Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 104. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 104.

Wakaingia kwenye gari, akajituliza akiegemea kiti, akabaki akiangalia nje, Jerry anacheka na ndugu zake. Hata hakujua alimaliza saa ngapi maana alibaki akijipapasa tumbo. “Njaa imeanza kukuuma?” “Kidogo. Ila nimefurahi kuona kila kitu kipo sawa.” “Hata mimi aisee! Bro amefurahia huyo, kama Jeremi! Anasema ni hivyo Marekani kumefungwa. Lakini ungeenda kujifungulia kule kama wengine.” Tuma akacheka tu na kunyamaza.

Hilo hata halikumshitua au kumbambaisha. Walizaliwa kijijini. Bila msaada wa mtu, mdogo wake yupo Ulaya, akisoma. Alijiambia alipoandikiwa mwanae, ndipo atakapokuwa tu. Akajituliza kitini.

~~~~~~~~~~~

“Shuleni kwa watoto wamenipigia simu.” Tuma akamgeukia maana hakujua kama anazungumza naye au yupo kwenye simu tena. “Unaongea na mimi?” “Ndiyo.” “Nilijua umerudi kwenye simu.” “Hapana. Naona nikushirikishe tu. Maana mara ya kwanza niliyabeba mwenyewe yakanilemea.” Ikabidi ajiweke vizuri na kuonyesha kujali.

“Kwema?” “Wamenitaarifu kuwa Sandra amewaambia wasindelee kupokea pesa za ada kutoka kwangu, maana muhula huu ndio mwisho. Anatoa watoto kwenye ile shule.” “Anawapeleka wapi?!” “Sijui Tuma. Na sitaki kujua. Niliamua kumsaidia ada, kama haitaji tena. Basi. Afanye vile anavyotaka na hao watoto.”

“Huwezi kufanya hivyo Jerry.” “Nitafanyaje Tuma? Sitaki kurudia yale maisha ya kubishana na Sandra. Maana swali moja kwake, litaanzisha mjadala ambao nitajikuta nazungumza jambo, akaishia kuniumiza tu.” 

“Kwani mara ya mwisho kuzungumza naye ni lini?” “Nilimtafuta yule wakili na kumtuma kwake kumwambia maswala ya ada itakuwa juu yangu. Na nitalipa shuleni moja kwa moja na nitawaambia michango yeyote ile watakayotakiwa, niwe naambiwa mimi. Mengine atashugulika nayo mwenyewe. Siku ile ya birthday yangu ilikuwa siku ya mwisho kuonana naye. Sijamtafuta tena.” Tuma akabaki akifikiria.

“Jerry, kwa namna yeyote ile, wale watoto bado ni watoto wako.” “Bwana hiyo kitu inaniuma Tuma! Na sijui hata kama wanajua maana ya baba wale. Natamani niamke, Mungu awe amebadilisha.” “Sasa kwa kuwa hajabadilisha, bado ni watoto wako. Nashauri tafuta kujua ni nini kinaendelea. Kuna leo na kesho. Hutaki uje ujilaumu baadaye.” “Hakika sitajilaumu.” Tuma akabaki akimwangalia.

“Hakika tena Tuma. Hapajawahi kuwa na mahusiano kati yangu na wale watoto. Kwanza hawanihitaji kabisa. Wananiona kero. Takataka ya mwisho kabisa.” “Najua kwa sababu niliangalia ile video wakati wakikuchomea vitu vyako. Ila jua ile si akili yao. Ni vile walivyokuzwa tokea watoto. Ninauhakika, watakuja kukua, watajua ukweli wa mambo, watajutia sana.” “Sio watoto waliotoka kwa yule mwanamke. Wapo kama mama yao na wajomba zao. Hivyohivyo. Hawawezi kubadilika kwa sababu zile nitabia za asili ya kwa kina Sandra. Ubinafsi. Dharau na kujithamini nafsi zao tu.”

“Tafadhali tuache Tuma. Itanivuruga.” “Wewe sio Sandra, Jerry. Unaubinadamu na akili kuliko Sandra. Ni mawili, mpigie simu huyo wakili mnayewasiliana kupitia yeye. Mtume amuulize Sandra kinachoendelea, au mtafute Sandra mwenyewe.” “Sandra, hapana.” “Basi zungumza na huyo wakili.” Akamuona anajifikiria. Ni kweli waliachana lakini wamebaki wazazi. Japokuwa hakuwa akitaka, lakini alijua kwa hakika hataweza kukwepa. 

Katikati Ya Watoto Na Maumivu

Akamuona anapiga. “Naona umepiga na Sandra yupo hapa na vijana wenu. Alikuwa akiniachia barua na maagizo.” “Anataka nini?” “Ni sawa nikimpa simu?” Jerry alijifikiria, mpaka akakata simu bila ya kujibu. Tuma kimya. 

Akamuona anasita ni kama anayetakiwa kufanya kazi nzito sana ambayo hayupo tayari kisha ikawa kama anayeombwa atumbukie kwenye tanuru la moto. Alibadilika mpaka sura ikawa nyekundu na masikio.

Akaendelea kuendesha akiwa kwenye hiyo hali mwishoe akamuona anapiga tena. “Mpe simu.” Akapokea Sandra.

“Unaendeleaje Jerry?” “Unataka nini?” Akauliza kwa jazba. “Sikutaka kukuudhi au kukiuka mashariti…” “Sandra?” Akaita kwa ukali mpaka Tuma akashituka na kumwangalia.

“Maisha hapa yamenishida Jerry. Mahitaji ni makubwa, ada unayonisaidia kulipa ni kubwa na ninashukuru, lakini mambo mengine nakwama. Ndio nimeona ni bora niwarudishe nchini kwao ambako shule ni bure.” “Saw..” “Kabla hujakata. Nina ombi.” Kimya ila Sandra kuumia kuona hata hajali kuwa anaondoka na watoto nchini!

Ila akaendelea. “Nilikuwa nimeandika kwenye hii barua lakini kwa kuwa tunazungumza naomba unisikilize Jerry.” Kimya. Mpaka Tuma akaingiwa na huruma. Maana hiyo sauti ya Sandra ilikuwa ikitetemeka kama aliyejawa hofu, anaongea na Mungu ana kwa ana. Isingekuwa kuona video zake na wanae, angesema anasingiziwa. 

“Naomba hiyo pesa ya ada, uwe unanipa mimi ili inisaidie huko na watoto.” “Sawa.” Akajibu bila kupinga. “Na nimekwama nauli ya mtoto mmoja.” Akaongeza kwa haraka kabla ya simu kukatwa. “Sawa.” Akajibu tena Jerry kwa ufupi.

“Ungependa kuwaaga?” “Hapana! Niwaage kwani wanajua hata umuhimu wangu!?” “Wanajua Jerry!” “Acha kunisanifu na kutaka kuniharibia siku yangu bila sababu. Lakini nakuhakikishia Sandra, kwa kuwa wewe umewanyima nafasi ya kuwafundisha hao watoto nafasi yangu kwao, ipo siku dunia itawafundisha kuwa wanayemuita fala, na majina hayo ambayo kwenu mmekuwa mkiniita mbele ya watoto wangu, nao wakanitambua hivyo, itawafundisha kuwa mimi ni baba yao.”

“Wame…” “Na mpaka watakapofika hapo, ndipo nitawapa tena nafasi kwenye maisha yangu. Sitaruhusu wewe wala wao mniumize tena. Kama ulivyosema, hatujawahi kuwa na mahusiano nao, ulisema mbele ya huyo mwanasheria wananidharau, hawana kitu cha kujifunza kwangu. Sasa kwa nini utake tena nizungumze nao?” “Wewe ni…” “Ili waharibikiwe huko mnakokimbilia, uje upate sababu ya kunitangaza kuwa ni vile nilivyozungumza nao?” Hakuwa hata akimpa nafasi ya kuzungumza.

“Shida yenu si ni pesa kutoka kwangu, nitampa huyo mwanasheria, mengine ni juu yako wewe mwenyewe. Kila la kheri.” Simu ikakatwa bila ya kuzungumza na vijana wake.

~~~~~~~~~~~

“Eti nawarudisha nchini kwao! Anafikiri ni rahisi hivyo!” “Kwamba anakwenda kuishi nao Marekani?” Tuma akauliza. Akamuona anacheka kwa masikitiko akitingisha kichwa. “Mbona nimesikia akisema huko shule ni bure! Na mnasema ni nzuri?” “Nisikilize Tuma, Marekani anayoijua Sandra ni ya Jemimi.” Tuma akawa hajaelewa.

“Huyu Sandra kwenda kwake kote Marekani, tokea mwanzo, ni mimi na tunashukia kwa Jemimi. Unapomsikia kaka yake akisema wanamdekeza Jemimi, jua maisha ya Jemimi huko ni nusu ya maisha uliyoona pale nyumbani kwao.” “Acha masihara Jerry!” “Acha Tuma. Ni vile yule mtoto ni mtulivu sana, na amechagua shule, hana mambo mengi.”

“Nyumba anayoishi Jemimi kule, ni kubwa, sisi wote na familia zetu tukifika kule tunatoshea, bila kubanana. Level tatu. Ina basement yenye kila kitu mpaka sebule, jiko na vyumba vitatu. Ndiko tulikokuwa tukikaa mimi na iliyokuwa familia yangu tukifika kule. Kwamba hata tungetaka kutoonana na watu wa juu, unaweza. Haya katikati ambako ndio pakubwa sana, kuna vyumba sita, ikiwepo ofisi ya Jemimi mwenyewe anakosomea na ndipo ilipo maktaba yake ndogo. Hapo anapapenda Hilda. Mpaka pamefanyika kama kwake na familia yake.”

“Juu kabisa ndiko kwao. Bro na familia yake na ndiko kuliko chumba cha Jemimi, kaka yake, ambacho anakifunga kabisa maana yeye anaraia pacha. Marekani na Uingereza. Na kazi yake anaweza fanya popote. Anafanya online kwa asilimia 90. Analipwa pesa hiyo! Utachoka. Kwa hiyo kama hayupo hapa nchini kwa mama yake, anaweza kuwa Uingereza kutimiza hiyo asilimia 10 ya kazi iliyobaki kama kuna kikao cha ofisi ambacho pengine watamtaka awepo, vinginevyo yupo Marekani kwa dada yake. Na usifikiri ni kwa bahati mbaya, bro anaweza kumuomba akakae na dada yake kidogo.”

 “Yule binti anawafanyakazi wakumsafishia ile nyumba. Kazi yake ni shule tu. Broaliinunua ile nyumba miaka ya zamani sana kupitia Jemimi na kaka yake. Kwamba imeshalipiwa yote, ni ya Jemimi na kaka yake. Anamagari ambayo hatumii, tunatumia tukifika pale. Mtaa anaoishi, ni ule wa kitajiri, hakuna uhalifu, na shule ni bora.”

“Yule binti akikohoa kule, kila mtu huku anajua. Ni roho na nafsi ya JJ. Mama yake hivyohivyo. Hajalia shida, ameshatimiziwa. Upangiliwaji wa nyumba yake kule, kazi ya mama yake.” “Kwani yule mkewe hana kazi?” “Kazi yake ndio hiyo. Anaweza akaondoka hapa anakwambia anakwenda kutengeneza kwa Jemimi. Atafanya manunuzi na kupapangilia hapo ndani, ilimradi tu Jemimi atulie shule.”

“Kaka yake naye yupo hivyohivyo. Unavyomuona anamjali mama yake vile, na dada yake hivyohivyo. Hataacha kwenda kumuangalia na kukaa naye. Ajue uhitaji na kuutimiza. Maana Jemimi hajui kulalamika.”

“Sasa maisha yale ndio Sandra anayodhania, Marekani yote ndivyo ilivyo, maana wote wamezalia pale kwenye ile nyumba, kwenye ule mtaa ambao shule zake kweli ni bure na nzuri sana. Ila na kodi za wakazi pale zipo juu. Mtu mwenye kipato cha kawaida, hawezi kwa namna yeyote ile kuishi pale. Kwanza hakunaga apartment. Wakazi wa pale walikataa kabisa kujengwa apartment ili kuzuia watu wa hali ya chini kuhamia maeneo yale.” Tuma akazidi kushangaa.

“Sasa si atarudi kwa Jemimi!” “Ni kama useme aende kuweka kidole chake kwenye jicho la bro.” “Acha Jerry!” Jerry akacheka kwa masikitiko. “Hathubutu. Na wote tunamjua bro. Kwa Jemimi huwa haweki mazingira ya makosa. Na haruhusu, muulize yeyote yule. Anampenda yule mtoto kuliko nafsi yake. Kwanza Jemimi mwenyewe anapendeka. Mtulivu mno, kwa hiyo wote kwenye familia yao, huwa wanahakikisha kwa maneno na vitendo, yule binti hapati ghasia ya namna yeyote ile.”

“Na kwa nini unafikiri anaitwa Jemimi?” Tuma akabaki akifiria. “Bro anaitwa Jeremiah. Alipomzaa yule binti alifurahi bro, akaapa kumlinda kuliko nafsi yake. Ndipo akampa jina hilo la wa Jeremiah. Jemimi.” Ndio Tuma kuelewa sasa. 

“Sandra hatathubutu kwenda hata kuomba maji pale maana atakuwa anaomba vita vikali sana kwa bro. Inamaana, hata nikimpa pesa kiasi gani, hatamudu kuishi mazingira kama yale. Hawezi kupata shule nzuri. Kazi ya pesa nzuri anaweza asipate kwa haraka, maana hata shule yake sio kubwa kihivyo, na alichosomea ndicho wazawa wengi weupe wa kule ndicho wanachopendeleana kazi. Patamshinda tu.” Tuma akashangaa sana.

“Sasa kwa nini humshauri?!” “Kwani ugomvi wangu na yeye huwa unatoka wapi? Ni kuona sina uwezo mkubwa wa kufikiria kama yeye. Kuna alichofikiria tayari huko kichwani kwake. Akazungumza na wale kaka zake wajuaji. Wakakubaliana, ndio anakwenda. Sasa muache akakumbane na uhalisia, atajifunza tu. Na wale vijana wake! Hakika nawahurumia. Tena kipindi hichi cha baridi kule! Hakika nawaacha kabisa, sitaki kuwaingilia, pengine ni muda umefika wa ulimwengu kuwafundisha wote watatu.” Tuma akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Akajiambia ya ngoswe, anamuachia ngoswe mwenyewe.

~~~~~~~~~~~

“Nimeshaagiza chakula kiletwe ofisini.” “Ujue Jerry unapeleka haya mambo bila makubaliano, jamani!” “Lazima niingie ofisini sasahivi, Tuma. Nina oda kubwa, ambazo bila ya kuzisimamia, sitakamilisha kwa wakati. Ofisi yako ipo vilevile. Tukifika watakuletea chakula chako ofisini, unakula huku unapitia kuanzia ulipoachia. Au umechoka unataka urudi nyumbani?” “Twende tu.” Maisha ya kazi kwa hao wawili yakaanzia hapo.

Tuma Na Jaribio la Kuolewa Kwa Mara Ya Pili.

JJ akakazania swala la ndoa kwelikweli. Hakuna kulala, hakuna kupumzika, anataka kukamilisha kila kitu mpaka ndoa ndani ya muda uliobaki wa Tuma kujifungua. Tuma akamtaarifu mama yake. “Mahari ya pili tena?!” Tuma hana mbavu. “Uzuri hamdaiwi mama yangu. Wewe niwekee mazingira ya kupokea tu. Zungumza na baba.” “Naanza na mjomba wako. Yeye ndio anamuwezea baba yako.” Wakajipanga wawili hao mpaka wakaridhika.

Sandra Na Mwanzo Mpya

Baada ya kukusanya pesa zake na kuuza vitu vingi, Sandra akaiacha nchi akiwa na pesa ya kutosha, kuelekea nchini Marekani, kuanza maisha akiwa na wanae wawili. Alipata mtu aliyekuwa akifahamiana na Cory, kaka yake, akawaahidi atampokea yeye na wanae, na kuwahifadhi kwa muda wakijipanga. Hilo likakaa sawa. Waliondoka nchini kwa shangwewakiagwa kwa mashamushamu! Ndugu wakimuonea wivu kuwa angalau yeye ameweza kikimbia kibano cha JJ. 

Sandra alifika nchini Marekani, baridi haswa, yupo na vijana wake. Hawajajiandaa sana wakijua wanakuja kupokelewa na kuingia kwenye heater. Wakaanza kumpigia simu Getu, ambaye ndiye wanafikia kwake. Walipiga mpaka walichoka. Hapokei.

Mwishoe akawa hapatikani kabisa. Akaamua kumtumia ujumbe kumkumbusha maana hapo yeye na wanae wanatetemeka baridi. Walishatoka kule wanakosubiria kupanda ndege au wanakoshuka kabla hawajatoka upande wa pili wanakochukulia mizigo, ambako ukitoka, huwezi rudi ndani mpaka uwe na tiketi ya kusafiria. Ambako angalau huko ndani kuna migahawa, na sehemu nzuri hata unaweza jilaza kwenye viti vyake.

Hapo walipo milango ilikuwa ikifunguliwa kila wakati watu wakiingia na kutoka. Baridi inaingia mpaka ndani. Wamechoka na safari. Mwenyeji hapokei simu. Ndipo akatuma huo ujumbe. ‘Mimi Sandra, dada yake Cory. Tumefika, tupo uwanja wa ndege.’Ule ujumbe hata haukufika. Kwamba hayupo hewani tena au ni kwamba amefungia simu zake.

Mtoto alipolalamika vichomi sababu ya baridi, ikabidi atafute usafiri wakatafute motel. Tena akatafuta ya hali ya chini, kubania vijipesa. Ilikuwa ni kazi sana kulala hapo. Sandra na vijana wake wamezoea maisha ya hali ya juu sana. Mahoteli waliyokuwa wakifikia kwenye nchi wanazoenda kwa mapumziko, wakiwa na Jerry ni 5 stars hotels. Leo wapo kwenye motel kama vinyumba vya kulala wageni uswahilini! Si wanae tu waliokuwa wakipata shida, hata yeye mwenyewe Sandra alikuwa akiteseka.

Kwa kuwa alimwambia mwenye taksii amtafutie sehemu ya bei nafuu, na yeye akampeleka kweli kwenye mazingira duni sana. Ila angalau wakaweza kupata joto. Aliagiza chakula kwa uber eat. Wakaletewa mpaka mlangoni. Wakala na kulala huku muda wote akiangalia simu kuona kama mwenyeji wake alimtafuta.

~~~~~~~~~~~

Getu alisoma na Cory chuo kimoja kilichopo mjini New Jersey. Walipomaliza karatasi za kuwaweka nchini ziliposumbua, Cory akaamua kurudi nyumbani, yeye akaamua kupambana na maisha ya hapo nchini. Hakuwahi kurudi nyumbani japo waliendelea kuwasiliana na Cory hapa na pale. Wakaja kupotezana mpaka Cory alipompigia simu na kumuomba ampokee dada yake na watoto. Alikubali bila ya shida, lakini ndio akapotea.

Kila Mchuma Janga, Hula Na Wa Kwao

Ndicho kilichompata Sandra, akala matokeo yote na wanae. Nchi ikawapokea vibaya sana. Wasiwasi ukamuingia, atafanyaje na watoto wawili hana pakwenda! Alikaa hapo kwenye hiyo motel duni akijaribu kumtafuta huyo dada bila mafanikio. Akamtumia ujumbe mwingine akimueleza walipo mpaka namba ya chumba chao kwenye hiyo moteli. Nao huo ujumbe haukuonekana kufika.

Siku hiyo jioni wakaamua kutoka kula nje. Ila nia pia ni kupunguza garama ya kuletewa vyakula hapo hotelini na pia angalau wanyooshe miguu. 

Basi, wakapata sehemu wanauza fast food. Wanauza burgers na fries. Akaingia hapo na wanae, wakakaa. Sehemu ilikuwa duni, akakutana na wateja wengine wakamtisha kwa muonekano wao. Hakukupenda akijihisi yeye na wanae hawatakuwa salama. Akaamua asikae, waagize na kuondoka kwa haraka.

Wakati wanatoka wameshapewa chakula chao, akapishana na mtu mlangoni akampiga kikumbo kwa nguvu sana nusura aangushe chakula. Chakushangaza huyo kaka akaanza kumfoka Sandra mpaka akaribie kumpiga kuwa anatembea vipi bila kuangalia mbele! Wandani nao wakatoka hapo nje ya mlango. Wakawazunguka yeye na watoto wake, wakiwatisha na kuwazonga wasijue kumbe wanawasachi mifukoni.

Wakawatisha na kelele nyingi za kihuni, wapo kwenye mshituko na hofu hata hawajui wanachofanyiwa hapo, lakini mwishoe Sandra akafanikiwa kuponyoka na watoto wake kwa haraka, kukimbilia motelini, wajifungie. Hapakuwa mbali na hapo.

Kuja kufika ndani wakihema, kujiangalia, watoto hawana simu wala waleti zao, na Sandra hivyohivyo. Mbaya zaidi kwa Sandra waleti yake ndiyo iliyokuwa na pesa yote aliyokuwa nayo mkononi aliyokuwa amekusudia kuja kuweka kwenye benki yake ya hapo nchini, na vitambulisho vyote ikiwemo hata Green Card yake, kasoro tu, hati za kusafiria aliacha, akawa anafungia kwenye masanduku yao. 

Ulikuwa msiba mkubwa sana. Alikuwa akilia hapo, wanae wakimtizama hawajui chakufanya. Wanatokaje kwenye hiyo hali hawana hata mawasiliano!

Ndipo wakaelewa zile fujo walizotoka kufanyiwa pale, wala haikuwa kuwadhuru ila kuwachanganya macho na akili viwe kwenye utisho wanao huku wakiwasachi mifukoni na kufanikiwa kuwasafisha kabisa. 

Kumbe tokea wanaingia pale, jinsi walivyojibeba na vile walivyozungumza, lafudhiyao tu, japo walizungumza kingereza, wakajua ni wageni. Wakamuona vile Sandra anavyotoa pesa wakati akilipia chakula, ndio wakapanga mpango mzima. Mmoja akawahi kutoka akiwasubiria nje huku wenzie wakisubiri kujidai wanataka kumtetea. 

~~~~~~~~~~~

Alikuwa na hali mbaya, hajui anapeleka wapi hao watoto na atawalisha nini! Angalau walikula siku hiyo. Kesho yake Sandra hakuwa na kitu kabisa. Na hajui jinsi ya kuwasiliana tena.

~~~~~~~~~~~

Yaani siku ya tano ndio anatokea hapo motelini. Akamwambia huwa anafanya kazi ya live in. Kwamba anakwenda kwenye nyumba za kulea wazee. Anakaa hukohuko kwa siku 7, halafu anapata off siku tatu, ndipo anarudi kwake. Akamwambia amefika hapo kwa ujumbe ulioingia eti siku hiyo, baada ya kuwasha simu yake.

~~~~~~~~~~~

Sandra akajiuliza, alishindwa vipi kupokea simu yake siku ya kwanza alipofika na kwa hakika ilikuwa ikiita kabisa, kuashiria aliona. Alishindwa vipi angalau kumtaarifu hayo kwa kifupi tu, basi kama kupokea ilikuwa shida ndio kushindwa hata ujumbe! Na kwa nini alikubali kuwapokea siku aliyomwambia wangefika hapo nchini kama aliyajua yote hayo! Akahisi kuna kitu hakijakaa sawa. Lakini kwa jinsi walivyokuwa kwenye shida, akaona afunike kombe, mwanaharamu apite. Watolewe hapo motelini ambako hata pesa ya kulipia hana tena.

~~~~~~~~~~~

Ikabidi kumkopa pesa kumalizia malipo ya hapo kwa siku walizolala. Wazi alionekana kutokufurahia hilo. Akalalamika kwa mengi, Sandra na vijana wake wakimsikiliza, lakini mwishoe akamkopesha. “Nitaihitaji pesa yangu kwa haraka sana.” Akaweka msisitizo. Akawalipia hapo na kuwachukua na gari yake. Kwanza ilikuwa imechoka, huwezi amini alisoma na Cory hapo nchini na ana shahada ya mbili.

Safari ya kwake hapakuwa mbali na hiyo mitaa. Ukiangalia tu, sio salama. Ila akamwambia anapenda hapo, sio garama. Ilikuwa ni apartment ya chumba kimoja tu. Choo na bafu humohumo, jiko na sehemu ya kulia chakula vipo sehemu moja. Padogo tu. Na sebule. Kwa mtu mmoja inatosha, lakini sio kumuongeza Sandra na wanae.

~~~~~~~~~~~

“Jamani hapa ni padogo kama mnavyopaona, kwa hiyo usafi ni lazima. Mimi sipendi sehemu chafu kabisa.” Akaanza mashariti. Akaweka mashariti mengi, ungejua ametoa msaada ambao ni zaidi ya uwezo wake.

Maisha ya hapo yakaanza. Dada ni mkali, hataki kelele, hataki uchafu hata tone la maji juu ya sinki ni uchafu. Watoto wa Sandra hawajui kazi, hawajui kujitumikia. Yaani siku ileile ya kwanza, kikaumana. 

Akawakalisha tena wote watatu na kuanza kuwakaripia kama watoto wadogo. Bwana dada aliongea huyo! Hana aibu, hamna ugeni. Aisee ilikuwa mbaya sana mpaka Sandra alipokwenda bafuni kuoga, akajikuta akilia sana. Hana jinsi ya kutoka hapo. Anamtegemea huyo dada ndio amsaidie kwa kila kitu.

~~~~~~~~~~~

Wanasema, mgeni njoo, mwenyeji apone. Getu akaponea hapohapo. Bila kumumunya maneno wala kupoteza muda, akawagawia majukumu Sandra na wanae. Akawaonyesha sehemu vilipo vifaa vya usafi na mashine yake ya kufulia iliyounganika na mashine ya kukaushia juu yake. 

Anataka kila aliyempa kazi yake ahakakikishe ni kamilifu wakati wote. Friji iwe imepangiliwa, ambayo ilikuwa kazi ya Brian, kiziwanda wa Sandra ambaye kwao alikuwa akifuatwa na chakula popote alipo, akimaliza basi dada afuate sahani na alichotumia. Iwe uma na kisu, au uma tu, na glasi. Yeye hatajigusa na wala hatashukuru ila kukosoa kwa ukali sana, akiwafoka wadada wa kazi wa hapo kwao.

Basi huyo Brian akaambiwa, friji, ndani na nje, iwe safi wakati wote. Hapo nje ya huyo friji asikute alama ya vidole hata mara moja. Mchana na usiku iwe safi. Kaunta za jikoni ziwe safi na kavu wakati wote, pamoja na meza yake ndogo ya kioo ya kulia chakula. 

Sandra kusugua bafu na choo. Kuwe kukavu wakati wote. Anayetoka kuoga, basi akaushe mpaka ukuta. Na usafi mpaka chumbani kwake maana wao aliwapa sebuleni. Wanalaza godoro sebuleni, analala na wanae.

Na wakiamka tu, basi Bright, kijana mkubwa, ahakikishe godoro linarudi na kupangwa vizuri chumbani kwa Getu, sebule inakuwa safi wakati wote. Getu hataki kukanyaga mchanga hata kidogo. Na anatembea bila hata soski, sakafu yake anawax na dawa maalumu. 

Hiyo ikawa kazi ya Bright kijana mkubwa wa Sandra aliyekuwa na jukumu moja tu huko kwao, shule. Mpaka kitanda alikuwa akitandikiwa na dada wa kazi. Ilikuwa Bright akitoka shule, anaposimama kuvua nguo, atatoa mpaka boksa hapohapo, anaruka na kuingia bafuni kuoga. Akimaliza kujikausha, basi taulo nalo ni popote litakapotua, dada ataingia chumbani kwake kurekebisha na kuwe kusafi wakati wote, Sandra hakuwa akipenda uchafu nyumbani kwake, kama huyo Getu. 

Sasa kibao kikageuzwa. Na Bright naye ilikuwa pia kufua. Na anafua nguo zote mpaka mashuka, kwa rangi akama alivyomfundisha Getu, hakuna kuchanganya. Sasa amkute anafua, amechanganya nguo kwa rangi tofautitofauti! Hutapenda kuwepo hapo.Getu hacheki na kima. Kila kitu chake anataka kibakie kilivyo, sio kuhamia kwao hapo, iwe kero kwake.

Mwalimu Dunia bado yupo darasani, somo linaendelea…

Mwalimu dunia akawa anaendeleza shule, hajamalizana nao wala hajafika katikati ya somo. Mitihani yake ni migumu na niya kila kukicha, hana muda wa maandalizi.Manyanyaso ya chakula pia yakawepo. Dada anakwenda kwa bajeti, sio kula kwa kumlemea. Sandra akawa akimbembeleza amsindikize akafuatilie vitambulisho vyake, ili aweze kupata kadi ya benki ili asaidie chakula, wanae wale washibe. Napo ikawa shida. Getu anamsema kuwa anaendekeza watoto. Hawafundishi bajeti. Anataka aache kazi zake afuatishe ratiba zake na wanae, hana muda huo. Ila atahitaji kulipwa hiyo ya chakula, asubirie.

Ikawa kuvutana na kubembelezana. Sandra akijua, akipata tu uwezo wa kufika benki, hapo amejikomboa. Atapata hiyo anayomdai, na ya ziada. Lakini Getu anamzungusha huku akiendelea kumdai kuanzia ile aliyomlipia moteli, na garama zao za kuishi humo.

Ukali wa kugomba kupitiliza kuwa nyumba yake haipo sawa ukazidi. Wale watoto wakawa wakishuhudia vile mama yao akitukanwa kama wasichana wa kazi waliokuwa wakiwafanyia wao kazi, kule nyumbani kwao. Anamgomba ni kwa nini ameshindwa kufanya hiki na kile wakati alikuwepo tu hapo. Anaongea akiingia na kutoka akisema watamlemea kama wanashindwa kuchangamka. Maisha ya hapo si kama nyumbani. Ilimradi tu.

Ile hali ikawa kama imemuathiri Sandra. Amekwama mahali, hajui anatokaje. Hana pesa, hana kitambulisho chochote kwa jina lake, hana usafiri wa kumtoa hapo kumpeleka popote. Huyo dada hakuwa na internet nyumbani kwake alishawaambia haishi hapo siku nyingi kwa hiyo, ni garama ambayo hakuwa tayari kuingia.

Maisha yakaendelea hapo, anaondoka hapo na kupotea hata siku 6 bila ya kuacha chakula cha kueleweka kwa Sandra na wanae, na hakumpeleka Sandra popote, nje ni baridi, hawezi toka kuzunguka kutafuta kituo cha polisi kuandikisha ripoti. Wakakwamahumo ndani kama wapo sayari ya mwisho au kwenye kisiwa kisicho na mawasiliano na yeyote. Hali ikazidi kuwa mbaya.

~~~~~~~~~~~

 Siku na hiyo Getu akarudi hapo nyumbani akamwambia Sandra amekwama, bili ya umeme ni kubwa na pesa ya pango haijatimia, inabidi kufuatilia pesa zake benki. Zikawa habari njema Sandra akijua atatoa pesa ya kutosha, hata ajikomboe, atoke hapo.

Wakatoka hapo akitaka watoto wabaki wafanye kazi, wasifuatane nao. Ikamuumasana Sandra, maana alishawaambia wanae watatoka wote angalau kuosha macho, maana walikaa sana ndani ambako wanatumika wakifokwa kwa kila jambo hata wanalopatia. Alipokataa mwenye nyumba na gari, akazidi kung’ata meno, akivumilia akijua wanakaribia kufika mwisho. 

~~~~~~~~~~~

Akamfikisha kituo cha polisi kuandikisha kesi ya kuibiwa vitambulisho vyake. Alipokuwa akitaja alivyoibiwa, Getu akisikiliza, moja wapo ikawa ni Green Card. Wivu ukaanza kumsumbua Getu. Yeye anasota hapo nchini, hana karatasi kama huyo Sandra, yaani yeye anakuja tu, anaweza ingia popote na kuchukua chochote! Roho yake ikamchukia kabisa Sandra kama Sandra alivyokuwa akichukia yeyote anayempita.

~~~~~~~~~~~

Kumbuka chuki yake kwa Pam, pale Pam alipoanzana na Mill, akampa gari na kubadilisha maisha! Pam akaanza kuvaa vya thamani ikamuuma kabisa Sandra mpaka kumfunga jela na kumpokonya gari. Wahenga husema, what goes around, comes around. Basi kipimo kilekile kikampata Getu, ila sasa chake kikawa chakushindiliwa. Akaapa kumkomoa.

~~~~~~~~~~~

Akiwa na barua ya polisi, kituo cha pili alichosisitiza Getu kikawa benki. Getu akamwambia kiasi cha pesa anachomdai, mpaka Sandra akashangaa. Na pia akatakaamsaidie pesa ya pango. Na hapo Sandra akajikaza. Akatoa hiyo pesa na pesa ingine nyingi akikusudia kesho yake akiondoka kwenda huko kazini, yeye na wanae wahame hapo, hata warudi hotelini kwa muda na kuhama mji kabisa. Getu anamwangalia kwa siri mapesa anayotoa, kimya.

Akatoka hapo na kwenda kufanya manunuzi ya vyakula hapo nyumbani, tena kwa kumlazimisha Sandra. Bwana alinunua mpaka sabuni za kufulia na kuogea! Walifanya manunuzi hayajawahi fanyika tokea wafike kwenye hiyo nyumba. Getu anafanya kuvuta tu, na kuweka kwenye cart kubwa ya supermarket. Wakatoka hapo wamejaza gari.

Alipomuomba apitie kumsaidia simu angalau apate mawasiliano, akamkatalia akisema amechoka, watafanya wakati mwingine. Na hapo hataki Sandra aguse simu yake kabisa. Sandra na wanae wakawa kama wapo kisiwa cha miaka ya mwanzo ya 90, mawasiliano ya shida.

~~~~~~~~~~~

Huyo Sandra na wanae masanduku yao walipewa kajiupande kadogo kwenye closetya Getu, chumbani kwake. Tena wakifungua, wakimaliza kutoa wanachotaka, walitakiwa warudishie kwenye kona yake, sio yazagae hapo kwenye closet.

Walirudi jioni, basi kwa kuwa Sandra alinunua vyakula kwa pesa yake, jioni hiyo akawapikia wanae kwa uhuru. Akapika chakula kingi tu chakuwatosha. Getu akiwaangalia tu. Wakala na kusafisha hapo, wakato godoro lao, baada ya kujisafi, basi akajilaza hapo na wanae. Kimya, Getu hataki kelele ili apate mapumziko yakutosha.

~~~~~~~~~~~

Alfajiri na mapema, walimsikia alipokuwa amemka na kujiandaa, wakajua anatoka. Wote wakafurahia. Maana, paka akitoka, panya hutawala. Akafanya yake kwa uhuru, wala haofii kuamsha waliolala hapo sebuleni. Akamaliza na kutoka.

Wakarudi kulala mpaka kwenye saa nne. Hakuna wakuwakera. Wakaamka na kula kwa uhuru. Vyakula si vipo bwana! Mama amefanya anunuzi ya kitajiri siku iliyopita, wakapata kifungua kinywa cha kukumbushia enzi. Akawaambia wanae mpango wake wakuondoka hapo.

Bwana watoto walifurahi hao. Wakaambiana hata wakipata sehemu ndogo kama hiyo, ni bora kuliko kuendelea kunyanyaswa hapo. Harakahara wakaoga na kukusanya kila kitu kilicho chao, tayari kuondoka. Sandra kuangalia pochi, hakuna hata harufu ya pesa. Getu alikomba pesa yote, na kuondoka. Walimsikia mama yao akilia huko kwenye closet kama amechinjwa. Walitaka kukimbia darasa, lakini mwalimu dunia akawaambia, bado shule haijaisha. Darasa linaendelea.

~~~~~~~~~~~

Siku walipozidiwa na njaa, Getu hajarudi zaidi ya majuma mawili, akajua wanae watakufa kwa njaa. Akawaacha watoto, yeye akatoka akiwa amejisitiri kwenda kusaka benki, akachukue tena pesa maana sanduku la barua, kuona kama benki ilishamtumia kadi yake, hawezi kufungua, funguo anayo Getu. 

Akatoka, barafu inamwagika, Sandra hana buti za barafu wala koti zito la baridi ya aina hiyo, Getu aliahidi angemsindikiza wakanunue, lakini ndio amepotea. Akiwa anatembea umbali mrefu bila ya kuona mtu, gari ya polisi ikasimama pembeni yake. Alilia Sandra polisi wasijue jinsi ya kumsaidia.

Wakampeleka kituoni ndipo akajieleza, wakamsaidia kumsindikiza benki, akafanikiwa kuchukua pesa chache zilizokuwa zimebakia. Hao polisi wakamsindikiza tena mpaka supermarket. Wakamuacha hapo akifanya manunuzi.

Akanunua vyakula na ndipo alipotafuta usafiri wa kurudi kwa Getu. Baridi ikiwa imeshampiga, mbavu zinambana. Akajikaza na kuwapikia wanae, yeye alishindwa hata kula. Akaoga maji ya moto sana. Akatoa godoro akaliweka hapo sebuleni anapolala na wanae, akalala wanae wakimuangalia kwa hofu. Maana alikuwa akihema vibaya!

                                    ~~~~~~~~~~~

Inaendelea…

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment