![]() |
Net akamuongoza njia mpaka hapo kitandani. “Ulikula
vizuri?” Net akamuuliza. “Nitakula tena nikiamka.” “Ulipenda supu na chakula
alichokutengenezea?” “Nimependa.” Net akashangaa safari hii maswali yake
yanajibiwa. Akamtengenezea kitanda, akapanda na kumfunika. “Asante.” Nusu Net
akae. Lakini akaona ajikaze. “Karibu. Unataka kitu chochote?” “Hapana. Nataka tu
kulala kidogo.” “Okay. Basi nitakuwa hapahapa chumbani. Ni sawa?” Tunda
akanyamaza.
“Acha nikusaidie ili upone haraka. Ukipona kabisa,
itakuwa afadhali. Lakini kwa sasa unahitaji msaada Tunda. Utajiumiza zaidi na
kushinwa kukaa na Cote. Ni sawa?” Tunda akatingisha kichwa kukubalia. “Basi
naomba ulale, unitume mimi. Nililala sana pale hospitalini, kwa hiyo najisikia
vizuri tu. Nitakuwa pale kwenye kiti.” Tunda akatingisha kichwa, akalala.
Alilala tu kama lisaa, akaamka. Akakaa kuhakikisha
amelala nyumbani, hajatekwa nyara. Net akamwangalia. “Hujalala Tunda!” “Nahisi
nimeingiwa hofu. Nahisi kama naweza kuja kuchukuliwa tena nikiwa usingizini!”
Net akasimama na kumsogelea pale kitandani. “Hii nyumba imezungukwa na polisi,
hakuna jinsi mtu yeyote akaingia humu ndani akaweza kutoka na wewe. Halafu
tumezuia wageni. Hata marafiki hawaruhusiwi kuingia humu kwa kuwa hatujui ni
nani atatumiwa kutudhuru. Kwa kifupi. Nipo mimi, Nana ambaye aliingia hapa
kukuangalia muda mfupi uliopita ukiwa umesinzia. Maya, Gino, Carter, Ms Emily
na huyu Cote. Naomba usiogope.” Tunda akajiweka sawa na kuegemea mto. Net akakaa pembeni yake.
Akamvuta mkono na kuubusu. Tunda akamwangalia na
kunyamaza. Wakatulia kidogo, akamuona Tunda anajivuta karibu yake na
kumuegemea. Net alitamani kumwambia asante. Akajikaza kiume. Akajilaza yeye
kwenye mto. Akamvuta taratibu akamlaza kifuani kwake, akamfunika na
kumkumbatia. Tunda akajipanga vizuri hapo kifuani akiwa amejilaza pembeni. Net
akambusu kichwani. Tunda akarudi kulala na Net naye akapitiwa na usingizi.
Malcom na Roy Tena.
W |
akati wao wamelala, Maya alikuwa na bibi yake sebuleni,
Carter akawaambia wapo afisa usalama wawili wanataka kuwaona. Bibi Cote
akamwambia Carter waingie. Wakaingia. Maya akatamani kucheka. Akaweka simu pembeni
na kuwasikiliza. “Huyu anaitwa Malcom.” Roy akamtambulisha mwenzake. “Na huyu
anaitwa Roy.” Malcom naye akamtambulisha Roy. Bibi Cote akajiweka sawa. Kimya
akiwatizama. “Mimi..” “Sisi.” Roy akamrekebisha Malcom.
Malcom akamgeukia Roy akakunja uso. “Anza kwa
kusema sisi.” “Hata hujasikia ni nini nataka kusema, umeshanirekebisha!” “Sasa
tumeingia wote wawili hapa, kwa nini uanze kwa kusema mimi na sio sisi?” “Wewe
nipe nafasi Roy. Kumbuka, acha haraka na usiongee.” “Sawa, maneno machache,
tufike kwenye pointi.” Roy akakubali bila ubishi na kuongeza, wenyeji wao
wakiwatizama tu.
Bibi Cote tuli akiwasikiliza walivyokuwa wakinong’ona.
Malcom akageuka tena ili kuendelea. “Kama nilivyotaka kusema. Sisi ni ofisa wa
CSIS, tulikuwa na Ma...” Roy akamkata kwa haraka kwa kukohoa kwa sauti.
“Tulikuwa na Miss Cote jana kwenye..” Akamgeukia Roy. “Uokoaji.” Roy
akanong’ona kama kumkumbusha. Ikabidi Maya acheke. “Wewe Malcom na Roy, Nana
ameshasikia stori zen...” “No Maya. Acha tusikie ni maelezo yepi yamepita.”
Bibi yake akamnyamazisha Maya kutaka wamalizie. Malcom akamtizama Roy na Maya.
Maya akazidi kucheka.
“Nana anataka kujua mlifikia wapi kwenye kuchagua
kitu cha kujia nacho hapa?” Wakawa kama hawajaelewa kidogo. Bibi Cote akawawahi
na kuwachanganya zaidi. “Ehe!” Bibi Cote akataka Malcom aendelee. “Yule
aliyemteka..” “Mambo ya kesi nazungumza na kiongozi wenu, Underson. Najua kila
kitu kinachoendelea.” Bibi Cote akamkata Malcom. Malcom na Roy wakaangaliana
wakaonekana wameingiwa hofu. Wakarudi nyuma kidogo.
“Au ndio hicho kilikuwa kiingilio chenu?” Bibi Cote
akawauliza. Wote wakatingisha kichwa kukubali. Maya akazidi kucheka. “Haya,
endeleeni na kitu kingine. Kuwa nyinyi ndio mliomuokoa Maya. Ehe?” Roy na
Malcom wakaangaliana. Maya akazidi kucheka kimya kimya huku ameinama. “Tulitaka kumwangalia Maya
kuju...” “Miss Cote!” Roy akamsahihisha tena. Malcom akamvuta Roy nyuma kidogo
wakageuka kuwapa mgongo, akamnong’oneza kitu. Akamwambia abaki palepale nyuma. Malcom
akarudi tena pale mbele ya bibi Cote.
“Nilitaka kujua Maya anaendeleaje. Maana mimi ndiye
niliyekuwa naye jana kule kwa Jake.” “Wewe hukusoma ripoti ya daktari?” Bibi
Cote akamuhoji. “Nilisikia mkisema mlimaliza chuo cha CSIS kama wanafunzi bora.
Mnawezaje kuja hapa bila kusoma ripoti?” Malcom akaanza kutetemeka. Roy
akanyoosha mkono kule nyuma. “Ehe Roy?” Bibi Cote akamuita akasogea. “By the
way hata hilo mimi nilimwambia. Ila kwa asili Malcom ni mbishi na hanisikilizi.
Ila hicho unachomwambia, nilimwambia kuwa mtamuuliza hivyo hivyo akasema..”
“Ripoti huwa haziongei uhalisia.” Akamalizia Malcom mwenyewe.
“Haya, karibuni mkae.” Maya akaanza kucheka upya,
safari hii kwa sauti. “Unamaanisha hapahapa?” Roy akauliza huku akijisogeza.
Bibi Cote akasimama na kutoka pale. “Uwakaribishe kwa chakula cha usiku.”
Akaongeza bibi Cote wakati anaondoka pale. “Umeona Malcom? Usiku wa leo
tunakula kwa kina Cote!” Roy akashangilia kwa sauti ya chini. “Humu ndani ni
pazuri sana Maya!” “Wewe si umesema tuseme Miss Cote?” Malcom akamshushua Roy.
“Come on Malcom, mbona na wewe unamuita Maya?” Wakaanza kubishana tena.
Maya akacheka huku akiwaangalia. “Mnajua
tuliwasikia tokea asubuhi pale hospitalini?” “Acha utani!” “Sasa unafikiri ni
kwa nini Nana alikuwa anataka kusikia mmekuja na stori gani? Kwa kuwa
aliwasikia mkipanga mipango yenu yote.” “Na Mr Cote alisikia?” Roy akauliza kwa
wasiwasi kidogo. “Na mke wake pia.” “Ni Roy huyo! Tunapanga mipango mingi
haikamiliki!” Maya akawa anacheka.
“Sasa tunaruhusiwa kukaa? Maana hii ni moja ya
kutimiza ndoto ambazo huwa zinagoma kuotwa.” “Ndoto gani Roy?” Maya akauliza
huku akicheka. “Sisi, kukalia viti vya kina Cote!” “Wewe jisemee mwenyewe.”
Malcom akajitoa. “Kuwa mkweli Malcom, lini wewe ulishawahi hata kufikiria
kufika humu ndani?” “Mara nyingi tu.” Malcom akajibu kwa uhakika. “Taja hata
mara moja.” “Natania bwana. Tukae?” “Nana ndio amewakaribisha hivyo.” “Isije
kuwa ameenda kuongea na bosi wetu!” Roy akatia mashaka. “Hawezi. Kaeni.”
“Uuuuuwiii!” Wote wakakaa huku wamefunga macho kama wanaosikilizia ile starehe
yake. Maya alikuwa tu akiwaangalia na kucheka.
Tunda & Net.
T |
unda alishituka kutoka usingizini, akakakaa kwa
haraka. Yule aliyesema hana uchovu kabisa, anamlinda hapo yeye Tunda alale tu,
yeye ndio alikuwa amelala usingizi mzito kama ametoka kulima siku nzima. Tunda
akamwangalia na kujiegemeza pembeni. Akamsikia mtoto wake akihangaika kitandani
akajua ameamka. Net aliyesema yupo hapo kusaidia hakuwa hata na habari.
Akajivuta taratibu kutoka kitandani na ule mshono wa uzazi, akiushikilia.
“Nipo Cote. Nipo hapa baby!” Tunda akaongea
taratibu kwa upendo huku akimsogelea. Akamnyanyua na kumbusu. “Gosh, you are so
cute!” Tunda akamwambia mtoto wake akimsifu kwamba yeye ni mzuri sana huku
akimbusu na kujishangaa machozi yakitoka. Akamuweka sehemu yakumbadilishia
diaper akambadili kisha akaenda kukaa naye kwenye kiti chake chakunyonyeshea.
Akamlaza katikati ya mapaja yake, akawa anamwangalia.
“Sasa wewe unafanana na nani? Eti
Cote jamani? Mzuri wa kupitiliza!” Tunda akawa
anamuuliza kwa upendo, huku akicheka na kujifuta machozi. Akanyanyua mkono wa
Cote akambusu. “Nakupenda sana Cote.” Tunda
akaendelea kuzungumza naye kwa sauti ya chini huku Cote naye akimwangalia. Kisha
akamuweka kwenye ziwa. “Unyonye sana mpaka umalize maziwa yote, usilale.” Tunda
alimwambia Cote mara alipoanza kunyonya. “Usilale bwana!” Akamkuna miguu.
Alikuwa amemkumbatia kabisa kwa mkono mmoja huku mto mdogo ukimsaidia kuegemeza
mkono wake, akamgeuzia tumbo lake kifuani kwake.
Net alikuwa amefungua macho akiwaangalia na
kuwasikiliza. Alipoona kimya, akatoka pale kitandani. “Sikuwa hata nimesikia
wakati Cote anaamka.” “Ulikuwa unakoroma Net! Umenifanya nishindwe kulala.” Net
akacheka na kujisogeza.
“Nikwambie ukweli Tunda?” Tunda akamwangalia.
“Nimekuwa na masaa 48 magumu, hayajawahi kunipata tokea nazaliwa. Ni zaidi ya
siku umekamatwa na kupelekwa jela. Zaidi ya zile siku ambazo nilikuwa nikikaa
pale jela na kukusubiri, zaidi ya kila kitu.” Tunda akarudisha macho kwa mtoto
wake. “Ulipokamatwa na mama, nilijua nitakutoa tu. Ulipokuwa ukikataa kuniona
jela, nilikuwa naumia lakini nilijua siku moja utatoka tu. Lakini sio kufuatwa
na Vic, tena tukiwa hatupo kwenye maelewano! Nipo kwenye kujiandaa kujieleza
kwa hilo, ndio wanakuiba! Na mimi ndio nilisababisha! Nikawa sijui kama
watakuokoa kabla ya kukudhuru au la! Niliingiwa hofu, nilikuwa siwezi hata
kufikiria.”
“Haya, nakupata, na wewe unaniaga!” “Nani
amekwambia siondoki tena?” “Hata kule kukushika tu naona kumenisaidia kulala
kwa masaa machache, nimepata nguvu.” Tunda akamwangalia na kurudisha macho kwa
mtoto. “Ila nafikiria huko unakokwenda utafute sehemu kubwa.” Tunda
akamwangalia. “Maana ujue mimi nipo nyuma yako.” “Huwezi kunifuata wakati
naondoka hapa kwa ajili yako Net. Umenikosea sana!”
“Ni kwa sababu nakupenda Tunda. Niliogopa kukwambia
kwa sababu ya kuhofia kukuingizia hofu au wivu kwa kitu ambacho hata
hakikuwepo! Hakika sikumbuki kuwa na Vic ule usiku ila kuamka pembeni yake.
Niliogopa, nahisi ungekuwepo ungenihurumia.” Tunda akamwangalia na kunyamaza.
“Naomba usiwahi wala kujaribu kujifananisha na Vic,
Tunda. Tafadhali. Nilikuwa Tanzania kwa ajili yako huku nikiwa nimemuacha huku
nikijua anatamani na kumtaka Nathaniel Cote. Vic hanipendi wala hanifikirii
mimi kama mimi na ndio maana inakuwa rahisi kuniumiza na kunitangaza kiuchafu
kiasi hicho. Usiniache Tunda mpenzi wangu. Ni heri nipoteze kila hela kwenye
akaunti yangu ila niwe na wewe. Unisamehe.” Tunda akanyamaza.
“Na siku ile kwenye chakula sikuwa nikikugombeza
wewe au kuona hukufanya vizuri. Nilidhani Gino anakudharau kwa kuwa ni wewe.
Wafanyakazi wangu wote wanajua mimi huwa siwezi kupoteza hata dakika moja. Wote
wanajua na ndio ulinzi wa ajira yao. Sikukusudia mpenzi wangu. Na wala sikujua
kama itakuumiza kiasi hicho! Namjua Vic, na nimekua naye, lakini sijawahi hata
kumuamini na jukumu hata lakumtuma afikishe kitu mahali. Nimefanya kazi na
wewe, najua utendaji kazi wako. Sina wasiwasi na wewe na ujue tu, ofisi ya Nana
ni yako.” Tunda akamwangalia kwa mshangao.
“Kweli Tunda. Nana akiondoka tu, ujue ile ofisi
inakuwa yako.” “Mimi bado nataka kuzaa watoto wengi.” Net akaanza kucheka.
“Usicheke bwana! Umenisababisha nizae kwa upasuaji kwa hiyo hata idadi ya
watoto inapungua!” Net akambusu shavuni. “Unataka watoto wengine wangapi?”
“Wakiwa wanatoka kama hivi Cote, nataka wengi sana.” Net alicheka sana. “Wewe
hebu muangalie. Ushawahi kuona kitu kizuri kama hiki hapa duniani?” Wote
wakamwangalia Cote.
“Sijawahi.” Net akajibu na kuinama na kumbusu
mwanae. “Hamna pesa inanunua kitu kizuri kama hiki.” “Ndio maana nataka waje
wengiii.” Net akacheka. “Nitamuuliza daktari ni lini naruhusiwa kubeba mimba
nyingine, halafu atupe dawa tuzae mapacha.” “Tunda! Kumbe unamaanisha!?”
“Sitanii mimi. Cote amenitia hamu. Na kwa kuwa umenikosea, katika hili huna
usemi Net. Mimi ndio naamua.” “Sawa Tunda. Tutazaa kadiri ya uwezo wako.” Tunda
akamwangalia tu.
“Usinichukie bwana Tunda. Mimi nakupenda wewe na
nimekuchagua wewe mpaka kifo. Nilikuficha sio kwa sababu nilifurahia kubakwa!”
Tunda akacheka. “Kwanza hata sikumbuki kubakwa na mtu mwingine ila wewe tu
mpenzi wangu!” “Acha kunipamba wakati umeniudhi!” “Basi mama. Ila ujue
nilikuficha kwa kuwa nakupenda na sikutaka kukupoteza.” Tunda akanyamaza.
“Tunda?” “Mbona hunipi hata nafasi ya kukasirika
Net jamani! Umenikosea, halafu unanighasi sipati hata muda wa kukasirika na
kufikiria.” “Sio mbali na mimi. Shetani atakuhubiria ya kwake. Adhabu
umeshatoa. Kuzaa watoto wengi mpaka useme basi. Nyumba hii igeuke kama shule ya
chekechea!” Tunda akacheka.
“Nataka kutembea kidogo Net. Dokta amesema
itanisaidia kupona haraka.” “Basi twende tukale wote mezani. Mlete mtoto,
ujiandae.” “Nenda kaniletee vitu vyangu vyote kule chumbani.” “Oooh Nooo.
Tushasameheana. Unarudi chumbani kwetu.” “Sijasema kama nimekusamehe Net!”
“Basi ngoja nipige simu niwaambie watuhamishie mizigo yetu wote.” “Hiyo ni fujo
Net! Wewe umekosa, kubali kosa na ukakae kule mpaka nitakapokuwa tayari.” Tunda
akasimama.
“Lete nikupokee wakati unajiandaa.” “Kama
nikujiandaa kwa kwenda kukaa pale mezani...” Akasita Tunda huku akimwangalia.
“Si useme tu? Mimi na Cote tutakusindikiza.” Tunda akamwangalia. “Ila ujue ni
kwenda tu kuoga na kubadili, usiku narudi huku.” “Tutarudi huku.” Net
akarekebisha kwa kujiongeza hapo, Tunda akatoka, Net akiwa amembeba mtoto wake
akafuata nyuma kwa haraka.
“Hivi wewe ni mtu gani hukubali kosa na kusubiri watu wakusamehe?” “Maisha yalishatupa hiyo nafasi jana. Ushukuru ulikuwa umelala. Ungekuwa unajua kinachoendelea, hakika Tunda, leo usingekuwa ukizungumzia kutengana. Ungetaka kukusanya kila mtu karibu yako. Mungu ametupa nafasi ya pekee, tuitumie vizuri.” Tunda akanyamaza huku wakitembea.
Wakawa wanapita pembeni ya sebuleni Maya akawawahi.
“Namuombeni Cote.” Akasimama kuwasogelea, na wale vijana wawili wakasimama kama
mshale walipomuona Net na familia yake.
“Huyu anaitwa Malcom.” “Na huyu anaitwa Roy.” Net
akanyanyua uso na kuwatizama maana alikuwa akimwangalia Cote pale mikononi
mwake akimpapasa. Na Tunda naye akawaangalia. Wakasogea karibu. “Sisi ni
maafisa wa CSIS, tulikutana jana usiku sana. Pengine hutukumbuki sababu ya giza
na ile hali ya wasiwasi pale.” “Yeah. Halafu tulikuwa maafisa wengi pale.”
Akadakia Roy na kuendelea. “Ila sasa sisi ndio tuliomuokoa Maya kwenye hatari
ya kifo.” Tunda akacheka na kujishika tumbo kwenye mshono alipofanyiwa upasuaji
kama anayezuia maumivu. Nakuzidi kucheka.
“Kwa hiyo, hiyo ndio stori mliyoipitisha?” Akauliza
Net huku akiwatizama. Roy na Malcom wakaangaliana. “Actually hiyo ni ya Roy.”
Malcom akajitetea. “Malcom yeye alitaka tuseme tu tulikuja kuangalia maendeleo
ya Miss Cote.” Roy naye akajibu. Maya alikuwa akicheka huku akiwaangalia. “Na
tungeshaondoka, ila Ms Cote ametualika kwa chakula cha usiku hapa. Ndio tumeona
tu tusubiri.” Roy aliendelea, Net akawaangalia na kuamua kuondoka na mkewe.
“Nilikwambia watu matajiri huwa hawana muda wa
maneno mengi Roy! Umeharibu!” Wakawasikia wanaanza kubishana kwa sauti ya chini
“Hapana bwana.” “Umeona jinsi alivyokuangalia?” “Basi nitarekebisha mezani.”
“Matajiri huwa hawazungumzi wakati wakula. Tafadhali usiendelee kuharibu Roy.”
“Fine! Nitanyamaza. Ila ukumbuke bila mimi, usingeweza kuwepo hapa. Usije
kulisahau hilo Malcom. Mimi..” Net akakohoa kidogo.
Wakageuka na kusimama mikono mbele. “Yes Sir?”
Wakamuitika Net kwa pamoja. “Tunashukuru kwa kumuokoa Maya.” Net akashukuru.
“See! Wazo langu limelipa Malcom.” Malcom akampiga ngumi nyuma ya mgongo, mpaka
Roy akainama, “Aaah!” Kisha Malcom akamjibu Net. “Tulikuwa tukitimiza wajibu
wetu, Sir.” Akajibu Malcom kwa unyenyekevu. “Ulitakiwa kusema it’s our pleasure, Malcom! Unaharibu juhudi zote!” Akiwa anajichua mgongoni, Roy akalalamika.
Tunda akacheka na kuondoka na Net, wakamuachia Maya mtoto.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda, Net na Tunda wakatoka chumbani,
Tunda akiwa ameoga na kuchana nywele vizuri. Akavaa na hereni vizuri.
Akapendeza sana. Bibi Cote akasimama
wakati wanaingia sehemu yakulia chakula. “Oooh my goodness! Angalau kunaonekana
kuna uhai!” Tunda akacheka na kumsogelea na kumbusu bibi Cote. “Najisikia
vizuri japo sijaweza kulala kwa muda mrefu sababu ya hofu!” “Karibuni sana
hicho kitendawili na fujo zote zitakuwa nyuma yetu, na tutaweza kulala vizuri.”
Net akaenda kumchukua Cote kutoka mikononi kwa Maya.
“Mbona sasa na nyinyi mmesimama!?” Tunda akawauliza
Roy na Malcom. “Malcom ameniambia nisimame.” “Kwa sababu Ms Cote alisimama.”
Wote wakawaangalia kama hawajaelewa. “Niliona kwenye movie ile ya Pretty
woman, walipokuwa
wakila, mtu akisimama, na wengine kwenye meza wanasimama. Mimi nikajua watu
wastaarabu wak,” “Matajiri.” Roy akanong’ona kumsahihisha. “Yeah matajiri na
wastaarabu ndio wanavyofanya!” Tunda akacheka sana huku akishika tumbo. Net
akamvutia kiti, Tunda akaenda kukaa.
“Sasa, sasa hivi nyinyi mnakuwa hampo kazini?”
Tunda akauliza. Wakaangaliana. “Aaahaa!” Akaanza Roy akanyamaza. Akabaki
akimtizama Malcom. “Nafikiri ile stori yenu ya kuwa mnamfuatilia mtu
mliyemuokoa jana wakati mpo kazini, ndio ingefaa kujibu sasa hivi.” Net
akaongea huku akimwangalia mtoto wake. “Hata mimi nilifikiria kujibu hivyohivyo,
Sir.” Roy akadakia. “Lakini tatizo likawa muda tuliofika hapa mpaka sasa!”
Akaongeza Malcom “Yeah.” Roy akaunga mkono hoja ya Malcom. Wote wakatingisha kichwa
kukubaliana.
Bibi Cote akawa akiwatizama tu. Maya na Tunda
wanacheka. “Kwani nyinyi kazi yenu ni nini huko CSIS?” Tunda akawauliza tena.
Wakaangaliana. Kisha wakamwangalia tena Tunda, halafu wakabaki wakiangaliana.
Wote wakawaangalia wao. Gino akaja pale mezani kuleta starter ya matunda na
salad, kisha akawauliza wao waletewe nini. Wakaangaliana kisha wakamwangalia
Maya, kisha wakamwangalia Gino. Wakajiweka vizuri. “Labda niulize. Tunaweza
kuagiza chakula chochote tunachotaka?” Roy akamnong’oneza Gino.
“Vipo ambavyo vipo tayari. Sijajua kama ndivyo
mngependa!” Gino akaongea kwa sauti ya chini na heshima. “Labda utupe
menu.” “Come on Roy! Hapa sio hotelini.
Na tangia lini umeanza kuchagua vyakula?” Malcom akamgeukia Gino. “Huwa
tunakula kila kitu. Hatuna allegies, na hatuna kitu tusichokula. Wewe tuletee
chochote.” “Yeah man! Kama alivyosema Malcom.” Bila ubishi, Roy akakubaliana na
Malcom, Gino akatoa tabasamu akataka kuondoka.
“Lakini..” Roy akamfanya Gino ageuke. “Kuna aina ya
juisi tulisikia huwa unatengeneza. Mimi naomba uniletee hiyo tafadhali.” “Hata
mimi tafadhali.” Akaongeza Malcom kwa heshima. Maya na Tunda wakacheka tena.
“Labda niulize, hapo mlipo mpo kikazi au?” Wote
wawili wakamgeukia bibi Cote, wakakuta akiwatizama huku ametulia tu. Kisha wakageukiana.
“Hapo ndipo mnapoogopa Nana asimpigie simu Mike?” Net akawauliza. “The
Director!” Wakahamaki kwa pamoja. “Kama alivyouliza mke wangu. Nyinyi kazi
yenu huko CSIS ni nini?” Net akauliza kwa msisitizo. “Mimi na Malcom ni
partners.” “Hilo halina ubishi.” Net akaongeza.
“Lakini ambacho watu hawajui ni kuanzia siku ya
kwanza chuoni.” “Mlishasema kule hospitalini.” Net akaongeza. “Hivi tulisha
sema eeh!?” Roy akajidai kuuliza kama hakumbuki huku akimwangalia Malcom.
“Ndiyo, ulisema Roy. Ulisema ndio uwe utambulisho wetu.” “Hiyo ilikuwa dhaifu
sana, isee!” “Umeamini sasa kile huwa nakwambia kila wakati?” Malcom akamuuliza
Roy.
“Lakini si tulimtoa Miss Cote salama bila
kudhurika?” “By the way ilikuwa ni mawazo yetu mimi na Roy.” “Hatukutumwa na
mtu. Ni wazo letu sisi wenyewe. Mbinu zote tulizotumia, ni akili yangu na
Malcom.” Akaongeza kujisifia Roy. “Kama mngekuwa mkiongea mezani,
ningewasimulia kitu kikubwa sana, na kizito ambacho Malcom peke yake,
namaanisha peke yake alikigundua tokea tupo chuoni. Ila sema Malcom amesema
huwa matajiri hawaongei mezani na hawasikilizi maneno mengi.” Akaendelea Roy.
“Tumekuwa mezani zaidi ya dakika 5 sasa.” Akaongea
bibi Cote. Roy akatulia kidogo kama ambaye hajaelewa bibi Cote anamaanisha
nini. “Anamaanisha umekuwa ukiongea tokea umefika hapa. Ni kipi kinakuzia
kuendelea kuongea sasa hivi, genius!” Malcom akamuelewesha na kumkejeli. “Hapana
hajasema hivyo bwana!” Roy akabisha. “Ndio maana nilikwambia huwa hawaongei
sana. Neno moja linakuwa limebeba maana kubwa.” “Imekuaje wewe umejua hivyo
halafu mimi nisielewe! Hajasema hivyo bwana!” Gino akaanza kutoa vyakula na
vinywaji kwenye kigari.
Roy akaanza kumsindikiza kwa macho kila
anachokifanya kwa kila mtu. “Stop staring, Roy!” Malcom akanong’ona. “Am not!”
“Yes you are.” Wakabishana kidogo wakanyamaza. “Anza kwa kuwapa wao chakula na
vinywaji.” Akaagiza bibi Cote. “Hapo hata mimi nimeelewa Malcom!” “Nini?” Malcom akamuuliza taratibu tu. “Anamaanisha
tupewe sisi kwanza chakula ili tunyamaze.” Meza nzima walicheka mpaka bibi Cote
mwenyewe.
Net akabaki akiwatizama. “Mmekuwa kazini kwa muda
gani sasa?” Ikabidi tu Net awaulize. “Miaka 5 tu, Sir!” Akajibu Roy kwa
heshima. “Kabla ya hapo mlikuwa wapi?” “Chuoni ndio kazini.” Akaendelea kujibu
Roy. “Huwa wanaanza kula wakati gani?” Akamuuliza Malcom kwa kunong’ona.
“Subiri Roy.” “Nafikiri ni wazo zuri. Labda wanaanza kwa kuomba!” “Au
wanasubiriana kila mtu mpaka apate chakula chake.” “Itakuaje kama wakichelewa
halafu tukaitwa kazini kabla hata hatujala? Unafikiri wanaweza kutufungashia?”
“Hapana Roy. Naomba usije kuomba kufungiwa chakula.” “Kwa nini?” “Tafadhali
usiombe chakula.” “Njaa inauma Malcom! Kumbuka hatujala tokea kahawa ya
asubuhi. Au tuanze sisi kula.” “No man. Play cool.” Wakaendelea kunong’ona
wakati wengine wakihudumiwa na Gino.
“Ni nini ulitaka kuongea Roy?” Akauliza Net. “Juu ya chakula? Nilikuwa namwambia Malcom..” Roy akauliza nakutaka kuendelea. “No man!” Malcom akamkatisha kwa haraka. Roy akakunja uso. “Kuwa sisi ndio tulimuokoa Miss Cote?” “No Roy. Hiyo wameshajua. Kwanza ni habari ya zamani sana.” “Si ni jana tu!” Roy akashangaa. “Yeah. Lakini imeshakuwa habari ya zamani. Umeirudia rudia sana mpaka imekosa maana.” “Really!?” Roy akauliza kwa kushangaa na kuumia sana.
“Yeah Man!” “Sasa unafikiri atakuwa anaulizia
nini?” Roy akauliza taratibu kwa sauti ya chini sana. “Ile ulisema ungeongea
lakini ni kwa kuwa tupo mezani na huwa hawaongei, lakini hajaacha kuongea mpaka
sasa.” “Oooh! Lakini sasa hivi sidhani kama niwakati wakuongea Malcom. Ona!”
Akamuonyeshea sahani iliyowekwa mbele yake jinsi ilivyopendeza. Na bakuli la
matunda pembeni akiwa bado hajamaliza, sahani ndogo ya salad ya ukweli yenye
vitu kibao na kila sahani ilipambwa vizuri. “Come on Roy!” “Fine.” Walikuwa
wameinamiana wao wawili wakinong’ona.
“Huhusu Malcom na bahari za Maya.” “Miss Cote.”
Malcom akamsahihisha. “Haa! Yaani nikiongea mimi ndio unanisahihisha! Wakati
tokea jana nakwambia ni Miss Cote, ukasema hakuna tatizo. Leo mimi nimesema
Maya, unaniambia Miss Cote! Lipi ni lipi?” “Wewe endelea na Miss Cote.” “Why?” “Wewe bakiwa na Miss Cote. Unaitamka vizuri sana kuliko jina Maya.” Roy
akacheka huku akitingisha kichwa kama anaye sikitika.
“Unajua sisi ndio tokea zamani tukiwa chuo, ndio
tulijua kuwa kuna kitu hakijakaa sawa kwenye kashifa za Miss Cote.” Malcom
akakohoa kidogo. “Fine. Ni Malcom. Mimi nikabisha kidogo, nikasema...” Roy
akatulia kidogo akawaangalia wote akasutwa na macho yao. “Hata nyinyi jamani si
mnajua wale watoto wanao tokea kwenye familia za pesa nyingi wanakuwa hawajui
ni nini chakufanya na pesa zao? Si ndiyo?” Meza nzima kimya. Wakabaki
wakimtizama. “Come on people! Hata kwenye movie huwa wanaonyesha?” Roy
akatafuta uungwaji mkono. Kimya.
“Anyway. Tulipokuwa chuoni, tulipewa kazi ya kufanyia utafiti zile kesi ambazo zinaonekana zina tija nyuma yake na hazijawahi kupewa kipaumbele. Tukapewa muda wakutafuta na kuja kuzitaja mbele ya darasa, zikishapitishwa, ndipo inakuwa ni kazi yako utakayoifanyia utafiti. Ikishapita, na ukafanikiwa kutafuta ushahidi wakutosha, tunamfuata mlengwa. Hata kama hana pesa, tunamwambia kuwa japokuwa kesi yake ilipuuzwa, lakini. Hapo ndipo yule mwanafunzi mshindi anasimamia hiyo kesi mpaka mwisho.” Roy akacheka kidogo.
“Tafadhali usiweke mzaha Roy!” Roy akatulia.
Akagundua wote wapo kimya wakimtizama. “Ooh yeah. Hakuna mzaha.” Akanywa juisi.
Kisha akaendelea. “Siku yakutaja kesi tulizochagua, maafisa ambao tulikuwa
chuoni wakati huo, wakaja na kesi nzito na za kusisimua. Wakazielezea mbale ya
darasa. Huyu Malcom akaja na kesi juu ya Miss Cote.” Akamgeukia Malcom. “Ni
sawa nikisema watu walivyofikiria au hicho kipengele nacho niruke?” “Wewe sema
tu.” Maya akaingilia na kumruhusu.
Wote wakamwangalia. “Sio kizuri Maya. Acha aongee
kitu cha maana.” Malcom akamgeukia Maya aliyekuwa amekaa upande wake wa kulia.
“Ni sawa tu. Mwache aseme.” Maya akasisitiza akimwambia Malcom kwa utulivu. “Okay.
Kila mtu alimcheka.” Ikabidi Roy aendelee maana Malcom na Maya walibaki
wakiangaliana.
“Mpaka akakataliwa asiendelee na hiyo hoja. Kila
mtu mpaka mimi nilimwambia hayo ndiyo maisha ya watoto wa mamilionea. Hawana
matumizi na pesa zao. Lakini japokuwa watu wote walimpinga Malcom, tuliporudi
chumbani, maana tulikuwa tunaishi chumba kimoja na Malcom tokea chuo. Malcom
akasisitiza kuwa bado kuna kitu hakijakaa sawa.” “Unamaanisha nini Malcom?”
Bibi Cote akamtaka Malcom aeleze mwenyewe.
“Inamaana mimi ninyamaze, si ndio?” Akauliza Roy
nakufanya wacheke. “Yeah Roy.” “Sawa. Na mimi hapo nimeleewa Malcom!” Roy
akainamia chakula chake akaendelea kula. “Mara ya kwanza Maya anaonekanika...”
Akasita. “Sawa tu.” “Ila sina nia yakufufu mambo ya nyuma.” Malcom akaongea kwa
sauti ya kumbembeleza Maya. “Ni sawa tu.” “Unauhakika?” Kila mtu akabaki
akiwatizama. “By the way Malcom huwa anamfuatilia Miss Cote tokea zamani.
Nikisema anamfuatilia namaanisha ni mmoja wa follower wake kila mahali.
Namaanisha kila mahali. Angalia Maya. Facebook, instagram, Twitt..” “Come on
Roy!” “Fine!” Roy akanyamaza. Maya akakunja uso.
“Ehe!” Net akataka Malcom aendelee. “Unakumbuka
picha na video mbaya za kwanza kabisa za Maya? Alionekana yupo chooni club.”
Kimya. Malcom akaendelea. “Choo cha club lazima kuwe na watu wakati wote na
kuwe na kelele. Lakini ile video alionekana yupo Maya tu na Jeremi.” Wote
wakashangaa kuwa mpaka anakumbuka jina. “Niliwaambia mimi! Anamfuatilia Miss
Cote kila mahali na kila mtu anayekuwa naye.” Roy akaongeza. “Anyway.” Malcom
akamkatisha huku akimwangalia machoni kama kumwambia anyamaze. Roy akainamia
chakula.
“Kama nilivyosema, walikuwa hao watu wawili tu.
Hakuna kelele nyuma ya ile video wala hakuna hata mtu anayepita! Nikajua ni
juhudi za makusudi kabisa za kuhakikisha wanapata ile video vizuri bila
mwingiliano. Kuna kipengele utaona kabisa ni kama Jeremi alijua anachokifanya
na hakuwa amelewa kama Maya ambaye alionyesha kulewa sana.” Malcom akaendelea.
“Katikati ya dakika ya 2 tuseme karibia ya tatu
hivi, Jeremi aligeuka upande wa pembeni kama mlangoni kuingilia hapo chooni
kama anayepokea maelekezo cha nini chakufanya pale kwa Maya ili asiharibu.”
Meza nzima kimya. Hakuna aliyeendelea kula. “Video ya kwanza kabisa ya Maya,
ukiangalia muonekano wa Maya kwenye ile video, haukuwa na tofauti na video ya
Mr. Cote.” Hapo wote wakaweka vijiko
chini. Roy akanyanyua kichwa na chakula mdomoni. Akakuta meza nzima imeduaa
macho kwa Malcom. Roy akameza kwa haraka. “Unakaribia kuharibu!” Roy
akanong’ona.
“Hapana. Nataka kujua.” Net akaweka msisitizo. “Mtu
anayetumia unga, ni tofauti kabisa anapoanza na anapokuwa mzoefu akiwa ‘high’.
Sijui kama uliangalia video yako Mr Cote na za Maya?” “Maya ni dada yangu!”
Akajibu Net. “Anamaanisha hawezi kuwa anaangalia hizo video.” “Nimeelewa Roy!”
“Nilitaka kuhakikisha tu.” “Nilichotaka kusema ni hivi, video za mwanzo wakati
Maya alipokuwa mgeni kabisa na yale madawa aliyokuwa akipewa kama unga, hakutoa
ushirikiano mkubwa kwa Jeremi, kama vile Mr Cote kwa Vic. Samahani Mrs Cote.”
Tunda akainama.
“Lakini pia kwenye video ya pili ya Maya, akiwa na
Dale pia kulikuwa na utata. Japokuwa Maya alionekana ameshazoea dawa, lakini
eneo la tukio lilikuwa lina maswali na vile video ilivyokuwa ikionekana.”
Malcom akakaa sawa.
“Video iliyochukuliwa kwa kuegeshwa na kuchukuliwa
kabisa na mtu wakati wa tukio, ni tofauti. Utagundua kwa engo na sehemu za
tukio linapofanyika. Angalia video ya Mr Cote na za Maya. Mr Cote yake
ilionekana kabisa ni kamera ilitegeshwa na ikahamishwa mara mbili tu. Halafu
hata Vic mwenyewe alionekana alikuwa akihangaika kutizama kwa makusudi hiyo kamera.
Alionekana akifanya juhudi za makusudi aonekane, wakati Mr Cote alionekana
hajui hata kamera ilipo au hata kutambua uwepo wa Kamera pale. Mkirudia
kuangalia ile video mtaona.” “Sidhani kama huo ni ushauri mzuri Malcom.”
Akanong’ona Roy.
“Ni kwa kujiridhisha tu, sio kutafuta kujiumiza.
Halafu ukirudi kwa Maya, wanaume wote aliokuwa akiwa nao kwenye video
walionekana walikuwa wakichukuliwa video na mtu. Na huyo mtu alikuwa
akiwachukua akiwepo hapohapo chumbani na alionekana alikuwa na uhuru
wakuzunguka kila pande. Utaona engo zote tena kwa 360. Lakini pia, utagundua
katika kila video ya Maya, wanakwepa vioo. Kuanzia ya kwanza kabisa kule choo
cha club, utagundua japo kulikuwa na vioo vingi ukutani, lakini walitafuta
sehemu ambayo haina kioo. Kwa nini! Kwa kuwa mchukua video angeonekana kwenye
hiyo video pamoja na wengine waliokuwepo kwenye hicho chumba au walio husika kwenye kuchukua ile video. Mtaangalia kwa makini tu, mtagundua haya
ninayosema.” Malcom akaanza kumvutia bibi Cote.
Aliwaeleza kwa kifasaha kama anayeelewa na
anauhakika. “Tuje ile ya kwenye gari, ni kama aliyechukua alikuwa ndani na nje
ya gari pia. Ni kama alikuwa na hiyo kazi makusudi kuhakikisha anampata Maya
vizuri. Usoni mpaka unyayo ili kusitokee na kuja kukanusha.” “By the way katika
huo uchunguzi wake akaanza kupatwa wivu.” “Unaongea nini Roy!?” Malcom
akashituka sana.
“Maya alipoingia kwenye mahusiano na Jake, uliona
kwenye instagram, nakumbuka ukakasirika na kuacha kumfuatilia tena.” “Haikuwa
sababu ya wivu bwana!” “Mmmmhhh!”
Akaguna Roy kwa kumsuta. “Sasa kwa nini hukusema?” Akauliza bibi Cote kwa kuumia sana.
“Unakumbuka utambulisho wetu? Ni Malcom na Roy tu!” “Anachomaanisha Malcom
hakuna anayetufahamu na hata tungeongea, zaidi wakati ule, hakuna mtu ambaye
angetusikiliza.” “Alielewa Roy!” “Nilikuwa najaribu kufafanua.” “Unakumbuka juu
ya maneno machache?” “Ooh yeah!” Akakubali Roy.
Hakunyamaza Roy, akaendelea tena. “Lakini na
maswala ya wivu yaliingilia.” “Hapana Roy!” Akabisha Malcom. “Sasa kwa nini
tumeriski ajira yetu tukajitosa kuja hapa kama sio dhamira kukuuma na
kukusuta?” “Hapana. Ni kwakuwa tulimuokoa jana..” “Yeah! Yeah! Yeah! Hata wewe
ulishasema hiyo habari ya uokoji imeshapitwa na wakati. Acha kurudirudia. Wewe
sema ukweli.” Malcom akanyamaza.
“Malcom huwa hajui jibu la hapana na ndio
kinachosababisha sisi kuingia matatizoni kila wakati.” Akaendelea Roy. “Japokuwa
alikataliwa hiyo kesi ya Miss Cote, lakini aliendelea kuifuatilia mpaka
tulikaribia kuingia matatizoni wakati tunahangaika kutafuta ushahidi wa
kutosha. Akiwa amefikia pazuri kabisa, akakatishwa tamaa na Miss Cote mwenyewe
pale alipotangaza kuwa amepata mwanaume wa ndoto zake. Ya kale yoote yamepita,
anaanza upya.” Maya akainama.
“Hapo ndipo Malcom akakata tamaa. Akaacha kabisa
kumfuatilia Miss Cote. Akachoma ushahidi wote na kuzira kabisa. Nikamuonya na
kumwambia atakuja kujuta. Akasema kama Miss Cote mwenyewe ameamua kuendelea na
maisha yake na yeye anaendelea, anaachana na kila kitu. Akakimbilia kuoa, ndoa
ikadumu kwa miaka miwili tu tena ya shida sana mpaka..” “Roy! Too much
information, Man!” “Fine. Lakini tupo hapa kwa sababu ya hukumu yako
Malcom. Alipoona video ya Mr Cote. Ndipo akakumbuka video za Miss Cote na
akasema isingekuwa kuzira wakati ule, haya yote yasingempata Mr Cote. Ndipo
matukio yakaanza kuongezeka hili na lile, tukaambiwa macho na masikio ya kila
mtu yawe kwa familia ya Cote. Mimi na Malcom tukakimbilia upande wa Miss Cote
kwa kuwa ni kesi tuliyokuwa tumeianza tokea chuo. Haikuwa rahisi kukubaliwa.”
Roy akacheka kama mazuri.
“Tulipambana mpaka tukakubaliwa sisi ndio tuwe
upande wa Miss Cote. Kuanzia kwenye mahojiano mpaka uokoa....” Pakatulia kidogo.
Roy akatoa sura ya utani. Akatulia kidogo. “By the way chakula ni kizuri sana.
Na ni kweli hii juisi ni ya kipekee.” Akasifia Roy. “Unataka uongezewe?” Tunda
akamuuliza. Lakini akamwangalia Malcom. “Hapana. Tupo tu sawa.” Akajibu Malcom,
Roy akapandisha nyusi zote juu, wakamuona ameinama kama ambaye hajaridhika na
jibu la Malcom. Tunda akacheka. Roy akaona aseme tu. “Tulikuwa tunazunguka siku
nzima, hatujapata muda wakula kwa hiyo..” “Tutamwambia Gino awafungashie.”
Akaongeza Tunda bila kutaka ajieleze sana. “Nitashukuru sana.” Akaitika kwa
haraka sana Roy bila kujivunga, Malcom akatingisha kichwa kwa kusikitika na
kuendelea.
“Nilichotaka kumalizia kabla ya kuondoka.” Malcom
akaanza tena. Wote wakamwangalia yeye. Akaendelea. “Wanaume wote waliokuwa na
Maya, wakati wote, zaidi kwenye video, walionekana wanajua kinachoendelea na
walifanya makusudi ili kutengeneza video nzuri, kama alivyokuwa akifanya Vic.”
Malcom akaendelea taratibu tu. “Kwa hiyo niligundua kuanzia mwanzo kuna mtu
alikuwa akimfanyia Maya makusudi. Lakini sikuwa nikijua ni nani na kwa nini.”
“Lakini unakumbuka Malcom wakati tupo chuo ulisema wazi kuwa itakuwa ni mtu
mwenye uwezo wa kipesa kwani anaweza kununua watu na kufunga hata club!” Roy
akamkumbusha na kuendelea.
“Maana video ya kwanza ambayo ni ya club, hapakuwa
na watu wala sauti. Inamaana alitaka kuwe kimya kabisa, watu wajue ni Maya. Na
ndipo mwisho ili kuthibitisha kuwa pale ni club, ndipo miziki ikasikika tena.”
Roy akaongeza.
“Binafsi nishukuru kwa kumwamini Maya. Hata sisi tulikuwa
kama wengine tu, tukijua ameamua kuwa mtoto mbaya. Hana matumizi na pesa zake,
basi. Hatukuchukulia maanani kuwa kuna mtu anamwangamiza. Najutia sana.
Natamani kama wakati ule ningetulia na kufuatilia kwa karibu, pengine Maya
asingechafuliwa kwa kiasi hicho.” Bibi Cote akaongea kwa kujutia.
“Lakini anyway, nishukuru kwa kuhakikisha
mlifuatilia, na kuweka wazi ukweli wote. Zaidi kwa kitendo cha kishujaa
chakumuokoa kwenye hatari ya kifo dhidi ya Vic. Nina uhakika asingeshindwa
kumuua. Vic alijawa na chuki mbaya sana dhidi ya Maya, tokea wapo watoto. Kwa
jinsi alivyonieleza Mike, isingekuwa kwanza Malcom kuingia pale ndani na kumpa
ushauri wa kumfunga Maya, hakika angemuua.” Wote wakashangaa kuwa tayari bibi
huyo ameshajua ukweli wote!
“Baadaye kuvunja dirisha na kumtoa! Hiyo
nitawashukuru daima. Sitasahau hilo. Ndio maana nilitaka na nyiinyi muwepo
kwenye mlo huu wa jioni hii, ambao ni maalumu kwetu. Mungu ameturudisha,
tumekuwa pamoja. Japokuwa tumepita au tunapita kwenye dharuba kali, lakini
tumesimama tena pamoja. Asanteni sana.” Bibi Cote akashukuru.
“Na mimi au sisi tunashukuru kutukaribisha. Asante
kutupa heshima ya kula pamoja na nyinyi. Tutahakikisha tunaendelea kusaidia
mpaka kufunga kesi nzima.” “Sasa hivi Jake na Vic wako wapi?” Akauliza Maya
akitaka kujua kwa undani, maana hata director wao, alizungumza juu juu tu pale
hospitalini.
“Hatuwezi kuongea kwa undani ila wapo chini ya
ulinzi mpaka daktari atakapothibitisha kuwa ni wagonjwa kweli wa akili, ndipo
watafungiwa kwa wafungwa ambao wanamatatizo ya akili. Ila ni watu ambao
hawatakuwa tena tatizo. Wamenyimwa hata dhamana. Kwa hiyo usiogope.” Malcom
akamtuliza Maya. Kimya. Kila mtu akabaki akiwaangalia wao. “Huu ndio ule muda
wakuaga kabla hatujaharibu.” Roy akainama na kumnong’oneza. “Yeah!” Malcom
akakubali. “Tunashukuru sana kwa chakula na kutukaribisha.” “Nina swali.” Net
akawawahi kabla hawajasimama, huku akimpapasa mtoto wake.
Roy na Malcom wakamwangalia kama hawaamini kama
wanataka kuulizwa wao. “Swali kwetu?” “Ndiyo.” Net akajibu, wakaangaliana na
kurudisha macho kwa Net. “Kwa uchunguzi kama huo ambao mmefanya nyinyi,
unatusaidia vipi watu kama sisi ambao ni wahanga?” “Labda nijibu mimi.” Roy
akaanza.
“Kwa upande
wa CSIS, imetusaidia kukamata wahalifu. Chanzo cha hizo dawa hatarishi na
kukomesha utengenezwaji wake haramu. Najua Ms Cote ataambiwa mambo yote
yalivyoendelea.” Akimaanisha bibi Cote. “Kwa hiyo itasaidia kujenga ushahidi
wenu mahakamani, kwa Vic. Mkishitaki kipekee kabisa, mbali na makosa mengi
yanayomkabili ikiwepo kukusudia kuua, kuwa alikuwa akitumia madawa hayo
kuwalevya kwa ajili ya ngono. Uzuri ni kwamba alikiri yeye mwenyewe. Na wauzaji
wamekamatwa. Haitakuwa kesi ngumu.” Roya akajieleza vizuri tu.
“Kingine tena kwa upande wenu.” Malcom akaongeza.
“Itawasaidia kusafisha majina yenu ambayo sasa hivi yamechafuka sana.
Kunyamazia tu, nikukubali kama vile ambavyo hakuna aliyekuwa amethibitisha kuwa
Maya,..” “Miss Cote.” Roy akarekebisha. “Tumeshapita huko Roy. Kwa hiyo kama
nilivyokuwa nikisema. Itasaidia kusafisha jina isiwe kama vile walivyokuwa
wakimsema Maya vibaya, wakidhani ni mtoto mchafu tu ambaye hajali kuonekana
hadharani akifanya mambo mabaya. Au hata wewe Sir.” Wakimaanisha Net.
“Kumbe zilikuwa zikifanyika juhudi za makusudi
kuwadhalilisha au tuseme kuwachafua.” “Na ndio maana wengine huitisha vyombo
vya habari na kuzungumza navyo. Lakini naamini mkizungumza na Mr Underson,
atawashauri vizuri zaidi kitu gani chakufanya.” Wakaweka heshima. “Asanteni kwa
kila kitu.” Net akawashukuru, na wengine wakashukuru.
“Ninawasindikiza Nana. Nitarudi baada ya muda mfupi
tu.” Maya akaaga. “Usisahau chakula cha Roy.” Tunda akamkumbusha Maya.
“Nitakula na Malcom pia.” Kila mtu akacheka.
Wakasogea pembeni ya pale mezani. “Maya!” Roy
akamuita taratibu, na kumkonyeza wasogee mbali zaidi. Maya akamfuata akiwa
anaelekea jikoni. “Naomba na ile juisi yenu, nimpelekee mama yangu aonje juisi
anayokunywa bibi yako. Najua atajisikia vizuri sana. Au unasemaje Malcom?
Tunampelekea sasa hivi.” Malcom akatingisha kichwa kwa kusikitika. “Really
Roy!” Malcom akashangaa sana. “Anatupa
chakula Malcom. Sasa kuna shida gani ya kuongeza na juisi?” “Hamna shida
kabisa.” Maya akajibu huku akicheka akaenda jikoni kuwachukulia chakula, wao
wakaondoka pale na kwenda kusubiria nje.
Baada ya muda mfupi tu, Maya akatoka na hivyo
vyakula, Gino akiwa amevifungasha vizuri na hiyo juisi. Roy akampokea na
kushukuru, akatangulia kwenye gari kama kuwapa nafasi.
Maya & Malcom.
W |
akaangaliana na kucheka. “Nimefurahi kukuona Maya.”
“Kwa nini?” Maya akauliza na tabasamu la aibu kidogo. “Hatukuachana vizuri.
Nikawa nawasiwasi sikujua unaendeleaje! Japokuwa daktari alisema upo sawa,
lakini sikujua moyoni unaendeleaje!” Maya akanyamaza. “Ulinichukia?” “Hapana
Mal. Ninakushukuru. Nimempata Tunda, na nimesafisha jina langu.” “Umemwambia
sasa Mrs Cote, ulichokuwa unajutia kuwa ametekwa kabla hujamwambia?” Maya
akacheka kidogo. “Bado unakumbuka tu!” “Siwezi kusahau.” Maya akacheka
taratibu.
“Sijapata muda bado. Amerudi na mambo mengi. Na pia
halali vizuri kwa hofu. Unakumbuka alitekwa akiwa usingizini, amerudishwa akiwa
usingizini. Hilo linamsumbua. Anaogopa asije akalala, wakamchukua tena.” “Hiyo
ni kawaida kabisa. Lakini itaisha na atakuwa sawa tu. Mtakuja kupata muda wa
mazungumzo kama zamani na utaweza kumwambia.” “Sasa hivi sidhani kama inamaana
tena?” “Kwa nini?” Maya akafikiria.
“Nitakuja kukwambia wakati mwingine.” “Kweli!?”
Malcom ni kama hakuamini kama Maya anafikiri kuja kumuona tena. Maya akacheka.
“Naamini tutakuja kupata muda mwingine wa kuzungumza.” Wakaangaliana na kucheka
kidogo.
“Nikuulize swali?” Maya akauliza kwa upendo. Malcom
mikono mfukoni huku akimwangalia. “Karibu!” Malcom akakubali. “Kwa nini
ulinikatia tamaa?” Maya akauliza kwa kulalamika kidogo. Malcom akanyamaza kwa
muda. Akamwangalia na kuangalia pembeni. Kisha akarudi kumwangalia Maya.
“Naomba nikujibu wakati mwingine. Isiwe leo.” Maya akanyamaza na kuinama.
“Ni sawa?” Malcom naye akauliza kwa kubembeleza
kama asiyetaka kuharibu. “Lini tutaonana tena?” Swali la Maya lilionyesha na
yeye ameingiwa na shauku ya kuja kumuona tena huyo Malcom. “Wakati gani unakuwa
na nafasi?” Maya akafikiria. “Sasa hivi nipo nyumbani na Tunda kumsaidia mtoto.
Kazi zangu nafanyia nyumbani tu.” “Ni sawa nikikupigia kesho tupange?”
“Nitafurahi kukusikia.” Maya akajibu na tabasamu zuri usoni.
“Okay. Nitakupigia kesho.” “Nitakuwa nasubiri simu
yako kwa hamu.” Malcom akachekeka na kumbusu shavuni. “Asante.” Maya
akashukuru. Malcom akacheka na kuondoka. Maya alijawa furaha. Akabaki
akijishika shavuni.
Baada ya kupitishwa
kwenye Moto,
Familia hiyo ya
Cote!
M |
aya akarudi alipoacha familia yake, wote
wakamwangalia. Akaanza kucheka. Net akainama na kumbusu mwanae, akaendelea
kumpapasa taratibu akimwangalia. “Malcom amekuja kuniona, Nana!” Bibi yake
akacheka. “Kwani ulikuwa ukimsubiri?” “Nilitaka kumuona akihangaika na
kujitahidi mpaka anifuate. Nilidhani anaweza
kutishwa na Cote. Lakini amepambana mpaka amekuja!” Tunda akacheka. Maya
akajifuta machozi ya furaha. “Mtu wa kwanza kuniamini na kunipigania, Nana!
Wengine walikuwa wakinitukana na kuniona mimi ni mbaya. Mal ameniamini.” Net
akanyanyua macho akamtizama dada yake.
“Asante Nana kwa kumkaribisha kwenye chakula.”
“Wanastahili. Nitazungumza na Mike juu yao, angalau awatizame kwa jicho la
pili.” “Asije akamuhamisha Malcom! Mwambie ambakishe hapahapa Norfolk.”
“Unajuaje kama anaishi hapa na si kwamba wameletwa maalumu kwa ajili ya hii
kesi yetu?” Net akamfanya Maya aishiwe nguvu.
“Don’t get too attach, Maya! Usije ukaumia tena.”
Kaka yake akamtahadharisha. “Nafikiri hilo umechelewa Net.” Akadakia Tunda,
wote wakamwangalia Maya. “Ni mtu mzuri jamani!” Maya akatetea. “Lakini kuwa
mwangalifu. Sitaki kukuona unaumia tena.” Net akaongea kwa kujali. “Sina
chakupoteza Net. Nimechafuka mitandaoni na kwenye kila familia. Siaminiki na
yeyote. Kila mtu ananiona ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote. Ndio
nilikuwa nikimwambia Tunda asubuhi ya ile siku kabla hajafuatwa hapa na Vic.”
Tunda akakumbuka.
“Nilikuwa nikilia kuwa Tunda ameondoka bila
yakumwambia kitu kilichonifanya siku ile nisilale. Lakini japokuwa sikuwa
nimemtajia kitu cha moja kwa moja, lakini alinifariji na kunijenga mpaka
nikaweza kwenda kazini. Ndio jioni yake nakuja kuona mtandaoni Vic
amenigombanisha na Tunda! Sijakaa sawa wanamteka!” Maya akakaa.
“Unajua Malcom alinikuta nalia pale nje ya club?”
“Alijuaje kama upo pale?” “Atakuwa alikuwa akinifuatilia. Nikamwambia nipo pale
namtafuta Tunda. Nikamuelezea nimeanza kwa kumtafuta Renee mwenyewe, hakuwa
akipokea simu zangu, nikamtafuta pia kupitia Gina, nimegonga mwamba. Sasa wakati
huo kwenye mahojiano Malcom alikuwa ameshaniahidi atanisaidia kumtafuta Andy
sijui Jake, ili kutafuta ukweli wa mambo yote! Ndipo nilipomwambia nipo pale
namlilia Tunda. Kuna kitu nilitaka kumwambia lakini nikashindwa. Ndipo
akaniambia atanisaidia kumpata Tunda na kusafisha jina langu.”
“Akaniambia ameshampata Andy ambaye ndio Jake. Na
mengine mengi tu. Ndio tukaongozana
kutoka pale mpaka kwa jake.” “Kwa hiyo kumbe mlishakuwa naye!?” Tunda akauliza
kwa kushangaa kidogo. “Wao wawili ndio walinihoji jana asubuhi. Kisha usiku
wake nikawa naye safarini kwenda nyumbani kwa Jake kama kwa masaa mawili na
dakika kadhaa, ambayo Malcom alinijenga na kunifanya nijisikie vizuri. Kwanza
yupo na akili za kiutuuzima. Anaongea na mimi akinifahamu vizuri na bado
aliniheshimu. Na kunifariji pia!”
“Mambo mabaya sana yalitokea nilipokutana na Jake,
sikutegemea kama angenitafuta tena. Lakini japokuwa anamuogopa Nana na Net,
amejikaza mpaka amekuja kuniona na heshima yake ipo vile vile na..” “Subiri
kwanza Maya. Unaposema mambo mabaya yalitokea ulipokutana na Jake, unamaanisha
nini!?” Net akamuuliza kwa mshtituko sana. “Siwezi kukwambia Net. Naomba tushukuru
Mungu tumempata Tunda kwa msaada wake, na lile tukio limeweza kufichua hila za
Vic.”
“Lakini pointi yangu ni kuwa, kwa yote katika yote,
bado Malcom amenitafuta wakati kuna mtu nilimsogelea kwa kumtaka akutane na
mimi kwa ushauri tu, aliniambia maneno mabaya sana.” “Alikwambia nini?” Tunda
akamuuliza. Maya akalia kwa uchungu sana. “Usilie sasa. Niambie kabla
hawajanichukua tena.” “Hawawezi kukuchukua tena
Tunda. Kwa mara ya kwanza mpaka nimeongea na Mungu kwa umakini sana.”
Wote wakacheka.
“Kweli. Nimemwambia Mungu asiruhusu
wakuchukue wewe kama alivyowachukua Papa na dad. Nahisi nitachanganyikiwa
Nana!” Kila mtu akamuhurumia Maya. Hawakujua kwake
imebeba sura hiyo. “Nitahakikisha kwa kila uwezo wangu niliopewa na Mungu hapa
duniani, hakuna atakayemchukua tena Tunda wala kumtoa kwenye maisha yenu.” Bibi
Cote akaongea kwa hisia zote na kwa kujiamini.
“Na mimi maombi yangu kwa Mungu, nitamsihi
nikiondoka hapa duniani, mbakie hivyo hivyo watatu na wengine waongezeke
pembeni yenu.” Ikawagusa wote mpaka Tunda akajirudi nafsini mwake. Wakatulia
kimya kila mtu akijifikiria.
“Ni nini huyo mtu alikwambia Maya?” Tunda akavunja
ukimya. “Sasa hivi wote tutakuangalia Maya. Hatujisahau tena. Na wala
hatutakupuuza. Umesikia?” Tunda akamfariji. Maya akatingisha kichwa. “Na mimi
nitajitahidi kugawa muda wangu angalau tuwe kama zamani.” “Nitafurahi Net.” “Najuta! Naona tulikuacha
kipindi kigumu sana ukiwa unatuhitaji. Lakini kama alivyosema Tunda, hutukuachi
tena peke yako.” Maya akafurahia hilo.
“I love you Maya. Na samahani sweetheart. Katika
muda wangu wote niliobakisha hapa duniani, nitajitahidi kuwa makini zaidi na
wewe. Sitaruhusu mtu akuumize tena.” Bibi yake pia akaongeza. “Thanks Nana.”
Maya akaenda kumkumbatia na kumbusu bibi yao.
“Alikwambia nini kilichokuumiza?” Bibi yake
akauliza na yeye. Maya akarudi kukaa. “Kipindi kile cha maandalizi ya harusi.
Nilitaka kumsaidi Tunda kwenye kitu fulani. Nikataka nifanye kwanza mimi
mwenyewe, kikikamilika na kuona au kujiridhisha kipo sawa, ndipo nimwambie
Tunda.” Maya akaendelea. “Nikamtafuta mtu ambaye anauelewa na hicho kitu.
Nikamuomba tukutane sehemu kwa maongezi ili anishauri kabla sijamfikishia wazo
Tunda.” Maya akaanza kulia.
“Alinipa maneno mabaya Nana, bila
hata kufikiria nitakachojisikia.” “Alikwambia
nini?” “Alisema hataki hata kuonekana na mimi
hadharani. Yaani kile kitendo cha watu kutuona naye hadharani nitamuharibia
maisha yake ambayo amehangaika sana kuyajenga. Nikashangaa sana. Nikamwambia
hata hajui ni nini nataka kumwambia!
Akasema yeye hayupo tayari nimuingize kwenye mitego yangu na kumfikisha
kama nilichofanya kwenye maisha ya vijana wengine niliowaharibia maisha yao
hapa Norfolk!” Maya akaendelea kuelezea huku akilia.
“Nikamwambia nilitaka tu kuzungumza
naye nimuombe ushauri juu ya harusi, sikuwa na nia mbaya. Akasema huwa naanzaga
hivyohivyo na kuishia kuwaharibu vichwa vijana wa Norfolk. Akaniambia kama
kweli ni maswala ya harusi, basi ahusike Tunda mwenyewe, au Stacy, lakini sio
mimi na yeye tu. Akanikatia simu.” Kila mtu
akaumia sana. Nakubaki kimya kwa muda kila mtu akiwaza lake na kutaka kumjua ni
nani huyo!
“Pole sana Maya.” Tunda akasimama na kwenda kumshika kwa kumkumbatia. “Pole. Sasa kwa nini hukuniambia?” “Nilijua ungetaka kumjua ni nani halafu ungemwambia Net, mkamchukia wakati ni kweli nilishaharibu sana. Ni ngumu kuaminika.” “Hata kama. Hakutakiwa kukwambia hivyo!” Bibi Cote akaongea kwa kuumia sana. “Lakini Maya, imekusaidia kukujenga na kujua watu wanaoweza kuwa na wewe sasa hivi. Katika yote, atakayerudi na kukuita rafiki, ujue huyo ndiye rafiki wa kweli.” “Sitaki tena rafiki Nana. Wote waliweza kununuliwa na Vic, au walijua Vic anawanunua watu kwa ajili ya kuniangamiza, wakaacha naanikwa uchi mitandaoni halafu wananyamaza tu! Acha nibaki na Tunda tu.”
“Hata mimi hilo naliunga mkono Maya. Hata kama wamemkamata Vic, lakini kuwa nao
makini. Sio watu wakuaminika. Marafiki gani ambao wanaweza kununulika na
kukubali kukudhuru? Ikitokea mtu mwingine akitaka kuwalipa wakufanyie kitu
kingine!” Net akaongeza.
“Kwanza na wenyewe lazima walipe. Nitazungumza na
Mike. Wameshiriki kwa namna moja au nyingine. Lazima na wenyewe wahusike kwenye
hukumu. Wamekutesa na kukudhalilisha kwa muda mrefu sana. Sitakubali waachwe
hivihivi. Lazima wajifunze kutocheza na sisi. Na iwe fundisho kwao na wote
ambao hata wanafikiria kuja kutudhuru baadaye.” Bibi Cote akaonekana
ameshakasirika. Akanyanyuka na kuondoka.
Maya naye akaona awapishe wanandoa hao na mtoto
wao. Akasimama na kwenda kumbusu Net akiwa amembeba Cote kisha Tunda. “Ulale. Usiwe na wasiwasi. Nimetoka nje nimekuta nyumba imezungukwa na polisi, hakuna
mtu wa kuingia na kukuchukua.” Tunda akacheka. Maya akaondoka.
Usiku, Net &Tunda Tena.
W |
akajikuta wamebaki wao wawili tu pale
mezani.“Twende ukalale. Nitakuwa na wewe.” “Wewe unaishia kulala bwana!” Net
akacheka kidogo. “Nilikuwa nimechoka akili Tunda. Niliingiwa hofu ya
kupitiliza. Kule kukukumbatia tu akili ikapoa. Mwili ukazima kabisa. Lakini
nakuahidi sasa hivi nitakuwa macho.” Tunda akafikiria. “Sitaki uwe macho. Wewe lala tu kama utataka
kulala. Najua mimi itachukua muda kurudia hali ya kawaida. Bado nina hofu.”
“Nikikwambia usiogope itasaidia?” Tunda akavuta pumzi kwa nguvu.
“Eti Tunda?” Akamwangalia Net. “Haisaidii Net. Labda kwako.” Tunda akasimama.
“Naomba mtoto nikamlaze.” “Lakini kesho itabidi Ms Emily akusaidie Tunda. Na ni
kwakuwa huamini watu wengine. Lakini unahitajika kupumzika kabisa.” “Kama Ms
Emily, sawa. Lakini sitaki mtu mwingine amshike mtoto wangu wala anisogelee,
Net. Nitachanganyikiwa!” “Sawa. Ms Emily atahamia kwako kwa muda.” Wakarudi
chumbani kwa mtoto.
Net kimya akifikiria alichomwambia Tunda. Akambadilisha mtoto, kisha akampa
Tunda amnyonyeshe. Yeye akakaa mbele yake ameinama. Tunda akajua sana
analowaza, ila akaamua amuache. Baada ya kumlaza mtoto, Tunda akarudi kukaa
palepale. Akamwangalia. “Ulimaanisha nini uliposema labda kwangu?” “Namaanisha
hiyo faraja ya usiogope, inakufaa wewe ambaye mabaya yanakuzunguka tu, lakini
hayakupati Net.” Tunda akaanza taratibu tu.
“Neno usiogope kwa kila anayejihusisha na wewe, ni neno rahisi sana na halina maana kwetu tunao jihusisha na wewe. Inakuwa ni kama ile habari ya kwenye bibilia ya kina Daniel, kwenye tanuru la moto. Wote waliotumwa kuwatupa kwenye tanuru la moto waliteketea lakini kina Daniel walibaki salama. Sasa ndivyo tulivyo tunao kuzunguka wewe."
"Gabriel alifariki kifo kibaya sana. Bethy yupo jela, hatakaa
akatoka. Mimi nilifungwa. Walinikamata mbele yako. Nilikaa jela miezi sita.
Lakini maisha yako wewe yaliendelea kama kawaida. Nimetoka na kuanza kupambana
tena na mama yako, na aliyekuwa mpenzi wako.” Tunda akacheka taratibu.
“Mama yako anahangaika kuniua. Mpenzi wako hana
mipaka kwangu. Katikati ya ulinzi mkali tu, wamefanikiwa kuniteka mimi! Lakini
si wewe Net. Wakati wote wewe upo salama.” Tunda akafikiria kidogo kisha
akaendelea. “Unajua alichopitia Maya ili Jake kuweza kufanya kazi ya watu
wanaoaminika hapa nchini kushindwa kunipata na kusafisha jina lako?” Net
akakunja uso na kubadilika kabisa.
“Ninacho maanisha ni kwamba, kuwa makini sana na
kila neno unalowaambia watu wako wa karibu wanao kuzunguka Net. Wanalipa garama
kubwa sana kwa wewe kuendelea kuwa Nathaniel Cote. Neno usigope pekee,
halitoshi kwa kule tunakopitia tunao kuzunguka, ila wewe. Kwako ni sawasawa.
Kwa sababu kwa hakika kwako kila kitu kitakuwa sawa. Usiogope. Hivi karibuni,
watasafisha jina lako. Kuwa ulilevya. Ndio maana ulifanya mapenzi na aliyekuwa
mpenzi wako na akakuchukua video bila ya wewe kujua. CSIS watakutetea, na
mahakamani watapitisha. Usiogope, kwa kuwa kila kitu kitakuwa sawa. Lakini ni
je, inakuaje kule alikopitishwa Maya kuhakikisha jina lako linasafishwa?
Madonda aliyopitia mpaka leo, akiwa anazungukwa na watu kama nyinyi?” Tunda
akamuuliza taratibu tu.
“Majuzi kabla hatujakutana kule kwenye kuonja
chakula ukagomba sana, Maya alikuja chumbani mara ulipoondoka tu kwenda kazini.
Niliongea na Maya, alikuwa akilia kwa uchungu sana kwa makuzi aliyokuwa. Ndani
ya hili jumba la kifahari. Wote mkiwa mnamajina mazuri kila mahali, isipokuwa
yeye peke yake akichafuliwa mitandaoni, lakini hakuna aliyejisumbua kujua ni
kwa nini! Hakuna aliyemsikiliza au kutafuta muda wa kukaa naye chini na
kuzungumza naye!”
“Maya anasema alipokuwa akitangazwa yupo matatizoni
ndio wote mlikuwa mkikimbilia eneo la tukio, lakini si kutaka hata kujua
anaendeleaje kwenye maisha yake ya kila siku au imekuaje amefika pale!”
“Nilikuwa na majukumu Tunda. Nilikuwa Tanzania! Ningefanyaje?” Net akajaribu
kujitetea.
“Mimi sijui maisha yenu Net. Lakini nataka
kukwambia hivi, kuwa makini na kila unalotaka kuzungumza na Maya na watu wanao
kuzunguka. Sasa hivi wote mnafikiri mnahusika na maisha ya Maya kwa kumwambia
nini afanye. Lakini yule mtoto hana tofauti na mimi Net. Maya amejilea
mwenyewe. Najua unaelewa ni nini namaanisha.”
“Wewe unajua majukumu ya bibi yako. Vile alivyokuwa
babu yako. Mama yako na wewe mlikuwa Tanzania. Nani alikuwa akimlea Maya ambaye
sasa hivi mnataka awe na maadili fulani!? Anayatoa wapi hayo maadili mazuri?
Nani aliwekeza kwenye maisha ya Maya mbali ya kumpa mapesa mengi yaliyokuwa
yakisubiriwa na maadui zake huko nje ili yamuangamize yeye mwenyewe?” Tunda
akaendelea kumuuliza taratibu tu.
“Maya huyu ni Cote, lakini jua maisha ya zamani
aliyoishi akihangaika mitaani akitafuta marafiki waliokuwa wakimtumia vibaya,
tena wakati mwingine kumfukuza kama mbwa mpaka awapelekee pesa, amejikuza
mwenyewe, Net. Amekuzwa na maadui zake huko mtaani.”
“Nikuulize tu Net, ulishawahi kujiuliza ilikuaje
Maya akaanza madawa?” Kimya. “Ulishatafuta muda wa kukaa naye na kuzungumza
naye mbali na kumtoa mtaani akiwa na madawa na kwenda kumfungia rehab? Mnamtoa
nyumbani alipokuwa peke yake, mnakwenda kumfungia tena rehab na madaktari ambao
hawamjui, wanampokea kama binti waliyekuwa wakimzungumzia Roy. Kitoto cha
kitajiri kinachotapanya pesa. Je, hata mara moja ulishajiuliza na kujaribu
kuzungumza naye?” Kimya.
“Mwanzo wake ni walimuwekea madawa kama hivi kwenye
kinywaji tu. Akalewa, wakamrudisha nyumbani. Anasema kutoka club, akaja kuamka
kitandani kwake kesho yake asubuhi. Alipokuja kuwauliza wenzake, wakamwambia
walimuwekea madawa makusudi ili kuondoa upweke. Yaani mpaka watu wamtaani
walikuwa wakijua kuwa Maya alikuwa mpweke, nyinyi mkashindwa!” Net akazidi
kuumia. Lakini kimya.
“Yule mtoto anasema walikuwa wakimlazimisha afanye
mambo mabaya, akikataa wanamfukuza. Na Maya anasema alikuwa hataki kuwaacha kwa
kuwa ndio watu pekee waliokuwepo kwenye maisha yake. Anasema alikuwa akichoka
kushinda humu ndani tu na Carter, ikabidi awe anawafuata hao marafiki ambao
walikuwa wamenunuliwa na mpenzi wako!” “Naomba usiseme hivyo Tunda. Unaniadhibu
vibaya sana.” Hapo ikabidi Net aongee.“Nilikuwa na Vic zamani sana. Na
nilishindwana naye na yeye alijua hatawahi kuwepo kwenye maisha yangu.
Usimtambue kama mpenzi wangu. Alikuwa.” Tunda akanyamaza.
“Niambie kile unachotaka nifanye Tunda. Tafadhali.
Sijui nini chakufanya!” “Ongeza umakini kwa watu wanaokuzunguka. Hilo tu.”
Tunda akasimama. “Naomba usiondoke Tunda. Tafadhali tuzungumze.” “Unataka
kuongea nini?” “Kaa basi.” Tunda akarudi kukaa na kumtizama.
“Inawezekana mimi nina udhaifu Tunda. Kuna mambo napelea.
Naomba unisaidie. Usinichukie. Niambie kile ambacho ungependa nifanye.
Nakupenda wewe na nimekuchagua. Sina mpango wa kukuacha, na hata ukitaka
tuachane, sitakuacha.” Tunda akainama.
Net akaenda kupiga magoti pale mbele ya Tunda na
kumshika mikono yote miwili. “Nitajirekebisha Tunda. Hata kwa Maya,
nitajirekebisha na nitakuwa makini hata kwa watoto wetu. Niambie kile
unachotaka nifanye. Nakuahidi nitafanya.” Kimya. “Nakupenda Tunda. Nakupenda
sana na ninaumia kuona unapitishwa huko unakopita. Natamani kama wangekuwa
wakinitendea mimi sio wewe. Sina jinsi. Niambie ni nini unataka nifanye,
nitafanya. Unataka nini?” “Twende ukanikumbatie pale kitandani, nilale mikononi
mwako.” Net akambeba kutoka pale kwenye kiti na kumuweka kitandani.
“Naruhusiwa hata kukubusu?” “Sijui Net! Bado nina
hasira.” “Najua. Kwa nini usiache nikukiss uone kama haitasaidia?” Tunda
akacheka taratibu. “Okay.” Akakubali. Net akamkumbatia pale kitandani na kuanza
kunyonya midomo yake taratibu huku akimpapasa. Taratibu akamuona ile tension
mwilini inapungua. Hakufika mbali, akaona anatulia na kulala. Akamkumbatia
vizuri na kumfunika, wakalala.
Usiku
wa Maya kwa bibi yake.
W |
akati bibi yake analala Maya akaingia. “Umelala
Nana?” Akaita Maya. “Bado. Njoo tulale
wote.” Bibi yake akawasha taa ndogo ya pembeni ya kitanda, Maya akapanda
kitandani. Bibi yake akamgeukia vizuri. “Kwa nini hulali?” “Namfikiria mama!”
Bibi yake akatulia. “Kwa nini anashindwa hata kutufikiria, Nana? Unafikiri dad alimlazimisha kuzaa naye?”
“Sijui Maya. Ila ninalojua, Mungu alinipa mimi watoto wawili. Basi.” Bibi Cote akatulia kidogo.
“Najuta kuwa sikuwa
makini kwenye makuzi yako. Najuta sana Maya.
Natamani kurudisha siku nyuma, nianze upya, lakini siwezi. Najuta sana.”
Wote wawili wakaanza kutokwa na machozi. “Unajua
ndio kitu alichonishinda nacho Vic? Alikuwa akiwa na wazazi wake wakiwa kwenye
kila hatua ya maisha yake. Najiuliza hivi ni kwa nini mama yeye alishindwa kuwa
na mimi! Angalau hata kunilea hata kidogo tu! Alihusika kwenye kuniadhibu lakini si kunilea!” Maya akaongea kwa
uchungu.
“Mama yako hakuwa mnafiki Maya. Alijitoa kwenu
mapema sana. Kosa ni langu mimi. Niliwapokea nikiwa na majukumu mengi sana.
Sikujua kuweka mipaka. Nikawekeza kwenye mambo mengi nikitetea watoto wengine
na kusahau watoto wangu mwenyewe!” Maya akataka kumsikia zaidi.
“Unamaanisha nini?” “Halikuwahi kuwa kosa la mama
yako Maya. Ni mimi nilizembea. Tokea mwanzo kabisa, mama yako aliwakataa
kuwalea. Ni kama alituuzia nyinyi. Akalipwa pesa na kurudi Tanzania. Wewe na
Net ni jukumu langu kwa asilimia 100, mimi ndio nilishindwa.” Akamuelezea Maya
kwa kifupi, Maya akaumia sana.
“Ritha ni jukumu langu. Na ni tatizo nililolilea
tokea uhai wa baba yako. Sikujua jinsi ya kufanya naye. Lakini naona sasa hivi
Mungu ameingilia kati, atashugulika naye. Nisamehe, na mwache Mungu ashugulike
naye.” Maya akamsogelea bibi yake, Bibi yake akamkumbatia. Wakatulia.
“Malcom!” Bibi
Cote akamchokoza. Akamsikia Maya akicheka. “Alinifuata Nana!” “Na ujue ameriski
sana kuja. Ingemgharimu kazi yake.” Maya akacheka kwa furaha. “Na nimemuona
jinsi anavyokuangalia!” Maya akacheka na
kujifunika na mto usoni. “Alikuwa
akitaka nini?” “Kujua ninaendeleaje mbali na vipimo vya daktari.” Maya akajibu
huku akicheka. “Sasa unaendeleaje mbali na vipimo vya dakatri?” Bibi yake naye
akauliza akicheka. Maya akazidi kucheka. “Sasa hivi baada ya Malcom kuja
naendelea vizuri.” Bibi yake akacheka sana.
“Ujue Nana, hakuna mtu aliyefika umbali wa Malcom
kwangu?” “Maya Cote! Punguza mwendo.” “Hudhani kama ananipenda?” “Sitaki
kukuona unaumia tena. Mpe muda na yeye umuone anafika wapi.” “Naona kweli nijipe muda. Kama kweli anania nzuri,
tutaona.” “Hilo ni wazo zuri. Na kwa kuwa anajua kabisa bosi wake ni rafiki
yangu, hawezi kufanya mchezo.” “Kweli.” Maya akatulia. Wakalala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Katikati ya ulinzi mkali wakiwa bado hawajui
hatari inawazunguka kutoka wapi na Ritha naye ameshamfikia nani mwingine ili
atimize azma yake ya kumdhuru Tunda, maana alishamletea Malinda mpaka ndani ya
jumba hilo ili akamfanyie kazi Tunda, Malinda amekufa, muuwaji wao hajakamatwa,
na Malcom naye ameongezeka kwenye picha. Bibi Cote ameapa mwisho wa Ritha mwenye
akili na makini kwenye mipango yake kuwa, umefika.
Nini kitaendelea? Usipitwe
0 Comments:
Post a Comment