Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Nilipotea! - Sehemu ya 20. - Naomi Simulizi

Nilipotea! - Sehemu ya 20.

 

N

et ni kama alipoteza dira, hajui chakufanya tena. “Naomba niondoke Net.” “Kumbuka tumekuja na mama! Naomba nikamchukue mama ili tuondoke pamoja. Sawa?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Asante sana Tunda.” Net alikuwa amesha changanyikiwa. “Twende basi ukasubiri kwenye gari.” Akarudi naye mpaka kwenye gari, akawasha gari, akamuacha Tunda amekaa humo ndani ya gari.

          Alikuta Mchungaji akimsubiri, bado haelewi kilichotokea. “Kuna nini, Net?” “Naomba tuwaulize hawa wazee, kwa nini Tunda amekimbia mara baada ya kuwaona.” Mmoja wao akasema sijui. “Wewe hujui lakini Mzee Meto namwenzie wao wanafahamu.” Net alikuwa amekasirika sana.

 “Hivi unajua ni kwa muda gani nimekuwa nikitaka huyu binti afikie haya maamuzi? Hivi mnajua ni jinsi gani nilivyomuhubiria? Nimemwambia huku kanisani lipo tumaini. Ameteswa na shetani kwa muda mrefu sana, nimemuahidi atapata pumziko. Halafu anakuja kukutana na nyinyi watu wa kanisani mliokuwa wateja wake!” “Wateja?” Mama Cote alishtuka sana. “Ndiyo. Tunda alikuwa akifanya biashara ya kikahaba.” Net alikuwa amekasirika sana, hata hakuwa akifikiria alichokuwa akiongea. Aliendelea kuropoka. Wote walikuwa kimya wakimsikiliza.

“Hivi mnajua mlichofanya nyinyi? Mmechukua tumaini la pekee lililokuwa limebaki kwa yule binti! Mtamfanya asiamini tena.” “Tulia Net. Kwa kuharibu kwa hawa wawili, hakuchukui nafasi ya Mungu hata kidogo. Kama wao wameshindwa, bado tunayo mifano mizuri ya watu wengi wanaoweza kuishi maisha maadilifu. Naomba ukamwite Tunda.” Mchungaji akapiga simu kwa baadhi ya wazee aliojua wanaweza kufika pale kwa haraka, wakaanzisha kikao.

Tunda akarudi ndani, wakamuomba aelezee mahusiano aliyokuwa nayo na wale wazee. Tunda akakiri kila kitu huku akilia na kusema ni kweli amechoka anatafuta njia ya kupumzika nakuondoa ile hukumu moyoni mwake lakini si pale. “Hamuwezi nyinyi kunisaidia. Hamtaweza hata kidogo.” Tunda akatoka. Net alimkabidhi funguo mama yake na kumfuata Tunda.

Ilikuwa ni aibu ya miaka kwa kanisa. Hakuna aliyeamini uchafu Tunda aliosema alikuwa akiwafanyia wale wazee. Net ndiye aliyeishiwa maneno kabisa. Alishindwa aongee nini na Tunda. Tunda alikataa kabisa kurudi kwa mama yake Net, akaishia kulala hotelini. Aliomba Net akamchukulie mizigo yake nyumbani kwao, usiku uleule.

 Tunda Arudi Arusha bila Msaada wa kiroho.

Kesho yake asubuhi na mapema, bila hata kumuaga Net, Tunda aliondoka jijini Dar kurudi Arusha kwa kutumia usafiri wa basi. Usiku ule ulikuwa mrefu sana kwa wale viongozi wa kanisa lile. Wale wazee walikiri uchafu waliokuwa wakifanyiwa na Tunda, na kesho siku ya jumapili kwenye ibada, walisimamishwa mbele ya kanisa na Mchungaji akawatenga.

Ilikuwa ni hali ya kusikitisha, kushtua na aibu kubwa. Kwani ni wazee walioheshimika sana pale kanisani na wao ndio walikuwa wakitoa michango mikubwa ya kifedha pale kanisani, wakisaidiana na Mama Cote. Mmoja alikuwa ana mke wake pale pale kanisani. Watoto wao walishakuwa wakubwa tu. Na Meto yeye alifiwa na mkewe, japo naye alikuwa Mzee wakuweza kumzaa hata Net. Alitambulishwa Tunda na huyo Mzee mwenzake. Tunda akamridhisha kwenye gari kitu alichopenda. Hakuhitaji kwenda naye popote. Kwa hiyo walimpenda Tunda, wakijua hawataweza kukamatwa. Waliegesha magari yao sehemu tulivu mida ya usiku giza limeshaingia. Tunda anafika hapo kwenye magari yao, anawahudumia, wanamlipa, maisha yanaendelea.

Mchungaji Amfuata Tunda.

Baada ya ibada yule Mchungaji alipanda ndege kuelekea Arusha na Net, kumfuata Tunda. Walimkuta amelala chumbani kwake. Mchungaji alimuomba waongee. Tunda alishtuka sana. Hakutegemea kuja kufuatwa tena baada ya kugundulika uchafu wake. Yule Mchungaji aliongea kwa muda mrefu na Tunda. Akimpa mifano hata ya watu waliokuwepo kwenye bibilia walioaminiwa na Mungu, lakini walikuja kumkosea Mungu, lakini baadaye walipotubu tena Mungu aliwasamehe. Alimpa mfano wa Petro aliyemsaliti Yesu mara tatu, lakini baada ya kutubu alisamehewa, na akamueleza jinsi Petro alivyokuja kuwa msaada mkubwa kwa kanisa mpaka sasa.

          “Kama sio Petro kukubali kosa, kazi kubwa ya kanisa iliyoifanya baada ya kutubu isingekuwepo leo. Kikubwa ni kukubali kuwa umekosa na kuhitaji msaada wa Mungu. Halafu Tunda, wale wazee hawatakuwa mfano wako wakuiga pindi utakapoamua kumpa Yesu maisha yako. Wote tunamwangalia mmoja tu, ambaye aliishi hapa duniani bila kutenda dhambi, Yesu.”

“Wote tunamtizama yeye peke yake. Hata mimi huwa najikwaa kwa namna nyingine, na ndio maana tupo kanisani. Kanisani ni kama hospitalini, Tunda mwanangu. Wote tuliogundua tunahitaji msaada wa Mungu, ndio tumekimbilia pale kama wagonjwa wanavyokimbilia hospitalini. Kanisani ndio mahali pekee utakapopata msaada. Sisemi kama utakuwepo kanisani na uendelee kutenda dhambi, hapana. Lakini ujue kuna madhaifu mengine yanachukua muda kuondoka, lakini utakapotulia kwa Mungu, ukanyenyekea, ipo nguvu na uwezo wa kushinda dhambi endapo utakusudia.” Yule mchungaji aliendelea.

“Mungu halazimishi mwanadamu kuacha kufanya dhambi. Mimi na wewe ndio tunachagua. Kwa hiyo unaweza ukawepo kanisani, na ukachagua kuendelea kutenda dhambi kama mtu wa nje kabisa, lakini haiondoi uweza na nguvu za Mungu. Utende dhambi, usitende, bado Mungu atabaki kuwa Mungu ila wewe ndiye utakayeteseka.” Net aliendelea kusikiliza na yeye kwa makini tu akiomba Mungu huo ukweli umuingie Tunda.

“Hakuna pumziko kwa mwenye dhambi, si sasa au baadaye. Bali ipo faraja, amani na utulivu kwa wale walioamua kweli kuishi maisha yakumpendeza Mungu. Mpe Yesu nafasi kwenye maisha yako uone. Mruhusu Net awe mwalimu wako, utajifunza mengi sana kupitia yeye. Nikijana aliyetulia sana na anamjua Mungu. Anaishi maisha ya kikristo kweli kweli, najua wewe ni shahidi.” Tunda akatingisha kichwa kukubali. Kidogo Mchungaji akapumua.

“Basi, na wewe unaweza kuwa kama yeye, kama utakubali, ukatii na kutubu. Je upo tayari?” Tunda alishatulia kabisa. Alimuelewa vizuri sana yule Mchungaji. Akakubali kuombewa. Aliongozwa sala ya toba na Mchungaji akamuombea. Tunda alikuwa na mapepo mengi sana.

Alikuwa amefungwa na nguvu za giza, nyingine tokea alipokuwa mtoto mdogo kwa baba Tom. Mashetani na majini mengine aliyapata akiwa na Sadiki. Tunda akiwa amepagawa hayo mapepo, aliongea mengi sana. Basi ikawa vurugu tupu hapo chumbani. Mchungaji na Net walimuombea, wakikemea yale mapepo yamtoke. Kuna yaliyokuwa mabishi. Yakidai hiki na kile. Lakini yule mchungaji alikazana akisaidiana na Net. Haikuwa kazi rahisi wala ya masaa machache.

Lilitoka pepo hili, na kuibuka jingine ndani yake. Wakidhani wamemaliza, linaibuka jingine. Mara liseme ni jini lililomuoa Tunda. Jingine lilisema ndilo linalomfanya awe na bahati na kuvutia wanaume kwake. Ikawa fujo. Tunda alijawa nguvu za giza. Lakini Net hakushangaa. Tunda alishamsimulia ibada za kipepo alizokuwa akifanya makaburini na huko Handeni alipokuwa na Sadiki.

Maombi hayo yaliendelea, mpaka yote yakamtoka Tunda. Akawekwa huru. Kuja kuangalia saa ni saa saba usiku. Ikabidi Mchungaji achukuliwe chumba hapo hapo hotelini. Kesho yake asubuhi akaondoka kurudi Dar, akiwa amefanikiwa kumpatia Mungu roho ya Tunda.

Maisha ya Tunda baada yakumpokea Yesu.

Net ndiye alikuwa na furaha kuliko hata Tunda mwenyewe mpaka Tunda akashangaa. Alikabidhiwa rasmi kazi ya kumtunza Tunda kiroho. Kitu cha kwanza alichomnunulia Tunda ni bibilia. Akaanza kumfundisha Tunda jinsi ya kusoma bibilia. Kitu alichogundua Tunda kwa Net, ni muombaji. Net alikuwa ni muombaji sana, kitu kilichokuwa kikimshangaza Tunda. Kwa jinsi alivyo Net, na maisha anayoishi, ingekuwa ngumu kumdhania kama ni mcha Mungu wa kiasi kile. Lakini Tunda alijua ndiyo siri yake kubwa ya hekima na utulivu alio nao.

Kwa harakaharaka wasichana wengi walikuwa wakichanganywa na Net, pindi wamuonapo. Lakini baada ya kukaa naye kwa muda mfupi, wengi walimkimbia. Mara nyingi Net alikuwa akimshukuru Mungu kwa kumuwahi. “Unamaanisha nini?” “Najijua hivi nilivyo Tunda. Si watoto au watu wazima wanao nijaribu kunitongoza. Isingekuwa Yesu kunificha, pengine sasa hivi ningeshakuwa nimekufa. Nashukuru Mungu kwa kunipa baba na babu wenye msingi imara wa dini, zaidi babu. Walinikuza kwenye maadili mazuri.”

“Yuko wapi sasa hivi baba?” “Alishafariki.” “Pole sana.” “Asante, lakini ilimuathiri zaidi Maya. Unajua yeye ndiye alilelewa sana na baba wakati mama yupo shuleni. Kwa hiyo baba alipofariki, ndipo mama alipoamua kurudi huku Tanzania.” “Kwani hamkuzaliwa hapa?” “Hapana. Tulizaliwa Canada. Mama alienda huko kimasomo, ndipo akakutana huko na baba. Hata msingi wa shule niliyokuwa nayo ilikuwa ni hukohuko, ndio maana ilinilazimu kurudi hukohuko kumaliza shahada yangu ya pili.”

“Alitangulia kurudi huku mama peke yake. Akatuacha kule mimi na Maya tukilelewa na bibi na babu. Mama alipoweka mambo sawa, nikaanza kuja huku mimi ndipo tukamchukua Maya. Maya hana muda mrefu sana hapa nchini. Na hapapendi kabisa. Anataka sana kurudi kwa bibi na babu. Lakini mama hataki, anaona kule hana uangalizi mzuri. Pale alipo hataki kufanya kitu chochote hapa nchini, anataka kurudi kwa bibi na babu.” “Labda mngemruhusu ili akasome.” Tunda akajaribu kushauri. 

“Mama hawezi. Ni mtundu sana Maya. Na amedekezwa sana na kina bibi. Hana maadili mazuri hata kidogo. Hata huko pia shule yenyewe hataki kwenda. Amemaliza high school tu, anatapanya pesa ya bibi na babu. Ndio maana mama ameamua kumchukua.” “Natamani kama mimi ndio ningepewa hiyo nafasi Net.” “Mungu amekupa nafasi nyingine Tunda. Unaweza kuwa chochote utakacho.” Tunda akainama kama anayefikiria kidogo.

“Lakini sikurudi tena shule. Naanzia wapi?” “Sio lazima ukasomea elimu ya msingi au sekondari. Kwa sasa unaweza kutafuta ujuzi wa kitu fulani unachopenda, kisha ukaanza kukifanyia kazi.” “Ni kweli. Labda nianze kufikiria na mimi nikitu gani napenda. Maisha hayakuwahi kunipa nafasi kama hii. Sasa hivi ninafuraha na amani. Siamini kama na mimi Tunda, nipo kwenye nafasi yakuchagua.” Net akacheka.

“Nikwambie ukweli Net, zile ndoto mbaya zimeisha. Halafu nilikuwa nina hofu fulani hivi. Kama wasiwasi moyoni. Umeshawahi kulala usiku au hata kuwa umekaa tu hivi, ukasikia moyo unashtuka?” Net akawa anafikiria. “Unaweza usijue, lakini nilikuwa na hiyo hali. Hofu kila wakati kama moyo unashtuka kila wakati.” “Kwa hiyo sasa hivi imeisha?” “Imeisha. Namshukuru Mungu. Najisikia huru.” “Afadhali.”

Cheni ya Mguuni ya Tunda!

Ilikuwa jioni wametoka kazini. “Nikuulize kitu Tunda?” “Niulize tu.” “Hiyo cheni ya mguuni ulipata wapi?” Tunda akakunja mguu akaitizama na kuizungusha kidogo. “Alinivalisha Sadiki. Nimeshindwa kuitoa Net.” “Kwa nini?” Tunda akafikiria. “Kuna jinsi Sadiki alikuwa akinifanyia, sijui niseme kunidekeza au nini! Lakini kuna jinsi alikuwa na mimi, alikuwa akinifanya kama yai! Alikuwa hapendi niwe na shida. Kabla sijalia shida, ananipa pesa. Manguo haya yote, ni ya pesa nyingi sana Net.” “Nakuona.” Net akaongeza.

“Basi ni Sadiki. Nilikuwa nikiwa naye, japo nilimdanganya jina, lakini sikuwa nikijitahidi kujifanya kuwa sivyo. Alinipenda yule kaka, karibu kuchanganyikiwa. Wakati mwingine nilikuwa nikimgombesha sana, lakini anavyojishusha, mpaka utamuhurumia. Sikuwa na shida na pesa nilipokuwa naye. Sikuwa nikihangaika kwa yeyote na chochote. Alinilipia kila garama, tena bila kuchoka au kulalamika.”

“Alikuwa akiniona nimetulia tu hivi nawaza kitu, basi hata kama alikuwa anafanya kitu, ataacha, anakuja japo aniguse. Nitakuwa mawazoni, naweza kushtuka kwa sababu ananisugua mahali kwa upendo. Kiganja, bega, ilimradi tu kunionyesha yupo na mimi.”

“Japokuwa alikuwa anasema ananufaika na mimi, lakini Net, Sadiki alihakikisha nina furaha wakati wote. Alinipenda sana. Nilipata miaka miwili ya aina yake na yule kaka. Hii cheni nimeshindwa kuitoa kabisa. Wakati mwingine najiona ni kama nipo na ule upendo wake. Sijui kama unanielewa?” Tunda akauliza na kuendelea bila kusubiri jibu.

“Sijapata mwanaume anayenipenda vile Net. Labda nikija kubahatika upendo kama ule tena. Huyo mwanaume ndiye atakayekuja kuitoa hapa mguuni kwangu. Lakini mimi nimeshindwa.” Tunda aliongea taratibu huku akiiangalia ile cheni na kuizungusha pale mguuni mwake. Net akavuta pumzi kwa nguvu maana alikuwa akimsikiliza kwa makini sana.

“Lakini sasa hivi hauhitaji upendo wa Sadiki, Tunda. Unaye Mungu aliye hai. Upendo wake unatosha. Usijifunge na upendo ambao haukuwa halisi. Nilivyokusikia juu yako na Sadiki, mlifanya mengi na ya kutisha huku akikutumia wewe kama chambo yakuvuta utajiri. Hudhani kama hiyo kitu inaweza ikawa imebeba mambo mengine?” Tunda akashtuka kidogo.

“Nikuombe kitu?” Tunda akamwangalia. “Naomba mimi niitoe, halafu nije niweke hapo nyingine.” Tunda akajifuta machozi. “Hamna sababu yakufanya hivyo Net. Acha tu. Lakini naomba nipe muda wakuja kuitoa. Isiwe sasa hivi. Najiona sipo tayari Net. Mmeniombea, naamini hii cheni haiwezi kuwa na madhara yeyote. Alininunulia cheni tatu. Shingoni, mkononi na mguuni. Akaniletea na kuniambia ni ishara ya upendo wake kwangu. Najiona sipo tayari kuviachia.” Net alibaki akimtizama.

“Ni sawa?” Tunda akauliza kwa upole. “Sio sawa Tunda.” Tunda akaumia sana. “Tena kwa maelezo hayo, ndio sio sawa kabisa. Kwa nini unataka kukumbatia upendo wa mtu aliyepita vibaya kwenye maisha yako?” Tunda akanyamaza.

“Unakuwa unang’ang’ania agano la mapenzi yaliyowekwa kwenye msingi mbaya na hatari sana kwako! Tumekuombea, na tunaendelea kuomba. Lakini unakuwa uko kwa Mungu huku umekumbatia maagano ya mtu mwingine kwenye ufamle mwingine! Hujui nia ya kukuvalisha hiyo ki ukweli.” “Aliniambia ni ishara ya mapenzi yake kwangu.” Tunda akatetea.

“Ndivyo yeye alivyokwambia. Unajuaje kama ni kweli? Halafu Sadiki alikuwa mume wa mtu. Unajifunga kwenye maagano ya ndoa ya mtu! Si sawa Tunda. Unatakiwa ubadilike hata kifikira. Kuwa upande wa Mungu huku ukitetea mapenzi ya wizi, unajifungulia milango mingine mibaya. Naomba ufikirie zaidi.” “Nimeelewa Net. Nitatoa.” Tunda akaongea taratibu.

“Lini?” Net akauliza bila kutaka kumpa nafasi Tunda. Tunda akanyamaza. “Tunda?” Net akamwita. “Unataka kuishi kama Tunda au Ani wa Sadiki?” Tunda akashtuka kidogo akamwangalia. “Ani alikufa na Sadiki, Net.” Tunda akajibu. “Haionyeshi hivyo. Bado yupo na maagano yake yapo hai!” Akamuona anaizungusha ili aitoe.

Net akasogea pale mguuni. Akapiga magoti. “Naomba mimi niitoe.” Tunda akamwangalia kama ambaye hamuelewi vizuri. “Ni sawa?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. Net akaitoa. Nakubaki ameishika. “Utaifanyia nini?” Tunda akauliza. “Sijui. Tumuombe Mungu. Kwanza akutoe kwenye haya maagano na akupe amani. Mengine Roho wa Mungu atatusaidia.” “Basi acha nikupe vyote. Na cheni ya mkononi na shingoni.” Tunda akaenda juu ya meza hapo hapo hotelini alipokuwa amening’iniza mikufu yake.

Akarudi na hizo cheni zote, akamuwekea Net mkononi. Ni kweli zilikuwa nzito. Net akamwangalia. “Nipo sawa Net. Nimeridhia kutoa.” “Hilo ndilo la muhimu. Wewe mwenyewe ukubali kutengana navyo kwanza. Ndio hata tukiomba na kuvunja hayo maagano, itawezekana.” “Basi tuombe wote.” Tunda akapiga magoti pale alipokuwa amepiga magoti Net akimvua. Net akacheka kwa furaha.

“Mungu atakupa mtu anayekupenda kwa dhati.” Tunda akacheka kidogo huku akifikiria. “Mmmh! Sidhani Net. Acha tu tuombe, niachane na Sadiki nitulie kwanza. Nishahangaika na wanaume mpaka nimekinahiwa nafsi. Umenipa mapumziko ambayo, hujui tu! Mungu atakuja kukulipa Net. Hujui kile umekifanya kwangu. Mungu akuonekanie na wewe siku utakapomuhitaji. Kwa lolote lile. Akumbuke kile ulichonifanyia mimi.” “Amina.” Wakatulia.

Net akaweka vile vitu pale kwenye kochi akaanza kuomba. Ameanza tu, akashangaa Tunda anaanguka tena na mapepo. Akajua ndio maana alikosa amani na ile cheni pale mguuni. Yale mapepo yakasema yalikuwa hapo kutunza agano. Na lile agano ilikuwa ni kama ndoa kati ya Tunda na Sadiki. Net alijua tu.

Kijana huyo wa kizungu, alitumia mamlaka yote aliyopewa na Mungu. Akiwa peke yake pale chumbani na Tunda akigaragara chini. Akaanza kutambaa kama nyoka na kutema mate kama nyoka. Safari hii Net hakutumia muda mrefu, akayaamuru yale mapepo yamtoke na yasirudi tena kwa kuwa Tunda ameshavunja yale maagano na amekiri kifo cha Ani.

Akajinyonga pale chini, yakatoka. Ndipo Tunda akazinduka sasa pale sakafuni. Net akamsaidia kusimama. Alijawa mate. Akawa amejichafua sana. “Nini kimenipata Net!?” “Ulikuwa na mapepo Tunda.” “Tena!?” Tunda hakuamini. Siku anaokoka alitolewa mapepo kwa majini.

“Yalikuwa yakilinda maagano yako na Sadiki. Mlikuwa mpo kwenye maagano yaliyoshikiliwa kwa nguvu za giza Tunda. Hizi cheni zilikuwa ni ishara za hilo agano.” “Mungu wangu!” “Usiogope. Umewekwa huru.” “Basi yeye Sadiki alijua anachokifanya. Mimi nikijua ni zawadi tu, kumbe ni mambo yake. Tena aliniletea akiwa ametoka safari. Ukute alizinunua ndio akaenda nazo kwa babu, wakazifanyia dawa. Sadiki alitamani sana anioe nijulikane mimi ni mke wake kihalali. Nilipokataa akaniomba angalau nimzalie hata mtoto mmoja! Napo nilikataa.” “Basi mshukuru Mungu upo huru. Anza upya ukitumia uhuru wako vizuri. Nenda kaoge. Nakusubiri.” “Acha nifute hapo chini sakafuni kwanza.” “Nenda ukaoge. Mimi nitaita mtu wa hoteli apige deki.” Tunda akaingia bafuni akamuacha Net akiita muhudumu kwa ajili ya kusafisha.

Tunda alitoka bafuni na kumuomba Net waombe tena. “Acha woga Tunda.” “Tuombe tena ili kuwa na uhakika yametoka yote.” Net akacheka. “Usinicheke bwana! Tena tupige magoti. Ujue mwenzio nilijua nimewekwa huru kabisa na hayo mapepo!” “Yapo maagano mtu unaingia. Kama si ya kimungu ni mpaka ukubali kuyavunja. Shetani anakuwa na haki nayo, Mungu hawezi kuingilia. Ukikubali kuyavunja, hapo Mungu anakuwa na uwezo wakukudai kwa shetani. Anakuwa na haki zote.” “Sasa hivi sitaki tena Net.” “Na Mungu ameliheshimu hilo, sasa hivi wewe ni wake.”

“Kwani wewe ulionyeshwa na Mungu juu ya hii sheni?” “Sio moja kwa moja. Ni kweli inakupendeza sana. Huwa siachi kuitazama hapo mguuni. Lakini kila nilipokuwa nikitazama sipati amani kama jinsi ilivyokukaa. Unajua kuna kitu kinavutia. Ukikitazama kwa karibu, kinatakiwa kifurahishe sio kukukosesha amani! Ndivyo sasa ilivyokuwa hiyo cheni kila nikiitazama kwa karibu, nilikuwa sipati amani.” Tunda akatulia.

“Tutakuja kurudisha nyingine hapo mguuni.” Tunda akacheka. “Sio lazima Net. Nakushukuru kwa kusimama na mimi. Hujanikatia tamaa.” Net akacheka akijiambia ‘hujui hata nusu yake!’ Wakapiga magoti, wakaomba, ndipo Net akaondoka pale na kumuacha Tunda amelala.

Maajabu ya zile Cheni!

Asubuhi Net alifika na kumpigia simu ashuke chini waende kazini. Tunda akamwambia aende chumbani kwake. Net akajua kuna jambo. Akatafuta sehemu ya kuegesha, akapandisha juu kwa haraka. “Vipi?” “Nimeamka asubuhi, zile cheni hazipo. Au ulizitupa?” “Hapana. Niliweka hapo juu ya meza. Zote tatu. Na niliziacha hapa wakati umelala.” “Basi zimetoweka.” “Mwache shetani achukue mali zake.” “Nimeshtuka Net! Yaani nilikuwa nimevaa na kujifunga mapepo!” “Lakini unachotakiwa kuwa nacho ni kuwa, umebakiwa na uhuru.” Wakaomba tena na kwenda kazini.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Net alitafuta kanisa pale pale jijini Arusha, wakawa wakienda na Tunda.  Alipata naye muda mwingi wakumfundisha kila baada ya kazi. Tunda alibadilika sana kimaisha hasa kimtazamo. Ile hukumu aliyokuwa nayo zamani iliisha kabisa. Tunda alisahau shida zote akawa akiishi kwa furaha. Net alijitahidi sana kumuelekeza kwenye neno la Mungu. Alimjengea msingi wa kusoma bibilia. Kila alipomuuliza swali Net, Net alijitahidi kumuelekeza kwakupitia bibilia.

Maya jijini Arusha, amtaka Tunda aishi nao.

Babu yao aliugua huko nchini Canada, ikamlazimu mama yao aende kumtizama, ndipo ikabidi Maya aende akaishi na Net jijini Arusha. Kwa kuwa Net ni kama alihamia Arusha, na kushindwa kurudi tena Dar kwa kila sababu. Kazi anazofanya Net haikumlazimu awepo Arusha na kushindwa kusafiri kwenda popote, lakini hakuacha kutoa sababu zilizoonyesha ugumu wakuliacha hilo jiji.

Ofisi ya Dar ambayo ilimuhitaji zaidi, kazi zake nzito ndio akawa akizifanya sasa kwa simu na kompyuta, tena kwa juhudi ili kumnyima mama yake sababu. Tunda hakujua anayopitia Net, ili kuwepo naye hapo Arusha. Alikuwepo hapo kwenye ofisi za usafirishaji, lakini alifanya na kazi za mama yake pia huko Dar.

Tunda alishangaa siku hiyo asubuhi Net anampigia simu kumtaka ashuke waelekee kazini, akiwa na Maya. Alifika garini akamkuta Maya anamsubiria kwa hamu. Walikwenda naye ofisini akiwa na Tunda wakati wote. Maya alionyesha kuvutiwa na Tunda kitu kilichomshangaza hata Net.

Alikuwa muongeaji sana tofauti na Net. Lakini binti mdogo tu na nadhifu. Baada ya kazi, waliamua kwenda kula wote watatu kwenye mgahawa wa pale pale hotelini anapoishi Tunda. Wakati wanakula wao watatu, akumuomba Tunda akaribie kuishi nao nyumbani kwao. Tunda akashangaa kujua kuwa Net ananyumba kule Arusha. “Nilifikiri unaishi hotelini Net!” “Hapana. Tulinunua nyumba.” Hata Maya akashangaa.

“Hujawahi kufika!?” Akamuuliza Tunda kwa mshangao. Tunda akacheka. Maya akamgeukia kaka yake. “You must be kidding me!” Akamwambia kaka yake. “Acha fujo Maya.” “Tatizo la Net, yupo sooooo..” Akawa anafikiria Maya jinsi ya kumsimulia Tunda jinsi alivyo Net. “Aaah! Sijui hata nikwambie nini! Lakini umenishangaza kushindwa hata kumkaribisha sehemu unayo ishi!” “Ningemkaribisha bwana. Sema tumekuwa na mambo mengi.” Tunda alishamjua Net ni mwadilifu sana na hana haraka.

 Maya aliaga kuwa anakwenda kutumia choo. Net akamgeukia Tunda. “Upo huru kuja kuishi naye kama unataka. Labda itamsaidia. Hana rafiki hapa nchini na kila kitu mama anachomwambia anaona anaonewa. Labda wewe unaweza kuwa karibu naye, ukamsaidia.”  Tunda akashangaa Net anazungumza nini!

“Net! Namwambia nini mimi Maya!? Mwenzangu amezaliwa uzunguni, mimi mtoto wa mtaani.” Wakacheka. “Inawezekana historia yako, ikawa msaada mkubwa sana kwake. Usidharau.” “Mmmh!” Tunda akaguna na Maya akawa amerudi akawakuta wanacheka. “Sasa Tunda umeamua nini? Nakuja kuishi hapa na wewe au wewe unakuja tuishi kule?” “Upo kama kaka yako!” Wote wakacheka.

          “Kweli. Wote hamsahau jambo, na mking’ang’ania kitu, kinakuwa hichohicho na mpaka mpate.” “Hiyo ipo kwenye damu. Sasa hujakutana na Nana. Nana ndio mbaya zaidi. Hajui jibu la ‘hapana’ anapotaka jambo lake. Na hapendi mtu aombe kitu ambacho hajakifikiria, au hana umuhimu nacho. Na anashangaa ukiwa unataka kitu halafu ukakikosa, ukatulia. Anasema inamaana unataka kitu ambacho kwanza kinakuwa hakina umuhimu. Na inamaana hujafikiria ndio maana ukikikosa inakuwa rahisi kuridhika.” Tunda akapata hapo somo.

“Nana ni nani?” Tunda akamgeukia Net. “Bibi ndio tunamwita Nana.” Net akajibu. “Oooh! Anaonekana ni smart.” Tunda akasifia. “Hujawahi kuona mwanamke kama huyo hapa duniani.” Tunda na Net wakacheka. “Lakini ni kweli. Nana yupo very smart. Wakati wote huwa anajua anachokitaka. Na kama alivyosema Maya, huwa hajui jibu la hapana, linapofika swala la kukamilisha jambo lake. Anaweza kuhamisha milima, ili kukamilisha swala dogo ambalo kwako linaweza hata lisilete maana.” Net akaweka msisitizo.

“Kwa hiyo tunakwenda au tunabaki?” Maya akarudia swali. Wakacheka. “Eti Net? Haitakuwa usumbufu?” “Hata kidogo. Ni sehemu kubwa. Utapata chumba chako na utanisaidia kusikiliza kelele za Maya, ili niweze kufanya kazi.” “Heeee!” Maya akalalamika nakukunja mikono kifuani kwake kama mtoto, akimtazama kaka yake. Wakacheka. “Basi nitahamia kesho. Acha nifungashe usiku wa leo.” Tunda akubali kwenda kuishi nao nyumba moja.

Tunda afanyika Msaada kwa Maya.

Nikweli alibadili maisha ya Maya. Kwa kuwa na yeye alikuwa akiongea kingereza kizuri, ilimrahisishia sana Maya kwenye mawasiliano, kwani mama yake ndiye aliyekuwa akimlazimisha kujifunza kiswahili. Tunda alimweleza maisha ya shida aliyopitia, bila kwenda kiundani zaidi, na kumwambia kama angepata nafasi kama yake, angeitumia vizuri sana.

Ilikuwa ni muujiza hata kwa Net. Maya alikuwa akimsikiliza sana Tunda kuliko mwanadamu yeyote yule aliyekwisha kuwa naye karibu. Kwa asili Maya alikuwa mbishi sana. Haambiliki na alilelewa maisha ya kudekezwa sana na bibi na babu yao. Hakuwa akijua shida hata kidogo. Tunda aliongea na Maya mpaka akakubali kurudi shule. Net alifurahi sana, akamshukuru Tunda. Alimpigia simu mama yake akiwa kule kule nchini Canada, Maya akarudishwa Canada kwa ajili ya kuanza chuo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hali ya babu yao ilizidi kuwa mbaya huko nchini Canada, ikamlazimu Net aende. Hawakuwa ni babu tu na bibi. Waliwalea Net na Maya tokea wadogo sana tokea  baba yao alipoanza kuugua mpaka akafariki. Na hata mama yao alipoondoka nyumbani kwa wakwe na kurudi nchini Tanzania, wao walibakia kwa bibi na babu yao. Walitunzwa wakachukua nafasi ya watoto kwa hao wazee waliokuwa wamepata mtoto mmoja tu ambaye ndiye baba yake Net na Maya.

Net alichukuwa jina la babu yake. Natheniel Cote. Ilibidi kuwa wakiandika sehemu muhimu wawe wanaandika Jr au Seniour ili kujua ni yupi. Shule zote za mahela yote hayo alizosoma Net, alikuwa akilipiwa na babu yao. Alipendwa sana, na alimkuza Net kwenye maadili ya msingi. Ndio maana Net alikomaa mapema japo alitoka kwenye familia ya kitajiri sana. Kila mtu alijua Net ndiye mrithi wa mali nyingi za huyo mzee Cote.

Kwa kuwa Maya alishaondoka nchini, wawili hawa walibaki wakiishi pamoja, kazini pamoja, kwenye gari pamoja. Japo haikuwa kwa muda mrefu, lakini palishajengeka ukaribu kati yao.

Net Arudi nchini Canada, Nakumlazimu kutengana na Tunda.

Tunda ndiye aliyemsindikiza Net uwanja wa ndege. Alikuwa amepooza. “Utakuwa sawa Tunda. Na nitakuwa nikikupigia simu kila siku. Kama ukiwa na maswali yeyote kazini, nikipiga simu nitakuwa nakusaidia.” “Lakini haitakuwa sawa kama tulivyokuwa wote! Najiona kama bado nakuhitaji sio tu ofisini, hata kwenye maisha ya kawaida. Naomba uniahidi kuwa utarudi Net.” Net alimuhurumia Tunda akajua aliingiwa na hofu na ndio maana hakumuaga mapema.

Tunda hakujua huyo Net alikuwa akisubiriwa kwa muda mrefu sana, lakini akawa akiahirisha safari kwa ajili yake. Kila alipojiambia ataondoka, alikuwa anaona bado hili na lile. Akawa akimwambia bibi yake nitakuja hivi karibuni. Lakini hakwenda mpaka alipoambiwa hali mbaya, anaweza asimkute babu yake, ndipo ikamlazimu kuondoka.

Akamgeukia vizuri. “Niangalie Tunda.” Tunda akamwangalia vizuri. “Nikikwambia hata mimi natamani nisiondoke, utaamini?” Tunda akatingisha kichwa kukubali. “Basi ujue nitarudi haraka. Niombee mambo yaende vizuri.” Walitafuta sehemu wakakaa, wakati wakisubiria muda wa Net wakuondoka. Tunda alikuwa amejisogeza karibu yake, ameinama. Hakuondoka mpaka Net alipoingia kwenye ndege. 

Maisha bila Net.

Tunda alitulia, akashika usukani. Ni kweli aliiendesha ile ofisi bila shida, huku akitumia gari ya Net na kuishi kwenye nyumba yao. Tunda hakuacha kuwasiliana na Net kumpa taarifa kwa kila kinachoendelea na kumtaka ushauri. Na kwakuwa na yeye alifanywa kuwa muweka saini benki, hata malipo mengine alifanya yeye mwenyewe, tena kwa uaminifu sana. Kila mwishoni mwa juma, alimtumia Net benki statement na ripoti ya matumizi yote. Walishauriana kwenye simu, na Net aliweza kuendesha mambo ya pale ofisini, akiwa mbali, kirahisi sana kwa msaada wa Tunda. 

Mapambano Bado Yanaendelea. 

Tokea aachane na Mama Cote pale kanisani hakuwa amemsikia tena huyo mama. Hata kupokea simu yake ya salamu hakupokea tena. Haikumsumbua Tunda kabisa, alijua ni hali ya ubusy kwani yule mama alikuwa muhangaikaji sana kisha akawa amekwenda nchini Canada kumuona huyo mgonjwa ambaye ni mkwewe.

Ilikuwa siku ya jumamosi ambapo Tunda alishazoea kufanya nusu siku alipokuwa na Net, lakini sababu ya kuwa peke yake aliitumia hiyo siku kukaa ofisini mpaka usiku. Alifanya mambo mengi, na akatayarisha ofisi ile kwa siku ya jumatatu. Kijana wa usafi hakuwa akija siku za jumamosi, kwa hiyo kila alipotumia ofisi siku za jumamosi, alijitahidi kuacha safi ili asimsumbue kijana wa usafi anapokuja siku ya jumtatu.

Alishaongea na Net wakati Canada ilipokuwa usiku wakapeana maelekezo na miahadi yakupigiana tena simu siku inayofuata, pale Tunda atakapo amka. Tunda akarudi nyumbani akiwa amechoka sana. Mlinzi akamfungulia geti, akamsalimia kwa kumpungia mkono akaingia ndani.

Alipoingia ndani, akakuta Mama Cote amekaa na msichana mwingine pale sebuleni. “Net hakuniambia kama mnaishi naye hapa!” “Sikuwa nikiishi na Net peke yake, mama. Maya ndiye alinikaribisha hapa.” “Maya!?” “Ndiyo mama. Shikamoo.” “Mwanzoni ulikuwa ukiishi wapi?” “Hotelini, mama.” “Kweli Net alikubali kukutoa kwenye nyumba za kulala wageni akakuweka hapa na mtoto mdogo kama Maya!?” Tunda akanyamaza. Hakuwa ameelewa kabisa, kwani Mama Cote aliyemfahamu yeye alijawa na hekima na mwingi wa shukurani. Na alimkarimu sana nyumbani kwake, akampa hata chumba chakuweka mizigo yake na kukitumia kama angelala.

“Kuna nini mama!?” “Nimeshtuka sana kukukuta nyumbani kwangu!” “Samahani mama, itakuwa Net amesahau kukwambia. Hata hivyo naweza kuondoka tu hata sasa hivi.” “Kabla hujaondoka nataka kukutambulisha kwa bosi wako mpya, huyu hapa. Anaitwa Safia. Safia amesoma na anauzoefu wa kazi, kwa hiyo atakusaidia sana.” “Karibu sana Safia. Basi jumatatu nitakuonyesha pale ofisini.” “Sio kumuonyesha tu! Nataka umkabidhi kila kitu, yeye ndiye atakuwa akikwambia kitu gani chakufanya.” Tunda alishtuka kidogo, lakini hakujali. “Sawa mama.” Tunda akaitika.

“Na atakuwa akitumia hicho chumba ulichoweka mizigo yako.” “Hakuna shida mama yangu. Nitaondoka na kila kitu.” Tunda akaingia ndani, akakusanya vitu vyake vyote, akaweka kwenye begi lake akaanza kulivuta kulitoa nje pamoja na mizigo yake mingine iliyokuwa na nguo, viatu pamoja pochi zake nyingi tu ambazo alipenda kubadili kama viatu. Akakumbuka amesahau funguo za gari ndani.

Akarudi wakati ameacha mizigo yake yote nje. Alipoingi tu, “Halafu binti!” Tunda hakujua kama anaitwa yeye, aliendelea kuelekea kule alipokuwa ameacha pochi yake aliyotumia siku hiyo. “Wewe Tunda, umeanza lini kiburi?” “Kwa nini mama?” “Nakuita kwa nini unanyamaza!?” “Sikujua kama unaniita mimi. Samahani.” Tunda aliendelea kujibu kwa heshima sana. 

“Naomba na funguo za gari. Atakuwa akitumia yeye hilo gari, kabla hatujamnunulia la kwake.” Tunda alifikiria kidogo. “Sasa hivi ni usiku mama. Naomba niondoke na gari, kisha nitarudisha gari asubuhi ili nisipate shida ya usafiri na mizigo yangu.” “Naweza kukuitia taksii.” Tunda akatulia kidogo, kisha akamsogelea Mama Cote.

“Kwani kuna tatizo lolote mama yangu? Mbona kama..” “Hakuna tatizo lolote. Mimi ndiye mmiliki wa kila kitu, au Net hakukwambia hilo?” “Nafahamu.” “Sasa unauliza nini endapo mwenye mali anadai mali zake!?” Tunda akabaki ameduaa.

“Na ninaomba funguo za ofisini kabisa, pamoja nafunguo za safe. Kwa kifupi naomba funguo zote za ofisi na simu ya ofisi pia naomba.” “Unamaanisha simu yangu ya mkononi!?” “Si ulinunuliwa kwa matumizi ya ofisini? Sasa unapunguziwa majukumu, huhitaji tena simu ya mkononi.” Tunda alibaki ametoa macho kwa muda.

“Vipi? Au uliahidiwa nini na Net? Isijekuwa navunja makubaliano fulani.” Tunda alivuta pumzi kwa nguvu, kisha akanyanyua pochi yake, akatoa simu na funguo zote za ofisi na gari kisha akamkabidhi. “Asante mama, usiku mwema.” Tunda akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ulikuwa ni mshtuko mkubwa sana kwa Tunda. Alijiuliza maswali mengi bila kupata jibu. Alifikiri hili na lile bila kuhisi kosa lake. Alikuwa na wakati mgumu sana akisubiria hiyo siku ya jumatatu, hata kanisani alishindwa kwenda.

Hakuwa na simu ya kuwasiliana na Net, kwa kuwa simu alinyang’anywa. Simu yake ilipotea kwenye mazingira ya kutatanisha. Hakujua kama aliiacha sehemu au aliibiwa kwenye pochi. Alijikuta hana simu ndipo Net akampa iliyokuwepo tu pale ofisini na kumtaka aitumie akisema ni muhimu kwa kazi kwa kuwa yeye alimwambia hana shida tena na simu. Hana mtu wakuwasiliana naye. Lakini yule mama alimpokonya. Ilikuwa simu nzuri sana.

Jumatatu ya machungu na mapinduzi!

Siku hiyo ya jumatatu aliamka mapema, na kuwahi ofisini. Alifika ofisini na kumkuta Mama Cote yupo ofisini kwa Net, na Safia yupo kwenye meza yake. Tunda aliweka pochi yake pembeni ya meza, akaingia kumsalimia Mama Cote. “Shikamoo mama.” “Naona hapa mambo yamekuwa yakiendeshwa kienyeji enyeji kweli! Sioni faili lako la kuajiriwa. Sioni vyeti vyako wala barua zako zakuomba kazi.” Tunda akabaki kimya, lakini mwili mzima ukitetemeka.

“Naomba ukaniletee vyeti vyako vyote vya shule,  ili tujue kama ni kazi ninakuajiri upande upi.” Tunda alibaki kama amepigwa na butwa. Kimya. “Umenisikia?” “Sina vyeti mama.” “Kwa nini huna vyeti?” “Sina vyeti kabisa.” “Kwani hukusoma!?” Yule mama akamuuliza kwa namna yakumdhalilisha mbele ya Safia na yule kijana wa usafi, waliokuwa wakisikiliza pale nje. Tunda akanyamaza.

“Hata cheti cha kidato cha nne huna!?” “Sina mama.” Tunda alishaanza kupaniki. Hofu yakufukuzwa kazi ikamjaa. “Wewe ulilemea upande mmoja tu, kutembea na wanaume za watu! Ukapata ujuzi wa kuvutia wanaume, ukakosa ujuzi wa ofisini! Sasa hapa Net wa kumrembulia macho ili aendelee kukuweka hapa ofisini, hayupo. Hii ni ofisi yangu. Nimehangaika sana kufika hapa nilipo. Sikutafuta pesa kwa kuvulia nguo waume za watu, nimehangaika mimi mwenyewe. Uzembe mdogomdogo sitaki. Hamkawii kunirudisha chini kimaendeleo!” Yule mama alianza kupiga mahesabu, kisha akanyanyuka.

Akafungua safe akatoa pesa. “Huu ndio mshahara wako wa mpaka siku ya leo. Rudi shule binti, acha kuruka ruka na wanaume. Ukishapata vyeti ndipo urudi tuzungumze.” Bila kuongeza neno, Tunda akapokea pesa yake, na kuondoka pale.

 Historia Yajirudia! Maisha mengine tena kwa Tunda mara baada ya kufukuzwa ‘Tena’ kwa kina Cote.

T

unda alirudi hotelini, akakaa chini asiamini kinachomtokea. Aliumia sana kusikia anatukanwa na Mama Cote, kwa kupitia maneno aliyosema kanisani, tena akiwa ameambiwa ni sehemu pekee ambapo atakuwa salama! Tunda akalia sana, lakini alikumbuka jinsi alivyofundishwa na Net kuomba.

Akapiga magoti akamuomba Mungu kwa kulia sana. Tunda akamlilia Mungu kwa uchungu akirudia rudia kumweleza maumivu aliyonayo. Hakuwa mjuaji sana wakuomba, lakini alijua kumueleza Mungu kile alichokuwa akijisikia. “Naogopa sana Mungu wangu. Nimeumia, nina maumivu makali sana. Sijasoma, sina kimbilio, sijui naanzia wapi tena maisha. Katika yote naomba nisaidie nilinde mwili wangu usiteswe tena. Sitaki kurudia yale maisha tena. Nisaidie kwa njia yeyote ile ili niweze kuishi kwa uwezo au karama yeyote uliyoniumba nayo, ukaweka ndani yangu kama alivyoniambia Net, kuwa kuna kipaji lazima umekiweka ndani yangu ambacho kitanisaidia. Usiniache tena. Milango yote naiona imefungwa, lakini najua Mungu wewe unaona kwa tofauti. Nisaidie.” Tunda akamaliza kuomba, akapata faraja ya ajabu.

          Wazo la kurudi Dar likamjia. Hakutaka kupoteza muda tena pale hotelini, akabeba mizigo yake yote, asubuhi hiyo hiyo akaenda kituo cha mabasi pale jijini Arusha, akakata tiketi yake akapanda basi kurudi Dar. Alionelea ni heri kurudi Dar, mji alioufahamu vizuri kuliko kuendelea kuishi Arusha. Hata hivyo vitu vyake vyote aliviacha huko.

Tunda arudi jijini Dar na kupambana Njiani na Jaribu akumrudisha kule Yesu alikomtoa kupitia Net.

Tunda alipata siti ya upande wa watu wawili. Pembeni yake alikaa baba mmoja mtu mzima kidogo. Walisha salimiana, lakini yule Mzee hakutosheka kumtizama Tunda. Na Tunda alijua. Akaamua kutoa bibilia yake asome ili kumfanya yule baba amuogope. “Soma kwa sauti basi na mimi nisikie neno.” Yule mzee alimtupia neno Tunda.

“Naweza nikakupa tu, usome mwenyewe.” Tunda akataka kumkabidhi. “Unakwenda kanisa gani?” Tunda hakuwa hata na kanisa analolifahamu huko Dar. “Ndio nahamia Dar, bado sijajua nitapata wapi kanisa.” “Ooh! Karibu sana jijini. Kwa hiyo hata sehemu yakuishi bado hujapata?” “Ndio naelekea huko. Naamini nikifika huko nitapata.” “Basi mimi niwe mwenyeji wako. Nina nyumba yangu napangisha vyumba huko Temeke. Naweza kukupangisha. Tena kuna mpangaji mmoja ametoka juma lililopita tu, nilikuwa nakikarabati hicho chumba. Ni chumba kimoja na sebule yake. Kwa kuwa ndio unahamia hata huna haja yakunilipa kodi kwa sasa, tutakatana juu kwa juu.” Tunda alitabasamu kisha akageukia dirishani.

“Vipi?” Akaendelea kutaka Tunda amsikilize. “Na kanisani nitakupeleka usiwe na wasiwasi.” Tunda alimgeukia yule Mzee akamtizama kwa muda, asiamini. “Au hutaki kuishi Temeke? Tunaweza tukashukia hotelini wakati tunatafuta nyumba nzuri ya wewe kuishi.” Tunda alifunga bibilia yake akairudisha kwenye pochi yake, .......

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ni sura tu ya matukio ndio inabadilika, lakini historia kujirudia kwa Tunda, inabaki palepale. Na hapo napo anafukuzwa baada ya kutenda mema, yakusifika na kuvutia, lakini napo ikadumu kwa muda tu, bila kujijua, akidhani ameokoka na dhoruba, kibao kimegeuzwa tena na Ulimwengu umeshamfungulia tena mikono kumpokea. Ahadi ya matunzo ipo kiti cha pembeni yake. Baba mtumzima kama wateja zake wa zamani. Amekwama, anahitaji msaada. Safari hii hakuna Net wakumuokoa. Tunda atafanyaje?

 Endelea kufuatilia kujua ni nini atafanya na  kwa nini Mama Cote naye ambadilikie gafla!!!!


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment