T |
unda alichoka kabisa. Akidhani
ile bibilia ingemtia hofu yule mzee, lakini ndio ikawa
njia moja wapo ya
kumtongozea. Akageukia dirishani. Moyoni akaanza kumwambia Mungu, ‘Nilikuomba unisaidie nisirudi
huko tena, lakini mtu wa kwanza unanikutanisha naye baada ya maombi, ni huyu!
Ni njia gani hii unatumia kunisaidia? Unanikutanisha na mtu kama huyu ambaye
anauwezo wa kunipa msaada wa vitu unavyojua wazi ndio ninahitaji kwa sasa! Kwa
nini hunihurumii? Nimeteseka miaka yote, ndio kwanza nafurahia utulivu nilio
nao. Umenipa furaha na amani, kisha unachukua kila kitu kwa wakati mmoja!
Umechukua kazi yangu, umenifukuza pale kwenye ofisi, halafu unaniletea mtu
wakunisaidia kurudi kwenye yale yale maisha niliyokwambia siyataki!’ Tunda
aliendelea kumlaumu Mungu kwa kunung’unika moyoni.
Akapitiwa
na usingizi, mpaka aliposhtuliwa na yule
Mzee kumwambia ashuke wakale. Tunda akakataa. “Asante, lakini sitakula.” “Kwa
nini?” “Nataka nipate muda wa kuongea na Mungu. Wewe nenda tu.” Yule Mzee
alimtizama Tunda kwa muda mrefu kidogo, kisha yeye akashuka.
Alibaki
peke yake kwenye basi, akafunga dirisha ili kupunguza fujo za watu wanaotaka
kumuuzia vitu. Akainama nakuanza kuomba upya huku akijiuliza yeye mwenyewe
maswali na huyo Mungu aliyetambulishwa na Net. Tunda aliomba huku akilia kwa
hofu ya itakuaje. Akaendelea kumsihi Mungu asimjaribu zaidi. Alijua wazi
mshahara aliolipwa na pesa nyingine alizonazo, haziwezi kudumu kwa muda mrefu.
Alifikiria
wapi pakwenda mara baada ya kushuka kwenye hilo basi! Nini chakufanya mara
baada ya kujua pakwenda! Yule mama alikuwa sahihi kabisa, hakuwa na cheti. Kama
pale kwenye ile ofisi aliweza kufanya kazi vizuri, wakaona utendaji kazi wake
na bado wakataka vyeti, nani atampa kazi bila vyeti wakati hawamfahamu? Maombi
ya Tunda yalichanganyikana na maswali mengi sana. Alibaki ameinama ili aombe,
akajikuta haombi tena anawaza tu.
Tunda na fundisho la
watoto njiani.
Aliamua
kukaa vizuri na kugeukia dirishani aendelee tu kuwaza. Aliona watoto wadogo
wawili wakicheza wakati mama zao wakiuza matunda. Mtoto mmoja alikuwa mkubwa
kidogo kwa mwenzake. Yule mtoto mkubwa alikuwa na gari alilokuwa ametengeneza
vizuri sana kwa vijiti, alivyovipangilia kwa ustadi, mpaka akatengeneza muundo
wa gari. Akaweka matairi ya mifuniko ya soda{Visoda}. Tunda alimuona jinsi
alivyokuwa akiendesha lile gari pembeni ya mama yake, akienda mbali kidogo na
kurudi, lakini si mbali na macho ya mama yake.
Mtoto wa
pili, yule mdogo, alikuwa akichezea vumbi tu, mwishowe yule mdogo akamuomba yule
mtoto mwenye gari ampe achezee na yeye. Bila tatizo, akampa.
Yule
mtoto mdogo, alionekana kufurahia zaidi lile gari kuliko mtoto mkubwa ambaye ni
mmiliki. Alitoa milio mbalimbali kwenye mdomo wake kuonyesha akiigiza mlio wa
magari ya kweli, kitu kilichomvutia Tunda na kuanza kucheka na kujikuta
akifungua dirisha na kuendelea kumtizama yule mtoto aliyeazimwa gari. Alitoa
mlio wa honi, kuweka breki kwa nguvu, huku akiendelea kucheza na gari ya
mwenzake.
Mwenye
lile gari alipoona yule mwenzake anafaidi na gari yake zaidi yake, akaamua
ampokonye, tena kikatili, kwa jeuri kwa kuwa lilikuwa lake. Tunda akashtuka kwa
kumuhurumia. Ulizuka ugomvi kati yao, lakini mwishowe mwenye nacho alishinda
baada ya wazazi kuingilia kati.
Yule
mdogo alianza kulia sana, akitaka lile gari ambalo halikuwa lake. Na yule
mwenye nalo akaanza kuchezea kama yule mdogo alivyokuwa akifanya. Alitoa milio
ileile, na alifanya zile zile mbwembwe kama mwenzake alivyofanya lakini
haikupendeza hata kidogo. Mwishowe akaigiza kuweka breki kama yule mtoto, lile
gari liligonga jiwe na kuharibika kabisa.
Lakini
kabla ya lile gari kuharibika. Wakati yule mkubwa akiendelea kuchezea gari
lake, yule mdogo aliacha kulia, akaokota boksi la biskuti, akatumia meno yake
kutengeneza madirisha na mlango. Kisha akaokota pale pale vijiti vile vya
kutolea uchafu kwenye meno ambavyo watu walisha tumia na kutupa tu.
Akaunganisha kadhaa ili viwe virefu na vigumu. Akatoboa sehemu ya kuchomeka
matairi, akaweka vile vijiti. Tunda bado akiwaangalia tu. Yeye ndani ya basi,
wale watoto nje pembeni kwa mama zao, na wao wakiongea yao na kubembeleza
wateja.
Kwa kuwa
yule mtoto mdogo hakuwa na visoda, au mifuniko ya chupa za soda, yeye aliweka
makaratasi magumu kidogo ndio yakawa matairi yake. Akaokota tena kijiti au mti
mdogo, lakini mrefu na mwembamba akachomeka nyuma ya lile boksi, iwe kama
usukani wake wakuongoza lile gari. Tayari akawa ametengeneza gari zuri tu, tena
kwa muda mfupi, akaanza kuliendesha.
Wakati
ndio analifurahia gari yake hiyo, ndio mwenzake akapata ajali na yakwake,
ikaharibika. Kwa hiyo akabaki yule mdogo ambaye alinyang’anywa gari, akiwa na
lake. Tunda alimuona yule mdogo akicheka sana. Akimcheka mwenzake, yule mkubwa
aliyekuwa amekaa chini hana tena gari. Lilikuwa ni tukio la muda mfupi tu,
lakini lilichukua akili za Tunda zote na kumfanya atulie na kutafakari.
Basi lilianza kuondoka huku bado Tunda
akiwawaza wale watoto. Alijiambia ni ujinga kuwaza jambo la kitoto kama lile,
lakini bado akili ilimrudisha pale kwenye wale watoto. Akasikia swali mayoni mwake,
‘Kama yule mtoto
asingepokwanywa lile gari, je angepata wazo la kutengeneza gari lake?’
Tunda alifikiria kidogo akaamua kujijibu. ‘Lakini
kweli! Afadhali alivyopokwanywa akapata akili ya kutengeneza gari lake.’ Tunda akajijibu. ‘Lakini alilia sana!’ Tunda akawaza kwa kumuhurumia yule mtoto.
Likapita swali jingine. ‘Kama angeendelea kulia pale alipokuwa amekaa pembeni ya mama
yake, bila kusimama na kuchukua hatua ya kutengeneza gari lake, angepata gari
jingine?’ Tunda akafikiria na kukumbuka lile tukio tena. Alikumbuka
jinsi mama yake alivyokuwa akimbembeleza kwa kumpa matunda ili atulie lakini
yule mtoto alikataa kata kata, aliendelea kulia akitaka gari ya mwenzake mpaka
alipoamua kunyanyuka na kutengeneza gari lake.
‘Afadhali alitumia akili. Angekubali tu kubembelezwa na mama yake akala
yale matunda, angesahau kabisa kitu anachokita, gari. Akabaki hana gari mpaka
sasa.’ Tunda akajijibu na swali jingine
likamjia tena. ‘Kwani angekubali faraja ya mama yake,
akaacha kutengeneza gari yake, ingeondoa ujuzi alionao wakutengeneza gari?’ ‘Hata
kidogo. Si angekuwa ni mjinga tu, amekataa kutumia ujuzi wake na kubaki
akililia gari la mwenzake!’ Tunda akajibu haraka haraka tena kwa hasira.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
hapo Tunda akapitiwa na usingizi, kisha akashtuka sana. Ikawa kama kitu
kimemuamsha huko usingizini “Mimi ni mjinga sana, hata yule mtoto anaakili
kunizidi mimi!” Tunda akamwambia yule Mzee na kumuacha akimshangaa. “Sipo hata
nusu ya yule mtoto!” Tunda akarudia kumsisitizia yule Mzee, lakini yule mzee
aliyekuwa amekaa pembeni yake akamtongoza, alijua Tunda anaota kwa kuwa alikuwa
amelala. “Binti, punguza sauti. Ulikuwa umelala, na hapa tupo kwenye gari.”
“Hapana sioti.” Watu wapembeni yao waliwageukia na wa mbele pia waligeuka kwani
Tunda alikuwa akiongea kwa sauti iliyojaa kufunguka kimawazo.
“Ni
kweli yule mtoto ana akili sana. Sikiliza nikwambie hiki kisa, kimetokea sasa
hivi mliposhuka kwenda kula.” Tunda akasimulia kile kisa chote cha wale watoto
na kuvuta masikio ya abiria wengi sana ndani ya lile basi. “Nisikilize vizuri.
Mimi nimetoka Arusha sasa hivi sababu ya kufukuzwa kazi ambayo niliifanya
vizuri sana. Sikuwahi kuiba, wala kukosea hata siku moja. Niliifanya kwa makini
na juhudi zangu zote. Niliifanya ile kazi mpaka usiku bila kuomba malipo ya
ziada.”
“Lakini
leo asubuhi mwenye ofisi amemleta mtu mwingine, na kunifukuza mimi kazi
kikatili, kwa kuwa tu sikuwa na vyeti.” “Kwa nini na wewe huna vyeti?” Yule
Mzee aliuliza swali lililomfanya Tunda aliyekuwa akisimulia kwa kuchangamka
apooze ghafla. Abiria wengine wakaongezeka kusikiliza. Maana wengi walikuwa
wakisinzia mara baada ya kula chakula basi liliposimama. Ila kwa sauti ya
kuchangamka ya Tunda, hata waliokuwa wamelala, wakaamka na kuendelea
kumsikiliza Tunda aliyegutuka baada yakubaini ule mfano unamuhusu. Kwanza kwa
sauti hiyo ya Tunda, lazima utataka kuisikiliza hata ukiwa mbali, utageuka tu
ili kutaka kuiweka kwenye sura husika. Kuiona sura ya hiyo sauti.
“Sikusoma
baba yangu. Nilipata hiyo bahati ya shule lakini ilichanganyikana na majanga
mengi yaliyonifanya nishindwe kusoma kabisa. Sikubahatika kulelewa na wazazi
wote wawili. Nimekuwa nikihama hama huku na kule.” Tunda akaelezea kisa chake
kilichowavuta watu wote sasa kwenye lile basi huku wakimuomba aongeze sauti.
Akapiga magoti kabisa kwenye kiti chake, nakusimulia. Wazazi wengine walianza
kumtukana mama yake Tunda, wengine bibi, wengine mama wa kambo wengine shangazi
ilimradi basi zima pakageuka kukawa gumzo juu ya Tunda.
“Lakini baadaye niliishi maisha machafu sana,
mpaka nikakutana na mtoto wa huyu mama aliyenifukuza kazi.” Napo hapo Tunda
aliwaacha midomo wazi. “Mmmh! Pole sana mwanangu. Dunia mzunguko! Inaweza
kukufanya ukafanya jambo ambalo hata hukutegemea.” Mama mmoja mtumzima pembeni
yake aliongea.
“Ndio
muache kuwasema machangudoa. Hamjui kwa nini wanafanya wanayofanya.” Dada
mwingine kiti cha mbele alidakia. “Ndio maana yake. Maana kuna watu wanapenda
kweli kuhukumu watu.” Mwingine akadakia. Abiria wengine wakawageuzia na wao
macho kuwasikiliza na wao wakizungumza kwa jazba.
“Lakini
mimi Mungu amenipa nafasi nyingine. Mtoto wa huyo mama alinirudisha kanisani,
nikatubu, Mungu amenisamehe. Nilitolewa majini kwa mapepo kwenye huu huu mwili
watu waliokuwa wakiutamani na kutumia. Wasijue walikuwa wakilala na majini pia.
Anyways, baada ya yote, huyo kijana akanipa na hiyo kazi niliyopokonywa.” Tunda
aliwakata maneno.
“Bahati
yako wewe ulimpata huyo kijana. Sasa unakuta ndio kama hivyo mtu hana maisha,
leo unamwambia aache uchangudoa, unataka aishije? Wewe umepata kazi, ndio maana
umeacha.” Huyo dada aliongeza, kila mtu alihisi yule dada na yeye ni changu.
“Lakini nisikilize dada,
nakwambia leo nimefukuzwa kazi. Hapa nilipo naelekea Dar, sina pakwenda, sijui
chakufanya na wala simfahamu mtu yeyote huko Dar japo nimeishi kwa miaka mingi
na nilikuwa na kwangu tena pazuri, kama nilivyowasimulia. Nipo kama hivi
mnavyoniona.” Tunda akaendelea akiwa amejawa nguvu hata asijue amewezaje
kuzungumza vile bila woga.
“Mlipokuwa
mmeenda kula nilibaki humu ndani nikilia, ndipo nikaona kisa cha hawa watoto.
Nikikwambia kulia, nilianzia kulia kule hotelini. Lakini huu mfano wa huyu
mtoto mdogo, umenifundisha au unanihusu. Huku kulia kutanichelewesha na mimi
kupata changu. Kurudi kuwa Changu ni kama nakubali faraja ya matunda ya muda
mfupi, itakayonifariji kwa muda mfupi tu, nakusahau nini nataka katika maisha.”
Tunda akaendelea.
“Lazima nisimame na mimi nitengeneze chakwangu.
Hata kama sijasoma, na mimi nitaanza kwa kuokota maboksi, vijiti vyakutolea
uchafu kwenye meno ambavyo watu wanatupa, nitatengeneza gari yangu kama yule
mtoto.” Kisha akauliza swali. “Kwani huyu aliyetengeneza hili basi tulilopanda
sasa hivi, si binadamu kama sisi tu? Alikubali kuacha vishawishi vyote,
akajikana na kukaa chini, akaunganisha vyuma na mipira mpaka tukaliita basi.”
“Basi na mimi nitatafuta cha kwangu. Sitaki kulia
tena wala kumchukia mtu. Nitajichelewesha kupata vyangu.” Tunda alishangaa
kuona watu wote kwenye basi wakimpigia makofi. Alishtuka sana, kwani bado
alikuwa amepiga magoti kwenye kiti chake akiongea kwa sauti na yule dada kwenye
kiti cha mbele kabisa aliyekuwa akitetea
uchangu. Akawa kama ameshtuliwa, akarudi kukaa vizuri na aibu ya ghafla usoni.
“Unaakili binti. Nakupongeza.” Yule mzee
aliyemtongoza na kumpa wazo hata lakumtafutia hoteli akajikuta akimpongeza tena
Tunda. Lakini kwa sauti ya chini iliyojaa aibu kidogo na kujirudi. “Asante.”
Tunda akacheka taratibu. “Na naomba nikuombe radhi.” “Wala usijali baba yangu.
Ulikuwa mtihani wangu huo. Mungu alitaka kunipima, ajue nimeamua vipi kutorudi
nyuma. Pale uliponiambia vile, ukaniona nimegeuka dirishani, nilikuwa
nikimlilia Mungu aniepushe na watu kama wewe. Kwa kuwa ndivyo nilivyoanza kazi
ya uchagudoa hivyohivyo.”
“Nilitoka hospitalini nikiwa sijui pakwenda. Wakati
nimeenda kula mahali, nikakutana na mmiliki wa hilo eneo. Ndiye niliyeanza naye
hiyo biashara. Akaniweka hotelini kama vile ulivyonishawishi mwanzo. Sasa na
wewe ulivyonitongoza, na ahadi ya pakuishi, niliumia sana. Nikakumbuka
niliingia kwenye ule uchafu mwanzoni kabisa sababu sikuwa na pakwenda. Sasa
nikaona historia inataka kujirudia tena. Inakuwa vile vile na sababu ile ile.
Ila nimekusudia baba yangu, sitarudi nyuma. Hata kama nitalala stendi ya
mabasi, acha nihangaike tu mpaka nione mwisho ni nini.” Yule mzee alijisikia
vibaya sana, na dhamira ikamsuta.
“Binti naomba unisamehe sana. Nimepitiwa na shetani
tu.” Tunda akacheka. “Yameisha baba yangu.” “Ila kile chumba nilichokwambia ni
kweli kilikuwepo, ila sijui kama dalali alishapata mteja! Kama upo tayari
kuishi maeneo ya Temeke, naweza kumpigia simu yule dalali ili asikikodishe tena
ili wewe ukaishi huko.” “Kodi ni kiasi gani?” “Yule mzee akamtajia.” Tunda
akafikiria kidogo.
“Naomba nikulipe ya miezi mitatu wakati najipanga
upya.” “Nitaongea na mke wangu tuone, maana ndio nyumba anategemea sana yeye.”
“Unaweza kuwasiliana nao hao watu wawili ili mpaka tukifika Ubungo kituo cha
mabasi, niwe najua kama nimepata au nihangaike kwingineko?” “Sawa.” Yule Mzee
akakubali.
Alimpigia simu dalali, dalali akamwambia ndio ametoka
kumpeleka mtu na mkewe hapo kwenye hicho chumba, wamepapenda na wamekubaliana
kesho awapeleke kwa mke wa yule Mzee wakaandikishiane mkataba. “Basi hebu usubiri kidogo, usikikodishe kwanza niongee na mke
wangu.” “Wanalipa kodi ya mwaka Mzee.” “Naelewa. Lakini hebu subiri.”
Akakata simu.
“Vipi? Amesemaje?” Tunda akauliza kwa wasiwasi
kidogo. “Anasema amepata mteja, tena mwenye kodi ya mwaka. Ngoja nimpigie simu
mke wangu kwanza kabla hajawakodisha.” Tunda akakosa raha. Akabaki kimya.
“Mimi nitalipia hiyo kodi ya huyu binti.” Tunda akashtuka
sana. Akamgeukia huyo aliyesema. Alikuwa ni kijana tu. Alikuwa amependeza,
akaonekana nadhifu, kijana aliyefanikiwa. Shingoni alikuwa amevaa cheni
aliyofanya juhudi za makusudi kuonekana. Ilikuwa dhahabu. Tunda muelewa vitu
vya thamani, aliweza kutambua uhalisia wa ile cheni shingoni kwa yule kaka. Na
saa nzuri sana tena ya thamani. Alikuwa amekaa kiti cha nyuma kabisa. Watu wote
wakamgeukia.
“Kwamba?” Yule Mzee akauliza kutaka uhakika kabla
hajazungumza na mkewe. “Nimesema mimi nitalipa hiyo kodi ya mwaka mzima ya huyo
binti. Kama kumtia moyo kwa maamuzi magumu anayofanya.” Tunda aliogopa sana.
Hakutaka kuja kudaiwa mapenzi baadaye. “Na wala hizo pesa hutazipata kwangu,
utazikuta kanisani kwetu. Nitamkabidhi mama Mchungaji wetu. Utakapokuwa tayari,
ukiipenda hiyo nyumba, wewe njoo kanisani kwetu utachukua pesa yako. Hata kama
hutaipenda hiyo nyumba, tafuta nyingine, ila ujue pesa ya kodi ya mwaka mzima
unayo tayari.” Tunda alianza kulia kwa furaha.
“Sikilizeni jamani.” Yule kaka akasimama. Akaanza
kuongea mambo ya Mungu. Watu walikuwa wakimwangalia bila kupepesa macho. “Huyu
Mungu yupo na wakovu ni halisi. Ukubali ukatae.” Yule kaka alianza kwa kusema
hivyo.
“Wengine tumeua, tukauza madawa ya kulevya,
tukavunja majumba ya watu, tumepita humo magerezani kama watu wanavyokwenda
dukani kununua sukari, mpaka Mungu alipoingilia kati. Huyu dada anachoongea
mimi namwelewa kabisa. Kuna mahali unapitishwa na maisha, msaada uliobaki pekee
nikusalimisha maisha kwa Yesu. Ni uamuzi mgumu, lakini unalipa sana baadaye
unapoamua kukubali nakubadilika.” Yule kijana akaendelea.
“Mimi nilipokubali kuokoka, nilipoteza kila kitu
mpaka mke alinikimbia jinsi nilivyofilisika. Tena akaolewa na mwenzangu
tuliyekuwa tukifanya naye biashara zetu za magendo. Nilirudishwa chini kabisa,
nikawa masikini, omba omba. Nilikuwa na sababu zote zakurudi kufanya niliyokuwa
nikifanya kwa kuwa nikweli nilikuwa nikitengeneza pesa ya haraka, lakini sikuwa
na amani niliyokuwa nayo kama baada yakumpa Yesu maisha.”
“Wengi walinicheka na kuniambia nimepotea njia,
lakini nilijua hawajui vile ninavyojisikia moyoni. Nilirudi kuosha magari
Ubungo, mpaka nilipopata wazo lakurudi migodini kutafuta madini. Sikuwa na
maandiko mengi kutoka kwenye bibilia, na nilikuwa mchanga sana Kiroho, lakini
nilikuwa nikimkumbusha Mungu kuwa ‘fedha
na dhahabu ni mali yake.’ Na mimi ni mali yake, nikawa nikimuomba Mungu
anikutanishe navyo. Basi kila nilipokuwa nikizama kule machimboni nilikuwa
nikimkumbusha Mungu hayo maneno. Ilinichukua miaka miwili migumu ya shida, nikiwa
kule kwenye machimbo ya dhahabu, mpaka nikafanikiwa. Na mimi sasa hivi namiliki
sehemu yangu huko.”
“Nilipochelewa ndege leo asubuhi, na kukosa gari ya
kukodi kunipeleka Dar, nilipata amani sana yakupanda hili basi, kwani imekuwa
muda mrefu, tokea nipande basi. Nimefurahi sana kukutana na huyu dada. Na
inawezekana lilikuwa kusudi la Mungu ili nikutane na Tunda. Mungu akubariki
sana dada yangu.” Akamtizama sasa Tunda, maana alikuwa ni kama anazungumza na
basi zima.
“Hakuna sababu yeyote itakayokufanya kuishi kwenye
dhambi na ikawa sawa. Hakuna. Hata ukijitetea vipi, hakuna. Dada Tunda
nakuombea Mungu akutie nguvu, umeanza hii safari si rahisi, lakini Mungu
hatakuacha, na kwa kuwa umefunguliwa ufahamu wako mapema, naona hutapata shida
kama wengine.” Yule kaka akaendelea.
“Tatizo la wana wa Mungu wengi ni pale tunapoonywa
na kukataa kubadilika. Au pale tunapoonyeshwa njia, tunakataa kufuata njia ya
Mungu, na kutengeneza njia zetu. Tunachelewa na wakati mwingine hatufiki
kabisa. Tunakubali faraja kama wewe ulivyosema. Faraja ya matunda, nakusahau
vitu vikubwa tunavyotaka. Kama Mungu amekwambia akota boksi la biskuti
utengeneze gari, okota na tengeneza. Acha ubishi, huwezi kujua katika kuinama
huko, utaokota nini kingine!”
“Wengi wanapenda kuletewa wakiwa wanaomba Mungu.
Haiwi hivyo kabisa. Muujiza wako uko pale unaponyanyuka na kuchukua hatua.
Pengine yule mtoto asingekubali kutengeneza gari yake, ungekuta bado analia
mpaka sasa, na asingegundua mbali ya vijiti, hata boksi pia linaweza
kutengeneza gari. Tusibaki kung’ang’ania vya watu. Tutafute vya kwetu.” Yule
kaka aliongea kwa mifano huku akisema maandiko kwa kichwa kitu kilichomshangaza
sana Tunda.
‘Mwenzangu
anaonekana amekaa kwenye wokovu muda mrefu! Anauwezo mkubwa wakusema maandiko
ya bibilia bila kusoma!’ Tunda aliwaza.
Alishangaa uweza wa kuchanganya kila analoongea na neno la Mungu. Ilimtia moyo
sana Tunda. ‘Kweli huyu Mungu ana watu
wengi! Wengine wanampenda na kuishi kwa dhati, wengine wanacheza. Ni uamuzi
wako wa kuamua uishije naye.’ Tunda aliendelea kuwaza wakati yule kaka
akizungumza mpaka akamaliza na kurudi kukaa nakuacha watu wote kimya kila mtu
akitafakari lake.
Walipofika Ubungo, yule kijana akamsogelea Tunda,
akampa kadi yenye mawasiliano ya Mchungaji wake. “Kuanzia kesho ukimpigia simu atakuwa
na pesa yako. Mungu akubariki sana, na kamwe usirudi nyuma.” “Asante sana kaka
yangu.” Yule kaka alikuja kufuatwa na gari nzuri ya kisasa, akaondoka. Tunda
alibaki ametoa macho. Alipokea muujiza wake bila kutarajia.
Maisha yamrudisha Tunda Jijini Dar, Na bila kutarajia, katikati ya
Jaribu kali, pakatokea mlango wake wakutokea.
Tunda
hakutoka hata hapo kituoni Ubungo. Akaenda kwenye ile hoteli pale pale ndani ya
Ubungo. Alishalala hapo na baba Tom, kwa hiyo alipafahamu. Akachukua chumba
hapo. Kulikuwa kumejaa kumbukumbu ya mambo mengi aliyoyafanya humo ndani ya
hiyo hoteli na baba Tom, lakini ikawa siku hiyo nayo amemuona Mungu. Akatulia
kwa muda akiwa amekaa kitandani tu. Asiamini yupo hapo na hata siku hiyo,
katikati ya jaribu gumu, lakini hana mtu anayetakiwa kumuhudumia kimapenzi ili
kupata pesa.
Akajisiki
machozi yakianza kumtoka. Akaamua kupiga magoti na kumshukuru Mungu huku
akilia. Alikaa kwa muda mrefu magotini akilia mbele za Mungu wake, akaishia kujiambia
hataweka kitu mdomoni mpaka mambo yake yakae sawa. Mpaka aushuhudie muujiza
wake kwa macho. Ni kama aliamua kufunga.
Siku
inayofuata, aliamua kutafuta sehemu ya kulipia ya kupiga simu. Akampigia simu
huyo Mchungaji ili kujua kama kweli kuna pesa au la. Mchungaji akamwambia ni
kweli mkewe alipewa pesa na kupewa maelekezo amkabidhi yeye. Tunda alifurahi
sana. Kilichofuata ni kwenda kuona hicho chumba. Yule mzee wa kwenye basi
mwenye nyumba alimpa namba yake ya simu na ya dalali. Alishazungumza na dalali,
akamwambia atamsubiri Temeke hospitali ndio kituo atakachokitumia kufika kwenye
hiyo nyumba.
Bila
kupoteza muda, Tunda akiwa ameacha mizigo yake hapo hotelini, akapanda daladala
mpaka Temeke kuona hicho chumba. Na kweli, aliweza kumtambua huyo dalali kwa
nguo alizomwambia atamkuta nazo, kwa kuwa Tunda alimwambia hana simu,
amwelekeze alivyo ili asimpotee. Akamchukua kutoka hapo kituoni mpaka kwenye
hicho chumba. Tunda akaridhika nacho.
Akapapenda,
akamuomba yule dalali atumie simu yake. Tunda akaongeza muda wa maongezi,
akampigia tena simu yule Mchungaji, akampa namba ya simu ya mkewe. Tunda akampigia
simu mke wa Mchungaji, yule mama akaamua amfuate.
Baada ya
muda kama wa lisaa, alishangaa gari nzuri sana, SUV nyeupe, kubwa, imevimba
vizuri, ikasimama mbele kidogo kituoni, pale pale Temeke hospitalini kama
walivyokubaliana. Tunda na yule dalali wakamuona mwanamke akishuka kwenye hiyo
gari. Alikuwa mtanashati, wakisasa. Akajitambulisha na kumwambia yeye ndiye
waliyekuwa wakiongea naye kwenye simu, akamwambia wengi wamezoea kumwita mama
Penny. Tunda akamsalimia na kujitambulisha na yeye.
Yule
dalali akawapeleka kwa mwenye nyumba. Hakuwa akiishi mbali na hapo. Mama
mchungaji akalipa ile kodi yote, Tunda akakabidhiwa funguo.
“Una kitanda?” Mama Penny akamuuliza wakati akimrudisha
Tunda hotelini. “Ndiyo. Nina kila kitu, lakini nimefungia mahali. Itabidi kesho
nitafute gari nihamie kwangu.” “Usiwe na wasiwasi, nitawatuma vijana wa pale
kanisani na gari ya kanisa ikusaidie kuhama.” Tunda hakuwa akielewa
kinachomtokea.
Akamgeukia mama Penny. “Nakushukuru sana dada
yangu. Mungu akubariki. Asante kwa kila kitu.” “Karibu.” Alijibu kwa ufupi tu. Akamshusha
hapo hotelini Ubungo, akaondoka na kumuacha Tunda na funguo za chumba chake na
sebule.
Ile furaha ikageuka kilio kwa Tunda. Alilia Tunda,
asiamini kama Mungu amemrudishia kwake. Kwa Tunda huo ulikuwa ni muujiza wa
kama kumfufua maiti. Ilikuwa ni zaidi ya kuponywa. Historia yakufukuzwa kwenye
majumba ya watu, kwa Tunda, haikuacha kujirudia.
Ametoka kufukuzwa kwenye nyumba ya watu Arusha.
Mama Cote alimtoa nyumbani kwake usiku. Akampokonya chumba alichopewa na Net,
funguo za gari na kazi. Anampa nini huyo Mungu kumfungulia mlango mkubwa kama
huo! Tunda alilia, asijue nini chakusema mbele ya huyo Mungu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake asubuhi alipigiwa simu na mtu wamapokezi
kuwa anamgeni pale mapokezi. Alipotoka alishangaa kukutana na mama Penny na
vijana. “Uliamka salama?” “Ndiyo. Japo sijala.” “Sasa itabidi ujikaze.
Nimewakamata hawa vijana wakusaidie kuhama kabla siku haijaanza, wakakimbilia
kwenye majukumu yao. Wakishakuhamisha ndipo tutatafuta sehemu ya kula.” “Sawa.
Nashukuru sana.” Tunda akachukua mizigo yake yote aliyokuwa nayo pale hotelini,
wakaweka kwenye gari ya mama Penny. Akalipia kile chumba, wakaondoka pale.
Tunda alikuwa kwenye gari ya mama Penny, na wale
vijana walikuwa wakiwafuata nyuma kwenye gari kubwa kidogo, aina ya Kenta.
Walitoka hapo Ubungo kuelekea Salasala nyumbani kwa Net alipokuwa ameacha vitu
vyake.
Walipofika pale, akawaambia wasubiri nje akagonge kwanza.
Aliwaambia hiyo nyumba inalindwa na mbwa mwenye mafunzo ya kijeshi. Ndiye Max.
Tunda alishapewa habari za Max. Net alikuwa akimsifia sana huyo mbwa. Alikuwa akisema
kwa huyo mbwa mmoja tu kulinda hiyo nyumba yake, ni sawa na kulindwa na askari
watatu wa kimarekani, tena waliokwisha kwenda kupigana vita huko Iraq. Huyo Max
alikuwa akihudumiwa nakutunzwa kwa hali ya juu.
Tunda aligonga kengele nje ya geti, baada ya muda
Emma akatoka. Wakasalimiana, akamwambia bado Net hajarudi nchini. Akamweleza
kuwa amefika hapo na wale watu kuchukua baadhi ya vitu vyake. Emma alikwenda
kumfungia Max, ndipo akarudi kufungua geti na ile sehemu alipohifadhiwa vitu
vyake.
Kutokana na ile sehemu kuwa ndogo sana, ilimbidi
Tunda kuchukua vitu baadhi, vingine akaacha pale pale. Emma alivifunika vile
vilivyobaki kama mwanzoni ili visiingie vumbi, wao wakaondoka. Huku Tunda
akiviambia vitu vyake vilivyobaki pale kwenye stoo ya Net, ‘ipo siku
tutarudi kuwa pamoja. Nipeni tu muda.’ Roho ilikuwa ikimuuma sana Tunda. Ni
kweli alikuwa na vitu vizuri. Hata wale vijana waliokuwa wakimsaidia kubeba,
walisifia na kuongeza umakini kwenye kubeba.
Walimrudisha mpaka Temeke kwenye chumba chake,
wakamsaidia kupanga vile vitu, kisha wale vijana wakaondoka. Tunda alikuwa
akicheka sana jinsi wale vijana walivyokuwa wakitaniana na mama Penny.
Walionekana wamezoeana vizuri. Yule mama alipohakikisha Tunda ameweka kila kitu
chake vizuri, alimchukua mpaka nyumbani kwake Tabata.
Walimkuta dada wa kazi, akiwa anaandaa chakula cha
mchana. Na yeye yule mama akaingia jikoni nakuanza kumsaidia yule dada huku
akimuuliza maswali Tunda. Baada ya muda mfupi sana, Tunda akajisikia yupo
nyumbani. Mama Penny alikuwa mcheshi wakupitiliza.
Mchungaji naye akaingia. “Wewe siulikuwa ukicheka
kila ninaloongea? Sasa kaja mwenyewe, utapasuka mbavu.” Tunda alikuwa akicheka
sana. Mchungaji na mkewe walikuwa kama ni mtu na rafiki yake. Walitaniana kwa
kila kitu.
“Hivi kuna wakati huwa wanakuwa serious hawa?”
Tunda alimuuliza msichana wa kazi. “Mmh!
Sikumbuki. Labda wakiwa kanisani kidogo, lakini watu wameshawazoea. Mtakaa
mkicheka hapa, mpaka mnaenda kulala. Hawaishiwi maneno hao na vituko.” Tunda
alikaa hapo mpaka usiku akarudishwa kwake na yule mama.
“Kesho unaratiba gani?” Yule mama akamuuliza Tunda
kabla hajashuka. “Bado natafuta kitu chakufanya.” “Sasa mimi ninafanya kazi ya
kupamba kumbi za sherehe. Kesho nina kwenda kupamba ukumbi mahali. Kuliko ukae
tu nyumbani, ni heri twende wote. Mimi sipendi watu wanaokaa kaa kihasa hasara,
mwishowe shetani anapata nafasi ya kukupa kazi zake.” Tunda akacheka.
“Unafikiri nakudanganya? Shetani anapenda mijitu
isiyo na kazi. Iliyokaa kaa tu haina kazi zakufanya, ndiyo anaanza kuipa kazi
zakijinga.” “Basi tutaenda wote dada yangu.” Yule mama akacheka kidogo kama
aliyefurahia utayari wa Tunda.
“Sasa mimi mambo yangu ni asubuhi ili jioni niwe na
familia yangu. Kwa hiyo asubuhi nakuja kukufuata. Au unasemaje?” “Sawa kabisa.”
Yule mama akacheka, akafungua loki ya mlango pembeni ya mlango wake, ndipo
Tunda akaweza kufungua mlango wake, wakaagana
na kushuka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alianza kulia tena mara baada yakufika chumbani
kwake, akapiga magoti pembeni ya kitanda chake. Alishindwa hata kumwambia Mungu
asante. Alibaki amepiga magoti akilia. Moyo wake ulijaa shukurani sana mbele za
Mungu. Nyumba ilikuwa nawapamgaji wengine wanne, wote walikuwa na familia
kasoro Tunda. Ilikuwa uswahilini tu, tena wala si uzunguni kama alikokuwa
akiishi karibu na baharini.
Uswahilini hapo ni kelele mida yote tena kitanda
chake kiliwekwa pembeni ya dirisha alilokuwa akisikia kila kitu wapita njia wakizungumza
nje. Choo anatumia na watu zaidi ya 15. Alishaambiwa kuna zamu za kusafisha
sijui choo, uwanja na mambo mengi. Ni maisha ambayo hakuwahi kuishi binti huyo.
Lakini alijawa na furaha ya aina yake. Alikubali yote bila shida. Furaha
aliyokuwa nayo moyoni, ni kama alipewa jumba la thamani sana.
Alipanda kitandani kwake, asiamini kama amerudi kukilalia
kitanda hicho alichokipenda na kukithamini sana. Aligaragara kwenye hicho
kitanda akinusa hayo mashuka yake kwa furaha sana. Akaanza kuongea na vitu vyake
kama binadamu. Akakumbuka kazi aliyoambiwa atafuatwa asubuhi asubuhi. Ikabidi
alale haraka ili aamke akiwa na nguvu.
Tunda aanza Safari ya Kupata chake. Bila kujijua, kwa kutii agundua
kipaji chake.
Aliamka asubuhi na mapema kuwahi
kuoga kabla wengine hawajaamka na watoto wao, akachelewa. Akaoga na kuvaa
akabaki kwenye kiti akimsubiria mama Penny. Akasikia mlango wa bati, mdogo tu wakuingilia
ndani ukigongwa, akajua ni mama Penny. Akatoka akiwa amebeba na pochi yake, ni
kweli alikuwa mama Mchungaji. Wakasalimiana, wakarudi kwenye gari na kuondoka.
Na hilo likamfurahisha mama Penny, hakutegemea kumkuta akiwa tayari kwa kiasi
hicho.
Waliongea
mambo mawili matatu mpaka walipofika kwenye ukumbi wenyewe. Ulikuwa ukumbi wa
kawada sana huko Mbezi ya kimara. “Si unaona hili liukumbi lilivyo baya? Sasa
utaona nitakavyo pabadilisha mpaka wenyewe watashangaa.” Akajisifia yule mama.
Wale wale vijana waliomuhamisha Tunda jana yake, waliingia na ile ile gari
iliyomuhamisha Tunda siku iliyopita, ila safari hii ilibeba viti vya maharusi
na mapambo. Walianza kushusha huku wakiendelea kutaniana.
“Leo
mama wametupa godauni.” “Hilihili leo, mpaka paeleweke hapa! Masaa matatu tu,
tunaondoka humu ndani. Nataka nikampikie mume wangu ugali wa bada. Mnaujua
lakini bada au mnanitolea mimacho tu?” “Umeanza mama Penny.” “Kumbe! Ndio muoe
muache kula magengeni! Wakati wenzenu wanaoa nyinyi mmekazana mnaomba. Mtaomba
mpaka Yesu anarudi anawakuta bado mnaomba. Hebu njooni tuombeni kwanza ndio
tuanze kazi.” Wote walikuwa wakicheka.
Tunda
alikuwa akiwashangaa furaha waliyonayo na yule mama. Wakashikana mikono,
wakaanza kuomba kwa pamoja ndipo wakaanza kazi. Walianza kazi kwa nguvu zote.
Wale vijana wakijua chakufanya. Na kweli baada ya masaa matatu na nusu ule
ukumbi ulibadilika kabisa. Walianza kupongezana. Mama Penny akawalipa pesa yao
pale pale wakaagana.
“Na wewe
hii ndiyo pesa yako.” “Wala sijafanya kazi kubwa sana!” Tunda alitaka kukataa.
Yule mama akambadilikia. “Huwa sipendi watu wajinga. Unanisikia Tunda? Kila
mtenda kazi anastahili ujira wake. Au husomi bibilia wewe?” “Nasoma.” “Sasa!?
Au maandiko ya bibilia yalisema kila mtenda kazi sana ndiye anastahili ujira? Acha kuzubaa! Mjini hapa. Kusanya
pesa, jenga nyumba, nunu magari ya maana, uache kuishi uswahilini. Unafikiri
nitakuwa nakuja kukuchukua kila siku?” “Hapana.”
“Ndio
unatakiwa uchangamke, unasikia? Umelipiwa kodi mara moja tu, ujue inayofuata ni
juu yako. Huwezi jua. Mara nyingine Mungu anatokea mara moja tu, na akitokea
usiachie hiyo bahati. Sasa hivi unakusanya kila kinachoingia. Hata kama kidogo.
Halafu huwezi jua hii ndiyo inaweza kuwa ajira yako. Au unaonaje?” Yule mama
akamuuliza.
“Nimeifurahia
sana.” “Basi jipe muda. Omba Mungu hizi tenda ziwe nyingi, ujifunze kwa haraka,
na wewe uwe na yako kama hii.” “Kama hii tena, sio uniajiri?” “Wewe mtoto wa
wapi lakini!?” Tunda alitulia kidogo. “Mbona neno ‘changamka hapa mjini’ ni kama hulielewi!? Wewe Dar yote hii
unafikiri harusi leo zinafungwa ngapi, au kuna sherehe ngapi zinazotaka wapambaji?”
Tunda akacheka baada ya kufikiria kidogo.
“Muone
kwanza! Ushapata jibu eeh? Sasa ndio uchangamke haraka, jifunze, pata ujuzi
halafu unachanganya miguu. Sio ukae hapa unasubiri ajira. Nikikufukuza kama
yule mama wa Arusha? Unahama tena kuajiriwa kwengine? Hapo Mungu alikuwa
anakufungua macho anakwambia uwe na chako! Shule sio kila kitu. Mwenzio
nimesoma, lakini napamba maukumbi. Naingiza pesa nyingi tena kwa muda mfupi.
Umeona kuna sayansi niliyotumia hapa? Ujuzi tu na utundu.” Akawa ni kama
anamfungua akili zaidi Tunda.
“Asante
sana.” “Asante kavukavu tu?” Mama Penny akamuuliza Tunda, akaanza kucheka tena.
“Sasa nifanyaje?” “Ukipata tenda ya kwanza unaninunulia pafyumu nzuri. Sio zile
zakuita nyuki au kuleta mafua.” Tunda aliangua kicheko zaidi, wakaondoka pale.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Yule mama alikuwa akifahamika
sana. Kwa juma moja hakuacha kupamba kumbi si chini ya tatu. Kuanzia kichen
party, send off, harusi, na kila shughuli zilizokuwa zikihitaji wapambaji,
aliweza kupata yeye hizo tenda, mpaka alikuwa akikataa. Alikuwa akiingiza pesa
nyingi kwa juma.
Kwa kuwa
alikuwa na watoto wadogo na huduma ya kanisani, mara nyingi alimtuma Tunda
kwenye vikao vya harusi kwenda kuonyesha picha za kumbi walizokwisha kupamba na
kuongelea gharama. Baada ya muda mfupi kweli Tunda akaanza kuwa mwenyeji na
mjuzi wa ile biashara.
Akajiongeza.
Akatengeneza albamu nyingine. Akapangilia picha na bei vizuri. Ikawa rahisi
kila akitumwa na mama Penny, anaonyesha picha na bei. Kwa muda mfupi Tunda
akaonekana amefikishwa kwenye uwanja wake anaomudu. Yeye ndio mtoa ushauri kwa
mama Penny, kitu kilichomfurahisha sana mama Penny. Lugha nzuri ya biashara
akawa anayo. Hakuna alikotumwa kwenye vikao viwe vya harusi au kiofisi, akarudi
bila hiyo kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa tunaanza kugawana. Wewe unapamba huku na
mimi napamba kule.” Tunda akaingiwa hofu. “Yaani bila wewe? Sitaweza peke
yangu.” “Wewe mtoto vipi!? Hata watoto wachanga huwa wanaacha kunyonya.
Ulipokuwa ukikubali kupokea kazi za watu, tena nyingi kwa tamaa, ulifikiria
nini? Unataka tuongozane kama makondoo mpaka lini!? Kwanza mimi huwa sipendi
kufuatwa fuatwa nyuma.” “Nikiharibu sasa?” Tunda alijawa na wasiwasi.
“Shauri
yako! Mimi hainihusu. Itakuwa ni juu yako wewe na hao waliokupa kazi. Mimi nachukua
ukumbi mmoja tena wakaribia na kwangu, nikimaliza kazi yangu nitakupigia simu
bosi wangu uje ukague, ukiridhika nataka pesa yangu uliyolipwa.” Tunda akazidi
kuchanganyikiwa.
“Sasa na
ule ukumbi wa tatu nani atapamba?” “Kwani wewe ulivyochukua kumbi tatu, kwa
siku moja, ulitegemea nini? Mwenzio nina mume na watoto. Kazi yangu moja tu kwa
siku na wewe unajua. Ulivyochukua kazi zote hizo, ulifikiri nini?” “Jamani mama
Penny!? Basi tufanye wote hizi zote halafu siku nyingine nitajipanga vizuri.”
Tunda akabembeleza akiwa na hofu.
“Akuu
wewe mtoto usinivunjie ndoa yangu. Baba paroko unamsikia Tunda.” Yule mama
alimwita mumewe. “Atalijua jiji! Na akikutana na walevi lazima wamshushie kipondo
kama ukumbi haujaisha kwa wakati.” Mchungaji na mkewe wakaanza kumcheka Tunda,
huku wakikumbushiana visa vya kazi hiyo ya upambaji kama wahusika wanakuwa
hawajaridhika na kazi.
“Sasa
nitafanyaje?” Tunda akauliza akilalamika. “Omba funguo za ukumbini ukalale nazo
kwako. Amka hata saa kumi za usiku, nenda kaanze kupamba. Tena nakupa Josh na
Julius wakusaidie. Wote wale wachapa kazi. Ukiamka mapema kwenye saa kumi
jioni, utakuwa ushamaliza kupamba kumbi zote mbili.” Hilo likamfurahisha Tunda.
“Sasa
mapambo?” Tunda akauliza tena. “Mapambo!?” Mama Penny naye akauliza kama anayemshangaa.
“Nauliza mapambo nitapata wapi?” “Piga magoti uanze kuyaomba kwa Mungu. Utakuta
Mungu kakushushia huko huko ukumbini yanakusubiri. Kila ukumbi atakuwekea
mapambo yake. Anza kuomba.” “Jamani mama Penny!” Kila mtu akaanza kucheka mpaka
msichana wa kazi jikoni.
“Kumbe!
Wewe hujui hii ni nyumba ya Mchungaji? Hapauzwi mapambo hapa. Ushauri
utakaopewa ni kuomba. Ukiona hapa unabanwa, rudi kwako kule uswahilini, kwenye
kelele, kajifungie anza kuomba kwa kulia.” “Au piga magoti nikuwekee mkono
Tunda.” Mchungaji akaongeza. “Jamanii!” Tunda akazidi kulalamika.
“Changamka
Tunda. Mjini hapa!” “Basi naenda kununua vitu vyangu.” “Kumbe unaakili?”
“Usafiri sasa?” Tunda akauliza tena. “Piga magoti Mchungaji akuwekee mikono ili
mkimaliza kuomba, ulikute gari hapo nje linakusubiri.” “Jamani mama Penny
wewe!” “Kwani wewe huamini nguvu ya maombi? Au hujasikia kama kuna miujiza?”
“Naamini lakini si kihivyo!” “Basi changamka. Una siku tatu za kukamilisha kila
kitu uingie kazini.” Tunda akaondoka.
Tunda
aanza biashara yake ya kupamba.
Usiku
huo hakulala. Akaanza kuandika kila kitu alichokiona kwa yule mama, ambacho
alijua atakihitaji na yeye. Kesho yake asubuhi akaanza kuzunguka madukani akiwa
na Julius ambaye ni mpambaji wa mama Penny na ni dereva wa ile Kenta.
Akaanza
kununua vitu kama vile alivyoviona kwa mama Penny. Anamwita Julius, anasogeza
gari, wenye duka wanamsaidia kupandisha vitu kwenye gari, Julius anamsubiri,
yeye anazunguka madukani peke yake.
Viti vya
kukalia maharusi ndivyo vilimtoa jasho. Alitaka kama vya mama Penny, ila bei
ilikuwa kubwa. Akaanza kujishauri akikumbuka akiba ya pesa aliyokuwa nayo.
Inamaana kazi yote tangia aanze kazi kwa mama Penny na ile aliyolipwa Arusha,
itaishia hapo kwenye manunuzi! Akajishauri Tunda. Lakini alitaka awe anafanya kazi
nzuri kama mama Penny. Ikabidi ajikaze tu, anunue kila kitu vile vile na vizuri
zaidi, mpaka akaishiwa kabisa.
Walirudi
nyumbani kwa mama Penny na mchungaji Tabata akiwa na mizigo yote aliyokuwa amenunua
Tunda. Tunda mwenyewe alikuwa hoi. Amechoka na ule weusi ukaongezeka kwa
kupigwa na jua pamoja na vumbi.
“Naomba unikopeshe pesa nikaongeze kwenye
mapambo.” Mama Penny akaanza kucheka. “Umeshaanza kupata akili eeh? Safi sana.
Sasa hapa kwetu kukopa ni mara moja tu,
na unalipa ndani ya juma moja. Ukizidisha siku saba unaanza kulipa na riba.”
“Mama Penny jamani!?” “Haya nenda kakope kwenye mabenki.”
“Haya basi nitakulipa nikilipwa baada ya kupamba.”
“Hiyo ndio akili. Sasa uchangamke na siku za alhamisi na ijumaa hapa mjini pia
kunakuwa na sendoff na Kitchen party. Zote hizo siku hakikisha unapata kazi.”
“Si nitachoka sana!” Tunda akashangaa. “Sawa. Nenda kalale. Kwanza hivi
umepaona nyumbani kwake?” Mama Penny akamuuliza mumewe.
“Hapana.” “Kama chumba cha mbwa! Hapafai.” “Jamani
mbona pazuri tu.” “Kama pazuri mbona mizigo yako ipo hapa? Si ungetoka Kariakoo
na kuipeleka kwako?” “Mama Penny wewe? Pale padogo halafu nahofia wezi.” “Sasa
unakataa nini na unaongea nini hapa? Dari lenyewe limeshuka mpaka mlangoni!
Yaani kuingia inabidi uiname na unakuwa kama unatumbukia ndani hivi. Tena kama
wewe baba Paroko na miguu mirefu hiyo! Lazima uiname ndio uweze kuingia
mlangoni, na ukifika ndani itakulazimu kukaa tu. Lasivyo utagonga dari.” Tunda
alianza kucheka huku anatingisha kichwa.
“Nitahama bwana.” “Utahama bila pesa? Nakwambia
fanya kazi kwa bidii. Unasema utachoka! Tena kesho kuna kazi nimepewa ni
kupamba ukumbi wa tamasha, pale Mlimani City, sitaweza kwenda namsindikiza mume
wangu kwenye huduma Morogorooo. Sasa itabidi uwahi ukapambe na hao vijana.” Tunda
akachoka kabisa.
“Utaniua mama Penny! Mlimani City? Nikiharibu?”
“Ndio utakuwa umeniharibia biashara. Na tunakuomba ule uondoke Tunda. Nina mazungumzo
ya faragha na mume wangu.” Msichana wa kazi alikuwa akicheka muda wote.
“Sawa bwana.” “Na tunakupa miezi miwili tu, hakuna
tena kutumia gari yetu kubebea vifaa vyako vya kupambia. Tafuta gari yako,
mrembo. Mjini hapa, watu tunaishi kwa mahesabu. Hakuna kuomba chumvi kwa jirani.”
“Gari!?” “Na hivyo vifaa vyako hapo stoo, kuanzia mwezi wa kumi na mbili utaanza
kulipia hicho chumba.” “Jamani mama Penny wewe!?”
“Sitaki hodi za asubuhi asubuhi wakati unakuja
kuchukua vifaa vyako ukapambe. Ni usumbufu Tunda.” “Si kwa muda tu!” “Muda
wenyewe ndio nakwambia mwisho ni mwezi wa kumi na mbili. Kwa hiyo wakati unapumzika
huko kwako hutaki kufanya kazi kwa bidii, ujue unatakiwa gari na nyumba kubwa.”
“Patamu hapo. Na vyote hivyo si chini ya mamilioni
ya pesa. Ukiiba tu, sisi tunakutenga. Ukihongwa tu, mimi Mchungaji nakupandisha
madhabahuni nakutangaza kuwa wewe ni mzinzi, kisha nakutenga mbele ya watu.”
Mchungaji akaongeza. Yule mama alisaidiana na mumewe kumshambulia Tunda.
“Hivi nyinyi mlikutana wapi?” Iliibidi Tunda
kuuliza jinsi wanavyopokezana maneno kwa kupatana, kama wamepanga. “Maana
mnafanana kila kitu!” Wote wakacheka. “Kanisani. Mimi nilikuwa kiongozi wa
vijana, na bibie hapa alikuwa ndani ya kundi. Akanipenda ndio nikamuhurumia
nikamuoa.” “Uringe. Alihangaika huyu, muone maneno mengi hivyo hivyo. Nilimtoa
jasho!” Tunda alikuwa akicheka sana.
“Kwa
hiyo mlianzana tokea wadogo?” “Nimemfundisha hesabu za sekondari huyo, usimuone
hivyo. Nilivyomuona anapenda pesa, nikaona nioe kabisa ili yeye awe anatafuta
pesa mimi nahubiri injili. Ukimfatilisha huyu, ndani ya miaka miwili utakuwa
mbali sana Tunda. Kazana, jiamini, utaweza tu.” “Umesahau kumwambia na awe
anatoa fungu la kumi kanisani.” Mama Mchungaji, yaani mama Penny, akaongeza,
nakumfanya Tunda aangue kicheko zaidi.
“Na sadaka kubwa kubwa. Umesikia Tunda? Sio zile
sadaka unatumbukiza kwenye kapu la sadaka umekunja ngumi. Na baraka za Mungu
zitakuwa ndogo ndogo hivyo hivyo”
“Nitatoa.” Tunda akakubali akicheka
Tunda
aanza kupambana jijini.
Mwanzo
wa Tunda haukuwa rahisi hata kidogo. Ilikuwa kazi tu. Hakuna masaji wala
kutengeneza kucha na kubadili nywele kila week. Alianza kufanya kazi kwa
bididii zote, akili ikiwa imetulia kazini asiharibu. Ndani ya juma moja alikuwa
akipata kazi si chini ya nne. Zote hizo anasukumiwa na mama Penny. Kuna siku
nyingine alikuwa akipamba kumbi mbili mpaka tatu.
Tunda
akawa busy. Mchana na usiku yupo na kazi. Hakuna waxing tena kwenye huo mwili
kutoa vinyweleo. Kazi tu. Anasaka pesa kwa juhudi zote. Na Mungu akawa
akimfungulia milango kwa namna ya ajabu. Akawa ni kweli anapata kazi. Kila
akijisikia kuchoka na kutaka kukataa kazi, alikuwa akijisuta na kukumbuka
maisha yake. Basi anatoka kitandani bila hata alam.
Alianza
kuingiza pesa na kufahamika mjini kwa kazi nzuri ya upambaji. Na akaongeza
uaminifu kama mama Penny. Mkikubaliana aina fulani ya mapambo, basi ujue
atakuwekea hayo hayo mapambo. Kama ni maua Rose, ujue hatachanganya wala
kukuibia. Uwe na pesa usiwe, basi atakupambia kutokana na pesa yako na vile mlivyokubaliana.
Alipata
familia kubwa pale kanisani kwa kina mama Penny. Tunda alijawa furaha, upweke
wote ukaisha. Akawa mtu wa furaha wakati wote, na nyumbani kwa mama Penny ikawa
ndio kituo chake kikubwa. Na mama Penny akafanyika dada kweli kweli. Ukimkosa
Tunda kwenye simu, muulize mama Penny. Mchana na usiku wawili hao walikuwa
wakiwasiliana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
mahangaiko mengi akichapa kazi mchana na usiku, akafanikiwa kuhama Temeke,
akapata nyumba. Haikuwa nzuri kama ile aliyoishi La dolce Vita, lakini ilikuwa
na ukubwa unaolingana na ile. Vyumba viwili kama ile, inajitegemea, maeneo ya
Kimara, karibu sana na Ubungo. Akaenda kuchukua vitu vyake vyote kwa Net,
akahamia kwake. Akaongeza bidii ili kupata usafiri pia. Kazi akafanya mchana na
usiku bila kuchoka wala kulalamika. Hakuna tenda yeyote alipata akaacha.
Alipopata
pesa, mama Penny akamsindikiza Tunda kununua gari. Kwa kuwa alikuwa na mambo
mengi, alinunua gari nzuri lakini sio kama ile ya Mama Mchungaji iliyokuwa ya
aghali sana. Tunda akapata usafiri wake wakumzungusha mjini.
Kila
mama Penny alipopata kazi nyingi alimpa na yeye. Watu wakaanza kumfahamu yeye
kama Tunda sasa. Akaanza kutafutwa yeye kama Tunda sio kwa kupitia tena mama
Penny. Na kazi zake zilikuwa nzuri sana. Akaanza kuuzika kama Tunda, na watu
wakaweza kutambua kazi zake.
Hakuwa
amesoma, lakini kwa hakika kile kilikuwa kipaji chake bila kuuliza.
Kilijionyesha kwenye kila kumbi aliyokuwa akipamba. Alijiongeza na ungeweza
kutofautishi ukumbi aliopamba yeye au mama Penny, japo walitumia karibu kila
kitu kinachofanana. Kipaji chake cha upambaji kilimkutanisha na watu waina
mbali mbali. Wasomi na wenye pesa. Wake za mawaziri na mabalozi.
Alipoona kazi inakuwa kubwa, hana haja yakusaka kazi, zinamfuata tu, akatafuta ofisi na kuajiri watu wawili waliokuwa wakipokea kazi kutoka kwa watu. Alifungua website ambayo ilijaa picha zakuonyesha kazi zake. Kwa muda mfupi sana Tunda akawa mashuhuri pale jijini. Lakini katika yote hakuacha kuwa karibu na Mungu wake. Msingi wa kusoma bibilia na kuomba aliokuwa amefundishwa na Net, hakuacha hata kidogo. Kila akirudi nyumbani kwake, atapiga magoti na kuomba Mungu japo kwa ufupi.
Kwa
Mara ya Kwanza, Tunda amsaka baba yake
jela.
Alianza
kuulizia kwenye magereza ya pale mjini, kutaka kujua alipofungwa baba yake,
mpaka akajua kule baba yake alipokuwa amefungwa na siku ambazo wanaruhusiwa
kutembelewa. Akaamua kwenda kumtembelea baba yake huko gerezani Segerea. Baba
yake alifurahi sana kumuona Tunda. Lakini alikuwa amedhoofu na hakuwa na furaha
hata kidogo.
“Wamenisingizia mwanangu. Kwa kuwa sina hela,
nashindwa kutafuta mwanasheria mzuri wakunitetea.” “Mimi nitakutafutia baba.”
Hilo likamfariji sana baba yake. Mtoto ambaye hakuwa hata anamtegemea, ndio
anaahidi kuwa mkombozi! Akashukuru.
“Unafanya nini sasa hivi? Umependeza mama.” Ilibidi baba yake kuuliza.
Maana ni kweli Tunda alionekana ametulia na pesa ipo.
Swali alilokuwa akilikwepa wakati ule akizunguka na
wanaume, ndilo hilo baba yake anamuuliza. Lakini safari hii akamjibu baba yake
kwa ujasiri wote. “Mungu ananilinda na kunitunza kwa namna ya ajabu baba! Mimi
mwenyewe bado nipo kwenye mshangao baba yangu. Napamba kwenye kumbi za shuguli
mbali mbali! Na wala sikurudi shule. Nilifundishwa tu.” Tunda akamuelezea juu
ya wakovu aliopokea, familia ya mama Penny na mafanikio yake. Baba yake akafurahi
sana, wakawa wanaongea mpaka muda ulipoisha, Tunda akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alianza kuzunguka kwenye ofisi za wanasheria pale
mjini. Akiongea nao, kuona kama wataweza kumsaidia baba yake. Akiwa anajaribu
kwenye ofisi nyingine, sekretari wake alimpigia simu kumwambia yupo mtu amesema
anataka kuongea na yeye mwenyewe. Tunda alichukua ile namba akapiga.
Walimuomba huduma yake ya upambaji na kumtaka afike
kwenye moja ya kikao chao cha ijumaa ili kuongea na wanakamati. “Mlishaona kazi zangu
lakini? Maana mnaweza kupitia kwenye website yangu, mkachagua muundo mnaoupenda,
kisha unapiga simu ofisini onatoa oda yako. Sio lazima mimi nikawepo kwenye
kikao.” “Tungependa kukuuliza maswali kabla ya
kuchagua.” Tunda akakubaliana nao muda na eneo atakalokwenda siku hiyo
ya ijumaa kukutana na wanakamati wengine.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa siku hiyo ya ijumaa jioni, Tunda akiwa
amejitayarisha vizuri kwenda kuonana na wanakamati hao. Alikuwa na kazi moja tu
siku hiyo. Alishakamilisha tokea asubuhi. Akarudi nyumbani, akapumzika na
kujiandaa tayari kwa kikao cha jioni. Kama kawaida yake, hakuwa akifanya makosa
kwenye mwili wake. Alipendeza sana, akachukua picha zote alizojua angehitaji
kuvutia wateja wake, akaelekea kwenye kikao.
Eneo tu walilokuwa wakikutania hao wanakamati,
Tunda alijua watakuwa na pesa. Aliingia kwenye hoteli hiyo iliyokuwa Masaki,
akasalimia pale mapokezi, kisha akampigia simu mtu aliyekuwa ameongea naye kwenye
simu, akafika pale mapokezi kumchukua.
Tunda alimuona yule kaka jinsi alivyobabaika baada
yakumuona. Akaongeza ujasiri. Wakaongozana mpaka upande wa chakula walipokuwepo
wale wanakamati wenzake. Walikaa ndani, kwenye eneo kubwa kidogo.
Waliunganishiwa meza mbili ili waweze kuonana. Tunda aliwasalimia bila
kuwaangalia huku akijaribu kuvuta kiti alichoonyeshwa na mwenyeji wake.
Ana kwa Ana na Net tena!
“Tunda!” Tunda alishtuka kidogo baada yakusikia
jina lake likitajwa pale mezani. Akanyanyua uso kutafuta aliyemwita na kukutana
na Net. Tunda akatoa tabasamu kubwa sana la mshtuko. “Net! Habari za siku!?”
Net alikuwa kwenye mshangao mkubwa sana, uliowafanya wanakamati wote wabaki
wakiwakodolea wao macho. Tunda alikaa chini, na kumwangalia tena Net, pembeni
ya Net, alikuwepo Gabriel. Tunda akashtuka sana, akaamua kutokuwaangalia tena.
Akabaki akimtizama mwenyeji wake tu.
“Naona tumeshatambulishwa jina, tumeshajua unaitwa
Tunda.” Yule mwenyeji akavunja ukimya. “Ndiyo. Ninaitwa Tunda, ndiye
ninayehusika na mambo ya upambaji. Uliniambia mlishapitia kwenye website yangu.
Si ndiyo?” Tunda akauliza huku akimtizama yule mwenyeji. “Ndiyo.” “Sio wote
bwana.” Mwingine akakanusha. “Basi haina shida. Nimewaletea baadhi ya picha,
ili muone baadhi ya kazi zangu kisha mchague.” Tunda akatoa zile picha
alizokuwa amezipanga vizuri kwenye albamu.
“Bei
zako zikoje?” Mmoja wao akauliza wakati akiendelea kuangalia. “Inategemea na
nini unataka ukumbini. Ukichagua moja ya picha hapo naweza kukutajia bei. Na
pia kama hakuna muundo hata mmoja mtakao kuwa mmependa hapo, naweza kuwapambia
kutokana na mtakavyo nyinyi. Mnaniambia nini mnataka, ukubwa wa ukumbi, meza na
idadi ya wageni mnao tarajia, nitaandika na kwenda kuwapigia mahesabu kisha
nitawajulisha. Mara nyingi najitahidi kwenda kutokana na bajeti ya mteja.”
Tunda akajieleza vizuri sana na sauti yake tulivu bila pupa, nakubaki
akiwasikiliza, ila macho yake yakiwa kwa mwenyeji wake tu.
Zile picha zilizunguka pale mezani watu wote
wakiangalia kwa kurudia rudia. “Kazi yako nzuri dada Tunda.” Mmoja wa
wanakamati akasifia. Tunda akatabasamu na kufanya azidi kuvutia kumtizama.
“Asante.”
“Umeolewa?” Mwanakamati mwingine akauliza. “Acha
hizo Tino, bwana! Wewe mtafute kwa wakati wako. Acha sisi tuongee mambo ya
maana.” Wote walianza kucheka mpaka Tunda akatabasamu na kuinamia kwenye picha
alizokuwa ameshika mkononi mwake. “Tatizo lako wewe Mgeekwa, unapenda kupania
mambo sana. Si watu bado wanaangalia picha? Sasa kuna tatizo gani mimi
nikaendelea kuongea na Tunda?”
“Utamchanganya bwana.” “Tunda mwenyewe haonekani kama ni mtu wakuchanganyikiwa
hovyo. Halafu jibu lilikuwa fupi tu, ‘ndiyo au hapana’ ili nipate nguvu ya
kuendelea kumtafuta baada ya hapa. Au hamtaki kikao kingine?” “Wewe si muoaji Tino. Acha fujo.” “Sasa ningemuoa nani
wakati Tunda ndio amekuja leo? Eti jamani?” “Mgeekwa anakubania tu.”
“Mmeona eeh? Tuendelee Tunda. Sasa vipi?” Tino
akaendelea kumchokoza Tunda. “Kwa kuwa wengi wenu hamkuwa mmeona kazi zangu,
nashauri mtembelee website yangu ili muweze kuona kazi zangu nyingine ili
mmfanye maamuzi sahihi. Kisha mnaweza kupiga simu ofisini ili kutoa maamuzi
yenu na kujua gharama zinakuaje.” “Bwana Tunda yupo kikazi! Na mimi nimesoma
Tunda. Nimeelewa kuwa hunitaki.” Kila mtu akacheka.
“Achana naye huyo Tunda. Tuendelee na kazi.”
Mgeekwa ambaye alionekana ndio muongoza kikao, aliingilia.
“Jamani
nyinyi mnamjua bibi harusi mwenyewe. Mimi naomba nikubaliane na Tunda.
Nikamuonyeshe, achague. Kisha tutakuja kuongea na Tunda.” “Au kwa nini
msitukutanishe naye, yeye mwenyewe huyo bibiharusi? Tuone kitu gani anataka. Na
kama atataka ushauri pia tunaweza kumshauri.
Anaweza kufika ofisini kwetu, ninao wataalamu pale watamshauri vizuri au
watamsikiliza anachotaka.” “Sisi tunakutaka wewe Tunda. Usitutupie kwa watu
wengine.” Yule mwenyeji wake akamkatisha.
“Msiwe na wasiwasi kabisa. Hakuna
kitakachoharibika. Naomba niwaache, tuwasiliane mtakapo kuwa tayari.” Tunda
akasimama. Net hakuwa ameongea kitu chochote alibaki akimtizama tu Tunda.
“Naomba nikusalimie pembeni kidogo, Net.” Tunda aliongea kwa sauti tulivu huku
akimtizama Net. “Mimi hutaki kunisalimia pembeni kidogo?” “Acha Tino, nini
lakini?” “Tatizo lako Mgeekwa, hutaki nioe kaka!” Tunda akacheka akiwa bado
amesimama. “Tundaaa!” Tino akarudia. Net akavuta kiti na kuondoka pale. Tunda
akamfuata nyuma. Net alikuwa akiongoza njia huku Tunda akimfuata nyuma.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Mbona huonekani kama una furaha, Net? Mzima?”
Tunda akauliza mara baada ya Net kusimama nje ya ile hoteli na kumgeukia Tunda.
“Kila kitu kipo sawa?” Tunda akarudia kwa upole akionyesha kujali. “Kwa nini
hukunitafuta tena Tunda?” “Mama alichukua simu kwa ghafla, Net! Sikuweza kuchukua
namba zako za simu. Nilishindwa jinsi ya kukupata. Hata nilipokwenda nyumbani
kwako kufuata baadhi ya vitu vyangu, Emma hakuwa anajua lini unarudi nchini na
hakuwa akijua njia ya kuwasiliana na wewe. Babu anaendeleaje?” “Alifariki.
Unasema mama alikupokonya simu!?” Tunda akatulia kidogo.
“Tunda?” “Kwani yeye amekwambia nini?” Tunda
akauliza. “Kwa nini unauliza swali juu ya swali Tunda? Nani anamjibu mwenzake?”
“Samahani Net. Hakunipokonya, bali alichukua.” “Ilikuaje?” “Net please!” Tunda
akamsihi kwa upole. Akimtaka ayaache tu. “What?” “Naomba tusiongelee mambo ya
nyuma.” “Kwa kuwa wewe ushapita huko?” “Hapana Net. Kwa nini tusiongelee mambo
ya sasa?” “Ya sasa yapi?” Tunda akanyamaza.
“Kama unashindwa kunijibu basi naona nikuache tu.” “Sishindwi
Net. Lakini sijui ni nini mama alichokwambia juu yangu?” “Kwa kuwa wewe huna
haja yakujua alichoniambia, mimi ninataka kujua nini kilitokea. Maana tuliagana
vizuri siku ile ya jumamosi, ukaniambia tutawasiliana kesho yake. Ndio nakuona
leo! Nakuuliza kulikoni, naona unashidwa kunijibu.” Tunda akaona ajieleze tu.
Net alikuwa amekasirika.
“Siku ile tulipoagana, mimi niliendelea kukaa pale
ofisini nikimalizia oda ya Nchawa. Si unakumbuka nilikwambia alipiga simu
akitaka tumpelekee mzigo wake wote kwa pamoja siku ya jumanne?” “Ndiyo.” Net
akajibu. “Sasa kumbuka nilikuwa sina lori kubwa. Yote mawili yalikuwa
yamepeleka mizigo mikoani. Wazo lilinijia kuazima kwa kina Masai, ili
nihakikishe napeleka mzigo wote siku ya jumanne ili kuhakikisha simpotezi Nchawa.
Maana alisema nikimfanikishia, atakuwa anatupa kazi kila week hata kama mara
mbili kwa week itategemea na sisi wenyewe na uwezo wetu. Sasa ikabidi kupambana
ili nisiharibu, nimfurahishe.” Tunda akaendelea.
“Niliongea na Masai mwenyewe akasema lori analo
lakini hana dereva anayemuamini. Dereva wake ambaye anatumia hilo lori amepatwa
na matatizo, hayupo kazini. Akawa amenipa namba za simu za watu kadhaa,
akaniambia huwa anawatumia mara moja moja. Nilikaa pale mpaka usiku nikijaribu
kutafuta dereva wakupeleka mzigo wa Nchawa Moshi, siku hiyo ya jumanne asubuhi.
Nilitaka kufikia jumatatu niwe nina uhakika na kila kitu. Dereva na usafiri
wenyewe. Nilikuja kukamilisha kila kitu usiku kama kwenye saa mbili.” Net
alikuwa akisikiliza tu.
“Niliporudi nyumbani baada ya kukamilisha kila
kitu, nikamkuta mama na Safia.” Tunda akatulia kidogo. “Nini kilitokea?” Kama kawaida ya Net, akataka amalizie. “Mama
alionekana amenikasirikia sana na zaidi hakupenda kabisa kitendo cha mimi kuwa
nikiishi pale bila yeye kuwa na taarifa. Alilaumu ni kwa nini uliweza kuruhusu
mtu mwenye tabia kama zangu kuishi mle ndani na Maya, na mambo mengine mengi
ambayo siwezi kurudia, itakuwa ni kama najitusi tena mwenyewe.”
“Lakini aliniambia Safia ndiye atakuwa bosi wangu,
anahitaji nimkabidhi kila kitu ikiwemo simu ile ya mkononi na usiku uleule
nimpishe Safia kwenye chumba kile nilichokuwa nikilala pale nyumbani kwake. Na
usiku uleule niondoe mizigo yangu pale. Nilimkabidhi kila kitu, tena nilimuomba
kwa kuwa ilikuwa usiku, na nilikuwa na mizigo, aniruhusu kuondoka na gari yako
kisha niirudishe kesho yake, lakini mama alikataa. Nilijaribu kumuuliza
kulikuwa na shida gani kwa nini amekuwa vile! Lakini mama alikuwa mkali sana,
Net. Alinitaka niondoke pale usiku uleule. Ikabidi niondoke na mizigo yangu
mpaka barabarani ndipo nikapata taksii.”
“Siku ya jumatatu asubuhi niliwakuta walishafika
ofisini, Safia alikuwa kwenye meza yangu. Nikaamua kwenda kumsalimia mama
ofisini kwako.” Tunda akanyamaza akageukia pembeni. Net akamuona Tunda akianza
kufuta machozi. Alilia sana Tunda. Net akamshika mkono akamvuta nyuma ya gari.
“Nini kilitokea Tunda?” Tunda alishindwa kuongea
kwa muda. Akajaribu kutulia ndipo akaendelea huku akilia. “Mama Cote alitumia maisha yangu ya nyuma kunidhalilisha
Net. Alinitukana mbele ya Safia na yule kijana. Akinitaka nirudi kwanza shule
niache umalaya, nikipata vyeti ndio nirudi pale kazini. Akanilipa na kunitaka
niondoke.”
“Kweli sijui ni baya gani
niliwatendea! Nilijitahidi kufanya ile kazi kwa kadiri ya uwezo wangu, na nilikusudia
kuacha yale maisha machafu Net. Niliacha umalaya. Niliumia sana kuona mama Cote
anatumia maneno niliyoongea kanisani tena mbele ya wazee, Mchungaji akinisihi
niseme tu, pale ni sehemu salama, na wewe ukasema nisiwe na wasiwasi, lakini
baadaye tena baada ya kutubu, na Mungu kunisamehe, bado nakumbushwa tena kwa
kutukanwa! Bila kosa! Niliumia sana Net. Sana.” Tunda
akajifuta machozi.
“Historia yangu yakufukuzwa
ikajirudia, Net. Alinifukuza mama yako usiku nikiwa na mizigo, na pale
ofisini akinitukana. Lakini nimesamehe. Sikutaka kurudia kuzungumzia na
wewe yaliyotokea kwa kuwa yananikumbusha mambo ambayo hayanijengi bali
kunibomoa. Isingekuwa Mungu, nisingeweza kurudi tena kanisani Net. Nisingeamini
watu wa kanisani, na nisingekuwa kanisani mpaka sasa.”
“Lakini Mungu ameniponya Net. Amenipa familia ya
kanisani. Nzuri sana. Nina mama na baba wa Kiroho wanao nifuatilia vizuri sana.
Tena wao ndio wamenisaidia kufikia hapa. Na wala sikurudi tena shule. Kwa elimu
ileile ndogo niliyonayo ninaweza kuishi.” Net alibaki kama amemwagiwa maji.
“Pole Tunda na samahani sana.” “Yameshakwisha Net. Mungu amenisaidi ninaishi
vizuri na nina amani.”
Simu ya Tunda ikaanza kuita. Akasogea pembeni
kidogo na kuanza kuongea. Alisikiliza kwa muda, akiwa kimya “Naomba subiri kidogo.” Net akamsikia Tunda akiongea kwenye simu,
akimwambia anayezungumza naye asubiri, kisha akamgeukia tena Net. “Net! Naomba
nikuage, Mungu akipenda tutaonana tena.”
Tunda alikuwa bado ameshikilia simu yake kama kuna mtu anayemsubiri
upande wa pili. Net alibaki akimwangalia. “Bye!” Tunda akamuaga, kisha
akaondoka pale akilifuata gari lake. “Samahani kuna mtu
nilikuwa nikizungumza naye hapa. Ehe! Kwa hiyo umesema inawezekana?” Net
akamsikia Tunda akiongea huku akiishia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Katikati ya mengi, Net arudi pichani. Nini kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment