Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! - Sehemu ya 22. - Naomi Simulizi

Nilipotea! - Sehemu ya 22.


S

iku inayofuata, Tunda akiwa ukumbini anapamba, mida ya saa mbili asubuhi, mmoja wa wafanyakazi wake, Jazi, alimpigia simu kumwambia ametoka kuzungumza na simu ya wateja wake wa siku iliyopita, wakina Mgeekwa, wanamuomba wakutane tena jioni yake, walishafikia uamuzi. Jazi alikuwa ameandika kila kitu chini, muda na mahali. Tunda akamtaka huyo huyo Jazi ndio aende kumuwakilisha muda huo utakapofika. Siku za jumamosi usingeweza kumuweka Tunda kwenye kikao chochote. Anakuwa busy kupita kiasi.

Ilipofika jioni Jazi alitoka kwenda kumuwakilisha Tunda kule kwa wale wanakamati alipokuwepo Net na Gabriel. Jazi alitoka pale akiwa amejiandaa kwenda kukamilisha oda, lakini alipofika pale walimkataa kabisa. “Tunda yupo na majukumu mengine. Chochote mtakachoniambia mimi, kitamfikia na yeye.” “Hapana. Kamwambie Tunda aje yeye mwenyewe. Na sisi pia ni wateja. Tunataka huduma yake. Kwani ni bure? Na sisi tutamlipa.” “Siku za jumamosi inakuwa ngumu sana kumpata Tunda jamani! Naomba mniamini kuwa, mkiniona mimi, ndio mmemuona Tunda.” “Bwana wee! Sisi tunamtaka Tunda. Wewe nenda zako.” Wote wakamshambulia Jazi kwa maneno wakimtaka Tunda, mwishowe Jazi akaondoka.

Alimpigia simu Tunda akiwa analia kuwa amedhalilika sana. “Usichukie Jazi, ndio changamoto za kazi hizo.” “Wamenifukuza, kama..” “Kwanza ujue wengi wao pale ni walevi. Wala usiumie. Umenielewa Jazi? Nitawapigia simu baadaye kuzungumza nao. Wewe rudi nyumbani ukapumzike. Pole sana.” Siku ya jumamosi ilikuwa siku ambayo Tunda anakuwa na kazi mbili au tatu. Sasa jumamosi hiyo alikuwa akipamba kumbi tatu, tena zote kubwa. Tangia saa 9 usiku au alfajiri, Tunda alishafika kazini kwenye ukumbi wa kwanza.

Alichokuwa akifanya ili kumaliza kwa wakati, kila ukumbi alitanguliza vijana wake waanze kupamba kisha yeye alipita kumalizia. Hakuwa akipokea simu ya mtu yeyote isipokuwa wafanyakazi wake na mama Penny, basi. Ile simu ambayo namba alikuwa akiwapa wateja, alikuwa hata hagusi siku hizo za jumamosi. Kwanza hakuwa akitoa kwenye pochi mpaka akimaliza kazi, ndipo ataitoa tena kwa ajili ya kumpigia simu muhusika, afike hapo, amkabidhi huo ukumbi, basi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku hiyo alishinda kwenye kazi mpaka ilipofika usiku ndipo aliporudi nyumbani kwake. Siku hiyo hakuwa hata na hamu ya chakula. Aliingia kuoga akatoka na kujitupia kitandani kwake. Ni kweli alikuwa akitengeneza pesa, lakini alihitajika nidhamu ya hali ya juu kwenye kazi hiyo. Kwa kuwa alikuwa akichukua kazi nyingi, ilibidi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha hakuna anapokosea, na hakuna anayemuudhi. Iwe wanaolipia pesa nyingi au wale wenye kutaka kupambiwa kwa kawaida tu, kote alihakikisha anaridhisha wateja wake. Na mara nyingi siku za jumamosi ndio alikuwa na kazi nyingi sana kuliko siku nyingine zote.

Akiwa anakaribia kupitiwa na usingizi, akasikia mlio wa sauti wa simu yake kuashiria ujumbe umeingia. Alijichukia kwa kutokuzima ile simu kabisa. Bila kutaka kuwasha taa, alinyoosha mkono kwenye meza ndogo pembeni ya kitanda chake, ili kuivuta simu yake na kuizima kabisa, ili apumzike.

Wakati anataka kuizima kabisa ile simu, akaonelea aone ule ujumbe ambao kwanza umeingia muda ule, ukawa umemtoa kwenye usingizi. Alitaka kusoma kesho yake lakini akaona amjue huyo msumbufu wake. “Anataka nini usiku huu jamani!” Tunda akajiuliza kwa hasira. Akasoma. ‘Najua una mambo mengi Tunda, lakini naomba utafute muda tuzungumze. Net.’ Tunda aliruka pale kitandani, akakaa. Akaamua kujibu. ‘Tunaweza kuongea wakati wowote.’ ‘Lakini leo hukupokea simu zangu kabisa, Tunda!’ ‘Samahani Net, sikujua kama ni wewe. Siku za jumamosi nakuwa na kazi nyingi sana. Kama simu siifahamu huwa sipokei. Sasa hivi ndio narudi nyumbani. Nimechoka kweli, hapa nipo kitandani.’ ‘Pole.’ ‘Asante.’ Tunda akajibu, kisha akatulia.

‘Lini sasa unaweza kuwa na nafasi?’ Net akatuma ujumbe mwingine. ‘Naweza kukupigia sasa hivi?’ Tunda akauliza. Mara akaona simu yake ikiita. “Net!” “Vipi?” “Safi tu. Nimeona ni heri tuongee tu kwa simu.” “Hutaki kuniona tena!?” “Hapana. Sio hivyo Net.” “Hivi unakumbuka uliniacha sehemu ya kuegesha magari?” Tunda akafunga macho na kuvuta kumbukumbu.

“Lakini nilikuaga Net.” “Unakumbuka mimi kukuaga?” “Hapana. Naomba unisamehe. Nimekuwa na mambo mengi kweli! Yananivuruga akili.” “Nini tena?” “Nahangaika kumtoa baba jela, anaumwa. Natamani atoke mapema ili akatibiwe.” “Umepata wakili mzuri?” Net akauliza kuonyesha kujali.

“Nafikiri hivyo. Sijui. Ndiyo yupo anahangaikia kufufa hiyo kesi. Ila baba amedhoofu sana, Net. Anatakiwa kutoka jela mapema ili awahi matibabu. Kesho nataka niende nikamuone tena.” “Pole sana. Tunaweza kwenda wote kumtizama?” “Twende wote jela!?” Tunda akauliza kwa mshangao.

“Si ndipo alipo?” Net akauliza kiustarabu tu. “Ndiyo. Bado yupo jela.” Akajibu kwa upole. “Basi tutaenda wote.” “Asante Net.” “Unaabudu kanisa gani?” Tunda akamuelekeza na kumwambia ni muda gani wanaanza ibada. “Basi nitakuja kanisani kwenu kukutembelea.” “Nitafurahi kukuona Net. Karibu.” “Asante. Basi ngoja nikuache upumzike, nitakuona kesho.” “Asante, usiku mwema.” “Na wewe pia.”  Waliagana, Tunda akabaki akijiuliza maswali mawili matatu, mwishowe akaonelea alale tu.

Jumapili. Net Kanisani kwa Kina Tunda.

Siku hiyo ya jumapili, alimkuta Net ameshafika kanisani akimsubiri nje ya gari yake. Tunda akaegesha gari yake pembeni ya alipokuwa amegesha Net gari yake. Kama kawaida yake hakujikosea. Alikuwa amependeza haswa. Alishuka akiwa ameshikilia pochi yake na bibilia yake mkononi. Akamsalimia Net huku akijaribu kuweka vitu vingine kama simu yake ya mkononi na funguo za gari ndani ya pochi yake.

“Karibu sana, hapa ndipo Mungu alinipa familia nyingine. Ni watu wazuri sana. Utamfurahia Mchungaji wetu na mkewe. Wamefanya hapa kanisani kukawa kimbilio la wengi. Wanahimiza sana vijana kufanya kazi kwa bidii. Mkewe ndiye mwenye kipaji cha kugundua vipaji vya watu na kuviendeleza. Yeye ndiye amenisukuma kwenye hii kazi ninayofanya, tena nikiwa na hofu nyingi kweli.” “Auntie Tunda!” Watoto wa Mchungaji walimkimbilia Tunda. Penny na mdogo wake Pendo.

“Dady ametufukuza ofisini kwake.” Tunda akacheka. “Huu ni muda wenu wa Sunday School. Muwahi msichelewe.” “Huyo ni mzungu?” Mmoja wao ambaye Tunda alimlaumu sana mama yake kuwa alimuharibu mwanae kwa vituko, Penny alimnong’oneza hilo swali Tunda lakini aliweza kusikika. “Na anasikia Kiswahili.” Tunda akamjibu, wote wakacheka.

“Umekamatwa leo na maswali yako yasiyoisha we Penny!” Mdogo wake alimwambia ndugu yake huku akimcheka. “Shikamoo. Naitwa Penny, kipenzi cha dady.” Penny akamwambia Net. Net alikuwa akicheka tu. “Muongo, mimi ndiye kipenzi cha dad and by the way, dady yetu ndiye bosi hapa.” Net akazidi kucheka.

“Nilikwambia hili kanisa lina vituko! Sasa bado hujakutana na wazazi wao. Ndio utachoka zaidi. Haya naomba muende Sunday school.” Tunda aliwashika vichwa na kuwageuza, kama kuwaelekezea upande lilipokuwepo darasa lao kwa kuwasukuma kidogo.

“Hata hatujamjua mgeni wakizungu sababu yako!” Walimsikia mdogo wake Penny akimlaumu Penny. “Ni mchumba wa auntie Tunda?” Pendo akamuuliza Penny, “Wewe! Akikusikia anko Juli, atakupiga makwenzi. Anko Juli ndio mchumba wa auntie Tunda.” “Muongo.” “Kweli.” “Muongo.” “Kweli tena. Nilimsikia mama akimwambia dady.” Waliwasikia wale watoto wakibishana huku wakielekea darasani kwao. Walijawa fujo na kelele kupita kiasi. Tunda alibaki akitingisha kichwa huku akicheka.

“Shalom!” Tunda na Net walishtuliwa na sauti iliyokuwa ikiwasalimia, maana akili zao zilikuwa zimezama kwenye mazungumzo ya wale watoto. Wote wakageuka. “Amina Juli. Shalom!” Tunda akajibu. Juli akamsogelea na kumkumbatia Tunda huku akimtizama kwa tabasamu. “Umependeza sana Tunda.” Tunda akacheka kidogo. “Usingenisifia ningeshangaa!” Wote wawili wakacheka.

“Ni kweli bwana. Au hutaki nikupe sifa zako?” “Hapana, nashukuru. Juli! Huyu anaitwa Net, Net huyu anaitwa Julius au Juli kama wengi tulivyozoea kumwita.” Walipeana mikono. “Net ndiye mtu aliyenitoa duniani nakunileta kanisani.” Tunda akaongeza huo utambulisho mfupi tu. “Tunashukuru bwana kwa kutuletea kondoo. Maana kuna vifaa vingine muhimu sana kanisani, ndio kina Tunda.” Juli aliongeza huku akicheka. Juli na Tunda walitaniana kidogo mbele ya Net, waliposikia nyimbo zimeanza kusikika kanisani, Tunda akamwambia Net waingie kanisani, ibada imeanza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda alikaa na Net mpaka mwisho wa ibada, ndipo walipotoka na kwenda kusalimiana na Mchungaji na mkewe ofisini. “Wote nilisha waambia juu ya Net. Nafikiri mnakumbuka.” Tunda akaongea kwa hakika akijua lazima Mchungaji na mkewe watakuwa wakimkumbuka tu Net. Wakabaki wametoa macho. “Jamani nyinyi! Net!? Pale kanisani alijitambulisha kama Nathaniel Cote, lakini kwa kifupi ni Net. Net yule niliyewaambia habari zake!” Tunda akashangaa wanawezaje kumsahau Net!

“Tunakumbuka sana. Lakini sikumbuki kama ulituambia kama ni mzungu!” Mama Penny akajibu na kumgeukia mumewe. “Au wewe baba Paroko unataarifa hizo?” “Hata kidogo.” Tunda na Net wakaanza kucheka.

“Unaposimulia jambo, usiwe unaondoa mambo ya muhimu.” “Sasa swala la uzungu wa Net ungeongeza nini kwenye ushuhuda wangu?” “Usitutanie kabisa wewe Tunda! Kuna uzito wake mkubwa sana. Wewe kutolewa jalalani na Mzungu na kuketishwa na wakubwa kama sisi, sio kitu kidogo!” “Mama Penny wewe! ” Tunda alibaki akimshangaa.

“Kabisa!” Kama kawaida ya mumewe kuunga mkono kila kitu anachoongea mkewe. Net alikuwa akicheka tu. “Kwanza ujue Net anasikia na kuongea Kiswahili fasaha kama mtu aliyezaliwa Tanzania. Yaani hata hapa anawasikia kila kitu.” Wakatulia kidogo. “Eti ni kweli?” Mama Penny akauliza huku akimwangalia Net ambaye yeye alikuwa akicheka muda wote. “Sasa unafikiri ile salamu ya pale kanisani alikariri?” Mama Penny akamtizama Net na mumewe. “Tunajua sana kama anajua kiswahili.” Mumewe akasaidia, wote wakacheka.

“Jamani nimefurahi kuona Tunda yupo na watu wanao mjali.” Ikabidi Net azungumze tu. “Sisi tumefurahi kukufahamu na kuja kututembelea Net. Hatujawahi kupata rafiki wa kizungu tangia tuanze hii huduma.” “Jamani Mama Penny wewe!” Tunda akazidi kushangaa. “Naongea moyo wangu. Kwa nini nisiseme ukweli?” “Mimi ndio kabisaaa, sijawahi kuwa na rafiki mzungu tokea nizaliwe.” Mchungaji akaongeza. Wote wakacheka.

“Net, tuondoke zetu.” Tunda akasimama. “Lazima twende naye nyumbani akale.” “Nina haraka mama Penny!” Tunda alitaka kukataa. “Haituhusu sisi. Ulimleta mwenyewe. Kama unaharaka ndio mtangulie nyumbani, sisi tutawakuta huko huko. Huwezi kumleta mgeni halafu ukaishia naye ofisini.” Mama Mchungaji akajibu.

“Atakuja nyumbani siku nyingine.” “Mbona hilo tunalifahamu? Na tutahakikisha lazima aje nyumbani siku nyingine. Leo haiwezi ikawa mwisho wake wakufika nyumbani kwetu” Tunda akatingisha kichwa, huku akiguna. Alijua jinsi mama Penny alivyo king’ang’anizi. “Twende Net mwaya.” “Ukajisikie nyumbani Net. Sisi tuko nyuma yenu tunakuja. Ngoja nikusanye vifaranga vyangu vyote. Tunakuja sasa hivi.” “Asante sana.” Net akashukuru wakatoka. 

Tunda na Net kwenye gari.

Wote wakajikuta wakianza kucheka tena mara ya kutoka hapo ofisini. “Huwa wanakuwa serious hawa?” Net akauliza. “Heri Mchungaji kidogo huwa anajitahidi, lakini huyo mkewe!  Sijawahi kumuona. Lakini anaupendo sana. Hana roho ya wivu hata kidogo, anapenda kila mtu afanikiwe.” Waliongozana mpaka kwenye magari yao.

          “Unataka tuendeshe magari mawili kama tupo kwenye msafara bwana! Njoo upande kwenye gari yangu, tutakuja kuchukua gari yako baadaye.” Tunda akacheka, akaona ni wazo zuri. Akaingia kwenye gari ya Net. Alipokaa tu, Net akamvuta mkono wake wakushoto akaangalia vidole vyake. “Mbona Juli hajaweka pete bado!?” Tunda akatulia kidogo kama anayefikiria.

“Hatujafika huko.” Tunda akajibu baada yakumuona Net akimtizama. “Mmefikia wapi? Maana naona mpaka mnakumbatiana.” “Nisalamu tu, Net jamani!” “Salamu yenu nyinyi wawili tu!? Mnasalimiana kwa kukumbatiana?” Tunda akatulia tena kama anayefikiria kwa kuvuta kumbukumbu. “Eti Tunda?” Net akauliza tena na kuwasha gari kisha akaondoa gari pale kanisani.

“Watu wengi huwa wanasalimiana pale kanisani kwa kukumbatiana.” “Oooh! Basi inabidi nirudi tena. Maana leo sikubahatika kukumbatiwa kabisa, na wala sikubahatika kuona watu wengine walio kumbatiana. Hata Juli mwenyewe hakunikumbatia na mimi ila wewe tu wakati tulikuwa tumesimama wote.” Tunda akanyamaza.

“Kwa hiyo sasa hivi mpo kwenye hatua gani ya mahusiano?” “Hatujafika popote.” “Anatambulika mpaka kwa viongozi wako kama ni mchumba wako, bado hamjafika popote!?” “Alinigusia tu nia yake yakutaka kunioa.” Tunda akaongea tu hivyo na kunyamaza, Net akamgeukia kama kumwambia aendelee, anamsikiliza.

“Ndio na mimi nikamwambia mama Mchungaji, au tuseme mama Penny. Yeye ndio kama rafiki yangu au mshauri wangu, nafikiri watoto walimsikia wakati akimwambia mumewe. Lakini hamna mwendelezo wowote.” “Unamaanisha nini?” “Tuliishia hapo hapo tu, Net!” “Mbona sikuelewi Tunda? Mtu alikufuata kukueleza nia ya kutaka kukuoa. Halafu unaniambia mliishia hapo hapo! Inamaana mmeishia hapo hapo kama wachumba,  au kama mke na mume au?” “Net jamani! Nilishindwa kitu chakumjibu.” Net akamgeukia huku amekunja uso.

“Huyu kaka anamtaka Tunda asiyemfahamu hata kidogo. Nilijua anataka kujiingiza kwa mtu asiyemfahamu kabisa. Anamuona Tunda aliyesimama pale, lakini hamjui Tunda wa kweli na maisha niliyoishi nyuma. Najua wazi Mungu amenisamehe, lakini hapa duniani mambo yote niliyofanya bado yapo kwenye akili na miayo ya watu, Net.”

“Mama yangu mpaka leo sina mahusiano naye kwa kosa la kutembea na mumewe na wanawake wengine wengi ambao nimevunja ndoa zao au nimeathiri ndoa zao kwa namna moja au nyingine. Ndugu zangu wenyewe hawaniamini hata na marafiki zao wakiume! Hebu niambie Net, huyu Julius siku moja akitaka kuja kukutana na familia yangu nampeleka wapi?” Tunda akauliza kwa upole.

“Wewe ulikaa na ndugu zangu kwa muda mfupi sana, lakini waliweza kukwambia mabaya yangu yote. Japo mengine ni ya uongo, lakini yanasababishwa na chuki waliyonayo juu yangu kwa yale niliyo watendea. Naogopa hata kufikiria swala la mahusiano na mtu yeyote yule, kuhofia kuja kunilazimu kueleza historia yangu ya aibu au chafu kama vile! Sitaki nije nianze kupenda, halafu nikaumizwa kwa maisha niliyoishi zamani.”

“Ni ngumu kuja kuishi na mwanaume halafu akaja kukuamini kwa asilimia zote kama ambavyo angemuheshimu mwanamke aliyeanza naye mahusiano ya kimapenzi. Namaanisha labda msichana aliyemkuta bikra. Kwangu itakuwa ngumu Net. Nilishaharibu sana maisha yangu.”

“Nikichelewa kurudi nyumbani, atahisi nimetoka kwa mwanaume mwingine. Nikichelewa kupokea simu yake, au niongea na simu na mwanaume yeyote asiye mfahamu yeye, au hata nikiwa na mahusiano ya kawaida tu na mwanaume mwingine, huyo mume au mchumba wangu atahisi vinginevyo. Kuja kuwa na mahusiano kwa upande wangu ni kukubali kuingia kwenye maisha yatakayoninyima uhuru, furaha, na naona nitakuwa najiingiza kwenye matatizo tu.”

“Nimeamua niishi hivihivi, hata hivyo nimeshakinahiwa, halafu ninahofu yakuja kuingia kwenye ndoa nikashindwa kuzaa. Nitateseka sana.” “Kwa nini?” Net akauliza.

“Mama aliponitoa ile mimba, sijui walinitoaje! Sijui kama haikuathiri kizazi changu au la. Sitaki kuingia kwenye ndoa, nikiwa na wasiwasi huu.” “Kwani hukuwahi kushika mimba tena?” Net akauliza huku akimtizama Tunda. Tunda akainama.

“Ni Baba Tom tu, ndiye mwanaume pekee niliye lala naye bila kondom. Alikuwa hataki hata kusikia neno kondom. Ila baada yakutoka pale, au baada ya pale kila mwanaume niliyewahi kulala naye, hata Sadiki nilihakikisha natumia kondom kila wakati. Sikuwahi au sikurudi tena kutotumia kondom. Hata hivyo wengi nilihakikisha nawamaliza nguvu zakutoweza kuniingilia. Niliishia kuwa..” Tunda akanyamaza. Akageukia dirishani, nakuanza kufuta machozi.

“Nisikilize Tunda. Hayo nimaisha uliyoishi zamani. Ulishakiri, Mungu amekusamehe. Hutakiwi kuendelea kuumia kwa ajili ya hayo. Huko umeshatoka, na umeamua kutokurudi tena. Naomba utafute jinsi yakutumia hayo maisha kuwa msaada kwa wengine. Nilazima ubadilishe kutoka kuwa aibu na kuwa msaada kwa mtu mwingine. Ukikubali kuwa ni kwa ajili yako tu, na ukakubali ikutese, kweli itakuwa shida ulizopitia ni bure kabisa. Umenisikia?”  Tunda alikuwa akiendelea kulia.

Net akamvuta mkono wake aliokuwa akijifuta machozi akaubusu kiganjani. Ilikuwa ni mara ya kwanza Net kumbusu Tunda. Mwili mzima wa Tunda ulisisimka. Hakuwahi kujisikia vile tokea anazaliwa. Eti mtu kumbembeleza akiwa mkosaji! Kwanza huo mwili wengi waliugusa ili kujinufaisha nao. Wakike kwa wakiume. Sasa leo anapokea busu la faraja! Ilikuwa faraja ya pekee kwake. Tunda hakuamini kupata busu kutoka kwa Net anayemfahamu akiwa mchafu vile! Hata hivyo ni Net jamani!

“Huna haja yakulia kabisa Tunda. Lazima tugeuze yale maisha yako kuwa msaada kwa wengine.” “Nitafanyaje?” Tunda akauliza huku akifuta machozi, hata yeye hakuwa anaelewa alipitaje kule kote. Aliwezaje!? Hapo alipotulia ndipo picha ya kila kitu alichofanya nyuma ikaanza kumjia. Wakati mwingine aliweza kuhudumia wanaume hata watatu kwa siku moja!

Kinyaa, shida na mateso yote aliweza kuyapuuza akawa akifanya kama mchezo mwepesi sana. ‘Niliwezaje!?’ Ni swali alilokuwa akijiuliza kila wakati Tunda bila kupata jibu. Achilia mbali kujidhalilisha alikopitia bila kufanikiwa. Ilikuwa ni kama chombo cha thamani sana, kinachostahili kutumiwa kuwekea chakula hata cha wafalme, halafu chombo hicho hicho umpe mtoto mdogo, asiyejua thamani yake, achee nje kwenye matope.

“Kwa kuwa habari mbaya zinazagaa kwa haraka,” Net akaendelea. “lazima wewe mwenyewe uwe msemaji wa habari zako. Geuza kuwa msaada kwa mabinti na vijana. Huwezi kujua hata wazazi wengine wanaweza kupona.” “Kweli Net!?” “Kabisa. Acha watu wakufahamu kwa yale maisha ya zamani, na waone kazi kubwa Mungu aliyofanya ndani yako. Hakuna mwanadamu ambaye angeweza kukutoa ulipokuwa Tunda, isipokuwa Yesu mwenyewe. Ulikuwa umefungwa na nguvu za giza tokea mtoto unaishi na baba Tom. Ufahamu wako ulitekwa, ulikuwa ukitumikia falme nyingine kabisa. Kwa nini usitumie kile ulichofanyiwa na Mungu kufungua wengine?” Net akaendelea taratibu.

“Wapo wengi wanapitia ulipopita wewe, lakini wanakosa msaada. Ona jinsi ulivyofanikiwa kwenye maisha kwa kukubali kutumia kipaji Mungu alichokupa tena bila shule ya maana. Lazima kutumia maisha yako yaliyopita kwa ushindi. Yale shetani aliyokuwa amekusudia kuwa mabaya kwako, Mungu amekugeuzia kuwa mema. Sasa kwa nini unalia tena? Lazima ufurahie kama mshindi na si uliyeshindwa. Eti Tunda?” Machozi ya Tunda yalikauka gafla, akajawa tabasamu kubwa usoni mwake.

“Nilimiss hayo macho na hilo tabasamu!” Tunda akajifunika uso wake na kucheka kwa sauti. Net akaendelea kumfariji, huku akiendesha mpaka Tunda akafunguka kabisa. “Unajua Net, Mungu anakutumia sana katika maisha yangu? Kila wakati huwa unanitoa sehemu moja na kunipeleka sehemu ya juu! Isingekuwa wewe unajua sasa hivi nisingekuwa hapa?” “Ndio nakushangaa sasa unavyokuwa unanikimbia kila wakati!” Tunda akacheka.

“Sijakukimbia bwana!” “Unanipuuza sana Tunda! Hunichukulii maanani hata kidogo.” “Jamani Net!” “Kweli Tunda. Hebu niambie ni juhudi gani umefanya kunitafuta tokea ulipoondoka Arusha?” Tunda akabaki kimya.

“Inawezekana Arusha ni mbali sana. Lakini tulikutana majuzi pale hotelini, ukaniacha sehemu yakuegesha magari! Niambie ukweli Tunda, hivi ulikuwa hata na mpango wakuja kunitafuta tena?” Tunda alijisikia vibaya sana. “Nilijua tungeonana tu.” “Kwa njia gani, Tunda? Maana hata simu yangu hukuomba na kikao kilichofuata ulimtuma mfanyakazi wako aje kwenye kikao sio wewe mwenyewe. Mimi ndio nahangaika kulazimisha mahusiano ambayo hata sijui niite mahusiano au sijui niitaje.” “Ni mahusiano Net.” “Ni mahusiano gani haya Tunda!? Mimi ndiye wakukutafuta kila wakati, lakini mwenzangu ni kama nakusumbua tu.”

“Hunisumbui hata kidogo Net.” “Unauhakika Tunda?” Tunda akatulia kidogo. “Nikwambie ukweli Net?” “Niambie tu.” “Naomba nielewe kabisa. Nakosa ujasiri kwako.” “Kwangu tena!?” “Kabisa Net. Sijui nikujishtukia au vipi? Najiona nakuchosha na kukugharimu sana. Kwa hiyo wakati mwingine najiambia kukaa mbali na mimi ni kama unapumzika. Naona kama kazi yako uliyoifanya kwenye maisha yangu ni kama imetosha, sasa hivi nalazimika mimi mwenyewe kusimama, sio kukuchosha zaidi. Sijui umenielewa?” Walifika nyumbani kwa Mchungaji.

“Tutazungumza vizuri baadaye.”  Net aliongea hivyo wakati anaegesha gari. “Lakini naomba uniamini kuwa hunichoshi Net. Nisamehe pale unapoona ni kama nakupuuza. Sasa hivi nipo kwenye wakati wa hekaheka. Siwezi kusema mgumu, ila ni kama mtoto ambaye yupo kwenye kutambaa, lakini mazingira yanamtaka akimbie. Nina majukumu ambayo yote yananiangalia mimi na lazima niyatimize.”

“Siku kama ya leo ndio huwa napumzika. Ila siku nyingine, akili inabidi kufanya kazi kwa haraka ili kuweza kuchukua hatua na nisiharibu.” “Am so proud of you Tunda. Najivunia sana. Nilifurahi sana kukuona juzi ukiongea kwa kujiamini. Tena ukijinadi kipaji chako!” “Yote hiyo ni wewe Net.” Net akacheka.

“Na wewe Tunda. Ulikubali na kuchukua hatua. Nilijua jinsi wanaume walivyokuwa wakikusumbua tulivyokuwa pamoja kule Arusha. Wenye pesa na wafanyabiashara wakubwa. Lakini ulitulia. Umenifurahisha.” “Asante.” Tunda akacheka taratibu na kumwangalia Net. “Umenisamehe sasa?” Tunda akauliza kwa kujali akibembeleza. “Tutaongea zaidi baadaye. Twende ili tusichelewe kila mahali. Si uliniambia kule jela wana muda maalum?” “Ndiyo.” “Basi tusalimie hapa, halafu tuwahi.” Wakachuka garini.

Kwa Mara ya Kwanza Net Nyumbani, kwa Mchungaji.

Wakamkuta Mama Penny alishafika. “Mlipitia wapi!?” “Net alitaka tupitie dukani angalau tusije mikono mitupu.”  “Ndio faida yakuwa na mahusiano na wazungu! Maana wageni wengine wakija humu ndani, utasikia naomba nikanunuliwe Fanta, mimi sipendi Coca, au sijui Sprite! Lakini watu walio staarabika wanakuja na zawadi mkononi.” Mama Penny aliongea akimsuta Tunda. Net akacheka tu.

“Yaani mama Penny! Mwenzio nakuwa nimechoka, na Fanta pekee ndiyo inaniburudisha.” Tunda akajibu. “Sasa uwe unanunua kreti nzima unaliacha hapa ndani, sio kusumbua watu.” “Huwa naacha, ila wanao wanamaliza.” “Ni Penny huyo, anti.” Pendo akadakia. “Hata dady anapenda Fanta.” Penny naye akaongeza na kufanya watu wote wacheke.

“Watoto hawana siri hawa! Kwanza mpenzi wangu huwa hanywi soda nyingi kwa siku, tatu mwisho.” “Sasa kama anakunywa tatu, na wanao mbilimbili, hiyo kreti inakaa siku ngapi?” “Na dada naye anapenda Fanta.” Penny akaongeza tena. “Haya umesikia wanao?” Tunda akadakia.  “Naombeni muondoke nyinyi watoto!” Mama yao akawafukuza. Wote walikuwa wakicheka. 

“Karibu Net. Hapa ndipo nyumbani kwetu wote. Tukupokee mzigo, ila huna haja ya kuja hapa na vitu bwana. Uwepo wako ni zawadi tosha.” “Asante Mama Penny.” Ulikuwa ni wakati Net alioufurahia sana. Alikula na kucheka tokea anaingia mpaka wanatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Sijawahi kuona Mchungaji na Mama Mchungaji wa namna hiyo!” “Nilikwambia mimi. Yaani mimi nilikuja na uchungu moyoni, hata sijui viliishia wapi, na lini! Wana jinsi ya kukuonyesha maisha sio magumu ki vileee!!” “Si umemsikia hata huyo mama mwenyewe anavyosema?” “Basi ndio usemi wake kila wakati. Eti, ‘acha kuwa serious wewe, maisha sio magumu hivyo!’ au utamsikia, ‘Usituharibie hali ya hewa hapa kwa kuwaza kama unataka kuumba dunia wakati Mungu mwenyewe alishasema imekwisha, kazi yetu sisi tutawale.’ Wakati wote husema watu tunashindwa hutawala sababu ya ujinga tu.”

“Usimuone maneno mengi vile, anapesa sana yule mama. Karibu kila siku anayo kazi inayomuingizia sio chini ya milioni. Kama sio kupamba, basi anabiashara zake nyingine. Jina lake linafahamika sana hapa mjini, ndiye aliyenisaidia kuniuza kwa watu mpaka sasa na mimi nafahamika au napata kazi kwa jina langu. Mkarimu na hana tamaa. Ukifanikiwa ndiyo furaha yake.” Tunda na Net waliendelea kuongea wakiwa wanaelekea kumuona baba yake Tunda jela.

“Nimefurahi Tunda. Nimepata wakati mzuri sana. Nilihitaji mapumziko ya akili baada ya mawazo mengi.” “Unawaza nini tena Net!?” “Nitakwambia tukitoka kumuona baba, kama bado utakuwa na muda wakunisikiliza.” “Hata kama ni saa sita usiku, nitakusikiliza Net. Unajua ni wewe pekee ambaye sina haja yakujificha kwako? Sina sababu ya kujifanya Tunda huyu wasasa tu. Nakuwa huru, najua nipo na mtu anayenifahamu vizuri, na bado amenikubali.” Net akamtizama Tunda na kutabasamu.

“Nini sasa? Si kweli?” “Ni kweli Tunda. Na sio kukukubali tu, najipendekeza pia.” “Jamani Net! Hujipendekezi bwana.” “Unauhakika Tunda?” “Kweli Net. Nakuwa nakosa tu ujasiri. Nilikwambia. Lakini nafurahia tukiwa wote. Unaniheshimu japo unanijua kuliko yeyote yule hapa duniani.” Walifika gerezani, hapakuwa mbali na nyumbani kwa mchungaji. Ni eneo hilohilo la Tabata. “Twende kwanza tukamuone baba, kisha tutaongea.” Wakashuka.

Net akiwa na Tunda gerezani.

Waliingia ndani japo muda ulikuwa unakaribia kuisha wa kuwaona wafungwa, lakini baba yake Tunda alifurahi sana kumuona Tunda. Waliongea kidogo, Tunda akamuahidi, kufanya kila awezalo kumtoa humo. “Tunda aliniambia jinsi ulivyomsaidia kumtoa kwenye matatizo. Nakushukuru sana. Nilimuacha mwanangu hospitalini bila msaada, tena nikijua kila mtu hamtaki!” Baba yake akaendelea.

“Nilipo hukumiwa pale mahakamani nililia kama mtoto wa kike nikimfikiria mwanangu pale kitandani hospitalini. Nilimlaani Mungu kwa kukubali mimba ya huyu mtoto itungwe siku nilipolala na mama yake. Na pesa yenyewe niliyompa ilikuwa ndogo kweli, sikujua kama nitakuja kumuona tena Tunda!” Tunda alikuwa ameinama tu kama anayefikiria wakati baba yake akisimulia. Akili zilimrudisha mbali, akabaki akimsikiliza Net na baba yake huku akifikiria hili na kukumbuka lile.

“Nakushukuru sana.” “Hata mimi namshukuru Mungu kunikutanisha na Tunda. Nampenda sana Tunda.” Tunda akashtuka sana. Hakutegemea kusikia Net anasema vile, tena akiwa na baba yake! ‘Upendo huu ni wa namna gani!?’ Tunda akajiuliza kwa mshangao akanyanyua kichwa na kumgeukia Net palepale walipokuwa wamekaa upande mmoja wakimwangalia baba yake. “Nisije kujichanganya. Nisifurahie mengine. Net ni mzungu. Neno upendo ni kitu cha kawaida kutamka kwa wenzetu.” Akajirudi Tunda, akiogopa kufurahia zaidi.

          “Ni kweli ni upendo pekee, ndio uliokuwa ukihitajika kumpokea Tunda. Nakushukuru sana.” “Asante baba. Tunaweza kuomba pamoja?” Net akauliza kiuungwana. “Mimi sijui kuomba Net, wewe omba tu kama utataka.” Baba yake Tunda akajibu. Na hapo ndipo Net alipomfundisha yule mzee kuomba, na kumuhubiria. “Hata Tunda amekuwa akinihubiria, lakini…” Yule Mzee akasita.

“Haina haraka baba. Pata muda wakufikiria, kisha utaamua.” “Nina dini yangu nzuri tu. Sitaki kubadili dini.” “Kuokoka si kubadili dini baba. Nikupatanishwa na Mungu. Bibilia inasema watu wote tumekosa na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. Kwa kutubu na kumkaribisha Yesu maishani mwako, nikukubali yale Mungu aliyokusudia kwa maisha yako. Kama ukiokoka, na ukaona dini uliyonayo inakusaidia kukusogeza karibu na Mungu, ujue upo katika njia sahihi.”

“Lengo la dini nikukupatanisha na Mungu, au iwe msaada kwa roho yako, basi.  Lakini kama itakuzuia kuwa na mahusiano na Mungu, basi itabidi ufikirie mara mbili, juu ya hiyo dini. Maana itakufaa nini kuwa na dini halafu ikakukosesha mbingu? Au itakusaidia nini kuiacha dini yako ukahamia kwenye kanisa, na pia ukakosa mbingu?” Net akaendelea.

“Lengo si kuhama kanisa moja kwenda jingine, lengo ni kuhama kutoka falme ya giza na kuhamia kwenye ufalme wa Mungu, na kukaa huko. Sio unahamia kwenye kanisa jingine, wenye jina fulani, ukajulikana na wewe upo kwenye kanisa hilo kumbe maisha yako ni chukizo mbele za Mungu. Ukibaki wewe peke yako na Mungu, hamna mahusiano yeyote, huo sio mpango wa Mungu.”

“Mungu anataka mahusiano na mtu mmoja mmoja si kanisa, wala dini. Ukifa leo mzee, hutaulizwa dini yako. Mungu atataka mahesabu ya jinsi ulivyotumia maisha yako hapa duniani.” “Maisha yenyewe yameisha haya kijana wangu. Nishatupwa huku.” “Nilikwambia usikate tamaa baba. Nahangaika kukutoa.” Tunda akaingilia.

“Hata hivyo, hata hapa ulipo pia utakuja kuulizwa na Mungu ulifanya nini?” “Ananiuliza nini huyo Mungu wakati yeye ndiye amenileta hapa, tena bila kosa!?” “Ewaa! Umezungumza sahihi kabisa. Kuwa Mungu alikuleta hapa kwa kusudi. Basi ujue lipo kusudi. Kwa nini iwe wewe na sio mwingine? Inawezekana kuna kazi anakupa humu gerezani uifanye au umeletwa humu kwa ajili yako mwenyewe. Unasema unayo dini. Huwa unasoma bibilia?” “Hapana, lakini nafahamu vihabari vyake.” Akajibu baba yake Tunda akiwa kama anavuta kumbukumbu.

“Unakumbuka historia ya Yusuph?” Yule mzee akatulia. “Kwa utizamaji huo, naamini unaijua habari nzima. Unakumbuka mwisho wake? Unakumbuka jinsi alivyotoka gerezani kitu Mungu alimfanyia?” “Si ndiye alikuja kusaidia ndugu zake?” Net akatabasamu kwa kuridhika.

“Si ndugu zake tu, watu wengi walipata msaada kupitia kukaa kwa Yusuph gerezani. Kama angelia na kubaki kulalamika, inamaana kuonewa kwake kule gerezani ingekuwa bure kabisa. Tunda amekupa ushuhuda wake?” “Upi tena?” Net akamtizama Tunda kama anayemuomba ruhusa, yakusema. Kwa vile Tunda anavyomfahamu Net, akajua hawezi kumdhalilisha kwa baba yake. Akamruhusu asimulie chochote na yeye akiwa na hamu yakusikia jinsi Net anavyoanza kutumia maisha yake kuwa msaada kwa wengine.

“Nilimwajiri Tunda kwenye kampuni ya mama yangu. Nikasafiri nikamwacha Tunda pale ofisini. Huku nyuma mama yangu alimfukuza Tunda vibaya sana. Aliondoka Arusha akiwa hajui chakufanya, akilia njiani akimlaumu Mungu. Lakini Mungu alimfundisha kwa mfano wa kupitia watoto, huku akimuonya kulia hakutamsaidia, mpaka atakapoangalia mazingira yanayomzunguka, akasimama na kuchukua hatua.” 

“Tunda alitii, ndio maana yupo leo kama alivyo. Kama Tunda angeendelea kulalamika mpaka leo asingekuwa hapo. Na yale ambayo shetani ameyakusudia kuwa mabaya kwake, yangeendelea kumkandamiza na kumwangamiza kabisa.”

“Usikubali maisha yako yakawa hayana maana. Kila kinachotokea katika maisha yako baba yangu, kitumie kutengeneza hesabu ya kumpa Mungu siku ukisimama mbele zake. Maana ni kweli wote atatudai tu siku moja. Lakini uzuri, kila utakapochukua hatua, yeye anakuwa na wewe, anakuinua, atakutia nguvu na kukubariki.” Tunda alikuwa akimwangalia Net bila kummaliza. Kijana mzuri wakuvutia kwenye kila jicho la mtu anayemtizama, mpaka watoto! Aliyesoma vizuri, anayejua maisha vizuri, na pesa nzuri yakueleweka na bado anasimama na Mungu wake!

“Kwa mfano mwingine tu. Najua unajua maisha ya Tunda kwa sehemu. Tena ni maisha yasiyofaa kutamkika mbele za watu. Lakini tutahakikisha, maisha hayo hayo aliyoishi Tunda, yanasikika, tena vizuri, mpaka watu wakombolewe. Tutafundisha vijana kwa wazee, wakina baba na mama, tutamfikia kila mtu kwa maisha aliyoishi Tunda mpaka watu wapate msaada. Nje na ndani ya nchi. Wazi wazi bila kificho mpaka shetani ataogopa kushika ndoa za watu, maisha ya vijana, watoto wa watu, kila baya lililotendeka kwa Tunda, tena sirini, tutatumia mwangani kufikia jamii nzima, mwenye sikio atasikia na kubadilika.” Tunda hakuwa akiamini. “Inamaana na yeye anajiweka!” Bado Tunda hakuwa ameelewa.

Ilimgusa sana baba yake Tunda. Hata yeye hakuwahi kuona mtu aliyempokea Tunda kwa kiasi hicho. “Asante sana kijana wangu. Asante baba. Na mimi Mungu akinipa uzima, na akanitoa humu ndani, nitaungana na nyinyi.” Net akacheka. “Si umeona Tunda? Tunazidi kuwa wengi? Sasa wewe Mzee tunaomba uanzie humo ndani. Kwa kuwa mimi na Tunda hatuwezi kufikia wafungwa wenzako, wewe ndio uwe nao.”

“Naanzaje wakati hata kuomba siwezi!?” “Tutakuwa na wewe kwa maombi. Na wewe kazana kusoma bibilia ili uwe unaongea habari unazozifahamu. Tutakuombea ili ujazwe na nguvu za Mungu, halafu mruhusu Mungu akutumie kwa jinsi apendavyo na alivyokusudia. Kama alikuleta huku, lazima ujue lipo kusudi, na yeye atakusaidia kufikia lengo.” Yule mzee alifurahi sana. Net alimuongoza sala ya toba, akamuombea na kumuachia bibilia yake. 

Baada yakutoka gerezani kumuona baba yake Tunda, Tunda & Net.

Tunda hakuwa akiamini. Alishindwa hata kuongea kwa muda. Net aliongea mambo kadhaa, yaliyomgusa na kumuogopesha Tunda. Hakuwa akiamini na aliogopa asije akafurahia kama alivyofurahia kwa Waziri Mbawala, ikawa tofauti. Ikaja kuwa ni Net aliongea yale yote sababu yakufikia roho ya baba yake. “Net anapenda watu watubu na wamrudie Mungu. Ingekuwa kunipenda mimi, angeniambia mwenyewe.” Tunda akaona ajitulize.

Net akaendelea kuendesha na yeye kimya, wakirudi kanisani kufuata gari ya Tunda. Alikaa kimya, baadaye ndipo akaweza kushukuru. “Nashukuru sana kwa kumsadia baba yangu. Umemuona jinsi alivyobadilika? Hata uso wake umechangamka. Asante sana. Mimi nimekuwa nikimuhubiria kwa muda mrefu sana bila Mafanikio.” “Ndio maana bibilia inasema katika kitabu cha {muhubiri 4:9 Two people are better off than one, for they can help each other succeed.} Au kwa Tafsiri ya Kiswahili ni {Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja, maana wapata ijara njema katika kazi au unaweza sema wanasaidiana kufanikiwa katika kazi}. Si umeona jinsi mimi na wewe tunavyoweza kufanya jambo likafanikiwa?”

“Mbona mimi pale sikusema kitu?” “Si kweli. Ulishapanda mbegu kwenye moyo wake, ukawa ukimwagilizia mimi nilienda kumalizia tu kuvuna.” Tunda akatabasamu kama anayefikiria. Wakawa wameshafika kanisani.

“Karibu nyumbani kwangu.” “Nilivyokuwa nasubiri kwa hamu huo ukaribisho!” “Bwana Net! Kwangu usisubiri kukaribishwa.” “Lazima nisubiri, na hivi kuna kina Julius tena!” Tunda akacheka na kushuka kwenye gari. “Unifuate nyuma, ndio itakuwa rahisi kufika nyumbani.” Tunda akafunga mlango na kuingia kwenye gari yake, kisha akaondoa gari yake, Net akawa akimfuata nyuma.

Net apasua jipu kwa Tunda.

Bado Tunda alikuwa akiishi pale pale maeneo ya Kimara, karibu sana na Ubungo. Alimkaribisha Net ndani, wakakaa kwenye makochi. “Hapa kwangu hakuna soda, nina maji tu. Ila naweza kwenda kukununulia kama utapenda. Mimi sio mpenzi sana wa Soda. Labda niwe nimechoka sana na kazi, ndio nitakunywa soda. Lakini sio hapa kwangu. Najitahidi zisiwepo.” “Hapana. Mimi nipo sawa tu. Bado nimeshiba.” Tunda akaweka vitu vyake ndani, akarudi kukaa hapo hapo kwenye kochi kubwa alilokuwa amekaa Net.

“Hongera. Naona nyumba imekamilika.” “Asante Net. Ndio moja ya vitu vilivyokuwa vikiniliza mwenzio! Sina ndugu wala ukoo wakusema nakwenda kutembea. Sasa hata nishindwe kuwa na kwangu! Ilikuwa ikiniuma sana. Nilianza kutafuta pakuishi hata kabla ya gari. Nilijiambia lazima nipate kwanza kwangu. Angalau nipate kimbilio.” “Hongera sana Tunda. Hakika umenifurahisha.” “Asante Net. Napambana kweli!” “Na juhudi zako zinakulipa. Nimepitia kwenye website yako, upo vizuri sana.” Hilo lilimfurahisha sana Tunda, kujua Net alimfuatilia zaidi.

“Nikuulize kitu Net? Nahofia nisiwe nimekuelewa vibaya.” “Karibu.” Net akajiweka sawa na kumgeukia. “Ulisema ‘utakuwa’ na mimi kunisaidia kutumia maisha yangu kufikia jamii?” Net akacheka pale Tunda alipoweka msisitizo kwenye ‘utakuwa’.

“Unajua umenipa hamasa sana? Ni kama umenitoa kwenye kona na kunivuta mwangani! Sasa hivi sioni haya tena. Lakini sijui ndio ninafanyaje! Umesema utanisaidia?” “Sio kukusaidia Tunda. Tutakuwa wote.” Tunda akawa bado kama hajampata vizuri. Net akaendelea.

“Nahisi ndio kazi Mungu anataka niifanye, labda mpaka kufa kwangu. Nimejaribu kukwepa, nikimpa Mungu sababu za msingi ili niweze kukwepa, lakini Mungu ananirudisha tu. Hata nifanye nini, bado najikuta nimerudi hapa hapa.” Hapo ndio akawa amempoteza kabisa Tunda. Akapandisha miguu yake kwenye kochi akaikunja vizuri nakumgeukia Net.

“Sikuelewi Net.” “Wewe kwa nini hushangai kila unavyozidi kunikwepa, ndivyo tunavyozidi kukutana?” “Net Jamani! Mimi mbona sikukwepi?” Net akacheka.

“Siku ya kwanza nafika nyumbani kwa shangazi yako, unakumbuka ulinifungulia mlango?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Huwezi amini, naweza kukwambia mpaka aina ya gauni ulilokuwa umevaa siku ile, jinsi ile picha ilivyo niganda mawazoni. Hayo macho yako ya kusinzia, siku ile ndio yalikuwa yamezubaa yakinitizama.” Tunda alicheka na kufunika uso wake.

“Nikaanza kujifariji ili niepukane na mawazo yako. Nikasema kule kupigwa na butwaa na kunishangaa ni kitu ambacho nishazoea kwa watu wengi hasa wadada. Huwa wananiangalia kwa namna yao, ambayo huwa hainisumbui hata kidogo, lakini wewe ikawa tofauti.” “Mimi nilikuwa nakushangaa ulivyo mzuri zaidi ya nilivyosikia sifa zako! Mzungu unayeongea kiswahili chenye heshima.” Net akacheka.

“Sasa nikaanza kupuuza. Lakini bado nikawa nasumbuka. Ndio maana nikawa nahangaika kuja pale nikuone ili nijue ulichonacho wewe cha tofauti na kinadada wengine ni kipi! Nikawa nakuja mchana na usiku, ili nikuone, lakini sikufanikiwa. Nikawa namuomba Mungu angalau uje basi hata kufungua mlango tena, lakini wapi.”

“Baadaye nikajiambia niachane na wewe, usinisumbue. Tena hapo ndipo nilipokuwa nikipata na habari zako mbaya kabisa. Nikawa nikijiambia nina sababu zote za kuwa mbali na wewe. Lakini nikawa najikuta nataka kukuona tu. Mwishowe nikajiambia siwezi kujitesa kwa namna hii ni afadhali nitafute hata sababu nikae na wewe, ili hata nitafute sababu moja utakayonikera, nikuchukie, niondoke zangu nirudi shuleni kwa amani niwe nimekutoa mawazoni.” Tunda alikuwa haamini.

“Unakumbuka niliwakaribisha kwenye maombi nyumbani? Hukufanikiwa kuja, na nia ya kuwakaribisha nyinyi wote mpaka Nyangeta ilikuwa nikupata muda na wewe, nyumbani kwetu. Maana pale kwa shangazi yako ilishindikana kabisa kwa kuwa kila nilipokuwa nikijaribu kukusogelea ndivyo Sera na mdogo wake walivyozidi kunifuata, na kuishia kukutukana mbele yangu kitu kilichokuwa kikiniumiza sana.”

          “Uliposhindwa kuja nyumbani siku ile, na mimi nikaona muda wangu wakurudi chuoni umefika, lazima niondoke, na mimi ni mtu ambaye nikianza jambo lazima nimalize, ndipo nikajitosa kumuomba shangazi yako nirudi kesho yake nije kuongea na wewe kabla sijaondoka. Kumbe ndio naharibu zaidi.”

“Nilirudi Canada chuoni, lakini sikuwa na furaha, nikafikiria kitu chakufanya, nikaamua kutafuta msichana wa kanisani ili tuwe na mahusiano kuepuka msongamano wa mawazo. Nilipata binti mzuri tu wa kanisa ambalo nilikuwa nikiabudu na bibi na babu. Wazazi wake walikuwa wakifahamiana na kina babu. Kwa kipindi hicho wakati mimi nipo chuoni na yeye pia alikuwepo chuoni, lakini ndio alikuwa akianza, mambo yalienda vizuri sana.”

“Hapakuwa na shaka kuwa siye mwanamke Mungu aliyenipa. Tulielewana kwa mambo mengi tu, mengine yalikuwa madogo madogo yakurekebishana kama wanadamu au tuseme yakuchukuliana.”

“Siku moja nikiwa na yule dada nikajikuta nikijiambia afadhali nimeweza kuachana na mawazo ya Tunda. Hapo ndipo ikawa ni kama nimerudisha kumbukumbu zote. Na ndio ilikuwa nakaribia kumaliza chuo, na kwa muda wote huo hata sikuwa nimekufikiria, tulikuwa na amani na furaha na Chloe. Nilijuta sana kuleta zile kumbukumbu zilizokuwa zikinitesa bila sababu. Sikuwa nakufahamu, halafu nilikuwa na sifa mbaya tu za kwako. Nikawa nikimwambia Mungu na kumkumbusha mabaya yako niliyokuwa nimesikia.” Tunda akainama nakujifuta machozi.

“Shule yangu ilipoisha, mama akaniomba nirudi nimsaidie kazi zake kwa muda. Kama nitavutiwa kuishi naye sawa, nikitaka kurudi kuishi Canada pia ni sawa. Nikakumbuka wosia aliokuwa ameniachia baba, juu ya mkewe. Baba alimpenda sana mama. Wakati wote alikuwa akiniambia hata kama akiondoka kesho, I should watch over Maya na mama, yaani nimtunze mkewe na Maya. Ukumbuke aliniacha bado nikiwa mdogo tu, lakini sikuwahi kusahau hilo. Alinilea kuwa mwanaume wa familia tokea mtoto na babu hivyo hivyo. Japokuwa mambo yangu yalikuwa yakienda vizuri kule, ilinibidi nirudi Tanzania kumsaidia kazi mama.”

“Nilimuomba Chloe aihirishe angalau mwaka mmoja ili tuje naye huku, nikishaweka sawa mambo ya mama, tungerudi. Lakini Chloe alikataa. Nikamwambia hata kama itatulazimu kufunga ndoa kwanza, naweza kumuoa kisha tukaja naye Tanzania, na babu alimwambia endapo ataacha chuo kwa ajili yangu, akapoteza udhamini, babu alimuahidi angemsomesha kwa gharama zozote zile mpaka amalize. Lakini alisema, anaweza kunisubiri kwa huo muda wa mwaka mmoja, lakini hakuwahi kufikiria kuishi maisha mengine nje ya nchini kwao na amejiwekea malengo ya kumaliza shule ndani ya huo muda, hawezi kusogeza. Nikamkubalia, nikaja huku.”

“Baada ya mwaka, nikarudi na kumwambia inabidi niongeze muda, maana mama alianza kupata tenda za ujenzi wa barabara zilizokuwa zikimuingiza pesa nyingi sana lakini zilihitaji mtu kama mimi kuwepo na kusimamia. Nikamuomba tuondoke naye, bado akakataa. Akasema atanisubiri tu. Nikaamua kumvalisha kabisa pete ya uchumba ili asije kubadili mawazo. Nikarudi huku nikawa nikifanya kazi kwa bidii sana ili nimwache mama kwenye mazingira mazuri, na wafanyakazi wazuri ili nirudi kwenye maisha yangu. Safari za Canada zikawa nyingi kumfuata Chloe kwa kuwa alianza kulalamika anachoshwa na mahusiano ya mbali.” Net akatabasamu.

“Mambo yalianza kunichanganya pale nilipokuona tena. Katikati ya kazi nyingi, na mahusiano ya lawama, kati yangu na Chloe, kwa nini sipigi simu, kwa nini siendi kumuona, na mambo kama hayo. Unakumbuka mazingira tuliyokutana tena? Ulikuwa na mwanaume na wazi alionekana ni mume wa mtu. Niliumia mpaka nilijichukia. Nilijaribu kujiliwaza kwa kukuunganishia na maneno ya kina Sera, na kusema sina haja yakuumiza akili zangu, kwa msichana ambaye hukuwa na maadili, mimi ni mchumba wa mtu. Unajua tena, ili kujipa aghueni moyoni. Lakini nilishindwa Tunda. Nilikuwa nikiumia sana. Na Mungu naye alikuwa akinikutanisha na wewe kwenye mazingira yaliyokuwa yakizidi kunitesa sana.”

“Nilikuwa nikiumia nakujiuliza chakufanya, sikuwa najua pakukupata wala sikujua chakufanya. Ukweli niliteseka Tunda. Kila nilipokuwa najaribu kukupuuza, ndivyo nilivyozidi kukufumania. Hasira juu ya kila mwanaume niliyekukuta naye ilinifanyanya nichukie hata kazi ya mama. Kwa kuwa wanaume wote niliokuwa nikikukuta nao, ni watu muhimu sana kwenye biashara za mama.”

“Nilishindwa kabisa kuendelea na ile kazi, nilijawa hasira, nikashindwa kuwa mvumilivu kwenye kila kitu. Mama alidhani nimechoka kuwepo hapa Tanzania, akanishauri nirudi tu kwa bibi na babu, lakini nikajikuta siwezi tena kuondoka kukuacha kwenye mikono ya wanaume wanaotaka kukuchezea.” Net alicheka kidogo kama anayefikiria.

“Huwezi kuamini kutoka kwenye kukuchukia sana kwa kunisababishia maumivu ya uchafu unaofanya, nikageuza hisia nikaanza kuona uthamani ulio nao. Na kuzidi kuchukia kila mwanaume anayekuchezea. Nilikuwa nikijiambia wanakuchezea kwa kuwa hawajui thamani yako. Unakumbuka yule Mzee tulikutana wote Mwanza pale baa akiwa amelewa, akikuelezea jinsi ulivyo mzuri, na kueleza mambo kwa undani kabisa?” Tunda alishinda hata kumtizama Net, akabaki ameinama.

Net akaendelea. “Ukweli nilikuwa nikiteseka sana. Mwishowe nikaamua kujisalimisha kwa Mungu. Nilikuwa sijui chakufanya Tunda. Kila ninapoenda nakutana na wewe ukiwa na wanaume tofauti tofauti, huku Chloe naye ananitaka nirudi tufunge ndoa, huku najiambia siwezi kukuacha. Nikamwambia Mungu akinisaidia nikakupata, ukakubali kubadilika, nitaondoka haraka sana kurudi kwa mchumba wangu.”

“Siku iliyoniuma zaidi ni pale nilipokukuta na Gabriel. Niliumia sana. Gabriel alikuwa rafiki yangu tokea Canada. Baba yake alikuja kusoma kule, akawa chuo kimoja na mama, kwa hiyo Gab alikuja Canada akiwa mtoto sana, nilizaliwa yeye akiwa na miaka kama mitatu hivi. Tuliishi nao Canada, wao wakarudi huku nchini, Gabriel akiwa na miaka 18. Na ndio watanzania pekee tuliokuwa nao karibu kule. Hatukuacha kuwasiliana na Gab mpaka sasa. Na hata anapokuwa akija Canada, yeye na mkewe au wazazi wake, wanafikia nyumbani kwetu. Kwa hiyo ni kama ndugu.”

“Kuja kujua ulikuwa na mahusiano naye, nikaamua kuondoka kabisa nchini. Lakini Gab aliniomba sana radhi, nikamwambia akuache kabisa na asirudie kukutafuta tena. Maana alikuwa yupo tayari kumuacha mkewe kwa ajili yako. Nilimwambia endapo atamuacha mkewe, kwa ajili yako ndio itakuwa hata mwisho wangu na yeye pamoja na familia yake yote. Yaani mpaka wazazi. Ndio Gab akakubali kukuacha kabisa. Na kuniahidi hatakutafuta tena.”

“Lakini aliniudhi sana siku ile ulipomfuata hotelini unamlilia shida halafu anakwambia atakupiga! Iliniuma toka moyoni. Unakumbuka nilikukuta umejificha kwenye kona ukilia?” Tunda alitingisha kichwa kukubali akiwa anafuta machozi.

“Pale nilikuwa nimeshazunguka sana. Na gari na kwa miguu huku nikikimbia kukutafuta. Nilijua ndio wakati pekee Mungu alionipa kukupata. Kwa upande mwingine nilifurahi kuona umefika mwisho, watu wote wamekukimbia. Nikajiambia nakaribia kumaliza kazi yangu. Nikupatanishe na Mungu, kisha niondoke niende kwa mchumba wangu.”

“Kule kuishi na wewe Arusha ikawa msaada kwangu mimi mwenyewe. Hukuwa umefikia hata maamuzi ya kubadili maisha, lakini nilikuwa nikifurahia sana tukiwa pamoja. Nikaona jinsi ile ofisi inavyokuwa, nikajiambia wewe ni mtu utakayenifaa kwenye mambo mengi. Kwamba ukikubali kumpa Yesu maisha, nitakuwa nimeua ndege wawili kwa jiwe moja. Nitakuwa nimemalizana na wewe kwa amani, na ofisi nitaiacha kwenye mikono salama. Sasa unakumbuka siku tumeenda kwa mama akakwambia nitasafiri?” Tunda akatingisha kichwa kukubali.

“Alikuwa akijua muda wangu wakuondoka moja kwa moja kwenda kwa mchumba wangu umeshakaribia. Maana nilishakuwa nimekupa muda, nikasema ninakuachia muda fulani, uje ufikie maamuzi ya kubadilika bila mimi kukulazimisha. Nikajiambia muda huo ukifika hujafikia maamuzi, nitaongea na wewe, ukubali au ukatae, nikajiambia nitaondoka. Ndio nikawa nimemwambia mama kuwa ikifika mwezi wa kumi na moja nitaondoka moja kwa moja. Kumbe ule muda niliokuwa nimekupa wewe kukuangalia, ndio kipindi hicho na mimi nilianza kukuzoea. Huwezi amini jinsi ilivyokuwa ngumu kukuacha usiku. Nilikuwa nikitamani niwe na wewe wakati wote.” Tunda akamtizama huku amekunja uso, haamini.

“Siku zikazidi kwenda, wewe ukaokoka, lakini nikawa nashindwa kabisa kuondoka. Chloe naye akawa amenipa muda, kuwa ikifika mwezi wa kumi na moja sijarudi kule, hataweza kuendelea kunisubiri tena. Nilikuwa tayari kwa hilo. Kila mama alipokuwa akiniuliza naondoka lini, sikuwa na jibu tena.”

“Ndipo babu akaugua sana, ikabidi niende tu lakini hapo nilishakuwa nimeahirisha sana. Kila Nana alipokuwa akinipigia simu akiniambia hali ya Papa, nilikuwa nikimwambia nitakwenda, lakini nashindwa kukuacha. Huo mchezo ukaendelea, ndipo nikaambiwa majibu ya hospitalini yameonyesha Papa hawezi kupona. Nana akaniambia Papa anataka kuzungumza na mimi. Lazima niende haraka.”

“Ndio nikaondoka ule mwezi wa 11 mwanzoni. Kwa hiyo ikawa nimefika kabla ya kipindi alichokuwa amenipa Chloe kuisha. Tukaanzisha mahusiano kwa uhakika, huku nikimuahidi kutokuondoka tena Canada. Hapo nikajihesabia nimemaliza kazi yangu. Umeokoka, na ofisi ipo kwenye mikono salama.”

“Ila sasa mahusiano yakawa mazito sana kwangu, kwani Chloe hakuwa Tunda. Sikuwa nikiona maisha yangu na yule binti hata kidogo. Babu alinishauri labda nimchukue nimpeleke sehemu mbali mbali ili kupata naye muda, labda zile hisia za mwanzoni zingerudi. Aliniambia ni kwa kuwa tuliishi mbali mbali kwa muda mrefu sana. Nikamuacha babu akiwa bado anaumwa nikaanza kuzunguka na Chloe.”

“Hata Papa alijua angekufa, kwa hiyo alitaka kuniona nimeoa kabla hajafariki. Madaktari walitupa muda uliobaki wa papa au babu uliobaki kuishi. Nikakusudia babu awepo kwenye harusi yangu, angalau anione tu nikioa kwa kuwa ni kitu alichokuwa akikitamani kuondoka akiwa ameniacha nimeanzisha familia yangu. Nilizunguka na yule dada, lakini hakuwahi kuwa Tunda. Alikuwa na sifa zote za kuwa mke wa mtu, lakini sio mke wa Net.”

“Nakumbuka tulitoka safari tulitua uwanja wa ndege na Chloe nikaenda moja kwa moja hospitalini kwa babu. Nilimkuta na bibi yuko pale, nikajikuta machozi yakinitoka, nikimuhurumia babu yangu, kuwa yale aliyotamani nimeshindwa kumpa.”

“Nakumbuka babu alinitazama kwa huruma, nikajikuta namwambia, ‘She is not Tunda.’ Alitabasamu na kuniambia kwa kifupi tu, ‘then go and tell her, NOW’. Nikachukua ushauri wa babu pale pale, sikutaka hata kusubiri. Nilitoka pale hospitalini nikamfuata Chloe nyumbani kwao. Nikamwambia sitaweza kumuoa tena, nampenda mtu mwingine. Ilikuwa ngumu sana, lakini niliona ni heri yale maumivu ya wakati ule kuliko aje aumie akiwa mke wangu.” Mwili mzima wa Tunda ulikuwa ukitetemeka.

“Basi, nilirudi hospitalini nikamwambia babu, babu alitabasamu na kuniambia hata baba yangu angekuwepo angenisifu kwa kufanya maamuzi magumu na muhimu kama yale. Kwa hukumu yakuona nimemshindwa kumpa babu yangu kile alichokitamani, kwa kutokuoa akiwepo, nilimuuguza bila kuondoka pembeni yake mpaka alipofariki. Zilikuwa zimebaki siku chache afariki, kwa hiyo mimi ndiye niliyekuwa naye pale hospitalini muda wote.” Tunda alikuwa ameinama huku ameficha uso wake akilia. Net akacheka tena.

“Ungenihurumia pale mama alipokuja kwa mazishi, halafu ananiambia uliondoka Arusha, hajui ulipo. Nilitamani wawe wamenizika mimi sio babu yangu. Nilikasirika sana. Nikahisi Mungu anataka kunichanganya akili tu. Nilikaa Canada sijui nirudi tena huku au niendelee na maisha yangu tu moja kwa moja hukohuko. Mama alipopata matatizo kwenye ile ofisi ya Arusha ilinibidi nirudi kuja kumsaidia.” Tunda akashtuka.

“Alipata matatizo gani tena!?” Tunda akajifuta machozi na kuuliza. “Safia alimtapeli. Kwa kifupi aliiba wateja wote wa mama, kwa kuwaambia hatuna uwezo wa kuwasafirishia tena mizigo yao. Kwa sababu tofauti tofauti. Mara awaambie malori yameharibika, au yote yamesafirisha mzigo sehemu nyingine, kumbe akawa ameingia ubia na mtu mwingine. Anamlipa kwa asilimia 40, kwa kila mteja anayempelekea. Kwa hiyo tukawa tunatumia pesa nyingi kujitangaza, wakipiga kuomba huduma, Safia anawapeleka kwenye kampuni ingine.”

          “Safia alipoona amenogewa, akaja kufungua kampuni kama ileile. Akawa anatumia magari yaleyale ya mama, lakini aliajiri madereva wake. Wale niliokuwa nimeajiri mimi aliwatafutia sababu, mama mwenyewe akawafukuza. Tena aliwafukuza vibaya tu. Basi, Safia akajinufaisha kwa gharama ya mama. Mama kuja kushtuka, akakuta alishafilisiwa kabisa na anadaiwa sana. Alimtia hasara kubwa tu.”

“Tuliuza ile nyumba ya Arusha na yale malori yakiwa kwenye hali mbaya sana, tukalipa madeni yote tukabakia na biashara za huku Dar tu.” “Pole Net.” “Mama amejifunza sana. Aliogopa kuniambia ukweli kama alikufukuza, alijua ningemlaumu sana. Lakini juzi tulipokutana pale hotelini, ulipokuja kwenye kikao,  ukanisimulia kila kitu, nikatamani kujua kwa nini alikubadilikia.” “Ulijua ni kwa nini?” Tunda akauliza kwa upole, lakini Net alionekana kusita kidogo.

“Nimbie tu Net. Nataka kujua nini nilifanya kiasi chakubadilisha moyo wa mama Cote. Alinipokea vizuri sana nilipofika Dar, na alinipenda hata kabla hajaniona akawa haishi kunisifia na kunishukuru kwa kazi nzuri niliyokuwa nikimfanyia. Lakini akaja kubadilika ghafla!” Net akavuta pumzi kwa nguvu huku amefunga macho kama anayejishauri.

“Net?” Tunda akaita tena taratibu akijua kuna kitu Net anataka kumficha. “Unawakumbuka wale wazee wa pale kanisani, ambao uliwahudumia?” Tunda alianza kuogopa. Alihisi kitu. “Mmoja wao alikuwa kwenye mahusiano na mama, walitaka kuja kuniambia, kisha wafunge ndoa.” “Mungu wangu Net!” Tunda aliweka mikono kichwani nakuanza kulia. “Kwa hiyo aliumia sana, ndio maana alikuchukia.”

    Tunda alihisi dunia imemwangukia mabegani. “Naomba uniombee msamaha kwa mama, Net. Uwii jamani! Balaa gani hili!?” “Tunda! Nimekwambia lazima ukubali kubadilisha historia ya maisha yako.” “Siwezi tena Net.” “Unaweza. Mama ni mmoja ya watu wengi walioumizwa na shetani kupitia wewe. Hujapata fulsa ya kusikia wengine wanasemaje. Huwezi jua ulivunja ndoa za wangapi. Inawezekana ni wengi sana, ndio maana unajukumu la kusimama sasa na kusaidia ndoa nyingine.” Net aliendelea taratibu. Hakuonekana na hasira hata kidogo.

“Ukikubali kushindwa, ujue wapo wengine wanaotumiwa na shetani kama vile ilivyokuwa kwako. Na ujue ndoa au mahusiano mengi yapo hatarini. Wewe sio wa kwanza Tunda, na wala hutakuwa wa mwisho. Wapo waliokubali na kutubu, na wapo wanaokataa na kuendeleza huo uchafu mpaka sasa. Wewe umechagua jambo jema, lazima usaidie wengine. Hata hivyo binafsi nakushukuru, maana bila wewe mama yangu angeolewa na mwanaume anayejua ni mcha Mungu, kumbe ni tapeli tu.” Tunda aliendelea kulia.

“Nakupenda sana Tunda.” “Naomba unisamehe Net. Nisamehe. Nimekuumiza sana. Naomba unisamehe.” Tunda akapiga magoti. “Yamepita hayo Tunda. Nitafurahi kama utaishi na mimi bila hukumu. Mungu amekusamehe, na ni kweli anakupenda. Aliniweka kwenye maisha yako makusudi kunifundisha upendo wake kwa watu tunao wahukumu. Tokea unaishi dhambini, wanadamu wakiwa wanakuchukia na kukuhukumu, Mungu alikuwa akinionyesha mimi upendo wake kwako wewe Tunda.”

“Alinitoa kwenye nafasi ya kukuchukia na kukupenda kupita ninavyoweza kukwambia. Aliuweka uthamani wako bayana kwangu. Na amekuonyesha hata wewe kwa vile alivyo kufanikisha. Amekusamehe, amekupokea na elimu uliyo nayo, na ameonyesha wasomi kuwa anaweza kubariki yeyote ampendaye. Unamaisha mazuri kuliko wasomi wengi hapa nchini! Zaidi amekupa furaha na amani.” “Amenipa na wewe.” Net akacheka. “Ndiyo, na mimi ambaye nitakuwa na wewe kwenye maisha yangu yote.” Tunda hakuwa akiamini.

          Alifunga macho yake tena na kuendelea kulia. Alianza kufikiria maisha yake kama mke wa Net, aliyekuwa anamezewa mate na warembo wengi, wasomi wa kila namna. Waliojitunza na kulelewa kwenye familia nzuri, lakini alishangaa vile Mungu alivyomtunza Net, kwa ajili yake yeye aliyekuwa akihangaika na wanaume wa watu! Tunda alishindwa kunyamaza. Net akamnyanyua pale chini, akakaa naye pale kwenye kochi na kubaki amemkumbatia.

“Nakupenda sana Tunda. Sana.” “Asante Net. Nashindwa niseme nini!” Net akacheka. “Kweli. Mpaka naogopa.” “Unaogopa nini sasa?” Tunda akanyanyua uso wake, akamwangalia. “Nagopa isije kuwa nipo usingizini halafu nikaamka nikakuta kila kitu ni ndoto tu.” “Nini unachohofia zaidi?” “Kukupoteza tena.” “Hata nikiamua kukutoroka, ujue Mungu wako atanirudisha tu.” Wote wakacheka.

Net akambusu Tunda kwenye kipanda uso. Hiyo ni mara ya pili Tunda kupata busu la Net. Kwanza ilikuwa kwenye mkono na hapo ni mara ya pili, na mara zote zilimsisimua. Hata kule kukumbatiwa ilikuwa ni mara yake ya kwanza. Tunda alijivuta karibu sana na Net na kumkumbatia huku akilia tena. Kwa mara ya kwanza alihisi ulinzi mkubwa sana. Alimkumbatia Net kwa kumng’ania huku akilia na kushukuru Mungu kwa kumthamini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Tunda aliyepitia kwa wanaume wengi, hakuwahi kukumbatiwa maishani mwake kwa namna ile ya upendo. Hata tu mtu kutoa muda wake na kumtaka atulie mikononi mwake. Si mama yake mzazi hata wanaume aliokuwa akiwahudumia ilikuwa ni yeye kuwahudumia kwa juhudi zote waridhike, basi, labda kidogo waziri Mbawala tena yeye mwenyewe Tunda alikuwa akiomba kukumbatiwa. Hakuwahi kupendwa na kuthaminiwa vile.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akiwa amejificha hapo kwa Net, wazo la kumtia hofu likamji. “Lakini Net! Umeshafikiria tutakuwa na mahusiano ya namna gani? Kila ninapopita yupo mtu anayenifahamu. Nimemuumiza mpaka mama yako mzazi, Gab naye ndio hivyo, itakuaje? Si itakuwa kama nakudhalilisha tu kila wakati?” “Wao walikuwa wezi tu, mimi ndio nimekabidhiwa na Mungu. Wanatakiwa waniogope mimi sio mimi kuwaogopa. Halafu Tunda, kila mtu anamapito yake, tumetofautiana tu matukio. Unakumbuka ule mfano wa Yesu walipomletea yule mwanamke kahaba?” Tunda akatingisha kichwa kukubali.

“Walikuwa na sababu zote za kumpiga mawe yule mwanamke. Lakini unakumbuka jibu la Yesu?” “Nakumbuka.” “Basi huna haja yakuwa na wasiwasi, na kama nilivyokwambia, hatutasubiri watu watumie maisha uliyoishi zamani kukunyanyasa. Sisi wenyewe tutayatumia kusaidia watu. Itasaidia kama utakuwa jasiri, hata kama watakushtukiza kwa nia ya kukudhalilisha, unatakiwa ujue jinsi ya kutulia wala usikubali hata mara moja mtu akakuumiza.”

“Itakuwaje kuhusu sisi wenyewe Net? Unaweza ukaniamini kama ambavyo ungemuamini mwanamke ambaye hakupita mapito kama yangu? Sitaki kuja kuumia tena. Sitaki uje unionyeshe upande wa pili wa maisha ambao sijawahi ishi, halafu ukanikimbia.” Tunda alianza kutokwa na machozi tena.

“Sijawahi kupendwa na kuthaminiwa tokea mtoto. Wala sijawahi kuishi kwenye familia na mimi nikahusishwa na kuthaminiwa mawazo yangu. Naogopa usije kunionjesha hayo maisha halafu baadaye ukaja kuniacha, Net au tukashindwa kuishi kwa amani sababu yakutokuniamini kila ninapokuwa na mtu mwingine au nimechelewa kurudi nyumbani.”

“Naomba Mungu anisaidie Tunda. Sitakuumiza hata kidogo. Nimeamua kuwa na wewe nikiwa nakufahamu vizuri sana. Sijakurupuka. Ni kitu ambacho nishajiuliza maswali yote ambayo wewe unaniuliza sasa hivi na Mungu amenisaidia kupata majibu yake. Hakuna kipya kitakachobadilika.”

“Nakupenda, na nimekusudia uwe mke wangu. Nakuahidi kukupenda Tunda. Nitakupenda kwa dhati na kukuheshimu, kama Tunda huyu niliyenaye sasa hivi hapa mkononi. Tunda aliyeoshwa na kutakaswa na damu ya Yesu. Sitaishi na Tunda yule wazamani.” “Asante Net. Nakushukuru kunipokea.” Tunda alijirudisha kujiegemeza kwa Net na kukunja miguu juu ya kochi. Wakatulia kila mtu akiwaza lake kama wasio amini.

Tunda alijituliza pale akiogopa hata kusogea. Kichwa pembeni ya shingo ya Net aliyekuwa amepitisha mikono yote miwili juu yake, akimpapasa taratibu kwa mkono mmoja mgongoni. Wakatulia. Kama ambaye haamini, akanyanyua uso kumtizama Net kuhakikisha kama ni yeye. Macho yakagongana. “Nimefurahi sana Net. Siamini!” “Hata mimi nimefurahi.” Tunda akajiweka sawa.

“Sasa ndio tunafanyaje?” “Hatuna sababu yakusubiri tena. Nataka kukuoa Tunda. Nataka uwe mke wangu. Nitaenda kuongea na mama, na wewe kamwambie Mchungaji wako. Taratibu za harusi zianze.”  Tunda akacheka. “Siamini kama na mimi nimepata mtu wa kunioa! Nilijikatia tamaa.”

“Naomba salamu za kukumbatiana na Julius ziwe mwisho.” Tunda alicheka kwa mshangao. “Husahau!?” “Nisahau wakati pale nilikuwa nammezea mate jamaa? Yeye amekumbatiwa wakati mimi sijawahi kukumbatiwa hata mara moja!” Tunda alizidi kucheka. “Eti na mimi nitaanza kuvaa pete za ndoa!” Net akacheka lakini Tunda alipooza ghafla na kujitoa mikononi mwa Net.

“Nini tena?” “Nisipo zaa je? Kama waliharibu kizazi changu wakati wananitoa ile mimba, nikapoteza uwezo wa kuzaa?” “Sijui Tunda. Ila nakuomba usiniingizie hofu nyingii. Naomba unipe nafasi nifurahie hii hatua niliyofikia leo. Hujui nilivyoteseka.” “Samahani Net. Nataka tusiharakishe, tupate muda wakutafakari kwanza tusije tukakosa raha baadaye na kulaumiana.” Hofu ilishamwingia Tunda, akamkumbuka Tunda halisia.

“Naomba unielewe Tunda. Haya mahusino yetu kwako nimageni, lakini si mimi. Mwenzio nimekuwa nayo kwa muda mrefu sana. Nakwambia hayo maswali yote nimeshajiuliza na Mungu amenipa jibu. Nikwambie swali jingine ambalo nimeshajiuliza?” “Swali gani tena!?” Tunda akauliza, akisikika kuishiwa nguvu.

“Itakuwaje kama tukienda kupima, nikakukuta umeathirika? Umeshafikiria hivyo?” Tunda alibaki kama amemwagiwa maji yabaridi. Akajivuta pembeni kabisa. “Sasa hata kabla hatujafika hospitalini mimi na wewe tukapewa majibu yako, mimi nilishachanganyikiwa, nilishakuuguza, tena nilishajiona jinsi nitakavyo kuuguza peke yangu kwa kuwa watu wamekususa, nimeshalia na kuomboleza na Mungu wangu, mwishoni nikaamua kumuachia Mungu, nitembee kwa hatua. Sitaki kuleta matatizo ya siku ya kesho, leo, Tunda. Ndio maana nakuomba uache angalau nifurahie hii hatua ya leo. Naomba tutembee hatua kwa hatua, ili tusije pitwa na chochote.” Tunda alijirudisha vizuri pembeni ya Net, akanyamaza asiamini kama Net ni mtu wa kubaki naye maishani. Sio muondokaji! Amekusudia kuwa naye.

“Sasa hivi kinachofuata nitaenda kumwambia mama. Halafu nianze maisha ya kuwa mchumba wa Tunda. Niwe namtoa mchumba wangu sehemu tofauti tofauti za starehe, nifanye yote ninayotakiwa kufanya kwa mchumba wangu, kabla sijawa mume. Sitaki kupitwa na hatua hata moja kwenye maisha yako Tunda. Hata kama tutaoana mwezi ujao, nataka hizo siku zilizobaki kabla sijakuoa, nikutunze kama mchumba wangu.”

“Nataka nifurahie hatua yangu ya uchumba na wewe, bila kuazima matatizo ya kesho. Leo nataka nikufurahie, msichana niliyekusubiri, na kukutamani kwa muda mrefu sana.” Tunda alikuwa akilia asiamini. Alijutia mapenzi aliyokuwa akiyagawa kwa kujidhalilisha. Hakujua kama yupo mtu mahali fulani anampenda nakumsubiri kwa kiasi kile.

“Nilikuwa nikimuuliza Mungu kwa nini anachelewa kukukabidhisha kwangu! Nilimuhakikishia kila kitu. Nilimwapia nitakupenda mpaka kifo. Nikamwapia sitakusaliti wala kukunyanyasa. Yote hayo niliyafanya kama mwehu ili tu anipunguzie siku za kunikutanisha na wewe.” Akajiegemeza kwenye kichwa cha Tunda, aliyekuwa amemkumbatia, na Tunda alikuwa bado amekaa ubavuni kwa Net, huku amekilaza kichwa chake hapo shingoni.

“Sina cha kusema Net. Sikuwahi hata kuwaza kama unamawazo na mimi! Nilijua utakuwa ukinichukia kwa kunifumania zaidi ya mara nne, tena na wanaume tofauti tofauti! Yaani hata sikuwahi kukuwazia hata sekunde moja. Ila nilikuwa nikikuogopa sana. Kila ulipokuwa ukinifumania nilikuwa nashindwa kulala kwa hofu.” Tunda akakaa vizuri.

“Nilijaribu kujipa moyo kuwa hunihusu, sikujui wala hunijui kwa hiyo haijalishi lakini nilishindwa hujiliwaza. Nikaanza kupunguza wanaume, nikabakia na wachache watakaonisaidia kuniweka mjini, lakini pia bado niliteseka. Haya, mama Cote aliponifukuza Arusha, sikujua hata kama utajali. Nikajua utashukuru Mungu kutuliwa mzigo. Sikuwahi hata kukuwazia kama unaweza kuja kunitafuta tena, Net!”

          “Nilipokuona pale juzi, nilifurahi kukuona kama mtu muhimu ambaye umehusika kwenye maisha yangu. Lakini sikujua hata kama nina maana yeyote kwako. Sikuwa hata nikijua kama uwepo wangu kama una maana yeyote ile au unafanya kutimiza tu wajibu kama mkristo tu wakawaida. Hakika wala sikudhani kama unaweza kuniwazia hivi. Nakushukuru kwa kutokunikatia tamaa.” Net alikuwa akimsikiliza huku akitabasamu. Alimvuta mkono mmoja, akambusu na kubaki wakiangaliana.

“Sasa inabidi nirudi nyumbani tu. Nikiendelea kukaa hapa, naweza kushindwa kuondoka kabisa.” Tunda akatabasamu. “Nitakuona tena lini?” Tunda akauliza, Net akacheka. “Kila siku nitajitahidi tuwe tunaonana. Ila kesho itakuwa mchana, kuna tenda naifuatilia. Nikipata hiyo, najua itamsaidia sana mama. Mambo yake yameenda pabaya sana. Biashara zake haziendi vizuri.” “Mungu atakusaidia Net. Nitakuombea.” Net akatabasamu. “Afadhali nimepata na mke muombaji.” “Umesahau wewe ndio ulikuwa ukinifundisha?” “Siwezi kusahau. Lala. Kesho tutapata muda mzuri wakuongea zaidi.” Net akaaga na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Usingizi haukuja kwa Tunda. Alivaa haraka haraka akapanda kwenye gari yake mpaka, Tabata, nyumbani kwa Mchungaji wake. Mlinzi alipoona gari ya Tunda akafungua geti. Shida ikawa kufunguliwa mlango kuingia ndani. “Bwana Mama Penny fungua!” “Hatukusikii, tumelala.” “Sasa mbona unajibu?” “Unataka nini Tunda kwenye dirisha la chumbani kwangu?” “Kuna kitu nataka kukwambia. Siwezi kulala mpaka tuongee.” “Kuna msiba?” “Hapana.” Tunda akajibu.

“Umefukuzwa kwenye nyumba?” “Hapana.” “Basi naomba utuache mimi na mume wangu, tumelala. Washirika wote tumewafundisha kuomba. Hakuna haja yakutugongea milango usiku au simu za usiku usiku hatutaki. Kama mtu anashida, unapiga magoti unaomba, halafu Mchungaji unaonana naye asubuhi.” Tunda akaanza kucheka.

“Sasa muda wote huo unaongea hapo kitandani, mama Penny, dada yangu, si ungeshakuwa umenifungulia mlango, tumeonge, na mimi nimeondoka?” “Sitaki kutoka kitandani bwana! Wengine nyumba zetu zina AC. Usiku tunawasha baridi. Nishajifunika, sitaki kutoka kitandani. Wewe niambie ukiwa hapo hapo dirishani.” Tunda akatulia kwa muda.

“We Tunda?” Mama Penny akamwita. “Nimepata mchumba.” Akaruka kitandani nakuanza kupiga vigelegele. Akawasha taa ya chumbani kwake huku akipiga vigelegele. “Acha kelele mama Penny bwana! Watoto wamelala.” Tunda aliongea kwa sauti ya chini kidogo, kama kumtuliza. “Siamini kama nimepata harusi yakusimamia!” Tunda na Mchungaji wote walicheka kwa sauti.

“Hebu amka baba Penny, tukapange mipango ya harusi.” “Hata mchumba mwenyewe hujaonyeshwa, unataka kuanza mipango!?” “Hebu amka bwana na wewe! Yeyote tutakayeletewa huyohuyo tutampokea ilimradi na mimi nisimamie harusi.” Alimsha watoto wote kwa vigelegele.

“Ingia ndani bibi harusi wangu.” Tunda alifunguliwa mlango. “Kuna nini mama?” Penny akauliza akiwa na usingizi. “Anti Tunda anaolewa?” Pendo naye akauliza baada yakusikia vigelegele vikiendelea bila jibu kutoka kwa mama yao. “Na yule Mzungu?” Penny akauliza tena. Tunda akacheka sana. “Penny wewe! Upo kama mama yako!”

“Hebu niambie Tunda. Mchumba ni nani?” Mchungaji alitoka na yeye akakaa kwenye kochi, mkewe alikuwa akiendelea kushangilia hata mchumba hajauliza. “Acha kelele bwana na wewe mama Penny. Mchumba mwenyewe hata hujamjua!” “Atakuwa ni yule mzungu tu. Wewe hukuwaona hapa walivyokuwa wakiangaliana? Yule mzungu alimpakulia chakula Tunda. Wewe hukuona? Atakuwa ni yeye tu. Eti Tunda mdogo wangu?” “Ni yeye.” Yule mama akaendelea kushangilia.

“Afadhali tutapakata vitoto vya kizungu.” Tunda akacheka sana. “Sasa wewe Penny mwanangu utakuwa msimamizi wa nyuma. Kazi yako kuangalia shela ikae vizuri.” “Sasa nikikaa nyuma, kwenye picha si sitatokea!?” “Utatokea kwenye harusi yako.” Mama yake akamjibu na kufanya wote wacheke.

“Mama Penny naomba ukae chini bwana tuongee.” “Tunaongea nini? Hapa ni mipango ya harusi tu.” “Si ndio hivyo sasa! Mimi nilijua wewe ndiye utakuwa mpambaji wa ukumbi na Mchungaji ndiye atatufungisha harusi.” “Aka! He! Wewe Tunda ukoje? Mimi na mume wangu ndio wasimamizi. Akitaka mwenyewe atafungisha hiyo ndoa, halafu atachukua nafasi yake ya kumsimamia bwana harusi tukitoka kanisani. Lakini mimi nasimamia kila mahali.” Tunda alitingisha kichwa huku akicheka.

“Sasa nani atapamba ukumbi!?” “Mimi na wewe haituhusu, kwani sisi wanakamati bwana? Hebu tuongee mambo ya msingi.” “Haya Penny na mdogo wako, mkalale.” Baba yao akaingilia. “Lakini mimi sitaki kusimamia nyuma, dady!” Penny akalalamika. “Mama yako ameshakwambia, utulie mpaka utakapokuwa mkubwa, ukileta mchumba wako, siku yako ya harusi utasimama mbele. Sasa hivi unakwenda kulala, kesho shule. Haya simama haraka kabla sijakubadilikia.” Tunda akabaki akicheka, Penny na mdogo wake wakasimama kuelekea chumbani kwao kulala huku Penny akilalamika “Na mimi nataka kutokea kwenye picha! Sitaki kusimama nyuma.” Akapotelea chumbani kwao huku akilalamika.

“Kweli hawa watoto wamepata wazazi!” Tunda aliendelea kucheka. Waliongea kwa muda mrefu sana, Tunda akitoa historia yake na Net, tena na tena huku machozi yakimtoka. “Ulikuwa unamzungusha Julius wa watu, kumbe unaye mwanaume wako!” “Mungu wangu nishahidi mama Penny. Sikuwahi kumfikiria Net kuja kuwa naye kwenye mahusiano hata kidogo!  Hata dunia yote tungebaki mimi na yeye tu, pia nisingefikiria kama yule kaka angekuja hata kutamani niwe mpenzi wake! Sikuwahi hata kumuhisi. Net anamaadili na msimamo wakupita kiasi. Kwanza nilikuwa nikimuogopa ile yakutetemeka.” Waliongea mpaka usiku sana, ndipo Tunda aliporudi kwake.

Kwa Net!

Huku kwa Net nako, alirudi mpaka nyumbani kwao. Alimkuta mama yake sebuleni akisoma kitabu. Alipomuona tu Net akaweka kitabu chini. “Sijawahi kukuona ukiwa na furaha hivyo! Kuna nini?” “Tunda amenikubali mama.” “Hebu tulia kwanza. Tunda amekukubali!?” “Yaani ni hivi, Tunda amekubali nije kuwa mume wake.” Yule mama alishtuka sana, akavua miwani. Net alimuona jinsi mama yake alivyobadilika.

“Tunda, Tunda!?” “Ndiyo mama. Tunda.” “Sijaelewa. Tunda huyu unayemzungumzia ndiye Tunda huyu Malaya! Aliyekwisha shika mimba ya baba yake. Aliyevunja uchumba wangu na kuvunja ndoa ya Mzee Mati baada ya mkewe kujua alikuwa akihudumiwa na huyo Tunda na kumpeleka na mwenzie Meto! Aliyetembea mpaka na Gabriel, ambaye ni kama kaka yako!? Achilia mbali msururu wa wanaume za watu ambao alishakuwa na mahusiano nao kimapenzi!?”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Itakuaje? Tunda akiwa na furaha yakupitiliza, maisha ya nyuma yanapambana kumtoa Tonge mdomoni


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment