G |
abriel alimuona vile Net
alivyobadilika. “What Net? Nini?” Gabriel aliuliza kwa kujihami baada ya
kumuona jinsi Netanavyomuangalia. “No man! Hamna neno.” Net alijibu na uso
ulionekana kusikitishwa sana na rafiki yake. “No.
Say it. Just say it Net. Kumbuka mimi nakufahamu wewe vizuri sana Net. Wewe
ongea tu kile kilichopo mooni mwako. Maana ni wewe mwenyewe ndiye uliyeniambia
niachane na huyu msichana. Tena kwa mikwara mingi sana! Nilikwambia jinsi
ninavyompenda Nancy.” “Hujawahi kumpenda. Ulikuwa ukitumia tu mwili
wake, lakini si kumpenda.” Net akamkatalia Gabriel na kumshangaza.
“Unajuaje!?
Nilimpenda na….” “Please don’t. Just Don’t. Nyamaza tu.” “What’s wrong with you Net? Unatatizo
gani Net!? Mbona mimi sikuelewi?” Net aligeuka akataka kuondoka, kisha
akamgeukia rafiki yake tena. “Na kwa taarifa yako tu Gabriel, jina lake ni
Tunda, sio Nancy.” Gabriel alibaki ametoa macho asielewe, huku manyunyu ya mvua
yakiongeza kasi kuashiria mvua kubwa inakaribia kumwagika.
Tunda
alienda kuchukua mizigo yake aliyokuwa ameiacha pale mapokezi asijue anarudije
Dar, na hata usiku huo anakwenda wapi. Alitoka pale hotelini taratibu huku
akilia kwa uchungu sana. Mvua kubwa na radi iliyoanza gafla ilimfanya akimbilie
kwenye moja ya jengo la hoteli hiyo. Alikimbia mwisho kabisa kwenye kona akajibanza
huku akilia kwa hofu.
Kwa
asili Tunda alikuwa muoga sana wa radi. Alianza kutetemeka baridi, kwani pale
alipojificha pia mvua ilikuwa ikimfikia na hali ya hewa jijini Arusha ilikuwa
baridi haswa. Tunda hakuwa hata amevaa sweta. Baridi na hofu vilimjaa, na kila
aliposikia ngurumo za radi alizidi kutetemeka na kuzidi kulia. Pesa ya kuchukua
taksii hakuwa nayo. Halafu akajiuliza, hata akichukua taksii, inampeleka wapi
usiku ule! Akaendelea kulia. Mambo yamembadilikia gafla.
Aliona
gari ikizunguka pale, ikienda na kurudi mara kadhaa. Tunda aliendelea kulia.
Baada ya muda akamuona mtu akikimbia, kwenda na kurudi. Mvua kubwa bado ilikuwa
ikinyesha. Kwa mbalii akasikia mtu akiita jina lake. “Tundaa! Tundaaaaaa!”
Alihisi ni mawazo. Lakini kila alipojaribu kupuuzia ile sauti ndivyo
alivyoisikia kwa karibu zaidi.
Akasimama
kutaka kuthibitisha kama ni mawazo yake au la. Akajitokeza pale alipokuwa
amejificha na kuchungulia nje huku radi ikipiga sana. “Tundaaa!” Ana kwa ana na
Net, aliyekuwa amelowa chapachapa. Net alikuwa akimwita kama mwehu.
Alipomtambua kuwa ni Net, Tunda alifunika uso wake nakuzidi kulia kwa aibu na
uchungu.
Net
alimsogelea karibu kabisa, akasimama mbele yake asijue aseme nini tena. Alibaki
akihema kama mbwa aliyekimbia mwendo mrefu sana. Akabaki akimtizama Tunda.
Tunda akajua ni yeye ndiye aliyemuona akikimbia. Wakabaki wamesimama pale.
Tunda akilia huku amejificha uso, akiwa amebeba mizigo yake, Net akihema.
“Twende
kwenye gari.” Net alimpokea mabegi yake, akayabeba kwa mkono mmoja, kisha akamshika
mkono Tunda kwa mkono wake mwingine, akamuongoza lilipokuwepo gari yake. Wote
wawili walikuwa wamelowa haswa. Akamfungulia mlango wa gari, kiti cha mbele,
Tunda akapanda na kujikunja kwenye kile kiti huku akitetemeka baridi. Net
aliwasha heater ili kuleta joto mle ndani ya gari. Tunda aliendelea kulia mpaka
alipopitiwa na usingizi. Hakujali anapopelekwa na Net, akalala.
Net
aliendesha mpaka hoteli nyingine mbali kidogo na ile hoteli aliyokuwepo Gabriel
na mkewe pamoja na mama yake Net, akaingia yeye mwenyewe kwanza akachukua
chumba ndipo alipoenda kumuamsha Tunda. “Twende ukalale ndani.” Net alimbebea
vitu vyake akaongoza mpaka chumbani. Kilikuwa ni chumba chenye kitanda kimoja
tu, kochi na choo humo humo ndani.
Akamuwekea
mizigo yake mle ndani nayo ilikuwa inachuruzika maji. “Pumzika nitakuona
kesho.” Tunda alishindwa hata kumtizama Net usoni. Alibaki akilia sana, huku
amefunika uso wake. Net alibaki kimya huku bado amesimama pale asijue aseme
nini.
“Nenda
kabadili nguo utaanza kukohoa. Nitawaambia hapo mapokezi wakuletee chakula.
Utataka kula nini?” Tunda akatingisha kichwa kukataa bila hata kumtizama. “Basi
nitakuoana kesho. Usiku mwema.” Net alisimama tena mlangoni kwa muda bila
kusema kitu. Lakini ni kama maneno mengine yaligoma kutoka, gafla akajikuta
hajui aseme nini tena. Akaona ni heri aondoke tu. Alipomuona Tunda anaelekea
bafuni, akatoka na kufunga mlango.
Kesho
yake asubuhi aliletewa kifungua kinywa na muhudumu wa ile hoteli, bila hata
yakupiga simu kuagiza. Mchana akaletewa tena chakula cha mchana. Lakini
ilipofika jioni aliamua kupiga simu mapokezi kuwaomba wasilete tena chakula
kingine usiku.
Ilipofika
saa mbili, akasikia mlango ukigongwa. Alisimama kwenda kufungua. Alikuwa Net.
Mwili mzima wa Tunda ulikuwa ukitetemeka baada yakumuona Net. Alimpisha
mlangoni, Net akaingia.
“Mbona
wameniambia umekataa chakula cha usiku?” “Bado nimebakiza kile cha mchana.
Sikula, nilikuwa bado nimeshiba” “Sasa sikitakuwa kimeharibika?” “Hapana. Bado
kizuri tu.” Net alikaa kwenye kochi nakujiegemeza. Tunda akabaki amesimama pale
pale mlangoni, Net akamgeukia. “Vipi! Mbona hukai?” Tunda alikwenda kukaa
pembeni ya kitanda akainama.
“Tumefungua
ofisi nyingine huku Arusha, nimekuwa huku kwa muda mrefu kidogo. Nipo kwenye
kutafuta watu wakunisaidia kazi. Kama unataka kazi, unaweza kupata.” Tunda
akatulia tu kama hakuwa akiongeleshwa yeye. Akabaki ameinama. “Tunda?” “Sijasoma
Net. Sina kitu kichwani. Elimu niliyonayo ni kama ya darasa la pili tu.” Net
alitulia akimwangalia mrembo mwenye elimu ya darasa la pili. Bado Tunda alikuwa
ameinama nakushindwa kumwangalia kabisa Net.
“Kila
kitu ni kujifunza Tunda. Ukiwa na nia hakuna kinachoshindikana. Hata hivyo sio
kazi zote zinahitaji elimu.” “Nitaishi wapi huku Arusha?” “Sio lazima
ukaendelea kuishi huku. Nahitaji msaada kwa sasa mpaka nitakapopata watu wa
kudumu. Ukipenda kubaki sawa, ukitaka kuondoka baadaye pia siyo mbaya.”
“Asante.” “Huwa unafanya kazi siku za jumamosi?” “Sina kitu chakufanya kwa
sasa, naweza kufanya tu kazi.” “Basi nitakuja kukuchukua kesho twende wote
kazini.” “Asante Net. Asante sana.” “Karibu. Nitakuona kesho.” Net akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net
alirudi pale hotelini asubuhi hiyo ya jumamosi akamkuta Tunda alishajiandaa.
Alimtizama mara mbili mbili, Tunda alikuwa amependeza sana, lakini uso ulijaa
majonzi. Net alimchukua mpaka ofisini. Ofisi ilikuwa nzuri na yenye vitu vya
kisasa tupu, lakini havijapangiliwa. Tunda akaanza kubabaishwa na aina ile ya
ofisi nakujiona hafai kuwepo kwenye meza nzuri za kiofisi, viti vyakuzunguka
kama vile na makabati ya kioo! Ilikuwa rahisi kuigiza ni msomi na anakazi
sehemu fulani. Lakini akakumbana na uhalisia, anatakiwa aishi kile alichokuwa
akikiigiza kwa muda mrefu, hofu yakuishi vile ikamwingia.
“Ninae
dada mmoja tu anayenisaidia. Naona kama analemewa kuwa peke yake. Jumatatu
utakutana naye, atakuelekeza baadhi ya mambo ya kufanya.” “Sidhani kama
nitaweza. Naona kama…..” Tunda akasita. “Sijui Net! Sina uwezo huo.” Net
alibaki akimwangalia anavyojitetea kwa kubabaika. “Siwezi kukaa kwenye ofisi
kama hii! Nitakuwa nikifanya nini?” “Mbona unashindwa kitu ambacho hata
hujajaribu Tunda? Umeshajua kazi yenyewe? Au hutaki kuwa hapa? Kama hutaki upo
huru kuondoka Tunda. Sitaki niwe nakulazimisha.” Tunda alianza kulia.
“Sina pakwenda Net. Ila nahofia kuharibu.” “Usigope.
Utafundishwa taratibu mpaka utaweza. Kwani ulikuwa ukiishi wapi?” “Nilikodi nyumba. Lakini nimeshindwa kulipa kodi. Mwenye
kampuni ya Ulinzi amenitumia ujumbe jana usiku kuwa, mlinzi aliyekuwepo pale
nyumbani akinilindia vitu vyangu, amempigia simu usiku huo kumwambia mwenye
nyumba ameenda pale na kuanza kunitolea vitu vyangu nje.” “Pole sana.
Unataka kwenda kuvichukua?” “Nitaviweka wapi? Nipo
kama nilivyo hivi.” “Hatuwezi kukosa pakuviweka. Tunaweza kuondoka kesho
siku ya jumapili na ndege ya asubuhi nakurudi jioni.” Kwa kulia, Tunda hata
hakusikia kauli sahihi ya ‘tuna’.
Yaani Net akijiunganisha. Akaendelea kulia.
“Sina hata nauli ya basi, nitaweza wapi ya ndege!?” “Kwanza
umekubaliana na wazo langu?” “Wazo ni zuri, lakini
utekelezaji wake ndio mgumu. Nikifikiria pakuweka hivyo vitu ndio
nachanganyikiwa kabisa. Sina ndugu wala rafiki kwenye ule mji.” “Kwanza
naomba unyamaze. Acha kulia. Halafu nashauri twende wote kwanza tukaviangalie
ndio tutajua pakuviweka.” “Asante Net.” “Basi
usilie. Tufanye kile kinachowezekana sasa hivi kwanza. Hatua moja hadi
nyingine. Sawa?” Hapo Tunda akawa ameelewa kuwa na yeye atasaidia. “Sawa?”
Tunda akatingisha kichwa kukubali. Net akaingia ofisini kwake, akamwambia Tunda
akae pale kwenye meza ya mapokezi amsubirie kidogo.
Walishinda siku nzima pale
kazini. Net akionekana ana kazi nyingi zakufanya. Alibaki ofisini kwake bila
kutoka. Tunda akahisi amemsahau. Akaangaza macho akijiuliza kitu chakufanya.
