Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Love At First Sight - Sehemu ya 79. - Naomi Simulizi

Love At First Sight - Sehemu ya 79.

“Yule mchungaji aliyetufungisha ndoa, unamkumbuka?” “Nilikuwa na furaha siku ile, hata sikumtilia maanani.” “Nilikuona.” Mill akaanza kucheka. “Nilikuwa siwezi kukaa! Zilikuwa ndoto ambazo hata sikuwa natarajia siku ile kama zingetimia! Ulifanya siri, sikuwa hata nahisi! Sasa kuja kuona kitu kizuri vile! Mpaka bibi na babu walikuwepo! Nilikuwa na furaha ya kupitiliza. Sikumbuki huwa na furahia ya namna ile maishani! Halafu eti ule usiku ukaisha vibaya kuliko siku zote tulizowahi kuwa nazo mimi na wewe!” “Sasa huko usirudi. Tuendelee kuanzia hapa.”

Akajaribu kutulia. “Niangalie, kuna habari njema zaidi. Acha kurudisha mawazo kule. Tumetoka huko na tumetoka salama na watoto wetu wote. Tulia.” Pam akavuta pumzi kwa nguvu na kurudisha mawazo pale. “Nilimuomba vile vyeti vyetu vya ndoa vikamilike kwa haraka kwa sababu nilikuwa nimeshazungumza na mwanasheria wangu wa Marekani, juu ya sisi kuondoka hapa nchini.” Pam akajikuta mpaka anakaa.

“Tulia sasa!” “Sijategemea!” “Bado. Subiri kwanza. Kwa hili lililotokea kwenye fungate shetani anaweza akawa alitaka kulitumia vibaya, lakini acha nikwambie ukweli.” Akamuona anacheka.

“Nini?” “Niliingiwa hofu Pam! Nikajilaumu sana. Wewe ulikuwa unasema umeua mtoto! Sasa mimi ndio ilikuwa mbaya zaidi. Siku ile umekimbizwa hospitalini, wakafanikiwa kukufanya ukalala, watu wote wakaondoka karibu panapambazuka, nikaachwa peke yangu, nilikuwa na hukumu, kifua kimejaa hofu na majuto ya kupitiliza siwezi tulia. Nilikuwa peke yangu pale chumbani, wewe umelala huna habari, chumba kimetulia, nasikia tu mapigo ya moyo ya mtoto kutoka kwenye mashine. Nikajikuta nimepiga magoti mimi mwenyewe, hakika nililia mbele za Mungu.” “Pole Mill.” Akacheka akifikiria kwa muda.

Anyways, nikajikuta natubu mimi binafsi na kwa niaba yako kama yule mchungaji alivyotufundisha siku ile ya harusi. Unakumbuka?” “Pale nilikuwa naona ananipotezea muda tu.” Mill alicheka sana. “Alifundisha kitu kizuri sana, usiku uleule nikakifanyia kazi. Nikafanya kama alivyosema kuchukua nafasi yangu kama kichwa cha familia.”

“Nikamuomba Mungu msamaha kwamba usiku wa kwanza tu kukabidhiwa jukumu, nimeharibuAnisamehe, anisaidie kuniwezesha, akulinde wewe, huyo mtoto na Shema. Huwa siombagi sana, ila ile siku aisee nilishindwa kulala. Mpaka nikasema Mungu alimtuma yule mchungaji kutufungisha ndoa, lakini ni kama aliniandaa kwa usiku ule. Hata leo nimezungumza naye sana.” “Yule mchungaji?!” “Kabisa. Nimejiona ni kama Mungu alimleta kwenye maisha yangu kwa makusudi. Ni baba mzuri kwakweli. Tuache hapo.”

“Namshukuru Mungu ni kama akawa amenijibu kwa haraka, nikawa najisikia amani, halafu nikashangaa ile damu kukata kabisa mpaka madaktari wakawa wanashangaa!” “Nilikuona kila wakati unanichungulia, silali!” Mill alicheka sana.

“Nilikuwa nathibitisha muujiza wangu! Nilikuwa kama siamini tena!  Ila naona Mungu anataka kuutumia ule ujinga wang..” “Sema wangu mimi.” “Hapana Pam. Nili overreact. Sikupaswa kukutisha kwa kiasi kile.” “Hiki kichwa kilihitaji aina ile ya maonyo.” Mill alicheka mpaka machozi.

“Mimi sikutanii bwana! Sikuwa najua kama nakuumiza kwa kiasi kile! Sema tu ujinga wangu.” “Basi niseme ujinga wetu. Mungu anataka kuutumia kwa wema.” Pam akakaa sawa asielewe lile tukio baya vile Mungu anatakaje kulibadilisha.

“Ehe!?” “Nyinyi watanzania si mmefungiwa kuingia nchini Marekani?” Pam alicheka, alicheka sana. “Mill wewe!” “Mna mambo mengi sana bwana! Na mbali ya hivyo, Uhamiaji kule hawafanyii kazi jambo lolote lakutoka hapa nchini kwenu. Sasa yule mwanasheria alikuwa akisubiria vile vyeti vya ndoa ili tu kujaribisha kuona kama tunaweza pata VISA yako wewe uweze kuingia na sisi.”

“Sasa siku ya jumanne akanitafuta nikawa nipo busy mpaka nikaja kumrudishia simu yake ilishakuwa jioni ndio nikamwambia anisamehe nimeshindwa kupokea simu zake, wewe upo hospitalini ulipata complications,  umelazwa.”

“Sasa, eti yeye akaona tushikie hapohapo. Maana wamarekani wamesema mtaingiakule kukiwa na sababu maalumu. Yeye yule mwanasheria anaona tutumie huo ugonjwa, na vyeti vya hospitalini vinavyotaka upate bedrest. Ataweka hoja kuwa, mimi ni lazima nirudi nchini Marekani, na wewe unahitaji msaada wangu kwa asilimia 100. Ukiwa mgonjwa na Shema pia. Ametupa pole lakini anasema tatizo letu limemrahisishia sana.” Wakacheka.

 “Kwa hiyo jioni hii nimemtumia vyeti vyetu vya ndoa, vipimo vyako vyote na mtotoambaye ni kama mmarekani.” “Subiri kwanza Mill! Huyu mtoto ambaye bado hajazaliwa!?” “Yaani huyo hata akizaliwa hapa nchini kwenu, siku inayofuata nikampeleka pale ubalozi wa Marekani, wanachukua taarifa zake, anakuwa ameshakuwa mmarekani na watanipa hati yake ya kusafiria, ambacho ni kitambulisho chake kinachomtambulisha kuwa yeye ni Mmarekani. Passport atakayopewa  inakuwa kama hii yangu na ya Shema, haraka sana tena bila maswali. Yaani hapo umenibebea mmarekani wangu. Ni wewe tu.” Pam akazidi kufurahi.

“Colins na madaktari wa pale wamenipa kila kitu kitakachohitajika kukusaidia kuonyesha unahitajika uangalizi wa karibu ili kukuombea uruhusiwe uingie kule kwa haraka.” “Na tusipofanikiwa?” “Hatutakuwa na chakupoteza kwa sasa. Muhimu tupo wote.” “Hutaondoka? Maana huyo raisi wenu bado yupo madarakani kwa muda mrefu!”

“Umepatia. Ni miaka minne tu, ataondoka, na pengine mambo yatabadilika. Tunabakia palepale, wewe tu ndio utakuwa huna uraia, ila mimi na wanao itakuwa rahisi. Ukiendelea hivi na pale kwa kina Colins nikaona wanaweza kukusaidia vizuri kama hivi, tutabaki hivi mpaka ujifungue, mtoto nitampeleka wampe uraia wake. Muda ukivuta, lazima mimi niende nikafungue biashara..” “Mill!” Hapo akamshitua na kupoteza furaha yote.

“Nitarudi Pam. Nitarudi mpenzi. Hii pesa tunatengeneza hapa si pesa, mama. Naenda tu kuanza, na safari hii nitakuwa nikirudi mpaka nchi ifunguke nije kukuchukua.” Pam akakosa raha kabisa.

“Pam, utakuwa na watoto wangu wawili. Sina sababu ya…” “Bora tuwe na pesa kidogo, ila tubakie wote Mill. Hivyo mimi vimenitia hofu.” “Basi tusiongelee hayo, tubakie na mipango ya kuwa pamoja.” Akamuona ametulia. 

“Jua nishatuma kila kitu mpaka cheti chetu cha ndoa. Nishajaza nyaraka zote za uhamiaji na kutuma barua ya maombi kuomba uwepo kule kwa uangalizi mzuri ili mtoto wangu azaliwe salama na wewe usidhurike. Tusubirie huku tukimuomba Mungu.” “Nina wasiwasi Mill.” “Mimi ndio nimekuingizia wasiwasi. Usiwaze kutengana ila angalia hili nililokamilisha leo. Sawa?” Akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Mill akajinyanyua kuanza kupata kissKissing zikaendelea mpaka akamuona ametulia kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa nina jambo jingine ambalo nataka ushauri wako.” Akatoka kitandani na kufuata laptop yake. “Unakumbuka nilikwambia nilikuwa nikitafuta nyumba?” “Nakumbuka.” “Jo, amefanikiwa kubadili mawazo yangu. Wanaonekana wazo la kubakia hapa nchini wastaafie hapa, kwa hali ilivyo sasa, hata watoto wao hawana amani tena. Wanaonekana wanaondoka hapa nchini.” Pam akaanza kumuhurumia mama yake akikumbuka kilichotokea. 

“Dada yake na mumewe wataondoka kwa haraka, afya zinasumbua, yeye anaonekana ameshajiingiza kwenye penzi la Dorothy.” Pam akacheka jinsi alivyosema. “Mama yako mkwe ujue!” “Mwenyewe anamuita hivyo. Na akimtamka, utafikiri kapata kabinti kadogoooo! Bwana anampenda Dorothy huyo!” “Kweli Mill!?” “Utajua kwa jinsi anavyomzungumzia.” “Ila sasa mbona leo imekuwa hivyo?” Akamsimulia kile alichosimuliwa na mama yake. Mill akawa kama hajaelewa.

“Sijui kilichotokea au kinachoendelea kwa Jo, ila kwa hakika najua anampendamama yako. Na si ya kuigiza, ni ile anayomjali kutoka moyoni. Nimemuangalia hata siku ile ya harusi, nilikuwa nao ukumbini kabla wewe hujafika, niliwaona wakiwa pamoja. Hata jinsi anavyomwangalia, utajua anampenda kwa dhati.” “Mmmh!” Pam akazidi kuchanganyikiwa asielewe.

“Tuendelee na yetu.” Akataka arudishe mawazo pale. “Upo mji kule anasema wamejijenga sana ndio kama familia yao nzima ipo hapo kwenye huo mji. Amenishawishina sisi tuhamie huko sababu ya kuwa nao pamoja, wasaidie kulea wajukuu.” “Hawa watoto wetu?” “Utaona umuhimu wake ukifika kule. Kuna kajiupweke fulani hivi, na ubusy wa maisha, watu wakaribu wanaongeza ladha yake.”

“Ila sasa mimi wasiwasi wangu ukawa kwenye huo mji wao, ni wa matajiri sana, kwa biashara ninayotaka kuanzisha nikahisi kama naweza nisifanikiwe. Ikabidi niwe muwazi kwake. Aisee jamaa anaakili ya hiyo biashara! Sasa sijui kwa sababu alikuwa daktari! Ameniambia ataniunganisha na watu, watakao nisaidia kuniletea wateja, bila kutangaza.”

Amenitia moyo na kunipanua mawazo mpaka amenitia morari na kunifanya nijisikie sikuwa nimefikiria biashara kwa ukubwa. Na amesema atakuwa akinisaidia hata nikitaka nimuweke kwenye bodi ya hiyo kampuni ili kuongeza ujasiri kwa watu wa kule, maana yeye alishakuwa daktari, ashawatibu, itasaidia sana.” “Hongera Mill!”

“Ila sasa kingine, kazi ya kutafuta nyumba ikaanza tena upya, ili kuhamia kwenye huo mji ambao wao wapo. Mtoto wa kike wa dada yake anakampuni kubwa sana ya Real estate. Wanahusika na kuuza, kununua viwanja na majengo. Akaniunganisha naye. Amenitumia baadhii ya nyumba ambazo zipo sokoni maeneo hayo anasema karibu na wazazi wake na huyo Jo.” Pam akashangaa sana.

“Mill, unapeleka mambo kwa haraka!” “Sana. Sitaki kuzembea Pam. Mungu akikutanisha na watu kama hawa kina Jo, kwa kule, si jambo dogo. Aina ya milango atakayonisaidia kufungua, na aina ya watu atakao nikutanisha nao, mimi mwenyewe ingenichukua muda mrefu sana kuwafikia, au pengine hata nisingeweza kuwafikiakabisa.”

“Ila nimemwambia akiwa ananisaidia kule, itakuwa ni ajira ambayo nitakuwa nikimlipa. Alicheka sana. Ila ameniambia nisiwe na wasiwasi, watanisaidia.” “Na nani?” “Madaktari wenzie.” Akakaa sawa. Akaona mambo yanazidi kuiva.

“Angalia hizi nyumba, bila kujali bei. Ila vile itakavyokupendeza macho.” “Nisipojali bei, utapata wapi pesa?” “Nimeshajipanga. Na tukiwa na nyumba hivi. Tena nikakuweka kwenye hiyo nyumba. Maana ameahidi atanisaidia kila kitu. Sihitaji kuwepo pale. Ila karatasi amesema lazima atanitumia tuziweke saini sisi wawili.” “Kwamba na mimi nipo?” “Kabisa. Wewe mke wangu. Sasahivi chochote ninachonunua kule, lazima na wewe uwepo, wajue hatudanganyi, na itaturahisishia kukupa na wewe VISA kirahisi. Usiharakishe. Pata muda hata kesho, pitia hizo nyumba zote kwa utulivu, utakayopenda utaniambia.” Pam akaanza kucheka.

“Hivi wewe Mill unanitania au?” “Kwa nini sasa?” “Wewe unataka kupoteza muda tu. Ushasahau uliponikuta na mwanao?” Mill akamuelewa nakuanza kucheka. “Kuanzia hapa Dar na kule kwa kina bibi, aina ya nyumba tulizokuwa tukiishi uliziona. Halafu eti leo unataka nichague nyumba Marekani! Kama si kunitania ni nini?” Mill alikuwa akicheka hana mbavu. 

“Hapa ninapoishi sasahivi mwenywe najiona nipo Marekani tayari!” Akarudisha macho kwenye laptop. “Majumba yote haya mwenzio naona miujiza mitupu, halafu unaniambie nichague moja kama si kutaka kunipa shuguli nisiyoweza ni nini!” “Haya mama, hizo zenye alama za moyo ndizoo nimezipenda. Sasa angalia kama kuna moja imekuvutia zaidi. Zote zipo sehemu moja na shule nzuri.” “Wewe chagua, umtumie. Mimi sina hata uelewa bwana. Hapa ninafuraha kupitiliza. Eti Pam naye anakuwa amenunua nyumba Marekani!” Mill alicheka, alicheka hakutegemea akili ya mkewe ilipokwenda.

“Pam mie?” “Eeeh!” “Acha masihara. Wewe chagua hapa, watutumie karatasi, niweke saini huku unanipiga picha au unichukue video kabisa.” Alicheka, alicheka mpaka machozi. “Usinitanie kabisa! Wewe hizi ndoto huku hazioteki.” Angalau kwa mara nyingine tena huo usiku wakafanikiwa kurudisha cheko walilolipoteza kwa miaka mingi sana. Kukawa na ujasiri wa kuwa wapo pamoja na wamehalalishwa. Wanazungumzia vyao.

~~~~~~~~~~~~~~

Mill!” Walishatulia kwa usingizi. “Bado sijalala. Unataka nini?” “Kutokana na mambo yalivyokwenda sivyo kati ya mama na Jo, leo, nikamuhurumia mama. Maana Jo aliwaalika kina bibi waende kwake. Wakampigia simu kutaka kujua muda wakwenda, ndio nikaawaambia waje hapa kwa sababu mimi nimepewa mapumziko. Samahani sikukwambia. Ni jambo lililonijia kwa haraka nikaona niwakaribishe hapa ili kumsitiri mama.”

“Mambo mawili. Unatakiwa mapumziko Pam, nani atawapikia chakula hapa? Maana sitataka uanze kuzunguka siku nzima hapa kwa ugeni usio haraka?” “Nitazungumza na Kamila anisaidie hata kutafuta mtu wa kuja kutupikia.” “Hapo umefikiria vizuri.” “Kwa hiyo huna shida ya wao kuja hapa?” “Hata kidogo! Kwa nini?” “Unajua ndugu zangu. Watakuja kujazana hapa, na itakuwa kelele siku nzima. Ukashindwa kupumzika.” “Haina shida kabisa. Ni hivyo tu mlibadilisha, lakini ilikuwa tukakutane kwa Jo wote. Aliniomba rasmi na sisi tuwepo.”

“Ila jambo la pili yule msichana wa kazi anatarajia kufika hapa kesho. Mjomba ndio alitakiwa kwenda kumpokea. Sasa kama atakuwa hapa kuanzia asubuhi, itakuaje? Maana tunamuhitaji huyo msichana Pam. Atatusaidia sana. Hii tabia ya Shema akitoka shule anaanza kukuita akiingia tu mlangoni!” Pam akaanza kucheka.

 “Leo nimemfundisha kujifanyia mambo yake nikiwa nimekaa hapahapa kitandani. Anakwenda na kurudi mpaka njaa zake zikaisha. Na kuhusu mjomba usiwe na wasiwasi, atajipanga. Hilo halina shida.” “Basi hamna neno. Na uwe huru tu sio mpaka uwe unaomba ruhusa kukaribisha ndugu zako. Wakaribishe na wajisikie nyumbani. Na hivi mama naye yupo hapahapa, watakuwa wakiua ndege wawili kwa jiwe moja.” “Nashukuru. Hao watu wamenibeba mimi na Shema! Haswa bibi na babu! Tena bila kulalamika ila kutukumbatia huku wakilaumiwa haswa. Nimefurahi angalau na wenyewe wameshuhudia na sisi tumepata kwetu.” Mill akatulia akifikiria.

Hakuna anayetoa kumzidi Mungu

Ujumbe ukaingia kutoka kwa mama yake wakati wanakaribia kupotelea usingizini. ‘Samahani najua huu muda si mzuri, lakini usitafute chakula. Kesho mapema tu, kitaletwa chakutosha. Kwa hiyo wakina Komba uwapigie kuwakaribisha tu, sio kuomba chakula. Na acha umbea, maswali mengine kesho. Lala.’ Pam akaanza kucheka maana alishataka kumuuliza kinaletwa na nani.

“Ni nini? Mbona unacheka?” “Mama ananijulia! Ila amesema chakula kitaletwa kesho, nisimuombe tena Kamila.” Mill akashangaa kidogo. “Anapata wapi chakula?” “Ndio ameniambia niache umbea, maswali yote hayo kesho.” Wakacheka na kulala.

Jumamosi.

Asubuhi akiwa anajiandaa ili ahamie kwa Pam, akapokea simu kutoka kwa mama yake. Wakasalimiana na kwenda moja kwa moja kwa alichompigia. “Asubuhi hii Eric amepiga simu.” Kimya akisikiliza. “Alidhania tupo pamoja.” Bibi mtu akaendelea. “Alitaka kuja kutusalimia na familia yake. Lakini nikamwambia kwanza wewe haupo hapa. Pili, leo wote tunakutana nyumbani kwa Pam. Tutashinda hukohuko. Nikamwambia hata cha mchana tunakula hukohuko. Hapa hatutakuwepo.” Kimya.

“Mama Eric?” “Nipo mama. Nakusikiliza.” “Ndio nikamwambia hapa hapatakuwa na mtu, nyumba nzima ya mjomba wake nao wanaelekea kwa Pam. Leo watu wamefurahia hakuna kupika.” Bibi mtu akaendelea kama kuna jambo anasita kusema.

“Ila mjomba wake akamwambia yeye atakuwepo hapa mpaka muda wa kwenda kumpokea msichana wa kazi wa Pam, ndipo ataungana nasi akiwa na huyo msichana wa kazi.” Kimya. “Mama Eric?” “Nakusikiliza mama.” “Ndio amemwambia mjomba wake yeye anaweza kwenda kumpokea huyo msichana wa kazi akamleta hapo kwa Pam.” “Ukamwambia nini?!”  Akauliza kwa mshituko.

“Maana ujue huyu Pam anatakiwa kupumzika, mama. Na wewe unawajua hawa wawili hawaivi. Unataka kuja kuanzisha fujo kwenye familia ya watu, tumtibue baba Shema anayelinda huyo mtoto kama mboni ya jicho lake. Hataki mkewe hata atoke kitandani! Na wewe unajua kabisa, mara ya mwisho hawa wawili walipigana hadharani.” “Nimemwambia katika hilo asubiri nizungumze na wewe kwanza.”

“Mimi naona kaka akamchukue tu huyo msichana yeye mwenyewe, Eric aachwe.” “Mtoto akinyea mkono huukati, Dorothy. Unanisikia?” Mama yake akaanza. “Huyu Eric anaonekana kwa mara ya kwanza anataka kujirudi.” “Anajirudi sasahivi akishaona mambo yametulia, hataombwa msaada ndio anarudi kuja kuharibu tena? Huyu mtoto hana tofauti na baba yake, mama. Tabia zao ni sawasawa. Anasubiria kwenye utulivu na amani ndipo anaingia ili aharibu. Sio mtengenezaji na hawezi mahusiano. Alimnawa dada yake mikono. Alimuacha Pam gerezani! Leo anakuja kumalizia msaada ambao hajautendea kazi, iwe kumleta tu hapa na kuanzisha vurugu.”

“Babu yake alimuuliza hivyohivyo kuwa, anataka kutufuata kwa Pam aliyemnawia mikono, na kumuacha gerezani! Akachukua maneno ya mtu baki na kuyaamini, akashindwa kumuamini dada yake, akamtangaza wizi usio wa kweli! Akasema alikosa, anataka kutengeneza.” “Mbona asitengeneze wakati wote huo iwe leo?” Mama mtu akaendelea kuuliza kwa hasira zaidi.

“Baba yako naye akamuuliza hivyohivyo. Anasema alikutana na Pam benki, akamuomba wazungumze. Pam akampa siku, na sehemu. Kufika hiyo sehemu yeye akiwa na nia ya kuomba radhi kwa dada yake, ndio Pam akaanza kumpiga. Anasema hakumrudishia, alimuacha tu.” “Ila alinipigia mimi simu aki…” “Mama Eric, na mimi nilikuwepo siku ile. Eric alimsemelea dada yake, na wewe ukamwambia angekuwa hajamnawia mikono Pam, ungekuwa na cha kuzungumza naye. Lakini alishamkana Pam. Si hivyo?” Mama yake akamuwahi maana alishamsikia amepandisha.

“Lakini…” “Hivi wewe unafikiri utamaliza vipi huu ugomvi wa hawa watoto kama sio kuingilia kati?” Mama yake akambadilikia, na kuwa mkali. “Eric ni mwanao kama Pam. Na sasahivi anataka kujirudi. Iwe kwa hila au la, lakini anajirudi. Na hili nimetoka kuwaambia hapa. Japokuwa ulitelekezwa, hukuacha imani yako kwa Mungu mpaka Mungu amekujibuUmerudishiwa zaidi ya hata uliyodhania? Nani alijua Pam yule aliyekuwa si kitu, leo atakuwa na kwake? Nani alijua wewe uliyekuwa mwisho wa dunia, Mungu angekutoa huku na kukurudisha mjini na kukupa maisha hayo?” Kimya.

“Sasa wewe unataka kushindana tena na Mungu? Utaweza Dorothy?” “Mimi sishindani na Mungu.” “Basi ACHA kuhesabu. Na acha kuangalia walioshindwakukusaidia wakati wa uhitaji wako, ila angalia kile Mungu amekutendea. Na ushukuru Mungu kwa walioshindwa kukusaidia, maana wangekuchelewesha kupokea kikubwa Mungu alichokuwa amekuandalia. Unanisikia Dorothy?” “Ni mpaka nizungumze na Pam mwenyewe mama!” 

“Na yeye Eric nimemwambia hivyohivyo. Kuwa, kichwa cha Pam na masikio yake huwa yanasikia lugha yako tu wewe. Endapo wewe ukikubali, ukazungumza na Pam, Pam hana jinsi ya kukataa. Ndio akaniomba mimi nizungumze na wewe maana anasema hata siku ya harusi alipata ugumu wa kuzungumza na wewe.” “Kwa hiyo ananisemea kwako?”

“Kwa sababu wote nyinyi mpo upande wa ubaya wake, hamtaki amani. Mpaka mjomba wake ametoka kumkemea asubuhi hii. Ndio nauliza, mlitaka mwisho wa hili jambo liwe nini kama hamtaki amani?” “Mama wewe unamuendekeza Eric ndio maana anashindwa kujirudi na kuwa…” “Si ndio huyo sasa anajirudi?! Mlitaka afanye nini?” Kwa asili mama Shelukindo ni mzungumzaji si kama mumewe. Na watoto wake walimjua yeye ni mkali kuliko baba yao. Na alimpenda sana Eric tokea mtoto.

“Zungumza na Pam, halafu unipe jibu. Na nia iwe kumaliza hili jambo, Dorothy sio kumuendekeza Pam. Maana na yeye anakajiukorofi kake, wote tunamjua.” “Sasa Pam amefanya nini?” “Kupigana na kaka yake hadharani.” Dorothy akaanza kucheka.

 “Pale nimezaa!” “Mkorofi sana Pam. Na angepigwa sijui angefanyaje?” “Ingekuwa mbaya zaidi. Bora hakumrudishia.” “Anasema alimmwagia soda mwili mzima na alikuwa amevaa shati jeupe, mwenzie yupo kazini.” Mama Eric hana mbavu.

“Ona unavyofurahia uovu wa Pam!” “Eric amezidi mama.” “Sasa hili jamboLAZIMA kumaliza Dorothy. Zungumza na Pam.” “Ila akikakataa uj…” “Kwako hawezi kukataa. Labda kama wewe ndio hutaki. Maana ni wewe tu ndio Pam hawezi kukukaidi.” “Katika hili mimi sijui mama. Acha nizungumze naye.” Wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~~

Akafika kwa Pam ikiwa imeshafika mida ya saa nne asubuhi. Pam alikuwa ameshapata kifungua kinywa na familia yake, amejilaza. Mill alikuwa yupo tu hapo akifanya yake. Shema akaenda kumfungulia na maneno mengiii. “Muite mama yako.” “Nakuja mama. Najivuta taratibu.” Akawa anashuka ngazi. “Naona unafuraha!” “Nina habari njema tupu mama yangu.” Akaanza akishuka ngazi.

Akaenda kujilaza kwenye kochi. “Haya?” Mama yake akamuuliza. “Tuanze na wewe. Chakula unakipata wapi?” “Basi hapo ulikuwa unakereka, hujalala vizuri.” “Kama ulikuwepo.” Wakaanza kucheka. Akamsimulia juu ya simu ya dada yake Jo, mpaka Pam akakaa.

“Sasa hapa nitafukuzwa Pam. Kwani huwezi kusikiliza kwa masikio tu?” Mama yake akanong’ona. Pam hana mbavu. “Mama wewe!” “Rudi kujilaza bwana Pam, wewe unataka kuharibu siku ya leo, tufukuzwe hapa wakati babu yako anakaribia kuja. Tena bibi yako anamuombea Eric na familia yake na wao waje.” Bwana hapo akamtibua Pam.

“Bibi anampendelea sana Eric.” Akaanza kugomba. “Alichonifanyia mimi haoni, leo anamtetea?” Akaendelea kugomba mama yake akimsihi apunguze sauti. “Na akija hapa ndio tutapigana mpaka nizae hapahapa.” Hapo Mill akashuka.

“Kwani kuna nini tena?” “Eti bibi anataka na Eric naye aje hapa.” “Tulia nimsimulie baba Shema, na uache kugomba. Rudi kujilaza hapo.” Akagoma. “Kama ndio hivyo naondoka, nikuache hapa peke yako, urudi kulala ndani maana wewe unaonekana hujiwezi.” “Na wageni wakija?” “Nawakaribisha kwangu. Wewe si huwezi kutulia.” Baba Shema akabaki amesimama anasikiliza na kuangalia.

Akamuona Pam anarudi kujilaza akilalamika. “Mimi sitaki Eric aje.” “Kwani kuna nini? Aliniacha gerezani mimi na mwanangu.” Ndipo mama Eric ikabidi kusimulia alichoambiwa na mama yake juu ya Eric. Baba Shema akakaa. “Mambo ya familia ni magumu mama, magumu sana.” Akaongea baba Shema akifikiria.

“Mimi mwenyewe nimeachiwa watoto wa baba, havina nafuu. Nakwenda nao hivyohivyo. Juu ya Eric nilishazungumza naye sana siku namkaribisha kwenye harusi. Pengine ameamua kujirudi. Sasa kwa nini sasahivi, ni swali ambalo hamna mwenye jibu.” “Jibu analo mkeo.” “Jibu gani!?” Pam akashangaa sana.

“Hakukuomba kikao wewe ukaishia kumpiga na kummwagia soda?” Bwana Pam alicheka, mpaka machozi. “Mkorofi wewe!” “Bwana siku ile nilikuwa na hasira. Na wasingenishika nisingemaliza.” Mill alikuwa akimwangalia, akitingisha kichwa.

“Basi jibu umelipata baba. Alitaka kumuomba msamaha huyu dada yake, akaishia kumpiga.” “Aliniacha gerezani.” “Ndio bibi yako amesema tuache kuhesabu, Mungu keshatulipa zaidi ya Eric ambavyo angetusaidia. Na anasema ukute kusaidiwa na Eric kusingevuta moyo wa Mungu na kutubariki kwa kiasi hiki.” “Mimi namjua bibi. Likija swala la Eric hatakosa neno lakusema.” “Nashauri hili jambo liishe Pam.” Akamtizama mama yake.

“Na liishe, kwamba akija hapa sio uanze fujo na maneno ya ukorofi.” “Kwamba wewe ushamsamehe?!” “Nitafanyaje na yeye ni mwanangu? Eti baba Shema?” “Kweli mama.” “Mmenigeuka, sasahivi wote mpo upande wa Eric wakati…” Akataka kuanza kulia.

“Wewe si ni mama? Tena Mungu akijalia utakuwa nao na wewe kama mimi, wawili.” “Huyu akiwa wa kiume nazaa tena mpaka..” “Pam!?” “Sasa wewe unafikiri nitaishia na madume matupu nikose wakunifunika nguo nikiwa mzee?” “Mimi nitakufunika.” “Wewe Mill! Unataka kuishia watoto wawili tu?!” “Hakika ikilazimu, watatu wawe mwisho Pam. Mzee Mgini alikuja kupata mtoto wa kike, mmoja tu, tena sijui ni namba gani! Ukute ni wa nane! Mimi watoto wengi vile kama mzee Mgini nimeapa sitaki. Ni fujo isiyo na sababu.” “Basi tunajaribu mpaka wa nne.” “Kazi itakuwepo.” Mama yake akaongeza akionekana amechoka.

“Hakika itabidi tuzungumze Pam. Kwetu watoto wakiume ndio wanazaliwa kwa wingi hata dada zake baba, na wenyewe wanazaa madume tupu. Sheila ni kama lulu kwenye ukoo. Hawana watoto wa kike. Sasa tutashindana na Mungu mpaka lini bwana?” “Sasa kwa uzaaji huo, ndio utakuja pata kina Eric. Utafanyaje?” “Usiombee mabayamama!” “Kwani na mimi niliombewa ‘mabaya’ na nani!? Lakini si ndio nikampata! Sasa nitamfanyaje na ni wangu? Na wewe unayo nafasi kubwa sana ya kunisaidia. Labda kama usema unataka na wewe kuyafanya maisha yangu yawe magumu zaidi hapa duniani. Hakuna kupumzika.” Hapo akamkamata Pam.

Huwa hataki mama yake apate shida. “Basi yaishe mama ila mwambie asi…” “Wewe acha ukorofi na yeye nitamwambia aache tabia zake kama baba yake. Basi. Na utulie hapo kwenye kochi kabla sijahamisha ugeni kule kwangu.” “Mama anavyoninyanyasa!” “Wewe mtaka watoto wengi, mmoja tu anakushinda hapo.” Mill akaanza kucheka. “Natulia mama jamani!” Akajilaza vizuri kabisa. 

Ndipo mama yake akampigia simu bibi yao kumwambia Eric anakaribishwa. “Sasa ujue anakuja na mkewe na watoto wote.” Bibi mtu akaongeza. “Mama na Eric! Umeamua kuleta ukoo mzima ukweni! Tutafukuzwa.” Hapo akaongea kisambaa.

“Wewe hutaki kuona wajukuu?” “Mama, umeshaambiwa wanakaribishwa. Njoo nao wote unao wataka wewe. Chakula chakutosha kipo.” “Na mimi natoka kwenda kuongeza nyama. Ni sawa nikija na Jerry?” Mill akauliza akisimama. “Wewe alika wote unaowataka. Tushaambiwa chakula kitakuwepo.” Mill akaondoka na kuwaacha hapo kisambaa kikiendelea ila kwa kicheko sio tena ugomvi.

Love At First Sight!

Kulichangamka hapo. Mill naye akaongeza vinywaji na hizo nyama, akawa amekaa na Jerry, Eric, babu na mjomba wakizungumza huku wakinywa mida hiyo ya jioni, vyakula viliachwa tu mezani unajipakulia utakavyo.

Muda wote Pam macho kwa mama yake. Ilipofika mida ya saa 11 jioni akamuona ni kama amepokea ujumbe. Akaonekana kubadilika kabisa usoni. Mara kadhaa akamuona anajaribu kujibu, kisha anafuta. Anajaribu tena. Kisha anafuta. Mwishoe akamuona anazima kabisa simu na kuiweka pembeni asijue na kwa Jo nako ilikuwa kama yeye.

Alimtumia ujumbe mfupi tu. ‘Dorothy!’ Ndio huo alikuwa akihangaika nao. Na Jo naye alishaona alivyosoma. Kule kuandika na kufuta, akijaribu tena na tena, Jo naye upande wa pili wa simu alikuwa akimuona. Mwishoe ikawa kimya. Kumbe aliamua kuchana nao na kuzima kabisa simu. Pam akamuona amepotea kabisa hapo. Akajua lazima ujumbe atakuwa umetoka Jo. Akamuacha, ila akamuagiza Shema amletee kitu cha kunywa. “Mpe bibi juisi ingine.” Ndipo mama yake akagutuka.

“Umemuona msichana wangu lakini?” Pam akamuanza mama yake makusudi tu kumchangamsha. “Mpaka mwezi uishe, Mill atakuwa anaongea kisambaa kizuri kuliko Shema.” Wote wakaanza kucheka. “Mumfundishe taratibu, ataelewa.” Bibi yake akatoa ushauri. “Nani wakumfundisha? Nimemuona Shema hata hajashituka, maana anamuelewa vizuri tu japo anamjibu kwa kiswahili kama anavyomfanyia bibi yake. Haya, mrembo wa mama naye kafurahi, kama kaletewa rafiki! Nawasikiliza hapa, lugha yao moja, vicheko muda wote.” “Na wewe?” “Mimi ndio najisahau hata sijui tunazungumza naye lugha gani! Mmeona sura ya Mill alipokuja hapa kumsalimia, halafu lugha zikagongana baada ya shikamoo?” Wote wakaanza kucheka.

“Baba Shema alianza vizuri akijaribu kumfahamu. Akaishia kumuangalia mkewe, na kuondoka.” Shangazi mtu akafanya wazidi kucheka. “Ndio atajifunza kisambaa mwaka huu. Na hivi hataki nitoke kitandani! Watajikuta wawili tu, hana jinsi ila kuzungumza naye.” “Shema atamsaidia.” “Shule nayo?” Wakazidi kucheka. 

“Nakwambia watajikuta yeye na Mill tu humu ndani, Shema yupo shule, mimi wamenifungia ndani.” “Basi kweli atakizungumza mwaka huu.” Wakazidi kucheka wakimteta Mill na huyo msichana mpya wa kazi. Kidogo Dorothy akajisahau na kuendelea kuzungumza.

~~~~~~~~~~~~~~

Watoto wa Eric walikuwa wakubwa kidogo kwa Shema. Mmoja wa kike, mkubwa wa kiume alikuwa nje akicheza mpira na Shema. Kama kawaida ya Shema, akishapata tu mtu akakubali kucheza naye, lazima atacheza mpira. Mill akaona atoke na yeye akacheze nao. Wale wanaume pale nao wakasimama na kutoka kama kwenda kuangalia. Nyumba ya Mill ilikuwa na ua mkubwa na imezungushiwa ukuta mkubwa sana. Sasa sababu mwanae ni mpenda mpira, akatenga sehemu maalumu kwa mpira wa miguu, akaweka goli kabisa ndipo hapo Shema hucheza, na wakati mwingine hata na baba yake. 

Jioni hiyo ndio wakawa wakicheza. Kelele zikaongezeka. Wanawake nao wakaona watoke wakaangalie. Wakatoa viti nje na vinywaji vyao wanaongea huku wakinywa, mwenye njaa anarudi ndani anachukua chakula, anarudi kukaa nje wanaendelea kuangalia mpira huku wakiburudika jioni hiyo jua kali lilishaisha, upepo wa jioni ukipuliza. 

Alikuwa akicheza Mill na kijana wake timu moja, halafu Jerry na mtoto wa Eric timu ingine. Eric alipoona timu ya mwanae inalemewa, na yeye akaingia. Ikawa ushindani mkubwa ila burudani, wanacheka kwelikweli.

~~~~~~~~~~~~~~

Mara geti likawa linafunguliwa. Ikawafanya wote wageuke kujua anayewatembele mida hiyo ni nani! Na wazi alionekana si mgeni hapo getini, maana geti lilifunguliwa bila ya kuuliza wenye nyumba. Ikavuta macho ya wote.

~~~~~~~~~~~~~~

Yapo Majanga Mengine Maishani Tunasababisha Kwa Upumbavu Wetu Wenyewe, Lakini Mungu Mwenye Rehema Huyageuza Kuwa Baraka. 

Usikate Tamaa. Hujachelewa.

Hakuna umbali mwanadamu anaweza kwenda, jicho na mkono wa Mungu vikashindwa kumfikia.

Inaendelea… 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment