![]() |
G |
abriel akajirudi kama ambaye hajui tena anachotaka. “Naomba usikasirike Nancy. Sikuongea kwa nia mbaya. Mke wangu ndiye mwanamke niliyedumu naye kwa muda mrefu sana. Hata sikumbuki ni lini nilimvulia nguo mwanamke mwingine. Labda zamani sana enzi za ujana huko chuoni. Tena sio hapa nchini. Kile kitendo nilichokufanyia pale ofisini kimenifanya nijione mjinga sana. Nilikufanya ufanye kitendo ambacho najua hata wewe hukutarajia.” Gab alijisogeza.
“Naelewa wewe ni binadamu
Gab. Siwezi kukuhukumu kwa lolote.
Yale yamepita. Nafikiri matatizo
uliyonayo na mkeo ndiyo yanakupelekesha. Unaonekana haujatulia kimawazo hata
kidogo, umejawa wasiwasi kupita kiasi! Wakati
kwa maongezi yako naona umefanikiwa sana
na kila kitu kinakuendea vizuri.
Kukwambia nikufanyie masaji, nikutaka kukusaidia tu, sio vinginevyo.” “Asante Nancy kwa kunifikiria. Sasa bado ofa ya masaji ipo au ndio nimeharibu?” Tunda akacheka taratibu. “Nishabadili nguo sasa
hivi, nimevaa nguo za kulalia tu.”
“Sasa zina
shida gani?”
“Hebu niangalie jinsi
nilivyo, Gab! Ni kama nipo uchi tu.
Sitaki unielewe vibaya na wewe ni mume
wa mtu.” Kule kuangalia ilikuwa kosa jingine.
Gab alibaki amemkodolea macho Tunda
aliyekuwa amejifunua kutoka kwenye
shuka, akapiga magoti pale kitandani ili
kumuonyesha nguo nyepesi aliyovaa. Tunda
alivuta shuka nakujifunika huku
akicheka. “Si umeona mwenyewe? Sio nguo za heshima.” “Hamna bwana. Mbona upo
sawa tu. Wewe nifanyie tu.”
Tunda alijua
wazi hata afanyaje, Gab hana jeuri
ya kumuacha usiku ule.
Kama
kondoo anayeenda machinjiaoni, Gab akasalimu amri. Alivua nguo na kukimbilia kitandani kwa masaji. Hakutoka pale kitandani mpaka palipo pambazuka. Tunda akaanza kutoka usingizini kabla yakufungua
macho, akakumbuka amelala na Gabriel. Alifurahi sana.
Akafungua macho taratibu akamkuta akimtizama.
Akatoa tabasamu lililojaa usingizi. “Wewe mtoto utaniua.” Gab akalalamika.
Tunda akacheka na kujitoa kifuani kwake,
akajilaza kwenye mto. “Mbona unanikimbia sasa?” “Siumesema unawahi
kikao asubuhi hii?”
“Nimeshawatumia
ujumbe tutafanya mchana. Rudi hapa
kifuani bwana.” Tunda akacheka
wakati anarudi. Gabriel ulalaji wake
sio hata nusu ya Mbawala Juniour.
Gabriel alimuweka kifuani kwake,
akamchezea taratibu mpaka Tunda
akalala. Alifurahia mikononi kwa
Gabriel. Alipenda harufu yake.
Alitamani asitoke hapo kifuani.
Hakuna kikao kilichofanyika siku hiyo wala siku inayofuata. Tunda na Gabriel walibakia hapo chumbani wakifurahiana.
Alikuwa ni kama chui aliyeona nyama.
Lakini alichomfurahisha Tunda ni
ustaarabu. Kumuomba na kumuuliza kama
yupo sawa au anataka kupumzika.
Alijawa shukurani kwa kila anachofanyiwa
na Tunda. Hakuacha kusema asante na kutaka kujua kama yupo sawa. Hakuna kitu
kidogo alichofanyiwa na Tunda asitoe
shukurani na kukielezea jinsi
alivyofurahia. Hilo Tunda alilipenda na kumfananisha kidogo na waziri Mbawala.
Wengine wote hawakuwa na tofauti.
Walimtumia tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya kutoka hapo, Gabriel akaanza kumganda sasa Tunda. Kila safari anayosafiri alitaka awe naye. Walisafiri nje na ndani ya nchi. Na kwakuwa alikuwa akimpa mapesa mengi, Tunda akaanza kupunguza wateja waliokuwa wakimuhonga pesa chache na sio wastaarabu. Wanaotumia mwili wake vibaya. Kama Mbawala Junior, akaanza kupuuza simu zake. “Pengo lake limezibwa na Gab.”
Akacheka Tunda wakati akisoma jumbe za
Mbawala Junior na kuzifuta. Hata
alipopiga simu, hakupokea tena.
Jeuri ikamjaa, akaanza kuringia wateja wake wengine. Pesa aliyokuwa akimwaga Gabriel, ilimtosha sana tu. Bila kutegemea, Gabriel
akawa zaidi ya Sadiki. “Mungu amenifuta machozi.” Tunda akajisemea.
Hapakuwa na kuloga, wala kukesha
makaburini. Gabriel hakutaka habari za
watoto wala kumpekua Tunda. Penzi na
starehe tu. Wote walikuwa watu wa
furaha. Hata walipokuwa jijini
Dar, bado walionana. Kituo chake kilekile. Mlimani city. Hata kama ni jioni au usiku
wakati Gabriel anarudi
nyumbani kwake, alisimama hapo.
Tunda alimfuata. Watatumia hata lisaa
kama akiwa na haraka au watakaa
hapo ndani ya gari kwa muda wa
Gabriel. Ndipo wanaachana.
Hazikuwa zikipita siku tatu bila wawili hao kukutana. Ilikuwa ni kama Gabriel hawezi kutoonana na Tunda tena. Malalamishi juu ya mkewe yakaisha kabisa. Gabriel akawa mtu mwenye furaha tu. Tunda alishamfundisha kupuuza
mambo madogo madogo. Basi amani ikaendelea
mpaka nyumbani. Kila mtu aliyaona mabadiliko ya Gabriel kitu kilichoibua maswali hata kwa mkewe ambaye walishazoea kujibizana kila wanapokuwa pamoja. Akashangaa ukimya na kunyamaza kwa mumewe. Usingemkuta Gabriel akibishana naye tena. Alitoka muda wa kawaida, na kurudi nyumbani muda wa kawaida. Tunda alishajiambia, ukila na kipofu, humshiki mkono. Hakuiba kwa kelele, ili asikamatwe mapema na kupokonywa tonge mdomoni. Basi, akaendelea
kunufaika na Gabriel na Gabriel akinufaika na Tunda. Maisha ya amani na utulivu yakaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Gabriel alimtaarifu Tunda msiba mkubwa uliotokea
kanisani kwao. Rafiki wa mkewe Gabriel,
Bethy alifariki akiwa anajifungua.
Aliacha watoto wakiume wawili na bado walikuwa
wadogo. Kwa ukaribu aliokuwa nao huyo
dada aliyefariki gafla na Bethy mkewe Gabriel,
ule msiba ulikuwa kama wao. Walilala
na kushinda msibani kipindi chote
hicho cha msiba, mpaka walipohamisha msiba huko kijijini kwao huyo marehemu. Kwa hiyo hapakuwa na kuonana tena. Tunda akaamua kutumia muda ule na wateja wengine.
Akiwa Dodoma na Naibu waziri wa ujenzi wa awamu
hiyo ya utawala, hakuacha kuwasiliana na Gab. Gabriel alilalamika vile alivyo
na hamu naye, na pindi watakaporudi mjini lazima waende kupumzika Nairobi. ‘Hata mimi
nipo mpweke sana Gab. Siku nikikukamata wewe! Utajuta.’ Gabriel alipiga simu
huku akicheka sana. “Utanifanyaje?” “Sitaki kukwambia. Lakini lazima utalipia huu upweke ulionisababishia.” Waliongea kwa muda mrefu, Gabriel akiwa anajiambia moyoni kuwa amepata mwanamke anayempenda kwa dhati
na kumridhisha kuliko hata mkewe, huku Tunda
naye akijiambia amepata mtu wake wa
kudumu. Lazima kumridhisha na kumuweka
karibu kwa garama yeyote ile. Na kweli,
linapofika swala la Gabriel, kila mtu
atasubiri. Na kila kitu kitasimama.
Gabriel kwanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi yule Naibu na kumwambia watatoka jioni kwenda mziki, lakini kabla ya hapo anakwenda kukutana na mtu anayetaka sana tenda ya ujenzi wa barabara
ya Nachingwea. “Bwana kwani lazima
ukaonane nae leo?” Tunda alilalamika. “Inabidi Teddy! Ni watu tunaoheshimiana nao sana. Na walishajenga barabara ya Mpanda bila shida. Tena mama yake ni mtu wa nyumbani
kabisa. Ni kabila moja, ni mama mzuri
sana.” “Kwa nini asitufuate klabu sasa?” “Hahahahah! Jamaa mwenyewe hata pombe hagusi. Twende bwana
hatutakaa sana.” Ikabidi akubali tu.
Tunda alivaa suruali iliyomshika
vizuri, na kiblauzi cha kung’aa, rangi za usiku. Ndogo nayo ilimshika juu vizuri. Chini ya hiyo blauzi ilikuwa
na muundo wa “V”Mbele na nyuma na
vimikanda
kama
shimizi. Kwa kuwa ilikuwa jioni na
wanakwenda mziki, akavaa kiatu kizuri
cha juu chenye uwezo wa kumbeba muda mrefu bila kuchoka. Hakika alipendeza Tunda. Alishikwa vizuri juu mpaka chini. Kila kitu kilimkaa vizuri. Na hapo alijulikana kama Teddy.
Net Naye Arudi Pichani.
K |
wa
mara ya kwanza tokea kwa Shangazi yake,
Tunda akiwa kwenye kuuza mwili wake,
akutana uso kwa uso na Net! Alifika
kwenye hiyo hoteli na huyo Naibu Waziri,
wakaelekea upande wa mgahawani,
wakamkuta Net alishawasili, akisubiria
tu hapo mgahawani. Tunda alishtuka sana.
Alitamani arudi kwenye gari lakini
yule Mheshimiwa alikuwa amemshika
mkono. Net alisimama
huku akimwangalia Tunda. “Umesubiri sana?” “Hapana kiongozi. Na mimi ndio nafika hapa.” “Huyu anaitwa Teddy,
niko naye hapa kipindi hichi cha Bunge.
Huwa anakuja kusaidia saidia ili kazi
ziende.” Kisha akamgeukia Tunda. “Teddy, huyu ni Nathaniel, ndio hao wajenzi wa barabara yeye na mama yake.” Tunda hakutaka hata kumpa mkono Net.
Akawazunguka na kutafuta meza na kukaa.
Wakamfuata na wao wakakaa hapo hapo
kwenye hiyo meza.
Muda wote wa mazungumzo kati ya Net na yule Mheshimiwa, Tunda alikuwa ameinama akichezea simu yake. Walipomaliza wakati yule Mheshimiwa akiagana na Net, Tunda akasimama na kuondoka bila hata kuaga, akaelekea kwenye gari. Tunda alibadilika kabisa mpaka yule Naibu alimuona. “Vipi? Mbona kimya?” “Kichwa kimeanza kuniuma
gafla.” “Basi turudi hotelini.”
Walirudi hotelini, akalala. Naibu asielewe kulikoni. Akajua mambo ya wanawake tu, atakuwa sawa.
Basi aliamka kesho yake yupo sawa, akafanya kilichompeleka Dodoma kwa huyo Naibu bila shida wala kinyongo, akimfurahisha
vilivyo. Akiwa kwenye vikao vya Bunge,
Tunda anazunguka na kuwapa wengine huo
mwili muda huo wa mchana wakati Naibu
yupo kwenye vikao vya Bunge.
Anarudi kulala, tayari kumsubiri Naibu waendeleze
mchezo huku akimsubiria Gabriel
amtafute. Tunda akaendeleza mchezo wake
huo, huko jiji kuu la nchi ya Tanzania
kama kawaida. Akiwazungusha wabunge kwa mawaziri. Wakubwa kwa vijana, mpaka
Gabriel alipomtafuta kuwa amerudi Dar, na wamemaliza msiba. Gabriel
huwa hasubiri. Tunda
alishakuwa ametengeneza pesa nzuri
tu, akafungasha vilivyo vyake, akarudi Dar kwa Gabriel kabla hata
Bunge halijaisha.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ratiba
za Tunda zikaanza
kutegemeana na ratiba za Gabriel.
Hakutaka Gabriel amkose muda na
wakati wowote anaomtaka yeye. Hata
kama ni usiku wa manane, Gabriel
akimwita popote, alienda. Simu
yake ilikuwa haisubiri. Ilikuwa na mlio
wake maalumu. Akipiga muda na wakati
wowote. Hata akiwa na mteja, huyo mteja
atasubiri. Gabriel kwanza. Alimchomoa
pesa nyingi sana, na Gabriel naye
alikuwa akizimwaga bila kufikiria mara
mbili. Kabla Tunda mwenyewe
hajaomba, alimpa. Tunda akawa na pesa,
kama yeye ndio mmiliki wa biashara
za Gabriel na Gabriel ndiye
mfanyakazi wake.
Gabriel hakuongopa. Tunda alipotua tu jijini, akakuta Gabriel anayo mipango tayari. Alimwambia atasafiri tena na mkewe. Lakini nilazima azungukie biashara zake tena huko Mwanza ndipo wasafiri na mkewe. Tunda alitua jijini asubuhi, jioni akawa tena kwenye ndege kuelekea Mwanza na Gabriel. Walitumia siku tatu pamoja. Gabriel akienda kuchungulia tu kwenye hiyo migahawa yake, na kurudi hotelini kwa Tunda. Baada ya hizo siku kuisha wakarudi
Dar, Gabriel na mkewe wakasafiri
tena. Tunda hakuuliza ni wapi
anakwenda. Alimuonyesha Gabriel
kuwa anaheshimu ratiba zake na
mkewe. Hana maswali na hata
alipokuwa mkewe akipiga simu na yeye
yupo naye, basi atanyanyuka hapo na
kuondoka kumpa nafasi yakuzungumza. Hilo
alilipenda sana Gabriel. Hakuwa
msumbufu.
Hakuwa akimtafuta Gabriel kwa simu wala jumbe, alimpa yeye ruksa kumtafuta muda na wakati wowote atakao, lakini sio yeye. Alimwambia hataki kuja
kumtia matatizoni. Hata namba yake ya
simu alimshauri ashike tu kichwani.
Penzi tamu la wizi likaendelea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifanya starehe nyingi sana alipokuwa na Tunda, tofauti na wateja zake wengine waliokuwa wakipenda kumfungia tu ndani. Na hapo aliweza kupata wateja wengine wa muda mfupi. Au hata marafiki zake huyo huyo baba. Wakiwa kwenye kunywa na kula huko kwenye starehe, akiona ameshalewa, basi Tunda anaweza kumtongoza mmoja wa rafiki zake, na kupanga naye miahadi ya mchana. Huyo baba akiwa ametoka kwenda kwenye shuguli zake, basi hapo ndipo Tunda atakutana na mwingine. Na uzuri wa huyu baba kwa kuwa alikuwa mtu mzima na mlevi, shuguli yake kwenye mapenzi
haikuwa kubwa sana. Aliridhika kwa haraka kitu ambacho hakikuwa kikimchosha Tunda. Basi hapo ataingiza pesa kwa huyo na wengineo. Atarudi kwake akiwa amejaa.
Fumanizi
Tena.
Siku ya tatu wakiwa Mwanza na yule mteja
wake, walikuwa mahali
wakinywa na marafiki zake yule baba. Yaani wafanyabiashara wenzake. Pombe
iliyokuwa ikinywewa hapo, vyakula,
ulikuwa utapanyaji mtupu. Na karibu wote
waliokuwa hapo mezani, Tunda
alishawadumia, ila hawakuwa wakijuana.
Kwa hiyo wote walikuwa wakiiba kwa yule
aliyekuja nae Tunda, kwa wakati tofauti
tofauti. Tunda akawa akinufaika nao,
wasijue.
Wakiwa
wamejawa vicheko vya kilevi hapo mezani, yule baba aliyekuwa amekuja naye Tunda, akapokea simu ilisikika ni ya kikazi. Walizungumza kidogo kisha akamwelekeza yule mtu aliyekuwa akizungumza naye kwenye simu pale alipo,
na kumtaka afike hapo kwa mazungumzo
zaidi. Yule mtu alimwambia atakuwepo hapo kama
baada ya dakika 15 tu. Vicheko
vikaendelea.
Tunda alitamani ageuke upepo apotee, pale Net alipowasogelea kwenye meza yao. “Najua hupendi mazungumzo ya baa. Lakini
sitakuweka sana.” Yule baba alisimama
kusalimiana na Net, lakini Tunda
hakutaka hata kumwangalia tena. Alimuona vile Net alivyokuwa
akimwangalia. “Samahani bwana,
sijatoa utambulisho. Akamgeukia
Tunda, “Joy, huyu anaitwa Nathaniel yeye na mama yake ni wateja wetu wakubwa. Tunawaingizia
vifaa vyao vya ujenzi hapa nchini.
Tusema ndio watu wanaochangia kutuweka
mjini.” Yule mteja wa Tunda aliongea huku
akicheka. “Hapana bwana!” Net alijibu kiuungwana kidogo.
“Kweli kabisa. Unafikiri bila tenda zenu, mjini pangekuaje? Haya huyu anaitwa Joy, ni nini.. Siunajua kuna umri
ukifika joto linapungua mwilini? Hata
bibilia imeshauri. Inabidi wazee tutafutiwe mabinti wadogo watupe joto kama mfamle Daudi aliyependwa sana na Mungu!” Yule Mzee alishakuwa amelewa, alikuwa akiongea sana. “Mabinti kama hawa ni hadimu sana hapa duniani. Au unasemaje Bosi wangu?” Yule Mzee alimuuliza Net huku
akimpiga piga begani. Net alitabasamu huku
akimwangalia Tunda. Tunda alishatoa simu
yake kwenye pochi akawa akiichezea
bila kunyanyua uso wake. Wakati mtumzima
huyo akiendelea kuropoka.
“Sijui tutegemee lini huo mzigo?” Net akauliza taratibu, ili kubadili mazungumzo ya yule mzee aliyokuwa akimsifia
Tunda tu badala ya biashara. Alitoa sifa
zake za uzuri wa Tunda mpaka umbile
lake, tena kwa undani bila kunyamaza
huku akiendelea kunywa. Tunda akasimama. “Vipi
tena?” “Naenda msalani.” Tunda akaondoka. Hakurudi mpaka alipoona Net ameondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Aliporudi tu Dar, mteja mwingine akamtafuta. Naye
pia ni miongoni mwa wateja wake ambao
Tunda hakuwa akimpenda sana, kwani alikuwa muoga sana ila bado anataka kuiba.
Kitu alichokuwa akimkubalia tu ni pesa alizokuwa akimuhonga. Alimpata kwa kumkonyeza akiwa amekaa na mteja mwingine kwenye baa. Alienda naye kwenye gari baada ya kumuaga mteja aliyekuwa amekaa naye siku ile na kwenda kumaliza haja za yule
mteja aliyemkonyeza kwa muda mfupi sana
tena kwenye gari kitu alichokifurahia
sana na kufanya kama mazoea.
Walikuwa
wakikutana sehemu zinazouzwa vyakula, tena muda wa mchana, wakati anakwenda kwa chakula cha mchana, na Tunda alikuwa akimuhudumia kwenye gari yake.
Kiti cha nyuma ambako vioo vilikuwa
giza. Tunda anamchezea, baada ya
muda mfupi sana, anakuwa amemalizana naye. Tunda anaondoka na yeye anakwenda kuungana na rafiki zake kwa chakula
cha mchana hapohapo bila kuchelewa.
Alimpenda sana Tunda kwa umaridadi wake.
Wepesi na usanifu wa alichokuwa
akimfayia. Kila akipata tu pesa, basi
lazima atamtafuta Tunda. Na hakuwahi
hata kuhisiwa na yeyote yule. Si marafiki
zake aliokuwa akitoka nao kwa
chakula cha mchana tu, hata mkewe
pia. Kwani alirudi nyumbani muda
wake wa kawaida bila kuchelewa na
wakati wote alikuwa ofisini au sehemu
husika ambayo hakuwahi kutiliwa
mashaka.
Siku hiyo walikubaliana wakutane na Tunda kwenye baa ambayo walikuwa wakiuza mbuzi na ndizi za kuchoma nzuri sana, karibu na ofisini kwake. Tunda alikipenda sana chakula cha pale. ‘Kama ni hapo
ujue ni mpaka nile kwanza. Siunajua
ninavyopenda mbuzi wa pale?’ ‘Sio tuchelewe sasa, Maria! Siunajua muda wangu?’ ‘Nishawahi kukuchelewesha hata mara moja?’ Tunda akamtumia
huo ujumbe. ‘Basi mama. Wewe
tangulia uagize chakula, mimi nikija
sitakaa sana, tunakwenda kwenye gari.’ Wakakubaliana.
Tunda alivaa
vizuri kama kawaida yake. Na alivaa
kigauni kilichokuwa kikiendana na sehemu anayokwenda kufanya shuguli yake.
Kigauni chepesi kilichochanua. Na kiatu
cha juu. Aliporidhika na muonekano wake
ndipo akatoka. Alitoka mapema kidogo ili
kupata muda wa kula. Alijitengea muda
wake ili usiingiliane na muda wa
mteja wake. Bila kuchelewa, kwa
kuwa alijua anachotaka, alipofika
tu akaelekea jikoni moja kwa moja, akaagiza chakula huku akiwasihi wasimcheleweshe. Kisha akatafuta sehemu akakaa.
Baada ya muda mfupi tu, chakula na kinywaji vikawa vimeshawasili hapo mezani kwake. Wakati akila
na yule mteja wake naye akawasili akiwa
na faili mkononi. “Sasa makaratasi ya
nini na wewe!?” Kuna mtu anakuja kulichukua hili faili.” “Si umesema una haraka
wewe! Akichelewa?” “Jamaa mwenyewe mzungu, anatunza muda sana.
Akikwambia dakika kumi ni kumi. Atakuja
sasa hivi, wewe malizia
hicho chakula. Tutaondoka sasa hivi.” Wakati ameinama anakata nyama nyingine ili aendelee kula, akasikia mtu akisalimia. Aliponyanyua macho alikutana na Net. Tunda alibaki kama amemwagiwa maji ya baridi. Net alibaki akimtizama Tunda. Akavuta pumzi kwa nguvu kisha akaweka mikono yake juu ya kiti kilichokuwa mbele ya macho ya Tunda na kubaki wakitizamana na Tunda aliyekuwa ameduaa. “Kumbe na wewe unamfahamu Maria?” Yule mteja akamuuliza Net,
lakini Net alibaki akimtizama
Tunda.
Tunda aliinama akachukua pochi yake akasimama. “No
no no nooo Maria! Huwezi kuondoka.
Lazima tumalizie mipango yetu.” Tunda alivuta kiti nyuma na kuanza kuondoka. Yule mteja wa Tunda alimkabidhi Net lile faili
bila maelezo yeyote,
akamkimbilia Tunda. “Maria! Maria!
Kuna nini? Simama basi tuongee.” Tunda hakugeuka nyuma akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Picha ya macho ya Net akiwa anamwangalia kila alipokuwa akimkuta na wateja wake, ilianza kumsumbua sana Tunda. Hakujua kwa nini. Alijifariji sana, na kujimbia hana haja yakumjali Net, si kitu kwake, lakini
moyo ulishindwa kupokea kabisa zile
taarifa zakumpuuzia Net. Aliendelea
kuteseka. Kila alipofunga macho alimuona
Net akimtizama. Mara nyingine
aliota Net amemfumania kabisa. “Kwani hata akinifumania kuna nini!?” Tunda alishtuka kutoka ndotoni nakuanza kujishangaa.
“Hanihusu, simuhusu.
Kwanza hata hanifahamu.” Tunda
aliendelea kujifariji.
Hodi ya kijana wake wa kazi ndiyo iliyomtoa
kitandani. Alikwenda kumfungulia mlango baada ya mlinzi kumfungulia geti. “Leo kazi kubwa ni usafi na kunyoosha nguo zangu.” “Sawa dada.”
Tunda
akaamua kurudi tena chumbani kwake
alikokuwa amekaa muda wote akijifikiria
baada ya ile ndoto yakufumaniwa na Net, akiwa katikati ya kufanya mapenzi na mteja
wake mwingine.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa anakaribia mlango wa chumbani kwake, akasikia simu yake ikiita. Aliikimbilia akijua ni Gabriel
tu, kwani ndiye mtu pekee aliyekuwa amebaki wakupiga simu. “Mbona mapema leo?” “Nimelala nakuota.”
Tunda alianza kucheka. “Na mimi nimekuota.” “Nafanya nini?” Gabriel akauliza
huku akicheka. “Mpaka tukikutana
ndio nitakuonyesha kwa vitendo.” “Unapenda kunichanganya akili
wewe Nancy! Utafanya nishindwe kufanya
kazi siku nzima.” “Naweza kukufuta hata kazini.” “Kweli?” “Lini umeanza kunitilia mashaka?” “Njoo basi
kwenye saa nane mchana. Usiache Nancy,
hali mbaya mwenzio.” “Hali mbaya vipi wakati umeamka pembeni ya mkeo?” “Sinilikwambia sababu zake
haziishi? Kama jana ameniambia amechoka
sana, nisimguse.” “Pole Gab.” “Nishazoea.” Gabriel alijibu kwa utulivu
kidogo. “Basi nitakuja saa nne. Usijali.”“Sawa.”
Mtu pekee aliyemchanganya akili Tunda ni Gabriel. Alianza kujitengeneza kuanzia asubuhi hiyo. Alibadili rangi za kucha zaidi ya mara tatu huku akitoa kasoro kila nguo. Mpaka alipopigiwa simu tena na Gabriel. “Kazi
haziendi huku Nancy. Njoo uokoe jahazi.”“Siumesema mpaka saa nane mchana?!” “Siwezi kufika
saa nane.” Tunda
alicheka sana. “Basi nakuja. Nipe kama lisaa.” Ilibidi
Tunda ajikubali tu ili asimchelewe
Gabriel ambaye alikuwa kama Mungu
mtu. Akatoka hapo kwake.
Alikwenda mpaka ofisini kwa Gabriel. Sekretari aliambiwa simu na wageni wote wasubiri. Wakajifungia na Tunda humo ndani ofisini kwa Gabriel. Ilikuwa saa sita mchana wakati Tunda akiingia humo ndani. Baada ya kama dakika 20 hivi, sekretari akampigia simu kumwambia BF anaondoka. Tunda alimuona Gabriel amepaniki. “Kwa
nini sasa hukuniambia kama ameshafika?
Subiri natoka sasa hivi.” Waliingia
chooni kwa Gabriel, akajisafisha vizuri
na kuvaa harakaharaka kisha akatoka nje
kabisa kumfuata huyo mgeni ambaye Tunda alisikia
jina moja tu, BF. Alimuacha Tunda
akijitengeneza huko huko chooni ili
atoke safi kama alivyoingia.
Tunda akiwa bado chooni, Gabriel alirudi pale ofisini kwake na mgeni wake. “Samahani sana. Nilikuwa na kijidharula
kidogo.” “Usijali.
Ninaharaka kidogo. Labda nikuwekee mafaili yote kwenye kompyuta
yako, baadaye ukipata muda
wakuangalia kila kitu na kuridhika,
ndipo utanipigia simu.” “Hamna shida kabisa.
Vipi mama lakini?”
Wakati
wameinamia kompyuta Tunda naye akatoka
kule chooni akaingia pale ofisini
ili kuchukua pochi yake na viatu alivyokuwa amevua katikati ya penzi, aondoke.
Fumanizi Baya,
Lililomgarimu Tunda.
K |
ule
kufungua mlango wa chooni kuliwafanya
wote wanyanyue uso na kumtizama Tunda.
Uso kwa uso na Net tena. Tunda alitamani
kurudi chooni lakini alikuwa ameshafunga
mlango nyuma yake. Net alisimama vizuri
akamwangalia Tunda na Gabriel. “Umeanza lini Gab?” Net alimgeukia Gabriel aliyeonekana kupaniki zaidi. “Eti Gabriel?” “Nancy huyu ni Net, rafiki
yangu sana tokea tupo wadogo kabisa.
Mpaka watu wametupa jina la BF, Best
Friend.” Gabriel na yeye alisimama huku
akitetemeka. Wazi alionyesha ameingiwa
hofu. Net alimtizama Tunda kwa muda,
kisha akatoka bila kuaga.
“Samahani sana Gabriel,
sikukusudia.” “Usijali Nancy, nimakosa yangu. Nilisahau kama jamaa aliniambia atakuja saa sita na
robo. Huwa anapenda kwenda sana na muda.
Kule kumuweka hapo nje wakati nipo na
wewe humu ndani atakuwa amekasirika
sana.” Tunda
alitoka kimya kimya bila hata
kuongeza neno. Akarudi kwake asijue
kama lile ni balaa au kuna mkosi
unaomfuatilia. Akakumbuka ndoto aliyoota
usiku wa kuamkia siku hiyo. Alitamani
kulia. Alipoteza wateja wengi sababu
ya Gabriel, hakuwa tayari kumpoteza Gabriel, mteja aliyekuwa akimlipa mapesa mengi sana. Ni kama yeye ndio aliyekuwa akimlipia garama zote kubwa za maisha. Wengine ni kama chakula, mavazi na saluni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ulipita
kama mwezi, Tunda
amejifungia ndani asijue chakufanya.
Gabriel aliacha kupiga simu kabisa
tokea siku waliyofumaniwa na Net
pale ofisini. Alishapoteza wateja
karibu wote. Tena kwa kufanya juhudi
za makusudi, kuwaambia kabisa
wasimtafute mpaka yeye
takapowatafuta ili wasije kumtafuta au
hata kutuma ujumbe anapokuwa na
Gabriel. Halafu ikatokea kwa bahati
mbaya, Gab akaziona na kumfikiria ni
Malaya tu akamuacha. Kwani mara
nyingine walikuwa wakicheza na Gabriel
games zilizopo kwenye simu yake.
Na
hakuishia hapo kwa hao wateja zake wangine, alikwenda umbali wakuwa block
kabisa ili hata ujumbe usije kuwa
unaingia akiwa na Gabriel. Pesa aliyokuwa
akihongwa na Gabriel ilikuwa ni sawa na
kuhongwa karibu na wanaume wengine wote
waliokuwa wamebaki . Shida ndogo ndogo na
kubwa za Tunda zilikuwa zikimwisha
alipokuwa na Gabriel.
Tunda aliendelea kuwaza juu ya maisha
yake, kwani nyumba
aliyokuwa akiishi alikuwa akilipia
kodi kwa dolla. Aliishi maisha ya
kifahari sana. Pesa yake ilikuwa
ikiishia kwenye kuvaa vizuri na
kujinunulia vitu vya thamani kana
kwamba hakuna kesho. Alikuwa anajiambia mwili wake ndio biashara yake. Lazima kuutunza vizuri. Basi Tunda alikuwa akiutunza huo mwili kama aliyeambiwa anaupungufu wa kinga mwilini. Alikuwa akinywa virutubisho vya huo mwili kwa gharama kubwa
sana.
Alijiunga na kampuni iliyokuwa ikileta virutubisho vya mwili vya asili nchini. Basi
alikuwa akinywa hivyo virutubisho kila siku bila kukosa. Hakuwahi kuishiwa. Kwa kumtizama tu Tunda, ungejua huo mwili unatunza vizuri. “Anayeendesha taksii, lazima atengeneze
hiyo gari ya biashara mara kwa mara
kuvutia wateja wake. Kusafisha,
matengenezo mazuri, kubadilisha oil,
na kujaza mafuta kila inapokaribia
kuisha ili asizimikiwe njiani akiwa na
mteja. Basi na mwili wangu ndio hivyo hivyo.” Tunda alikuwa
akijikumbusha hayo mara kwa mara juu ya kujijali.
Basi ukimkuta ndani ya Sauna, ametulia kimya. Na alithamini pia muda wa masaji. Hoteli yeyote aliyokuwa akienda na wateja zake, ilikuwa ni lazima aulizie kama
wanatoa
hizo huduma. Na kama zipo, atatumia
ipasavyo. Hata kulala, alilala kwenye
kitanda cha garama kama mfalme na hata
mashuka yake alijifunika mashuka mazuri
sana. Na alihakikisha kama hayupo
kazini, anapata muda wakutosha wa kulala. Usingemkuta
anakula takataka. Chochote alichojua kitamnenepesha, alikula kwa hamu, tena kidogo sana. Kwanza alikuwa akila virutubisho ambavyo vilimfanya hasikii njaa hovyo. Na akila mlo mmoja mkubwa, basi.
Mara nyingi
hakuwa akipika chakula nyumbani
kwake. Isipokuwa vitu vidogo kama
kukaanga mayai tu na kuchemsha
maziwa. Vyakula vingine alikuwa
akila kwenye mahoteli. Tena ya maana
tu. Na kila alipokuwa akienda kwenye
biashara zake, alihakikisha anarudi
nyumbani na chakula chakula kesho
yake. Hakuwa akipenda kuwa karibu
na moto wa jikoni kwa muda mrefu.
Kwa muda wote huo alioishi peke
yake, baada yakutoka kwa shangazi
yake, Tunda alijipenda sana. Alikuwa
ni kama anajilipia miaka yote
aliyoteseka tokea anatolewa kwa bibi
yake akiwa bado binti mdogo.
Kwa
kumwangalia tu, ungejua mwili huo unashugulikiwa vizuri. Mwili mzima
utafikiri amepigwa msasa wa ukweli. Aina
ya lotion na mafuta ya nywele yaliyokuwa yakiingia mwilini mwake, ilikuwa pesa yakutosha. Yalimfanya ang’ae kama nyoka juani. Nywele ambayo sio 100% human hair, haikuwa ikiingia tena kichwani mwake. Saluni alizokuwa akienda kutengenezwa Tunda, ni za wake wa mamilionea wa mjini na kina mama wanaoshika pesa nzuri. Kwa hiyo, bili au garama zilizokuwa zikimkabili kwa wiki tu, ili kumfanya aendeshe maisha yake, ilikuwa juu sana kama matumizi ya familia moja kwa mwezi. Achilia mbali hiyo kodi aliyokuwa akilipa kwa madola, kwa mwezi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku
zikazidi kwenda, Gabriel hamtafuti.
Garama zote akaanza kulipa yeye mwenyewe
kwa kutumia akiba aliyokuwa nayo.
Kilichommaliza zaidi hiyo kodi ya miezi
mitatu. Na akajua miezi mitatu huwa
haikawii kuisha. Atapata wapi pesa
ingine ya kodi!? Mwenye nyumba wake
alikuwa makini, hakuwa akitaka
kupitishiwa kodi yake zaidi ya juma
moja. Ikabidi kuanza kusaka wateja
wake wazamani bila mafanikio. Kwani
na hali ya uchumi wa Tanzania
ikazidi kuwa ngumu, kila mtu alilalamika
pesa hamna. Hata yale mabuzi aliyozoea kuyashtukiza
yaliacha kuhonga, walianza kumkopa.
Hali ikazidi kuwa mbaya. Wengi wa wateja wake alipowafuata, waliishia kumlisha, nakumtumia bila kumpa pesa. Akaamua atulie, kwa kuwa pia alikuwa akitumia taksii kumzungusha kwa hao wanaume walioacha kumlipa. Ikabidi
hata masharti aliyokuwa amemuwekea yeye mwenyewe
Gabriel, kukiuka. Kutomtafuta yeye mpaka
Gabriel mwenyewe amtafute. Tunda akaanza
kutuma jumbe, bila kupata majibu
kabisa. Siku zikazidi kwenda. Mwezi wa
pili, watatu, na wa nne tokea ukimya
wa Gabriel. Na muda wakulipa tena
kodi ukafika bila Tunda kukusanya
pesa hata nusu ya hiyo kodi.
Wasiwasi
ukazidi kumwingia. Ikambidi aingie
mtaani kusaka wateja kwa nguvu zote ili angalau kupata kodi tu.
Akajiambia mengine yanaweza kusubiri,
ila sio kufukuzwa pale anapoishi.
Alihangaika mpaka alipokata tamaa.
Akaanza kumfuatilia tena Gabriel
kujua alipo. Kitendo cha kupita muda
wote huo wa miezi minne tokea
kumsikia na kumuona Gabriel kuliongeza wasiwasi usioweza kutamkika.
Gabriel hakuwa mtu wa kukaa kimya kwa
muda mrefu hivyo.
Hofu aliyokuwa nayo Tunda, hakuwa akiweza hata kupata usingizi. Alijawa hofu ya nini chakufanya. Hakuwa na tumaini tena na maisha yalikuwa lazima yaendelee. Tena kwa haraka na bili zilikuwa zikisubiri kulipwa. Akiba yake aliyokuwa nayo alishalipia kodi ya miezi ile ambayo Gabriel hakuwepo nchini, aliposafiri na mkewe.
Aliporudi
Gabriel ndio ni kama alikuwa
akijikusanya tena na ndio Net
akaingilia. Akaja kulipa tena kodi
nyingine baadaye. Akajimaliza kabisa.
Sasa anafanyaje tena! Hana ndugu
wala rafiki wakumkopa pesa au kumsitiri.
Tunda alikuwa peke yake hapa duniani.
Hakuna hata aliyejua anapoishi. Hana
biashara yoote anayojua na kuweza kuifanya isipokuwa kuuza huo mwili ambao umeanza kutumiwa kwa kukopwa. Tunda alianza kuisha mwili kwa wasiwasi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Maji yalipofika shingoni, akaamua kwenda ofisini kwa Gabriel. Akaambiwa amesafiri kikazi yupo jijini Arusha. Tunda alifurahi sana. Kwani alishajua viwanja vyake vyote Gab awapo jijini Arusha. Hakutaka hata pakuche. Akarudi kwake, kufungasha huku akiwa ameshampigia simu kijana anayemsaidia kukata tiketi za ndege. Akamsihi
afanye juu chini,
kuhakikisha anampatia tiketi ya
kumfikisha Arusha siku hiyo.
Akiwa nyumbani kwake anafungasha, yule kijana akamwambia amempatia tiketi lakini akamtajia pesa kubwa kwa makusudi akijua lazima atamlipa sababu Tunda alimpigia akiwa anambembeleza sana na kumuonyesha ni muhimu. Hata hivyo alimjua Tunda anayo pesa. Ni mteja wake wa muda mrefu na huwa akimpatia tiketi, haachi kumlipa za nyongeza kama shukurani. Na kweli, Tunda hakumbishia. Akamwambia anaitaka kwa bei yoyote ile, amuwekee.
Akachukua taksii mpaka uwanja wa ndege. Pesa
ndogo aliyokuwa amebakiwa nayo kama akiba, ndio hiyo hiyo aliyokuwa akiitumia kwa garama zote hizo kumfikisha Arusha akiwa na uhakika itarudi tu punde Gabriel atakapoiona sura yake.
Alifika Arusha kulikuwa na dalili ya
mvua. Akachukua taksii tena, moja
kwa moja kwenye hoteli aliyojua
lazima Gabriel atakuwepo. Hakuwa na
pesa yakutoshea kuchukua chumba
pale kwenye ile hoteli wala nauli
yakurudia. Hata pale alipokuwa akiishi
mwenye nyumba alishamwambia amepata ubalozi ambao unataka kumkodishia mfanyakazi wao ile nyumba kwa pesa kubwa zaidi ya ile anayolipa Tunda kila baada ya miezi mitatu. Alimwambia wao wapo tayari kulipa kodi ya mwaka.
Kwa hiyo akamwambia inabidi aongeze kodi, na baada ya week hiyo kuisha kama bado pesa yake
haijaingia kwenye akaunti yake,
atatolewa vitu vyake nje, maana ulishapita
mwezi bila Tunda kulipa. Kwa hiyo Gab
pekee ndiye mkombozi aliyebaki anayeweza
kulipa mapesa yote yale kwa mara moja.
Giza
lilikuwa limeshaingia, pale Tunda
alipokuwa akishushwa pale hotelini na
manyunyu ya mvua
yalianza kudondoka moja moja.
Alikwenda mpaka mapokezi akamkuta
muhudumu anayefahamiana naye,
akamwambia Gabriel yupo upande wa bustanini anakula. Tunda alifurahi sana. Akaingia chooni akajitengeneza vizuri ndipo akaelekea alipo Gabriel.
Cha Mtu,
Mavi.
A |
limkuta
Gab amekaa peke yake pale mezani lakini
kulikuwa na vinywaji vingine pale
mezani. Tunda alihisi hayupo peke
yake. “Gab!” Tunda aliita kwa upole
akitegemea Gabriel angefurahi sana
kumuona. Gabriel akasimama kama
mshale. “Naomba uondoke Nancy, hapa nipo na mke wangu. Maisha yetu ya ndoa yanaendelea vizuri. Sitaki uniharibie tafadhali. Nimetubu kwa Mungu na mke wangu nimemwambia mapungufu yake, amejirekebisha. Ndoa yetu sasa hivi ina amani. Tena hapa nipo na BF, mama yake na mke wangu. Naomba uondoke kabla hawajarudi.
Wameenda msalani. Ondoka Nancy
tafadhali.” Tunda hakuwahi kumuona
Gabriel huyu. Alikuwa amehamaki. Mkali
kama pilipili.
Kwa shida alizokuwa nazo, ikabidi ajikaze. “Nimeishiwa pesa, sina hata shilingi! Nyumba yenyewe ninayoishi wananifukuza. Pesa ya mwisho niliyokuwa nayo ndio nimekata tiketi ya kukufuata huku, hata pesa yakuchukua chumba sasa hivi hapa sina. Nitaenda wapi usiku huu na ninaona mvua inaanza? Naomba nisaidie.”Akiwa kwenye mshtuko wa kufukuzwa vibaya vile, Tunda alijikaza na kubembeleza kwa sauti ya chini tu. Lakini wazi alisikika kama anayetaka kulia.
“Kwa nini uje bila taarifa Nancy!? Hilo sio
tatizo langu. Naomba uondoke tafadhali.
Toka kabla sijakupiga.” Tunda aliumia sana, akajikuta akilia nakushindwa kujizuia pale mbele ya Gabriel.
Alikumbuka alivyofukuzwa na mama yake
bila baba Tom kumtafuta tena. Gabriel
hakuwa na tofauti ya shukurani kwa Tunda
kama baba Tom. Wote walijua
kumpamba wawapo kitandani. Aliinama na
kuficha uso wake akilia mbele ya
Gabriel, asijue anakwenda wapi usiku ule, huko arusha!? Manyunyu
yakazidi kuongezeka.
“Nimekwambia ondoka Nancy. Na usije kunitafuta tena.” Gabriel aliongea kwa ukali zaidi huku akimsogelea
Tunda kwa hasira kali sana usoni. Tunda
alishtuka sana hakuamini kama Gabriel
anaweza kupiga mwili huohuo aliokuwa
akiusifia na kumshukuru
kwa kumtuliza akiwa na matatizo
yake! Akasogea huku anaficha uso zaidi
asije akampiga usoni huku akilia na kutetemeka.
Tunda alikuwa kwenye mshtuko mkubwa
sana. Alitetemeka mpaka mwili ulionekana
ukitetemeka. Kitu kilikuwa kimemkaba
Tunda, alishindwa hata kuongea tena
ila kujinusuru asije kuishia kupigwa
pale.
Akaamua aondoke tu. Wakati anageuka ili aondoke alimuona Net amesimama pembeni
yao akiwasikiliza. Hakutaka
hata kumsalimia, kwani hakujua
amesikia mangapi. Akaondoka pale akilia
kwa uchungu na aibu. Akabaki
Net na Gabriel
wakiangaliana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
v Haya,
historia inajirudia tena kwa Tunda. Kama
alivyoondoka vibaya nyumbani kwa bibi na
babu yake, baba yake mzazi, baba Tom,
Shangazi yake, ndivyo anavyofukuzwa tena na Gabriel aliyebaki tegemeo lake
pekee.
v Anakaribia
kufukuzwa kwenye hiyo nyumba aliyokuwa
akiishi kwa kulipa kodi kwa dola, ambako
hapajulikani. Tena nyumba yenyewe imejaa
vitu vya thamani vitupu! Hana ndugu,
hana rafiki wala sehemu si ya kuhifadhi hivyo vitu vyake tu, hata yeye mwenyewe. Hana shule
kichwani, hana biashara yeyote inayoweza
kumwingizia kipato, na mbaya zaidi
safari hii hana hata pesa ya kuanza
chochote.
v Akiwa
hospitalini baada ya kufukuzwa kwa
shangazi yake nusu mfu, baba yake mzazi alimuachia pesa hospitalini
iliyomsaidia kumkutanisha na
Sadiki.
Sadiki amekufa, akamuachia hivyo vitu vyote vya thamani na pesa iliyomkutanisha na Kinny. Sasa safari hii Tunda yupo peke
yake kwenye jiji la ugenini. Hauziki
tena. Safari hii Tunda atafanyaje?
Usikose mwendelezo wakusisimua zaidi. Ndio mambo yanazidi kupamba
moto. Endelea kuwa na Tunda.
0 Comments:
Post a Comment