelea na maisha. Tulia kabisa, mpe
muda kama alivyoomba. Kama ni wako, atarudi, kama sio wako basi. Naomba
ujiandae twende kanisani.” Alihakikisha Tunda amevaa vizuri, akampa kifungua
kinywa akamwambia aache gari yake yeye
atamuendesha. Kidogo Tunda akatulia.
Maneno mengi ya Mama Penny yalianza kumfanya Tunda aanze
kucheka njiani. Alimpa vituko vya wanae na mikasa mbali mbali ya siku iliyopita
wakati ameenda kupamba. Tunda alikuwa akicheka, japo kinyonge.
Walifika kanisani, kwa kuwa Tunda alikuwa amechoka sana
aliingia moja kwa moja ndani kanisani akatafuta kona ambayo alijua watu
hawatamsogelea akaenda kukaa na kuinama ili alale kidogo. Mama Penny kama
kawaida yake ya kuwahi na kuhakikisha kanisa limekaa vizuri. Kuanzia usafi wa
mazingira, chooni, ndani na nje ya kanisa, na kumalizia kupamba kabla mumewe
hajaja na watoto, aliendelea na pilika pilika zake wakati Tunda amelala
kanisani.
Ibada ilianza, watu waliingia na kwa kuwa Tunda alijua kila
mtu anamkwepa, hata Julius mwenyewe hakuonyesha kutaka kuwa karibu naye tena,
kwa hiyo hakutaka kusumbua nafsi yake, alibaki ameinama bila kusimama wala
kumsalimia mtu. Ibada iliendelea, nyimbo mbalimbali ziliimbwa, lakini
hakuinuka.
Alisikia watu wa viti vya mbele wakihamishiwa viti vya nyuma
kabisa kule alipokuwa amekaa yeye, huku akisikia minong’ono kuwa kuna wageni
ambao watakaa viti hivyo vya mbele. Tunda aliwaza kidogo. ‘Kina nani hao!? Mbona Mama Penny hajaniambia kitu chochote?’
Lakini kwa kuwa alikuwa amechoka sana, hakutaka kuendelea kufikiria juu ya
mambo ya wageni wakanisani wakati ya kwake yanamshinda! Akabaki ameinama
vilevile.
Watu waliendelea kuimba na kucheza wakati bado Tunda amekaa
chini huku ameegemeza kichwa chake kwenye kiti cha mbele yake, anasinzia.
Mara akasikia Mchungaji akiongea na watu wote wakakaa, ndipo
Mchungaji alipokaribisha watu watoe ushuhuda. Walisimama watu wachache
wakashuhudia yale mambo Mungu ametenda, kisha akasikia Mchungaji akisema,
naomba mtulie kimya, msikilize. Kwani waumini wengine walikuwa wakishangilia
yale waliyokuwa wakishuhudia wengine.
“Naomba msikilize kwa makini sana yale Mungu amefanya kwenye
maisha ya huyu binti.” Kanisa zima likatulia.
“Nimepata msaada
Gabriel. Nimesamehewa dhambi. Huko kwenye hayo maisha sitakaa nikarudi tena.
Nilitumikishwa na ibilisi mchana na usiku. Mungu amenifungua, nipo huru. Nimeanza
biashara yangu kwa jasho langu bila kuhongwa, na sasa hivi ninafurahia maisha.”
Tunda alisikika akilia kisha akaendelea.
“Sasa hivi anayeishi hapa ni Tunda, aliyesamehewa dhambi na kuishi
maisha ya nidhamu mbele za Mungu. Na mabaya yote niliyofanya zamani, Net
amenipokea na ananipenda kwa dhati. Naridhika na pesa ninayoingiza kwa jasho
langu na mapenzi ya Net, basi.”
Ile sauti ikapotea. Tunda akahisi yupo usingizini anaota.
Alianza kutetemeka palepale alipokuwa amekaa, akashindwa hata kusogea.
Alijiambia ni ndoto kwani alikumbuka ni maneno aliyokuwa amemwambia Gab. ‘Lazima hii
ni ndoto! Hii ni ndoto tu.’ Tunda aliwaza huku
akifuta machozi. Alihisi ni uchovu wakuto kulala vizuri kwa muda mrefu.
Akaona kabla hajaharibu zaidi pale kanisani anyanyuke,
akatafute taksii, arudi nyumbani akalale. ‘Isije kuwa naanza
kuchanganyikiwa!’ Akajisemea Tunda
akilini.
Suprise!
Tunda akahisi ukimya mkubwa sana pale kanisani, akaamua
kunyanyua kichwa. Hakuamini baada yakumuona Net amepiga goti pembeni yake. “Net!?” Tunda akashtuka sana kumuona Net pale. “Ni nini, kina...” Tunda akasita. Mambo mengi
yakaanza kupita akilini. Akatulia kidogo. “Naomba
nisamehe Net. Nia ilikuwa nzuri, sikutaka kuwachonganisha na Gab. Lakini
nakuahidi siku nyingine sitakuficha kitu. Nisamehe.” “Kama utakubali
nikuoe.” Net akazidi kumchanganya Tunda. Usingizi, kutokulala kwa muda mrefu
kwa wasiwasi na uchovu kwa ujumla, vilimfanya ashindwe kuelewa kwa haraka.
“Nini!?” Alijaribu kukausha machozi kwenye macho
yake ili amtizame Net vizuri, lakini machozi yalikuwa yakichirizika kama maji.
“Nataka uwe mke wangu Tunda.” Ilibidi tu ainame. Alishindwa kujibu, wala
kuelewa kwa sekunde kadhaa. Net aliacha kupokea simu zake na kujibu jumbe zake,
leo anatokea kanisani, anasema nini! Alishindwa kuinuka wala kuongea.
“Kiss her already!” Sauti ya kizungu ya kike, ilisikika
ikipaza sauti ikimtaka Net ambusu Tunda. Baadhi ya watu wakaanza kucheka.
“Nathaniel Cote!” Ilirudia tena kumwita kwa msisitizo. “We are at the Church,
Nana!” Net akababaika akijua maadili ya kiafrica na hapo walipo, kanisani!
Anaanzia wapi kumbusu Tunda! “So what?” Bibi yake akamshangaa kinachomshinda ni
nini kutoa busu kwa mpenzi wake. “Nooo!”
Net akakataa kwa mshangao.
“I thought we raise you well!” Aliendelea kumchokoza Net.
“Yes you did.” “Then man up and kiss her.” “No Nana! We are here.., you know?”
Net akajaribu kumuonyesha mazingira na watu waliokuwepo pale, wanao wazunguka.
Kama kumkumbusha ni Africa!
“See what you have done to him? He can not even kiss his own
fiancé.” Yule bibi alimgeukia Mama yake Net nakumlaumu. Lakini Ritha alibaki kimya, akacheka kidogo
tu kwa kujibaragusa. Maya yeye alikuwa akicheka sana mpaka machozi pamoja na
watu wengine waliokuwa wakiwaelewa.
“I told you Nana! Look at him. She can not even kiss Tunda!”
Maya akaongeza. Net na Maya walikuwa wakimwita bibi yao Nana na babu yao papa.
“I bet your papa is very embarrassed by you, right now! Can’t imagine your
dady!” Yule bibi aliendelea kumchochea Net akimwambia anawaaibisha babu yake na
baba yake huko walipo.
“What am I suppose to do? She can not even look at me.” Net
akasikika akijitetea kwa bibi yake kuwa hajui chakufanya kwani hata Tunda
mwenyewe hamwangalii. “Mam up! Lift her up, hold her in your arms and then kiss
her. That’s all!” Bibi yake akajibu kwa msisitizo akimwelekeza kitu chakufanya
mjukuu wake kama asiyejua.
“You mean now?” Net
akauliza akionyesha wasiwasi huku akimwangalia mama yake. “Right NOW Son. Do
it.” Akajibu yule bibi kwa msisitizo kwamba huo ndio wakati wa kumnyanyua
Tunda, kumuweka mikononi vizuri na kumbusu. Kisha yeye na Maya wakaanza
kushabikia kwa kuimba, “Do it! Do it! Do it! Do it!” Waliendelea kuimba kama
kumtia morali Net, Ritha kimya.
Net alibadilika rangi akawa mwekundu mpaka jasho, kwa hofu. Maya
na bibi yake hawakunyamaza mpaka Net aliposimama na kumnyanyua Tunda.
Akamkumbatia huku akimsugua mgongoni. “I said kiss her not petting her back!
What’s wrong with you!?” Bibi yake alipaza tena sauti kwa mshangao kuwa
alimwambia amnyanyue na kumbusu, sio kuishia kumbembeleza tu! Bado watu walikuwa
wakiwatizama na walioelewa kucheka.
Net akajikaza. Akamvuta Tunda nyuma kidogo, akashika shingo
yake kwa mikono yake yote miwili huku akimtizama, kisha akaanza kumbusu. Yule
bibi na Maya wakaanza kushangilia kishabiki, ndipo watu wakaanza kupiga
vigelegele. “You are a man now.” Bibi yake akamsifia kwa sauti ya juu kuwa
ameshakuwa mwanaume.
Net alipiga tena magoti na kuuliza swali huku ameshikilia
pete yake. “Will you mary me, Tunda!” Tunda aliendelea kufuta machozi huku
akitingisha kichwa kukubali. Mambo aliyokuwa akiyaona kwenye luninga, aliona
yanamtokea siku ile. Net alimvuta mkono na kumvalisha ile pete. Tunda
hakunyamaza. Busu hilo alilokuwa amelitunza muda wote, ameishia kulipata
Nathaniel Cote, kijana wakichotara, aliyebeba damu nyingi ya weupe.
Net akamshika mkono wakataka kutoka nje. “No no no nooo. Hold
up son!” Net akasimamishwa na bibi yake. “What!?” Net akamuuliza huku
akimtizama bibi yake kwa mshangao. “She is not your wife yet!” Akamuonya mjukuu
wake asije nogewa, si mkewe. “I know Nana! I just want her to calm down and
then we will be right back.” Net akajitetea kuwa anakwenda tu kumbembeleza ili
atulie, kisha warudi. Maana ni kweli Tunda alishindwa kunyamaza. Kitu kilimkaba
kooni, akawa haelewi tena. “You better!” Bibi yake akaweka msisitizo. Wote
wakacheka, Net akatoka na Tunda nje.
“Nilijua umeniacha Net. Nilijua hunitaki tena.
Kwa nini ulinifanyia hivyo?” “Samahani sana Tunda.
Sikukusudia kukutesa kwa muda mrefu mpenzi wangu. Nilitaka kukufanyia surprise
kwa jinsi ulivyonifurahisha.” “Nimekufurahisha na
nini tena!?” “Nyamaza kwanza.” “Hapa nina
usingizi na njaa, Net. Sijalala vizuri tangia siku ile ya mwisho
tulipowasiliana. Nilichanganyikiwa, nilijua umeniacha!” “Naanzia wapi
Tunda!? Siku ile mnawasiliana na Gab, ule ulikuwa mtego tu.” Tunda akashtuka
sana.
“Sitaki kukutia hofu, lakini nakutahadharisha tu.
Unafuatiliwa sana. Wapo watu hawaamini kama kweli unanipenda kwa dhati,
wanafikiri upo na hila.” “Kina nani!?” “Hilo sio la msingi ila ujue
wanakufuatilia. Kuanzia siku ya kwanza Gabriel anakutumia ujumbe, halafu
ukashindwa kuniambia, walianza kunicheka sana. Siku ulipoenda kukutana naye
alikuwa amevaa spika, unasikika live, na kuna mtu walimuweka kuwapiga picha. Niliumia sana nilipopigiwa
simu kuambiwa umeshafika eneo la kukutania na Gab. Mwili wote ulikuwa
ukitetemeka, nikiwaza itakuwaje kama utamkubalia Gab. Nilikuwa nashindwa hata
kupumua. Nilitamani kuja pale nishuhudie, lakini nikajikaza.”
“Ikabidi kuja kuwapigia tena simu kuuliza mambo yalikwendaje,
ndipo nikaambiwa kwa sasa umemkataa. Ndipo ikabidi kufuatilia mazungumzo yote
waliyokuwa wamekurikodi. Nilifurahi sana, na kumshukuru Mungu wangu.” Hofu ilimwingia Tunda mwili mzima ukaanza kutetemeka.
“Sasa
baada ya hapo, nikawa kama nimewasuta, lakini bado hawaamini. Wanahisi kwa kuwa
ni Gabriel. Umemkataa kwa kuwa alikuumiza na umejua kuwa tunafahamiana.
Wakasema kama ingekuwa mwanaume mwingine mwenye pesa ungemkubali tu. Lakini
kwangu nilikuwa nafuraha yakupitiliza. Nikawa nina kazi yakurudia rudia yale
mazungumzo kati yako na Gab.” Tunda alibaki anashangaa nakushindwa hata
kujisogeza akifikiria kwa upya ni nini alizungumza na Gab siku ile.
“Nilifurahi
nakushindwa hata kusubiri tena. Nikampigia simu Nana kumwambia kuwa nataka
kuoa. Ndipo aliposema nilazima awepo kwenye kila hatua mpaka ndoa. Ikabidi
nikate tiketi ili nikamfuate, aje ashuhudie ninavyokuvalisha pete ya uchumba.
Sikujua kama naweza kuchukua muda mrefu kiasi hiki Tunda. Nilijua naenda Canada
mara moja kumfuata Maya na bibi, kisha nirudi nao baada ya siku mbili, kisha
nikuvishe pete ya uchumba wao wakiwepo. Lakini kufika kule kuna mambo
yakajitokeza, ikabidi nimsubirie Nana kidogo. Tumeingia jana. Nimepata ule
ujumbe wako wa jana, nikajua hali yako ni mbaya, ikabidi kumuomba mama Penny
akupigie ili akutulize.” Tunda akashtuka
kidogo.
“Mama Penny!?” Tunda akauliza kwa mshangao. Net
akacheka kidogo. “Ndiyo, mama Penny. Anafahamu kila kitu. Na hata nilipokuwa
kule niliongea na Mama Penny nikamuomba aniandalie mazingira yote, ili nikija
iwe ni kukuvalisha hii pete tu. Lakini aliniambia nifanye haraka una hali
mbaya. Pole sana mpenzi wangu. Sikukusudia kukutesa.” Bado Tunda alikuwa kwenye
mshtuko na hofu.
“Twende
ukalale sasa hivi, ili baadaye uweze kuhudhuria tafrija. Mama Penny amenisaidia
kukuandalia tafrija nyumbani kwa mama ambako bibi na Maya ndiko walikoshukia
hapo. Wale wageni wote niliokuja nao hapa kanisani kwenu ni wakutoka kanisani kwetu,
na wengine nimarafiki zangu wa hapa na wachache tumekuja nao kutoka Canada.
Wapo na marafiki niliokua nao tokea watoto. Wapo wawili, sijui kama umewaona?”
“Mimi nimekuona wewe tu pale ndani.” Net akacheka kidogo.
“Basi na wao wamechangia kuchelewa
kwangu. Nilipowaambia naoa, wakataka tuongozane nao waje huku nchini.
Wanaondoka kesho asubuhi kurudi kuwahi majukumu yao. Jana nilipofika tu,
nilienda kuongea na baba yako. Ilibidi kuomba kuwa ni dharula ili waniruhusu
kumuona maana ilikuwa sio siku ya kuwatembelea. Nikaruhusiwa. Amefurahi sana.
Amesema kesho tumpelekee picha.” Tunda alihisi yupo usingizini.
“Ungeniua Net!” “Sitarudia tena kufanya hivyo.
Kwanza nilitaka kukupa onyo. Usiwahi kunificha jambo, na pia nilitaka
kukufurahisha.” “Samahani Net. Naahidi sitarudia
tena. Umenipa somo ambalo nimejifunza kwa mateso sana. Nilijua umeniacha!” Machozi
yakaanza kumtoka tena Tunda.
“Lakini pia imekusaidia kufikiria
Tunda. Angalau umejua kama unataka kuwa mke wangu au la. Unajua nilikuja
kujilaumu? Ni kama nilikuja kukuvamia tu! Tokea mwanzo kila kitu kikawa
kinaenda kwa vile nilivyokuwa nikitaka mimi. Angalau umepata muda mtulivu
wakuwaza.” “Sikuhitaji muda wa kujua kama nakupenda
au la Net. Nakupenda.” “Sasa hivi nimehakikisha.” Net alimvuta tena na
kuanza kumbusu midomoni. Hiyo furaha aliyojisikia Tunda, hakuna jinsi angeweza
kueleza. Alikuwa akikwepesha hiyo midomo akitaka kuja kupata busu la uhakika.
Na kweli Mungu akamsaidia na kupata busu la Net. Alikuwa akifurahia sana.
Japokuwa Tunda alishakuwa na wanaume
wengi hakuwahi kupata busu kama lile. Net alimshika vizuri na kwa heshima
wakati akimbusu kama anashika mwili wa thamani sana kumbe ni mwili wa Tunda
uliopitiwa na wanaume kibao, na yeye akilijua hilo. Tunda alilihisi lile busu
katika kila kiungo cha mwili wake. Machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka si
huzuni tena, asiamini.
“Asante sana Net. Asante.”
“Umeipenda pete?” Tunda akanyoosha mkono wake na kuanza kuiangalia ile pete.
“Nzuri sana. Nimeipenda. Asante.” “Hiyo ni pete ya bibi. Alivalishwa na babu,
alinitunzia kwa muda mrefu akasema nikipata mwanamke ninayempenda, nimvalishe.”
Tunda akacheka.
“Anaonekana mcheshi!” “Anavituko
huyo! Akiamua kukufungulia moyo, wala huhitaji siku nyingi zakumzoea. Ila
anatupenda sana mimi na Maya.” “Nikwambie kitu Net?” Net alikuwa bado
amemkumbatia Tunda, hapohapo nje ya kanisa huku akimwangalia kwa upendo kama aliyeokota
lulu kumbe ni Tunda kituko kwa wengine.
“Mmhh!” “Umenipa heshima ambayo
sikuwahi kufikiria hata siku moja kama naweza kuja kupata. Sikujua hata kama
nastahili! Hapa nahisi nipo ndotoni. Asante sana.” “Wewe ni wathamani sana
Tunda. Sio kwangu tu, hata machoni pa Mungu, ndivyo anavyokuona. Sijafika hata
nusu ya punje ya mchele, vile Mungu anavyokupenda na kukuheshimu.” Kabla
hajambusu tena, “Mnaitwa na Mchungaji mkaombewe.” Mama Penny alitoka na
kuwakuta bado wamekumbatiana wakitaka kupeana mabusu tena.
“Asante sana mama Penny, kwa kila
kitu. Naamini mpaka sasa tupo sawa.” “Karibu Net. Kila kitu kipo sawa kabisa.”
“Tunashukuru sana, lakini naomba baada ya maombi tu, nimrudishe Tunda nyumbani
akapumzike kidogo, halafu tutakuja kwenye tafrija baadaye akishatulia.”
“Mnaacha wageni wenu hapa!?” “Wewe si upo?” Net alimshangaza mama Penny.
“Leo ni siku yangu na Tunda.
Nataka aifurahie. Kwa jinsi alivyochoka hivi, sidhani kama atafurahia chochote
kwenye tafrija.” “Utamuaga mama yako?” Akauliza mama Penny. “Nitaongea naye.
Kwa kuwa tafrija itakuwa saa moja usiku, nyinyi mkitoka hapa mnaweza kwenda
nyumbani kwa mama moja kwa moja, au mkaja hiyo jioni. Sisi tutakuja huko
jioni.” “Sawa.” Akakubali mama Penny.
Tunda akamsogelea Mama Penny.
“Kumbe ulikuwa unajua kila kitu, halafu ukaniacha mwenzako nalia mchana na
usiku!” Mama Penny akaanza kucheka. “Net aliniomba sana nisikwambie, nivumilie.
Mimi mwenyewe nilikuwa nikiumia, lakini nilijua mwisho wa yote utacheka tu.
Haya hebu jione jinsi ulivyopendeza na hiyo alumasi hapo kidoleni, mdogo wangu!
Mvumilivu hula mbivu.” “Lakini mmenitesa sana!” Wakacheka huku wakimuomba
msamaha, mwishowe wakaingia ndani.
Net na Tunda walipiga magoti mbele
ya kanisa, wakaombewa. Net alitoa neno la shukurani, nakurudia historia yake fupi
yeye na Tunda, kisha akaomba aondoke kabla ya ibada haijaisha. “She is not your
wife.” Bibi yake akarudia kwa sauti. “I know Nana.” “Just saying!” Kila mtu alicheka, Net akaenda kumbusu mama
yake, na bibi yake akataka kutoka. “Heyyy! What about me!?” Maya alishangaa
kuona kaka yake anampita. “Tunda amechoka.” “It doesn’t take even a minute to
give sugar to your baby sister!” “Fine!” Net akarudi akabusu mdogo wake.
“Happy?” Net akamuuliza mdogo wake. “Oooh yeah!” Net akacheka na kumrudia Tunda
aliyekuwa amemuacha amesimama, akamshika mkono. “She is not your wife.”
Alisikia bibi yake akirudia tena kumkumbusha kuwa bado si mkewe, wasije
wakapitiliza huko waendako. “I said, I know.” Net akamjubu bibi yake kuwa
analijua hilo, huku akiondoka na Tunda akiwa amemshika mkono.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika nyumbani kwa Tunda, akiwa anasinzia. Aliingia
bafuni, akaoga tena hasa kusafisha uso uliokuwa umechanganyikana machozi na
vipodozi. Akavaa nguo za kulalia kabisa,
akatoka pale sebuleni alipokuwa amemuacha Net. “Mbona nguo za kulalia tena!?
Tutawaweka sana watu kule kwenye tafrija Tunda! Nilitaka upumzike kidogo tu.”
“Utaniamsha muda unaotaka tuondoke. Nimechoka sana Net, nataka nilale vizuri.”
“Pole.” Net akamsogelea, akambusu tena bila kumkumbatia ila kumshika tu
kichwani ili kuweza kumbusu. Akamuachia.
“Twende nikusindikize.” Akamshika mkono na kuingia naye
chumbani kwake, Tunda akiwa na wasiwasi. Alimuogopa sana Net. “Njoo hapa.” Net akajilaza kitandani, kisha
akavuta mto akaweka chini ya kichwa
chake. “Njoo ulale hapa.” Tunda alibaki amesimama, akakunja uso akionyesha
wasiwasi na hofu. “Njoo usiogope, Tunda.” “Kifuani kwako!?” Akauliza kwa hofu
kidogo. “Hutaki?” “Sio..” Tunda akasita. “Usiogope, njoo. Nataka ulale vizuri.
Ni leo tu, hutazoea.” Tunda akacheka. “Nitagoma kuamka mimi!” Tunda akamfanya
Net acheke.
“Ndio nabembelezea msamaha, kwa kukutesa kwa siku zote hizo.”
Tunda akatabasamu, akapanda kitandani na kujivuta mpaka kifuani kwa Net. “I
miss you so much Net.” “Miss you too, babe. Nitaongea na Mchungaji wako,
atusaidie tufunge harusi mapema. Nataka tuanze kuishi pamoja.” Tunda akapitisha
mikono yake kifuani kwa Net, akamkumbatia kwa nguvu na kupitiwa na usingizi
bila ya kujibu kitu. Net aliendelea kumpapasa taratibu maeneo ya mgongoni na
begani, huku akimbusu kichwani mpaka na yeye akapotelea usingizini.
Tafrija ya kuvalishwa pete ya uchumba Tunda.
Ilikuwa
ni kwa mara ya pili Tunda kufika nyumbani kwa mama Cote. Mara ya kwanza
alipopelekwa kutubu akiwa mwenye dhambi haswa. Baada ya kukiri alishajihusisha
kimapenzi na mchumba wa mama Cote, uadui ukaanza. Sasa anarudi kwenye jumba
hilo kama mchumba wa Net. Ilikuwa nyumba yenye thamani za kisasa, tena za aina
yake. Nyumba nzuri, iliyojengwa kwa namna yake. Magari yaliyokuwepo hapo nje
sehemu yakuegeshea tu magari, Tunda akajua ni watu wenye uwezo watupu
watakaokuwepo huko ndani.
“Umependeza
sana Tunda.” Tunda akatulia kidogo. “Nini?” “Itakuaje nikifika huko ndani
nikakutana na..” Tunda akanyamaza. Net akamuona akifuta machozi huku akiangalia
nje ya dirisha. “Naomba uniangalie Tunda.” Tunda akamgeukia. “Naona kama nakuingiza aibu tu Net!” “Naomba
usipeleke mawazo yako huko kabisa. Kila mmoja utakayemkuta humo ndani
anahistoria yake. Sema ya kwako umeigeuza imekuwa yamsaada.” Net aliendelea
kumtuliza akisikika ametulia kabisa, bila hata wazo la pili la wasiwasi.
“Nilifurahi
sana jinsi ulivyoweza kuongea na Gab. Umethibitishia kila mtu umeshakomaa
Kiroho. Tumia ujasiri huo huo kwa kila atakayekusogelea. Na hakikisha
unajitambua acha hofu kabisa. Nipo na wewe nikikujua vizuri, na nimeridhika na
wewe. Kwa hiyo tembea mbele ya watu ukiwa huna hofu. Umenisikia?” Tunda
akatingisha kichwa kukubali.
“Haya
naomba tabasamu. Maana hii yote nimeandaa kwa ajili yako. Nataka ufurahie.
Sawa?” Tunda akacheka taratibu. Walikuwa wameegesha gari nje ya hiyo nyumba ya
mama yake, sehemu ya kuegesha magari. Net akamvuta karibu na kumbusu tena na
tena bila kumuachia kama mwenye kiu naye mpaka simu yake ilipoanza kuita. “Mama
huyo!” Net akasema wakati anaiangalia simu yake akaamua kupokea. Alisikiliza
kidogo mama Cote akiongea, kisha Net akajibu. “Tupo
hapa nje, tunaingia ndani sasa hivi.” Akakata na kumbusu tena Tunda.
“Twende, Nana ameanza kusinzia.” Wote wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bibi yake Net alimuomba
Net, amvalishe tena ile pete Tunda huku
akichukuliwa vizuri video kama kumbukumbu ya familia, akidai kuwa siku hiyo
ndipo anapomkabidhi Tunda cheo cha Bi. Cote rasmi kama mrithi wake. Kwanza alivaa
pete aliyochumbiwa nayo yeye na pili anaolewa na mjukuu wake mwenye jina kama
la mume wake. Alisema anakikundi cha marafiki zake kanisani huko nchini Canada,
anafanya nao bible study, walimuomba arikodi kila kitu ili akifika awaonyeshe.
Zile zilikuwa habari zilizomtibua mama yake Net, na kumnyima raha kwenye ile
shuguli nzima.
Mama
Penny alikuwa ameandaa sehemu si ya nje, lakini si sebuleni. Kulikuwa na eneo
la ndani lakini kama baraza kubwa tu lililokuwa limezungushiwa kuta nzuri mpaka
juu ambako ndiko vyumbani. Chini kwenye hilo eneo la katikati kulikuwa kama na
bustani tena ambayo ilishamtoa macho Tunda tangia mara ya kwanza anaingia
kwenye hiyo nyumba.
Haikuwa
bustani kubwa lakini duara kubwa iliyozungushiwa majani mazuri, yaliyokatwa
chini yakawa kama mkeka. Vyungu vya thamani vyenye maua mazuri yaliyokuwa
yamezunguka kwenye hayo maua na pembeni ya kona kwenye hilo baraza zima na
nguzo, mama Penny alitendea haki. Kuzunguka hilo eneo zima kulikuwa na fremu za
picha nzuri sana na aina mbali mbali ya maua. Ndipo mama Penny akapaandaa
vizuri na kupendeza.
Yote
hiyo alifanya Net kwa ajili ya Tunda. Sasa mpambaji akawa ni mama Penny,
nyumbani kwa Ritha, mama yake Net, asiyempenda Tunda. Leo Tunda anavalishwa
pete nyumbani kwake akiwa ameonya asikanyage pale tena. Mbaya zaidi,
anavalishwa pete ya thamani sana, urithi ambao yule bibi aliuwekea maana kubwa
mbele ya watu! Mambo hayo yote wanayafanya nyumbani kwake! Hakuna jinsi mtu
angeangalia moyo wa huyo mama ulivyochafuka, akaweza kueleza wengine.
Alikuwepo
kanisani na pale kwenye ile tafrija japo ni nyumbani kwake, lakini sababu ya
uwepo wa huyo bibi milionea ambaye hata Tunda hakujua uzito wa huyo bibi kuwepo
pale. Alisikia akipiga kelele kanisani, akitaniana na Maya na Net. Asijue uwepo
wa huyo bibi hapo nchini hata usalama wa taifa nchini Tanzania na Canada,
unajua kama yule bibi yupo nchini Tanzania.
Waalikwa
ambao Net alimwambia wengine ni wakutoka kanisani kwao na marafiki, wengi pale
ni askari kanzu na usalama wa taifa walikuwa wamejaa hapo, kuhakikisha huyo
bibi, raia muhimu sana wa huko nchini Canada yupo salama, na hakuna
linalotokea, mpaka anarudi nchini kwake salama.
Na hao
wazungu wachache aliowaona Tunda pale, hawakuwa ni rafiki wa karibu tu wa Net ,
ni askari waliopitia mafunzo makubwa sana ya kiaskari ya kimataifa, walifika
nchini na huyo bibi kwa ajili ya usalama wake tu. Kwanza alitua nchini na ndege
yake ambayo ndio ilibidi kufanyiwa taratibu ya eneo la kutua hapo nchini
Tanzania. Kimya kimya bila gazeti lolote kuripoti ujio wa bibi huyo nchini
Tanzania.
Mama
Cote, au Ritha, alijua ni mapesa ya kiasi gani yamemwaga kwa huyo bibi
anayefanya mchezo na kuonekana wa kawaida sana kuwepo hapo. Ritha alipigia
mahesabu ya huyo bibi kuwepo tu hapo! Tena kwa ajili ya Tunda, ambaye
amempokonya ndoa na mapenzi ya mtoto wake! Anamwita Malaya. Anajua wazi,
amemchagua Net badala ya Gab kwa kuwa anamfahamu Net, anataka kunufaika naye.
Ritha akajiambia hiyo pesa angefanyia kitu kikubwa sana badala yakupoteza kwa
malaya, Tunda.
Kila
neno alilotamka bibi Cote, halikuwa bure. Hakuwa mropokoji. Ni mwanamke
aliyekuwa akiongea na maraisi na watu wakubwa sana ulimwenguni. Pesa yake na
kile anachokifanya nchini Canada, kama mwanaharakati wa mambo ya wanawake si
nchini kwao tu, bali ulimwenguni, kilimketisha na wakuu wa ulimwengu huu na
kumwingiza sehemu kubwa mbalimbali hapa ulimwenguni. Alishahutubia mara kadhaa
kwenye vikao vikubwa vya UNO. Kila aliloongea, watu walilinukuu na kulisikiliza
kwa makini sana hata kugeuza ni habari ya kuuza gazeti lolote lile haswa nchini
kwao anakofahamika na familia hiyo kufuatiliwa kwa karibu sana.
Ritha
alijua na kuzidi kuumia kwa kila neno analozungumza huyo bibi Cote usiku huo
kwenye tafrija hiyo. Alijua si mropokaji. Kwa hiyo hata usiku huo hakuna
aliloropoka hata moja juu ya Tunda na Net. Inamaana ni maneno au hotuba maalumu
aliyokuwa ameiandaa kwa muda mrefu kuja kuzungumza kwenye tafrija ya Net
akichumbia. Na lazima hiyo hotuba au hayo maneno anayoongea hapo yamesomwa na
kurudiwa na msaidizi wake wakaafikiana na ndipo anatamka mbele ya huo umati
kirafiki tu kama akizungumza na familia yake, lakini wazi anajua ni habari
nzito nchini kwao siku inayofuata, japo amezungumzia nchini Tanzania. Na
akitamka yeye, ndio mwisho.
Ni
ukweli ambao hakuna ambaye angesema, Tunda angeamini. Kwa hakika Tunda hakuwa
akijua lolote lile juu ya Net mwenyewe wala huyo bibi. Net alikuwa makini sana
anapozungumza na Tunda. Na alifanya makusudi akijua umuhimu wa mwanamke
atakayemuoa. Sio tu kuitwa mke wa Nathaniel Cote, alijua atabeba majukumu
mazito sana. Tunda asijue.
Net
hakuwahi kujifungua kwa Tunda zaidi ya idadi ya waliozaliwa nyumbani kwao. Kile
anachofanya pale nchini. Kazi za mama yake. Hakuwahi hata kuropoka utajiri
mkubwa unaomsubiri nchini Canada. Au anavyosubiriwa kwa hamu huyo mke wa Net,
huko nchini Canada. Hata kujulikana jina tu, ingekuwa habari ya kuuza magazeti.
Picha yake ndio kabisa. Tunda hana hili wala lile. Anajionea ni bibi amekuja
kwenye shuguli ya mjukuu akichumbia. Basi. Kumbe ameingia kwenye historia kubwa
sana.
Vyombo
vya habari vya nchini kwao na watu wengi walio ijua hiyo familia, na
kuifuatilia walitaka angalau kupata fununu kujua hata kwa fununu tu,
atakayekuwa mke wa Net. Anaposema video nzuri ichukuliwe Net anapochumbia kwa
ajili ya marafiki zake wa kanisani, sio kwa sura hiyo aliyoelewa Tunda hata
kidogo. Ni kumbukumbu ya vizazi hadi vizazi na ni habari nzito sana ambayo mtu
anaweza hata kuuza kwa pesa nzuri tu za kicanada. Nathaniele Cote amechumbia
siku hiyo! Ilikuwa ni habari kubwa yakuuza magazeti nchini kwao.
Lakini
Tunda yeye kila kitu aliona kawaida tu, na Net alikusudia iwe hivyo. Hakutaka
askari yeyote avae sare na wala pale pasionekane risasi yeyote ile hata ya
kiunoni mwao. Kwa hiyo kila mgeni akaonekana wa kawaida. Nadhifu na wengi
wamevaa suti. Kumbe suti hizo zimeficha mengi. Tunda na kina mama Penny pamoja
na wageni wengine wakawa hawaelewi kinachoendelea. Kumbe hiyo nyumba ilikuwa
chini ya ulinzi mkubwa sana tokea huyo bibi anafika pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Yakawekwa
mazingira mazuri pale. Katikati ya kula na kunywa, watu wakicheka, Net akapiga
tena goti akimuuliza Tunda aliyekuwa amesimama, kama atamkubali amuoe, “Will you mary me?”. Tunda akakubali, kwa kusema, “Yes.” Net akamvalisha tena ile pete akiwa amepiga
magoti vilevile. Kisha akasimama, akamkumbatia vizuri na kumbusu Tunda.
Haikuwa
mara ya kwanza kwa Tunda kupata busu au kukumbatiwa na mwanaume. Baba Tom
alishambusu akiwa bado mdogo na mwili huo ulishashikwa na wengi tu. Kimapenzi
na kupigwa kama mwizi. Lakini busu la Net na jinsi alivyomgusa huo mwili!
Ilikuwa tofauti kabisa. Hakuna aliyeona asitamani. Wenye wivu ndio walizidi
kuumia.
Net
alijua wapi amshike kabla ya kumbusu, na hata jinsi alivyomwangalia baada ya
kumshika kabla ya kumbusu, akili na mawazo ya Tunda alijua wazi anapendwa na
kuthaminiwa sana. Ile hofu na aibu mbele ya wateja wake ilimuisha kwani ni
kweli walikuwepo wanaume wakutosha tu ambao walikuwa wateja wake, lakini kwa
jinsi Net alivyo mtizama na kumshika, hakuna jinsi Tunda ungemkumbusha kuwa
alishakuwa changu, ukamuumiza.
Mama Cote na Tunda tena.
Wakati watu
wakiwa wanaongea na kucheka, huku wakila na kunywa, Mama Penny na mumewe
wakaamua kuaga. Muda ulishakwenda. Watoto wanatakiwa shuleni kesho yake.
Wakamuaga Net na Tunda. Wao wakaondoka. Kwa kuwa walikuwa wamekaa meza moja na
Tunda, walipoondoka, Net naye akasimama, akamwambia Tunda atarudi baada ya muda
mfupi. Tunda naye akaamua kuingia ndani kutafuta choo kilipo ili angalau
ajitengeneze vizuri na kujirudishia vipodozi na nywele. Kujitengeneza.
Wakati
anatoka chooni, mama Cote au Ritha alikuwa akimsubiria mlangoni akiwa amejawa
wivu baada ya kuona jinsi mkwewe alivyomthamini Tunda. Na ni kama alitangaza
kumpa Tunda cheo kikubwa sana ambacho hakuwahi kupata mtu sahihi wakumpa ila
Tunda. Lakini alitangaza kwa kujihami huku akisema, atatangaza rasmi au
atamkabidhi rasmi cheo hicho baada ya kupata muda wakutosha wamazungumzo na
Tunda.
Tunda
alicheka tu kwa kuwa yule bibi aliongea kama kitu cha utani, kumbe ni jambo
zito lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu sana. Wengi walitamani kujua cheo
hicho angalau yule bibi anamfikiria kuja kumkabidhi nani! Nani angekuwa mrithi
wake! Nani anakalia kiti hicho! Angalau kwa fununu tu. Leo kwa mara ya kwanza,
anatangaza, tena nchini Tanzania! Hata Net na Maya walibaki mdomo wazi. Hawakuamini.
Lakini
si Tunda ambaye hakujua chochote. Alimuona jinsi Maya na wale wageni wote
kutoka Canada wakishtuka mpaka kusimama na kushangilia sana, na Net kubadilika
mpaka rangi ya sura akiwa ametoa macho asiamini kile bibi yake anafanya kwa
Tunda. Tunda mwenyewe hata asielewe ni nini bibi huyo anaongea. Akajiambia ni
mambo tu ya kizungu.
Tunda
akawa ndio ametamkwa kwa mara ya kwanza na bibi huyo kuwa ndiye atakalia kitu
hicho baada yake. Ritha alijua ni habari itakayoenea sana nchini Canada na
picha za Tunda kuanza kuonekana huko na habari zake kufika kwenye nchi mbali
mbali za wawakilishi wa umoja wa bibi huyo. Tunda hana habari.
Picha
nyingi zilipigwa asijue umuhimu wake. Aliona mpaka rafiki wa Net wakimuomba
akae vizuri wampige picha akiwa peke yake tena kwa kupokezana. Akiwa anacheka
tu, akakubali kufuata maelekezo. Marafiki hao wakampiga picha akiwa peke yake,
kisha wakamuomba mmoja mmoja wapige naye picha. Kwa zamu. Nyingine wakapiga
wakiwa na Net. Ikawa shamra shamra imeongezeka gafla baada ya tangazo la bibi
huyo, Tunda hana habari.
‘Tunda!’ Ritha aliumia sana. Bibi
Cote alitamka kumkabidhi Tunda kiti ambacho inamaana yeye hakustahili! Tena
anatamka hayo mbele za watu bila hata kuzungumza na wao kwanza kama familia,
wakajua kama amekusudia kuwa ni Tunda! Hata wao watu wa karibu ndio wanasikia
pale kama watu tu wa nje! Yule bibi hakumshirikisha yeyote. Yaani pale ndio
anatoa hiyo habari kwa mara ya kwanza.
Alihisi
ni kama yule mama mkwe wake ametangaza kumtoa kwenye familia kwa wazi tena kwa
kumdhalilisha vibaya sana. Ni kama anasema Tunda ni bora kuliko yeye! Alichukia
sana kuona anadhalilishwa pale mbele za watu tena nyumbani kwake! Ni Tunda,
binti anayejihesabu amempita kwa kila kitu! Leo anapewa heshima yote aliyokuwa
amebeba yeye, na kudhani anastahili yeye Ritha! Hasira zilizidi kumpanda na
kumchukia Tunda zaidi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba
tusogee hapa pembeni tuzungumze.” Tunda akamfuata nyuma. Akashangaa anamtoa
kabisa pale mpaka sehemu ya nje karibu na mlango wa kutokea. Akaangalia kulia
na kushoto, wakajikuta wawili tu. Kulikuwa na askari kanzu wawili nje ya huo
mlango walionekana kwa kupitia kioo cha mlango. Yule mama akaonekana kuridhika
na hiyo faragha.
Akamgeukia
Tunda. “Upo hapa leo sababu ya huyu bibi, tu.” Mama Cote akaanza huku amemkazia
macho. “Umenielewa Tunda? Unaweza kumdanganya kila mtu hapa, lakini sio mimi.
Mimi sio mtoto mdogo au mjinga kama hao wanaume zako uliokuwa ukiwavulia nguo
na kuwaloga. Najua janja yako. Upo hapa na kumkataa Gabriel kwa kuwa umejua Net
anapesa kuliko Gab. Anamapesa ya urithi wa babu yake na bibi yake akifa ndio
kabisa. Yeye ndio anakuwa mrithi au mtawala wa mali zote za Cote.” Tunda
akakunja uso. Hayo yote hakuwa hata akiyajua. Na wala hajui kama hiyo familia
ya Cote ina mali za hivyo!
“Sijui
unamlogea wapi mtoto wangu! Sijui kama na yeye unamfanyia sadaka za makaburini
au la! Lakini mimi na wewe tunajua wazi, kwa akili za Net hawezi kukupenda mtu
kama wewe hata kidogo. Nina uhakika kuna ulichofanya kwa Net. Wewe ni mzoefu wa
ushirikina, hushindwi kuzika akili zake. Na ninajua wazi, yale majini
yanayosadikika kukutoka, hayajatoka. Bado yanaharibu akili za wanaume, ndio
maana na Net amechanganyikiwa.” Ritha akataka kuendelea.
0 Comments:
Post a Comment