Maana muda ulizidi kwenda, yeye amekaa tu. Mwishoe akaamua kusafisha na kupanga
ile ofisi iliyokuwa imejaa vitu vizuri,
lakini hakuna mpangilio.
Akazunguka hapo ndani akakuta
jiko na choo. Akapata vifaa vya usafi. Akaanza kusafisha. Net bado alikuwa
ofisini kwake. Tunda hakujua kinachoendelea huko ndani. Ofisi yake ilikuwa
ndani na mlango umerudishiwa. Pako kimyaa. Tunda akaanza kusafisha na kupanga
ofisi nzima bila kusababisha kelele. Aliendelea kusafisha kwa haraka huku
akimsubiria bosi wake atoke ampe kazi.
Baada ya
muda ndipo Net akatoka nakubaki akishangaa. “Nimesafisha na kupanga. Sijui ni
sawa?” Tunda alimuwahi huku akimalizia kuweka mafaili yaliyokuwa sakafuni, na
kuyapanga kwenye kabati ambalo bado lilionekana jipya tu, zuri sana lenye
milango ya kioo mbele, lakini lilikuwa tupu kabisa. “Ona kulivyopendeza!
Angalau panaeleweka sasa hivi. Halafu unasema huwezi kufanya kitu chochote!
Hapo si umefanya kitu kizuri kabisa? Pamependeza sana. Mama akija kurudi tena
atashangaa sana.” Tunda alifurahi kuona amepongezwa.
“Nimewasiliana
na watu wa ndege, tumepata tiketi ya asubuhi sana. Utaweza kusafiri asubuhi
hiyo?” “Nitaweza. Asante.” “Twende basi tukale, uwahi kulala. Kesho nitakuja
kukuchukua mapema sana.” Net alimpeleka sehemu ambayo alidhani Tunda hapafahamu
kumbe vilikuwa ndio viwanja vyao yeye na Gabriel. Net alimwambia waende wenyewe
jikoni wakachague nyama.
Wakaongozana
mpaka kwenye dirisha la jikoni. Walikuta watu wengine wakisubiri. Na wao
wakajiweka kwenye foleni yakusubiria. Mchoma nyama ndani alipomuona tu Tunda,
akaanza kumchangamkia, kwani alimfahamu yeye na Gabriel jinsi walivyokuwa
wakiwapa tip/pesa pale kila walipokuwa wakienda kula nyama choma.
“Mzee yuko wapi?” Yule kijana
alimuuliza akiwa ameonyesha kumchangamkia kweli Tunda huku akiendelea kuchoma
nyama. Tunda akaanza kubabaika, Net alibaki kimya pembeni. “Au leo uko peke
yako?” “Sikuja naye.” Tunda akajibu kwa shida kidogo huku akijikanyaga kanyaga.
Walirudi mezani Tunda alishindwa
kuongea kabisa. Wahudumu wote walimuulizia Gabriel, mwishowe Tunda akaamua
kuondoka pale. “Naomba nikakusubirie kwenye gari, Net.” “Basi ngoja niwaambie
watuletee chakula hukohuko kwenye gari, tutaenda kula hotelini.” Tunda
alijisikia vibaya sana. Akatoka pale bila hata kusubiria zaidi.
Baada ya
muda akamuona Net anarudi garini na chakula. “Naona tumefanyiwa upendeleo.
Nilienda kuaga, naona wamenikabidhi chakula.” Tunda akakumbuka walikuwa
wakifanyiwa hivyo hivyo kila walipokuwa wakienda pale na Gabriel kwa kuwa
Gabriel alikuwa akiwapa tip nzuri.
Walirudi
hotelini Tunda akiwa kimya kabisa na Net hakutaka kuuliza. Net aliwasha tv mara
tu alipoingia chumbani kwa Tunda na kujitupa kwenye kochi. Alikula chakula
chake huku akiangalia tv. Alibadilisha tv huku na kule ili kupata taarifa ya
habari wakati akiendelea kula. Alipomaliza kula na kuangalia taarifa ya habari,
akataka kuondoka. Tunda na yeye alikuwa ameshamaliza kula.
“Nitarudi kesho asubuhi na
mapema, Tunda. Usichelewe kulala.” “Lakini Net.” Tunda alimuwahi Net akiwa
anataka kutoka, akiwa amesimama, na yeye akasimama huku akibabaika sana.
Alimuogopa sana Net, hata hakuwa akiweza kumwangalia vizuri. Net alibaki akimwangalia
vile anavyotetemeka mbele yake. “Kuna nini?” Net akamuuliza taratibu. “Au usiku
mwema.” Tunda alishindwa kuongea kwa hofu, akaamua kumuaga tu.
Net akarudi kukaa. Taratibu
machozi yalianza kumtoka tena Tunda. “Vipi Tunda?” “Naona
tuache tu.” “Nini?” Net akauliza. “Hiyo
safari ya Dar. Nitakuja kwenda wakati mwingine.” “Kwa nini? Unajua
nimeshakata tiketi?” “Samahani, lakini nadaiwa.
Siwezi kurudi mikono mitupu, bila pesa za watu.” Net akatulia kidogo.
“Nani
anakudai?” Net akauliza. Tunda akajifuta machozi na kujaribu kutulia. “Kodi ya
miezi 3, kampuni ya ulinzi na kijana niliyemwajiri wa kazi.” “Kwa hiyo unataka
kukimbia deni?” Net akamuuliza taratibu tu. “Sijui
chakufanya Net. Sielewi nitafanya nini. Kwa mfano yule kijana wa kazi alikuwa
akinipigia simu siku nzima ya leo akitaka nimpe pesa yake. Ndio jioni hii
nimemtumia ujumbe, wakumtaarifu kuwa bado sijapata pesa, ila anaweza kwenda
kuchukua kitu chochote kwenye vitu vyangu kama kujilipa. Hajanijibu. Haya, yule
mmiliki wa kampuni ya ulinzi alinipigia simu siku ya jana akinitishia
kunipeleka polisi kama sitampa pesa yake. Ameniambia jumatatu ndio mwisho.
Nataka na yeye nimuombe kama anaweza kuchukua baadhi ya vitu vyangu, akae navyo
mpaka nitakapo mlipa. Ila kodi ndio inanichanganya zaidi, sijui nitafanyaje!”
“Usiwe
na wasiwasi, wewe twende tu. Watumie ujumbe sasa hivi, waambie ukutane nao wote
hapo nyumbani kwako, siku ya kesho asubuhi ya saa nne. Na uwaambie wasichelewe,
kwa kuwa tunarudi kesho hiyo hiyo huku Arusha. Hatutakuwa na muda wa kumsubiri
mtu.” Tunda alifuta machozi kwa mikono yake, akafuata simu yake, akatuma ujumbe
kwa wote kama alivyoambiwa na Net.
“Nimeshawatumia.”
“Naomba uniambie kila mmoja anakudai kiasi gani. Nitawalipa kwa hundi.
Unafikiri ni sawa? Maana sina pesa hapa mfukoni.” “Hawatakuwa na shida.
Wanachotaka ni kulipwa.” Tunda akajibu na kumtajia kwa woga sana kiwango
anachodaiwa na kila mmoja wao. “Lakini Net, naweza
kuwaomba niwalipe kidogo kidogo. Sio lazima kuwalipa zote kwa pamoja.”
Net akasimama. “Usiwe na wasiwasi. Wewe lala. Nitakufuata kesho.” “Asante sana Net. Nakushukuru.” “Karibu. Usiku
mwema.” “Na wewe.” Net akatoka.
Alipofunga mlango tu, Tunda
akaanza kulia kwa uchungu sana. Net alibaki nje ya mlango akimsikiliza jinsi
anavyolia kwa kuugua. Alitamani arudi ndani, lakini aliona aache tu. Tunda
aliendelea kulia kwa muda mrefu sana huku akigugumia kama mtu asimsikie.
Alifika mwisho kabisa. Kama ni kuzama kisimani, basi alishazama na kunywa maji
mengi sana, akabaki akielea kama mzoga.
Aibu ilikuwa imemuandama, hofu
ndiyo ilizidi kumtesa. Net ndiye mtu wa mwisho kabisa kwenye Maisha yake
angetamani kuwa naye karibu, kwa vile anavyomfahamu kwa uchafu wake. Alijua Net
anamjua jinsi alivyo mchafu, yeye mwenyewe alijionea kinyaa. Net je? Alijiuliza
huku akitamani asiwe Net anayemsaidia. Lakini hakuwa na namna nyingine.
Alibanwa vyakutosha. Net aliposikia kimya, akajua amepitiwa na usingizi, ndipo
alipoondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
N |
et alifika hotelini hapo asubuhi
hiyo na mapema akamkuta Tunda alishajiandaa, anamsubiria akiwa mnyonge na macho
mekundu. Alionekana aliamka na kuanza kulia tena. Net aliogopa kuuliza asije
akaanzisha kilio kingine na kushindwa kuwahi ndege. Waliondoka mpaka uwanja wa
ndege, akaacha gari lake uwanjani hapo, wakaenda kupanda ndege kuelekea Dar.
Tunda alipofika tu kwenye ndege, alilala mpaka Net alipomuamsha kuwa wamefika.
Alikuwa amechoka, zaidi akili.
Ndege
ilitua jijini Dar, Net akamkuta Wanja, mtu anayemtumia kwa maswala ya usafiri
hapo Dar. Alikuwa akimiliki magari makubwa na madogo anayofanyia biashara.
Ndiye aliyemuomba afike hapo awasaidie usafiri wa kuwapeleka kwa Tunda akijua
hata huko atakuwa msaada wakupata usafiri mwingine. “Nakushukuru sana Mkuu, na
samahani kwa kukusumbua najua leo jumapili ni siku ya familia.” “Hamna shida
kabisa. Nilipomwambia tu wife kuwa ni wewe, akaniambia nikimbie haraka sana.” Wote wakacheka. Tunda alikuwa ameingia chooni
mara tu walipotoka kwenye ndege. Kwa hiyo Net alikuwa na mwenyeji wake tu
wamesimama wakiongea wakati wakimsubiria Tunda.
Alitoka
chooni, na kuwasogelea pale walipokuwa wamesimama. Jicho kwa jicho na mteja
wake huyo Wanja. “Judy!” Tunda aliinama. Net akabaki akiwatizama, kama
aliyeshtuka. Hakutegemea hata Wanja! Alionekana mtu wa familia na mwadilifu.
Wanja akajaribu kupotezea, lakini asijue Net anaelewa kila kitu. “Nafahamiana
na huyu dada alinisaidia lifti kipindi gari langu lilipoharibika. Hata jina
lake simfahamu vizuri.” Akajichanganya. Gafla akasahau kuwa alitoka kumwita
Tunda, jina la Judy na wala Tunda hakuwahi kumiliki gari. Akajitetea kwa
kubabaika sana huku akiongopa. “Ooh! Kumbe hamna haja ya utambulisho? Basi
twendeni.” Net akajibu na kuwaacha wakitizamana nyuma yake. Kisha wakamfuata.
Tunda
alipanda garini akabaki ameinama bila hata kuongea. Tunakutegemea wewe Tunda
ili utuambie ni wapi unaishi na utuongoze njia. Nataka tuone vitu vyenyewe
kwanza ndipo nijue ni aina gani ya gari itahitajika kuvibeba.” Tunda akanyanyua
uso. Hakuwahi kutaja jina la mtaa anaoishi hata mara moja. Ni kama alilifuta
hilo jina kichwani mwake kwa makusudi ili asije wahi hata kuropoka kwa mtu.
Akabakia kujua njia tu.
“Nielekee
wapi?” Wanja ambaye ni dereva akauliza wakati anatoa gari pale uwanja wa ndege.
“La Dolce Vita.” Tunda akajibu taratibu. Mpaka Net akamgeukia. “Unamaanisha
unaishi mitaa ya karibu ya ile hoteli ya La Dolce Vita ya Oyster bay!?” Net
akauliza kwa mshangao. “Ndiyo. Twendeni mpaka kule baharini kabisa. Nyumba
haipo mbali na ilipo hoteli.” Tunda alijibu kwa upole, Net akaelewa ni kwa nini
anadaiwa kodi kubwa vile. Dereva akakanyaga mafuta, Tunda akarudisha uso wake kuangalia
chini .
Dereva
alipofika mpaka baharini akataka kuelekea Coco Beach, Tunda akamwambia akate
kona kulia. Akamuelekeza mpaka kwenye nyumba aliyokuwa akiishi.
“Hapa
ndio kwako Tunda!?” Net akauliza kwa mshangao. “Ndiyo.” Nyumba ndogo lakini
nzuri sana. Ilikuwa ya kisasa. Kuanzia getini mpaka ndani, ungependa. AC
ilikuwa nyumba nzima. Pasafi. Kuja kuona hivyo vitu vyenyewe vya Tunda, ambavyo
baadhi vilishaanza kutolewa nje, Net akamwangalia Tunda.
Vilikuwa
vitu vizuri, vilivyotangaza utajiri mtupu kwa kuviangalia tu kwa macho. Marembo
ya dhahabu nzuri iliyokatwa kwa ustadi yalizungushiwa kwenye kila kifaa cha
Tunda. Kitanda, meza zake, makabati, vioo vyakujiangalia, meza yakujitengenezea na viti vyake, kila
kitu kilikuwa na marembo mazuri sana na manyoya mazito meupe.
“Ulipata wapi haya makochi, meza…!? Kila kitu!”
Wanja aliuliza kwa kushangaa sana. “Nilienda kununua Arabuni.” Tunda alijibu
kiunyonge bila ujasiri.
“Daah! Ni vizuri sana. Sijawahi on ahata kwenye
picha! Na vinaonekana ni vya thamani sana. Kwa ile lori yangu, Mkuu, itabidi
kubeba hata mara tatu. Hivi vyombo ni vingi sana na vyote vinaonekana ni vya
thamani sana. Tukivibebanisha, tutaharibu.” Net alibaki kimya akiwaza huku
akiangalia vile vitu vyote, akifikiria pakuviweka. “Unapakuviweka lakini?” Wanja akamuuliza Net. “Maadamu tupo hapa,
lazima tutatafutia ufumbuzi. Hatutashindwa. ” Net akajibu na kuendelea. “Ili
kuokoa muda, naomba ukatutafutie usafiri unaweza kubeba hivi vitu.” Wanja
akaondoka na kuwaacha Tunda na Net.
Baada ya muda kidogo, akaingia mwenye nyumba na
mwenye kampuni ya ulinzi. Ni kama waliongozana. Tunda akasalimia. “Ulituambia
tuje leo.” Mwenye nyumba akavunja ukimya. Net akawasogelea. “Nashukuru kwa kuwa
hapa. Niombe kama mtaridhia, mpokee hundi.” “Bila shida. Ilimradi tumalizane
kwa amani.” Mwenye kampuni ya ulinzi akajibu.
Net
alikuwa ameshawaandikia hundi zao kutokea Arusha. Alichofanya ni kumkabidhi
Tunda anayewafahamu, ili awakabidhi bila kuchanganya. Tunda akazipokea huku
akitetemeka. Hata mikono yake ilikuwa ikionyesha jinsi anavyo tetemeka. Akasoma
kiasi kwenye kila hundi, akawakabidhi kila mmoja wao.
Net hakuwa ameandika majina yao, ila pembeni ya
sahihi aliandika sababu. Ya kwanza, ‘Kodi ya Tunda.’
Hundi ya pili, ‘Ulinzi wa Tunda.’ Hundi ya tatu,
‘Mfanyakazi.’ Tunda mwenyewe akashangaa vile
alivyoandika. Alimtajia tu walipokuwa hotelini, aliondoka pale Tunda akiwa hana
uhakika kama atakumbuka. Lakini alikumbuka na akaandika kiasi kwa usahihi.
Aliwakabidhi hao wawili. Wakashukuru. Wakamsikia mwenye nyumba akimwambia mwenye
kampuni ya ulinzi angependa waendelee kulinda hapo mpaka mpangaji mpya
atakapohamia hapo week inayokuja. Wakakubaliana, wakaondoka. “Nashukuru Net.” Net akamgeukia Tunda, akamuona
anafuta machozi. “Karibu.” Net akajibu.
Baada ya muda wakati Tunda akikusanya vitu vyake
vizuri, Net akifungua vitu kama kitanda, nakumsaidia Tunda kuweka vitu vyake
pamoja na kirahisi ili viweze kuhamishika, kijana wake Tunda, wa usafi na yeye
akafika hapo akiwa na usafiri wa baiskeli akiwa na maboksi mengii. Tunda akamtambulisha
kwa Net. “Wewe naomba tumalizane ukishatusaidia kuhamisha hivi vitu hapa.
Nitakulipa. Ni sawa, au kuna mahali unataka kuwahi?” Net akamuuliza. “Hamna
shida Mkuu.” Akakubali kwa haraka bila shida.
Wakaungana kufungasha pale pale nje. Ni kweli vitu
vyake karibu vyote vilikuwa nje. Nguo na viatu bado vilikuwa ndani, na vyombo
vya jikoni. Wakasaidia kwa juhudi zote ili gari litakapofika iwe ni kupandisha
tu.
Walifanya kazi kubwa. Mpaka lori linafika hapo,
walikuwa wameshakusanya karibu kila kitu. Net alimwambia Tunda yeye asibebe
vitu vizito. Wao watasaidiana kubeba. Kazi yakupandisha ikaanza, huku Tunda
akipandisha nguo zake na viatu. Alikuwa ameweka kwenye masanduku na maboksi
aliyoletewa na yule kijana wake wa usafi. Alimuagizia usiku uliopita.
Alimwambia afike hapo kuchukua pesa zake, aje na maboksi makubwa na magumu. Na
kweli yule kijana alifanya hivyo. Yakamsaidia sana Tunda.
Net na yule rafiki yake, Wanja pamoja na kijana wa
Tunda na dereva wa lile lori walisaidiana kupandisha vitu vyote kwa tahadhari.
Net akihakikisha hakiharibiki kitu hata kimoja. Akasimamia upangwaji wake, vitu
vingine vikawekwa kwenye hiyo gari kubwa iliyokuwa imekuja kuwapokea uwanja wa
ndege. Hasa viatu na nguo za Tunda. Walipohakikisha kila kitu kipo ndani ya
magari, ndipo Net akamwambia rafiki yake apande kwenye lori, yeye ataendesha
gari lake na Tunda. Wawafuate nyuma. Tunda akamuona akizungumza nao yeye akiwa
anasubiri ndani ya hiyo gari ya Wanja, akamuona Net anarudi. “Tuondoke sasa.”
Akawasha gari na kuondoka, Tunda hata hakuwa akijua wanaelekea wapi. Akaamua
kunyamaza tu.
Akaona Net akiongoza njia mpaka Salasala. Tunda
alikuwa ametulia kimya akimtizama na kumtafakari bila jibu. Kijana mtulivu.
Alionekana kila kitu anakipigia mahesabu na kukifanya kwa makini sana kama
asiyetaka kufanya kosa. Yupo makini, na kila walipopita na Tunda, alikuwa
ameshaandaa mazingira. Kuanzia wanatoka Arusha, mpaka hapo walipo wanahamisha
vitu vyake. Watu waliokutana nao pia aliwaandaa siku moja kabla. Anakwenda kwa
muda na mpangilio. “Huyu kweli mzungu.”
Alijisemea Tunda.
Waliendesha kimya kimya. Hakuna aliyemuongelesha
mwenzake. Kutoka hapo Oysterbay mpaka Salasala. Tunda alikuwa amejiegemeza
kimya, haamini kama Net anamtua mzigo mkubwa vile! Akaona wamefika. Net alipiga
honi mara moja tu, geti likafunguliwa. “Hapa ni wapi?” Ikabidi Tunda aulize
sasa. “Ni kwangu, lakini siishi hapa kwa sasa. Naishi na mama na mdogo wangu
akiwa likizo. Kwa hiyo vinaweza kukaa tu hapa.” Tunda akajiweka sawa pale
kitini ili kuangalia.
Na
yenyewe ilikuwa nyumba nzuri sana. Ilijengwa peke yake ndani ndani kidogo
kwenye huo mtaa wa Salasala. Juu ya mlima. Ukisimama kwa nyuma, unaona bahari
kwa kwa mbali na nyumba nyingine. Madhari yake na ramani, Tunda akabaki
akishangaa. Ni kama kulipitishwa gari kubwa la greda ili kuchonga sehemu fulani
fulani za bustanini. Kulizungushwa rembo za namna yake. Mbele ya hiyo nyumba
kulikuwa na sanamu ya kipekee, inayotoa maji mdomoni, yaliyotengeneza bwawa la
rangi ya bluu, humzunguka huyo sanamu. Na lile bwawa lilijengewa kisanifu.
Tunda akabaki anakodoa macho.
Net
akavuta gari mpaka pembeni ili kupisha lori iliyokuwa imebeba vitu vya Tunda.
Akawaonyeshea ishara wapite kama wazunguke nyuma kidogo. “Twende tukawaelekeze,
halafu ndipo tutakuja kuchukua vitu vya humu ndani ya hili gari.” Net akashuka,
Tunda naye akafuata. Net akamuelekeza dereva wa lori mpaka kwenye kinyumba cha
nyuma. Tunda na yeye anafuata nyuma. Kumbe ilikuwa stoo. Walipoingia, palikuwa
pakubwa. Humo ndani ni pasafi na kumepangiliwa pia.
Akaingia
kijana aliyemsalimia kwa heshima sana Net. Tunda akajua ni mfanyakazi wake.
“Vipi Max?” Akamsikia akimuulizia yule kijana. “Nimetoka kumuogesha sasa hivi
na kumpulizia dawa. Yupo sawa.” “Chakula chake bado kipo?” Net aliendelea
kuuliza. “Bado kipo kingi tu. Week hii ndio ya chanjo. Nakumbuka. Nitampeleka.”
Akajibu yule kijana. “Sawa sawa.” Net akajibu na kumgeukia Tunda.
“Huyu
anaitwa Emma. Ndiye anayeishi hapa.” Akamtambulisha kwa Tunda. “Emma, huyu ni
Tunda, ndiye mwenye hivi vitu vyote.” Wakasalimiana, Tunda akawa anajiuliza
sasa Max ni nani!? Ila kama kawaida yake, akajua hayamuhusu. “Karibu dada.”
Akampa mkono Tunda. “Asante.” Tunda akashukuru na kumgeukia Net. Macho
yakagongana. “Asante Net.” “Karibu. Njaa inauma sana?” “Hapana. Sijisikii kula
kabisa.” Tunda akaanza kutokwa na machozi. Dereva na rafiki wa Net wakaingia na
wao.
Net
akamshika mkono Tunda na kumsogeza pembeni mpaka sehemu iliyokuwepo makochi.
“Naomba utulie. Tumeshapata hii sehemu. Tunaweza kuhifadhi hivi vitu kwa muda
wote mpaka utakapokuwa tayari kuvichukua. Kaa hapa kwenye makochi, ni pasafi
tu. Nisubiri tusaidiane kushusha vitu, tuondoke. Unataka soda?” “Hapana.” Tunda akakataa. “Basi nitamtuma Emma
akuletee maji ya kunywa.” “Asante.” Ndilo
neno ambalo Tunda lilikuwa likimtoka kila mara. “Naomba utulie. Naamini kila
kitu kitakuwa sawa. Sawa?” Tunda akajifuta machozi, na kuvuta pumzi. “Nakushukuru Net.” “Karibu. Basi ngoja tuanze
kazi.” Akamuacha amekaa hapo, akawasogelea wengine.
Akamuona
anawaonyesha sehemu ya kuviweka vile vitu vya Tunda. Ukweli palikuwa pakubwa na
pazuri. Ilikuwa ni bohari ndio, lakini sakafu yake ilionekana nzuri sana.
Upande yaliopo hayo makochi, kulikuwa na kinanda cha kawaida tu. Tv kubwa
imening’inizwa na meza yakuchezea tenesi. Kuliwekwa kapeti chini. Zuri sana.
Upande
kulikuwa na vifaa vilivyofunikwa na mashuka makubwa. Tunda hakujua ni nini
kilichofunikwa humo ndani ya hayo mashuka. Ila nakwenyewe kulikuwa kusafi. Kona
ingine kulikuwa na chumba alichohisi ni choo. Ndio upande mwingine ulikuwa wazi
kabisa. Ndipo alipoona akielekeza watu waweke vitu vya vyake.
Alimuona Net akivipangilia vizuri.
Walisaidiana wote wanne. Net, Emma, rafiki wa Net, Wanja, ambaye alishakuwa
mteja wa Tunda na dereva wa lile lori. Walifanya kwa haraka mpaka wakamaliza.
Net akamlipa yule kijana wa lori, akatoa lori yake pale.
Net
alilisogeza ile gari ndogo karibu kabisa na mlango. Tunda alipomuona anashusha,
akamsogelea. “Usibebe vitu vizito. Emma atatusaidia.” Net na Emma wakashusha
mpaka wakamaliza. Vitu vyote vya Tunda viliweza kutoshea kwenye huo upande tena
bila kubebanisha. Tunda alibaki na maswali lakini aliogopa kuuliza zaidi kwani
alijua Net ndiye ana maswali mengi zaidi yake. “Asante sana Net. Nakushukuru.”
“Karibu.” Akabaki amesimama kama anataka kuuliza swali, Net akaelewa. Akaomba
Emma na rafiki yake wasubiri nje.
Wakabaki
wao wawili. Akamgeukia Tunda. “Sijui nibebe nini kwa kuwa sijui nitakuwa kule
kwa muda gani!” Tunda akaonge kinyenyekevu. “Inategemea na wewe. Unataka kuwepo
Arusha?” “Sina uchaguzi Net. Kama unafikiri naweza
kufundishika, nikaelewa, nitashukuru.” “Naamini utaweza tu. Ondoa hofu.”
Tunda akajifuta machozi tena. “Basi naomba muda
mfupi wa kuchukua baadhi ya nguo na vitu nitakavyovihitaji.” “Sawa.” Net
akatoka nje kama kumpa nafasi.
Tunda
alichukua begi kubwa. Akaanza kufungasha. Kila kitu alitamani kubeba. Kila kitu
aliona kina umuhimu. Akaanza kulia kuacha vitu vyake. Alilia Tunda, asiamini
kuwa ndio ni kama anaanza tena maisha. Alipenda kwake. Alifurahia kila kitu
chake kwani alinunua si kwa bahati mbaya. Kila kitu alinunua kwa kusudi. Leo
anaviacha stoo! Mpaka lini! Hilo ndilo lilimuogopesha Tunda.
Net akarudi. “Nikusaidie nini?” Akasimama kwa haraka kama aliyefumaniwa tena. “Unaweza kuchukua mabegi hata mawili au matatu. Beba vile utakavyo. Tutalipia kwenye ndege.” Net akaongeza. “Asante.” Tunda akainama kuendelea kufungasha mpaka akamaliza na kujifuta machozi vizuri. “Naona hivi vitatosha. Asante.” “Basi acha nikusaidie kubeba. Wewe beba huo mkoba mdogo. Tuondoke sasa hivi, tuwahi.” Net akachukua yale mabegi wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
|
Walirudishwa uwanja wa ndege, na
Wanja tayari kwa safari ya kurudi jijini Arusha. Wakiwa kwenye ndege Tunda
akiwa amekaa dirishani, Net alimuona akivuta pumzi mara kadhaa na kuzishusha
huku akifuta machozi. Baadaye alimuona akijivuta karibu naye, akajiegemeza
pembeni yake, akalala. Net alimuhurumia sana Tunda. Alionekana amechoka, zaidi
mawazo. Akabaki akimtizama akiwa usingizini, akamfunika vizuri na mtandio wake,
akabaki akimtizama huku akimtafakari.
Walifika
Arusha, Net akachukua gari yake sehemu alipokuwa ameegesha asubuhi, akamrudisha
hotelini kwake. Wakaingia ndani, kama kawaida yake, alikaa kwenye kochi, kwa
mara ya kwanza Tunda akakaa pembeni yake, kama anayetaka kuzungumza kitu lakini
anasita. Net aliligundua hilo kwa hiyo hakutaka kuaga kwa haraka, akataka
kumsikiliza. Akaamua kuagiza chakula kiwafuate palepale chumbani.
Baada ya
muda kikaletwa. Net akiwa anaangalia luninga kama kawaida yake, huku
amejiegemeza kwenye kochi, akimsubiri aongee. Kimya. Alimuona vile
anavyotetemeka mpaka mikono iliyokuwa imeshikilia ile sahani ya chakula.
Mwishoe akamuona amekiweka mapajani, napo sahani ikawa inacheza. Kwamba
anatetemeka mpaka miguu. Net akaendelea kula na kubadili channels kama kumtoa
kwenye mawazo.
Walimaliza
kula bado Tunda alishindwa kuongea. Net naye akawa kama hana haraka. Akaendelea
kuangalia tu luninga. Akibadili hiki na kile. “Huwa unapenda kuangalia nini
kwenye tv?” Akamuuliza Tunda. Tunda akaanza kufikiria. Hakuwa hata akiangalia
tv. Ilikuwepo kwake kama haipo. “Sio mpenzi sana wa tv.” Akajibu taratibu. Net
akamwangalia. “Lakini huwa nawasha na kuangalia chochote kilichomo.” Akaendelea
Tunda kama anayejitetea.
“Na
movie?” Akamuuliza tena. “Napenda ila isiwe za vita au watu wasipigane.” Net akacheka.
Nia yake ilikuwa kumtuliza tu ili aongee. Wakatulia kidogo. “Net!” “Vipi?”
“Asante.” Net akatabasamu. Maana alishapokea hizo asante, kama nikuziweka
kwenye gunia, zingekuwa zikifurika. “Asante kwa kila kitu. Namaanisha kila
kitu. Angalau sasa hivi naweza kulala vizuri. Sidaiwi tena. Hiyo kodi ilikuwa
inanifanya sipati usingizi. Nilijiingiza kwenye gharama ambazo sikuwa najua
nitajitoaje.” “Pole.” Tunda akatulia kidogo.
Kisha
akaendelea. “Sitaki kurudia yale maisha tena Net. Hapa hotelini ni gharama sana
na kwa kuwa nitakuwa hapa Arusha kwa muda, labda nitafute chumba cha kupanga
kwa muda.” “Wazo zuri. Lakini naomba tufikirie kazi kwanza. Tuna mambo mengi
sana pale ofisini, hizi gharama za hapa hotelini unapoishi, ofisi italipa.” “Je
nikishindwa hiyo kazi Net? Huoni mtakuwa mmepoteza pesa bure? Kwa nini usione
kwanza utendaji kazi wangu, ukiridhika ndipo angalau utajua hata kama mnanilipa
kiasi gani?” “Acha wasiwasi Tunda! Kila kitu kitakuwa sawa.” Akajibu hivyo tu,
tena kirahisi tu. Akakaa tena kidogo, akamuaga kwa makubaliano yakumfuata hapo
kesho yake kwenda kazini.
Nafasi Nyingine Tena.
I |
lipofika saa mbili kamili, Net
alikuwa akigonga mlangoni. Hakuingia hata ndani. “Kama upo tayari, twende.” Tunda akachukua pochi yake kwa haraka na kutoka.
Walifika kazini siku hiyo ya jumatatu asubuhi, Net akapokea simu kutoka kwa
dada aliyekuwa amemuajiri pale ofisini na kumwambia anauguliwa na mumewe
hataweza kufika kazini mpaka atakapopona. Tunda aliingiwa na hofu sana.
“Usiogope, nitakuelekeza utaelewa tu. Hata yeye mwenyewe mimi ndiye niliyemfundisha.
Halafu mimi mwenyewe nitakuwepo, nitakusaidia.” Tunda akakubali lakini bado
alikuwa na hofu sana.
Na hivi
Net alionekana makini, hakurupuki! Ni kama hana mlango wa makosa kwenye maisha
yake, wasiwasi ulizidi kumwingia Tunda. Hata wateja aliokuwa akiwahudumia kwa
ngono, wote waliokuwa wakikutana na Net, au aliofumaniwa nao na Net, walianza
kutoa sifa za Net hata kabla hawajakutana naye. Hata Tunda alipokuwa akiwaambia
wamwambie Net wakutane club au baa, walikuwa wakisita na wengine kukataa
kabisa. Kwamba yupo makini, anakwenda na muda, muadilifu, hataki hata kugusa
pombe na kadhalika. Sasa leo umkutanishe na Tunda aliyekwisha kumfumania mara
kadhaa, na kila wanayekutana naye, ameshamuhudumia!
Hofu
iliyokuwa imemjaa Tunda, alitamani yeye ndio akakae na huyo mgonjwa, muhusika
arudi pale kazini. Lakini akajikumbusha hayupo kwenye kuchagua. Amewekwa
hotelini ili afanye kazi. Vitu vyake vipo kwenye stoo ya Net, juhudi zake ndio
zitakazomfanya avirudishe chini ya himaya yake. Hana pakwenda, hapo alipo ndipo
mwisho. Lazima atulize akili, aelewe.
Tunda
akatulia kuelewa kwa makini. Na Net naye alimuelekeza taratibu bila haraka,
kuhakikisha hapaniki na anaelewa ni nini wanafanya bila shida. Ilikuwa ni
Kampuni mpya ya usafirishaji. Walihusika na watalii pamoja na kusafirisha
bidhaa ndani na nje ya nchi. Net alimwambia ndio wanaanza tu. Kwa upande
wawatalii wao walikuwa ni wakala tu. Wanafanya kazi na mahoteli mengi makubwa
ya hapo nchini, walioingia nao ubia.
Wakipokea
wao wateja, watatumia usafiri wao kina Net. Lakini watalala kwenye hoteli zao.
Kisha hoteli kuwalipa wao asilimia fulani kwa kuwaletea watalii au wateja. Iwe
mbugani au mijini na vijijini. Kina Net wao ndio walitumika kama wasafirishaji.
Unahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, basi wanakuwa na malori makubwa na
madogo, inategemea na ukubwa wa nyumba au ofisi unayotaka kuhamisha. Unayo
bidhaa kubwa au ndogo, unataka usafirishe ndani ya nchi au nje, wao kina Net,
watakusafirishia.
Kampuni
yao ilikuwa ikiitwa African Cote transit. Jina
la Net alikuja kugundua kuwa ni Nathaniel Cote. Kwa hiyo akahisi labda ile
kampuni ni yake. Ila kama kawaida ya Tunda, haulizi kisichomuhusu, ila kufuata
yake. Akaweka akili na kuendelea kumsikiliza Net. Kazi yake ikawa kupokea kazi
zote kutoka kwa wateja. Kujua aina ya mzigo au watalii. Anaandika kwenye
kompyuta kutokana na aina. Kwa urahisi tu, kompyuta yenyewe inamletea aina ya
magari ambayo yapo.
Kama ni
wateja wa kuzungushwa mjini, basi itampasa kumsomea mteja aina ya magari ambayo yapo kwa wakati huo. Kama ni
mbugani hivyohivyo. Kama mtu anayehama kutoka sehemu moja kwenda nyingine,
Tunda alifundishwa aina ya maswali ya kuuliza. Ukumbwa wa vifaa vya hiyo nyumba
anayohamisha. Umbali, na kadhalika.
Kama ni
bidhaa, alimfundisha maswali yakuuliza pia. Ukubwa wa hiyo bidhaa, aina yake, umbali
wakupelekwa na kadhalika. Kwa hiyo kazi kubwa ilikuwa ni kuelewa vizuri wateja,
kuandika na kutoa lugha nzuri kwa kila mteja.
Hilo kwa
Tunda likawa halina shida. Kwanza hana tatizo kubwa la lugha. Angalau lugha
mbili muhimu alikuwa akizifahamu bila shida. Kingereza na Kiswahili. Pili,
Tunda alijaliwa ulimi laini. Mtulivu na anayo lugha ya ushawishi. Akizungumza
na wewe hata ukitaka kugairi, atakupanga mpaka ukubali.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kazi
ikaanza. Tunda na Net wakisaidiana bega kwa bega. Kwa kuwa ilikuwa siku ya
kwanza, Net alikuwepo kumsaidia. Walikuwa naye hapo mezani wakifanya pamoja.
Alimsikia Net jinsi anavozungumza na wateja. Maswali gani anayajibu. Akawa anaandika
yale maswali aliyoona wateja wengi wanauliza.
Tunda
alijua ni kweli wanatengeneza pesa. Walikuwa busy kupita kiasi mpaka ile hali
ya hofu kwa Net ikaanza kupungua kwa kuwa walikuwa wamekaa naye hapo mezani
siku nzima. Wakizungumza wao wawili, wateja na Tunda ilimlazimu kuuliza maswali
ili akija kuachiwa pale, asiharibu.
Hakuna
aliyekumbuka kula. Mpaka inafika jioni ya saa kumi na mbili, ndio pakatulia.
Simu zikaacha kupigwa. “Mambo yatabadilika Tunda. Utakuja kupata muda
wakupumzika. Mwanzo mgumu.” “Hamna shida kabisa. Nimefurahi kuweza kuwa busy
hivi. Imenisaidia sana.” Net akacheka kidogo.
“Hujuti
kukubali?” “Hata kidogo. Angalau akili yangu imetulia kwa muda nakuacha
kujifikiria. Lakini najua wewe njaa itakuwa ikikuuma.” “Na wewe?” “Mimi sio mlaji
sana. Umeona kile kichupa nilichokunywa mchana?” Net akakumbuka kumuona akinywa
kitu. “Ni meal replacement. Inachukua nafasi ya mlo mmoja. Imebeba virutubisho
vingi tu. Kwa hiyo wakati mwingine ni kinywa ile, nikapata na matunda, inakuwa
inanitosha.” Net akatabasamu. Maana kwa kumwangalia tu, utajua huo mwili
unatunzwa vizuri.
“Mbona
na mimi hukunipa sasa?” Tunda akababaika kidogo. Akataka kujitetea, Net
akimtizama. “Unisamehe tu. Sikujua kama ungependa. Nimebakiza vingine hotelini.
Nilikuja navyo kutoka Dar. Naweza kwenda kukupa.” “Nashukuru. Ila sasa hivi
njaa inaniuma sana. Nataka kula chakula chakueleweka. Twende tukale chakula
kabisa.” Wakaanza kufunga kazi kwa siku ile, na kutoka pale.
Walirudi
hotelini na kuagiza chakula. Kililetwa chumbani. Wakaanza kula. “Nikuulize
Net?” “Uliza tu.” Net akajibu huku wakila. “Nimeona ofisi ndio mpya. Lakini
mnao wateja wengi. Mnafanyaje?” Net akameza chakula kilichokuwepo mdomoni ili
aweze kuzungumza.
“Chakwanza,
kujitangaza. Nimejitahidi kutangaza na nimehakikisha watu wengi wametusikia na
kufahamu huduma yetu. Nilitangaza kwenye maredio, televisheni, na kugawa
vipeperushi kwa wingi. Mjini, mitaani na maofisini. Ukiangalia hapa nchini,
wengi wanatumia kupanga. Kama sio nyumba anayoishi, basi ofisi. Sasa ili kuwapata
hao watu, basi, nimeweka uwanja mkubwa kwa watumiaji wote. Wenye pesa na wasio
na pesa nyingi wanaweza kutumia huduma zetu. Ndio maana utakuta kuna aina
tofauti tofauti za magari. Hiyo inategemeana na uwezo wa mtu. Sijui nimejibu?”
Net akauliza.
“Hapo nimeelewa.”
“Lakini umeonaje? Si ni kazi inayowezekana?” “Nafikiri. Si bado tutakuwa wote
ili kuhakikisha siharibu?” Net akacheka. “Tunda wewe ni muoga sana. Acha
kufikiria kuharibu kwanza. Naomba ufikirie ni jinsi gani utaboresha. Ni vipi
pale patanufaika kwa Tunda tu kuwepo pale. Tunda huyohuyo unayemfahamu wewe,
mfikirie ni kwa jinsi gani pale pamebahatika kupata uwepo wako. Ukifikiria kwa
namna hiyo, utaona mambo yatakavyokuwa rahisi.” Tunda akatoa tabasamu kama
anayefikiria.
“Niamini
Tunda, kila mtu anahaiba yake na kitu kinachomfanya awe yeye. Wewe unajijua.
Sasa jifikirie hivyo ulivyo unawezaje kupanufaisha pale! Jiweke kwenye nafasi
ya kama ile kampuni ndiyo imebahatika kumpata Tunda. Jiambie kwanza hivyo.
Hivyo tu. Weka mbali maswala yakukaa darasani na elimu. Wewe tu kama ulivyo.
Jiambie kampuni ya Cote, imebahatika kumpata Tunda. Sasa utainufaisha vipi!
Utaona jinsi itakavyokusaidia kukubadilisha mtazamo wako. Kwanza hofu
itaondoka, na utashangaa utapata ujasiri wa umiliki.” Tunda akacheka kidogo.
“Kesho
tutaanza kwa kukupa nafasi upokee simu.” Tunda akastuka. “Net!” “Si umenisikia
leo jinsi nilivyokuwa nikipokea simu?” Tunda akakubali. “Basi fanya hivyohivyo
na usiogope kuuliza mteja maswali kuhakikisha unamuelewa. Ukiona anaomba huduma
ngumu kwako, au humuelewi, mwambie ili kumuhudumia vizuri, unamuunganisha na
mtu atakayeweza kumsaidia vizuri zaidi. Basi, niunganishe naye kwenye simu
yangu. Ila kwa kesho, pia tutakuwa wote. Usiogope.” Tunda akacheka kwa hofu.
“Sawa.
Nitajitahidi Net.” “Hayo ndio maneno. Na ninakuhakikishia utaweza tu. Sio ngumu
kabisa. Kwanza ile kompyuta ipo pale kukusaidia kukupa kila jibu. Si umeona?”
“Nilikuona jinsi unavyofanya.” “Sawa sawa.” Wakazungumza kidogo, Net akaondoka.
Siku ya Pili, Tunda kazini.
Tunda alitegesha alamu ili
imuamshe mapema kidogo. Akaoga na kujitayarisha. Kwa kuwa alirudi na baadhi ya
vitu vyake kutoka Dar, Tunda alijitengeneza kawaida, kiofisi kama vile
alivyokuwa akiwatengeneza kina Fina mwilini mwake anapokwenda kulaghai wanaume.
Alivaa vizuri. Kiofisi. Kama msomi mwenye majukumu mazito. Ila kiheshima kwa
kuwa alikuwa na Net.
Akaagiza
kifungua kinywa. Chake akala. Cha Net, akaomba wamfungie maalumu kwa ajili ya
kula ofisini. Alimuona akinywa kahawa, na walikuwa na microwave ofisini. Akaomba
waweke kila kitu tayari na kuwaambia atapitia hapo mgahawani.
Net
alifika hapo. Hakupanda juu kwenye chumba cha Tunda. Akampigia simu kuwa
ashuke. Kwa haraka bila kuchelewa, akapitia mgahawani akachukua kifungua kinywa
cha Net, akatoka nje. Alitoka kwenye mlango wa hoteli, Net akiwa kwenye gari
akimtizama. Hakika Tunda alikuwa amependeza. Kigauni chakuchanua chini kama
mwamvuli, juu kilimshika na kilikuwa kata mikono. Kilimfika chini kidogo tu ya
magoti. Kiatu cha kufunika, cha juu. Hereni ndefu bila cheni shingoni ila
hakuacha kuvaa ile ya mguuni na mkononi.
Pochi inayoendana na kiatu alibeba mkono wa kushoto, mkono wa kulia chakula cha
Net.
“Waw!” Akajisemea Net mwenyewe wakati akimwangalia
akimsogelea. Mwishoe akaamua kwenda kumpokea. “Hii ni kwa ajili yako.” Tunda
aliwahi wakati Net amemsogelea na yeye akawa ameshafika karibu ya gari.
“Asante. Sasa mbona ya kwako sioni?” “Uliniambia leo ni zamu yangu kupokea
simu. Sasa wakati mimi nazungumza na wateja, wewe unakula.” Net akacheka.
“Naona mudi wa kazi ameanza kukuingia.” Wakacheka. Net alikuwa ameshapokea kile
chakula. Akamfungulia mlango, Tunda akapanda. Na yeye akaingia garini nakuanza
kunywa kahawa yake. Kimya mpaka kazini.
Walipoingia tu, simu zikaanza. Net akakimbilia na
kupokea. Tunda akaanza kuwasha kompyuta akijua wazi Net atahitaji. “Naomba nikupe mtu ambaye atakusaidia.” Tunda
akashtuka na kumgeukia Net. Net akamkabidhi simu. Tunda akavuta pumzi. “Halow!” Tunda akaipokea. Net akavuta kiti nakuanza
kula pale pale kwenye meza bila hata kumtizama Tunda.
Mteja alikuwa akisafirisha mzigo kutoka Arusha
mpaka Moshi. “Ni mzigo wa aina gani na unaukubwa gani?”
Alimsikia Tunda akiuliza taratibu tu. Akamuona anaandika huku akisikiliza kwa
makini tu. “Kwa aina hiyo ya mzigo, tunaweza kusafirisha.
Lakini naomba nishauri.” Mpaka Net mwenyewe ikabidi atulie asikilize huo
ushauri. “Asante.” Akamsikia Tunda akishukuru na
cheko kidogo. Akahisi amesifiwa huko kwenye simu. Sauti ya Tunda ni kweli
ilikuwa nzuri.
“Nimesikia aina ya gari unayotaka. Na
ukisisitiza unakwepa garama. Lakini naona mzigo wako unathamani kubwa.
Isingekuwa vizuri kwanza tukufikishie pale ukiwa haupo kwenye hali nzuri. Lengo
letu kama kampuni sio kukusafirishia tu. Tungependa kuhakikisha tunafikisha mzigo
wako ukiwa salama pia.” Net mwenyewe
akashangaa. Tunda akaendelea kusikiliza, akamuona anacheka.
“Hapana. Nitakupa kwa bei nzuri tu.
Naomba nipe kama dakika moja au mbili, nikutajie aina ya magari yatakayofaa kwa
bidhaa yako.” Tunda akabonyeza spika, akaweka
simu chini, akaanza kuperuzi kwenye kompyuta. Net kimya. “Lakini hujanitajia jina lako.” Wakamsikia yule mteja.
Tunda akaanza kuogopa. “Mrembo? Maana nataka kila
nikipiga, niwe nasikia hiyo sauti nzuri. Au siruhusiwi?” Tunda na Net
wote walikuwa wakisikiliza.
Tunda
akanyanyua simu. “Naitwa Tunda na nimepata aina mbili
ya magari ambayo nafikiri yatafaa kwa mzigo wako.” Tunda hakutaka
kuendeleza maongezi juu yake. Akamtajia hayo magari na bei yake. Akampa nafasi
achague. Akachagua moja na kutaka namba ya simu ya Tunda. “Naomba utumie hii ya ofisi kwa kikazi.” Net akajua
anatongozwa na ameombwa namba yake binfsi ya simu. Yule mteja akaendelea
kuongea, Net akamuona Tunda anakosa raha, akamuomba yeye hiyo simu.
Tunda
akamkabidhi Net simu. “Malipo ni kama alivyokwisha
kukwambia. Tutajitahidi kufika sehemu ya kuchukua mzigo kwa wakati na wewe
tunaomba uwataarifu kuwa dereva wa kampuni ya Cote, atafika hapo akiwa na
kitambulisho chetu. Asante.” Net alizungumza hivyo tu, na kukata simu.
Tunda akasimama na kutaka kuondoka.
