Kwa mara ya kwanza Nelly akawa amepata mtu wa kumtafakari mbali na Jax ambaye ni kweli amemlea kama mtoto wake. Billson alimshangaza na kumchanganya vyakutosha. Mwanaume anayejielewa. Msomi. Hakuonyesha kama ni mtanzania ila asili ya Africa. Kingereza chake! Nelly akajaribu kuweka ile lafudhi kwa mataifa mbalimbai mpaka akachoka. Billson alijaliwa umbile zuri japo ni mtumzima. Mkubwa kiumri kwa Nelly. Amejawa mamlaka! Nelly akacheka na kutingisha kichwa. Akatulia akisubiria aone anataka kumpeleka wapi, lakini akagundua hata hawakuwa wameambiana muda na mahali pakukutana. Na yeye Billson hakutokea tena siku na muda wa kazi mpaka Nelly akajua amegairi.
![]() |
Wakasimama wakitizamana. “Unaendeleaje Nelly?” Mwishoe Bill
akamsalimia na cheko kama anayemuweza. “Mimi mzima!” Nelly akamjibu kwa
mshangao na kumuuliza. “Uliniambia tunakutana mara nne tu, tena weekend. Sasa
sasahivi unafanya nini hapa!?” Billson akacheka. “Nelly! Wewe unawasiwasi gani!
Unashida gani na watu kiasi ya kwamba uwepo wao unakutisha kiasi hicho!”
“Naomba mkoba wangu nirudi nyumbani nikapumzike.” “Umekula mchana?” “Anayekupa
habari zangu hajakwambia na hilo?” Bill akamcheka akimtizama.
“Najua hapo unaumia maana kuna linaloendelea, wewe hujui. Hivi nilikwambia kuwa ni sawa wakati mwingine
uwe unaongozwa?” “Ni wakati gani wewe huwa unaongozwa?” “Sasa hivi. Chagua
sehemu yeyote twende tukapate mlo wa usiku pamoja. Popote unapopata wewe.” Nelly
akashangaa sana.
“Nani amekwambia mimi nataka kwenda kula na wewe!? Nimekukubalia siku
za weekend tu, tena mara nne tu. Naomba usiweke mazoea Billy!” Akataka
kumpokonya mkoba wake, Billy akamkwepa. “Njaa inaniuma Nelly. Tafadhali naomba
tukale.” “Mimi sitaki kwenda popote na wewe.” “Unaogopa nini?” “Sikufahamu Billy!
Sijui wewe ni nani na kwa nini upo hapa na mimi, na kwa nini umenikazania hivi!
Haijawahi nitokea maishani!” “Umeshajiuliza ni kwa nini haijawahi kukutokea?”
“Sina muda wakupoteza.” “Ni kwa kuwa unaogopwa Nelly. Mimi siogopi. Twende
tukale.” “Wapi tena!?” “Tutumie gari yako. Tukishakula, utaniacha hapo, mimi
nitatafuta usafiri wakunirudisha kwangu.” Nelly akafikiria, akamwangalia
Billson. Akakuta anamcheka.
“Naomba nikwambie ukweli Billy.” “Iwe kesho. Leo nina njaa Nelly. Sitaki
kusikia chochote ila chakula tu.” “Sasa mbona ni kama ulitaka jibu la swali
lako, nataka kukujibu unakwepa?!” “Kwa sababu unachotaka kunijibu sio chenyewe.
Hata huo ukweli unaotaka kuniambia sasa hivi, sio wa swali langu. Tafadhali
nisaidie usafiri nikapate chakula.” “Kwa nini upo hapa Billy?” “Dereva
amenishusha hapa.” “Unajua fika hilo sio jibu la swali langu.” Billson akacheka
sana.
Nelly akaelekea sehemu anapoegesha gari yake. Billson akamfuata.
“Unataka kuniacha?” “Natamani kama ningeweza.” Billy akazidi kucheka. “Ushaanza
kuamini kuwa huwa sikwepeki?” Nelly hakumjibu, akataka kufungua mlango, Billy
akamuwahi akitaka kumfungulia. “Hata gari yangu pia unataka kunifungulia mlango
jamani!?” “Unahofia utapoteza nini kwa mimi kushika gari yako na kukufungulia
mlango?” Kimya. “Eti Nelly?” Nelly akampisha kabisa hapo mlangoni. Akamfungulia
mlango na kumpisha kumuashiria aingie. Akaingia bila kuzungumza, Billy akamfungia
mlango na yeye akapanda. Nelly akaondoa gari akiwa ametulia.
Mwishoe akamuuliza. “Ungetamani kula nini?” Billy akafikiria bila
kupata jibu. “Njaa inaniuma sana, siwezi kufikiria tena. Sijala tokea jana.”
“Kwa nini!?” “Nimekuwa na majukumu mengi, nimeshindwa kuweka chakula mdomoni.”
Akamuona anavuta kiti nyuma, na kujiegemeza kama anayetaka kupumzika kabisa.
“Usilale sasa! Kwa hiyo utakula chakula chochote?” “Tena kikinifuata hapa ndio
itakuwa vizuri kabisa.” Nelly akampigia mtu simu kumwambia anakwenda hapo.
Amtayarishie chakula. Akifika atampigia ili alete chakula garini. Billson
kimya.
Mara kadhaa Nelly alimwangalia kwa kujiiba, akamuona amefunga macho
kabisa. “Billy?” Baada ya muda akamuita, akamuona amefungua macho. “Asante kwa
nyama choma. Nilipenda.” “Karibu.” Akabaki akimwangalia, Nelly akaendelea
kuendesha. Kimyakimya mpaka kwenye moja ya hoteli nzuri tu, lakini Billy
akashangaa huduma zinawafuata nje. Akaanza kucheka. “Ni nini sasa?” “Usiniambie
huwa unakuja sehemu nzuri kama hii, na kuishia kula garini!” Nelly akanyamaza,
hakujibu. Na yeye Bill akanyamaza.
“Nelly?” Nelly akamgeukia.
“Sio watu wote ni wabaya.” “Mimi sijawahi kukutana na hao binadamu wazuri.”
“Hudhani ni kwa kuwa umechagua kutowatambua?” Billy akamuuliza vizuri tu, Nelly
akanyamaza. Chakula kikaletwa. Wakaulizwa vinywaji. Nelly akataka wine.
“Tafadhali naomba utusubiri kidogo.” Akamuomba muhudumu awapishe kabla yeye
hajaagiza kinywaji chake. Nelly akashangaa. “Naomba nikuombe kitu, Nelly.” Nelly
akamwangalia.
“Moja ya sifa zako nilizosikia ni kuwa huwa hunywi pombe ya aina
yeyote ile siku za kazi. Na ikitokea unakunywa, basi kuna jambo halijakaa
sawa.” Hapo alimshangaza zaidi Nelly mpaka akamgeukia vizuri. “Nani anayekupa
bahari zangu Billy wewe!?” “Niambie katika hilo nipo sahihi kwa asilimia
ngapi?” Nelly akamtizama na kunyamaza.
“Basi inamaana ni kweli. Naomba sasa hivi usinywe kwa sababu yangu mimi. Upo sawa kabisa, naomba usiogope kiasi chakutaka kujituliza kwa wine. Sijui kama umenielewa?” Nelly akanyamaza. “Nipo hapa nikitaka utulie kabisa. Najua hujanizoea, na bado una maswali mengi juu yangu. Usiwe na wasiwasi. Haupo hapa na mume wa mtu.” Nelly akamwangalia. Billy akahakiki ndio uliokuwa wasiwasi wake.
“Nisingekufuata mpaka ofisini kwako, kama nia yangu ni kukuingiza kwenye
wizi wa kijinga hivyo. Humuibii mtu. Mimi si mume wa mtu wala sina majukumu ya
kifamilia. Mtoto wangu wa mwisho yupo chuo kikuu na hayupo hapa. Na hata kama
akiwepo hapa, sina chakujificha. Unanielewa?” “Kwa sehemu.” Nelly akajibu.
“Nashukuru kwa hiyo sehemu ndogo uliyoruhusu kuelewa. Nakuhakikishia
upo salama. Usiogope.” Nelly akaanza kula chakula chake, Billy akamuita
muhudumu. Wote wakaagiza juisi. Wakatulia garini wakila. Kimya. Wakala mpaka
wakamaliza. “Mimi unaweza kuniacha tu hapa, nisikusumbue.” “Utarudije sasa
nyumbani?” “Nitachukua usafiri hapa. Usijali kabisa. Wewe nenda ukapumzike.
Nitakuona kesho.” “Sawa.” Nelly akakubali bila kutaka kumlazimisha akihofia
asije kuwa na mipango yake mingine, akawa anaingilia.
“Uwe makini huko barabarani Nelly. Nitakuona kesho.” Billson akaongea
kwa kujali, Nelly akamtizama na kuinama kwa muda. Billy akabaki amekaa garini.
Wakatulia kwa muda. “Kesho nitakukuta wapi, na mida gani?” Nelly akafikiria
kidogo kisha akawa amepata jibu. “Labda hapahapa, kwenye mida ya saa sita.”
Billy akajua ameshaanza kumuweka sawa. Kwamba amekubali muda wake! Akafurahia
hilo. “Basi mimi kuanzia saa sita kasoro nitakuwa hapa nikikusubiri.” Nelly
akamwangalia. Akakunja uso kidogo, na kunyamaza.
“Nimefurahia huu wakati Nelly.” “Wa kula hapa garini!?” “Kabisa. Chakula
kizuri, na tukapata wakati wa pamoja pia.” Nelly akakunja uso kama ambaye
haelewi. Billy akacheka na kuaga. “Usiku mwema.” “Na wewe pia, Billy.” Akatoka
hapo garini. Nelly akaondoka bila yakupoteza muda. Akamuacha hapo.
Jumamosi.
Mara ya Kwanza.
S |
aa sita kasoro
tano, Nelly akawa anaegesha gari yake hapo nje ya hoteli waliyokuwepo usiku
uliopita. Wakati anashuka garini, akamuona Billy akimsogelea. Akacheka kwa vile
alivyokuwa amevaa. Pensi nyeupe na shati nzuri la maua, miwani ya jua na kofia.
Chini akavaa sendozi nzuri za ngozi. Na miguu yake meupe ikazidi kuvutia kwenye
sendozi hizo za kiume. Moja kwa moja Nelly akajua wanaelekea maeneo ya ufukweni
kwa aina ile ya mavazi aliyovaa. “Umependeza sana Nelly!” “Asante. Na wewe uko
vizuri. Umependeza.” Billy akacheka. “Asante. Nikupokee mkoba?” “Hii ni pochi
Billy!” “Si ndio hiyo!” “Hapana. Naomba kubeba pochi yangu.” Safari hii Nelly
akaongea kike sio kwa amri. Billy akacheka.
“Sawa. Basi twende, rubani atakuwa akitusubiria!” Nelly akahisi
hajasikia vizuri. “Rubani kama muendesha ndege?!” “Ndiyo.” Gari anayoendeshewa
Bill bado ilikuwa ikiwaka kuashiria yupo dereva ndani. Mbele kulikuwa na
dereva. Wao wakakaa nyuma. Ukweli na Nelly alipendeza. Kwa kuwa hakuwa akijua
wanapokwenda, alivaa ‘casual’. Ila akajiweka vizuri kuanzia juu mpaka
chini. “Tunakwe..” Nelly akakumbuka aliambiwa ni suprise. Akanyamaza.
Billy akaanza kucheka. “Safi sana. Naona sasa hivi tunakwenda sawa.” Nelly akatabasamu
na kutulia.
“Ulikuwa na usiku mzuri?” Nelly alishapotelea mawazoni, akamgeukia.
“Usiku, ulilala vizuri?” Akarudia swali. “Ndiyo. Na wewe?” “Na mimi nililala
vizuri sababu ya kushiba vizuri.” Nelly akamwangalia tena na kunyamaza. “Si
unajua unaruhusiwa kuuliza?” Billy akamwambia hivyo kama aliyejua yupo na
maswali mengi. “Uliniambia siruhusiwi kuuliza tena.” Nelly akajibu na kumfanya
Billy azidi kucheka. Kimya mpaka uwanja wa ndege lakini upande mwingine wa
ndege binafsi, tena ndogo. Nelly akazidi kushangazwa.
“Twende.” Wakatoka hapo kuelekea ndani kabisa kuliko na ndege ndogo. Nelly
akashangaa anasalimiana na rubani wa helikopta moja iliyopo pembeni kabisa kama
tayari kwa safari. Kisha akamwambia wapo tayari. “Billy!?” Nelly akamuita. Billy
alipomgeukia akamuona kama ameingiwa hofu, asielewe ni hofu ya nini.
Akamsogelea karibu. “Naomba usiogope Nelly. Na ujue tutarudi leo jioni. Usiku
utakuwa kwako. Panda.” Nelly akajishauri na kuamua kwenda tu. Akamtanguliza
yeye wa kwanza ndipo akafuata yeye. Rubani akawapa maelekezo. Walikuwa wao tu, wawili kama abiria. Nelly akabaki ameduaa kama ambaye hajui kinachoendelea na
hajamuelewa kabisa huyo rubani.
Billy akamgeukia tena pale walipokaa. “Vaa hiyo headphone ili kuziba
masikio na kelele, kichwa kisiume. Najua hujawahi kupanda helikopta lakini
nakuhakikishia upo salama kabisa, usiogope.” Nelly akaanza kuvaa, Billy
akamsaidia. Akamuweka sawa masikioni. Wote walipokuwa tayari rubani akaondoa
hiyo helikopta. Ule mlio na vile walivyokuwa wamekaa wakiona nje kabisa, hofu ikamzidia
Nelly. Billy akamuona.
“Nilidhani ungependa kuangalia nje!” “Hapana Billy, mimi nina acrophobia. Siwezi kuangalia sehemu ya chini kwenye umbali mrefu. Hata nikiwa juu gorofani, naogopa kuangalia chini. Siwezi. Na wakati wote kwenye ndege huwa sikai dirishani, hata iweje.” Billy akapoa kabisa. Alijua anamfanyia jambo kubwa la kifahari, lakini ikawa tofauti kabisa. Ukweli Nelly alionekana ameingiwa na hofu haswa.
“Basi usiangalie nje, niangalie mimi.” Akamvuta mkono wake na
kuukumbatia katikati ya viganja vyake. “Samahani. Sikujua kama ingekuwa adha.
Nilitaka ufurahie.” “It’s okay.” Nelly akamjibu akiwa haangalii nje ila hapo
ndani tu tena ameinamisha uso kabisa, akionekana jasiri huyo, amekamatika.
“Nelly?” Akamwangalia. “Nilikwambia kama umependeza?” “Sikujua natakiwa
nivae nini! Nimevaa tu gauni.” “Upo sawa kabisa. Na hilo gauni limekukaa vizuri
sana. Una umbile zuri, Nelly!” Nelly akavuta mkono wake kutoka hapo mikononi
mwake. Billy akacheka. “Unaogopa nini Nelly!?” “Huku tulipo ni juu sana.” “Bado
hilo sio jibu lake.” Nelly akamwangalia tu na kunyamaza. Billy akamsukuma
kidogo kwa bega lake, kisha akamvuta tena mkono. “Utakuwa sawa. Usiogope.” Nelly
akamwangalia tena na kunyamaza.
Wakatulia mpaka walipoambiwa wamefika, anatafuta kutua. Nelly
akainama kabisa ili asione. Rubani akawashusha sehemu nzuri sana, katikati ya
kisiwa, bichi nzuri. Nelly akamwangalia Billy. “Mpaka hofu imeisha! Ni wapi
hapa?” Angalau hilo likamfurahisha Billy. “Unguja. Tulishawahi kufika huku na
wenzangu, nikatamani kuja kurudi. Twende tuzunguke zaidi. Unaweza kutoa viatu
ili utembee vizuri kwa uhuru bila shida.” Hilo likawa jema kwa Nelly kwani
alivaa sendozi za juu kidogo. Akavua. Yeye Billy akabakia na sendozi zake mguuni.
Akamsaidia kumbembea Nelly viatu.
Wakatembea kwa muda tu, Nelly akifurahia ile hali ya hewa pale, Billy
alimpa na yeye kofia na miwani nzuri sana ya jua. Vikamfaa. Kimya kila mmoja
akitembea na kuwaza lake. Bahati mbaya akakanyaga jiwe likamuumiza. Akataka
kunyamazia, lakini Billy akaona. “Naomba kuona.” “Hapana, nipo sawa.” “Nimejua
limekuumiza Nelly. Tafadhali naomba na mimi kuona.” “Hamna kitu! Nipo sawa.” “Nelly!
Hivi unajua ni sawa na wewe kusikia maumivu na kusema unamaumivu au umeumizwa?”
Nelly akanyamaza. Billy akatafuta sehemu nzuri akakaa kabisa. “Naomba ukae hapa
na unipe mguu wako.” “Mimi nipo sawa Billy! Usijali.” “Najali.” Wakabaki
wakitizamana kwa muda. Nelly amesimama, Billy amekaa kabisa mchangani,
akimsubiria.
Nelly mtoto mgumu, aliyejilea mwenyewe akili na mawazo kwa Jax tu,
hakuwa na muda wa mambo madogomadogo kama hayo. Akakunja uso na kukaa. Akatoa
miwani ya jua akijishauri kama anampa mguu au la. Billy naye akabaki akisubiria
tu. “Mimi sioni sababu. Nimesema nipo sawa, nipo sawa.” “Kuna ugumu gani kunipa
nijionee mimi mwenyewe?” Kimya, Nelly akiwa amekunja uso.
“Eti Nelly? Unaogopa nini hicho kinachokufanya unafunga milango yako yote
ya fahamu na kutaka usiwe kama wanadamu wengine wakawaida tu!? Ni nini?” “Nipo
sawa, Billy!” “Kama wewe unaona sawa, kuna shida gani na mimi nikaangalia,
nikajiridhisha mimi mwenyewe nikaona kama ni sawa? Hakuna mwanadamu anakuwa na
maumivu, halafu anayakataa maumivu kwa kusema yupo sawa, ila kusema nitakuwa
sawa, ndio sahihi!” Nelly akajifikiria na kuamua kujiweka sawa.
Akakusanya gauni lake vizuri katikati ya mapaja yake na kusogeza mguu
mbele kidogo kama kumuelekezea Billy. “Ni sawa nikiuweka hapa?” Billy akauliza
kiustarabu, lakini Nelly akamwangalia tu na kugeukia pembeni. Billy akaunyanyua
ule mguu uliokuwa umeumia akauweka mapajani kwake. Akautoa michanga kwa
kupangusa taratibu, Nelly macho pembeni. Akaangalia. “Pamechanika kidogo.”
“Lakini hakuna maumivu! Mimi nipo sawa.” Akataka kuvuta mguu wake, Billy
akamzuia. Akaacha na kutulia.
Billy akaanza kuuminya taratibu, Nelly akiwa amepotelea mawazoni, ila
akamuona anatulia kabisa. Akaendelea kumchua kama anayemfanyia masaji, Nelly
akatulia kabisa ila macho kwingine, mawazo hayapo pale. Akamvuta na mguu
mwingine. Hakukataa. Akamgeukia vizuri. “Imejaa michanga!” Nelly akaongea
akijihami. Billy akaendelea kumpangusa.
“Nikuulize swali Nelly?” “Juu ya hofu yangu?” “Hapana. Hilo utanijibu
utakapokuwa tayari. Ila ujue ni deni. Nitataka kujua, na sitakuuliza tena.
Swali ni, wakati wewe ukimlea Jax, nani alikuwa akikulea wewe?” Mwili mzima wa Nelly
ukafa ganzi. “Maana nilimsikiliza Jax kwenye neno lake la shukurani
akikutambua wewe kama mlezi pekee ambaye amemfahamu hapa duniani. Na wewe si
mkubwa sana kwa Jax. Kama nimeelewa vizuri, inamaana mlikuwa yatima, si ndivyo?”
Nelly akanyamaza. “Nelly?” “Baba ambaye alikuwa wa mwisho kufariki baada ya
mama, aliniacha mimi nikiwa kidato cha nne, Jax anakaribia miaka mitano. Kwa
hiyo sikuwa mtoto ambaye nahitaji kulelewa.”
“Binti yangu wa mwisho nilikwambia yupo chuo kikuu. Unakumbuka?” Nelly
akamwangalia na kunyamaza bila kujibu. “Anaishi na mama yao. Mpaka sasa bado
tunamlea!” Nelly akamuelewa anachomaanisha. “Mimi sihitaji kulelewa. Kwa hiyo
kama tupo hapa kwa sababu ulimsikia Jax akiongea siku ile, ukaingiwa na huruma,
ukatuhurumia, sisi hatuhitahiji kuhurumiwa. Tupo sawa kabisa.” Akavuta na miguu
yake pale alipokuwa ameshikiliwa kwa upendo.
“Lakini bado hujajibu swali langu! Kwamba hata ndugu hawakuwasaidia?” “Hapana Billy! Binadamu wakipewa nafasi na Mungu hugeuka kuwa kama wanyama. Nyumba tuliyokuwa tukiishi na wazazi ilitakiwa kuwa ni mali yetu kihalali, baada ya wazazi kufariki. Ndipo mimi na Jax tulizaliwa pale, lakini garama niliyolipa ili tu kwanza kuweza kuwa na Jax kwenye nyumba moja na kumlea!” Nelly akatulia kidogo, kisha akamuona anatingisha kishwa kama anayekataa au mwenye masikitiko, kisha akaongeza.
“Isee ilinigarimu sana. Nilitumika mpaka
nilipokuja kufanikiwa kuipata nyumba yenyewe kihalali, nilikuwa siwezi kulala
humo.” “Kwanini?” Nelly hakutaka kujibu hilo,
akaendelea. “Niliishia kuiuza na kununua ninakoishi sasa hivi, na Jax akiamua.
Kujibu swali lako, hapana. Mimi mwenyewe ndiye nilibakiwa na jukumu la kumlea
Jax mpaka kumfikisha pale alipo.” Nelly akatulia kidogo.
“Najua sipo sawa. Au kama ulivyosema sipo kama binadamu wengine.
Lakini nilijeruhiwa mno. Nipo hapa nilipo au tumefika hapa unavyotuona mimi na
Jax, ni kwa kujisulubisha na kujikana mno. Hata jina alilokuwa akiniita mama
yangu, ilibidi kufa ili mimi na Jax tuwe hivi tulivyo. Ule uasili wangu wa
kwanza kabisa, ulikufa kwa kuuwawa kilazima na mimi mwenyewe kushiriki.
Ilinibidi kufanya kisheria pia nikiwa hata kinafsi nilishakufa.” Billy akawa
hajaelewa kidogo.
“Hivi unavyoniona, jina langu kamili, umri wangu pia, ilibidi
kubadili ili kufikia umri ambao naweza kuirithi ile nyumba na kukabidhiwa Jax.
Hiyo inaweza ikasikika ni rahisi, lakini sasa hiyo safari niliyopitia mpaka
ndugu kukubali, ndipo nilipofikishwa kwenye kumuogopa binadamu, Billy. Mali ilikuwa
ni halali yetu, lakini ilinibidi kulipa garama mbaya sana, ili tu kutufikia
mimi na mdogo wangu.” “Baba hakuacha mirathi?” Nelly akasimama kabisa na
kuondoka hapo kuashiria kutotaka kuzungumzia hilo. Billy naye akasimama
kumfuata. Nelly mbele, yeye nyuma wakitembea.
Ukweli hilo eneo la ufukweni hapo Unguja, lilikuwa zuri na safi
kuvutia. Maji mazuri na mchanga mweupe ulioweza kuonekana mpaka nje ufukweni. Wakaendelea
kutembea kwa muda. “Njaa inaniuma Nelly.” Billy akaongea akiwa nyuma yake.
“Turudi ndani hotelini tuone kama tunaweza kupata chakula kizuri.” Nelly
akageuka kutoka alipokuwa akielekea, na kurudi hotelini upande wa mgahawani.
Ilikuwa hoteli kubwa sana ya kitalii. Na wazungu wengi walikuwa wamekaa
ufukweni wakipata jua msimu huo wa baridi nchi zao za Ulaya.
Wakaingia na kukaa sehemu ya mgahawani. “Nikwambie kitu Nelly?”
“Tokea lini umeanza kuniomba ruhusa ya kuzungumza?” Billy alicheka sana. “Wewe
ni mtu wa namna gani Billy!?” “Ukiendelea kuwa na mimi utanifahamu tu. Lakini
ninachotaka kukwambia ni..” Muhudumu akawasogelea, wakaagiza matunda, wakati
wakisubiria supu.
Nelly akatulia kabisa akiangalia upande wa baharini. “Nelly?” Akamuita.
Nelly akamgeukia. “Ukweli ni siwezi hata kuhisi maumivu ya ulikopitishwa
maishani kwa kuwa mimi nilikulia sehemu nzuri sana. Wala sitaona aibu kusema au
sitakudanganya. Nilizaliwa na wazazi waliokuwa wanauwezo na walikuwa tayari
kupata watoto. Nikimaanisha walikuwa wamejiandaa na sisi. Tulisoma vizuri na
malezi mazuri. Mama mzuri wa moyo aliyekuwa akitupenda sana, na baba yetu
hivyohivyo. Sijui shida ya malezi kama ulikopita wewe, lakini kwa kukusikia kwa
kiasi tu, japo hujawa muwazi kwangu zaidi, najua uliumizwa sana. Naomba nikupe
pole. Japo najua haitasaidia, na pengine umeshapata pole nyingi sana na ya kwangu
inaweza isilete maana, lakini naomba upokee na mimi pole yangu. Pole.” “Asante
Billy, japo sijawahi kuzungumzia hili na
yeyote yule.” “Basi nashukuru mimi kuwa wa kwanza kujua, na pole.” Nelly akatulia.
Kisha akamwangalia, akakuta bado Billy akimtizama. “Umechoka?”
“Hapana, ila sitajali kurudi nyumbani.” “Kuna kitu kizuri nimekuandalia jioni.
Naomba uvumilie.” “Jioni!?” “Unajua sasa
hivi inakaribia saa kumi jioni! Ndio maana nilitaka tupate tu supu ili kuacha
nafasi ya mlo mzuri wa jioni.” Nelly akabaki akifikiria.
“Kabla hujahitimisha kwa kuiona siku ya leo ni mbaya kwa kukupandisha
helikopta, naomba nimalize mipango yangu yote ya leo niliyokupangia ili
ujumuishe makosa yangu yote.” Nelly akajicheka alipokumbuka hali yake ndani ya
ile helikopta. “Halikuwa kosa Billy! Mimi ndio natakiwa kuomba radhi
nimekukatili.” “Hata kidogo. Nilifanya kwa ajili yako nikitaka kukufurahisha
tu.” Nelly akakunja uso kwa mshangao mpaka cheko likaisha usoni.
“Kwamba ulikodi helikopta kwa ajili yangu mimi!?” “Oooh yeah!” Nelly
akashangaa sana. “Kwa nini!?” Billy akacheka tu na kunyamaza akimwangalia vile
Nelly alivyoshangaa. “Kwa nini upoteze pesa yote hiyo kwa ajili ya...” Nelly
akasita na kubaki akifikiria huku amekunja uso. “Samahani sana Billy! Hakika
sikujua kama ulikodi kwa ajili yangu! Natamani ungenishirikisha kwanza!”
“Nilijua ungekataa. Sasa wewe ulifikiri mimi huwa nazungushwa hapa nchini na
helikopta!” “Sijui Billy! Wadhifa wako na ulivyo hivyo, havipingani na aina
hiyo ya usafiri. Nikajua pengine uliona ndio itakurahisishia kufika hapa kwa
urahisi! Hakika sikujua kama ni kwa ajili yangu! Kwanza kwa nini unifanyie yote
hayo!?” Billy alibaki akimtizama tu.
“Kwa nini Billy!? Hunifahamu, sikufahamu, ni kwa nini uende umbali
wote huo na kupoteza pesa!? Na ninajua utakuwa umepoteza pesa nyingi sana!”
Billy kimya akimtizama. “Tafadhali usifanye hivyo kwa ajili yangu Billy. Mimi
si aina hiyo kama ya wanawake unaowafikiria wewe.” “Wa namna gani?” “Sijui Billy!
Lakini tafadhali usipoteze muda wako na pesa kwa ajili yangu! Mimi sipo...” Nelly
akasita. Wakanyamaza.
Matunda yakaletwa. Wakaanza kula. Walio staarabika hao walijua
kutumia vifaa vya mezani vilivyo. Kimya kila mtu akila. “Billy?” Nelly akaita.
Billy akamwangalia. “Nashukuru.” “Kwa nini?” “Kuweza kunifikiria. Ila tafadhali
usihangaike na mimi. Mimi najijua. Nitakuvunja tu moyo. Nakuona wewe ni mtu
mzuri. Mimi...” “Wewe ni mtu mbaya!?” “Sana Billy. Sana. Mimi mwenyewe huwa
mpaka naogopa kujifikiria. Moyo wangu umejawa madonda ambayo hayajawahi kupona
na sijui kama yatakuja kupona. Mimi mwenyewe najichukia, sina uwezo wa kumpenda
mtu mwingine.” “Mbona umeweza kwa Jax?” “Jax alifanyika kama mtoto wangu, Billy!
Mtoto ambaye sikuwa na pakumuacha au kumkwepa. Lakini kama ningekuwa na ndugu wakueleweka,
nahisi na yeye nisingekuwa naye. Lakini imenilazimu.” Nelly akajiweka sawa.
“Nimemlea Jax na aina hii ya moyo, yeye mwenyewe amekiri kwangu kuwa imemuathiri.” “Haiwezekani!” Kidogo Billy akashituka na kuumia. “Hajakosea. Na wala hakuniambia kwa nia ya kuniumiza. Ila nataka kukwambia, nilimlea nikiwa naumizwa vibaya sana bila yeye kujua ninakopita ili yeye apate pakuishi, akue vizuri na aende shule vizuri. Kwa hiyo maisha yangu yalijaa uchungu mno. Moyo ulikuwa ukienda mbio wakati wote kwa hofu na maumivu kila wakati. Na ikanilazimu kuendelea ili tusiharibikiwe. Imemuathiri Jax, wote tumebakia sisi tu. Japo angalau yeye alijaribu, lakini pia alishindwa."
"Ninachotaka kukwambia Billy,
mimi si mtu unayetaka kuwa naye karibu. Sio mimi. Na ninakuhakikishia kabisa,
kile unachodhania nipo, au nitakuja kuwa, sipo na sina huo uwezo. Tafadhali
acha kujisumbua na mimi. Na nimekwambia kwa undani ili uelewe, ili usiendelee
kupoteza muda wako kwa kuwa najua unayo majukumu.” Billy akavuta pumzi kwa
nguvu na kuchukua uma wake tena. Akala matunda kadhaa na kumeza.
“Ndani ya hii hoteli, kuna chumba nimekodi kwa ajili yako. Ukiingia
humo, utakuta mtu wa kukufanyia masaji. Utapumzika. Kisha atakuja mtu mwenye
mavazi. Atakuletea nguo za usiku tofautitofauti na viatu. Utakavyochagua kuvaa
kwa chakula cha usiku leo, ujue ndio vitakua vyako moja kwa moja. Kwa hiyo
chagua vitu utakavyopenda kubakiwa navyo. Kama utataka akutengeneze na nywele,
ameniahidi atakuja na kijana wake. Watakufanyia kile unachopenda. Saa moja na
nusu usiku, gari itakuja kutuchukua hapa, itatupeleka sehemu kwa chakula cha
usiku.” Nelly akabaki amemkodolea macho kama asiyeamini alichosikia.
“Umenielewa?” “Kwa nini unafanya yote hayo Billy wewe!?” “Leo ni mara
yetu ya kwanza kutoka pamoja. Tulikubaliana ziwe nne. Mara ya nne unikumbushe
hili swali, nitakujibu. Lakini kwa sasa naomba tutembee kwenye makubaliano
yetu.” Nelly akanyamaza kabisa.
Baada ya supu akamsindikiza mpaka nje ya chumba alichomkodishia. Hapo
ni baada ya kupita mapokezi na kupata kadi ya vyumba vyao. “Nitakuwa kwenye
sauna kwa muda, kisha chumbani. Saa moja na dakika 15 nitakuwa hapa nje
nikikusubiri. Na nitawaambia hao dresser, baada ya masaa mawili kuanzia sasa
ndipo waje, watakuwa wamemaliza kukufanyia masaji, umepumzika na upo tayari kwa
kuvaa.” Nelly akatulia kidogo kama anayefikiria.
“Unanisikia?” “Nashukuru Billy. Asante.” Kama ambaye angalau alikuwa
akisubiria hilo. Akacheka. “Namaanisha. Hakuna mtu ambaye amewahi kunifanyia
yote haya! Nashukuru. Asante.” “Karibu. Basi acha na mimi nikakae kwenye sauna
kidogo.” Japokuwa Nelly alishangaa mwanaume huyo kukaa kwenye sauna, lakini
akaelewa ndio maana ana ngozi nzuri vile.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Japokuwa Nelly alikuwa na pesa, na tangia anafanikiwa moja ya agenda
zake ni kuvaa vizuri. Tena sana, akitumia pesa nyingi sana kujiweka nadhifu,
akinunua vitu vyake ndani na nje ya nchi, lakini siku hiyo alikutana na huduma
ya tofauti! Alishangaa aina ya huduma aliyopewa siku hiyo. Hata siku hiyo haikuwa
mara yake ya kwanza kufanyiwa masaji. Tena alishafanyiwa ndani na nje ya nchi
pia, lakini siku hiyo ikawa tofauti. Alilala hapo akihudumiwa kuanzia uso
uliokuwa umepakwa vitu vya asili, akimfikiria Billy na kushindwa kumuelewa.
Akiwa kwenye masaji akalala usingizi mzito, asijue ni kwa nini kumbe
aina ile ya masaji inasaidia kufanya misuli kupumzika kabisa. Na kwa aina ile
ya maisha ya Nelly kufanya kazi mchana na usiku bila kupumzika, mwili ulikuwa
umechoka bila yeye kuipa akili yake ruhusa ya kufikiria kuchoka. Akajikuta
amepotelea usingizini katikati ya masaji na miziki mtulivu. Alikuja kuamshwa na
watu wawili ambao mmoja alimwambia achague nguo, mwingine alikuwa akitayarisha
meza na vitu vya kumtengeneza nywele na uso. Kumbe mtu wa masaji alishaondoka
muda mrefu sana.
Matayarisho ya kwenda kwa chakula cha usiku yakaanza, Nelly asielewe
wanakwenda wapi huko ambako anatakiwa kupendeza kwa kiasi hicho cha kumwaga
pesa nyingi hivyo! Na hakujipunja. Alichagua vitu vya thamani tupu. Kuanzia
nguo, viatu, hereni, mkufu mzuri sana na alijua ni garama. Na vyakuvaa mkononi.
Akacheka moyoni. “Ameyataka mwenyewe. Acha pesa imtoke ili asirudie tena.”
Akajisemea moyoni wakati ameachwa mwenyewe hapo chambani akijitizama na
kusubiria muda atoke.
Chakula cha Usiku Mjini
Unguja.
Mara Yao Ya Kwanza.
N |
elly alitoka
akiwa amejawa na furaha na ametulia. Akili safi na mwili uliopata mapumziko ya
miaka kwa aina moja tu ya masaji, tena ya muda mfupi aliokuwa amepatiwa.
Walimchua misuli yote mpaka anaamka, akahisi mwili si wake. Mwepesi na akili
safi. “Ndio maana wengine wanavicheko kila wakati! Kwa aina hii ya masaji,
lazima kila siku ujisikie vizuri.” Akajisemea Nelly akiwa anatoka chumbani
kwake. Akakuta Billy akimsubiria nje ya chumba chake. Billson alipomuona na
tabasamu kubwa vile, akajua masaji aliyoagiza imefanya kazi yake.
“Ulipata mapumziko mazuri?” “Mwili nausikia kama wa binti wa miaka 13!”
Billy akacheka. “Nilijua utapumzika tu.” “Nilihitaji kwakweli, japo sikujua
kama naweza pata aina hii ya masaji! Kwani wanafanyaje!?” Billy akacheka tena.
“Nawapenda kwa sababu na mimi huwa wananisaidia sana kunipumzisha haswa kipindi
ninachokuwa na uchovu wa mwili, mawazo na majanga ya maisha.” “Wewe unayecheka
kila wakati unakuwa na majanga gani ya maisha?” “Unafikiri ni wewe peke yako tu
ndiye ambaye wanadamu wamekutenda?” Nelly akamtizama kama asiyeamini.
“Twende, dereva atakuwa amefika. Asitusubirie muda mrefu.” Wakatoka
wakitembea. “Mbona leo huniombi kunishika mkono na hivi nilivyopendeza!?” Billy
alicheka sana. “Nelly!” “Mimi mwenyewe najua nimependeza. Angekuwa Jax
angeniomba kunishika mkono.” “Nilikuwa najishauri Nelly! Usiku wa leo sitaki
uishie pabaya. Nataka wakati mzuri. Sasa sikutaka historia ijurudie. Maana mara
ya mwisho nilipokuomba, ulinikatalia mbele ya kadamnasi.” “Sikuwa nimefanyiwa
aina hii ya masaji.” Billy akacheka sana.
“Usifanye mchezo na masaji ya mchina.” “Ni mjapani.” Billy
akamsahihisha akicheka. “Ewaa! Umemtoa wapi huyu kijana!? Amenichoma choma na
kama vijisindano, akaniwekea mawe ya moto hivi kwenye uti wa mgongo halafu...”
Billy akazidi kucheka maana Nelly akawa kama anavuta kumbukumbu. “Aisee acha
kabisa!” “Huwa ananisaidia sana. Ni mtaalamu. Hata ukiwa na msongo wa mawazo
kiasi gani, kwake utatulia tu.” “Sasa wewe Billy una msongo gani wa mawazo?
Kazi nzuri, inamaa pesa nayo ni nyingi tu. Watoto unao. Hujakua kwa hekaheka
kama wengi wetu. Mzuri wa sura na umbile.” Hapo Billy akacheka mpaka akasimama.
“Kumbe mimi mzuri!” “Najua unajijua sana ndio maana unavijimaringo
vyako hivi. Kwa hiyo nina maana vyote hivyo vinaweza kukupa mwanamke yeyeote
unayetaka. Kwanza wakisikia tu unafanya kazi World Bank na jina la cheo chako,
watakutaka tu. Sasa unamsongo gani wa mawazo?” “Maisha yana mtindo wa kumsumbua
mwanadamu bila kujali ulivyo na
ulichonacho. Hakuna mwanadamu ambaye hana matatizo Nelly. Sema wengine tumeamua
kupambana nayo kwa staili ingine bila hasira. Tena baada yakuona hasira na
uchungu ni kujiumiza mwenyewe.” Hapo Nelly akanyamaza na wakawa wamefika kwenye
lifti. Wakatulia wakisubiria.
Ilipofunguka na baadhi kushuka, wakaingia na kukuta watu wengine
ndani. Nelly akatulia hapo ndani lakini Billy yeye akawaangalia aliowakuta humo
ndani na kusalimia. Macho na akili zake vikatua kwa mtoto wenyewe asili ya
kizungu. Akaanza kumuuliza maswali na kumtania mpaka wazazi wake na huyo mtoto
wakaanza kucheka na Billy. Akaongea lugha iliyoendana na huyo mtoto akawa
akijibu na kucheka sana mpaka Nelly asiyependa watu na ambaye hakuwasalimia
akawageukia. Akaona vile yule mtoto anavyocheka na Billy. Akageuka vizuri.
“Unawatoto?” Akauliza mama mtu. “Binti wakubwa sasa. Wa mwisho yupo
chuo. Lakini napenda sana watoto na ninamisi huo umri wa fikra zisizo na hatia.
Kuongea chochote bila wazo la pili.” “Kutokudanganywa.” Akaongeza baba yake
yule mtoto. “Ewaa!” Akaitika Billy kwa haraka na kufanya wote wacheke kwa
pamoja. “Tunae kaka yake huyu, hapa tunapozungumzo yupo na adhabu huko chumbani.
Haruhusiwi kutoka.” Akaongeza mama mtu. “Basi naamini mnaelewa
ninachozungumzia.” Billy akaongeza na kufanya wacheke zaidi. Wakazungumza
kidogo, lifti ikafunguka.
Kwa kuwa Billy na Nelly walikuwa karibu na mlango walitakiwa wao
watoke kwanza. Billy akamgeukia yule binti. Akainama kabisa mbele ya yule mtoto
na kumwambia kama anayenong’ona ila kwa sauti ya juu tu iliyoweza kusikika kwa
wote. “Do your parents a favour.” “What?” Kakamuuliza Billy
akicheka. Kalionekana ni kachekaji sana. “Don’t grow up so fast.”
Akachekaa sana. “Okay?” Billy akamuuliza. “Okay.” Akakakubali
akicheka sana. “Good! Deal.” Bill akampa na mkono kabisa kwamba
wamekubaliana, asikue kwa haraka. Akaaga wazazi wake wakaondoka na Nelly ambaye
alishatoka hapo ndani akisubiria nje.
“Nelinda, naomba nikushike mkono.” Nelly alishituka sana. “Umejuaje
hilo jina!?” Billy akajua ameharibu maana mpaka tabasamu ilimuisha Nelly usoni.
“Kwanza situmii hilo jina kabisa. Nani amekwambia!?” “Naomba usipaniki Nelly.
Samahani.” Akatulia akimwangalia vile alivyobadilika na kugeukia pembeni. “Nelly?”
Kimya. “Na naomba usifikirie kuondoka hapa sasa hivi. Nimekuandalia usiku mzuri
sana. Nataka tukapate chakula kizuri na wakati mzuri.” Nelly akawa kama
anajishauri. “Twende.” Akamshika kabisa na mkono, wakatoka pale Nelly akiwa
amepoa kabisa.
Kweli walikuta gari likiwasubiria nje ya hoteli. Billy akamfungulia
mlango, na yeye akafunguliwa na dereva. Wakaondoka hapo. “Samahani, sikujua
kama hutumii hilo jina.” “Hilo jina liliuwawa kwa garama kubwa sana, Billy.
Naogopa hata kulisikia.” “Nakuahidi sitarudia tena. Samahani.” “Nani anakwambia
habari zangu Billy? Nimeshajua si Jax, kwa sababu Jax hajakua na hilo jina na
nilishamkataza tokea mtoto mdogo kuwa asiwahi kuniita hivyo kwa usalama wake na
wangu. Ni kama hilo jina halijui kabisa.” “Sitakwambia Nelly. Ni moja ya kiapo
nilichotoa kwa huyo mtu. Naomba uelewe na ukubaliane na hilo. Mimi ni mgumu
sana kuvunja viapo haswa ninapokuwa nimeahidi mimi mwenyewe nikiwa na akili
zangu timamu.” Nelly akanyamaza.
“Umenichukia?” “Hapana, Billy.” Akajibu Nelly na kutulia. “Umefanya
uchaguzi mzuri sana wa vazi. Umependeza sana Nelly. Sana.” “Natamani nilale
hivihivi.” Billy akaanza kucheka tena. “Acha nikwambie ukweli Billy. Mimi
napenda kuvaa. Tena kuvaa vizuri.” “Nimekuona.” Billy akakubaliana naye. “Lakini
linapofika swala la nguo za ‘Gucci’ huwa
nafikiria mara mbilimbili. Na ninaweza sema ninayo magauni yao machache sana,
hayazidi magauni matatu.” Billy akazidi kucheka. “Kwamba unayakumbuka?” “Kwamba
yamewekwa mahali maalumu. Nikirudi kutoka kazini, na yule msichana wa kazi akiwa
ameondoka kwangu, na yenyewe yawe yamebaki pale.” Billy akazidi kucheka.
“Usicheze na ‘Gucci!’ Yanaongeza
ujasiri na furaha.” “Kwa hiyo hapo unafuraha?” “Huoni mpaka nimeomba kushikwa
mkono?” Billy alikuwa akimtizama Nelly asiamini kama ni yeye. Kweli alikuwa
ametulia na amependeza sana. Alipambwa vizuri na kiutaalamu, hakupoteza uzuri
wake wa asili.
“Nakushuru Billy. Japokuwa sijajua kwa nini unamwaga pesa zako
hivi...” “Mimi simwagi pesa zangu. Najua kutumia pesa zangu vizuri, na sehemu
sahihi.” Nelly akamwangalia na kuamua kuendelea. “Kama nilivyokuwa nikitaka
kusema. Japokuwa sijui nia yako, acha kwa leo moyo wangu ufurahie japo kwa muda
kabla sijarudi kwenye ulimwengu wangu.” “Huna haja yakurudi kwenye huo
ulimwengu na kupoteza furaha yako ya leo, Nelly. Unaweza kuishi huko ila ukaamua kuwa na
furaha tu.” “Ni rahisi wewe kusema kuliko mimi kuishi.” Billy akacheka tena
akionekana anafikiria kidogo.
“Tatizo lako wewe unadhani wewe ndio unamatatizo mengi hapa duniani.
Watu tunamatatizo Nelly! Nikikwambia yangu unaweza ukadhania ni hadithi. Lakini
ilibidi kuchagua. Watu kukutenda ni jambo moja, huna uchaguzi na huna jinsi.
Ila kuendelea kujiadhibu kwa ulivyotendwa, hilo ni jambo la pili na ni uchaguzi
binafsi kila mtu anatakiwa kuamua na kuishi hivyo.” Nelly akamtizama na
kunyamaza bila kujibu.
Hawakuwa wakienda mbali na ni kama dereva alijua wanakoelekea. Akaona
gari linaingia sehemu ambayo hapakuwa na nyumba. Akajiweka sawa kuona hicho
alichoandaliwa na Billy. Akaanza kucheka vile alivyokuwa anapokelewa na taa
zilizopangwa kwa mstari, tena chini mchangani kama kutengeneza njia. Akacheka
na kutingisha kichwa. Billy akamuona na yeye akacheka.
“Kazi unayo Billy! Sasa yote haya kwa nini!?” “Wewe twende.” Gari
lilikuwa limeegeshwa, akamfungulia mlango, akashuka. Alipokwenda upande wa pili
wa gari, akasimama kwanza. “Billy wewe! Haya mambo umeyafanya saa ngapi!?”
“Pesa yangu ndio inanitumikia.” Akaongea bila hata kuuma maneno. “Mwenzio haya
mambo nimeona kwenye filamu tu!” “Hata mimi. Nikajiuliza hivi ni kwa nini watu
wengine ndio waendelee kunufaika na pesa yangu halafu mimi mwenyewe mtafutaji
hata sifaidi! Ndio nikaona tuje tufurahie pamoja. Nikawaonyesha filamu
niliyokwisha ona kama hivi, nikatamani siku moja na mimi kuja kuwa sehemu kama
hiyo. Walipoelewa na kuniahidi wanaweza kunitengenezea sehemu kama hii, nikawalipa
wanitengenezee.” Nelly akarudisha macho kwenye hiyo sehemu. Akacheka taratibu.
“Kweli pazuri.” “Basi twende tukatumikiwe. Na mimi ni mara yangu ya
kwanza kuwa kwenye madhari nzuri hivi. Nilitaka na wewe uwepo, tupumzike wote.”
“Nashukuru.” Wakaanza kutembea kusogelea hiyo sehemu iliyokuwa imeandaliwa
maalumu kwa ajili yao. Ni taa zilizowekwa tu hapo ndizo zilizoweka mwanga eneo
hilo zima. Kukawashwa na moto maalumu wa umeme, si wa mkaa ili usizime kwa
upepo. Kwa hiyo huo moto ukusaidia kuleta hali ya joto kiasi maana ilikuwa
karibu na ufukweni, usiku huo tayari kulikuwa na baridi. Hakika kulivutia.
Kibanda kilichokuwa kimejengewa hapo kilipambwa vizuri sana. Halafu
kulikuwa na mziki mzuri. Nelly akazidi kucheka kwa kuhamasika zaidi. “Aisee hii
ni nzuri na sahihi! Kwa kutizama tu, akili inatulia!” “Nimefurahi kama umefurahia
Nelly. Sikujua kama ungependa kwa kiasi hiki!” Wakaenda kukaa. Akasogea
muhudumu wa kiume na kuanza kuwafungulia vinywaji hapo mezani. Na vyenyewe
vilikuwa hapo na kupangwa vizuri.
Duniani Tunayo Dhiki.
Wakafunguliwa champaign. “Nataka tu toss.” Billy akaanza
wakati glasi yake imeshapata kinywaji hicho cha champaign. “Kwa ajili ya nini?”
Nelly akauliza baada ya muhudumu kumaliza kumuwekea na yeye kinywaji kwenye
glass yake. Akawapisha kabisa pale. “Kwa ajili yetu na maisha.” Nelly
akafikiria kidogo. “Mimi naona si kwa maisha. Labda kwa ajili yetu tu.” Bill
akacheka na kuweka glasi yake chini.
“Nilikwambia jinsi nilivyokuwa nimezaliwa kwenye neema?” “Na wewe
mwenyewe umejawa neema.” “Sikatai. Sisi ni watu wa Zimbabwe, lakini mimi na
ndugu zangu ni raia au tulizaliwa na kukulia kwenye mji wa Valencia, nchini
Spain. Baba na mama walipofika tu huko miaka hiyo, wote wakajiingiza kwenye
kazi za medical kitu kilichotusaidia sana kimaisha.” “Inamaana kama
madaktari?” “Baba ndio alikuwa daktari. Alitumwa na serikali yake kusoma. Ila
kwa kuwa alifanya vizuri sana, alipomaliza, akarudi nchini Zimbabwe akatumika
kwa miaka waliyokuwa wamekubaliana na nchi yake iliyompelekea huko kusoma.
Akaoa na kuamua kurudi tena Spain. Anasema alipapenda sana na alikusudua kuja kuishi
huko. Kufupisha habari kwa upande wao, mama naye alipofika huko akasomea mambo
ya unesi. Basi wote walifanikiwa sana.” “Bado wapo?” “Mpaka leo wapo.” Nelly
akashangaa sana.
“Baba anasema sisi tuna genes za kuishi miaka mingi. Lakini
pia nafikiri ni jinsi ya kutunza hii miili, Nelly. Sisi tumejifunza kutunza
miili yetu kutoka kwa wazazi. Wanausemi unaosema kuwa hii miili huaribika. Kwa
hiyo linapofika kwenye kuitunza ni kipaumbele, ili iweze kukutumikia. Sasa hawa
wazazi wangu hawa, wanandoa ya mpaka sasa hivi. Simaanishi kwamba wanandoa ya
ajabu sana, ni kama wanadamu wengine tu, ila sisi watoto wao tulivutiwa au
niseme mimi nilivutiwa zaidi na jinsi walivyoweza kuwa pamoja mpaka kutulea
sisi. Nikimaanisha katika ugumu wote wa maisha, lakini walimudu kuwa pamoja.”
Billy akanywa kinywaji kingine si ile champaign. Ni kama aliona isubiri kwanza.
Wakaletewa na supu. “Kunywa hiyo supu ikiwa ya moto kabla haijapoa.”
“Nakusikiliza.” “Najua. Lakini kula wakati nikizungumza.” Nelly akachukua
kijiko maalumu chakunywea supu, akaanza kunywa. “Mlizaliwa wangapi?” “Watatu.
Nina kaka yangu na dada yangu. Yeye ndio wa mwisho. Mama alisema alikusudia
lazima aje kuwa na mtoto wa kike. Anasema asingeacha kuzaa kama asingepata
mtoto wa kike.” “Kwa nini!?” Nelly akashangaa sana.
“Anasema akiwa nesi aliona mengi. Akamuomba Mungu aje azae mtoto wake wa kike, wakumvalisha nguo
atakapokuwa mzee, sio wakwe.” Nelly akatulia kidogo. Billy akamuona amepotea
kabisa pale. “Nelly?” Akamuita. Nelly alikuwa akikoroga supu yake, akamtizama. “Kwetu
ilikuwa tofauti Billy. Baba hakufurahia kabisa kitendo cha mama kuzaa mtoto wa
kike.” “Ambaye ni wewe?” “Yeah! Alimnyanyasa sana mama kiasi cha kumuathiri.
Nafikiri pia ikaanza kumuingia na mama kuona kama alikosea na kumfanya aishi
vile na mimi. Hatukuwa na mahusiano mazuri sana na mama. Sasa sijui ni kwa hilo
au sababu ya mateso ya baba! Lakini ni jambo ambalo baba alihakikisha na mimi
naelewa. Kwamba hakufurahia kupata mtoto wa kike. Na alisema waziwazi ni aibu
kwao kwamba hana mrithi.” Billy akamuhurumia.
“Na mbaya zaidi, nafikiri mama alishindwa kupata mimba ya pili kwa
haraka. Nikabakia mimi tu zaidi ya miaka kumi. Aisee tulijua na kuelewa hakuwa
akipafurahia pale kwetu sababu ya kukosa mtoto wa kiume. Alikuwa anaweza
akapotea hata mwaka, ndipo anarudi. Na akirudi hata msichana wa kazi kama ni
mgeni, atajua shida yake ni kutojaliwa mtoto wa kiume au mkewe hana uwezo
wakumpa mrithi. Alikuwa mnyanyasaji mno, kiasi cha kusikia ile hali mpaka
moyoni. Alimdharau mama kwa kumpiga makofi hata mbele ya watu endapo akifanya
jambo asilolipenda yeye.” Nelly akafikiria kidogo akawa kama amepata jinsi ya
kumuelezea Billy akamuelewa anachozungumzia.
“Yaani anaweza kumtuma maji ya kunywa mbele za watu. Mama akimletea,
anagomba labda glasi ina maji nje, hajaikausha vizuri. Atapigisha ile glasi chini
kwa nguvu na kumchapa mama makofi hapohapo.” “Haiwezekani Nelly!” “Kweli Billy!
Siwezi kusahau hiyo hali. Mpaka sasa huwa nakaa najiuliza, hivi mwanadamu
anawezaje kumruhusu mwanadamu mwenzie amtendee hivyo!? Kwa nini mama aliruhusu
hiyo hali!?” “Labda kiuchumi.” “Usifikiri baba alikuwa ni mtoaji! Hapana. Tena
kwa kusikia kabisa akisema hawezi kupoteza pesa yake kulea mke wa mtu. Yaani
mimi.” “Nelly!?” “Nakwambia ukweli Billy, sidanganyi. Alichokuwa akisema eti
yeye hawezi kuhangaika kufanya kazi, aje alishe mtu atakayekuja kuzalishwa na
mwanaume mwingine. Kwa kusema waziwazi.” Nelly akaendelea kuzungumza kwa
uchungu, asikumbuke ni Billy ndiye aliyekuwa akizungumzia juu ya familia yake.
“Na ninapokwambia alikuwa akiondoka hata mwaka, jua ni mama ndiye
aliyekuwa akiendesha familia japo nyumba ni yeye baba alikuwa ameijenga.
Anyways, tuendelee na wewe. Vyangu vitakushangaza tu.” “Hapana. Nimefurahi
kukusikia. Nimepata majibu ya maswali mengi sana juu yako.” Nelly akacheka kwa
kuguna akaendelea kunywa supu yake, Billy akimtizama.
“Nakusikiliza Billy.” “Kwa aina ya ndoa ya wazazi wangu, mimi na kaka
yangu tukaambiana baba alibahatika kwa kuwa alioa mtu wa nyumbani.
Tukakubaliana tukaoe nyumbani. Lakini baadaye kaka yangu akapata mwanamke
kulekule, mwenye asili ya kizungu, akaamua kuoa. Mimi nikakazana, nikarudi
Zimbabwe nikapata mwanamke, akakubali kwa haraka sana tukaishi naye Spain. Ndoa
ikafungwa ya kimila, nikapata mke, tukarudi Spain. Mungu akajalia watoto hao
wawili wa kike.” Akamuona Billy anacheka kwa kusikitika.
“Nini?” “Mimi sikujua kama kuna shida kati yetu mpaka nilipokuja kujua
mwenzangu anamahusiano na rafiki yangu.” Hapo Nelly akaweka kijiko chini.
“Rafiki ambaye aligeuka kama ndugu ambaye tulikuwa naye pamoja ila mwenzangu
hakuwa akifanya kazi nje ya nchi kama hivi mimi. Alikuwa akiishi na kufanya
kazi hapohapo nchini. Mweupe wa hapo. Hivi unajua Anele aliniacha kwa ajili
yake!” “Subiri kwanza Billy! Alikuachaje?!” Billy akajicheka kwa kujidharau na
kutingisha kichwa kwa masikitiko, Nelly akimtizama kama asiyeamini.
“Aliniacha kirahisi kabisa bila shida akisema yeye hana furaha kwenye
ndoa yetu. Alitegemea tungekuwa tukiishi wote lakini amekua na ndoa ya peke
yake, mimi sipo nyumbani. Amekua akilea watoto peke yake. Haijulikani kama
ameolewa au la! Watoto wanamtambua Carlos kama ndio baba yao. Kwa hiyo kule
kumfumania na Carlos haikuwa bahati mbaya, ni mahusino ya muda mrefu na anashangaa ni kwa nini nimechelewa
kugundua. Akaita hiyo nayo ni ishara ya kuwa ndoa yetu ilishakufa muda mrefu
bila mimi kujua. Akatafuta mwanasheria kwa ajili ya talaka. Hivi
tunavyozungumza, Anele na Carlos walioana, wanaishi pamoja. Mbaya zaidi,
wanaishi na binti yangu mdogo ambaye na yeye anamtambua Carlos kama baba.” “Billison!”
Nelly akashangaa sana, ila Billy akacheka.
“Acha Nelly! Nilikaribia kujipiga risasi kujiua. Lakini binti yangu
huyo mkubwa akanisihi sana nisije kumuacha hapa duniani kwa kujiua. Alihama mji
kabisa, mpaka leo ameshindwa kuzungumza na mama yake, ila mdogo wake yupo na
mama yake. Na wanaendelea vizuri tu.” “Pole sana Billy.” “Ndio maana unapomzungumzia
mwanadamu, nakuelewa Nelly. Carlos alikuwa rafiki akinichekea, nisijue alikuwa
akilala na mke wangu! Ameoa mwanamke niliyemuhamisha nchi na hana haya wala
hajutii! Anasema Anele hakuwa na furaha na alikuwa mpweke.”
“Kwani hamkuwa mkiishi pamoja?” “Unajua hizi kazi Nelly. Na yeye
nilikuwa nikimwambia. Ni kwa muda tu wakati natafuta nafasi ya kazi kama
niliyonayo sasa hivi. Nilimwambia garama zetu za maisha zipo juu sana. Kuendelea
kuishi vile, ni lazima na mimi nikue kimaisha. Kazini. Ili tuishi kwa furaha
zaidi. Nilimwambia ni kwa muda tu, tungetulia pamoja. Akaniambia ameelewa.”
“Kwani yeye hakuwa na kazi?”
“Hapana. Ila kutumia. Hujawahi ona mwanamke mwenye matumizi na pesa kama yule
na huyo mtoto wake wa mwisho. Anele ni garama haswa. Sasa aina ile ya matumizi
ilikuwa nilazima nifanye kazi. Unaingiza huku, huku zinatoka. Nilikuja kugundua
pia alikuwa akijenga sana kwao. Hapa ninapokwambia huko Zimbabwe ana mahoteli.
Na yote hiyo ni pesa yangu.” “Sasa alitegemea upataje pesa mkiwa mnaishi naye
tu nyumbani!?” “Asante.” Billy akashukuru kwa Nelly kuelewa.
“Ndio nakwambia hivi, namuelewa mwanadamu. Nilikaribia kurukwa na
akili na ndio kujiua. Mbaya zaidi kaka yangu yeye ambaye alioa mwanamke wa
palepale, mwenzangu ndoa yake inaendelea mpaka leo! Mimi niliyetaka ubora zaidi,
nikakwama. Baba alipoona nipo vile ndipo akaniambia nitakosa na kazi ambayo
imeshanigarimu ndoa na mtoto. Maana aliniacha nikiwa nakaribia kupandishwa
cheo. Akaniambia nichague kujiumiza zaidi nife au nikubali matokeo na
niendelee. Mama akaniambia kuchagua furaha ni rahisi japo nimeumizwa,
itanisaidia. Haikuwa rahisi Nelly. Kwa kuwa binti yangu alimchagua Carlos na
mama yake, ikabidi niwaachie ile nyumba nikarudi kuishi na wazazi. Ndipo binti
yangu mkubwa na yeye akanifuata. tukiishi hapo mpaka alipomaliza chuo.
Akachukua kazi mji mwingine kabisa, na mimi nikachukua cheo nchini Uingereza.
Nikaishi Uingereza kwa miaka zaidi ya mitano ndipo nafasi ya huku ikatokea.
Nikamwambia baba narudi kuishi Afrika. Binafsi alinipongeza. Alijua ningechukia
kabisa Afrika. Lakini ikawa kinyume. Ndipo nilipo.” Nelly akanyamaza
akifikiria.
“Kwa hiyo Nelly, mimi ilinibidi kuchagua fungu la pili. Furaha.”
Nelly akamwangalia. “Si rahisi, lakini ilinibidi kufanya juhudi za makusudi
kuishi hivi unavyoniona leo. Nilipoteza nyumba ambayo nilifanya kazi kwa juhudi
kwa makusudi kuilipia mpaka kumaliza. Lakini sasa hivi anaishi Anele na Carlos.
Nimepoteza mtoto kwa rafiki yangu. Hutamsikia akinipigia simu kunijulia hali,
labda iwe ni birthday yangu. Mara zote mimi ndio huwa namtafuta, napo hana muda
mwingi na mimi kwenye simu, inakuwa kama nampotezea muda.” “Ukienda
kumtembelea?” “Ndio hivyohivyo. Haonekaniki kama ni jambo analotaka. Lakini na
mimi huwa najitahidi. Kila kwenye birthday yake huwa nakwenda kumuona. Hata
akinipa dakika 10 pia nashukuru. Nikimuomba tutoke kwa chakula, anaweza akataka
lazima mama yake na Carlos nao wawepo sababu ndio familia yake.” “Billy!” Nelly
akashangaa sana.
Billson akacheka kwa masikitiko. “Acha tu.” “Unafanyaje sasa!?” “Baba
aliniambia lazima nijue ninachotaka na kuhakikisha nakipata. Maadamu ni binti
yangu, na ninataka muda naye, akasema hiyo ndio iwe garama yakulipa. Kuendelea
kuwakubali hao wawili wawepo kwenye maisha yangu tu. Kwa hiyo huwa nikitaka
kuonana naye, mara nyingine huwa nakwenda palepale nyumbani.” “Mmmh!” Nelly
akachoka kabisa. Wakamaliza supu. Wakaletewa chakula. Wakaanza kula kimyakimya
tu kila mmoja akiwaza lake.
Akamuona Nelly anacheka mawazoni ila tabasamu usoni. “Nini?” “Hivi
kama nikuondoka hapa kisiwani usiku huu na hivi nilivyoshiba, tunaondokaje?”
“Kuna chaguzi mbili. Ipo ndege ya kimataifa kutoka nje ya nchi, inapitia hapa
leo usiku wa saa tano kuelekea Dar. Nimeambiwa tunaweza kupata nafasi first
class. Au unaweza kurudi kulala kwenye kile chumba. Nimelipia mpaka kesho.”
“Wewe umeamuaje?” “Nitaamua baada yako. Kama utaamua kulala, ujue na mimi
nitalala mpaka kesho ndipo tuondoke wote. Ila kama unaamua kuondoka, pia ujue
tutaondoka wote. Uamuzi ni wako.” Nelly akatulia akifikiria.
Akagundua Billy anamtizama. Akamwangalia. “Unapenda kuniangalia
wewe!” “Kwa kuwa unavutia.” “Acha hizo bwana! Ila ujue nimefurahia. Kila kitu.”
“Mmmh! Sidhani kama ni kila kitu. Helikopta?” Nelly alicheka sana baada ya
kukumbushwa. “Aisee ile ilikuwa mbaya!” “Niliona, hata rubani aliona na kujua.”
Nelly akazidi kucheka. “Sawa. Kasoro helikopta. Ila vingine vyote nimefurahia.”
“Nimekuona. Leo umekuwa watofauti Nelly. Unacheka!” “Sijapata huu wakati
tokea...” Akafikiria bila kupata jibu. “Aisee sijawahi kupata huu wakati Billy!
Sijawahi.” “Basi nimefurahi kama umefurahia.” Wakatulia, mziki ukitumbuiza
taratibu.
“Billy?” Akamuita kama aliyekuwa mawazoni. “Mimi napenda kucheza.”
“Nilikuona siku ile na mdogo wako.” “Nilipokuwa masomoni nikifanya shahada
yangu ya tatu, nchini Uingereza, nikajiambia nifanye kitu kigeni na chatofauti
kwa kujipongeza kufikia pale nilipo. Ndio nikachukua dance classes.
Madarasa yanayofundisha jinsi ya kucheza, nje ya pale chuoni.” “Hongera sana.”
“Sikuishia hapo. Nilipoona nirahisi nikaongeza na ice skating.” Billy
alicheka sana. “Kwa kusema hivyo, naomba tucheze wote.” “Mimi si mtaalamu wa
kucheza, Nelly.” “Kwa kuwa leo nina mudi nzuri, nitakufundisha.” “Okay.” Billy
akasimama na kwenda kumnyanyua pale.
Nelly akaanza kucheza mbele ya Billy, Billy akaanza kucheka.
“Fuatisha sasa, acha kusimama tu.” Nelly akaongea akicheza. Walicheza wakicheka
kwa muda mrefu tu. Ukaja mziki wa taratibu. “Bado unataka kucheza na mimi?” Akauliza
Billy kiustarabu. “Oooh yeah! Come here Billson.” Akamuita kwa ishara ya
kidole. Billy akacheka akimsogelea. Akamshika taratibu wakaanza kucheza.
“Sijui nimeanza kulewa!” Billy alicheka sana akijua ni kweli ameanza
kulewa. “Huu uchangamfu si kawaida yangu!” “Mimi naona ni kupata wakati mzuri.”
“Eti eeh?” “Yeah.” “Nakushukuru Billy. Na kama hutajali, naomba leo nilale hapa
mpaka kesho. Hata hivyo Jax leo atakuwa kwake, sina sababu ya kurudi.” “Kwani
huwa anakuwa kwako?” “Anakua kwangu na hajui kupika. Ana kazi ya kutengeneza
juisi na chai tu. Kwa hiyo akiwepo nyumbani huwa na jitahidi kuwepo ili
nimsaidie chakula.” “Haina shida. Tunaweza kuondoka kesho.” Walicheza hapo kwa muda, kisha wakarudishwa
hotelini.
~~~~~~~~~~~~~~~~
B |
illy
alimrudisha mpaka chumbani kwake na kumfungulia kabisa mlango. “Hii mara ya
kwanza imeisha vizuri.” “Tutaona ya pili, tatu na nne itakavyokwenda?” Nelly
akauliza. “Yeah. Nimeshaanza kuwa na hamu na ya pili.” Nelly akacheka.
“Tutakwenda wapi?” “Nilikwambia sitakwambia Nelly!” “Sawa. Ila usifanye garama
kwa kiasi hiki. Au niambie tuchangie.” “Wewe panga safari zako, unialike. Kama
nitakua na muda nitakufikiria.” Nelly alicheka sana. “Basi kama ni hivyo na
mimi nitakufikiria.” “Sio katika hizi safari tatu zilizobaki. Hizi
tumeshakubaliana.” Wakakaa hapohapo mlangoni na kuendelea kufahamiana taratibu.
Billy akaagiza vinywaji, wakaletewa hapohapo walipokuwa wamekaa. Nje ya mlango
chumbani kwa Nelly. Kila mmoja akatamani kumuuliza mwenyeziwe swali la msingi,
lakini wakaona wawe na kiasi. Wakanyamazia.
0 Comments:
Post a Comment