Joshua
alifika hapo mapema sana siku hiyo mpaka akawashangaza. “Kwema?” akauliza baba
Naya wakati akimfungulia. “Nilitaka kuja ili tukusindikize na Naya. Angalau
tuwe pamoja, Naya asijikute amebaki peke yake pale kituo cha mabasi.” “Hapo
umefanya vizuri, nashukuru sana.” Akaingia ndani na kumkuta Naya akiwa
ameshamaliza kuandaa sanduku la baba yake. “Karibu
Joshua, na asante kwa kuja.” “Karibu. Nisaidie nini?” “Kuweka hili sanduku
kwenye gari ndipo tutoke moja kwa moja, awahi.” Joshua akatoa sanduku,
baada ya muda mfupi sana wote wakajikuta kimya, ndani ya gari ya Joshua wakielekea
kituo cha mabasi makubwa yaendayo mjini Mbeya. “Unipigie simu kila wakati,
baba.” “Nitafanya hivyo.” “Ukichelewa ujue nitakufuata.” “Tutawasiliana. Usiwe
na wasiwasi. Naomba tulia kazini mama. Tusiharibu kila mahali. Ila naomba
usisahau kupita kule dukani jioni ili uwasaidie kufunga mahesabu.” “Nitakwenda.
Wewe usiwe na wasiwasi na huku. Ila kuwahai kurudi kwako baba. Mimi nataka
kuolewa. Na siwezi bila wewe kuwepo.” Baba yake akanyamaza. Baba Naya Mjini Mbeya. Baba Naya
alifika mjini Mbeya bado ilikuwa mapema tu. Akachukua pikipiki mpaka kwa Malon.
Akamkuta kijana ambaye anaishi hapo na wanafahamiana sana tu kwani naye
alikuwepo kipindi akifanya kazi hapo, Mpoki. “Bosi hayupo. Aliondoka na mzigo
siku tatu zimepita sasa.” Akamwambia baba Naya. Ndipo akajua walikuwa
wakizungumza na Malon akiwa Dar. “Unakumbuka kumsikia Bale akiweka mipango
yeyote ya baada yakutoka hapa?” “Bale ana mipango mingi mzee wangu! Halafu
mbishi. Ameondoka hapa akiwa amekosana na kila mtu.” “Mpaka wewe!?” “Mimi
alikuwa akinidharau na kuniona nimezubaa. Ila usiku alipokuja kuchukua mizigo
yake hapa, ali...” Akasita. “Naomba
nisaidie hata kujua pengine ni wapi hata alitamka anafikiria kwenda. Sio lazima
ikawa kwa hakika. Hata kutamka tu.” “Nina shemeji yangu aliyemuoa dada yangu
tunayefuatana. Wao wanaishi mjini. Alikuja hapa siku moja, wakati tukizungumza,
Bale akanifuata na kuanza kugomba kwamba naongea tu badala ya kufanya kazi.
Ndipo shemeji akamwambia alikuwa akinipa dili nzuri itakayonitoa haraka
kimaisha. Bale akavutiwa nakutaka kujua nini maana mimi nilikataa.” “Ni
biashara gani?” Baba Naya akataka kujua. “Shemeji
anaingiza nguo kutoka Zambia. Zaidi vitenge. Wanaduka hapo mjini. Sasa
akamwambia hiyo biashara inalipa sana, lakini amesikia au sijui kuna
mtu amempa dili nyingine kuwa huwa wanaingiza na kutoa mirungi.
Wanaficha kwenye mizigo ya nguo wanapitisha pale mpakani, inalipa sana. Mimi
nilikataa. Na Bale ni kama alikataa siku hiyo. Ila usiku alipokuja hapa,
aliomba namba ya simu ya shemeji, akasema atamtafuta ili kumuulizia zaidi. Sasa
sijui!” “Nashukuru sana, Mpoki. Unaweza kunisaidia namba ya simu ya Bale pamoja
na shemeji yako?” “Ya Bale sina. Ila naweza kukupa ya shemeji na ya huyo dada
yangu. Ni watu wakarimu sana. Hawana shida.” Baba Naya akachukua namba na
kutoka kwa haraka akiwa ameacha mizigo yake yote hapo. Akiwa
anatembea kwa haraka akirudi mjini Naya akampigia. “Pole
baba.” “Asante mama. Ila nawahi kurudi mjini kukutana na mtu ambaye pengine
anajua atakapokuwa ameelekea Bale.” “Nakuombea baba yangu. Ila naomba unywe
hata maji.” “Mpoki amenipa chai ya rangi hapo, nimekunywa ndipo nimetoka. Kwa
hiyo nipo sawa. Hapa natembea kuwahi mjini.” “Pole baba
yangu. Nakuombea ufike salama. Nitakupigia tena. Acha niweke sawa haya mambo ya
hapa dukani kwako. Nanaa naye kuna kitu alikuwa akinifundisha hapa, ukija
nitakwambia na wewe. Naona itakurahisishia.” “Nashukuru mama. Sasa mwenzio
umemuacha wapi?” “Nimemuacha kazini, nimekuja huku kwenye duka lako na gari
yake. Atanifuata nyumbani akitoka kazini. Alikuwa na mambo mengi leo nikajua
nikimsubiria sitaweza kuwahi huku Kibaha na hizi foleni. Tumekubaliana aje
nyumbani baadaye. Atamtumia dereva wake na gari ya ofisi kumleta.” “Na Zayoni?”
“Nilimkuta hapa. Yupo mzima tu. Naona anasaidia kweli! Wanamsifia.” “Nimemuona
jinsi alivyoweka juhudi. Sasa huyo ndio wakumfundisha, ili aje
anifundishe na mimi.” Naya akacheka. “Naona
ameshajua zaidi yangu. Nanaa alikuwa akinielekeza kwa kupitia yeye maana ndiye
aliyekuwa akijua vizuri mambo ya hapa kuliko hata mimi. Ni mambo ya bidhaa za
hapa, bei na mahesabu yake kwa kutumia kompyuta, ili kwamba hata nikiwa kazini
niwe najua ni nini wameuza, nini wameishiwa au kupungua, ili niweze kuagiza kwa
haraka. Sasa Zayoni naona bei zote zipo kichwani na kumbe anajua unapoandika
vitu vilivyopo stoo! Basi amemrahisishia kweli Nanaa.” “Basi huyo atakufaa.
Acha niwahi mama.” Wakaagana, baba Naya akijua akili ya Naya ikitulia, ataweza
kuongoza hapo vizuri, hapata haribika jambo. Hilo likampa moyo. ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ Baba
Naya akamkuta dada yake Mpoki na kumwambia mumewe hayupo, amekwenda kusambaza
mzigo. “Unajua chochote juu ya Bale?” “Mpoki amenipigia simu muda si mrefu na
kuniambia unakuja, wewe ni baba yake Bale. Lakini hata hamfanani!” “Wanafanana
na mama yao. Unajua alipo?” “Alikuja nyumbani usiku usiku, akaomba hifadhi, ila
kesho yake akaondoka. Baba Tupo, ndiye aliyemsindikiza mpaka kituo cha mabasi
akielekea kwa rafiki yake ambaye alikuwa amsubirie, waende huko Zambia.
Nimempigia baba Tupo kumuulizia baada ya kuagana na Mpoki, akasema
hajawasiliana nao tena. Hajui kinachoendelea huko lakini anasema kijana wako ni
mchangamfu, yupo tayari kupambana. Atafanikiwa tu, usiwe na wasiwasi.” Akampa
moyo asijue bado hata hajamsogeza karibu na mwanae! Bado kumpata Bale kukawa ni
msururu wa watu hapo katikati na bado wote hawana taarifa kamili za Bale. “Nashukuru
mama. Sasa unaweza kunisaidia namba yake ya simu?” “Ya baba Tupo?” “Na ya huyo
ambaye Bale aliyekwenda kwake.” “Acha tumuulize baba Tupo, maana si kwamba ni
watu wenye mahusiano! Ni mtu tu waliyekutana kwenye biashara. Akampa hilo wazo.
Akataka kushawishika hapa ili akafanye na hiyo biashara ya mirungi, lakini mimi
nilimkataza kabisa.” Moyo wa baba Naya ukazidi kuumia kila akisikia aina hiyo
ya biashara mwanae aliyokimbilia. “Watoto
wetu wadogo. Akija kukamatwa huko Zambia! Si ndio maisha tena basi! Nimemuonya
na kumuapisha asijejaribu. Bora turidhike na kidogo tunachopata.” “Ni kweli
mama. Umetumia hekima.” “Acha nimpigie, akurushie namba ya huyo mtu.” “Niombee
na yake tafadhali ili nikikwama huko, nipate mtu wa kumuuliza.” Akampa
namba ya simu ya mumewe, huyo baba Tupo, kisha akapiga simu na kumpa baba Naya
mwenyewe azungumze naye. “Ongea naye tu ili umuulize maswali yote
unayotaka.” “Nashukuru mama.” Akapokea simu. “Shikamoo
mzee wangu.” Akamsalimia kwa heshima. Baba Naya alipoitika
akaendelea. “Nimempigia simu jamaa mwenyewe, hapatikaniki. Atakuwa bado yupo
Zambia. Yeye anabiashara kubwa kuliko hii yetu. Anasambaza vitenge mpaka
mikoani, na hapo ndipo nilipojua siri ya mafanikio yake kuwa kumbe huwa anachanganya
na hiyo mirungi. Amesifia sana. Na hata alipozungumza na Bale alimwambia
wasizungumze kwa simu, aende hukohuko akajionee kwa macho. Ndipo Bale akaondoka
hapa. Sikuwafuatilia tena kwa kuwa wote si watu ninaofahamiana nao kwa karibu.
Bale nilikutana naye akiwa anamfoka shemeji, na huyo jamaa nilikutana naye
madukani huko Zambia na kugundua kuwa na yeye ni Mtanzania. Ndipo tukapata
muda, akanishirikisha siri ya mafanikio yake. Nilipokuja kumwambia mke wangu
alinikatalia kabisa na kuniapisha nisiwahi hata kuja kumtafuta tena asije
akafanikiwa kunishawishi. Kwa hiyo tokea kijana wako aondoke hapa na kuwa na
uhakika wamewasiliana na atampokea, basi sijamtafuta tena mpaka hii leo na
sikufanikiwa kumpata.” “Unajua
anapoishi?” “Sifahamu. Ila nakumbuka aliniambia maduka yake yapo karibu na
mpakani mwa Tunduma.” “Kwa hiyo hata Bale alikwenda huko Tunduma?” “Sina
uhakika sana. Nilichofanya mimi ni kumpigia simu. Bale akaomba
kuzungumza naye mwenyewe. Wakapanga mpaka aina ya mabasi yakupanda na wapi ashuke.
Nikamsindikiza kituo cha mabasi, nikamuacha hapo. Sikujua kilichoendelea. Ila
tulipokutana Zambia, katika mazungumzo yetu, nakumbuka kumsikia akisema hivyo.”
“Nakushukuru sana. Asante. Nakutumia na namba yangu ili ukiiona inaingia kwenye
simu yako, tafadhali pokea. Pengine nitakuwa nikihitaji maelekezo huko.”
“Kwamba unakwenda!?” Akauliza kwa mshangao kidogo. “Ndiyo.
Naona nikaanzie huko Tunduma.” “Kwani huwa hamuwasiliani na kijana wako?”
“Hapana. Ndio maana naona nikamtafute ili nijue hali yake.” “Kwa nini usisubiri
mpaka jamaa atakapopokea simu?” “Asipopokea? Iweje iwe alikusudia kubadili
namba ya simu?” “Kweli.” Akaafikiana naye. “Acha nirudi kwa Mpoki,
nilale mpaka kesho na mimi niwahi mabasi ya kwenda Tunduma.” “Basi nitakuja
kukuchukua mzee wangu, nikusindikize. Mimi ninao usafiri. Usihangaike usiku wakati
vijana wako tupo.” “Nashukuru sana.” Baba Naya akashukuru
na kurudisha simu ya mama Tupo, dada yake Mpoki. Akatoka hapo kurudi kwenye
makazi ya Malon, alipoacha mizigo yake kwa Mpoki. Safari Moja Yaanzisha Ingine. Akiwa
njiani akiwaza na kupanga hili na lile na maombi akimsihi Mungu ulinzi kwa Bale
huko alipo, akakumbuka jinsi maisha yalivyo ya ajabu. Akakumbuka alipo kwa
wakati ule na alikotoka. Akavuta pumzi kwa nguvu akitafakari. Akiwa hana uwezo
kama alionao wakati huo alikuwa na familia. Mke na watoto. “Mama Naya!” Akamkumbuka
mkewe kwa kuumia sana. Akakumbuka alikopita na mkewe akilalamikia mali mchana
na usiku! Sasa Mungu wake ndio amemjibu. Tena huyo Mungu amejibu kwa moto.
Akacheka na kutingisha kichwa kwa masikitiko. Hata majirani walishuhudia Mungu
alichomtendea kwa jinsi nyumbani kwake tu palivyo badilika. Duka alilonalo
mjini Kibaha! Lakini familia haipo kama mwanzo. Mkewe amefariki
mambo yakiwa ndio yanakaribia kubadilika, na Bale kaondoka nyumbani akipishana
na mafanikio mlangoni kwao! Alilokwenda
kutafuta huko nje kwa shida na matusi akisimangwa na kuhatarisha maisha yake
amepishana navyo mlangoni kwao. Wakati mafanikio ndio yanaingia kwao, yeye ndio
anatoka! Baba Naya akaumia sana. Yote aliyokuwa akimuomba Mungu miaka yote
akifunga na kuomba, eti ndio anajibiwa wakati huo! Tumaini la pesa limechupua.
Baba Naya tayari anayo miradi ya kueleweka tena ya uhakika akiwa ameshikwa
mkono na Geb Magesa anayeijua hiyo biashara haswa. Kila alilomshauri
limekamilika tena limekamilika kwa kiwango cha juu. Mambo yake yamekaa vizuri.
Akazidi kuumia kila akifikiria alichoacha nyumbani kwake lakini watu muhimu
kwake wanapungua! Akakumbuka
ahadi za Mungu kwa mwanadamu. “Ibrahimu aliahidiwa uzao mkubwa,
akaamini mpaka kuitwa baba wa imani, lakini alikufa bila kuushuhudia huo uzao
mkubwa zaidi ya hao watoto wawili tu!” Akawaza baba Naya na kuendelea
kukumbuka. “Musa naye alihangaika kuwatoa wana wa Israeli huko Misri
ili kuwapeleka mji wa ahadi, lakini yeye mwenyewe hakuingia mji wa ahadi japo
Mungu alimuonyesha kwa mbali.” Akazidi kusononeka kila huo ukweli
ulipokuwa ukiendelea kufunguka moyoni mwake. “Lazima nimpate Bale.
Sitarudi nyumbani mpaka nimpate Bale.” Akaazimia moyoni mwake. Lakini
anakopanga kwenda, hapajui! Naya naye anamuhitaji. Furaha aliyokuwa nayo Naya
akiisubiria hiyo ndoa! Baba Naya akavuta pumzi kwa nguvu akitembea. Naya
alikuwa akimuhesabia baba yake siku zilizobaki ili aolewe na Joshua. Kila siku
akiamka lazima amwambie baba yake siku zilizobaki awe mke wa Joshua.
Akamuhurumia endapo chochote kikitokea kwake. “Lakini ni lazima nimpate
Bale. Nitajua hukohuko niendapo. Hata kama itanigarimu pumzi yangu ya mwisho.
Lazima nimpate Bale.” Wasiwasi
ukaanza kumuingia kila alipokumbuka umbali mwanadamu anaoweza kwenda akitaka
jambo lake. Akamfikiria vile Bale alivyoanza akiwa na haraka ya kufanikiwa,
akajua wanaweza kumtumia vyovyote ili kujinufaisha na kijana wake. “Mungu
wangu turehemu. Najua nimekosa sana na sistahili hata rehema zako, lakini Mungu
wangu, nakusihi nirehemu tena. Nitazame mimi na wanangu tena, tena kwa upya.” Baba
Naya akamsihi Mungu kwa hofu akitembea kurudi kwenye makazi ya Malon. Hakutaka
hata kuchukua usafiri umrudishe. Mawazo
yakamrudisha na kwa Zayoni. Akamuhurumia ambavyo alivyo mdogo. Bado anaomboleza
msiba wa mama yake. Bado baba Naya hakuwa akijua atakachokabaliana nacho huko
mbeleni. Hakujua huyo mwenyeji wa Bale ni mtu wa namna gani kwa hakika. Ila kwa
kusikia kwamba ni mfanyabiashara mkubwa na mzoefu wa biashara haramu,
akajua hatakubali kuangamia kirahisi endapo kama amemuingiza kijana wake kwenye
matatizo au kama yeye ndiye anayenufaika na kijana wake. “Umbali gani
atakwenda kuficha maovu yake?” Akajiuliza. “Lakini lazima
nikamkabili kwa namna yeyote ile. Liwalo na liwe, nitajua mbele ya safari.” Nani wa
kumuachia mji wake ambao kwa muda mfupi sana umebadilika haswa! Jengo jipya na
zuri lipo nyuma ya nyumba yao ya kawaida tu. Kulitengenezewa uzio mzuri kama
alivyoshauri Geb kuepusha wezi kuweza kuingia hapo galani kiurahisi. Geb
alishauri hata aridhi ya kutembelea hapo isibakie mchanga tu. Ifunikwe na
vitofali na kutengenezwe mifereji maalumu kuelekeza maji ya mvua sehemu ingine
yasije kuja kuingia galani. Yote hayo yalifanyika kwa muda mfupi bila kutarajia.
Ikawa kama alivyotamka Mungu na mambo kutokea hapohapo! Kama mama Naya
angefufuka na kurudishwa nyumbani kwake, asingeamini. Kuanzia getini mpaka
kuzunguka nyumba, kukawa kumepangiliwa kwa ustadi mpaka njia maalumu pembeni ya
hiyo nyumba, nzuri maalumu kwa malori kuingia kwa urahisi kushusha mazao
galani, na majunia ya mkaa sehemu yake. Akacheka baada ya kukumbuka nguvu ya
pesa. “Wewe ni Mungu, na zaidi yako hakuna mwingine.” Akajikuta
akiutambua mkono wa Mungu akimshangaa pale anapoamua kutenda jambo lake. Hata
gari ya Naya aliyopewa na Joshua iliweza kuhifadhiwa hapo nyumbani kwao kwa
sababu ya mazingira mazuri na ulinzi mzuri. Kila alichoshauri Geb, alihakikisha
kinafanyika tena kwa kusimamia yeye mwenyewe na mafundi wake. Kwa vipimo sahihi
alivyotaka Geb mpaka akatoa kitu kizuri sana tena chathamani! Pesa
yote aliyokuwa akiwekeza hapo alikuwa akiwaandikia kisha kumkabidhi baba Naya
mwenyewe na Joshua, kwa makubaliano atakuwa akimkata tararibu kwenye biashara
watakayokuwa wakifanya pamoja. Ikawa unafuu sana kwa baba Naya. Hakuanza kwa
aibu ya kukopakopa wakwe bila ujasiri wa kurudisha au kupewa bure. Ilikuwa
kwenye mkataba wao wa biashara. Kumlipa Geb kwa kadiri watakavyoendelea. Hapo
napo Geb akawa amewekeza kupitia baba Naya. Ameongeza soko la uhakika na ni
kama ametunza pesa yake. Akajikuta
akimshukuru mkewe kwa kusaidia kulipia hilo eneo ambalo limekuja kuwa msaada
mkubwa sana. Akajua na yeye anajukumu la kuwaacha wanae sehemu nzuri na
kuendelea hapo alipowaacha endapo hatakuwepo, sio kuwaacha hapo na kujikuta
wanarudi chini kabisa. Akafikiria
nani wakumuachia majukumu yake. Baba Naya akajaribu kuwatafakari ndugu zake
mmoja hadi mwingine, wakajua wote watasumbua sana watoto wake. Akajua
hawatashindwa kuwapokonya mali zote endapo ataacha chini ya usimamizi wao.
Ndugu wa mkewe ndio kabisa. Kwanza hawakuwa wakimpenda baba Naya kwani wote
hawakutaka ndugu yao aolewe naye. Walimpinga sana, lakini mwishoe mama Naya
akaolewa tu. Na kadiri mambo yalivyokuwa yakiwaendea vibaya, hawakuacha kumkubusha
na kumwambia, ‘Tulikwambia sisi!’ Akaona hao sio wakuwagusa kabisa. Na baada ya
kumzika mkewe, wote walitaka vitu vya dada yao kana kwamba hakuwa na watoto. Na
pia kudai pesa zaidi, wakisema wanataka akiba yake yote na watakayolipwa
serikalini kwa ajili ya ndugu yao pia wapewe. Ukatokea ugomvi hata kati yao
wenyewe lakini mwishoe baba Naya akakubaliana nao, nakuwapa alivyoweza. Akabaki
akitafakari akimtafuta mtu sahihi wakumuachia maagizo/wosia endapo chochote
kitamtokea huko anakokwenda kumsaka mwanae, na asirudi. Baba Naya kwa Joshua. Akajikuta
anampigia simu Joshua. Akapokea kwa haraka sana. “Samahani
kwa usumbufu Joshua.” “Bila shaka mzee wangu. Vipi huko?” “Ndio nimepiga
angalau nikupe maendeleo ya huku.” Hilo likamfurahisha
sana Joshua kuona amekumbukwa na kuthaminiwa. Baba Naya akamueleza yote bila
kumficha. “Kesho nitaelekea Tunduma, nikaanze kumsaka. Nimepewa jina moja tu
la huyo mwenyeji wake huko, inavyoonekana ni mtu mashuhuri huko. Naamini
nitampata tu ili anisaidie kunisogeza kwa Bale. Lakini Joshua?” “Nakusikiliza
mzee wangu.” “Kuna kitu hakipo sawa. Nakwambia haya ili kukuomba unisaidie kuwa
karibu na huyo mama mzazi pamoja na mdogo wake. Sitarudi mpaka nimpate
Bale. Ambayo sijui ni lini na nini kitatokea huko. Lakini nimekusudia kupambana
kufa na kupona, mpaka nimpate Bale.” “Tunakuombea kila kitu kiende sawa.” Joshua
akajaribu kumtia moyo asielewe undani wa hiyo simu ya baba Naya. “Nashukuru
lakini kufa kwangu mimi ni faida. Sitapoteza. Hilo siogopi, ila
nafikiria wanangu.” Hapo Joshua akaongeza umakini akiwa ameshituka kidogo. Baba Naya
akaendelea. “Sina ndugu wakaribu wa kunisaidia kwa umbali mrefu kusema
chochote kikitokea kwangu, wanaweza kusimama na watoto wangu. Nimeona alipougua
mke wangu mpaka kifo chake. Tulipata ushirikiano mdogo sana kutoka kwa ndugu.
Sasa kila nikiwawaza wanangu endapo mimi sipo, zaidi Zayoni, nawahurumia sana.”
“Naomba usiwe na wasiwasi mzee wangu. Kila kitu kitaenda sawa.” “Naelewa kabisa
Joshua. Hata kuondoka kwangu hapa duniani ni kwenda sawa. Mama Naya
hajapoteza hata kidogo. Tuliobaki ndio tumepoteza. Inaweza ikawa hivyohivyo na
kwangu. Mimi nisipoteze ila wanangu. Naomba nisikilize tu tafadhali.”
“Sawasawa.” Hapo Joshua akajua amepigiwa kuachiwa wosia. Akatulia kabisa
akimfikiria Naya. “Mungu
saidia chochote kisitokee.” Akajikuta
na yeye akiomba baada ya kufikiria endapo huyo baba akifa huko. Akajua ndio
atampoteza na Naya kabisa. “Zayoni ni muoga sana. Asubuhi leo alipoamka
na kujikuta peke yake na hata mlinzi hayupo, alinipigia simu akilia sana.”
“Mlinzi alikwenda wapi tena!?” Joshua akauliza akionyesha kujali na
kushangazwa kwani hata yeye aliyajua makubaliano kati ya baba Naya na hiyo
kampuni ndogo ya ulinzi inayolinda nyumbani kwake. “Nafikiri
aliondoka kabla ya mwenzie wakulinda kutwa hajaja kumpokea. Sasa hiyo
imemuogopesha sana Zayoni, ilimbidi aondoke hapo aende kukaa na mlinzi wa
kwenye duka la Kibaha.” “Nitakwenda kuzungumza na walinzi leo.
Hivi hapa ndio nakwenda kuwaona. Nilikuwa na vikao mpaka
mida hii. Naya aliondoka na gari yangu kwa kuwa asubuhi unakumbuka mimi ndiye
niliyekuja kuwachukua?” “Ameniambia nilipozungumza naye jioni hii.” “Basi nipo
njiani. Nitakwenda kuliweka hilo sawa kuhakikisha mlinzi wa usiku hatoki mpaka
wa kutwa awe amefika.” Joshua akamuhakikishia. “Nitashukuru
sana. Na huyo wa usiku zungumza naye juu ya gari ya Naya. Huwa nikiwepo
mwenyewe nazunguka usiku mpaka kule kwenye ghala. Na mara zote anakuwa amelala.
Sasa mwambie sipo, lazima aongeze umakini.” Baba Naya akaendelea. “Zayoni
hayupo kama watoto au vijana wengine wanavyotakiwa wawe. Nalo hilo ni moja ya
makosa niliyoyafanya kwenye malezi yao hao. Alikuwa karibu sana na mama yake.
Yaani sasa hivi ndio kama anawekwa kwenye ulimwengu mgeni sana kwake. Yupo
kwenye kujifunza maisha kama mtoto mchanga. Alibebwa na mama yake akimfanyia
kila kitu mpaka kumsaidia kufikiria. Itachukua muda, lakini namuona yupo tayari
kujifunza. Ila kwa sasa tafadhali usimsahau. Ataharibikiwa kabisa
akijikuta yupo kwenye huu ulimwengu peke yake, akitakiwa kufanya maamuzi na
kuchukua hatua yeyote ile akiwa peke yake.” “Nitahakikisha yupo salama.
Nimeweza kumsoma, uzuri yupo tayari kujifunza.” “Nashukuru sana.” Akaendelea. “Tafadhali
swala la ulinzi hapo usisahau Joshua. Panaonekana pako shamba kidogo lakini si
salama. Nimeacha mwanangu hapo, wasije kuwaingilia usiku endapo wakijua
mwenyewe sipo.” Joshua akajua anayezungumziwa hapo ni Naya tu. “Nitaweka
msisitizo mzee wangu. Hilo usiwe na wasiwasi nalo kabisa. Nitahakikisha leo
hilo linakaa vizuri.” Hapo napo Joshua akaahidi. “Nashukuru.
Kingine na cha mwisho. Najua nilikuapisha juu ya Naya. Naomba niongeze ombi
hapo.” “Karibu.” Joshua alikuwa akiendeshwa na gari ya kazini kwao akipelekwa
Kiluvya kwa kina Naya na si nyumbani kwake. “Naya ni mtoto niliyelea mimi
mwenyewe kuanzia ni mdogo sana. Aliugua sana wakati yupo mdogo mpaka tulifikiri
pengine tungempoteza. Akiwa kwenye hiyo hali mama yake akashika mimba ya Bale
iliyokuwa na yenyewe akimsumbua sana mama Naya. Kutwa yupo hospitalini kwa hili
au lile juu ya huo ujauzito. Kwa kuwa kulikuwa hakuna matumaini ya kuishi kwa
Naya, mama yake akaweka tumaini kwenye mtoto aliyekuwa amebeba, hiyo mimba,
ambaye ndio Bale, wakati akijiuguza, mimi nikihangaika na Naya.” Akaendelea. “Katika
miujiza ambayo imenifanya nibakiwe na Mungu, hata kama mazingira na watu
wakinikatisha tamaa, ni Naya. Ipo siku aliugua. Akabanwa akawa anashindwa
kuhema kabisa. Ilikuwa ni usiku, mama yake ndio amejifungua Bale. Nilikimbia na
Naya hospitalini, wakati tupo mapokezi nikisubiria ahudumiwe, akaacha kuhema kabisa,
mwili wake ukaanza kupatwa baridi kama aliyekufa. Bado nilikuwa nimempakata tu,
na hakuna aliyenipa hata huduma ya kwanza. Nilijua wazi amekufa na
ndivyo hata mama yake alijua tusingefika mbali kwa ile hali aliyoipata usiku
ule. Nikajua wangemchukua mtoto wangu na kwenda kumtupa chumba cha maiti kwa
haraka, wakati walishindwa kumuhudumia kabisa.” Joshua kimya
akisikiliza. “Nilitoka
naye pale mapokezi, nikaenda kukaa naye nje, nikiwa nimempakata tu. Ila
nilijiwa na uchungu wa ajabu sana. Sikuwahi kuomba maishani kama ule
usiku nikiwa peke yangu. Pengine niliomba kama nilivyomuombea mama yao kipindi
hiki mgonjwa mpaka akafariki. Niliomba Joshua, mpaka nikaanza kusikia mwili wa
Naya unaanza kupatwa joto.” “Waw!” Joshua akashangaa
akisikia mwili kusisimkwa. “Kufupisha
habari, kuanzia siku hiyo ndipo nilipogundua Mungu yupo, ila yeye ndiye
atendaye wala si mwadamu. Ikaniongezea ujasiri wa kuombea watu hata nikiwakuta
na hali mbaya ya namna gani huwa siogopi kuomba kwa kuwa nilishakutana na Mungu
aliyenitendea. Naya ni muujiza wangu ambao nashindwa kuutangaza kwa
wengine kwa kuwa hakuna aliyeshuhudia usiku ule nikiwa nimempoteza na kurudishiwa.
Natamani wangempima kisha akaonekana alikufa na Mungu kumrudisha, lakini Mungu
alinitendea mimi tu, nikatambua nguvu na uweza wake, basi.” Joshua
akabaki akimshangaa Mungu. “Naya huyo
amekua mikononi mwangu si kwa mama yake, kwa sababu ya kupishana kidogo tu na
Bale. Mama yake alikuwa karibu sana na Bale tokea anazaliwa, nikaona Naya
anakua kama mtoto ambaye hatukuwa tumejiandaa kuleta mdogo wake, ndipo ikabidi
sasa mimi kuongeza umakini kwa Naya asijisikie mtoto wa nje ya familia. Kama
aliyesahauliwa au haiitajiki. Wakakua pamoja na wote nikiwatizama tabia zao.” Akaendelea. “Katika
watoto wangu wote, ni Bale peke yake ndiye mwenye uwezo mkubwa sana wa
kuthubutu mambo magumu hata kama wote wakimpinga. Hilo nililiona tokea mdogo.
Anayo karama na kipaji kikubwa sana ambacho Mungu alimjalia, na shetani amejua
hilo ndio anataka kumtumia vibaya. Lakini Naya hakuumbwa hivyo hata kidogo.
Bila mtu kumshika mkono, hana uwezo wa kwenda mbali na ndio maana unaniona nipo
naye karibu sana.” “Popote
unaweza kumuweka Bale, akaweza kujiongoza na kuishi lakini si Naya. Naya
akikuamini wewe, basi unaweza kumfanya mateka wako kirahisi sana. Ukimuongoza
vizuri, na kumtia moyo, ujue atafuata na kufanya vizuri sana. Lakini mtu
huyohuyo akatokea kumyumbisha kwa maneno au kwa matendo kidogo sana, anarudi
chini kabisa na kupoteza dira. Hiyo ndio siri na udhaifu wa Naya. Yupo hapo
alipo kwa kusimama naye kwa maombi haswa maana alikubali
kujiingiza kwenye mahusiano ambayo hayakuwa na msimamo. Kwa hiyo kila
yalipoyumba, basi na yeye aliyumba.” “Hili
lililompata Bale, ingekuwa ni Naya, angesharudi nyumbani kwa haraka sana na
angekuwa amepoteza dira kabisa, sio kama hivi Bale alivyokusudia kuendelea
kupambana mpaka kufikia lengo. Nilipogundua huo udhaifu wa Naya, ilinibidi mimi
nivae sura ya umama ili kumfikisha hapo alipo. Hana kimbilio ila mimi,
na sasa hivi afadhali namuona ameweza kuegemea kwako. Ndio maana kauli ya
kwamba, ‘sitaolewa mpaka wewe uwepo,’ zipo nyingi sana kwake na ametoka
kunitumia tena ujumbe kama huo, sasa hivi.” “Kweli!?” Joshua
akashangaa. “Kabisa. Na
usifikiri anatania! Kwa kuwa kwake kuingia kwenye hiyo ndoa, anajua nitaingia
naye huko. Kwamba ugumu wowote atakaokumbana nao huko, anajua nitakuwepo naye.
Kwa hiyo hicho anachokisema ni zaidi ya maneno tu. Anamaanisha kabisa.
Haamini kama anaweza kukaa huko sawa bila mimi kuwepo. Chochote kikitokea
kwangu ujue atachanganyikiwa na kuharibikiwa kabisaa. Na akiharibikiwa
Naya ujue na Zayoni hivyohivyo. Zayoni hayupo kama Naya, japo kwa haraka haraka
unaweza fikiri wanafanana. Zayoni yeye anatakiwa kujua maisha tu kwa uhalisia,
basi. Anaweza kuishi kwenye mazingira yeyote lakini anaweza asimfikie Bale, ila
haitaji sana kushikwa mkono kama Naya ambaye Zayoni anamtizama kama mama wa
pili.” “Ninachotaka
kukuomba ni hiki. Japokuwa kiapo chetu kiliishia ni umrudishe Naya nyumbani
pindi mkishindwa,...” “Haitatokea mzee wangu. Nilikuahidi na ninaahidi tena.”
“Hapana Joshua. Naomba unisikilize tu. Hakuna anayeingia kwenye ndoa akiwa
anategemea talaka. Talaka ni moja ya ajali mbaya sana za ndoa.
Wengi huwa hawapangi. Lakini huwa zinatokea. Ikitokea kwenu, kwa kuwa mimi
nimekusoma na nimekuona si myumbishwaji. Unao msimamo wako. Unaaminika kwenye
maeneo mengi niliyokufahamu mimi, basi usiache kuwa karibu na Naya.
Mahusiano hayo ya kimapenzi yakiisha, ubaki undugu kati yenu. Simama
naye ili asiyumbe tena.” “Kama si
kuzembea kwetu sisi wenyewe kwenye maeneo fulanifulani na kumsababisha Naya
kujiingiza kwenye aina hiyo aliyojiingiza kwenye mahusino yanayotugarimu mpaka
sasa, nina uhakika Naya angekuwa mbali sana. Kumekuwa na kuyumbishwa yumbishwa
sana ndio maana unamuona ni kama yupo anaanza. Lakini anao utajiri mkubwa sana
ndani yake. Lakini kama binadamu wengine wote, akawa nahuo udhaifu. Hapo
ulipomfikisha na kumfanya anaweza kufikiria na kutenda, tafadhali pasiyumbe
tena. Simama naye tu. Anakupenda na anakuheshimu wewe. Hata akiwa
amekasirika najua atakusikiliza tu.” Akaendelea. “Nimehangaika
sana kwa maombi na juhudi kufika hapo mliponisaidia wewe na mwenzio
kufika. Naomba wanangu wasije kuanza tena chini. Naomba simama kama kaka yao.
Hayo mengine Mungu akijalia, basi tutashukuru. Ni hilo tu. Nimeona nikwambia
kwa kifupi ili uelewe na nisiwaache wanangu bila muelekeo endapo chochote
kitatokea kwangu.” Baba Naya akahitimisha. “Japokuwa
naamini utakuwepo. Na Mungu atakurudisha kwetu salama. Naamini utaona utuuzima
wangu na Naya. Nakuahidi sitamuacha Naya, hata iweje. Kwanza nahisi mimi ndio
namuhitaji sana Naya kuliko anavyonihitaji mimi. Halafu, kwa kuwa nimepata
baraka zako, basi na mimi nakuahidi kusimama nao kama kaka kwelikweli. Naona ni
bahati mzee wangu. Sikujaliwa familia, naona Mungu ameamua kunikabidhi nikiwa
na umri huu, akijua nipo tayari na ninaweza. Basi naamini Mungu atanisaidia.”
“Nashukuru Joshua. Basi acha nikuage kwa sasa. Mtanipigia mkiwa pamoja. Na kama
kuna maswali wewe nipigie tu, nitapokea. Na kama sitapokea basi nitarudisha
simu yako.” “Bila shaka.” Hapo baba Naya akapata amani kabisa. Akili ikahamia kwa
Bale. Baba Naya, Tunduma. Alifika
mida hiyo akiwa amekusudia kutafuta nyumba za kulala wageni ndipo aanze
kumtafuta huyo mtu aliyepewa jina moja tu la Mbabe. Aliposhuka tu akatafuta
taksii na kuomba impeleke kwenye nyumba za kulala wageni. Aliyemchukua kwenye
gari yake akawa mcheshi kwelikweli mpaka akamfanya baba Naya amuulize.
“Unamfahamu Mbabe?” “Sana tu. Mpaka kwake napafahamu. Walimuweka ndani huko
mpakani, ametolewa kwa dhamana. Anajuana na wengi yule! Akiwa ndani, wengi
watakufa njaa. Macho ya wengi yanamwangalia. Kwa kifupi Mbabe ni ulaji wa wengi
wenye vyeo na mamlaka. Huwezi kumgusa yule! Yaani waliposikia amekamatwa
mpakani, bila kuomba msaada unaambiwa watu wenyewe wakaenda kumtoa!” Akaongea
kishabiki bila kufikiria anazungumza na nani. “Walimuweka
ndani kwa kosa gani?” Hilo swali likamfanya mpaka dereva amgeukie. “Vipi?” Baba
Naya akamuuliza. “Kwani wewe nani?” Akamuuliza kwa wasiwasi kidogo na kumfanya
baba Naya afikirie kwa haraka ili asije haribu. “Kwa nini unamuulizia Mbabe
halafu kumbe humjui yeye mwenyewe wala habari zake!?” “Nimepewa namba yake
tokea mbali. Nina shida ambayo nimeambiwa ni yeye tu ndiye anayeweza
kunisaidia.” “Kwa hiyo nikupeleke kwake moja kwa moja?” “Hapana. Nipeleke
kwanza hotelini kisha nitamtafuta kuanzia hapo.” Akashangaa yule dereva
ananyamaza kabisa hata uchangamfu ukamuisha. Baba Naya akamtizama. “Vipi
bwana?” “Mimi sitaki kupelelezwa. Ni hilo tu.” Akanyamaza na kumshangaza baba
Naya. Naye akanyamaza. Akamfikisha hotelini, akamuacha nje kabisa kama
anayemkimbia. ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ Baba Naya
akachukua chumba na kuingia ndani baada ya kuandikisha jina lake. Giza lilikuwa
limeshaingia. Akaonelea ampigie simu Naya kisha Joshua ili kuwataarifu kama
amefika salama. “Nipo na Joshua hapa. Naweza kuweka spika.” “Afadhali.
Itarahisisha.” Akakubali baba Naya. “Pole na safari.” Akamsikia
Joshua. “Asante lakini ilikuwa safari nzuri na huyo mtu, ni kweli
anafahamika. Dereva taksii aliyenibeba alionekana kumfahamu vizuri ila ni kama
mtu anayeogopewa sana hapa kwenye huu mji. Na kuna kitu ambacho aliniambia
kimenitia wasiwasi.” “Ni nini baba?” “Alisema kuwa alikuwa amekamatwa. Akawekwa
jela, ila ametoka kwa dhamana. Nilipomuuliza alifungwa kwa kosa gani,
akabadilika kabisa. Ni kama mtu aliyeingiwa hofu!” “Isijekuwa ni mtu hatari
baba!” Naya akatahadharisha. “Inavyoonekana
ni hatari. Lakini yeye ndio mwenye jibu la mtoto wangu! Siwezi nikaishia
njiani. Hata kama analindwa na askari wote wa huu mji, lazima nikutane naye tu,
anipe majibu yakueleweka.” “Mimi naomba kuwa mwangalifu baba Naya. Mwenzio bado
nakuhitaji. Maisha yang..” “Naomba utulie Naya. Tumeomba, amini kila
kitu kitakuwa sawa.” “Hapana Joshua. Mama tulimuombea sana, lakini akatuacha.
Mungu hapotezi ila sisi ndio tunapoteza. Mimi naomba uwe makini baba Naya.
Tafadhali sana. Ujue umebaki peke yako kwenye maisha yetu. Hatuna kimbilio.
Umeona ndugu zenu jinsi walivyo! Naomba uhakikishe unarudi nyumbani.” “Naya!” “Naogopa
Joshua. Naogopa sana. Zimebaki siku 5 tu, tufunge ndoa. Mimi bila baba sitaweza. Unafanya
kitu kizuri sana na mimi nakuunga mkono baba. Lakini naomba usiyatupilie maisha
yako kabisa. Ukiona kumekuwa kugumu na hatari, rudi tuanze kutafuta ushauri kwa
wataalamu wa mambo ya sheria, watushauri pakuanzia kuliko kuwa tu huko ukihatarisha
maisha yako huku hujui kama Bale ni kweli kwa hakika yupo matatizoni au
amechagua kuendeleza maisha yake bila sisi. Halafu ikatugarimu maisha ya baba
wakati mwenzetu yeye kumbe hana anachopoteza! Hapana baba. Mimi na Zayoni
tunakuhitaji. Kama yeye Bale hatutaki sisi tu..” “Naomba tulia Naya, mama. Ndio
nimefika tu.” Baba yake akamtuliza. “Acha
niulize kwa amani tu. Nikiona ipo hatari, basi nitarudi tuanze upya kiutaalamu
nikiwa nina angalau taarifa za kuwapa chombo cha usalama, wajue pakuanzia.
Nitakuwa mwangalifu. Na nikiona mambo yanachukua muda mrefu na hayana sura ya
kueleweka, pia nitarudi kuomba msaada wa kisheria. Sitaki muahirishe harusi
yenu kwa ajili ya hili.” “Hapo sawa.” Naya akaitika. “Hapana Naya. Umejibu
bila kufikiria na kuelewa ni nini nimekwambia.” Naya
akatulia kidogo na kufikiria. “Nimekwambia
sitaki uharishe harusi yenu. Tarehe hiyo iliyopangwa, tuliomba kwa Mungu
na imepata kibali.” “Sijaelewa.” Hapo Naya akakaa
sawa. “Kwamba unasema nifunge harusi aidha wewe upo au haupo?!” Naya
akauliza kwa mshangao kana kwamba anahisi hajamuelewa vizuri baba yake. “Unanisikia
Joshua?” Baba Naya akamuuliza na Joshua akiashiria Naya
ameelewa. “Nakusikiliza mzee wangu.” Joshua
akaitika. “Shetani ni mvurugaji, na hajawahi kupenda ndoa tokea kuumbwa kwa
misingi ya ulimwengu. Alipoona Adamu na Hawa wanaamani na mipango yao
inaendelea vizuri pale bustanini na Mungu yupo katikati yao, akaingia kwa hila
katikati yao. Akaanza kwa kumvuruga Hawa akijua mbegu yake ya uharibifu
haitaishia kwa wao wawili tu ni mpaka kwa watoto wao. Nafikiri mnakumbuka kilichotokea
kwao na mpaka watoto wao kuja kuharibikiwa mpaka kaka mtu kumuua mdogo wake.”
“Mimi nakumbuka.” Joshua akaitika Naya alishaanza kulia. “Ukimpa
nafasi shetani kidogo tu, hana mipaka. Ataingia na kuwavuruga mno. Lazima kazi
zake tuzidhibiti na tuzikomeshe kwa maneno na vitendo. Unanisikia
Naya?” Kimya. “Safari hii hutaanza, hutasita
njiani wala hutayumbishwa hata na mimi. Mnazo baraka zangu tayari.
Tumefunga tukimuomba Mungu sisi wote na kina Magesa. Tukaikabidhi siku hiyo
mbele ya Mungu. Mungu ameikubali na mambo yote yapo sawa, sasa hakuna kurudi
nyuma. Unanisikia Naya?” “Naamini utarudi mapema baba. Hakika Mungu aingilie kati jamani!
Haitakuwa sawa kwangu. Mama asiwepo na wewe pia baba jamani! Sidhani kama
Joshua atajali kuahirisha kwa siku chache tukusubirie.” “Hapana
Naya. Unakumbuka ni kwa muda gani umekuwa ukisubiri hiyo siku?” “Muda
mrefu baba.” Naya akajibu akilia sana. “Basi
nataka usiahirishe. Jua nipo na wewe kwa maombi. Kabla, wakati na baada ya hiyo
harusi yako. Shetani ni kama simba aungurumae. Anazunguka zunguka akitafuta mtu
wakumrarua. Hila zake ni dhahiri kabisa. Anayo mitego kila iitwayo leo.
Hasinzii wala halali. Huwezi jua tukiahirisha kwa hili, kesho atarudi kwa lipi!
Unanielewa Naya?” Naya akaendelea kulia. “Na kuliko
kuendelea kukwama kwenye hili, ukilia usiku kuchwa, nakuomba ukumbuke kwenda
kushugulikia maswala ya shule ya mtoto. Hataki kukaa bweni, lakini kwa muhula
wa kwanza lazima aende wakati tukijipanga upya. Nimezungumza naye sana tu.” “Hataki
baba. Mimi nikiongea naye anaishia kulia. Asijeona tunamtupa sababu mama
hayupo! Naomba tumuache tu, baba. Mimi nitakuwa naye na nitajua chakufanya
shule zikifungua. Asije akafeli akiwa huko shuleni ikawa haina maana tena ya
yeye kuwepo shuleni. Nilimuahidi mama, nitakuwa naye tu. Usiwe na wasiwasi.” Naya
aliongea akijaribu kumtuliza baba yake lakini na machozi mengi yakitoka kama
mvua. “Hapo
utakuwa umefanya vizuri. Lazima Zayoni asome. Asiishie kwenye biashara kabla ya
kupata shahada hata moja. Mama yake amesisitiza hilo. Ametaka asome.” “Atasoma
mzee wangu. Na mimi nitahakikisha anasoma. Usiwe na wasiwasi. Sisi tunakuombea
huko mambo yaende vizuri, na urudi salama.” “Nashukuru
Joshua. Acha nikapate muda wa maombi, kisha nipumzike. Nianze siku ya kesho
nikiwa nina mawazo yaliyotulia.” “Usiku mwema.” Joshua akaaga. “Naya mama
mzazi?” “Mimi nipo baba, nitakupigia wakati nalala.” “Naomba
upunguze wasiwasi. Na muamini Mungu kila kitu kitaenda sawa.” “Nitakupigia
baba. Naomba usiache kupokea, lasivyo nitakuwa na wasiwasi.” “Basi
sitalala mpaka nikusikie.” “Hapo sawa.” “Si na
asubuhi tena ni hivyohivyo?” Naya akacheka akifuata machozi. “Mimi
sitanii bwana!” “Mbona hilo nalijua mama! Asubuhi nayo nihakikishe napokea simu
bila yakuchelewa.” “Hapo sawa.” Kidogo wakacheka. “Naomba
kabla hatujaagana mzee wangu, naomba uende mapokezi. Omba jina kamili la hiyo
hoteli, namba zake za simu na huyo muhudumu aliyekuwepo hapo sasa hivi.” Joshua
akafanya wote watulie. “Ni kwa nia nzuri tu. Sijui kwa nini nimejisikia hivyo.
Ila naona si wazo baya na sisi tujue ulipo. Naomba tusikate simu. Uliza halafu
Naya atakuwa akiandika. Ikiwezekana omba mpaka kuona kitambulisho chake.
Tusirudie kosa tulilofanya kwa Bale. Aliondoka, hakuna aliyefuatilia alipo na
kwa nini hakuwa akipokea simu zetu. Ilitupasa kufanya kama hichi unachokifanya
mzee wangu sasa hivi. Sasa hivi tunalipa garama ambayo tungeweza kuepuka
kabisa.” Joshua akafanya wote wajifikirie. Baba Naya akatoka hapo
chumbani kwake na kwenda mapokezi bila kubisha. Wakamsikia
muhudumu ni kama anakataa kutoa kitambulisho chake baada ya baba Naya kuomba.
Lakini Naya akamwambia baba yake basi ampe namba ya hapo na jina
la hapo. Kisha apige simu akiwa hapohapo na ahakikishe anapokea kujiridhisha
hajampa namba za simu za uongo na baba yake apige picha kitabu cha wageni kwa
nje na ndani aliposainisha yeye baba Naya. Baada ya ubishi wa muda mrefu
kidogo, wakafanikiwa bila kitambulisho cha huyo muhudumu wa zamu. Naya
akaandika. Na baba Naya akawatumia hizo picha alizopiga za hicho kitabu na
akatoka nje kabisa, akapiga picha na hilo jengo na kuwatumia. “Jambo la
mwisho kabisa. Ila usione ni usumbufu mzee wangu.” “Bila shida.” Baba
Naya akaafiki kwa haraka. “Kwenye simu yako naomba nenda kwenye Settings,
kisha bonyeza Location, ili kuweka On. Hiyo itatusaidia
kujua popote ulipo.” Mpaka Naya akashangaa. Kimya
kidogo. “Umefanikiwa baba? Au unataka arudie?” Naya
akamuuliza. “Au mtumie hayo maelekezo kwa ujumbe na afanye sasa hivi kabla
hatujakata simu.” “Nimeshafanikiwa. Si kinachotakiwa ni pale ndani ya Location kwenye On kuwe
na rangi ya bluu?” “Ewaaa! Hapo sawasawa kabisa.” Hapo Joshua
akaridhika ndipo wakaagana. Naya Kwa Joshua. Naya
akamgeukia Joshua. “Kwani wewe utakubali kufunga ndoa bila baba Naya?” “Unataka
jibu la ukweli au la uongo?” “Nataka jibu la kwamba tutafunga ndoa baba Naya
akiwepo.” “Sawa. Tutasubiri. Ila na yeye ameongea kitu cha msingi
sana na ukweli mgumu pia. Sasa na mimi nataka kujua Naya. Utakuwa tayari
kusubiri mpaka lini? Je, ikatokea baba harudi pengine mpaka mwezi, hajampata
Bale, na yeye amesema nilazima ampate Bale.” “Siku zikikaribia bado hajampata,
nitamkatia tiketi ya ndege. Aje awepo kwenye harusi yangu kisha arudi kuendelea
kumtafuta Bale.” “Unakimbia kunijibu swali langu Naya, na wewe unajua.” “Wewe
usiwe na wasiwasi, tutafunga ndoa yetu siku tuliyopanga.” “Sawa.”
“Na baba Naya akiwepo.” Naya akaongeza. Joshua akamwangalia na kunyamaza. Hakuna Msiba Usiokuwa na Mwenzie. Usiku
alipoondoka tu Joshua baada ya kula pamoja hapo nyumbani kwao, na kuhakikisha
kila kitu kipo sawa, akazungumza na walinzi ndipo akaondoka, Naya akakimbilia
kumpigia simu baba yake. “Baba Naya?” “Nipo mama. Umenikuta nimepiga
magoti, ndio namalizia kuomba.” “Basi omba na mimi baba. Nimeingiwa hofu, sina
amani!” “Sababu ya wasiwasi wakufikiri sitakuwepo kwenye harusi
yako?” “Kumbuka tulivyoomba pamoja baba! Kweli usishuhudie? Hakika omba
na mimi baba. Umpate Bale akiwa salama ila tu anahangaika kutafuta pesa, wewe
urudi salama. Mwambie Mungu asinijaribu kupita uwezo wangu. Hakuna mlango
utanitoa hapo nikatoka salama.” “Naomba tulia tuombe. Na wewe mwambie Mungu wako
hayo uliyoniambia sasa hivi. Ila sio kwa kilio hivyo na kumtisha Mungu. Wewe
msihi. Mungu anatuwazia mema.” “Na mimi nimepiga
magoti.” Baba Naya akaanza. Kabla
hajafika mbali Naya akiwa anamsikiliza baba yake akiomba, akasikia kishindo
kama mtu anamgongea kwa nguvu. Wakatulia. “Ni nini baba?” “Kama
wananivunjia mlango wangu!” Naya akashituka sana. “Piga
kelele baba. Piga kelele kwa sauti ya juu.” Naya akaanza yeye
kupiga kelele. Akasikia mshindo unaongezeka. “Ni kina nani nyinyi na kwa nini
mnavunja mlango wangu, badala ya kugonga tu taratibu?” Naya akamsikia baba yake
akiuliza kwa sauti ya juu akishindana na ile kelele. Mwishoe
akasikia mshindo mkubwa, mlango ukijigonga ukutani kama uliokwisha vunjwa, baba
Naya akasikika akipiga kelele kidogo, mshindo mzito. Kimya. Hakumsikia tena
baba yake. “Mbembeni, ameshazimia huyo.” Naya akafunga mdomo
kwa nguvu ili aweze kusikia yeye asisikike kule kwenye simu ya baba yake. Kwa
mbali akasikia vishindo. Kisha kimya. Alishituka Naya, akabaki amepiga magoti
akitetemeka. ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ Zayoni
akaingia. “Kuna nini Naya!? Umepiga kelele kwa sauti mlinzi amekuja
kunigongea!” “Wamemchukua baba kutoka hotelini. Wamemteka nyara. Nimesikia
Zayoni, nilikuwa nikiomba na baba.” “Mimi
naogopa Naya.” Hapohapo Naya akampigia Joshua. “Vipi,
nilijua upo na baba!?” Joshua akapokea na kuuliza swali. “Wamemchukua
Joshua. Wamemvunjia mlango wakati tunaomba naye. Wakampiga nikisikia, akapoteza
fahamu ndio nikasikia mmoja anamwambia mwenzie wambebe.” “Naomba
usilie, fikiria. Wakati mimi napiga simu ya pale alipochukua chumba.” Joshua
akakata, akageuza kurudi Kiluvya akiwa amechoka na amekaribia sana nyumbani
kwake akapumzike. Baada ya
muda Joshua akampigia tena Naya. “Naya?” Joshua
akaita baada ya Naya kupokea ahijua kwa hakika atakua akilia sana. “Nipo
Joshua. Najaribu kufikiria.” “Safi sana. Hapo sawa, kuliko kulia, tutashindwa
kufikiria.” Joshua hakutegemea, hapo kidogo akampongeza. “Sasa ile
simu ya pale uliyopiga akapokea yule muhudumu sasa hivi haipatikaniki ila ya
baba inaita tu. Nimefikiria kwa haraka. Kama kweli waliingia kwa mshindo,
inawezekana ile simu imeruka chini ya kitanda au baba ametoa sauti akaiweka
mfukoni kwa haraka wakati wakimvamia, kuendelea kuipiga, cha kwanza, kama ipo
chini ya kitanda ni kuimaliza charge ambapo tutashindwa
kuifuatilia mtandaoni. Nitampigia sasa hivi James, anisaidie kuniambia
inaonyesha simu ipo wapi. Na cha pili sasa, kama yupo na hao watu wabaya,
kuendelea kumpigia bila sisi kujipanga, itasababisha wajue anayo simu na
kuitupa njiani tusijue wanapompeleka.” Naya alikuwa kimya
muda wote akisikiliza tu. “Unanisikiliza
mpenzi wangu?” “Nasikiliza. Ila Joshua?” Naya akamuita kabla
hajakata. “Nipo Naya, wangu.” “Nilazima nimpate baba.” “Najua mpenzi wangu.
Najua.” Joshua akaafiki na kukata simu. Naya
akanyanyuka kwa haraka kama anayekomboa wakati. “Unafanya nini, Naya?” “Lazima
nikamtafute baba, Zayoni. Naondoka kesho asubuhi.” Naya akajibu akikomboa
wakati. “Unataka kuniacha peke yangu!?” Zayoni akashangaa sana, akawa kama
amemkumbusha Naya. Akaweka kila kitu chini. Akatulia akifikiria anafanyaje na
huyo kijana wa kiume aliyelelewa naye humohumo ndani ya nyumba lakini hakuwa
akimfahamu kwa umbali huo. “Lazima nikamtafute baba. Nina uhakika kuna kitu
kinachomuhusu Bale, wanaficha. Tukimpata baba tutajua juu ya Bale pia.” “Basi
twende wote. Siwezi kubaki peke yangu.” Naya akafikiria akijua kabisa kwenda
naye ni kuongeza mzigo, ila jinsi ya kumkatalia. “Tumsubiri
Joshua tujipange kwa pamoja. Ni kama baba ametuacha wote kwenye uangalizi
wake.” “Hata mimi baba alinipigia simu alipokuwa Mbeya, akasema nimsikilize na
kutii kila kitu atakachoniambia Joshua. Anaonekana anamsimamo na anauwezo
mkubwa sana ndani yake. Nikimfuatisha sitakuwa kama nilivyo. Akasema amemuona
‘ndiyo’ yake huwa inabaki kuwa ‘ndiyo’. Hayumbishwi. Akaniambia nahitaji mtu
kama huyo ili kufika mbali. Nisiwe mbishi.” Naya akaingiwa na wasiwasi. Akajaribu
kufikiria ndipo akagundua ni kama baba yao alikuwa kama akiacha wosia. “Mungu
tusaidie!” Naya akaanza kulia. “Unafikiri na yeye
atakufa?” Zayoni naye akauliza akianza kulia tena. “Sijui,
Zayoni. Lakini Mungu aingilie kati kwakweli.” Wawili hao wakaanza
kulia hakuna wakumbembeleza mwenzie. Wakajaribu tena kumpigia Bale kwani Joshua
aliwaonya kutompigia simu tena baba yao. Simu ya Bale haikuwa hewani. Akataka
kumpigia tena Malon lakini akasita na kuacha. Wakabaki kumsubiria Joshua. Baada ya
muda Joshua akaingia akisikika akizungumza na simu. Simu ya Naya ikaanza kuita
chumbani. Akaikimbilia akidhani pengine ni baba yao, lakini alikuwa ni Nanaa. “Tupo
njiani. Pole sana.” “Asante.” “Unahitaji kitu chochote tukujie nacho?” “Maombi
tafadhali. Naombeni mumuombee baba yangu jamani.” “Usilie.
Naona kaka James anahangaika huko, atafanikiwa tu. Tunakuja.” Naya
akakata simu na kutoka chumbani kwake. Akamkuta na Joshua naye amemaliza
kuzungumza na simu. “Nataka
kukipambazuka, niende kumfuata baba. Nitumie maelekezo na picha alizotutumia,
mpaka pale hotelini.” “Naomba kwanza utulie Naya.” “Siwezi
Joshua. Ninachoomba ni unisaidie kubaki na Zayoni kwa muda huo nitakapokuwa
safarini halafu na mambo ya harusi yaendelee kama alivyosema baba. Mpaka siku
ya karibu na harusi kama sijampata nitarudi tufunge ndoa, kisha nirudi
niendelee.” “Naomba ukae.” Akamvuta mkono mpaka kwenye kochi. “Cha
kwanza, hatuwezi kwenda tukiwa hatujui tunakabiliana na watu wa namna gani.
Tukienda bila kujipanga, kilichompata baba kitatupata na sisi, kisha wote
kuishia mateka. James anafuatilia simu ya baba kujua alipo. Huyu niliyekuwa
nikizungumza naye ni GM. Anakuja hapa. Lakini pia anaye mtu anafahamiana naye
kwa karibu huko Tunduma. Amempigia simu. Anaonekana anaweza kutusaidia.
Anamfahamu huyo mtu baba aliyekwenda kumtafuta ili kupata habari za Bale. Na
kumbe ni tabia zake kutumia vijana wadogo kumfanyia biashara zake za magendo,
na mengine mengi GM anakuja kutueleza kwa undani. Kuanzia hapo ndipo tutajua
chakufanya. Vile nilivyokupigia simu nikakukuta umetulia, naomba endelea
hivyohivyo. Ukitulia tunaweza kufikiria.” “Nashukuru Jos..” Simu ya Joshua
ikaanza kuita tena. Enzi Zarudi! Joshua
akaitoa mfukoni kwa haraka. Kisha Naya akamuona amekunja uso. Akabaki
akiitizama simu yake. “Haiwezekani!!” “Ni nani!?” Naya akauliza baada yakuona
sura ya Joshua ni kama hakuwa kiitarajia hiyo simu. Ikaita mpaka ikakata Joshua
bado akiwa anaitizama na mshangao mkubwa sana usoni mwake. “Ni nani!?” Naya
akauliza kwa wasiwasi zaidi. “Benadina!!” Hapo Naya akanyong’onyea maana kwa
ule mshangao wa Joshua, kumbukumbu haikuchukua muda mrefu kumrudia. Swali
likabaki kwa Naya kama bado walikuwa wakiwasiliana! Na kwa nini bado Joshua
anayo namba yake mpaka siku hiyo! Na huyo Benadina anaujasiri gani wa kumpigia
Joshua mida hiyo! Naya akainama akifikiria akiwa na wasiwsi zaidi. “Kumbe
bado Benadina yupo kwenye picha! Na matatizo yangu haya ya familia yasiyoisha,
huyu Benadina anayepiga simu usiku kwa uhuru wote huu, si atafanikiwa kwenye
moyo wa Joshua!” Wivu ukaanza kumsumbua Naya. Lakini akajirudi baada
ya kukumbuka hata yeye anayo namba ya simu ya Malon na bado wanawasiliana. Hofu
ikaanza kuongezeka. “Nitampoteza baba na Joshua! Mungu nisaidie.” Akawaza
Naya, kisha akajifuta machozi akiwa amejiinamia. Simu ya Joshua ikaanza kuita
tena. Safari
hii Joshua akapokea. “Kumu, anaongea.” Akaanza hivyo Joshua
baada ya kupokea. “Ni mimi Benadina!” “Okay?” Joshua akaitika hivyo
kama anayemwambia kwa hiyo! Kidogo Naya akapata faraja. “Nimekuwa
nikikupigia ila ukawa hupokei, ndio ikabidi kutumia hii namba ambayo najua
unaifahamu siku zote.” “Huyo aliyekupa namba yangu, alisahau kukwambia huwa
sipokei namba nisizozifahamu.” “Ndio maana imenibidi kuhangaika mpaka kupata
namba yangu ya zamani. Tena nimeinunua kwa mtu na kwenda kuandikishana naye
polisi kwamba nimeichukua mimi na sitafanya uhalifu wasije kumkamata yeye.” Joshua
kimya akisikiliza. “Nimehangaika
hivi kwa kuwa nina shida na wewe.” “Nakusikiliza.” Joshua
akaongeza. “Naomba isiwe kwenye simu Jo. Tafadhali sana. Naomba tukutane na
nimuhimu sana.” “Kwanza umepiga wakati mbaya sana ambao umenishangaza. Huu ni
usiku sana. Unapata wapi ujasiri wakunipigia simu mida hii ya usiku hivi?” “Ni
kwa sababu nina shida sana.” “Sidhani kama shida ndiyo imekufanya
upige mida hii, ila dharau.” Naya akashukuru
Mungu. “Hapana Jo,
naomba usikasirike na ku…” “Niite Joshua.” Joshua akamkatisha na
kuendelea. “Mbali na kuwa huu ni muda mbaya, unaonyesha dharau zako kwa wazi
kwangu, pia sio kipindi sahihi ambacho naweza kukusaidia kwa lolote.” “Kabla
hujasikiliza jamani!?” “Ni kwa kuwa mimi nakufahamu. Na nina uhakika na uwezo wangu. Mimi
sitakuwa msaada kwako. Umeendelea na maisha yako zaidi ya miaka 15 sasa, na..”
“Ni miaka 21 na miezi..” “Naomba nimalizie. Nisingependa kukukatia simu,
tafadhali nisikilize. Kwa kipindi hicho chote umeweza kuwa salama bila mimi,
naamini utakuwa sawa tu. Tafuta msaada kwengine ila si kwangu. Kwaheri.” Mpaka
Naya akashangaa na kumwangalia. “Na kitu
kingine cha mwisho, tafadhali USINIJARIBU.” “Sikuwa na nia ya kukuudhi Joshua.”
“Na ninakuonya, usirudie kunipigia tena simu. Mchezo wowote unaotaka kuucheza,
sipo tayari na sina muda. Nimekuwa muwazi kwako, na kwa heshima tu. Tafadhali
kuwa muungwana.” Joshua akakata simu, na kutoka kabisa pale. Akamuacha Naya
na mshangao wa muda mpaka akasahau kama amepoteza baba. ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ Baada ya
muda wakasikia mlinzi akifungua tena geti, wakajua ni kina Magesa. Baada ya
kuegesha gari, wakamsikia Joshua akimsalimia mama G, Naya akajua wamefika wote
kwa pamoja. “Poleni sana.” “Asante mama, na poleni na nyinyi kwa usumbufu,
najua usiku umeendelea!” “Hata kidogo. Bado hatukuwa tumelala. Naya
anaendeleaje?” Wakasikia majibizano yakisogelea mlangoni, Naya akasimama na
kwenda kuwafungulia mlango. “Karibuni.”
“Pole bibi harusi wangu.” “Asante. Ila nina tumaini. Nashukuru Mungu Joshua
alitumia akili, akachukua habari nyingi na majina ya alipokuwepo baba. Nina
imani tutampata tu.” “Hata mimi nimemwambia, alifanya vizuri sana. Imekuwa
rahisi mno.” Akaongeza Geb. “Kweli?!” Naya akauliza kwa wasiwasi tena. “Ooh
yeah.” “Karibuni ndani ndipo tuzungumze vizuri.” Joshua akaingilia
nakuwakaribisha. “Samahanini jamani, nimeshindwa hata kuwakaribisha! Nimeingiwa
hofu, mara tumaini linanijia! Basi imekuwa mvurugano tu.” “Tunaelewa wala
usijali.” Akajibu mama G. “Vipi
Zayoni?” Geb akamsalimia. “Mimi naogopa.” Akajibu Zayoni akitetemeka midomo.
“Pole. Lakini nina imani kubwa kwamba tutampata baba. Kwa muda mfupi sana,
tumefika pazuri.” Geb akamtuliza. “Huyo jamaa, Mbabe kama anavyojiita, ni jina
la mtaani tu. Nimetumiwa jina lake kamili. Na ni kweli anayo pesa kulingana na
huo mji wake na analindwa na wale askari walioharibika kwa kupenda hongo.
Anasema ni ngumu kumfikia, lakini anasema palepale wapo askari ambao
wamechoshwa na tabia zake. Hiyo ndio itakuwa nguvu yetu.” “Na
kutokana na taarifa pamoja na picha ambazo Joshua amenitumia, nikamuuliza. Ni
kweli ile nyumba ya kulala wageni ipo na jina ni sahihi. Sio mbali na kituo cha
mabasi, kitu kinachofanya wahuni wengi kupapeda hapo kwa kuwa panafikika kwa
urahisi na ipo mjini. Amenipa namba ya simu ya askari ambaye anamuamini sana,
amesema yeye anaweza kutusaidia kwa karibu. Na yeye hatamwambia mtu haya
tunayoyajua sisi juu ya baba Naya.” Geb akaendelea. “Ndio
nasubiria azungumze naye. Atutambulishe kwake, ndipo na sisi tumpigie.” “Lini?”
Naya akauliza kwa haraka. “Nimemwambia huyu jamaa yangu, atusaidie iwe leo
kabla hapajapoa. Najua usiku umeendelea sana. Lakini nimemuomba ampigie simu
huyo askari na kumwambia tunamsubiria yeye tu. Akitoa baraka zake, na sisi
tumpigie. Wakati James anafanya uchunguzi wake, basi na sisi tupate mwenyeji
huko wa uhakika.” “Samahani Geb. Sijui kama nikuchanganyikiwa! Sijaelewa.” Naya
akaongea kwa wasiwasi. “Chakwanza
naomba utulie Naya. Najua ni hali ngumu, lakini tulia na kuendelea kuomba.
Shetani ni mvurugaji mno. Na furaha yake ni kuona anapoharibu, kunatoa
mafanikio mazuri. Kila wakati jambo zuri linapotaka kutokea, ambalo haliendani
na mipango yake, huwa anamtindo wa kutupia jambo hapo. Akijua ameshindwa
kabisa, ila tu nia ni kuwavuruga, zaidi akili. Nguvu yako itakuwa ni kuzitambua
hila zake na kubaki umesimama imara.” “Kama alivyosema mfamle Daudi kwenye
bibilia Zaburi 23:4. Kwamba, ‘nijapopita kwenye bonde la
uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya,’ si unakumbuka
ni kwa nini alisema hivyo?” Mama G akamuuliza. “Alijua
Mungu yupo naye.” Naya akajibu taratibu. “Ewaaa! Basi amini hata hapa, sasa
hivi, na kule baba alipo, Mungu wetu yupo naye. Tena inawezekana akatoka huko
akiwa na jambo zuri, hiki kilichompata, kikawa faida wala si hasara. Tulia
kabisa uuone na wewe mkono wa Mungu.” “Amina.” Naya akajibu na kuinama kama
anayefikiria hapo kitini. Joshua akamvuta mkono. “Naomba usiogope Naya.”
“Naogopa mambo mengi Joshua! Naogopa sana. Kumbuka hatuna mama. Bado Bale
hatujui alipo! Baba naye hatujui alipo! Harusi imekaribia. Sijui
tukiahirisha kwa hili, inakuwa mpaka lini!” Naya akaanza kulia. “Natamani
isingekuwa wakati huu jamani! Zimebaki siku 5 tu na mimi natakiwa niwe
nimeolewa! Halafu haya yote yanatokea!” “Baba yako alinipigia
simu jana jioni, Naya. Mimi sijui ni kwa nini! Sijui Mungu wake alimuonyesha
nini! Lakini alinisihi sana tarehe tuliyopanga harusi ifungwe, nihakikisha ndoa
inafungwa.” Naya akazidi kulia. “Na mimi pia alinipigia mida ya mchana
hivi. Akaniachia maagizo hayohayo. Nilishangaa kidogo mpaka mikampigia mama,
nikamwambia maagizo yote aliyoniachia baba Naya. Tena mimi alinipigia akiwa
njiani akielekea huko.” Geb akaongeza kwa mama yake. “Ni kama aliyejua kama
kuna jambo baya linaweza kumpata!” Nanaa akaongeza. Naya akaendelea kulia. Joshua
akamvuta tena mkono kama kumrudisha hapo. “Kesho tunakwenda mimi na GM.” Naya
akashituka sana na kumwangalia Joshua kisha Geb. “Ndicho nilichokuwa
nikikwambia. Tutatumia msaada huo wa James na huyo polisi wa huko. Kuna jamaa
yetu wa usalama naye nimemuomba anitafutie askari ambaye atakubali kuongozana
na sisi kesho. Tutaondoka hapa sisi wanne, na ndege ya asubuhi kama
tukifanikiwa kuipata. Ili itusogeze karibu na huo mji, kisha nimemuomba huyo
jamaa yangu aje atupokee. Kesho hiyohiyo tutahangaika kwenye huo mji, mpaka
tumpate baba Naya na kujua maswala ya Bale kwa hakika.
Nashauri tutulie.” Akaongeza Geb. “Zayoni
na Naya, tunafanya kila tuliwezalo, kumpata baba na Bale. Hatutakubali
kushindwa kirahisi hivi. Pateni muda wa kupumzika, na sisi acha tuondoke
tukajipange vizuri.” Naya alifurahi sana mpaka akajikuta anapiga magoti. “Jamani
nawashukuruni sana. Asante Joshua mpenzi wangu. Geb, asante sana. Wewe Nanaa
ndio naogopa utanichoka!” “Sio rahisi kiasi hicho na shetani anajua. Amekutana na
sisi, atahangaika mpaka aelewe safari hii amecheza pabaya. Aache utani!” Nanaa
akajibu. “Mama
G, nakushukuru mama yangu.” “Wewe usilie na usipige magoti. Kila kitu
kitakwenda sawa na mapenzi ya Mungu wala si michezo ya shetani yatatumia kwa
wakati. Sisi tumeshamtambua na hila zake. Huwa akipita sehemu tunamjua kabisa
na kumshugulikia. Usiogope. Tulia. Jua ndoa ipo na kesho tutapata majibu ya
baba pamoja na Bale.” Joshua akamsaidia kukaa. “Pole
Naya. Pole sana. Naamini kila kitu kitaenda sawa.” “Sasa
hivi na mimi nimepata amani.” Yakaanza maombi hapo. Wakamsihi Mungu kwa
kutubu na kujitakasa. Wakamuombea baba Naya huko alipo pamoja na Bale ambaye
sasa habari yake ikawa imebadilika. Hofu yakuwa pengine yupo hatarini na yeye
ikawa bayana. Wakamuombea. Kisha wakakabidhi mipango yote kwa Mungu, mama G
akiwa ndio kiongozi wao. Mpaka wanamaliza wakawa wameongeza kiwango cha ujasiri
si woga tena. Simu ya
Geb ikaanza kuita, akaipokea kwa haraka. “Naomba nikuweke kwenye
spika, nipo na yule ndugu yangu niliyekwambia tutakuwa naye huko.” “Hamna
shida.” Mtu wa upande wa pili akajibu. Geb na Joshua wakatoka nje
kuzungumza na huyo mwenyeji wao wa huko Tunduma. Wakapata na namba ya huyo
polisi, naye akakubali kuzungumza nao. Wakampigia. Wakamueleza kwa kifupi habari
nzima juu ya baba Naya na sababu iliyompeleka huko kuwa ni kumtafuta Bale na
amechukuliwa akiwa anazungumza na binti yake. “Mbabe ni
jeuri kweli sababu ya watu wanao mzunguka. Na huwa kuna mambo anafanya ya
udhalilishaji kabisa akijua hakuna wakumgusa, ila uuaji sio asili yake labda
awe ameanza sasa. Kwa nilivyowasikia, itakuwa amemchukua kwenda kumtisha tu ili
aogope na kuondoka kwa sababu ni kweli biashara zake anategemea vijana. Sasa
nina habari ingine inaweza kuwashitua kidogo lakini msikate tamaa.” “Ni nini
tena!?” Akauliza Joshua. “Siku
chache zilizopita, alikuwa amekamatwa huko Zambia. Wakamfunga. Ikasikika
alikuwa na vijana wake wengine wawili, ambao huwa wanamsaidia kupitisha mizigo
yake mpakani. Kilichoniudhi na kuniumiza zaidi ni vile alivyotolewa yeye tu
dhamana. Akatoka rumande, na nasikia ni kama amekana kabisa kuwa hakuwa pamoja
na hao vijana! Eti anasema hao vijana walikwenda kwa mipango yao binafsi yeye alifanya
kuwaonyesha tu njia na alishawapa madhara kabla ya kwenda lakini eti wao vijana
walikubali kwenda naye. Lakini inavyosemekana, na mtu wake wa karibu kabisa ni
kwamba alivuka nao mpaka, au alikwenda nao ili kumsaidia kupitisha mali
zake, akiwa amewaahidi eti wakifanikiwa, atawalipa asilimia fulani ya hiyo
mizigo. Sasa walipokamatwa ndipo amewakana ili asije akawajibishwa!” Joshua
na Geb wakaumia sana. “Sasa
hakuna wakumwajibisha?” “Kwenye huu mji ameweza kushika wakubwa wengi. Anakula
nao, na wengine wanasema ni kama anawafanyia wengi wa hao wakubwa biashara,
kisha wanalipana humo kwa humo. Kwa hiyo kuwekwa kwake ndani ni kukwamisha
wengi, kitu ambacho hawawezi kukubali. Sijui kama mnanielewa?” “Sisi hatutaki
matatizo na yeye. Tunachotaka ni watu wetu, basi. Ila akijidai mjuaji, hapo na
sisi hatutakubali.” Joshua akatahadharisha. “Kabisa. Hapo hatutanyamaza
wala kutulia. Kesho tutakuja na watu wa usalama. Tunaomba na wewe uungane na
sisi.” Akaongeza Geb. “Mimi bado
ni mkazi wa hapa, jamani. Baada ya yote haya nitabaki huku. Naomba niwasaidie
kuwapa muongozo tu lakini sio kuwa kimbelembele.” Joshua na Geb wakaangaliana. “Hata mpaka sasa umeshakuwa msaada wa kutosha. Tunashukuru. Hiyo
kesho tukija..” Wakaweka mipango yakueleweka ndipo wakaagana. ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ Wakarudi
ndani kuwaambia mipango yote na kile walichosikia kutoka kwa huyo afande. Nalo
hilo likawa jambo jema. Wakazungumza mambo mawili matatu, kina Magesa
wakaondoka, akabaki Joshua na kina Naya. “Nashauri Zayoni akapumzike. Amelia
muda mrefu sana.” “Kichwa kinaniuma.” Akalalamika. Naya
akampa dawa za maumivu, akaenda kupumzika, ndipo wakabaki wao wawili. “Nikuulize
swali Joshua?” “Juu ya Benadina?” “Hapana. Baba kwanza. Unafikiri alijua kama
kuna baya litampata ndio maana alikuwa akiacha ujumbe kwa kila mtu?” “Sijui
Naya. Pengine ule wasiwasi alikuwa nao juu ya Bale na habari za huyo mwenyeji
wake huko zilishamuogopesha lakini kwa kuwa alishakusudia kwenda, akakubali
liwalo na liwe, ila sasa akawa na wasiwasi, na hakutaka awaache pabaya. Si
lazima ikawa alipata maono ya nini kitamtokea! Naomba usiwe na wasiwasi Naya.
Tutembee kwa hatua. Tutakubaliana na hatari ya kesho, kesho yenyewe. Leo baba
ametekwa akiwa mzima na katikati ya maombi. Kwa sehemu tumejua mtekaji si
muuaji ni mtishaji tu. Tumemuomba Mungu amlinde huko alipo. Naomba tuwe na
imani.” “Nakushukuru kwa kusimama na mimi Joshua. Asante.” Joshua akamuhurumia. Naya
akafikiria. “Kwa hakika kama isingekuwa wewe, nahisi sasa hivi ningekuwa
nimechanganyikiwa. Fikiria ndio hii hali ingenikuta na mchumba ni Malon!
Ndio yupo kwenye kile kipindi chake cha kupotea na mimi ndio nipo hivi!”
“Hajakutafuta tena?!” “Hapana Joshua. Sasa fikiria haya ndio maisha niliyokuwa
nayo na yeye. Anakuacha katikati ya hali kama ile niliyompigia na kumwambia
kabisa nina shida! Amepotea. Atakuja kurudi wakati mwingine tena, akiwa na
mipango yake. Lakini Joshua, Mungu amekuleta kwangu, naomba Benadina asinipokonye.”
Joshua akafikiria kidogo. “Nini?”
Ikabidi Naya aulize baada yakumuona amekunja uso na kutingisha kichwa. “Sijui
Naya! Lakini kuna kitu hakipo sawa juu ya Benadina.” Joshua akanyamaza tena
kama anayefikiria tena. “Sijui ni kwa nini, lakini nahisi kuna jambo zaidi ya
hiyo simu. Tuache tu, lakini naomba usitishwe na Benadina. Huyo mtu sijamsikia
kwa muda mrefu sana. Sana. Eti leo, nikiwa nataka kuoa, yeye alishaolewa
na ana watoto juu, ndipo anitafute kuwa anataka msaada wangu! Hapana
Naya. Kuna kitu kinachoendelea. Ila tuyaache tu. Na wewe naomba utulie.
Nitarudi, tutafunga ndoa yetu, changamoto nyingine tutaendelea kupambana nazo
tukiwa ndani ya ndoa.” “Kwa hiyo umekubali na wewe tuendelee!?” Naya akauliza
kwa unyonge kama anayetamani jibu jingine. “Kabisa.
Sio lazima ikawa sherehe, ila ndoa lazima Naya. Tunastahili kuishi pamoja.
Sitajali hata kama tutakuwa sisi tu kama tulivyokuwa hapa na kina Magesa,
tukala viapo vyetu vya ndoa, kisha tukaja kufanya sherehe wakati mwingine. Hilo
naomba ulifikirie na ukubali tu. Ona huku unakoishi, na kule ninakoishi mimi,
halafu kipindi kama hiki! Vita yetu itakuwa rahisi tukiishi pamoja, karibu,
kama mke na mume! Itaturahisishia. Au unaonaje?” “Ni kweli. Hata mimi natamani
Joshua. Ukweli najiona kabisa nipo tayari kuishi na wewe. Wala sioni haya
kusema.” “Hapo nashukuru. Basi tuombe Mungu kila kitu kiende sawa. Kitakachobadilika
ni aina ya harusi tu, lakini sisi tunaendelea na ndoa yetu.” “Sawa.”
Wakakubaliana. Naya akahamia kwenye kochi alilokuwa amekaa Joshua. Kochi dogo
tu, lakini linaweza kukaa watu wawili. Akajisogeza karibu, akapitisha mikono
kama kumkumbatia kwa nguvu juu ya kiuno karibu na mbavuni, akamlalia Joshua kwa
upendo. “Namshukuru
Mungu kwa ajili yako Joshua. Wewe ni wa kuaminika. Hata baba ameliona hilo.
Amemwambia na Zayoni, akusikilize.” “Kweli Naya?!” Joshua hakutegemea.
Akamshungulia pale alipokuwa amejiegemeza. “Ndivyo alivyoniambia Zayoni usiku
huu ulipoondoka. Binafsi mimi nishahidi wa hili. Najua umechoka, lakini ona
ulivyofikisha hili jambo mbali kama uliyekuwa umejipanga! Umetafuta watu sahihi
wakutusaidia na kusimama na sisi. Umelibeba hili jambo kama baba Naya ni baba
yako!” “Ni baba yangu, Naya.” “Hapana Joshua. Najua unajua ninachomaanisha.
Heshima uliyompa baba imefanya mpaka hata kina Geb wanamuheshimu sana. Mpaka
najisikia vizuri nikimuona mtu kama Geb jinsi anavyozungumza na baba! Najua yote
ni kwaajili yako. Heshima na thamani uliyompa, ndio imefanya na wengine
wamchukulie hivyo. Hata yeye baba ameliona hilo na akaniambia. Nashukuru mpenzi
wangu. Asante.” “Karibu, na naomba usilie. Twende ukalale.” “Hapana Joshua wewe
ondoka, nitakuwa na wewe kwenye simu mpaka ufike, ukilala na mimi ndio nilale.
Sasa hivi hofu imepungua kwa asilimia kubwa, nenda tu kapumzike.” “Basi
nitakupigia na asubuhi. Nitaanzia ofisini. Nikafanye vikao vya asubuhi, niweke
mambo sawa, ndipo niondoke.” Joshua akaondoka baada ya kuagana na Naya. ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~ Usikose
Muendelezo kujua kitakachoendelea kwa baba Naya, na Bale. Wote wapo wapi? Nani
anahusika na kumteka nyara baba Naya? Benadina naye anatokea wapi tena?
Nani amempa namba ya Joshua? Kwa nini iwe sasa hivi? Usikose
Muendelezo. |
Kuhusu Msimulizi.

Hi, I am the author of NaomiSimulizi Blog.This blog is to provide you with daily stories and share my personal style.
Blogu Marafiki
-
-
Love At First Sight - Sehemu ya 12.16 hours ago
-
-
DAG Project : Young Women Meetup1 year ago
-
Zinazosomwa Zaidi
-
T unda alitamani isiwe siku ile au alfajiri ile tena. Ndio kwanza alikuwa akipitiwa na usingizi. Alijitahidi kumuonyesha hajamsikia. Akage...
-
U l ikuwa ni mzozo wa muda mrefu sana. Bado Tunda alikuwa amesimama pale pale katikati ya sebule, akisikiliza tu. Mwishowe aliitwa dada wa...
-
Bado ndoto za mafanikio, UTAJIRI kushinda familia fulani, kuhangaika kufanikisha familia iishi kwenye jumba fulani, zuri na la kifahari, k...
-
Kesho yake Chezo aliamua kumfuata Malon nyumbani kwake. Bado Chezo hakuwa ameoa, baba yake ndio alikuwa mfanya biashara kama Malon. Malon ...
-
Hadithi hii ni kazi ya utunzi tu. Majina, sehemu na matukio yote yaliyotumika kwenye hadithi hii ni mawazo ya mtunzi wa hadithi hii. ...
-
Kwa kuwa baba yake na wadogo zake wakiume walimudu ile biashara ya kusambaza mayai na maziwa. Wakati mwingine kuku, Naya akajikuta yupo tu...
0 Comments:
Post a Comment