Naya
aliondoka kwao na baba yake pamoja na Zayoni akawashusha na wenyewe kwenye
saluni ili kukatwa nywele na kutengenezwa vizuri ili na wenyewe wajiwakilishe
vizuri. Kisha akaondoka hapo akiimba taratibu tu akielekea saluni. Simu ya
Joshua ikaingia. “Mama Kumu?” Naya akaanza kucheka. “Uwe unaniita ita hivyo mara
kwa mara ili nizoee kabisa.” Joshua akaendelea kucheka. “Umeamka
salama mpenzi wangu?” “Salama kabisa, na maandalizi ya kukabidhiwa mke na Mungu
yameshaanza.” “Maandalizi gani?” “Acha haraka Naya. Usiku wa leo si unalala
hapa?” Naya alicheka sana.
“Nataka
ukiingia hapa, usitamani kutoka.” “Ndio maandalizi mazito hivyo!?” “Sana Naya.
Nimesubiri kwa uaminifu wote, eti! Mpaka Mungu mwenyewe ameniheshimu! Acha
nisimuangushe Mungu wangu, nimuonyeshe hajakosea, nipo tayari na wewe.” “Jamani
Joshua wangu! Kwa hiyo tutakaa hapo mpaka lini ndio tunasafiri?” “Mimi
nilikuomba usiku mmoja tu, Naya. Angalau safari yetu ya ndoa ianzie kwenye
chumba chetu, kitanda chetu, ndipo tusafiri, twende mapumzikoni kwengine.”
“Basi na wewe ujiandae kupata usiku mtulivu. Ni mimi na wewe tu. Bila...” Naya
akiwa amesimama kwenye mataa, akisubiria taa zimruhusu huku akizungumza na
Joshua asubuhi hiyo, akashangaa Malon anamgongea kioo cha dirisha ya gari.
“Malon!” “Bila
Malon!?” Joshua upande wa pili wa simu akawa hajaelewa usiku huo
mtulivu anaoahidiwa na Naya bila Malon, anahusika vipi tena! “Hapana
Joshua. Malon kwenye kioo cha dirisha langu, asubuhi hii! Weka mute huko kwako
asikusikie, mimi namfungulia mlango nimsikilize.” “Naya!” Joshua
akaita. “Tafadhali weka mute Joshua. Weka tu, niamini. Ili tumsikie.” Kwa
kuwa walikuwa wakizungumza kutumia spika za gari hiyo ya kisasa ya Naya, Naya
akajifanya kama amemaliza mazungumzo, akarudisha simu kwenye pochi kama
kumuonyesha Malon ambaye bado alikuwa akimtizama nje ya dirisha la upande wa
abiria, akitaka amfungulie mlango, kuwa amemalizana na mtu aliye kuwa
akizungumza naye. Kumbe bado Joshua alikuwa hewani ameweka mute kama
alivyoombwa na Naya.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya
akatoa loki ya mlango, akaingia. “Naona jamaa yako anahangika kweli kukuharibu
akili. Anahakikisha anakupa mavitu ya bei nyingi, ili ujisahau kama wewe
unajukumu la familia.” “Na naona kwenye hilo amefaulu. Kwa nini unanivizia
mabarabarani Malon!? Nikusaidie nini?” “Mimi siye ninayetaka msaada wako Naya,
ni Bale. Unamuacha Bale anateseka hivihivi?” “Ndiyo.” Naya akamjibu,
taa zikaruhusu. “Kweli Naya?! Umepatwa nini wewe?” “Haya ni mapenzi Malon, na
msimamo kwenye malengo. Naolewa na Joshua. Tena leo. Ni baba peke yake ndio
angesimamisha hii harusi, pengine na Joshua kama atabadili mawazo. Lakini mpaka
sasa hivi tunavyoongea hapa, Joshua wangu anajiandaa kwa ajili yangu, na baba
Naya anajiandaa kunitoa kwa baraka zote, RASIMI mbele za watu na Mungu,
kunikabidhisha kwa Joshua. Upende, usipende. Umuadhibu Bale kwa hili au sisi
kwa kutuficha Bale alipo, jua, leo nakwenda kulala kitandani kwa
Joshua.”
“Acha
kuniumiza kwa makusudi Naya!” “Pole sana, ila sina jinsi ya kukusaidia.
Tafadhali acha kunivizia mabarabarani Malon.” “Umeamua kumtupa Bale kabisa
sababu ya Joshua?” “Mimi na wewe wote, hata Bale anajua, Joshua si
tatizo. Yeye mwenyewe na haraka zake, na ubishi yupo huko alipo. Na japokuwa
unajitahidi sana kuwachonganisha Bale na Joshua, lakini Malon, Joshua wangu
hajali. Hapa tunavyozungumza pesa yake inatumika kumsaka Bale huko Mbeya.
Askari wawili wapo huko wakilipwa na Joshua kumsaka Bale.”
“Hawawezi
kumpata Bale kwenye ule mji. Mimi nishatengeneza marafiki pale, najuana na
watu, na wakubwa wa polisi mpaka magereza. Chochote kinachoendelea pale
naambiwa. Wewe hushangai nimejuaje kama Bale amefungwa na hao askari wenu
wanamuulizia kama mmoja wa wafanyakazi wangu?” “Mimi sijui Malon, na
hayanihusu.” “Basi jua Bale hawezi kapatikana bila idhini yangu.” Naya
akashituka sana. Akaanza kutafuta sehemu aegeshe gari. Akamwangalia akiwa
amekunja uso kisha akarudisha macho barabarani.
“Wewe
hushangai kwa mji kama ule mpaka leo askari wawili wameshindwa kupata fununu za
mtu kama Bale, ila mimi nimejulishwa kila kitu?” “Unamaanisha nini Malon?” Naya
akaegesha gari. “Namaanisha hamuwezi kumpata Bale bila mimi.” “Kwa kuwa
wewe ni nani na unahusika vipi?” “Najua wewe ni mbishi Naya. Ila jiulize tu,
kwa nini mpaka leo wameshindwa kujua alipo Bale?” Naya akatulia akifikiria.
“Watu wanaishi kwa akili.” “Ukimaanisha wewe? Kwamba unaishi kwa akili kwa
kumfungia Bale?” “Hata ukinidharau, lakini ndio ujue hamtampata Bale.”
“Sasa
labda mimi nikuulize Joshua.” “Mimi sio Joshua, ni Malon. Acha dharau Naya,
kujifanya gafla umenisahau mimi sababu ya mpuuzi uliyekutana naye jana tu! Hivi
nyinyi watu mnakumbuka nilipowatoa kweli au mmesahau kabisa sababu ya huyu
mpuuzi.” “Naona umeamua kurudia na yale matusi yako. Wokovu tena basi?”
“Hayakuhusu Naya.” “Huyo mpuuzi anayekuumiza kichwa, anakuwa mume wangu Malon.
Iwe kwa kupenda kwako au la. Vyovyote unavyomtambua wewe, Joshua ananioa Malon,
sibadiliki. Halafu hakuna aliyesahau wema wako ila...” “Ila nini Naya?
Ila nini? Baba yako ananifukuza mimi sababu ya Joshua! Hakika nitawakumbusha
mimi ni nani?” “Kwa kumficha Bale?!” Naya akamuuliza kwa mshangao sana.
“Kwamba
unamuadhibu Bale kwa sababu ya mimi kuolewa na Joshua?” “Na kukukumbusha
ulipotoka Naya. Bila mimi usingekutana na Joshua. Pesa yangu ndio
iliyokusomesha, na kukupa ajira. Narudia tena, bila mimi usingekutana
hata na huyo Joshua.” “Kwani wewe ulinikuta barabarani?! Eti Malon? Maana
ulinikuta nikisoma. Japo baba yangu alikuwa akikopakopa na kunyanyaswa
akizalilishwa, lakini alihakikisha nipo shuleni. Na shule yangu haijawahi
kusubiri. Baba alihakikisha nasoma bila ya kusimama. Tafadhali usije sahau hilo.
Sikuwahi kufukuzwa shule sababu ya ada, eti wewe ndio ukanirudisha shule!”
“Unasahau vipi Naya wewe! Unasahau vipi hali niliyokukuta nayo?” “Ilikuwa
mbaya, wala sitasahau, lakini sikuwahi kushindwa kusoma, wala
baba yangu hakuwahi kushindwa kunisomesha. Mimi sijui ulikuwa
ukizungumza nini na Bale. Sijui alikwambia nini, lakini Joshua.” “Mimi ni
Malon. Acha..” “Unajua namaanisha wewe.” “Gafla unajidai hunijui Naya wewe!?
Hakika mtanikumbuka, mtanitafuta na mtanisihi.” Naya
akashangaa sana.
“Mbona
unataka kuanzisha vita na mimi bila sababu Malo!? Ni nini nimekukosea wewe?”
“Kunililia ukiwa na shida, na kunikimbia baada ya kufanikiwa.
Hilo nitakulipa Naya. Nakuonya achana na Joshua, rudisha akili zako kule
zilipokuwa. Sisi tulikuwa na malengo makubwa sana, mpaka majina ya watoto
tulikuwa nayo! Leo unakwenda kujiingiza kwa mwanaume mwingine tena kwa
kunitamkia wazi kuwa eti unakwenda kulala kwake! Hakika nakuonya
Naya.” Naya alibaki na mshangao lakini hofu ikaanza kumuingia.
“Labda
nikuulize Malon. Hivi wewe ulitegemea nini kutoka kwangu kwa maisha yale?”
“Kipi kigeni ambacho nilikianzisha na kushindwa kuendelea na mahusiano yetu
Naya, kama sio ulikuwa ukinitumia tu?” “Malon! Umerudia bangi wewe?” “Wewe
ulitaka niache wanawake, niokoke, nitulie na wewe. Nimefanya hayo yote.
Nimehangaika, eti leo anatokea mwanaume mwingine baki tu, ndio unaniacha
hivihivi! Hakika sikubali Naya. Nguvu ileile uliyotumia kuwa na mimi
ukijidai unanivumilia kumbe ili utumie pesa yangu, ndio nguvu hiyohiyo uitumie
kujirudi kwangu na tuendeleze familia yetu. Usinifanye mimi mjinga na
mtoto.” Joshua naye alikuwa akisikiliza.
“Mimi
nilijitoa sana kwako. Nimekupeleka mpaka kwa mama yangu. Ukawafahamu ndugu
zangu, ukajidai mkwe, eti leo ndio unanikimbia! Hakika sitakuruhusu
Naya. Mimi sio mjinga. Nishaona wasichana kama nyinyi wengi tu. Mnasaidiwa
mpaka mnakuwa watu, kisha mnajidai kuwakimbia wanaume ambao wamewasaidia!
Hakika sio mimi. Mimi sijinyongi wala sili sumu, lakini nitahakikisha
unakumbuka nilipokutoa Naya.” “Malon, nahisi wewe bangi zimeanza kukuharibu
kichwa mpaka unasahau unazungumza na nani!”
“Najua
sana nazungumza na wewe?” “Sidhani Malon, na umekusudia kujiumiza na kunipa
shutuma bila sababu, na hakika siumii Malon. Kama lengo lako ni kunishutumu
uniumize, hakika sijali. Nilikufanyia yote. Nilikutaka ukiwa na pesa, na
ulipokuwa huna pesa. Na nilikuomba utulie, hata kama hujasoma, mimi
ningekutunza. Sikukwambia hivyo mimi ila ukaishia kunikataa na kunisukumia kwa
wanaume wengine ukiamini sitapata mwanaume kama wewe? Hukutegemea mimi kama
naweza kupata mwanaume kama Joshua, ndio maana ukajiamini kuniacha kila wakati
na kurudi vile utakavyo. Sasa hivi umeona nimekomesha huo mchezo wako, ndio
unajidai kunitisha!?” Naya na yeye akambadilikia.
“Sasa na
mimi nakwambia Malon, hunitishi.” “Huijui jela Naya. Hujui anachofanyiwa
kaka yako.” “Hakika sijali Malon.” “Kweli wewe katili Naya na sikutegemea!
Yaani upo radhi ukalalwe na Joshua tu, halafu kaka yako, damu yako, aendelee
kuteseka!” “Kama nimekuelewa sawasawa ni kuwa sharti la kutupa fununu za
Bale,..” “Sio fununu, ni kumuweka huru.” Malon akamsahihisha. “Sawa. Kwa mimi
kuachana na Joshua, si ndiyo?” “Yaani hii harusi ya leo isifungwe. Achana na
Joshua, tuendelee.” Naya akacheka sana.
“Wewe ni
katili Naya! Hakika sikukujua hivyo.” “Wewe nilikutoa jela Malon, bila msaada
wako. Tutampata Bale, na tutamtoa jela. Naomba shuka kwenye gari langu. Usinitishe
wala kuniwekea hukumu. Sijakutenda lililo baya, wala sikuwa na mpango wa
mwanaume mwingine ila wewe tu. Wakati wote nilijua leo ndio ingekuwa siku yetu.
Lakini uliishia kutothamini, ukinidharau. Amini unachoamini ili kujiridhisha,
lakini kwako sitarudi Malon. Niite jina lolote litakalokufurahisha wewe,
lakini kwako sirudi. Na nakushauri safari hii acha bangi kwa ajili yako mwenyewe
si yangu, maana kwa jinsi nikikuangalia sasa hivi, umemrudisha yuleyule Malon
aliyekuwa akiniliza mchana na usiku. Na mwisho wako sio mzuri Malon. Uliyatoa
mapepo, ukayaumiza. Unayakaribisha sasa hivi kwa hasira ambayo ni uongo
kabisa hata wewe unajua. Hali yako ya sasa hivi itakuwa mbaya kuliko ile ya
mwanzoni. Rudi kwa Yesu, Malon.”
“Acha
kunizungusha kwa maneno mengi, Naya. Nakuonya. Hakika nakuonya.”
“Utanifanya nini Malon wewe? Kwa kutuficha Bale alipo?!” “Naya! Wewe unanijua
vizuri sana. Nakuonya.” “Labda sasa hivi nitambulishe nazungumza na Malon yupi!
Yule wa Morogoro, au huyu wa Dar aliyekiri wokovu au...” “Malon aliyejeruhiwa
moyo na asiyekubali kushindwa.” “Haya shuka kwenye gari yangu haraka Malon.
Naona umeshapandisha hasira, mikono inakutetemeka, utaishia kufanya fujo hapa
na unanichelewesha naenda saluni.”
“Naya!” “Naolewa na Joshua, Malon. Hilo
ulikubali au ulikatae, jua nafsi yangu, akili na hiari yangu vimemchangua
Joshua, na ndie mume wangu. Wewe nimemalizana na wewe Malon.” “Utarudi tu.”
“Kwa namna yeyote unayopanga kunirudisha kwako, jua nampenda Joshua, na ndiye
atakayepata kiapo changu cha hiari na dhati kuwa nitasimama naye mpaka kifo.”
“Na
kuhusu Bale?” “Hayakuhusu tena. Shuka.” “Nyinyi familia ya ajabu kweli hata
naanza kuona Bale yupo sahihi. Mnakwenda kushangilia, mwenzenu yupo
matatizoni?” “Hata yeye ningemshauri aoe kama mimi nipo sehemu ambayo wanajua
kwa wakati huo hawezi kunisaidia. Bale hajasahaulika. Anatafutwa na mimi
naolewa. Ondoka Malon.” “Utakuja kujuta Naya, na hakika sitakuhurumia.” “Kwa
sasa sihitaji huruma yako Malon. Nilishaiomba hiyo huruma na kuililia zaidi ya
miaka mitano, ukashindwa kunipa kwa sababu hukuwahi kuwa nayo.” Simu ya Naya
ikaanza kuita kwenye pochi na mlio kusikika kwenye gari. Malon akaangalia.
“Natafutwa
Malon, naomba shuka.” “Utanifanya nini? Sishuki.” Malon akagoma kushuka
kabisa, simu ya Naya ikaendelea kuita. “Nilikuwa dereva wako kwa zaidi ya miaka
5, nakuzungusha kwenye gari yangu, sasa hivi ndio unajidai kunifukuza! Sitoki
sasa.” Malon akapiga ngumi ya nguvu kwenye gari ya Naya ila upande wa
dashboard/pale mbele. Hofu ikamuingia Naya akiogopa asije akampiga maana Malon
alikuwa mwepesi sana wa kupiga. Alijua anayo bangi tayari. Hayupo sawa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Bado masaa machache harusi ya Naya ifungwe. Malon yupo garini amegoma kushuka na vitisho vingi tu. Nini kitaendelea na Malon amesema hakubali kushindwa!!?? Simu ya Naya ikakata na kuanza kuita tena. Naya akabonyeza sehemu ya kupokelea simu kwa haraka. “Bibi harusi wangu unachelewa bwana! Mimi nimemuahidi Joshua kumpelekea mke nyumbani kwake mapema. Mbona unaniangusha?” “Malon yupo kwenye gari yangu, anafanya fujo Nanaa. Naogopa, mwambie Joshua atakuwa ananiona nilipo.” Hapo hapo Nanaa akampigia simu Joshua. Joshua akapokea. “Mumeo yupo sekunde chache sana afike hapo. Nilishamtafuta, na mimi nina kuja nipo njiani.” Nanaa akaogopa akajua kumbe hali imeshakuwa mbaya.
Naya
akabaki akitetemeka anamwangalia Malon akataka kushuka yeye akimbie, Malon
akamgundua. “Ukishuka tu hapo, nakuitia mwizi. Watoto wa mjini wakupige mpaka
wakuue.” Kioo cha Naya kikagongwa. Akageuka kwa haraka. “Geb!” Naya akataka
kushuka kwa haraka, Malon akamrudisha ndani kwa nguvu kwa kumvuta gauni
aliyokuwa amevaa.
“Acha
kujidai mwehu, Naya.” Akaloki milango yote. Geb akaona. Akajaribu kufungua kwa
nje mlango haukufunguka. Bado alikuwa kwenye simu na Joshua. “Yupo naye
ndani, ameloki milango kwa ndani na anamzuia Naya kutoka. Nipo nikifikiria kitu
chakufanya.” “Naya anahali gani?” Joshua akauliza
akiendelea kukanyaga mafuta kwani na yeye alishatoka nyumbani tokea Malon
anaingia kwenye gari ya Naya, kama aliyekwisha kuingiwa na wasiwasi kuwa, Malon
amejuaje Naya alipo asubuhi hiyo na mapema mpaka kuweza kumpata barabarani!
Alipoanza kusikia ukorofi wa Malon kwenye simu, ndipo akamtumia ujumbe Geb kwa
haraka na eneo analomuona Naya yupo. Geb alikuwa kwenye ofisi zake, jengo la
Magesa hapohapo Ubungo akisubiria muda aelekee nyumbani kwa Joshua tayari kwa
harusi. Yeye na watoto wa kiume walishakatwa nywele, na wenyewe walikuwa
wakisubiria muda waende nyumbani kwa Joshua ambako wangevaa hukohuko shuguli
ianze.
Ndani ya
dakika tano, Naya akiwa garini na Malon anamzuia kushuka, Geb amesimama nje ya
mlango wa Naya akijaribu kumwambia Malon ashuke wazungumze, Joshua alifika hapo
bila hata salamu, akagonga kioo cha dirisha la upande wa abiria wa mbele,
alipokuwa amekaa Malon, akagonga na jiwe kwa nguvu sana kama mara mbili tu,
kioo kikapasuka vibaya sana. Kabla taarifa hazijakwenda kichwani, akamvuta
Malon kwa kupitia dirishani kwa nguvu. Kukaanza kuvutana. Malon anatoa damu,
Joshua anatoa damu mikononi wanakovutana na Malon.
Naya
akafungua mlango kwa haraka na kukimbilia nje, na Joshua na yeye kwa kutumia
mkono mmoja akafungua mlango kwa nguvu, Malon akajivuta kwa haraka na yeye
akatoka nje akimfuata Joshua. Kwa asili Malon ni mjenga misuli, mpenda ngumi.
Alichokua akifanya Joshua ni kumkwepa na kumrushia ngumi. Geb akakimbia na
kwenda kuwaamulia pamoja na mtu mwingine aliyekuwa karibu.
“Sasa
nyinyi si mnajidai wajanja kwa kuwa mnayo pesa? Mimi nitawaonyesha kama mimi ni
mtoto wa mjini. Hata mtoe mamilioni ya pesa kiasi gani, hamtakaa mkampata
Bale.” “Tafadhali naomba nisaidie kurudisha gari ya Naya.” Joshua akamgeukia
Geb bila kumjibu Malon. “Twende Naya.” Akaenda kumvuta Naya aliyekuwa amesimama
kwa mbali kidogo.
“Hujaumia?”
Joshua akauliza kwa kujali. “Wewe ndio unatokwa na damu Joshua! Pole.” “Nipo
sawa. Twende.” Joshua akamshika mkono, wakawa wanaelekea alipokuwa ameacha gari
yake. Malon akawakimbilia. “Sikubali umchukue Naya. Wakati mimi namtunza
na kumsomesha, wewe ulikuwa wapi? Mimi nimehangaika naye, eti wewe sasahivi
ndio unakwenda kumzalisha tu, hata hujahangaika naye kama mimi!” Malon
akaendelea kuongea akiwa mbele ya Joshua. Alikuwa amebadilika Malon, anatisha
kwa hasira.
“Unadai
kiasi gani?” Joshua akamuuliza. “Naona hilo ndilo la msingi. Wewe piga mahesabu
yako, tujulishe ulipwe.” “Nani amewaambia mnaweza kunilipa mimi!?” Akamgeukia
na Geb aliyeongeza. “Mnaweza kunilipa muda na mapenzi niliyompa Naya, alipokuwa
akipitia kipindi kigumu? Thamani yake ni nini?” Malon akauliza.
“Sina shida
na pesa zenu. Sikuwekeza kwa Naya na familia yake ili waje wanilipe pesa! Naya
ni mwanamke wangu, na tulikuwa sawa tu mpaka wewe ulipotokea. Matatizo
kwenye wapenzi ni jambo la kawaida. Huwezi ukatokea tu eti na kumchukua
akidhani malipo ni pesa! Nendeni kanunue malaya kibao huko mjini muoe. Acheni
upuuzi na dharau.” Akataka kumsogelea Naya, Naya akakimbia kwa haraka mpaka
kwenye gari la Joshua na kujifungia.
“Hawezi
kujificha mjini. Nitamkamata tu. Asijidai sasa hivi mjanja. Alipokuwa na shida
zake hakuwahi hata kuthubutu kuniacha. Muulizeni huyo. Hata alipokuwa
akinifumania na wanawake, uchi kabisa, mbona alikuwa anarudi mwenyewe bila
kumtafuta? Eti sasa hivi namwambia nimetulia na nimeokoka ndio ananiacha kama
sio alikuwa akinitumia tu? Sasa kamwambie Naya, nitamkamata tu.”
“Acha
kumtisha Naya. Utamfanya nini?” “Atakuja kusimulia nitakapo mkamata.
Labda ahame dunia.” “Na ujue nakwenda kukushitaki. Nitaripoti vitisho vyote
ulivyovitamka hapa.” “Nenda kasemelee polisi. Nani amekwambia mimi natishwa na
polisi? Wewe unaijua polisi mapokezi, mimi najua mpaka ndani, kwa kuishi tokea
mtoto. Uliza utaambiwa. Mimi polisi ndio maeneo yangu ya matembezi. Acha upumbavu
wewe.” Malon akaondoka, Joshua akarudi kwenye gari na kuondoka. Walishajaza
watu hapo. Geb naye akaita mtu ili aje achukue gari ya Naya. Akabaki amesimama
akisubiria.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Naya
alikuwa ametulia garini kwa mshituko, asiamini kama Malon amemgeuka kwa kiasi
hicho! Kutoka kwenye kumbembeleza mpaka kumdai! Akapoa kama amemwagiwa maji. Hata
hakuweza kujigeuza hapo kitini, wala kuuliza wanapokwenda. Wote kimya, Joshua
akiendesha gari. Simu ya Joshua ikaanza kuita. Akaitizama, alikuwa Geb,
akapokea. “Naya ameacha simu kwenye pochi yake hapa, inaita. Nanaa ameniambia
ni yeye ndiye anayempigia, anasubiriwa saluni.” “Hapana Geb. Inavyoelekea Malon
anamfuatilia Naya. Siwezi kumpeleka popote isipokuwa nyumbani ambako nina
uhakika atakuwa salama. Hatatoka hapo leo wala kesho. Kama wanaweza kumfuata
hapa wamtengeneze sawa, ikishindikana basi. Mwambie Nanaa wao wakimaliza,
wamfuate hapa. Atakuwa sawa tu.” “Kama nimekuelewa vizuri ni kwamba maswala ya
saluni kwa Naya tena basi.” Geb akataka uhakika ili arudishe majibu ya
kueleweka kwa mkewe anayemsubiria bibi harusi huyo saluni.
“Kabisa.
Tafadhali naomba mwambie Nanaa namshukuru, lakini Naya atakuwa sawa tu. Amjie
na nguo zake, basi itoshe. Ila kama wakipata mtu wa saluni atakayeweza kuja nao
hapa akamsaidia Naya, pia ni sawa. Nitalipia hata na ya usumbufu. Ikishindikana
basi, Geb. Leo lazima nimuoe Naya. Sijali atakavyoonekana, ilimradi awe yeye,
basi.” “Hata mimi nakubaliana na hilo. Tusije kujilaumu.” “Nashukuru Geb.”
“Unahitaji kitu chochote sasa hivi?” “Naomba kama masaa mawili kuanzia sasa ili
kuweza kujiweka sawa, mimi na Naya. Atulie kabisa, turudishe mawazo kwenye
harusi. Hii siku isipoteze lengo.” Geb akaelewa ndio
anaambiwa waachwe kabisa hata hayo mazungumzo yaishie hapo.
“Basi
nitawacheki baada ya masaa mawili kuanzia sasa. Na Nanaa pia nitamwambia
hivyohivyo. Ila nawasihi mtulie. Msiogope kabisa. Swala la ulinzi hapo lipo
vizuri. Hilo nimehakikisha na nitampigia simu Gamba kuzungumza naye tena juu ya
hiki alichozungumza Malon. Tujue anamaanisha nini anaposema hata tufanye nini
hatutaweza kumpata Bale!” “Sijui Geb, lakini mimi kuna kitu nahisi hakipo sawa.
Haiwezekani kwa askari wawili, wazoefu, na kwa magereza machache hivyo awe Bale
anashindwa kupatikana!” “Unahisi nini?” “Siwezi kusema moja kwa moja, ila
nataka tu kukwambia kuwa, kuna kitu hakipo sawa na yeye Malon ndiye anayejua.
Na kama ulivyomsikia leo, ili asaidie ni Naya amrudie. Sasa sijui! Wazo la
kuzungumza na Gamba naunga mkono. Naomba unijulishe.” “Sawasawa. Naya
ananisikia?” Geb akauliza. Joshua akamgeukia Naya aliyekuwa ametulia
sana.
“Upo Naya?” “Anakusikiliza.” Joshua
akamjibia. “Najua upo kwenye mshituko na yote aliyoyafanya na
kuzungumza Malon. Naomba nitoe tu ushauri, tusubiri kwanza kumshirikisha baba
Naya, iwe ni mpaka tumejua nini chakufanya, ili tusimuongezee wasiwasi usio na
jibu. Na ashirikishwe endapo tu Naya unabadili mawazo juu ya harusi.” “Mimi
naolewa na Joshua. Leo. Mengine nitajua mbele ya safari.” Akajibu
Naya.
“Basi
naomba tujipange kabla hatujaongeza sintofahamu kwa baba. Ameruhusiwa kwa
masharti ya mapumziko ya siku mbili mfululizo. Nashauri ibakie hivyo. Atulie
kabisa wakati sisi tukijipanga.” “Hata fujo alizofanya Malon hapa
nisimwambie!?” “Hapana Naya.” Joshua na Geb wakajibu kwa pamoja. “Hana
atakachofanya au kusaidia kwa sasa. Fujo zimeshatokea, ameondoka. Leo nashauri
kama alivyosema Geb, tuache iishe hivyo. Haina sababu. Mzee bado hayupo
sawa.” “Sawa. Maana hata leo asubuhi alikuwa akisema anaomba muujiza wa
Bale atokee hata asubuhi hiyo. Kwa hiyo basi acha tu nimuache.” Naya
mwenyewe akaafiki.
“Wazo zuri.
Acha niwaache mkatulie. Ila si tumekubaliana harusi bado ipo? Eti Naya?” Geb
akaweka msisitizo wa swali kwa Naya kama ambaye anamjua Joshua vyakutosha na
maamuzi yake. “Ipo Geb. Lakini!” Akajibu Naya na kuwatia wasiwasi
kidogo. Joshua akamgeukia akiendelea kuendesha akielekea nyumbani kwake Goba
akitokea Ubungo.
“Nini
tena!?” Joshua akauliza kwa wasiwasi kidogo. “Nataka tu
kusema mimi nampenda Joshua kwa dhati. Sijampendea pesa wala sijamuuacha Malon
kwa sababu ya tamaa kwa Joshua. Mungu wangu nishahidi jamani. Mimi sijamkimbia
Malon baada ya kunisaidia sana. Sikuwa nikimtumia hata yeye Malon anajua kuwa
anadanganya na amekusudia kuniharibia tu kwa Joshua. Nakupenda
Joshua. Na Malon nilikuwa nikimvumilia tu si ili kunufaika naye, ni kwa
kuwa mimi nilijua kila mahusiano yapo na matatizo yake, nikawa nikivumilia. Ila
ni kweli hakuwa akijua kujirudi, mimi ndiye niliyekuwa nikijirudi hata kama
yeye ndiye aliyekosa. Pengine hilo ndilo kosa langu. Ila mimi sina tabia za
tamaa. Na Mungu wangu ni shahidi.” Naya akaendelea akisikika
kujitetea kwa hofu.
“Hata kama
leo Joshua akifukuzwa kazi na kupoteza kila kitu, mimi nitamtunza Joshua wangu
bila shida. Hata kama kwa kurudi kuanza kuishi naye kwa baba Naya wakati
tukijipanga upya.” Mpaka Joshua mwenyewe akacheka kama Geb. “Kweli
Joshua. Hakika sitakukimbia mimi. Hata uugue sasa hivi au uwe mlemavu wa
kitandani tu huwezi hata kugeuka, ujue mimi nitabaki na wewe mpaka wewe
mwenyewe uniache.” “Nashukuru Naya. Na naomba usilie. Achana na mambo ya
Malon.” Joshua akaendelea.
“Ni jana
usiku tu, Geb alinipigia baada ya kuachana pale na kunitahadharisha na maneno
anayosema huyu Malon. Akanionya niwe nayo makini sana. Haswa kipindi hiki
anachofanya juhudi zote kukurudisha kwake. Anaweza kuongea chochote ili tu
kumwaga sumu ya chuki na hata kama ni kweli Bale alisema, mtu mwenye hekima,
asingeweza kuzungumza. Angenyamazia tu. Anaongea waziwazi kusudi tu kutuvuruga.
Usijali juu ya maneno ya Malon.” “Na pia si yakupuuza Joshua.” Akaongeza
Geb na kuendelea.
“Katika
kuropoka kwake akiwa na hasira amezungumza maneno mengi ambayo inabidi
tukitulia na mambo ya harusi yakiisha, kama bado Bale hajapatikana, lazima
kutafakari zaidi kujua jinsi ya kuendelea kuanzia hapo.” “Sawa Geb. Lakini
lazima leo tufunge ndoa.” “Hilo limekaa sawa kaka. Tutakuja na watoto kama
tulivyopanga na nitamwambia na Nanaa afanye hivyohivyo. Hata yeye walimpambia
hotelini tu, chumbani kwake. Kwa hiyo nafikiri ni kitu kinachowezekana.” Wakakata
simu baada ya kukubaliana. Joshua akaendelea kukanyaga mafuta. Wote kimya kila
mmoja akiwaza lake.
Nyumbani Kwa Joshua.
Kukawa
kimya mpaka alipofika nyumbani kwake mlinzi akamfungulia geti wote wakiwa
kimya. Joshua akavuta gari mpaka karibu na mlango, akashuka na
kwenda kumfungulia Naya mlango na kwa kuwa Naya alishazoea kufunguliwa mlango,
akasubiria kitini. Akamfungulia. Lakini kabla hajashuka, akageuka na kuanza.
“Nakupenda Joshua. Nakupenda sana mpenzi wangu. Naomba Malon hata asikuharibu
akili. Mimi sikupendei pesa na sikutumii. Nakupenda na ninakuhitaji. Naomba
usiniache sababu yake kwa kuwa hata ukiniacha wewe, ujue hatanioa. Shida
yake ni asinione mimi na mtu wa maana kama wewe. Alipokuwa akirudi na kunikuta
na wanaume wa ajabu, hakuwahi kulalamika ila kufurahia kuwa utabiri wake
umetimia. Sasa, sasahivi amenikuta na wewe, ndio anahangaika.” Naya akaendelea
kujitetea akibembeleza.
“Haya
yote aliyoyasema leo, ujue ni njia tu ya kuniharibia kwako baada ya kukuona upo
na msimamo, na huna mpango wa kuniacha ndio maana amekuja kwa nguvu zote, maana
hajawahi kuyasema haya hata mara moja na kwa mwanaume mwingine yeyote. Naomba
uniamin...” “Achana na Malon. Naona anataka kukuharibu wewe akili.
Usimfuatishe. Atakuharibia siku yako ya leo, naomba tulia. Mimi
nimeshamuelewa ndio maana unaona hata sishindani naye kwa maneno wala ngumi.
Najua ni mfa maji, hataacha kutapatapa. Ila kama nilivyokwambia, kukusikia
hivi, kunazidi kunitia moyo.”
“Na kama
nilivyosema, nahisi kuna kitu hakijakaa sawa Naya. Sitaki kusema moja
kwa moja nisije nikaweka mawazo yasiyo sahihi kwenye mioyo ya watu kwa haraka,
nakufanya wote tufikiri kama ninavyofikiri mimi halafu ikawa sio sahihi
tukashindwa kupata mawazo tofautitofauti yakutusaidia. Ndio maana nakuwa kimya
kila anapozungumza ili kumsikia yeye zaidi. Najua katika zungumza yake ya jazba
naweza kuokoteza neno moja.” Naya akakaa akakunja uso.
“Sasa
kama leo umeokota nini!?” “Acha niweke yote kwa pamoja.” “Kwa hiyo bado
unanipenda?” Naya akauliza na tabasamu la penzi. “Ngoja nifikirie.” Naya
akacheka sana. “Vile ulivyoniokoa kama ninja!” Joshua akacheka mpaka akainama.
“Mimi nikajua ungepigana leo!” “Aniharibu muonekano wangu wakati leo nataka
niweke kumbukumbu ya mpaka vitukuu!!” Naya alicheka sana. “Kwa hiyo hutaki
ngumi!” “Mikono hii ya kalamu, mama Kumu! Najua mipaka yangu.” “Bora mpenzi
wangu. Ila nakwambia ukweli kabisa, hivyo unavyomnyamazia ndio ujue unampandisha
hasira.” “Nimemuona! Ndio maana anaropoka sana! Hajui mimi sitishwi hovyo.”
Akajisifu Joshua na kumshika mkono Naya kama anayetaka kumshusha.
“Mkono
unatoa damu Joshua. Twende nikakusafishe mpenzi wangu.” “Joshua Kumu
anavyopendwa!” “Nakuhitajiwa pia.” Joshua akacheka sana wakiingia ndani.
Walichofanya ni kusafisha mkono na kuhamia kochini, kukaanza kubembelezana na
mabusu ya kina. Nanaa na timu yake wanaingia hapo, hawakuamini. “Mimi nilijua
hali ni mbaya, tunakaribia kuahirisha harusi!” Nanaa aliingia bila hata hodi,
akiwa na mizigo pamoja na mtu mmoja tu. “Bwana harusi wangu yupo tayari
kunioa. Harusi ipo.” Wakaendelea na yao yakiwa yamebakia tu masaa
machache ndoa yao ifungwe.
Kisasi.
Huku kwa
Malon alijawa hasira, na ndipo alipoamua kuendelea na mipango yake ya kikatili.
Alikwenda kwa Naya akiwa anampa nafasi ya mwisho kabisa. Alijiambia anakwenda
kuzungumza naye kwa mara ya mwisho kuona kama anaweza kumbadilisha mawazo. Moyo
wa Malon ulibadilika kabisa na kuanza chuki ya ajabu kwa familia hiyo baada ya
mazungumzo yake ya mwisho na baba Naya usiku uliopita.
Wakati
Joshua akisikiliza mazungumzo ya Malon na Naya garini na kuyarikodi kwa
uthibitisho endapo chochote kikitokea, kumbe Malon naye aliingia garini akiwa
anarikodi na yeye mazungumzo yake na Naya kwa kutumia simu yake kama
alivyofanya siku iliyopita. Alianza kurikodi tokea anakwenda nyumbani kwa
Joshua akiwataka ndugu wa Naya wazungumze pembeni na kukataa kumsikiliza na
kwenda tena nyumbani kwao akitaka wazungumze, wakahitimisha na baba Naya kwa
kumuaga rasmi kama anayemtoa kwenye familia yake. Malon alikuwa na mazungumzo
yote hayo kwenye simu yake.
“Si
wanajidai wajuaji na wamesoma! Sasa acha niwaingize shule ya mtaani
niliyohitimu mimi.” Akaadhimia Malon. “Wanajidai wanavijihela hapa
mjini, sasa acha niwaonyeshe na mimi pesa ninayo, sihitaji chechi zao ila
kuwatia adabu wasiwe wanachukua wake za watu huku wakiwarubuni kwa mali.
Wapuuzi wakubwa.” Malon akazidi kujipandisha hasira. Alichofanya akiwa
na hasira, ni kutoa hiyo simu mara alipofika nyumbani kwake na kuanza kupakuwa
mazungumzo ya siku hiyo yote kwenye kompyuta yake kama alivyokwisha pakua ya
siku iliyopita.
Akaanza
kuyatengeneza yale mazungumzo ya kwenye kompyuta akiwa ameyatengenezea faili
jingine tena la kisasi. Hayo ya mara ya pili ya kisasi, akaanza kuyatengeneza
atakavyo yeye. Akikata mazungumzo mengine na kubakisha mazungumzo yanayomuhusu
Bale tu, tena majibu aliyoyataka yeye. Jinsi alivyokuwa akizungumza nao
akiwaambia anayo jinsi yakumpata Bale, anachohitaji ni hiyo familia tu
kujitenga pembeni na kusikiliza, lakini wakakataa kumtoa Joshua, wakataka na
Joshua awepo. Akaweka na ya mara ya pili alipowafuata nyumbani, baada ya kutoka
kwa Joshua. Na bado akafukuzwa bila kutaka kumzungumzia tena Bale!
Na mazungumzo yake na Naya pia asubuhi hiyo garini! Tena, akayatengeneza vizuri
akitoa mengine mengi tu, na kubakisha aliyojua yanaweza kusikika vile atakavyo
yeye, endapo akiongeza nguvu kidogo.
Kwa Bale.
Malon
alichukua hatua ya haraka sana usiku mara baada ya kupiga simu ya Bale na
kumkosa, usiku ule alipopigiwa simu na Naya akimuulizia Bale na kumwambia
asubiri atampigia kwanza Bale, akikubali awape namba yake ndipo atawarudishia
majibu na kupotea kabisa, siku tano zilizopita. Alichofanya Malon alipomkosa
Bale akawazimia simu Naya na ndugu zake, akaanza yeye kumsaka Bale. Malon mtoto
wa mjini akazipata habari za Bale kwa haraka sana. Akamtuma mmoja wa askari
ambaye walitengeneza naye mahusiano hapohapo mjini Mbeya, kwa makusudi kabisa
ili wamlinde yeye na chochote kitakachotokea. Akataka hao askari wawe upande
wake.
Walichofanya
Joshua na Geb siku nne zilizopita, yeye Malon alikifanya kwa haraka bila shida.
Aliwajua askari kwa kuishi nao akiwa amefungwa jela. Aliielewa lugha yao kwa
urahisi sana na kuweza kupanga nao mambo. Baba Naya anafika Tunduma kumsaka
mwanae, askari wa Malon alishakuwa amepata habari kamili za Bale, na uzuri
akawa Bale amerudishwa viwanja vya nyumbani, Mbeya kwenye makazi ya Malon.
Malon akatoa pesa nyingi tu kutolewa kwa Bale. Isivyo kawaida, akahakikisha na
jina lake linafutwa kabisa wala hakuonekana kama alipitishwa huko magerezani.
Baba Naya
na kina Joshua wanatua jijini Dar wakiwa wametokea Mbeya na Tunduma, hawajui
Bale alipo, kumbe Bale alihamishwa tu. Kutoka rumande, akapelekwa asipo pajua
na asio wajua. Akaambiwa akae hapo asubirie maelekezo na akaagizwa asitoke
lasivyo atarudishwa rumande ili akahukumiwe kwa makosa yake. Kwa kuwa amri hiyo
alipewa na askari hao waliomtoa, tena wenye sare kabisa, Bale akatii bila
shida. Tena akaona ni bora hapo alipohamishiwa kuliko rumande. Ikawa kama
amefungiwa tena, lakini anatoka tu nje kama kawaida, akitaka mwenyewe, bila
kulindwa, na yeye hakuwa akienda popote, na kurudi ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Malon
akaandaa ushahidi wake, akasubiri kama ataweza kuingia nyumbani kwa Joshua siku
hiyo jioni. Kama angekuwa hajafukuzwa kwa kina Naya, Kiluvya, angerudi na
kuondoka na usafiri wa ndugu, kwenye kibasi. Lakini Malon alifukuzwa mbele ya
bibi. Anarudije tena kuomba apande basi ya kwenda harusini na yeye hatakiwi!
Akatulia akiwaza mpaka ilipofika mida ya harusi hiyo kufungwa akatoka hapo ili
kwenda kujaribisha kama ataweza kuingia, lakini alishindwa kabisa. Kulikuwa na
ulinzi mkali, tena askari wageni kabisa. Hata walinzi wa Joshua mwenyewe
walikuwa wakipokea amri kutoka kwa askari hao waliokuwa wameletwa rasmi kuhakikisha
Joshua anaoa jioni hiyo.
Hakuna
magari yaliyoruhusiwa kuingia ndani ya ua. Kulikuwa na ulinzi haswa. Unaingia
kwa kadi, unaachana na gari yako nje ya geti, askari maalumu ndio wanakwenda
kukuegeshea gari yako. Jina lako lifanane na kwenye kadi. Hata ndugu ilikuwa
hivyohivyo mpaka watoto. Asiyekuwa na kadi siku hiyo hakuruhusiwa, na picha za
Malon zilikuwa getini askari wote walionyeshwa kuhakikisha haingii humo. Kwanza
watu hawakuwa wengi. Joshua asiye na ndugu ila wafanyakazi wenzake, tena
wachache tu na familia ya kina Magesa. Na ndipo wakaongezeka ndugu wa upande wa
mama Naya. Upande wa baba Naya pia walikuwepo lakini wachache, kwa hakika watu
walikuwa wachache sana.
Pakaandaliwa
vizuri, kila kitu kilipangiliwa kwa ufanisi bila mwanya wa makosa. Geb
muendesha shuguli nzima alishafikiria kila kosa na kutafutia ufumbuzi kabla ya
muda wa harusi kufika. Hapakuwa na jambo lililoendeshwa kiholela. Halafu ni
Joshua Kumu anayeoa! Pesa ipo, amekaa miaka yote akiiota hiyo siku atakayopewa
mke! Hakutaka kosa litokee. Malon alisubiri nje ya geti mbali kidogo akisubiria
kama kunaweza kupatikanika na mwaya aingie lakini hapakuwa na nafasi. Walioacha
magari yao nao walipewa namba maalumu. Wakati wakutoka, unaonyesha namba yako,
unaletewa gari yako nje ya geti, na kuondoka. Malon alipoona amebakia peke yake
pale nje, akaona aondoke kabla askari hawajamfuata.
Naya Kumu.
Naya
alipendeza haswa pamoja na wapambe wake wote mpaka watoto. Baba yake mwenyewe
ndiye aliyemkabidhisha kwa Joshua mbele ya umati na mchungaji, wakatoa viapo
vyao hapo, wakabarikiwa, Naya akawa Naya Kumu rasmi. Zikapigwa picha za kutosha
ndipo Naya na Joshua wakaenda kubadilisha nguo wakati wageni wao wanaingia
kwenye cocktail. Cocktail yenyewe iliandaliwa kwa
umaridadi wa namna yake. Viliwekwa vitoweo vya kila namna, kwa pishi lake tena
vizuri. Vikapambwa kwa kuvutia waalikwa walio bahatika kuingia harusini.
Wakaachwa waalikwa wote wakila na kunywa, na mazungumzo ya hapa na pale, wakati
kwa mara ya kwanza, maharusi hao wapya, wanapata faragha ya penzi kabla ya shuguli
nzima ya sherehe iliyoandaliwa.
![]() |
![]() |
Kitanda Cha Ndoa.
“Ndio
maandalizi yote haya!” “Hiki chumba hakijawahi kuingia mwanamke Naya. Kitanda
hiki hakijawahi kulaliwa na mtu mwingine isipokuwa mimi tu. Sijashika mwanamke,
nikafanya naye mapenzi, kwa umri wa kumzidi Zayoni. Nilikuwa nasubiria kwa hamu
mno. Haya yote nimeandaa kwa ajili yako Naya. Kukuonyesha natambua na kuhitaji
uwepo wako hapa. Nakupenda sana Naya.” “Jamani Joshua wangu! Nakushukuru na asante
kunithamini. Naamini tutakuwa na wakati mzuri wageni wakiondoka.” Naya
akamsogelea ili ambusu.
“Hiyo cockail huko,
imenigarimu zaidi, ili kufanya wageni wanisubirie angalau kwa lisaa na dakika
20, nipate na wewe muda hapa kitandani.” “Joshua!” Naya hakuamini. “Hakika
nimemwambia Geb nahitaji huu muda na wewe tu. Yaani tukitoka hapa, tunakwenda
kula nao huko chakula cha usiku, wewe ni mke wangu kabisa, nikamshukuru Mungu
kwa yote.” Joshua alishamgeza akaanza kumbusu shingoni akimfungua gauni jeupe
alilokuwa amevaa. Naya akaanza kucheka akifurahia. “Nikusaidie kutoa shela?”
“Hiyo ni kazi yangu leo. Nilikuwa nikilala hapa, nafikiria huu wakati.
Hatujasimama hapa kwa bahati mbaya, Naya.” Joshua akaanza bila papara.
Naya
ambaye alikuwa hajawahi kumvulia mwanaume mwingine ila Malon. Asiyejua mikono
ya mwanaume mwingine ila Malon. Ufanyaji wake wa mapenzi ulikuwa ukiendana na
Malon, jioni hiyo akaonjeshwa mengine kwa kituo na utuli, penzi la Joshua.
Joshua alikuwa mtulivu mno na alifanya kila kitu kwa hisia akimuuliza kama yupo
sawa, na kuhakisha Naya yupo tayari kwa kila safari anayoanzisha. Joshua
alifululiza mchezo kwa makini mno mpaka wakamaliza.
“Joshua
wewe ni mtaalamu wa mapenzi kama uliyesomea bwana!” Joshua alicheka sana.
“Kweli mapenzi ni sanaa ya ajabu! Natamani tusitoke wala kumaliza, Joshua!
Tukae tu hapa kitandani. Unishike hivihivi.” Hapo Joshua akajisikia vizuri.
“Nimefurahi kama umefurahia. Hujaumia kweli hata kidogo!?” “Aisee wewe upo
makini Joshua, mpaka umenigusa moyo wangu! Unanijali mpaka kwenye mapenzi!”
“Nywele zako zinasema tofauti Naya. Nanaa atanichukia.” Naya akajishika kwa
haraka.
“Bwana
Joshua!” “Hukuwa umeelewa nilipokwambia hali mbaya! Nilikuwa na uchu na wewe
Naya! Hiyo shingo nilikuwa nikiitizama, nameza mate nisiamini kama ipo siku
midomo yangu itafanikiwa kupita kama leo.” Naya akajifunika kwa haraka akicheka
kwa aibu. “Joshua! Kumbe ulifika mbali hivyo!” “Leo pale kwenye kochi nilikuwa
siwezi kusimama, bora alivyokuja Nanaa. Nilitamani uendelee kunilalia
vilevile.” “Nilijua, na mimi nikaanza kuzidiwa pale.” Wakacheka.
“Nakupenda
Joshua. Nakupenda sana. Naomba usije badilika. Unihitaji hivihivi.”
“Mungu atanisaidia Naya. Naamini na nimekusudia kutorudia kosa la baba yangu.
Namsihi Mungu wewe ndio uwe wa kwanza hapa ndani na wa mwisho, mpaka kifo.” “Na
mimi.” Mapenzi mengine yakaanza tena. Naya hakujali nywele wala urembo tena.
Joshua mpenda kuchezea nywele, kila wakati Naya alisikia mikono yake kichwani,
zaidi alipokuwa akinyonya midomo yake. Hodi ya mlangoni ikawatoa katikati ya penzi.
“Naya
anatakiwa kutengenezwa kidogo kabla ya tafrija.” Alikuwa Nanaa. Joshua
akaangalia saa. Zilikuwa zimebaki dakika 6. “Mbona unanipunja muda wangu
Nanaa!?” “Joshua wewe! Unakaba mpaka sekunde!?” Nanaa akalalamika nje ya
mlango. “Usiku wa leo wote wako Joshua! Nipe Naya akatengenezwe bwana. Geb
hataki kupoteza hata dakika moja ya ratiba. Mwishowe ataingia ukumbini akiwa
hayupo nadhifu.” “Basi Nanaa, anakuja. Mpe dakika 3 tu.” “Naya, naomba
usichelewe.” Akamsikia Naya akicheka ndani.
Tafrija.
Wageni
wote walikuwa wamekaa kwenye chumba hicho cha tafrija wakiwasubiria bwana na
bibi harusi hao. Mwendesha ratiba akaomba watulie ili maharusi hao waingie.
Mlio mzuri bila maneno ukaanza kusikika. Uliporudia mara ya pili, ikasikika
sauti ya Joshua kwenye kipaza sauti akiimba vizuri sana. Watu kimya
wakimtafuta, aliporudia kwa mara ya pili, Joshua akawa akiingia ukumbini na
kipaza sauti akiimba. Watu wakaanza kupiga makofi lakini MC akaomba watulie
kidogo, ndipo ikasikika sauti ya kike ikipokea. Alikuwa Naya Kumu.
Naya
aliingia akiimba kwa sauti nzuri, akipandisha na kushusha kwa ustadi sana wimbo
wa kwanza kabisa Joshua kumuimbia wakiwa botini. Watu wakashindwa kuvumilia,
wakaanza kupiga makofi wakishangilia sana. Naya aliimba kama watu wawili
tofauti. Ndipo akapokea Magesa. Akaimba kwa kujiamini na kuvutia wengi. Aliimba
bila kukosea, bibi yake akasimama kumshangilia mpaka pale mbele na kumbusu
kabisa akionekana amehamasika haswa. Joshua akampokea, akaja Naya, wakati Magesa
anamalizia, Naya na Joshua wote wakawa wamefika pale mbele alipokuwa amesimama
Magesa. Wakamsaidia kumalizia. Wakaimba wote watatu. Naya macho kwa baba yake
kila wakati akiimba mpaka machozi kwa hisia zote wakimshukuru Mungu wao, na
kuzitangaza rehema zake hapo ukumbini.
Hisia kwa
wakati huo zilizokuwa zikiendelea hapo kwa Naya, ni kutamani mambo yaishe hapo
kwa haraka, arudi kitandani na Joshua. Kila wakati alirudia kumnong’oneza
sikioni akimwambia anampenda. Joshua akajua amemtendea haki kitandani, maana hata
sauti yake sikioni ilisikika ya huba. Ukweli hata hapo kwenye tafrija Naya na
Joshua pia walipendeza sana. Wenzie kwenye kitengo chao wote walikuwepo pamoja
na viongozi wenzake Joshua. Tafrija ilikuwa fupi tu, hapakuwa na mambo mengi.
Joshua na Naya wakasimama mlangoni wakiaga watu kwa kushika mkono mmoja mmoja.
Joshua alikuwa na cheko huyo, ungejua ametulizwa. Hata usoni alionekana
ametulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mwishoni
kabisa, kama kawaida yao, wakabaki wao tu. Yaani na kina Magesa na baba Naya
wakipongezana na kumshukuru Mungu pamoja ndipo wakahitimisha siku hiyo. “Twende
nikusindikize baba Naya.” Naya akamsogelea baba yake na kumshika mkono akitaka
watoke naye, baada ya kuaga, akitaka akapumzike. Kila mtu alimuelewa, ni jana
yake tu alikuwa hospitalini amelazwa. Alikuwepo hapo akijikaza tu, lakini
ukweli alitakiwa bado awe amepumzika.
“Nashauri
Joshua ufuate nyuma. Unaweza kushangaa mke yupo Kiluvya!” Ukazidi utani hapo,
wakimtania Naya na baba yake. “Nikienda nitarudi. Nakwenda kuhakikisha ame...”
Watu wakaanza kucheka. “Jamani kwani ni vibaya!” “Basi ndoa itakushinda au
itabidi baba Naya ahamie hapa, au Joshua ahamie Kiluvya.” “Jamani mama! Si hata
Joshua alisema nitakuwa nakwenda kutembea!” “Haya naomba msindikize baba, na
Joshua anakuja kumuaga, urudi Naya. Usiniletee utani mimi. Na wewe Nanaa
kusanya vifaranga vyako, weka kwenye gari, twendeni. Naya usitoke leo hapo
getini.” “Sawa mama. Mimi namsindikiza tu baba Naya mpaka..” “Kwenye gari tu.
Zayoni atakwenda kumpikia chai, na sisi kesho tutawapelekea chakula.” “Kweli
mama?!” “Kabisa. Si anao wageni bado pale?” “Ndio maana nilikuwa na wasiwasi
nani atamsaidia!” Naya akaongea akimwangalia baba yake.
“Naomba
tuliza mawazo, Naya. Ratiba yao ya chakula yote imeandaliwa. Watakuwa
wakipelekewa chakula mchana na usiku. Zayoni atasaidiwa mambo ya dukani. Mzee
atapumzika. Nataka na nyinyi mpumzike kabisa. Usiwe na wasiwasi. Umesikia Naya
mwanangu?” “Nashukuru mama yangu. Hapo nitatulia kabisaa. Ilimradi baba Naya
anachakula! Anapata muda wa kupumzika, hapo sina neno. Na sasa hivi nakwenda
kumchukulia chakula...” “Nimekwambia maswala ya chakula niachie Naya. Mbona
hivyo!?” Wote wakaanza kucheka tena.
“Cha
usiku huu tu! Hajala vizuri. Nimeona sahani yake wakati inatolewa pale ukumbini
wakati wa sherehe. Hajala vizuri.” “Basi kazi ipo! Mimi nilijua tupo naye pale
mbele kumbe akili ipo kwa baba Naya!” Nanaa akaongeza akimshangaa bibi harusi
wake. “Baba anaumwa jamani!” “Naomba tulia Naya. Mimi mzima. Sikula sana sababu
nilikula sana pale kwenye cocktail. Nilikutana na vitoweo vyangu
ninavyovipenda, nikala kupitiliza. Tulia hapa na mwenzio.” Baba yake
akamwambia. “Basi twende nikakuge. Kesho au kesho kutwa, nasafiri mwenzio.”
Naya akamvuta mkono baba yake, wakawa wanaondoka, nakuacha wengine wakicheka.
“Ndio
unaachwa hivyo!” Mama G akamchokoza Joshua. “Subutu! Nampa dakika 5 tu, na mimi
nakwenda kumkumbusha ameolewa, na tunaaga wote, anatakiwa kurudi.” Wakaendelea
kucheka wakitaniana.
Kwa Malon&bale.
Wakati
Joshua akifaidi penzi la mkewe, Malon anaumia akiona amesalitiwa na kudhulimiwa
mwanamke wake. Hakuwa na mwingine wakumlaumu isipokuwa Naya na baba yake.
Zayoni akawa amejiingiza yeye mwenyewe kwenye orodha ya wakosaji wa Malon, kwa
kumuuliza swali mbele ya watu. Malon akahesabu kuwa, alimfedhehesha
mbele ya umati. Malon alishindwa kulala wala kutulia usiku huo kila
alipokumbuka Naya yupo na mwanaume mwingine usiku huo na si yeye tena! Kwamba
yupo mwanaume mwingine anamgusa Naya kimapenzi! Alishindwa kabisa kulala. Usiku
huohuo akakusanya vitu vyake akatoka jijini Dar, safari ya Mbeya ikaanza akiwa
amejawa hasira haswa. Aliendesha usiku huo mpaka kesho yake mchana anafika
Mbeya, bado hajachoka kwa hasira.
Akamtafuta
askari aliyemuomba amtoe Bale rumande, akampeleka alikomficha Bale aliyekuwa
amelala bado na uchovu wa kufungwa. Bale alishituka sana na kushangaa alipotoka
usingizini na kumkuta Malon ndiye anayemuamsha. “Nini kinaendelea Malon!?” “Ni
unyama na ukatili mtupu Bale! Mimi nimekuhurumia, nikaona nikusaidie tu.
Japokuwa nilikuwa na mambo mengi Dar, lakini nikashindwa kuvumilia. Nikatumia
pesa nyingi sana, kuhakikisha nakutoa jela na kukufutia makosa yako yote.”
Malon akiwa na hasira akamwambia mengi ya kumuumiza sana Bale.
Jinsi
alivyotupwa na ndugu zake. Hawamjali. Wanaendelea na maisha kama yeye
sio mmoja wao. “Naya ameolewa jana. Na sherehe kubwa kabisa. Ndugu zako ni
wakatili Bale, sijawahi ona! Nimewafuata zaidi ya mara mbili nikiwasihi
tusaidiane kukutafuta, wamekataa na bibi yako pia alikuwepo ila akanyamazia na
kukubali mambo yaendelee hivyohivyo, pamoja na wajomba zako! Eti baba yako
anasema upo jela kwa kujitakia na unalipa garama.” Malon akamsikilizisha
mazungumzo kati yake na ndugu wa Bale wakimjibu juu yake yeye Bale, yale tu
aliyotaka yeye Malon, Bale ayasikie.
Mpaka
Bale anamaliza kusikiliza, akaamini kile alichokuwa akikihisi na kumlalamikia
Naya na baba yake siku chache kabla hajaondoka nyumbani kwao kuwa kweli baba
yake amegawa nafasi yake kwa Joshua. “Kwamba wanamthamini Joshua
kuliko mimi!” “Labda kwa vile ambavyo amembadilishia mzee maisha, akapagawa.”
Malon akampandisha chuki na wivu zaidi kwa kumsimulia mapya na mageni
aliyoyakuta nyumbani kwao. Mpaka aina ya gala ambalo baba Naya
analo hapo nyumbani kwao. “Mzee amenifukuza mimi niliyekuwa
nikiwasaidia! Tena usiku! Hakika huwezi kumjua mwanadamu mpaka ashike
pesa.” Malon akaongea mengi ya uchungu na ya kuumiza. Mpaka giza linaingia, na
wao wakawa wametengeneza kundi lao.
Zikawa
kambi mbili sasa. Malon amejishindia Bale. Tena Bale akamuheshimu zaidi kwa
kumtoa jela. Akajisikia amebakiwa na Malon peke yake, na anao wajibu wakulipa
fadhila kwa ndugu huyo. Akasahau dhambi zake zote. Akabaki akimsikiliza yeye. Na
kambi ya pili sasa ni ya Joshua ambaye amejishindia mke, baba Naya, na Zayon
wakiungwa mkono na kina Magesa. Wawili hao wakapandishana morari wakikumbushana
upinzani mkali unaowakabili kutoka kwenye kambi ya kina Joshua. Joshua na Naya
wakiwa fungate wanafurahia ndoa, Malon na Bale wanajipanga kuwaonyesha
na wao ni wa muhimu na wanauwezo mkubwa. Bale anajipanga kuingia
vitani kukomoa familia yake akidhani yupo ukurasa mmoja na Malon, kumbe mwenzie
Malon anakadhalika tena yakutisha. Hawakuwa ukurasa mmoja kama
alivyosikika Malon.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Sababu ya
janga la gonjwa la corona, lililokuwa likiendelea duniani, Naya na
Joshua wakashindwa kutoka nchini kwa mapumziko yao ya fungate. Wakawepo tu
mjini Bagamoyo, kwenye moja ya hoteli kubwa na ya kisasa, wakihudumiwa. Kazi
yao ikawa kufurahia tu wakiridhishana bila kuchoka. Joshua alikuwa likizo kama
Naya. Wakaamua kutumia siku 14 fungate. Walikuwa na wakati mzuri, tulivu, wa
kwao tu wenyewe. Na simu wakakubaliana kuzima kabisa. Japokuwa walikwenda
wenyewe, lakini Geb na Nanaa walijua maharusi hao walipo.
Zilishapita
siku 7 wakiwa mapumzikoni. Naya akamuomba Joshua angalau asikie sauti ya baba
yake. Likawa sio tatizo. Wakampigia kwa pamoja, wakawa wanazungumza wote
wakiuliza hili na lile. Kwa kicheko kile, baba Naya akajua mwanae anawakati
mzuri. “Bibi alishaondoka?” “Wapo. Naona safari hii nitakuwa naye. Ameamua
kubaki anisaidie kulea.” “Baba wewe! Sasa anamlea nani hapo wakati Zayoni
ameshakuwa mkubwa anakwenda sekondari!?” “Wewe ukirudi muulize bibi yako. Ila
yupo, na amerithi chumba chako.” Naya akacheka kwa
kuguna.
“Ila
amefurahia kweli harusi yako. Kila wakati anamuita Zayoni amuonyeshe tena picha
zenu.” Naya akacheka sana. “Na hapo ndio urafiki na
Zayoni umekolea! Kila saa anamuita. Zayoni anamwambia anampendea picha tu.” Naya
na Joshua wakacheka. Mzee akasikika yupo vizuri na Naya akaelewa kuwa ndio bibi
amefika hapo nyumbani kwao. Wakazungumza kidogo ndipo wakaagana.
SUKARI YAINGIA SHUBIRI.
Siku ya
14 asubuhi waliamka wakijua ndio wanakwenda kuanza sasa rasmi maisha
ya unyumba. Maana baada ya harusi, walikaa hapo ndani, nyumbani kwa Joshua kwa
siku 4 mfululizo. Mpishi wa Joshua akifika jikoni, anapika, wakiamka wanakuta
walishapikiwa. Wao ni kula na penzi. Jumba zima wao wawili tu, wakiwa huru
kufanya mapenzi popote watakapo. Ikawa Joshua ameshatumia siku 18 za likizo,
Naya siku 20 kwa kuwa yeye aliwahi kuchukua likizo. Ukweli walipumzika
vyakutosha. Kutoka kwenye kufanya kazi mfululizo na shule, hatimae Joshua
akapata mapumziko tena safari hii akiwa na mwanamke!
Walitoka
hapo hotelini kurudi kwao mida ya mchana. Alianza
kuimba Joshua. Alisikika mwenye furaha haswa. Naya akamsaidia kuimba
kidogo. Akawa kama amekumbuka kitu. Joshua akamuona anatoa simu yake kwenye
pochi na kuiwasha. Akajua anayetaka kupigiwa ni baba Naya tu. Yeye akaendelea
kuimba wakati Naya akiweka simu yake sawa na kupiga. “Unasikika
mwenye furaha, mama!” “Nimepumzika vizuri baba yangu. Nina amani na furaha.” Naya
akaendelea kuzungumza na baba yake, Joshua na yeye akasalimia. Wakaomba
wamsalimie na bibi pia. Akasikika bibi kufurahi kweli kwamba na yeye amepewa
heshima kuzungumza na mume wa Naya. Naya akamtania hapo ndipo akaendelea
kuzungumza na baba yake pamoja na Zayoni.
Wakaagana
kwa makubaliano, jumapili baada ya ibada wote watakuwa hapo nyumbani kwa Naya
kwa chakula cha mchana. Nalo hilo bibi akalipigia vigelegele. “Joshua
mwenzio kapendwa baba.” Naya akamtania baba yake. “Mbona hilo
nalijua!” Baba Naya akajibu taratibu bila shida, na kufanya wacheke.
Wakaendelea kuzungumza kidogo kisha wakaagana.
Walifika
nyumbani kwao bado ilikuwa mapema tu, hata giza halijaingia. Lakini
walikubaliana siku hiyo ni Naya aanze kuweka vitu vyake na yeye chumbani kwa
Joshua, ili chumba kichukue sura ya chumba cha mke na mume. Mizigo yake yote
ilishaletwa kutoka Kiluvya. Ilikuwa imefungiwa kwenye chumba kingine ila chini
ya gorofa siko juu kilipokuwa chumba chao wao na vyumba ambavyo Joshua
alivitenga maalumu akisema ni vya watoto wao watakao jaliwa na mungu.
Wakati
Naya yupo kwenye hicho chumba akitizama mizigo yake, huku akichambua nguo zake
na viatu vyakupandisha juu chumbani kwao, Joshua akaingia. Hamu ikampata Naya
baada yakuona aina ya mavazi aliyovaa Joshua na rangi zake baada ya kubadili,
akataka penzi kutoka kwa mumewe akilalamika amemfanyia kusudi kumtamanisha.
Joshua naye hakutaka kusubiri. Hapohapo chumbani juu ya nguo za Naya, penzi la
haja likachezwa, Naya akigugumia kwa furaha. Likaongezeka na jingine tena,
penzi la haja lakuridhishana likatendewa haki. Wakaishia kulala hapohapo
sakafuni mpaka usiku ndio wanashituka na kugundua walilala hapo.
Baada ya
kujisafi, Joshua naye akasaidia kubeba vitu alivyochagua Naya alivyoona
vitaendana na chumba cha mumewe. Takataka alizoona hazitaendana na
mama mwenye nyumba hiyo akabakiza kwenye mabegi. Wakasaidiana kupanga
mpaka wakamaliza. Joshua akaridhika kwamba kimekuwa chumba chao, sio chake peke
yake tena. Na hapo tena penzi jingine la kukaribishwa hapo chumbani likaanza
tena. Wakamaliza, wakaanza kuongea taratibu kitandani wakibembelezana na mabusu
ya hapa na pale mpaka wakapitiwa usingizi.
Wakiwa
wamelala, wakasikia kengele inaita kama wana mgeni usiku huo. Joshua akafungua
macho na kuangalia saa. Akashangaa kidogo baada yakuangalia muda. Naya
aliyekuwa amekumbatiwa amelala kifuani akakaa baada ya kusikia kengele ikizidi
kuita. Joshua akavaa kwa haraka akatoka hapo chumbani. Naya akamsikia akishuka
ngazi kwa kukimbia kidogo.
Joshua
akasogelea mlangoni. “Ni nini?” Joshua akauliza akijua wazi ni mlinzi huku
akitaka kuchungulia kwa tundu maalumu la mlango kuona aliyepo nje akitaka
uhakika na anayemgongea usiku huo. “Geb na Nanaa.” Joshua akashituka sana
kusikia sauti ya Geb usiku huo. Akawafungulia kwa haraka. Wasiwasi ulimzidia
baada yakuona sura zao, zaidi Nanaa mwenye maneno mengi. “Naya amelala?” “Wote
tumeamka sababu yenu. Kwema!?” “Si kwema Joshua.” Geb akajibu wakaelekea
subuleni.
“Ni
nini!?” Geb akamsimulia kwa kifupi na kumshitua sana Joshua mpaka kusimama.
“Mungu wangu uko wapi!?” “Naomba tulia Joshua. Tafuta jinsi ya kumtoa Naya
hapa, tena kwa haraka.” Joshua akarudi juu akiwa anatetemeka asijue anamwambia
nini Naya.
“Ni kina
nani!?” Naya akamuwahi mumewe mara tu alipoingia. “Geb na Nanaa. Ila
wanatusubiri hapo chini, wanataka tukazungumze.” Naya kajishika moyo. “Usiku
huu! Mungu wangu, naomba isiwe ni baba Naya. Mungu nisaidie.”
Joshua akamsikia Naya akiomba akiwa amejiinamia. “Vaa tukawasikilize.” Joshua
mwenyewe alikuwa ameingiwa hofu ya ajabu. Ukweli ujio wa Geb na Nanaa usiku huo
palikuwa hakuna kujifariji isipokuwa lipo jambo zito zaidi upande wake
Naya. Geb asingemfuta Joshua hata iweje mida hiyo mpaka iwe ni jambo zito sana
tena linalomuhitaji Naya wala si yeye. Joshua hana biashara, hana ndugu
wakutolewa kwenye kitanda ambacho bado kina harufu ya fungate!
Moja kwa
moja Naya alijua kabisa ni jambo linalomuhusu yeye. Tena wazo la kama ni Bale
alilipinga, akajiambia kama ingekuwa Bale yupo matatizoni, baba yake angesubiri
papambazuke ndipo aombe msaada kwa watu. Alimjua baba yake sio wakulia shida
usiku wa manane. “Mungu nisaidie!” Naya akaendelea kumsihi
Mungu akizidi kuingiwa hofu hapo kitandani na kushindwa hata kujisogeza.
Naya
alikuwa mtupu kabisa hapo kitandani amekumbatiwa na Joshua, anapapaswa. “Twende
mpenzi wangu.” Joshua akamsihi tena taratibu akimuhurumia. Akatoka na kuvaa
harakaharaka. Wakatoka kwa pamoja. Vile alivyomuona tu Nanaa, akajua mambo si
mazuri. “Ni baba Naya ndio amefariki?” Naya akauliza swali la moja kwa
moja walipofika tu hapo sebuleni walipokuwa Geb na mkewe. “Mnajua nisingewasumbua
kama si muhimu.” Joshua kimya mapigo ya moyo yakienda kasi. “Ni baba Naya?”
Naya akarudia tena swali lake lakini safari hii akimwangalia Geb aliyekuwa
akizungumza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati ikionekana ipo amani kubwa, ndipo na uharibifu
unaponyemelea. Endelea kufuatilia kujua nini kinaendelea!!
0 Comments:
Post a Comment