N |
et akacheka kwa kumsikitikia
mama yake. “Usidharau hoja zangu Net! Sio watu wote ni waadilifu kama wewe.
Watu wanaishi kwa ujanja ujanja sana hapa mjini!” “Binafsi nakuelewa kabisa
mama yangu. Nakuelewa. Hapo ulipo sasa hivi, nilishakuwepo. Nikaamua kumchukia
kabisa Tunda. Nikaamua kurudi Canada, nikataka kumuoa Chloe, lakini
nilishindwa. Sijui Mungu ameniunganishaje na Tunda, mama! Nampenda Tunda. Na
ninaona yeye ndiye atakamilisha hata maisha yangu yakumtumikia Mungu.”
“Unajuaje kama ni Mungu ndiye anayekuunganisha na Tunda?” Mama Cote akauliza na
kumfanya Net akunje uso.
“Sasa wewe unafikiri nini!?” “Watu wanatumia nguvu
za giza Net.” Net akasimama. “Unajua nini mama, sina jinsi ya kukubadilisha
hapo ulipo na kile unachokiamini. Naamini Mungu kwa wakati wake, atakusaidia na
wewe. Maana hata mimi haikuwa kazi ya siku moja.” “Nisikilize Net. Usifanye
haraka kuondoka. Uchawi upo, na unafanya kazi.” “Kuliko nguvu za Mungu!?” Net
akamuuliza mama yake kwa mshangao, nakubaki akimtizama.
“Uniambie leo, kama tulichokuwa tukikiamini hakina
uwezo wa kutulinda na hila na mitego ya shetani! Kwamba shetani amefanikiwa
sana, na ana nguvu zidi ya maombi, na uwepo wa Mungu!” “Bibilia imeruhusu
kujaribu kila roho. Wewe endelea, na mimi sitatulia mpaka nijue ni roho gani
inafanya kazi ndani ya yule binti.”
“Kuwa tu
mwangalifu mama yangu. Mungu hajaribiwi. Usije ukafika umbali ambao ukashindwa
kurudi kwa mapenzi yako ya umama kwangu. Yapo mambo mengine ya Mungu, huwa
hayachunguziki kwa akili za kibinadamu. Huwa hayana majibu. Humpa amtakaye.
Muone pale Mungu alipomuweka Tunda. Ulimfukuza kikatili sana. Lakini ona Mungu
jinsi alivyomfanikisha hata kifedha.”
“Wapo wapambaji wangapi hapa mjini? Lakini
ukiangalia kazi ya Tunda, jinsi alivyojipanga, anavyozungumza na wateja wake!
Huwezi kujua ni Tunda ambaye hakusoma. Ana kazi nyingi mpaka nyingine anakataa.
Ushajiuliza ni kwa nini yeye, na wapambaji ni wengi? Leo kila mtu analalamika
maisha magumu. Kwa nini Tunda anastawi kwenye nchi ya watu wanaolia shida?” Net
akauliza.
“Nilishakujibu
Net. Shetani anao uwezo. Na yeye pia hufanikisha watu wake.” “Kwa maana
nyingine unasema hata kazi anazozifanya, na kufanikiwa pia ni kwa ajili ya
ushirikina?” “Huwezi kujua.” “Basi shetani ni mzuri mama. Kama wewe unayemuomba
Mungu, umefika hapo ulipo. Ulimtoa Tunda kwenye ofisi yako Arusha, ukaibiwa
mpaka kufilisiwa kabisa. Halafu Tunda anayemtumikia shetani amefanikiwa hivyo,
kwa nini tunaenda kanisani na sio huko anakokwenda Tunda?”
“Maana yeye anaonekana ana amani kuliko watu wengi
sana ninao waona. Au ana marafiki wa ukweli, kuliko watu wengi wanao kuzunguka
wewe mama.” “Sio kweli.” Akabisha. “Ni wewe mwenyewe umekuwa ukiwalalamikia kwangu
marafiki wanao kuzunguka. Huna rafiki wa kweli mama. Mwangalie Tunda na mama
Penny aliyesimama kumlinda Tunda mbele yako! Wewe unaye huyo mtu ambaye anaweza
kukukingia kifua pindi watu kama wewe wakisimama mbele yako?” Mama Cote
akababaika sana.
“Nimehangaika sana kufika hapa nilipo Net. Siwezi
kuruhusu Malaya yeyote yule aje kwenye maisha yetu na kurithi jasho langu.
Tunda anajua kuwa wewe unapesa, ndio maana anakuwa kama malaika wa nuru.
Atakwambia na kukujenga kwa maneno yanayoendana na vile ulivyo ili aweze
kukuaminisha.” Bila kujijua, kwa jazba mama Cote akaanza kufungua alichoficha
ndani. Net akabaki akimsikiliza.
“Aliweza
kulala na kina Meto, Mati na Gabriel, watu wa maana wa kanisani kwa kutumia
uongo unao endana na wao. Alipokuchunguza wewe na kukujua upo hivyo, ndipo
akaamua kuja na gia ya kukuokokea. Anajiliza bila kuchoka kwa kuwa nia
nikufikia mfuko wako. Na usifikiri wewe utakuwa wa mwisho. Utamuoa na bado atakuwa
na wanaume wengine. Siwezi kukubali eti wote tutumbukie kwenye mtego wa kijinga
hivyo! Nitakuwa mama wa ajabu sana, kuruhusu uangukie kwa mwanamke kama Tunda.”
Mama Cote hasira zilishapanda.
“Mimi nakuonya tu mama. Usipambane na Mungu. Hautashinda.
Na utaikumbuka siku ya leo.” “Wewe niache mwenyewe. Una wasiwasi gani? Kama
kweli amesimama, tutajua tu. Na wala sitajuta kwa kuwa Mungu ameniruhusu
kujaribu kila roho. Na yeye nitamjaribu mpaka niridhike. Kama wewe ulipata muda
wa kumuelewa mpaka ukamsamehe basi tupe
na wengine nafasi.” “Sawa mama yangu.” Net akamuhurumia mama yake. Akatamani
isingekuwa Tunda ndio anayesimama kati yao.
Hakuwahi
kusumbua nyumbani, leo amependa ndio imekuwa tatizo! Alikuwa ni kijana wa ‘ndiyo’
kwa mama yake, kila wakati. Aliacha kazi na maisha mazuri nchini Canada,
akaamua kuja kuishi na mama yake ili amsaidie kazi. Alimuhurumia, lakini
hakujua kitu chakufanya. Ni Tunda, msichana anayempenda na amekusudia kuwa
naye.
“Au hasira hii
kali kwa Tunda ni kwa ajili ya Meto!?” Net
aliwaza wakati akimtafakari mama yake asielewe ukweli mzima juu ya chuki ya
mama yake. Akanyanyua uso akamtizama mama yake. Akamkuta bado akimwangalia.
“Unaendeleaje na Meto?” Net akamuuliza mama yake taratibu tu. “Nimeamua
kuachana naye kabisa. Japokuwa amekuwa akinitumia jumbe zakuomba msamaha lakini
nimeamua kumuacha kabisa. Nimeumia mno. Sina jinsi yakueleza mtu akaelewa.
Nimeumia sana. Nimeamua niache kabisa kufikiria swala la ndoa tena.”
“Sitaweza
kuja kumuamini tena maishani. Itanisumbua mno. Nimekuwa naye kanisani,
akiniambia na kunionyesha jinsi alivyo muaminifu kumbe anaishi maisha machafu
huko nje! Nitakuja kumuamini vipi tena? Naanzia wapi kumuamini tena? Mtu
anayekwambia hiki na kuishi vile! Hapana. Nimeamua kuishi tu peke yangu. Naona
nimeshapoteza kila mtu sababu ya Tunda. Mimi ndio nimebaki muathirika wa maovu
ya huyo Tunda. Naamini Mungu atafanya kwa wakati wake.” Mama Cote
akajilalamisha akimtuhumu Tunda.
“Naelewa, unasababu zote za kibibilia
zinazokuruhusu kuachana na Meto. Zote kabisa, zinazokuruhusu kutokusamehe
kutokana na kosa la uzinzi, lakini pia unasababu zote kabisa za kibibilia
zinazokufanya usamehe, mama. Naomba upime kwa manufaa yako si yamwingine.
Unataka nini? Kusamehe na kuwa mwenye furaha tena, au kutokumsamehe na
kuendelea kuwa mpweke?”
“Nitarudi nyumbani, lakini hivi karibuni nitamuoa
Tunda, huwezi jua Mungu atatupa watoto lini! Hutakuwa ukiniona kama hivi.
Nitakuwa nikihudumia familia yangu. Nitaumia kukuona unaendelea kuishi mpweke
mpaka kifo chako. Samehe kwa ajili yako. Naamini amejifunza na hatarudia. Ona
jinsi alivyokubali kutengwa mbele ya kanisa, amevuliwa madaraka pale kanisani,
amebaki kuwa mtu wa kawaida tu. Angeondoka kama mwenzake, lakini yeye amekubali
kutumikia adhabu yake. Huhisi kuwa amejutia kitendo alichofanya?” Mama Cote akajifuta
machozi.
“Ukute na mapenzi ya kweli ndiyo yanambakisha pale
kanisani, mama. Anataka uone na uamini kuwa amejutia kitendo alichofanya.
Amemwambia Mchungaji ni kitendo alichofanya mara moja, tena baada ya mwenzake
kumuunganisha na Tunda na kumwambia amemtafutia binti atakayemsaidia kwa kuwa
amekaa muda mrefu bila mke. Anasema hata hakumwingilia Tunda. Ilikuwa kwenye
gari tu, tena mara moja. Anajuta sana.”
“Halafu ni mzee mwenye uwezo, huwezi sema
anakupenda kwa kuwa unapesa, kama wanaume wengine wanavyokufanyia. Yule mzee
haiitaji hata shilingi yako. Nakuomba mama yangu, pata muda ufikirie juu ya
hilo.” Net akasimama na kwenda kumzungushia mama yake mikono. Akambusu
kichwani. Mama Cote akajivuta chini kidogo na kujiegemeza kwa mwanae. “Is gonna
be fine mama.” “Hope so Net. Hope so baby.” Walikaa pale kwa muda, Net akaanza
kumchokoza mama yake, na kuanza kucheka. “Kuna mtu aliniambia nisichanganye
mambo ya familia na kazi. Sasa hivi ni asubuhi mama, acha nirudi kazini.” Mama
Cote akacheka. “Amebarikiwa mwanamke aliyekuzaa.” Net akacheka akambusu tena na
kuondoka.
Mama Cote aanza mikakati
yake kwa Tunda. Aanza kumuhusisha na Bethy.
Ni kweli
mama Cote alishindwa kuvumilia. Moyo wake ulimkataa kabisa Tunda. Kila alipojitahidi
akashindwa. Chuki juu yake ikazidi. Akaona isiwe shida, asije akafa pale
ofisini. Akakumbuka Net alimwambia angerudi nyumbani, lakini siku za karibuni
atamuoa Tunda. Na wakipata watoto anaweza hata asiwe anamuona. “Siwezi nikamuachia huyu Malaya, atawale
mtoto wangu. Ameshanichukulia ndoa, hawezi kunipokonya Net.” Mama Cote
akawaza nakuzidi kujipandisha hasira. Akampigia simu Bethy, mke wa Gabriel.
Akaomba wakutane kwa chakula cha mchana.
Bila
kubisha, kwa kuwa mama Cote alikuwa kama mkwe wake, na wapo karibu, Bethy
akakubali. Walipanga wakutane saa sita mchana. Wote walifika bila kuchelewa
kwenye mgahawa huo. Wakaagiza vinywaji, wakaanza kuzungumza.
“Unamjua mwanamke aliyekuwa amemchanganya Gabriel
wakati ule?” Mama Cote akauliza. “Mpaka akataka kuniacha?” Mke wa Gabriel,
Bethy akauliza na kuguna. “Ulishamjua?” “Nilivyokuwa nimechanganyikiwa wakati
ule, na Gab alikataa kabisa kumtaja. Aliniambia tatizo haliko kwa huyo mwanamke
wa nje, tatizo liko kwangu. Nikaonekana mimi ndio mbaya! Akieleza mabaya yangu
kwa kila mtu! Nilichofanya nikukubali kosa ili akose sababu.” “Basi mwanamke
huyo huyo, sasa hivi ndiye amemwingia na Net. Net amechanganyikiwa anataka
kumuoa.” Bethy alishtuka, mpaka akasimama.
“Ni jini nini huyo dada!?” Bethy akauliza na
mshangao mkubwa usoni. “Afadhali wewe unanielewa Bethy. Maana ile hali
iliyokuwa imempata Gabriel, ndiyo anayo Net sasa hivi. Kaa chini.” Bethy
akarudi kukaa akiwa bado na mshangao mkubwa sana. “Haiwezekani mama! Ipo namna.
Net na Gab ni kama ndugu wa damu! Kwa akili za Net, hawezi kumuoa mwanamke
aliyelala na Gab. Hata iweje, hawezi. Mimi namjua Net. Ipo tu namna mama Cote.”
Hapo akamfurahisha mama Cote.
“Afadhali kama sasa unanielewa wasiwasi wangu
ulipo. Maana Net hasikii wala haoni! Yule binti anatafuta wanaume wenye pesa
tu. Sasa anaona umeshindwa kwa Gabriel, amehamia kwa Net kwa kuwa sasa hivi
anajua Net anapesa nyingi za urithi. Siwezi kukubali yule binti akaolewa na
Net. Heri kufa kuliko kumuona anaolewa na Net. Yaani na yeye aje aitwe Cote!
Nahisi nitakufa.” Mama Cote akaweka msisitizo akitoa ya moyoni kwa Bethy.
“Hata mimi sikubali! Kwanza alivyonitesa kwenye
ndoa yangu! Gabriel alinianika na kunichafua bila aibu wala huruma, kama
hanifahamu ili tu kupata sababu ya kuwa naye! Hakika lazima kumuwekea kikomo.
Mchafu na mshenzi wa tabia. Amenyimwa aibu kwa kiasi gani!” Hapo wakawa
wameshapatana.
“Sasa tutafanyaje?” Mama Cote akauliza.
“Nikumfungua macho Net, kwa kuweka wazi mabaya yake yule msichana. Ni rahisi
sana mama. Wewe wala usihangaike na Net tena. Mimi namjua Net jinsi alivyo na
msimamo. Ukiendelea kumpinga, ndio utampoteza.” “Mara ya pili? Alishahama na
nyumba sababu ya kumkatalia kuwa na huyo binti! Kwanza anaitwa Tunda. Wala si
binti, Malaya yule.” Mama Cote akavyoza.
“Mama wewe! Net aliyekuwa anasema hana mpango
wakuondoka nyumbani, anataka aishi na wewe, leo ameondoka kwa ajili ya huyo
Tunda!” “Kwani hamjui kama amehama nyumbani?” “Siku hizi ukaribu na Gab ni kama
umepungua. Siwasikii.” “Anaishi kwake, Salasala. Na utengano huo wa Net na Gab,
sababu kubwa ni huyo Tunda. Atavuruga kila aina ya mahusiano na kila nyumba!”
Mama Cote akazidi kumwaga sumu kupandisha hasira ya Bethy zaidi.
“Mama Cote huyo msichana ana kitu. Sio bure.”
“Nimemwambia Net mimi. Hajaniamini. Alimsaidia mwenzie kuokoa ndoa yake.
Akaweka sawa akili ya Gabriel, naona amenaswa yeye sasa hivi. Na amembana kweli
Net! Anataka kufaidi kwa wote wawili!” “Itabidi kumuweka mwangani haraka.”
Wakapandishana morali, wakapanga na mipango yao ya jinsi ya kumuangamiza Tunda
na kumuweka mwangani. Zaidi kumtenga na Net. Wakakubaliana vizuri, ndipo
wakaachana.
Vita ya Tunda yaanza bila kujijua.
Akiwa
anafurahia penzi jipya. Jumbe za hapa na pale, kutolewa kwa chakula kiwe cha
mchana au usiku, Tunda hakuwa na taarifa juu ya mipango mikali dhidi yake. Siku
hiyo akiwa ofisini kwake, alikuja kijana na maua mazuri sana ameyashika mkononi
na kadi. Aliingia hapo ofisini na kwenda moja kwa moja kwenye meza ya Bety.
Akamwambia ametumwa kwa Tunda. Tunda alikuwa akiwasikiliza. Bety akamuelekeza
kwa ndani kidogo, ilipo ofisi ya Tunda.
Tunda
alikuwa amekodi kama nyumba. Lakini mbele kulikuwa na ofisi, nyuma kulikuwa na
vyumba ambavyo ndiko alikokuwa akihifadhia vitu vyake vyote vya kupambia.
Yule kijana akaingia alipokuwa
amekaa Tunda. Akamsalimia na kumkabidhi yale maua na kadi. Tunda alimshukuru
akiwa amejawa furaha, akijua vinatoka kwa Net. Akatoa ile kadi kutoka kwenye
bahasha, juu iliandikwa ‘I am Sorry!’ Tunda akakunja uso. Akaamua afungue
ili kujua inatoka kwa nani huyo anayemuomba msamaha!
Moja kwa
moja Tunda akasoma chini kujua inatoka wapi. Akakuta imesainiwa na Gabriel.
Ilionyeshwa imeandikwa na Gab mwenyewe, akiomba msamaha, na kumtaka waonane
baadaye kwa mazungumzo. Tunda alicheka, akamuomba yule kijana aliyetumwa kuleta
yale maua na kadi arudi navyo na kumuonya asiwahi kurudi tena pale. Yule kijana
akatoka na kila kitu alichoingia nacho. Maua na ile kadi. Alitamani kumwambia
Net, lakini akaona itakuwa uchonganishi. Akaamua kunyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni
Net alifika pale ofisini kwa Tunda ili wakapate chakula cha usiku pamoja.
Wakiwa hotelini, Net alimuona vile Tunda alivyobadilika. Net akajaribu kuuliza
lakini Tunda akamwambia nikuchoka tu. Baada ya chakula cha pamoja, waliagana
kila mmoja akarudi kwake.
Akiwa
anataka kulala, ujumbe ukaingia. ‘Naomba tuonane kesho
saa nne. Nina kitu cha msingi sana nataka kuzungumza na wewe. Gab.’ Alimtajia
na eneo la kukutana. Tunda akabaki akiitizama ile simu kwa muda akifikiria
chakumjibu Gab, akaamua apuuze.
Kesho
yake tena akiwa ofisini, ukaingia tena ujumbe mwingine. ‘Ulipata ujumbe wangu? Nitakuwepo pale nikikusubiri Tunda. Tafadhali usipuuze
hata kidogo.’ Tunda alianza kufikiria ni kitu gani hicho cha muhimu
Gabriel anataka kuzungumza naye! Swali jingine lililomsumbua ni wapi Gabriel
amepata namba yake? Akajiuliza hili na kujishauri lile, bila jibu.
Alibaki
akimfikiria Gabriel. Alikuwa muungwana sana kipindi yupo naye. Kwa kifupi ni
kama walishakuwa kwenye mahusiano ya karibu tofauti na wateja zake wengine. Gab
alitumia muda mwingi na Tunda akimueleza matatizo yake ya ndani sana na
kumfariji. Ndiye mteja pekee aliyekuwa akimpigia simu hata usiku sana na Tunda
alipokea hata awe amelala na mtu. Alitoka na kwenda kuzungumza naye.
Muda
mwingi walipokuwa wakiwa pamoja walitumia ndani kitandani wakizungumza na
mapenzi, tofauti na wateja zake wengine ambao ilikuwa ni kazi tu. Tunda alimfahamu Bethy na watoto wao wawili.
Mara nyingi Tunda alikuwa akituma salamu za hao watoto kupitia Gabriel. Bethy
alimfahamu kwa mabaya yake aliyokuwa akimfanyia Gabriel. Mbali ya nia yake
yakumchomoa pesa, Tunda na Gabriel wakajikuta wanakuwa kama marafiki. Wakiambiana
ya ndani sana. Haswa Gabriel ndiye aliyejikuta akimwambia Tunda mambo yake,
kwani alisema hana pakusemea.
Alisikia
mama Cote akiropoka kwa hasira siku alipomfuata ofisini kwake na kwenda
kumtukana, kuwa alitaka kumuacha Bethy kwa ajili yake. Vikafanyika vikao vya
nguvu ili kubadili akili yake Gabriel na kumrudisha kwa mkewe. “Kama kweli
alinipenda kwa kiasi hicho, ni kwa nini anifukuze vibaya vile?!” Tunda
akajiuliza. Akakumbuka jinsi alivyomtishia kumpiga kama hataondoka kwa haraka.
Tena akiwa ametoka kulimlilia shida usiku ule wa baridi na mvua, akamkatalia
kumsaidia. Tunda akakumbuka hofu iliyokuwa imemkamata usiku ule akiwa hana
tumaini jingine tena, hasira zikampanda zaidi. Akaamua kumpuuza. Akaendelea na
kazi zake.
Ilipofika
saa nne, ujumbe mwingine ukaingia. ‘Naona unasoma kila
ujumbe ninao kutumia Tunda. Nimeshafika hapa, nakusubiri. Nitakuwa nje tu, wala
hatutajificha.’ Alisoma ule
ujumbe. Kule kujua watakuwa nje, hadharani kukamtia moyo Tunda. Akaamua kwenda
kumsikiliza ili amalizane naye amuache kwa amani. Ila akakusudia hatampa sikio
lake tena kwa matatizo yake. Akanyanyua pochi yake na kutoka akiwa ameshapanga
hoja zake.
Gabriel
kwa Tunda Tena.
Kweli
alimkuta Gab akimsubiria nje ya huo mgahawa. Amekaa peke yake. Akamsalimia
baada ya kumsogelea. “Habari yako
Gabriel!” Hakutaka hata kumpa mkono. Gabriel alinyosha mkono, lakini Tunda
alivuta kiti na kukaa. “Sina muda mrefu sana. Naomba tuanze mazungumzo.”
“Hutaagiza kitu chochote?” “Hapana.” Tunda alimkatalia huku akimtizama machoni
ishara yakutaka aanze kuongea.
“Nakupenda Tunda. Nataka kukuoa.” Tunda akacheka
kwa kejeli. “Asante na hapana.” Akajibu hivyo tu na kusimama. Akavuta pochi
yake na kuanza kuondoka. “Sijamaliza Tunda. Naomba unisikilize.” Tunda
akasimama. “Nilikosea sana kukuacha. Lakini Net ndiye aliyenishawishi. Baada ya
siku ile nilijuta sana. Sikuwa na furaha tena baada ya kukupoteza wewe. Kila
aliyeniona alijua lipo tatizo.” Gab aliongea kwa upendo akibembeleza.
“Maisha yanakosa ladha bila wewe Tunda. Nakupenda
na ninakuhitaji. Nimekutafuta sana, mpaka siku ile nilipokuona kwenye kikao cha
harusi, yule mwenyekiti ndiye aliyenipa namba yako. Nakupenda Tunda, sitafanya
ujinga niliofanya zamani. Nitakutunza, utakuwa wangu tu. Hakuna mwanamke
anayenijulia kama wewe.” Tunda alibaki amesimama akimkodolea macho.
“Nakupenda Tunda.” Tunda alikuwa amekunja uso wa
mshangao. Gab akamsogelea na kumkumbatia. Tunda akamsukuma. Kilikuwa ni kitendo
cha muda mfupi hata Tunda hakujua kama angemkumbatia.
“Kwanza naomba nikusahihishe Gab. Hujawahi kuwa na
mahusiano na Tunda, ila Nancy. Pili, sikuwahi kukupenda kama ninavyompenda Net,
wewe nilikuwa nikikutumia kama wewe ulivyokuwa ukitumia mwili wangu kama
wanaume wengine tu.”
“Sasa hivi anayeishi hapa ni Tunda, aliyesamehewa
dhambi na kuishi maisha ya nidhamu mbele za Mungu. Kina Nancy walishatolewa
kwenye huu mwili muda mrefu sana. Hawapo na wala hawatakaa wakaishi tena
kutumia huu mwili uliotakaswa na kuoshwa na damu ya Yesu. Narudia tena,
anayeishi hapa ni Tunda ambaye hujawahi kumfahamu ila Net.” Tunda akaendelea
taratibu.
“Net
anamfahamu Tunda wa zamani sana ambaye hata angejiita Nancy, ninauhakika wewe
Gabriel usingethubutu hata kumsemesha. Net huyohuyo, anawafahamu na kina Nancy,
Fina, Ani, Maria na wengineo wengi tu walioishi kutumia huu mwili wangu. Tena
aliwafahamu kwa kuwafumania na huuhuu mwili wangu, kila mmoja kwa wakati wake.”
“Alishanifumania nikiwa Nancy. Nafikiri unakumbuka.
Maana tulikuwa wote na wewe ukimtumia Nancy kupitia huuhuu mwili. Haya,
alishanifumania nikiwa Maria, na wengine wengi tu Net aliokuwa akiwafumania
kupitia huuhuu mwili. Wakiishi vile watakavyo na kujipa majina watakayo wao.
Lakini akiwa ananijua mimi kama Tunda ambaye wewe ulimfahamu kwa upande mmoja
tu, Nancy.”
“Ninachotaka kukwambia Gab, kwa mabaya yote
niliyofanya zamani, na yeye Net kujua kwa kushuhudia na kuambiwa. Tena mengine
mabaya, machafu, yasiyoweza kutamkika hata kwa watu na sijawahi kumwambia mtu
yeyote hapa duniani, nilikiri mimi mwenyewe kwake Net. Nikiwa nimefika mwisho.
Wewe na wenzako waliokuwa wakitumia huu mwili kwa majina tofauti tofauti,
mliponitelekeza. Nafikiri unakumbuka jinsi ulivyonifukuza kinyama kana kwamba
tulikuwa maadui wakati nilikupa sikio langu hata saa sita za usiku.
Nilikusikiliza Gab na kukufariji bila kuchoka. Sasa siku ile uliponifukuza
kikatili huku ukitishia kunipiga nikiwa nakulilia shida Gab. Mvua na baridi ya
Arusha ikinipiga. Tena nikiwa nimekwambia wazi, sina pakwenda usiku ule. Net
alinipokea vilevile.”
“Net alihakikisha ananitoa kwenye kila kifungo
kilichokuwa kinanishikilia bila kuchoka kwani haikuwa rahisi wala kazi ya siku
moja. Ndani ya muda huo, nimemdhalilisha Net, ninauhakika wewe usingeweza Gab.
Ziko siku nilizotaka kubebwa juujuu, nikiwa na Net na wanaume waliokuwa
wakiutumia huu mwili wangu. Net alinipigania na kunitoa mikononi mwa wale
wanaume wawili waliokuwa wakining’ang’ania usiku ule. Ziko sehemu nilizopita
naye Net, ambazo wahudumu walinitambua mimi kama mwanamke wako, wakikuulizia
wewe. Lakini Net alibaki na mimi akinivumilia.”
“Haikuwa rahisi hata kidogo kwa Net. Mimi mwenyewe
nilikuwa najiuliza anawezaje! Aibu na fedheha niliyokuwa nikimtia. Lakini Net
alisimama na mimi. Akanisaidia kuanzia pale uliponiacha wewe, nikiwa na kina Nancy
na wengine wengi ndani yangu, mpaka msalabani ambako niliwekwa huru. Amenifundisha
kuomba na amenijenga kiakili. Naishi kama msomi sasa hivi, nakuingiza pesa kwa
kazi ninayofanya, kwa shule fupi aliyonipa Net nikiwa naye Arusha.”
“Alianza na mimi chini sana kwa elimu yangu ndogo
ambayo ninauhakika nisingeweza kuajiriwa popote kwani hata kazi aliyoniachia
nayo nilifukuzwa kwa kuwa sikuwa na vyeti japo niliimudu kazi vizuri tu. Net
akiwa amenifundisha. Alinielimisha na kunijenga mchana na usiku bila kuchoka
ndio maana sasa hivi ninaketi na wakuu sababu ya Net.”
“Na huo ndio nahesabu kuwa ni upendo. Upendo na
jinsi anavyonithamini Net, hata ungenipa miaka kumi nifikirie kama nastahili
hivyo, nisingekuja na jibu ya jinsi alivyo Net kwangu. Hakuna mwanadamu amewahi
kuwa karibu na mimi, isipokuwa ananufaika na mimi kwa namna moja au nyingine,
wewe ni shahidi. Ulikuwa karibu na mimi ulipokuwa unamatatizo na Bethy. Ulikuwa
kama umechanganyikiwa kwangu Gab. Sijui kama unakumbuka! Mlipopatana na Bethy,
hukuniaga kwa heshima Gab. Ulinifukuza vibaya sana. Kwa kuwa ulikuwa
umeshamaliza matumizi yako kwenye huu mwili kama wanaume wengine, lakini si
Net.”
“Sihitaji kutuzwa na yeyote kama ulivyosema mwanzo
kuwa unataka kunioa na kunitunza. Nancy aliyekulilia shida wakati ule
ukamfukuza, aliondoka na shida zake zote. Huyu Tunda anaridhika na pesa anayoingiza
kwa jasho lake na mapenzi ya Net, basi. Nakushauri na wewe uanze kuridhika na
mkeo. Ulifanya kosa sana kukubali kuwa na mahusiano na Nancy.”
“Wakati ule ulitakiwa unisaidie, kwa kuwa kwanza
wewe ulishapata neema ya kushinda dhambi. Ulikuwa na uwezo wa kuishi maisha
matakatifu, lakini ukakubali kunitumia mimi niliyekuwa nimefungwa na nguvu za
giza! Nilikuwa na majini yaliyokuwa yakinitesa, Gab. Sikuwa nalala vizuri kwa
hofu nikitumikishwa kwa hili au lile, mchana na usiku. Ulitakiwa unisaidie
kunitoa kwenye ile hali kama Net alivyofanya.” Tunda akaanza kutokwa na
machozi.
“Lakini ukiwa na uelewa kabisa wa baya na jema, ulitumia
mwili wangu kama wanaume wengine wasiomjua Mungu! Nimepata msaada Gabriel.
Nimesamehewa dhambi. Huko kwenye hayo maisha sitakaa nikarudi tena.
Nilitumikishwa na ibilisi mchana na usiku. Mungu amenifungua, nipo huru.
Nimeanza biashara yangu kwa jasho langu bila kuhongwa, na sasa hivi ninafurahia
maisha.” Tunda akafuta machozi.
“Naelewa unamatatizo na mkeo, lakini Gabriel,
hakuna kinachomshinda Mungu. Mgeukie Mungu. Kuhangaika na wanawake
hakutakusaidia, wote tunamadhaifu yetu, yanatofautiana majina tu. Rudi kwa
mkeo, anza upya. Naomba uniache na usirudie tena kunitafuta, lasivyo
nitamwambia Net.” Gab alikuwa amesimama amepigwa na butwaa kama sanamu. Tunda
akageuka nakuondoka bila hata kugeuka nyuma. Alimuacha Gab akiwa amesimama
palepale, akaingia kwenye gari yake akiwa na hasira sana, akarudi kazini kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net
alimpigia simu baada ya muda kumtaka watoke kwa chakula cha mchana, lakini kwa
kuwa hakuwa sawa kutokana na yale mazungumzo, akaona wasikutane. “Net yupo
makini sana. Akiniona tu, atajua kuna kinachoendelea. Tokea jana ameanza
kunitilia mashaka.” Tunda akawaza.
Akaona ampe sababu ya kiuungwana. Akamwambia ana kazi nyingi zakufanya siku
hiyo, labda wakutane kesho yake.
“Mbona kama haupo sawa? Kwema?” Alitamani kumwambia Net, lakini
akasita. Hakutaka kugeuka kuwa mchonganishi. “Tunda!
Vipi?” “Kwema kabisa, ninashuguli nyingi tu. Naomba tuongee baadaye.”
Akaamua kumuaga kwa haraka. Dhamira ilimsuta, kila kitu kwenye mwili wake
kilimshawishi kumshirikisha Net juu ya Gab, lakini akasita.
“Hata hivyo hatarudia tena. Gabriel ni mstaarabu
sana.’ Tunda akajipa moyo lakini bado
hakuwa kwenye hali nzuri kabisa. Akili ilikuwa imevurugika kabisa. Siku nzima
alishindwa kula kwa hofu yakuonana na Gab bila kumwambia Net. Historia ya
maisha aliyoishi nyuma ya kupanga wanaume wengi kwa wakati mmoja ilimsumbua
sana Tunda, akijua wazi Net anamjua alivyo mtaalamu kwenye hilo. “Sasa akija
kujua kuwa nilikutana na Gab bila kumtaarifu, tena tukiwa tumezungumza asubuhi
hiyohiyo, atajua narudia yale maisha ya kina Nancy.” Wasiwasi ulizidi
kumtesa Tunda. Akaona afunike dhambi ya kwanza, yakuonana na Gab bila
kumtaaribu Net.
Hata
jioni ile aliamua kumkwepa kabisa Net. “Naomba nikuone
kesho Net.” “Kuna nini? Mbona kama nahisi unanikwepa!?” “Hapana.” “Naomba kama
kuna kitu chochote kile uniambie Tunda.” “Hamna Net. Kesho tutaenda kumuona
baba?” Akaamua kubadili kabisa mazungumzo. “Mmefikia
wapi na yule wakili mpya?” “Anaonekana atatusaidia. Japo wanadai pesa nyingi
kidogo.” “Unataka msaada?” Net akauliza wakiwa bado wanazungumza kwenye
simu.
“Hapana Net. Asante sana. Nitaweza tu.” “Ukikwama, usiache
kuniambia.” “Nitafanya hivyo, japo..” Tunda akasita. “Nini?” “Natakiwa kulipa kodi ya mwaka mzima pale ninapoishi,
na hapa ofisini pia wamenipandishia kodi!” “Wanataka kiasi gani?” Net
akauliza. “Kuna kazi mbili kubwa nimepata mwezi huu na
nyingine ndogo ndogo, naamini mpaka mwishoni mwa mwezi nitakuwa nimekamilisha
pesa yote. Nakwambia hivi kwa kuwa nitakuwa na shuguli nyingi sana huu mwezi,
ili kujaribu kukusanya hiyo pesa. Kwa hiyo usipokuwa ukiniona mara kwa mara
ujue ni kwa muda tu.”
“Naelewa. Ila siku za jumamosi nitakuwa nikija kukusaidia. Si unajua
siendi kazini?” “Kweli Net?” “Kabisa. Hata kukusogezea maua, si itakuwa msaada
pia?” “Uwepo wako tu ni msaada tosha. Nitafurahi sana, lakini nakuwa na kazi
nyingi hata muda wa kula huwa nakosa.” “Usijali. Kwa hiyo umekataa kuniambia
kinachokusumbua sasa hivi?” Tunda akasita japo alijua Net sio mtu
wakumpotezea. Hasahau jambo. Lakini akajiambia ni heri nusu shari, kuliko shari
kamili. Akakusudia asimwambie. “Hamna kitu cha
kukwambia Net. Kesho tutaonana. Usiku mwema.” “Asante na wewe.” Tunda
akakata simu lakini akiumia sana moyoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi
nyumbani kwake akiwa amechoka zaidi mawazo. “Huu ujinga sitakuja kufanya
tena.” Akajiambia. “Siku nyingine ni heri tu nimwambie mapema. Nimejawa
hofu sina amani!” Tunda akaendelea kuwaza. Akaingia kuoga na kupanda
kitandani bila hata kula. Kwa kuwa alishaagana na Net, alimpigia simu Mama
Penny akaongea na watoto kidogo, wakaagana.
Kosa La Siri Laleta Balaa & Aibu!
Akazima
sauti kabisa kwenye simu zake zote mbili na kujiweka vizuri kitandani. Akatulia
akijaribu kulala lakini dhamira ilikuwa ikimsuta haswa na kushindwa kulala. Ni
Net aliyemlipia gharama yote hiyo! “Nani ameniloga Tunda mimi!? Hivi ni kwa
nini hata nilikwenda kuonana na huyo Gab! Heri ningemshirikisha kwanza Net,
akanishauri au nikamsikia anasemaje juu ya hili. Net ananithamini sana,
nawezaje kumsaliti. Hii ni tabia ambayo lazima niiache.” Wakati anaendelea kuwaza, akaona taa ya simu
yake inawaka. Jumbe nyingi za picha zikiingia kwenye hiyo simu yake ambayo ni
ya watu wa karibu tu ndio wana namba hiyo.
Akavuta
ile simu yake ili afungue aone ni picha gani. Kwa kuwa ilikuwa ni simu ile
isiyo ya biashara, akahisi labda mama Penny anamtumia picha fulani za mapambo
ili aone. Maana ni tabia yao, kutafuta picha za kumbi mbali mbali zilizopambwa
vizuri mtandaoni na kurushiana ili kuiga.
Alikaribia
kufa kwa mshtuko. Zilikuwa ni picha zake na Gabriel, walipokuwa wamekaa pale
mgahawani na nyingine Gab amemkumbatia. Halafu mbaya zaidi, mtumaji alikuwa
Nathaniel Cote. Bila kufikiria au kujijua Tunda akaitupa ile simu mbali akaruka
pale kitandani. Uchovu wote ulimwisha, akabaki amejishika moyo wake. ‘Mungu wangu nisaidie. Mungu niokoe. Uwii
jamani!’ Tunda akaanza kulia. ‘Ni mkosi gani huu!?’
Baada ya
kulia kwa muda, akaona kulia haitasaidia. Ni heri amtafute tu Net ajieleze.
Kwani Net alituma picha tu bila ujumbe wowote.
Tunda akaokota
simu yake kwa haraka nakuanza kumpigia Net. Lakini iliita bila kupokelewa.
Alipiga zaidi ya mara kumi bila majibu. Akaamua kutuma ujumbe. ‘Net, haipo kama inavyoonekana kwenye hizo picha. Tafadhali
pokea simu nikuelezee ilivyokuwa.’ ‘Nilifikiri hakuna cha kuniambia Tunda!
Naomba nilale. Mimi nitakutafuta.’ ‘Lini?’ Tunda akauliza kwa ujumbe. Kimya.
Akasubiri
jibu kwa muda, alipoona hajibiwi akaamua kutuma tena ujumbe mwingine. ‘Lini
utanitafuta Net?’ ‘Nitakapokuwa tayari.’ ‘Sawa Net. Lakini sijafanya kitu
kibaya. Mungu wangu nishahidi mpenzi.’ Hakupata jibu lolote. Hakuna usiku uliokuwa mrefu kama huo.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda
aliamka na kubaki akiangalia simu yake akisubiri labda Net atapiga. Lakini
hakuona kitu. Hapakuwa na simu wala jumbe za mapenzi asubuhi hiyo. Akasubiri na
kusubiri, kimya kwenye hiyo simu. Siku hiyo hata mama Penny hakumpigia. Ila
simu ya kikazi ikaanza kuita mfululizo. Akakumbuka uhitaji wa pesa alio nao,
akaamua kwenda kazini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alikwenda
kazini, siku nzima macho yalikuwa kwenye simu yake. Alibeba simu zake mpaka
chooni, bafuni kila mahali, lakini hapakuwa na ujumbe wowote. Usiku alikaa
kitandani bila kulala akisubiri simu kutoka kwa Net lakini Net hakukosea hata
kupiga. Tunda akaamua kutuma ujumbe. ‘Pole na kazi
Net.’ Kimya. Akatuma ujumbe mwingine. ‘Bado
nasubiri simu yako Net.’ Kimya. Tunda akaamua kulala na simu zake zote
sauti mpaka mwisho.
Ikawa asubuhi
ikawa jioni, siku tatu mfululizo bila kusikia chochote kutoka kwa Net. Tunda
alikuwa halali vizuri kwa mawazo. Alilia na kujibembeleza. Alijuta sana
kutokumshirikisha Net juu ya Gabriel. ‘Net hawezi kuniamini tena, atajua nimerudia tabia zile mbaya.’
Tunda alikuwa akiwaza huku akilia.
Akaamua
kumtumia ujumbe mwingine tena. ‘Net mpenzi wangu naomba
katika yote usifikirie kuniacha. Utaniua. Nina hali mbaya, nakaribia
kuchanganyikiwa. Tafadhali nipigie.’
Kimya.
Kanisani nako moto.
Kanisani
nako habari zilishafikishwa na Jaz msichana aliyekuwa akifanya kazi ofisini kwa
Tunda na kushuhudia mama Cote akiongea mazito ya Tunda kwa kuumia. Walio na
uwezo waliendelea kupeleleza zaidi, kama vile ilivyo kawaida habari mbaya
huenea kwa haraka sana. Walioweza kuongeza ubaya ili kunogesha ubaya wa Tunda
waliongeza. Ilimradi tu.
Tunda
alipoenda katikati ya juma kwenye vipindi vya kanisani kama kawaida yake,
hakuihitaji kuuliza. Ule uangaliwaji wake, alijua tu walishafikishiwa habari.
Kila aliposogelea kundi, walipomuona walinyamaza. Alipoamua kukaa, walinyanyuka
mmoja baada ya mwingine. Akajikuta anabakia na wawili au watatu.
Kikafika
kipindi cha maswali wakati wa bible study siku hiyo ya jumatano. Mmoja wa
wanawake ambaye aliheshimiana sana na Tunda, akanyoosha mkono. Mchungaji
akamchagua aulize swali. Swali lake ndilo lililomchosha Tunda, akaamua
anyanyuke na kuondoka kabisa. “Nina swali Mchungaji. Lakini litakuwa nje kidogo
na ulichofundisha leo.” Akasimama. “Karibu.” Mchungaji alijibu huku akimtizama.
“Naelewa kuwa watu wanapookoka wanasamehewa dhambi.
Lakini kama ni mtu ameanzisha biashara kwa pesa za umalaya na yeye bado
anajiita ameokoka, na yupo kanisani, anaabudu pamoja nasi, huku akijua kabisa
anaishi kwa pesa za dhambi. Je ni sawa?” Alipoweka tu kituo, mwenzake akadakia.
“Maana humu makanisani kumejaa kondoo na mbwa mwitu.” Mwengine akadakia.
“Tujihadhari jamani, chachu ndongo huchachua donge zima! Tuna vijana wetu
wadogo humu ndani.” Mwingine akaongeza kwa hekima tu. Ikaibuka minong’ono,
ndipo Tunda akanyanyuka nakuondoka. Siku hiyo Mama Penny hakuwepo. Alirudi
nyumbani kwake kama mgonjwa. Akapanda kitandani na kuanza kulia kwa uchungu wakupitiliza,
kama aliyefiwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda
hakujua chakufanya tena. Alishindwa hata kumwambia mama Penny kwa hofu. “Mama Penny na yeye hawezi kunielewa! Atajiuliza
niliwezaje kwenda kuonana na Gab bila hata kumwambia hata yeye, kama Net
nilishindwa! Watajua bado naishi yale maisha kwa siri. Mungu nitetee!”
Tunda akaendelea kulia na kujutia.
Alijimbia endapo wale watu
wakijua tena hata Net alimuacha kwa ajili ya kwenda kuonana na mwanaume
mwingine ambaye alikuwa na mahusiano naye zamani, tena alikwenda kwa siri,
ingekuwa mbaya zaidi! Hofu ilizidi kumwingia Tunda.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Je, Lipi JEMA kwa Tunda? Yale maisha na ujanja ujanja aliyokuwa akiishi kama kina Nancy akililiwa na kina Gab mpaka
sasa, hata Arusha aliacha wafanyabiashara wakubwa tu wakipishana ofisini
kwa Cote, wakimtongoza AU hivi alivyookoka anashindwa
kuaminika na kupokelewa kwenye jamii? Tena
wakitumia vibaya siri zake alizokiri kanisani, ili kupata ukombozi!?
Kwenye penzi la Net ambalo hata hakuwahi
kufikiria kama anaweza kuja kustahili kupendwa kwa kiasi hicho, AMELIKOROGA YEYE MWENYEWE. Na hata Net akimrudia, amekutana na
kipingamizi kikubwa, mama Cote anayemfahamu ndani na nje kama tapeli la mapenzi, anamwita ‘Malaya’. Amesimama kama Mlima akiapa Tunda hatakaa kuwa mrithi
pamoja naye, yeye aliyehangaika kuanzia chini. Na ameanza kukusanya majeshi
yake. Ameshampata Bethy ambaye naye amempandisha hasira na amekusudia kumlipa Tunda
kisasi kwa fedheha aliyomsababishia. Kwa ufupi vita ya Tunda ndio imeanza
rasmi.
Sasa
bora lipi?
v Vile alivyoacha ukahaba akakimbilia kanisani na
siri alizozitoa madhabahuni kwa Mungu akikiri makosa, ndizo zinazomwangamiza
sasa au
v Vile alivyokuwa amepagawa na mapepo, akitumiwa
mwili wake lakini heshima na pesa ilikuwepo? Alikosa soko kwa muda tu. Lakini
Tunda huyu wa sasa hivi anatakiwa mpaka na Gabriel na ameacha wanaume
wakimpigania jijini Arusha.
1.
Nani ametuma zile picha?
2.
Itakuaje kwa Net?
3.
Umbali gani mama Cote na
Bethy watakwenda kumuangamiza kabisa Tunda.
4.
Bethy atafanyaje akijua nia ya mumewe ya
kurudiana tena na Tunda?
5.
Gabriel atafanyaje baada ya
kujua mwanamke aliyetaka kumuoa tena akiwa tayari kuacha kila kitu, Net kama
ndugu wa karibu akamkataza, ndiye na yeye Net anaye?
6.
Tunda ataamua lipi juu ya
maisha yake, Net akiwa ameota mbawa? KIMYA. Mama Penny hawezi kumshirikisha
tena kwa chochote ili amshauri, kwa kosa la kwenda kukutana na Gab kwa siri?
7.
Nani atasimama na Tunda huyu
tena? Aliyekiri kuokoka, lakini kashfa ya kukutana kwa siri na Gabriel,
mwanaume aliyekuwa naye kwenye ukahaba zamani, inamkabili?
Kanisani moto, kazini
moto, aliowaibia waume zao nao moto! Itakuaje?
Yooooooote, na ya kusisimua, yanapatikana mbeleni.
Vita ya kiroho na ya kimwili kwa Tunda inaanza rasmi. Tena akiwa na adui wasomi, wanaakili ya kufikiria/kupanga
na wanayo pesa. {Mama Cote & Bethy}.
Usikose Mazito ya nilipotea.
0 Comments:
Post a Comment