Kazi Tena.
![]() |
Saa 11
alfajiri, Joshua akawa ameshawasili nyumbani kwa kina Naya, Kiluvya. Naya naye
alishakuwa tayari, akatoka bila hata Joshua kuingia ndani ya geti.
Safari yakurudi mjini, ikaanza. “Vipi tumbo lakini?” “Nakunywa zile dawa,
limetulia kabisa. Ulilala salama?” Joshua akacheka. “Unacheka nini sasa?” “Jana
umekoroma Naya.” Naya alicheka mpaka akajificha. “Ilikuwa kwa sauti?” Joshua
akazidi kucheka. “Sasa na wewe kwa nini hukukata simu bwana!” “Nipitwe!” Naya
akazidi kucheka kwa aibu. “Bwana Joshua! Ungekata!” Joshua akamwangalia na
kuzidi kucheka.
“Sio
vizuri bwana!” “Usijali.” “Mimi najali.” “Basi acha nikutetee. Ulikuwa
umechoka. Unaumwa, na ukalia sana na kutapika. Ndio ukalala, nakupata utulivu
mzuri ndio maana ukawa unakoroma.” “Umeona eeh!” Joshua akazidi
kucheka. “Sasa na wewe ulilala saa ngapi?” “Nilichelewa sana kulala. Kuna
kazi nilitaka niikamilishe ili uipitie kwanza ili wakati mnakaa leo na Jamal,
ujue ni nini chakuzungumza naye.” Naya akashangaa mpaka akamgeukia. “Fungua
dashboard hapo mbele, utoe karatasi. Zipo mbili tu.” Naya akafungua akianza
kuhisi kutetemeka mikono. Akamwangalia tena na kumeza mate akijaribu kufungua.
“Asante Joshua. Asante sana.” Joshua akajua amebabaika. “Sijafanya kitu cha
ajabu wala sijakufanyia kazi yako, usizoee.” Naya akacheka kidogo na
kuzitoa hizo karatasi. Mwanga wa hiyo droo ya gari ukazimulika, zilichapwa
vizuri. Zilionekana safi.
“Ni
yaleyale mawazo yako, nimeyaweka kitaalamu zaidi. Nitataka leo mkae na Jamal,
lakini kabla ya hapo, nataka utizame kile nilichoandika mimi, na
ulinganishe na mawazo yako, vile unavyofikiria wewe. Kama kuna kitu unataka
kurekebisha, rekebisha mapema na chapisha upya kabla hujakutana na Jamal ili
mtakapokutana, mkamilishe na Jamal, jioni nataka hitimisho iwe imenifikia.” “Nakushukuru
sana Joshua.” “Nilikwambia usizoee?” Naya akacheka kwa hofu kidogo. “Ni kwa
kuwa ulikuwa mgonjwa, umekosa kazini jana, leo umetaka kurudi kazini na ndio
siku nataka kufunga hilo zoezi. Sitaki upitwe wakati ulitoa wazo zuri sana.”
“Nakushukuru sana kwa nafasi unayoniamini nayo Joshua. Asante.” “Karibu.”
Wakatulia kidogo.
“Nikwambie
kitu Joshua?” “Karibu?” “Siku ile ya kikao kuna mawazo nilitaka kutoa.”
“Nilisikia.” “Nani alikwambia?” “Mbali na ile rikodi aliyonipa Jema, yule
msaidizi wa CEO alinitafuta tena kuniambia juu ya hilo.” Naya akaingiwa hofu.
“Yule baba! Anasemaje!?” “Anataka kujua ni nini ulikuwa ukizungumzia na
tunafanya nini kuhakikisha tunakubakisha kwenye kampuni yetu.” “Joshua!”
“Nilikwambia maji yametibuliwa. Changamka. Huu ndio wakati wako wa kung’aa.
Acha woga, ongeza ujasiri ili watu wakuone Naya kama Naya, sio Naya nyuma ya
Joshua. Unanielewa?” “Ndiyo.” “Ukiitwa popote, hakikisha unaacha historia kali,
mpaka waje wakuite tena maana sasa hivi wewe bado upo ngazi ya chini sana. Lakini
kwa hiki ulichofanya juzi, kinaweza kukupandisha juu kwa haraka kama utaendelea
hivyohivyo. Jifunze kwa makini na hakikisha kila kitu unapatia. Tena unapatia
haswa.” Naya akajituliza kupokea hekima za Kumu.
“Ondoa
woga, fanyia mazoezi kila unachotaka kuzungumza mbele ya watu ili uwe fasaha,
uongee kiutaalamu. Sio kurudiarudia jambo moja mara nyingi. Unachosha watu
wakubwa wenye nyadhifa zao, ambao wanakusikiliza. Pia itakusaidia kupangilia
mawazo yako. Sio unachanganya pointi. Sijui kama unanielewa?” “Nakuelewa.”
“Basi ni hivyo tu vyakuongeza kwenye haiba yako ya uchapakazi na kwenye hiki
kitengo.” “Nimesikia kufanya kazi karibu na wewe ni ngumu sana.” Joshua
akakunja uso kidogo na kutulia.
“Wanasema
eti unataka mtu...” “Asiye mzubaifu kwa kuwa sina muda wakurudia jambo mara
mbili. Nataka mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiria, kujituma mwenyewe bila
kumfuatilia nyuma na roho ya uthubutu bila mipaka. Ndio maana mimi vikao vya
kitengo kizima sifanyi kila siku au niseme mara kwa mara. Sina muda wakuanza
kujibu maswali ya hakuna sukari, sijui maziwa ya chai!” Naya akacheka kwa hofu.
“Ndio
maana nimechagua watu wachache ambao nikizungumza mara moja, wanaelewa na
kutenda. Halafu wao nao ili wasipotee kwenye kujibu hoja za chai, na wenyewe
wanawaachia kina Jamal. Kwa hiyo ndio maana unaona nafanya kazi kwa mwendo
kasi. Sijui kusubiri. Hilo nalo ndilo tatizo langu. Nikishapima jambo na
kujiwekea mikakati yake, huna jinsi ya kunibadilisha. Siwezi mtu mzembe
mwenye visingizio. Kwanza...” “Huna muda wakupoteza.” Naya akamalizia
kama aliyekuwa akimnukuu mtu. “Nani anakupa habari zangu Naya!?” Joshua
akauliza akicheka kidogo. “Nimekufahamu na sifa zako nyingi hata kabla
sijakuona Joshua Kumu, mungu wa Coca.” Joshua akacheka na kutulia.
“Nitajitahidi
Joshua.” “Na mimi nitakuwa nyuma yako kukutia moyo.” Naya hakutegemea.
Akamwangalia. “Najivunia sana wewe Naya. Sana. Huna sifa mbaya pale kazini. Ni
nzuri tupu! Na ninajua utafika mbali sana.” “Asante.” Naya akatulia, akawa
hajui azungumze nini tena. Joshua alishabadilika pale akawa bosi wake. Akatulia
kabisa wakaendelea kuendesha.
“Joshua?”
Naya akamuita tena taratibu. “Nikuulize?” “Karibu.” “Katika swala la mshahara,
niliambiwa wakati wa ajira, unaweza kuzungumza. Sisi wametuanzia chini sana
kwakweli. Natamani kuongezwa. Sasa nitaje kiasi gani? Nahofia nisije nikataja
kubwa na kuharibu.” “Huwezi kuharibu kwa kuwa tunakuhitaji. Watakachofanya
nikukuomba upunguze tu. Na kwa hakika sijui mishahara yenu japo najua wangu
unaimbwa na kila mahali!” Naya akacheka kidogo na kuinama kama anayefikiria.
“Sasa inakuaje wewe unalipwa pesa yote hiyo!?” Akauliza kwa hofu kidogo. “Ndio
thamani niliyoweka kwenye kazi ninayowafanyia.” Joshua akajibu kwa kujiamini
haswa.
“Wewe
ndiye unayewauzia huduma. Wakitaka wananunua, wakishindwa unapeleka biashara
yako kwa wengine. Si ndivyo biashara ilivyo?” “Ni kweli.” “Usipojiweka thamani
wewe mwenyewe, basi ujue wengine watakuthaminisha kwa vile wanavyotaka wao.
Lakini ukijijua wewe ni nani, na ubora wa huduma yako, basi, unajiuza kwa
urahisi sana.” “Ni kweli. Lakini nilisikia na Pepsi walitaka kukununua mwaka
jana, kwa pesa zaidi ila ukakataa. Ni kwa nini?” Joshua akacheka sana.
“Kweli unazo habari zangu!” “Niambie kwa nini?”
“Moyo
ulisita Naya. Nimefika hatua ya maisha, si pesa tena inaniongoza, ila kibali
kutoka kwa Mungu. Hata uniambie utanipa mabilioni ya pesa, kama Mungu hayupo
kwenye hilo jambo na hiyo pesa, hutanisogeza hata kidogo, kwa kuwa najua mwisho
wake wa huko nitakapokwenda bila Mungu, nikuharibikiwa vibaya
sana. Heshima Mungu aliyonipa pale, hailinganishwi na pesa.” “Kumbe
unajua!?” “Oooh yeah!” Joshua akakubali kwa haraka sana.
“Ninazungumza
na watu hao! Hata nikikwambia unaweza ukashangaa.” “Nimesikia ukizungumza, hao
makaburu wanaandika.” Joshua akacheka kidogo. “Sasa hao ni wa chini ya hao
ninaokwambia. Nikiwa nakwenda kwenye vikao Afrika ya kusini, hakika mimi
mwenyewe huwa naingiwa hofu. Nakuwa sina jinsi zaidi ya kujifungia kwenye
chumba walichonitayarishia, nakupiga magoti kunyenyekea mbele ya Mungu. Si
kawaida Naya! Ila ni Mungu tu, wala si mimi hata kidogo. Hakika ni
Mungu.” Joshua akaendelea kumtukuza Mungu wake Naya akimsikiliza. Akasikika ni
kama mtu anayeogopa kuchukua sifa ya mtu mwingine. Kujihami kwa hali ya juu,
akisema si yeye ila Mungu.
Walifika
ofisini alfajiri hiyo kama waliotokea nyumba moja. “Nakuacha ukafanye kazi.”
“Kwa hiyo ndio sitakuona tena mpaka jioni?!” Joshua akacheka. “Nakupa muda
wakujiandaa. Kaandae utakachokionyesha kwa Jamal. Na hakikisha kinakuwa kina
saini yako sio ya yoyote.” Naya akatulia kidogo. Joshua akajua hajaelewa. “Kazi
yako yoyote ile, lazima mtu yeyote akiitizama, hata kama haupo pale, ajue ni
yako. Hata kuzungumza pia. Ndio maana ulipotoa wazo lako au ulipokuwa
ukizungumza, Njama alikuwa akisisitizia watu wakusikilize kwa makini, watagundua
kuwa ni mimi nazungumza kupitia kinywa chako. Ni kwa kuwa wameshajua jinsi
ninavyozungumza. Ni siri nakupa na wewe. Hakikisha kazi zako zinabeba
jina lako. Ziwe za kipekee ndipo utakua kwa haraka.” Naya akaanza kubabaika.
“Nitafanyaje
Joshua? Sina uzoefu!” “Hivyo nilivyokuandikia ni mfano wa Joshua wa miaka ya
zamani. Nikajiongeza mpaka kufikia hapa. Lakini hivyo nilivyokuandikia hapo,
ndicho au ndio jinsi ilivyonitoa. Ni msingi wangu. Sasa na wewe angalia jinsi
yakupangilia mawazo yako. Nina uhakika hapa kazini hakuna anayetumia namna hiyo
hata kidogo. Ukiiga, na kujiongeza kidogo tu, utabaki kuwa yako daima. Kila
utakapokuwa ukiongea au kuandika hivyo, watajua ni Naya tu. Unanielewa?”
“Naomba nikaanze halafu nikutumie uangalie kabla ya kukutana na Jamal.” “Hapana
Naya. Hapo ndio nitakuwa nikikufanyia kazi. Na ndipo wazo la kutoa woga
linapokuja. Fanya kuanzia hapo. Nitakachokiona baada ya hapo nitajua ndio kazi yako
na umejiongeza mwenyewe na utaendelea kadiri siku zinapozidi kwenda.” Naya
akapoa ni kama akawa amekumbushwa nafasi yake na ya Joshua.
“Usinikasirikie.”
“Hapana Joshua. Nakushukuru sana kwa kunijenga. Nakuahidi sitakuangusha.”
Joshua akafurahia hilo. “That’s the spirit. Huo ndio moyo ninaotaka. Nilijua
ungekasirika!” Akaongea kwa kujivuna. “Hata kidogo. Nahitaji kujengwa kama mtu
mzima si kuendelea kulelewa kama mtoto mdogo. Na kusukumwa kama hivyo.
Nimejificha vyakutosha.” Joshua akajua somo limemuingia. “Uwe na siku njema.
Ufanikiwe katika ufanyalo.” “Amina Naya. Nitakuona baadaye, kila la kheri.”
Naya akashuka garini kama akimbie kwa hamasa.
Moja kwa
moja kwenye meza yake akawasha kompyuta yake, macho kwenye zile karatasi
akisoma na kushangaa. “Hata ningepewa mwaka mzima, nisingepata wazo la
kuandika kwa namna hii!” Naya akaendelea kusoma vile ilivyoandikwa kwa
mtiririko wa ajabu! “Ni kweli Joshua anakipaji cha pekee!” Naya
akaendelea kushangazwa na ule mpangilio wa kazi.
Ili ile
kazi ikae kichwani, akaanza kuichapa kwa upya. Neno kwa neno huku akijaribu
kuondoa maneno magumu ambayo yanasikika kabisa ni ya Joshua, akaweka maneno
yaliyobeba lugha nyepesi. Ilikuwa kama ripoti kwa lugha ya kingereza ila
alichotaka kisikike kwenye tangazo, akaweka kwa lugha ya kiswahili. Naya
aliipanga na kutengeneza vizuri. “Hawatanikamata na kujua Joshua
amenitayarishia kweli!” Hofu ikamwingia Naya. Lakini akakumbuka Joshua
kumwambia kuwa ni kazi ambayo pale haifahamiki. Akaendelea kuandika na kujaribu
kuikariri vizuri. Akajaribu hata kuzungumza kwa sauti bila kusoma. Akarudia
tena na tena mpaka akaona muda wa watu kuingia ofisini unakaribia.
Akaamua
kuangalia kama kuna kazi hazikumalizika siku ambayo hakuwepo kazini, akagundua
ni nyingi. Naya akashangazwa sana. “Inamaana Jamal hakupita humu ndani
kwamba hajaona!” Naya akashangaa sana ila aliwajua wenzie. Ilimradi wawepo
pale ndani, basi. Sio kufanya kazi, ila stori na macho kwenye simu muda wote.
Akaanza kufanya kazi kwa haraka.
Wafanyakazi
wengine wakaanza kuingia na kumshangaa Naya. “Si tuliambiwa unaumwa!”
“Nimepona.” Naya akajibu kwa ufupi akiendelea kufanya kazi mpaka saa mbili
kamili Jamal alipoingia nakushangaa Naya yupo kwenye kiti chake akifanya kazi.
“Mama Kumu!” Jamal akaita akimshangaa, Naya akajikuta akiitika na
kugeuka bila kufikiria. Kumbe nyuma ya Jamal sehemu ya kuingilia alikuwa
amesimama Joshua mwenyewe. Naya alishituka, Joshua akacheka taratibu
akimtizama. Kama kawaida yake, mikono mfukoni. Jamal akageuka alipoona macho ya
Naya yameduaa nyuma yake. Akageuka. “Kumbe kiongozi upo nyuma yangu?
Namshangaa Naya! Si alitakiwa kupumzika siku mbili!?” “Hana muda...”
“Wakupoteza.” Akamalizia Jamal, wakacheka.
Joshua
akawasogelea. “Nimepata ujumbe wako, ndio nataka tukakamilishe na Naya baada
yakutoka kwa HR. Au kuna mabadiliko?” “Mimi nimekuja kumtakia kila la kheri na
kumkaribisha rasmi kundini.” “Hatujafika bado kwa HR! Akikataa?” Jamal
akauliza. “Ndio maana nimekuja kutongoza. Nabembeleza ili akifika huko asikatae.
Wewe vipi Jamal? Nipishe.” “Samahani Kiongozi.” Jamal akanyanyua mikono juu
akicheka na kuondoka. Naya akacheka kwa aibu. “Njoo.” Akamwita kwa kumkonyeza
na sauti ya chini. Joshua akazunguka kule alipokaa.
“Nisamehe
nimeitika kwa jina la mama Kumu, sikuwa nimefikiria. Jamal alinishitukiza.”
Akamnong’oneza sikioni, Joshua akacheka. “Kumbe ndivyo wanavyokuita?” “Hapana!
Yaani leo ndio mara ya kwanza.” Joshua akacheka. “Kumbe! Saafi sana mama
Kumu.” Naya akampiga kidogo. “Nimefurahi uliitika. Usingeitika ndio
ningesikitika.” “Kweli?!” “Kumbe! Inamaana ungekuwa umenikana.” Akashitukia
Joshua anamvuta karibu, akamshika vizuri. Mkono mmoja kiunoni na mwingine
shingoni, kisha akampa busu kwenye mdomo, palepale mbele ya watu, tena
wafanyakazi ambao wapo chini yake! Ilikuwa ndio mara ya kwanza. Naya
hakutegemea. Japokuwa alishituka sana, ila kadiri alipomshikilia vizuri na
kuendelea kumbusu, Naya akatulia na kurudisha busu taratibu. Hakutegemea
kufurahia busu la mtu mwingine mbali na Malo. Alijisikia vizuri mpaka
akajisogeza vizuri.
Joshua
alijawa maadili sana. Hakutarajia kupata busu kutoka kwake hata kwa kujisahau.
Hakuonyesha dalili hata yakuja kumgusa siku za karibuni. Ni kama huo upande wa
mapenzi hakutaka uwe wazi kabisa. Naya alishangaa ila akafurahia. Akajikuta
amejisahau na yeye akamshika bila kujua ni wapi. Haikuwa muda mrefu sana,
akamuachia, Naya akainama kwa aibu. Akamnong’oneza. “Nakupenda Naya.” Naya
akacheka na kumwangalia. “Nimefurahi!” Joshua akacheka taratibu. “Usizoee.”
Akamnong’oneza. “Siku njema.” “Na wewe Joshua. Nimefurahi.” Naya akasisitiza
akicheka. Joshua akaondoka akicheka na kumuacha Naya mwenye maswali. Watu wote
walibaki wameinama. Alipotoka tu Joshua, wote wakamwangalia Naya. Naya akarudi
kukaa na kurudisha macho kwenye kompyuta yake.
“Upo
tayari?” “Naomba dakika 5 tu, Jamal, bosi wangu. Kuna kazi ya jana namalizia.”
“Daah! Nakushukuru Naya. Jana nilibanwa kupita maelezo nikashindwa kupitia
hapo.” “Dakika 5 tu. Nakuja bosi wangu. Acha tupaache hapa vizuri.” “Lakini
usichelewe tafadhali. Hii kazi inatakiwa leo jioni iwe imeshakamilika. Na Kumu
akisema jioni, anataka iwe ni masaa machache kabla hapajaitwa jioni. Kama usemi
wake unaopenda kuusema mwenyewe Kumu.” “Early is on time, On time is
late, Late is an exceptable.” Kibasa aliyekuwa ametulia kwenye meza yake,
mfanyakazi wa hapo wa muda mrefu kidogo, aliyejulikana kama msaidizi wa Jamal
kwenye hicho kitengo chao kabla Naya hajaingia kwenye picha nakufanya majukumu
mengi bila kutumwa wala kutambulika, akamalizia usemi wa Kumu anaoupenda
kuusema sana, aliotaka kusema Jamal kwa Naya. Hawakujua kama wengine
wanawasikiliza. Wakamgeukia na Jamal akaongeza. “Umesikia?” Naya akacheka.
“Nimesikia bosi wangu.” “Basi changamka mama.” “Sitakuchelewesha.” Jamal
akatoka Naya akarudisha macho kwenye kompyuta. Akili ilishachanganywa na
Joshua. “Anajua ku ku...” Naya akacheka mawazoni na kujishika
midomo kisha akaendelea na kazi baada ya kukumbuka anasubiriwa.
Shari Yaleta Kheri.
Siku hiyo
Naya akaingia ofisi ya mwajiri kuajiriwa rasmi. Alijawa wasiwasi alimtaka Jamal
awe naye kwenye kila hatua. Jamal akamtajia pesa ambayo aombe kwa mshahara.
Hilo likawa msaada. Akajaza karatasi zote za ajira kwa haraka, Jamal akitaniana
na wafanyakazi wa kile kitengo mpaka akamaliza ndipo akatoka naye kwenda
kufanya kazi.
Kwanza
akashangazwa na vile Naya alivyopangilia ile kazi. “Wewe mtoto!” Jamal
akamfanya Naya acheke. “Mbaya au nzuri?” “Mpaka najisikia kutupa kazi yangu!”
Naya akacheka sana. “Nakuachia kitengo Naya.” “Wale watu wako sitawaweza Jamal.
Mimi siwezi kelele nyingi, nitaishia kufanya kazi zote peke yangu kisha
nitakuchelewesha.” “Wala usijali. Natoa ile fujo yote pale, natafuta wengine
wachache. Nishamwandikia Joshua. Nasubiri akitulia na kuidhinisha, ijumaa hii
napunguza watu pale na kutoa onyo.” “Jamal!” “Nimechoka Naya. Umeona kazi
ulizokuta pale? Inamaana bila mimi kupiga kelele, hawafanyi kazi. Usipokuwepo
wewe, inamaana kazi kazitafanyika. Wale ni watu wazima, si watoto. Kama hawana
shida na kazi, basi wapishe watu wenye shida.” Naya akanyamaza. Walikuwa chumba
cha mkutano, wao wawili tu.
Njama Tena.
Njama
akaingia. Jamal akamtizama na kuendelea na kazi. “Sijaelewa?” Akaanza Njama.
“Yaani huyu mtoto kaja juzi tu, anachukua nafasi yangu?” “Acha kutupotezea muda
Njama. Kama unatatizo, nenda kasemelee tena kama mtoto.” “Hakika
mtaniona mbaya.” “Sio wewe uliyekataa kufanya kazi na Naya?” “Si hakuwepo?” “Na
mimi je?” Jamal akamuuliza. “Sio wewe uliambiwa na Kumu unipe kazi yako ili...”
“Ili uniibie?” “Basi kwa taarifa yako tu, nipo hapa na Naya, amenikabidhi kazi
yake. Nzuri kuliko yangu na hakuweka hata jina lake. Hakuna kuibiana Njama.
Tunafanya kazi kama timu moja. Na hiyo ilikuwa hivyo tokea zamani mpaka
wewe ulipoleta ujinga wako wa kitoto.” “Kwa hiyo ndio...” “Tupishe
Njama. Kama unamatatizo yako, peleka mbele ya safari.” Akamgeukia Naya.
“Endelea na kazi.” Naya akainama.
Vita ya Mapenzi.
Njama akasogea
pale alipokaa Naya na kuvuta karatasi moja aliyokuwa akiisoma na kuandika.
Jamal akasimama kama mshale na kumsukuma Njama huku akimpokonya ile karatasi ya
Naya mpaka ikachanika. Naya akashangaa ngumi zinaanza kurushwa kati ya Jamal na
Njama. Hapohapo akampigia simu Joshua. Katikati ya kikao, Joshua
akapokea. “Njama anafanya fujo hapa tulipo na Jamal.” “Mko wapi?” “Chumba cha
mkutano.” Joshua alitoka akikimbia bila yakuaga katikati ya mkutano.
Kwa kuwa lilikuwa jengo moja, akafika kwa haraka na wafanyakazi waliosikia ile
fujo na wenyewe wakakimbilia hapo. Wakakuta wakipigana haswa, wakirushiana
ngumi kana kwamba ni wanandondi waliokuwepo ulingoni. Joshua akawaamulia na
askari wakawa wamefika.
“Ameanza
kumfanyia fujo Naya.” Jamal akamfanya Joshua kushituka sana, akamwangalia Naya.
“Amekufanya nini?!” Naya alikuwa kwenye mshituko, akashindwa kujibu. “Nimevuta
tu karatasi ndio...” “Subiri kwanza Njama. Naona umevuka mpaka, na hapo
sitakuruhusu. Naya ni off limit.” Kumu akaongea kwa hasira. “Si
umemchukua mwanamke wangu! Unampa mabusu hadharani kutangaza ushindi wako
kwangu!” Naya akazidi kuingiwa hofu akajua maneno yalishaenea wasijue walipigwa
picha na hiyo picha ikasambazwa. Kwa muda mfupi tu, kampuni nzima ilishapata
picha yao wakiwa wanapeana mabusu. Ila Joshua alishatumiwa na Fina, alishajua
akiwa mkutanoni.
Njama
akaendelea kulalamika. “Isingekuwa wewe, sasa hivi mimi ndio ningekuwa na Naya.
Tulikuwa tumefikia mwafaka na ile safari ya Mbeya ilikuwa niende mimi, lakini wewe
ukanipora safari yangu ili ukamchukue mwanamke wangu. Niliambiwa kila kitu.
Naya alishanikubali ila wewe ndio umemchanganya.” Jema akaingia
akikimbia. “Acha uongo Njama.” Naya alijibu midomo
ikimcheza kwa hofu, wafanyakazi wengine waliowahi hapo wakiwatizama.
“Hiki
kinachotokea ndicho kinachokufanya unikatae Naya. Unataka Joshua akupandishe
cheo kwa haraka na unasahau maisha ni zaidi ya hapa!” Njama akazidi kupayuka
kwa sauti ya juu iliyozidi kuvuta wafanyakazi wote wa masoko hapo kwenye ukumbi
wa mkutano na wengine hata wa nje na kuzidi kumiminika hapo, na kuzidi
kumuogopesha Naya.
“Mpumbavu
tu wewe. Akutake nani?” Jamal akamkejeli, Njama akataka kumrushia ngumi lakini
Jamal akakwepa. Askari wakamshika Njama na kumfunga pingu kwa haraka kama na
wao walikuwa wakimsubiria. “Ulichokuwa unakitafuta tokea majuzi, umekipata
sasa.” Jema akamtupia neno wakati wanamtoa nje huku Njama akiendelea kupayuka.
“Sijawahi
kumkubali. Usimwamini, anadanganya.” Naya akajitetea kwa Joshua huku
akitetemeka kwa hofu. “Huna haja yakujitetea Naya.” Joshua akamsogelea.
“Hujaumia popote?” “Jamal aliniambia nisogee mbali.” Joshua akamgeukia Jamal.
“Asante aisee.” “Mpuuzi kweli! Amechana kazi zote alizokuwa ametoa Naya na
kutupa laptop yangu. Ndio tulikuwa kwenye marekebisho!” “Huna kopi yeyote
kwenye kompyuta?” Joshua akamuuliza Naya. “Ninayo nimeacha kwenye ile kompyuta
yangu, ofisini.” “Basi kaprint tena kisha mje muendelee.” “Sijui kama hii
laptop yangu itafanya kazi tena! Ameitupa kwa nguvu kweli na mimi sikuwa
nimetunza kazi yangu sehemu nyingine ila hapa tu.” Jema akaiendea laptop ya
Jamal ambayo Njama aliitupa kwa hasira, akamuokotea.
Joshua
akavuta pumzi kwa nguvu. “Nenda kalete tena kazi yako Naya, na mimi nitajaribu
kuwasha kompyuta yangu nione.” Jamal akamtuma. “Lakini Joshua, nashauri urudi
kwenye kikao. Umewaacha wote wapo mtandaoni wakikusubiria wewe. Naya yupo sawa,
acha mimi nitasimamia hili zoezi. Tafadhali Kumu.” Jema akashauri kwa kusihi,
Joshua akabaki akifikiria. “Tusije haribu kote, Kumu! Tafadhali nenda
kamalizie kikao. Nakuahidi hapa patakuwa sawa.” Wafanyakazi wote walibaki
wakiangalia kinachoendelea na kusikiliza. “Lazima nizungumze na Naya kwanza, nimtulize
mimi mwenyewe. Waambie wanipe dakika 6 tu, nitarudi.” Joshua akatoka kwa haraka
bila hata kusubiri jibu la Jema. Jema akatingisha kichwa na kutoka kurudi
kwenye kikao akikimbia.
Yeye
Joshua alishatoka na kumfuata Naya akamkuta amesimama pembeni ya kompyuta yake
kama asiyejua chakufanya. Alikuwa peke yake pale, wengine wote walikimbilia
eneo la tukio. “Naya!” Joshua akamuita. “Sikuwahi hata kumuonyesha dalili za
kuja kumkubali baadaye. Anadanganya.” “Naomba utulie.” “Na pengine labda
tusingekiss! Inaonekana kuna mtu alitupiga picha akasambaza hizo picha mpaka
zikamfikia Njama.” “Au ni mtu wa Njama, alitupiga picha makusudi na kumtumia
Njama. Na Njama akazisambaza makusudi ili...” “Kutuharibia! Mungu wangu Joshua.
Labda...” “Tusikiss tena?” Joshua akamuuliza taratibu tu.
“Au mimi
niache kazi hapa nikatafute kwengine.” Joshua akakunja uso. “Kwa ajili ya Njama
au mimi na busu nililokupa asubuhi?” “Hapana Joshua. Nimefurahia sana, na
nilikwambia, ila sitaki niharibu sifa yako njema.” “Kwa nani!?” “Sijui Joshua!
Ila ninachojua nakupenda wewe.” Hilo likamfurahisha Joshua. Akamsogelea.
“Nitakubusu kokote, mbele ya yeyote, muda wowote ninaotaka mimi kama wewe
hutakuwa na shida.” “Mimi napenda.” Naya akajibu kwa aibu akitabasamu kidogo.
Joshua akamvuta karibu yake na kumbusu tena na tena. “Hutaacha kazi uliyoanza
rasmi leo. Nilikwambia dhoruba inapopita, lazima sisi kina KUMU.” Akimuonyeshea
na yeye Naya, “Ndio tubaki tumesimama.” Naya akacheka.
“Hawajawahi
kumuona Kumu kwenye mapenzi. Watazoea tu.” Naya akambusu hapo midomoni akatulia
kwa muda, Joshua akimsikilizia, kisha akamwachia na kucheka. “Mimi nakupenda
Joshua.” “Asante Naya. Acha nirudi kwenye kikao, na wewe rudi kazini ukiwa
umetulia. Au unataka tukae wote?” Naya akashangaa sana. “Hapana Joshua!
Nitakuwa sawa. Na samahani kukupigia. Sikujua kama ...” “Muda na wakati wowote unaponihitaji,
nipigie.” Naya akacheka taratibu mbele yake. “Nashukuru. Haya nenda.” Kumu
akambusu na kutoka kwa haraka akiangalia muda huku akipishana na wafanyakazi
wengine wa hapo ofisini waliokuwa wakirudi hapo. Walimpisha kama wanaoogapa
hata kugusana naye.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya
kuhangaika bila mafanikio akijaribu kufufua kompyuta yake ikabidi Jamal achukue
kazi ya Naya kama ndio wamefanya wote. Hata hivyo akili ilishachanganyikana.
Alikuwa hawezi kufikiria tena baada ya ugomvi alioanzisha Njama. Waliandikisha
maelezo kwa askari. Naya peke yake na Jamal hivyohivyo wakieleza jinsi
ilivyokuwa, Njama akaonekana ndiye mwenye makosa. Akachukuliwa na yeye maelezo
yake yakiwa yanaandikwa kwa makini ili asije kugeuka baadaye.
Kabla ya
kutoka kazini kwenye mida ya saa 8 mchana, Jamal akawa ameshawakilisha kazi kwa
Joshua kwa njia ya barua pepe na kumkabidhi Fina kabrasha lililokuwa na kazi
nzima. Joshua hakuwepo ofisini, Fina alimwambia ametoka. Naya akarudi ofisini
mara baada ya kuruhusiwana na Jamal. Akarudisha akili kazini. Ukweli
ilikuwa ngumu kumsema Naya. Hata kabla ya kuanzana na Joshua, Naya alikuwa
akichapa kazi na Jamal kumsifia kila wakati akitaka wote waige mfano. Hakuwa na
maneno mengi ila kazi kila awapo kazini. Hapo Naya anarudi kwenye meza yake
akiwa na ajira kamilifu na mshahara mzuri. Akawa amewapita hata
aliowakuta hapo kwenye hiyo kampuni na wenzake alioanza nao kazi pia. Kimya.
Akajua wameongeza heshima sababu ya Kumu pia. Akajichekea moyoni akijua wapo
wanaoumia. Hakujali.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Nimekuacha
na njaa, Naya wangu! Nivumilie mama. Jioni tutakula vizuri.” Akageuka na
kumuona Joshua. Akaweka matunda mezani. “Na wewe?” “Sina muda. Nasubiriwa. Wewe
kula. Nitakuona baadaye. Si upo sawa?” Naya akatingisha kichwa
kukubali. “Ukimaliza kabla yangu, njoo unisubirie ofisini kwangu.” “Sawa. Na
asante kwa matunda.” “Karibu. Baadaye.” Joshua akatoka kwa haraka. Naya akabaki
akitizama yale matunda pale. Yaliwekwa vizuri, yakapambwa kwa unadhifu, zabibu
zikavutia pale juu ya matunda yote. Akacheka wakati akivuta yale matunda kwenye
chombo kizuri sana ila juu iliwekwa mfuniko wa wazi kuonyesha ule umaridadi
ndani. Wenzake wote wakabaki wakimwangalia. Kulikuwa na uma pembeni, Naya
akatoa, akaanza kula huku akifanya kazi. Hakunyanyuka hapo mpaka jioni akifanya
kazi.
Ngumu
kumlalamikia kuwa ameajiriwa kabla yao kwa kuwa ni kweli alikuwa akichapa kazi
bila ya kutumwa wala kulalamika. Akikaa hapo, hatanyanyuka wala kuzungumza na
watu hovyo akizungumzia habari nje ya kazi. Mtulivu, usingemkuta akibishana kwa
lolote. Jamal alimpenda tokea hata hajaanzana na Joshua. Wivu uliwasumbua
lakini ilikuwa ngumu kusema amependelewa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jioni
wenzake walitoka wakiwa kama wamemziria kazi. Alijua, lakini hakujali hata
kidogo. Akazifanya bila hata kujali au hata kumwambia Jamal. Jamal alitingwa na
kitu kingine, hakurudi tena hapo ofisini kwao. Naya akaendelea na kazi akiwa
amejawa morari akijua yeye ni mwajiririwa halisi pale, mshahara upo juu, na
kikubwa zaidi akajua anakubalika. Joshua yupo upande wake! ‘Nivumilie
tafadhali. Naomba tena nusu saa. Unaweza kuja kunisubiria ofisini kwangu.’
‘Hamna shida. Wewe endelea tu, usijali. Nitakuwa hapa ofisini kwetu, na mimi
nikimalizia kazi.’ ‘Ndio maana nakupenda.’ Naya akacheka na
kuendelea na kazi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akiwa
amepotelea kwenye kazi akasikia. “Utajuta kunifahamu!” Naya akageuka na
kucheka. “Hata kidogo. Nimepata muda wa kufanya kazi zaidi. Njoo nikuonyeshe
kitu.” Joshua akamsogelea. “Nataka kukuonyesha wewe na unishauri kabla ya
Jamal.” Joshua akaenda kusimama nyuma yake ili aangalie. “Inabidi kutafuta
laptop yako.” “Ninayo. Malo alininunulia tokea nipo chuo, ila sikujua kama
naweza kuitumia hata kwa mambo ya kazini!” “Haina shida.” “Haya. Unakumbuka ile
safari ya Mbeya?” “Ile uliwaambia kwenye kikao kuwa ulifanyia kazi survey?”
Naya akamgeukia vizuri kwa mshangao.
“Jema
aliniambia hata Jamal alionyesha ni kama hakujua ni nini unazungumzia au ni
kama alisahau. Ninachotaka kukwambia ni kuwa, hii tabia hii, itakufikisha mbali
sana. Kuzingatia au kuwekea maanani vitu kama hivi. Ni mimi huwa nawatuma ili
nipate maoni ya watu. Kumfikia mtumiaji moja kwa moja. Ila nataka kukwambia
ukweli Naya, sijawahi kupata majibu ya kueleweka kama hivyo wewe.”
“Labda uangalie kwanza ili nisikuvunje moyo Joshua!” Akamtahadharisha. “Sijali
itaonekana vipi, lakini ile tu kutenga muda na kufanyia kazi, kwangu
inanirahisishia sana kujua wapi nifanye nini. Kwa hiyo umenifurahisha.” Naya
akacheka na kumfungulia ile kazi kwa ujasiri.
Akamuona
Joshua anacheka mara alipoiangalia tu. “Nimeiga ufanyaji kazi wako. Kama vile
ile uliyonipa asubuhi.” “Daah! Unaakili sana Naya! Umepangilia vizuri sana.
Sasa hii usiite tena kazi yangu. Hii ni yako. Na usijibadilishe ila kujiongeza
ukiendelea kutokea hapa.” “Kwa hiyo umependa?” “Sio tu kupenda, umenisaidia
sana na hichi ninachotaka kukizindua. Naomba nijitumie, ili nitumie kwenye
kikao cha wote kesho asubuhi.” “Hamna shida kabisa.” Naya akafurahia sana kuona
Joshua amemkubali kazi yake.
“Naruhusiwa
kufanya marekesbisho kidogo?” Joshua akauliza kwa heshima. “Sio makubwa. Ni
lugha kidogo tu.” “Nakushukuru Joshua. Najua umechoka.” Naya akampisha pale
kwenye kiti. “Kaa yeye.” Akaanza kuisoma hiyo kazi kwa makini na kuifanyia
marekebisho kidogo huku akirudia kusoma tena na tena mpaka akamuona ameridhika.
Akaandika jina la Naya mwisho kabisa ya ile kazi kisha Naya akamuona
akajitumia. “Nakushukuru Joshua.” “Karibu japo naona umeshakuwa mtaalamu!”
Akampongeza. “Nina mwalimu mzuri je!” Joshua akacheka akisimama. “Inatosha kwa
leo. Tuondoke hapa.” “Bado kitu kimoja.” Naya akarudi kukaa.
“Unakumbuka
kusikia kuna suluhisho nililifikiria?” “Nakumbuka. Na ninakuomba kitu kimoja.
Usimuonyeshe mtu yeyote hata Jamal, mpaka nitakapo kwambia. Itoe kabisa kwenye
komputa ya hapa kazini, jitumie kwenye email yako ambayo sio ya hapa. Kisha
futa ili ikabakie kwenye hiyo kompyuta ya nyumbani tu. Nina sababu yangu.
Nitakwamwambia tukifika kwenye gari.” “Sawa.” Naya akafanya kama
alivyoelekezwa, akafunga kompyuta, kisha wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa
kwenye gari Naya akamuomba Joshua ampitishie madukani mara moja. “Hujachoka
tu?!” “Ni kitu nimejiambia ni lazima nifanye leo.” Joshua akampeleka mpaka
Mlimani City kwenye mall. “Sasa wewe usiingie. Nisubirie kwenye gari.” “Ndio
nini Naya!?” “Joshua! Nataka niende mwenyewe.” “Basi tuingie wote, mimi
nitakuwa nikisubiria nje ya kila duka utakalokuwa ukiingia.” Naya akafikiria
kidogo kisha akakubali, wakashuka wote.
Na kweli
Joshua akasubiria nje. Lakini kwa aina ya duka aliloingia Naya, akajua ameenda
kumnunulia na yeye zawadi, asijue ni nini. Lilikuwa duka la kiume, tena la bei.
Na kwakuwa alishamwambia havai vitu vya hadhi ya chini, Joshua akajua
itamgharimu, ila akamuacha tu. Akatulia nje kama mlinzi. Baada ya muda Naya
akatoka na mifuko miwili. Joshua akacheka. “Nikupokee?”
“Hujachungulia nikiwa ndani?” “Mimi ni mwaminifu Naya.” “Sawa. Basi twende.”
Wakarudi garini.
Mapenzi.
Walipofika
tu garini Naya akaanza. “Hizi ni zawadi zako. Zipo mbili. Moja ya kuwa mpenzi
mzuri. Unayenipenda na kunitanguliza mimi katika kila jambo. Nimeona, na
ninataka kukwambia nathamini sana hiyo.” Naya akaanza kulia, Joshua
hakutegemea. “Usilie sasa.” “Hakika unanipenda
Joshua. Katika kila fujo upo na mimi kama Naya, unanijali vile ninavyojisikia,
kitu ambacho sijawahi pata kwa mwanaume yeyote hapa duniani! Unajali hisia
zangu kwanza. Nakushukuru na usije kubalika.” Joshua akacheka sana.
“Yaani hizi shukurani zimejaa na vitisho!” “Mimi sikutanii bwana.
Uendelee kunijali hivyohivyo hata tukiwa wazee au na watoto, mimi nibakie
wakwanza.” Joshua alicheka sana mpaka akapiga makofi. Naya akajifuta
machozi.
“Na hii
ya pili ni ya kuwa mfano wangu wa kuigwa. Unaniongoza vizuri.” “Kweli Naya!?”
“Kabisa Joshua. Kwa muda mfupi tumekuwa wote hata nyumbani wanaona mabadiliko.
Nakua kimawazo. Na kazini pia unanijenga. Isingekuwa wewe, mimi leo ningeacha
kazi.” Joshua akakunja uso. “Kweli Joshua. Mimi sehemu za fujo siziwezi.” “Hata
siku moja, mwanadamu asikuondoe sehemu Mungu aliyokuweka.” “Unaelewa sasa kile
ninachozungumzia? Hayo maadili mimi sikuwahi kuyafanyia kazi. Ndio maana
nakushukuru na ndio maana hata nyumbani wananishangaa. Hii leo tu, kama
usingekuwa wewe haupo na mimi, baba angekuwa kwenye simu siku nzima nikimlilia.
Lakini najihisi nampumzisha. Hata yeye ataweza kufanya mambo yake sio kunifuata
nyuma kila wakati na matatizo yangu.” “Yetu. Sasa hivi kila kilicho
chako ni chetu.” “Nakushukuru Joshua.” Akamkabidhi ule mfuko.
“Kabla
sijafungua na kuangalia kilichopo ndani nataka ujue nimefurahi sana kukusikia
ukiona uzee wako na mimi. Au watoto wako, mimi ndio nikiwa baba
yao.” “Sasa wewe ulifikiri nani atakuwa baba yao?!” “Sijui Naya! Wewe ni mzuri
sana na bado mdogo. Upo na nafasi yakuendelea kuchagua.” “Hapana Joshua. Naomba
Mungu hilo eneo niwe nimefunga na wewe.” “Kweli unaomba au ni usemi tu?”
“Hakika naomba Joshua. Tena nakuombea wewe ndio uwe wa mwisho. Hili zoezi la
mapenzi linachanganya Joshua! Na uzuri wowote unao uona kwangu, sijawahi
kuthaminiwa hivi kama wewe unavyonithamini. Hebu niambie Joshua, wewe
utajisikiaje, tunakuwa kwenye mahusiano, halafu unasikia nakuwa na
wanaume wengine, nalala nao tu hovyo halafu narudi kwako kila wakati
nakuomba msamaha na kukwambia lakini nakupenda, ila naendelea tu kulala nje
hovyo?” “Vibaya.” Joshua akajibu.
“Hapana
Joshua. Vibaya haijaweza hata kueleza hiyo hisia yake. Ni mbaya! Hakika
niamini mimi ni hisia ambayo hutaki mtu apitie. Unajiona hutoshi. Huwezi.
Upo na kasoro. Huwezi kumtosheleza ndio maana anakwenda kutafuta kwa
wengine. Inaathiri utu kuliko nitakavyokwambia. Kila anayekutizama unajua
anakudharau, zaidi marafiki wa karibu wanao wafahamu nyinyi wote wawili na
wanayajua maisha machafu ya mwenzio! Huna ujasiri hata mbele yao! Lakini
kwako nalala nikijua nikiamka kesho, bado Joshua yupo na hakutakuwa na
sifa mbaya. Imeniongezea ujasiri na imekuwa kama dawa inayoanza kunitibu
taratibu.” “Mimi sitakubadilikia Naya. Kwanza nitamkosa Mungu wangu na
mimi sina mpango wa kukosana na Mungu wangu. Nayajua maisha bila Mungu. Huko
sirudi. Wewe niombee tu niishi maisha marefu.” “Nitazidi kukuombea.” Joshua
akafungua huo mfuko akicheka.
“Akatoa
tai nzuri sana. Naya alipomuona anacheka baada ya kuishika, akajua ameipenda.
“Nakushukuru sana. Ni nzuri.” “Nimefurahi kama nimepatia.” “Sana. Itaendana na
mavazi ninayovaa ofisini.” Akaongeza akiangalia ndani. Akamuona anacheka. “Kila
ukinywa chai au kawahawa, uwe unamkumbuka Naya.” Joshua akacheka sana baada ya
kusoma. ‘My Heart Is Whenever You are’ Ndio maneno yaliyokuwa
yameandikwa hapo juu ya hicho kikombe. “Kwa hiyo moyo wako upo popote
nilipo?” Joshua akauliza akicheka. “Ndio ramsi. Najifunga kwako tu
Joshua.” “Daah! Mungu anipe nini Joshua Kumu!? Asante sana Naya. Na ninakuahidi
sitakuumiza.” Akafungua mlango. Naya akashangaa anatoka.
Akaenda
kufungua mlango pale alipokuwa amekaa, akaanza kumbusu ila kwa heshima bila
kuvuka mipaka. “Naomba tukasherehekee kumpongeza Joshua, kupata mwanamke wake
peke yake.” Naya akacheka. “Hivi tulivyo!?” “Hivyohivyo.” “Na hizi nguo za
kazini!?” “Ndio siku Mungu wangu amenitendea muujiza wangu. Nifanyaje?”
Naya akacheka. “Shuka twende.” Naya akashuka garini. “Lakini acha nimpigie simu
baba nimtaarifu nitachelewa kidogo.” “Sawa.” Naya akazungumza na baba yake kwa
kifupi tu, wakatafuta mahali pakula hapohapo kwenye moja ya migahawa ya Mlimani
City.
Wakaka na
kuagiza. Ukweli haikuwa siku ramsi, siku ya kazi tu, lakini walipata wakati
mzuri sana. Mtulivu. Wao wenyewe, japokuwa walizungukwa na watu wengine, lakini
kila mmoja wao akili ilikuwa kwa mwenziwe. Joshua akakuza maneno ya Naya kana
kwamba ameapiwa kanisani mbele ya kadamnasi! Naya alimuona vile alivyofurahia
na kuonyesha kwake ni jambo kubwa sana. Walimaliza kula ndipo wakaondoka kurudi
nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakiwa
njiani Joshua akaanza kuimba wimbo wake wa ‘Great is your Mercy towards
me’. Joshua aliimba mpaka Naya akasisimkwa mwili tena kana kwamba huo
wimbo anausikia kwa mara ya kwanza. “Joshua wewe ni mwimbaji sana!” Joshua
akaendelea kuimba, kumbe alikuwa na cd yake hapo kwenye gari. Akaiweka, ndipo
Naya akawasikiliza vizuri hao waimbaji wa huo wimbo. “Kumbe wakiimba wengi kwa
sauti tofauti tofauti inavutia!” “Inakosekana sauti yako tu!” “Wewe unaimba
sana Joshua mpaka unaogopesha!” “Usiogope. Naomba shika tu maneno kisha jaribu.
Sitajali utakavyosikika. Ila nitapenda tukija kuimba wote.” Naya akacheka
akifikiria. “Nakuahidi itavutia zaidi ya hivi unavyonisikia mimi.” “Sawa. Basi
nipe muda.” Wakaendelea na safari yao.
“Nikuulize
kitu Joshua?” “Karibu.” Naya akatulia kidogo, Joshua akamtupia jicho na
kurudisha barabarani alipokuwa akiendesha. “Itakuaje juu ya Njama?” “Kwanza
unajua walimpeleka polisi?” “Joshua!” “Kweli. Ni kama wale askari na wenyewe
walikuwa na hasira naye. Nilisikia aliwatukana kabla ya leo. Kwa hiyo na
wenyewe ni kama wamemkomoa. Amejiharibia sana Njama. Hawezi kuja kuajiriwa kwa
urahisi. Maana hata ofisi za mwajiri kwenyewe ameharibu. Nasikia aliwajibu
vibaya sana viongozi wake. Sasa hayanihusu mimi, ila ninachojua, hatarudi kuja
kufanya tena kazi chini yangu. Kwanza siwezi kuja kumuamini tena.” “Sasa nani
atafanya kazi zake?” Naya akaendelea kudodosa.
“Si
utalemewa sana!?” “Ile nafasi yake niliitengeneza tu mimi mwenyewe tena kwa
kugombana sana na haohao aliowatukana huko ofisi za mwajiri.” “Walimkumbusha
siku ya kikao.” “Kwa hiyo haikuwa ramsi. Kwa kuwa niliitengeneza mimi mwenyewe,
nimeshajua chakufanya.” “Unamchukua Jamal?” Naya akadodosa zaidi. Akamsikia
akisema, “Mmmmhhh...” Huku akifikiria kama ambaye anapingana mawazoni. “Njama
alifaa kwenye ile nafasi.” Naya akawa kama amemuelewa.
“Nilitaka
mtu mwepesi. Sijui kama unanielewa?” “Nafikiri nakuelewa.” “Yeah. Nilitaka mtu
kama Njama, ambaye anaweza kubeba mawazo yangu kwa haraka na kuyafanyia kazi
bila visingizio. Mtu akishakuwa ni wa visingizio mara kwa mara, huwa simuwezi.”
Naya akajua hatawezana na Jamal. Jamal analalamikia sana kitengo chake. Yaani
waliopo chini yake.
“Hichi
ulichofanya wewe ndio nakitaka kukiona kwa mtu anayekuwa karibu yangu. Nikimpa
wazo, alielewe na kuzalizasha kwa haraka. Na nione matunda kwa haraka bila
visingizio. Mfano ni wewe na siku ya leo. Ungekuwa na sababu zote zakutofanya
uliyoyafanya leo. Au kutoendeleza ile kazi ya Mbeya kwa sababu kwanza hata
kiongozi wako alikuwa hakumbuki! Lakini umeenda umbali mkubwa sana na ndio
maana sikutaka umpe wewe hiyo kazi. Itamuongezea yeye sifa, na atakushikilia
ili uendelee kufanya kazi zake, yeye akipokea sifa. Sijui kama unanielewa!”
Joshua akauliza na kuendelea.
“Tunafanya
kazi kama timu. Ndicho ninachotaka. Ila hata wao huwa nawaambia na kuwapa
nafasi ya kukua huku wakionekana. Mimi si mtu wakuchukua sifa ya mtu.” “Hilo
nimesikia.” “Basi. Huwa nawaambia nilazima tufanye kazi kwa ushirikiano,
lakini...” “Shine.” Naya akamalizia, Joshua akaitika na kuendelea. “Kabisa.
Ng’aa. Tujue kwamba kitengo cha masoko kinafanya kazi nzuri sana, lakini yupo
anayekwenda mstari wa mbele, anachukua muda wakufikiria na kufanya jambo la
kufanikisha timu nzima. Na huwa kila mwisho wa mwaka natoa award. Zawadi
kwa waliofanya jambo kwenye kundi, tena naalika kabisa wakubwa ili wawatambue
kwa sababu na mimi nimekua. Kutoka sehemu moja mpaka hapa. Kazi zangu
zilionekana. Sikubahatisha na ninajua tupo pamoja ila kila mmoja amejaliwa na
Mungu kwa namna yake. Sina...” “Tamaa na vitu visivyo vyako.” Safari hii Naya
akamfanya Joshua acheke.
“Naya!”
“Nakwambia mimi nakujua Joshua kabla sijakutana na wewe! Ndio maana hujawahi
kufika nyumbani na kunisubiria, wakati wote unanikuta nipo tayari. Maana
niliambiwa Kumu anausemi wake wa, ‘early is on time, on time is late,
late is an exceptable’ usemi wa Kumu huo.” Joshua akacheka sana.
“Wanakunukuu kila mahali mpaka kule uzalishaji wanajua. Kumu akikwambia anataka
bidhaa tarehe 15, basi ukitaka umfurahishe, hiyo bidhaa ikamilike kabla ya hiyo
tarehe.” Joshua akazidi kucheka.
“Nina
shida ya kusubiri. Itabidi unizoee tu. Nikishajua kitu kinawezekana, ni changu,
mimi natakiwa nichukue hatua, huna jinsi ya kunibadilisha hapo.” “Niliambiwa
kuna wakati ulihamishia ofisi kule uzalishaji, mpaka ikabidi uongozi mzima
uingilie kati, walikuwa wakifanya kazi masaa 24, bila kupumzika ili
kukukamilishia.” “Na niliuza bidhaa huo mwezi, mpaka walishangaa. Imeingia
kwenye historia ya hapa.” Akajisifu. “Hongera Joshua.” “Ni Mungu. Sasa ndio na
wewe. Japokuwa upo ngazi ya chini, hakikisha unang’aa na usikubali mtu
akachukua sifa yako. Hata kama nikiongozi, kama hii kazi ya leo.” Naya akawa
hajaelewa.
“Baada
yakusoma hii kazi uliyonionyesha sasa hivi, ndio nimegundua kazi aliyoniletea
Jamal haikuwa yake ila ni yako.” Naya akatulia kidogo. “Lakini yeye ameileta
kwangu akionyesha mlifanya naye!” “Laptop yake Njama aliiharibu ndio akasema
tulete yangu. Imekaa vizuri.” “Jamal anajua kama nikitoa kazi, nataka majina ya
wahusika wote. Ameandika jina lake tu bila kukuweka na wewe.” Naya akashangaa
sana. “Sasa kwa nini amefanya hivyo?! Wakati hakufanya chochote!?” “Ndio maana
nataka uongeze umakini ukijua mwanadamu ni kiumbe hatari sana. Na ni mzuri sana
kutumia mwanadamu mwingine kujinufaisha.” Joshua akaendelea.
“Mara nyingi
watu hupenda watu wanao nufaika nao. Jamal anakupenda sana na anakutetea kila
mahali. Lakini kwa kuwa pia unamfanikishia mambo yake. Amepunguza kelele kwa
kuwa anajua wewe upo kufanya kazi za kitengo kizima, yeye akifanya mambo yake.
Huzungumzi, hulalamiki, kwa hiyo sifa zote ni zake. Kitendo cha kutoweka
jina lako kwenye ile kazi ndio kimenishangaza. Nilimuhisi tu kwa kuwa kazi zake
huwa nazijua, hana uwezo wa kuandaa kazi kama vile. Nilipoona tu ile nikaitilia
mashaka, kama ni wewe au kweli ni yeye amebadilika. Kwa hiyo ongeza umakini
kwenye kazi zako. Na hilo nitalirudia tena kwa wote ili ajue hata nyinyi wageni
mnajua. Wasiwatumie tu.” Naya akatulia na wakawa wamefika nyumbani kwao,
akashangaa geti lipo wazi.
Malon.
“Kutakuwa
na mge...” Naya akasita baada ya Joshua kuingia mpaka ndani na kuona aina ya
gari iliyokuwepo hapo nje ya nyumbani kwao. Joshua akamwangalia. “Ni Malon?”
Naya akainama kama anayefikiria. Joshua akajua kama ni yeye. “Sina haja
yakuingia ndani. Naweza kukushusha tu, nikaondoka ili kukupa muda na mgeni
wako. Nimekuahidi kukusubiri Naya, mpaka utakapokuwa tayari. Sitabadilika.”
“Sihitaji muda mbali na wewe Joshua.” Joshua akacheka kidogo akionekana hilo
limemfurahisha. “Twende wote ndani ili na wewe umsalimie.” “Unauhakika kama upo
tayari Naya?” “Nilimaanisha kila neno nililokwambia pale Mlimani City, Joshua.
Sitabadilika kwa kuwa unanipa sababu zote zakutobadilika. Twende wote.”
Hapo Joshua akashuka kijasiri.
Naya
akachukua zawadi aliyokuwa amemnunulia baba yake, akashuka nayo pamoja na pochi
yake. “Nikusaidie?” “Hapana. Nipo sawa tu.” Wakaongozana wote kimya. Naya
akaingia yeye wa kwanza. “Karibu Joshua.” Akamkaribisha akiwa ndani macho nje.
Watu wa ndani wote wakawageukia wao. “Shikamoo baba.” Akaanza Naya, na Joshua
naye akamsogelea na kumsalimia. “Naona umegeuzwa dereva!” Joshua akacheka.
“Hapana mzee wangu. Tukiwa kazini tunakuwa na mambo mengi, hata kuonana ni
shida. Huu ni muda wa pekee ndio tunapata humo barabarani.” Akajibu Joshua kwa
heshima.
Akamsikia
Naya amemsalimia Malon, Joshua akawageukia. “Mimi mzima, mama. Nimekuja kukuona
tu. Nilikuwa Mbeya wakati tukizungumza. Nikajua leo ungepumzika!” “Nilitumia
zile dawa ulizoniambia, naona zimenisaidia. Nashukuru kujali.” “Karibu na
afadhali. Nimeleta na heating pad.” “Nilikwambia usisumbuke Malo!” “Kwamba
umeshanunua?” Malon akauliza. “Bado lakini nitanunua.” Joshua kimya
akisikiliza. “Sasa kuna sababu gani ya kununua ingine na wakati hii ipo hapa na
mimi situmii! Hata kama maumivu yameisha, unakumbuka ilivyokuwa ikikusaidia?”
“Nakumbuka.” Naya akajibu kwa hofu kidogo. “Basi itumie tu na kuitunza kwa
kipindi utakachohitaji. Unakumbuka kunywa maji yakutosha lakini?” “Malon, huyu
ni Joshua.” “Namfahamu Naya. Ulinitambulisha tulipokuwa Mbeya. Au umenisahau?”
Akamgeukia Joshua na kumuuliza kiungwana tu.
Baba
Naya, Bale na Zayoni kimya wakisikiliza. “Japokuwa siku ile hapakuwa na
utambulisho ramsi, lakini bado na kukumbuka.” Akajibu Joshua. “Joshua huyu ni
Malon, nafikiri nilikwambia juu yake. Malon, huyu ni Joshua. Mpenzi
wangu.” Naya akaingilia na kutoa utambulisho zaidi. Pakazuka ukimya kidogo.
Naya akamgeukia baba yake. “Nina habari njema.” Akamshika na Joshua. Baba yake
akacheka. “Nini?” “Hapa unaponiona mimi, ni muajiriwa kamili wa Coca, na
mshahara mpya.” Baba yake akacheka tena. “Pongezi sana mama yangu mzazi. Na
asante sana Joshua najua na wewe unachangia.” “Hata kidogo mzee wangu. Yote ni
Naya mwenyewe. Mimi mwenyewe najihisi nimebahatika! Naya anaakili sana. Bado
anashangaza watu pale. Kwa hiyo kwa asilimia 100 ni yeye na Mungu wake.” Joshua
akamsifia Naya wakiwa bado wamesimama.
“Na hii
ni zawadi yako baba yangu. Najua unaniombea sana. Na ulikuwa ukinisindikiza
kazini kila siku asubuhi ili niwahi.” “Na kukutengenezea maji ya moto ya kuoga
pamoja na...” “Chai.” Bale akaongezea kwa mdogo wake, Zayoni
aliyeongeza wakati Naya akimshukuru baba yake. Wakacheka. “Na mimi
zawadi yangu ya kukufulia ipo wapi?” “Na wewe Zayoni umefua siku moja tu tena
jana wakati naumwa, leo unataka zawadi! Hapana bwana.” Joshua akabaki kucheka.
“Hata
kama ni siku moja tu, lakini si amekusaidia siku ya shida yako! Ulitakiwa
kumnunulia mtoto zawadi yake, lasivyo usimfulie tena.” Naya akachukua
kandambili mlangoni na kumrushia Bale pale alipokuwa amekaa na Malon, Bale
akakwepa akicheka. “Umbea tu na kutaka kunichonganisha na Zayoni. Endelea mwaya
kunifulia Zayoni mdogo wangu, ipo siku nita...” Kila mtu akazidi kucheka. “Ona
anavyomrubuni mtoto! Hakuna kumfulia tena mpaka zawadi.” “Hayakuhusu Bale.” “Na
hivi nimerudi mwenyewe, labda Malon anichukue twende naye.” “Afadhali. Tena
ondoka naye sasahivi. Wenyewe tulikuwa na amani! Sijui kwa nini hujafeli huko
chuo ukarudia hata miaka mitatu tena!” “Majibu bado mama. Ila dua la kuku
halimpati mwewe. Nishamaliza, nipo mtaani na wewe. Mtetezi wa Zayoni nimerudi.
Ndio maana mtoto amekonda!” Wakaanza hao wawili kubishana mpaka karibu Naya
aanze kulia.
“Haya,
Bale nenda. Toka hapo.” “Sasa mimi nimefanyaje baba jamani!?” “Nenda Bale.
Unamliza mwenzio wakati amekuja na habari njema hapa!” “Zakutaka kumwonea mtoto
tu!” Naya akakaa pembeni ya baba yake akaanza kulia, Joshua akiwaangalia ndugu
hao, Malon alishawazoea.
“Mimi
naondoka humu ndani kama Bale ndio amehamia hapa rasmi.” Bale
akazidi kucheka na kurudi. “Akiondoka Naya, nachukua chumba chake.” Naya
akamrushia tena kiatu, Bale akakwepa. “Naenda kukufungashia mizigo yako.” Naya
akazidi kulia. “Mimi nakwambia kila siku, usimsikilize huyo anaishia kukuliza,
ona sasa.” “Mimi sijui kama nitakuja kuolewa humu ndani jamani!” Naya
akalalamika akilia. Wote wakacheka. “Twende zetu Joshua
wangu.” “Sasa mwenzio mbona humpi chakula? Bale amepika...” “Sitaki
chakula cha Bale. Kinaweza kumkaba Joshua wangu bure!” Bale
akasikika akicheka ndani. “Joshua alikisifia sana chakula changu.” Bale akajibu
akiwa chumbani. “Alikuwa muungwana tu. Toka hapa. Chakula chako kibaya tu.” “Nimekwambia
usimjibu.” Baba yake akamuonya. Bado Joshua alikuwa amesimama hata hakuwa
amekaa.
Naya
akasimama na kujifuta machozi. “Twende Joshua wangu. Watu wa humu ndani...” “Ni
wema sana na ...” “Toka zako Bale.” Naya na yeye akamkatisha, wakamsikia Bale
akizidi kucheka. “Nikujie na mizigo yako yote? Ili ukitoka ndio iwe moja kwa
moja?” “Baba unamsikia Bale lakini?” “Bale wewe ndio
unakaribia kuondoka usiku huu.” Hapo Naya akafurahi. “Au baba umfukuze, japo
kwa huu usiku tu wa leo sisi tufurahie ajira yangu?” Wote wakazidi kucheka.
“Mimi nanyamaza baba. Atakayeongea tena ndio atoke.” “Nyinyi hamuoni hata aibu
mbele za wageni jamani!?” “Namshangaa Naya.” “Mfukuze baba. Alisema mwenyewe
atakayezungumza ndio aondoke. Hii nyumba ilikuwa na amani kabla halijamaliza
chuo. Limerudi na kuanza fujo! Sijui yukoje Bale! Twende zetu Joshua.” Bale
akazidi kucheka.
“Wakataka
kutoka, Naya akawa kama amekumbuka. “Malon asante kwa kuja kuniona na vitu
ulivyoniletea, lakini hapana.” Naya akarudi mpaka pale alipokuwa amekaa
Malon na Bale, kwenye meza ya chakula. “Nakushukuru. Ila nataka nianze
kujitegemea na kujifikiria mwenyewe. Umenisaidia vyakutosha. Sasa basi.”
“Unakunywa maji lakini? Macho yanaonekana yamechoka na midomo imekukauka.” “We
Malo! Hivi unanisikia chochote ninachoniambia?” “Na wewe unanisikia chochote
ninachokuuliza?” “Mimi nakusikia ila sitaki kukujibu.” Wakamsikia Bale
akicheka huko chumbani. Naya akatulia akiangalia mlango alipokuwa ameenda Bale
kisha akaendelea.
“Kwa hiyo
hunywi maji ya kutosha na ninajua utakuwa umetapika sana.” “Naya anakunya maji,
na hata hapo kwenye gari ameacha maji ya chupa niliyokuwa nimempa. Na
alipotapika sana, nilimpeleka hospitalini akawekewa maji yakutosha tu.” Akajibu
Joshua. “Kwa hiyo swala la unywaji wake maji usiwe na wasiwasi nalo.
Anazingatia.” Pakazuka ukimya kidogo.
“Labda
nikuulize Joshua. Kuna tatizo gani kwa Naya kupokea kitu chochote kutoka kwangu
hasa akiwa yeye hana hicho kitu?” Naya akashituka mpaka akatoa macho.
“Tafadhali naomba usianze na Joshua! Tafadhali sana Malon! Joshua ni mstaarabu
sana sio kama...” “Mbona ni swali dogo tu Naya?! Kwa nini unanigombesha?” “Wewe
tulipokuwa wote ulikuwa ukikubali nipokee vitu vya wanaume wengine?” Naya
akamuuliza.
“Tena
ulikuwa mkali hutaki hata nizungumze na mwanaume mwingine kama wewe haupo
wakati ulijua mimi sio muhuni! Haki yakumuhoji Joshua wewe unaipata wapi?
Naomba muache Joshua.” “Mimi sijauliza kwa ubaya Naya. Maana uliniambia hata
gari umenirudishia sababu umeanza mahusiano na Joshua! Nikajua wazi yeye ndiye
anayekukataza. Sasa nikajiuliza huyu Joshua anayepokonya usafiri mmoja tu wa
familia, anataka nyinyi hapa muishije! Najua wewe anakusaidia usafiri. Na
wengine!?” “Naomba Malon uondoke.” “Usinifukuze Naya. Nipo pia hapa kuzungumza
biashara na Bale. Na wala sifanyi fujo. Hata kama utaolewa na Joshua, mimi ni
kama mtoto wa humu ndani tu. Hapa ni nyumbani, huwezi kunikwepa.” “Bora
nisingewahi kurudi hapa ndani.” Joshua akarudi.
“Hapana
Naya. Wala usilie. Njoo.” Akamvuta karibu na kumshika mkono. “Sijitetei, lakini
najua tunatofautiana kimaadili. Wewe sijui umekuzwa vipi, tunaweza kutofautiana
makuzi. Lakini mimi kama mimi, sipendi kusaidiwa majukumu yangu.” “Kusa...”
“Tafadhali naomba nimalize.” Malon akataka kumkatisha, Joshua akawa muungwana
tu. “Sasa hivi Naya ni wangu na ni jukumu langu pia. Nafikiri mimi ndiye
ninayetakiwa kumtunza Naya nikijua bado ni binti ya mtu na anaishi na mzazi
wake. Sitavuka mipaka na wala sitamuacha Naya akateseka. Na kwa kifupi tu
Malon, sitafanya kwa mashindano na wewe au mtu mwingine yeyote yule, ila ni kwa
kuwa nampenda na kumfikiria Naya. Sitaki kumtesa, ila tupo kwenye kujenga msingi
wetu mimi na yeye. Kwa kile Mungu atakachotujalia, tutajenga. Sisi
wawili, tukimtumainia Mungu bila mkono wa mtu mwingine yeyote yule. Hata kama
tunaanzia chini sana, tena kwa kuhangaika, lakini itakuwa ni msingi wangu mimi
na Naya. Tutavumilia huku tukimwamini Mungu kwa baraka zaidi.”
“Kwa hiyo
Malon, kama alivyosema Naya, tunashukuru sana kwa misaada yako, lakini, hapana.
Ulishapata hiyo nafasi. Na kwa maelezo ya Naya, uliitumia vizuri sana hiyo
nafasi bila ubahili. Lakini Mungu amemtoa Naya kwako, amenikabidhi mimi
kwa upendo kabisa. Nikiwa simstahili Naya, Mungu amenipa. Najua mengine Mungu atatuwezesha
tu. Ameniambia alizungumza na familia juu ya swala la gari, wakaelewa.
Ipo siku mimi na Naya tutakuwa msaada kwa familia, lakini sio kwa kukutumia
wewe. Ni hilo tu.” Joshua akawafunga wote midomo, Naya akafurahi sana.
“Twende
Joshua wangu.” “Usiku mwema wote. Mzee wangu!” Joshua akamgeukia kwa heshima.
“Mimi nikitoka, ndio nitakuwa nikitoka moja kwa moja mpaka tena kesho.” “Asante
sana Joshua. Nakushukuru kwa hiyo kazi ya kuja kumchukua na kumrudisha huyu. Ni
kweli inampunguzia usumbufu.” “Itaisha tu mzee wangu. Nimemuagizia gari yake,
itachukua kama majuma matano mbele, lakini itafika tu.” Wote wakashangaa mpaka
Naya mwenyewe akashangaa. “Umemuagizia aina gani ya gari!?” Bale akatoka
chumbani kwa haraka. “Nafikiri bado ninazo picha zake hapa. Hata Naya mwenyewe
sikuwa nimemwambia. Nilitaka iwe suprise.” Joshua akatoa simu yake
mfukoni.
Mpaka
Naya mwenyewe akasogea karibu kuona picha. “Kweli Joshua!?” “Kweli. Niliiagiza
Japan siku ile tu tuliporudi kutoka kuendesha boti. Usiku. Acha nikuonyeshe.”
Na Zayon akasogea. Joshua akaperuzi kwenye simu yake, akapata. “Hii hapa.”
Akamkabidhi simu Naya. “Mungu wangu Joshua! Hii gari ni kama hiyo ya Malon hapo
nje sema..” Naya akabaki ametoa macho. “Uliniambia unapenda aina hizo za magari
ila unahofia mafuta.” Naya akamwangalia Joshua kama asiyeamini, Bale
akampokonya ile simu. “Hii ni ya kijivu inayong’aa vizuri!” Akasifia Bale.
“Tuone.” Baba yake akataka kuona na yeye, Bale akamsogelea baba yao kwa karibu
na kumuonyesha. “Ni nzuri sana.” Akasifia.
“Sijui
hata niseme nini Joshua! Sikuwa najua!” “Tuombe Mungu ifike salama wasiibe vitu
vya ndani. Ni ya kisasa. Inavitu vingi sana, vipya na vya kisasa, tekinologia
mpya. Nina uhakika utaifurahia tu.” “Nakukushukuru hata kutufikiria tu.
Hivyo itakavyokuja, vyovyote vile, pia nakushukuru sana.” “Karibu.” Naya
akabaki akimwangalia kama haamini. Joshua akacheka. “Ila usingeagiza ya aina
hiyo! Siitakuwa gharama sana!” “Wewe ndio hustahili vya gharama?” “Si kwa kiasi
hiki Joshua! Halafu huku mbali na...” “Acha woga Naya.” Joshua akamtuliza,
Malon kimya kwenye meza macho kwenye simu yake. “Na mimi utanifundisha
kuendesha?” Zayon akauliza. “Ukifikia umri wa kuendesha nitakufundisha Zayon.”
Bado wote walikuwa kwenye mshangao, hapakuwa na utani. Bale akachukua tena ile
simu kutoka kwa baba yake, akabaki akingalia lile gari.
“Bale kwa
kupenda magari! Mrudishie simu yake arudi kwakwe, akapumzike.” Baba yake akamshitua
Bale, akacheka na kumkabidhi simu Joshua. “Isee hiyo gari nzuri sana.
Hongereni.” “Asante.” Naya akajibu kwa haraka na cheko akimwangalia Joshua.
“Nimefurahi!” Joshua akacheka taratibu kisha akaaga tena, ndipo wakatoka.
“Kwa nini
hukuniambia Joshua!?” “Leo nimeropoka tu. Sikutaka nikwambie mpaka ifike. Ila
ndio ujue muda wetu wa njiani utapokonywa.” “Kweli bwana. Tutarudi kwenye
simu.” “Sio sawa na kuwa pamoja kila asubuhi na jioni.” Wakawasikia Naya na
Joshua wakizungumza hapo nje, mwisho sauti zikaanza kusikika kwa mbali, wakajua
anamsindikiza garini.
“Nimefurahi
ulivyoweza kutulia na kumjibu vizuri Malon! Kweli Mungu amekujalia hekima
Joshua. Malon ni mkorofi sana. Ungemjibu vibaya pale, angekubadilikia!” “Kidogo
ameniudhi. Alikusudia kuniharibia pale kwenu na ndio maana niliamua tu kusema,
nikihofia gari isije kuja, nikaonekana nilinunua sababu ya maneno yake ya leo!”
“Pole Joshua wangu. Naomba sisi tuendelee kama ulivyosema pale ndani. Au kama
tulivyofanya leo kazini kwa Njama.” Joshua akavuta pumzi kwa nguvu kama anayejaribu
kutulia. “Nenda kapumzike. Mimi nikitoka kuoga, nitakupigia kama bado hujalala,
tuzungumze kidogo.” “Basi nitakusubiri mpaka unipigie.” “Basi acha nikaoge
halafu nikupigie.” Joshua akaondoka, Naya akarudi ndani akiwa ametulia kabisa.
“Umependa
zawadi yako?” “Nimebaki nikiingalia tu hii saa.” “Umeipenda?” “Sana. Naona na
Bale ameomba niwe namuazima.” Naya akacheka. “Kama umependa, nimefurahi.” “Sasa
si utakuwa ukiishiwa pesa yote mama yangu! Usinunue vitu vya gharama hivi!”
“Nataka na wewe uonje matajiri wanavyojisikia baba yangu.” “Na mimi
nataka kuonja matajiri wanavyojisikia.” Zayoni akaongea kwa kulalamika na
kufanya wacheke. “Haya vaa hii saa mpaka unapokwenda kulala ndipo unipe.” Baba
yake akampa hiyo saa, Malon akiwa ametulia kimya hapo mezani, Bale akamsogelea
kumalizia mipango yao. Naya akapitiliza chumbani bila kuwasemesha tena, ila
akajua Malon amekasirika sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Hakuwahi
kupenda kupitwa. Na yeye ndiye alijithaminisha kuwa aliwekeza kwa Naya kwa
viwango vya juu sana, hakuna mwanaume anaweza kufika hapo. Ndio maana aliingia
na kutoka kwenye maisha ya Naya vile anavyojisikia yeye, akijua hakuna mwanaume
anaweza kufikia hicho kiwango alichoweka kwa Naya. Sasa anatokea Joshua, mwenye
sifa zote za mama Naya, tena nakupitiliza! Anajielewa! Sio mbambaishaji!
Anamipango ya kueleweka! Ndio kwa mara ya kwanza anatokea mwanaume kwa Naya,
Malon anakosa mwanya. Naya alikuwa akimcheka moyoni kwani alishamwambia
hatakuja kupata mwanaume kama yeye.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaelekea
kuoga kwa haraka, alipotoka tu bafuni, bluetooth sikioni, wakamsikia
akizungumza. “Bado sijafika.” “Pole. Basi acha
nikusindikize mpaka nyumbani.” “Nashukuru.” Joshua akajibu,
maongezi yakaanza katikati yao, Naya akiwa amejawa furaha yakupitiliza. Gari ya
nguvu inakuja! Alijawa furaha sana. Na kitu kingine kikajengeka kwa
Joshua. “Joshua ananifikiria sana!” Akawaza Naya na kuanza
kumsihi Mungu awasaidie kitu chochote kibaya, kisitokee katikati yao. Wakaagana
baada ya masaa kadhaa mbele. Alimsubiri mpaka alipokuwa tayari na yeye kuingia
kuoga. Ndipo wakaagana.
Naya akaona haitoshi. Akamtumia na ujumbe. ‘Nakushukuru kwa kuweza kunifikiria na kuniweka mimi mbele ya hata vitu nilivyovikuta ni vya muhimu kwako, Joshua. Asante sana na Mungu azidi kukubariki. Usiku mwema.’ Joshua anatoka bafuni, akakutana na huo jumbe. Akakaa na taulo kiunoni. Akasoma ule ujumbe kwa kurudia. Akajisikia faraja kuona Naya anatambua juhudi zake. ‘Nakupenda Naya. Nilikuwa nikimsihi Mungu atuepushie majaribu. Chochote kisitokee katikati yetu na kututenganisha.’ Naya aliposoma tu, akampigia. “Nilijua umeshalala!” Joshua akashangaa wakati akipokea simu ya Naya. “Nimeanza kusinzia. Kichwa kimechoka sababu ya fujo za leo, ziliniingia akilini. Lakini nimetaka kukwambia na mimi nimeomba hivyohivyo. Mungu atusaidie, chochote kisitokee katikati yetu.” Mazungumzo yakaanza tena kwa wapenzi hao, Joshua kwa ujasiri wote akiwa ameshatambulishwa mpaka kwa Maloni kuwa ni mpenzi, na baba Naya kuendelea kumshukuru mbele ya Malon akiwa hata hajui kama kuna gari imekuja.
Siku Inayofuata.
Alamu
ilimuamsha Naya hata asijue Joshua alikata simu saa ngapi, na kama Malon
aliondoka muda gani. Akacheka akifikiria kama na usiku huo alikoroma, Joshua
akimsikiliza. Akajitayarisha kwa haraka wakati baba yake akimtayarishia
kifungua kinywa ambacho huwa kinamsaidia sana. Mara nyingine anashindwa hata
kula mchana au kabla ya kuja Joshua kwenye maisha yake, alikuwa akibania pesa.
Badala yakula kazini mchana, akipata hicho kifungua kinywa, ni mpaka arudi kula
hapo nyumbani. Alijua kwa hakika pesa yake inategemewa sana hapo nyumbani kwao,
hakuruhusu matumizi yasiyo lazima hata kidogo.
“Naona
Bale ameamua kufanya biashara na Malon.” Baba yake akajaribu kutupia neno
wakati Naya akila. Naya akatulia bila ya kujibu. Baba yake alijua amesikia
“Naya?” “Nimesikia baba.” “Najua umesikia.” Akatulia kidogo kisha akamgeukia
baba yake pale alipokuwa amekaa sebuleni. “Unajua ningetamani Malon asiwe
anakuja hapa nyumbani. Na wote niliwaambia baba. Lakini kwa sasa hatuna jinsi.
Tunafanya kile kinachowezekana. Bale amemaliza chuo na anatafuta
kujishughulisha. Kama Malon anaonekana kuwa msaada kwake, hata yeye
nilizungumza naye kuwa aendelee naye tu. Lakini si kitu ambacho nafurahia baba
yangu. Ila hatuna jinsi. Tunashika pale Mungu anapofungua mlango.” Baba yake
akanyamaza, Naya akaendelea kula mpaka alipoona simu yake inaita. Akajua Joshua
ameshafika nje na kugeuza gari tayari.
“Nashukuru
kwa chakula, baba Naya. Joshua ameshafika.” “Uwe na siku njema.” “Na wewe.
Nitakupigia baadaye. Ila pesa ya rangi pamoja na vitasa nimetuma sasa hivi.
Utakuta kwenye simu yako.” “Na Bale naye alihitaji pesa kidogo. Sijui kama
alikushirikisha!” “Nitampigia. Ila pesa bado ipo. Usiwe na wasiwasi.” Naya
akatoka kwa haraka. Yeye ndio alikuwa kama mtunza pesa hapo kwao. Hata baba
yake alipotoka Mbeya kikazi, alimpa yeye pesa aliyotengeneza. Akawa kama ndio
muendesha bajeti ya familia yao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua
akamuona jinsi alivyoingia akiwa usoni amepoa. Akajua kuna kitu hakijakaa sawa.
“Uliamka salama?” “Nashukuru Mungu niliamka salama.” Akajibu kisha akacheka.
“Nilikoroma?” Joshua akacheka na yeye. “Jana hukukoroma. Kwanza nimegundua wewe
sio mkoromaji. Juzi ulionekana ulichoka.” Naya akacheka. “Wewe ulilala saa
ngapi?” “Kwenye saa nne na nusu. Sikuchelewa sana. Nilikuwa nimechoka. Ila
nashukuru nilimaliza vitu vyote nilivyojipangia kufanya jana.” “Afadhali. Kwa
hiyo ulilala vizuri?” “Bila hata ndoto mpaka alamu iliponiamsha.” Naya
akacheka. “Na mimi hivyohivyo hata sikujua ulikata simu muda gani.” Wakaendelea
kuzungumza kidogo lakini kila mtu akiwa na lake.
“Nimesikia
Bale anaanza rasmi kufanya biashara na Malon!” Naya akabaki ametulia tu. Joshua
akamwangalia. “Ndiyo.” Akajibu tu hivyo kwa ufupi, wakanyamaza kidogo, ila Naya
akajua anawajibika kujieleza zaidi. “Hali ya uchumi pale nyumbani ipo chini
sana Joshua. Kwa sasa kama nilivyokwambia, wote tunategemea hii kazi yangu.
Baba amehangaika sana kutafuta biashara na kufanya biashara zingine, hata kwa
kurudia alizokuwa anauzoefu nazo imeshindika na anajikuta anapoteza tu pesa.
Bale amemaliza chuo, inamaana hata ile pesa ndogo aliyokuwa akipewa chuoni ya
mkopo, haipo tena. Cheti hakijatoka. Hawezi kuanza kuomba kazi popote. Mimi
mwenyewe nilikaa muda mrefu nikihangaika kutafuta kazi bila mafanikio.
Nimezungumza naye kwa muda mrefu sana juzi ambapo sikwenda kazini, tukafikiria
jinsi yakufanya, akaona ni heri akafanye kazi kwa Malon, kama alivyokuwa
akifanya baba, lakini na yeye ajitahidi awe anakusanya mazao na kumtumia huku
baba, auze, bila kuanza kwa mkopo mkubwa sana.” Naya akajieleza kifasaha.
“Kwa hiyo
atakuwa akiishi na Malon?” Joshua akauliza zaidi. “Ndiyo na hapana. Malon
atakapokuwa anakuwa huko mashambani, inamaana atakuwa naye. Lakini Malon huwa
anasafiri nje ya nchi mara kwa mara. Kwa hiyo atakapokuwa hayupo, inamaana Bale
atakuwa akibakia huko akikusanya mazao. Malon alimlipa baba vizuri kwa muda
aliokwenda kumfanyia kazi. Sijui kwa Bale wataelewana vipi! Lakini amesema
atakuwa huko kwa malengo. Kazi na yeye kuanzisha kitu chake akijifunza kwa
Malon. Baba amemsifia sana Malon jinsi anavyoifanya hiyo biashara, ndio Bale
anataka na yeye akajifunze kutoka kwake. Akija kupata ajira, basi amuachie
baba.” “Sio wazo baya. Mwanzo huwa unakuwa mgumu, na wakati mwingine milango
inayokuwa ikifunguliwa na Mungu sio yote inatamanisha kuingia humo, ila
inabidi tu.” Naya akanyamaza, hakujibu hilo.
Asubuhi
hiyo pakawa patulivu wakiwa wanaelekea kazini, ila wote wawili walijua kwa
hakika, hicho si kitu wanachokifurahia, ila hapakuwa na jinsi. Na hapo Joshua
alishindwa kuingilia mipango ya familia. Kwanza hata aina hiyo ya biashara
hakuwa akijua. Na hakutaka kutoa wazo la kumtafutia kazi Bale, kuhofia
kuonekana anashindana na Malon. Akaona anyamaze.
“Ungependa
kula nini mchana, ili nimwagize Jozee apike na kukuletea kazini.” Naya alikuwa
amepotelea mawazoni. “Na wewe utakula au ni kwa ajili yangu tu?” “Inategemea.
Si unajua ratiba zangu zinavyokuwa ngumu?” “Wewe ungependa kula nini?” Joshua
akacheka. “Naya! Nimekuuliza wewe.” “Hata sijui! Sasa hivi nimeshiba halafu
nina mengi nafikiria. Swala la chakula hata halipo! Kama ni kwa ajili yangu tu,
usihangaike tafadhali. Nitakuwa sawa.” “Sio usumbufu. Ndio kazi yake. Namlipa
kwa ajili ya hiyo.” “Basi naomba nifikirie.”
“Unawaza
nini sasa wakati mambo yako yanajipanga vizuri?” Joshua akamuuliza. “Kazini
umejitengenezea sifa nzuri. Mimi nipo na wewe. Nimekuahidi sitabadilika. Ni
nini tena kinakunyima raha?” “Natamani mambo yangekuwa tofauti Joshua. Asiwe
Malo.” Naya akalalamika. “Ni ukurasa ambao nilitamani niufunge kabisa. Lakini
Bale na Zayoni walitokea kuelewana sana na Malon, akawa kama kaka kwao, hata ni
ngumu kuingilia. Halafu Bale yeye sio mtu wa marafiki, ila akatokea kumkubali
Malo. Kwa kuwa Malo naye ni mtu ambaye akiamua kuwepo kwenye maisha yako,
anajali sana na anajua kumfuatiliza mtu mpaka akafanikiwa kwenye moyo wa Bale.
Sasa na yeye Malo marafiki zake walimkimbia. Najua Bale atakuwa mtu wake wa
karibu sana kitu ambacho sina jinsi ya kukizuia, na mimi namjua Malon. Alichokifanya
jana usiku pale, wala sio mwisho wake.” Joshua akakunja uso kidogo.
“Kwamba
aina ile ya maswali...” “Na kunifuatilia, hataacha. Malon hajui jibu la hapana,
Joshua. Anafanya kile akili yake inamtuma. Mimi sitaki anifuatilie tena
nyuma! Sitaki tena. Nafikiria..” Naya akanyamaza. “Nini?” “Natamani kuhama
pale, nijitegee mwenyewe, lakini baba na Zayoni wananitegemea! Au wananihitaji
sana. Kuondoka kwenye maisha ya Zayoni sasa hivi itakuwa kumchanganya. Baada ya
mama kufariki, tulihangaika sana kumfanya awe vile. Hata sijui!” Naya
akafikiria tena kidogo. “Nafikiri nitazungumza na Bale, yeye ndio azungumze na
Malon. Mambo yao wasinihusishe mimi.” “Unafikiri Bale atakubali?” “Bale
anapenda yeye ndio anilize lakini sio mtu mwingine.” Wakacheka.
“Hata kwa
mama alikuwa akinitetea sana. Na nimemuona akinitetea kwa wanaume wote
niliokwisha kuwa nao karibu, kasoro tu Malon! Nafikiri ni kwa kuwa alijua
nilikuwa nikimpenda sana, hakutaka kuingilia. Ila safari hii itabidi nizungumze
naye vizuri. Katika mahusiano yao, mimi nisihusishwe, na amwambie Malo
ni kaka yao wao sio mimi. Mimi sitaki anifuatilie kabisa.” Hapo Joshua
hakuchangia.
“Unajua
ratiba yangu umeibadilisha? Lakini ni kama nimeanza kuipenda.” “Kivipi?” Naya
akauliza. “Badala ya kufanya kazi zangu binafsi usiku nikiwa nimechoka, mida
hii ninayoanza kazi bila simu za Fina na Jema, nafanya mambo yangu pale ofisini
akili ikiwa safi! Nahisi nitaiendeleza hii ratiba. Niwe naamka alfajiri kila
siku na kufanya mambo yote. Ikifika saa 11 na nusu jioni, nafunga kazi, nakuwa
kinyumbani nyumbani tu.” Wakaendelea kuzungumza. Naya akajua ndio amebadilisha
mazungumza juu yake na Malon.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Watoto wa mtaani wameingia
nyumbani kwa baba Naya wanataka KUOA. Hakuna mwenye dalili yakutoka wala kukubali kushindwa. Wote
wanajua wanachokitaka. Malon yupo, Joshua naye yupo ndani ya nyumba na ahadi ya
kutomkimbia Naya.
Safari hii Malon amerudi kama mtoto wa familia na
mipango ya PESA kwa Bale si
kwa Naya tena kama zamani. Na hajui
jibu la Hapana na ameahidi kuendelea kuwepo.
·
Je, safari hii nayo atasimamia mipango anayoweka na Bale? Kwa umbali
gani, hasa akijua nafasi yake kwa Naya si ya kuchezea tena na milango ni kama
imefungwa? Au ataondoka tena kama kawaida yake akitoa sababu makinifu?
·
Joshua naye ameingia pichani akiwa anajua
anachokitaka na kuvunja usemi wa Malon kuwa Naya hatapata mwanaume kama
yeye! Usemi aliohangaika nao sana baba Naya kuuvunja kwa kufunga na kuomba
bila hata Naya mwenyewe kujua kama baba yake anatengua
hiyo kauli katika ulimwengu wa roho na kumuweka huru binti
yake bila ya kumuingilia maamuzi yake ila kuomba mume sahihi kwa Naya.
o
Sasa amekuja Joshua. Itakuaje?
o
Je, yeye ndiye?
o
Kwa umbali gani?
o
Au na yeye atatafuta sababu yakuondoka kama Malon anavyofanyaga
pale maji yatakapozidi unga?
·
Wote Watoto wa mtaani. Kasoro Joshua hakuvuta bangi ila na yeye pia
hajui jibu la Hapana na
mpambanaji pia. Naya ndiye amebeba hatima ya yote.
o
Nani mume wa Naya?
o
Itakuaje?
Usikose
muendelezo kujua itakuaje kwenye mchakamchaka wa Maisha unao changanywa na MAPENZi pamoja na PESA!
0 Comments:
Post a Comment