“Karibu sana. Ningekushika mkono, sema natokwa jasho kama unavyoniona.” “Jasho hilo la ushindi au kufungwa tu?” Jo akauliza kiutani. “Mimi na baba tunawafunga.” Shema akadakia akisogea na mpira wake. “Shikamoo.” Walishazoeana na Jo. Alikuwa naye kipindi wazazi wake wapo fungate la hospitalini.
“Na sasahivi nimekuwa hodari wa aina ile ya danadana uliyonifundisha.” Jo akazidi kucheka. “Umeweza kabisa?” “Sana. Muulize baba na yeye nimekuwa nikimfundisha.” “Ameniambia ni danadana za kibrazili. Wewe ndio ulimfundisha.” Mill akafnaya Jo acheke. “Nilipokuwa Brazil kikazi, ndio vijana wa kule tuliokuwa tukiwatibu walikuwa wakija kila siku jioni kule kambini tulipokuwa tukiishi, tunacheza nao mpira.”
“Na wa Brazili wanavyoabudu mpira!” “Kumbe unawajua?” “Sana. Si ndio kina Pele, vijana wa zamani waliowaachia kina Ronaldo?” “Ewaaa! Utafikiri mpira ulizaliwa kwao! Watoto wanacheza mpira, kama hivyo Shema.” “Basi naona na aina hiyo ya danadanaumemuongezea umahiri. Anasema wenzie wanataka afanye kila wakati.” Wakawa wanacheka hapo waliposimama.
“Aisee karibu sana.” “Asante. Acha nisalimie wazazi.” Akawasogelea. “Shikamoo mama.” “Naona wewe si mkulima mzuri baba!” “Mmemaliza chakula chote?” “Vile vinonovinono vyote tumekula. Tokea tulipoambiwa safari ya kwako inakufa, inabidi tukutane hapa sababu ya Pam kupewa mapumziko, sisi tumeamkia hapahapa, tuna kazi ya kula tu. Umechelewa.” Asijue alivyoshukuru Mungu jinsi aibu yake ilivyofunikwa! Maana alishituka kutoka usingizini, akaanza kumuhurumia Dorothy na ugeni aliouanzisha, halafu akapotea.
“Hamna neno mama. Dorothy atakwenda kunikusanyia masalia yaliyobaki, na mimi nipate kitu.” Akanyanyua kichwa kumwangalia, ndipo macho yakagongana. Kiroho cha Dorothy kikaenda shwaaa! Akakwepesha. Jo akamtizama kwa muda huku akiendelea kusalimia wengine mpaka kwa mke wa Eric.
“Nakukumbuka wewe ndio mke wa Eric.” “Ndiyo. Shikamoo.” Akasimama kabisa na kumsalimia. Hapo akawa mnyenyekevu haswa. “Na huyu ni binti yenu wa pili.” “Unakumbukumbu! Kaka yake ndio yule anakimbizwa na Shema.” Kidogo wakacheka.
“Hutamuweza Shema kwa mpira. Na ni tokea mtoto anaupenda mpira.” “Na anaumudu.” Jo akamjibu nyanya yake Shema, akimsifia na kuendelea kushika watu wengine mkono akiwasalimia.
“Mimi siwezi kuamka hapa Jo. Ila nimefurahi sana umekuja. Na chakula chako nimekufichia.” Jo akacheka sana. Mama yake akamwangalia kama kumsuta Pam, Pam hana mbavu kama Jo. “Kumbe ugeni wangu na mimi ulikuwa ukisubiriwa?” “Sana. Na mwambie dada yako, kwanza asante sanaa. Adumu mno, halafu naomba namba ya simu ya huyu mpishi. Amenitendea vyema kupita kiasi.” “Wewe punguza kupenda kula.” Mama yake akamfanya azidi kucheka.
“Wewe salimia, ukae, uletewe chakula.” Pam akaongeza akionyesha furaha ya wazi kabisa. “Naona changu nikakile ndani na Dorothy.” Akawa anaongea huku akimwangalia lakini Dorothy mwenyewe akawa hamwangalii. Pam mshabiki akawa anacheka kimwangalia mama yake.
Akaenda kusalimia walipokuwa wamekaa wanaume. Ikawa salamu nzuri hamna hata aliyejua kama kuna jambo. Na Jo mwenyewe alionekana kawaida kabisa. Cheko na hivi Mill alishamchangamkia na Pam, akajua ipo amani, kutengeneza ni padogo tu. Maana alijua kipimo cha hasira ya Dorothy ni Pam.
~~~~~~~~~~~
Alipomuona anamalizia kusalimia, akamgeukia Pam, “Kuna kitu unataka ndani?” “Hapana mama yangu.” “Basi naenda kumwandalia Jo chakula.” Akaondoka akionekana amepoa. Mke wa Eric akataka kuongozana naye akasaidie, Pam akamuwahi kumuita. “Kaa, tu. Mwache aende mwenyewe.” Akarudi kukaa. Jo akabaki akiangalia anapoelekea Dorothy, Pam akakohoa. Alipomwangalia, akamfanyia ishara afuate. Kama akimbie!
~~~~~~~~~~~
Akamfuata mpaka ndani kwa Pam na Mill, jikoni. “Nakushukuru kunifichia aibu yangu.” “Ilikuwa ni aibu yangu mimi wala si wewe.” Akajibu akiwa hamwangalii ila kujaribu kufikia sahani. Jo akatulia akiwa amesimama nyuma yake. “Dada Josephine alileta chakula kingi, nikupakulie nini?” “Kwanza Josephine ni dada yangu mimi, kwako ni wifi ambaye ni kama mama yako mkwe.” Akawa kama anayejaribu kumfikishia ujumbe. Akatulia.
“Pili, unajua mimi mida hii siwezi kula hivyo vyakula. Nimekuja kukuona wewe, Dorothy. Na kukuomba msamaha.” Ndipo akageuka. “Unaendeleaje?” Dorothy akamuuliza akionyesha kujali ila si kimapenzi. Akabaki akimwangalia. Dorothy akaona arudishe sahani.
Akamsogelea, alipotaka kumgusa, akasogea na kigari chake kama kumkwepa. “Ndio umenichukia kwa kiasi hiki Dorothy?!” “Hapana. Ila naomba tuzungumze kwanza. Ni sawa tukienda kwangu? Hapa wanaingia na kutoka kufuata chakula.” “Ni sawa, kama ukinikaribisha.” “Karibu.” Akaongoza njia akimfuata nyuma mpaka kwenye kanyumba kake.
“Karibu ukae.” Akakaa akimwangalia. “Nilikuomba msamaha kwa kilichotokea siku ya alhamisi Dorothy, sijasikia jibu.” “Binafsi sikuona kosa, ila nilitaka kukwambia kitu.” Akaanza taratibu tu akionekana ameshakuwa mwekundu haswa. Anatetemeka mpaka mikono kama hofu.
“Nakusikiliza na naomba utulie Dorothy. Jua upo na mtu anayekupenda.” Akakunja uso na kuinama kwa muda. “Niambie.” “Baba yake Eric alinikuta nikiwa nimetulia, sina hata wazo la mwanaume au mahusiano, kama hivi. Akaanzisha jambo akisema ananipenda na kwenda mpaka kwa baba yangu akipiga magoti kisha akaja kunigeuka.” “Mimi nahisi alikutamani tu. Hakukupenda kwa dhati.” Dorothy akashangaa sana.
“Yeye atakuwa alikuona. Akababaishwa na uzuri wako. Pengine ulimkataliamapenzi, ndio akaona njia pekee ya kukupata basi iwe ndoa. Akufikishe kanisani, ili akakutoe nguo. Alipofanikisha janja yake ndio ukawa huna thamani tena.” Dorothy akabaki amekodoa macho haamini.
“Mimi si mkristo mzuri sana kama dada na shemeji. Lakini kuna sehemu huko kwenye kitabu cha Mungu wanazungumzia juu ya upendo wa kweli.” “Bibilia?” “Ewaah! Wanasema eti upendo wa kweli huvumilia. Hufadhili, eti hauoni wivu.” Dorothy akainama. “Halafu eti wanasema upendo wa kweli hauna majivuno, hauna wivu, eti hauna kiburi. Wakaongeza nakusema eti huwa haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake. Chakushangaza eti wanasema kwenye upendo wa kweli hakuna kukasirika upesi.” Dorothy akachoka kabisa.
“Ni parefu. Usifikiri wamemaliza!” Dorothy akamwangalia asiamini. “Eti wanasema huo upendo wa kweli hauweki kumbukumbu ya mabaya. Eti unavumilia YOTE!Hustahimili Yote. Hutumaini YOTE. Chakushangaza na kikubwa wanasema eti huo upendo wa kweli, HAUSHINDWI KAMWE. Labda pasiwe na huo upendo.” “Ndio bibilia inavyosema hivyo?!” “Si maneno yangu mimi! Nakwambia utashangaa sana jinsi inavyosema juu ya upendo unapokuwepo sehemu. Huulizi! Unakuja na hizo sifa zote.” Dorothy akabaki akishangaa.
“Mimi mwenyewe nilishangazwa hivyohivyo. Ila ikanifanya nifikirie sana. Kwamba kinyume na hayo yote, inamaana hapakuwahi kuwa na upendo wa kweli. Au wewe unasemaje?” “Naona sijui tena!” Alichoka Dorothy mpaka akashindwa kuendelea, na yeye alimfanyia kusudi.
“Tuachane na hayo ya baba Eric. Huyo tushajua hakuwa na upendo wa kweli kwako. Alikutamani tu. Endelea?” “Na nini sasa?!” “Nilikukatisha. Samahani. Endelea. Ulisema kuna jambo tuzungumze kwanza.” Alihangaika Dorothy hajui hata azungumze nini tena. Maana ni kama Jo alishamuwahi! Kuja kulalamika kwa chochote au kusitisha mahusiano, tayari ataonekana yeye ndio hana upendo wa kweli. Acha azungumze. Na yeye Jo kimya akimwangalia anavyomzunguka kwa mafumbo akimtumia baba Eric.
“Kwa hiyo unakuwa unakwama! Hujui kama huyu mtu anakuwa na upendo wa kweli kwako au anakuwa anadhania tu, halafu baadaye anakuja kugundua amefanya makosa. Anamuacha mwenzie hajielewi. Maana unakuta mtu hakuwa hata na wazo! Anaanzisha jambo halafu anakuwa anamchanganya mwenzie kiasi cha kwamba mwenzie anakuwa anajilaumu. Au anahisi ni kama ameingilia penzi la mtu. Anakwama.” Akamuelewa.
“Kwani yeye anakuwa na upendo wa kweli kwa huyo mwenzie mchanganyaji?” Akamuuliza makusudi Dorothy wa watu. “Si ndio hapo sasa huyo mtu anakuwa amechanganyikiwa, hajui tena!” “Kwamba hajui kama anampenda au hampendi mwenzie!?” Akamuuliza kwa kumshangaa kabisa.
Akakwama. “Eti Dorothy?!” “Huwezi mlaumu mtu. Maana anaweza fikishwa mahali haelewi tena.” “Sidhani kama sehemu iliyokuwa kuna mapenzi ya kweli, eti changamoto ikamfanya akasahau kama anampenda mwenzie au la. Pengine pawe hapakuwahi kuwa na mapenzi kabisa.” “Unaweza kukuta palikuwa na mapenzi ya kweli ila kunabakia na hukumu ya kuwa wewe ni mwingiliaji wa mapenzi ya watu. Unakuwa mvurugaji tu.”
“Kwamba mwenzie anakuwa na mpenzi mwingine!?” “Ndiyo. Tena moyoni mwake kabisa, unakuwa hujui nafasi yako ni ipi?” “Halafu anakuwa akimwambia nini?” “Hata sijui tena!” “Lazima kujua Dorothy. Maana huo ndio msingi wenyewe. Mazingira yanaweza yakavurugika, lakini lazima kuwepo na msingi wao, wao wawili wa kusimamia. Hata iweje. Kuwepo na msingi. Sasa kama mpaka hapo hapana neno lolote linalokumbukwa, basi kama kuna nia ya dhati, ni bora kuanza kujengwa msingi kwa upya na safari hii kuhakikisha wote wapo upande mmoja.” Dorothy akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
“Au wewe unasemaje?” “Mimi sasahivi naona sijui tena. Tuyaache tu, naona nazidi kuchanganyikiwa.” “Pole.” Akasikika eti kumuhurumia kabisa.
“Nilikumiss Dorothy.” Akamwangalia na kunyamaza. “Nimekuja kugundua nimeshakuzoea, kukaa mbali na wewe inakuwa kama adhabu! Nilikuwa nikitembea na jambo nililoshindwa kulimaliza.” “Umeshalimaliza sasa?” “Kwa asilimia kubwa, ila kuna jinsi fulani moyoni najipa matumaini nahisi kwa asilimia 100, wewe Dorothy unaweza kunisaidia zaidi. Ndio maana nimeona nije tu nilivyo.” Akashindwa hata chakujibu.
“Kwa jinsi nilivyousoma moyo wako. Na jinsi ulivyonichukulia kipindi cha tatizo langu, ninauhakika kwa asilimia 100, hakuna mwanamke ambaye angenibeba vizuri, na kunisitiri kama wewe.” Akachoka kabisa. Asijue mwenzie anacheza na saikolojia yake, kumrudisha kwenye mstari.
“Ingekuwa mwingine, leo hata Pam asingenipokea kwa upendo hivi. Na Mill asingebaki akiniheshimu, na Shema kufurahia kuniona. Ungesusia hata chakula cha wifi yako. Lakini ona jinsi ulivyonibeba vizuri, mpaka najua Mungu alikusudia kunikutanisha na wewe. Alijua kipindi kama hiki nitakuhitaji.” Akabaki kimya akipambwa hapo.
“Si umeona hata wewe ni kweli?” “Basi mimi naona yaishe, ilimradi unaendelea salama.” Akamcheka nafsini kwake maana alimfanyia kusudi. “Sasa nina zawadi zako.” “Umenunua lini tena?” “Leo. Nimetoka kununua, ndio nikaja hapa moja kwa moja.” “Usingehangaika!” “Nitapata wapi mwanamke kama wewe? Acha tu nikuonyeshe shukurani zangu za dhati na msamaha wa kuharibu siku yetu.” Akatoka bila ya kusubiria jibu, Dorothy amepigwa butwaa.
~~~~~~~~~~~
Kina Pam wakaona anaanza kushusha mifuko mizuri maalumu kwa zawadi, tena mikubwa. Mitatu. Akatoa na bouquet kubwa ya maua mazuri sana.
“Sasa mwambie mama, mjukuu anapenda chokleti sana.” “Hizihizi?!” Jo akamuuliza akicheka. “Tena nahisi hizo ndio zaidi. Anacheza humu tumboni, hatulii, nahisi amejua kuna chokleti.” Jo akatingisha kichwa akicheka maana mimba yenyewe mtoto hata hajaanza kucheza. “Nitamfikishia ujumbe.” “Na mimi, Jo.” Shema akaongeza kwa mama yake. “Usimwambie Jo. Mwache akafurahie zawadi zake. Hawa watanunuliwa za kwao.” Mill akaingilia akimwangalia Pam. “Sio mimi ni mwanao huyo!” “Wewe umezidi uroho bwana, acha kumsingizia mtoto.” Bibi yake akafanya wacheke. Jo akaondoka.
~~~~~~~~~~~
Akashitukia anaingia na hiyo mifuko. “Mimi hayo mavitu mengi hivyo sitaki kama sisi wenyewe hatuko pamoja, Jo.” Ikabidi asimkabidhi, aweke pembeni maana alishakwepa kabisa kama hataki kupokea. “Tupo pamoja Dorothy. Unafikiri kwa nini nipo hapa?” “Sijui! Lakini mimi nataka sisi ndio tuwe ukurasa mmoja, sio jambo baya linakupata, unashindwa kunishirikisha!” “Siku ile sijui nilipatwa na nini Dorothy!” “Naomba jaribu kueleza vile ilivyokuwa vinginevyo najisikia ni kama nipo sehemu ambayo sitakiwi!”
“Basi acha nikwambie ukweli.” Akamvuta mpaka karibu yake, akakaa kwenye kochi Dorothy mbele yake wakiangaliana. “Unakumbuka swali lako la mwisho lililo…” Akasita. “Haribu kila kitu?” “Sio kuharibu, bali kuniweka hukumuni. Nilimuapia Betty mimi na yeye katika uzima hata mauti. Sikuwahi msahau Betty hata kwa siku moja. Picha yake ilikuwa pale kama kunikumbusha kile kiapo nilichotoa kwake, kila ninapoamka au ninapokwenda kulala.”
“Lakini kwa siku kadhaa, nakuapia tena, sikuwa nimeiona ile picha mpaka uliponikumbusha wewe kwa lile swali ukitaka kujua kama ndio yeye.” Akatulia kidogo. “Nilipatwa hukumu ya ajabu, na kujihisi nimemsaliti.” Dorothy akaumia mpaka usoni.
“Ndio maana nimekwambia ni kama naingilia mapenzi yenu!” “Hapana Dorothy. Mimi mwenyewe nilishindwa kukubaliana na ukweli. Nikajiingiza kwenye maaganomengine mapya na mwili wa Betty ambaye alishaondoka hapa duniani. Maana kiapo cha mwisho nilimuapia nikiwa namwangalia akiwa amelazwa kwenye sanduku, pale kanisani watu wakimuaga. Akili na moyo wangu vilikataa kama siku ile ndio ilikuwa safari yake ya mwisho, nilijitengenezea kichwani hali ya kunifariji kuwa Betty amelala tu pale, yupo na mimi kila mahali. Nilikataa kama ameshaondoka hapa duniani. Sikuwahi maliza msiba wa Betty kwa sababu hata sikuwahi kukubali kama hayupo.”
“Maana kokote nilikokuwa nikienda kuanzia pale, nilijiambia ndio tumestaafu kama tulivyokuwa tumepanga tustaafu tukiwa bado na nguvu, tumeamua kufanya ninachofanya na yupo na mimi kila nilipo. Tunasaidia watu wenye uhitaji. Nilikuwa kila nikipata wakati mgumu, jambo linanitatiza, nilikuwa natafuta utulivu sehemu, nazungumza naye kupata ushauri wake. Ikanisaidia kwa muda ule kuendelea. Lakini kila mtu aliyekuwa akitujua sisi wawili, alikuwa akinionya vile ninavyoishi. Ila mimi nilipinga kwa sababu nilijiona bado nipo na Betty. Sijapungukiwa.”
“Watu wakaendelea kunionya na kuniambia kuendelea kuishi vile, simtendei haki hata Betty mwenyewe.” Dorothy akawa hajaelewa. “Yaani kwa jinsi vile Betty alivyokuwa,asingefurahia kuona maisha niliyokuwa nikiishi. Na hata mama yake aliniambia. Akija tokea Betty akakuta nikiishi vile, nitamuumiza sana. Betty alikuwa akinipenda sana na alitaka kuniona na furaha wakati wote. Nafikiri hicho ndicho kilinifunga kwake na kushindwa kuendelea. Lakini..” Akawa kama anayefikiria.
“Kwa mara ya kwanza nikawa nimekupata wewe ambaye unaweza kunifanya nikawa na furaha mpaka kusahau matatizo yangu. Kumbuka tulianza kuamka pamoja. Tuna chatkabla ya kutoka kitandani, na wakati wa kulala ikawa hivyohivyo. Ukawa mtu wa kwanza kuzungumza na mimi, na wa mwisho mpaka nafunga macho kulala. Na hilo si jambo baya, lakini kwa mara ya kwanza akili ikawa haijamuwaza Betty kabisa, na hata kama alipita mawazoni, basi alipita kwa wepesi sana sio maumivu au kuweka kituo kama kabla ya wewe kuja kwenye maisha yetu. Ndio maana siku ile ulipomleta nikajisikia ni kama nimehukumiwa, kwamba nime nime nime…” Akainama.
“Mimi nashauri usiharakishe Jo. Tulia umalize hili jambo.” “Bila wewe sitamalizaDorothy. Tafadhali nisaidie kwenye kipindi hichi kigumu. Nataka na nakuomba tuendelee. Siwezi kuanza. Naomba nipokee hivi nilivyo, nisaidie. Taratibu tu, najua nitakuwa sawa. Nimeamua, na najua kwako nipo sahihi.”
“Wanataka niende nikafanye therapy, sijakataa. Lakini naomba wewe ndio uwe therapist wangu.” Akamshangaza sana. “Ndio nitakusaidiaje Jo! Pengine wataalamu watakusaidia zaidi!” “Kwa muda mfupi nimeona wewe umeweza kunifanya nikalala bila hata dawa ya usingizi. Unanipa furaha na umenisaidia nimeweza kuendelea kuliko kwenda kwa wataalamu watakao nigarimu mahela, na sidhani kama watanisaidia.”
“Na nakuahidi na mimi mwenyewe nimeanza kuchukua hatua za awali. Tunafanya pamoja sio kwamba nakuachia peke yako na sitaki unione mzigo. Kwa mara ya kwanza nimechukua na nimekubali kumpumzisha Betty kwa amani.” Dorothy akabaki akimwangalia. Hajaelewa. Akajua.
“Yaani kwa mara ya kwanza maishani nimekubaliana na ukweli kwamba Dorothy ameshatimiza kusudi lake lilomleta hapa duniani. Ametangulia kupumzika. Mimi natakiwa kuendelea kuishi. Nimekubaliana na huo ukweli, na kumuacha apumzike kwa amani.”
“Kwa hatua ingine, nimefanya mimi mwenyewe. Niliamka asubuhi, nimekusanya vitu vyake vyote. Nimefunga kwenye sanduku moja, nikapata muda na dada kumaliza naye msiba wa Betty, basi.”
“Kwa hiyo hivi unavyoniona ni mimi Jo, niliyefiwa na mke wangu. Kumbukumbu zake sitaepuka maana ameniachia kumbukumbu kubwa mayoni, ndio maana nakuomba na wewe uwe unanisaidia. Usinichukie.” “Siwezi kukuchukia ila nilitaka uhakika Jo. Sitaki nijikute narudia kosa. Unakuwa na mtu ambaye haupo moyoni mwake. Inauma. Inauma sana.” “Sio na mimi. Nakupenda Dorothy, nakupenda sana. Isingekuwa ni wewe, nisingerudi leo. Nakuhakikishia. Maana nimejaribu kwa wanawake wawili, na kuachana nao ilikuwa kama nafuu kwangu. Nilikuwa nikifurahia. Wewe nakupenda na ninakuhitaji. Nimerudi kwako nikijua utaniweza. Niambie hutanikimbia kipindi hiki nakuhitaji.” “Siwezi.” Akamsogelea kupata kiss.
Alipoona hajakataa, akaendelea. Tena na tena. Kisha akamuachia. “Si utanisaidia?” “Utakaponiambia, lakini sio kunyamaza kimya nakuwa sijui nifanye nini!” “Basi nitajirekebisha. Nilikumiss Dorothy!” “Mimi sikujua kama utarudi tena. Nilijua ndio umekumbana na ukweli, ukajua umefanya kosa kuwa na mtu kama mimi.” “Nakutaka mtu kama wewe.” Ikabidi tu acheke.
“Najua unajua ninachomaanisha, Jo!” “Ulivyo na jumla yako yote, nakuhitaji. Vile unavyojiona. Vile ulivyoaminishwa kuwa upo, jua hivyohivyo, NAKUTAKA wewe Dorothy. Huna utakacho nikatishia tamaa, kikanibadili. Moyo umependa.” Dorothy alicheka sana.
Kissing zikaendelea. Kila mmoja alikuwa na hamu na mwenzie. “Mbona sitosheki?” Dorothy akacheka kwa aibu. “Sikupati nitakavyo.” “Nipo na msichana, anaweza ingia.” “Ila chumbani kwako hawezi, si ndio.” Akatingisha kichwa kukubali. “Nataka kukukumbatia. Nikuweke mikononi, mwili wangu ujue na akili ziamini upo na mimi, ndio nitatulia. Unafikiri ni sawa?” Wakajisahau hao wawili. Wakahamia chumbani na Dorothy akafunga mlango kabisa.
Wakahamia kujilaza kitandani ili Jo apate romance aliyokuwa akitaka, ya kujinafasi. Vilinoga, Dorothy alishindwa kumuachia. Hakuwahi pata kissing za masikio na shingo, siku hiyo alipata. Jo alifanya yake kumuaminisha ni wa thamani. Na hivi rangi yake ilikuwa ikimzingua, alikuwa akimlamba kama pipi, Dorothy akigugumia raha na kusahau kama wazazi wanasubiri. Mapenzi hayana umri!
Huku Kwa Wageni.
Waliokuwa wakicheza mpira walicheza mpaka wakachoka, Jerry akaaga na kuondoka maana kesho yake anaanza kazi, lazima ajipange. Maisha mapya ndio yanaanza ramsi. Bila Sandra aliyetawala na kuongoza maisha yake kwa miaka mingi sana. Imekuwa kama kuku wa kufungwa ndani, ameachiliwa katikati ya mji wenye magari mengi.
Mill akamsindikiza mpaka garini wakazungumza kidogo na kuondoka, njaa ikiwa imeshaanza kwa kucheza mpira wa ushindani, ila aibu hawezi rudi ndani na kuomba tena chakula. Na pesa chache alizokuwa amepewa na mdogo wake ilimbidi kununua nguo mpaka za ndani. Kisha kupeleka alizokuwa amevaa kwa dobi ili afuliwe amrudishie Sandra kama walivyokubaliana akiondoka kwake.
Hajawahi jifulia mwenyewe ni miaka mingi sana umri wa mtoto wake wa kwanza. Tena alikuwa akifua alipokuwa shuleni tu, huko bweni. Jerry alikuwa mtoto wa kitajiri, akiwa nyumbani kufanyiwa kila kitu. Kazi yao ilikuwa shule na starehe za kiheshima za watoto wa kitajiri.
Wazazi wao walipofariki maisha yaliyumba, lakini baadaye ndipo wakaoana na Sandra, wakafanya kazi kwa bidii, pesa ya wizi wakaizalisha, maisha yakarudi kuwa ya juu zaidi. Napo tokea anaingia kwenye ndoa, alikuwa akihudumiwa kila kitu kama Sandra mwenyewe. Nyumba ilikuwa na mashine, na watumishi, wanafanya kazi zote, wao ni ofisini tu kuhakikisha pesa inazalishwa nyingi bila kupungua. Mikono ilishasahau anafua vipi suruali ya jinsi. Kwa hiyo hapo napo pesa yakufuliwa ilimtoka.
Haya, Jerry si mvaa mitumba, sio mwenda Kariakoo. Anavaa kutokana na ubora wa nguo, inamaana kwenye maduka ya garama kwelikweli ndani ya malls. Nguo chache tu, pesa zikamuishia. Hapo hana hata pesa ya kula ila gari amejaza mafuta aweze kufika kazini. Maisha ya ubachela yameanza na ugumu kwelikweli. Ila akashangaa anafuraha ya ajabu kila anapokumbuka hayupo tena chini ya Sandra. Ikawa kama aliyerudishiwa uhuruambao hakujua kama ameupoteza kwa miaka mingi sana.
Kejeli Zilizovunja Moyo.
Katika mahusiano yao hawa wawili, maneno ya dharau na amri kila wakati kwa mumewe vilikuwa kama sumu iliyokuwa ikitiririka polepole bila kuonekana. Kila kejelina kila neno la kubeza lilichoma moyo wa mwenzie kimyakimya, Sandra akiona ni SAWA TU, asijue vile anavyomuachia Jerry, mwanaume mtulivu, mzuri hata kwa utendaji kazi akijituma mchana na usiku, majeraha yasionekana lakini yenye maumivu nakubwa.
Walianza kwa mapenzi makubwa, Sandra kufurahia kufanikiwa kumpata mwanaume kama Jerry! Status ya juu, amesoma, mzuri wa sura ambaye hata rafiki zake walikuwa wakisema ni mzuri kupita yeye mkewe, lakini Sandra akafanikiwa kumfikisha Jerry mpaka kanisani. Mungu akajalia watoto wawili wazuri kwa muonekano kama baba yao kitu Sandra alikuwa akijivunia akisema kama ni karata, basi yeye amelamba dume!Lakini kidogokidogo akaanza kupoteza heshima na kuishi kwa mazoea, na kusahau kabisa upendo wa kwanza uliowafunga pamoja.
Mwishoe yakabakia mazoea na si mapenzi tena bali watu wawili, mmoja anayekumbuka ndio chanzo cha msingi wa uchumi wa familia, Jery akamfanya kama mfanyakazi aliyemuajiri tu, akiyabeba bila pakujua pakulalamika ila kutii kila anachoambiwa na mkewe bora liende akidhani ni vyao.
Maisha yake yakajaa ukimya mzito, ushahidi kwamba anadharauliwa na kupelekeshwa na mkewe haukuwa wakutafuta. Si nyumbani walipo watoto na wafanyakazi wao ambao nao wakageuka ni wa Sandra, kuwa anawalipa yeye, na kazini nako wote waliona aina ya ndoa yao.
Leo Jerry anafukuzwa kikatili, kwa aibu na fedhea kubwa, hana chakula, hana pakuishi, anaishi kwa mama mkwe wake Mill, hana gari, ila anaendesha alilopewa na mdogo wake, hata pesa ya kununulia chupi aliyovaa alipewa na mdogo wake, analala kwa kujibana jotoni, lakini anamwambia Mill baada ya muda mrefu sana, hatimae analala usingizi mnono akijiona yupo huru.
~~~~~~~~~~~
Baada ya Jerry kuondoka, Mill naye akaingia kuoga, Shema akafuata nyuma. Pam akarudi nawageni ndani, akawaambia wasichana wapashe vyakula moto ili wale kabla hawajaondoka. Mama yake akawa bado hajarudi. Mill na Shema wakatoka kuoga, wakakaa mezani kula tena cha usiku, kwa pamoja, Dorothy hajarudi.
Wakati wakimalizia kula, Eric akamshukuru Pam kusudi. “Asante kutukaribisha, tumepata..” “Uliniacha jela Eric. Wewe na mkeo mliniacha nikiwa mjamzito, eti ili nipate shida nijifunze.” “Ndio maana nilitaka kukuomba msamaha Pam na kukuelewesha kilichotokea. Sandra nilikuwa nikiheshimiana naye sana. Sikujua kama angeweza kunidanganya.”
“Wewe uliamini maneno ya mtu baki si kwa bahati mbaya, ni kwa sababu roho yako ni mbaya, hukutaka kunisaidia, uka..” “Baba Shema, mkeo anazidi kupandisha hasira. Na akiwa juu huyo hana wakumtuliza ila mama yake ambaye simuoni hapa. Mtulize mkeo.” Bibi yao akaingilia, mama yao hajarudi yuko kwenye kupendana na Jo. Malavu dave.
~~~~~~~~~~~
Upo usemi uansema, one man’s trash is another man’s treasure. Eric alipoona familia yake haifai, akaachana nao. Akamuacha mama yake akisota mavumbini, dada yake jela tena akiwa mjamzito mpaka alipokuja Mill na Jo.
Kile alichokiona Eric na baba yake si mali, ni takataka, hao wamarekani wawili, Jo na Mill, wameng’ang’ania kwa udi na uvumba.
Na kile Sandra alichoona ni takataka, akiishi naye kama kijakazi, Jerry, akamfukuza akimdai hata chupi aliyovaa, akidhani anamuumbua, leo amemtupa katikati ya jiji la Dar, lililojaa warembo wanaomlilia Mungu awape mwanaume aina ya Jerry.
Ni nani naye atakuja jishindia Jerry au Sandra atakuja kukumbuka shuka kumekuchwa?
Usipitwe…
0 Comments:
Post a Comment