“Njoo
kwanza Tunda.” Tunda akarudi. “Nisikilize. Kwanza umefanya vizuri sana. Hata
mimi sikutegemea.” Tunda akatabasamu na kufuta machozi. “Kweli kabisa. Na
ninataka uelewe hivi, kazi kubwa hapa au utakayofanya ni kuhudumia wateja wa
aina tofauti tofauti. Usiogope kwangu au kwao. Fanya kazi vizuri, wakifika
kwenye mambo yao binafsi, wajibu vile unavyotaka wewe. Usiogope. Sijui kama
unanielewa?” Tunda akavuta pumzi.
“Lazima
ufikie hatua uweze kutofautisha kazi na mambo binafsi. Na ile kauli ya ‘sina
uwezo wa kuchagua’, ufike mahali ijifute. Wewe ndio ubakiwe kiongozi wa
maisha yako. Yaani wewe ndio unajukumu lakuongeza nafasi kwenye maisha yako.
Uchague chakufanya ukiwa unafikiria ili kuepuka majuto ya baadaye. Sijui kama
umenielewa?” “Nimeelewa.” “Haya. Tuendelee na kazi.” Tunda akacheka na kurudi
kukaa.
Kufika
mchana, hofu ikawa imemuisha kabisa Tunda. Anapokea simu kwa ujasiri wote. Net
alishangaa vile Tunda anavyozungumza kingereza kizuri. Akahisi Tunda
alimdanganya. Alimwambia hajasoma. Na ni mtanzania! “Kingereza amekijulia wapi?” Akajiuliza Net kwa kadiri alivyokuwa
akimsikiliza akikizungumza na wateja kwa ufasaha bila hofu na ujasiri usoni.
Hakuna
aliyekumbuka chakula cha mchana. Kukawa busy mpaka jioni tena kama jana yake,
ila siku hiyo walikaa hapo mpaka usiku wa saa moja. “Naona utajuta.” “Kwa
nini?” “Si hivi unavyotumia muda mwingi hapa ofisini!” “Kwanza ndio nafurahia.
Kwa mara ya kwanza maishani naona nafanya kitu cha kueleweka na mtu
anakifurahia. Nashukuru kwa hii nafasi Net.” Tunda aliongea kwa upole. “Karibu.
Na ninaona umeshakuwa mtaalamu.” Tunda akacheka taratibu wakati wanatoka.
“Ni
hivyo hivyo tu, tena naona na umejaliwa lugha ya ushawishi. Hiyo pia
itakusaidia zaidi.” Tunda akatabasamu. Walikuwa kwenye gari. “Hata nikiwa mbali
na pale. Ukipata mteja ambaye unataka nizungumze naye, kama nilivyokufundisha
jinsi ya kuunganisha. Kwa simu ya mezani na ya mkononi. Rahisi tu. Niunganishe
na yule unayetaka nizungumze naye.” “Sawa.” Tunda akaitika `.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Tunda na
Net wakaendelea kufanya kazi kwa bidii zote. Wakisaidiana bega kwa bega. Wateja
wao wengi walikuwa wafanyabiashara wakubwa hapo nchini na watalii.
Walisafirisha bidhaa kubwa na za thamani huku wakipokea watalii nje na ndani ya
nchi. Walikuwa wakipokea watalii kutoka nchi mbali mbali. Net alijitangaza
kwenye website iliyokuwa ikivutia watalii kutoka nchi mbali mbali.
Tunda alimshangaa
uwezo wake wakuzungumza lugha. Alikuwa akiongea lugha tano tena kifasaha. Kama
sio kingereza au Kiswahili, Tunda alimuhamishia simu Net popote alipo azungumze
na aina hiyo ya wateja. Na Net aliacha kusafiri. Akawepo Arusha kwa muda huo
aliokuwa na Tunda hapo. Kwa hiyo, hiyo miezi ya mwanzoni ikawa rahisi kwa
Tunda.
Wafanyabiashara
wengine waliomsikia Tunda kwenye simu walipatwa tamaa. Baada yakushindwa kupata
namba zake za simu, walikuwa wakiamua kufika kabisa hapo ofisini, ilimradi tu
kumuona nakujaribu kumtongoza. Tunda akashangaa sana. “Kipindi nilipokuwa na shida
nao, wote walijificha, sasa hivi ndio wanajitokeza!” Tunda
akajiuliza. Net alikuwa akimtizama kwa karibu na alijua nia ya wengi wao.
Kila
walipofika pale, Tunda alipowasukumia kwa Net, bado walitaka kuzungumza naye
Tunda zaidi. Ghafla yeye akawa wamuhimu kuliko mwenye kampuni! Tunda akajua ni
janja yakumpata tu . Akawa
akiwakwepa kiustarabu lakini akimaanisha kabisa. Alishatendwa na kuwatumikia
hao wanaume, hakuwa na hamu tena. Alikinahiwa na swala la mapenzi, Gabriel
akawa amegongelea msumari wa mwisho.
Hakuwa
akijua kama anaweza kufanya kazi kama wasomi wengine kwenye ofisi kama ile.
Tena alifanya vizuri sana, mpaka mama yake Net aliyekuwa akizungumza naye
kwenye simu alikuwa akimfurahia sana. Tunda alifanya kazi kwa bidii sana bila
kuchoka wala kulalamika na Net alimwambia atamlipa. Akajiambia hana sababu
yakuuza mwili wake tena. Kwa mara ya kwanza akawa amepata nafasi ya kuchagua
nini afanye kwenye maisha yake. Kuuza mwili au kufanya kazi ili kujipatia
kipato. Sasa kwa kuwa wanaume walishamtenda na kutumia huo mwili vibaya, kwenye
swala la biashara ya ngono, akaona aweke kikomo. Hakuna aliyemkubalia.
Hakuwa
na jumamosi wala jumapili, pale alipokuwa na mambo yake yakufanya ofisini,
hakuangalia muda hata kidogo. Aliongeza juhudi kazini. Hakujiangalia yeye tena.
Akataka kumfurahisha Net na kulipa fadhila. Tunda alijua pesa inayomtoka Net
kwa kuwekwa pale hotelini. Sasa ili kulipa fadhila, ni kuweka juhudi. Net
mwenyewe alikuwa mchapa kazi. Wakaendelea kuchapa kazi kwa pamoja
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
moja ilikuwa jumamosi. Walifanya kazi hiyo week, kuanzia asubuhi mpaka usiku.
Jumatatu mpaka siku hiyo jumamosi usiku. Net akamwambia Tunda wanastahili
kwenda kula chakula kizuri sehemu kama kujipongeza. Tunda akacheka akijua wazi
amefurahia. Waliingiza pesa hiyo week. Kuanzia dola mpaka pesa ya madafu.
“Unahamu
ya kula nini?” Akamuuliza Tunda. “Mimi ikishafika usiku kama hivi,
nilishakwambia, siwezi kula kitu kigumu. Sitaweza kulala.” Tunda akajibu na
kumalizia kufunga kompyuta aliyokuwa akitumia.
“Lazima
tujipongeze.” Tunda akacheka. Siku za jumapili ilikuwa wakionana jioni. Tena
kwa muda mfupi. Net alikuwa akimpitia hapo hotelini kama kumsalimia tu. Wakati
mwingine alikaa kidogo, wakati mwingine aliondoka. Tunda hakujua anaishi wapi.
Kama ameoa au la. Anaye mwanamke hapo Arusha au la. Katika watu aliowaogopa
hapa duniani ni Net. Alimuogopa huyo kaka kupita kiasi. Mbali na mambo ya kazi,
hakuwa na ujasiri wakumuuliza chochote.
“Nishushe
mimi hotelini. Wewe nenda tu Net.” “Hapana bwana. Hii ni tunajipongeza
wafanyakazi wa Cote. Wewe vipi Tunda?” Tunda akacheka. “Twende basi ukale hata
matunda wakati mimi nakula nyama choma. Njaa inaniuma.” Wakakubaliana.
Walitafuta
hoteli nzuri. Ni kweli Net hakupenda sana kwenda baa, labda awe anakutana na
rafiki zake au mambo ya biashara, ndipo itamlazimu kwenda. Waliingia sehemu ya
chakula. Tunda akaagiza maji na fruits salad. Akiwa hana hata habari kama
atamwingiza Net matatizoni siku hiyo. Alikuwa amependeza japo alikuwa ameshinda
kazini siku nzima tena siku ya jumamosi.
Aibu ya Mwaka kwa Tunda Mbele ya Net.
Net
aliagiza chakula chake na juisi ya embe. Hiyo hoteli juu ilikuwa na vyumba na
kumbi ya mkutano. Hali ya Tunda ikabadilika ghafla hata kabla chakula
hakijaletwa, Net asielewe ni kwa nini. Meza ya pembeni, mbele kidogo, akaona
wamekaa wanaume wakila na kunywa huku wakiongea na kucheka. Watatu wa hao
waliokuwa wamekaa hapo kwenye hiyo meza, Tunda alishawahudumia. Tena wakiwa
kwenye baa.
Wote
waliokuwa wamekaa pale walikuwa marafiki, walikuja mjini Arusha kwenye mkutano.
Na wote walikuwa wakifanya kazi ofisi moja. Kwenye NGO ya kigeni. Vijana wenye
pesa na wasomi tu. Sasa watatu wao pale ndio hao Tunda alishawahudumia zaidi ya
mara moja. Mmoja alimpata kwa kuiba namba ya simu kwenye simu ya mteja
mwingine.
Wawili
aliwatongoza baada ya kukutana nao baa. Akafanya ule mtindo wake wakumchomoa
mmoja baada ya mwingine. Siku ya kwanza akampata mmoja wao wakiwa wamekaa wote
mezani wakinywa. Akatoka naye nje, akamalizana naye kwenye gari. Akamuomba
namba yake Tunda. Wakaja kukutana tena kwenye nyumba za kulala wageni. Akampa
kwa mapana na urefu. Wakati akiwa anaoga aondoke pale hotelini, kabla Tunda
hajamfuata huko bafuni, akaiba ya watatu. Kwa kuwa aligundua hao wawili
walikuwa karibu akajua lazima atakuwa na namba yake ya simu. Na kweli
akafanikiwa.
Siku
inayofuata, akampigia simu huyo wa tatu, akijidai anamuulizia yule wa kwanza
kabisa ambaye alienda naye baa ndipo akakutana nao wote. Akamzungusha kwa
maneno mazuri kwenye simu, mpaka akajikuta na
yeye anaomba penzi. Tunda akajidai kumkatalia kwa kumwambia wenzake
watajua kwani alishaonekana na wote akiwa na yule rafiki yao. Akambembeleza
akimwambia yeye ni mtu mzima, sio mropokaji. Basi, akachukua chumba mahali,
Tunda akaenda kumpa kwa mapana na marefu. Na yeye huyu wa tatu akajua kuwa
anamuibia rafiki yake. Ikawa siri yao wawili, ila nafuu zaidi kwa Tunda
anayewazunguka wote. Marafiki hao watatu wasijue wanapewa uroda na mwanamke
mmoja.
Siku
ingine aligonganisha magari wakiwa baa. Alijikuta na wote watatu meza moja,
akiwa ameenda na yule yule wa kwanza, yule wa pili aliyemsaidia kumpata wa tatu
akapewa penzi kwenye gari mpaka akatafuta chumba, akamtumia ujumbe wakiwa pale
pale mezani kuwa watoke nje. Tunda alipopata ujumbe akiwa anacheza game yake
pale kwenye meza ya wale marafiki walevi, akarudisha ujumbe akamwambia anatoka,
ila asubiri baada ya dakika mbili kamili ndipo amfuate.
Basi wakafanya hivyo. Alipotoka
tu, yule watatu naye akatuma ujumbe kuwa anamuhitaji. Akiwa anamsubiria yule wa
pili, ndani ya zile dakika mbili akachat na watatu. ‘Ushawahi
kuonja vya garini?’ Akamtumia ule ujumbe. Watatu akajibu kwa haraka. ‘Hapana mama. Ila nipo tayari kujifunza.’ ‘Basi nisubiri.
Nikija kuomba funguo za gari hapo mezani. Unifuate baada ya dakika tatu tu.’
‘Asante mama.’ Usiku huo akawapa dozi marafiki wote watatu bila wao
kujijua.
Kwani
alipomalizana na wa pili, akamwambia arudi ndani haraka na asiseme kitu. Baada
ya muda, akarudi na kumwambia yule wa kwanza tumbo limejaa gesi. Anaomba funguo
za gari yake aende akatafute dawa za gesi kwenye duka la madawa. Katikati ya
pombe na vile anavyohudumiwa na Tunda, akatoa funguo za gari. Tunda akatoka,
yule rafiki wa tatu akafuata nyuma. Alichofanya Tunda nikuhamisha upande
lililokuwepo hilo gari. Akaenda kulificha mbali kidogo, hapo hapo baa. Dakika
tano zikawa nyingi. Akamalizana na rafiki watatu. Akamshukuru sana na kufurahia
ule wepesi. Akampa mahela, akamwambia arudi ndani kwa haraka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sasa
wote watatu wakawa wanajua uwezo wa Tunda wa mapenzi, na wale wawili
walishapewa penzi la garini tena kwa muda mfupi sana na wote wakijua wanamwibia
mwenzao. Na hawakuwahi kukamatwa hata mara moja. Yule mwizi wa halali, wa
kwanza akawa amemuona Tunda pale kwenye meza. Akaamua kwenda kumsalimia Tunda
pale pale mezani alipokuwa amekaa na Net.
“Habari
Lina?” Akanyoosha mkono kwa Tunda. Net akamgeukia yule kijana na kumtizama
Tunda. Tunda akakwepa ule mkono kwa kunyanyua glasi ya maji. “Nzuri tu.” Akajibu
Tunda na kunywa maji. “Nikuombe msamaha. Majuzi ulipokuwa ukinitafuta, nilikuwa
nimebanwa kweli ndio maana nikashindwa kabisa kupokea simu yako.” Yule kijana
alijieleza kwa Tunda. “Hamna neno. Nilielewa.” Akajibu Tunda taratibu, Net
akisikiliza.
“Vipi,
umehamia Arusha nini?” Akamuuliza Tunda. “Nipo kikazi. Huyu ni bosi wangu.”
“Oooh! Nimefurahi kukufahamu Kiongozi.” Akampa mkono Net, yeye Net akaupokea
mkono na kujibu salamu. “Nipo hapa Arusha na wenzangu. Tumekuja kikazi. Nipo
gorofa hii ya pili tu. Hapa hapa hotelini. Nakukaribisha.” Akamgeukia Tunda.
“Asante, lakini hapana. Nipo busy na kazi.” Tunda alimjibu kwa msisitizo tena
akimtizama machoni.
“Kesho ni jumapili Lina. Najua hufanyi kazi.
Na mimi kuanzia asubuhi nitakuwepo tu hapa hotelini. Kwa nini usije? Sitakuweka
sana.” Tunda alitamani kama aondoke lakini ikamlazimu kujibu tu. “Nina mipango
mingine. Tafadhali naomba uondoke ili nile. Unanisimamia hapa, tunashindwa
kula. Nimeshakwambia hapana, inatosha.” Chakula kilikuwa kimeshaletwa.
“Au umekasirika
sababu sikupokea simu yako?” Akaendelea kusisitiza. Mpaka Net akaweka kisu na
uma chini. “Hapana sijakasirika ila sitaki kuonana na wewe tena. Naomba
utupishe.” “Daah! Sawa Lina. Lakini…” Tunda akavuta kiti kwa nguvu na kusimama.
Akamtizama machoni. “Samahani Lina, sikutaka kuwakwanza.” Tunda akaondoka
kuelekea chooni, yule kijana naye akaondoka. Harufu ya pombe ndiyo ilikuwa
ikitoka mdomoni kwake na kuenea pale kwenye meza ya Net na Tunda.
Wakati
anarudi, ndio anatoka choo cha kike anaingia pale mgahawani alipomuacha Net,
akakumbana na wale wengine wawili. “Samahani Lina, tunaweza kuzungumza kidogo
hapo nje?” Mmoja wao akaanza na yule mwingine akabaki ameduaa. Kumbe wote
waliaga pale mezani kwa rafiki zao kuwa wanakwenda msalani, kumbe walikuwa wakimfuata
Tunda. Mmoja akawa amewahi.
Kabla
Tunda hajajibu, mwenzie akadakia. “Mimi ndio nataka kuzungumza naye mara moja
hapo nje. Hatutachukua muda mrefu, si ndio Lina?” Watatu akadakia, akijua Lina
mwenyewe anaelewa. Huwa wanamalizana kwa muda mfupi sana, asijue na rafiki yake
naye anachomtakia huyo Lina sio mazungumzo. Ni huduma kama anayoitaka yeye.
Wakiwa
wote wamelewa, wakaanza kubishana. “Mimi sitachukua naye muda mrefu. Dakika
tano tu.” “Aliyekwambia mimi ninamchukua kwa muda mrefu ni nani? Natoka naye
mara moja tu, tunarudi.” Wakajibishana wale marafiki wawili, mmoja akiwa
amemshika mkono Tunda. Tunda alitamani kukimbia lakini akajikuta wote
wamemshika mkono. Mmoja huku mwingine kule. Ndipo ulipozuka ugomvi, wote
wakimng’angania huyo Lina, hakuna anayetaka asubiri kwanza.
“Nakwambia
mimi ni mara moja tu! Mbona unafanya mambo ya kitoto, Zimbe?” “Wewe ndio
nakuona huelewi. Nimekwambia hata mimi sitamkawisha. Anarudi sasa hivi.” Watu
wote mle ndani macho ya kawa kwao wote watatu. Tunda anatetemeka, anataka
kubebwa juu juu ili watoke naye pale ndani. Uzuri wakaanza kurushiana wao
ngumi, na kumuachia Tunda. Hakujua Net alipotokea, akamsogelea pale akiwa
ameshika funguo za gari na pochi yake. Akamshika mkono kwa nguvu, akamvuta
kumtoa pale.
Waliingia
kwenye gari, Net akaondoa gari kwa haraka Tunda akitetemeka kama aliyetoka
kwenye friza. Hata asante alishindwa kusema kwa aibu. Alipofika hotelini,
alichukua pochi yake na kushuka kwa haraka kama anayekimbia. Net akaona amuache
tu usiku huo. Hata yeye hakumfuta nyuma. Akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kuanzia
siku hiyo Tunda alijiapia kutotembelea tena sehemu za starehe au kwenye mabaa.
Na kwa kuwa Net alikuwa mstaarabu, hakuwahi kumuuliza tena juu ya ule mkasa.
Ila alimuona ile hofu ya mwanzoni kabisa imerudi vile vile. Tunda aliacha hata
kumuangalia machoni. Mara nyingi ilipomlazimu kumuongelesha alimuongelesha
akiwa anaangalia pembeni. Kama yupo ofisini basi macho kwenye kompyuta au
mafaili. Labda Net afanye juhudi za makusudi kumwita jina lake. Hapo atageuka
na kukwepesha macho kwa haraka. Alikosa ujasiri kabisa, akapooza hata tabasamu
likamwisha.
Wakajikuta
muda mwingi wanakuwa pamoja ofisini, wakitoka hapo, anamrudisha hotelini. Week
ya tatu Net alipata kijana wa usafi. Akamwambia Tunda atakuwa akifika hapo
kusafisha na kutoka mchana. Na huyo ndio mara nyingi Net alianza kumtuma kwenda
kuwanunulia chakula na kuwaletea hapo ofisini au wanapitia sehemu. Net anaingia
ndani. Ananunua chakula, wanaenda kula hotelini huku Net akiangalia taarifa ya
habari. Aliondoka muda alioona Tunda anataka kulala. Hakuna maongezi. Kimya
kimya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Karibu
ya mwezi kuisha tangia aanze kazi, Net alimwambia inamlazimu kwenda Dar kwenye
ofisi nyingine ambapo yupo mama yake. “Kuna mambo kadhaa yakuweka sawa.
Ungependa tuongozane?” Akamuuliza Tunda. “Hapana. Wewe nenda tu. Niache mimi
hapa. Nikikwama nitakujulisha.” “Hutaki kuona ofisi ya Dar?” “Halafu hapa
tufunge!?” Tunda akauliza kwa mshangao kidogo.
“Hapana.
Si unajua hiyo kazi unaweza kufanya popote tu?” Akamuuliza na kumuelekeza kuwa
nikupokea simu ambazo wanaweza kuzihamishia hata kwenye simu ya Net au yake. Na
kompyuta wanaweza kutumia laptop tu ambayo wanaweza kwenda nayo popote. Tunda
akaelewa ila akanyamaza. “Hatutakaa muda mrefu.” “Kama sio lazima, naomba
uniache hapa Net. Tafadhali.” Tunda akaongea kwa upole.
“Sio
lazima Tunda. Ila sikutaka ubakie hapa peke yako kazi zikakulemea.” “Nitakuwa
sawa. Nikishindwa jambo, nitakutafuta unisaidie. Ila nakuahidi kila kitu
kitakuwa sawa.” Akasisitiza, Net akamwangalia. “Samahani lakini. Naomba
usifikiri nakukaidi au nakataa kazi. Ndio maana nimeuliza kama kunakitu
chakikazi natakiwa kufanya mimi huko. Uliponiambia hapana, ndio maana nimeomba
nibaki tu.” Tunda aliongea kwa utaratibu na kujihami.
“Sasa
hivi natamani maisha haya niliyonayo Net. Napenda hivi ninavyoweza kukufanyia
kazi. Au kujiona nafanya kitu chamaana. Acha akili zangu zitulie kazini kwa
muda. Nimepoteza muda mwingi sana kwenye lile jiji. Mbaya zaidi nimepoteza ‘kwangu’!
Inaniuma sana kujiona nimegeuka kuwa mgeni kwenye nchi yangu mimi mwenyewe!
Nyumbani kwangu ndio ilikuwa kimbilio langu. Nikishahangaika huko, nilikuwa
nikijifariji ninalo kimbilio. Sasa hivi sina. Hii kazi ndio imegeuka kuwa
kimbilio. Nikiamka asubuhi, najiambia ninakitu chakufanya. Inanipunguzia
mawazo. Kuja kurudi Dar kama mgeni, nikijua sio kwangu tena, itaniumiza zaidi.
Ndio maana nakuomba kama sio lazima, kwa sasa naomba nibaki tu hapa.”
“Nimeelewa.
Hamna shida. Tutawasiliana basi. Ukikwama usisite kunipigia. Na bado zile simu
unazotaka mimi nijibu, endelea kuwahamishia kwangu.” “Asante Net. Ungependa
nikusindikize uwanja wa ndege?” Tunda akauliza kwa upole akionyesha kujali.
“Ningeshukuru. Tena itakuwa vizuri nikuachie gari. Nitaondoka na ndege ya
mchana. Utanipeleka na wakati wakurudi ningeomba uje kunipokea.” “Sawa. Lakini
naomba usinielewe vibaya.” Bembeleza hiyo ya Tunda. Net mwenyewe alikuwa
akilainika.
“Nimeelewa
kabisa. Usiwe na wasiwasi.” Wakatulia kidogo. “Basi nitakuona kesho. Nitakuja
kukuchukua asubuhi twende kazini, mchana ndio utanisindikiza.” “Sawa. Usiku mwema.”
“Na wewe.” Net akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net na
Tunda walifika uwanja wa ndege, wakabaki kwenye gari upande wa kuegeshea
magari. Hawakushuka. Kila mtu kimya kwa muda. Net macho kwenye simu yake, Tunda
ametulia tu pale kwenye kiti kama hayupo garini. Hana simu mkononi. Ametulia
kimya.
Baada ya
muda akaita. “Net!” Akaita kwa upole. Net akamgeukia. “Unarudi lini?”
“Nitajitahidi nisikae sana. Kuna kitu ulitaka kuniagiza? Hata kwenye vitu
vyako. Nitakwenda kule Salasala kumuona Max.” “Max ni nani?” Ikabidi kwa mara
ya kwanza Tunda kuuliza kitu mbali na kazi.
“Kumbe
siku ile sikukuonyesha?” Tunda akatingisha kichwa kukataa. “Ni mbwa. Nilimnunua
na akapatiwa mafunzo ya kiulinzi. Mzuri sana. Ananisaidia sana pale kwa ajili
ya ulinzi. Yeye tu na Emma wanatosha.” Tunda akatabasamu. Net akacheka. “Ni
mzuri sana. Nampenda.” “Mimi muoga wa mbwa.” “Max utampenda. Tutakuja kwenda
wote siku moja, nikutambulishe. Kwa sasa ananijua mimi, Emma na daktari wake.
Ni mkali au hatari kama akijua sio mtu salama.” Tunda akacheka na kutulia.
Wakatulia
hapo kwa muda. Net alianza kuona uzito wa ile safari. Walishakuwa kwa karibu
sana na Tunda karibia mwezi sasa. Kula na kuwa pamoja kila siku, tena kwa
ukaribu! Tunda anautulivu fulani hivi, huchoki kuwa naye. Akaona uzito
kumuacha. Akamwangalia, akamuona amegeukia dirishani kama anayewaza. Na yeye
akatulia tu akimwangalia na kupotelea mawazoni.
Tunda
akageuka, akamuona amejiegemeza kwenye kiti chake akimwangalia. “Huna haja
yakunisindikiza mpaka kule.” Ikabidi amuwahi. “Sawa.” Tunda akakubali. “Kama
hutataka lakini.” Akajihami Tunda asijefikiri anamkwepa. “Hamna neno.” Akajibu
taratibu. “Au ungependa kufika mpaka kule ninapoingia kupanda ndege?”
Akababaika tena kwani aliongea bila kufikiria baada ya Tunda kugeuka na kugundua
anamwangalia. Akapaniki. “Ni sawa tu. Wakati wakuja kukupokea pia nikusubirie
hapa hapa?” Tunda akauliza taratibu bila kuonyesha tatizo lolote.
“Utakavyopenda. Ila tutawasiliana.” “Sawa. Uwe na safari njema.” “Asante na
wewe ubaki salama. Unipigie ukikwama.” “Naamini kila kitu kitaenda sawa.” Tunda
akajibu.
“Inamaana hatutawasiliana mpaka nirudi?”
Akajiuliza Net. Akaona amejifunga kwa maneno yake mwenyewe. “Unarudi hotelini
au kazini?” “Sasa hivi nimapema sana. Acha nirudi ofisini tu. Nifanye fanye
kazi upaka usiku, ndio nirudi kulala.” “Basi nikifika tu nitakujulisha.”
Akachomekea Net na kujishtukia. “Na kujua umefikia wapi huko kazini.” “Sawa.”
Tunda akajibu. Net akaona asije kuongea mengi na kuharibu zaidi, akashuka
garini japo muda haukuwa umefika. Tunda akarudi kazini akitumia hiyo gari ya
Net.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net
alitua jijini Dar, akili zikiwa Arusha. Mama Cote alikuwepo uwanja wa ndege
kumpokea mwanae. Hawakuwa wameonana karibia mwezi. Kila weekend alipokuwa
akimpigia simu nakumtaka arudi nyumbani, Net alisema yupo busy labda weekend
ijayo. Siku zikazidi kwenda akahisi lipo jambo tu huko Arusha. Net sio mtu wa
kung’angania Arusha na kushindwa kumuona mama yake zaidi ya majuma matatu tena
akiwa hapo hapo nchini! Akajua lipo jambo kwa kijana wake. Na kwa kuwa
alishazungumza na Tunda kwenye simu, akamsikia sauti yake, vile anavyoongea,
akajua huyo Tunda pengine ndiye anayembakisha huko Arusha.
“Vipi
Tunda?” Mama yake akauliza kiuchokozi tu na Net akajua. “Naona anaendelea
vizuri. Kazi nyingi ameshazijua. Wateja wengi amewamudu.” “Lazima. Ana lugha
nzuri. Namaanisha sauti.” Net akacheka. “Umeanza mama Cote.” “Jamani!” Wote wakacheka. “Sasa kwa nini hukuja naye?”
“Si yupo kazini mama jamani!” “Sawa, namaanisha weekend zile nyingine?
Mkaribishe nyumbani. Hizo kazi mnaweza kufanyia hata huku Dar kama ulivyokuwa
ukifanya.” Net akatingisha kichwa. “Sawa mama.” Wakacheka.
Net
alikaa Dar siku mbili tu, tayari akawa anataka kurudi Arusha. Ghafla chakula
cha Dar kikaanza kuwa hakiliki vizuri, masaa hayaendi. Ofisi ya Arusha ikawa
inamuhitaji sana, basi ikawa vurugu. Akamuaga mama yake. “Nilijua week hii
utamalizia huku urudi jumatatu! Maana leo ni ijumaa. Jumapili twende wote
kanisani. Hata mchungaji amekuwa akikuulizia.” “Nitarudi weekend ijayo.” Mama
yake akajichekea moyoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni
hiyo akampigia Tunda simu. “Nimepata tiketi ya
asubuhi.” “Basi nitakuja kukupokea.” “Sawa. Ila kama utakuwa na mambo mengine
naweza kuchukua taksii.” “Hamna neno. Nitatokea ofisini. Nitakuja kukupokea,
halafu unirudishe ofisini kama umechoka unaweza kuniacha tu wewe ukapumzike.”
“Sawa. Lakini nafikiri na mimi nitarudi ofisini.” “Sawa.” Tunda akajibu
taratibu kama kawaida yake.
“Kuna kitu chochote unataka nikujie nacho kutoka huku?” Net
akauliza. Tunda akafikiria kidogo. “Sidhani Net. Nipo
tu sawa. Asante sana.” “Basi nitakuona kesho asubuhi.” “Uwe na safari njema.”
Ikabidi kuagana tu. Hapakuwa na nyongeza.
Jumamosi Siku Isiyo ya Kazi, Net Arudi Arusha.
Kesho yake Net alitua uwanja wa
ndege wa Arusha, Tunda akiwa anamsubiria hapo nje, wala si kule kwenye gari.
Net akafurahi sana kumuona pale. “Pole na safari.” “Asante. Na asante kwa kuja
kunipokea.” Tunda akatabasamu. “Nimefurahi umerudi.” Tunda akaongea kwa upendo
kama aliyekuwa ameachwa hapo kwa muda mrefu. Net kijana wa kizungu akacheka. Na
macho yake yale ya rangi ya bahari, Tunda akakwepesha huku akinyoosha mkono
ampokee.
“Sio
mzito!” Net akajihami kama asiyetaka kupokelewa, anaweza kubeba kila kitu yeye
mwenyewe. “Lakini angalau nikupokee. Usibebe kila kitu peke yako.” Akampa mkoba
wa laptop. “Nimekuletea movie za stori kama unazopenda.” Tunda akacheka.
“Asante. Nitaangalia kesho jioni. Asubuhi nataka niende kazini kidogo.” Net
akanyamaza. Ni siku ya jumapili. Yeye alikuwa lazima kwenda kanisani. Wakarudi
ofisini mpaka jioni.
Jumamosi
huwa kijana wa usafi hafiki hapo ofisini. Walikuwa wao tu wawili. Net alifikia
kwenye meza ya Tunda. Tunda akashangaa haingii ofisini kwake. Yupo tu hapo
mezani kwake akifanya kazi zake hapo hapo. Japokuwa alikuwa akimuogopa, lakini
alifurahia uwepo wake hapo. Hawakuwa wameonana kwa ‘Siku mbili! Nzima’.
Wakashinda wote hapo wakifanya kazi pamoja. Hapakuwa na maongezi mengi. Tunda
anamuogopa Net. Zaidi ya kumjibu endapo atauliza, basi hatazungumza chochote.
Net naye kimya akifanya kazi zake kwenye laptop yake, Tunda asijue ni nini
kinachomfanya kijana huyo kuwa busy kwenye hiyo laptop kila wakati. Kazi
zikaendelea kwa utulivu siku hiyo ya jumamosi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakaendelea
kufuatana. Kazini, hotelini kwa Tunda mpaka wakiagana kwenda kulala. Mwishowe
Net akaonelea kutafuta vitu ambavyo angefanya pamoja na Tunda kila wawapo
pamoja, baada ya kazi angalau wazoeane au kupata kitu chakuzungumza mbali ya
kazi. Akaanzisha siku na muda wao wakuangalia movie pamoja.
Wakitoka
kazini, badala ya kukimbilia rimoti na kuanza kuangalia taarifa ya habari peke
yake, alimtaka Tunda wakae wote hapo waangalie movie pamoja, au wacheze karata.
Basi watacheza hapo kisha anaondoka na kumuacha Tunda. Lakini hakuwahi
kumuuliza Tunda swali hata mara moja juu ya mara zote alizowahi kumkuta na
wanaume au hata kisa kile alichotaka kubembwa juu juu. Tunda alishindwa
kumuelewa kabisa Net. Walicheza na kuzungumzia kile kilichopo mbele yao tu kana
kwamba hakuwa akimfahamu.
Kitu
alichokigundua kwa Tunda kila walipokuwa wakiangalia tv hapo kwenye kochi,
chumbani kwa Tunda, Tunda alijivuta pembeni yake, alikunja miguu yake vizuri na
kuweka mikono yake juu ya kochi kama mto na kulala usingizi mzito sana. Net
alijaribu kubadili aina ya movie. Alileta za visa vya kusisimu, wakati mwingine
historia za kusisimua lakini mara zote Tunda aliishia kulala kabla hata
hazijafika hata nusu! Na ulalaji wake ulikuwa wa usingizi mzito sana, na mara
nyingi Net aliishia kumfunika pale pale kwenye kochi na Tunda aliishia kulala
hapo mpaka asubuhi, kwani alishamuomba wakati akiwa anaondoka asiwe anamuamsha ili ahamie kitandani, alitaka
aondoke kimya kimya amwache tu vile vile alivyolala.
Yeye Net
alikuwa akifurahia sana kuwa na Tunda, lakini wawe wanazungumza. Macho na sauti
ya Tunda ni kweli vilimsumbua Net. Alikuwa akipenda awe anamtizama sio vile
anavyokwepesha macho au basi angalau azungumze ili tu asikie ile sauti yake
akizungumza naye yeye. Na iwe kwa muda mrefu. Kila alivyojitahidi Net, Tunda
hakuwahi kubadilika. Wakati mwingine anaweza akanyamaza hapo chumbani kana
kwamba hayupo. Atatulia kimya, akijitahidi ni kutoa tabasamu.
Net
alijua kwa hakika anamuogopa sana. Swala la afanye nini kuondoa ile hofu ndio
ukawa mtihani mkubwa. Tunda kimya. Kila alipoanza maongezi alianza kwa kumwita
jina lake, kumfanya angalau Tunda
amtizame ayaone hayo macho.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Uliniambia unapenda sana kuangalia movie za stori,
Tunda. Kwa nini kila nikiweka movie unalala? Nataka tuwe tunaongea bwana!
Tunakuwa ofisini busy week nzima, angalau jumamosi jioni au jumapili tuseme
ndio tunapata muda wakupumzika na wewe unalala! Au hufurahii hizi movies
ninazochagua mimi?” “Ni nzuri sana tu. Mbona mwenzako huwa naangalia tena kwa
kuzirudia rudia? Kila nikitoka kazini, ukiondoka au nikishtuka usiku nakujikuta
nimebaki peke yangu, naziangalia.” Net hakuelewa.
“Sasa
kwa nini hutaki kuangalia na mimi?!” “Hata nikikwambia hutaelewa Net.” “Bila
kunijaribu!?” Tunda akanyamaza. “Au nakukera nikiwepo hapa?” “Nisingelala Net.”
Net akakunja uso kidogo kama ambaye hajaelewa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Net naye atafika wapi kwa Tunda anayemfahamu kwa mabaya matupu? Kwanza alisikia
sifa zake kwa binamu zake kina Samantha. Akazithibitisha yeye mwenyewe kwa
kumfumania. Net mwenyewe ni nani? Ana nia gani? Usikose muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment