N |
![]() |
“Unampenda
sasa hivi baada ya watu wote kumkinahi huyo msichana!?” “Nampenda Tunda. Hata
babu anajua.” “Sasa babu yako hayupo hapa. Mimi ndiye nipo. Nimesema huyo
kahaba hatakaa akakanyaga humu ndani, na wala hutamuoa. Amekosa soko kwa wanaume
wote wa hapa Tanzania ndio anakufuata wewe! Haitakaa itokee Net. Labda kama
mimi sio mama yako.” “Najua ni habari mpya kwako mama. Unahitaji muda wa
kuzitafakari. Tunda ndiye mwanamke atakayekuwa mke wangu. Naomba upate muda wa
kutafakari na kukubali. Kwa kuwa hilo linatokea. Tena ninataka kumuoa haraka
sana.”
“Na
kwambia Net, labda kama mimi siye niliyekubeba tumboni miezi tisa. Hutamuoa
Tunda. Labda usubiri nife kwanza, ndipo umuoe huyo Malaya, lakini sio sasa.”
“Naona unahitaji muda mama. Na mimi nipo tayari kukupisha. Nahamia nyumbani
kwangu ili kukupa nafasi.” “Yaani unaniacha mimi hapa peke yangu sababu ya
Tunda!?” “Umesema hutaki kumuona Tunda anakanyaga nyumbani kwako. Na mimi
nimekuhakikishia nilazima nitamuoa Tunda. Sasa unafikiri itakuaje? Nakupa
nafasi ya kutafakari, utakapokuwa tayari kumpokea Tunda, unajua pakunipata mama
yangu.”
“Kweli
Net!?” “Nimeamua mama. Lazima nitamuoa Tunda. Unajua ninavyokupenda na
kukuheshimu. Lakini katika hili huna nafasi hata kidogo. Ni eitha ukubali
uungane nami katika kukamilisha furaha yangu, au utajumuika nasi hiyo siku
utakapo kuwa tayari. Haina haraka. Naelewa kuwa unahitaji muda, chukua muda
wowote unaotaka hapa duniani. Lakini ujue jinsi unavyochelewa ndivyo
utakavyopitwa na hatua muhimu sana kwenye maisha yangu, na ningetamani uwepo
kushuhudia. Maana nitaoa mara moja tu maishani, na nitamuoa Tunda.” Net
akaingia ndani na kuanza kufungasha vitu vyake huku akiviweka kwenye gari lake,
usiku uleule.
Alipomaliza,
akamsogelea mama yake, akambusu. “Nampenda sana Tunda, mama yangu. Na nimaamuzi
niliyoyofanya kwa muda mrefu sana, sijakurupuka. Nimempokea vile alivyo.
Nakuombea Mungu na wewe uweze kumsamehe kabisa na umpokee. Maana ndiye
atakayekuwa mke wangu.” Net akaondoka nakumuacha yule mama haamini kama Tunda
amefanikiwa kumchukulia wanaume wawili, aliobakiwa nao hapa duniani, ambao
aliwapenda na wenyewe walimuonyesha mapenzi na heshima zote.
Jumatatu!
Tunda
aliamshwa na ujumbe mzuri kutoka kwa Net. ‘Naweza
kukupigia?’ Tunda akamtumia huo ujumbe. Baada ya sekunde chache simu
yake ikaanza kuita. “Uliamka salama?” “Ndiyo. Asante
kwa ujumbe mzuri.” “Karibu. Mchana utakuwa na ratiba gani?” “Nitakuwepo tu
ofisini.” “Naweza kuja kukuchukua tukale wote chakula cha mchana?” Tunda alifurahi sana. Akacheka.
“Unacheka nini sasa?” “Bado siamini! Nina furaha ya ajabu ambayo
siwezi nikaeleza mtu akaelewa! Sikuwahi kufikiria kama naweza kuja kupendwa.”
“Nakupenda mpaka nakuonea wivu.” Net akajibu na kumfanya Tunda
azidi kucheka. “Nina mahali nakwenda asubuhi hii, sina
uhakika nitamaliza saa ngapi, lakini nikitoka tu nitakuja kukuchukua tukale
wote. Ila ukiona nachelewa, uende tu, nitakutoa jioni.” “As a date?” “Yes
Ma’am!” Tunda akazidi kucheka.
“Kwani siwezi kupata vyote?”
Tunda
akauliza kwa deko. “Wewe tu na ratiba yako. Ukiwa
tayari tutaenda kula wote chakula cha mchana na nitakutoa usiku.” “Basi
nakusubiri mpaka utoke.” “Sawa.” “Usisahau kupata kifungua kinywa, Net.”
“Nitachelewa. Sitaki kuwapa sababu ya kuninyima hiyo tenda.” “Pole. Nakuombea
ufanikiwe.” “Asante.” Wakaagana, lakini Tunda akabaki kitandani
akiendelea kurudia rudia ujumbe aliotumiwa na Net.
‘Hakuna usiku niliolala vizuri kama usiku wa siku ya kuamkia leo.
Nikijua wewe ni wangu na utakuwa wangu daima. Asante kwa kunikubali Tunda.
Nakupenda na ninaahidi kukupenda na kukulinda daima.
Net.’
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda
aliingia kuoga na kujitengeneza vizuri kama kawaida yake, akijiandaa kutoka na
Net kwa chakula cha mchana. Alijizungusha kwenye kioo kwa muda mrefu sana.
Alibadilisha muundo wa alivyoweka nywele, akabadilisha nguo zaidi ya mara tatu,
rangi ya kucha. Kila kitu hakuridhika nacho.
Simu
yake ikaanza kuita. “Huu sio wakati wakunipigia kabisa,
mama Penny. Nimechanganyikiwa.” “Kinacho kuchanganya nini?” “Sina nguo kabisa.”
“Umegawa zote!?” “Hapana bwana. Net anataka tutoke naye kwa chakula cha mchana
na usiku atanitoa pia.” “Kumbe na wewe unachanganywa na vitu vya kijinga kama
hivyo!? Hebu vaa utoke hapo kwenye kioo.” “Ulijuaje kama nipo kwenye kioo?”
Tunda akaanza kucheka.
“Hapa jasho linanitoka!” “Acha ujinga Tunda. Wewe ni mzuri tu. Na
chochote unachovaa kinakupendeza.” “Kweli dada?” “Sikudanganyi. Unavutia kwa
kila nguo unayoweka mwilini mwako. Sijawahi kukuona
umechukiza. Si ningeshakwambia?” “Kweli wewe ungeshaniambia.” Wote
wakacheka.
“Nagawa watoto mwenzio.” “Nipe Penny.” “Huyo ukimtaka hata sasa hivi
nenda kamchukue hukohuko shuleni.” “Kafanyaje tena msimamizi wangu wa harusi?”
“Si Julius kapita hapa nyumbani asubuhi hii, kuna mambo alikuwa anaongea na
Mchungaji, kawakuta mezani wanakunywa chai ili waende shule. Acha aanze
kumcheka Julius. Eti anamwambia, ‘Mwenzako auntie Tunda anaolewa na Mzungu!’ Nusu nikae chini.”
“Mungu wangu, Penny jamani!” “Ungemuonea huruma Julius jinsi
alivyoshtuka na kumgeukia Mchungaji kumuuliza.” “Uwii! Nilitaka kuja kuzungumza
naye mwenyewe.” Tunda
alikaa chini. “Sikutaka aje asikie kutoka kwa mtu mwingine jamani! Julius ali..” Tunda
akasita.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alikumbuka
jinsi Julius alivyomweleza kuwa anampenda. Alitangaza kwa kila mtu pale
kanisani kuwa Tunda ndiye atakuwa mkewe. Kanisa zima walijua mwisho wao itakuwa
ndoa tu. Julius alikuwa kijana aliyetulia sana na mcha Mungu, kitu kilichokuwa
kikimuogopesha sana Tunda. Ni kijana aliyekuwa na maadili mazuri,
hakutofautiana sana na Net.
Wakati
wote hakuwa akielewa hivi mtu unawezaje kumkosea Mungu kwa uzinzi! Mara kadhaa
kwenye maongezi yake na Tunda, alimuonyesha kushangazwa na watu wanaokuwa na
mahusiano ya kimapenzi kama si nje ya ndoa basi kabla ya ndoa. Tunda alimuona
ni mwanaume mzuri, mwenye juhudi, lakini alijua hawezi kuja kumfaa hata kidogo.
Alijua atashtuka sana akija kujua historia yake.
Hakumjibu
moja kwa moja hapana, lakini alimwambia wapeane muda wakufahamiana zaidi. Kila
Tunda alipokuwa akitaka kumweleza ukweli juu ya historia yake ya maisha,
alishindwa kutokana na mwelekeo wa mazungumzo ya Julius. Familia yake, ndugu
zake, jinsi walivyokuzwa na jinsi anavyoelewa misingi ya familia inavyotakiwa
kuwa. Utaratibu wa wazazi wake kutaka kufahamiana vizuri na wazazi wa kila mkwe
anayeletwa nyumbani kutambulishwa kwao kabla ya ndoa. Huo ulikuwa mtihani
mkubwa sana kwa Tunda.
Ukizingatia
baba yake yupo jela kwa kosa la wizi na mama yake ndiye hataki hata kumuona
Tunda kwa kosa la kulala na mumewe. Mama yake alimchafua Tunda kupita kiasi.
Alijua pindi ukweni watakapotaka kukutana na wazazi wake, haitawezekana kabisa
kueleza ukweli juu ya wazazi wake. Kwa hiyo aliendelea kumzungusha Julius ili
siku aje amwambie ukweli au yeye mwenyewe aje ajue historia yake na kuamua
kuachana naye kabisa.
Uzuri wa
Julius hakuwa na makuu. Kila kitu alimshirikisha Mchungaji wake, hata kukutana
na Tunda walikutana nyumbani kwa Mchungaji, au ofisini au sehemu ya hadharani
kwenye macho ya washirika wengine. Kwa hiyo hata hakuwa akimwambia Tunda maneno
yeyote yale ya kimapenzi, kwa hiyo hata Tunda hakuwa na hisia zozote zile za
kimapenzi juu yake kama Net aliyekuja kwa muda mfupi. Akaeleza nia yake
yakutaka awe mkewe. Kama tu Julius. Lakini Net yeye akambusu, kamkumbatia na
kumfariji katika hofu yake.
Kwa siku
moja tu, Net akawa ameshampita mbali sana Julius aliyekuwa na Tunda hapo
kanisani wakati wote na kutangaza kuwa Tunda ni mkewe. Japokuwa alikuwa amesoma
na kazi nzuri, lakini bado alikuwa na misingi mikali ile ya zamani kabisa ya
wokovu. Alifuata sheria zote za maadili ya kanisani. Hakuwahi kuwa na faragha
na Tunda.
Jumbe
alizokuwa akimtumia Tunda kila siku ni neno la Mungu, asubuhi na usiku muda wa
kulala. Akijitahidi sana atamtumia nyimbo za dini. Lakini alimsifia kila
alipomuona kuwa umependeza sana na kumkumbatia, tena wakiwepo watu. Basi.
Alikuwa kaka mtaratibu sana. Tunda hakutaka kumuumiza hata kidogo alitaka kuja
kujitoa taratibu akimtafutia sababu.
Sasa
akaja Net. Anayemjua ndani na nje. Net anaonyesha uozo wa Tunda unathamani kwa
kusaidia wengine. Kaka wakizungu. Mzuri. Akapata faragha. Kayasema yote.
Kamuweka Tunda mikononi na busu! Ahadi ya kuwa naye daima, ipo. Net amekiri
hajakurupuka. Alikuwa akimfuatilia na kumpenda tokea ni kahaba.
Net
amemsindikiza Tunda mpaka kwa baba yake gerezani. Akaonyesha heshima yote kwa
baba yake Tunda. Akamtamkia kuwa naye katika kila hatua yake hapo jela. Net
anamfahamu Tunda na uozo wake wote. Huwezi kumlinganisha na Julius hata kidogo.
Julius anamfahamu Tunda nadhifu ambaye anasubiri kwa wakati muafaka, atakuja
kupelekwa kwa wazazi wa Tunda ambao anadhani nao wapo na hali kama wazazi wake.
Kwa hakika Tunda alijua Julius hawezi kuja kuwa mumewe, lakini pia hakutaka
kumuumiza. Julius alikuwa mtaratibu na
muungwana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“We Tunda?” “Nipo. Namuwaza mchumba Juli.” “Pole mwaya. Utafanyaje?”
“Itabidi nimtafute na kwa mara ya kwanza nimwambie ukweli.” “Utakuwa umefanya
vizuri. Nitakupitia ofisini kwako. Nina safari ya huko.” “Umempikia kitafunio gani mchungaji?” “Sitaki kuombwa.” “Mimi
na wewe mama Penny!” “Nishakufungashia. Nitakupitishia. Usijali.” “Ndio maana
nakupenda.” “Acha kuniibia. Na utoke hapo kwenye kioo, uende kazini.”
Tunda akacheka na kukata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda
alifika ofisini, akakuta wafanyakazi wake walishafika. Alijawa furaha hata wao
waligundua hilo. Walianza kutaniana, baada ya muda kidogo zikaanza simu za
wateja na wengine wakaanza kuingia mle ofisini wakitaka kuonana na Tunda kwa
ushauri na kuona picha za kazi alizokwisha fanya. Wengine walikuwa wakiangalia
picha, wengine wakiongea nao huku wakiuliza maswali. Pakawa na shuguli nyingi
tu asubuhi hiyo.
Mama
Cote kwa Tunda.
Wakiwa
kila mmoja akihudumia wateja wake, Mama Cote akaingia pale ofisini kwao. Tunda
alipomuona aliwaomba wateja aliokuwa akizungumza nao, wamsubiri kidogo, akamsogelea
Mama Cote. “Shikamoo Mama.”
“Umenivunjia uchumba wangu. Sasa hivi ningekuwa nimeshaolewa na mimi.
Isingekuwa mama yako kukutoa mimba, ungekuwa umezaa na baba yako. Ushajiuliza
umevunja ndoa ngapi mpaka sasa hivi? Umeshajiuliza ni maafa kiasi gani
umesababisha kwenye jamii?” Tunda alikuwa kwenye mshtuko, akabaki ameduaa.
“Au umeshajiuliza ni majeraha kiasi gani
umesababisha kwenye maisha ya watu? Kana kwamba haitoshi umeingia kwenye maisha
ya Net! Kijana mdogo asiye na hatia. Na
yeye unataka kumuongeza kwenye idadi ya wanaume utakao kuwa umewavulia nguo
hapa duniani! Wameshafika wangapi? Eti Tunda?” Wateja wote walibaki
wakimsikiliza yule mama huku wakimwangalia Tunda.
“Unataka kulala na baba na mtoto wake!? Yule
mchumba wangu mimi ni kama baba yake Net. Umelala naye, halafu sasa hivi
umemgeukia mwanae! Huna kinyaa!? Basi kama hilo hulijali, umelipuuza, basi
kumbuka mahusiano uliyokuwa na kaka yake, Gabriel! Umemchanganya Gab karibia
amuache mkewe kwa ajili yako, mpaka watu tukafunga na kuomba ndio Gab akashtuka
na kukujua kama wewe ni shetani.” Tunda kimya.
“Jamani wewe binti! Wewe ni mchafu wa kiasi gani?
Umenyimwa aibu na huruma kabisa!
Umeingia mpaka kwenye nyumba ya Mungu! Umeangusha wazee wakanisa. Gab alikuwa
kijana ambaye ametulia kwenye ndoa yake, mcha Mungu, lakini umefanikiwa
kumuangusha dhambini yule kijana!”
“Naomba umuhurumie Net, tafadhali. Amejitunza
mwanangu maishani mwake kote. Leo unataka kumuharibia mwanangu maisha! Na
ninajua wazi, umeokoka kwa ajili yake. Umeokoka ili umpate mwanangu. Tunda
muogope Mungu wewe mtoto! Hata kama huna dhamira, lakini nataka kukwambia Mungu
yupo na anakuona kwa unalotaka kumfanyia Net. Nakuapia kweli kabisa Tunda,
Mungu atakuadhibu kwa ukatili na unyama unaotaka kumfanyia mtoto wangu.
Hajafaidi maisha hata kidogo, leo unataka kuja kumuua na UKIMWI!”
0 Comments:
Post a Comment