![]() |
“Pengine
inaweza isiwe wakati muafaka sasa hivi, lakini nilitaka kuwashukuru. Geb na
mkeo, pamoja na Joshua pia.” Wote wakaongeza umakini kama ambao wanataka kusikia
zaidi. “Baba ameniambia yale fundi wenu anafanya kule na nguvu nyingine ya watu
mliyomuongezea ili kukamilisha vizuri na kwa haraka. Nashukuru. Najua
nimeshamshukuru Joshua tena na tena, lakini na nyinyi nawashukuru sana.
Imemchangamsha sana baba na amepata tumaini la ajabu! Alikuwa akinimbia kwa
hakika upo wakati wa Mungu na ukifika, huwa Mungu mwenyewe
anasimama kwelikweli ili kuhakikisha alilokusudia linatimia. Anasema alikuwa
akiomba bila kuchoka, huku akisubiri lakini hakujua kwa hakika, Mungu atatenda
vipi ili kukamilisha makubwa aliyokuwa akimuomba. Ila ameamini huwa anatumia
yeyote ili kukamilisha jambo lake.”
“Anasema
hakuwahi kufiri kwa umbali huo mpaka alipomuona akitembea kwake akiwatumia
nyinyi watu baki tu. Joshua aliposikia tu wazo lake, anasema ikawa ni kama
amelizungumza kwa upya kwenye sikio la Mungu moja kwa moja, na kuwatuma nyinyi
wote kusimama na yeye. Baba yangu ni mkimya sana. Mnaweza msiyasikie haya yote
kutoka kwake mwenyewe, na mkaelewa furaha yake ndio maana nikoana niwafikishie
shukurani zake na zangu. Asanteni sana. Nawashukuru sana. Baba yangu
anaimani ile inayowakera wengi na wakati mwingine anadharauliwa kwa hiyo imani
yake mpaka kuonekana ni kama hajui anachoongea na pengine mzubaifu. Lakini kwa
mara ya kwanza, nimeona nyinyi mliweza kumsikiliza na kuamini mawazo
yake mkaweza kusimama naye. Ndio maana nimeona nisiache huu wakati upite tu,
niwashukuru.” Wakamsikia Nanaa anacheka.
“Kwanza
karibu Naya. Ila sisi wenyewe na mama tulikuwa tukimsengenya Geb. Tukasema amempenda
baba Naya, na kumuheshimu sana Joshua. Geb sio mtu wakupigia simu
mafundi akiwa nyumbani au tuseme kuzungumzia mambo a kazi nyumbani zaidi
anapokuwa na wanae, labda iwe dharula napo hapokei simu mpaka kule kazini
wanamjua. Ikifika jioni au akitoka kazini, simu zote zinahamia kwangu. Sasa
kuja kumuona anahangaika na mafundi na kuwaeleza nini chakufanya kule kwenye
sehemu ya baba Naya! Tena mpaka usiku! Mama mwenyewe alikuwa akishangaa ila
akasema tumuache tu.” “Ni kwa kuwa ni mtu anayeonekana anajua nini anataka.
Mtulivu, yupo tayari kujifunza halafu...” Wakamuona Geb kama amesita hivi
akifikiria.
“Anyways, ni
mtu mzuri.” Nanaa akacheka. “Wewe umempenda tu. Si useme!” Geb akacheka kama
anayefikiria. “Nafikiri kuna namna Mungu amefanya mioyo yetu ipatane tu.
Nikizungumza naye sioni ugumu wa kufikia moyo wake au mawazo yake na akili.
Sijui kama mnanielewa?” Geb akauliza na kuendelea. “Kuna mtu unapata naye muda,
hata kama ni lisaa kwa muzungumzo tu. Kila anachozungumza, unaona kabisa sicho
kilichopo moyoni mwake. Hupati kile kitu sahihi. Na si kuwa anakudanganya, ila
inakuwa ngumu ku..” “Inamaana baba Naya hana hila?” Nanaa akamsaidia kwa
kifupi.
“Ewaa!
Unaweza kusema hivyo, lakini pia anacho kitu cha tofauti, nimeshindwa kukisema
ila ni mtu ambaye...” Akasita tena. Wote wakacheka. “Hana hila aisee, halafu
mnyenyekevu mno. Huo uzubaifu unaosema Naya, kwangu naona ni unyenyekevu tu.
Baba yako anao uelewa wa mambo! Sana. Ukiwa tayari kusikiliza, anayo
machache, lakini anao uelewa. Si mjinga. Ila ni..” “Hekima?” “Sawasawa Joshua.
Ni mtu niseme kwa jinsi nilivyomsoma kwa haraka, anahekima hii ya duniani. Ya
kawaida tu. Anaweza kuishi na yeyote, na popote. Awe huyo mtu yupo juu sana.
Kifedha, elimu au hata maneno mengi ya kujifanya yupo juu sana kuzidi yeyote
yule, lakini baba Naya hatahadaiki na kupoteza dira atabaki mtulivu tu. Halafu
akiwa na mtu wa chini, pia, atajua jinsi ya kuwa naye. Anajua ni wakati gani
wakuzungumza na yeyote. Hata kubaki kimya kwake, ukiwa makini naye, utagundua
ni jibu pia.” Geb akaendelea.
“Anasikiliza
na anakubali mabadiliko ndio maana nimemuona itakuwa rahisi kukimbia naye
kufika mwendo mrefu kwa urahisi kuliko kuanza na mtu ambaye kwanza mbishi.
Mjuaji. Hana nia. Inachukua muda mrefu sana kwanza kumfikia yeye mwenyewe ndipo
ije maswala ya biashara. Inachelewesha. Nafikiri mmenielewa.” “Tumekuelewa
mpenzi wangu. Kwa kweli baba Naya kapendwa. Sifa zote hizo ni zake tu,
na zinatoka kwako Geb, mume wangu!?” Wakacheka sana.
“Lakini
ni kweli. Pengine iwe nimemsoma vibaya tu. Ila ndivyo alivyo. Ni watofauti.”
“Naenda kumwambia mama!” “Sasa unaenda kumwambia nini!? Mimi sijasema kitu cha
ajabu.” “Ushawahi kuyasema yote hayo kwa nani, Geb wewe!? Huwa unabaki kutizama
tu mtu, na kunyamaza.” Geb akacheka na kutingisha kichwa. “Nitakupigia kesho,
Naya. Muwe na usiku mwema. Kila kitu kitakwenda vizuri kabisa, wala msiogope.”
“Asanteni.” Wote wakashukuru kwa pamoja. Kina Magesa wakaondoka. Angalau
wakaagana wakicheka sio kama walivyotaka kuondoka kabla.
Naya&Joshua
Naya
akamshika mkono Joshua na kumvuta mpaka kwenye gari yake akiwa anamuongoza
njia. “Ulisema kuachana sio chaguzi tena. Acha kutishwa na Malon. Maneno ya
Zayoni pamoja na Bale au hata mimi mwenyewe. Yaani kutishwa kwa jinsi
nilivyoishi na Malon. Usitishwe. Nimeishi vile na Malon kwa kuwa sikuwa
najua kama naweza kupata mtu bora kama wewe na pia kwa ukweli kwangu
hakuwa mkatili, kasoro yake ilikuwa moja tu, umalaya. Vinginevyo alikuwa
mtu mzuri ndio maana nilikuwa najikuta narudi kwake. Ninachotaka kukuhakikishia
Joshua ni kuwa nakupenda na sitakusaliti sababu ya Malon. Kwa
kuwa nilishaamua kumuacha hata kabla yako. Wewe ni muujiza wangu Joshua. Mungu
alikuleta akijua nakuhitaji. Siwezi kurudi nyuma. Naomba usitishwe. Simama na
Naya huyu aliyekushika hapa.” Joshua akavuta pumzi kwa nguvu na kubaki
akifikiria bila kujibu.
“Hakika utanioa
Joshua.” Ikabidi tu Joshua acheke. “Kwa lazima?” “Hakika tena. Mimi nimechoka
hii michezo yakuanza kila wakati. Mwenzio napenda maisha kama hivi Nanaa.
Kuolewa na kuwa na watoto wake. Akatulia nyumbani kwake na mume anayesema
anampenda na yeye anampenda. Hayo maisha nayatamani Joshua, wala sitaona haya
kusema. Na nakutaka wewe Joshua Kumu.” “Wala sina mpango wa kukuacha Naya. Ila
napata ujasiri zaidi kukusikia ukisema hivyo. Wewe Naya. Hapo unanipa ujasiri.”
“Basi mimi ni wako Joshua Kumu. Wala usiwe na wasiwasi, tuombe Mungu
atufanikishe kwenye mipango yetu tu. Mengine tuachane nayo. Mimi nakupenda
mpenzi wangu.” Naya akaongea kwa kubembeleza. Yakaanza mabusu hapo sehemu ya
kuegeshea magari. Yakaendelea yakutosha tu mpaka akamuona ametulia kabisa,
ndipo safari yakurudi Kiluvya ikaanza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika
nyumbani wakamkuta baba Naya sebuleni. “Mmekuwa na wakati mzuri huko?” “Mambo
yalitaka kuharibika kidogo, baba.” Naya akamsimulia baba yake. “Nisikilize
Naya. Kwa jinsi alivyonisimulia Zayoni na shauku aliyokuwa nayo Bale juu ya hii
safari, kwa hakika sasa hivi yupo sehemu sahihi kwake. Na mimi si mtu sahihi
kabisa hata kumtafuta kwa sasa tena kwa haraka, sababu yupo kwenye kurekebisha
makosa yangu yote anayojua nimefanya maishani ili asije kuwa kama mimi.
Mwache kabisa. Akitaka kututafuta, atatutafuta tu. Lakini acha kuwaingilia. Kaa
pembeni ” Naya akatulia.
“Na
Joshua na wewe usihangaike na familia yangu. Angalia ya kwako Mungu anayotaka
kukupa. Jenga kwako, lasivyo utajikuta unawekwa njia panda na kushindwa kuwa
mwaminifu kwa Mungu kwa atakachokukabidhi. Sijui kama unanielewa?”
“Nakusikiliza mzee wangu.” “Yapo mengi sana yanaendelea hapa ndani, na sitaki
uchanganywe na kujikuta unapoteza dira. Sikutegemei kwa chochote hapa nyumbani
kwangu. Sitegemei utukomboe kwa chochote kile. Au sikutegemei eti ndio uanze
kufanya mambo humu ndani kwetu. Tafadhali endelea kujenga kwako bila
kuyumbishwa ukimtegemea Mungu. Na uache kujilaumu juu ya Bale. Hawa wawili wana
maelewano yao, hata wewe usingeweza kuingilia. Malon ni mfano wa kuigwa
kwa Bale. Hakuna yeyote kati yetu ambaye angeweza kumtuliza Bale ila Malon. Ungeweza
kumatafutia kazi, kisha kuja kuiacha katikati na kumkimbilia Malon. Hudhani
huko nako ungeharibu?” “Na mimi nimemwambia hivyohivyo.” Naya akadakia.
“Kabisa.
Mwacheni kabisa Bale. Mimi mwenyewe ndio nitajaribu kwa ujumbe kumuuliza kama
alifika salama. Akijibu sawa. Asipojibu nitabaki kumuombea. Basi.
Nyinyi msijihusishe nao kabisa.” “Nimeelewa mzee wangu.
Na ninaamini kila kitu kitakwenda sawa kabisa. Tuendelee kumwamini Mungu
pamoja. Najua sijakuwa kwenye familia kwa muda mrefu tokea mama aliponiacha.
Lakini ninauelewa na mambo ya familia. Familia ya Naya itakuwa familia yangu.
Ni Mungu mwenyewe ameniweka hapa, sina chakukwepa na siwezi kuepuka chochote.
Tafadhali kama kuna uwezekano wa kunishirikisha chochote bila kificho msisite
na msione ni usumbufu. Sisi ni familia sasa. Muwe huru na amani. Unapoona
anahitajika Naya, naomba ujue ni mimi pia, kwa hiyo usiwe na shaka, tafadhali
nishirikishe tu mzee wangu.” Baba Naya akanyamaza. Wakatulia.
“Nashukuru
sana kwa kunitambulisha kwa kina Magesa. Naona amekusudia kwelikweli kusaidia.”
Baba Naya akavunja ukimya, nakufanya Naya na Joshua kucheka kidogo wakamkumbuka
Nanaa. “Amefanya nini tena?” “Kuna sehemu kuna mtu alikubali mwanzoni
kunikodisha ili kuweza kuhifadhi bidhaa. Nilipokwenda kuzungumza naye jioni hii
kabla hamjaondoka, naona amepatwa tamaa, ameamua kumkodisha mtu mwingine kwa
bei ya juu kidogo. Sasa Geb alitaka fundi wake akapaangalie kama patafaa
kuwekea bidhaa kabla hatujaanza. Sasa nikamjulisha kumwambia kama hilo eneo
sijafanikiwa. Nafikiri atakuwa amemwambia Magesa mwenyewe. Mlipoondoka tu, Geb
mwenyewe amenipigia. Baada ya kuuliza maswali mengi ameomba kama kesho mida ya
saa 6 mchana kama wanaweza kuja hapa na kupaangalia huko nyuma nilikokuwa
nikifuga ng’ombe.” Naya akashangaa.
“Baba,
kwamba uweke huko nyuma!?” “Sijui mama! Lakini Geb anasema Yesu alitema mate
kwenye udongo, akatengeneza tope na kumpaka kipofu, akaweza kuona. Anasema
Mungu anauwezo wa kutoa chochote kutoka udongoni na kukipa uhai, kikawa kitu
cha ajabu sana. Anasema ilimradi kuwe na aridhi, popote, basi chochote kinaweza
kutokea hapo. Anasema ipo nguvu kwenye kile alichosema Mungu kuwa popote
unapokanyaga, amekupa. Amesema anataka kuja kuona nilipokanyaga, na kile Mungu
anataka kunipa.” Wakamsikia Joshua akicheka taratibu.
“Geb
mwenyewe!?” Naya akauliza akishangaa. “Yeye mwenyewe amesema anakuja kesho saa
sita mchana kama nitakuwepo.” “Kweli amekupenda! Mkewe anasema si kawaida yake.
Mzito sana kwa watu.” “Na ana mambo mengi mpaka amenishangaza!” “Wakati wa
Mungu umefika kwako baba yangu. Maombi yako yamefika mbele ya kiti cha enzi,
ndipo anakuinulia watu sahihi kutimiza kusudi lake. Geb ana mambo mengi sana.
Si mtu wakuyafanya yote hayo, ila ni Mungu tu.” Joshua akaongeza.
“Ila
nahofia sana pesa. Kwa mtu kama yule mawazo yake hayawezi yakawa ni ya pesa
ndogo! Sitaki kumkatisha tamaa.” “Maji yameshatibuliwa mzee wangu. Ni wewe
kuingia tu. Usiogope. Geb anajua nini anafanya. Akiwa anakujua wewe ni nani.
Hawezi kuanzisha jambo akashindwa kulimaliza. Acha tuone anakushauri nini, kisha
tuzungumze kuanzia hapo.” “Ila Joshua, hakika nakushukuru sana.” “Ni Mungu,
mzee wangu. Wala si mimi. Amenitumia tu. Na nisingefanya mimi, basi
angekuinulia mtu mwingine. Tumshukuru Mungu.” “Hata na wewe nakushukuru kwa
kukubali kutumika. Asante. Haya yote nahisi pia anafanya kwa heshima yako.
Jinsi mnavyoishi huko. Nashukuru.” “Karibu sana mzee wangu.” Angalau
mazungumzo yakabadilika. Joshua na yeye akaomba kwenda kuona huko nyuma ya
nyumba ya kina Naya. Wakatoka kwenda kuzunguka usiku huohuo nyuma ya hiyo
nyumba.
“Kumbe
una eneo kubwa hivi!” “Ni pakubwa ila nilishindwa tu kupaendeleza. Na mke wangu
alipofariki ndio kila kitu kikakosa maana. Hata mifugo ikanishinda.” “Pole
sana.” “Asante. Lakini najua sikutakiwa kufanya hivyo. Ni moja ya makosa
ninayojutia. Haikuwa biashara kubwa lakini si sawa na kukaa bure na kuanza
upya.” Hapo Joshua hakuongeza akanyamaza.
“Hapa
lazima Geb atatoa kitu kizuri sana, acha atushauri hiyo kesho. Anaakili ya
ajabu sana yule kiumbe. Hafikirii vitu vidogo na dhaifu. Halafu haogopi
kuthubutu. Acha tuone na hapa nako Simba wa kabila la Yuda anataka
kutoa nini!” Joshua akaongea kwa kuhamasika mpaka Naya na baba yake wakacheka.
“Kweli kabisa. Huyu Mungu ana mtindo wake wakustahilisha watu wanao onekana
dhaifu, wasiostahili kwenye macho ya wenye hekima hii ya duniani, kwa makusudi
tu. Ili wanaosikia masikio yao yawashe, na wanao ona wasiamini mpaka wajue na
hapo napo Mungu ametembea na kujibu kwa moto. Acha atembee aweke mambo
sawa na sisi tushuhudie ukuu wake kwa mara nyingine tena.” Joshua akaendelea.
“Wakati
nikilala mtaani. Nikihangaika sina jinsi ya kibinadamu ya kunitoa pale, kipo
kipindi nilikuwa nikimuomba Mungu kama kutimiza wajibu tu, maana ni kweli kwa
akili zangu nilijua fika naomba yasiyowezekana. Nikaendelea hivyo mpaka yeye
mwenyewe Mungu akanihurumia akijua nimeshakata tamaa, ndipo akanikutanisha na
like andiko la (Waphilipi 4:19.)” Wakamuona baba Naya anacheka. “Hata mimi ndio mstari pekee
unaoendelea kunitia moyo kubaki magotini. Maana kwa namna ya kibinadamu mimi
kama mimi nimeshafilisika mpaka mwisho. Nimejaribu mengi bila mafanikio.
Nimekosea kwingi mpaka nikakosa tumaini. Kwa namna ya kibinadamu, mwingine
angenishauri tu nisiendelee kuomba. Niache tu, sistahili. Lakini kila
nikikumbuka hapo, ni kwa kadiri ya utajiri wake Mungu si mimi na
mazingira yanayonizunguka, narudi kuomba na nakuwa radhi kusubiri.”
“Sawasawa.
Kumbe na wewe upo hivyohivyo! Yaani mimi mzee wangu, huo mstari huo, ndio unanipa
ujasiri wakusimama hata mbele ya wakuu. Bila kujali rangi zao wala vyeo vyao na
vile wanavyovimiliki. Hakuna mlango amewahi kufungua Mungu nikaogopa kuingia,
sababu ya huo mstari nikijua atanipa hata hekima kwa kadiri ya utajiri
wake, si wangu.” “Bwana mbona mnashangilia tu wenyewe mimi mstari wenyewe
hata siujui!” Naya akalalamika nakufanya Joshua na baba Naya wamgeukie na
kucheka.
Walishahamasishana
hapo! Baba Naya alipenda sana neno la Mungu. Mkimya, lakini ikifika kwenye
maandiko huchangamka kwelikweli. Hapo akawa amefikishwa kwenye eneo lake.
Akafurahia mpaka ungeona moyo wake. “Baba jamani! Na wewe Joshua acha
kunicheka.” “Unaujua sana mama yangu mzazi! Ni vile haujaushika tu kichwani.
Ila huwa nakukumbusha sana na wewe. ‘Naye Mungu wangu atawajaza
ninyi na kila mnachohitaji, kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya
Kristo Yesu’. Umekumbuka sasa?” “Huo naujua. Ulikuwa hata ukimwambia mama.”
“Basi na mimi huwa na usimamia kwenye maeneo mengi sana.” Joshua akaongeza. “Ni
kwa kuwa unafaaa katika kila eneo la maisha ya mwanadamu. Pale hekima ya
mwanadamu inapopungua, ukidhani umefika mwisho, basi Mungu anakukumbusha ni
kwa kadiri ya utajiri wake. Mungu tu. Anakushusha na kukufanya
umtizame yeye peke yake kama mfamle Daudi alipofikishwa mahali akatambua kuwa
msaada wake ukatika Bwana, aliyeziumba mbingu na nchi. Wala si ufalume wake na
mengi ya thamani yanayomzunguka ila Mungu tu. Acha nikuache Joshua ukapumzike
maana sitamaliza juu ya huyu Mungu.” Wakacheka.
“Lakini
upo na eneo zuri sana. Huna haja yakukodi popote. Na uzuri kampuni yake
inamafundi kabisa, tutamuomba atupe haohao mafundi wake. Huu msitu ukikatwa
vizuri na eneo lake likachanganywa na hayo mabanda yaliyokuwa ya ng’ombe,
kutapatikana gala zuri tu. Tusubiri tuone.” “Asante Joshua.” Naya naye
akashukuru. Joshua akacheka na kumwangalia Naya. “Karibu.”
Wakazungumza wakiwa hapohapo nyuma ya nyumba, ndipo Joshua akaondoka.
Jumatatu.
Kama
kawaida Joshua akaenda kumchukua kwenda kazini. “Nilishakwambia asante kwa kuja
mbali kote huku kunifuata?” “Zaidi ya mara 10.” Naya akacheka. “Wewe ni mchumba
mzuri sana.” “Usizoee. Gari yako imeshafika. Kesho unatakiwa kwenda kukamilisha
kuisajili.” “Joshua!” “Sikutanii. Walikuwa wanahangaikia kuitoa bandarini na
ukaguzi kuhakikisha kila kitu kipo kama nilivyoona kwenye picha. Hakujaibiwa
kitu, ndipo wanataka kutukabidhi.” Simu ya Naya ikaanza kunguruma kwenye pochi
yake. Akashangaa asubuhi hiyo ni nani awe anampigia.
Wazo
likamjia. “Bale.” Akachangamka kutafuta simu yake. Alipotoa akakuta ni simu ya
Malon. Akapoa gafla kama aliyemwagiwa maji. Joshua akamuona. “Nani?” “Mimi
sijui.” “Hamna jina!?” Naya akanyamaza akiitizama ile simu ikiita mkononi mpaka
ikakata. Joshua akahisi. “Ni Malon tena?” Kabla ya Naya kujibu ikaanza kuita
tena. Ikaita mpaka ikakata tena. Kisha ukaingia ujumbe. ‘Ni mimi
Bale. Nilitaka kukutaarifu nilifika salama.’ ‘Kwani simu yako imepatwa na
nini?’ Joshua akamuona anaandika ujumbe bila ya kujibiwa swali
lake. ‘Imekorofisha. Sasa kwa nini hutaki kupokea simu yangu?!’ ‘Hiyo sio
simu yako ni ya Malon. Nipigie kwa simu yako.’ ‘Nimekwambia imekorofisha,
Naya!’ Naya akahisi anamdanganya.
Simu
ikaanza kuita tena. Ikaita na kuita. Joshua kimya. ‘Ni nini
Naya?’ Ujumbe mwingine ukaingia. Naya hakujibu. ‘Inamaana
hatutawasiliana tena!?’ Naya akafikiria kwa haraka kisha akamjibu. ‘Leo
nitakutumia simu ingine, Bale. Ili tuwasiliane ila si kwa kutumia simu ya
Malo.’ ‘Unanitumia simu ingine wapi na wewe hutaki tuongee?’ ‘Usiwe na
wasiwasi.’ Naya akamjibu hivyo na kumpigia simu yake mwenyewe Bale.
Kweli haikuwa hewani. Akaona ampigie simu baba yake.
“Mama
mzazi?” “Kwani ulirudi kulala?” “Hapana. Kwema?” “Mbona sasa sauti yako ipo
kama ulirudi kulala?” Akamsikia kama anahasira. “Nilikuwa
nikiomba mama! Vipi?” Naya akatulia kidogo. “Eti mama, vipi?” “Bale
amenipigia kwa simu ya Malon. Anasema eti simu yake imekorofisha.” “Inamaana
gani?” “Mimi sijui baba. Ila namuhisi vibaya. Bale ameondoka hapa nyumbani
simu yake haina shida kabisa! Naomba ukamnunulie simu kisha umtumie.” Baba
yake akatulia. “Mimi nitakurushia pesa.” “Acha nizungumze nao wote wawili kwanza.” Naya
akanyamaza. “Na Naya.” “Mimi nipo lakini...” Naya akasita. “Naomba
ukatulize akili kazini. Umenielewa?” “Nahisi
nimeshaanza kukasirika baba! Bale ananifanyia makusudi.” “Wewe usiwe
na wasiwasi na Bale. Mimi nitazungumza naye. Na kama kuna uhitaji kweli wa
simu, mimi nitakwenda kumnunulia na nimtumie. Uwe na siku njema. Usiende
kuharibu kazi za watu huko. Katulize akili ili ufanye kazi vizuri.” “Asante
baba.” Naya akakata.
“Samahani
Joshua. Nilikasirika ndio maana niliona nimpigie tu simu baba.” “Mimi
nisingekufanyia hivyo Naya. Siwezi nikakupuuza wewe hata iweje.” Naya akafunga
macho. Hakujua kama Joshua angechukulia hivyo. “Samahani Joshua. Sikuwa
nikikupuuza.” “Ila ni nini Naya? Nakuuliza, hunijibu, unaendelea kuchat, kisha
unampigia simu baba na kuniacha mimi hapahapa!” “Nahisi napaniki Joshua.”
“Unapaniki nini!?” “Nahisi nimeingiwa na hofu mimi mwenyewe. Sitaki
chochote kitokee.” “Sikuelewi!” “Sitaki chochote kitokee kati yetu sisi, halafu
ukaniacha. Napaniki.” Joshua akatulia kidogo kama anayefikiria.
“Huyu ni
Bale akinitafuta kwa kutumia simu ya Malon, anasema simu yake imekorofisha.”
Kimya. “Samahani Joshua. Sijakupuuza.” “Kwanza nahisi hujaelewa Naya. Sipo na
wewe kubahatisha. Sipo kwenye majaribio kwamba najaribu nikiona vinashindikana
nakuacha!” “Kweli Joshua? Sio kwamba...” “Naya, kama wewe ni mke aliyenipa
Mungu, hakuna atakayekutoa kwangu. Vya kwangu huwa Mungu ananipa nguvu
yakuvitunza. Nilikwambia huwa nina vitu vichache na Mungu huwa ananipa uwezo wa
kuvitunza. Nahisi bado hujanijua na kunielewa. Malon hanitishi mimi, Naya! Hata
kidogo. Hata nikimsikia namsikia kwenye upande wa vitisho tu, kama
aliyeshindwa. Wasiwasi wangu ni wewe Naya. Naona umempa nguvu kubwa sana
zaidi hata anavyojua yeye. Yeye mwenyewe anajua amepoteza nguvu kwako ila wewe
huonekaniki hivyo Naya.” “Mimi napaniki kwa ajili yako Joshua! Sitaki
kukupoteza.”
“Hutanipoteza.”
“Unauhakika Joshua?” “Kabisa. Ni vile hunifahamu Naya. Nisingekuwa hapa nilipo
kama ningekuwa mtu wa kuyumbishwa yumbishwa. Naishi kwa vitisho kila siku. Kazi
yangu yenyewe tu ni vitisho tupu. Natishwa na soko la dunia. Natishwa na soko
la hapa ndani ya nchi. Lakini nipo hapa nilipo, na bado nimesimama nikiongoza
kampuni kama ile! Unafikiri ni kwa nguvu zangu?” “Sijui Joshua! Mimi nimechoka
na michezo isiyoisha.” “Basi usicheze.” Naya akawa hajaelewa.
“Mimi ni
wako na nimekuhakikishia kuwa sina pakwenda. Nipo na wewe. Ishi hivyo. Acha
kutishwa na jumbe.” “Naomba unihakikishie hutaniacha nikapotea na kuniacha
nirudi tena kwa Malon, Joshua.” “Hata kama ukitaka mwenyewe?” “Joshua! Hata
kama leo nikaamua kurudi kwa Malon ujue hakuna mwendelezo wangu na Malon.
Ukiniacha leo, ujue ukija kuniona mwakani, nitakuwa Naya huyuhuyu, sina ndoa
ila nimerudi kuwa mpweke zaidi. Mimi namjua Malon, Joshua. Kile umeona
amemfanyia Bale, ndio mchezo wake hata kwangu. Hakujawahi kuwa na muendelezo.
Tunaanza na mipango inayosikika vizuri lakini haijawahi kutimia. Ndio maana
naogopa usije ukachoka na kuniacha kwa sababu yake ukadhani ni mpinzani wako.
Mimi ndio nitabakia kuumia na kubaki mpweke mpenzi wangu. Natamani maisha kama
yale ya Nanaa! Nataka kutulia na mtu wangu. Nakutaka wewe Joshua, ndio maana
unaona napaniki. Sitaki kurudia ule upweke ulionikuta nao. Umebadili maisha
yangu, Joshua! Umeleta tumaini ambalo hata sikujua kama lipo! Sitaki
kukupoteza.” “Hutanipoteza. Nimekusudia kuwa na wewe.” “Kwa hiyo utanigombania
hata iweje?” Hilo swali likamfanya Joshua acheke.
“Usicheke
bwana! Mimi ndio kilio changu kilikuwa kwa Malon. Anichague mimi zaidi ya tamaa
zake na kila kitu, nibakie mimi tu.” “Basi Naya, nitakupigania.” “Kweli Joshua?
Mimi sikutanii. Usije kunibadilikia bwana!” “Nakuahidi Naya.” “Mpaka kifo?”
Joshua akacheka na kutulia mpaka walipofika kazini maana walikuwa wamekaribia.
Akaegesha gari na kumgeukia Naya. “Nitakulinda, na kukupigania mpaka kifo
changu. Wewe ni wangu. Na hutarudi kwa Malon.” Naya akacheka kwa furaha.
“Muone!” “Nimechoka mwenzio! Mimi nakutaka wewe kwa hali na mali. Sitaki eti ije
itokee siku eti wewe upo na mwanamke mwingine sio mimi!” Joshua akacheka sana.
“Kweli tena. Uning’ang’anie mpaka kifo changu.” “Sawa Naya Kumu. Naahidi.
Naapa. Na Mungu anisaidie.” Wakatulia. Akamsikia Joshua anacheka kidogo.
“Nini?”
“Sikujua kama na wewe unanihitaji kwa kiasi hicho! Kila nikipata huo uhakika,
napata moyo. Nakupenda Naya. Na hata mimi sitaona haya kusema nakuhitaji.
Nataka alichonacho Geb. Familia na mke anayemtaka na kumlinda akihakikisha
anabakia kuwa wake daima. Nataka kutulia, nifunge hiki kipengele. Sasa kwa kuwa
wewe umenihakikishia tena, tena kwa umbali huo, moyo wangu umetulia.
Twende tukaanze siku yetu tukijua tulichonacho kinawindwa, na sisi tupo
kukitetea mpaka kifo. Si ndivyo?” “Hivyo viapo vingesindikizwa na mabusu
mazito.” Joshua alicheka mpaka machozi. “Nakupenda Joshua. Nakupenda
sana na ninakuhitaji. Mungu asaidie chochote kisitokee kati yetu.” Joshua
akajivuta kidogo pale kitini na kweli akalitendea haki hilo busu alilotaka
Naya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa
baba Naya akaamua kuanza kumpigia simu Bale. Chakushangaza yake ikaita kisha
ikakatwa. Naya hakuwa akimpata kaka yake, lakini simu za baba Naya ziliingia na
kukatwa mwisho ikawa haipatikaniki kabisa. Akaamua kumpigia Malon. Ikawa ikiita
bila kupokelewa. ‘Mimi ni baba yake Bale, naomba kuzungumza na Bale kama upo naye
karibu.’ Akatuma huo ujumbe na kusubiri bila mafanikio. Akapiga tena,
safari hii simu ya Malon nayo ikawa haipo hewani. Akatuma ujumbe kwa wote
wawili. ‘Tafadhali naomba Bale anipigie. Nawatakia siku njema.’ Akatuma
huo ujumbe lakini hapakuwa na majibu wala hakuna aliyempigia. Mpaka wanakwenda
kulala usiku huo hawakumsikia tena Bale, wala Malon na wote simu zao hazikuwa
zikipatikana tena.
Kwa Bale.
Wakati
mapenzi yamepamba moto kati ya Naya na Joshua, wote wamehakikishiana kifungo
cha mpaka kifo, huku kwa Bale naye akakusudia kutulia na kuwatafuta pindi
atakapofanikiwa sana ili kuja kuwasuta. Na kweli akakusudia kurekebisha makosa
ya baba yake akikumbuka yote aliyokuwa akilalamikia mama yao. Bale akakusudia
kutokuja kuwa kama baba yake. Akajituma haswa huko Mbeya akiwa kwa Malon. Lengo
ni kufanikiwa sana. Na Malon akipiga mahesabu jinsi ya kumrudisha Naya kwenye
hemaya yake, ila akihisi kushindwa na Bale anashindwa kuwa msaada kama
alivyotarajia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Geb
alifika nyumbani kwa baba Naya na kustaajabu sana. “Ni vile ni wewe mzee wangu.
Ningekupa pesa ya kukufanya unipe hili eneo bila kufikiria mara mbili.” Vijana
wake Geb wakacheka taratibu. “Hili eneo ni zuri sana. Hapa tumesimama kwenye
ardhi ambayo inaweza kukupa majibu ya mambo mengi sana.” “Kama nini?” Akauliza
baba Naya akitaka kumsikia Geb. Akamuona anafikiria huku akiangalia lile eneo.
“Kuna aina fulani ya nyumba huwa najenga.” Akamuona ametulia akifikiria.
Akaangaza macho kulia kuchoto, mbele na nyuma. “Kwa vipimo,” Akaanza kutaja
namba za ukumbwa wa eneo. “Kwa kutoa gala na sehemu ndogo ya kuhifadhia vifaa
na ukapata ofisi ndogo tu kwa kutunza kumbukumbu zako, tutahitaji eneo la
ukubwa...” Akafikiria na kutaja huku akiendelea kuangalia.
“Na kwa
harakahara nikiangalia hapa. Hutamaliza eneo lote. Upande ule wenye ule msitu
pale ambako ndipo kunakopokea upepo, naona patafaa. Lazima kujengwa kwenye sehemu
ya juu kidogo kuepuka maji ya mvua yasiingie ndani na kupokea upepo kwa wingi
mazao yabaki makavu. Jengo lenyewe lijengwe kwa muundo wa...” Akawa akiongea
huku akifikiria. Akamuona anafikiria kwa mikono yake sasa kama anayefanya
vipimo. “Hapana. Hiyo inazuia kuweza kuongezeka kwa jengo jingine biashara
ikipanuka zaidi.” Akajipinga mwenyewe akiendelea kuzungumza wote wakimsikiliza.
Kisha
akamgeukia baba Naya. “Unamjua jirani yako upande huu?” “Namfahamu. Ana eneo
kubwa, nyumba yao ndio ipo mbali na hapa. Hapo amepaacha tu.” “Safi sana. Sasa
nashauri ukamtembelee umuombe akuuzie sehemu ya eneo lake linalopakana na eneo
lako kwenye upande wa huu msitu ili huku kwengine usibomoe, uache kwa baadaye
kama endapo utataka kupaendeleza. Mtajie pesa unayojua itamuhadaa nakumfanya
akubali kwa haraka. Usimtajie pesa atakayokutaka afikirie kwanza ndipo aje
akupe jibu. Hapo utafungua jibu la hapana au kurudi kwako na bei kubwa
zaidi.” Baba Naya akapoa. Alichokihisi kwa Geb kinatimia. Akili yake ni ya
kufikiria makuu na yeye pesa hana.
“Ipo hivi
mzee wangu.” Akamuomba wasogee pembeni. “Naomba nipate vipimo kuzunguka huo
msiti hapo.” Akawaambia vijana wake ili abakie na baba Naya peke yao.
Aliporidhika wapo peke yao akamgeukia. “Pesa unaweza kukopa popote na kwa
yeyote, ila si ardhi. Sijui kama unanielewa?” Akaanza Geb. “Wengi wanaweza kuwa
na pesa ila hawana ardhi. Ardhi ni utajiri ambao hubadilika thamani kwa
kuongezeka, ila pesa hubadilika thamani kwa kushuka.” Baba Naya akacheka.
“Aliyeshika ardhi, si sawa na aliyeshika pesa. Nikiwa na milioni 100 leo,
mwakani thamani yake inaweza kushuka, nikajikuta hiyo milioni 100 haina uwezo
kama wewe uliyekuwa na heka 100 mwaka jana na juzi. Wewe thamani yako
itaongezeka, mimi nitapungua. Ndio maana tunakopa pesa kununua ardhi. Wasio na
uelewa ambao wanatusaidia sisi, ni wale wanao uza ardhi kupata pesa wakiwa na
shida. Hiyo ni siri alinipa baba yangu, na wewe nakuibia. Usiogope kununua
ardhi kwa kuwa hupotezi.” Geb akaendelea.
“Walipokonya
mali za baba yangu sababu ya baba kuja kuwa na mama yangu. Hapo maeneo ya
Kibaha. Lakini mzee wangu, nilihakikisha narudisha mali ya baba yangu yote bila
wao kujua.” “Geb!” “Kabisa mzee wangu. Walimuadhibu kwa kosa la kutoka nje ya
ndoa, japo hakumuacha mkewe ila ile tu kuwa na mama pia. Matokeo ya hayo makosa
ni mimi na dada yangu Grace. Wakampokonya jasho lake kwa kuwa yeye ndio alikosa
kwenye ndoa! Akaachwa hana mali. Ni miaka mingi sana, alikufa akiwa hana kitu
kabisa. Ila akahangaika sana akabahatika mali chache ambazo alikusudia akifa
amuachie mama. Na kweli ikawa hivyo lakini naye mama aliuza ili nisome.
Nilihakikisha namrudishia mama ardhi yake kama vile alivyopewa na baba, na
kurudisha mali zote za baba. Zimerudi kuwa ni za Magesa tena. Sio Magesa yule
wa kwanza, ila Magesa mimi na Magesa wajao. Ndugu wa mke wa kwanza waligawana
na kuuza hovyohovyo, nimerudisha zote. Ukiwauliza wao, pesa wamemaliza, ila
mimi nimebakiwa na ardhi ya baba yangu. Sijapoteza. Na inazidi kuongeza thamani
na kuleta utajiri.”
“Ninachotaka
kukwambia ni nini! Ni kwamba unachohitaji ni ‘ndiyo’ ya mwenye ardhi. Hiyo tu.
Ukishapata ‘ndiyo’ yake, unamkabidhi pesa, unatunza ardhi. Halafu itamkie kitu
ile ardhi, jipe muda kama Mungu alivyomtoa mwanadamu kwenye ardhi. Akamfinyanga
kwa makini na ustadi, uone kama hujatawala hili eneo na kila atakayekuona
atakuita heri kwa kuwa umeijua siri! Utakuwa umejiunganisha
na siri ya kiMungu. Ardhi haijawahi kumtupa mwanadamu, mzee wangu.” Mpaka hapo
baba Naya akawa amehamasika.
“Usiogope
madeni. Chukua pesa mfukoni mwa walionazo, kisha fanyia makubwa. Wapo wenye
pesa wanatapanya kwa kuwa hawajui nini chakufanya, kwa hiyo wanapoteza. Wewe
unalo wazo, fikia malengo kwa kutumia pesa zao.” “Nakushukuru sana Geb.
Nitakwenda kisha nitajua ni kiasi gani.” “Hapana mzee wangu. Sasa hivi unahangaikia
‘ndiyo’ ya mwenye ardhi. Usiweke pesa mbele. Akishasema ‘ndiyo’ tu,
hakuna kulalika mpaka umepabadili pamekuwa kwa jina lako wewe. Usiogope pesa, ogopa
HAPANA ya kuuziwa. Ombi lako ukiwa unaenda kwake ni Mungu akupe kibali, akubali
kukuuzia. Nenda ukitaka ardhi sio ukiwa unaogopa bei. Utashangaa jinsi mazungumzo
yenu yatakavyokuwa marahisi. Hutakuwa na hofu, ila ujasiri na atakuuzia tu.”
“Nimeelewa.” Baba Naya akakubali.
“Baba
yangu alikuwa akisema, ‘linalowezekana leo, lisingoje kesho.’ Sijui kama umeelewa?”
“Nimeelewa.” “Basi, sasa naomba mimi nikuache. Tutawasiliana ukishatoka
kuzungumza na mwenye shamba.” Geb akawapa maelekezo wale mafundi wake zaidi
kiongozi wao kwamba apime kisha amtumie vipimo kamili kwenye eneo aliloona,
kisha akaondoka na kumuacha baba Naya na mawazo ya hofu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaona
ampigie simu Naya. Akamuelezea kwa ufupi mazungumzo yake na Geb na hofu
yake. “Sitaki hawa watu wanione kama mzigo, mama. Au wasije niona
mzubaifu. Maana hata kama tukipewa hilo shamba hapo nyuma, tunapata wapi pesa?
Nani wakunikopa? Sitaki mahusiano yakujengwa kwenye misaada, mama. Sitaki aina
hiyo ya mahusiano. Sitaki ujikute unafungwa tena kwenye mahusiano ya pesa,
ukabaki ukilipa fadhila.”
“Kwa jinsi
nilivyowasoma hawa watu baba, ni watu wa umoja. Wakisha kufahamu na kukupokea,
unakuwa mmoja wao. Mimi mwenyewe mpaka imebidi kuzungumza na Joshua. Wanagawana
vitu vyangu vya harusi bila kujali bei. Tena mama yao ndio anavigawa. Hawawazi
bei ila kufanikisha jambo. Nimetoka kuzungumza na huyo Grace muda si mrefu
akiwa na Nanaa kwenye simu. Yaani baba, mimi mpaka nimewashangaa! Shuguli yangu
wameibeba kama yao na kwa moyo mmoja mpaka wamenishangaza! Wote wanaongea lugha
moja na mama yao ndio anawasisitiza hataki wamuharibie harusi.” “Hiyo harusi
yenu!?” Baba Naya akauliza kwa kushangaa.
“Harusi
yetu baba! Mpaka ananishangaza. Amegawa majukumu na anasisitiza anataka aletewe
vitu vizuri, kama mimi naishi pale kwao! Kwa hiyo usiogope baba. Umekuwa
ukiomba sana. Inawezekana huu ndio wakati wa Mungu kwako. Usirudi nyuma, songa
mbele. Nenda kazungumze naye. Mzee Kwayu haonekani kama anampango na hilo eneo.
Hana pesa, ukimwambia unampa pesa hata kesho, hawezi kukataa.” “Sasa huo ndio
wasiwasi wangu mama. Hiyo kesho pesa naipata wapi, mama!?” “Nenda kisha tutajua.
Naomba usiogope.” Akavuta pumzi kwa nguvu na kumuaga mwanae.
‘Joshua!’ Naya
akamtumia huo ujumbe. ‘Nipo kwenye simu na GM, nitaitika mama Kumu.’ Naya
akacheka baada ya kusoma huo ujumbe, lakini akajua Geb anamtaarifu
kilichoendelea. Akatulia. Mipango ikaendelea.
Kimeumana.
Huku kwa
Bale bado hakuwa amewasiliana na mtu yeyote yule wa nyumbani kwao. Juma la
kwanza likapita, na la pili akiwa kwa Malon. Kula kulala, na uwepo wa kila
mmoja kwa mwenzie kuanzia asubuhi mpaka jioni, uhalisia ukaanza kuchukua
sura yake. Akamfahamu Malon ambaye Naya hakuwahi kumfunua kwao. Siye waliyekuwa
wakikutana kwa mazungumzo ya dakika chake kisha kuagana. Sio Malon
anayetaka kuonekana bora zaidi ya wanaume wote wa Naya. Hapana. Malon halisi ambaye
yupo kazini. Anayepambana kwenye maisha. Kwanza anayechukia umasikini
kwa vitendo, pili anayewahakikishia watu shule si kila kitu, na yeye
hakukosea kukataa shule. Hakutaka chochote kitokee kwenye biashara zake, na
hakutaka kugawana utukufu na yeyote yule kwenye mafanikio yake. Kwa hiyo
hakukaribisha akili ya mwingine yeyote yule ili wasije jipatia utukufu kwenye
mafanikio yake. Alitaka mafanikio yake yawe yeye kama Malon, sio mtu mwingine.
Sasa
akakutana na Bale na yeye anao moto wa maendeleo. Afanikiwe na kufedhehesha
watu wa nyumbani kwao. Akitaka kuwa kile mama yake alimsikia
akilalamikia. Kufikiri kwa haraka na kutenda. Kipaji chake cha uongozi, elimu
aliyo nayo, sasa amewekwa kwenye eneo la kazi. Akachangamka kwelikweli akitaka
kuwa kama Malon, asijue anachangamkia sehemu iliyobeba hatima na malengo
makubwa sana ya Malon. Vikaanza kuumana.
“Kabla
hatujakwenda mbali naomba nikuweke sawa, Bale.” Malon akamfuata akiwa katikati
ya wafanyakazi wengine, Bale akijua yeye ni kiongozi wao. “Nataka utambue
nafasi yako hapa. Na hilo sitaacha kuliweka wazi. Si kwako tu, ni kwa kila mtu
anayekuja kunifanyia kazi. Kwa baba yako sikulazimika kwa kuwa
alionekana anajua nafasi yake.” Malon akaanza na kumshitua kidogo Bale.
“Hichi
unachokiona hapa, nimeanza kuanzia chini kabisa nikiwa najijua mimi ni nani,
nafasi yangu na ninakwenda wapi. Hapakuwa na sayansi iliyotumika hapa wala
elimu ya chuo Kikuu ile mnayokaaga nyinyi darasani, wanaume wenzenu
wakiwadanganya juu ya mambo ambayo hata wao hawayajui na yameshindwa kuwaweka
mjini, kama hivyo wewe. Wakishamaliza kuwadanganya huko darasani, wanarudia
dhiki zao na kuwafanya nyinyi wafuasi wao. Mnakaa huko vyuoni miaka mingii
mkifundishwa ujinga ambao unashindwa hata kuweka chakula mezani. Mnarudi mtaani
kuombaomba walewale ambao mliwaacha, mkajidai nyinyi ndio wasomi.” “Mbona
unaanza matusi Malon!?” Bale akashangaa sana. Akahisi Malon hayupo sawa, kama
ambaye ameshavuta bangi inayomzungusha kichwa anaongea tu.
“Ninapoongea
sitaki uniingilie Bale. Mimi sio Naya au baba yako unayemjibu utakavyo. Upo
kwenye himaya yangu nataka heshima. Unanisikia Bale? Sitaki ujinga na
sitaki ujuaji kwa kuwa huna unachojua.” Bale hakutegemea. “Acha kutoa
macho ukishangaa. Mimi nakuwa muwazi kwa kuwa sitaki unirudishe chini.
Unanielewa Bale? Sitaki uniharibie hapa. Sitaki ujuaji. Usilete elimu yako ya
darasani kwenye biashara yangu kwa kuwa mimi nakujua wewe na unakotoka. Huo
ujuaji unaotaka kuwaonyesha wafanyakazi wangu, kama kweli wewe ni mjuaji kama
unavyojionyesha kwao, si ungekusaidia wewe mwenyewe na baba yako?” “Acha
kumtukana baba yangu Malon. Hausiki hapa!” Bale akasikia kuumia.
“Haa!
Anayemtukanaga baba Naya hapa ni nani kama si wewe?!” Malon akamuuliza kwa
ukali kabisa. “Ushawahi kunisikia mimi nikisema vibaya wazazi wangu hata siku
moja? Muulize Naya. Mimi nilikataa ushauri wao. Sikufuata walichokuwa wakitaka,
lakini sikuwahi kuwatukana hata mara moja. Nilichokuwa nikifanya ni kusikiliza,
sijibu na kuondoka. Mimi huwa nabishana na watu wengine lakini
hutanisikia nikijibishana na wazazi wangu hata mara moja. Ndio
maana mimi mzee alikuwa akinipiga karibu kuniua, lakini sikuwa na mjibu na
nilikuwa sifanyi anachotaka nifanye. Piga simu hii hapa muulize Naya kama
katika mabaya yangu yote kama alishawahi kunisikia au hata kusikia fununu kama
mimi nilikuwa nikibishana na wazazi wangu kama hivyo wewe ulivyokuwa
ukimjibu baba yako kama hana akili nzuri! Uliza.” Bale kimya.
“Wewe
ndiye unayemtukana kila leo na kusema amezubaa, hana uwezo wa kufikiria!
Lakini baba yako alikuja hapa na shida zake, akaelewa nafasi yake, akatumika na
kuondoka bila tatizo. Uliza wote hao wanamfahamu na kumuheshimu yule mzee, kwa
kuwa walimuona akitumika hapa bila maneno mengi ila kazi tu mpaka siku
anaondoka hapa, wanahuzunika. Mpaka leo wanamuulizia baba yako unayemdharau na
kumsema vibaya!”
“Sasa
wewe umekuja tu na kuanza kutawala wenzio! Unawafoka na kuwapanga
utakavyo! Unaweka mashariti na mipango yako bila kuniuliza!?” “Nia ni kutaka
kusaidia Malon! Kitu kisiharibike.” “Ushajiuliza wakati wewe upo darasani nani
alikuwa akiwaongoza hawa?” Bale kimya.
“Acha
ujuaji wa kijinga. Hawa hawajasoma lakini wanaijua hii kazi kuliko wewe
uliyekaa darasani miaka yote hiyo! Wanakucheka tu hao na kukudharau wakikusema
kwa kilugha chao, wameshakusoma na wanaambizana kuwa unajidai ni mjuaji wakati
hujui chochote! Wanakukebehi tu. Na ujue wazi unajidhalilisha tu hapa. Wanajua
mambo hao, zaidi yako. Nimekaa nao hao waulize kama kuna nilipokosana nao.
Japokuwa unawaona hawana shule kichwani lakini mashine zote hizo wanajua kuzitumia.
Nikiwa Dar, wao ndio nawaachia kila kitu! Hatujawahi kupishana nao hata mara
moja. Nawaheshimu sana hao wote, maana ndio wanaoshika hatima ya biashara
yangu! Halafu wewe unakuja kuwafoka wanaume wazima hao na familia zao!
Nipo ndani huko nakusikia ukiwapanga kwa ukali, halafu sasa hujui ni nini
unazungumzia! Acha kabisa Bale. SITAKI ujuaji. Hapo tutakosana na sina
utani, muulize Naya. Huwa ananijua na kila anayenifanyia kazi ananitambua.
Linapofika swala la biashara zangu sitaki utani na sitaki ujuaji. Mimi ndiye
najua nini kifanyike, nani akifanye na kwa muda gani.”
“Umeletwa
na shida ya kazi, fanya majukumu yako, heshimu wengine, kaa pembeni. Unanielewa
Bale?” Kimya. “Wakati nyinyi mnafundishwa zile hesabu zenu walizochanganya
namba na herufi, wenzenu tulikuwa mtaani tukisaka pesa. Washamaliza
kuwadanganya huko darasani eti ndio unataka kuja kunitibulia hapa kwangu!
Sitakuruhusu Bale. Washa simu yako mpigie dada yako atakwambia ninavyokuwa
linapofika kwenye swala la biashara zangu. Sina udugu, sina mchezo. Naya
mwenyewe alikuwa akijua kutumia tu, hajui nilikokuwa nikitoa pesa.” “Ni nini
Malon? Kweli ndio unamsema vibaya Naya kwa namna hiyo! Sio wewe ulikuwa
ukimsifia na kipaji cha ajabu!” Bale akashangaa sana.
“Unakosa
pointi ya muhimu sana Bale. Swala la kipaji cha Naya na matumizi ya pesa yangu
na upatikanaji wa pesa yangu ni vitu tofauti kabisa. Kipaji cha Naya
kilijulikana sababu ya heshima yake kwenye biashara zangu, ndipo akaweza
kufikia pesa yangu. Na hakuna mwanaume ataweza kumuinua Naya kama mimi.
Na ndio maana unaona vipaji vyote vimekufa alipoamua kuniacha mimi. Katika
harakati zake zote za kunufaika na pesa yangu, mwenzio alijua kuniheshimu mimi
na mipango yangu. Hakuwa bosi wangu. Alijua hayamuhusu, kazi yake ikabaki
kutumia tu akiwasaidia nyinyi wote. Ninachotaka kukwambia Bale, jua,
tambua na elewa nafasi yako. Wewe ni mfanyakazi kama wafanyakazi wengine wote
hapa. Wote mnafuata maelekezo yangu. Vikikushinda ondoka. Kabla hujaona
upande wangu mwingine ambao ujue hutaupenda na sikutanii. Muulize Naya.
Tabia zako za ubishi na ujuaji, tafadhali hapa si sehemu yake. Kuwa makini.”
Malon akaondoka.
Wafanyakazi
wengine wakaanza kucheka waziwazi na kubadili kilugha. Bale alijua wazi
wanamsema yeye huku wakimcheka. Akaumia sana asiamini alichokifanya
Malon. “Ameshindwa vipi kuniita pembeni na kuzungumza na mimi!?” Akajiuliza
Bale akiwa hajui chakufanya tena. Aondoke au abaki hapo!
Maamuzi Magumu Kwa Bale.
Yalikuwa
mazingira magumu kwa Bale kuwepo katikati yao tena. Akaamua kutoka hapo kabisa
eneo hilo la shambani ili akajitulize mjini. Hapo walipokuwepo kwenye ghala za
Malon na mjini palikuwa na umbali wa kutosha tu. Lakini hasira na fedheha
ikamsaidia kutembea bila kuchoka katika jua hilo mpaka mjini. Akaenda kukaa
kwenye moja ya mgahawa akiwa anatokwa jasho kwelikweli. Akaagiza kinywaji na
kubaki hapo akitafakari maneno ya Malon na kushindwa hata kunywa. Chupa ya soda
ikabaki mbele yake ikiwa vilevile hata hajagusa japo alishafunguliwa, akabaki
akitafakari. Akasikia kuumia sana, hakujua nani wa kumlaumu.
Akatamani
kuwasiliana na nyumbani kwao, akakumbuka yameshapita majuma mawili tokea atoke
nyumbani kwao, na kugoma kuwasiliana nao kabisa. Mwanzoni alianza kwa kuzima
simu yake, mwishoe akamuomba Malon amtafutie line nyigine, akabadili namba yake
kabisa na kumuonya Malon asije pokea simu zao, ndipo wakakubaliana wazifungie
kabisa. Ndipo hata Malon akawa hapatikaniki na baba Naya pamoja na Zayoni. Ila
hakufungia simu za Naya, hapo Malon alikataa. Bale akalikumbuka hilo. Akapoa.
Aliondoka akiwa amejawa tumaini akijua atarudi akiwa amefanikiwa sana. Siku
hiyo tumaini zima lilimuishia. Malon alimtoa juu sana na kumrudisha
chini, akajiona mjinga kupita kiasi.
Akabaki
hapo akiwaza. Akapotelea mawazoni kabisa. Mawazo yakamrudisha kwa mama yake.
Akatamani kama mama yake angekuwa hai angekuwa na kwa kurudia. Akapotelea
mawazoni akiwa amejawa uchungu wa kupitiliza.
Yaliyo Sirini, Mwangani.
Wakati
amepotelea mawazoni akaona gari ya Malon imesogea mpaka kwenye nyumba za kulala
wageni iliyokuwepo karibu na alipokuwa amekaa. Malon akashuka na kuingia ndani.
Akajiweka sawa. Baada ya kama dakika saba tu, akaona gari ingine imesimama
hapo. Akashuka mdada mrembo tu, akaingia ndani. “Nisimfikirie Malon
vibaya. Amenihakikishia ameokoka na ameacha tabia za wanawake.” Akamtetea
moyoni mwake kwa hofu. Akakumbuka tabia za Malon za kupenda wanawake. “Ila
ile ilikuwa ni kwa sababu ya bangi. Malon ameokoka na ameacha bangi. Sijasikia
hata harifu ya bangi! Wanao vuta ni wale vijana tu si...” Akasita Bale
na kujikuta akitetemeka kwa hofu huku akiomba Mungu asiwe amekosea kwa kiasi
hicho. “Haiwezekani!” Akapinga na kujikuta macho yamegomea
kwenye nyumba ya kulala wageni. Akikumbuka hali ya Malon asubuhi hiyo wakati
akimfoka kama aliyepagawa.
Alikaa
hapo mpaka giza likaanza kuingia hata asijue kama ulishapita muda mrefu kiasi
hicho. Baada ya muda akawaona Malon na yule dada wakitoka pamoja.
Safari hii wakaondoka na gari ya Malon. Bale akaanza kusikia jasho likimtoka
mida hiyo ya jioni, mjini Mbeya ambako baridi ilishaingia. “Mungu wangu
nimefanya haraka kumuamini M..” Akasita na kubaki akisindikiza
gari ya Malon kwa macho.
Alikaa
hapo mpaka usiku kabisa. Alikuja kushituliwa na muhudumu kuwa wanafunga. “Kwani
sasa hivi ni saa ngapi?” “Inakwenda saa sita kaka yangu. Mpaka jikoni
wamefunga.” Bale akatoka hapo hata hamu ya kurudi kwa Malon ilikuwa imemuisha.
Akatembea taratibu kurudi mpaka nyumbani kwa Malon. Alikuta gari yake kuashiria
alisharudi. Alichofanya ni kuingia kwenye chumba alichopewa akitumie na mwenzie
Mpoki, akakusanya vitu vyake vichache akaondoka akiwa amemuaga Mpoki. “Naomba
mwambie kama kuna malipo yeyote anayoona nastahili, anirushie kwenye simu
yangu, namba ambayo alininulia yeye mwenywe.” Usiku huohuo Bale akaondoka
nyumbani kwa Malon.
Naya&Joshua.
Huku kwa
kina Naya mambo yalikuwa yamepamba moto. Mapenzi mazito. Joshua na Naya wakiwa
wanakaribia ndoa yao. Amani na furaha vikawa vimetawala. Naya akiwa katikati ya
familia ya kina Magesa kama mmoja wao. Nguo nzuri ya harusi kwa Naya ikawa
imeshapatikana. Zikawa zimebaki siku chache tu harusi yao ifungwe. Nanaa na
mama Magesa walimuandalia Naya kichen Party nzuri sana. Watu
wachache tu tena wakaribu. Wakakodi ukumbi mdogo tu wakutoshea wageni wao, na
kualika wanawake wa kanisani kwao pia. Wengi waliokuwa na mama Naya tokea Naya
ni mtoto mdogo akikua hapo kanisani. Naya alikuwa amejawa furaha ya kupitiliza
asiamini yote hayo anafanyiwa yeye tu! Alijawa furaha ya ajabu.
Mambo
yalikwenda vizuri kina Geb nao walimfanyia Joshua Bachelor party.
Wakakutana wenye pesa zao na kusheherekea Joshua kuuacha ukapela. Ukawa wakati
mzuri sana jioni hiyo, baba Naya akiwa kwenye shuguli zake. Mambo yakibiashara
ndio yalikuwa machanga, akawa busy akihakikisha kitu
hakiharibiki kwenye biashara zake.
Baada ya
kila kitu Joshua akaenda kumchukua Naya ili amrudishe mwenyewe nyumbani. “Mimi
Joshua Kumu, nimepata kitu chema! Umependeza sana Naya na onaonekana
unafuraha!” “Sana!” “Nimefurahi kukuona hivyo.” “Hii furaha itakamilika
nikishavaa ile shela, na pete ya ndoa. Ndio nitafurahi zaidi.” “Zimebaki siku
chache sana furaha yetu ikamilike. Twende ukapumzike. Maana mama amenisisitiza
nikurudishe nyumbani moja kwa moja asisikie unazurula mtaani.” “Mama G!” Naya
akakumbuka na kuanza kucheka wakati mzuri alioupata usiku huo. Akaongeza. “Hata
mimi amenisisitiza.” Wakacheka wakiwa njiani wanarudi Kiluvya kwa baba Naya.
Wakaanza kuimba wakipokezana mpaka walipofika.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakamkuta
baba Naya amekaa sebuleni. “Umejawa na furaha mama!” “Sana. Tumecheza
sana ukumbini, tukawa tunacheka mno. Hakika nimekuwa na wakati mzuri baba
yangu. Hivi zawadi zinakuja nyuma. Nimeacha wakipakia kwenye gari ya kina
Magesa ili dereva alete. Ila nimefurahi.” Baba Naya akacheka kidogo wakamuona
ameinama. Naya akahisi anajambo akamkonyeza Joshua kama akae.
Akaenda
kukaa pembeni yake. Joshua naye akakaa. “Umekula vizuri, baba Naya?” Naya
akaanza. “Sitaki kukuharibia wakati wako, lakini..” Akasita. “Nini?” “Kuna kitu
hakipo sawa kwa Bale, Naya. Naweza nikakosa lugha yakueleza lakini moyoni
mwangu najua kwa hakika lipo jambo. Hii ni siku ya pili moyo wangu unauma,
nashindwa kutulia juu yake. Nimeomba na kushindwa kula tokea jana,
lakini nimeshindwa kabisa kupata amani. Tokea juzi najaribisha simu yake, haipo
hewani. Na Malon hivyohivyo.” “Lakini si umekuwa ukiwapigia na mara zote
unakuwa ukisema huwapati? Mwache tu baba pengine hataki mawasiliano na sisi.”
Wakamuona anatingisha kichwa anakataa.
“Hapana
Naya. Kuna kitu hakijakaa sawa. Nimeomba Mungu hata anionyeshe kwenye ndoto,
lakini haijatokea. Moyo umejawa hofu ya ajabu! Tafadhali mpigie wewe Malon.”
“Baba!?” “Tafadhali mama. Nisaidie tu ili moyo wangu utulie. Mwambie nataka tu
kujua kama yupo mzima, basi. Hilo tu.” Naya akamwangalia Joshua. “Mimi mwenyewe
nilitumia simu ya GM kumpigia sikumpata. Sijui kwa nini, tokea wakati ule, kwa
mara ya kwanza na mimi leo nilimkumbuka Bale, na kumuomba GM anipe simu yake
nimjaribu nikijua simu zangu amezuia. Lakini hata ya GM haikwenda! Nashauri
kweli tumpigie Malon ili kujua.” “Mimi leo nilikuwa na furaha sana jamani, sitaki
kutibuliwa!” Naya akalalamika. Joshua akamtizama kama anayemkumbusha kitu. Naya
akatoa simu yake kwenye pochi.
Mtaka Cha Mvunguni, Sharti Ainame.
Naya
akampigia Malon hata bila hata kuitafuta namba yake. Ilikuwa tu vidoleni kwake
hakuhitaji kukumbushwa. Bado ilikuwa imebaki kichwani mwake hata vidole
havikuomba msaada. Akapiga na kubonyeza spika ili wote wasikie. Iliita mara
moja tu akapokea usiku huo mpaka Naya akashangaa. “Naya mama,
umenikumbuka?” “Samahani nimekupigia mida mibaya, lakini nilikuwa ninas hida na
Bale. Baba hampati kwa simu, naomba tuzungumze naye.” “Mimi nilijua yupo huko!” Naya
akamtizama baba yake kwa wasiwasi. “Nasikiliza. Muulize aliondoka lini?” Malon
akawa ni kama amemsikia baba yake akajibu. “Nafikiri siku kama
nane zimepita sasa au kumi! Bado hajawatafuta tu?” “Hivi Malon wewe kichwa
chako kikoje jamani!? Kwa nini unakuwa na mtoto wa mtu unashindwa kuwasiliana.”
“Heee! Naya! Bale si mtoto mdogo. Anaposema hataki kuwasikia nyinyi kabisa,
mimi nilitakiwa kufanya nini?!” Malon akamuuliza kwa
kumshangaa.
“Ni kwa
nini wewe uliondoka naye bila kuzungumza na yeyote?” “Pengine wewe hujui,
lakini baba yenu alikuwa akijua na kunishukuru kabisa kwa kumpa nafasi ya kazi
huyo Bale!” “Hiyo ilikuwa mara ya kwanza Malon! Kukawa na maelewano mazuri
mpaka ukamkimbia, ndipo...” “Subiri kwanza Naya. Naona mnatafuta mtu wakumlaumu
kwa mambo yenu ya kifamilia! Sijui ni nini kinaendelea huko, mnashindwa kuweka
mambo yenu sawa, naona mnataka kuniingiza na mimi! Ulinikataa, nikaamua
kuwaacha kabisa. Safari hii nikaheshimu maneno yako. Lakini Bale akawa ananisumbua
siwezi kulala na siwezi kubadili namba, kwa kuwa alikuwa akizijua namba zangu
zote na akawa anatumia zaidi ile ya biashara ambayo wateja wangu wote wanayo.”
“Malalamiko
juu yenu zaidi mwanaume wako yalikuwa hayaishi! Analalamika kuchoshwa na
umasikini wa nyumbani kwenu ambao hauishi, anaomba msaada. Ninazo jumbe zake
mpaka leo, naweza kuwatumia muone.” “Haina haja.” Naya akajibu.
“Bale hana maadili
kabisa. Amekuja hapa mkorofi na mjuaji anataka kutawala biashara zangu wakati
hajui misingi yangu! Anataka kuwa kiongozi wa watu aliowakuta kazini, wanaojua
kazi zangu kuliko hata yeye na shule yake ambayo amekuwa akijisifia nayo hapa
kijijini! Haambiliki. Nimezungumza naye, kama kawaida yake, hawezi kusikiliza
mtu, yeye ndio yupo sahihi wakati wote, anataka kujibishana! Mimi sina muda wa
kijinga Naya. Na unanijua nilivyo makini na biashara zangu. Siwezi kuruhusu
mtoto aliyekuja leo tu, hajui hata maisha ni nini, aniharibie mimi! Hapana.
Nilipojaribu kuzungumza naye, amekasirika na kuondoka siku ileile niliyomuonya
aache kufoka wafanyakazi wangu na kumtaka awe na heshima. Kwanza wengi wao hapa
wamemzidi hata kwa umri! Watu na familia zao, wenye wake na watoto, eti yeye
anawafanya wajinga na kuwafoka hovyo! Nilishindwa kuvumilia, Naya.” Malon
akaendelea.
“Alivyo mtu
wa ajabu, aliamua kuondoka bila kuniaga. Tena muda, anamuaga mfanyakazi wangu
ambaye anatumia naye chumba sio kwamba mimi nilikuwa mbali! Hapana.
Nipo chumba cha pili tu. Ameondoka na kumtuma mfanyakazi wangu eti anataka
nimlipe pesa yake kwa kumrushia kwenye simu yake!” “Namba gani ya simu uliyomrushia
pesa?” Naya akauliza. “Siwezi kukupa hiyo namba
kwakuwa alinionya kabisa nisikupe wewe wala mwanaume wako anayemsema ni
mnyanyasaji. Anapenda yeye tu ndio awe nacho si..” “Malon, tafadhali naomba
namba ya Bale hiyo unayoifahamu. Bale hayupo hapa nyumbani, na hajulikani
alipo. Tafadhali Malon.” Naya akamkatisha akimsihi.
Kidogo
akatulia. “Basi acha nimpigie kwanza yeye mwenyewe nimuulize. Akikubali ndipo
nitakutumia.” “Tafadhali mwambie baba anawasiwasi sana. Anaomba apokee simu
yangu. Ilimradi tu tujue kama yupo salama, hatutamsumbua. Ni salamu tu.”
“Nitafikisha ujumbe.” “Na naomba ukumbuke nakusubiria Malo. Usipotee.”
“Mimi nipo Naya, ila wewe ndio nakushangaa unataka kujiingiza kwenye matatizo!
Unataka nini Naya, mpenzi wangu? Tulipokuwa pamoja na familia ilikuwa pamoja.
Amani, utulivu na heshima. Sasa kwa nini unataka kuharibu tulichonacho na
kujiingiza kwenye ndoa ambayo...” “Nasubiria namba ya simu ya Bale, Malon.
Tafadhali sana.” Naya akakata.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wote
walikuwa wakisikiliza, wakabaki kimya kila mtu akiwaza lake wakimsubiria Malon.
“Nikuletee chai, baba?” “Nashukuru mama, ila acha tu.” “Bale ni mzima baba,
usiwe na wasiw...” Kisha akasita. “Naamini atakuwa mzima. Atakuwa amepata kazi
sehemu ingin...” Akasita tena akipingana na mawazo yake mwenyewe. Bale hakuwa
mwenyeji huko mjini Mbeya. Hawakuwa watoto waliokuzwa mbali na hilo jiji la
Dar. Bale ameondoka hapo kumfuata Malon ndio mara yake ya kwanza kusafiri
kwenda mikoani tena peke yake. Akaanza kuingiwa na yeye na
hofu. Akaona anyamaze na yeye asubirie.
Furaha
yote ikaisha, wakabaki na wasiwasi. Tumaini likabaki kwa Malon pekee anayeweza
kuwasiliana na Bale. Wakasubiri zaidi ya dakika kumi na tano, Malon akawa
hajarudisha bado simu aliyoahidi kurudisha. Akaenda kubadili nguo za shuguli
alizokuwa amevaa na kuvaa nguo za kawaida tu kisha akarudi kukaa hapo sebuleni
wakisubiria simu ya Malon. Baada ya lisaa Naya akaamua kumpigia yeye, simu yake
na yeye ikawa haipo hewani. “Haiwezekani!” Naya hakuamini. Akaamua
kumpigia tena Malon, hakumpata. “Hakika siamini!” “Nipe na mimi namba yake,
nimjaribishe kwenye simu yangu.” Joshua naye akaanza kumpigia bila mafanikio.
Naya
akamwangalia baba yake. “Sio mwenyeji sana kule Mbeya, lakini itabidi kesho
niende.” “Kweli baba!?” “Kabisa mama. Sina jinsi. Wale vijana wote wa Malon
nafahamiana nao na walitokea kuniheshimu sana. Nitaanzia kwao. Angalau kujua
kama kuna ambaye alikuwa karibu na Bale pengine alimsikia hata akiweka mipango
fulani. Nimtafute mpaka nimpate. Nikimuona na nikaridhika yupo sawa ni kwamba
hataki tu kutuona, nitamuacha na kumuomba angalau awe anatuma ujumbe hata mara
moja kwa juma tu. Basi. Nitamwambia hana sababu ya kuwa akipiga ila salamu tu
basi tuwe tunajua yupo mzima.” Naya akapoa kabisa.
“Lazima
niende mama, lasivyo sitaweza kufikiria. Nina hali mbaya sana ndani ya moyo
wangu. Naugua kiasi cha kushindwa kutulia.” “Natamani kukusindikiza!” “Hatuwezi
wote kukwama kwenye jambo moja. Acha mimi niende tutakuwa tukiwasiliana.”
“Naomba uwe unanikumbuka na mimi, baba. Sitaolewa bila wewe na siku
zimebaki chache.” “Nitarudi mama. Nitarudi. Niombee nifanikiwe mapema.”
“Ungehitaji msaada wowote, mzee wangu?” “Maombi tafadhali. Kule macho yangu
yasipofika, basi Mungu amtizame na kumlinda.” “Tutakuombea. Ulikuwa ukifikiria
kuondoka na usafiri gani?” “Basi tu. Nitatumia basi ndio itakuwa rahisi kufika
huko kwake. Nikianzia stendi ya mabasi, naweza kufika huko. Pana umbali kidogo
na mjini lakini napakumbuka. Nitafika tu.” “Nilifikiri kwa usafiri kwa ndege
utafika haraka ukiwa hujachoka!” “Labda wakati wa kurudi. Lakini kwenda, acha
nitumie tu basi. Itaniwia rahisi. Nashukuru.” “Acha nikamwandalie sanduku la
safari. Mbeya huwa kunakuwa na baridi.” Naya akaongea kwa unyonge akianza kuona
dalili mbaya juu ya harusi yake.
“Usiku
mwema Joshua. Tutawasiliana.” “Ni sawa tukiomba pamoja?” Akauliza Joshua.
“Tumuombee Bale na safari yako mzee wangu. Tumsihi Mungu awe na wewe katika
yote. Arahisishe mambo yote na akulinde. Njoo Naya.” Wakasimama na kushikana
mikono. Joshua akaanza kuomba kwa kutubu. Yeye mwenyewe na kuwatubia wote mpaka
Bale. Akatubu kwa popote pale walipomkosea Mungu na kumsihi Mungu awasamehe na
kuwarehemu. Aliomba Joshua mpaka baba Naya akapokea. Ukawa usiku wa maombi ya
namna yake. Wakaomba amani na utulivu katikati yao, ndipo Joshua
akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bale Yuko Wapi? Ni nini kitaendelea kwa familia hiyo?
Harusi ipo?
0 Comments:
Post a Comment