W |
![]() |
“Nisikilize na kuniangalia vizuri, wewe Mama Cote.
Mimi ndio mama Penny. Dada yake Tunda. Ukiuliza hapa jijini mimi ni nani,
utaambiwa. Sijali wewe ni nani, unakiasi gani cha pesa benki wala unaendesha
gari gani. Mwanao ndiye aliyejileta mwenyewe kwa Tunda. Nenda kamtapikie mwanao
sio mdogo wangu.”
“Na kama unataka kuolewa, tafuta mwanaume mwenye
uwezo wakutawala zipu za suruali zake. Mlango huo hapo, potea kabla
sijakucharua. Na nikikusikia tena siku nyingine unamfuata Tunda, utaniona
mbaya. Potea bila hata kufungua mdomo wako tena hapa. Kimya, toka.” Mama Cote
alifungua mlango akatoka.
Tunda alianza kulia kama amechinjwa. Alilia
hakutaka hata mtu amguse, tena mbele ya watu. Akaingia ofisini kwake, akachukua
pochi yake na funguo za gari, akaondoka.
Ilimbidi Mama Penny ndio amalizane na wateja huku
akihakikisha hawamkimbii Tunda. Kama alivyo na maneno mengi. Aliongea mpaka
wote wakamuona Mama Cote ndiye mbaya. Wakati Mama Penny amefanikiwa
kuwashawishi na wote wakakubali kutoa oda zao, na yeye mwenyewe akahakikisha
amewaandika na kuchukua pesa za kuweka nafasi zao, ili ofisi ya Tunda isichukue
wateja wengine, kwa kuwa wale wafanyakazi wa Tunda walikuwa kama wamepigwa na
ganzi. Hakuna aliyeweza kuongea wala kusogea, Net naye akaingia.
Alitoa tabasamu baada yakumuona Mama Penny
aliyekuwa ametambulishwa na kufika nyumbani kwake siku iliyopita. “Kina Penny
hawajambo?” “Wazima. Namshukuru Mungu.” Net akashangaa kuona ile sura ya mama
Penny ya ucheshi imepotea. “Najua nimewahi kidogo, lakini tulikubaliana na
Tunda kwenda kupata chakula cha mchana pamoja. Sijui nimemkuta?” Net akauliza
kiuungwana tu.
“Mimi ni mkweli, na huwa sizunguki nikitaka kuongea
jambo langu. Tunda kaondoka hapa kama yupo uchi. Mama yako kamvua nguo Tunda.”
“Tena kamvua haswa.” Mmoja wa wateja akadakia. “Huyo ndio Net mwenyewe!?”
Mwenzake akauliza.
“Basi siye habari za Tunda tunazo zote! Kazitapika
mama yako mzazi. Alitaka kuzaa na baba yake, lakini mama yake akamtoa mimba.
Haya, kavunja uchumba wa mama yako. Katembea na kaka yako. Kalala na wazee
wakanisa, yote hayo tumeyajua leo.” Yule dada mteja wa Tunda akaongea
kishabiki. “Bwana mama yako anaongea!” “Kule si kuongea, nikuchambua!”
Wakacheka na kugonga. Net alibadilika akawa mwekundu.
“Nafikiri sina haja yakuongeza na hayo unayasikia
kutoka kwa wateja wa Tunda wanaohitaji huduma ya Tunda hapa ofisini kwake
alipopaanzisha kwa jasho lake, lakini mama yako amemudu kuja kumdhalilisha hapa.
Sasa ninachokuuliza wewe Net ni kitu kimoja tu. Kwa nini hukuanza kumwambia mama
yako kwanza, mkishakubaliana na mama yako, ndio ungemfuata Tunda? Unajua
historia yake tokea mwanzo. Kwa nini umekuja kumtonesha vidonda Tunda?”
“Alishatulia, maisha yake yalishabadilika, leo
umekuja na mama yako, tena umemfuata Tunda wewe mwenyewe, wala hakukutafuta
msichana wa watu! Halafu haya ndiyo mnayomlipa? Tunda ameanza chini kabisa, amesimamisha
hii biashara kwa jasho lake! Bila kulala usiku na mchana anahangaika kutafuta
pesa.” Mama Penny akaendelea.
“Hivi unajua ni watu wangapi walikuja kumposa Tunda
pale kanisani akawakataa? Ulimuona Julius? Anamtaka Tunda mpaka kesho, na
anapesa yule kijana sio za kurithi, pesa yake mwenyewe. Anampenda Tunda na yupo
tayari kumuoa Tunda hata leo jioni, ila Tunda mwenyewe aliamua kutulia kwanza
kidogo. Amekuamini wewe, akakukubali, leo mnakuja kumvuruga kiasi hiki!?”
“Nampenda Tunda, mama Penny. Sihitaji kuomba ruhusa
kwa mtu yeyote kumuoa Tunda. Namfahamu Tunda, si kwa kusimuliwa. Nayajua maisha
ya Tunda ndani na nje na nimemkubali kama alivyo.” Net akaendelea.
“Mama amekuja hapa na amefanya aliyoyafanya kwa
mshtuko. Hakutegemea kama mimi naweza kumuoa Tunda. Aliyomwambia Tunda leo,
ndiyo aliyoniambia mimi jana kama kunikumbusha kuwa Tunda ni nani. Lakini
sikujali. Niliamua kumuacha nimpe muda, atakuja kuelewa baadaye kuwa ninamuoa
mwanamke ninayempenda. Hakuna kitu wala mtu atakayebadilisha mapenzi yangu kwa
Tunda. Kwanza Tunda yuko wapi?” “Kaondoka.” Mama Penny akajibu kwa jeuri.
“Unamaanisha nini?” “Namaanisha Tunda ameondoka
hapa bila yakuaga, tena akiwa analia sana. Isingekuwa mimi kumfukuza mama yako
humu ndani, hata wewe ungemkuta akiendelea kutukana hapa. Ilikuwa mbaya sana
Net. Ni udhalilishwaji wa hali ya juu, sijawahi ona. Ni ngumu kuamini kama
mwanadamu anaweza kumfanyia mwenzake hivyo! Tena eti anatumia maneno ya Tunda
aliyotubu kanisani! Mnaabudu kanisa gani hilo ambalo halifundishi washirika
wake kusamehe na kuheshimu watu!?” Mama Penny alikuwa akiwaka kama moto.
“Sasa ukicheza kidogo tu Net, nakuhakikishia Tunda
ataolewa mchana kweupe, tena wewe na mama yako mkishuhudia. Tena ataolewa na
mwanamme atakayekuwa akijua historia ya maisha yake, akamkubali na kumuheshimu.
Nyinyi si mnadhani nyinyi ni watakatifu kuliko watu wote? Sasa mwambie mama
yako asubiri kadi ya harusi ya Tunda. Labda mimi nisiwe Mama Penny.
Nakuhakikishia Net, Tunda ataolewa. Msimbabaishe. Kwa kipi mno!?” Mama Penny
alikuwa amekasirika, anaongea bila kumeza mate, ikambidi Net abaki akimsubiri
amalize.
“Unafikiri Tunda anaweza kuwa amekwenda wapi?” Net
akatupia hilo swali kwa haraka. “Sijui. Lakini nataka kabla hujamtafuta Tunda
hakikisha unaandaa mazingira ya kumuweka Tunda. Tunda ameteseka tokea mtoto
mdogo. Kwa mara ya kwanza sisi ndio familia yake, na yeye ndio ametulia. Sitaki
ulazimishe kumuoa halafu akaenda kuteseka.”
“Hayo mazingira tutayatayarisha mimi na Tunda.
Siwezi kujitayarisha kwa nisicho kijua, mama Penny. Lasivyo nitajikuta hata
Tunda sitamuoa kwa kupoteza muda nikisitasita kwenye njia panda. Leo ni mama
yangu, kesho anaweza kuwa mama yake Tunda mwenyewe au mtu mwingine. Nitajuaje?
Tunda anahitaji kuwa na uhakika kuwa ninampenda, basi. Naamini akikubali hilo,
na kuamini kuwa anastahili, wengine hawatamsumbua.” Net akaendelea.
“Sasa hivi anakimbia kwa kuwa anajiona ni kweli
hanistahili. Lakini mimi ndiye naona simstahili kabisa Tunda. Nampenda na
ninamthamini sana Tunda. Hakuna kitakachonizuia kumuoa Tunda. Si mama yangu, si
mtu yeyote yule na sitapoteza muda kufanya walimwengu wakubaliane na maamuzi
yangu. Ninamuoa Tunda, tena nitamuoa si muda mrefu kuanzia sasa. Hata wewe
mwenyewe ujiandae kwa harusi yangu na Tunda.” Net alionekana na yeye
amekasirika sana.
Akatoa simu yake nakuanza kumpigia Tunda. Ilikuwa
ikiita tu mwishowe ilikatwa na kuzimwa kabisa. Tunda akawa hapatikani kabisa
kwa simu. “Naomba ufikirie Tunda anaweza kuwa amekwenda wapi.” “Nimekwambia
sijui.” Mama Penny akajibu tena kwa
hasira. Net akatoka pale akiwa hajui pakuanzia lakini akaona akamwangalie tu
nyumbani kwake.
Net amsaka tena Tunda.
Akatoka
kwenye ofisi za Tunda zilizokuwa karibu na Moroco, njia yakuelekea Kawe mpaka
Kimara nyumbani kwa Tunda. Akafika, kukawa kunaonyesha wazi hakuna dalili ya
mtu ndani. Akarudi tena ofisini kwa Tunda, hakuwepo. Siku ya Net ikawa
imeshavurugika. Hajui pakumpata tena Tunda. Akaenda kuegesha gari sehemu na
kuendelea kumpigia bila kuchoka. Mwishoe akaamua kwenda kumtizama kwa Mchungaji
wake. Akatoka hapo kwa kasi, akielekea Tabata huku akijaribu kumpigia simu.
Simu yake haikuwa hewani kabisa.
Akafika
nyumbani kwa mchungaji wake, akakuta na Mama Penny na yeye ndio anaingia
nyumbani kwake. “Tunda amefika hapa?” “Na mimi ndio nafika sasa hivi.” “Basi
naomba ukamwangalie ndani.” “Kwa nini usimpe muda akatulia?” “Nimekwambia
nimeamua kuwa na Tunda, katika shida na raha. Hatakaa akalia peke yake tena na
hii safari ya kudhalilishwa haitaishia leo. Atafuatwa na watu wengi tu. Sasa
ukisema nimpe muda, nitampa miaka mingapi? Na sina uhakika kama mama yangu
hatamfuata tena.” Net akajibu na yeye.
“Ndio
maana nakwambia ukaanze kuongea na mama yako kwanza kabla ya Tunda.” “Sitaishi
na mama yangu, nitaishi na Tunda ambaye atafuatwa na kila aina ya watu wakitaka
kumlaumu kwa maisha aliyoishi zamani. Kazi yangu ni kumjenga Tunda mke wangu,
wengine sio jukumu langu. Nilikwambia na nimerudia tena. Sasa unanisaidia
kumtafuta Tunda au nihangaike mimi mwenyewe?” Mara ujumbe ukaingia kwenye simu
ya Net.
‘Net! Nakuomba sana uniache, na usinitafute tena. Sikutaki na sipo
tayari kuolewa na wewe. Nafikiri nilikurupuka kukukubalia. Sikuwa nimefikiria
vizuri. Sasa hivi nimefikiria na nimeamua sitaki kuolewa na wewe tena. Endelea
na maisha yako na mimi uniache na maisha yangu kabisa.’
“Namimi naomba kusoma huo ujumbe.” Net akampa Mama
Penny simu yake. Akasoma. “Utafanyaje?” Mama Penny akauliza kwa kutulia kidogo
baada ya kusikia hekima za Net. Net akajaribu kumpigia, simu ikaita mara tatu
mwishowe ikakatwa na kuzimwa kabisa.
Akafikiria kama dakika moja kisha akampigia simu
mtu. “Haloo!” “Vipi Net?” “Nahitaji msaada wako, ndugu
yangu.” “Niambie kaka.” “Naomba uniambie hii namba ya simu, huyu mtu mara ya mwisho
amewasiliana na mimi alikuwa wapi?” “Naomba kama dakika tano, nitakupigia.”
“Sina dakika tano kaka.” “Kuna mtu amenisimamia mbele yangu, Net!” “Naomba
umwambie akusubiri.” “Daah! Haya kaka.” Net hakutaka hata kukata simu.
Baada ya muda mfupi sana akasikia akiitwa. “Net?” “Nipo kaka.” “Kigamboni.” Akamtajia hilo eneo
tu aliloona mtandaoni mara ya mwisho simu ya Tunda ilipo. Net akamgeukia Mama
Penny. “Unafikiri Tunda anaweza kuwa Kigamboni kwa nani?” “Sijui.” Net akarudi
kwenye simu. “Unaweza kuniambia eneo alilopo?”
“Itachukua muda kidogo Net.” “Basi nakuomba unisaidie kuangalia. Ukipata,
unipigie simu. Mimi naelekea hukohuko Kigamboni. Hata kama ni usiku, tafadhali
unijulishe. Naenda kusubiria simu yako huko.” “Lakini kwema Net? Kama ni mwizi
kwa nini tusimtafute Pius mtu wa usalama. Watamkamata sasa hivi.” “Hapana sio
mwizi ni mpenzi wangu. Tafadhali usimwambie mtu yeyote. Wewe tafuta eneo husika
alilopo. Utakuwa umenisaidia sana.” “Sawa Net. Kuwa makini huko.” Net
akakata simu.
“Naomba nikuachie namba yangu ya simu. Endapo Tunda
akikutafuta, naomba unijulishe na umwambie na mimi nipo huko huko Kigamboni,
sitaondoka huko mpaka anione.” Hakusubiri jibu. Akamkabidhi mama Penny kadi
yenye namba zake za simu na kuingia kwenye gari lake. Akaondoka Tabata
akielekea Kigamboni kumsaka Tunda.
Akiwa njiani mama Penny akampigia. “Umefika wapi Net?” “Bado nipo njiani kuelekea Kigamboni
kwenda kumtafuta Tunda.” “Samahani sana Net, nahisi bado nilikuwa na hasira.”
“Naelewa kabisa. Najua kitendo alichofanya mama ni kibaya. Lakini sina uwezo wa
kuzuia watu wengine waongee nini na wafikiri nini juu ya mahusiano yangu na
Tunda. Ningetamani kufanya kama ulivyonishauri, mama Penny. Lakini naona
nitapoteza muda mwingi sana hapo. Naona nitakuwa ni kama nazuia maji ya mvua
yasiingie mchangani! Sitaweza, na nitajichelewesha sana.”
“Nakuelewa. Naweza kuhisi mahali alipo
Tunda.” “Wapi?” “Hukohuko Kigamboni. Kuna hoteli moja tulikwenda wakati fulani
kama familia, kutembea tu. Lakini Tunda alipapenda sana, akasema ni patulivu anaweza
kupanga mambo yake yakapangika. Akaja kurudi tena huko akiwa peke yake, akakaa
huko kama siku tatu, aliporudi ndipo akafungua na ile ofisi. Huwa anakwendaga
huko mara kwa mara. Ukimuona huko naomba usimwambie kama mimi ndio nimekwambia
alipo.” Mama Penny akampa jina la hoteli na sehemu
iliyopo. “Asante sana.” Net akazidi kukanyaga
mafuta kwa nguvu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alifika
pale hotelini, giza lilikuwa limeshaingia. Akaulizia pale mapokezi, akaambiwa
mahali kilichopo chumba alichokodi Tunda, tena baada yakujieleza sana mpaka
wakamwamini. Alipofika mlangoni akamsikia Tunda akilia kwa uchungu sana. Net akasimama
pale nje kwa muda akitafakari nini chakufanya, kwani aliendesha akiwa na wazo
lakumpata Tunda tu, bila kujua nini chakumwambia pindi akimpata.
Kilio
cha Tunda, kilimfanya ashindwe kuvumilia. Akagonga. Alisikia kile kilio
kimekoma. Net akarudia kugonga tena. Kimya. Akarudia kugonga mara mbili
mfululizo. “Nani?” Tunda akauliza kwa upole,
kisha akaendelea. “Nilisema msiniletee chakula.”
Alimsikia akijieleza bila kufungua mlango.
Net
akagonga tena. “Ni mimi. Naomba unifungulie Tunda.” “Net!?”
“Ndiyo.” Kimya kilitanda kwa muda. “Tunda?” “Nilikutumia
ujumbe kwa simu Net. Hujapata?” “Nataka uniambie mimi mwenyewe
ukinitizama machoni Tunda, kama mimi nilivyofanya wakati nikikwambia nakupenda.
Si kwa kunitumia ujumbe.” Akamsikia Tunda akianza kulia tena bila kufungua
mlango. “Siwezi
Net. Sitaweza tena.” “Naomba unifungulie mlango Tunda.” Tunda alilia
kwa muda, kisha akafungua mlango taratibu.
Macho yake
meupe yalikuwa yamebadilika yakawa mekundu sana. Alivimba uso kwa kulia. Net
alikwenda moja kwa moja kwenye friji ndogo iliyokuwepo pale chumbani akatoa
maji na kumpa Tunda. “Kunywa kwanza haya maji.” Tunda akayaangalia yale maji
kwa muda, akafuta machozi na kamasi zilizokuwa zikimtoka kwa mkono wake kisha
akapokea yale maji akanywa kidogo huku wakiwa wamesimama.
Net
akavua viatu akapanda kitandani. “Njoo hapa.” Net akionyesha huku akipiga piga
kile kitanda taratibu kumuonyeshea pakukaa. Tunda akabaki akiangalia huku
akiendelea kulia. “Njoo, Tunda.” “Siwezi Net. Sitaweza kabisa.” “Umeshaniambia
hilo zaidi ya mara moja. Nakuomba uje hapa.” Tunda akaongeza kulia akafunika
uso wake kwa viganja vyake akabaki amesimama akilia sana. Net akaenda kumfuata
pale alipokuwa amesimama akilia, akamshika mkono na kumsogeza mpaka kitandani.
Kitanda
kilionekana kisafi na kimetandikwa. Wazi alionekana hakuwa amekaa kitandani
hapo tokea alipoingia kwenye chumba hicho. Net akampandisha kitandani, akaweka
kichwa chake kwenye mto, kisha akamfunika, na kuvuta mto mwingine juu kidogo ya
kichwa cha Tunda, akajiegemeza na yeye huku akimtizama. Tunda bado alikuwa
akilia.
Akaingia
chooni, akachukua kitaulo kidogo na kukilowesha na maji ya baridi akarudi nacho
pale kitandani nakuanza kumfuta nacho kichwani huku akiweka nywele zake vizuri,
akizitoa usoni nakuzirudisha nyuma. Tunda alikuwa amegeukia ukutani akilia. Net
aliendelea kumfuta taratibu mpaka alipotulia. Akaweka kile kitambaa pembeni
akarudi kujilaza pembeni yake.
Akambusu
upande wa kichwa aliokuwa pembeni yake. Tunda akajivuta karibu yake, kisha
akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama kusafisha kifua chake.
“Pumzika kidogo. Mimi nitakuwepo hapahapa. Ukiamka ndio tutakula.” Tunda
hakujibu, lakini baada ya muda Net akamsikia akihema taratibu kama mtu
aliyekwisha pitiwa na usingizi. Naye akajiegemeza vizuri pale kitandani
akapitiwa na usingizi pembeni yake.
Jumanne!
Hakuna
aliyeshtuka mpaka ilipofika asubuhi. Tunda hakuongea chochote aliamka na kwenda
kuoga bafuni. Alishtuka sana baada yakujiangalia kwenye kioo na kuona jinsi uso
wake ulivyo vimba. Alitoka na kurudi kukaa kwenye kochi. Akapandisha miguu yake
kwenye kochi, akabaki amejikunja. Net na yeye akabaki akimwangalia.
Baada ya
muda akasimama, akaenda kumzungushia shuka pale pale kwenye kochi, kisha
akambusu tena kichwani. “Na mimi
nakwenda kuoga. Nimeagiza watuletee kifungua kinywa huku chumbani. Najua baada
ya muda mfupi sana watakugongea mlango, uwafungulie.” Tunda akatingisha kichwa
kukubali. Net akaelekea na yeye bafuni.
Baada ya muda Net akatoka akakuta kifungua kinywa
mezani. “Nimeagiza tu, sijui utapenda?” Tunda hakujibu ila akaanza kulia tena. “Naomba
tule kwanza Tunda, halafu tutazungumza.” “Sitaweza
Net. Naomba uendelee na maisha yako.” “Mimi naendelea na maisha yangu.
Umeniona nikikimbia au nimesita mahali? Eti Tunda?” Tunda akaendelea kulia.
“Kwa nini unanikazania mimi, badala
ya kuoa msichana mwengine? Wasichana warembo wako wengi tu. Na wengi
wanakupenda Net na wanahistoria za maisha za kueleweka. Kwa nini usichague hata
mmoja wao, ukamuoa !?” “Mimi mwenyewe sijui
Tunda!” Net akakaa mezani nakuanza kufungua zile sahani. Hakuwa amevaa shati,
alibaki na suruali yake na kinguo kidogo cha ndani ya shati, cheupe. Sio
singlendi ila t-sheti nyepesi tu.
“Njoo tule. Au unataka nikusogezee hapohapo kwenye
kochi?” Tunda akainama na kuanza kulia tena. “Kwa
nini hutaki kunielewa Net!?” Net akasimama na kuhamia pale kwenye kochi
alipokuwa amekaa Tunda.
“Naona unataka tuzungumze kwanza kabla ya kula.
Naomba ufute machozi, ndio tuzungumze.” Tunda alijitahidi kukausha machozi,
lakini mengine yaliendelea kutoka. Akafuta tena na tena. “Nakusikiliza Tunda.” “Naona mimi sipo tayari kuolewa.” Tunda aliongea
huku akilia. “Naomba ufafanue. Hutaki kuolewa na mimi au hutaki kuolewa
kabisa?” “Vyote.” “Kwa kuwa mama yangu
amekwambia hutakiwi kuolewa na mimi au kwa kuwa umefikiria ukagundua
hunipendi?” Tunda akaanza kulia tena kwa kuficha uso wake.
“Naomba uniambie ukweli kabisa Tunda. Kama kweli
umegundua hunipendi, na siwezi kuwa mume wako, uniambie sasa hivi. Nitaondoka,
na hutakaa unione tena. Maana sitakuwa na jinsi nyingine ya kutengeneza maisha
yetu yakawa ya amani na furaha kama hutakuwa unanipenda. Na sitataka kuoa
mwanamke ambaye hanipendi. Nakuapia Tunda, sitakaa kukusumbua tena, endapo
utanitamkia leo, hunipendi. Nitaondoka sasa hivi na sitakusumbua tena. Naomba
uniambie ukweli.” Tunda akaendelea kulia.
“Tunda? Nataka kujua hutaki kuolewa na mimi kwa
kuwa hunipendi au kwa kuwa mama yangu amekudhalilisha?” “Siwezi kuwa mke wa mtu yeyote Net. Hata kama nakupenda kwa kiasi gani!
Siwezi.” “Ni lini ulishakuwa mke wa mtu, ukashindwa? Mimi mwenyewe
siwezi kusema siwezi kuwa mume wa Tunda, wakati sijawahi kukuoa. Au siwezi
kukuahidi nitakuwa mume mzuri sana kwako wakati hata sijui mume anakuaje!”
“Lakini najua mapenzi ya kweli niliyonayo kwako, na
msaada wa Mungu, vinanitosha kunitia nguvu ya kuanza safari yetu ya mapenzi. Na
hata wewe huhitaji vitu vingi sana kuwa mke bora kwangu. Mapenzi na Mungu
uliyenaye inatosha kukupa moyo wakujua unaweza. Hakuna sifa nyingine au
hatuhitaji mtu wa tatu, au kitu cha tatu kutufanikishia ndoa nzuri, Tunda.”
“Lakini kama hamna mapenzi kati yetu wala hakuna
hofu ya Mungu katika mahusiano yetu, ni kweli hatutafika mbali. Ninaweza nikaoa
binti ambaye hajawahi hata kuguswa na mwanaume yeyote, na mama yangu akampenda
sana, lakini mimi na yeye tukashindwana vibaya sana. Historia za nyuma za maisha
yetu na mtu watatu katika maisha yetu, vyote hivyo havituhakikishii usalama wa
ndoa yetu.” Net akaendelea kuzungumza naye taratibu, wakati Tunda akiendelea
kulia.
“Itakusaidia nini mama yangu akupende halafu mimi
nikawa sina mapenzi ya dhati kwako? Utaishi na mimi kwenye maisha yako yote
yaliyobaki hapa duniani. Na kwa bahati mbaya sana, kwa historia yako ya nyuma
watu kama mama hutawaepuka Tunda. Wapo, watakuwepo na wataendelea kuwepo katika
kila hatua ya maisha yako, ili kukurudisha chini. Leo wamekujia kwenye upande
wa ndoa, amenikimbia na kunitumia ujumbe mkali sana kuwa hunitaki tena.”
“Bahati mbaya sana, mama amekutukana ofisini kwako
mbele ya wateja wako, haya umeshaachana na mimi, na ile ofisi nayo utafunga na
kuacha ile biashara kabisa? Maana kwa jinsi nilivyowasikia wale wateja
niliowakuta pale ofisini kwako, wameshabikia sana. Tena wao ndio wamenisimulia
mambo yote mama aliyokwambia, sasa kama wamenieleza mimi hivyo, ujue
watatangaza kwa kila mtu watakaye weza kumfikia. Eti Tunda?” Tunda akaanza
kutulia. Yale maneno yakaanza kumwingia.
“Utakimbia wangapi na mpaka wapi? Mama yangu tu
peke yake amekukimbiza mpaka Kigamboni. Haya, akija na mama yako mzazi siku ya
harusi yetu? Si ndio utaniacha madhabahuni wewe!?” Tunda akacheka kidogo.
“Unacheka Tunda? Huo sio ukweli?” “Nilipaniki Net.”
“Lakini nilishakupa tahadhari mpenzi wangu! Hao
watu hatutawaepuka kabisa. Watakuja, tena sitashangaa hata watakuwepo wakutaka
kuweka pingamizi kwenye harusi yetu. Wapo na jinsi siku zinavyozidi kwenda na
watu wakagundua tupo pamoja, ndio watazidi kumiminika. Hapo bado hawajaja
watakao kwambia walikuwa wapenzi wangu, wewe ndiye uliyesababisha tukaachana.” “Kwani na wewe ulikuwa na wasichana wengine!?” Net
akacheka kidogo.
“Muone anavyopenda kujihami! Acha kuhangaika na
watu wa nje Tunda! Anguko kubwa na la hatari ni la kutoka ndani yako Tunda, si
nje. Usiruhusu watu wachezee hisia zako kiasi hicho! Huwezi kubadilisha kila
mtu, lakini unaweza kubadili nafsi yako. Hicho ndicho kitu cha msingi
ulichofanya, basi. Huwezi kusaidia wengine. Wewe ndiye unayejua ulipotoka,
ulipo na unapokwenda. Acha kutafuta nani atakuelewa na nani atakukubali.
Utapoteza muda mwingi sana hapo, na malengo pia. Umenielewa?” Tunda
alishabadilika sura yake, akawa anatabasamu. Akatingisha kichwa kukubali.
“Nikuombe kitu Tunda?” Tunda akatingisha kichwa
tena kukubali. “Naomba usiwe mwepesi kubadilika hasa katika mahusiano yetu. Mtu
akikuudhi kidogo tu, unaona mimi ndiye wakuniadhibu na upo tayari kuniacha.” “Sikuwa nakuadhibu Net. Maneno ya mama yako yalinifanya
nifikirie na kuona ni kama kweli sikutendei haki kunioa. Ni kama nilikuwa
nakuokoa kutoka kwenye janga.”
“Sio kwa namna ile Tunda! Naomba matatizo
yasitufanye tukimbiane bali tukimbiliane. Usinikimbie na kujificha. Uliniumiza
sana kuona hutaki kupokea simu zangu kabisa, mwishowe unazima kabisa simu yako
ili nisikupate!” “Samahani Net, nilipaniki.
Nikajawa majuto, aibu ya kudhalilishwa. Halafu nikachukia sana kuona furaha
yangu imedumu kwa masaa machache tu. Nikajiona vile ambavyo sistahili kuolewa.”
Akajifuta machozi.
“Naelewa
kabisa Tunda. Matatizo ni mengi, tena sasa hivi yatakuja zaidi na zaidi, ila
ukumbuke haupo tena peke yako. Kila tatizo utakalopata sasa hivi, hata liwe
kubwa kiasi gani, usinikimbie, tujifunze kutatua matatizo yetu pamoja.” “Kwa
hiyo huniachi?” Tunda akauliza kwa aibu kidogo.
“Kama ukiniambia hunipendi, sitakuwa na chakufanya
Tunda. Nitaondoka. Lakini si vinginevyo.” “Nakupenda sana Net, lakini mama yako
alinishtukiza, sikuwa najua chakufanya.” “Pole. Lakini ngoja nikwambie ukweli
Tunda. Utakuwa mke wangu, na utaishi na mimi. Lazima nikueleze ukweli. Sawa?”
Tunda akatingisha kichwa kukubali.
“Umeumiza watu wengi sana na mimi nikiwa mmoja wao.
Ilinichukua muda na kwa msaada wa Mungu kuweza kukusamehe na kukupenda tena.
Nakuomba wape watu wengine nafasi kuwathibitishia umebadilika. Usikimbie na
usiwachukie, wape muda. Watakuja kukuamini na waume zao, watoto wao, au tuseme
watakuja kukuamini tena, mpenzi wangu. Tuwape muda ili Mungu ashugulike nao.
Inaweza ikachukua muda mrefu. Tena tunaweza kujikuta tukabakia mimi na wewe tu, lakini lazima
tukubaliane kwa chochote na lolote, kuwa tutakuwa pamoja na hatutakimbiana.”
“Ukipata tatizo utanikimbilia mimi sio kunifukuza.
Hiyo itakuwa ndio nguvu yetu na wewe ukikubali kuwapa watu nafasi ili waje
kukuamini tena, haitakuumiza tena. Utajua wanahitaji muda wa kupona majeraha
uliyowaachia.” Tunda akajifuta machozi yaliyoendelea kutoka.
“Najuta Net! Najuta sana.” “Naelewa. Na ninajua unajuta sasa hivi kwa kuwa
ulipatanishwa na Mungu na unayo ofisi inayoweza kukufanya uishi vizuri na mimi
nipo hapa. Lakini wakati ule hukua na njia nyingine yakuishi Tunda. Hukua na
kimbilio, hukuwa na mtu wakukuongoza vizuri. Ulitupwa ulimwenguni ukiwa hujui
chakufanya, na akili yako ikakupeleka kufanya kile uwezacho ili kuishi. Usikae
muda mrefu sana hapo ukijilaumu. Sasa hivi tafuta jinsi ya kusaidia ulio waumiza.”
“Nitafayaje? Maana ile njia ya kwanza
uliyonipa ndio imeshashindikana. Maneno yatazagaa sana. Nimeshachelewa. Sasa,
sasahivi nifanyaje?” “Kwanza usiwe
unakimbia.” Tunda akacheka kidogo huku akijifuta machozi. “Sitakimbia tena Net.” “Afadhali.” Net akamsaidia
kukausha machozi.
“Pili,
unatakiwa wewe mwenyewe ukumbuke umesamehewa na Mungu, huna hatia na unahitaji
kusamehewa na wanadamu pia.” “Net! Siwezi kurudi kwa mama yangu kumuomba
msamaha kwa yale aliyonitendea. Kwanza yeye
mwenyewe ndio amenisababishia yale maisha. Alinitupa wakati namuhitaji.
Nimekuwa nikibakwa yeye akiwepo!” Tunda alianza kulia tena.
“Yeye ndio anatakiwa kuniomba msamaha!” “Sikiliza Tunda. Kwa jinsi ulivyonisimulia,
sidhani hata kama mama yako anajua upande wa pili wa hii stori. Yeye anachojua
ni mtoto aliyekataa shule na kuwa na mahusiano na mume wake. Au sikuelewa sawa
sawa?” “Ni kweli. Si baba wala mama wanaojua ukweli
wote.” “Basi hao ndio watu wakwanza na wamuhimu wakuanza nao.”
“Narudije kwa mama yangu Net!?” “Nitakusindikiza. Akikubali kukusikiliza sawa.
Akikataa pia ni sawa, tutampa muda na yeye wakufikiria na tutamwambia
pakukupata endapo atakuwa tayari kuzungumza na wewe. Lakini hakikisha unafanya
upande wako na swala la kusamehewa na kutokusamehewa sio juu yako tena.” “Asante
Net. Na mama yako nitafanyaje?” “Huyo atakutafuta kama atakuwa tayari
kukusamehe. Mwache kabisa.” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha
taratibu akijua ukweni hali ni mbaya kwa hakika.
“Nakushukuru Net. Lakini ni ngumu, ni ngumu sana!
Ni rahisi vile nilivyokuwa nikiishi pale kanisani kwa kina mama Penny. Hakuna anayenijua na kuninyoshea kidole. Kila mtu
ananiheshimu na kumpenda Tunda aliyesamehewa dhambi.” “Yalikuwa
mapumziko ya muda Tunda na yameisha. Hata kama sio swala la kuolewa ndilo lingekurudisha
mwangani ili kusafisha na kutibu madonda uliyoyaacha kwenye mioyo ya watu, basi
ungerudishwa kwa njia nyingine. Muda umefika. Mungu ameona upo tayari kusaidia
watu wengine. Na mimi nipo na wewe, siwezi kukuacha peke yako.” Tunda akafuta
machozi na kujisogeza vizuri kwa Net, Net akamkumbatia.
“Nakupenda
Tunda.” “Sasa hivi ndio nakuelewa ukisema hivyo Net. Asante.” Net akacheka. “Sasa leo ni jumanne, siku ya
kazi mama. Kukaa hapa hotelini ni kuzuri sana, lakini ile ofisi uliyofungua kwa
kuteseka, itafungwa kama ukiendelea kujifungia huku, na Net akikukumbatia.”
Tunda akacheka.
“Narudishaje uso wangu kwa wale wafanyakazi wangu?”
“Nimependa sana hiyo sentensi. Ni wafanyakazi wako. Wapo chini yako. Anza kwa
kuwaambia ukweli. Tena sio kwa mapana, kilekile walichomsikia mama akisema,
unawambia ni kweli, lakini..., hapo ndio unawaeleza juu ya Tunda huyu na
kuwasaidia hata kama na wao wanawazo la kufanya kama uliyofanya wewe, basi wasithubutu.
Waambie upo tayari kuwasaidia kwa namna yeyote ile kwa kuwaeleza madhara yake.”
Net aliongea na Tunda mpaka Tunda akapata nguvu mpya.
“Hivi nilikwambia kuwa nakupenda?” “Mmmmhh!” Net
alijidai kufikiria kidogo. “Sikumbuki. Ngoja nitoe simu yangu niangalie ujumbe
wako wa mwisho ulikuwa unasemaje.” Tunda akampokonya ile simu na kuufuta ule
ujumbe kisha akachukua simu yake na kumtumia ujumbe mwingine.
‘Net! Namshukuru sana Mungu kwa kukuleta kwenye maisha yangu. Sijui
ningekuwa wapi sasa hivi bila wewe mpenzi wangu. Nakushukuru kwa kunipokea
jinsi nilivyo. Nilikuwa kama glasi iliyovunjika, lakini umeanza kunijenga upya.
Najua ipo siku nitafikia ukamilifu ambao nitakuwa ni mke utakayenifurahia. Nipe
tu muda. Nakupenda sana Net, naahidi kuwa mwaminifu kwako daima.
Tunda!’
Net
alimuona Tunda akifuta machozi, kisha akatuma ule ujumbe. Akachukua simu yake
mara baada yakuona ujumbe umeingia, nakuanza kusoma. Tunda alimuona
akitabasamu.
‘I love you too, Tunda. Nakuahidi kuwa na wewe daima. Kwenye mvua na
jua, nitakuwepo kukushika mkono, ili usianguke tena. Nitakupenda, nitakutunza
na kukulinda daima.’
Nathaniel!
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda
alirudi nyumbani kwake akabadili nguo na kurudi ofisini kwake. Alimkuta
mfanyakazi mmoja, Bety na kuambiwa mwingine Jaz, ambaye alimtegemea sana, na
ndiye aliyemtuma hata kwenye kikao alichokuwa amekutana na Net, ameacha kazi.
Aliumia sana na hofu ilimnyemelea. Wale wasichana wote, Bety na Jaz, walikuwa
wakiabudu pamoja kwenye kanisa la kina mama Penny. Alijua kanisa zima litamjua
Tunda wa zamani na kupoteza heshima aliyokuwa ameshapata pale kanisani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa muda
mfupi aliokuwa amesimama pale mbele ya Bety, mfanyakazi wake, taarifa nyingi
zilianza kuingia kichwani kwake. Picha ya pale kanisani kutengwa na watu,
ilianza kumjia. Aliona vile watu watakavyokuwa wakikaa vikundi kumsema na
kumnyoshea vidole.
Pale
kanisani ni mahali pekee alipopata marafiki na familia. Alipenda kwenda
kanisani iwe katikati ya juma au mwishoni sababu ya furaha na amani aliyokuwa
akipata. Si wakubwa wala wadogo waliokuwa wakimuheshimu. Mama Penny na mumewe
hawakuacha kumsifia hata mbele za watu.
Kwa mara
ya kwanza maishani mwake Tunda alianza kuishi maisha ambayo wanadamu wengi
wanayatamani. Kuheshimiwa, kupendwa na bila wasiwasi wa kesho. Akiwa na pesa na
uhakika hata akifa kesho anaenda mbinguni kwa Mungu wake. Alishasahau kulia kwa
huzuni, uso wake ulijaa furaha kila wakati. ‘Kweli naanza kulipa gharama ya niliyoyatenda! Ni kweli Mungu
amenisamehe, lakini siwezi kuacha kulipa gharama.’ Tunda akajiwazia nafsini
mwake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Lakini
akamkumbuka Net, jinsi alivyomwambia huo ndio wakati wakutokurudi nyuma, lazima
apambane akisaidia aliowaumiza na mabinti wengine wanaopitia kwenye hali kama
yake. Akamgeukia Bety aliyebaki pale ofisini. “Nilifanya maamuzi mabaya sana
zamani. Sina jinsi ya kujitetea, na mama Cote hakukosea kabisa. Kwa yale
niliyoyafanya sistahili kusamehewa wala kuheshimiwa kwenye jamii. Inanipasa
kukaa mbali kabisa na watu. Lakini sitafanya hivyo. Ni uchafu wangu, lazima
nisafishe mimi mwenyewe. Atakayeweza kuwa na mimi kunisaidia sawa,
atakayeshindwa pia nitaelewa. Hata kama na wewe unataka kuondoka ni sawa tu,
sitakuzuia.” Tunda akaendelea taratibu tu.
“Nataka
kusaidia watu wanaopitia kwenye hali niliyopitia mimi. Kukimbia ni kukubali
wengine watumbukie kwenye shimo nililokuwepo mimi. Lakini Mungu alinihurumia
akanitoa huko. Kujificha na kutosimama tena mimi ninayejua ukweli wa maisha
yangu, nikumkatalia Mungu kusaidia kuwatoa watu wengine waliopo kwenye hiyo
shida, kupitia mimi.”
“Net alikubali kutumiwa na Mungu akanifikia mimi,
na kunitoa kwenye yale maisha machafu. Amenipatanisha na Mungu, Mungu
umenitakasa, amenisamehe na amenibariki. Kama niliweza kumtumikia shetani bila
aibu wala hofu, hata sasa sitaogopa tena.” Tunda alidhani alikuwa akiongea na
yule mfanyakazi wake aliyebaki lakini kumbe alikuwa akiiambia nafsi yake
iliyokuwa imeshakata tamaa. Alihakikisha anaiweka sawa nafsi, mwili na roho
yake iliyokubali kuwa imesamehewa. Alivuta pumzi kwa nguvu akatoa tabasamu pale
alipoona ameishinda nafsi yake na mwili uliomshawishi kutokusonga mbele kwa
hofu na aibu.
“Kwa hiyo Bety, upo na mimi au na wewe unataka
kuondoka?” “Mimi nipo dada yangu. Sina hata pakwenda. Huu mshahara unaonipa
hapa, unategemewa sana. Halafu na mimi najua kukosa na kusamehewa. Najua kulipa
gharama ya makosa. Nimefurahia huo moyo wa utayari, maana ni kwambie ukweli tu,
vita yako ndiyo imeanza. Hutapumzika. Hata wale waliokuwa wakikupenda,
watakugeuka na kuwa kama mwiba kwa maneno.”
“Lakini huwa haidumu muda mrefu, endapo ukisimama
kama ulivyosimama hapa mbele yangu na kuamua kupambana. Ila ukianza mchezo
wakurudi nyuma na kwenda mbele, utakaa hapo kwa muda mrefu sana, na wengi
hushindwa katikati na kuamua kurudi kabisa walipotoka.” Yule dada hakujua ni
kwa kiasi gani anamjenga Tunda. Waliongea kwa muda mrefu sana siku hiyo
wakisimuliana mambo mengi ya maisha yao. Uhusiano wao ukahama, kutoka kwa bosi
na mfanyakazi, wakajikuta wameanza kuwa marafiki.
Kwa
Mara ya kwanza, Net amtoa Tunda kama mpenzi.
Jioni
Net alifika nyumbani kwa Tunda kumchukua kwenda kupata naye chakula cha usiku.
Akabaki akimtizama. “Bwana Net! Utanifanya nishindwe kutembea.” “Umependeza
sana Tunda mpenzi wangu. Siamini kama jioni hii, mimi ndio napata bahati ya
kukaa na wewe meza moja na kukutizama.” Tunda akacheka. Alijisikia vizuri sana
kuona bado Net anaona thamani yake.
“Asante.
Hata wewe umependeza na unanukia vizuri. Nimependa ulivyovaa. Simple but
classic!” Tunda mjua thamani ya mavazi na vitu, alishampigia mahesabu kuanzia
juu mpaka chini, akajua hajajifanyia ubahili. “Asante. Basi twende ili tukapate
muda wa kutosha huko.” Wakaondoka hapo nyumbani kwa Tunda, Tunda asijue wanapokwenda.
Net
alimtendea haki vile alivyopendeza na sehemu aliyompeleka. Kwanza gari
ilipokelewa nje ya hiyo hoteli. Valet. Akashuka na kwenda kumfungulia mlango na
kumkabidhi kijana wa Valet funguo za gari yake kwamba yeye ndio akatafute
sehemu ya kuegesha gari. Kiatu cha juu alichokuwa amevaa Tunda na aina ya
gauni, ungependa kumtizama. Alipendeza haswa. Net alishindwa kumuachia mkono.
Wakaingia
akiwa amemshika mkono. Ungependa kuwatizama. Tunda huyu anapendwa. Yupo na Net,
anayemfahamu. Ungependa kuiona furaha yake usoni! Alijitengeneza vizuri tu
usoni na hereni zake zilimkaa vizuri.
Walifika
kwenye meza, Net akamvutia kiti, akakaa. Akampa busu la shavuni na kwenda kukaa
mbele yake. “Asante.” Tunda akashukuru akiwa amejawa tabasamu. “Tunda wewe ni
mzuri sana.” “Kweli Net au unanipa tu moyo?” Tunda alidhani ni kwa kuwa anajua
historia ya kutukanwa weusi wake, ndio maana anamsifia. “Nilikwambia sura yako
ilibaki akilini mwangu karibu kuchanganyikiwa!” Tunda akaanza kucheka.
“Mimi
sio mtu wakuchanganywa hovyo. Wewe ulinichanganya Tunda! Ulinivutia mara tu
nilipokuona. Nikatamani kupata na wewe huu muda ambao Mungu anatupa sasa hivi.
Nakupenda Tunda.” “Asante Net. Nakushukuru sana. Sina jinsi nikaeleza mtu
akanielewa juu yako Net. Lakini Mungu anajua kile alichonitendea kupitia wewe.
Wala sikustahili. Lakini Mungu amenirehemu.” Wakatulia kidogo, kama kila mtu
akiwaza lake.
Muhudumu
akafika kutaka kuwahudumia. Kila mmoja akaagiza kinywaji chake, kisha Net
akaagiza Champagne isiyo na kileo. Tunda akacheka. “Lazima tutoss kwenye first
date yetu.” Net akaweka msisitizo. Kwa Tunda kila kitu alipenda na kufurahia.
Hata mengine hakuyawazia, akabaki kupokea tu kwa shukurani.
“Niambie
habari za kazini.” Tunda akamuelezea juu
ya msichana aliyeacha kazi, lakini Net akamwambia huo ndio wakati wakujua watu
wa destiny/hatima yake. “Ndio nini?” Net akacheka. “Unajua katika maisha kuna
watu wa aina tatu. Na lazima wote uwe nao makini sana, ili usiachwe ukiwa
umeumia na kumkosea Mungu wako.” Net
akaanza.
“Ukiwa
kwenye shida fulani, Mungu hutuma watu wakukutoa pale kwenye shida na
kukusogeza mahali fulani. Iwe kwenye misiba, harusi, na matukio fulani Mungu
anayojua utahitaji watu. Huwa hao watu hawakai hata kidogo. Wakishakutoa kwenye ile hali tu, au wakishatimiza kusudi,
utakuta kunatokea sababu isiyo hata na msingi wanaondoka kwenye maisha yako. Na
pia sio wavumilivu hata kidogo. Usipojua kuwatumia vizuri, hupita kwa haraka,
hawakai. Kwa hiyo ni lazima ujue ni nini unataka ili wakitokea, unachukua kile
unachoona kitakufaa kwenye maisha yako, na wao wapo tayari kusimama na wewe
kwenye hilo. Tena kwa haraka. Nilikwambia huwa hawakai?” Tunda akatingisha
kichwa kukubali.
Akarudi muhudumu na vinywaji vyao wote na ile
champagne aliyoagiza Net. Wakamiminiwa kwenye glasi nzuri sana maalumu kwa
champagne na juisi zao. “Lazima tufanye toss.” Tunda akacheka kwa furaha wakati
ananyanyua glasi yake. “Tuna toss kwa ajili ya nini?” Akauliza Tunda. “Mwanzo
wa safari yetu mpaka kifo kitakapo tutenganisha. Tuombe Mungu atushike mkono
katika kila hatua.” Net akaeleza kwa ufupi kile anachoomba na kutamani kuona
kwenye hayo mahusiano, Tunda akimsikiliza. Kisha akasema, “For us.” Tunda
akagonga glasi ya Net taratibu na tabasamu usoni. “For us.” Na yeye akajibu
kwamba yote ‘kwa ajili yao’. Kisha wakanywa kwa pamoja.
Wakatulia kidogo. “Umeishia juu ya watu wa aina ya
kwanza Net.” Tunda akavunja ukimya akimtaka Net aendelee. “Yeah. Watu wa aina
ya pili, Mungu huwaleta kukamilisha huduma/maono/au
kazi fulani aliyokupa. Na hao pia huwepo kwa
kukusaidia kutimiza hilo kusudi tu. Wapo kwa ajili ya lile lengo tu.
Kuhakikisha linatimia. Mvua inyeshe, jua litoke, mpaka lile lengo likamilike au
lisimame. Lile tu. Usijichanganye, na kuwapa mambo au malengo yako mengine ya
maisha yako. Ujue utaumia. Kama ni huduma iliyopo ndani yako. Inakuwa ni ile
tu. Iwe Kanisa au huduma kubwa Mungu anayotaka kukutumia wewe ikamilike.
Atakutumia hao watu kwa hilo tu.”
“Hawawezi kusimama na wewe katika mambo mengine. Ni
hilo tu. Na mara nyingi hawa watu wanakuwa na uwezo mkubwa kukuzidi wewe. Iwe
fedha au wakati mwingine hata uelewa wa mambo fulani fulani. Kama ni kanisani,
watasimama na wewe katika ile huduma ya kanisani. Wakikusaidia na kukuelekeza
jinsi ya kufanya. Wewe utakuwa na yale maono ya kanisa, lakini wao wanaweza
wakawa na uelewa labda ya jinsi ya kuendesha kifedha. Wapi mtapata pesa.”
“Nini mfanye ili kusaidia ile huduma iendelee.
Watakuja wale watu wa aina ya kwanza, watafanikisha mambo fulani kwenye ile
huduma, wataondoka kwa sababu moja au nyingine, lakini hawa huwa wanabaki na
wewe. Na huwa Mungu hawaweki wakawa wengi. Unaweza kuta kanisa zima wakawa hata
wasiozidi watano.”
“Watasimama na hiyo huduma tu kuhakisha haifi labda
wewe mwenyewe uamue kuacha. Lakini hao watu watakuwepo kwenye ile huduma, au
kazi Mungu aliyokupa. Hivi nilishakwambia usijichanganye
na kuanza kuwapa kazi au malengo yako mengine? ” Net akarusha swali,
Tunda akacheka.
“Umeshaniambia.” “Ukicheka hivyo na macho hayo,
unazidi kunichanganya kabisa.” “Acha bwana Net. Niambie juu ya watu wa aina ya
tatu.” “Upo makini sana mpaka unaniogopesha! Utafikiri upo darasani unachukua
dondoo za mtihani!” “Hujui nikiasi gani unanisaidia Net. Sio kwamba sina elimu
ya darasani tu, sina elimu yeyote ile ya mambo ya jamii. Sikubahatika kulelewa
na mtu yeyote. Nimejikuza mwenyewe. Yale yaliyokuwa sawa kichwani mwangu ndio
nilikuwa nikifanya. Ndio maana huwa sipendi kuacha kwenda kanisani ili nijue na
Mungu naye anataka nini kwa wanadamu, na huwa napenda kwenda kukaa nyumbani kwa
Mchungaji ili nione familia huwa zinakuwaje. Mke na mume huwa wanatakiwa waishije!”
Tunda akaendelea.
“Niliishi na baba na mkewe, lakini hawakuwa
wakielewana sana. Yule mama ndiye aliyekuwa kama mtawala pale ndani. Baba
hakuwa akiongea. Haya, nyumbani kwa mama na mumewe, mama hakuwa na muda kabisa
na mambo ya familia. Baba Tom ndiye aliyekuwa kama mama. Alifanya mambo yote ya
pale ndani, na msichana wa kazi ndio alijua kupikwe nini, siku gani afanye
nini, yaani alipewa uhuru wote pale ndani.”
“Mama hakuwa akikaa sana pale ndani na akija
anakuwa na watoto wake tu. Halafu pia baba Tom alikuwa mbabe sana. Sio kwangu
tu, hata kwa mama. Akionyesha yeye ndio mtawala pale. Mwenye mali. Wote tumevikuta
na tunaweza kuviacha siku atakayoamua yeye. Kwa hiyo hivyo unavyoongea na mimi,
natamani kukusikiliza na kukuelewa vizuri. Inanisaidia kuliko vile
unavyofikiri. Sikuwahi pia kuwa na rafiki. Kwa hiyo unaweza kufikiri vile
nilivyo na taarifa chache za maisha.” Net akatabasamu.
“Lakini hujachelewa Tunda. Upo katika wakati sahihi
na Mungu atakuletea watu sahihi kukusaidia kuishi maisha aliyokukusudiwa uishi.
Na ninakuombea sana tu. Mungu hawezi kukuacha.” “Asante Net.” Tunda akatabasamu
nakumfanya Net atabasamu na kubaki akimtizama.
“Nini sasa?” “Nafurahi kukuangalia Tunda. Una uzuri
ambao mtu akitulia na kuamua kukuangalia vizuri, hawezi kutosheka.” “Ukifanya
hivyo nitakuwa nashindwa kukutizama machoni.” “Unakumbuka kipindi tupo Arusha?”
“Nakumbuka.” “Nilikwambia kutoniangalia, ndio adhabu yangu tosha.” Tunda
akacheka kwa sauti na kufanya waliokuwa wamekaa meza za jirani kuwageukia.
“Unajua Net?” “Ehe!” “Sikuwahi kuwaza hata kidogo,
kama kijana wa kizungu anaweza kunipenda mimi! Haswa wewe Net. Mama alishanikashifu
juu ya haya macho nakuniambia yapo kama ya paka. Huu weusi wangu ndio ilikuwa
kabisa. Alikuwa anasema ninamfanya atapike.” “Yeye ni mweupe?” Net akauliza.
“Kwa asili sio mweupe sana, lakini huwa
anajiongeza. Kwa hiyo ukimuona ni mweupe kukukaribia wewe.” Net hakuongeza neno
hapo. Tunda akaendelea. “Kwa hiyo nilikosa ujasiri kabisa na kila kitu kwenye
huu mwili.” “Huo ulikuwa ni uongo wa shetani. Tena ukute hata mama yako hakuwa
akijua analoongea. Alikuwa akiropoka tu sababu ya hasira. Lakini shetani
akahakikisha anapigia mstari hilo neno, ili awe anakukumbusha mara kwa mara
kukutesa tu. Mimi napenda wasichana wazuri na huwa nawajua. Wewe ni mmoja
wapo.” “Net wewe! Kwa hiyo ulishawapenda wangapi?” Net na yeye akacheka sana,
tena kwa sauti ya juu. Aligundua ameropoka.
“Nimeropoka Tunda. Sikuwa na maana ya kupenda kwa
jinsi hiyo. Kuna watu wanavutia kuangalia, mpaka unajiuliza siku wanaumbwa huko
tumboni, Mungu hakuwa na kazi nyingi siku hiyo au anakuwa anakusudi nao gani
hapa duniani! Na wengi wamekuwa wakichezewa na shetani kwa kupitia uzuri wao.
Naomba tuache hilo, tusizungumzie tena. Ni sawa?” “Mmmh! Nimeanza kupatwa
wivu.” Net akacheka zaidi.
“Usiwe na wasiwasi Tunda. Mungu amenipa mrembo
wangu, macho yangu yametulia kwako tu. Mungu amenijalia kuridhika na
anachonipa, sitamani visivyo vyangu. Ni wewe tu.” Tunda akatabasamu kidogo kama
anayefikiria.
“Asante. Niambie juu ya watu wa aina ya tatu.” Akabadili mazungumzo. “Kweli umekusudia
kujifunza. Haya, hawa watu wa aina ya tatu, Mungu anakuletea ni watu wakudumu. Mvua inyeshe, jua litoke wapo na
wewe katika kila jambo kwenye maisha yako. Mtakwaruzana, lakini baada ya muda mfupi
mnarudisha mahusiano. Wapo kukujenga na kukufanya uwe vile uonekanavyo.
Umeshawahi kusikia ule usemi unaosema, ukitaka kujua tabia za mtu, angalia aina
ya marafiki wanao mzunguka?” Tunda akatingisha kichwa kukataa.
“Basi ndio ujue. Marafiki wabaya huaribu tabia
njema. Sio uanze kukimbia watu lakini! Unaweza kukuta Mungu anakuletea mtu ili
umsaidie. Jukumu lako ni kumsaidia. Akikubali kubadilika sawa, akikataa
unamruhusu apite, lasivyo ukimng’ang’ania utajikuta na wewe unanza kuwa njia
panda na kutilia mashaka hata baadhi ya mambo uliyokuwa ukiyaamini. Kwa kuwa na
wao wataanza kukuhubiria njia zao. Umeridhika sasa?” “Sana.” Waliendelea kuzungumza
jioni hiyo mambo mengi sana. Nia ya Net nikumfahamu Tunda, kwa ngazi ya kutaka
awe mke wake. Ajue ataishi na mtu wa namna gani.
Chakula
kikaanza kuletwa kama alivyoagiza Net. 3 full course. Yaani milo mitatu.
Wakaanza na appertizer. Kwa kuwa alijua Tunda mpenda matunda na mboga mboga
hasa mida ya jioni, akaomba wampe menu yenye appertizer za matunda. Tunda akachagua
matango yaliyokatwa na kupambwa vizuri na nyanya juu yake yakiwa na sour cream
katikati. Yeye Net akataka aletewe supu.
Baada ya
muda mfupi tu vikaletwa. Wakaanza kula hiyo appertizer na vinywaji vyao,
taratibu tu. Muhudumu alikuwa akipita mara kwa mara kuongeza juisi na kuuliza
kama wanahitaji chochote. Mwishoe alikuja kutoa vyombo vya appertizer. Wakabaki
wametulia tu.
Muhudumu
akarudi tena na menu ya main course sasa. Kila
mmoja akaagiza chakula. Ila Tunda alitaka mboga mboga na samaki wakuchomwa asiye
na mifupa. Net akaagiza mlo uliokamilika. Aina ya huduma waliyokuwa wakipewa,
na ile sehemu tu, Tunda alijua pesa itamtoka Net. Chakula kililetwa wakaendelea
kula taratibu huku wakizungumza hili na lile bila kuvuka mipaka, wakati
mwingine kimya.
Wakamaliza
chakula, ikaja dessert. Net alitaka aletewe kipande cha cheesecake. Tunda akataka mchanganyiko wa matunda. Strawberry na
zabibu. Vikaletwa vimewekwa kwa kuvutia, safi. Baada ya utulivu wa pale na
kupepesa macho, Tunda akagundua kitu cha tofauti pale. Akacheka na kumwangalia
Net. “Nini?” “Hii sehemu iliandaliwa maalumu kwa ajili yetu?” Net akacheka
kidogo.
“Maana nimeona tumepewa meza ya pembeni. Kuna
mpaka mishumaa! Patulivu, hakuna mtu huu upande wote, ni sisi tu! Halafu pako
romantic, madhari ya kimahaba.” “Umependa?” Net akauliza. “Sana Net! Unauliza
tena? Mimi Tunda nani anifanyie mambo haya!? Au umenisahau?” Net akacheka
taratibu. “Unastahili zaidi ya hivi Tunda. Ni vile leo ilikuwa siku ya kazi
nilikuwa na mambo mengi ndio maana matayarisho yamekuwa hivi. Lakini unastahili
zaidi ya haya. Na nimefurahi kama umefurahia.” Ilimgusa sana Tunda. “Nashukuru
sana Net. Asante. Sasa hivi nimetulia na kuangalia vizuri, ndio nimegundua!
Nashukuru kwa kuniheshimu na kunithamini. Asante Net. Hakika sikutarajia kitu
kama hiki! Ni mambo nayaona kwenye sinema! Sikutegemea!”
“Acha kulia sasa. mimi nataka ufurahi!” Tunda akaendelea kujifuta machozi.
“Hakika sikutegemea hata kidogo! Kwa ajili yangu mimi Tunda?” “Wewe
mpenzi wangu.” “Asante Net. Mimi najua unajua kama
namaanisha.” “Nimefurahi kama umefurahia. Halafu unakumbuka nilitoa
cheni mguuni kwako kisha nikakuahidi nitairudisha nyingine hapo?” Tunda
akakumbuka na kucheka akijifuta machozi.
“Nilikwambia
haina haja Net! Yale yalipita.” “Lakini nilimuonea wivu yule aliyeweka ya
kwanza. Jinsi ulivyoivaa na kuiweka maana kubwa sana! Ulishindwa kuitoa Tunda.
Unakumbuka sifa za mtu uliyeniambia unataka aje airudishe hapo mguuni?” Tunda
akanyamaza, akainamia matunda yake kama anayefikiria kwa muda.
“Wakati
ule niliongea vile nikiwa najua wazi hakuna atakayeweza kuja kuitoa ile cheni
Net. Kwanza sikujua kama hata kuna mtu atajali kiasi cha kunifikiria kwa namna
ile. Halafu sikujua kama naweza kupata mtu atakayenipenda, kunijali na
kunithamani kwa kiasi kile cha Sadiki. Ilikuwa na nguvu fulani na maana kubwa
sana moyoni kwangu. Sikujua kumbe ni nguvu za giza.” Tunda akatulia kidogo.
“Anyway.”
Tunda akaendelea. “Wewe nilikuruhusu uitoe nikiwa hata sijui kama unanipenda
ila nilijua unanijali kwa namna fulani. Halafu nilikuheshimu kwa umbali
uliolipa gharama kwenda na mimi. Halafu ukawa umeshaniogopesha kuwa nakuwa bado
nipo kwenye maagano na Sadiki au kwenye ndoa ya Sadiki na mkewe.” Net akacheka
taratibu huku akimwangalia jinsi anavyoongea taratibu kwa sauti yake tulivu.
“Nikaona
nikukubalie wewe ndio uwe umeitoa. Angalau kuweka historia yangu mwenyewe kuwa
ni wewe ndiye ulinitoa kwenye vifungo vyote. Hata hivyo nilijiambia sitaweza
kupata tena mtu niliyetamani aje anitoe hiyo cheni hapo mguuni. Kwa hiyo
nikaona ni heri nikupe tu wewe hiyo nafasi, uwe umeandika historia nzima
yakunifungua vifungo vyote. Sikujua kama nastahili au hata kuja kupendwa kimapenzi
na kuheshimiwa. Nilijua ni ndoto ambazo zinaweza zisitimie Net.” Tunda
akaendelea taratibu.
“Tokea mtoto, au tokea natolewa kwa bibi na babu, kila mtu, si
wakike hao kina mama nilioishi nao au wanaume wote niliokuwa nao, wamekuwa
karibu na mimi kwa ajili ya kujinufaisha kwa namna moja au nyingine. Lakini sio
kunitizama mimi kama Tunda halisi. Kwa hiyo nikakuruhusu wewe uitoe, lakini
sikuwa hata na wazo kuwa unanipenda hivi Net! Ningejua wakati ule, nahisi mimi
mwenyewe ningekuomba unitoe.” Net akacheka tena, Tunda akajifuta machozi.
“Basi
naomba nirudishe nyingine.” Tunda akatoa macho. “Kwamba umetengeneza kama
ile!?” “Tofauti kidogo.” Tunda akacheka asiamini. “Asante Net.” Net akapiga
magoti, Tunda akanyanyua mguu juu kidogo, Net akamvalisha ile cheni ya mguuni.
Kisha akaizungusha kidogo kitu kilichomfurahisha sana Tunda. Alijisikia vizuri.
Alikuwa akicheka huku akifuta machozi. Net akamnyanyua ule mguu na kuubusu
akiwa amepiga goti kwa mguu mmoja vilevile. Tunda hakuamini.
“Hii imenikaa vizuri zaidi.” Akajisifia Tunda. “Na nimeipenda sana Net, japo sijaona muundo, lakini
nimependa.” Mwanga wa pale haukuwa mkali sababu ya Net mwenyewe. Alitaka
mwanga hafifu na mishumaa iwashwe. “Asante
sanaaaa.” Net akacheka na kusimama. “Karibu.” Akambusu shavuni. “Sasa
kwa kuwa naona umevaa cheni shingoni na mkononi umeweka bangili nzuri, hivi
utakuja kuvaa wakati mwingine.” Net akaweka kijimfuko mezani.
“Acha
mchezo Net! Hivi navua hapahapa!” Net akaanza kucheka. “Ili uvae hivi?”
“Hapana. Ili univalishe hivi.” Net akaendelea kucheka wakati Tunda
anaanza kuvua. “Basi acha nikuvue mwenyewe na kukuvalisha.” “Hapo sawa.” Tunda
akakubali. Akanyanyua nywele alizokuwa amezibana sehemu moja, mkia
ukining’inia, Net akamfungua ile cheni ya shingoni na kuweka yake. Akampa mkono
wa kushoto, akafanya hivyohivyo.
“Ningejua
nisingeagiza dessert.” Net akazidi kucheka. “Kwamba hii ndio ingekuwa dessert
yako?” “Kabisa Net!” Tunda alijibu huku akijiangalia ile cheni mkononi na ile
ya shingoni. “Asante sana Net.” Tunda akasimama na yeye akaenda kumbusu pale
alipokua amekaa, shavuni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Japokuwa
alikuwa na mambo mengi kazini kwake, lakini Net alijitahidi kupata muda na
Tunda kwa kadiri alivyoweza. Upendo wa dhati ulianza kujengeka katikati yao.
Jumbe na simu za hapa na pale hazikuwa zikiisha. Mama yake Net alishangaa kuona
Net hamuulizi kitu chochote juu ya fujo alizomfanyia Tunda. Alihisi wameachana,
lakini furaha aliyokuwa nayo Net, alijua kijana wake yupo kwenye mapenzi. Mama
Cote mawazo akahamisha kwenye mali zake. Akiwinda jasho lake.
Kwa Ufupi Juu ya Ritha, Mama
Cote au Mama Net na wakweze, ndoa yake na wanae.
Net
ndiye aliyeachwa mrithi wa mali zote za bibi na babu yake, endapo bibi yake pia
akifariki. Na pia endapo mama huyo angefariki, pia Net ndiye angebaki mrithi
tu. Sasa kitendo cha msichana mwenye sifa kama Tunda kujitokeza kwenye maisha
ya mwanae, na kukimbilia kanisani alipo Net, tena akiwa ameanza na Gabriel,
akaja wale wazee. Tena wote walikuwa wana hali nzuri ya kifedha! Moja kwa moja
yule mama alijua Tunda anataka tu mali. Kitu ambacho asingeruhusu mama huyo.
Pesa
yake aliihangaikia mwenyewe, tena kwa kulipa gharama kubwa sana. Alitua nchini
akiwa hafahamiani na yeyote aliyemsaidia kufika hapo alipo sasa. Kampuni hiyo
ya Cote Ltd, aliianzisha hapo nchini yeye
mwenyewe. Kuanzia ni jina tu, mpaka sasa inafahamika nakutajwa mpaka bungeni na
waheshimiwa kama moja ya kampuni iliyofanikiwa na kupigiwa kelele na baadhi ya
wabunge kuwa, inatakiwa kufikiriwa kupewa kipaumbele kwenye tenda za ujenzi wa
mabarabara, yenyewe kwanza kabla ya kampuni za kigeni, kwa kuwa ni ya mzawa na
hajawahi kuharibu.
Ritha
alirudi nchini akiwa peke yake, shule kichwani, pesa nyingi benki, na juhudi
zake. Mumewe alipofariki yeye ambaye alikuwa anajulikana kama mke kihalali,
akanufaika na mafao yote ya mumewe. Akachanganya na pesa aliyofanyia kazi kwa
shida sana na baridi kali akiwa nchini Canada, na pesa aliyopewa na wakweze
ikiwa imebeba siri nzito ambayo si baba yake Net ambaye ni mumewe Ritha,
aliyefariki, wala watoto wake, {Net na Maya} na utuuzima huo, walijua siri
hiyo. Siri hiyo alikufa nayo Mzee Cote na sasa amebaki nayo bibi yao tu.
Ritha au
mama Net, aliipenda pesa na kuijua. Alikuwa na malengo ambayo hayakuwahi kusimamishwa
na mtu au kitu. Lilipofika swala la maendeleo yake au malengo aliyojiwekea,
hata watoto wake walisubiri. Watoto hao wawili aliokuwa amezaa na huyo mwanaume
wa kicanada aliyefariki, aliwaacha kwa wakweze, wakitunzwa tokea watoto.
Kuanzia malazi, mavazi huku wakisomeshwa mashule ya gharama sana yeye akihangaikia
maendeleo yake.
Hata
kabla kifo cha mumewe, aliishi kama mwanamke aliyetimiza jukumu lake la kuzaa
kwa uchungu, kisha basi. Mumewe alitunza hao watoto wakati yeye akiwa na sababu
ya shule. Akasoma shahada zote, mumewe na wazazi wake wakisaidiana kulea hao
watoto wawili aliokuwa amezaa. Wakidhani shule itakapoisha ndipo atatulia,
haikuwa hivyo. Shule iliisha yakaja malengo yake mengine na mipango ambayo
iliwapelekea Maya na Net kuchukuliwa kuwa kama watoto wa huyo babu na bibi.
Mengi ya siri yalikuwa yakiendelea kwenye ndoa ya wazazi wao, lakini huyo babu
na bibi hawakuwahi kumwambia Net au Maya ukweli.
Watoto
hao walichojua ni mama anasoma, shule imemfunga, ndio maana baba anawalea peke
yake. Baba alipoanza kuugua, wakarudi kuishi kwa bibi na babu. Wakijua majukumu
ya mama ni mengi, inabidi bibi na babu kusaidia kuwalea wote watatu. Dady
ambaye ameanza kuugua na wao watoto. Kumbe lipo jambo kubwa na la siri
linaloendelea, wao wakiwa hawajui bibi na babu wakifunika ili watoto wakue kwa
amani kumbe Ritha, mama yao anahangaika kutimiza ndoto zake ambazo hazikuwahi
kusubiri.
Rita
alijua kupambana bila kuchoka. Ni wale wakina mama wanayoipenda na kuifurahia
pesa na mafanikio yao. Aliitafuta pesa bila hofu wala kujivunga. Ila kihalali
sio kama Tunda. Kwa kukaa darasani kwa shahada mbili za uhandisi, akaja
kuongeza na shahada ya mambo ya utawala kwenye biashara.
Jina
hilo la Cote, alilipenda na lilimletea heshima kubwa kila lilipotamkwa. Si
kwenye mabenki ambako walijua kiwango cha pesa kwenye maakaunti yake yote, hata
kwenye maofisi alikokuwa akifanya nao biashara. Mwanamke wa kwanza, msomi,
muhandisi mzuri mkubwa sana nchini. Anayegombania tenda za ujenzi wa barabara
nchini Tanzania pamoja na mashirika mageni tena makubwa! Hana sifa mbaya na
wala haaribu kazi yeyote. Pesa yake imenyooka, haina maswali. Hana mikopo
nchini Tanzania.
Mbali na
hapo, kwa mali na utajiri wa wakwe zake akijua kijana wake Net ndio mrithi wa
mamali yote ya wakwe zake. Akipata Net, ndio na yeye ataponea hapo hapo. Hata
akifilisika nchini Tanzania, anaweza akaishi kitajiri, asiwahi kuja kufanya
kazi tena maishani, kwa mali nyingi za wakwe zake. Leo Tunda aje aitwe na yeye
Cote! Hakuwa tayari hata kidogo.
Net
akiwa kijana mkubwa, yupo chuoni, hata kabla yakukutana na Tunda, ndipo akaanza kuishi na mama yake akiwa
hamfahamu au amefichwa ukweli wa huyo mama. Akijua anatekeleza agizo la baba
yake la kumtunza mkewe na Maya, kumbe Ritha alitumia akili kumtega Net.
Taratibu bila haraka, kila alipokuwa akija likizo kumsalimia mama yake chini
Tanzania, Ritha aliweka mitego yake. Bila kujijua, Net akanasa yeye mwenyewe na
kuchagua kuishi Tanzania moja kwa moja na mama yake, Canada akageuza kukawa
matembezi.
Haikuwa
ni mapenzi ya mama kwa mtoto tu, Ritha alijua atanufaika sana na mtoto huyo kwa
wakati huo kwa maadili mazuri aliyojengewa na babu na bibi yake. Kwa kazi na
majukumu mazito ya Ritha hapa nchini, kijana kama Net ndiye aliyejua atamfaa.
Ritha alijua mwanae huyo ni msomi, mchapakazi, mwadilifu, hawezi kumwibia au
kumgeuka kwa lolote. Akamuweka sawa kwa gia ya umama, mpaka Net akajikuta
anaacha maisha yake nchini Canada, malengo ya babu yake, na kuamua kumtumikia
mama yake bila Net mwenyewe kujua hila ya mama yake.
Akajikuta
anamtumikia mama yake kwa upendo mkubwa sana. Lakini Ritha alikuwa mwanamke
makini sana na kichwa yake ilikuwa ikifanya kazi kwa haraka. Anafikiria na
kuona mbali. Hilo hata wakwe zake walikiri kuwa anazo akili nzuri zakufikiria
na Mungu alimpa na za darasani pia.
Aliacha
watoto wake nchini Canada kwa wakwe zake kwa sababu zake yeye mwenyewe binafsi . Akaja kujitajirisha nchini Tanzania.
Mzee Cote na mkewe walikuwa wacha Mungu waliofanikiwa sana nchini Canada. Ni
watu waliojaliwa uadilifu na ndipo Net alikopata tabia njema. Matajiri wasio na
hila, waliotafuta mali kwa mikono yao. Japokuwa Ritha aliondoka nchini Canada
na kuwaacha hao watoto, lakini wao hawakutaka waje wamchukie mama yao au
watengane na mama yao.
Watoto
hao walipofikia umri mkubwa kidogo, hasa Net, kipindi cha likizo zao, babu na
bibi yao walikuwa wakihakikisha wanarudi nchini kumuona mama yao. Lakini tokea
mara ya kwanza Maya anafika nchini
Tanzania, hakukupenda hata kidogo. Hakutaka kabisa kuishi Tanzania, alidai
hawezi kuishi bila bibi na babu yake. Kwani Maya ni kama hakuwahi kulelewa na
mama yake kabisa.
Alizaliwa
mama yake akiwa anasoma. Akaishia kulelewa na baba yao. Kuanzia mchanga kabisa.
Baba yake ndiye aliyemlea Maya kwa uzima na ugonjwa. Kliniki na shule. Usiku na
mchana, Maya alilelewa na baba yake huku mara nyingi akipelekwa kwa bibi na
babu yake siku za ijumaa na kwenda kufuatwa siku za jumapili tokea mtoto, hata
wazazi wake walipokuwa wakisafiri, Maya alibakishwa kwa bibi yake na babu yake.
Hakujua maisha mengine mbali ya hao wazee. Na walimdekeza sana Maya, kitu
kilichokuwa kikimkera sana Mama Cote. Wazazi aliowatambua Maya ni bibi na babu
yake. Ambao waliwaita Nana na Papa. Hapo ndipo alipojua mapenzi ya wazazi
kutoka kwa wazee hao.
Mama Cote aamua kuvunja ukimya kwa mwanae, baada ya kumvaa Tunda.
Maisha
yaliendelea pale ofisini kana kwamba hakuna analojua Net, kuwa limetokea. Au
mama yake amelifanya kwa Tunda. Nidhamu kazini na heshima kwa mama yake
vikabaki vilevile. Hakumuuliza lile alilolifanya wala hakuonyesha hata dalili
kuwa anakitu na mama yake. Maisha yakaendelea kama kawaida pale kazini, lakini
bado alikuwa akiishi nyumbani kwake Salasala. Hakurudi nyumbani kwa mama yake.
Siku
hiyo kama kawaida yake yakuwahi ofisini, Net alifika ofisini kwake asubuhi na
mapema akaingia ofisini kwake nakuanza kuongea na Tunda huku akifanya shuguli
ndogo ndogo palepale mezani kwake. Akiwa anaongea naye, akasikia wafanyakazi
wengine wakisalimia nje ya ofisi yake. Akajua mama yake amefika.
Moja kwa
moja akaingia ofisini kwa Net. “Do you have a minute?” Mama yake akamuuliza
kama anao muda mfupi wa mazungumzo, ni kama kumtaka akate simu ili wazungumze.
“Yes boss!” Net akajibu kwa heshima tu na kumfanya mama yake acheke.
Wakati
wote alipokuwepo ofisini, Net alimtania mama yake kwa kumuita bosi. “Ukimaliza
kuongea na simu uje basi ofisini kwangu.” Mama yake akafunga mlango nakutoka. “Tunda! Bado upo?” “Nipo.” “Tutaongea baadaye, naona bosi
wangu ameshafika. Ameniita ofisini kwake.” “Haya. Kazi njema.” “Na wewe. Lakini
usisahau kuwa nakupenda.” “Nilikuwa nakaribia kusahau.” “Usithubutu.”
Tunda akacheka na kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net
aliingia ofisini kwa mama yake na tabasamu kubwa usoni. Mama yake akabaki
akimtizama. “Uliniita mama. Au sikukusikia vizuri?” “Nakusubiri uniulize.” Mama
yake akajibu. “Nikuulize nini tena!?” “Tunda hakukwambia?” “Juu ya nini? Maana
naongea na Tunda mambo mengi sana.” “Net Please!” “What mama!?” “Acha kunifanya
mimi mtoto mdogo. Niulize tu.” “Sijui unataka nikuulize nini mama yangu! Ni
kweli sijui!”
“Hakukwambia kwamba nilienda ofisini kwake?” “Oooh!
Ulivyokwenda na kutumia siri za madhabahuni kwa Bwana, alizokiri, akasemehewa,
Mungu akasema amezifuta dhambi zake zote na hatazikumbuka kamwe. Akamuahidi
Tunda kuziweka mbali dhambi zake kama mashariki na magharibi, nakumwambia ile
hati yake ya mashitaka haipo tena, kumbe wewe ambaye upo kanisani ukisema
unampenda Mungu na kutambua nguvu ya msalaba na damu ya Yesu, kumbe umebaki na
hati ya Tunda! Ndio umempokonya Mungu, unayo sasa unaitumia kumuadhibu Tunda!
Hilo ninalijua mama.” Yule mama akanywea kabisa.
“Sasa kwa nini hukuniuliza ukabaki kufanya kila
kitu kama kawaida tena vizuri?” “Kwanza sijui maisha mengine mbali na hivi.
Kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu mamlaka. Tukiwepo hapa ofisini wewe ni
kiongozi wangu. Umeniajiri na unanilipa mshahara. Hakuna jinsi naweza kufanya
tofauti, kwa kuwa sijui mbali ya hivi kuwa natakiwa nifanyaje! Ndivyo dad
alivyo nilea na babu kuweka msisitizo kwa vitendo mpaka na yeye anakufa.”
“Pili, nilifundishwa na mtu ninayempenda na
kumuamini kuwa, nisichanganye mambo ya familia na kazi. Ya nyumbani niache
nyumbani na kazini niache kazini. Na ukumbuke sisi hatuishi nyumba moja.” Mama
Cote alikumbuka kuwa ni yeye ndiye aliyemfundisha hivyo.
“Tatu niliogopa mama. Niliogopa kujiingiza kwenye
vita isiyonihusu na ninajua nitashindwa tu. Kwa kuwa unachokifanya wewe mama,
unagusa mboni ya jicho la Mungu. Unafanya kitu hatari sana mama yangu.
Unamchokoza Mungu aliyemtafuta Tunda na kumpata kwa gharama kubwa sana, ambayo
hata uuze mali zako zote huwezi kufikia thamani ya gharama Mungu aliyotumia
kumkomboa Tunda.”
“Kutoka kwenye maisha aliyokuwa akiishi, bila
wazazi wakumfundisha baya na jema, kama mimi na Maya tulivyobahatika. Akaishi
maisha machafu sana, Mungu akanituma kwa Tunda, ambaye nilimshuhudia kwa
kumfumania, si chini ya mara tatu, nilimfumania yule binti. Na kila nikikumbuka
sasa hivi sura nilizokuwa nikiziona wakati namfumania sio kama ya sasa
alipotangaziwa uhuru na Mungu.”
“Alionekana amechoka na anatumikishwa na ibilisi. Furaha
aliyonayo sasa hivi Tunda, wazi anaonekana si kazi ya mwanadamu mama, ni Mungu
ndiye aliyehusika kujenga moyo wa yule binti. Sasa nawezaje kugusa na kukilaani
kile Mungu alichokiita kitakatifu? Nawezaje kuanza vita ninayojua nitaishia
kushindwa tena kwa laana na adhabu juu?” Sio kuwa Mama Cote hakuwa akimjua
Mungu. Mumewe alikuwa mtu wa Mungu na wakweze pia walikuwa wakimjua Mungu kwa
kuishi maisha ya kikristo ya ukweli. Walimpokea akiwa msichana wa kawaida
kabisa. Wakaishi naye katika misingi ya kiMungu. Huyo mama alishaokoka lakini
kwa malengo akiwa na huyo baba yake Net.
“Naomba ufikirie na mimi Net. Kidogo tu.” Net
akabaki akimtizama mama yake. Mama Cote akaguna. “Nahisi ninawapenda wanangu
kupita kiasi. Ndio maana najitahidi kuwalinda na kila aina ya kitu ninachojua
kitakuja kuwaumiza. Nakupenda Net. Sitaki uje ushie pabaya.” “Na mimi nalijua
hilo mama, ndio maana nimeshindwa hata kukuchukia. Najua jinsi unavyonipenda na
jinsi unavyonilinda. Isingekuwa hivyo najua wazi nisingekuwa hapa na nisingekuwa
hivi nilivyo sasa hivi. Nakushukuru sana.” Net akamsogelea mama yake kwenye
meza aliyokuwa amekaa, akazungusha kiti chake, akambusu kichwani na kupiga
magoti.
“Nakupenda sana mama yangu na ninatamani kila mama
angekuwa kama wewe mama. Labda tusingepata watoto wa mitaani au labda
kusingekuwepo kwa asilimia kubwa mabinti kama kina Tunda. Tunda hakupata bahati
kama anayochezea Maya sasa hivi. Maya anaishi maisha kama ya Tunda, wakati
tumehangaika kufanya kila tuwezalo. Tunda amekubali kubadilika baada yakupata
msaada wa Kiroho na Kimwili. Ndio maana mimi nampa nafasi. Mbali ya hapo sijui
ni kwa nini nampenda Tunda kimapenzi. Ni kweli nampenda Tunda, mama. Na ninajua
ndiye atakayekuwa mke wangu.” “Nakuona jinsi ulivyobadilika.” Net akacheka.
“Ananifanya niwe nafuraha sana.” “Lakini kwa nini
usipate muda wakufikiria Net? Kwa nini unataka kuingia sehemu ambayo..”
“Nimefikiria mama.” Net akamkata mama yake kabla hajamaliza usemi wake. “Hapana
Net. Naomba ufikirie na mimi. Kaa hapo nchini tujiulize pamoja.” Net akaenda
kukaa.
“Huyu
Tunda anamaswali mengi kuliko jibu moja tu kuwa ameamua kuokoka. Kumbuka jinsi
alivyotusimulia jinsi alivyompata Gabriel. Ni binti ambaye anaonekana
akikusudia kumpata mwanaume, anatumia kila njia. Haonekaniki kama ni binti
ambaye anakusudia kutulia. Alianza na wale wazee wawili. Tena wote wenye pesa.
Kutoka kanisa hilohilo, akamtega Gabriel, kijana aliyesimama kwenye wokovu.
Asiyejua dhambi. Akamtega mpaka Gabriel akachanganyikiwa. Unakumbuka hali ya
Gabriel lakini?” “Nakumbuka.” Net akajibu.
“Sasa niambie ule msimamo wake wakuwa radhi
kumuacha mkewe, aliyeanza naye tokea zamani, na kutaka kumuoa Tunda, unatofauti
gani na wewe sasa hivi?” Net akacheka kidogo. “Usicheke Net. Gabriel alikuwa
hivyo hivyo! Akiwa tayari kuacha mali zote na watoto wake, ili awe na Tunda! Ni
vikao vingapi vilifanyika kumrudisha Gab kwa mkewe kutoka kwa Tunda? Mpaka wewe
ulipoingilia kati baada ya kumfumania na Tunda na kujua msichana mwenyewe ni
Tunda ambaye hana mwanaume mmoja. Ukazungumza na mwenzio mpaka akakuelewa,
akarudi kwenye ndoa yake. Sasa eti na wewe unaona mwenzio amepona, na wewe
unataka ukajiingize huko huko! Ni nini Net mwanangu?!”
“Mimi
nilimfahamu Tunda kabla ya wanaume wote hao kumchezea. Nimekutana na Tunda
baada ya kufukuzwa kwa mama yake aliyekuwa au asiyejua ukweli wote juu ya
Tunda. Mumewe au baba yake wa kambo Tunda aliyekuwa akitumia mwili wa Tunda
bila mama yake kujua. Tokea ni katoto mpaka msichana mkubwa ndani ya nyumba
hiyohiyo yule baba alikuwa akimtumia Tunda mpaka akashika mimba, mama yake
akamfanyia hila yakutoa mimba, nakumtelekeza hospitalini.” Net akaendelea
taratibu tu.
“Nimekutana
na Tunda akiwa amehamishiwa kwa shangazi yake, wakimtesa, Tunda hatizamiki, kwa
mateso na kunyanyaswa nyumbani kwa shangazi yake, hiyo ni miaka zaidi ya mitano
iliyopita. Lakini akiwa kwenye ile hali, mimi nilimpenda Tunda. Nilitaka
kumwambia, lakini wakampiga sana na kumsingizia swala la wizi, na kutelekezwa tena
hospitalini.”
“Akiwa
hajui pakwenda, kwani aliyemuuguza alikuwa baba yake ambaye aliishia jela,
alitoka pale na kumlazimu kuishi anayoishi.” “Lakini hayo si anakwambia Tunda
mwenyewe? Unajua ni stori gani aliyompa na Gabriel mpaka akafanikiwa kumuweka
kitandani?”
0 Comments:
Post a Comment